Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Answers to Primary Questions by Hon. Innocent Lugha Bashungwa (15 total)

MHE. GIMBI D. MASABA aliuliza:-

Serikali imekuwa ikiwapangia wakulima wa pamba bei ndogo wakati wa mavuno bila kuzingatia gharama kubwa walizotumia kipindi cha uzalishaji:-

Je, Serikali haioni sasa wakati umefika kuwaacha wakulima wauze pamba kwa bei kubwa wanayotaka wao?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. INNOCENT L. BASHUNGWA) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa ni mara yangu ya kwanza kujibu maswali ya Waheshimiwa Wabunge, kwa ridhaa yako, naomba nitumie nafasi hii kwanza nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa nguvu ya kuweza kusimama hapa.

Mheshimiwa Spika, pia nitumie nafasi hii kipekee kumshukuru sana Mheshimiwa Rais wetu, Dkt. John Pombe Magufuli pamoja na wasaidizi wake kwa kuniamini na kuniteua katika hii nafasi ya Naibu Waziri wa Kilimo. Namuahidi Mheshimiwa Rais pamoja na wasaidizi wake, nitafanya kazi kwa uadilifu na kwa maarifa yangu yote katika kutekeleza majukumu ambayo wamenikabidhi.

Mheshimiwa Spika, pia nitumie nafasi hii kukushukuru wewe pamoja na Waheshimiwa Wabunge kwa support yenu mpaka nikaweza kufika hapa. Ninawaahidi ushirikiano na naamini mtanipa ushirikiano katika kutimiza majukumu yangu. Pia nitumie nafasi hii kuwashukuru sana wapiga kura wangu wananchi wa Karagwe.

Mheshimiwa Spika, baada ya utangulizi huo, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Gimbi Dotto Masaba, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali haiwapangii wakulima bei ya kuuza pamba bali huratibu upatikanaji wa bei nzuri ya pamba kwa wakulima. Sheria ya Pamba Na.2 ya mwaka 2001 inaipa Serikali kupitia Bodi ya Pamba jukumu la kukaa na wawakilishi wa wakulima na kampuni za kununua pamba kukubaliana bei elekezi ambayo inazingatia gharama za uzalishaji.

Mheshimiwa Spika, kwa wastani gharama za uzalishaji wa ekari ya pamba inakadiriwa kuwa Sh.488,000.

Ekari moja iliyotunzwa vizuri hutoa wastani wa kilo 1,000 sawa na kuzalisha kilo moja kwa Sh.488. Bei iliyopangwa na wadau wa pamba yaani bei elekezi ya msimu wa mwaka 2018/2019 ilikuwa Sh.1,100 ambapo kwa mkulima aliyezalisha kwa tija ya kilo 1,000 kwa ekari na kuuza kwa bei hiyo hakuuza chini ya gharama za uzalishaji.

Mheshimiwa Spika, wakulima wa pamba ni wadau muhimu katika kupanga bei ya pamba kwa kila msimu. Serikali inatambua umuhimu huo, hivyo imefanya maboresho katika mfumo wa uuzaji kwa kufufua na kuimarisha vyama vya ushirika kwa lengo la kuongeza fursa ya wakulima kushiriki katika soko kupitia ushirika wao. Upangaji wa bei ya pamba huzingatia vigezo mbalimbali ikiwemo bei ya pamba nyuzi katika soko la dunia, kiwango cha kubadilishia fedha, bei ya mbegu za pamba, gharama za usafirishaji, uchambuaji na uwiano kati ya nyuzi na mbegu.

Mheshimiwa Spika, kwa mfano, katika mwezi Septemba, 2018, baadhi ya wakulima wa Mkoa wa Simiyu waliuza pamba kwa Sh.1,200 kwa kilo juu ya bei elekezi kutokana na mabadiliko ya bei ya pamba katika soko la dunia.

Mheshimiwa Spika, fursa ya wakulima wa pamba kuuza bei wanayotaka itaongezeka kwa kuwa Serikali inaendelea kuhamasisha uwekezaji katika tasnia ya pamba hasa kuongeza viwanda vya kuchakata pamba hapa nchini. Aidha, Serikali inaendelea kujenga uwezo wa wakulima ili kuongeza tija katika zao la pamba na hatimaye kuongeza uzalishaji na pato la mkulima mmoja mmoja.
MHE. BONIPHACE M. GETERE aliuliza:-

Kwa kuwa msimu wa pamba wa mwaka 2018/2019 ulikuwa na bei elekezi ndogo ya Sh.1,100 na kwa kuwa mara nyingi bei hizo elekezi zinapendekezwa kwa msukumo wa bei ya pamba duniani:-

(a) Je, Serikali katika msimu wa mwaka 2019/2020 ina mkakati gani wa kuinua bei ya wakulima kutoka Sh.1,100 hadi Sh.2,500?

(b) Kwa kuwa kuna Vyama vya Ushirika na Benki ya Wakulima, je, Serikali ina mkakati gani wa kumaliza tatizo la usambazaji wa mbegu za pamba katika Wilaya ya Bunda na hasa Jimbo la Bunda ambapo kila mwaka kunakuwa na uhaba wa mbegu na kutofika kwa wakati?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. INNOCENT L. BASHUNGWA) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Boniphace Mwita Getere, Mbunge wa Jimbo la Bunda, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-

(a) Mheshimiwa Spika, bei za mazao na bidhaa mbalimbali hutegemea nguvu ya soko kwa kuzingatia kiwango cha uzalishaji (supply), mahitaji (demand), ubora na viwango vinavyohitajika katika masoko ya ndani na nje na ushindani uliopo katika masoko husika.

Mheshimiwa Spika, kuongezeka kwa bei ya pamba kutoka Sh.1,100 hadi Sh.2,500 katika msimu wa ununuzi wa 2019/2020 kutategemea nguvu za soko hususani kupanda kwa bei ya pamba katika soko la dunia. Aidha, pamoja na kutegemea nguvu ya soko la dunia, Serikali inatekeleza mikakati ya kuhamasisha uwekezaji katika Viwanda vya Nyuzi na Nguo ili kuimarisha soko la ndani na ushindani.

(b) Mheshimiwa Spika, Serikali imechukua hatua ya kuongeza upatikanaji wa mbegu za pamba nchini, ambapo katika msimu wa mwaka 2018/2019 jumla ya tani 27,851 zilizalishwa na kusambazwa kwa wakulima ikilinganishwa na tani 20,496 zilizozalishwa msimu wa mwaka 2017/2018 ikiwa ni ongezeko la asilimia 36. Aidha, kati ya mbegu zilizozalishwa mwaka 2018/2019, tani 1,075 zimesambazwa katika Wilaya ya Bunda ikilinganishwa na tani 688 zilizotumika msimu wa kilimo wa mwaka 2017/2018 ikiwa ni ongezeko la asilimia 56.

Mheshimiwa Spika, Benki ya Maendeleo ya Kilimo inahudumia sekta ya kilimo kwa ujumla wake kwa kutoa mikopo yenye riba nafuu ukilinganisha na benki zingine. Aidha, Benki ya Kilimo inatarajia kushiriki katika ununuzi wa pamba sambaba na benki nyingine zilizopo nchini kwa kutoa mikopo kwa kampuni zitakazoshiriki katika ununuzi wa pamba kama ilivyofanyika msimu wa ununuzi wa mwaka 2018/2019.
MHE. DKT. GODWIN O. MOLLEL aliuliza:-

Aliyekuwa Naibu Waziri wa Kilimo, Mheshimiwa Olenasha alitembelea Wilaya ya Siha kufuatilia ubadhirifu kwenye Shamba la Ganrangua na SACCOS ya Sanya Juu wa shilingi milioni 337 na Siha Kiyeyu shilingi milioni 840 ambapo aliiagiza TAKUKURU kuchunguza ubadhirifu huo:-

(a) Je, Serikali iko tayari kufanya upembuzi na kutambua mashamba ya umma, yasiyotumika vizuri na kurejesha kwa wananchi kwa kutumia vijiji na ushirika wao kama wazo la kwanza la Baba wa Taifa J. K. Nyerere, mfano wa baadhi ya mashamba hayo ni Kafoi Farm (Mifugo), Leoni(Ushirika-Mfilisi), Msingi (Ushirika-Mfilisi), Pirita (Ushirika- Mfilisi), Pongo (Ushirika-Mfilisi) na mengine mengi?

(b) Pamoja na juhudi nzuri zilizofanywa na Waziri Mkuu kuhusu ubadhirifu KNCU, je, Serikali ina taarifa kuwa ubadhirifu kwenye mali za KNCU na Vyama vya Ushirika ni mkubwa na unaendelea kulindwa na wahusika hawagusiki na bei ya zao la kahawa linaendelea kuathirika?

(c) Je, Serikali inaweza kuwaeleza nini wananchi wa Siha kuhusu Shamba la Gararagua lililouzwa na KNCU mwaka 2014 na makabidhiano kufanyika mwaka 2016, likitoka mkononi mwa Ocean Link lakini Kampuni hii mpya imepata EPZ Exemption mwaka 2012 na je, Serikali haioni kuna harufu ya ufisadi?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. INNOCENT L. BASHUNGWA) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Godwin Oloyce Mollel, Mbunge wa Jimbo la Siha, lenye sehemu (a),(b) na (c), kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, upembuzi na utambuzi wa mashamba umekuwa ukifanywa na Serikali kila inapohitajika ili kufanya maamuzi sahihi ya matumizi ya mashamba. Mashamba ya Leoni, Msingi, Pirita na Pongo yanamilikiwa na Vyama vya Ushirika isipokuwa Shamba la Kafoi ambalo linamilikiwa na mtu binafsi. Mashamba haya yalikuwa na migogoro kwa muda mrefu kati ya vyama na wawekezaji ambao kwa sasa migogoro hiyo imekwishatatuliwa. Aidha, Serikali kupitia Tume ya Maendeleo ya Ushirika inasimamia kwa karibu vyama husika ili kupata wawekezaji wapya kwa maendeleo ya wanachama wa Vyama vya Ushirika na wananchi wa Vijiji vya Wilaya ya Siha.

Mheshimiwa Spika, ni kweli Serikali imechukua hatua kwa viongozi na watendaji waliobainika kujihusisha na ubadhirifu wa mali za KNCU kwa kuwafikisha Mahakamani kwa kesi ya uhujumu uchumi. Aidha, Serikali kwa kupitia Tume ya Maendeleo ya Ushirika katika kutekeleza jukumu lake la ukaguzi wa mara kwa mara kwa Vyama vya Ushirika, itaendelea kufanya ukaguzi kwa Vyama vya Ushirika, ikiwemo KNCU na pale itakapobainika kuwa kuna ubadhirifu wa mali za vyama, Serikali haitasita kuwachukulia hatua wale wote wanaohusika bila kujali nyadhifa au uwezo wa aina yoyote walionao.

Mheshimiwa Spika, Shamba la Gararagua limeuzwa na KNCU mwaka 2014 kwa kuzingatia taratibu za manunuzi. Aidha, msamaha wa kodi yaani exemption uliotolewa kwa mwekezaji huyo mwaka 2012 unahusiana na uwekezaji wa Shamba la Kifufu na siyo Gararagua.

Mheshimiwa Spika, kuhusu tuhuma za ufisadi, Wizara itafuatilia suala hilo na itakapobainika kuna viashiria hivyo, Serikali itachukua hatua stahiki kwa mujibu wa sheria.
MHE. NASSOR SULEIMAN OMAR aliuliza:-

Kilimo cha mazao ya viungo vya chakula ni biashara yenye tija kubwa duniani kwa sasa:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kuhamasisha kilimo hicho hapa nchini?
NAIBU WAZIRI KILIMO (MHE. INNOCENT L. BASHUNGWA) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Nassor Suleiman Omar, Mbunge wa Jimbo la Ziwani, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua umuhimu wa mazao ya viungo kutokana na mchango wake katika kipato cha mkulima mmoja mmoja na pia katika kuliingizia Taifa fedha za kigeni. Kutokana na umuhimu huo, Serikali kwa kushirikiana na sekta binafsi imeandaa mkakati wa kuendeleza mazao ya viungo (Spice Sub Sector Strategy twenty fourteen) ambao unalenga kuongeza uzalishaji na tija.

Mheshimiwa Naibu Spika, maeneo mahususi katika mkakati huo ni utoaj mafunzo ya kuongeza ujuzi katika uzalishaji kwa wataalam na wakulima, uanzishwaji wa vituo vya kukusanyia mazao na kupanga madaraja na kuunda masoko ya pamoja ya wakulima.

Mheshimiwa Naibu Spika, maeneo mengine mahsusi yanayofanyiwa kazi ni kuhamasisha na kusimamia uanzishwaji wa vitalu vya kuzalisha miche na mashamba ya miti mama kwa ajili ya kuzalisha miche bora ya aina za mazao hayo. Mkakati huo unatekelezwa kwa pamoja na wadau mbalimbali zikiwemo Taasisi zisizo za Kiserikali na Vyama vya Wakulima ambazo ni pamoja na Sustainable Agriculture Tanzania, Chama cha Wakulima wa Viungo, Amani (CHAWAVIA) na Jumuiya ya Wakulima wa Viungo Wilaya ya Muheza.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali pia imeandaa mwongozo wa uzalishaji wa mazao ambao umeainisha maeneo yanayofaa kwa uzalishaji wa mazao mbalimbali yakiwemo mazao ya viungo. Mwongozo huo unalenga kuonesha fursa za uzalishaji wa mazao mbalimbali yakiwemo mazao ya viungo. Wizara ndani ya miezi sita ijayo itakamilisha zoezi la usajili wa wakulima wa mazao mbalimbali nchini ikiwemo mazao ya viungo kwa kubaini idadi yao, ukubwa wa mashamba na mahali alipo ili kuwahudumia kwa ufanisi zaidi na kuongeza tija.
MHE. MARGARET S. SITTA aliuliza:-

Moja kati ya changamoto zinazowakabili wakulima wa tumbaku katika Wilaya ya Urambo ni madeni yanayotokana na mikopo ya pembejeo ikiwemo mbolea:

(a) Je, Serikali inachukua hatua gani ili kuwasaidia wakulima kuepukana na changamoto hii?

(b) Je, Serikali ina mkakati gani wa kushusha bei ya pembejeo ili kumsaidia mkulima?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. INNOCENT L. BASHUNGWA) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Margaret S. Sitta, lenye vipengele (a) na (b), kama ifuatavyo:-

(a) Mheshimiwa Naibu Spika, kuanzia mwaka 2008, Serikali imeboresha mfumo wa upatikanaji wa pembejeo za zao la tumbaku kwa wakulima kupata pembejeo kupitia vyama vya ushirika tofauti na ilivyokuwa kabla ya mwaka 2008 ambapo pembejeo za tumbaku zilitolewa kupitia kampuni zinazonunua tumbaku kwa kuwakopesha wakulima na kuwakata wakati wa mauzo. Utaratibu huo ulikuwa na changamoto kadhaa ikiwa ni pamoja na riba kubwa isiyo na tija kwa mkulima.

Mheshimiwa Naibu Spika, ili kuondokana na madeni yatokanayo na riba za mkopo wa pembejeo, Serikali imewahamasisha wakulima kupitia vyama vyao vya ushirika kuainisha mahitaji ya pembejeo mapema na wamekubali kukatwa kiasi cha fedha kutokana na mauzo ya tumbaku ili kuagiza pembejeo hizo kwa wakati. Mfano Chama cha Msingi cha Kahama (KACU) wamekubaliana kukatwa Sh.60 kwa kila kilo kwa lengo la kukusanya takribani shilingi bilioni 3 zitakazotosheleza kuagiza asilimia 75 ya mahitaji ya pembejeo. Utaratibu huo unafanyika kwa vyama vyote ambapo wakulima watanufaika kwa kupata bei ndogo kuliko ile ya kukopa.

(b) Mheshimiwa Naibu Spika, Mfumo wa uagizaji Mbolea kwa Pamoja (Bulk Procurement System - BPS) ulianzishwa kwa lengo la kupunguza gharama au kodi kwa wakulima. Hata hivyo, mfumo huo unategemea bei ya mbolea iliyopo katika soko la dunia kwa wakati huo. Kutokana na changamoto za ongezeko la bei ya mbolea katika soko la dunia, Serikali inasimamia Mfumo wa Uagizaji wa Mbolea kwa pamoja ili kuhakikisha kuwa wakulima wakiwemo wa zao la tumbaku wanapata pembejeo kwa wakati na kwa bei nafuu.
MHE. FRANK G. MWAKAJOKA aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itaunga mkono tamko la Kilimo ndiyo Uti wa Mgongo wa Taifa kwa vitendo?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. INNOCENT L. BASHUNGWA) alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Kilimo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Frank George Mwakajoka, Mbunge wa Jimbo la Tunduma, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa muda mrefu Serikali inatambua na inaunga mkono tamko la Kilimo ni Uti wa Mgongo kwa Taifa. Umuhimu wa sekta ya kilimo unajidhihirisha katika viashiria mbalimbali vya kiuchumi na kijamii kama vile mchango wa kilimo katika ajira, pato la Taifa, usalama wa chakula na malighafi za viwandani. Takribani asilimia 65.5 ya wananchi wameajiriwa katika sekta ya kilimo, asilimia 28.7 ya pato la Taifa hutokana na sekta ya kilimo, mazao ya chakula huchangia kiasi cha asilimia 65 ya pato la Taifa litokanalo na kilimo. Zao la mahindi huchangia zaidi ya asilimia 20 ya pato la Taifa litokanalo na kilimo, mazao ya chakula na biashara yanachangia asilimia 70 ya kipato katika maeneo ya vijijini. Aidha, sekta ya kilimo ni muhimu katika mikakati ya kuendeleza sekta ya viwanda nchini kwa kuchangia takribani asilimia 65 ya malighafi za viwanda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inayo mikakati na mipango inayolenga kuimarisha sektya kilimo ili kuongeza tija na uzalishaji wa mazao ya kilimo pamoja na kuwapatia wakulima masoko ya uhakika. Sera, mikakati na mipango inayotekelezwa ni pamoja na Sera ya Taifa ya Kilimo ya mwaka 2013, Programu ya Kuendeleza Sekta ya Kilimo Awamu ya II (ASDP II) pamoja na sera, mikakati na mipango mingineyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, moja ya jitihada madhubuti ya kutambua Kilimo ndiyo Uti wa Mgongo ni kuanzishwa kwa Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) ambayo inatoa mikopo ya riba nafuu ya asilimia 8 tu. Aidha, Serikali imeendelea kupunguza ada, tozo na kodi katika kilimo, kuimarisha huduma za utafiti ikiwa ni pamoja na kuanzisha Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) na kuimarisha ushirika ili uweze kuwezesha na kusimamia masoko ya mazao ya kimkakati.
MHE. ENG. EDWIN A. NGONYANI aliuliza:-

Je, Wizara ya Kilimo inashirikianaje na Wizara nyingine zinazohusika na uwekezaji wa mambo ya nje kutafuta soko la tumbaku nchini Misri badala ya kulazimika kutumia nchi za Uganda na Kenya peke yake?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. INNOCENT L. BASHUNGWA) alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Edwin Amandus Ngonyani, Mbunge wa Namtumbo, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2014/2015, uzalishaji wa tumbaku ya moshi (Dark Fire Cured Tobacco- DFC) ulisimama Mkoani Ruvuma kutokana na kukosa soko. Jitihada za Serikali zikawezesha kampuni ya Premium Active Tanzania Limited kuonesha nia ya kununua tumbaku hiyo ya DFC ambayo hapa nchini huzalishwa Namtumbo na Songea Vijijini, Mkoani Ruvuma. Kampuni hii ilieleza kuwa lipo soko kubwa la tumbaku aina ya DFC nchini Misri na Algeria, lakini tumbaku ya Tanzania inauzwa kwa bei ya juu kutokana na kodi inayotozwa ikilinganishwa na aina hiyo ya tumbaku kutoka nchi za Uganda na Kenya kwa kuwa nchi hizo Uganda, Kenya, Algeria na Misri ni wanachama wa Jumuiya ya COMESA na kwa hiyo kodi za kuingiza tumbaku, chai na bidhaa nchini Algeria na Misri kutoka Uganda na Kenya ni za chini ukilinganisha na Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na hilo, Wizara ya Kilimo inashirikiana na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kuanzisha mazungumzo na Nchi Wanachama wa COMESA na nchi kama Misri na Algeria kupitia Balozi zetu ili kuandaa makubaliano maalum yaani bilateral agreement yatakayowezesha nchi yetu kupeleka tumbaku katika nchi hizo kwa kodi nafuu. Mazungumzo hayo yamefikia hatua nzuri na matarajio ni kufungua milango ya soko hilo na hivyo kuongeza kipato kwa wakulima na Taifa kwa ujumla. Aidha, makubaliano hayo yakikamilika Tanzania inaweza pia kuuza chai nchini Misri na Algeria kwa faida kuliko ilivyo hivi sasa au badala ya kuuza chai kupitia mnada wa Mombasa nchini Kenya.
MHE. RICHARD P. MBOGO aliuliza:-

(a) Je, ni lini Serikali italeta mbegu bora ya tumbaku kama inayolimwa katika nchi nyingine Kusini mwa Jangwa la Sahara?

(b) “Produce cess” ilishushwa kutoka asilimia tano mpaka asilimia tatu ili mkulima afaidike kwenye bei ya kuuza lakini hakuna utekelezaji kwa Makampuni ya Kununua Tumbaku na kwenye Halmashauri mapato yameshuka. Je, Serikali inaweza kupitia upya Sheria hiyo na kurudisha kama awali?

(c) Je, ni lini Serikali itakaribisha Kampuni nyingine za kununua Tumbaku ili kuongeza ushindani na kuondoa hofu kwa wakulima?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. INNOCENT L. BASHUNGWA) alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Richard Philip Mbogo, Mbunge wa Nsimbo, lenye sehemu (a), (b) na (c), kama ifuatavyo:-

(a) Mheshimiwa Mwenyekiti, uhitaji wa aina ya tumbaku hutofautiana kati ya mteja na mteja. Tumbaku inayozalishwa nchini kwa sasa inatokana na mbegu zinazopendwa na wanunuzi waliopo. Wizara imepokea maombi kutoka Nchi ya China ya kuuziwa aina ya tumbaku inayotokana na mbegu zinazolimwa katika Nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara. Utaratibu wa kupate mbegu za tumbaku aina za PVH 2254 na KRK 26 kutoka Malawi na aina ya MHW 86 kutoka Zambia umeanza ili mbegu hizo ziweze kuzalisha tumbaku inayokidhi soko la China kuanzia msimu wa 2020/2021.

(b) Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba Serikali ilipunguza ushuru wa mazao ya biashara katika mwaka wa fedha 2017/2018, kutoka asilimia tano hadi asilimia tatu ili kuongeza kipato cha wakulima. Utekelezaji wa Sheria hiyo umefanyika kwa mwaka mmoja tu wa fedha wa 2018/2019, hivyo Serikali itafanya tathmini ya utekelezaji wa sheria hiyo na kama itabainika utekelezaji wake katika tasnia ya tumbaku hauna tija kwenye mapato ya Halmashauri na kipato cha mkulima, Serikali haitasita kuchukua hatua na kupitia upya sheria hiyo.

(c) Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kupunguza ukiritimba wa Kampuni zinazonunua Tumbaku nchini, Serikali inaendelea kuweka mazingira wezeshi ili kuzivutia kampuni nyingine zaidi na kuleta ushindani. Kufuatia jitihada hizo, Serikali imefanikiwa kupata kampuni zingine za kununua tumbaku ikiwemo Kampuni ya British-American Tobacco (BAT) ambayo imeonesha nia ya kununua tumbaku yetu moja kwa moja kutoa kwa wakulima. Taratibu za kufanikisha mpango huo zinafanyika ili Kampuni hiyo iweze kununua tumbaku ya wakulima kwa msimu wa Mwaka 2019/2020. Aidha, katika hatua nyingine, Serikali inakamilisha taratibu za kulipata soko la China kwa kutumia mbegu za tumbaku zinazozalishwa katika nchi zilizopo Kusini mwa Jangwa la Sahara.
MHE. FREDY A. MWAKIBETE aliuliza:-

Wananchi wa Kata za Mpombo, Kandete, Isange na Luteba pamoja na Kata za Kabula, Lwanga na Lupata wanalima zao la chai kwa wingi lakini bei ya zao hilo ipo chini:-

Je, ni lini Serikali itatafuta soko la uhakika la zao la Chai ambalo litasababisha kupanda kwa bei kuliko bei ya sasa ya Shilingi 315 kwa kilo?
WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA alijibu:-

Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Fredy Atupele Mwakibete, Mbunge wa Busokelo, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Bodi ya Chai Tanzania iliitisha kikao cha wadau wa chai kilichofanyika Aprili, 2019 kutafuta ufumbuzi wa changamoto mbalimbali za wakulima ikiwa ni pamoja na kupanga bei elekezi ya chai kwa mwaka 2019 kwa kuwashirikisha wadau wote. Mkutano huo wa Wadau wa zao la chai ulifanyika tarehe 3 Aprili, mwaka 2019 Mufindi Mkoani Iringa na Wajumbe walipitisha bei elekezi ya majani mabichi ya chai kwa mwaka 2019 kuwa ni shilingi 315 kwa kilo.

Mheshimiwa Spika, jitihada za Serikali kutafuta masoko ya mazao ya kilimo nchini ni jukumu endelevu. Kwa upande wa zao la chai, jitihada zinafanyika ili kuhakikisha kuwa chai inayozalishwa inauzwa hapa nchini bila kuwalazimu Wakulima kusafirisha chai yao kwenda kwenye mnada wa Mombasa. Katika kutekeleza hilo, Serikali inakamilisha mkakati wa kuanzisha soko la chai Tanzania kwa kuanzisha mnada wa Kimataifa wa Chai Jijini Dar es Salaam.

Mheshimiwa Spika, katika kutekeleza uanzishwaji wa mnada wa chai nchini Tanzania kikosi kazi kiliundwa ambacho kinajumuisha Bodi ya Chai (TBT), Soko la Bidhaa Tanzania (TMX), Bodi ya Usimamizi wa Stakabadhi wa Ghala, Chama cha Wakulima wa Chai Tanzania, Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania, Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara (TANTRADE) pamoja na Wakala wa Maendeleo ya Wakulima wadogo wa Chai Tanzania yaani (TSHTDA). Maandalizi ya mnada huo yanatarajiwa kukamilika mwezi Septemba, 2019 ili tuwe na mnada wetu utakaosaidia kupunguza gharama za usafirishaji wa chai nje ya nchi na faida inayopatikana iongeze bei ya mkulima.

Mheshimiwa Spika, nashukuru. (Makofi)
MHE. NEEMA W. MGAYA aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itawalipa fidia wananchi wa Makambako ili kupisha ujenzi wa soko la Kimataifa?
WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA alijibu:-

Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Neema William Mgaya Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, mradi wa ujenzi wa soko la Makambako ulianza baada ya Serikali kuona umuhimu wa kujenga masoko ya kimkakati (Strategic Markets) kwa lengo la kuwezesha upatikanaji wa masoko ya uhakika kwa mazao ya Wakulima. Soko hilo lilibuniwa, ili kufanikisha upatikanaji wa soko la uhakika kwa mazao ya kilimo hususan nafaka za mahindi na mchele ambazo huzalishwa kwa wingi katika Mikoa ya Njombe, Ruvuma na Mbeya.

Mheshimiwa Spika, napenda kumfahamisha Mheshimiwa Mbunge kwamba, mwaka 2018 Serikali ililipa kiasi cha shilingi 3,026,341,089.58 ikiwa ni fidia kwa wananchi 209 wa Makambako ili kupisha ujenzi wa soko hilo. Aidha, wakati wa ulipaji fidia, walijitokeza wananchi 15 ambao wakati wa uhakiki wa mwisho hawakupatikana na wananchi 20 ambao hawakuwepo kwenye daftari wala taarifa ya uhakiki. Kwa muktadha huo, Serikali imeamua kufanya tathmini tena kwa wananchi ambao hawajalipwa fidia zao ili waweze kulipwa kama wanastahili.

Mheshimiwa Spika, ninaupongeza uongozi wa Mkoa wa Njombe na Waheshimiwa Wabunge wanaotoka Mkoa huo kwa ushirikiano walioutoa katika zoezi zima la ulipaji fidia kwa wananchi waliopisha mradi wa ujenzi wa soko la Kimataifa la Makambako. Zoezi la ulipaji fidia kwa wananchi wote litakapokamilika litawezesha mradi husika kutekelezwa bila kuwa na vikwazo.
MHE. DKT. MARY M. NAGU aliuliza:-

Serikali iliondoa kodi kwenye mbegu za mahindi mwaka 2017 – 2018:-

Je, ni lini Serikali itasimamia upunguzwaji wa bei kubwa ya mbegu za mahindi na pembejeo?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. INNOCENT L. BASHUNGWA) alijibu:

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Mary Michael Nagu, Mbunge wa Hanang, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuchukua hatua ambazo zinzsaidia kupunguza bei za pembejeo ikiwa ni pamoja na kufuta ada na tozo zilizokuwa zinatozwa na taasisi za udhibiti wa pembejeo za kilimo. Katika kipindi cha mwaka 2017 na 2018 Serikali imefuta ada na tozo 12 katika tasnia ya mbegu kwa lengo la kupunguza gharama za uzalishaji na bei ya mbegu.

Mheshimiwa Spika, mnamo mwezi Februari, 2019 Serikali imekutana na wadau wa pembejeo za kilimo kwa lengo la kujadili maendeleo ya pembejeo za kilimo, ikiwemo kujadili suala la bei ya mbegu. Katika kikao hicho wadau walikubaliana kufanya utafiti wa kuhusisha taasisi ya udhibiti wa mbegu Tanzania (TOSCI) na Chama cha Wafanyabiashara wa Mbegu (TASTA) ili kutathmini gharama za uzalishaji na usambazaji. Jitihada zinazoendelea ni kutafuta vyanzo vya fedha ili kumuwezesha mshauri elekezi kufanya tathmini hiyo. Matokeo ya tathmini hiyo yatawezesha upangaji wa bei ya mbegu ambayo itamnufaisha mkulima na mzalishaji. Ahsante.
MHE. JASSON S. RWEIKIZA aliuliza:-

Ugonjwa wa Mnyauko wa Migomba umekuwa tatizo kubwa na la muda mrefu na limewaathiri Wakulima wa Migomba Mkoani Kagera:-

Je, ni kwa nini Serikali haichukui hatua za makusudi za kupambana na ugonjwa huo na kuutokomeza kabisa?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (INNOCENT L. BASHUNGWA) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Jasson Samson Rweikiza Mbunge wa Bukoba Vijijini kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, mnyauko wa migomba kitaalamu unaitwa unyanjano wa migomba. Husababishwa na vimelea aina ya bacteria ambao hushambulia aina zote za migomba na jamii yake. Ugonjwa huu unasambazwa na ndege, nyuki, binadamu, ngedere na tumbili; miche iliyoathirika; vifaa vya shambani vilivyotumika kwenye migomba iliyoathirika na vifungashio vya kusafirisha ndizi.

Mheshimiwa Spika, kwa kipindi cha kuanzia mwaka 2006 - 2014, Wizara ya Kilimo kwa kushirikiana na Uongozi wa Mkoa wa Kagera tumekuwa tukitoa mafunzo ya kutokomeza ugonjwa huo kwa wakulima na Maafisa Ugani kwenye Wilaya zote zilizoathirika. Serikali imekuwa ikiendesha kampeni ya kung’oa migomba yote iliyoathirika, kukata Ua Dume na kuitekeleza. Halmashauri zote za Wilaya ya Mkoa wa Kagera ziliweka sheria ndogo ndogo za kuwataka wakulima kung’oa na kuchoma au kuzika migomba yote ailiyoathirika. Zoezi hilo lilipunguza ueneaji wa ugonjwa huo kwa asilimia 70.

Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea kufanya tafiti za kuzalisha miche bora ambayo haina vimelea vya ugonjwa wa unyanjano kupitia Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) ikishirikiana na Shirika la Belgium Technical Cooperation. Hadi sasa miche bora milioni sita imezalishwa na kusambazwa kwa wakulima katika Mikoa ya Kagera na Kigoma.

Mheshimiwa Spika, Serikali inatoa wito kwa wakulima kote nchini kutumia mbegu bora za migomba aina ya Shia 17, Shia 23, Nshakara, Nyoya na Kinohasha zinazozalishwa katika Taasisi za Utafiti Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine Mikocheni, Uyole, Kibaha, Maruku na Tengeru ili kuongeza tija katika uzalishaji na kutosafirisha ndizi zilizofungashwa na majani ya migomba kutoka mashamba yaliyoathirika.

Mheshimiwa Spika, ahsante.
MHE. ENG. EDWIN A. NGONYANI aliuliza:-

Mkoa wa Ruvuma umepata mnunuzi wa tumbaku ambaye amekubali kuwawezesha SONAMCU kufufua kiwanda cha kuchambua tumbaku na kugeuza green leaf kuwa dry leaf. Aidha, kutokana na changamoto za kodi na soko mnunuzi huyo hajaweza kutekeleza azma yake.

Je, Serikali inasaidiaje kutatua changamoto zinazomkabili mnunuzi huyo?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. INNOCENT L. BASHUNGWA) alijibu:- Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mhandisi Edward Amandus Ngonyani, Mbunge wa Namtumbo kama ifutavyo:-

Mheshimiwa Spika, kufuatia kuondoka kwa kampuni mbili za ununuzi wa tumbaku Mkoani Ruvuma msimu wa 2014/ 2015, wakulima walikosa soko la uhakika. Kutokana na hali hiyo Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali pamoja na Mheshimiwa Mbunge Ngonyani walifanya juhudi za kutatua changamoto hiyo.

Mheshimiwa Spika, jitihada hizo zilisaidia kupatikana kwa mnunuzi wa tumbaku ambaye ni Kampuni ya Premium Active Tanzania Limited ambayo ilianza kununua kilo 250,000 na sasa imeongeza hadi kilo 1,000,000. Serikali pia inapongeza nia ya kampuni hiyo ya kutaka kukiwezesha Chama Kikuu cha Ushirika cha Mkoa huo cha SONAMCU kufufua kiwanda cha kuchakata tumbaku.

Mheshimiwa Spika, kwa msingi huo Wizara ya Kilimo ipo tayari kushirikiana na Wizara ya Fedha na Mipango na mwekezaji huyo kutafuta ufumbuzi wa changamoto za mnunuzi huyo ili kuhakikisha kuwa kampuni hiyo inatimiza azma hiyo njema kwa wananchi wa Mkoa wa Ruvuma na taifa kwa ujumla, ahsante.
MHE. DKT. SHUKURU J. KAWAMBWA aliuliza:-

Wananchi wengi katika Kata za Fukayosi na Kiwangwa Bagamoyo wanalima mananasi kwa wingi sana.

Je, nini mkakati wa Serikali kuhusu kuwajengea viwanda vya kuchakata zao hilo ili kuboresha kipato cha wakulima hao?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA (K.n.y. WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Viwanda na Biashara napenda kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Shukuru Kawambwa, Mbunge wa Bagamoyo kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua kuwa Wilaya ya Bagamoyo ni moja kati ya Wilaya zinazolima mananasi kwa wingi Mkoani Pwani. Kwa kutambua uwepo wa malighafi hiyo kwa wingi, Serikali inaendelea kuhamasisha sekta binafsi kuwekeza katika viwanda vya kusindika matunda ikiwa ni pamoja na mananasi yanayolimwa katika Wilaya ya Bagamoyo. Hii inaendana na matashi ya dira yetu ya Taifa ambayo inatambua kuwa sekta binafsi ndiyo engine ya ukuzaji uchumi wa viwanda.

Mheshimiwa Naibu Spika, juhudi za Serikali za kuhamasisha uwekezaji viwandani zimezaa matunda ambapo kwa sasa kuna viwanda viwili vikubwa vya kusindika matunda katika Wilaya ya Bagamoyo vya Elven Agri Co. Ltd. na Sayona Fruits Co. Ltd. vyenye uwezo wa kusindika tani 28 za matunda kwa siku na kuajiri jumla ya wafanyakazi 755.

Aidha, ili kuwa na uhakika wa malighafi za kutosha kwa mwaka mzima, tunashauri Mheshimiwa Mbunge kuendelea kushirikiana na Serikali kuhamasisha uzalishaji wa aina nyingine za matunda yatakayotumika baada ya msimu wa mananasi kupita ili kuwezesha viwanda kuzalisha kwa kipindi kirefu kwa mwaka. (Makofi)
MHE. RUKIA K. AHMED aliuliza:-

Mazingira ya kufanya biashara nchini ni magumu na hii ni kwa wafanyabiashara wa ndani na wa nje:-

Je, ni lini Serikali itaondoa urasimu ili wananchi waweze kunufaika?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU SAYANSI NA TEKNOLOJIA (k.n.y. WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Viwanda na Biashara, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Rukia Kassim Ahmed, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imekuwa ikibuni na kutekeleza mikakati na mipango mbalimbali kwa kuhakikisha uwepo wa mazingira bora ya ufanyaji biashara nchini. Kwa mwaka 2017, Serikali kwa kushirikiana na wadau wa Sekta binafsi ilifanya uchambuzi wa kina wa mazingira ya biashara nchini kwa sekta zote na kubaini changamoto mbalimbali zikiwemo mwingiliano wa sheria. Kufuatia changamoto hizo, Serikali iliandaa Mpango wa Kuboresha Mfumo wa Udhibiti wa Mazingira ya Biashara Nchini (Blue Print for Regulatory Reforms to Improve the Business Environment for Tanzania) ambao umeridhiwa na Baraza la Mawaziri kwa ajili ya utekelezaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mpango huo utasaidia kuondoa mwingiliano wa sheria na kupunguza urasimu kwa wafanyabiashara wakati wa kupata huduma katika Taasisi mbalimbali za Serikali. Mpango wa Utekelezaji wa Blue Print umekamilika. Sambamba na hilo, Serikali tayari imetekeleza baadhi ya mapendekezo ambayo ni ya kiutawala na yasiyohitaji mabadiliko ya sheria. Mfano, katika Sekta ya Kilimo na Mifugo, jumla ya tozo 114 na tano za OSHA zimeondolewa na mapendekezo ya kuondolewa tozo nyingine kupitia Muswada wa Sheria ya Fedha wa mwaka 2019 yameshawasilishwa Wizara ya Fedha na Mipango.

Mheshimiwa Naibu Spika, moja ya mafanikio ya jitihada zinazofanywa na Serikali katika kuboresha mazingira ya biashara ni kwa Tanzania kuendelea kuongoza kwa uwezo wa kuvutia mitaji kutoka nje (Foreign Direct Investment) katika nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki tangu mwaka 2012.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mujibu wa Ripoti ya Uwekezaji ya Dunia (World Investment Report) inayotolewa na Shirika la Biashara na Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNCTAD) ya mwaka 2018, Tanzania imeongoza katika nchi za Afrika ya Mashariki kwa kuvutia mitaji ya jumla ya Dola za Marekani 1,180 ikifuatiwa na nchi ya Uganda kwa Dola za Marekani 700. Aidha, Serikali itaendelea kuhakikisha maboresho yanayofanyika yanadumishwa na kuendelea kubuni mikakati ya kuboresha zaidi mazingira ya kufanya biashara nchini. (Makofi)