Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Assa Nelson Makanika (2 total)

MHE. ASSA N. MAKANIKA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana na niipongeze Serikali kwa hatua ambazo imezichukua juu ya zao hili la michikichi, lakini vile vile nimpongeze Mheshimiwa Waziri Mkuu, ameonesha jitihada za kipekee sana katika kusaidia zao hili la mchikichi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na upungufu wa mafuta katika nchi yetu, niipongeze Serikali tu kwamba ni kweli imewekeza jitihada kwenye kuzalisha mbegu lakini napenda kujua Serikali imejiandaaje katika kuokoa mafuta yanayopotea kwenye Mkoa wetu Kigoma katika kuwekeza kwenye teknolojia? Kwa sababu kuna mafuta mengi sana yanapotea, hata hii miche iliyopo inapoteza mafuta mengi sana kabla ya kuwekeza kwenye miche mipya hii ambayo ameisema Naibu Waziri. Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali moja la nyongeza la Mheshimiwa Makanika, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hivi Serikali tumeanza maongezi na wenzetu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, TIRDO na SIDO kwa ajili ya kuja na teknolojia rahisi. Kwa sababu tume-invest katika miche baada ya miaka mitatu itaanza kutoa matokeo. Sasa itakapotoa matokeo tunakuja na mfumo wa ku-develop teknolojia ndogondogo ambazo katika household level, wananchi wataanza kukamua mafuta na kuyafanya kuwa crude ili yaweze kuzalishwa na kupunguza upotevu unaoongelewa.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Mbunge amerudia jambo hili mara ya pili, katika Kamati vilevile ali- raise concern hii, nataka nimhakikishie kwamba tunajadiliana na wenzetu wa Wizara ya Viwanda na Biashara ili kuja na teknolojia ya kupunguza hasara na upotevu.

Vilevile kuja na teknolojia rahisi ya ku-process mafuta katika primary level, katika level ya crude, pale ambapo miche hii itakuwa ime-mature na kuwafanya wakulima badala ya kuuza matunda wauze mafuta crude kwa processor wa secondary level.
MHE. ASSA N. MAKANIKA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa kuuliza swali la nyongeza. Kwa kuwa umuhimu wa reli hii ya kutokea Tunduma kwenda Kasanga unafanana kabisa na umuhimu wa barabara inayoanzia Mwandiga na kuelekea Chankere na inayopita nyuma ya Hifadhi ya Gombe na mpaka kwenda kwenye Bandari ya Kagunga. Je, Serikali haioni kuna umuhimu sana wa kuikamilisha barabara hii haraka iwezekanavyo kwa sababu, barabara hii ni barabara kwanza ya kiuchumi, lakini barabara hii pia ni barabara ya kiulinzi kwa sababu, ukanda huu hatuwezi kuwafikia wananchi wetu pasipo kupita nchi jirani ya Burundi. Je, Serikali haiwezi kututoa kwenye utumwa huu wa kupitia nchi jirani kwenda kuwahudumia watu wetu?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Makanika, Mbunge wa Kigoma Kaskazini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali itaendelea kutenga bajeti kwa ajili ya ujenzi wa barabara maana anayoongelea ni Barabara ya Mwandiga – Chankere hadi Kagunga. Serikali itaendelea kutenga fedha kwa ajili ya kusanifu barabara hiyo kwa sababu, barabara hiyo bado haijafunguliwa na tunajua kwamba, ni barabara muhimu sana kwenda Bandari ya Kasanga.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, Serikali inatambua umuhimu wa barabara hiyo kuwahudumia wananchi wa Kagunga. Mheshimiwa Makanika amekuwa anafuatilia sana hii barabara, nimhakikishie kwamba, Serikali inalifahamu na nadhani pia, ilikuwa ni ahadi ya Mheshimiwa Waziri Mkuu kwamba, hii barabara iweze kufunguliwa. Kwa hiyo, Serikali inatafuta fedha kuona kwamba, barabara hii inafunguliwa. Ahsante.