Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Assa Nelson Makanika (2 total)

Hotuba ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyoitoa wakati wa Ufunguzi wa Bunge la Kumi na Mbili, Tarehe 13 Novemba, 2020
MHE. ASSA N. MAKANIKA: Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote nichukue nafasi hii kumshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa Rehema ambaye kwa kweli amemwezesha kila mmoja wetu kufika mahali hapa. Jambo la pili, nichukue nafasi hii kumshukuru Mheshimiwa Rais pamoja naChama changu Cha Mapinduzi ambacho kwa kweli kimeweka imani kubwa kwa sisi vijana, kimetuamini katika umri huu, ni jambo kwa kweli kwa kumshukuru Mheshimiwa Rais na Chama chetu Cha Mapinduzi. Kwa kweli ni jambo ambalo mimi katika umri huu nisiposhukuru tena mara ya pili nitakuwa sijamfanyia haki Mheshimiwa Rais kwa kusema ahsante sana Mheshimiwa Rais. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na hotuba zake mbili ambazo alizitoa Mheshimiwa Rais nitajikita kuchangia sanasana katika hotuba yake aliyeitoa Novemba 13 mwaka 2020. Kumekuwa na jambo ambalo ningependa nizungumzie katika hotuba ya Rais na jambo lenyewe ni juu ya kilimo. Jambo la mafuta ya kula limekuwa nicross cutting issue na imekuwa ni current matter ambayo kwa kweli inaendelea kujitokeza mwaka hadi mwaka na mimi leo nitakuwa na mchango kidogo juu ya suala hili.

Mheshimiwa Naibu Spika, upungufu wa mafuta ya kula hapa nchini naomba iwe ni ishara ya Serikali yangu ya Chama Cha Mapinduzi na chini ya Jemedari Dkt. John Pombe Magufuli kuwa ni ishara ya kutuonyesha kwamba tunahitajika kufunga kamba ndani ya viuno vyetu ili tuweze kufikia azma ya viwanda kikamilifu. Kwa takwimu tu haraka haraka nchi yetu inaonyesha kabisa kwamba inazalisha tani laki mbili za mafuta ya kula, lakini mahitaji yetu ni tani laki tano kwa mwaka, hivyo tunakuwa na upungufu wa tani laki tatu ambazo nchi yetu inaagiza tena hasa katika nchi za bara la Asia san asana Malaysia na nchi ya Indonesia.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa tafsiri hiyo inaonyesha kabisa kwamba tunachukua pesa nyingi za kigeni kwa ajili ya kuagiza bidhaa hii ya mafuta ambayo nikisoma hotuba ya Mheshimiwa Rais ukurasa wa 15, naona hii ni aibu kubwa kwa nchi kama Tanzania ambayo ina ardhi yenye rutuba kuagiza mafuta nje. Kwa hali halisi ilivyo nakulingana na matamko mengi ambayo Serikali imekuwa ikitoa, naomba nijielekeze kuionesha Serikali kwamba kuna wajibu mkubwa wa kuelekeza katika zao hili la mbegu ambapo mafuta yanatokana na mbegu hizo.

Mheshimiwa Naibu Spika, mfano, mwezi Mei, 2017 aliyekuwa Waziri wa viwanda wakati huo Mheshimiwa Mzee wangu Mwijage alinukuliwa akisema: “Takribani asilimia 70 ya mafuta ya kula yanayohitajika kutumiwa hapa nchini huagizwa kutoka nje ya nchi, maana mafuta yanayozalishwa na viwanda vyetu hayatoshelezi kabisa.”

Mheshimiwa Naibu Spika, si hivyo, tarehe 4 Septemba2018bado kauli hii imeonyesha kabisa kwamba bado hatujajitosheleza katika kuzalisha mafuta ambayo yanatosha kutumiwa na watu wetu. Hivyo Mheshimiwa Waziri Mkuu alinukuliwa naye pia akisema kauli ambayo inafanana nahiyo nami nitamnukuu kwa kifupi sana, anasema: “Hivi sasa nchi yetu inatumia takribani dola za kimarekani milioni mia mbili tisini na nne kila mwaka kuagiza mafuta nje ya nchi.”

Mheshimiwa Naibu Spika, tafsiri ya hali hii inaonyesha kwamba pamoja na kuwa na janga la corona ambalo limeikumba dunia na limelikukumba dunia na limezikumba baadhi ya nchi bado inaonyesha changamoto hii imekuwa ikijirudia mwaka hadi mwaka, nini kifanyike na ushauri ambao naona nishauri Serikali yangu. Naona kwamba ni vema zaidi ikajielekeza kwenye kilimo cha mazao ya mbegu, kama karanga, zao la chikichi ambalo kwa kweli nimshukuru sana Mheshimiwa Waziri Mkuu amekuwa akionesha jitihada kubwa, amefika Kigoma katika kulishughulikia zao hili la chikichi. Itoshe tu kusema kwamba zao hili la chikichi linaonesha katika takwimu za kidunia kwamba ndilo ambalo limeziwezesha nchi zingine kamaNchi za Malaysia kuweza ku– supplykwetu mafuta haya ya kula na hata kusambaza duniani kote.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna faida kadhaa tukijielekeza katika kilimo cha mazao yanayotokana na mbegu. Faida ya kwanza ni jambo la uhakika ambalo soko letu la ndani tutaweza kulihudumia kwa kujitosheleza na hatimaye tutaepuka kuagiza mafuta haya ya mchikichi. La zaidi sana, itakuwa ni ishara tosha ya kwenda kutekeleza ndoto madhubuti ambayo ya kutibu aliyonayo Mheshimiwa Rais ya kuweza kuzalisha ajira milioni nane alizozisema katika Ilani ya Uchaguzi kwenye ukurasa wa tano.

Vile vile tukifanya hivyo kuwekeza katika mazao haya, itakuwa ni ishara tosha kabisa kwamba tutaifanya nchi yetu kuweza ku-export zaidi mafuta na hatimaye kutoka kwenye kundi lakuwa importation country na hiyo hiyo itatuwezesha hata kuimarisha shilingi yetu na hali ya shilingi yetu itakuwa imara.

Mheshimiwa Naibu Spika, nirudie kauli ya Mheshimiwa Rais aliyoitoa katika hotuba yake ya Novemba 13, amesema kabisa: “Kwa haya machache ninaona ni vyema zaidi Wizara husika ikachukua hatua madhubuti na kujielekeza katika mazao haya ya mbegu ili tuweze kuepukana na changamoto hii ya mafuta ambayo inajitokeza mwaka hadi mwaka”. Kwa nchi nilizozitaja kama Malaysia na Indonesia lakini nchi kama Malaysia walichukua mbegu kwetu Kigoma katika Kata ya Simbo na wakapeleka kwao kwa ajili ya kuzalisha mafuta.

Mheshimiwa Naibu Spika, naona kengele imelia, nilikuwa na mengi ya kuchangia ila mchango wangu nitauleta kwa maandishi ili Serikali waweze kuona mawazo yangu juu ya hotuba ya Mheshimiwa Rais.

Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana na naunga mkono hoja. (Makofi)
Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022
MHE. ASSA N. MAKANIKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia katika Mpango huu wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote, nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu na kuipongeza sana Wizara kwa kuleta Mpango huu. Nitajikita katika vipaumbele vitano vya mpango huu na nitajikita kwenye kipaumbele namba tatu ambacho kinasema, kukuza biashara na kipengele namba nne.

Mheshimiwa Mwenyekiti, moja kwa moja nijielekeze kushauri mambo kadhaa kwa ajili ya Mpango huu ambao umekuja mbele yetu. Kwanza, nitazungumzia mpaka wetu wa Kongo na Kigoma. Mpaka huu kihistoria unaonyesha kwamba umekuwa na mchango mkubwa wa kukuza uchumi katika Mkoa wetu wa Kigoma na hata kwa Taifa letu la Tanzania. Hivi karibuni hali ya kibiashara Mkoani Kigoma imedorora na imekuwa ni ya chini sana kwa sababu mpaka ule umekuwa hauthaminiwi. Hii ni kutokana na sera za kiuchumi ambazo kwa kweli Serikali ikizifanyia kazi tunaweza tukatoka mahali hapa tulipo na kuelekea sehemu ambayo tunataka twende. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikisoma historia ya mpaka ule wa Kongo na Tanzania inaonesha kabisa mwaka 1986 mpaka 1993 kulitokea Mkuu wa Mkoa wa pale kwetu Kigoma, Mkuu wa Mkoa wa kumi kama sijakosea, alikuwa akiitwa Christian Mzindakaya. Mzindakaya alifanya mambo makubwa sana katika uongozi wake ambayo yaliweza kuitoa Kigoma mahali ambapo katika hali ya uchumi ilikuwa ni kwenye shimo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, yeye alifanya vitu vichache tu; alichokifanya ni kurekebisha baadhi ya sera za kiuchumi, mfano visa fee ya wa Kongo kuja pale Kigoma aliweza kuishusha, lakini akaondoa na usumbufu wa wageni ambao umekuwepo hivi sasa na unashusha uchumi katika mkoa wetu wa Kigoma. Hivi sasa Mkongo akitoka Kongo kuja Kigoma anasumbuliwa na taasisi nyingi, akiingia tu kidogo TRA atakuwa nyuma, akikaa kidogo hata Polisi atamfuata kwenye hotel. Jambo hilo limekuwa likiwachukiza na hatimaye linaweza kushusha uchumi wetu. Naishauri Serikali kwamba kwa kutumia tu mpaka wa Kongo tunaweza tukapata mapato makubwa sana na tukaweza kusaidia hali ya uchumi katika Mkoa wetu wa Kigoma. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile nizungumzie zao la kahawa. Zao la kahawa linaweweseka sana na nimeweza kushauri hata hapo nyuma nimekaa na Naibu Waziri Kilimo nikamweleza, zao la kahawa linadorora kutokana na vyama vya ushirika tulivyonavyo. Vyama vingi vya ushirika mpaka dakika hii havijawalipa wakulima pesa zao na hawa wakulima wamewakopesha toka mwaka jana na wengine mpaka dakika hii wanawadai. Mfano pale jimboni kwangu kuna Chama cha Kalinzi Mkongoro kina wanachama 273 bado kinadai pesa zake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii hali inasababisha zao hili la kahawa na tena kahawa inayotoka Kigoma imeonesha inapendwa duniani kote. Kwa namna hii ambavyo tunalimbikiza madeni ya wakulima kwa kweli inashusha hali ya zao hili la kahawa na kusababisha kukosa mapato mengi kwa sababu zao la kahawa ni la tatu kwa kuingiza fedha kigeni hapa nchini kwetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kulingana na muda pia nigusie kipengele cha elimu. Ni kweli tunaandaa vijana wetu…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. ASSA N. MAKANIKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru na naunga mkono hoja. (Makofi)