Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Asya Sharif Omar (3 total)

Hotuba ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyoitoa wakati wa Ufunguzi wa Bunge la Kumi na Mbili, Tarehe 13 Novemba, 2020
MHE. ASYA SHARIFU OMAR: Mheshimiwa Spika, ahsante sana, kwanza napenda nitumie nafasi hii kumshukuru Mwenyezi Mungu, lakini kipekee nikishukuru Chama changu cha Mapinduzi ambacho kimeniamini na kikanipa nafasi na mimi nikawa Mbunge wa Bunge hili la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kipekee naomba niwashukuru Wajumbe Wanawake wa UWT wa Mkoa wa Kaskazini Pemba wanaotokana na Chama Cha Mapinduzi ambao nao walinipa imani ya kuweza kufika katika Bunge lako hili tukufu la Kumi na Mbili la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa upekee naomba nichangie hoja ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli. Mimi binafsi nikiwa Mbunge wa Bunge hili tukufu ambaye natokea Mkoa wa Kaskazini Pemba nasema hoja ile ya Mheshimiwa Rais ambayo ameiwasilisha katika Bunge hili naipongeza sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wananchi wa Kisiwa cha Pemba kwa mara hii wameonesha umahiri na wameandika historia katika kisiwa chetu. Hii ni kutokana na utekelezaji wa Ilani ambao ulionesha imani kubwa kwa wananchi na Watanzania kwa ujumla wakiwemo wananchi wa Pemba. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba niipongeze Tume ya Uchaguzi, Tume hii ilifanya kazi nzuri ambayo wananchi wale waliweza kutumia haki yao ya demokrasia kwa uwazi na uhuru bila kulazimishwa wala kuonewa. Vyombo vya habari, nitakuwa mwizi wa fadhila kama sikuvishukuru, vilifanya kazi nzuri sana bila upendeleo. Hii ni kuonekana kwamba nchi yetu ina amani, utulivu na mshikamano. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa heshima kubwa ya Bunge hili tukufu, niishukuru Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa ushirikiano mkubwa ambao umetujengea uwezo sisi Wabunge kushirikiana na Bunge letu hili na kuunganisha Watanzania wote bila ubaguzi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sisi wanawake wa Mkoa wa Kaskazini Pemba wengi tunajishughulisha na shughuli za kilimo na uvuvi. Lakini ni juzi tu kupitia Muungano huu tuliokuwa nao Serikali imeweza kusaini suala zima la uwekezaji wa utalii.

Mheshimiwa Spika, kama unavyofahamu Kisiwa chetu cha Zanzibar kinajishughulisha sana na masuala ya utalii, ni imani yangu kwamba wanufaika wakubwa tutakuwa sisi wanawake na vijana, kama ulivyosema Bunge hili huwezi kuliita ni Bunge la vijana au ni Bunge la wazee. Sasa sisi kule Pemba, wanaume hao kutokana na mambo ya dini, tunaolewa, tunakuwa na wake wenza wanne au watano. Sasa fursa hizi za Serikali… (Makofi)

Mheshimiwa Spika, samahani ni wanne. Kwa sababu fursa za Serikali zimeweza kutoa suala la ujasiriamali na kweli lazima tuseme ukweli wanawake wajane tuko wengi sana. Kwa hiyo, ni imani yangu kwamba Serikali itaendelea kutusaidia katika kuona nyanja hizi za uchumi ambazo zitawezesha wanawake kupata ajira.

MBUNGE FULANI: Sawa sawa.

MHE. ASYA SHARIFU OMAR: Mheshimiwa Spika, haiwezekani wanawake wote waajiriwe kwenye Serikali, ni lazima na ajira binafsi ziwepo. Tunampongeza sana Mheshimiwa Rais kwa imani yake. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo
MHE. ASYA SHARIF OMAR: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwanza naomba nichukue nafasi hii nikushukuru wewe binafsi kwa kunipa nafasi hii na mimi kuwa mchangiaji katika Wizara hii ya Habari. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mimi ninalotaka kuliongelea kwenye Wizara ya Habari kwanza ni kuwapongeza namna utendaji wao wa kazi za kila siku hasa kupitia vyombo vyetu vya Serikali ikiwemo TBC. Vyombo vya habari vya Serikali vinafanyakazi kubwa sana, lakini pamoja na kazi kubwa inayofanywa bado ipo haja kwa Wizara ya Habari kuona wanafanya kila jitihada kuangalia waandishi wa habari kwa vile wao ndiyo waelimishaji wa jamii ndiyo ambao wanapasha umma katika habari mbalimbali za nchi yao.

Mheshimiwa Spika, lakini pia waandishi wa habari hawa wana kazi ya kuelimisha umma, wana kazi ya kuburudisha, wana kazi ya kuonesha namna gani wanamichezo na sanaa wanafanya katika nchi yao. (Makofi)

Mimi ningeongelea jambo moja kwa waandishi wa habari, bado waandishi wa habari wanapaswa kuenziwa, wanapaswa kulindwa katika masuala mbalimbali yakiwemo maslahi yao, lakini pia yakiwemo masuala la overtime kama tunavyofahamu waandishi wa habari wanafanyakazi sana hasa wa vyombo ya Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, waandishi wa habari hawa ni mashahidi sisi wote kwamba wanafanyakazi bila upendeleo lakini wanajituma usiku na mchana sijui Wizara ina mpango gani kuona inaandaa fidia maalum pale waandishi wa habari wanapopata ajali wakiwa kazini. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya maelezo haya naomba kuunga mkono hoja, ahsante. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum
MHE. ASYA SHARIF OMAR: Mheshimiwa Spika, ahsante sana, kwanza nichukue nafasi hii nikushukuru sana kwa kunipa nafasi na mimi ya kuchangia Wizara hii ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum.

Mheshimiwa Spika, kwanza nichukue nafasi hii ya mara ya pili kusema tunakupongeza wewe binafsi kwa namna unavyoliendesha Bunge hili tukufu, tunakuombea kwa Mwenyezi Mungu aendelee kukulinda na tunasema tupo pamoja na wewe, mwanamke anaweza na ndiyo maana ukaweza. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya shukrani hizo, mimi nianze kuchangia na kuchangia nianze kumpongeza Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Mama Samia Suluhu lakini na Rais wetu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Mheshimiwa Dkt. Hussein Ali Hassan Mwinyi kwa namna wanavyoendelea kutuongoza katika nchi hii katika nyanja mbalimbali za kimaendeleo, kiuchumi, kijamii na kisiasa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mimi nianze kuchangia hoja yangu kwenye wizara hii kwenye suala zima la ukatili wa wanawake na suala la uzalilishaji wa kijinsia wakiwemo watoto.

Mheshimiwa Spika, ni dhahiri kwamba wanawake wengi wanakabiliwa na suala la udhalilishaji wa kijinsia ikiwemo ukatili na ukatili huu ambao wanapata wanawake wengi ikiwemo kutekelezwa na familia, na hii hutokea pale baadhi ya wanaume wanaposahau wajibu wao wakawaacha wanawake hawa na mzigo wa watoto. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wanawake hawa wengi wanapatwa na vilema kutokana na ukatili unaoendelea kwa baadhi ya maeneo katika nchi yetu. Wanawake hawa pia wananyang’anywa mali ambazo wamezichuma pamoja na mwanaume ambaye walifunga ndoa. Kufuatia hali hii mimi nina ushauri wangu kwa Wizara husika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwanza naiomba Serikali kuwajengea uwezo wanawake hawa kielimu ya uthubutu ili wanawake hawa sasa waweze kuvunja ukimya. Wanawake wengi wamekuwa kimya sana, wamekuwa wanaogopa. Sasa kuogopa kwao hii inapelekea wanapata maumivu makali ya kunyanyaswa bila ya sababu ya msingi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niiombe Serikali kupitia Wizara hii kuwachukulia hatua wale wote ambao wanahusika na udhalilishaji wa kijinsia kwa wanawake na watoto. Ni dhahiri kwamba wanawake wanateseka kwa kulea watoto peke yao, lakini inapelekea kuwa na ongezeko kubwa la watoto mtaani kwa sababu watoto hao wanakosa matunzo ya baba na mama na wanasahau kwamba mwanamke yule hakuweza kuzaa peke yake, alizaa kwa ushirikiano na baba. Lakini leo cha kushangaza sijui inakuwaje mwanamke huyu anatekelezwa na watoto. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niiombe sana Serikali impe nguvu mwanamke anapofika kwenye vyombo vya maamuzi ili kuweza kupata haki ya kuwatunza Watoto, lakini pia kuendelea kufurahia maisha yake. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nasema kwamba wakati umefika wa wale wote wanaozalilisha watoto na kuwatumikisha wakiwa na umri mdogo kufunguliwa kesi maalum. Kuna wimbi kubwa la baadhi ya watu kuwaajiri Watoto au niseme ajira za watoto. Hili wimbi ni kubwa sana, hata hapa Dodoma tumejionea baadhi ya maeneo kuna watu wanawaajiri, tukiwauliza anakwambia mama ndiyo amenipeleka kule mimi nifanye kazi za majumbani. Kiubinadamu haielekei, mtoto ana miaka 12/13/14 mtoto wa mwenzio unakwenda kumtuma, hasomi. Hivi kweli kama ni wa kwake angefanya hayo? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naiomba sana Wizara husika jambo hili msilifumbie macho, mlichukulie hatua kwa sababu ni jambo lipo na linaathiri nguvu kazi. Lakini naendelea kusema watoto wana haki ya kuishi, watoto wana haki ya kusoma, watoto wana haki ya kusikilizwa, watoto wana haki ya kucheza. Lakini yote haya leo hawayapati, baadhi yao hawayapati; na hawayapati kwa sababu watu wamekosa imani, lakini watu wanajaribu. Naamini Serikali yetu sisi iko imara na uwezo uko wa kuweza kushughulikia watu wa aina hii ili wasiweze kutuharibia Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya maelezo hayo kabla sijaunga mkono hoja. Nasema kwamba, naomba nimnukuu Mheshimiwa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Mama Samia Suluhu kwa kauli yake ambayo ameisema hivi karibuni kwamba; “sasa umefika wakati tupaze sauti zetu kila mtu kwa nafasi yake, alipo popote kuhakikisha kwamba tunapinga vitendo hivi vya ukatili wa kijinsia....” (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Malizia Mheshimiwa sekunde 30.

MHE. ASYA SHARIF OMAR: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Nakushukuru, naunga mkono hoja. (Makofi)