Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Amina Ali Mzee (3 total)

MHE. AMINA ALI MZEE: Mheshimiwa Spika, ahsante. Nashukuru kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, lakini niulize maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, hatua zipi zinachukuliwa na Serikali kuwawezesha vijana wanaofanya biashara mtandao ili kuwezesha mapato ya Taifa?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, je, Serikali ina mpango gani wa kutoa elimu na mikopo ili kuwezesha upatikanaji wa ajira ya ndani na nje ya nchi?
NAIBU WAZIRI WA MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Amina Ali Mzee, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kama nilivyosema katika jibu langu la msingi, Serikali kazi yake ni kuhakikisha kwamba inaweka mazingira wezeshi kwa vijana ili waweze kufanya biashara hiyo. Sambamba na hilo kupitia biashara zozote za kimtandao Serikali imeweza kurasimisha shughuli hizo kwa kuanzisha sheria ya makosa ya kimtandao maana yake kwamba kijana ili aweze kujua mipaka ya namna gani biashara yake akaifanye.

Mheshimiwa Spika, vilevile kuna Sheria ya Mawasiliano ya Kieletroniki na Posta ya Mwaka 2010, hii yote inatoa guidelines za namna gani kijana anaweza kuingia katika biashara hiyo.

Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo kwa sababu unapofanya biashara lazima kuna transactions zitakuwa zinafanyika, ili sasa kumlinda katika zile transactions Serikali pia ilichukua jukumu la kuanzisha Sheria ya Miamala ya Kieletroniki ambayo sasa transaction yoyote inakuwa inatambulika, anapokuwa anafanya hizi biashara.

Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo kupitia Wizara yetu kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu kupitia vijana hawa, Serikali ina mpango mzuri wa kutoa elimu ambapo vijana watakuwa wanajua namna gani na sehemu zipi wanaweza kuwa wanapata mikopo kwa ajili ya kujiongezea kipato na hatimaye tunaongeza pato la Taifa letu.

Mheshimiwa Spika, nakushukuru.
MHE. AMINA ALI MZEE: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, naomba kuuliza swali moja la nyongeza kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, natambua wanufaika wakubwa ni vijana Watanzania: Je, Serikali ina mpango gani wa kupanga fedha kwa ajili ya kukiendeleza chuo hiki? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA, AJIRA NA WENYE ULEMAVU (MHE. PATROBAS P. KATAMBI): Mheshimiwa Spika, tayari Serikali imeshakuwa na mpango wa kujenga jengo hilo litakalokuwa na urefu wa ghorofa sita na tayari fedha zimeshatengwa kwa ajili ya shughuli hiyo. Kwa hiyo, tunamshukuru sana Mheshimiwa Amina kwa kuwa mfatiliaji.

Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo, tuna habari nyingine njema ambayo Mheshimiwa Rais Mama Samia Suluhu Hassan ameshatoa zaidi ya shilingi bilioni 54 kwa ajili ya kuwasaidia vijana zaidi ya 150,000 ambao wataenda kupata mafunzo mbalimbali katika vitengo hivyo ikiwemo uchumi wa bahari. Ahsante. (Makofi)
MHE. AMINA ALI MZEE: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri. Usalama wa vyombo vya majini ni lazima kwa maisha ya watu na mali zao. Je, Serikali inafanyaje kila baada ya muda kuvifanyia ukarabati kisheria?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali moja la nyongeza la Mheshimiwa Amina Ali Mzee, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba usalama ni jambo la msingi na ni lazima lifanyike. Kwa sheria yetu tunafanya ukaguzi kila mwaka kwa vyombo vyote vya majini na kwenye maziwa makuu, na huwa tunatoa cheti kinachoitwa seaworthiness certificate. Hata hivyo, hatulazimiki tu kwa mwaka, tunaweza tukafanya pia kwa wakati wowote inapobidi shirika lijiridhishe na vyombo hivyo. Ahsante.