Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Amina Ali Mzee (4 total)

MHE. AMINA ALI MZEE Aliuliza:-

Je, Serikali imejipangaje kuhamasisha vijana nchini kujiunga na biashara mtandao?
NAIBU WAZIRI WA MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI Alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Amina Ali Mzee, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuchukua hatua mbali mbali katika kuweka mazingira wezeshi nchini ya kuvutia wananchi wengi kujiunga na biashara mtandao hususan vijana. Mwaka 2015 Serikali ilitunga Sheria ya Miamala ya Kielektroniki kwa lengo la kutambua miamala ya kielektroniki inayofanyika kimtandao.

Mheshimiwa Spika, Serikali kwa sasa inapitia Sheria na tozo mbalimbali ambazo ni kikwazo kwa vijana, wabunifu wa TEHAMA na wale wanaochipukia (start-ups) ili kuweka mazingira wezeshi ya vijana kushiriki kwenye biashara mtandao. Hii hatua inakwenda sambamba na maboresho yanayoendelea ya kupunguza tozo za leseni za maudhui mtandaoni, kazi ambayo inatarajiwa kukamilika mwezi Oktoba, 2021.

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Shirika la Posta Tanzania imeanzisha jukwaa la kutangaza na kuuza bidhaa na huduma kwa njia ya mtandao ambapo maduka 270 ya kuuza na kununua bidhaa yamesajiliwa na jukwaa hili ambalo linapatikana kupitia tovuti https://www.postashoptz.post. Jukwaa hili limeunganishwa na mtandao wa vituo 670,000 duniani. Jukwaa hili linatoa fursa kwa wafanyabishara ikiwemo vijana kutumia mtandao huo kufanya biashara mtandao kwa kuunganisha wauzaji na wanunuzi wa bidhaa na huduma ulimwenguni. Ahsante.
MHE. AMINA ALI MZEE aliuliza: -

Je, Serikali inatumiaje Chuo cha Bahari cha DMI kuendeleza vijana wa Kitanzania ili kukabiliana na changamoto za ajira?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA, AJIRA NA WENYE ULEMAVU (MHE. PATROBAS P. KATAMBI) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Amina Ali Mzee, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Chuo cha Bahari Dar es Salaam (DMI) ni Chuo cha Serikali ambacho kimeanzishwa kwa Sheria ya Bunge Na. 22 ya mwaka 1991 Chuo kinatoa elimu na mafunzo katika sekta ya usafiri wa njia ya maji na hivyo kina mchango mkubwa katika kukuza ajira nchini.

Mheshimiwa Spika, katika kukabiliana na changamoto za ajira, Chuo cha DMI kina kitengo maalum cha uwakala wa ajira za mabaharia (DMI Crewing Agency). Kitengo hiki kilianza kazi mwaka 2018. Kina usajili Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) kwa ajili ya kutafuta ajira na mafunzo melini kwa vijana wa Tanzania kwa meli za ndani na nje ya nchi yetu hususan kwenye mashirika mbalimbali ya meli ikiwemo Azam Maritime, Zan Fast Ferry, TPA Kyera, Greece Marine Company na Verba Shipping Company.

Mheshimiwa Spika, kwa kutambua umuhimu wa kuwawezesha wahitimu wa Chuo cha DMI na mabaharia wa Tanzania kupata ajira katika meli za Kimataifa, Serikali inaendelea na taratibu za kuridhia Mkataba wa Kimataifa wa Kusimamia masuala ya Bahari duniani (IMO Convention
– Maritime Labour Convention). Kuridhiwa kwa mkataba huu, kutawezesha kutoa mafunzo na ajira kwa mabaharia takriban 150 ambao ni sawa na 25% ya wahitimu kwa mwaka. Ahsante. (Makofi)
MHE. ASYA SHARIF OMAR K.n.y. MHE. AMINA ALI MZEE aliuliza:-

Je, lini Serikali itaanza ujenzi wa madarasa na mabweni ya Chuo cha Usafirishaji (NIT) Mabibo?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Uchukuzi naomba kujibu swali la Mheshimiwa Amina Ali Mzee, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2022/2023 Serikali kupitia East Africa Skills for Transformation and Regional Integration Project (EASTRIP), mradi unaofadhiliwa na Benki ya Dunia, imeanza ujenzi wa mabweni mawili yenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 1,500. Ujenzi wa mabweni hayo umefikia asilimia 28. Aidha, kupitia mradi huo Serikali inajenga jengo lenye Madarasa ya wanafunzi 1,500 pamoja na maabara na karakana yenye kuchukua wanafunzi 500 kwa wakati mmoja ambapo ujenzi huo umefikia asilimia 30.

Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea kukamilisha ujenzi wa Kituo cha Rasilimali Mafunzo (maktaba) chenye madarasa yenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 1,653 kwa wakati mmoja ambapo ujenzi huo kwa sasa upo kwenye asilimia 85.

Aidha, katika mwaka wa fedha 2023/24, Serikali kupitia mapato ya ndani ya Chuo, itaanza ujenzi wa Jengo la Kitaaluma la ghorofa tano litakalokuwa na uwezo wa kuchukua wanafunzi 4,700 kwa siku, mara litakapokamilika.
MHE. AMINA ALI MZEE aliuliza:-

Je, ni lini Mkongo wa Mawasiliano wa Taifa utapelekwa katika Wilaya 14 ikiwemo za Mjini Magharibi na Kusini Unguja?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Amina Ali Mzee, Mbunge wa Viti Maalum Zanzibar, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Wakala wa Miundombinu ya Mawasiliano Zanzibar imefikisha huduma za Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano katika Mikoa na Wilaya zote za Zanzibar. Mjini Magharibi inapata huduma kupitia vituo vilivyopo maeneo ya Jamhuri Garden, Fumba na Ofisi za Miundombinu ya Mawasiliano Zanzibar (ZICTIA) na Kusini Unguja inapata huduma kupitia kituo kilichopo Paje.

Mheshimiwa Spika, hadi sasa jumla ya Wilaya 43 nchini zimefikiwa na Mkongo wa Mawasiliano wa Taifa. Kwa bajeti ya mwaka wa fedha 2021/2022 jumla ya Wilaya mpya 23 zitafikiwa na hivyo kuwa na jumla ya Wilaya 66 nchini zenye huduma ya Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano.

Mheshimiwa Spika, Serikali imepanga kuwa Wilaya zote nchini zitafikiwa na huduma za Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano ifikapo mwaka 2025. Mwaka wa fedha 2022/2023 Wilaya zingine mpya 15 zitafikiwa na hivyo kuwa na jumla ya Wilaya 81. Wilaya zinazobaki zitafikishiwa huduma za Mkongo wa Mawasiliano wa Taifa kwa kipindi kinachobaki kufikia 2025 kama ilivyopangwa. Ahsante.