Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Asia Abdulkarim Halamga (15 total)

Hotuba ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyoitoa wakati wa Ufunguzi wa Bunge la Kumi na Mbili, Tarehe 13 Novemba, 2020
MHE. ASIA A. HALAMGA: Mheshimiwa Spika, kwanza nichukue nafasi hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuniwezesha kufika katika Bunge lako hili tukufu. Nichukue nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzaia Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwa kupata kura za kutosha na za kihistoria ambazo toka tumeingia katika chaguzi za vyama vingi uchaguzi wa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli ameshinda kwa kishindi, ninampongeza sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nichukue nafasi hii pia kukishukuru Chama chetu Cha Mapinduzi pamoja na jumuiya zake zote kwa kazi kubwa na nzuri wanayoifanya wakati wote na hatimaye tumekwenda kwenye uchaguzi na Chama Cha Mapinduzi tukashinda kwa kishindo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini bila kusahau Jumuiya ya Umoja wa Vijana kwa kuhakikisha kuwa inalinda na kutetea itikadi ya Chama Cha Mapinduzi wakati wote.

Mheshimiwa Spika, nina mengi ya kuchangia lakini kulingana na dakika tano ninaomba niende kwa haraka. Niende kuwasemea vijana ambao wametoka juzi JKT. Vijana takribani 10,000 ambao wamepata mafunzo mbalimbali ya kijeshi na ya kuweza kuzalisha na kutengeneza uchumi katika Taifa letu. Vijana hawa wamekwenda kukaa kwa miaka mitatu Jeshini pamoja na kupata mafunzo, vijana hawa wamerudi mtaani hawana ajira na wote tunafahamu JKT haiwezi kuajiri vijana hawa wote.

Mheshimiwa Spika, niishauri Serikali kuona sasa ni namna gani tunaweza kuwasaidia vijana hawa wakawezeshwa. Mfano, tuna Kambi ya Makutupora ambayo inazalisha zabibu, tuone vijana hawa wanaotoka katika kambi hii na tayari wana mafunzo ya kutosha wanawezeshwa ili na wao waweze kulima zabibu kwa sababu wana ujuzi huo na ikiwezekana Makutupora ipokee zao hilo kutoka kwa vijana hawa na kuwezesha nchi yetu kufikia sasa kile kilimo ambacho ni nia na dhahiri ya Mheshimiwa Rais kupitia hotuba yake. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pamoja na hayo tunao mfano wa Kambi zingine, tuna kambi ya Kigoma kule ambayo inalima mchikichi, tuna kambi ya Ruvu. Wote hawa vijana wana mafunzo ya kutosha, tuone sasa Serikali kwa namna gani inawawezesha kiuchumi ili vijana hawa kwa miaka hiyo mitatu na sasa hivi wako mtaani, hawana mitaji hawajui pa kwenda, hawana chochote. Tunazalisha bomu lingine katika nchi yetu bila kujua utatuzi wa vijana hawa wanapotoka makambini wanakuja kufanya nini huku uraiani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunaishukuru Serikali kwa nia njema ya kuwasaidia vijana kwa kutoa mikopo kwa vijana, akina mama na watu wenye uhitaji maalum mikopo ya asilimia 10. Tuombe sasa Serikali ifike ichukue hatua ya kuona mbali zaidi kwa kuwakopesha vijana mmoja mmoja na ikiwezekana Serikali kupitia Halmashauri ijifunze namna gani Bodi ya Mikopo inavyoweza kuwakopesha vijana na kila mwaka kurudisha fedha hizo na basi vijana hawa mmoja mmoja waweze kuaminika na kukopeshwa na Serikali kwa kijana mmoja mmoja badala ya vijana kwa makundi. Ni kweli, njia ya vikundi ni njia sahihi lakini sio vijana wote wanaoweza kupitia makundi kwa sababu hawalingani mawazo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kusemea suala la mkopo Serikali yetu ya Chama Cha Mapinduzi kupitia Ilani yake, lakini pia hotuba ya Mheshimiwa Rais lengo ni jema, yote yaliyoandikwa kama dhamira hii tutaichukua, viongozi wa Serikali tukaenda kutekeleza na kusimamia…

(Hapa kengele ililia kuasiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. ASIA A. HALAMGA: Mheshimiwa Spika, ninaunga mkono hoja kwa asilimia zaidi ya 1,000. Ahsante sana kwa kunipa nafasi. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
MHE. ASIA A. HALAMGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi na mimi ya kuweza kuchangia kwa ufupi katika Bajeti ya Wizara ya Mambo ya Ndani kwa mwaka 2023/2024.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niungane na wote ambao wameweza kumpongeza Mheshimiwa Rais pamoja na Waziri, Naibu Waziri, Wizara nzima kwa ufanisi wao wa kazi na utendaji wao wa kazi. Nichukue nafasi hii kutoa pole sana kwa wananchi wa Endasak, Wilaya ya Hanang kwa kuunguliwa na soko usiku wa kuamkia juzi, lakini niendelee kuwapa pole kwa sababu wafanyabiashara wengi ni wa hali ya chini kabisa hususani akina mama ambao wameweza kupteza mitaji yao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi hii kumpongeza Mkuu wa Wilaya pamoja na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya lakini kubwa zaidi wananchi wa Endasak na wa Wilaya ya Hanang’ kwa kukabiliana na moto ule japo umeweza kuleta hasara lakini walihangaika usiku kucha na kufanikiwa kuuzima japo hawakuweza kufanikiwa kuokoa vitu. Adha hii ambayo imeweza kuwakuta wananchi hawa ni kwa sababu Mkoa wa Manyara kwanza kijiografia kutoka Wilaya na Wilaya, Wilaya iliyopo karibu ni kilometa 75, kwa hali ya kawaida Wilaya nyingi unatembea takribani kilometa zaidi ya 300 na hivyo kunapotokea janga na kwa sababu hatuna gari la zimamoto madhara yanakuwa ni makubwa zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo ninamuomba Mheshimiwa Waziri uzingatie jiografia ya Mkoa wa Manyara ukubwa wake na uzingatie sasa tuweze kupata gari kwa sababu hatuna gari la zimamoto, gari lililopo lipo Babati Mjini na hatuna visima maalum kwa ajili ya maji, pia hatuna mabomba maalum kwa ajili ya uzimaji wa moto. Kwa hiyo, tunakuomba sana unapokuja kuhitimisha hoja yako basi uhakikishe kwamba Mkoa wa Manyara tupate usafiri huo ili kuweza kukabiliana na majanga yanapotokea ndani ya Mkoa wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo nakushukuru kwa kunipa nafasi. (Makofi)
Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022
MHE. ASIA A. HALAMGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia katika Mpango huu wa Maendeleo wa mwaka 2021/2022.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa nachukua nafasi hii kuendelea kumpongeza Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwa kazi kubwa na nzuri ambazo anazifanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi hii pia kumpongeza Waziri wa Mipango pamoja na timu yake yote, bila kusahau Kamati ya Bajeti kwa hotuba yao nzuri waliyotuletea. Naomba nijikite kuchangia katika eneo la kilimo na hasa kilimo cha ngano. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Manyara kupitia Wilaya ya Hanang ni miongoni mwa sehemu inayolima ngano kwa asilimia kubwa. Nikichukua takwimu za Serikali ambazo zimetumia fedha ya kwenda kununua ngano katika msimu uliopita, Serikali ilitumia zaidi ya shilingi trilioni 1.3 kwa ajili ya kununua zao hili la ngano na kuliingiza nchini. Nitakuwa mchoyo wa fadhila kama sitaweza kuipongeza Wizara ya Kilimo kwa kuamua sasa Wilaya ya Hanang kuwa kitovu cha kilimo hiki cha ngano. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika kuhakikisha kwamba sasa zao hili na kilimo hiki katika Mkoa wa Manyara, hususan Wilaya ya Hanang, tunaomba sasa Serikali ichukue hatua ya kuleta mbegu kwa wakati na kwa haraka kama ambavyo imetufanyia kwa sasa kutuletea tani 22 kwa ajili ya mbegu. Naiomba sasa Serikali kupitia mnunuzi ambaye iliamua awe Bakhresa kuja kununua ngano hizi za wakulima zaidi ya tani
477.8 ili wakulima hao waweze kukidhi kilimo chao kwa wakati na tuweze kwenda sambamba na uchumi wa viwanda kupitia malighafi watakazozitengeneza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Hanang ina ekari zaidi ya 100,000 ya kilimo cha ngano. Pamoja na ekari hizi, ekari 40,000 ziko kwa mwekezaji anayeitwa Ngano Limited. Tunaomba sasa, kwa sababu Serikali imeamua Hanang iwe kitovu cha ukulima cha ngano ili kuweza kukidhi mahitaji ya ndani ya nchi, mwekezaji huyu wa Ngano Limited mikataba yake iweze kuangaliwa kwa sababu anamiliki ekari zaidi ya 40,000 lakini halimi kiwango hicho cha ekari 40,000 na ekari hizo zilikuwa ni pori.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wa Hanang wanatamani kweli kulima ngano ili kukidhi haja ya Serikali, lakini tunaiomba Serikali kupitia Wizara ya Kilimo, iweze kumsaidia mwekezaji huyu mkataba wake, kwa sababu eneo alilonalo ni kubwa na limekuwa ni pori. Kama tumeamua kweli kuwekeza katika ngano, basi ikiwezekana shamba hilo liletwe katika halmashauri, halmashauri ilimiliki kwa maana ya Serikali au wananchi waweze kugaiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwekezaji huyu anamiliki eneo la Gidamocha, Sechet pamoja na Murjanda. Wananchi wanapoingia kulima hata kidogo tu, mwekezaji huyu anakwenda kuweka mazao sumu, mazao ya wananchi yanakufa, lakini pia halimi eneo hili la ekari 40; na lengo la Serikali ni kuhakikisha tunafikia…

Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kukuza uchumi, naipongeza Wizara ya Habari, Sanaa na Utamaduni kwa kazi kubwa ambayo inafanya, lakini naomba sasa Wizara ifike mahali iweze kuwasaidia wasanii wetu. Kwa sababu ni ukweli usiopingika, wasanii wanaingiza mapato. Vijana pamoja na ninyi wazee humu ndani mnapenda burudani, basi ifike sasa, Wizara iweze kuona ni namna gani inaweza kuwasaidia vijana hawa ku-promote kazi zao na hasa kimataifa ili wasanii hawa waweze kukubalika Kimataifa kama ambavyo Nigeria na nchi nyingine zinavyofanya. Wasanii wetu wana uwezo mkubwa wa kuliingizia Taifa letu pato kubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Tanzania Mungu ametubariki sana…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. ASIA A. HALAMGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa ajili ya muda, ndiyo nilikuwa nimeanza. Naunga mkono hoja. Naendelea kumshukuru Mwenyekiti wetu na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa huruma ya Serikali na hata leo Serikali hii kwa huruma yake, ina hadi watu ambao walifukuzwa kwenye vyama vyao, lakini Serikali kwa sababu imezingatia maslahi ya Watanzania imeweza kuwaweka humu ndani ili kuendelea kuchukua michango yao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Nasema tena, naunga mkono hoja. (Makofi)
Azimio la Bunge la Kutambua na Kuenzi Mchango wa Rais wa Tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, kwa Utumishi wake Uliotukuka Pamoja na Azimio la Bunge la Kumpongeza Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
MHE. ASIA A. HALAMGA: Mheshimiwa Naibu Spika, asante sana. Kwanza nianze na kuunga mkono azimio hili, maazimio yote mawili.

Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwa kuenzi na kutambua mchango wa Rais wa Awamu ya Tano, Hayati Dokta John Pombe Magufuli. Kweli ni wingu la simanzi lililotawala anga ya nchi yetu kwa kupoteza jemadari wetu wa mapambano, baba yetu, mzalendo wa zama zetu, rafiki yetu na Rais wa Awamu ya Tano, Hayati Dkt. John Pombe Joseph Magufuli. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kukupa pole wewe na Watanzania wenzangu wote kwa msiba mzito uliolikuta Taifa letu kwa kumpoteza Rais wetu mpendwa Hayati Dkt. John Pombe Joseph Magufuli. Sisi vijana wa nchi hii tutamkumbuka Mheshimiwa Magufuli kwa kutuonesha njia sahihi ya kuipenda nchi yetu, kuilinda nchi yetu na kuwa majasiri katika kuitetea nchi yetu kwa gharama yoyote ile. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sisi vijana tutamuenzi Hayati Rais Magufuli kwenye vitu vikuu vitatu, miongoni mwa vitu vingi alivyoacha alama katika mioyo ya Watanzania, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, moja uzalendo. Hakuna kati yetu atakayepingana na ukweli kwamba, Hayati Rais Magufuli alikuwa mstari wa mbele pasipo kupepesa macho au pasipo kuwa na simile ya aina yoyote katika kuilinda na kuitetea nchi yetu dhidi ya adui yoyote wa nchi hii. Uhodari wake katika kulinda rasilimali za nchi hii, leo tuna ukuta wa Mererani, leo tuna Twiga Cooperation Limited na mengineyo mengi ikiwemo umahiri na uhodari wa utoaji huduma serikalini na zaidi kutetea dhana na kuaminisha kuwa nchi yetu ni nchi tajiri sana kupitia rasilimali zetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mbili, uongozi wenye maono (Visionary Leader). Hayati Rais Magufuli ametufunza kuwa viongozi kwa kuangalia kesho na kukubali kufanya kazi ya kutesema ili kesho ya nchi yetu iwe nzuri zaidi.

Mheshimiwa Naibu Spika, tutazame miradi mikakati aliyoiona na kuisisitiza na kutimiza kama Bwawa la Umeme la Mwalimu Nyerere, ili kuzalisha umeme kwetu wa kutosha na hatimaye tunavyokwenda kujenga uchumi wa viwanda basi suala la umeme lisiwe lenye kutatiza tena. Mradi wa reli ya umeme ambayo licha ya kuunganisha mikoa ya kati na bandari yetu tunaenda kuunganisha nchi jirani kwa kuleta tija kwenye kufungua fursa za biashara na kufanya bandari yetu kukua. Vilevile Tunalinda miundombinu ya barabara na zaidi kupunguza muda wa usafirishaji wa mizigo, gharama za usafirishaji na pia kwani usafiri wa reli ni wa gharama nafuu kuliko wowote duniani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tatu, mtaani kuna usemi tulikuwa tunataniwa sana na majirani zetu wa Afrika Mashariki kwa sera nzuri…

Mheshimiwa Naibu Spika, bado tuko katika siku 21 za maombolezo na ndiyo maana binafsi nimeamua kuandika kwa ajili ya kuendelea kuomboleza kifo cha Mheshimiwa Rais, lakini pia kwa ajili ya kumpongeza Mheshimiwa Rais Mama Samia Suluhu Hassan. Kwa hiyo, msinishangae kwa kusoma, kusoma nayo ni sehemu ya utaratibu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hakika hakuna kitabu kitakachotosha kuongelea umahiri na uhodari wa uongozi wa Rais Magufuli zaidi ya kwamba Hayati Dkt. Magufuli ameacha uongozi wenye alama wa vit una alama ndani ya mioyo ya Watanzania. Nilihakikishie Bunge hili na Watanzania wote kuna kina Magufuli wengi ambao wamezalishwa katika kipindi chake. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nifupishe kwa kusema, Raha ya Milele Umme Ee Bwana, na Mwamba wa Milele Umuangazie. Apumzike kwa amani, amina.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kutoa na kuunga mkono azimio la kwanza, sasa niende azimio la pili… (Kicheko)

(Hapa baadhi ya Wabunge walizungumza bila kufuata utaratibu)

MHE. ASIA A. HALAMGA:…la kumpongeza Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania...

…kuchekwa pia ni sehemu ya kuendelea mimi kuwa imara. Tuendelee kumpongeza Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, hakika sisi kama vijana tunajivunia. Kwanza hatuna hfunaye kwa kuwa tunachokipigania sasahivi kwa Watanzania ni maendeleo na maendeleo hayo hayatoki sehemu nyingine tofauti na kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi, ambayo mwaka 2020 Mheshimiwa Mama Samia alipita kuinadi, na hapa Bungeni ndicho tunachoendelea kukitimiza. Tuendelee kumpongeza mama yetu na tumhakikishie kama vijana humu ndani tutahakikisha yale yote yatakayoletwa na Wizara na Mawaziri na Serikali juu ya maendeleo ya Watanzania na hasa kwa kuzingatia ilani yetu tutaunga mkono kwa asilimia 100. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue nafasi hii kumpongeza Makamu wa Rais Mteule kwa kukalia kiti chake. Hivi karibuni tunaamini anakwenda kuapishwa. Sisi kama vijana hatuna hofu naye, tuna imaninaye kubwa kwa sababu, amehudumu katika Serikali ndani ya nchi na nje ya nchi. Hatuna hofu wala shaka na Dokta Mpango. Hakika tumepata Makamu wa Rais na sisi kama vijana tutahakikisha tunaunga mkono Serikali yetu na viongozi wetu ili kuendeleza amani, umoja na mshikamano wa Watanzania kwa maslahi mapana ya vijana sisi na vijana wajao.

Mheshimiwa Naibu Spika, nilitangulia kwa kusema kwamba, bado nipo kwenye simanzi japo tuna furaha ya kuwapata viongozi thabiti na madhubuti katika taifa letu. Naomba kwa siku ya leo niwe nimeishia hapo, asante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. ASIA A. HALAMGA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi nami kuweza kuchangia bajeti ya mwaka 2023/2024.

Kwanza nianze kutoa pongezi za dhati kwa Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama yetu Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kazi kubwa ambazo anazifanya za kimaendeleo katika nchi yetu, lakini katika kuhakiisha kwamba anaendelea kupambana bila kulala, bila kuchoka, kuhakikisha anaendelea kutatua changamoto kubwa ya ajira tuliyokuwanayo vijana wa Kitanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa kufanya hivyo, nichukue nafasi hii kumshukuru sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kutoa zaidi ya Shilingi bilioni 39.8 kwenye Kiwanda cha Mkulazi, Kiwanda cha Sukari Morogoro ambacho mpaka sasa hivi kimeshaajiri takribani zaidi ya vijana 154 wa Kitanzania wako kazini. Mpaka sasa hivi zaidi ya hekta 2,900 zimeshaweza kufanyiwa kazi. Tunatarajia ndani ya mwaka mmoja zaidi ya tani 50,000 zitaweza kuzalishwa na hivyo itakuza mnyororo wa thamani ya uchumi kwa maana ya kuanzia ndani ya nchi yetu kuondoa tatizo la sukari, lakini pia baada ya kukidhi soko la ndani tunaweza kupeleka na soko la nje na hivyo kuliongezea Taifa letu mapato.

Mheshimiwa Spika, niendelee kuchukua nafasi hii kumshukuru sana Mheshimiwa Rais pamoja na Wizara ya Kilimo kwa ubunifu wa skimu za umwagiliaji ambao tunaamini utaenda kutatua tatizo kubwa sana; kwanza la ajira; na pili, utaenda kukuza uchumi wa nchi yetu kwa sababu ni kilimo ambacho kitakuwa ni cha muda wote na kitaendeleza mnyororo wa thamani. Naishukuru sana Wizara ya Kilimo, lakini niiombe sasa, kwa jitihada hizo ambazo imeanza kuzifanya, basi ni vyema wakashirikiana na watu wa JKT kwa maana ya kuwatumia vijana walioko makambini kwa mfano, kambi yetu ya Makutupora, kwenye kilimo cha alizeti; Kambi ya Chita kwa maana ya kilimo cha mpunga na maeneo mengine kadha wa kadha. Kwa sababu tayari tuna nguvukazi ya Taifa hili ambayo ipo na yenye maadili makubwa na inaendelea kulitumikia Taifa letu.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, tunaweza tukawasaidia vijana hawa kupitia JKT ili kuendelea kuhakikisha nchi yetu ya Tanzania kupitia kilimo kama ambavyo Waziri ameweza kuweka mipango thabiti ya kilimo cha umwagiliaji, basi tunaunganisha nguvu ili kuweza kukidhi soko la ndani, lakini kuendelea kufanya mazingira rafiki kwa vijana wa Kitanzania kuona tija ya kilimo na baadaye kuweza kukopesheka ili wao wenyewe wawe ni sehemu ya mitaji na sehemu ya uzalishaji kwa maana ya wao binafsi, kwa kuwa tayari Wizara imeshaonesha wapi tunaelekea? Wapi tunakwenda? Kilimo Tanzania chenye tija kinawezekana. Hongera sana Mheshimiwa Rais, hongera sana Mheshimiwa Waziri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nichukue nafasi hii kuendelea kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kuhakikisha anaendelea kuwakwamua wananchi wake na hasa kupitia kilimo, na viwanda. Mheshimiwa Rais kupitia watu wa Poland waliweza kuingia makubaliano na Serikali ya Tanzania kupitia Shirika la Maendeleo la NDC na kuleta matrekta ndani ya nchi yetu ya Tanzania, matrekta yaliyoletwa na Kampuni ya Ursus ambayo yaliweza kukopeshwa kwa wakulima wetu hapa nchini kwa maeneo tofauti tofauti. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nitoe masikitoko yangu kwa niaba ya wananchi, wakulima ambao waliweza kupokea matrekta hayo. Matrekta hayo yalivyoingia ndani ya nchi yetu, kwanza wakulima ambao walikuwa na sifa hizo za kupokea walitakiwa waende kuchukua matrekta hayo kwa usafiri. Maana yake wasiyatembeze mpaka maeneo wanapofika, bali watafute fedha waende wakachukue matrekta hayo.

Mheshimiwa Spika, wananchi walikopa, waliuza vitu vyao, wakasafiri wakaenda kubeba matrekta hayo na kuyapeleka site. Wananchi wamefika na matrekta hayo, na kwenye mkataba walikubaliana miaka miwili wataendelea kupewa huduma ya vipuri, lakini matrekta hayo yamefika kwa wakulima, na ndani ya nchi hakuna vipuri. Mkataba umekiukwa kwa sababu hawakuletewa vipuri hivyo ndani ya nchi yetu. Nini ambacho kimetokea?

Mheshimiwa Spika, kilichotokea ni umasikini mkubwa kwa wakulima wetu ambao walikopa fedha zao, badala ya kuwekeza kwenye msimu ambao siku zote wamezoea kulima kwa kawaida, walijiwekeza wakaenda kuchukua matrekta hayo. Matrekta yamefika shambani, hayana vifaa, yameharibika. (Makofi)

MHE. TABASAM H. MWAGAO: Mheshimiwa Spika, taarifa.

SPIKA: Mheshimiwa Asia Halamga, kuna Taarifa ya kutoka kwa Mheshimiwa Tabasam Hamis Mwagao.

T A A R I F A

MHE. TABASAM H. MWAGAO: Mheshimiwa Spika, nataka kumpa taarifa msemaji wa taarifa hii ya haya matrekta ya Ursus. Matrekta haya yakiingia shambani linakatika vipande viwili. Hatujui aliyekwenda kuyanunua haya matrekta. Kwa hiyo, tunaomba iundwe Tume ya Bunge kwenda kuchunguza mradi huu wa haya matrekta kutia watu umasikini. Watanzania wakulima masikini wamekwenda kufilisika. Ahsante sana. (Makofi) [Maneno Haya Siyo Sehemu ya Taarifa Rasmi za Bunge]

SPIKA: Nachelea kumuuliza mchangiaji kwa sababu imetajwa hapo kampuni mahususi na tusije tukaingia kwenye mgogoro wa kibiashara hapo. Hoja ya Mheshimiwa Asia Halamga sikuiingilia kwa sababu inahusu vipuri vya hayo matrekta ambayo yametajwa jina, lakini sasa ule udhaifu wa hayo matrekta anaouonesha Mheshimiwa Tabasam, nisingependa Bunge lijielekeze huko kwa sababu, sina taarifa. Tusije tukaingia kwenye mgogoro wa kibiashara kwamba, mtu anaharibiwa biashara yake.

Kwa muktadha huo, Mheshimiwa Tabasam, hilo eneo la kuonesha udhaifu wa hayo matrekta kwa sababu ya hoja hiyo ya kibiashara isije ikatuletea changamoto hapa, maana mimi sina hiyo taarifa, inaondolewa kwenye Taarifa Rasmi za Bunge.

Mheshimiwa Asia Halamga, malizia mchango wako.

MHE. ASIA A. HALAMGA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naomba tu sasa kwa sababu watu hawana ufafanuzi mzuri juu ya matrekta haya, niendelee tu kuchangia kwa kusema kwamba matrekta haya wakulima wetu, kwanza wakati wanakwenda kuyachukua walitakiwa waingize fedha kwenye akaunti ya mtu binafsi ambaye alikuwa anasimamia. Wananchi wakaingiza fedha kwenye akaunti hiyo ya mtu binafsi, lakini matrekta nje ya mkataba ule ambao wamekubaliana kwamba walete vipuri na vipuri havikuja, wananchi sasa hivi wameanza kukamatwa.

Mheshimiwa Spika, mbaya zaidi, wananchi walianza kuitwa na watu wa TAKUKURU na walikuwa wanafanya bargaining. Baada ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu kupitia Ripoti ya CAG ambapo alipoongelea masuala ya TAKUKURU kutokuingilia masuala haya ya fine na kadhalika, wakaweza kusimama, lakini watu hawa NDC wakaamua kutumia watu wa Majembe Auction. Watu wa Majembe Auction wanakwenda kuwakamata wakulima na bahati mbaya sana wakiwapigia simu wanaanza ku-bargain nao kwamba umelipa lini?

Mheshimiwa Spika, sasa hivi wakulima wamepewa akaunti nyingine ambayo wanatakiwa walipie sasa rasmi hiyo fedha, lakini fedha ya mwanzo ambayo wameitoa na kuweza kupata matrekta kipindi cha mwanzo, fedha ile haitambuliki.

Mheshimiwa Spika, kama hiyo haitoshi, wananchi hawa wamekosa jukwaa, kwanza la shirika lenyewe kwa sababu wametafuta nafasi mra kwa mara waweze kuongea nao kwa sababu tayari wako nje na mkataba, hawajapata nafasi ya kukaa nao. Haitoshi, wananchi hawa ambao ni wakulima wameshakuja mara kadhaa Dodoma bila mafanikio ya kukutana na viongozi wa Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wananchi hawa wameandika barua hii hapa na ilikwenda kwa Wizara ya Viwanda na Biashara, wananchi hawa hawajaweza kupata majibu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mimi natokea Wilaya ya Hanang. Ukifika Wilaya ya Hanang unakutana na wamama ambao wamekimbiwa na waume zao kwa sababu wanaenda kukamatwa na Majembe Auction kule chini. Wamama hawa wameshindwa kuwapeleka watoto shule…

MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Spika, taarifa.

SPIKA: Nani amesimama kuhusu taarifa?

MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Spika, niko huku.

SPIKA: Aah, Mheshimiwa Flatei.

T A A R I F A

MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Spika, nataka nimpe Taarifa mzungumzaji. Pamoja na kutokuwa na vipuri ndani ya nchi, wanaenda kuchukua vipuri hivyo nje ya nchi. Pia Jimbo la Mbulu Vijijini kuna tatizo kama hilo hilo na taarifa hii ni ya kweli.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Huyo alikuwa anachangia, lakini muda wako umekwisha Mheshimiwa Asia Halamga; nakupa dakika moja umalizie hoja yako.

MHE. ASIA A. HALAMGA: Mheshimiwa Spika, nakuomba dada yangu uniongezee muda hata wa dakika mbili niweze kumalizia.

Mheshimiwa Spika, kwa sababu ya kumalizia na kwa sababu ya tija katika Taifa letu dhidi ya makampuni ambayo yanaweza kuleta vifaa ndani ya nchi yetu na kwenda kuwatia watu wetu umaskini na ambaye anapata doa siyo mtu wa nje, anayepata doa ni Serikali ya Tanzania wakati Mheshimiwa Rais ameamua kuwasaidia Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pendekezo langu la kwanza ninaiomba Serikali kwanza ikubali kukaa na hawa wakulima ili iweze kujua changamoto zao ni zipi ndani ya nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, suala la pili; ninaiomba Serikali iweze kuangalia kampuni hii kama ina tija au kama haina tija kwa sababu zoezi lenyewe lina tija kwa wakulima, ninaomba iwezekane kampuni ibadiliswe. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa kumalizia; suala la ushoga. Niombe, wasanii wetu ndani ya Nchi yetu ya Tanzania na kupitia BASATA. BASATA wimbo ukiingia doa kidogo la kama tusi au maadili hapohapo wanafungia wimbo, watoto wa kike wakivaa vimina hapohapo wanafungiwa wimbo.

Mheshimiwa Spika, lakini kuna tija gani ya watoto wetu wa kiume kuvaa mawigi, maziwa au makalio ili kuonesha sanaa? Kwani hakuna njia nyingine ya wasanii wa kiume wa Tanzania kuweza kupeleka ujumbe bila kuvaa mavazi ya kike? Wanavaa mawigi, wanapaka poda, wanapaka wanja; wanafundisha nini wakati wao ni kioo cha jamii kwa watoto ambao wanachipukia? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi, ninaunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Madini
MHE. ASIA A. HALAMGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kuweza kunipa nafasi nami ya kupata kuchangia katika bajeti ya Wizara ya Madini 2023/2024.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nichukue nafasi hii kumshukuru sana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama yetu Samia Suluhu Hassan, kwa namna ambavyo anaendelea kutengeneza mazingira bora ya wawekezaji, lakini na wawekezaji wa ndani na kuendelea kuangalia Wizara ya Madini kama sehemu ya kuongeza kipato ndani ya Taifa letu. Vile vile bila kusahau niendelee kupongeza kazi kubwa ambayo inafanywa na Waziri, Mheshimiwa Dotto Mashaka Biteko pamoja na Naibu wake na timu nzima ya Wizara. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nianze kwa kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, sisi watu wa Manyara tunasema tunamwombea kwa Mungu afya njema lakini kura tulishamaliza kupiga, tunasubiri sanduku tuletewe ili tuweze kuzidumbukiza na ni kura za ndio. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tulifanya hivyo kwa sababu, tunamshukuru alituletea zaidi ya Shilingi Bilioni 5.9 kujenga one stop center ya ununuzi wa madini katika Mji wa Mererani. Vile vile, tunaishukuru Serikali ya Awamu ya Sita kupitia kwa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, mpaka sasa tayari tumeshapokea kiasi cha fedha cha Shilingi Bilioni 1.59 ambao ujenzi umeshaanza ghorofa la kisasa la soko liliwekwa pale katika Mji wa Mererani na sisi tumepata sehemu ya kuwa tunakwenda kupigia picha kwa sababu ni kazi nzuri ambayo imefanywa na Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mpaka sasa hivi floor hizo nne tayari Serikali ya Mkoa imeshaanza kupata maombi ya wafanyabiashara, yaani jengo halijakamilika lakini wafanyabiashara tayari wamekuja wanahitaji kupangisha. Hakika hongera sana kwa Wizara ya Madini, ahsante sana Rais Samia Suluhu Hassan. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kupongeza jitihada zizo, tuendelee kumshukuru kwa namna ya kipekee, Watanzania wote kwa ujumla kwa sababu wanaochimba Mererani ni Watanzania kutoka pande zote za nchi yetu. Tuna kila sababu ya kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuweza kuruhusu Kitalu C ambacho kilifungwa zaidi ya miaka minne huko nyuma na sasa vijana zaidi ya 100 wameshapata ajira na ajira zinaendelea kutoka, lakini pia kipato kinaendelea kuongezeka kwa wananchi mmoja mmoja, kwa wachimbaji, lakini pia pato kubwa kwa Serikali. Ahsante sana Rais Samia Suluhu Hassan. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuishukuru Serikali yetu Tukufu ya Chama cha Mapinduzi, niombe Serikali mambo yafuatayo katika Mji wa Merelani kwa maana ya machimbo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba sana, Mji wa Mererani ili kupata madini yale kupasua miamba kunatumia baruti na vumbi ni kubwa na wananchi wetu wanapata ugonjwa wa TB. Katika Mji wa Merelani TB ni kubwa sana na ukiangalia kwenye takwimu mara ya mwisho mwezi wa Nane mwaka 2022, watu waliojitokeza kupima ni watu 2,024, lakini watu waliokutwa na maambukizi kwa wale ambao walipima kwa hiari ni watu 382 na ambao wanapata dawa mpaka sasa ni watu 371.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi letu kwa Serikali, kwanza kabisa tunaomba wachimbaji hao wadogo matibabu yao na hasa vumbi hili na athari ya ugonjwa wa TB, matibabu wanaenda kupata katika Mkoa wa Kilimanjaro Hospitali ya Kibong’oto. Mheshimiwa Waziri tunalo eneo kubwa linaloweza kujengwa hospitali na kuweza kuwasaidia idadi kubwa ya wananchi walioko Mererani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia shift moja wanapoingia kufanya kazi kwenye ile migodi ni zaidi ya wananchi 2,000 mpaka 3,000 na idadi kubwa ni kundi la vijana. Kwa hiyo, ili tuweze kulinda rasilimali na nguvu kazi ya vijana wa Kitanzania, basi tuweze kupeleka huduma ya afya katika Mji wa Mererani kwa sababu ni idadi kubwa ya vijana wa Kitanzania wanafanya kazi pale.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo Mheshimiwa Rais nia yake ni njema, dhamira yake ni njema na lengo ni jema. Sambamba na kujengwa Mji wa One Stop Centre pale Mererani, tumuombe sasa Wizara ya Maji iende sambamba na ujenzi huu ili kukuza, kwa sababu mji ule sasa hivi una watu wengi, una wakazi wengi ambao ni Watanzania kutoka maeneo yote, lakini changamoto ya maji ni kubwa. Tuendelee kuomba japo tunamshukuru Mheshimiwa Waziri wa Maji anaendelea kupambana, lakini bado tuombe speed iongezeke ili kuweza kutatua changamoto hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo tunaomba ujenzi wa barabra. Barabara zilizopo ni mbovu, zimekuwa ni shida. kwa hiyo, tunaomba sana Wizara nyingine ziende sambamba na lengo la Mheshimiwa Rais la kuhakikisha One Stop Center hiyo inakuwa ni ya kisasa na Mji wa Mererani unafanana na kile ambacho kinatoka katika pato la Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuiombe GST iweze kuja kuendelea kufanya utafiti, lakini pia kuleta vifaa. Ndani ya Mkoa wa Manyara hatutegemei tu madini ya tanzanite, yapo madini mengi mfano kule Simanjiro kuna green garnet lakini changamoto iliyopo ni umeme, barabara pamoja na maji. Kwa hiyo, tukipata umeme itasaidia sana wananchi wadogo wadogo kutokutumia gharama za kutumia jenereta na kununua diesel. Kwa hiyo, tunaomba sana ili kuendelea kukuza pato la wananchi na pato la Taifa, basi miundombinu kama umeme, maji yaweze kupelekwa pamoja na barabara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, yapo madini mengine ya dhahabu kule Mbulu ambapo mashapo yapo ya kutosha, lakini wananchi hawa wa kawaida wadogo wadogo hawana sehemu rasmi ambapo wanaweza wakatoboa wakajua mwamba upo hapa. Kwa hiyo, tuiombe sana GST iweze kuja kufanya kazi ili kuwarahisishia wananchi wetu wadogo wadogo wafanye kazi si kwa muda mrefu, lakini kazi yenye faida na kulinda uchumi wao mdogo na mtaji wao mdogo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, yapo madini Kiteto, Mkoa wa Manyara karibu maeneo yote yana madini, lakini kwa namna ya kipekee niongelee Wilaya ninayotoka Wilaya ya Hanang. Hanang ukienda Gehandu, ukienda Mogitu, ukienda Gendabi, tuna madini ya chumvi wanakuja watu kutoka nchi zingine wananufaika, tunakuomba sana Mheshimiwa Waziri tunaomba mtoe support kwa wawekezaji wetu wadogowadogo wa ndani ili waweze kukuza uchumi na waweze kuvuna rasilimali hii kubwa katika nchi yetu na iweze kuleta mapato. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunao uwezo wa kuchimba simenti kule badala ya kuendelea kutumia simenti kwa kununua kwa bei ghali, tunaweza kuwaleta watu kule na wakaweza kutusaidia. Hali kadhalika ipo chumvi ya kutosha tunaomba sana Serikali yetu sikivu ituletee wawekezaji ili na sisi siku moja wananchi wa Hanang waweze kuona kuna kiwanda kiko kule na waweze kupata ajira na kusaidia wananchi wa chini na kusaidia pato la Taifa la nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba sana kwa heshima na taadhima Wizara ya Kazi, mwanzoni kulikuwa kuna kampuni ya Tanzanite ambayo ilikuwa na wafanyakazi wengi sana na kamapuni hiyo ilikuwa ina muunganiko na STAMICO lakini baada ya kampuni hiyo kuondoka ama kuacha kufanya kazi ya uchimbaji, zaidi ya Watanzania wafanyakazi 540 wanadai zaidi ya Bilioni 2.5 tunaiomba sana Wizara ya Kazi iendelee kuwasikiliza wananchi hawa itatue kero, maana imekuwa ni kero kwa viongozi wetu wa Chama cha Mapinduzi wanapokuja Mkoani wananchi hawa ndio wamekuwa ni kimbilio lakini tunaiomba sana Serikali kupitia Wizara ya Kazi iweze kuliangalia jambo hili na wananchi wale wajivunie kufanya kazi ndani ya nchi yao ya Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kumalizia mabadiliko ya Sheria ya Muundo wa Utumishi, tuombe sana Mheshimiwa Waziri mabadiliko haya hebu yamalizike mchakato wake ili kuweza kuwasaidia watumishi wako wa Wizara kuweza kupata kipato wanachostahili, kwa sababu kazi wanayoifanya ni kubwa wanaletea nchi yetu kipato kikubwa, lakini maslahi yao ukienda kuangalia watumishi hawa hakika hayastahili na tunahitaji kupata watu ambao watazidi kuwa waaminifu, kuwa wazalendo japo sasa hatuna shaka na uadilifu wao na uzalendo wao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa heshima na unyenyekevu mkubwa mimi binafsi na ninaamini na Watanzania wote na hasa Wabunge tuliomo huku ndani, ni nani kama Samia Suluhu Hassan, ni nani kama Samia Suluhu Hassan? Nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuweza kuchangia tunampongeza sana mama yetu kipenzi Rais Samia, Watanzania tumemuelewa Serikali ya Awamu ya Sita inafanya kazi, tunayaona wananchi huko chini, mimi kama kijana na vijana wenzangu tutasema mema yanayofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mama yetu Samia Suluhu Hassan. Ahsante sana Serikali ya Awamu ya Sita, ahsante sana Serikali ya Chama cha Mapinduzi. Ahsante kwa kunipa nafasi. (Makofi)
Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2021/2022 – 2025/2026
MHE. ASIA A. HALAMGA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi niweze kuchangia Mpango huu wa Tatu wa Maendeleo.

Mheshimiwa Spika, nianze kwa kumpongeza Waziri kwa uwasilishaji mzuri. Baada ya kumpongeza niombe nijikite katika sehemu mbili, moja ikiwa sehemu ya viwanda na ya pili ikiwa sehemu ya miundombinu.

Mheshimiwa Spika, naomba nianze na miundombinu. Awamu ya Nne ya Serikali yetu iliyopita ilifanikiwa sana katika kuhakikisha kwamba inaunganisha barabara katika kila mkoa ili kuhakikisha kwamba huduma za maendeleo zinapatikana kwa wananchi, lakini pia kupunguza gharama za maisha kwa wananchi wetu.

Mheshimiwa Spika, Serikali ile ya Awamu ya Nne iliamua kujiwekeza katika chombo kinachoitwa TANROADS. Katika kujielekeza katika chombo cha TANROADS tuliweza kufanikiwa kuunganisha mikoa mingi, na wote ni mashahidi, mikoa mingi sasa inafikika kwa kiwango cha lami.

Mheshimiwa Spika, ili kukuza uchumi wetu ni lazima sasa Serikali ione kwa namna gani ambavyo TANROADS wanapata asilimia 70 ya fedha lakini tuna chombo kingine ambacho tumeamua sasa kuboresha kwa maana ya barabara za vijijini, chombo kinachoitwa TARURA.

Mheshimiwa Spika, na tukiweza kufanikiwa kuiboresha TARURA tutafanikiwa kufungua barabara zetu za vijijini na tutarahisisha huduma. Huduma ya kwanza tutakayoweza kurahisisha ni huduma ya pembejeo na kuwasaidia wakulima wetu kwasababu tunalenga uchumi wa kilimo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tuombe sasa kwa kuwa TANROADS sasa hivi wamebaki kuunganisha maeneo machache lakini pia maeneo yao makubwa ni kuangalia marekebisho pale ambapo panaharibika. Kwa maana hiyo kazi kubwa TANROADS imeshaifanya. Basi tuombe sasa Serikali iamue kuwekeza nguvu katika chombo chetu cha TARURA na kuongezewa fedha ili tuweze kufanikiwa kuleta maendeleo kwa Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kuchangia hapo kwenye chombo cha TARURA kuongezewa fedha ili kuweza kukuza uchumi, niombe sasa nijielekeze katika kilimo cha alizeti, hasa kwa upande wa Kanda ya Kati. Serikali ilikuja na mpango mzuri na maono bora ya kuhakikisha kwamba kunaanzishwa kwa viwanda mbalimbali kulingana na jiografia ya maeneo yetu.

Mheshimiwa Spika, kuna zao la alizeti ambalo kwa kiasi kikubwa linalimwa katika Ukanda huu wa Kati. Tuombe sasa kuanzishwa kwa kiwanda kikubwa cha mafuta ya alizeti ili kukuza zao la alizeti katika kanda hii ya kati. Na namna ya kuanzishwa kwa kiwanda hicho kikubwa maana yake ni kwamba kitabeba viwanda vidogovidogo, kitarahisisha wakulima kuongeza bidhaa na kuwa na soko la ndani la uhakika kwa maana tutakuwa tuna kiwanda kikubwa lakini kile kiwanda kikubwa kitakuwa kimebeba nembo ya Tanzania, ambapo baada ya kupata soko la ndani la uhakika tutatoka kwenye soko la nje, litakalokuwa limebeba brand ya Tanzania na kuhakikisha kwamba tunapata soko la uhakika la huko duniani huku ndani tukiwa tumeshakidhi vigezo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika kuhakikisha kwamba zao hilohilo la alizeti pamoja na kuanzishwa kwa kiwanda kikubwa kitakachowasaidia wakulima wetu wa wafanyabiashara, tuhakikishe pia tunatoa mbegu iliyo bora kwa muda na wakati kwa wakulima wetu ili kuweza kufanikisha dhana tuliyoamini, dhana ya viwanda.

Mheshimiwa Spika, naomba nimalizie kwa Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Ajira na Vijana. Tunao vijana wenzetu kwenye makampuni na mashirika mbalimbali ambao wameweza kupata ajira zinazoweza kuwasaidia.

Mheshimiwa Spika, lakini tunaomba Wizara iende ikaangalie, vijana wengi wanafanya kazi lakini hakuna mikataba inayowalinda. Hivyo, tukiweza kusaidia vijana wakapewa mikataba na ajira za kudumu ama mikataba inayoeleweka, itaongeza mapato kwasababu wataweza kupata sehemu ya kulipa kodi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa siku ya leo mchango wangu ulikuwa ni huo, naomba nikushukuru kwa kunipa nafasi. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa
MHE. ASIA A. HALAMGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia katika Wizara hii muhimu sana ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa kwa nchi yetu. (Makofi)

Kwanza niendelee kuwapongeza kwa sababu wao wamekuwa ni sehemu kubwa ya maandalizi ya vijana weledi na wenye uzalendo katika Taifa letu.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba nianze kwa kutumia Randama ya bajeti yao ambayo imegusia mfano wa kilimo cha mpunga kule Chita mkoani Morogoro. Kilimo hicho cha mpunga ambacho kinafanywa na wenzetu wa JKT wameweza kutumia mwaka 2019/2020 katika bajeti, wametumia fedha shilingi milioni 775 katika kulima kilimo cha mpunga. Lakini matarajio yao watakapouza wanatarajia kuuza kwa shilingi milioni 778. Na ukienda kuangalia faida watakayokuwa wamepata watakuwa wamepata milioni 22 kwa hali ya kawaida ni hasara.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo nini mchango wangu; mchango wangu; kwa kutambua kazi kubwa inayofanywa na JKT na hasa vijana wanapopelekwa makambini na kutumia muda mrefu kukaa kambini na baadaye kurudi mitaani, bado kulalamika tatizo la ajira. Mchango wangu ninaiomba Wizara ya Kilimo iweze kushirikiana na JKT kwa maana ya kutoa mbegu pamoja na pembejeo za kilimo ili kuweza kufikia uchumi wa viwanda ule ambao tuanutarajia kwa sababu tayari tuna watu wa uhakika wa uzalishaji katika nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini niombe pia kutumia Wizara ya Elimu, kwa maana ya kupeleka mafunzo yanayotolewa SIDO pamoja na VETA ili tuweze kuwaandaa vijana hawa katika ujasiriamali wa kilimo na waweze wao wenyewe kutengeneza viwanda ili wanapotoka huku nje sasa waweze kujiajiri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, halikadhalika ninaiomba Wizara ya Viwanda na Biashara kuweza kuingia na kuungana na JKT kwa maana ya haya mazao ambayo tunayaandaa na kuyalima Wizara ya Viwanda ikiangalia hapa Chita tayari wanaenda kupata hasara kwa sababu kwanza hawajapata soko la uhakika. Lakini kama Wizara ya Viwanda na Biashara ikiwatengenezea soko la uhakika watu wa JKT kwa namna ambavyo wanazalisha tutakuwa na uhakika wa moja kwa moja viwanda vyetu kuwa na nafaka na rasilimali ya kutosha na hatimaye kukidhi soko la ndani na baadaye kwenda kwenye soko la nje. Lakini hapa kwenye soko la nje bado nitaiomba Wizara ya Mambo ya Nje kuendelea kutafuta masoko ya uhakika ili baadaye tuweze kupata fedha za kigeni na hii itatusababishia baada ya vijana hawa kumaliza mafunzo yao kambini basi wasitegemee ajira ya moja ya moja kwenda Jeshi la Wananchi bali tuwe tumezalisha vijana ambao wao wenyewe wakitoka nje watakuwa ni wazalishaji na tunaposema uchumi wa viwanda basi tayari tutakuwa na watu wa uhakika lakini pia tunatengeneza walipa kodi wa baadaye ambao ni wazalendo na wenye tija katika nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, bila kusahau katika Wizara hizo, Wizara ya TAMISEMI pamoja na Ofisi ya Waziri Mkuu kupitia mifuko ya uwezeshaji kijamii ili tunapokuwa tumewaandaa vijana hawa na wameanza kushirikiana na Wizara hizi vijana hawa watapata mikopo ya moja kwa moja. Kwa hiyo, tutakuwa tumewatengeneza watu ambao wakitoka baada ya mafunzo yao miaka mitatu kumaliza Jeshini, basi tunakwenda kuwapa vijana ajira ya moja kwa moja bila kutegemea kuajiriwa tu Jeshini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tukifanya hivyo hakika suluhisho la ajira litakuwa limepatikana kwa vijana wengi katika nchi yet una hasa vijana wa kizalendo ambao wanatengenezwa na JKT. JKT inafanya kazi kubwa na nzuri sana ya kuwatengeneza vijana lakini bado tunawapa mzigo wa lawama. Wizara hizi zote zikiweza kushirikiana, ni uhakika kwamba Jeshi letu litakuwa linatengeneza vijana wenye tija na hakutakuwa na malalamiko bali tutakuwa na wafanyabiashara na wazalishaji wakubwa wa ndani na nje ya nchi kwa maana ya masoko. Tutakuwa na masoko ya uhakika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niendelee hapo hapo kwa kutolea mfano. Tunayo Kambi ya Makutupora, hali kadhalika makambi haya yanapoanzishwa yanakuwa ni kwa ajili ya operesheni maalum. Sasa kambi ya Makutupora yenyewe ni kwa ajili ya kilimo cha zabibu na alizeti. Serikali ikiamua kuwekeza vizuri katika kilimo na hasa vijana hawa wanapoingia huko ndani na wanakuwa na tija, tukiwawezesha ni dhahiri kwamba baada ya muda mfupi hatutakuwa na changamoto ya kupata hata mafuta ndani ya nchi. Tutakuwa na uhakika wa kuzalisha mafuta ndani ya nchi lakini pia kukidhi soko la ndani na hatimaye kwenda kwenye soko la nje. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kuyachangia hayo, niendelee kushukuru na sasa niende kwenye maombi; ninaiomba Wizara hii, vijana wanapoingia kambini kuna posho ambayo wanapewa kila mwezi. Posho ile ilipangwa kwa muda mrefu. Kulingana na gharama na mahitaji ya sasa hivi, fedha zile kwa sasa haziwatoshi wale vijana kule makambini. Kwa hiyo, tunaomba Wizara ilibebe hili na ichukue iweze kuongeza fedha za kujikimu ili walau hata wanapotoka waweze kubana fedha na hatimaye wakitoka nje wawe wamejiwekea mtaji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue tena nafasi hii kuendelea kuiomba Wizara, vijana hawa wanapomaliza mafunzo, wanapata nafasi mbalimbali za kwenda kuajiriwa na makampuni binafsi, lakini wanapoajiriwa na makampuni binafsi, vijana hawa hawapewi mikataba. Sasa tuombe Wizara isaidie, ni kweli, vijana hawa wanasaidia na kampuni binafsi kupata ajira, lakini ajira hizo zinakuwa hazina uhakika kwa kuwa hawana mkataba wa kudumu ambao unaweza kuwasababishia wao kwanza kujiamini kazini kwamba ajira moja kwa moja, lakini pia wakishakuwa na mkataba watatusaidia hata kuingiza mapato Serikalini kwa sababu tutakuwa walipa kodi wa uhakika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunayo majeshi yetu ambayo kwa muda fulani huwa yanafanya kazi maalum. Mfano, kule Mererani, pale tunavyo vyombo mbalimbali vya ulinzi na usalama na wanapata posho fulani hivi ya kujikimu, lakini kwa wenzetu Jeshi la Polisi wapo eneo moja. Naomba nsivitaje vyombo kwa majina, lakini vyombo vya ulinzi na usalama vinavyolinda katika eneo la Mererani vinapata posho, lakini Jeshi la Polisi askari polisi walioko pale hawapati posho.

Naiomba Serikali ilione basi kwa kuwa hawa wote ni vyombo vya ulinzi na usalama basi wote waweze kupewa posho ya kuweza kujikimu ili wasipate tamaa ya wao kuona ni sehemu hata ya kutorosha hiyo mizigo inapokuwa hapo bali na wao wajisikie ni sehemu ya Jeshi, sehemu ya ulinzi, wote wawe na furaha kuliko hawa wanapewa, hawa hawapewi. Na hii iwe sio tu kwa Mererani, kwa maeneo yote ambapo kuna kazi maalum na vyombo vya ulinzi fulani vinapata posho na vyote viko pamoja basi wote waweze kupewa posho hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho kwa kumalizia, ninaomba bima za wanajeshi na familia zao; wameshatoa fedha lakini bado hawajapatiwa bima zao za afya, Waziri naomba uliangalie hili wapatiwe bima zao kwa wakati. Lakini pia katika bajeti hakujatengwa hela ya tafiti. Tuombe sasa ili Jeshi letu liweze kufanikiwa zaidi tunahitaji fedha ya tafiti. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi na kuniachia dakika. Shsante sana na naunga mkono hoja. (Makofi)
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo kwa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024
MHE. ASIA A. HALAMGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ili kuweza kuchangia katika Mpango wa Bajeti wa Mwaka 2023/2024. Nitaanza kuchangia katika Sekta ya Maliasili na Utalii. Sekta hii ndani ya Taifa letu inachangia pato la Taifa kwa asilimia 17.6, pia inachangia fedha za kigeni kwa asilimia 28. Sekta hii inafanya vizuri sana na tunaona kabisa katika pato la Taifa ni sekta muhimu kwa Taifa letu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina mapendekezo yafuatayo katika sekta hii ya Maliasili na Utalii. Kwenye bajeti iliyopita tuliamua kwamba ndege zetu tuongeze VAT, kwenye hili naomba tulipitie upya kwa sababu ukizingatia Sekta ya Maliasili na Utalii ilikumbwa na janga la Covid 19 na iliweza kuathiri kidogo uchumi na hasa ukiangalia mataifa ya jirani kupitia ndege hizi za kukodi kuna kitu cha kujifunza kupitia tozo hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kuendelea kutatua migogoro kati ya wananchi na hifadhi, lakini mapori yetu tengefu, tutakuwa tumefanya jambo kubwa sana, kuondoa migogoro ili kuhakikisha kwamba hifadhi hizi zinaendelea kufanya vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niipongeze Serikali kwa kuweza kuanzisha na kuipa TANAPA, kutoka hifadhi 16 hadi kufikia hifadhi 22 na Hifadhi hizo zikiwa Nyerere, Burigi, Ibanda, Kyerwa, Rumanyika, Kigosi na Mto Ugala. Wote sisi ni mashihidi kazi kubwa ambayo ameifanya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama yetu Samia Suluhu Hassan kwa kutangaza filamu ya Royal Tour na wote ni mashuhuda wakubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo ukifika Mkoa wa Kilimanjaro, Arusha, Manyara, kanda zote ambazo zina utalii tunashuhudia kabisa hoteli zimejaa, ziko booked, zingine mpaka mwakani. Kwenye hizi hifadhi mpya ambazo tumeziongeza tukiweza kuweka malango kila hifadhi, ili tukatangaze utalii, sio tu kwa kanda ya kaskazini, tukaongeza na kanda zingine ili kupitia filamu hii ya Mheshimiwa Rais, ambayo imeonesha tija kwa muda mfupi na maeneo mengine yakiweza kupandishwa utalii wao, basi tutapandisha mapato katika nchi yetu na hasa kwa kupata fedha za kigeni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi karibuni kupitia fedha za UVIKO, Wizara ya Maliasili na Utalii wameweza kupata vifaa mbalimbali, mfano, Miradi ya REGROW, wameweza kupata vifaa vya kuweza kutengeneza barabara na leo watu wanaopita barabara ya Arusha kwenda Serengeti ni mashihidi wakubwa namna ambavyo barabara zimenyooka na zinaweza kufikika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya mradi huo kukamilika, Miradi ya REGROW, tunaomba bajeti iangalie vizuri sekta hii ili miradi hiyo basi tutakapokuwa tumebaki nayo sisi, iweze kuwa na tija na tuweze kuiendesha. Sio tu mradi unapokamilika tushindwe kuuendesha na hasa tukizingatia tija ambayo imeonesha kwa muda huu mfupi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, bado tuna kazi hifadhi yetu ya Nyerere kule tumeweza kuianzisha, askari kule wako zaidi ya 120, lakini nyumba zao ziko 30. Tuna kitu cha kufanya ili kuendelea kuhakikisha kwamba sekta hii tunaisimamia vizuri na inaendelea kuleta tija kwa Taifa letu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuchangia hayo katika Maliasili, naomba niende Wizara ya Kilimo. Katika Ilani yetu ya Uchaguzi ya Mwaka 2020 - 2025, tunaona katika ukurasa wa 42(4) imeongelea suala kubwa la kusaidia nchi yetu katika suala la kilimo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika ilani imeongelea kutoka tani 63,000 hadi kufika 2025 tunatarajia kuwa na tani zaidi ya 200,000 za zao la ngano. Zao la Ngano kwa sasa ndani ya nchi yetu tunatumia fedha kubwa za kigeni kuagiza zao hili nje ya nchi na hasa Nchi ya Ukraine. Bahati mbaya sana wote tunajua hali halisi ya Ukraine kwa sasa, najaribu kujiuliza na kutafakari, je, vita ikizidi kuendelea Ukraine sisi tutakuwa na hali gani, ilihali tuna mashamba makubwa katika nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikitolea mfano wa shamba la NAFCO lililopo Wilaya ya Hanang ambayo lipo chini ya Mwekezaji anayeitwa Ngano Limited. Nimemfuata kaka yangu Bashe sio chini mara moja wala mara mbili, mtu huyu ana hekari takribani 40,000 ambazo hazina tija kwetu sisi Watanzania kwa sababu hakuna anachokizalisha. Inasadikika wamemwongezea tena hekari 10,000, tuna kila sababu ya kuiangalia eneo hili kwa jicho la pili ili tuweze kusaidia nchi yetu katika kukuza ngano na hasa tukizingatia Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi ya 2020.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mtu yule pamoja na kumpa hekari 40,000 pamoja na kutokuzalisha kwake, bado anaendelea kuvamia maeneo ya wananchi wadogo wadogo na anaendelea kusababisha migogoro, kati ya Serikali na wananchi, huku tukizingatia hana chochote ambacho anaingiza kwenye nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, yapo mashamba makubwa mengi katika nchi yetu KTPL yako kule Morogoro, yapo mashamba saba ya maua na mbogamboga kule Arusha, yako mashamba makubwa Songea ya NAFCO. Mashamba haya yana tija gani kwa Taifa letu. Nashauri mashamba haya makubwa yaondolewe chini ya Wizara ya Fedha na yaweze kukabidhiwa Wizara ya Kilimo na iweze kuyasimamia mashamba haya ili tuone tija kwa Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, yapo mashamba makubwa wenzetu wanajeshi wanalima kilimo, lakini miundombinu hatuwawezeshi tunaendelea kutengeneza malalamiko, migogoro na kuona wenzetu hawafanyi kazi ambayo inayostahili. Tunaomba mashamba yote makubwa kwenye nchi hii tuweze kuwakabidhi Wizara ya Kilimo na waje na majibu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano leo, JKT vijana wanafundishwa silaha, wanafundishwa kufanya kazi, wanafundishwa kilimo. Tuna mashamba makubwa katika Taifa letu, lakini tujiulize leo tunanunua ngano Ukraine, leo tunanunua alizeti nje ya nchi na bado vijana hawa hawana ajira. Serikali imejipangaje kutumia nguvu kazi ya vijana katika kuleta uchumi katika nchi yetu na hasa rasilimali tuliyokuwa nayo, rasilimali ya ardhi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niendelee kusisitiza mwekezaji anaitwa Ngano Limited katika Wilaya ya Hanang, naomba mkataba ukapitiwe upya, hana manufaa yoyote katika Taifa letu kwa sababu hana anachokizalisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa siku ya leo, mchango wangu unaishia hapa. Nakushukuru kwa kunipa nafasi. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Madini
MHE. ASIA A. HALAMGA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuweza kuchangia katika Wizara ya Madini.

Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa nianze kwa kumpongeza Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa na nzuri ambazo anazifanya katika nchi yetu. Nimpongeze Mheshimiwa Waziri Doto Biteko na timu nzima ya Wizara ya Madini kwa namna ambavyo tunaona wanavyochapa kazi na kuhakikisha kwamba rasilimali hii muhimu katika Taifa inaendelea kuwa ni chanzo cha mapato kwa Taifa letu.

Mheshimiwa Spika, nichukue nafasi hii kumpongeza ndugu Fabian Mshai RMO wa Mererani pamoja na timu nzima ya watumishi Mererani. Pia niishukuru na kuipongeza Serikali kwa kuamua sasa soko la Tanzanite litoke Arusha na kuletwa Mererani wilaya ya Simanjiro katika mkoa wa Manyara. Vilevile nimpongeze Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa kuja kulizindua soko la madini katika mji wa Mererani Simanjiro ndani ya mkoa wa Manyara.

Mheshimiwa Spika, pamoja na pongezi za kumpongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa kuja kufungua soko hilo niendelee kumshukuru na kumpongeza kwa uzalendo wake Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan katika kutengeneza filamu ya Royal Tour ambayo moja ya maeneo ambayo yalitumika ni pamoja na mji wa Mererani katika machimbo yanayochimbwa Tanzanite tunamshukuru kwa uzalendo wake kwa kutangaza tanzanite ulimwenguni kote kwa sababu wapo watu waliokuwa wakipotosha tanzanite haitoki Tanzania, tanzanite haitoki Manyara.

Mheshimiwa Spika, tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kulinda urithi wetu, wa nchi yetu ya Tanzania kwa kuitangazia dunia tanzanite ni ya Tanzania tanzanite inatoka Manyara, tanzanite inatoka Mererani.

Mheshimiwa Spika, baada ya pongezi hizo, iliamuliwa kwamba sasa soko lijengwe Mererani tunaomba mchakato wa ujenzi wa soko ufanyike kwa haraka kwa sababu tayari maamuzi ya viongozi wetu wakuu wa nchi yalishafanyika na walishatoa maagizo. Ujenzi huo utasaidia sana kurahisisha ajira kwa vijana wengi. Sasa, tunaomba Wizara ya Fedha sasa taratibu zote zimeshakamilika michakato yote imeshakamilika iliamuliwa kutolewa bilioni 5 lakini kwa kuanzia ilitakiwa itolewe fedha kiasi cha bilioni 20.

Mheshimiwa Spika, unapotetea maslahi ya mkoa unaotoka, unapotetea maslahi ya vijana kuna wakati mwingine kidogo ... naomba niendelee...

(Hapa Mheshimiwa Asia A. Halamga aliacha kuongea kwa muda mfupi)

SPIKA: Haya Mheshimiwa Halamga nakutunzia dakika zako pumua kidogo kaa kidogo achangie Mbunge mwingine utarejea kumalizia hoja yako.

MHE. ASIA A. HALAMGA: Mheshimiwa Spika, naomba niendelee

SPIKA: Ahsante sana.

MHE. ASIA A. HALAMGA: Mheshimiwa Spika, naomba niendelee niko vizuri kijana wako.

SPIKA: Haya ahsante sana.

MHE. ASIA A. HALAMGA: Mheshimiwa Spika, ahsante Wizara ya Fedha inaendelea kutucheleweshea kutoa fedha hiyo, ambapo inatakiwa itoke bilioni moja kwa ajili ya kuanza ujenzi. Tunaomba Wizara ya Fedha wasikwamishe jitihada za Mheshimiwa Rais na hiyo fedha itoke ili ujenzi uanze. Lakini pia tunaipongeza Wizara kwa sababu baada ya soko hilo kukamilika kule ndani kuna package za mafunzo mbalimbali juu ya uchakataji wa madini pamoja na upandishaji thamani vito kwa ajili ya vijana. Hivyo itasaidia kuendelea kutoa fursa za ajira kwa vijana wetu wengi.

Mheshimiwa Spika, Mkoa wa Manyara ni mkoa uliobarikiwa kwa madini, yako madini ya aina mbalimbali. Tuiombe Wizara sasa kuendelea kufanya utafiti kwa sababu tunayo madini ya grafit yako wilaya ya Hanang, tunayo madini ya green garnet yapo Mererani, tunayo Mabel kwa ajili ya tiles yapo Simanjiro, tunayo gold inayopatikana Basutu, tunayo madini Babati vijijini, tunayo madini wilaya ya Mbulu. Mkoa mzima wa Manyara umejawa na rasilimali hii muhimu katika nchi yetu, tuombe Wizara itoe hela ya tafiti.

Mheshimiwa Spika, lakini pia kwa kumalizia tunaiomba Serikali, kile kinachotokana na madini tuombe Serikali irudishe fedha kwenye jamii kwa maana ya huduma za afya, barabara pamoja na maji. Lakini pia Mji wa Tanzanite City…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Ahsante sana.

MHE. ASIA A. HALAMGA: ahsante naunga mkono hoja kwa asilimia zote. (Makofi)
Azimio la Bunge la Kuridhia Kufutwa kwa Hifadhi ya Taifa ya Kigosi ili Kuruhusu Kuanzishwa kwa Hifadhi ya Msitu wa Kigosi na Azimio la Bunge la Kuridhia Kurekebisha Mpaka wa Hifadhi ya Taifa ya Ruaha
MHE. ASIA A. HALAMGA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuweza kuchangia katika maazimio haya mawili, Azimio la Kigosi pamoja na lile la Ruaha.

Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa nitumie nafasi hii kumpongeza kwa moyo wa dhati Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, lakini pia kuwapongeza Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri na Katibu Mkuu.

Mheshimiwa Spika, hakika sisi Wanakamati tunaona sasa namna gani sekta ya maliasili na utalii inakwenda kuwa na tija katika Taifa letu, na hasa kwa kuendelea kutatua migogoro ambayo imekuwa ikiikabili sekta yetu ya maliasili na utalii.

Mheshimiwa Spika, nitaanza kuchangia kwa eneo la Ruaha kwa maana ya kule Mbarali. Niendelee kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kutoa ekari zaidi ya 74,000 na kuweza kuwagawia wananchi. Mheshimiwa Rais ana nia njema na Watanzania na ndiyo maana ameweza kutoa sehemu hii ya eneo hili ili wananchi hawa waweze kwenda kujiendeleza kimapato kwa maana ya kuyatumia sasa maeneo haya kwa uzalishaji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tutumie nafasi hii kuendelea kumshukuru Mheshimiwa Waziri kwa kuungana na Kamati na kwenda Mbarali na kuona tatizo na changamoto ambayo imeweza kuwakuta wananchi, kero ambayo ilikuwa Kapunga I kupitia Kapunga II ambayo amepewa mwekezaji.

Mheshimiwa Spika, tunaendelea kuipongeza Serikali kwa kuwa sikivu kwa kuona sasa ni busara kutoa baadhi ya maeneo na kuikabidhi Serikali ili wananchi waweze kupatiwa na kuendelea kutatua mgogoro kati yao na zile hisia walizokuwa nazo kuhusu kupendelewa kwa mwekezaji. Kwa hiyo, niipongeze Serikali kwa kuitoa hiyo sintofahamu kwa wananchi kuhusu kupendelewa kwa mwekezaji.

Mheshimiwa Spika, sasa tuiombe Serikali, wananchi wanakuwa na mgogoro na mwekezaji kwa sababu eneo lake lina manufaa, lina miundombinu ya kutosha ambayo inaweza kumzalishia na kumpatia kipato. Tuombe sasa na upande huu wa wananchi ambapo ni eneo la Kapunga I liweze kuwekewa miundombinu, na hii Wizara ya Kilimo pia ishirikishwe ili wananchi wale lile eneo ambalo wamepatiwa liweze kuwa na tija ya uzalishaji na kuondoa migogoro ambayo imeweza kuonekana kati yao na mwekezaji.

Mheshimiwa Spika, eneo lile likiwekewa miundombinu litaendelea kuwapunguzia wananchi gharama kwa sababu hata kwa sasa kule kwa mwekezaji wanakodisha lakini wanakodisha kwa gharama kubwa sana. Wakipewa eneo lao hili wataweza kupata ghrama nafuu na kuweza kunufaika nalo.

Mheshimiwa Spika, tuendelee kutoa rai kwa timu ya Mawaziri nane. Tumeona mfano leo Azimio hili limeweza kuingia huku Bungeni na linakwenda kupita kwa sababu ni azimio ambalo lina tija kwa Watanzania. Ile timu ya Mawaziri nane ina kazi sasa ya kuleta kile ambacho wamekwenda kukifanya kwa sababu ni maeneo makubwa na mengi wameweza kwenda kuyafanyia kazi, Serikali imegharamika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa waje watuambie ni maeneo yapi ambayo tayari migogoro imekwisha ili wananchi kuendelea kuondoa sintofahamu na wabaki wakiendelea kuifurahia Serikali yao kama ambavyo wanaifurahia sasa huko Mbarali pamoja na Kigosi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kuyasema hayo, niende sasa kwenye eneo lingine la Kigosi. Tunaipongeza sana Serikali na tunampongeza sana Mheshimiwa Rais kwa kutoa zaidi ya shilingi bilioni 2.5 kuwekeza miundombinu ya kisasa kwa ajili ya viwanda vya kuchakata asali.

Mheshimiwa Spika, hii italeta tija sana kwa wananchi na hasa wananchi wa maeneo ya Mlele, Kibondo, Nzega, Sikonge, Bukombe. Nitoe rai kwa wananchi hao, Mheshimiwa Rais ana nia njema, eneo hili limeenda kutolewa kwa wananchi, basi tuombe Serikali kupitia TFS ambayo ndio inaenda kuwa msimamizi kuhakikisha kwamba wananchi hawa wanapewa nafasi ya kuingia na wasipewe vikwazo, tusianze habari ya vibali vingi.

Mheshimiwa Spika, wananchi wafuate utaratibu na Wizara watumie nafasi hii sasa kutoa elimu kwa wananchi, nini ambacho wanatakiwa kufuata na taratibu zipi za Kiserikali zinatakiwa kufutwa ili wananchi hawa sasa waende kunufaika kama ambavyo walikuwa wakinufaika mwanzo kwa kufanya matambiko, lakini pia kuweka mizinga yao. Pia bila kusahau wahakikishe kwamba wanaenda kuhakikisha vijana wanakwenda kupewa elimu ili na wao, hili eneo ambalo limetolewa na Mheshimiwa Rais liweze kuwa na tija ya kuongeza uzalishaji.

Mheshimiwa Spika, niendelee kuipongeza Wizara kwa kuendelea kutafuta masoko China pamoja na Marekani. Bado malighafi, nyingi zitahitajika hapa kwa hiyo ni jukumu la Wizara sasa kwenda kutoa elimu ya kutosha kwa wananchi ili maeneo haya Mheshimiwa Rais aliyoyatoa yaweze kwenda kuwa na tija.

Mheshimiwa Spika, niendelee kuipongeza sana Wizara kwa kuendelea kutatua changamoto na huu ni mfano mzuri, sisi kama Kamati tutaendelea kuwaunga mkono katika kuhakikisha kwamba tunalinda rasilimali zetu, tunazitunza, tunazihifadhi lakini pia tunatoa fursa kwa wananchi wetu.

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi na naunga mkono hoja kwa maazimio yote mawili. Ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa
MHE. ASIA A. HALAMGA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia katika Wizara hii ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa.

Mheshimiwa Spika, kwanza nichukue nafasi hii kuwapongeza kwa kazi kubwa na nzuri ambayo wanaifanya ya kuwalea vijana lakini kuwajenga katika kulitumikia taifa lao, katika uzalendo wa Taifa lao, lakini kwa sasa kuwatengeneza katika mazingira ya kujitegemea kwenye uchumi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nichukue nafasi hii kumshukuru kwa moyo wa dhati Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, lakini pia kumpongeza na kumshukuru Mkuu wetu wa Majeshi kwa namna ambavyo waliweza kuwalea, kuwachukulia vijana kwamba wanaweza wakakosea, lakini wakaendelea kulelewa vijana wale ambao walifukuzwa kambini na leo wamerudishwa, tunaishukuru sana Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ni ukweli usiopingika vijana wale walifanyakazi kubwa sana ya ujenzi wa miradi mbalimbali katika nchi yetu. Lakini ninaombi kwa Mheshimiwa Waziri, nakuomba sana, wapo vijana ambao walikuwa kwenye kambi ya Ukonga wao walitumika kabla ya wale ambao walikwenda kujenga ukuta wa Ikulu na Mererani. Vijana wale walishiriki kujenga maeneo mbalimbali, wamejenga Bwawa la Umeme Rufiji, wamejenga ujenzi wa Chuo cha VETA Lindi; Chuo cha Ualimu Kigoma; Bandari Kavu Kwala; Ofisi ya Manispaa Kinondoni; majengo mapya Mzumbe na maeneo mbalimbali katika nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini baada ya kazi kubwa hiyo yote vijana ambayo waliifanya, vijana wale waliweza kuchukuliwa na kurudishwa Mgulani na baada ya hapo wakatawanyishwa kurudi majumbani na sasa vijana wale wapo tu majumbani wamekaa. Lakini tunaiomba sasa Serikali, tunaiomba sana Serikali iweze kuwafikiria vijana wale kwa jicho la pili kwa sababu ni hazina kwa taifa letu kwa kuwa wamepata ujuzi mbalimbali ujuzi wa kijeshi lakini na ujuzi pia wakuweza kujiwezesha wao wenyewe kiuchumi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nichukue nafasi hii pia Wizara hii inawatengeneza vijana vizuri sana katika kwenda baadaye kujiajiri. Wanajengwa katika kilimo, ufugaji, uvuvi, lakini baada ya hapo pamoja na Serikali kwamba imewekeza nguvu kubwa kwa vijana hawa, vijana hawa wanaondoka wanakwenda kuwa hawana tija kwa sababu hawana uchumi mwingine ambao unawawezesha kuweza kuendeleza ule ujuzi wao ambao wamepata wa kilimo, lakini pia uvuvi pamoja na mambo mengine. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, JKT inafanya mausala ya kilimo, tumeweza kuambiwa hapa pale Chita mwaka jana walilima kilimo cha mpunga, walitumia fedha nyingi sana kuwekeza, lakini hatima yake faida waliyopata ni ndogo kuliko fedha ambayo wamewekeza. Niombe sasa waweze kuwafikiria vijana wale ambao wanawapatia mafunzo wanapotoka kwa sababu bado Jeshi lina maeneo makubwa vijana hawa kwa sababu wana ujuzi na Serikali iweke mkono wake hapa. Ofisi ya Waziri Mkuu ina mikopo mbalimbali ya kuwawezesha vijana, tuone wanawezaje kuwawezesha vijana hao kwa sababu wana ujuzi wanapokuwa wametoka waandaliwe kwenye kilimo ili wanapolima wao, jeshi hili linajua kwamba sisi tunalima hapa mpunga, lakini tuna vijana pembeni ambao wanazalisha na wataleta kwenye jeshi ili tuweze kuunganisha nguvu ya pamoja na hatimaye jeshi hili katika upande wa kilimo liwe lina tija. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini halikadhalika, niombe jeshi letu hili linafanyakazi kubwa sana ya kuwaanda vijana, basi lisijifungie liweze kuunganisha nguvu na Wizara ya Kilimo kwa sababu tayari tunaona Wizara ya Kilimo imeshatoa fursa kwa vijana na vijana hawa tayari wameshaandaliwa siyo vijana tena wa kwenda kuanza kuwafundisha. Lakini Wizara ya Viwanda na Biashara ili vijana hawa waweze kupatiwa fursa ya masoko pale ambapo watakuwa wamepewa mitaji na kuweza kuwajenga vijana vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini vijana wale ambao niliwaongelea mwanzo walikuwa chini ya Kanali Ashraf Bakari Hassan. Niendelee kusisitiza kwamba tuone vijana wale waangaliwe kwa jicho la pili. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kazi kubwa inafanyika Kikosi cha Mizinga, tuombe sasa nguvu kubwa ipelekwe kule ili kuweza kuendeleza vipaji vya Watanzania vya kuweza kutengeneza vitu mbalimbali na vikaweza kutusaidia sisi wenyewe bila ya kutumia gharama kubwa ya kwenda kuagiza vitu nje ya nchi. Jeshi letu lipo vizuri sana ni kiasi tu cha kuwezeshwa ili waweze kutenda miujiza, kutenda maajabu ambapo itasaidia sana kupunguza gharama ya hivyo vitu ambavyo tunaviagiza kutoka nje ya nchi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi, naunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. ASIA A. HALAMGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi na mimi kuweza kuchangia katika Wizara ya Maliasili na Utalii.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nianze kwa kutoa pongezi kubwa kabisa kwa Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Rais Samia Suluhu Hassan, kupitia filamu ya Royal Tour Mheshimiwa Rais ametoa muda wake, Mheshimiwa Rais ametuheshimisha Watanzania na faida nyingi tunaziona zimeanza kutokea, lakini tunaamini baada ya mwaka mmoja tutaona manufaa makubwa katika nchi yetu kupitia filamu ya Royal Tour iliyotambulishwa na Mheshimiwa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa muda mfupi huu tu tayari mapato yameanza kuongezeka, lakini pia imesababisha kuendelea kutambulika kitaifa na kuendelea kuongeza mahusiano kati ya Tanzania na nchi mbalimbali huko ulimwenguni, huko duniani. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue nafasi hii kuupongeza Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (CCM), kupitia Katibu Mkuu wa Vijana kwa kuwahamasisha vijana wa Kitanzania na hivi leo tunavyoongea wameondoka Dodoma vijana kutoka mikoa mbalimbali wakielekea Ngorongoro kwa ajili ya kuendeleza muendelezo wa filamu hii ya Royal Tour na vijana wa Kitanzania hawa wanaenda kushuhudia maajabu ya nchi yetu ya Tanzania. Ni zaidi ya vijana 963 kwa hiyo, tumpongeze Katibu Mkuu wa Umoja wa VIjana, Ndugu Kenani Kihongosi, Wenyeviti wa Vijana wa Mikoa pamoja na Makatibu wao kwa kuhamasisha vijana wengine wa Kitanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue nafasi hii kumpongeza Waziri Mheshimiwa Pindi Chana, Naibu Waziri, lakini pia Katibu Mkuu. Ni kwa muda mfupi wameteuliwa kwenye Wizara hii, lakini tunaona namna gani ambavyo wamejipanga kuifanya kazi na kwa nini wamejipanga kuifanya kazi?

Mheshimiwa Naibu Spika, zipo changamoto mbalimbali ambazo ziko ndani ya Wizara, lakini unaona wameendelea kuungana na Serikali kupitia timu ya Mawaziri nane kuweza kutatua changamoto mbalimbali za kimipaka kati ya hifadhi pamoja na vijiji. Niendelee kutoa rai ya kushirikisha Wenyeviti wa Serikali pamoja na viongozi wa ngazi za chini katika kutatua na kubaini mipaka kati ya vijiji na hifadhi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niendelee kuipongeza Wizara kwa kuendelea kusimamia miradi mbalimbali ndani ya Wizara ikiwemo mradi wa REGROW kule Iringa, mradi wa Saanane kule Mwanza, Geti la Nabi kule Serengeti na miradi mingine mbalimbali katika nchi yetu ya Tanzania. Kwa namna ya kipekee niendelee kukushukuru na niishukuru Wizara kwa kufungua mlango unaopita Mamire katika Hifadhi ya Tarangire njia ambayo inakuja Babati, tunawashukuruni sana kwa sababu tunauona sasa Mkoa wa Manyara utaunganika na Kanda yake ya Kaskazini kwa maana ya utalii wa kuanzia Tanga, Kilimanjaro, Arusha na sasa hivi sasa Manyara imeenda kufunguliwa kwa kufunguliwa Geti la Mamire. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tuiombe Serikali kwenda kutengeneza changamoto tuliyokuwanayo kwa sasa ni barabara. Tunaomba tutengenezewe barabara ili sasa Mkoa wa Manyara uweze kufunguka na bahati nzuri Mkoa wa Manyara una vivutio vingi vipya na Mheshimiwa Waziri nichukue nafasi hii kumpongeza RC wetu Makongoro Nyerere pamoja na ma-DC wote wa Mkoa wa Manyara kwa kuendelea kuutangaza utalii na kuibua vivutio vipya vya utalii. Kufunguka kwa geti hilo kutasaidia Mlima Hanang, kule Mbulu kuna kanisa la kipekee kabisa na maeneo mengine mbalimbali. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, siku ya leo katika Wilaya ya Hanang, DC wetu Janeth Mayanja atakuwa na shughuli ya kuitambulisha Royal Tour ndani ya Wilaya, lakini kwa kuwakaribisha wadau mbalimbali na kuendelea kutangaza Wilaya, lakini Mkoa, kwa ujumla wake Wizara ya Maliasili na Utalii. Nikuombe Mheshimiwa Waziri baada ya kumaliza kupitishiwa bajeti karibu sana Mkoa wa Manyara uje ujionee kazi wanazozifanya viongozi wa Serikali, lakini kazi wanazozifanya wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kwa kipekee niwashukuru vijana wa Mkoa wa Manyara kwa kutengeneza filamu ya Royal Tour ya kwetu ya Mkoa. Nimuombe Mheshimiwa Waziri, uniruhusu siku moja nikuletee vijana wale uje utambue kazi kubwa ambayo wameifanya ya kuungana na Mheshimiwa Rais ya kutangaza utalii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kwa kipekee niwashukuru vijana wa mkoa wa Manyara kwa kutengeneza filamu ya Royal Tour ya kwetu ya mkoa nimuombe Mheshimiwa Waziri uniruhusu siku moja nikuletee vijana wale uje utambue kazi kubwa ambayo wameifanya ya kuungana na Mheshimiwa Rais ya kutangaza utalii.

Mheshimiwa Naibu Spika, niende sasa kwenye changamoto wanazozipitia vijana katika masuala ya ajira na mazingira ya kazi na leo nitaongelea vijana ma-tour guide pamoja na wapagazi ambao ni vijana wanaohusika na kupandisha mlima. Miaka kumi iliyopita Wizara pamoja na makampuni ya utalii pamoja na wapagazi na tour guides walikubaliana haya yafuatayo; kwanza, vijana kwa siku watakuwa wanalipwa dola 10 ambao ni wapagazi, lakini ma-tour guides watalipwa dola 20. Sasa kiwango hiki cha fedha kwa kwelli kwa sasa hivi hakikidhi mahitaji ya vijana wa kitanzania tunaomba sheria ije na ibadilishwe ili vijana hawa waweze kupata maslahi.

Mheshimiwa Naibu Spika, pili, lakini sambamba na kutangaza wageni wetu kuja nchini kwetu watu namba moja ukiachana na Migration wanaofanyakazi kubwa ya kuwa-handle wageni na wanaoishi nao na kuisemea vizuri nchi yetu ni hawa vijana ambao wanaopandisha watu milimani ama wanatembea nao kuwaonesha vivutio mbalimbali vya nchi yetu. Tunaomba Wizara isimamie makampuni vijana hawa wanawapandisha watu milimani wakiwa wana masweta ya kawaida. Kwa hiyo, tuombe Wizara isimamie vijana hawa wapandishe na wafanye shughuli hizi wakiwa na vifaa ambavyo vinastahili, lakini kwa kuzingatia maslahi ya vijana hawa.

Tatu, tuombe Wizara imefanya vikao mbalimbali na wadau wa utalii, lakini tuombe Wizara sasa ikutane na vijana hawa ili kuweza kujua changamoto mbalimbali ambazo zinawakuta kwa sababu wana kero nyingi na wanatamani Serikali yao iwasikilize ili kuweza kuboresha sasa idadi kubwa hii ya wageni wanapokuja waweze kupokelewa na picha nzuri ya vijana wa Kitanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunao watu wanaitwa waiter ama waitress kwenye mahoteli, kwa asilimia kubwa vijana hawa wa Kitanzania wanasomea na baada ya kusoma wakienda kuajiriwa hawaajiriwi wanaitwa ni ma-trainee anakaa trainee mwaka wa kwanza, mwaka wa pili miaka mitano mtu anaenda kuzeeka hapa kuna kichaka cha kuficha ajira ya Watanzania, ajira ya vijana haki stahiki zao. Kwa hiyo tuombe vijana hawa iwe kuna kikomo cha mtu awe amefuzu elimu yake na anapoenda kuajiriwa awe ni mwajiriwa na siyo ni trainee tena. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tuiombe sasa Serikali kwenye ripoti ya CAG imeeleza kwamba kuna vitalu vilitangazwa na vikalipiwa, sasa tuombe tusichafue na tusijitie doa vile vitalu ambavyo vimelipiwa wale watu vitalu hivyo wapatiwa na kuendelea kuhakikisha kwamba ni kweli tumeutangaza utalii ni kweli zile fursa na faida tunaziona kwa watu hawa kuondolewa usumbufu huo katika kupewa vitalu vyao. Lakini pia tukumbuke kwamba tuna kila sababu sasa ya kuweza kuongeza muda wa vitalu kwa sababu vitalu mtu anapochukua ana...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Ahsante.

MHE. ASIA A. HALAMGA: Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja na naendelea kupongeza Serikali kwa kazi nzuri. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo
MHE. ASIA A. HALAMGA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuweza kuchangia katika Wizara hii ya Sanaa, Utamaduni na Michezo. Kwanza nianze kwa kutoa pongezi za dhani kwa Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu, Naibu Katibu Mkuu na timu nzima ya Wizara kwa kazi kubwa ambayo wanaifanya. Moja ya kazi kubwa ni pamoja na kutangaza lugha yetu ya Kiswahili katika Tamasha la Dubai Expo kule nchini Dubai. Tunawapongeza sana, lakini hata katika bajeti yenu mmeonyesha namna gani mtaendelea kununua vifaa vya kutafsiri lugha ili kuendelea kukuza lugha yetu ya Kiswahili.

Mheshimiwa Spika, nachukua nafasi hii kumpongeza kwa dhati kabisa Rais wa Jamhuri wa Tanzania, Mama yetu Samia Suluhu Hassan kwa kutenga Shilingi bilioni moja ya kuongeza katika Mfuko wa Maendeleo ya Sanaa. Hii iwe rai kwa Watanzania na wadau wengine mbalimbali kuweza kuchangia mfuko huu ili uweze kuwasaidia vijana wengi wa Kitanzania.

Mheshimiwa Spika, naomba niongelee katika Wizara hii Shirikisho la Maonesho ya Sanaa na Ufundi Tanzania. Kwenye bajeti ya Wizara hatuoni sehemu ambapo shirikisho hili limepangiwa bajeti, lakini tukiangalia shirikisho hili limebeba ajira kubwa za Watanzania, kwa marika tofauti tofauti; vijana akina mama, wazee na makundi mengine mbalimbali. Shirika hili la Maonesho ya Sanaa wapo wachongaji, wachoraji, wabunifu wa mavazi, wabunifu wa mapishi, watu wa sarakasi na ma-MC.

Mheshimiwa Spika, ukiangalia, pale ambapo wageni mbalimbali wanakuja kwenye nchi yetu, kitu cha kwanza cha utamaduni tunachokwenda kutambulika nacho ni hivi vikundi vya ngoma, vinakwenda kupokea misafara mbalimbali lakini vinashiriki katika matukio mbalimbali, ndani ya nchi yetu. Itapendeza tukiona watu hawa wanawekwa kwenye bajeti wanatambulika kwa sababu wana mchango mkubwa katika nchi yetu ya Tanzania lakini wamebeba ajira nyingi za kuleta maendeleo katika nchi yetu.

Mheshimiwa Spika,…

MHE. SAASHISHA E. MAFUWE: Mheshimiwa Spika, taarifa.

SPIKA: Mheshimiwa Asia Halamga kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Saashisha Mafuwe.

T A A R I F A

MHE. SAASHISHA E. MAFUWE: Mheshimiwa Spika ahsante. Nilitaka kumpa taarifa kwamba BASATA nchini Tanzania imesajili mashirikisho manne, lakini haya mengine yanasemwa sana isipokuwa Shirikisho la Sanaa za Maonesho Tanzania, humo ndani kuma ma-MC, ma-DJ, halafu kuna shirikisho sasa la ufundi. Kwa hiyo, nilikuwa nampa taarifa pia kwamba hivi ni vyombo muhimu sana na visaidiwe na bahati nzuri wana uongozi wao unaongozwa na Mama Henjewele.

Mheshimiwa Spika, ahsante sana.

SPIKA: Sasa wewe ulikuwa umeshaota kuwa hayo hana kwenye mchango wake? Maana alikuwa hajamaliza bado. Mheshimiwa Asia Halamga.

MHE. ASIA A. HALAMGA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Namshukuru ndugu yangu Mbunge wa Jimbo la Hai kwa kuliona hili na yeye, hakika lina mchango mkubwa sana kwa Taifa letu. Hili nisiendelee kuchukua muda kwa sababu ameliongelea pia kwa mapana yake, niombe tu sasa Wizara, lile jengo la Maonesho la BASATA lililopo pale Ilala, basi vikundi hivi vikikusanywa na wakawa wamepewa eneo lile, itasaidia sana hata wageni wanapotoka maeneo mbalimbali ikatambulika kwamba jengo fulani ukifika utakutana na vinyago vinavyochongwa na vijana wa Kitanzania na akina mama wa Kitanzania; vitu kama shanga, bangili, nguo za kiasili, iko center moja ambapo tunaweza tukavipata. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kuchangia mchango wangu katika eneo hilo, naomba niende kwenye suala la riadha. Nianze kwa kutambua kwanza mchango mkubwa wa watangulizi wetu ambao wamefanya vizuri sana katika mchezo wa riadha. Napenda kumtambua Mzee Filbert Bayi, Gidamis Shahanga, Selemani Nyambui, Juma Ikangaa, Mwinga Mwanjala na Simon Robert. Tunatambua mchango mkubwa sana wa wazee na waasisi hawa katika mchezo wa riadha. Naomba Wizara isiache, iendelee kuwatumia kwa sababu waliwahi kuwa na mchango mkubwa katika Taifa, lakini hata sasa bado wana ushauri mkubwa katika Taifa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nachukua nafasi hii kumpongeza kijana Emanuel Giniki anayetokea Wilaya ya Hanan’g katika Mkoa wa Manyara kwa kufanya kazi kubwa na nzuri na kuweza kushinda mashindano ya riadha kule nchini Geneva tarehe 15 /5/2022. Hivi karibuni vijana wawili wa Kitanzania akiwemo Emanuel Giniki wanatarajia kwenda nchini USA kwa ajili ya mashindano ya kidunia.

Mheshimiwa Spika, naomba Wizara iweze kuwaweka vijana hawa kambini. Changamoto inayowakuta wanariadha wengi ni mazingira na maandalizi ya kwenda kushinda kwao kwa sababu hawana makambi rasmi ya kuweza kujiandaa kwa ajili ya kwenda kupambana huko duniani. Wote tumeshuhudia na tumefurahia alivyokuja hapa amepeperusha bendera ya Kitanzania vizuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa tuweze kuwatumia vijana hawa kwa kuhakikisha kwamba viwanja wanavyotumia vinakuwa na mazingira bora na pia vifaa vya michezo mbalimbali ya riadha wanaweza kupatiwa na wanaendelea kupeperusha bendera ya nchi yetu ya Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niendelee kuwapongeza CHANETA kwa kufanya kazi kubwa na nzuri sana. Tunaamini sasa watarudisha heshima ya mpira wa pete na kama ambavyo Serengeti Girls kwenye mipira mbalimbali hii ya kiume sasa wameanza kufanya vizuri, na tunaona kwa namna ambavyo wanawake wote ambao wamefanya mashindano, wameweza kuiletea heshima nchi yetu. Tunaamini CHANETA ikipewa nguvu itafanya vizuri zaidi na kuendelea kuongeza nguvu ya kupeperusha bendera vyema na kuleta vikombe vingi katika nchi yetu ya Tanzania kupitia CHANETA na mipira mbalimbali ya miguu inayofanywa na wanawake wa Kitanzania.

Mheshimiwa Spika, niendelee kuiomba Wizara, kuendelea kutoa semina mbalimbali kwa wasanii. Wasanii wengi saa nyingine wanaadhibiwa siyo kwa kupenda kwao. Wasanii wa Kitanzania ni vijana ambao wanahitaji semina za mara kwa mara, na ikimpendeza Mheshimiwa Waziri waweze kutoa elimu za ujasiriamali kwenye makundi haya, kwa sababu kile kidogo wanachokipata waweze kukihifadhi ili kiweze kuwa na maslahi bora na tija kwao kwa sababu bado ni vijana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi, mchango wangu wa siku ya leo unatosha, niwe nimeishia hapo.

Mheshimiwa Spika, ahsante sana, naunga mkono hoja. (Makofi)
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 na Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025
MHE ASIA A. HALAMGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi na mimi ya kuweza kuchangia katika mpango wa mwaka 2024/2025.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa nianze kwa kuipongeza Serikali kupitia Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa ambayo anaifanya haswa ya kuendelea kuisimamia miradi mikubwa katika nchi hii ambayo inaendelea kutoa fursa kubwa na kuendelea kutanua fursa kwa asilimia zaidi ya sabini kwa vijana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nje ya kumshukuru Mheshimiwa Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania niwapongeze sana Mawaziri, Waziri wa Fedha, Waziri wa Mipango kwa mpango huu wa mwaka 2024/2025. Naomba sasa niende kwenye mchango wangu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ili mipango hii iweze kwenda na ili mipango hii tuweze kuhakikisha inaweza kufanikiwa, kwanza kabisa lazima tujiwekeze katika miundombinu ya umeme katika nchi hii. Bwawa la Mwalimu Nyerere linakwenda kuifungua nchi, lakini Serikali ya Chama Cha Mapinduzi, Serikali ya Awamu ya Sita imeendelea kuhakikisha inaendelea kuleta miradi mikubwa katika nchi hii ambayo yote inahitaji umeme. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, umeme wa Bwawa la Mwalimu Nyerere peke yake hauwezi kuja kutosheleza bado tunahitaji tuendelee kuweka fedha nyingi za kuhakikisha tunaendelea kutengeneza njia nyingine za kuweza kuvumbua umeme ili uweze kuwa suluhisho la matatizo na changamoto kwa Wananchi wa Tanzania na hususan vijana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia namna ambavyo umeme unakuza pato, kukatika kwa umeme ni hasara kubwa katika nchi. Kwa sababu, wapo watu wa welding ambao ni vijana wanategemea, wapo watu wa ice cream wanafunga huko wanategemea. Kwa hiyo, umeme unagusa watu wadogo na watu wakubwa. Unagusa viwanda vidogo na viwanda vikubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, lazima katika mpango tuendelee kuhakikisha watu wa nishati na haswa kwenye umeme wanatengewa fedha na umeme mwingine unaendelea kuibuliwa ili kutatua kero ya umeme katika nchi yetu na kuweza kuhakikisha hakuna siku inayosababishwa na kukatika kwa umeme mapato ya nchi yanapungua katika nchi yetu ya Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu wa pili nijielekeze kwenye JKT. Hapa niongelee masuala ya kilimo, kwanza ninaishukuru sana Serikali kama kijana wa Kitanzania, kwa kupitia JKT kuwatengeneza vijana wetu katika uzalendo lakini kuwatengeza vijana wetu katika kupata ujuzi wa stadi za maisha za kuja kuweza kujipatia kipato.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunatumia gharama kubwa sana na vijana hawa wanakaa kwa miaka mitatu kambini. Wana ujuzi mkubwa mno ambao sisi wenyewe Serikali tumewaweka katika uzalendo lakini katika ujuzi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze Waziri wa Kilimo kwa ule mpango wa BBT. Mpango wa BBT, JKT wengi kupitia mazao ya mnyororo wa thamani, kilimo cha JKT wangeweza kuwatumia vijana wale wanapomaliza baada ya miaka mitatu leo tungetemea JKT sio sehemu tu ya kulima bali tuone sasa JKT inaenda kuwa na viwanda vidogo vidogo ili kutoa ajira kwa vijana wale ambao tayari kwa miaka mitatu tumewapa study na skills za maisha ambazo wanaweza kabisa kusaidia nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kama asilimia 40 tu ya vijana wanaotoka JKT ndiyo wanaoweza kuajiriwa kwenye vyombo vingine vya ulinzi na usalama lakini karibu asilimia 60 inarudi nyumbani na tayari tumewapa skills za maisha. Sasa ni lazima tuondokane na mazoea ama kukariri ama kutumia tu kanuni zile kwamba, ni kwa mujibu wa sheria na wakimaliza waende nyumbani lakini tuna uwezo wa kuwatumia kama ambavyo BBT imeweza kutoa ajira zaidi ya watu 800. Tayari tuna rasilimali na nguvukazi hii ambayo tayari ina nidhamu, ina weledi na inajua inafanya nini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, BBT imefanya vizuri sana lakini kila mkoa una vijana katika nchi hii, mradi huu ukiweza kuongezewa nguvu na ukaenda kila mkoa ili kuweza kurahisiha mradi huu kwa kule mikoani utawasaidia vijana wengi katika nchi yetu ya Tanzania na haswa nikiuchukulia mfano Mkoa wangu wa Manyara, hauhitaji kusubiri uweke miundombinu ya maji bali mvua zenyewe za msimu zinakuja mara kwa mara na kwa wakati na tuna uwezo wa kufanya uzalishaji mkubwa na ukawa na manufaa katika nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niongelee suala la chumvi. Tumekuwa na chumvi nyingi sana katika nchi yetui ya Tanzania na haswa nikitolea mfano Mkoa wa Lindi. Ipo chumvi kule ya kutosha ambapo Waziri wa Viwanda, tungeweza kui-process kuweka viwanda vidogo vidogo ingeweza kusaidia Watanzania wasinunue chumvi inayoandikwa imetoka nchi fulani wakati ndani ya nchi yetu tuna chumvi ya kutosha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitolee mfano wa wilaya ninayotoka, Wilaya ya Hanang. Kwa mwaka mmoja inazalisha zaidi ya tani 35,000 za chumvi; hiyo ni kwa kutumia local kabisa huko chini (njia za kawaida kabisa za kienyeji) lakini tunatarajia Waziri wa Mipango uone namna gani aidha tunapata wawekezaji wakubwa. Pia, kuna wawekezaji mle ndani wadogo wadogo wakawezeshwa ili kuweza sasa kwa sababu tukipata vyombo vya kisasa, maana yake kwa mwaka tuna chumvi zaidi ya tani 70,000. Tutaendaje kununua chumvi kutoka nchi nyingine wakati ndani ya nchi yetu tuna uwezo kabisa wa kutengeneza viwanda vidogo vidogo, na kuwatafuta wawekezaji. Lakini nje tu ya kuwa na chumvi ya Tanzania bali ni kutoa ajira kwa vijana, kina mama na wananchi wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tuendelee kuliona hili kwa mapana yake, kwa ukubwa wake. Zile rasilimali ambazo tunazo tukaweza kuzitengenezea viwanda vidogo vidogo na kutafuta wawekezaji na tukaweza kufanya vizuri zaidi na kuingiza mapato katika nchi yetu. Fedha za Kitanzania lakini pia za kigeni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi yetu ya Tanzania imebarikiwa sana. Hapa naomba niongelee upande wa mashamba na ninaomba nijikite sehemu ambayo ninaifahamu vizuri, sehemu ambayo ninayotoka. Kule Hanang kuna shamba la Basutu. Shamba la Basutu kwa sasa hivi mwekezaji ana takribani ekari 40,000 ambazo zimeanza uzalishaji lakini katika ekari 40,000 ni ekari 22,000 ambazo ameweza kuzilima na ekari 18,000 zimebaki kama msitu. Nini ambacho ninataka kukiomba? Serikali ya Wilaya kwa maana ya halmashauri inategemea shamba ambalo ni ekari 9,000 ambalo halmashauri inalimiliki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa fedha zile za halmashauri zinaingiza mapato kwenye halmashauri na mchakato wa fedha hizo ndiyo unaotumika katika mgao wa asilimia nne kwa wanawake, nne kwa kinamama na mbili kwa watu wenye ulemavu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo niiombe Serikali katika mpango wenu shamba lile la ekari 9,000 libaki kwenye halmashauri ili halmashauri iendelee kuingiza kipato kwa sababu mpaka sasa hivi inatumia karibu shilingi bilioni moja kujiingizia kipato. Kwa hiyo, niiombe sana Serikali kwamba, kwa upande wa wawekezaji tumwangalie kwanza mwekezaji wa kwanza ekari 40,000 kazilima ekari 22,000 na ekari 18,000 zimebaki hazina kazi sasa tuchukue tena ekari 9,000 tuwape tena wawekezaji? Hebu niombe kwanza study nzuri ifanywe kwa huyu mwekezaji wa kwanza tuone anatuingizia tija gani katika nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naona kengele imegongwa lakini niendelee kuipongeza Serikali ya Awamu ya Sita kupitia Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa namna ambavyo anatupambania vijana. Ukiangalia kwenye elimu, miundombinu mikubwa ambayo inaendelea kutengenezwa kwenye nchi hii vijana ndiyo nguvu kazi ambayo inatumika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi. (Makofi)