Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Ally Mohamed Kassinge (13 total)

MHE. ALLY M. KASSINGE aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itaanza ujenzi wa Kiwanda cha Mbolea katika Mji wa Kilwa Masoko kitakachotumia malighafi inayotokana na gesi asilia ya Songosongo?
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Viwanda na biashara, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ally Mohamed Kassinge, Mbunge wa Kilwa Kusini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Mpango wa Matumizi ya Gesi Asilia kwa maana Gas Utilization Master Plan imepanga kutumia kiasi cha futi za ujazo trilioni 0.7 za gesi asilia kwa uzalishaji wa Mbolea. Utafiti unaonesha kuwa Tanzania ina kiasi cha akiba ya gesi asilia kilichogunduliwa na kuthibitishwa takribani futi za ujazo trilioni 57. Hazina hii ya gesi tuliyonayo kwa sasa katika visima vyetu vya gesi asilia inatosha kwa matumizi ya viwanda vya mbolea.

Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua umuhimu wa kuwa na kiwanda cha mbolea kwa kutumia malighafi ya Gesi Asilia. Hivyo, Serikali kupitia Kituo cha Uwekezaji (TIC) na TPDC, Tume imeendelea na juhudi za kupata wawekezaji kwa ajili ya kuwekeza kwenye viwanda vya mbolea. Hapo awali Serikali iliwahi kufanya majadiliano na kampuni ya Ferrostaal na Helm kutoka Ujerumani. Serikali imeendelea kufanya majadiliano na wawekezaji wengine akiwemo Dangote, Elsewedy kutoka Misri na Minjingu Mines Limited ambao wameonesha nia ya kufanya uwekezaji huo.

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Kituo cha Uwekezaji (TIC), TPDC, PURA, EWURA na Wizara inaharakisha kukamilisha majadiliano hayo na hatimaye kupata wawekezaji wenye uwezo wa kujenga viwanda vya mbolea kwa lengo la kumaliza tatizo kubwa la uagizaji mbolea nje ya nchi. Pindi majadiliano hayo yatakapokamilika ni imani ya Serikali kuwa ujenzi wa kiwanda hicho utaanza mara moja. Nakushukuru.
MHE. ALLY M. KASSINGE aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itaanza kutekeleza mradi wa maji kutoka Mto Mavuji kwa ajili ya wakazi wa Miji Midogo ya Kilwa Kivinje na Kilwa Masoko?
NAIBU WAZIRI WA MAJI alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Maji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ally Mohamed Kassinge, Mbunge wa Kilwa Kusini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ilipata mkopo wa masharti nafuu kutoka Serikali ya India kupitia Benki ya Exim India jumla ya Dola za Marekani milioni 500 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi katika Miji 28. Mji Mdogo wa Kilwa Kivinje na Kilwa Masoko ni miongoni mwa Miji itakayonufaika. Utekelezaji unatarajiwa kuanza mwishoni mwa mwezi Aprili, 2021 na unatarajiwa kuchukua miezi 24 kukamilika.
MHE. ZUBERI M. KACHAUKA K.n.y. MHE. ALLY M. KASSINGE aliuliza:-

Je, Serikali iko tayari kuunga mkono juhudi za wananchi wa Kata ya Makata - Liwale ambao wameanzisha ujenzi wa Chuo cha VETA na madarasa mawili yamekamilika?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia naomba sasa kujibu swali la Mheshimiwa Zuberi Mohamed Kachauka, Mbunge Liwale kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua jitihada zinazofanywa na wananchi za kuona umuhimu wa kuwa na Chuo cha Ufundi Stadi katika maeneo yao wakiwemo wananchi wa Kata ya Makata - Liwale.

Mheshimiwa Mwenyekiti, azma ya Serikali ni kujenga Chuo cha Ufundi Stadi katika kila Wilaya nchini. Katika kutimiza azma hiyo, Serikali inaendelea na ujenzi wa Vyuo vya Ufundi Stadi katika Wilaya 29 nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa Serikali inaendelea na mpango huu kwa awamu, nashauri wananchi wa Kata ya Makata waendelee na juhudi hizo wakati Serikali inaendelea kutafuta fedha. Aidha, niombe uongozi wa Wilaya ya Liwale uwasiliane na uongozi wa VETA kuweza kuona namna ya kupata msaada wa kitaalam kuhusu ujenzi wa majengo ya Vyuo vya Ufundi Stadi. Ahsante.
MHE. ALLY M. KASSINGE aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itawezesha upatikanaji wa mawasiliano ya simu katika Kata ya Likawage na vijiji vyake vya Likawage, Nainokwe na Liwiti?
NAIBU WAZIRI HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa na kwa unyenyekevu kabisa naomba upokee salamu za pongezi kutoka kwa wananchi wa Jimbo la Bariadi kwa wewe kuchaguliwa kwa kishindo kabisa kuwa Spika wa Bunge letu la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba kwa niaba ya Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ally Mohamed Kassinge, Mbunge wa Kilwa Kusini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote tulibaini uwepo wa changamoto ya mawasiliano ya simu katika Kata ya Likawage na vijiji vyake vyote. Hivyo, Serikali ilitangaza kata hii katika zabuni ya awamu ya tano ya mwaka 2021.

Mheshimiwa Spika, kata hiyo ilipata mtoa huduma wa Kampuni ya Tigo iliyokamilisha ujenzi wa minara miwili mnamo mwezi Oktoba, 2021. Ujenzi wa minara hiyo umetatua tatizo la mawasiliano lililokuwepo katika Kata ya Likawage na vijiji vyake. Nakushukuru.
MHE. ALLY M. KASSINGE aliuliza: -

Je, ni lini Ripoti ya Ukaguzi ya Chama cha Msingi Nanjirinji ‘A’ itatolewa ili hatua zichukuliwe kwa wahujumu wa fedha msimu wa 2021/2022?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Ally Mohamed Kassinge, Mbunge wa Kilwa Kusini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Ripoti ya Ukaguzi wa Chama cha Msingi cha Ushirika cha Nanjirinji ‘A’ ilikamilika Desemba, 2021 na kuwasilishwa kwenye Mkutano wa wanachama tarehe 23 Mei, 2022. Aidha, ukaguzi ulibaini kuwepo kwa udanganyifu katika nyaraka za mauzo ya ufuta na hivyo kusababisha malipo ya shilingi 93,476,190 kutolipwa kwa wakulima 89 waliouza kilo 39,319 za ufuta.

Mheshimiwa Spika, kutokana na hali hiyo, Serikali imechukua hatua ya kuvunja Bodi ya Chama hicho na taarifa ya uchunguzi imewasilishwa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Lindi kwa ajili ya uchunguzi zaidi na hatua za kisheria kwa waliohusika na ubadhirifu huo.
MHE. ALLY M. KASSINGE aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itaanza mchakato wa ujenzi wa Bandari ya Uvuvi katika Mji wa Kilwa Masoko?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ally Mohamed Kassinge Mbunge wa Kilwa Kusini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali imeshaanza ujenzi wa Bandari ya Uvuvi katika eneo la Kilwa Masoko Mkoani Lindi. Mkataba wa ujenzi wa Bandari hiyo ulisainiwa tarehe 07 Juni, 2022 kati ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi na Mkandarasi ambaye ni Kampuni ya M/S China Harbour Engineering. Aidha, maandalizi ya awali ya ujenzi wa Bandari hiyo yameanza na ujenzi unatarajiwa kukamilika ndani ya miezi 24. Ahsante.
MHE. ALLY M. KASSINGE aliuliza: -

Je, mazungumzo ya Serikali na wawekezaji kujenga Kiwanda cha Mbolea Kilwa Masoko kwa kutumia gesi asilia yamefikia wapi?
NAIBU WAZIRI WA UWEKEZAJI, VIWANDA NA BIASHARA alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Ally Mohamed Kassinge, Mbunge wa Kilwa Kusini kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua umuhimu wa viwanda vya mbolea na namna uzalishaji wa mbolea nchini utakavyoongeza tija kwa wakulima na hatimaye kupata mavuno mengi na viwanda kupata malighafi za kutosha kwa ajili ya kuchakata. Serikali inaendelea na majadiliano na wawekezaji mbalimbali wakiwemo Kampuni ya Dangote, Elsewedy na PolyServe ili kuharakisha uwekezaji wa Kiwanda cha Mbolea Kilwa Masoko.

Mheshimiwa Spika, nakushukuru.
MHE. ALLY M. KASSINGE aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itakamilisha utekelezaji wa Sera ya kupeleka umeme Vijijini kupitia Mpango wa REA III Mzunguko wa Pili?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nishati, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Ally Mohamed Kassinge, Mbunge wa Kilwa Kusini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, mradi wa kusambaza umeme vijijini, awamu ya tatu mzunguko wa pili unaosambaza umeme vijijini vikiwemo vijiji vya Kilwa Kusini vyote, unatarajiwa kukamilika ifikapo mwezi Desemba, 2023. Aidha, Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Dkt. Samia Suluhu Hassan imeongeza wigo wa mradi toka kilomita moja kwa kila kijiji na kufikia kilomita tatu (1+2) katika usambazaji wa umeme katika vijiji ili kuwafikia wananchi wengi zaidi.

Mheshimiwa Spika, awamu hii ya REA III Round II itakapokamilika hakuna kijiji ambacho kitabaki bila umeme.
MHE. SAMWELI X. HHAYUMA K.n.y. MHE. ALLY M. KASSINGE aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itajenga Soko la Samaki Kilwa Kivinje?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ally Mohamed Kassinge, Mbunge wa Kilwa Kusini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2022/2023, Serikali imefanya tathmini ya athari za mazingira na kijamii katika eneo la Kitongoji cha Miramba kilichopo Kilwa Kivinje kwa ajili ya kujenga miundombinu ya kuhifadhia mazao ya uvuvi ya chumba cha ubaridi, vichanja vya kukaushia dagaa na kuweka mtambo wa kuzalisha barafu na wa kukaushia dagaa kwa kutumia umeme.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2023/2024, Serikali kupitia Programu ya Kuendeleza Kilimo na Uvuvi inayofadhiliwa na Mfuko wa Kimataifa wa Kuendeleza Kilimo (IFAD) itaweka miundombinu hiyo katika eneo hilo. Aidha, Serikali itaendelea na mpango wa kufanya tathmini ya athari ya mazingira na kijamii kwa ajili ya ujenzi wa soko la samaki katika eneo hilo kulingana na upatikanaji wa fedha.
MHE. ALLY M. KASSINGE aliuliza:-

Je, lini Serikali itatunga Sera ya Ugatuaji wa Madaraka na kutunga sheria ili kuzijengea uwezo Mamlaka za Serikali za Mtaa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ally Mohamed Kassinge, Mbunge wa Jimbo la Kilwa Kusini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imekamilisha maandalizi ya Rasimu ya Sera ya Taifa ya Ugatuaji wa Madaraka ambapo wadau mbalimbali wameshirikishwa na kutoa maoni yao. Aidha, Rasimu hiyo imewasilishwa katika ngazi ya maamuzi kwa mapitio na maelekezo zaidi.
MHE. ALLY M. KASSINGE aliuliza:-

Je, ni lini wananchi 144 wa Kilwa Masoko ambao maeneo yao yalichukuliwa kwa lengo la upanuzi wa Kiwanja cha Ndege watalipwa fidia?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE) alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Ally Mohamed Kassinge, Mbunge wa Kilwa Kusini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kutekeleza zoezi la ulipaji fidia kwa wananchi waliopisha upanuzi wa Kiwanja cha Ndege cha Kilwa Masoko, Serikali imehuisha uthamini wa mali za wananchi ndani ya kipindi cha robo ya kwanza ya Mwaka wa Fedha 2022/2023, ambapo idadi ya wananchi iliongezeka kutoka 144 waliofanyiwa uthamini mwaka 2013 hadi kufikia wananchi 438.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sasa Serikali ipo katika hatua za mwisho za maandalizi ya uwekaji wazi Daftari la Fidia (Valuation Report Disclosure) kwa wananchi husika kabla ya kuwasilishwa kwa Mthamini Mkuu wa Serikali kwa idhini, ahsante.
MHE. ALLY M. KASSINGE aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itafanya marekebisho ya Kanuni za Uvuvi za mwaka 2020 ambazo zinalalamikiwa na wadau wa Sekta ya Uvuvi?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ally Mohamed Kassinge, Mbunge wa Kilwa Kusini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi, inaendelea kufanya marekebisho ya Kanuni za Uvuvi za Mwaka 2020 ili kuboresha shughuli za uvuvi nchini na biashara ya mazao ya uvuvi ndani na nje ya nchi kwa kuzingatia maoni ya wadau wa sekta ya uvuvi na maoni yaliyotolewa na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo kwenye Vikao kati ya Wizara na Kamati hiyo vilivyofanyika tarehe 30 Machi, 2020 na tarehe 25 Agosti, 2021. Aidha, Marekebisho ya Kanuni husika yanatarajiwa kukamilika mwezi Julai, 2022.
MHE. ALLY M. KASSINGE aliuliza: -

Je, lini Serikali italipa fidia kwa wananchi 438 Waliofanyiwa uthamini kupisha upanuzi wa Kiwanja cha ndege Kilwa – Masoko?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Uchukuzi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Ally Mohamed Kassinge, Mbunge wa Kilwa Kusini kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, katika kipindi cha robo ya mwisho wa mwaka wa fedha 2022/2023, Serikali ilikamilisha zoezi la Uwekaji Wazi Daftari la Fidia (valuation report disclosure) kwa wananchi 438 waliofanyiwa uthamini ili kupisha upanuzi wa Kiwanja cha Ndege Kilwa Masoko.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hatua hiyo, mnamo mwezi Agosti, 2023 Wizara ya Fedha ikishirikiana na Wizara ya Uchukuzi, Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) na Ofisi ya Ardhi Mkoa wa Lindi, walifanya na kukamilisha zoezi la uhakiki wa daftari la fidia.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya hatua hizi, zoezi la ulipaji wa fidia litaanza mara baada ya Wizara ya Fedha kukamilisha taratibu zote za kifedha.