Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Ally Mohamed Kassinge (9 total)

Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022
MHE. ALLY M. KASSINGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote nikushukuru kwa nafasi, lakini pia kwa sababu nachangia kwa mara ya kwanza, nami nitumie fursa hii kuanza kwa kumshukuru Allah Mwenyezi Mungu Subhanah Wataala, lakini pia kuishukuru familia yangu, wapigakura wangu wa Jimbo la Kilwa Kusini, pamoja na Chama changu Chama Cha Mapinduzi kilichonipa dhamana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya shukrani hizo naanza kuchangia nikianzia na sekta ya viwanda. Sekta ya Viwanda katika nchi yetu ipo malighafi ambayo bado hatujaweza kuitumia na hapa nazungumzia malighafi ya gesi asilia. Katika Wilaya ya Kilwa eneo la Songosongo tunazalisha gesi pale ambayo inatumika kuzalisha umeme au kufua umeme, lakini mabaki yanayotokana na gesi asilia bado hayajaweza kutumika kwa ajili ya viwanda na hapa nazungumzia viwanda vya mbolea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nishauri kupitia Mpango huu Kiwanda cha Mbolea Kilwa Masoko kitakachotokana na malighafi ya gesi asilia kiingie katika Mpango huu tunaoenda kuutekeleza kwa ajili ya maendeleo ya Watanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, nije kwenye Sekta ya Kilimo; eneo mahususi ambalo tutawasaidia wakulima wetu ni kuhusianisha kilimo pamoja na Sekta ya Viwanda. Mosi, viwanda vya kuwawezesha wakulima wetu kupata mbolea kwa urahisi vianzishwe karibu na maeneo ambayo viwanda hivyo vitawasaidia wakulima kwenye maeneo husika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Nyanda za Juu Kusini ambapo kwa kiwango kikubwa wenzetu ndiyo wakulima wakubwa wanaozalisha kwa ajili ya kulisha nchi na ziada mpaka tunaambiwa kwamba kuna chakula au mahindi yamebaki huko yamekosa soko, nashauri kupitia Mpango huu kuanzishwe kiwanda cha mbolea Wilaya ya Wanging’ombe, Mkoani Njombe ambapo tayari wananchi wametoa eneo la kutosha. Kwa kufanya hivyo tutaweza kupunguza changamoto ya pembejeo ya mbolea katika msimu wa kilimo. Wizara ya Kilimo itakuwa inapunguza kazi ya kutoa bei elekezi kwa sababu ya mbolea inayotokana na sekta binafsi, tukianzisha kiwanda pale tutasaidia Mikoa ya Njombe, Mbeya, Iringa, Ruvuma na Katavi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kuna eneo la sekta ya uvuvi, Mpango unaelezea suala zima la uvuvi katika kuanzisha bandari za uvuvi lakini hii iende sambamba na masoko ya samaki. Wilayani Kilwa hususani Kilwa Kivinje ni miongoni mwa maeneo ya uzalishaji mkubwa wa sekta hii ya uvuvi ikiwa ni pamoja na Mafia. Nashauri kupitia Mpango huu tuanzishe bandari za uvuvi Kilwa Masoko na Mafia na tuanzishe soko kubwa la samaki pale Kilwa Masoko kwa sababu nchi jirani na hususani Congo wanakuja kununua samaki tani kwa tani lakini Serikali hatujaweza bado kuratibu eneo hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya mchango huu, naunga mkono Mpango huu na nashauri upitishwe kwa mujibu wa mapendekezo tunayoyatoa Wabunge hapa Bungeni. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
MHE. ALLY M. KASSINGE: Mheshimiwa Spika, nitumie fursa hii kwanza kukushukuru binafsi kwa kuniona. Pili, kushukuru kwa hotuba nzuri ya Wizara ya Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa ikiwa ni sambamba…

SPIKA: Waheshimiwa Wabunge tusikilizane, huyu anayeongea ndiye aliyechukua Jimbo la yule Mbunge ambaye alikuwa anajiita Bwege. Sasa mbadala wake ni Mheshimiwa Kassinge, karibu sana hiyo ndiyo bunduki mpya ya CCM. (Makofi)

MHE. ALLY M. KASSINGE: Mheshimiwa Spika, niendelee kupongeza Ofisi ya Rais, TAMISEMI, kwa mawasilisho ya hotuba ya bajeti, lakini kwa kuaminiwa na mamlaka katika timu zote kuanzia Mheshimiwa Waziri na Wasaidizi wake, lakini pia Katibu Mkuu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, eneo langu la kwanza la uchangiaji ni kuishauri Ofisi ya Rais, TAMISEMI kuja na sera ya ugatuaji ili maeneo ya mgawanyo wa madaraka katika maeneo yote ya siasa, utawala, fedha yabainike baina ya Serikali Kuu na Serikali za Mitaa.

Mheshimiwa Spika, jambo la pili, katika eneo la mapato ya halmashauri, kuna eneo la mapato ya ushuru wa mazao produce cess. Ushuru huu umekuwa ukitofautiana kati ya halmashauri moja na halmashauri nyingine. Niishauri Ofisi ya Rais, TAMISEMI iweze ku-harmonies ili ushuru huu uwe sawa na halmashauri zote na kuondoa mgogoro au mgongano ikiwa ni sambamba na kurudisha asilimia tano ya ushuru wa mazao badala ya asilimia tatu ya sasa hivi, kwa sababu utafiti umebainisha kwamba wanaochangia halmashauri katika ushuru huo wa mazao asilimia tatu ni wanunuzi na si wakulima.

Mheshimiwa Spika, pili, kuna eneo hili la property tax ambalo baadhi ya Wabunge hapa wamelizungumzia. Kimsingi hili ni eneo la ushuru au mapato ya Local Authority, lakini hali ilivyo sasa hivi inakusanywa na halmashauri lakini ina hesabika kuwa ni mapato ya Serikali Kuu. Nishauri eneo hili lirudishwe halmashauri na hayo ni mapato ya halmashauri ili zikajenge barabara. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia kuna ushuru wa halmashauri wa kimazoea (traditional) wa siku nyingi, ushuru mdogo mdogo wa wajasiriamali, wauza vitumbua, wauza mahindi ya kuchoma na kadhalika.

Lengo la Serikali kutoa vitambulisho kwa wajasiriamali lilikuwa ni lengo zuri na kazi hii inafanywa vizuri na Watendaji wa Halmashauri kukusanya fedha kupitia vitambulisho 20,000 kwa mwaka, lakini mapato yanahesabika si mapato ya halmashari bali ni mapato ya Serikali Kuu, yanakwenda Hazina moja kwa moja. Niishauri Ofisi ya Rais, TAMISEMI na Serikali kwa ujumla, mapato yanayotokana na wajasiriamali wadogo wadogo yarudi halmashauri yakajenge barabara. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kushauri masuala ya kisera sasa nije katika eneo langu la uongozi na uwakilishi kwa maana ya changamoto zilizopo katika Jimbo la Kilwa Kusini, nikianza na eneo la barabara zinazohudumiwa na TARURA. Naomba hapa nitoe takwimu; kuanzia mwaka 2017/2018 – 2019/2020, Halmashauri ya Kilwa imekuwa ikipata fedha za barabara billioni moja plus kidogo hivi, lakini kuanzia 2021 imekuwa ikishuka ni mpaka kufikia Sh.984,000,000 na hali hii imeendelea kushuka mpaka bajeti hii tuliyonayo. Kwa hali halisi ya urefu wa barabara za Kilwa ambazo ni zaidi ya kilomita 1,000, Sh.984,000,000 hazitoshi.

Mheshimiwa Spika, nashauri tuongeze bajeti hii ili ikahudumie barabara zile. Hapa naomba nizungumze barabara mahsusi na naomba hizi zipewe kipaumbele. Barabara ya kutoka Hoteli Tatu - Pande, Hoteli Tatu – Lihimalyao, sisi Wanakilwa hii ni barabara ya kimkakati inaenda kuhudumia wakazi wapatao 30,000 ambao ni wazalishaji wakubwa wa korosho, kwa hiyo itakuwa ni barabara ambayo itajenga uchumi katika eneo hili. Nishauri kupitia Ofisi ya Rais, TAMISEMI, barabara isiingie katika utaratibu wa maintenance, badala yake iingie katika utaratibu wa development na itengewe fedha za kutosha ili ipitike kipindi chote cha mwaka. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mwisho Sekta ya Afya. Hospitali yetu ya Wilaya ya Kilwa imechakaa vya kutosha…

SPIKA: Kengele imeshagonga. Ahsante sana Mheshimiwa Kassinge.

MHE. ALLY M. KASSINGE: Kwa hiyo tunaomba hospitali ikarabatiwe, kama si kujenga hospitali mpya.

Mheshimiwa Spika, nakushukuru na naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora
MHE. ALLY M. KASSINGE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante na nianze kwa kuchangia hotuba ya bajeti ya Wizara Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora. Lakini kwa upekee nianze kutambua changamoto za watumishi hususani kundi la walimu.

Mheshimiwa Naibu Spika, walimu ni sehemu ya watumishi katika nchi hii lakini kama tunawasikiliza vizuri inaweza ikawa ni miongoni mwa kundi lenye changamoto nyingi zaidi ikiwemo kama ambavyo Wabunge wengine wamechangia kucheleweshwa kupandishwa kwa madaraja ikiwemo mapunjo baada ya kustaafu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hapa nina case study mbili naomba nizitaje; katika Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa, kuna mwalimu anaitwa Mwalimu Hadija Salum Bugurumo alistaafu mwaka 2020; alistaafu akiwa na Daraja F, mshahara aliolipwa ni wa Daraja E, na kwa maana hiyo anadai mapunjo. Pia kuna mwalimu anaitwa Mwalimu Salma Khamis Kaisi, naye kadhalika alistaafu mwaka 2020 lakini alipandishwa daraja tangu mwaka 2017 na amelipwa mafao yake ya kustaafu kwa mapunjo bado wanaidai Serikali mpaka leo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa masikitiko makubwa hawa ni walimu wangu ambao wamenifundisha mimi shule ya msingi Mnazi Mmoja, Kilwa Masoko na wamesema mwanangu, mwanangu katusaidie kutusemea huko na hapa nawasemea, Serikali iwasikie. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hayo pia, kama ambavyo Wabunge wengine wamechangia kumekuwa na changamoto kubwa sana ya kupewa gharama za kusafirisha mizigo baada ya kustaafu. Walimu wangu wawili hawa ambao nimewataja kwa mfano tu kwa niaba ya wengine walio wengi nao pia wanakumbwa na kadhai hii hawajalipwa mizigo ya kustaafu bado. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya eneo hilo, nizungumzie pia mazingira ya ufundishaji kwa walimu. Kada zingine hapa Tanzania kumekuwa na namna fulani fulani hivi ya kufikiriwa kimotisha motisha zipo kada ambazo wanalipwa kinachoitwa ration allowance, zipo kada wanalipwa on call allowance kwa maana ya kada ya sekta ya afya, ambayo hiyo on call allowance kwa sababu ya ule muda wa ziada mtumishi wa sekta ya afya anapoitwa kwa ajili ya kwenda kutoa huduma. Lakini walimu hawajafikiriwa, huko nyuma tulipata kuambiwa kwamba kulikuwa na kitu kinachoitwa teaching allowance na hii ilizingatia mazingira ya walimu yalivyokuwa magumu katika kuandaa somo lenyewe, kufundisha na kufuatilia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ualimu hauishii kufundisha tu darasani unaandaa scheme of work ya mwaka mzima kama si kwa muhula mzima, ukitoka hapo unaanda lesson plan, ukitoka hapo unaandaa lesson notes, ukitoka hapo unasahihisha kazi na kufuatilia mwafunzi mmoja baada ya mwingine, lakini pia work load ni kubwa. Mwalimu anatakiwa afundishwe wanafunzi 40 mpaka 45 kwa darasa moja. Walimu wetu hawa wanafundisha wanafunzi mpaka 200 kwa darasa moja hii ni work load kubwa wafikiriwe na wao kupata teaching allowance wapate motisha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie suala la watumishi nitumie lugha kwamba wametelekezwa, hawa walikuwa ni watumishi waandamizi wakapata nafasi za kuteuliwa na mamlaka zao, mamlaka zao za uteuzi baada ya kuwaacha katika nafasi hizo hawajarudishwa bado katika utumishi wa umma na ndio maana nimetumia lugha ya wametelekezwa. (Makofi)

Naomba Ofisi ya Rais Utumishi iwafikirie watumishi hawa kwa sababu na wao ni watumishi kama watumishi wengine na wana haki ya kufikiriwa, hawajapata pension zao, hawajapata maslahi yao yoyote, wamebaki kama walivyo kama wakiwa ndani ya nchi yao, hii sio sawa Ofisi ya Rais iwafikirie hawa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho niseme kwamba wale watumishi ambao walifikia nafasi za uteuzi kama vile Wakurugenzi, Ma-DAS na wengine na wakaingia katika mchakato wa uchaguzi, baadhi hawakutoka katika sekta nje ya utumishi wa umma tunafahamu ambao wametoka katika utumishi wa umma na bado wameendelea kutelekezwa miezi tisa kama wenzangu wamezungumza.

Mheshimiwa Naibu Spika, na hapa nina case study moja ya mtumishi ambaye alikuwa Mtendaji wa Kata Manispaa ya Kinondoni na baadae akawa DAS - Mbeya na baadae akaenda kugombea mpaka leo hajarudishwa katika utumishi wa umma. Tunaomba Serikali iwafikirie hawa ili tusiandae kundi kubwa la huko mbele ya safari ambao watakuwa ni wa kuipinga Serikali ambayo kwa kweli walihitumikia kwa uadilifu mkubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maji
MHE. ALLY M. KASSINGE: Mheshimiwa Spika, ahsante. Awali ya yote namshukuru Mwenyezi Mungu kwa fadhili zake kuu. Pia nianze na nukuu, wakati nachangia Wizara hii ya Maji Maandiko Matakatifu ya Quran sura ya 21 aya ya 30 ambapo Mwenyezi Mungu anasema: “Wajaalna minalmaa- i kulashai-in-hayaa.” Tumejaalia kutokana na maji kuwa ndiyo chanzo cha uhai wa kila kitu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa maandiko haya matakatifu tafsiri yake ni kwamba Wizara ambayo anaisimamia Mheshimiwa Jumaa Aweso na timu yake ndiyo uhai wetu sisi na viumbe vingine. Kwa maana hiyo, ni Wizara ambayo ni tegemeo kubwa la maisha yetu. (Makofi)


Mheshimiwa Spika, kwa spirit hiyo hiyo, mimi binafsi sina shaka kabisa na kiongozi wa Wizara hii Mheshimiwa Jumaa Aweso, sina shaka kabisa na Naibu Waziri, dada yangu Mheshimiwa Eng. Maryprisca, sina shaka na Katibu Mkuu, ndugu yangu Eng. Sanga; Naibu Katibu Mkuu pamoja na timu yote ya Wizara, wapo sawa sawa. Hata meneja wangu wa RUWASA katika Wilaya ya Kilwa Eng. Ramadhani Mabula yupo sawa sawa na tunakwenda naye vema. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa imani tuliyojenga kwenu Wizara ya Maji, nitumie fursa hii kutoa ushauri ufuatao: kwamba kama ilivyo katika umeme, Wizara ya Nishati imekuwa na jukumu na juhudi za kutafuta vyanzo vya umeme kila angle na maji kadhalika mtafute vyanzo vya maji kila angle; katika chemichemi, katika mito, mabwawa, maziwa, maji ya ardhi kwa maana ya underground water na maji ya vyanzo vya asili.

Mheshimiwa Spika, katika eneo hili, niseme tu kwamba kuanzishwa kwa RUWASA miaka miwili iliyopita kumeleta matumaini makubwa kwa Watanzania, lakini ukiangalia mwenendo na utendaji kazi wa RUWASA ni kama vile unaleta tija zaidi kwenye miradi mikubwa mikubwa na hususan kwenye vyanzo vikubwa vya maji hasa Maziwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kule vijijini ambako hatutegemei sana kupata maji kutoka vyanzo vikuu, kidogo nitoe ushauri. Kuna Wakala wa Uchimbaji wa Visima na Mabwawa (DDCA), miaka miwili iliyopita nahisi ufanisi wake wa kazi umepungua. Nadhani kuanzishwa kwa RUWASA umeifanya DDCA isiwe mamlaka kamili au wakala kamili, ni kama unit tu hivi ndani ya Wizara. Nashauri kupitia Bunge lako kwamba DDCA ipewe nguvu kamili. Ilikuwa na waatam wa kutosha, ilikuwa na mitambo ya kutosha. Tulikuwa tukiona magari yakipita na ma- drill yakipita na ma-compressor kwa ajili ya kwenda kuchimba visima vijijini.

Mheshimiwa Spika, Mbunge wa Itilima atakuwa mfano moja wapo wa kutoa ushuhuda huo, kuna visima vingi vimechimbwa na DDCA na ilikuwa na uwezo wa kuleta mapato takribani shilingi bilioni 12 kwa mwaka. Haya siyo mapato madogo. Tuitathmini miaka miwili iliyopita kwa mwaka 2021/2022 kiasi gani cha fedha kimepatikana kutoka wakala wa huu. Kimeweza kuchimba visima vingapi katika vijiji vyetu?

Mheshimiwa Spika, nashauri DDCA ipewe nguvu na mamlaka kamili, Wahandisi wale ambao walikuwa ni washauri wa kitaalam, wako wapi sasa hivi? Mitambo ile iko wapi na iko mingapi na inafanya kazi gani? Nitoe kama hadidu za rejea kwa Waziri akaifanyie kazi ikiwezekana aunde Tume au kikosi kazi mahsusi cha kutathmini utendaji kazi wa DDCA kama kuna upungufu uboreshwe kwa lengo la kusaidia hususan visima vijijini.

Mheshimiwa Spika, hapo hapo nikumbushe Wizara ya Maji; katika Wilaya ya Kilwa hususan Jimbo la Kilwa Kusini, tarehe 15 Septemba, 2009 aliyekuwa Waziri ya Maji wakati huo Mheshimiwa Mwandosya aliahidi kuchimba bwawa katika Kijiji cha Limaliyao, ambapo bwawa lile lingechimbwa lingeweza kusaidia upatikanaji wa maji kwa watu takribani 15,000. Naikumbusha Wizara ikafanyie kazi. Tangu agizo lile la Waziri, hakuna ambacho kimefanyika mpaka sasa.

Mheshimiwa Spika, namwomba sana Mheshimiwa Jumaa Aweso ndugu yangu, ninaimani na timu yake, atume wataalam wake wakafanyie kazi kutafuta eneo ambalo tunaweza tukapata bwawa kwa ajili ya maji ya Wana- Limaliyao, kwa sababu hawataweza kunufaika na mradi mkubwa wa maji kutoka chanzo chochote cha mto. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wakati nikishauri hivyo pia, niendelee kuishukuru na kuipongeza Wizara. Nimeona kupitia kitabu cha bajeti kwamba katika vijiji vyangu kadhaa nitapata miradi ikiwepo Kilwa Kisiwani, nashukuru sana. Pia ikiwemo Likawage, nashukuru sana; pia ikiwemo na Kiu, nashukuru sana.

Mheshimiwa Spika, nimkumbushe Mheshimiwa Waziri, ahadi yake ya kunisaidia kisima cha maji katika Kijiji cha Nainokwe, naomba itekelezwe kupitia mpango huu…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Ahsante sana.

MHE. ALLY M. KASSINGE: Mheshimiwa Spika, pia mpango ule wa miji 28, ukumbuke na Mji wa Kilwa Masoko na Mji wa kilwa Kivinje.

Mheshimiwa Spika, ahsante, naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari
MHE. ALLY M. KISSINGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kumpongeza rafiki yangu Dkt. Faustine Ndungulile kwa kuwa Mtanzania muasisi wa Wizara hii mpya ambapo Mheshimiwa Rais amemdhamini, amemuamini na kwa changamoto ambazo Wabunge tunazielezea katika Bunge lako Tukufu, naamini kabisa rafiki yangu Mheshimiwa Ndugulile ataweza kuitendea haki Wizara hii. Atasaidiana na timu yake Mheshimiwa Naibu Waziri, Katibu Mkuu na watendaji wote katika Wizara hii, tuna imani nanyi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo langu la kwanza la mchango, ni kuishauri Serikali Wizara hii ya Mawasiliano Teknolojia na Habari kupitia taasisi yake ya TCRA. Kimsingi TCRA ni regulator, lakini Watanzania tunahitaji kufahamu ina regulate nini, masuala yote ambayo TCRA inadhibiti yafahamike. Kama ingelikuwa ni mpira tasnia ya kabumbu au kandanda maana yake ni kwamba TCRA ni referee na makampuni ya simu ndiyo timu wachezaji, sisi watumiaji ndiyo washangiliaji na washabiki. Tunataka tujue sisi washabiki nini TCRA ina regulate. Twende mbali zaidi ipendeze zaidi tufikie wakati kwamba sisi washangiliaji, watumiaji, tupate muda wa kupata forum ya kutoa maoni yetu kwa huyu regulator anayeitwa TCRA. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili gharama za simu. Huko nyuma tulikuwa tunatumia gharama za simu kwa utaratibu wa ukinunua Sh.1000 au Sh.2000 maana yake ndivyo utakavyotumia, lakini kumekuwa na utaratibu sasa wa kununua bando au vifurushi, imekuwa kana kwamba ni lazima ununue vifurushi, hivi utaratibu huu TCRA na Mheshimiwa Waziri wanasemaje, kwamba ni lazima Watanzania tulazimishwe kutumia simu kwa utaratibu wa vifurushi, usipohitaji vifurushi unataka utumie moja kwa moja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, bado kuna matatizo na tunahisi kwamba sisi wadau wa tasnia hii ya mawasiliano kuna kuibiwa kupitia utaratibu wa vifurushi. Kwa mfano, unakuta unajiunga kifurushi cha wiki au kifurushi cha siku cha saa 24, badala ya kutumia akiba yako kadiri ulivyoweka, muda ukifika wa saa 24 imekata, sasa hii iliyokatwa inakwenda wapi, hapa ndiyo ambapo tunamtaka regulator, TCRA asikilize maoni ya sisi wadau ambao ni watumiaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kutoa ushauri kwa Wizara hii, nianze sasa kuelezea changamoto ambazo zipo katika Jimbo langu la Kilwa Kusini lakini pia Jimbo la mwenzangu, jirani yangu ndugu yangu, Mheshimiwa Ndulane la Kilwa Kaskazini. Katika Wilaya ya Kilwa, wilaya yenye kata 23, kata 22 hazina uhakika wa mawasiliano. Nitumie fursa hii kumkumbusha rafiki yangu Mheshimiwa Dkt Ndungulile, nimefika ofisini kwake mara kadhaa kumkumbusha kwamba Likawage ambayo ni kilometa zaidi ya 110 kutoka Makao Makuu ya Wilaya hawana mawasiliano, kitu ambacho ni tishio kwa usalama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tukumbuke kwamba Kata hii ya Likawage na Vijiji vyake vyote vitatu vya Likawage na Inoke na Liwiti, ni kata ambayo ipo katika eneo kubwa linazungukwa na Mbuga ya Selous. Wanapata shida ya kwenda kupiga simu mbali karibu na mpakani ukielekea Njinjo kule na usalama wa maisha yao unakuwa hatarini, tunapata shida kupata taarifa za dharura ikiwemo misiba, lakini shida kubwa ni suala la mtandao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri alinipokea vizuri ofisini kwake na kupitia sasa katika mjadala wa bajeti yake, nimkumbushe ahadi yake ya kuhakikisha kwamba Wanalikawage wanapata mnara wana uhakika wa mawasiliano. Sambamba na hilo bado zipo kata zingine ambazo mawasiliano ni shida katika Wilaya ya Kilwa ikiwemo Kata ya Nanjilinji hususan Nakiu pamoja na Kigombo, lakini pia ikiwemo Kata ya Lihimalyao hususan Kisongo na maeneo ya Mabanda kule. Pia Kata ya Kandawale, Kipatimu, Miguruwe, Mitole, Kibata, Kinjumbi, Namayuni pamoja na Chumo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba sana Wizara hii inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. Faustine Ndungulile awatendee haki Watanzania wa Wilaya ya Kilwa kuhakikisha kwamba wanapata mawasiliano ya uhakika. Mbaya zaidi hata zile sehemu ambazo mawasiliano yanapatikana, uhakika wa 4G haupo. Kwa hiyo tunaomba kwamba minara hii sasa iongezewe nguvu ili watanzania wa Kilwa nao waishi kidigitali kama maeneo mengine ya mijini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya hayo, naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja. (Makofi)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi
MHE. ALLY M. KASSINGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Nami nianze kuchangia Hotuba ya Bajeti ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi, kwanza kabisa kwa kupongeza uongozi wa Wizara ambao kwa ujumla umeanza kuleta matumaini mazuri kwa Watanzania hususan kwenye Sekta ya Mifugo na Uvuvi. Kwa hiyo, nawashukuru na ninawapongeza sana viongozi kuanzia Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri na Makatibu Wakuu wote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kubwa zaidi ambalo linatupa matumaini ni kwamba uongozi huu umejikita kwenye ubobezi wa sekta wanazosimamia. Ukiangalia Katibu Mkuu wa Uvuvi, amejikita katika masuala hayo, Katibu Mkuu wa Mifugo kadhalika ni mzoefu wa masuala hayo. Ndugu yangu Mheshimiwa Ulega, Naibu Waziri ni mzoefu wa masuala hayo kitaaluma na pia kimakuzi. Kwa hiyo, Watanzania hatuna shaka katika hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kwanza ambalo nataka kuanza kuchangia katika hotuba hii, kwanza kabisa ijitambue kwamba ni Wizara ya Mifugo na Maendeleo ya Uvuvi na siyo Wizara ya Mifugo na Kukwaza Uvivu Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nazungumza hivi kwa sababu mengi ambayo wachangiaji wenzangu wamezungumza, niwarejeshe tu katika kanuni za mwaka 2020, kanuni ya 66(1)(d)(f)(g). Vifungu hivi vinakwaza kabisa maendeleo ya uvuvi katika nchi yetu ya Tanzania. Sihitaji nidadavue vinakwaza vipi? Bahati nzuri wachangiaji wenzangu waliotangulia wameelezea. Naomba katika mabadiliko ya kanuni Mheshimiwa Waziri anayokwenda kuyafanya, azingatie haya ambayo kwenye vifungu nivyovitaja yanakwanza uvuvi Tanzania. Hilo la kwanza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, naomba wataalam wa Sekta ya Uvuvi, wanapokwenda kutengeneza kanuni mpya, ziwe ni kanuni shirikishi na pia ziwe ni kanuni zinazoendana na mazingira husika. Kwa mfano, sisi watu wa Pwani, taratibu za uvuvi zinazingatia masuala ya nyakati, nyakati za pepo na miandamo ya miezi. Kwa mfano, unapokataza watu wasivue mchana kwa ujumla wake tu, wakati taratibu za uvuvi wa baharini zinazingatia mwandamo wa mwezi, kuna kipindi cha mwezi mchanga, kuna kipindi cha mwezi mpevu, kuna kipindi cha mwezi mwangavu, hilo lizingatiwe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine kuna hawa samaki maarufu kama Kambakochi au Kambamiti. Kule Kilwa ni tofauti na Rufiji ambapo Kilwa uvuvi wa Kambakochi unatakiwa uanzie mwezi Januari, lakini leseni ambazo Wizara inatoa inaanzia mwezi Aprili. Maana yake ni kwamba mpira unapigwa huku, golikipa anaangukia huku; tofauti kabisa. Hapa tunaomba izingatiwe pia, ndiyo maana tunasema kwamba sheria hizi na kanuni hizi ziiwe shirikishi, ziulize wazoefu wa maeneo husika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo ninaomba ni kukuza Sekta ya Uvuvi na hususan katika Sekta ya Wilaya ya Kilwa, ni kuhakikisha kwamba pale Kilwa Kivinje ambapo nimejiridhisha kabisa samaki wengi ambao wanaliwa Tanzania wanatoka Kilwa; ukiona samaki wanaliwa Dar es Salaam wanatoka Kilwa, ukiona samaki wanaliwa mikoa mingine ya Kusini, wenzetu jirani zetu Mtwara na Ruvuma wanatoka Kilwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushahidi wa hili wale ambao wanatumia barabara hii maarufu kama ya Kibiti - Lindi, ukifika pale Somanga, ukinunua samaki unakuja Dar es Salaam au unakwenda Mtwara au unakwenda Ruvuma maana yake hao ndiyo samaki wa Kilwa. Kama hivyo ndivyo, kuna haja ya kuanzisha soko la samaki la kisasa pale Kilwa Kivinje ili wavuvi wetu wawe na uhakika wa soko. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitoe taarifa tu kwenye Wizara hii, katika utaratibu usio rasmi jirani zetu wa Kongo wanakuja Kilwa kununua samaki tani za kutosha. Tumeandaa utaratibu gani wa kuingiza mapato ya Taifa kwa kuuza samaki nje ya nchi? Tuko katika utaratibu usiosimamiwa vizuri na Wizara. Nashauri katika eneo hili, Wizara isimamie inavyotakiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine Mheshimiwa Waziri, matumizi ya nyavu zilizozuiliwa. Kimsingi nyavu hizi, wananchi wetu wavuvi hawa masikini wa Tanzania wanavua kulingana na aina ya samaki wanaovua. Kwa mfano, dagaa wote tunawafahamu, wanahitaji milimita kumi. Wote tunajua dagaa ni visamaki vidogo vidogo sana, vinahitaji milimita sita, ikizidi milimita saba. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tangu kumetolewa zuio la kukataza zuio la kukataza uvuvi wa nyavu hizi, uvuvi wa mchana, wavuvi wetu wamebaki kuwa masikini, wamechomewa nyavu zao, wamechomewa vyombo vyao, vimeangamizwa, hii ni msiba mkubwa katika Taifa hili na siyo haki kufanya katika nchi ambayo iko huru. Malengo na matarajio ya Watanzania ni kuona kwamba kila sekta inasaidia wahusika. Kama ni Sekta ya Kulima isaidie wakulima, Sekta ya Uvuvi isaidie wavuvi, Sekta ya Ufugaji isaidie wafugaji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sihitaji nizungumzie kilio cha Wana-Kilwa cha kuchomewa nyavu zao, kuangamiziwa vyombo vyao vya uvuvi, kilichofanywa huko na Waziri ambaye amemaliza muda wake. Nina matarajio mazuri na Mheshimiwa Waziri wewe kaka yangu, hautafanya kama mwenzako aliyekutangulia. Utakuwa ni msikivu, utakuwa ni mwenye huruma kwa Watanzania masikini hususani wavuvi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, niseme tu kwamba katika mpango wa Wizara wa kuanzisha bandari za uvuvi, nimeona imetajwa Mbegani hapa, lakini mwanzoni Kilwa ilikuwa kwenye mpango. Tunaomba mpango huu kwa miaka mitano hii, Kilwa isisahaulike. Kilwa Masoko pale kuna kina cha kutosha, kuna bandari ya asili. Kwa hiyo, ule mpango wa miaka mitano ubaki vile vile. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. (Makofi)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Hesabu za Serikali kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Hesabu zilizokaguliwa za Serikali Kuu, Mashirika ya Umma na Kaguzi za Ufanisi kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021, na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Hesabu za Serikali za Mitaa zilizokaguliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021, na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kuhusu Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021
MHE. ALLY M. KASSINGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipatia nafasi ili nami jioni ya leo nichangie hoja zilipo mezani. Pia kwa upekee wake nitajikita zaidi kwenye hoja ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) kama ambavyo imebainisha na taarifa ya CAG kwa hesabu za kuishia Juni, 2021.

Mheshimiwa Mwenyekiti, siku ya leo nitakuwa na hoja kubwa mbili tu. Hoja ya kwanza ni uwezo wa halmashauri zetu katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo. Kwa mujibu wa taarifa ya CAG kumekuwa na changaomoto katika kutekeleza miradi ya maendeleo katika mamlaka zetu za Serikali za Mitaa, na kwa ridhaa yako naomba nitoe mifano michache;

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikianza na Halmashauri ya Mji wa Newala, sekta ya elimu peke yake Shule ya Msingi Lidumbe mradi wa nyumba ya mwalimu umetelekezwa tangu mwaka 2015. Shule ya Msingi Mnaida, mradi wa nyumba ya mwalimu umetelekezwa tangu mwaka 2012. Shule ya Msingi Mcholimbili, mradi wa nyumba ya mwalimu tangu mwaka 2018.

Mheshimiwa Mwenyekiti, halmashauri ya Wilaya ya Bumbuli, madarasa 25 yametelekezwa, nyumba za walimu 37 zimetelekezwa, maabara 26, zahanati 12 na mabwalo ya chakula mawili. Halmashauri ya Kasulu miradi 34 ambayo imeanzishwa na jamii imetelekezwa, haikuweza kukamilishwa. Nimalizie kwa mifano michache na halmashauri ya Kigoma Ujiji, kati ya miaka mitatu hadi kumi na moja, miradi yenye thamani ya shilingi 1,251,000,000/= imetelekezwa bila kukamilishwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nini maana yake hapa? Maana yake ni kwamba, fedha za Watanzania walipa kodi zimeangamizwa bila kuleta tija yoyote. Jambo kama hili, sisi kama wabunge, wawakilishi wa wananchi ambao ndio walipa kodi haipaswi kulinyamazia. Hapa tumezungumzia fedha ambazo zimeingizwa kwenye miradi hii ya muda mrefu ambayo haikukamilika na haitumiki. Maana yake ni kwamba fedha za Watanzania zimekwenda bila kuleta tija. Hilo ni eneo la kwanza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, chanzo kikubwa ni kwamba halmashauri zetu hatujazijengea uwezo katika maeneo mawili; eneo la kwanza ambayo ni usimamizi na eneo la kutoa ruzuku kwa halmashauri zetu katika kutekeleza miradi ya maendeleo. Baadhi ya Wabunge hapa wamechambua, kwamba kumekuwa na uwiano usioridhisha wa kutoa ruzuku za miradi ya maendeleo katika halimashauri zetu. Zipo halmashauri ambazo zimepata ruzuku zaidi ya asilimia 100 na zipo ambazo zimepata ruzuku chini ya asilimia 40, kwa mujibu wa taarifa ya CAG. Hii imesababisha ndio matokeo ya miradi zaidi ya miaka minane, imetelekezwa na haina tija yoyote.

Mheshimiwa Spika, jambo la pili ambalo ni matokeo ya haya ni usimamizi usioridhisha wa mamlaka zetu za Serikali za mitaa kwenye vyombo vyake vya usimamizi. Hapa kwa upekee kabisa niseme, regional secretariat (Sekretarieti za mikoa). Kimsingi, kwa utendaji usioridhisha wa halmashauri zetu, mtu wa karibu kabisa ambaye ndiye mkono wa karibu wa ofisi ya Rais, TAMISEMI wa kusimamia ni Ofisi ya Mkuu wa Mkoa chini ya Sekretarieti ya mkoa. Lakini, ni kiwango gani sekretaieti zetu za mikoa tumeziweshesha kusimamia halmashauri? Ni kwa kiwango gani watendaji pamoja na maafisa waliopo pale kwenye sekretarieti za mikoa wamejengewa uwezo wa kusimamia Mamlaka zetu za Serikali za Mitaa.? Ni kwa kiwango gani mamalaka zetu za sekretarieti za mikoa watendaji wake wamekuwa na uzoefu wa kutosha wa usimamizi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa. Hili ni janga na ni jukumu la Serikali kuliangalia eneo hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la pili mahsusi ambalo ningependa kulitolea uchambuzi katika taarifa hii ni mfumo wa ukusanyaji wa mapato. Halmashauri 46, kwa mujibu wa taarifa ya CAG zenye POS 1,355 hazikuwa katika mfumo wa kukusanaya mapato mpaka ripoti hii inatolewa. Pia halmashauri nane zilipoteza POS 34 na halmashauri 27 zilifanya marekebisho ya ankara kiasi cha shilingi bilioni moja milioni mia sita na ushee, bila kiambatisho.

Mheshimiwa Mwenyekiti, huko nyuma kulikuwa na utaratibu katika halmashauri zetu, watendaji wasio na nia njema ya nchi hii kuiba fedha za wananchi wakati tukitumia mfumo wa stakabdhi za kuandika kwa mikono maarufu kama HW5. Kulikuwa na utaratibu wa kupoteza vitabu kwa makusudi wakati tayari fedha zimekusanywa, halafu watendaji wasio na nia njema walikuwa wanapiga hizo fedha. Tulipoleta mifumo hii ya ukusanyaji wa fedha kwa njia za kielektroniki tulidhani utakuwa ndio mwarobaini wa kurekebisha mapungufu haya. Badala yake watendaji hao hao wasiokuwa na nia njema na nchi yetu, wamekuwa wakitumia mifumo hii hii ya kielektroniki, kwa maana ya mashine za kukusanyia mapato lakini bado wanapiga kwa namna hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, unapoambiwa kwamba halmashauri nane zilipoteza POS maana yake ni kwamba walikusanya halafu fedha za Watanzania zikaenda mifukoni mwa watu binafsi halafu baadaye wanasema POS zimepotea. Hili ni jambo ambalo haliwezi likakubalika. Pia tunaambiwa kwamba katika halmashauri ambazo zimakaguliwa na CAG kwa taarifa ya kuishia Juni, 2021 kiasi cha shilingi bilioni 17 za mapato zilikusanywa na POS lakini hazikupelekwa benki. Maana yake ni kwamba zilibaki kama fedha mbichi na zilitumika zikiwa fedha mbichi bila kupelekwa benki. Sasa haya mambo ni msiba mkubwa sana katika taifa hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwasababu hiyo nilikuwa na mapendekeo yafaatayo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kwanza, kama nilivyosema, kwamba haya yote ni matokeo ya mifumo ya usimamizi isioridhisha. Kwa hiyo jukumu la kwanza kabisa ni kuimarisha mfumo wetu wa usimamizi hususani kuimarisha eneo lile la regional secretariat ili Ofisi ya Rais TAMISEMI isipate shida sana, kwamba Maafisa wa TAMISEMI kuhangaika kuwa wanashuka kwenye halmashauri. Tuna halmashauri 184 nchi nzima, watumishi au maafisa wa Wizara hawatoweza kutosheleza kuzunguka kwenye halmashauri 184 kwaajili kutoa au kujenga uwezo kwa watendaji wetu au kusimamia miradi. Jukumu la regional secretariat ni kuisaidia Ofisi ya Rais TAMISEMI, kwa maana ya Wizara, kwa niaba yake, kuzisimamia hizi halmashauri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia uwezo wa kiutendaji na wa kiuzoefu wa maafisa waliopo kwenye regional secretariat zetu unakuwa si kwenye kiwango ambacho wangeweza kuzisimamia halmashauri hizi.

Mheshimiwa Mwenyekti, jambo lingine ambalo nimeliona ni changamoto na nipendekeze hapa ni muundo wenyewe uliopo kati ya watendaji wa halmashauri na muundo wa regional secretariat.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi karibuni Ofisi ya Rais TAMISEMI ilipitisha muundo ambao ulinakwenda kutekelezwa na watendaji wetu wa halmashauri lakini muundo huu kimsingi si muundo ambao ulikuwa shirikishi. Sisi kama Madiwani, Wabunge hatukushirikishwa katika kupendekeza muundo huu. Hata hapa Bungeni sidhani kama kulikuwa na semina ya kuonesha kwamba tunaenda kutekeleza nuundo huu. Sasa tunapotekeleza muundo ambao umetoka juu na kushuka tu kutekelezwa kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa bila kuhusisha wadau wakaingiza inputs zao matokeo yake ndiyo haya ambayo CAG anakuja kuyaibua. Utaratibu huu wa mapungufu ya kiutendaji na usimamizi yataendelea kuwa ni mwiba katika nchi hii mpaka pale ambapo muundo wa usimamizi utakapokuwa umekaa vizuri.

Mhehimiwa Mwenyekiti, naomba kuunga mkono hoja.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2021 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2021
MHE. ALLY M. KASSINGE: Mheshimiwa Spika, ahsante awali ya yote niungane na wenzangu kukupongeza wewe kwa kuchaguliwa na Bunge hili kuwa Spika wetu na kwa kweli sisi Wabunge tuna imani kubwa. Tunaomba Mungu akusimamie. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya pongezi hizo ambazo pia zimfikie Mheshimiwa Zungu Naibu Spika, nianze sasa kwa kuchangia hoja au taarifa ya Kamati ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) kama ambavyo imewasilishwa na Mwenyekiti wetu, mama Grace Tendega, ikiwa ni hesabu za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali katika Mamlaka za Serikali za Mitaa kuishia mwezi Juni, 2020. Ni ukweli kwamba Serikali imekuwa na juhudi za dhati kabisa kupeleka fedha katika Mamlaka za Serikali za Mitaa, kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ikiwemo sekta ya afya, sekta ya elimu na sekta nyinginezo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia kumekuwa na utaratibu wa kupeleka fedha kwa utaratibu wa flat rate kwa kila halmashauri, kwa mfano, Serikali imekuwa ikipeleka fedha kwa ajili ya ujenzi wa mabweni kwenye shule zetu za sekondari. Hapo awali ilikuwa ni Shilingi milioni 75 na baadaye ikawa ni shilingi milioni 80, lakini kumekuwa na namna tofauti tofauti katika utekelezaji wa eneo hili.

Mheshimiwa Spika, katika baadhi ya halmashauri Shilingi milioni 80 imetosheleza kabisa kujenga bweni moja la wanafunzi kukaa idadi ya watoto 80 ikiwemo facilities za ndani ya bweni hilo, kwa maana ya vitanda, lakini katika baadhi ya halmashauri shilingi milioni 80 hazijatosha na hakuna ambacho kimefanyika na kazi haina viwango. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika hili nina maeneo mawili ya kuzungumzia. Eneo la kwanza ni kuwapongeza wale ambao kwa dhati kabisa wamefanya vizuri ikiwemo, halmashauri ya Wanging’ombe ambayo ni Jimbo la Mheshimiwa Festo Dugange. Wamejenga shule, wamejenga mabweni kule katika Sekondari ya Wanging’ombe, wamejenga bweni katika Sekondari ya Wanike kwa Shilingi milioni 75 na imetosheleza hakuna namna yoyote ya harufu ya ubadhirifu wa fedha. Hata hivyo, katika halmashauri zingine shilingi milioni 80 imezama, mabweni hayajakamilika, vitanda hakuna na bado fedha haitoshelezi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hiki ni kiashiria tosha kabisa kuna mazingira ya dalili ya matumizi mabaya ya fedha hizi za umma. Katika hili niseme pia kwamba Serikali imekuwa ikipeleka fedha hizi bila kufanya tathmini ya kina. Katika maeneo mengine ni kweli kumekuwa na dalili za ubadhirifu lakini katika mazingira mengine ambapo facilities zote ikiwemo bidhaa za madukani, zinapatikana kwa urahisi na zile bidhaa ambazo zinapatikana kwenye mazingira halisi ikiwemo mchanga, mawe, kokoto zinapatikana, bado fedha hizi hazijatosha.

Mheshimiwa Spika, sasa niseme tu kwamba wakati Serikali ili kuzipunguzia mzigo wa hoja halmashauri zetu, zinapeleka fedha hizi kwa utaratibu huu wa flat rate, zingefanya kwanza tathmini ya kimazingira ili kujua kila halmashauri na kila maeneo yanahitaji shilingi ngapi? Kwa mfano, katika baadhi ya halmashauri zimekuwa mbali na maeneo ambayo bidhaa za viwandani zinapatikana. Huwezi ukapeleka utaratibu wa flat rate na wakafanya kama vile ambavyo wangeweza kufanya vingine kwa vizuri zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kutoa ushauri huu, niunge mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)
Azimio la Bunge la Kuridhia Itifaki ya Mkataba wa Umoja wa Nchi Huru za Afrika wa Kuzuia na Kupambana na Ugaidi ya Mwaka 2004
MHE. ALLY M. KASSINGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru nami kwa kupata nafasi hii ya kuweza kuchangia hoja iliyopo Mezani inayohusu Itifaki ya Mkataba wa Umoja wa Nchi Huru za Afrika ya Kuzuia na Kupambana na Ugaidi ya Mwaka 2004.

Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote nami nipongeze sana Wizara hii, nikianza na Mheshimiwa Waziri, ndugu yangu, Mheshimiwa Eng. Masauni, kwa kazi nzuri ambayo anaifanya katika Wizara hii; na Naibu Waziri, kaka yangu, Mheshimiwa Sagini, ambao kimsingi sisi kama Kamati tumeshirikiana nao vizuri sana katika kuchakata itifaki hii mpaka leo inawasilishwa hapa Bungeni, nasi Wabunge tunapata nafasi ya kuchangia kwa lengo la kuomba Wabunge wenzetu waweze kuridhia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze na nimshukuru pia Mwenyekiti wangu wa Kamati, kaka yangu Mheshimiwa Vita Kawawa kwa namna ambavyo ametuwakilisha vizuri sisi Wanakamati wenzie katika kuwasilisha yale ambayo tulipokuwa kwenye Kamati ndiyo tumekubaliana kama Maoni ya Kamati ya kuwasilishwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mchango wangu nitakuwa na mambo machache sana ya kuchangia ambayo yataongozwa na swali moja tu kwamba kwa nini sisi Tanzania kupitia Bunge lako hili tuweke Azimio hili la kuridhia itifaki hii. Jambo la kwanza nature ya ugaidi wenyewe. Kimsingi dhana ya ugaidi si dhana ambayo inafanyika katika utaratibu wa kindani kwa maana locally, kinyume chake ni dhana ambayo inavuka Taifa moja mpaka Taifa lingine kwa maana ni dhana ya kimataifa. Kwa maana hiyo, kama ni jambo la kimataifa hatuwezi sisi Tanzania ambao tunajiita nchi iliyo kamili tukabaki wenyewe bila kushirikiana na nchi zingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, sisi Watanzania tukiridhia Itifaki hii, tutakuwa na fursa ya kuweza kushirikiana na nchi zingine za Afrika. Tukumbuke katika wasilisho ambalo Mheshimiwa Waziri amewasilisha hapa ni kwamba nchi 45 za Afrika zimesaini Mkataba huu ikiwemo Tanzania. Katika nchi hizo 45 ni nchi 21 ambazo zimeridhia na kwa maana hiyo sisi Watanzania tukiuungana au tukiridhia tutakuwa tumeungana na nchi zingine za Afrika 21 ikiwa ni pamoja na jirani zetu wa nchi kama za Rwanda, South Africa, Burundi, Lesotho, pamoja na nchi nyingine za Afrika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la tatu, kwa nini turidhie? Itakuwa imetupa nafasi au fursa ya kufanya marekebisho ya Sheria yetu iliyotungwa mwaka 2002, Sura Na. 19 ambayo tunasema ni Sheria ya Kuzuia Ugaidi na kwa maana hiyo tutakaporidhia Itifaki hii tutaweza kuwa na fursa ya kubadilisha Sheria yetu na kuwa Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Ugaidi ambapo sababu sheria zinatungwa hapa Bungeni, Wabunge tutakuwa na nafasi pana zaidi ya kutoa mawanda ya maelezo yetu maana wazoefu katika kuchangia sheria ambayo itakuwa na maslahi kwa nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, kwa nini turidhie? Viashiria vya matukio ya kigaidi ni viashiria ambavyo katika nchi yetu tumeanza kuvisikiasikia kipindi kifupi kilichopita, lakini pia miaka kadhaa imepita nchi jirani siyo tu viashiria badala yake ni matukio ya kigaidi yameweza kutokea. Wote tunakumbua matukio ambayo yametokea Kenya miaka kadhaa iliyopita. Hivyo basi, hatuwezi kuwa salama kama jirani zetu au hata ndani ya nchi viashiria hivi vinatokea na sisi tuone kwamba tuko radhi hatuwezi kuridhia Itifaki hii, tukabaki salama hapana. Niombe sana Waheshimiwa Wabunge tuunge mkono Itifaki hii ili nchi yetu iweze kusaini na kuridhia ili tuungane na nchi zingine za Afrika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. (Makofi)