Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Dr. Amandus Julius Chinguile (16 total)

MHE. AMANDUS J. CHINGUILE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali yetu yenye kutia matumaini lakini bado kwa umuhimu wa barabara hii wananchi wa Jimbo la Nachingwea watapenda kusikia commitment ya Serikali. Kwa kweli, katika hili viongozi wengi wanahukumiwa kutokana na barabara hizi pamoja na mambo mengine. Je, nini commitment ya Serikali juu ya kuanza ujenzi wa barabara hii kwa kiwango cha lami?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, viko vijiji vya Ikungu, Chiola kuelekea Ruangwa, hapa tayari walifanyiwa tathmini na wenzetu wa TANROADS. Watu wa TANROADS walikuja wakafanya tathmini wakiamini kwamba barabara itapita upande wa kulia baada ya muda wakarudi tena wakafanya tathmini upande wa kushoto. Kwa hiyo, hawa wananchi wamezuiliwa kwenye maeneo yale wasifanye maendelezo. Ni lini Serikali itakwenda kutoa ufafanuzi wa jambo hili, ili wananchi wa maeneo yale waweze kuendelea na shughuli zao? Ahsante sana.

SPIKA: Hiyo ni kwa barabara ya Nachingwea – Ruangwa?

MHE. AMANDUS J. CHINGUILE: Mheshimiwa Spika, ndiyo.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali ya nyongeza ya Mheshimiwa Chinguile, Mbunge wa Nachingwea, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, commitment ya Serikali ni kwamba tayari fedha ya awali za kuanza ujenzi kwa kiwango cha lami zimeshatengwa. Pia barabara hii imeahidiwa kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi na pia ni kati ya barabara ambayo Mheshimiwa Rais ameahidi kuijenga kwa kiwango cha lami katika kipindi hiki cha miaka mitano.

Mheshimiwa Spika, swali la pili ambalo ameuliza kwamba kuna wananchi ambao wameshindwa kuendeleza maeneo yao kwa sababu ya watu wa TANROADS waliokwenda kupima, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge wa Nachingwea kwamba suala hili linaendelea kufanyiwa kazi. Naomba kama kuna changamoto yoyote tofauti ambayo pengine mimi nitakuwa siifahamu basi tuwasiliane naye ili niweze kujua changamoto halisi ni ipi.

Mheshimiwa Spika, ahsante.
MHE. AMANDUS J. CHINGUILE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, kuna sintofahamu kwenye Jimbo langu la Nachingwea kuhusu pembejeo. Wizara ya Kilimo ilitoa tamko kwamba msimu huu wa korosho wakulima hawatakuwa na makato yoyote yatakayokatwa kuhusiana na pembejeo hizo. Hata hivyo, karatasi au fomu wanazosaini wakulima wetu kwenye zile AMCOS inaonekana kwamba kuna makato watakuja kukatwa kwa sababu ya kuchukua hizo pembejeo. Nini tamko la Serikali kuhusu suala hili? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, nimekusoma na nimekuelewa.

Mheshimiwa Spika, labda nirudie tena na niseme kupitia Bunge lako Tukufu kuviambia Vyama vya Ushirika vya Mkoa wa Lindi, Mtwara na Pwani, Serikali ya Awamu ya Sita ya Mama Samia Suluhu Hassan, imetoa ruzuku ya shilingi bilioni 61 kuwapa wakulima wa korosho wa maeneo hayo kwa ajili ya majaribio, asikatwe mkulima yeyote hata senti moja tutakapokwenda kwenye msimu.

Niwaombe Wakuu wa Wilaya wahakikishe kwamba hakuna mkulima yeyote anayesainishwa fomu yoyote ya kuonyesha kwamba anadaiwa hata senti moja. Pia nivitahadharishe Vyama vya Ushirika visijaribu kumkata mkulima shilingi 100, itawagarimu. (Makofi)
MHE. AMANDUS J. CHINGUILE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kuniona. Kwanza nipende kuipongeza Serikali kwa kutuletea zaidi ya bilioni 1.9 kwa ajili ya ukarabati mkubwa kwenye Chuo hiki cha Nachingwea:-

Mheshimiwa Spika, swali langu, chuo hiki ni kikongwe, Je, Serikali sasa haioni haja ya kuanzisha kozi maalum ya masomo ya sayansi, ili tuzalishe wataalam wengi, na hasa kwenye masomo haya ya sayansi kwenye Chuo cha Nachingwe?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Spika, kwa vile ametuletea wazo, basi tunaomba tulichukue twende tukalifanyie utafiti, tuangalie uhitaji wa kozi hiyo katika eneo hilo. Iwapo kama Serikali itabaini kwamba, upo huo uhitaji tutaweza kuingiza kwenye mipango yetu. Ahsante.
MHE. AMANDUS J. CHINGUILE Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Katika Jimbo langu la Nachingwea kuna Chuo cha Ualimu lakini hakitoi kozi ya sayansi. Je, Serikali ina mpango gani wa kuanzisha kozi ya sayansi katika chuo hiki cha Nachingwea?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge wa Nachingwea, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kuna Chuo cha Ualimu pale Nachingwea kwa vile Mheshimiwa Mbunge ametoa ushauri, naomba tuuchukue ushauri huu twende tukaufanyie tathmini ili tuweze kuangalia kama kuna uhitaji wa kuanzisha kozi hiyo ya sayansi katika chuo hicho.
MHE. AMANDUS J. CHINGUILE: Mheshimiwa naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri nina maswali mawili ya nyongeza.

Kwa kuwa, kuna baadhi ya vitongoji katika vijiji hivyo havijawekwa kwenye orodha ya mpango wa kuwekewa vitu kwa ajili ya kuchotea maji. Je, Serikali inaweza kupokea maombi mapya sasa maalum kwa ajili ya kuongeza vituo vya kuchotea maji kwenye vijiji ambavyo vimepitiwa na mradi huu?

Swali la pili, miradi mingi kwenye Halmashauri zetu imekwama kwa sababu ya upatikanaji wa mabomba ambayo yananunuliwa kwa pamoja kupitia RUWASA Makao Makuu.

Je, Serikali sasa inatuhakikishiaje kwamba mabomba sasa yanakwenda kupatikana kwa wakati ili kutokukwamisha miradi mingi kwenye Halmashauri zetu?
WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, moja ya jukumu mahsusi na Wizara ya Maji ni kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya maji safi na salama, tunao huu mradi mkubwa ambao unajengwa na kuna baadhi ya vitongoji ameviainisha ambavyo vinahitaji maji, nataka nimhakikishie kukamilika kwa mradi huu na hivyo vitongoji navyo vitapokea kuhakikisha nao wanapata huduma ya maji safi na salama. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara ya Maji kupitia Wakala wa Maji Vijijini ni kuhakikisha tunatatua changamoto ya maji katika maeneo ya vijijini. Tulikuwa na changamoto ya manunuzi na tumepewa ombi na maelekezo ya Bunge ni kuhakikisha manunuzi haya yanafanyika katika maeneo ya Mikoa, tulishakaa na wenzetu wa manunuzi kwa maana ya RUWASA maelekezo ya Wizara ni kwamba manunuzi yote yanatakiwa kufanyika katika Mikoa husika ili kuharakisha utekelezaji wa miradi. (Makofi)
MHE. AMANDUS J. CHINGUILE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa nafasi. Kwa kuwa nchi yetu imejaliwa wahitimu wengi wa vyuo vikuu kila kona wakiwemo kule Nachingwea. Je, Serikali inachukua vigezo gani kuwapeleka

hawa vijana wetu ambao wametapakaa nchi nzima huko Israel? (Makofi)
WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge wa Nachingwea, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, cha kwanza hii programu inakuwa coordinated na Serikali kupitia Wizara ya Mambo ya Nje kwa kushirikiana na taasisi ya Ministry Affairs ya Israel for International Development and Corporation. Mara nyingi Serikali huwa inatoa window na huwa kuna utaratibu maalum ambao unatumika namna ya kuwapata vijana wanao-apply na kuweza kwenda kushiriki katika windows za namna hii.

Mheshimiwa Spika, tumekutana na ubalozi wa Israel hivi karibuni na kujadiliana nao namna ya kuboresha huduma ya kuwapata vijana, kwa sababu wapo vijana ambao wana apply kwa ajili ya kwenda kufanya jambo A, wakifika kule wanajikuta wamekuwa committed kufanya jambo lingine tofauti na kile ambacho walitarajia. Tumeongea na Ubalozi wa Israel, tunaendelea nao na mazungumzo tukishirikiana na Wizara ya Mambo ya Nje, badala ya kuwasafirisha hao vijana. Tunavyo vituo vingi katika nchi yetu. Ushirikiano ule wa utalaam tuweze kuutumia ndani ya nchi na waweze kuja kutusaidia ndani ya nchi yetu. (Makofi)
MHE. AMANDUS J. CHINGUILE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Jimbo la Nachingwea lina kata 36, kati ya hizo kata mbili hazina watendaji wa kata, lakini lina vijiji 127 na vijiji 37 havina watendaji wa vijiji. Na kwa kuwa tunajua watendaji hawa ndio wanaosukuma shughuli zote za maendeleo katika maeneo yetu;

Je, ni lini Serikali itatoa vibali kwa ajili ya kupata hawa watendaji ambao watatusaidia kwenye maendeleo kwenye maeneo yetu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu kata mbili ambazo hazina watendaji na vijiji 37 ambavyo havina watendaji kule Nachingwea ni adhma ya Serikali kuhakikisha kwamba kila kata, kila kijiji kina watendaji. Kadri ya bajeti itakavuoruhusu basi viabali hivi vitaendelea kutolewa. Na nikutaarifu tu Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali iko mbioni kuajiri watendaji wa kata katika kata zote ambazo ziko wazi nchini. Kwa hiyo ni kuvuta Subira, nikuhakikishie kwamba hilo linafanyiwa kazi.
MHE. AMANDUS J. CHINGUILE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Kwa kuwa nchi yetu kwa sasa ina wahitimu kila kona, na kwa sasa kwa sababu mfumo ulioko wa kuomba ajira una changamoto na una manung’uniko mengi.

Je, Serikali iko tayari sasa kupitia mfumo huu wa sasa ili kupeleka kwenye kila Jimbo idadi sawa ambayo itakwenda kutibu sasa tatizo hili la manung’uniko ambalo kwa kweli kila kona lipo? (Makofi)
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA N AUTAWALA BORA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali hili halitofautiani nalile lililoulizwa na Mheshimiwa Mtemvu, tofauti ni kwamba Mheshimiwa Mtemvu kasema Wilaya lakini Mheshimiwa Mbunge kasema Jimbo. Kama nilivyosema tunaendelea kufanya utafiti kwa kutumia mifumo lakini na uhalisia wa jambo lenyewe kama tunaweza tukalitekeleza katika usahihi sana kinyume na utaratibu wa sasa wa kushindanisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama kuna upungufu kwenye kushindanisha au kama hakuna uwazi wa kutosha kwenye kushindanisha inaweza ikawa kazi nyepesi zaidi kushughulikia kuliko kutafuta mfumo utakaoweza kuja na majawabu haya. Hata hivyo, katika jibu langu la msingi nimesema kwamba tutajitahidi kuandaa, tumeunda timu ambayo inaendelea kufanya utafiti hata sasa wako kazini watatuletea majawabu ya namna gani tunaweza kufanya yote mawili mfumo na uhalisia ili tuweze kuona manung’uniko haya yanakwisha kabisa. (Makofi)
MHE. AMANDUS J. CHINGUILE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi.

Tarafa ya Ruponda katika Wilaya ya Nachingwea haina Jengo la Mahakama ya Mwanzo; je, ni lini Serikali itajenga Jengo la Mahakama ya Mwanzo kwenye Tarafa hii ya Ruponda iliyoko Makao Makuu ambayo yako kwenye Kata ya Ruponda? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Spika, naomba sasa nijibu swali Mheshimiwa Amandus Chinguile, Mbunge wa Nachingwea, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Tarafa hii ya Ruponda ambako Mheshimiwa Mbunge ametamka, iko kwenye mpango wetu wa bajeti. Kwenye zile Mahakama 60 tunakwenda kujenga Mheshimiwa Mbunge, na tunafahamu ina umbali wa zaidi ya kilometa 14 kufuata huduma eneo lingine. Kwa hiyo, liko kwenye mpango tumeweka. Ahsante. (Makofi)
MHE. AMANDUS J. CHINGUILE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa mfumo wa ajira ulioko sasa una manung’uniko mengi; Serikali haioni iko haja sasa ya kupitia mfumo wenyewe kwa ujumla ili uwe rafiki kwa vijana wetu walioko? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Amandus kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, wakati tunawasilisha bajeti ya Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora, hoja anayoeleza Mheshimiwa Mbunge ilitolewa pia katika kikao kile na yalikuwa ni makubaliano ya Bunge lako kwamba tutayachukua mawazo mazuri yale na kwenda kuyafanyia kazi, na haya yote yatakapokuwa yamekamilika basi yatakuja kuonekana katika sera na sheria ambazo baadae nafikiri zinaweza zikabadilika kutokana na mawazo mazuri ya Bunge lako.

Mheshimiwa Spika, nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba maagizo ya Bunge yanaendelea kufanyiwa kazi, na tutakapokuwa tayari tutakuja kuleta taarifa katika utaratibu wa vile vikao vyetu.
MHE. AMANDUS J. CHINGUILE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi na mimi niulize swali la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, barabara ya Masasi – Nachingwea yenye kilometa 45 upembuzi yakinifu na wa kina umefanyika zaidi ya miaka tisa iliyopita. Ni lini Serikali itaanza ujenzi sasa barabara hii kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, ahsante, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Chinguile, Mbunge wa Nachingwea, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli barabara hii ambayo inaunganisha Wilaya ya Masasi na Wilaya ya Nachingwea, kwa maana ya Mikoa wa Mtwara na Lindi, ni muhimu sana. Nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba barabara hii kama bajeti ambayo tunategemea kuiwasilisha wiki ijayo itapita, ipo kwenye mpango kwa ajili ya kuanza ujenzi kwa kiwango cha lami. Ahsante. (Makofi)

MHE. AMANDUS J. CHINGUILE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Jengo la Mahakama ya Wilaya ya Nachingwea ni chakavu na limejengwa tangu enzi za wakoloni. Je, nini mpango wa Serikali wa kujenga jengo jipya litakaloendana na hadhi ya Wilaya?
NAIBU WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Spika, ninapenda kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge wa Nachingwea kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwamba ni kweli kama nilivyoeleza kwenye swali ambalo nimetoka kulijibu muda siyo mrafu, tunayo majengo ambayo yamechakaa lakini tunayo majengo ambayo yamekosa hadhi, kwa maana ya uhalisia wa miradi tuliyonayo kwa mwaka huu ambao unakwenda kumalizika tulikuwa tulikuwa na miradi 22, mwaka ujao tutakuwa na miradi 13 na inawezekana kabisa katika mwaka ujao ukawa umeingia kwenye mpango wa kuangalia uwezekano wa kujengewa Mahakama nyingine. Kwa hiyo, naomba tu Mbunge awe na utulivu katika kipindi hiki kwa sababu miradi yote mpaka kufikia 2025 tutakuwa tumekamilisha majengo yote ya ngazi ya Wilaya asante.
MHE. AMANDUS J. CHINGUILE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi na mimi niulize swali la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, kwenye Jimbo langu la Nachingwea kuna viwanda viwili ambavyo kwa muda mrefu havifanyikazi; Kiwanda cha Lindi Pharmacy lakini pia Kiwanda cha Mafuta Ilulu.

Nini mpango wa Serikali kufufua viwanda hivi ili viweze kuzalisha ajira kwa vijana wetu? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UWEKEZAJI, VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge wa Nachingwea kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli Serikali kupitia ubinafsishaji tulibinafsisha viwanda 156 lakini katika viwanda hivyo viwanda 88 ndiyo vinafanyakazi vizuri, 68 vilikuwa havifanyikazi vizuri na moja ya maeneo ambayo tumekwishayafanyia kazi ni kuvirudisha baadhi ya viwanda ambavyo vipo 20, mojawapo vikiwa hivi viwanda viwili ambavyo alivitaja Mheshimiwa Mbunge, Kiwanda cha Mafuta Ilulu na kile kingine cha kubangua korosho cha Nachingwea.

Mheshimiwa Spika, lakini katika hatua za awali tumeshafanya tathmini viwanda hivi ni kati ya viwanda ambavyo tutaviweka katika maeneo ya uwekezaji kwa ajili ya kuzalisha bidhaa kwa ajili ya mauzo nje (SEZ).

Kwa hiyo, tayari tumeshachukua hatua mbalimbali na sasa tunaendelea kutafuta wawekezaji ambao tutashirikiana nao, ili wazalishe bidhaa aidha za mafuta au kubangua korosho kama ilivyokuwa awali kwa ajili ya kuuza nje. Kwa hiyo, tayari tumeshachukua hatua kwamba hivi vitakuwa chini ya maeneo huru ya uwekezaji kwa ajili ya mauzo nje na hivi viwanda vitafufuliwa tutakapopata mwekezaji mapema iwezekanavyo. Nakushukuru sana. (Makofi)
MHE. AMANDUS J. CHINGUILE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Jengo la Mahakama ya Wilaya ya Nachingwea ni chakavu na limejengwa tangu enzi za wakoloni. Je, nini mpango wa Serikali wa kujenga jengo jipya litakaloendana na hadhi ya Wilaya?
NAIBU WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Spika, ninapenda kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge wa Nachingwea kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwamba ni kweli kama nilivyoeleza kwenye swali ambalo nimetoka kulijibu muda siyo mrafu, tunayo majengo ambayo yamechakaa lakini tunayo majengo ambayo yamekosa hadhi, kwa maana ya uhalisia wa miradi tuliyonayo kwa mwaka huu ambao unakwenda kumalizika tulikuwa tulikuwa na miradi 22, mwaka ujao tutakuwa na miradi 13 na inawezekana kabisa katika mwaka ujao ukawa umeingia kwenye mpango wa kuangalia uwezekano wa kujengewa Mahakama nyingine. Kwa hiyo, naomba tu Mbunge awe na utulivu katika kipindi hiki kwa sababu miradi yote mpaka kufikia 2025 tutakuwa tumekamilisha majengo yote ya ngazi ya Wilaya. Ahsante.
MHE. AMANDUS J. CHINGUILE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Serikali ina mpango gani wa kujenga barabara ya Nanganga – Nachingwea kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Spika, katika jibu la msingi nilisema kwamba barabara ya Nachingwea – Nanganga ipo katika hatua za mwisho na tunategemea katika zile barabara ambazo tunategemea kuzisainia kwa pamoja hiyo barabara ni mojawapo ya Nanganga – Nachingwea. Ahsante.
MHE. AMANDUS J. CHINGUILE: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali lakini nina maswali mawili ya nyongeza. Ziko Leseni zimetolewa kwa ajili ya shughuli za utafiti kwenye maeneo mbalimbali nchini, ikiwemo Jimboni Nachingewa lakini wahusika hawajafanya shughuli hiyo iliyokusudiwa kwa muda mrefu sasa.

Je, Serikali haioni sasa iko haja ya kupitia sheria yetu ili kuweza kuondoa utitiri wa hawa watafiti ambao kimsingi hawatimizi majukumu hayo? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili, je, Mheshimiwa Waziri yuko tayari kuambatana na mimi baada ya kipindi hiki cha Bunge ili kwenda Jimboni Nachingwea kuona halihalisi iliyoko na kuwatia moyo wachimbaji wadogo wadogo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Spika, napenda kumjibu Mheshimiwa Chinguile, Mbunge makini wa Nachingwea, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kuhusu waliopewa leseni na wamezilaza hawazifanyii kazi; mwezi wa tisa na mwezi wa kumi tulitoa kama ndiyo kipindi cha mwisho, waweze aidha kufanyia leseni zao kazi au zifutwe. Tangu tangazo hilo litoke, zaidi ya leseni 7,000 zimeshahuishwa na kuna wale ambao hawajaweza kuhuisha mpaka tarehe 30 mwezi uliopita, mchakato wa kuzifutia hizo leseni unaendelea. Hatukuishia hapo, zilizokwishaharibiwa kwa kutofanyiwa kazi huko nyuma, maeneo zaidi ya 48 zimegawiwa kwa wachimbaji wadogo.

Mheshimiwa Spika, hivyo hata katika jimbo lake, wale ambao watashindwa kuendeleza leseni kwa mujibu wa tangazo hilo la Serikali kupitia Wizara ya Madini, watarudisha hizo leseni na tutawapa wale ambao wako tayari.

Mheshimiwa Spika, kwa swali lake la pili, mimi niko tayari baada ya Bunge hili, nitampangia ratiba. Tutafika huko tuwatie moyo wachimbaji wadogo wanaofanya shughuli zao na kuwahamasisha wengine watumie fursa zilizoko katika Wizara ya Madini kupata uwekezaji ambao utawainua katika Maisha yao. ahsante sana. (Makofi)