Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Dr. Amandus Julius Chinguile (15 total)

Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022
MHE. AMANDUS J. CHINGUILE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia kwenye Mpango wa Serikali. Awali ya yote nimshukuru Mwenyezi Mungu aliyenijalia na mimi kuwa mmoja wa Wabunge wa Bunge hili la Kumi na Mbili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kipekee nikishukuru sana Chama changu Cha Mapinduzi kwa kunipa nafasi ya kuwa mgombea na hatimaye kuchaguliwa na wananchi wa Jimbo la Nachingwea kwa kura nyingi za kishindo.

Nimshukuru sana Mheshimiwa Rais, Mwenyekiti wetu wa chama kwa kazi kubwa aliyoifanya akisaidia na Mheshimiwa Makamu wa Rais na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Wamezunguka nchi nzima kunadi Ilani ya CCM wakishirikiana na viongozi wetu waandamizi wa chama na hatimaye Wabunge wengi tukarudi ndani ya Bunge, wengine kwa mara ya kwanza kwa kishindo kikubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunawashukuru sana. Wengi tumeingia ni kwa matumizi hayo, kwa harakati hizo za viongozi wetu wakuu, lakini zaidi ya hayo kutokana na kazi nzuri iliyofanywa ya kutekeleza Ilani ya Chama Cha Mapinduzi na comrade wetu, jemdari wetu, Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Joseph Magufuli. Pamoja na kazi hiyo nzuri, pamoja na pongezi hizo ambazo nimempatia Mheshimiwa Rais, sasa nijielekeze kuchangia kwenye Mpango huu wa Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye halmashauri nyingi ikiwemo ile ambako mimi natokea, uchumi wetu ni kilimo. Pamoja na Serikali imeelekeza hapa maelekezo yake kwamba, itawekeza zaidi na kuimarisha upatikanaji wa pembejeo, bado nishauri kuna migogoro mingi ambayo iko kwenye maeneo mengi na hasa wafugaji na wakulima. Nikitolea mfano kwa Jimbo langu la Nachingwea kuna mwingiliano mkubwa baina ya wafugaji na wakulima. Niishauri Serikali tutenge maeneo maalum yatakayowawezesha wafugaji kwenda kukaa kwenye eneo ambalo sasa litakuwa na miundombinu yote kwa maana ya maji na malisho badala ya kufanya ufugaji wa sasa wa kuhamahama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, tunapokuwa tunazungumzia kilimo ni eneo mtambuka, wakulima wetu wengi wanalima kilimo cha kizamani sana, wanatumia jembe la mkono. Kwa kweli katika hili niiombe sana Serikali iwekeze vya kutosha ili wakulima wetu waondokane na kilimo kile cha kizamani, waende sasa kuingia kwenye kilimo cha kisasa. Katika eneo hilo basi tuongeze kwenye rasilimali watu kwa maana ya wale wataalamu wetu wa kilimo waende zaidi kwenye vijiji vyetu, wakatoe elimu zaidi na kuwasaidia wakulima wetu ili waweze kulima kilimo cha kisasa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Tanzania yetu ni Tajiri, tuna madini, lakini tuna maliasili ya kila namna, Mwenyezi Mungu ametujalia sana. Katika hili yako maeneo ambayo bado hatujayafanyia kazi kwa upande wa madini. Nikitolea mfano kule kwetu eneo la Nditi, Kiegeyi, bado tumeomba vibali, tumeomba leseni ya uchimbaji kwenye maeneo yale, lakini bado Wizara haijatilia mkazo . Nashukuru Mungu nilizungumza na Mheshimiwa Waziri wa Madini akaniahidi atatembelea kule Nachingwea…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Kengele imegonga Mheshimiwa.

MHE. AMANDUS J. CHINGUILE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana na naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi
MHE. AMANDUS J. CHINGUILE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Nami niungane na wenzangu kumshukuru sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wakati nachangia Bajeti Kuu ya Serikali mwaka 2022 niligusa barabara ya Masasi - Nachingwea na Liwale. Wakati naendelea na mchango, alisimama Waziri wa Fedha, Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, Waziri bingwa kabisa na Mcha Mungu akanipa taarifa ya kwamba haijaondolewa barabara hiyo, bado itajengwa kwa kiwango cha lami. Kadri miezi ilivyokuwa inaenda sasa kwenye ukomo wa mwaka wa Serikali, nilikuwa naendelea kupata shida, lakini leo ninayo furaha, wakati wa bajeti ya Mheshimiwa Waziri, ukurasa wa 11 nimeona ujenzi wa barabara hiyo kwa kiwango cha lami unakwenda kufanyika na mkataba utafanyika kabla ya mwezi Juni 30.

Mheshimiwa Spika, habari hii ni njema kwa wananchi wa Jimbo la Nachingwea. Barabara hii wanufaika siyo tu Jimbo la Nachingwea, ni majimbo manne; Jimbo la Nachingwea, Jimbo la Liwale, Jimbo la Masasi na Jimbo la Ndanda. Kwa niaba ya Wabunge ambao hawatapa nafasi ya kuchangia kwenye bajeti hii wanayotokea kwenye maeneo hayo, tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa jambo hili jema. Barabara hii tulilia kwa miaka mingi, tulisema kwa muda mrefu, tulipiga magoti, lakini leo Mheshimiwa Rais anakwenda kujenga historia kujenga barabara hii. Tunamshukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pili, namshukuru sana Mheshimiwa Waziri wa Ujenzi pamoja na Manaibu wake, pia na Katibu Mkuu anayeshughulikia ujenzi, Mhandisi Aisha na Katibu Mkuu mwingine na Naibu Katibu Wakuu na watumishi wote wa Wizara hii. Tunawashukuru na tunawapongeza sana kwa kazi hii ya kihistoria. Leo wananchi wa Nachingwea wameniambia niseme kwa unyenyekevu mkubwa, tunamshukuru Mheshimiwa Rais na kazi yetu ni kuendelea kumwombea. Sisi mwaka 2025, mguu kwa mguu na Mheshimiwa Rais. Kazi hii ni ya kihistoria na haijawahi kutokea na hatukuwahi kulala usingizini. Jambo hili ni kubwa. Waliniambia nisiseme sana, nisije nikapoteze madhari ya kushukuru. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimeagizwa pia nikumbushe jambo moja ambalo nimekwenda mara kadhaa kwenye ofisi yake. Tunao wananchi ambao walipisha upanuzi wa uwanja wa ndege wa Nachingwea. Namwomba sana Waziri, jambo hili tumezungumza mara kadhaa alifuatilie kwa karibu ili wananchi wale ambao walipisha kwa nia njema upanuzi wa uwanja wa ndege wa Nachingwea, kwa sababu tathmini imeshafanyika waweze kulipwa ili waweze kuendelea na shughuli zao.

Mheshimiwa Spika, kwa unyenyekevu mkubwa, baada ya kusema maneno hayo, kwa niaba ya wananchi wa Jimbo la Nachingwea, nashukuru sana na ninaunga mkono kwa asilimia mia moja.

Mheshimiwa Spika, ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Rais, Tawala Za Mikoa Na Serikali Za Mitaa
MHE. AMANDUS J. CHINGUILE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi na mimi nichangie kwenye Wizara hii Ofisi ya Rais TAMISEMI. Awali ya yote nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa afya lakini pia nichukue nafasi hii kumpongeza pia dada yangu Waziri Mheshimiwa Ummy na Naibu Mawaziri kwa kuaminiwa na Mheshimiwa Rais kuongoza Wizara hizo. Natambua kazi nzuri inayofanywa na Wizara hii ya TAMISEMI kwenye sehemu ya elimu, afya mmefanya kazi kweli kweli tunawapongeza sana.

Mheshimiwa Spika, lakini hata hivyo, wacha nizungumzie kidogo suala la TARURA. Ukiona mtu mzima analia kwakweli kuna jambo. Kwenye suala la TARURA Waheshimiwa Wabunge wengi kila anayesimama analia kuhusu TARURA, TARURA shida, changamoto.

Katika hili niiombe sana Serikali waone namna watakavyokuja na muarobaini kuhusu TARURA. Lakini TARURA hii nitaizungumzia kwenye maeneo mawili, la kwanza kwenye muundo wenyewe wa TARURA. Yuko mtu anaitwa mratibu anakaa pale Mkoani, yeye ndiyo anafanya kila kitu, tender anatoa yeye na kila kitu. Sasa tumemuacha huyu meneja ambaye yuko Jimboni, wilayani ambaye anajua sasa barabara gani ni kipaumbele, yuko hana shughuli yoyote na hata tukizungumzia kwamba anashauri kule mkoani bado anayeshauriwa ana mambo mawili, kukubali au kukataa huo ushauri. Siku ya siku bado mkoani ndiyo wenye mamlaka ya kuongeza wapi kipaumbele. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo jingine ukosefu wa hii bajeti. Kwa kweli mimi niiombe sana Serikali, dada yangu Ummy najua ni mchapakazi sana. Mheshimiwa hebu njoo na muarobaini kuhusu TARURA ni namna gani tunaweza tukaongeza mapato yatakayotuwezesha kufanya kazi kwenye sehemu hii ya TARURA, nikuombe sana na naamini hili kwa uchapakazi wenu kwa uzuri kama mlivyofanya vizuri kwenye maeneo mengine ambayo nimewapongeza. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nizungumzie pia kuhusu watumishi hasa watumishi wa afya na walimu. Huko nako ni shida, sisi tunaotoka pembezoni mwa nchi, hawa watumishi huwa wanaomba maombi ya moja kwa moja kwenda kwenye maeneo yale kwa ajili ya kupata cheque number tu lakini baada ya hapo wote wanaomba kuondoka kwenye maeneo yale.

Mheshimiwa Spika, niiombe sana Wizara, hebu tuwe na mpango maksudi wa kuhakikisha kwamba hao wanaoomba kwenye maeneo yale kwakweli wanakwenda wakiwa na ari ya kufanya kazi na sio tu kwenda kwenye maeneo yale kwa ajili ya kuchukua cheque number. Hapo hapo niendelee pia kushauri Wizara kwamba basi tuwape kipaumbele, wako vijana ambao wametoka na wana-apply kutoka kwenye maeneo yale wameshayazoea. Hebu tuwape kipaumbele, sizungumzii kwamba wale wengine wasipate nafasi, la hasha lakini basi tuone mpango ambao utatuwezesha na sisi tulioko pembezoni mwa nchi kuweza kupata watumishi ambao kwa kweli watakuwa na ari ya kufanya kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo jingine nizungumzie kwenye maboma. Maboma haya yako maboma ya zahanati lakini pia maboma ya shule za msingi na sekondari. Hebu tuuone huu mpango mkakati, kabla ya kuendelea na vipaumbele vipya tuone mpango mahsusi wa kwenda kumalizia haya maboma. Lakini tukifanya hivyo twende sambamba sasa na kuhakikisha vituo vyetu, shule zetu zinakwenda sasa kupata watumishi wa kutosha na hapo niende kule kwangu kwenye jimbo langu la Nachingwea, kuna kituo chetu cha afya Kilimarondo. Mheshimiwa Waziri ikikupendeza, ukipata nafasi twende utembelee eneo lile. Daktari yupo lakini pia na watumishi wengi wapo lakini hawatoshelezi. Eneo lile ni mbali kabisa kutoka Makao Makuu ya wilaya. Tuone namna maeneo yale tunavyoweza kuyapa kipaumbele ili basi waweze kupata watumishi watakaokidhi kwenye maeneo yale. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niendelee kuzungumzia pia suala la Posi, zile mashine za kukusanyia mapato. Huko nako iko shida. Wataalam wetu walio wengi haawana ufahamu wa kutosha na hasa kwenye zile kata. Tujikite kutoa elimu namna gani ya kutumia zile mashine kwa ajili ya kukusanya mapato.

Mheshimiwa Spika, kinachotokea, kwa sababu maeneo mengine wako waliopata shoti kwa namna hii mashine ile hawezi kuitumia vizuri. Badala yake sasa wakati wa kutoa ripoti anakuta anachotakiwa kuwasilisha ni kikubwa kuliko alichonacho. Kinachotokea sasa wanafunika zile posi, anaiweka pembeni anaendelea. Sasa tuwe na mpango huo wa kutoa elimu kwa hawa wataalam wetu kule chini, tunajua wengine hawana taaluma hiyo ya uhasibu. Basi tuwape walau zile kozi ambazo zitawawezesha kupata ujuzi huo. Lakini pia kuhakikisha tunafuatilia kadri inavyowezekana, kadri tunavyopata muda ili mapato yanakusanywa kisawasawa. Kuna mapato mengi yanapotea na nina hakika tukiimarisha kwenye eneo hilo kwa kweli tutafanya vizuri kweli kweli. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wako vijana wengi ambao kwa kweli wanalia. Nikionesha hapa message za simu za kila Mbunge hakuna atakayekuwa anasema mimi sina message ya kijana kutoka kwenye Jimbo langu hana ajira. Mheshimiwa Waziri nikuombe sana, tunajua kwamba kipato chetu tunachokusanya ndicho kinachokwenda kuajiri vijana au ajira mpya. Tuone namna ya kuongeza ajira, vijana wetu wako wasomi, wako huko mashambani, vijijini wanao ujuzi wa kutosha. Tuone namna ya kuwatumia hawa kwa ajili ya maendeleo ya Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, bado niendelee kuzungumzia tena wale walimu au watumishi wanaotoka kutoka maeneo mengine kuhitaji kuhamia maeneo mengine hebu tujaribu namna ya kuyaona hapa. Mheshimiwa Waziri wako watumishi ambao wanataka kutoka Tanga kwenda Nachingwea mahali ambapo tuna shida ya watumishi sasa process zile zinazotumika ili huyu mfanyakazi kurudi kule ambako moyo wake unatamani ni shida.

SPIKA: Ahsante Mheshimia Chinguile.

MHE. AMANDUS J. CHINGUILE: Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja. Nakushukuru sana kwa kunipa nafasi. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maji
MHE. AMANDUS J. CHINGUILE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kuniona na kunipa nafasi na mimi nichangie Wizara hii ya Maji.

Mheshimiwa Spika, nami niwashukuru sana viongozi wetu wa Wizara, kwa kweli Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri vijana mnatuheshimisha sana kwa sababu mnachapa kazi nzuri. Kwa kweli hii inaonesha kwamba vijana wakipewa nafasi wanaweza. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pamoja na pongezi hizo, yako maeneo ambayo na mimi nitayazungumzia kwa jimbo langu; kuna Vijiji vya Namanga, Rweje, Mchangani pamoja na Kiegei, Matekwe na Nakilimalono. Maeneo haya tayari upembuzi yakinifu ulishafanyika na vibali kwa ajili ya uendeshaji wa miradi ya maji kwenye maeneo haya tayari vilishatoka lakini kwa bahati mbaya sana maeneo haya hayajapelekewa fedha. Naomba sana wakati anahitimisha hotuba yake aseme lolote kwa ajili ya maeneo haya.

Mheshimiwa Spika, ukitoka Nachingwea Mjini kuelekea Liwale ni kilometa 5 tu, ukipita nyakati za usiku utakuta moto unawaka siyo wachawi, hawa ni kinamama ambao wanahangaika kuhamia maji, inasikitisha! Maeneo hayo sisi tunakua hali iko hivyo mpaka sasa hali iko hivyo.

SPIKA: Kuhamia maji ndio nini?

MHE. AMANDUS J. CHINGUILE: Mheshimiwa Spika, wanakwenda kwa ajili ya kusubiria maji kwenye vile visima vidogo vidogo. Sijui Kiswahili chake rahisi niseme nini lakini kwa kweli ni kuhemea lakini kwa kweli wana shida kwenye maeneo haya. Hata ukizungumzia kama kuna mafanikio ya maji yamepatikana maeneo haya ni lazima uangalie kushoto, kulia maana hawatakuelewa. Kwa hiyo, nimwombe sana Mheshimiwa Waziri pamoja na juhudi zote ambazo amezifanya maeneo haya kwa kweli yapewe kipaumbele.

Mheshimiwa Spika, yapo maeneo ya Matekwe yana mabwawa ambayo yalichimbwa maalum kabisa kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji lakini mpaka leo kazi ile mahsusi iliyokusudiwa kwenye mabwawa haya haijatekelezwa. Niishauri Wizara badala ya kusubiri mradi huu ambao hatujui utaanza lini wafikirie namna ya kutuma wataalam ili waone maji haya yanapoweza kutumika kwa matumizi ya kunywa kwenye maeneo husika. Maeneo haya ni mbali na maeneo ya mjini, kwa kweli sio tu wanakunywa maji machafu lakini wanakunywa maji ambayo mbuzi, ng’ombe, tembo na wanyama wengine wanatumia. Kwa hiyo, niiombe sana Wizara ipigie mstari wa huruma kabisa kwenye maeneo haya ili wapiga kura wangu wa Jimbo lile la Nachingwea waweze kufaidika pia na miradi hii.

Mheshimiwa Spika, kuna mradi wa maji wa kutoka Masasi kuja Nachingwea lakini kupitia kwenye Kata ya Ndomoni, nashukuru Ndomoni maji yamefika. Hata hivyo, kwenye kata hiyo hiyo kuna eneo lingine ambalo lina watu wengi la Ndomondo na Makitikiti. Nimuombe sana Mheshimiwa Waziri pamoja na mafanikio haya ya mradi huu kuufikisha hapa, aone namna ambavyo atawapelekea maji watu wa maeneo haya ya Ndomondo na Makitikiti. Kwa sasa wanakwenda kilometa nyingi kutafuta maji na hii sasa kwa wale ambao kwa kweli wameoa ni shida. Wapo watu ambao sasa wamekuwa na mapengo baada ya kupewa vipigo na wanaume zao maana anaondoka asubuhi anarudi saa 8 na hii si sawa.

Mheshimiwa Spika, uko mradi wa maji wa Mbwinji umefika Nachingwea, naishukuru sana Serikali lakini tunahitaji huu mradi utanuke kwenye baadhi ya maeneo. Najua Mheshimiwa Waziri anaufahamu vizuri hebu atusaidie ili watu wengi zaidi waweze kupata maji haya safi na salama kutoka kwenye mradi huu wa Mbwinji.

Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo, yako maeneo ambayo wenzetu wa TASAF walishachimba visima vya maji sasa yamebaki mashimo. Namwomba sana Waziri akipata muda twende Nachingwea tukaone maeneo haya, vile visima havijawahi kutoa maji hata siku moja. Tulichoshuhudia ni wale wataalam wa maji waliokuja kuchimba vile visima wametuachia mashimo lakini sio hivyo tu, wametuachia na wapwa zetu kule jimboni. Hatukuhitaji wapwa, sisi tumehitaji maji! (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Spika, haya nayazungumza kwa uchungu kwa sababu yako mashimo, unafika kijijini unakuta mashimo manne matano na yote hayajatoa maji. Hii ni hasara kwa Serikali. Waziri naomba twende kwa pamoja tujue ni nini kilichotokea maeneo haya.

Mheshimiwa Spika, najua huu muda umenipa wa ziada lakini kwa kweli inasikitisha sana ningepata muda mrefu ningezungumza mambo mengi ungejiuliza haya mambo yanafanyika Tanzania au lah! Nimuombe Waziri tukiambatana pamoja na mimi kwa kweli atakwenda kujionea mwenyewe. Haya mambo yapo, pamoja na kuwasifu kwa kweli mnafanya kazi nzuri twende tukakamilishe kazi hii ambayo kwa kweli taifa linatutegemea sana.

Mheshimiwa Spika, ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto
MHE. AMANDUS J. CHINGUILE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Awali ya yote nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa zawadi ya uhai. Pia niwashukuru wananchi wa Jimbo la Nachingwea kwa namna wanavyonipa ushirikiano tangu wamenichagua kuwa Mbunge wao na nawaahidi sitawaangusha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nijielekeze moja kwa moja kwenye mchango wangu kwa Wizara hii ya Afya. Tunayo changamoto ya watumishi wa afya, kwa mfano kwenye Halmashauri yangu ya Jimbo la Nachingwea, mahitaji ni watumishi 1,077 na waliopo ni 305, upungufu ni 772, hatuwezi kufanya kazi kwa namna hii.


Mheshimiwa Naibu Spika, kwa namna hiyo nichukue nafasi hii kuwapongeza sana watumishi wa afya wa Jimbo la Nachingwea kwa kazi nzuri wanayoifanya pamoja na upungufu wao huo. Mahitaji ya Hospitali ya Wilaya ya Nachingwea ni watumishi 256. Mpaka sasa wako 169, sasa hawa 136 wanakwenda sasa kugawana kwenye zahanati 35 na vituo vya afya vitatu, haiwezekani! Niiombe sana Wizara kwenye hili waone namna watakavyokuja na mpango wa kutatua changamoto hii ya watumishi wa afya.

Mheshimiwa Naibu Spika, niishukuru sana Wizara walitujengea jengo zuri pale walituletea milioni zaidi ya 400 kwa ajili ya jengo zuri la Mama na Mtoto kwenye Hospitali yetu ya Wilaya ya Nachingwea. Pia walituletea milioni 200 kwa ujenzi wa Kituo cha Afya cha Naipanga, nawashukuru sana. Pamoja na shukrani hizi jengo lile la mama na mtoto ni zuri, lakini mpango wake ni kupatikana kila Idara, Idara ya upasuaji jengo ni tupu halina kifaa hata kimoja.

Mheshimiwa Naibu Spika, niiombe sana Wizara na nimezungumza mara kadhaa na Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri, wameniahidi, lakini basi angalau wakija kuhitimisha waseme lolote ili wananchi wale wa Jimbo la Nachingwea waweze kupata faraja. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunayo changamoto ya ambulance. Ambulance tunayoitegemea sasa ni ya Kituo cha Afya Kilimarondwa ambacho ni kilometa 96 kutoka kwenye Hospitali ya Wilaya. Ile ambulance ya wilaya pale ni mbovu haiwezi tena kuendelea na kazi. Sasa tufikirie kwamba ambulance inatoka kilometa 96 inakuja kutoa huduma katikati ya Wilaya ambapo ni umbali na barabara ni ya vumbi. Kwa kweli Wizara ione namna itakavyotusaidia kwenye Jimbo hili la Nachingwea ili na sisi tupate ambulance. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na yote niendelee kuishauri Wizara, wenzangu wamesema hapa, sasa hivi tunalo ongezeko kubwa sana la magonjwa ya saratani na hasa ya shingo ya kizazi, lakini pia na magonjwa ya ini. Hebu tuone namna ambavyo wataalam wanaweza kufanya utafiti ili kubaini chanzo cha ongezeko la magonjwa haya kwa sasa ni nini, ili basi tuweze kutoa elimu kwa wananchi wetu na kwa hiyo tutapunguza wagonjwa wanaohitaji sasa kupata huduma kwenye maeneo haya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nijielekeze zaidi kwenye magonjwa ya malaria kipindi kilichopita tuliendelea kutoa elimu kubwa sana kwenye magonjwa haya kupambana na ugonjwa huu wa malaria. Sasa ni kana kwamba tumepunguza speed, niiombe Wizara turudi, kulikuwa na mipango hapa ya kugawa neti na vitu vingine, ile mipango bado iwe endelevu. Yapo maeneo ambayo kama hatutapeleka elimu ya kutosha bado wananchi wetu ni kana kwamba wanasahau.

Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru sana na naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi
MHE. AMANDUS J. CHINGUILE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi, pamoja na kazi nzuri inayofanywa na wizara yetu ya Ujenzi, nichangie kwenye eneo la barabara ya Kibiti - Lindi, barabara hii haina muda mrefu lakini kwa sasa ina maeneo korofi kweli kweli niombe wizara ifanye kadri inavyoweza ili yapitie maeneo haya na kuyarekebisha mara moja. Maeneo haya Mbwemkuru, Malendego mpaka Nangulukuru kipande hiki ni kibovu kweli kweli na kinaweza kikasababisha ajali endapo hazijachukuliwa hatua za makusudi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninzungumzie eneo la barabara za kutoka Nangulukuru kwenda Liwale, Liwale – Nachingwea, Nachingwea – Ruangwa, Ruangwa - Nangulukuru. Maeneo haya yamedumaa kwa sababu pamoja na mambo mengine ni hali ya barabara ya maeneo haya, tukijengewa barabara maeneo haya hata kiuchumi yatakwenda kuimarika.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa kwa masikitiko makubwa niendelee kusema tu kwamba maeneo haya tunazalisha korosho kwa wingi, tunazalisha ufuta kwa wingi, lakini barabara zake ni mahandaki. Niombe sana sana wizara iweke upendeleo maalumu kabisa. Mheshimiwa Mbunge wa Liwale hapa amezungumza, amezungumza jana tena kwa hisia kali kabisa, kwa kweli ipendeze baada ya Bunge hili au wakati Bunge linaendelea Mheshimiwa Waziri aende akatembelee haya maeneo akajionee mwenyewe. tunachokizungumza tunamaanisha watu wetu wanapata shida kweli kweli. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa kwa unyenyekevu mkubwa nizungumzie kipande cha barabara kutoka Masasi kwenda Nachingwea. Wakati tunafunga kampeni za uchaguzi mwaka jana aliyekua Rais wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli hayati alizungumza na wapiga kura wa Jimbo langu la Nachingwea kwa njia ya simu na kati ya vitu alivyowaahidi ni barabara hii ya Nachingwea kwenda Masasi kwa kiwango cha lami. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kwenye kumbukumbu ya barabara hii upembuzi yakinifu umeshakamilika miaka mitano iliyopita, lakini mwaka 2016 ilitengewa shilingi bilioni moja kwa maana ya kishika kasima hakuna kilichoendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kumi na saba kumi na nane ilitengewa bilioni 3.5 hakuna kilichoendelea 2018/2019, 2019/ 2020 ikatengewa bilioni 1.3, 2020/2021 ikatengewa bilioni 1.4 mwaka huu imewekewa bilioni 1.5. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niombe sana Waziri atakapokuja kujibu hapa kwa kweli nitashika shilingi kama huna maelezo yatakayotoa matumaini ya lini barabara hii itajengwa, na kwenye hotuba yako huku nimeona Mheshimiwa Waziri amesema Serikali inaendelea na kutafuta pesa kwa ajili ya ujenzi wa barabara hii ya Masasi – Nachingwea.

Mheshimiwa Naibu Spika, imetafutwa kwa miaka mitano, upembuzi yakinifu na vitu vingine vimeshakamilika hebu tuchukuwe juhudi za makusudi kwa ajili ya watu wetu hawa. Watu hawa wanajuwa kujiletea maendeleo yao wenyewe lakini kama miundombinu ikiwa ni shida kwa kweli hii haikubaliki. Nitaishikilia shilingi hiyo Mheshimiwa Waziri mpaka mwisho ili nione unawatendea haki wananchi wa Jimbo langu la Nachingwea. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo nizungumzie pia changamoto nyingine ya kipande cha barabara nilichokizungumzia cha kutoka Nachingwea – Ruangwa. Tukumbuke Ruangwa yupo Mheshimiwa Waziri Mkuu anateremka Uwanja wa Ndege wa Nachingwea hii barabara ni mbovu. Naomba tufanye juhudi za makusudi ili kuwezesha hata viongozi wetu wakiwa wanateremka uwanja wa ndege waweze kutembea kwenye barabara ambazo kwa kweli watakuwa na usalama zaidi.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia barabara ya kutoka Masasi - Lindi ina matuta na mimi nafikiria hawa wakandarasi au wahandisi wetu walifikiria nini maana haya matuta ni makubwa kiasi ukiendesha speed hata kama ni 60 ukipita kwenye hilo tuta utapata ajali tu.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Ahsate sana, kengele imegonga.

MHE. AMANDUS J. CHINGUILE Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. (Makofi)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2022
MHE. AMANDUS J. CHINGUILE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru na mimi kwa kunipa nafasi. Mimi ni mjumbe wa Kamati ya Utawala na Serikali za Mitaa. Awali niunge mkono maoni ya Kamati zote mbili kwa asilimia mia moja.

Mheshimiwa Spika, nimshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa namna ambavyo anafanya bidii ya kuhakikisha maisha bora ya Watanzania yanendelea kupatikana.

Mheshimiwa Spika, nimpongeze pia Mheshimiwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na timu yake kwa kazi kubwa na nzuri ambayo wameendelea kuifanya. Wakati wamekuja mbele ya Kamati tuliendelea kuridhishwa sana na utekelezaji wa maazimio ya Bunge lako. Pia nimpongeze Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, TAMISEMI na timu yake kwa kazi kubwa na nzuri, kwakweli kazi zinaendelea kufanyika.

Mheshimiwa Spika, hata hivyo ninanyongeza ya ushauri kwenye maeneo kadhaa kwa sababu maazimio haya na maoni ya Kamati na mimi ni sehemu yake.

Mheshimiwa Spika,najielekeza kwenye TARURA, tuendelee kuwapongeza, wenzetu TARURA wanafanya kazo kubwa na nzuri kwelikweli katika maeneo ya nchi yetu. Hata hivyo bado niendelee kuomba kwa Serikali waendelee kuwezeshwa kifedha, bajeti yao iongezwe na hasa kwenye eneo la dharula. Inapotokea Msimu wa mvua hali inakuwa ni ngumu na wanakuwa na kazi kubwa kwelikweli. Wakiwezeshwa wataendelea kuimarisha utoaji wa huduma, na kwa kweli miundo mbinu kwenye maeneo yetu itaendelea kuimarika.

Mheshimiwa Spika, kwenye eneo hilo hilo la TARURA tuliendelea kushauri na bado naendelea kusisitiza kuishauri Serikali; bado eneo la manunuzi liendelee kusogezwa namna ambavyo itawezekana kufika kwenye eneo la Wilaya. Kwa namna ilivyo sasa hivi manunuzi na tendering hufanyiwa kwenye ngazi ya mkoa. Wale mameneja wa TARURA walioko kule wilayani kwenye halmashauri wanabaki kama PS, hawana mamlaka kwa hawa wakandarasi kwa kuwa tayari wamepewa tender kutoka huko mkoani. Sasa matokeo yake wanakosa namna ya kusimamiwa vizuri kule kwenye halmashauri; na hata sisi tulioko kule tunashindwa namna ya kuwasimamia vizuri. Lakini kazi inayofanyika na TARURA ni nzuri na wanaendelea kufanya kazi kwenye mazingira hayo.

Mheshimiwa Spika, naomba nitoke hapo nijielekeze kwenye mradi wa ujenzi wa Shule za Sekondari. Niipongeze sana Serikali kwa uamuzi huu; na kweli hizi shule ni nzuri na zinapendeza. Hata ukifika kule kwenye jimbo langu la pembezoni la Nachingwea unakuta shule iliyojengwa kwa mradi huu wa SEQUIP inapendeza kweli kweli, tunaishukuru Serikali.

Mheshimiwa Spika, lakini bado na mimi niendelee kusisitiza kwenye eneo lile la gharama halisi ya hizi shule. Milioni 470 yako maeneo mengine huwezi kumaliza uhitaji wa hiyo shule. Bado tuendelee kuangalia kulingana na eneo. Huwezi kufananisha eneo la Dar Es Salaam na eneo la Nachingwea au kule Tunduru. Niiombe sana Serikali ipitie upya jambo hilo, na kama ni suala ambalo linaweza likarekebishika basi tuweze kupata ufumbuzi wa haraka.

Mheshimiwa Spika, nijielekeze kwenye mchango tena kwenye Kamati ya Huduma. Nimepitia vizuri hapa, lakini yapo mapendekezo kadhaa na maoni ambayo Kamati wametoa. Ni ukweli usiopingika kwamba kwenye ukatili wa kijinsia wako baadhi ya wanaume na wenyewe wanapata kadhia hiyo. Kwa sababu ya kitamaduni ya Kiafrika na Kitanzania hatuna mahala pa kulalamika, yawezekana wengine tuko ndani humu lakikini hakuna anayeweza kutuzungumzia.

Mheshimiwa Spika, kwenye mapendekezo ya Kamati na mimi naomba nipendekeze nyongeza kwenye ukurasa wa 41(i) kuishauri Serikali, kufanya utafiti wa kina kujua nini chanzo cha ongezeko la ukatili wa kijinsia nchini hususani kwa wanawake na watoto. Hapa iongezwe na wanaume, kwa sababu tunachoshauri hapa ni kufanya utafiti. Kama bado wako wanaume ambao nao wanakumbwa na mazira haya tujue.

Mheshimiwa Spika, hii inaweza ikawa ni kichekesho lakini yapo. Wapo wanaopigwa, wapo wanaofungiwa na manyanyaso mengine kadha wa kadha. Lakini ugumu wa kujitokeza na kusema mimi nimefanyiwa haya mazira kwa sababu ya tamaduni zile zile za Kitanzania na Kiafrika tunashindwa kufanya hivyo. Lakini huo ndio uhalisia; na kwa sababu hapa tunachoshauri ni kwenda kufanya utafiti basi na hilo ipendeze liingie kwenye utafiti ili watuletee sasa tafiti zinasema nini. Hilo jambo lipo sawa basi kama halipo tutamshukuru Mungu, tutaendelea na lile lile kwamba wanawake na Watoto.

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo naendelea kurudia tena yale maoni ya Kamati na mimi ni sehemu yake. Kwa hiyo naunga mkono kwa asilimia mia moja. Nakushukuru sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora
MHE. AMANDUS J. CHINGUILE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru kwa nafasi. Awali ya yote nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa zawadi ya uhai, lakini kipekee nimpongeze sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kazi kubwa na nzuri anayoifanya kwa ajili ya kuboresha maisha ya Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze sana Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Dada yangu Mheshimiwa Jenista Mhagama na Naibu Waziri, Mheshimiwa Deo Ndejembi, kwa kweli, wanafanya kazi nzuri. Na mimi ni Mjumbe wa Kamati ya Utawala na Serikali za Mitaa, yako mambo mengi tumewashauri, lakini tumejadiliananao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nijielekeze moja kwa moja kwenye upungufu wa watumishi. Kwenye Jimbo langu la Nachingwea kwa mfano, kwenye elimu ya msingi mahitaji ni watumishi 1,319 waliopo ni 788, upungufu ni 531. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye elimu sekondari. Mahitaji ni 786, waliopo ni 412, mapungufu ni 374. Na afya vilevile nae neo la utawala kwa maana ya maafisa watendaji wa kijiji na wa kata. Eneo hili tulitolee macho kwa ukubwa wake na hasa maeneo haya ambayo ni mikoa ya mipakani, Lindi, Mtwara na maeneo mengine. Twendeni tuyape kipaumbele cha makusudi kabisa. Na hapa ndipo tunapokuja sasa kuona namna ambavyo wenzetu wanaoomba kwa mfumo huu wa mtandao akipangiwa kwenda Nachingwea anasema niko tayari, lakini akifika baada ya miezi mitatu, baada ya muda anasema sasa baba ni mzee kwelikweli, amezeeka baada ya mwaka mmoja? Haiwezekani! (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, anachagua kwenda Nachingwea ni kwa sababu, nafasi iko Nachingwea, lakini akishapata check number basi anakumbuka sasa kumbe naweza nikaomba kwa sababu sheria ipo na inamruhusu yeye kuomba uhamisho baada ya muda fulani. Kwenye hili, mimi nishauri Serikali yangu, tuone namna ambavyo tutatoa kipaumbele kwa wale wenye sifa ya kufanya hizi kazi wanaotokea kwenye maeneo haya; na hii itatusaidia, wale vijana wako. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi hii imejaliwa wasomi kwelikweli katika kila kata, kila wilaya, wasomi, ma-graduate ni wengi kwelikweli wapo. Ni Serikali tu kuweka utaratibu mzuri wa kuwatumia hawa ma-graduate ili tusipate upungufu huu kwa sababu ya watumishi wengine kuhama. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni kwa wale makaimu. Nilitoa taarifa hapa kwa Mbunge mwenzangu, sasa naona nilielekeze hilo. Kwa mfano, Halmashauri yangu ya Wilaya ya Nachingwea ziko idara na vitengo vinne kuna makaimu, lakini kibaya zaidi yuko kaimu anakaimu zaidi ya miaka 11, hii haikubaliki. Sasa hapa utamleta sasa mtumishi ambaye wewe umeona ana sifa kutoka eneo lingine, huyu mtu nimesema hapa tunampa ugonjwa wa sonona, tunamsababishia pressure na magonjwa mengine yasiyoambukiza, hii si sawa. Na kama ni vetting tunamuacha miezi sita ya kisheria, anakwenda mwaka, anakwenda miaka miwili… (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Mbunge ni vizuri hilo jina ulilosema anakaimu miaka 11 ukawapatia pia Mawaziri badae.

MHE. AMANDUS J. CHINGUILE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nitafanya hivyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, inapomletea sasa mkuu wa idara kutoka eneo jingine na yeye awe chini yake kwa kweli, unamuacha kwenye mazingira magumu sana huyu mtumishi. Hii si sawa na haikubaliki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, maelekezo yako nimeyapokea nitafanya hivyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni juu ya wastaafu, kuna suala la uhakiki. Hili ni kizungumkuti, kila mwaka wanakwenda kuhakikiwa mkoani; ni jambo jema kuhakiki kama wazima au la, lakini suala la kutoka huko vijijini waliko kwenda mkoani jambo hili ni gumu na hawa wastaafu walio wengi hali zao ni ngumu kwelikweli. Hapa Waheshimiwa Wabunge wenzangu wamesema… (Makofi)

MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Taarifa, Mheshimiwa Kuchauka.

T A A R I F A

MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa nampa Taarifa muongeaji, hili suala la kwenda kuhakikiwa mkoani limekuwa ni janga kwelikweli. Mtu anatoka Kijiji kwa mfano Mpigamiti, kilometa zaidi ya 30, aje Liwale Mjini kilometa 50, atoke Liwale Mjini kwenda Lindi ambako ni kilometa 360. Huyo mstaafu huyo ana umri wa miaka 80 au mwingine ana miaka labda 75 hivi, unamtakia kweli maisha mema?

Mheshimiwa Mwenyekiti, na mzigo huu. Kwa hiyo, nampa Taarifa anachikisema ni sahihi kabisa kwamba, huu mzigo tunaubeba sisi Wabunge. (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa unapokea Taarifa?

MHE. AMANDUS J. CHINGUILE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naipokea kwa mikono miwili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii si sawa na bahati nzuri hao wastaafu walio wengi wamechoka sana. Tuone namna ya kuwawekea mazingira rahisi sehemu ambayo ya kuhakiki, wanaweza kufanya kule Halmashauri, lakini pia tunaweza tukaboresha kwa namna nyingine ambayo tunaona inafaa zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni kwenye hizi ajira mpya zinazotolewa, hili nalo ni tatizo lingine. Tatizo sio kupata ajira, tunajua na tunaiheshimu sana mamlaka, na kwakweli kubwa zaidi niipongeze Serikali kwenye eneo hili kwa kutoa hizo ajira. Kazi kubwa hiyo mmefanya tunawashukuru, lakini ni namna gani hawa vijana wanakwenda kupata hizi kazi? Ni kizungumkuti. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, na huu mfumo wa ajira kwa maana ya kuomba kwenye mtandao si Rafiki na hasa kwa wale vijana walioko vijijini. Huu mtandao una changamoto, unaweza ukakaa wiki nzima bado wewe unaendelea kuingia online na mtandao hausomi, badala yake hata muda wa kuomba hizo nafasi umeshapita. Tuone namna tutakavyowasaidia hawa vijana kweli wa Kitanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wako Wabunge hapa wamesema ni vizuri sasa tukaona mgawanyo mzuri kwa kutumia wilaya, majimbo, namna tutakavyoona inafaa ili kila kijana Mtanzania aweze kunufaika na hizi ajira zinazotoka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine la mwisho, niwapongeze sana wenzetu wa TASAF na hasa kwenye ile miradi ambayo wameitekeleza, wanafanya kazi nzuri sana. Nimesema mimi ni mjumbe wa kamati na tumeona miradi mingi inapendeza kwelikweli; tumekwenda Zanzibar, kazi nzuri tumeiona. Mheshimiwa Waziri pamoja na timu yako ya TASAF mimi nawapongeza sana. Kazi hii nzuri iendelee, lakini pia sasa mtolee macho na maeneo mengine ambayo hamjafika kwenye miradi ya kimkakati ikiwemo kule Nachingwea, Liwale, Rwangwa na maeneo mengine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
MHE. AMANDUS J. CHINGUILE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Awali ya yote, namshukuru Mwenyezi Mungu kwa zawadi ya uhai. Kwanza namshukuru Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan. Mambo anayoitendea Tanzania tangu ameingia madarakani ni makubwa, nasi wote ni mashaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ni Mjumbe wa Kamati ya TAMISEMI, na kwenye hili nampongeza Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Mheshimiwa Angellah Kairuki kwa kazi nzuri, na speed hii aliyoanza nayo naamini Halmashauri zetu sasa ziko salama. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niwapongeze pia Naibu Waziri Mheshimiwa Festo Dugange na Mheshimiwa Deo Ndejembi kwa kweli wamekuwa wakizunguka kwenye halmashauri zetu wakikagua utekelezaji wa maono ya Mheshimiwa Rais namna fedha ambavyo amezipeleka. Hawa wanaendelea kufuatilia kwamba zinakwenda kufanya kazi sawa sawa na maelekezo ya Mheshimiwa Rais, tunawapongeza sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya pongezi hizo nimesema ni Mjumbe wa Kamati ya TAMISEMI. Kwenye ziara yetu tuliona miradi mingine ambayo imechelewa kukamilika na kati ya sababu wanasema ni mvutano wa wapi mradi utekelezwe. Wala haiingii akilini na kwenye jambo hili niiombe sana sana sana TAMISEMI hapa kubwa ni ushirikishwaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati miradi inakwenda wenzetu wataalamu kule site hawashirikishi wadau muhimu wanaohusika kwenye ile miradi wakiwemo Waheshimiwa Wabunge. Huku ndani tunafanya kazi ya kusemea Majimbo yetu sasa miradi ikiwa inakwenda ni vizuri tushirikishwe ili kwenda sawa sawa kutokwamisha hii miradi kwa sababu ya kuvutana ni wapi mradi ukajengwe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niiombe sana Wizara ielekeze wataalam wetu kule watushirikishe, washirikishe Waheshimiwa Wabunge, lakini pia na wadau wengine ili kwenda kutekeleza miradi hii kwa wakati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ni Mbunge wa Jimbo la Nachingwea na Makao Makuu ya Wilaya ya Nachingwea ni mamlaka ya Mji Mdogo zaidi ya miaka 10 sasa. Tumeshatuma maombi ya kuwa Mji kamili zaidi ya miaka saba iliyopita. Niiombe sana sana Wizara jambo hili ni jema na sisi litakwenda kutuongezea uwezo kama halmashauri. Niwaombe sana muone namna ambavyo mtaharakisha jambo hili jema ili Nachingwea sasa Mamlaka ya Mji Mdogo iwe Mji kamili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunao upungufu kwenye Sekta ya Afya na kwenye Sekta ya Elimu. Kwenye eneo hili nimshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kutoa sasa kibali kwa ajili ya kuajiri watumishi wapya kwenye eneo hili la elimu pamoja na afya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kule kwangu kwa mfano; tukiwa tunazungumzia habari ya kuboresha miundombinu kwa maana ya majengo, yako majengo chungu nzima ambayo bado wananchi walijitolea bado hayajakamilishwa. Tunashukuru kwa namna ambavyo Serikali imetuletea madarasa, imetuletea vituo vya afya ni jambo jema lakini ziko nguvu za wananchi ambazo zimelala na bado hazijulikani hatma yake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niiombe sana sana sana Wizara waende kumalizia yale maboma ambayo wananchi walijitolea na nguvu zao wanaziona. Tuna vituo vya afya, tuna shule lakini pia tunazo zahanati. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niendelee kidogo kuzungumza kwa habari ya upungufu wa nyumba za waalimu. Mfano mdogo Nachingwea mahitaji nyumba ni 413; zilizoko ni 72. Sasa utaona hiyo walimu wa sekondari mahitaji ni 413, zilizopo ni hizo 72, upungufu ni 341. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hawa walimu wetu wanafanya kazi nzuri namimi nitumie nafasi hii kuwapongeza watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Nachingwea kwa kazi kubwa wanayoifanya kwenye elimu, kwenye afya na maeneo mengine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye elimu Nachingwea tunajivunia hata kwenye rekodi ya sasa tumekwenda sana na Lindi kiujumla kama Mkoa lakini kwa hali hii tuiombe sana Serikali ipeleke fedha kwa ajili ya kujenga nyumba za walimu ambazo kwa kweli upungufu ni mkubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, matundu ya choo kwenye shule za sekondari. Mahitaji ni 564, yaliyoko ni 318; upungufu ni 246. Hebu angalia hiyo tofauti bado tuna kazi ya kufanya. Tunatambua na tunashukuru kwa kazi kubwa iliyofanyika lakini bado tunaomba zaidi kuendelea kutusaidia kwenye halmashauri hasa hasa hizi zilizoko vijijini kwa sababu zilisahaulika kwa muda mrefu. Sina mashaka na Mheshimiwa Waziri najua kazi hii utakwenda kuibeba vizuri na kazi hii itakwenda kufanyika vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, TARURA. Wenzangu wamesema hapa kazi nzuri inayofanyika na TARURA hakuna asiyeiona. Waheshimiwa Wabunge wenzangu mtakubaliana kwamba TARURA wanafanya kazi nzuri chini ya Mtendaji Mkuu na Mkurugenzi wetu wa barabara Engineer Komba wanafanya kazi nzuri pamoja na watumishi wote wakiwemo wale wa Halmashauri yangu ya Wilaya ya Nachingwea. Wanafanya kazi nzuri. Basi tuiombe sana Wizara iendelee kuangalia namna ambavyo wataongeza fedha ili hawa watendaji wetu mahiri kabisa watuboreshee miundombinu yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano kabla Mheshimiwa Rais Mama Samia Suluhu Hassan kuingia; Nachingwea fedha ya matengenezo ya barabara tulikuwa tunapata shilingi bilioni moja. Baada ya kuingia Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imebadilika bajeti ya mwaka ni zaidi Shilingi bilioni tatu. Tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo hili ni jema na sisi kama Wabunge tunapaswa kuungana kwa kauli moja kuendelea kumtia moyo Mheshimiwa Rais, anatuheshimisha. Kazi inayofanyika kwenye Majimbo kwa kweli kila mmoja anajua na tunacho kitu cha kusema 2025 na kule Nachingwea wanasema wao 2025 na Mama Samia wala hawafichi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wao wanasema na Mama Samia. Wanajua haya yaliyobaki kama changamoto anakwenda kuyatatua kwa kipindi hiki ambacho kipo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie kidogo habari ya Shule ya Mchepuo wa Kiingereza, shule za msingi. Kuna utitiri huo wa halmashauri zetu kuanzisha hizo shule za mchepuo wa kiingereza, ni jambo jema lakini jambo hili linakwenda kuweka matabaka tena. Niiombe Wizara twende tukaboreshe shule zetu za msingi zillizoko kwenye vijiji vyetu. Tupeleke waalimu wa kutosha, tupeleke vitendea kazi vya muhimu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana na ninaunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Maji
MHE. AMANDUS J. CHINGUILE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi, na kwa hakika siyo tu kwa kunipa nafasi, wewe umekuwa ni mwalimu na pia umekuwa ni mlezi. Umekuwa ukituongoza vizuri katika Bunge letu, na kwa kweli unaingia sasa kwenye rekodi ya Maspika wa viwango. Nakupongeza sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, awali ya yote, namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa zawadi ya uhai. Pili, namshukuru sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kwa kweli Wana-Nachingwea wametufanyia vitu vingi sana, siyo tu kwenye sekta hii ya maji, amegusa karibu maeneo yote. Kwa hiyo, tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais.

Mheshimiwa Spika, kipekee kwenye jambo hili la maji, wakati nikiwa mwanzoni wa Ubunge wangu, nililalamika sana hapa kuhusu suala la maji na hasa kwenye Vijiji vya Mchangani na Namanga. Leo nasimama nikiwa na furaha kwamba vijiji hivi; Kijiji cha Mchangani sasa maji yanamwagika. Hii ni kazi nzuri ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia kwenye Kijiji cha Namanga, kwenye huo mradi wa Namanga ambao una zaidi ya Shilingi milioni 700, muda wowote kuanzia sasa mkandarasi yuko site, anaendelea kufunga pump. Kwa hiyo, maji yanaenda kutoka sasa, muda siyo mrefu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, siyo hivyo tu, kwenye ukurasa wa 35, Hotuba ya Mheshimiwa Waziri, Serikali inakwenda kutekeleza mradi mkubwa wa maji ambao utanufaisha Wilaya ya Ruangwa na Nachingwea pamoja na Wilaya ya Lindi.

Mheshimiwa Spika, naishukuru sana Serikali kwa mradi huu, kwani unaenda kuwatua ndoo wamama wa Nachingwea, Ruangwa pamoja na Lindi. Tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais, Mheshimiwa Waziri pamoja na Naibu Waziri na timu yake. Ombi langu kwenye eneo hili, Mheshimiwa Waziri aende kuhakikisha mradi huu unakamilika kwa wakati. Watu wana matumaini makubwa sana na mradi huu ambao unakwenda kunufaisha vijiji 56. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri alimwagiza Mheshimiwa Naibu Waziri kuja kwenye Jimbo langu la Nachingwea, na kwa kweli alijionea kwa macho namna ambavyo watu wanahainga kwenye suala la maji kwenye Vijiji vya Ngunichile. Alikwenda Namikango, na pia viko vijiji vingine; kuna Mbondo, Kilimarondo na Matekwe. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwenye eneo hili la Ngunichile, hakuna chanzo cha uhakika, na tuliomba visima virefu. Kwenye bajeti hii ambayo imepita, tuliomba visima tisa, lakini vilivyoidhinishwa ni vitano. Mheshimiwa Waziri nakuomba sana, tumalizie tu hivyo vinne, peleka fedha kwenye Jimbo langu la Nachingwea ili wananchi wale waendelee kufaidi matunda ya kazi nzuri ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, uko mradi wa Mbwinji ambao unanufaisha Wilaya ya Masasi na Nachingwea. Kwa sasa wataalam wetu wanakamilisha usanifu wa mradi mpya, mradi pacha kwenye mradi huu wa Mwbinji. Namwomba sana Mheshimiwa Waziri, andiko hili litakapokuwa linafika kwenye Wizara, ajitahidi kuhimiza hizo fedha kufika kwa wakati kwa sababu tunakwenda kunufaisha vijiji zaidi ya 18 kwenye Jimbo la Nachingwea na vijiji sita kwenye Wilaya ya Ruangwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, iko changamoto ya wenzetu wa RUWASA, wanafanya kazi nzuri sana, na hasa viongozi wa Mkoa wa Lindi pamoja na timu yake, pia Engineer wa Nachingwea, Engineer Sultan pamoja na timu yake wanafanya kazi nzuri sana. Hata hivyo, wanafanya kazi kwenye mazingira yasiyo rafiki sana, hawana usafiri wa uhakika. Gari waliyonayo ni ya tangu 2010, imechoka. Engineer anaweza kwenda mahali kushuhudia au kufuatilia miradi ya maji, anakwama huko. Pia halina uhakika tena kwa sababu linagharimu matengenezo makubwa ya mara kwa mara.

Mheshimiwa Spika, namwomba sana Mheshimiwa Waziri, atuletee gari jipya Nachingwea ili vijana wale walio tayari kufanya kazi hii ya kizalendo waendelee kusimamia miradi hii ambayo Mhehsimiwa Rais anatupatia kwenye jimbo letu. Siyo hivyo tu, kwenye eneo hili, hata watumishi ni wachache. Tunao wahandisi wawili, tunaye dereva mmoja, secretary mmoja, pamoja na mwenyewe Engineer. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika hali hii, hawa wanafanya kazi kwa muda mwingi kuliko ilivyo kawaida. Kwenye hili sasa, naomba sana, vijana hawa wanaofanya kazi ya kizalendo, Mheshimiwa Waziri apate nafasi ya kututembelea ili tumwonyeshe kwa macho kazi nzuri na kubwa ambazo wanazifanya ili waone namna ya kuwatumia kwa ukubwa wake zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pamoja na hayo yote, ni vizuri tuhakikisha hawa wakandarasi ambao wanapewa miradi, wanakamilisha kwa wakati. Huu mradi ambao nimepongeza na kuusifia wa Namanga, ulitakiwa ukamilike kwa muda mrefu uliopita, mwaka 2022 mwezi wa Kumi na Mbili. Baadaye wakasema kwamba kuna ununuzi wa pamoja wa mabomba na kadhalika. Kwa hiyo, akaongezewa tena muda, akasema mwezi wa Nne. Bado ikaendelea kurushwa hiyo, mpaka sasa hivi ambapo wamefikia hatma ya mradi huu.

Mheshimiwa Spika, namwomba sana Mheshimiwa Waziri, kwenye mipango yetu wakati tunaenda kutekeleza hii miradi, tuhakikishe tunakwenda kutekeleza kwa wakati, na hii itakwenda kuimarisha, hata namna ambavyo wananchi wanaona hii miradi inakwenda. Kuna maeneo mengine ukifika ukawaeleza, kwa sababu tayari wameshashuhudia miradi, wakati wa mwanzo wanaambiwa mradi huu utachukua miezi sita, au miezi 18, baadaye inaongezwa tena. Halafu ile ya kuongezwa kimya kimya, inaleta sintofahamu, na wakati mwingine sisi wawakilishi tunaonekana hatuko sawasawa.

Mheshimiwa Spika, kwa kazi nzuri inayofanywa na Mheshimiwa Waziri pamoja na Naibu wake pamoja na wataalam wake, mimi kama Mbunge wa Nachingwea, naridhika sana. Ninaamini hata haya niliyoyasema kwa uchache yanakwenda kufanyiwa kazi. Mheshimiwa Waziri ukipata nafasi tembelea Nachingwea. Sisi hatuna zawadi kubwa kule, hatufugi ng’ombe, ila tutakushikia kuku. Hizo ndiyo mila za watu wa Kusini, na hiyo ndiyo itakuwa zawadi kubwa kabisa kuliko yote.

Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi, na ninaunga mkono hoja kwa asilimia mia moja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari
MHE. AMANDUS J. CHINGUILE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Awali ya yote nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia afya na hatimaye kupata nafasi ya kuchangia kwenye Bunge lako Tukufu.

Mheshimiwa Naibu Spika, niungane na wenzangu kumshukuru sana na kumpongeza Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan. Kwa kweli ameendelea kufanya mambo makubwa kwenye nchi yetu, ameendelea kuifungua Tanzania lakini kwa mkataba huo tulioshuhudia wa utiaji saini, ujenzi wa minara zaidi ya 700 ni kielelezo tosha kwamba Mheshimiwa Rais anafanya kazi nzuri isiyo na mfano.

Mheshimiwa Naibu Spika, pili, nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri wa Habari kwa kazi nzuri anayoifanya pamoja na Naibu Waziri na watendaji wake wote. Mheshimiwa Naibu Waziri, Wizara hii ndio coordinator wa Wizara zingine. Wizara hii ikifanya vizuri wote tunakubaliana kwamba mawasiliano kwa sasa ndio habari ya dunia. Habari ya TEHAMA kwa sasa ni habari ya dunia, Mheshimiwa Waziri Nape anafanya kazi nzuri, anafanya kazi nzuri na kwa kweli tunajivunia namna ambavyo Tanzania inakwenda kidijitali, hakuna mfano. (Makofi)

MHE. JUSTIN L. NYAMOGA: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

TAARIFA

MHE. JUSTIN L. NYAMOGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Napenda kumpa taarifa mchangiaji anachangia vizuri sana kuisifia na kuwasifia Waziri na Naibu Waziri na kwa ushahidi tu ni kwamba Jimbo la Kilolo limepata minara tisa na kata tisa ambazo hazikuwa na minara zote sasa zinaenda kuwa na mawasiliano. Kwa hiyo sifa anazozitoa ninao ushahidi na nimependa kumpa taarifa ili aelewe kwamba hakosei. (Makofi)

NAIBU SPIKA: Ahsante. Mheshimiwa Amandus taarifa hiyo.

MHE. AMANDUS J. CHINGULE: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa hiyo naipokea kwa sababu ndio hali halisi iliyoko kwenye maeneo yote ya Tanzania kwa sasa. Kwa kweli tukipongeza kitu ambacho kiko wazi kila mmoja anakubaliana na sisi na ndio maana hata michango ya leo ya Waheshimiwa Wabunge imekuwa ni ya kidijitali kama ambavyo Mheshimiwa Waziri amesoma hapa na mimi nitajitahidi kutumia dakika chache sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, bahati nzuri sana umefika Nachingwea, wakati wa kampeni ulikuja kufanya kampeni kule Nachingwea na nakushukuru sana. Yako maeneo kwenye Jimbo la Nachingwea ukifika unazima simu kwa sababu haina kazi tena, inakuwa ni kama kopo. Baada ya hapo maana yake ni kwamba kuna maeneo ambayo sasa hayo ndiyo unaweza ukatumia simu. Sasa nishukuru kwanza Serikali na nimshukuru Mheshimiwa Waziri nimeona hapa kwenye ukurasa wa 100, nimeona minara inakuja Nachingwea.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa pamoja na shukrani hizo nimwombe sana Mheshimiwa Waziri, jiografia ya Nachingwea ni kubwa, nimwombe kwa heshima na unyeyekevu mkubwa atuongezee minara Nachingwea, tuongezewe minara ya Nachingwea. Mji wa Nachingwea kwa namna ulivyo jiografia yake Waziri anafahamu, misitu ni mingi na mbuga kule Selous anajua ipo. Kwa hiyo ukienda katika baadhi ya maeneo, kwa sababu ya miti na maeneo yale kuwa na mbuga hii ya Selous, unakosa mawasiliano kwa namna ya jiografia ya wilaya yenyewe ilivyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, nilisema kwamba nitazungumza kwa ufupi sana. Mheshimiwa Waziri aendelee kuchapa kazi, aendelee kuchapa kazi. Sisi tupo na tunaona kazi inayoendelea na kwa kweli hata suala la utapeli wa kwenye mitandao, niwaombe tu hao ndugu kama wapo na wanasikia, watafute shughuli zingine za kufanya. Kwa namna spidi ya Wizara hii inavyoendelea ni imani yangu kwamba muda si mrefu hao nao wanakwenda kufa. Sasa ili wasife kifo kibaya cha kutangazwa kwenye mitandao, wakati ni huu wa kujisalimisha kuacha shughuli hiyo na kutafuta shughuli nyingine halali ambayo itawapatia kipato. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana, naunga mkono kwa asilimia mia moja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Kilimo
MHE. AMANDUS J. CHINGUILE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwa kunipa nafasi, awali ya yote ninamshukuru sana Mwenyezi Mungu aliyenijalia uhai na hatimae kusimama mbele ya Bunge lako Tukufu kutoa mchango wangu kwenye Wizara hii ya Kilimo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninampongeza sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama yetu Mama Samia Suluhu Hassan kwa kweli bajeti hii sasa inakwenda kujibu mahitaji ya wakulima wetu ya muda mrefu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia ninamshukuru na kumpongeza sana Mheshimiwa Bashe, kwa kweli anafanya kazi nzuri sana. Mheshimiwa Waziri umekuwa ni kielelezo kwa vijana wachapa kazi sana pamoja na Naibu Waziri mnatuheshimisha sana. Mheshimiwa Waziri ninakushukuru na kukupongeza sana namna ambavyo umeshughulika na Ushirika, kati ya maeneo ambayo walikuwa hawamuelewi Mheshimiwa Rais anataka nini ni eneo hili la ushirika. Mheshimiwa Waziri nikupongeze tena kwa kazi hiyo nzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitajielekeza kwenye suala la mbegu ya alizeti. Katika Halmashauri yetu ya Wilaya ya Nachingwea tulitumia mapato ya ndani tukanunua tani moja na nusu mbegu hizi za alizeti na tukatoa kwa bei ya ruzuku kwa wakulima mapokeo yalikuwa ni mazuri sana, sasa kwenye mpango wa Wizara juu ya kutoa ruzuku hii kwenye mbegu za alizeti Mkoa wa Lindi haumo, ninamuomba sana Mheshimiwa Waziri aiangalie Lindi hususani kwenye Wilaya hii ya Nachingwea ambayo tayari tumeshaanza kuonesha nia na wakulima wetu wamepokea vizuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo jingine ninaishukuru sana Wizara kwa kutoa bei elekezi kwenye pembejeo, huu ni mwanzo mzuri Mheshimiwa Waziri, kazi hii iendelee, hii itatufanya wakulima wetu waweze kupata bei nafuu na hivyo kuondoa ile changamoto ya bei kupanda mara kwa mara. Mheshimiwa Waziri eneo jingine ni kwenye upatikanaji wa pembejeo Jimbo langu la Nachingwea uhitaji kwa msimu huu ni tani 1,000, mpaka sasa tumepokea Sulphur peke yake tani 99, tunaona bado upatikanaji umekuwa ni wa chini mkituwezesha kupata kwa muda muafaka itatusaidia kuzalisha kwa wingi zaidi pia kuendana na muda. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitumie nafasi hii kuwashukuru na kuwapongeza sana wakulima wa Wilaya ya Nachingwea kwa kazi nzuri na kubwa wanayoifanya. Hata hivyo, ipo changamoto na kadhia ya Tembo, nafahamu kwamba ninachangia kwenye Wizara ya Kilimo lakini mazao yanayoshambuliwa ni ya kilimo, Wanyama hawa waharibifu ni kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii. Adha hii ni kubwa na kwakweli kwenye maeneo yetu huko changamoto hii ni kubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tarehe 16 juzi yupo mwananchi mmoja amekanyangwa na kuuawa na tembo, Serikali hii ni moja, Wizara ya Kilimo niiombe sana kwa sababu mazao haya yanayoharibiwa ni mazao yatokanayo na kilimo lakini waharibifu wapo kwenye Wizara ya Maliasili na Utalii, zungumzeni lugha moja ili muone namna ambavyo hawa wananchi wetu mtawasaidia, changamoto hii ni kubwa kweli kweli, yapo maeneo ambayo ukifika leo utawaonea huruma, anakwenda shambani anakwenda kufanya nini kwa sababu hawa wanyama wameshaharibu sana. Maeneo ya Namapwia, Nditi, Kata ya Ngunichile, Namikango, Lionja, Kipara, Kilimarondo, Matekwe, Kiegei hali ni mbaya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa Mheshimiwa Msambatavangu juzi alizungumzia hapa juu ya afya ya akili, hebu huyu mkulima ambaye amefanya kazi kubwa kwa kilimo tena cha kizamani kwa jembe la mkono halafu hawa Wanyama wanakwenda kufanya uhabiribu, matokeo yake kwa kweli huyu mtu anaweza akapata tatizo la afya ya akili. Katika hili ninaiomba sana Serikali izungumze lugha moja, Wizara ya Kilimo, Wizara ya Maliasili na Utalii na hapa nisema tu Mheshimiwa Waziri wa Maliasili na Utalii najua bajeti yake inakuja kwenye hili aandae kwa kweli maelezo ya kina yatakayonifanya nisiondoke na Shilingi yake kurudi nayo kule Nachingwea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hali inatisha hali ni mbaya na sisi kama wawakilishi hatueleweki na mara kadhaa nimekwenda na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii alituahidi kutujengea kituo na kutuletea Askari, mpaka sasa hicho kituo hakuna na eneo hilo ni kubwa. Siyo hilo tu, kwenye Mkoa wa Lindi yapo maeneo mengine ambayo yamekubwa na kadhia hii, kwenye Jimbo la Mchinga kwa mfano, eneo la Milola, Kiwawa, huko nako waliahidiwa kujengewa kituo huko kwa ajili ya Wanyamapori eneo la Lutamba-londo bado hicho kituo kiliahidiwa tangu 2020. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninayasema haya kwa uchungu zaidi kwa sababu maisha ya yule mpiga kura wangu hayawezi kurudi tena hata kama akipata fidia, hayawezi tena kurudi kwa sababu tayari ameshafariki, tuchukue hatua sasa kabla ya madhara mengine zaidi kutokea. Hii siyo la kwanza mwaka jana mwezi wa Novemba hawa tembo walishawahi kusababisha tena madhara ya namna hiyo ya kuuawa kwa mtu mwingine, tulikwenda na Naibu Waziri alikwenda kutoa pole hapo, tunachotamani hapa ni kupata dawa ya kudumu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Waziri wa Kilimo wananchi wale sasa wanakata tamaa kwa sababu hakuna namna ya kwenda shambani tena. Hawa tembo sasa ukienda maeneo haya kwa mfano ya Namapuya ni kama ng’ombe sasa wapo tu wanazagaa, hata leo ukifika inatisha, hii hali hatueleweki.

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa.

MHE. AMANDUS J. CHINGUILE: Ahsante, naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa
MHE. AMANDUS J. CHINGUILE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi na mimi nichangie kwenye Wizara hii ya Ulinzi. Awali ya yote nimpongeze sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu kwa kuona umuhimu wa kuongeza bajeti kwenye Wizara hii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nilipongeze sana Jeshi letu la Ulinzi wa Tanzania, kwa kweli wamekuwa ni kielelezo, wazalendo na wachapakazi. Jeshi letu linafanyakazi vizuri, lakini siyo tu kwenye masuala la ulinzi na usalama, wanatoa huduma za afya, lakini kwenye elimu, ujenzi na huduma nyingine za kijamii, hongereni sana makamanda wetu na wapiganaji wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nina maeneo mawili naomba kuchangia; kwenye jimbo langu la Nachingwea kuna mgogoro wa muda mrefu wa ardhi baina ya wananchi na Jeshi letu. Jeshi linafanyakazi nzuri na kwa kweli tunaishi nao vizuri sana. Upo mgogoro kati ya 41KJ na 843KJ; mgogoro huu ni wa muda mrefu, aliwahi kuja aliyekuwa Waziri wa Ulinzi wa wakati huo ambaye sasa ni Rais wa Zanzibar na alitoa maelezo, alizungumza na wananchi akasema watalipwa. Lakini baada ya muda alikuja afisa mwingine kutoka Makao Makuu ya Jeshi, akasema hawatalipwa ardhi badala yake watalipwa yale maendelezo waliyoyafanya kwenye ile ardhi. Wananchi wale kwa upendo mkubwa na jeshi na mahusiano mazuri waliridhika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya muda alikuja afisa mwingine kutoka Makao Makuu ya Jeshi, akaongea na wananchi hawa tena akasema hakuna malipo mengine yatakayofanyika, si yale ya ardhi wala si yale ya maendelezo. Hawa wananchi wana mapenzi mazuri na tunaishi nao vizuri sana hawa wanajeshi na kati ya huduma za afya ambazo zinatolewa vizuri ni kwenye Hospitali Kuu ya Jeshi Majimaji Nachingwea, wanafanyakazi nzuri na wananchi wakawaida wanakwenda kupata huduma hapo. (Makofi)

Sasa niiombe sana Wizara ione umuhimu wa kuondoa changamoto hii kwa haraka ili wananchi hao waweze kujua hatima yao. Hawana maneno wananchi hawa, wapo tayari kupokea maelekezo yoyote ambayo yatatolewa na Serikali. Kwa unyenyekevu mkubwa naiomba sana Wizara ili hao wananchi waweze kujua hatima yao. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tuna shule ya sekondari Farm 17; eneo hili ni la Jeshi lakini kielelezo cha kwamba tuna maisha mazuri, tunaelewana vizuri na wanajeshi, jeshi wametupa Halmashauri eneo hili tulitumie kama shule ya sekondari. Eneo hili ni muhimu na sisi tunahudumia zaidi ya kata tatu wanatumia hii shule ya sekondari.

Sasa ombi langu, eneo hili sasa niiombe sana Serikali, nimuombe sana Mheshimiwa Waziri, mfikirie kutuachia, kwa sababu kwa sasa tukitaka kufanya miundombinu ukarabati ni lazima tupate kibali kutoka jeshini. Eneo hili tukilipata, mkituachia rasmi, mkitukatia eneo hili ambalo linazunguka shule tutawashukuru sana ili tuweze kuboresha miundombinu na wananchi wa maeneo yale waweze kupata huduma bora kwa ajili ya kupata ile elimu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niendelee kumpongeza tena Mheshimiwa Waziri kwa kazi nzuri anayoifanya ameingia kwa kweli tunaona Wizara hii inamelemeta. Nakushukuru sana. (Makofi)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria, kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023
MHE. AMANDUS J. CHINGUILE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi, nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia uhai. Kipekee, nampongeza sana na kumshukuru Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kazi kubwa na nzuri ambayo ameendelea kuifanya kwenye Majimbo yetu yote. Ukiacha Elimu na Afya na maeneo mengine ya Miundombinu, tumeshuhudia upelekaji wa magari ya ufuatiliaji pamoja na Ambulance kwa siku za hivi karibuni. Tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, nampongeza na kumshukuru sana Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Mheshimiwa Mchengerwa, tangia ameanza kuhudumu kwenye Wizara hii pamoja na wasaidizi wake, Waheshimiwa Manaibu Mawaziri, pamoja na Makatibu wote, Katibu Mkuu na Manaibu Makatibu Wakuu, wameendelea kuwa na kiwango cha 5G. Endeleeni kupiga kazi, mimi kama Mjumbe wa Kamati ya TAMISEMI, naendelea kuunga mkono kazi hii njema. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza Serikali kupitia Wizara ya TAMISEMI, kwa kuendelea kufanyia kazi Maazimio na Ushauri wa Kamati kuboresha Elimu Mtandao. Kwa sasa, Serikali inafanya majaribio ya kutoa elimu kwa njia ya mtandao. Tumeshuhudia kama Kamati, Mwalimu mmoja wa Kemia au Biology anafundisha kwenye shule tatu kwa wakati mmoja, yeye yuko Kibaha lakini darasa lingine liko Dodoma, na liko eneo lingine. Kwa hiyo, hii ni hatua nzuri na naendelea kuipongeza Serikali kwa kazi hii kubwa ya kuendelea kufanyia kazi maoni ya Kamati pamoja na ya Waheshimiwa Wabunge.

Mheshimiwa Mwenyekiti, malengo ya kuanzishwa kwa Shirika la Kibaha, yalikuwa ni pamoja na kufanya Tafiti kwenye maeneo mbalimbali yakiwemo Elimu. Kazi hii kubwa na nzuri ambayo nimeipongeza hapa, ya kuendelea kuboresha Elimu Mtandao, imefanywa na Shirika letu la Kibaha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Shirika la Elimu Kibaha ndiyo wamefanya kazi hii kubwa na nzuri. Kwa masikitiko, ni kwamba hili Shirika la Elimu Kibaha, tayari imeshatangazwa kuvunjwa. Mapendekezo na Ushauri wa Kamati kwa msimu uliopita, ilikuwa ni kuitaka Serikali iboreshe Shirika la Elimu Kibaha na siyo kuvunjwa. Kwa sababu bado malengo ya kuazishwa kwake yapo na tunayahitaji kama Watanzania. Tunakumbuka kuna Hospitali pale ya Tumbi, ilifanya kazi kubwa na nzuri kuanzia kipindi cha Mwalimu Nyerere, bado kazi ile ipo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa Hospitali ile imerudi kuwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa na jambo hili kwa kweli kama Mjumbe wa Kamati, naona si sawasawa. Bado naiomba Serikali kupitia upya maamuzi yake hayo ya kuvunja Shirika la Elimu Kibaha ambalo kwa sasa tunaona ipo haja na iko sababu ya kuendelea kuliacha Shirika hili liendelee kufanya Tafiti za Elimu na maeneo mbalimbali kwa ajili ya maendeleo ya nchi yetu. (Makofi)

MHE. GODWIN E. KUNAMBI: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Amandus, kuna Taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Godwin Kunambi.

TAARIFA

MHE. GODWIN E. KUNAMBI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza mchangiaji kuhusiana na Shirika la Elimu Kibaha. Mimi ni mdau pale, nimewahi kupita pale Kibaha Folk Development College (Chuo cha Maendeleo ya Wananchi Kibaha), kwa kweli Shirika la Elimu Kibaha ni muhimu sana na linatoa watu wengi. Mfano mzuri mimi Mheshimiwa Kunambi niko hapa, ni zao la Folk Development College pale Kibaha. (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Amandus, Taarifa hiyo unaipokea?

MHE. AMANDUS J. CHINGUILE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naipokea Taarifa hii nzuri na inayoleta sasa kumbukumbu nzuri ya kazi njema ya Shirika la Elimu Kibaha. Bado naendelea kumuomba Mheshimiwa Mwenyekiti wakati wa kuhitimisha Hoja yake, aone namna atakavyoliweka vizuri ili tuitengeneze kama Azimio la Bunge. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, najielekeza kwenye TARURA, sisi Waheshimiwa Wabunge tunaotokea vijijini, hali yetu kwa kweli ni mbaya. Kuna wakati unalazimika kutokufika Jimboni kwa kutumia gari maana yake lazima uvuke kwenye madaraja yaliyovunjika kwa kutumia namna nyingine ya usafiri kufika ndani ya jimbo lako. Taarifa iliyotolewa hapa, tumeona na tumesikia, Waheshimiwa Wabunge wote kwa ujumla wetu namna bajeti ilivyopelekwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niendelee kuunga mkono Taarifa hii ya Kamati, Serikali iendelee kupeleka fedha kwa wakati. Hali ni ngumu na hasahasa karibu tunajiandaa kurudi kwenye Majimbo yetu, wanachi wanatamani kupata majibu kwa Waheshimiwa Wabunge, nini tumesikia kutoka kwa Serikali. Wakipeleka fedha kwa wakati, itaweza kutusaidia zaidi na mambo mengine na shughuli za kimaendeleo zitaendelea kufanyika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Jimbo langu la Nachingwea, siyo Barabara tu za TARURA, hata TANROADS. Ukitoka Ndanda, huwezi kufika Nachingwea barabara imekatika, ukitoka Masasi, huwezi kufika Nachingwea barabara imekatika, kwa hiyo, achilia mbali Barabara za TARURA. Sisi watu wa Nachingwea hatuna mbadala, jana nimepata taarifa basi linaishia Masasi, kutoka hapo wananchi wanavushwa kwenda upande wa pili kwa hiyo hii haileti picha nzuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda kwa Mheshimiwa Kuchauka kule Liwale, hali ni mbaya nayo, ukienda huko Mbarali hali ni hivyohivyo. Kwa hiyo niombe sana Serikali, jambo hili ni jambo la dharura na ni lazima tuchukue hatua sasa. Haina mbadala, Wananchi wa Tanzania wanahitaji huduma kila kona. (Makofi)

MHE. JUSTIN L. NYAMOGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Amandus, Taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Lazaro Nyamoga.

TAARIFA

MHE. JUSTIN L. NYAMOGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza mchangiaji, wakati anaendelea kutaja, nilitaka tu kumtarifu kwamba, hata Kilolo kwenyewe, barabara hazipitiki kabisa maeneo yote na madaraja yamevunjika. (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Amandus, Taarifa ya jirani yako unaipokea?

MHE. AMANDUS J. CHINGUILE: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye kadhia hii, kwenye changamoto hii, hata ukienda Kiteto huko, hali ni hiyohiyo. Tunasema kwa uchungu na tunaiomba Serikali kuchukua hatua sasa, hali yetu siyo nzuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema haya, najielekeza kwenye eneo lingine la maboma hasa ya Zahanati na Vituo vya Afya. Wananchi waliitikia wito na kuendelea kuhamasika kujenga majengo ya Zahanati wenyewe kwa nguvu zao lakini na Vituo vya Afya, majengo haya yako mengine yamekaa kwa zaidi ya miaka minne, miaka mitano, miaka miwili na kadhalika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa, hapa nguvu za wananchi zimekwenda, niombe Serikali kuweka Mpango Mahususi, Mpango wa haraka ambao unakwenda kufanya kazi ya kumalizia maboma haya kwa wakati. Zile ni nguvu za wananchi ambazo zimekwenda. Tukifanya hivi maana yake tunawavunja moyo wananchi wetu, hawawezi tena kufanya shughuli zingine, basi tuone nguvu hizi ambazo tayari wameshaziweka kwa kujenga haya majengo…

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa.

MHE. AMANDUS J. CHINGUILE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono Hoja za Kamati zote mbili. Nakushukuru sana. (Makofi)
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2021 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023
MHE. AMANDUS J. CHINGUILE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili nizungumze kidogo kuhusu Bajeti Kuu ya Serikali. Awali ya yote, nimpongeze sana Mheshimiwa Rais kwa kazi nzuri na kubwa anayoifanya, kwa kweli Watanzania wanaona. Hata wale ambao wanasema hawaoni basi moyoni wanajua na wanakiri kwamba Mheshimiwa Rais mama Samia Suluhu Hassan anaupiga mwingi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nijielekeze kwenye barabara. Iko barabara ya Nachingwea – Masasi, upembuzi yakinifu na usanifu wa kina umefanyika na umekamilika zaidi ya miaka tisa iliyopita, lakini imetengewa fedha zaidi ya miaka mitano mfululizo lakini haijapelekwa hata senti moja. Kwenye hotuba ya bajeti ya Waziri wa Kisekta aliizungumzia hii barabara ya Masasi – Nachingwea kwamba iko kwenye mpango wa kujengwa kwa kiwango cha lami. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia alielezea ujenzi wa kiwango cha lami barabara ya kutoka Nachingwea kuelekea Liwale. Sasa wakati Mheshimiwa Waziri wa Fedha anasoma hii Bajeti Kuu sijasikia. Sasa nikawa napitia kishikwambi changu nikasema labda hii page imeruka au namna gani? Tukiwa tunaomba hizi barabara, tunaomba kutufungua ili na sisi kimaendeleo tuwe sawasawa na maeneo mengine, hali huko ni ngumu. Ukizungumzia barabara ya kutoka Masasi – Nachingwea, Nachingwea – Liwale, Liwale - Nangurukuru, Nachingwea kuelekea Ruangwa wakati wa masika huwezi kupita. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tumeshuhudia hapa nilikuwa na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, tulikaa mahali tumesimama zaidi ya masaa mawili, hiyo barabara ni mbovu. Sasa sijui tumekosea wapi na kwenye hili nimwombe sana kaka yangu Dkt. Mwigulu Nchemba atakapokuja kuhitimisha, wananchi wale wa Masasi, Nachingwea, Ruangwa na Liwale wanataka kusikia barabara hii mpango wa kujenga ukoje? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Waziri wa Ujenzi ametupa matumaini makubwa, lakini sasa kwa hotuba hii sielewi kama atakuja kuhitimisha mwishoni au la lakini kwa kweli wanasubiri kusikia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nitoke hapo nijielekeze kwenye kilimo. Tunaishukuru Serikali ya Awamu ya Sita kwa kutupatia pembejeo za kilimo na hasa kwenye zao la korosho, tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais. Kwenye hili naomba nishauri eneo moja, tuna changamoto ya upatikanaji wa hiyo Sulphur. Makisio ya mwaka huu ni kupata tani 25,000, lakini mpaka sasa imepelekwa tani 10,000, tayari msimu unakwenda. Maana yake hapa wakulima watapata pembejeo wakati muda wa kuzitumia umeshapita, sasa eneo hili nishauri sana Serikali kwa sasa tunatumia vyama vikuu vya ushirika kununua hizi pembejeo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa niombe jukumu hili tuwape Bodi ya Korosho Tanzania, kwanza ni chombo cha Serikali, lakini pia tunaweza tukazipa taasisi zingine za Kiserikali na hii itatusaidia hata wakati wa kufanya auditing. Natambua Wizara ya Kilimo inafanya kazi nzuri basi na lenyewe walichukue ili waweze kulifanyia kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie kidogo suala la tembo. Nilisimama mbele ya Bunge lako Tukufu, nikalia sana, nikalalamika sana juu ya kadhia ya tembo na nitumie nafasi hii kumshukuru sana Mheshimiwa Rais, kumshukuru sana Mheshimiwa Waziri Mkuu na Waziri pamoja na Naibu Waziri wa Sekta ya Maliasili na Utalii, tunawashukuru sana, jambo lile wamelifanyia kazi na kazi inaendelea. Tunajua kwamba changamoto haijaisha na naamini kwamba bado wataendelea kutuondolea kero hii ili wananchi wangu wa Jimbo langu la Nachingwea waweze kuishi kwa raha kama maeneo mengine. Tunawashukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nizungumzie kidogo juu ya asilimia 10. Wakati inatengwa ile asilimia 4:4:2, ziko halmashauri zingine mapato yake ni kidogo sana, hayatoshelezi. Sasa leo Mheshimiwa Waziri wa Fedha anasema twende tukaondoe asilimia tano…

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa kuna taarifa. Mheshimiwa Waziri wa Fedha.

T A A R I F A

WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Naibu Spika, natambua kuwa nitakuwa na muda wa kujumuisha, lakini nimehofia nisije hoja zikawa nyingi nikasahau jambo hili. Naomba nimpe taarifa Mheshimiwa Mbunge makini kabisa anayeongea kwamba hii barabara anayoitaja ni kweli ni omission, tuliisahau kuiorodhesha, kwa hiyo iingie kwenye kumbukumbu za Hansard kwamba na yenyewe ni sehemu ya zile barabara zilizowekwa kwenye ule mpango ambao Mheshimiwa Waziri wa Ujenzi aliusema. (Makofi)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa taarifa hiyo.

WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, iingie kwenye kumbukumbu kama ilivyotajwa kwenye Wizara ya Kisekta, imo kwenye utaratibu ule ule na wananchi wote na Wabunge wote wa Kusini waipate hivyo kama ambavyo ilisomeka kwenye Wizara ya Kisekta. (Makofi)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa taarifa umeipokea?

MHE. AMANDUS J. CHINGUILE: Mheshimiwa Naibu Spika, naipokea kwa mikono miwili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nilikuwa naendelea na mchango wangu kwenye asilimia 10, bado mahitaji ya watu wetu kwenye haya matumizi ya asilimia 10 ni makubwa kuliko hata hiyo asilimia 10 inayopatikana. Kwa hiyo, niiombe sana Serikali bado hii asilimia 10 kwa maana ya 4:4:2 tuiache, badala yake sasa tutafute vyanzo vingine ambavyo tutakwenda sasa kuwahudumia wale wamachinga.

Mheshimiwa Naibu Spika, tukumbuke kwamba hizi fedha pia na hao wamachinga ni sehemu ya wale vijana ambao wanakopa, ni sehemu ya wale akinamama ambao wanakopa. Hilo naomba lizingatiwe.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo nataka kulizungumzia ni kwamba, kipo Chuo cha Ualimu Nachingwea, ni chuo kikongwe na cha muda mrefu sana. Tulizungumzia hapa juu ya kuiomba Serikali ione uwezekano wa kukipandisha kile chuo kuwa Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, chuo hiki ni kikubwa, chuo hiki kina eneo, lakini pia Nachingwea ni tajiri kwa maeneo, tunayo maeneo mengi ya kutosha, wakiwa tayari tutawapa maeneo ya kutosha kabisa. Chuo hiki kinabeba wanafunzi kutoka kwenye maeneo mbalimbali ya nchi yetu. Kwa hiyo, wakitupatia, hii ni fursa kwa uchumi wa Nachingwea, lakini pia tutakuwa tunasogeza elimu zaidi kwenye maeneo ambayo vijana wanatoka huko.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu ya furaha ya kusikia lile jambo la barabara, nisije nikaondoa utamu huu, hapa tayari nimeshaanza kupokea message za kupongeza. Nikushukuru sana na naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja. (Makofi)