Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Aloyce Andrew Kwezi (3 total)

MHE. ALOYCE A. KWEZI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, kwa kuwa matatizo yaliyopo katika Jimbo la Tabora Mjini ya walimu na madawati yanafanana kabisa na matatizo yaliyopo katika Jimbo langu la Kaliua nilikuwa naomba niulize maswali mawili ya nyongeza. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, moja; Kaliua katika shule zetu za Usenye, Usinge, Ufukuto na maeneo mengine tuna upungufu wa walimu wa msingi na sekondari wapatao 873.

Je, Serikali ni lini itatupatia walimu hao? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pili, Kaliua tuna upungufu wa takribani madawati 4009. Je, Serikali ni lini itatupatia madawati hayo au fedha kwa ajili ya kukamilisha? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE.DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Naibu Spika, Ahsante sana. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Aloyce Kwezi, Mbunge wa Kaliua kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la kwanza la Mheshimiwa Mbunge alikuwa anazungumzia kwamba katika Jimbo lake kuna upungufu wa walimu 873 na akataka kufahamu ni lini Serikali tutapeleka walimu hao? Mimi nimuahidi tu kabisa kwamba katika mgawanyo ambao tutakwenda kuajiri wale walimu 6000 basi sehemu ya walimu wale baadhi tutapeleka katika Halmashauri yake na Jimbo lake la Kaliua.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini jambo la pili kuhusu madawati, changamoto ya madawati kama tulivyoahidi na tumetenga katika bajeti yetu ambayo Waheshimiwa Wabunge mliipitisha kwamba katika yale madawati 710,000 sehemu ya hayo madawati tutapeleka katika jimbo lako. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge usiwe na wasiwasi na hilo. Ahsante. (Makofi)
MHE. ALOYCE A. KWEZI: Mheshimiwa Spika, ahsante, naomba kupata ufafanuzi. Wilaya ya Kaliua hatuna ofisi ya OCD (jengo la polisi la Wilaya); je, Serikali iko tayari kutenga bajeti kwa ajili ya ujenzi ambapo pale Kaliua eneo lipo tayari?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, Serikali ipo tayari kushirikiana na Wilaya ya Kaliua ili kuhakikisha kituo hicho kinajengwa. Kwa kuwa tayari wana eneo, tutawasiliana na IGP ili kwenye mpango wake wa miaka kumi wa kujenga vituo vya polisi ngazi ya Wilaya, Kaliua iweze kupewa kipaumbele pia.
MHE. ALOYCE A. KWEZI: Mheshimiwa Spika, napenda kuuliza swali; katika Jimbo la Kaliua kuna Kata ambazo ziko kwenye programu ya kupata mawasiliano ya simu hususani Iyagala, Isawima pamoja na Ugunga; je, ni lini Serikali itaanza utekelezaji wa kuweka minara katika eneo hilo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge wa Kaliua, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, utekelezaji wa ujenzi wa minara katika maeneo mbalimbali nchini unaendelea na uko katika hatua mbalimbali. Nimhakikishie kabisa Mheshimiwa Mbunge kwamba, tumetoa maelekezo kwa watoa huduma, ndani ya Mkataba ambao tumekubaliana nao, hatutowaacha ifike miezi ishirini ndiyo tuseme kwamba umekamilisha au haujakamilisha. Tumepeana kwamba kila baada ya muda fulani watupatie taarifa ya utekelezaji wamefikia wapi ili tuweze ku-monitor na ku-evaluate kadri mradi wa utekelezaji unavyoenda. Kwa hiyo nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kuhusu Jimbo la Kaliua utekelezaji utaendelea na sisi Serikali tunalitazama kwa makini sana ili wananchi wa Kaliua waendelee kupata huduma ya mawasiliano, nakushukuru sana.