Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Aloyce Andrew Kwezi (5 total)

Hotuba ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyoitoa wakati wa Ufunguzi wa Bunge la Kumi na Mbili, Tarehe 13 Novemba, 2020
MHE. ALOYCE A. KWEZI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana na mimi naomba nianze kwa kuwashukuru sana wananchi wangu wa Jimbo la Kaliua lakini pili naomba nimshukuru sana Mheshimiwa Rais na Chama changu Chama cha Mapinduzi na tatu nishukuru familia yangu kwa kusimama na mimi katika kipindi chote cha uchaguzi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimesimama hapa ili niweze kuishukuru sana Serikali kwa michango mizuri ambayo imeweza kutusaidia. Suala la kwanza ni kama alivyotoka kuliongelea Mbunge mwenzangu hususani maji. Tabora tumepata Mradi wa Ziwa Victoria wa shilingi bilioni 617 na tunaamini kabisa kuanzia mwezi wa Tano tunatarajia kabisa maji yale yataelekea katika jimbo la Kaliua, Sikonge na maeneo mengine.

Mheshimiwa Spika, kwa fadhila hizo tunaishukuru sana Serikali kwa upendo wa wananchi hususani kuwatua akinamama ndoo kichwani, naomba nichukue nafasi hii kushukuru kwamba Hospitali ya Wilaya ya Kaliua kwetu tulikuwa hatujakamilika, lakini hivi karibuni tumepokea zaidi ya shilingi bilioni moja kwa ajili ya kukamilisha Hospitali ya Wilaya ya Kaliua. Lakini tumepokea fedha za madarasa tumepokea, fedha za maabara na tumepokea fedha za ukumbi kwa Mkurugenzi, naomba nimshukuru sana Mheshimiwa Rais, na nishukuru watendaji wote wa upendo kwa niaba ya wananchi wote ambao tunaendelea kuwasaidia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mimi ningependa kuboresha sehemu ambayo Wabunge wenzangu wamechangia wengi wamechangia hususani suala nzima la barabara. Barabara naona changamoto kubwa kwanza ni kubadilisha ceiling ya TARURA lazima fedha ziongezwe TARURA ili wananchi waweze kunufaika na barabara za vijijini. Hivi tunavyoongea, zipo kata mpaka sasa hivi hazifikiki kata kama Usinge kwenye jimbo langu barabara imekatika, kata kama Useni kilometa 60 barabara imekatika kwa kweli hiki kitu kinatuumiza sana na mimi nilikuwa najiuliza kwa sababu nilikuwa Mtendaji kipindi cha nyuma, hivi zile fedha za emergence ziko wapi siku hizi? Mimi ninajua ni Mfuko wa Dharura inapotokea dharula basi una-take cover muda ule ule, barabara inakatika kata zaidi ya watu 60,000 inaachwa Mfuko wa Dharura tunakwenda kwa stahili gani hii.

Mheshimiwa Spika, emergence fund iwe kwenye level ya mkoa ili taarifa zinapofika ndani ya wiki moja basi tunapotoa taarifa kwamba kuna barabara imekatika kule wananchi wasibaki kisiwani, kwa hiyo nilikuwa nashauri hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini jambo lapilli ningelipenda kushauri ni suala nzima la afya. Sisi wote tuko hapa kwa sababu mama zetu walijifungua vizuri ndiyo maana tumefikia level hii na ninaipongeza kwa kuanza vituo vya afya vile 487 ambavyo tumeanza navyo. Mimi nina uzoefu kidogo kwenye sekta hii, operation kwenye kituo cha afya kimoja natoa mfano wa Kilolo kilikuwa kinaitwa Kidabaga, ndani ya miezi mitatu mama zangu waliokuwa wanajifungua walifanyiwa operation akinamama 158; sasa nilikuwa najiuliza hivi kwa kweli tunashindwa kwenda kama tumeweza kwenye kata, kama tumeweza kujenga shule za kata, ni kwa nini tusiongeze nguvu zaidi kwenye vituo vya afya ili kila kata iwe na kituo cha afya? Kwa sababu ajali nyingi za bodaboda zinatokea, operation zingeweza kutusaidia x-ray zinakuwepo pale kwenye kituo cha afya, lakini akinamama wanaojifungua ndiyo naona ni shida kubwa sana kutoka Makao Makuu ya Wilaya mpaka ukafike kijiji cha mwisho kilometa 250 kituo hakipo. Ni lazima tuangalie hiki kitu na tukipe kipaumbele cha pekee. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini jambo la tatu ambalo mimi ningeweza kushauri Serikali nilikuwa naishauri Serikali kuhusiana na suala zima la hifadhi, nakushukuru sana Waziri Mkuu Mungu akubariki sana ulipotoa ufafanuzi kuhusiana na mipaka ni kweli kabisa ni changamoto na ningeshauri pamoja na Waziri wa Maliasili, lakini ashirikishwe Waziri wa Ardhi kwa sababu unaweza ukakuta unasema mpaka huu hapa, wananchi wanasema mpaka wetu unahishia hapa siku zote, professionally watu wa ardhi watuambie kwamba huu mpaka unapita eneo fulani kwa kweli kumekuwa na changamoto sana hususani Kaliua kwenye suala nzima la hifadhi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba niseme naunga mkono hoja nashukuru sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora
MHE. ALOYCE A. KWEZI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana naomba nichukue nafasi hii kwanza kumpongeza Waziri kwa uteuzi, Naibu Waziri nakupongeza watumishi wote wa Wizara hiyo ya Menejiment ya Utumishi wa Umma. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nichangie kwa kuangalia wananchi na watumishi walioko katika jimbo langu, Jimbo la Kaliua, pale tuna watumishi karibu 2,800; wamenituma watumishi hawa, natambua pamoja na watumishi wengine kwenye utumishi wetu kwenye nchi hii ya Tanzania wanaitaji kulipwa fedha zao kwa maana ya madai, madai haya mara ya mwisho imelipwa mwaka 2016; mwaka 2017 uhakiki umefanyika wa madai ya likizo, madai ya matibabu, madai ya uhamisho, madai ya mafunzo watumishi hawa hawajawahi kulipwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa tumefanya uhakiki nchi nzima, lakini kulipa hatujawahi kuwalipa. Ninamuomba Mheshimiwa Waziri ahakikishe watumishi hawa tuwarudishie morali yao ya kufanya kazi kwa kuhakikisha wamelipwa maslahi yao. (Makofi)

Niomba niongelee malimbikizo ya mishahara, hapa napo kuna changamoto kubwa sana, mtu amepanda daraja mwaka 2012, mwaka 2014 mchahara ukabadilika anadai malimbikizo, sasa miaka hii yote malimbikizo bado hajalipwa, shida ni nini? Watumishi hawa tunawavunja mioyo, watumishi wamefanya kazi kubwa sana za kubadilisha maendeleo makubwa sana kwenye nchi yetu, hata kwenye jimbo langu bado wanaendelea kujenga hospitali, madarasa wanasimamia wanafundisha watoto wetu, lakini kwa kweli morali ya watumishi inashuka.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia watumishi hawa hata increment mara ya mwisho ni mwaka 2014 kupata increment, walikuwa wanapata kila Julai wanapata increment kwenye mshahara kunaongezeka fedha kidogo, wanaweza kukopa, sasa matokeo yake kule kwenye utumishi sasa hivi mimi naona kama hadhi ya watumishi wa umma imeshuka kidogo. Imeshuka kwa sababu watumishi wanakopa kuliko kiwango, napengine tumewadhibiti kupitia mfumo wa Lawson wa utumishi ambao upo kwamba wanakopa one third, lakini wanakwenda kukopa kwenye wakopeshaji bubu.

Mheshimiwa Naibu Spika, wanakabidhi saa nyingine mpaka kadi zao benki, sasa tunakwendaje? Mimi nilikuwa namuomba Mheshimiwa Waziri waangalie sekta ya utumishi waiboreshi ipasavyo, na pengine kwa wale wastaafu sasa, hapa napo kuna shida, mstaafu anastaafu anadai malimbikizo hajalipwa, lakini kinachoumiza sana wastaafu unapostaafu unafatilia michango yako unakuta Wizara ya Fedha namuomba sana kaka yangu Mheshimiwa Mwingulu Nchemba watumishi unakuta hatukuchangia ipasavyo na ninyi pale mnachelewesha pelekeni zile fedha za wastaafu kwenye Mifuko ya Hifadhi ya Jamii, wastaafu hao waweze kulipwa fedha zao. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wewe umestaafu umefikisha miaka 60, umefikisha miaka 55 unakuta kuna gap kubwa sana huku nyuma, una miaka miwili kwamba hukuchangia, fedha yako haijaenda, anaanza kuzunguka huyu mzee, utumishi wa umma anatakiwa aone furaha ya kulitendea kazi Taifa lake, lakini hapa bado lipo shida. Niombe nashukuru sana wakati wanawasilisha TAMISEMI hapa wakaongea kwamba tunaenda kuziangalia RS zile Sekretari za Mikoa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi namshauri Waziri wa Utumishi, shida iko hivi pale kwenye RS ili twende na utendaji mzuri watumishi wengine wa RS wamekuwa ni ma-junior hawajafikia kwenye senior post, hawajafikia kuwa waandamizi. Sasa mtu ajafikia kuwa mwandamizi kwenye Halmashauri kuna watu wana miaka zaidi ya kumi na tano, Maafisa Mipango, Maafisa Utumishi, Wakuu wa Idara, wenye sifa za kutosha kupanda kwenda RS, tumewaacha wale pemeni, tunaangalia RS mtumishi ana miaka miwili, anakuja kuongoza, ana mwongoza Afisa Mipango mwenye miaka 15. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, yaani kuna muda tulikuwa tunaona vichekesho kwa sababu wewe inabidi kumshauri sasa kwamba ndugu yangu hiki hapa kipo moja, mbili, tatu. Sasa ni nini hiyo succession plan iko wapi, maana yake mfumo wa kurithishana madaraka wale ambao wako competent kwenye level ya Halmashauri wapande kwenda Mikoani wale ma-senior. Sasa sisi tunaacha huku tunampa mtu wa miaka miwili anamwongoza mwenye miaka 20 yule kule ana Ph.D ana Masters, anafanya kazi vizuri, kwa nini tusichukuane yule tukapandisha wale ambao wanaanza at least ajifunze? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, na hili linafanana, shida ambayo ilitukuta kwa Hayati ndio succession plan yenyewe hiyo, mama yupo competent kachukua nafasi pale, shida iko wapi? Kwa nini huku bado kuna gap? Kwa hiyo, nilikuwa nashauri tuangalie vizuri eneo hilo ili tuweze kwenda pamoja. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kingine kikubwa zaidi ni kuboresha vitendea kazi, tunawasaidia Waratibu wa Elimu wa Kata pikipiki, tunasahau Watendaji wa Kata, Maafisa Tarafa. Sasa kwenye kata mkubwa wa kata ni Afisa Mtendaji wa Kata, sasa Afisa Mtendaji wa Kata pembeni hakuna ka- incentive kokote kwake, tumeangalia yaani chini yake kule kuna mtu anapata posho ya madaraka, sasa kwa nini na wenyewe tusiwaangalie ili twende vizuri?

Mheshimiwa Naibu Spika, upungufu kwenye sekta ya utumishi, nataka nichangie sehemu moja mahususi kweli kweli. Maana ukiangali Maafisa Kilimo wachache, hata kwenye jimbo langu ni hivyo hivyo, ukiangalia manesi wachache, ukiangalia sijui nini wachache. Lakini hebu twende kwenye human resource allocation tupange watumishi wetu vizuri, centers zina watumishi wamezidi. Centers kubwa zinawatumishi wamezidi, miji zimezidi, manispaa zimezidi, sijui wapi imezidii, kule unakuta mwalimu wawili, watatu. Ukiangalia sehemu fulani hakuna uwiano wako 40/50 sasa tunasaidia Taifa au tunakwendaje kwenye mfumo huo? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nilikuwa nafikiria tuwapange kwanza vizuri hao, lakini tuajiri watumishi wa kutosha kwenye sekta zetu. Afisa Ugani mmoja ana control kata mbili tunategemea kweli kilimo kiinuke hapa? Bado itakuwa ni changamoto. Utumishi niwashauri kingine, ikama zinaidhinishwa kila mwaka za kuajiri, tuna miaka hatujaajiri.

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga hoja mkono, ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi
MHE. ALOYCE A. KWEZI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwanza, naomba nichukue nafasi hii kuwapongeza Wizara hii ya Ujenzi kwa kazi nzuri ambazo wanalifanyia Taifa letu na hususani Mkoa wa Tabora ambao kwa kweli sehemu kubwa tunakwenda vizuri. Nisisite kumpongeza Mheshimiwa Waziri, Katibu Mkuu wake pamoja na Meneja wetu wa Mkoa wa Tabora. Meneja yule kwa kweli ningeomba Wizara pengine hata mmuandikie barua ya pongezi kwa kazi nzuri ambazo anaziendeleza katika Mkoa wetu wa Tabora. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi yangu maombi tu, pale Kaliua barabara ya kutoka Urambo imepita Kaliua na sasa ipo mpaka karibia na Usinge, lakini bypass ya kwetu pale ni kilometa 5.5. Kwa sababu barabara imepita kulia, imeacha Kata za Ushokola, Kaliua Mjini pamoja na Kasungu, maeneo haya yote naomba hii barabara ambayo inapita katikati ya Mji na Stendi na wafanyabiashara wakubwa wa Kaliua pale tuwasaidie tuweze kujenga ile bypass ili waone faida nzuri ya utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili ambalo naomba ni kuanzia Usinge, wanapojenga ile barabara ya Kazilambwa – Chagu, kutoka pale ni kilometa 4 kuingia Usinge Mjini. Naomba na penyewe wasije wakasahau kuhakikisha kwamba hata kama siyo mwaka huu, wakianza mwaka huu Kaliua hizo kilometa 5.5 basi kwa Usinge mwakani wanaweza wakaweka kuingia mjini kwa sababu Usinge ni sehemu kubwa na ina kata karibu tatu na karibia asilimia 23 ya wakazi wa Kaliua wanapatikana Usinge pamoja na Kata ya Usenye. Kwa hiyo, tunaomba hizo lami kilometa 5 waweze kutusaidia pale Kaliua Mjini na kule kilometa nne. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, la tatu, naendelea kuwashukuru, kuna barabara nimeona kubwa kweli ya kutokea Kahama – Ushetu – Igwisi – Kazaroho – Kaliua – Zugimlole kilometa 60 mpaka Mpanda, tumeona pale mmetuwekea daraja. Kwa awamu hii mimi naunga mkono kwa kweli tujengeeni kwanza daraja, mmetuandikia hapa mnatutafutia fedha, hizo fedha mhakikishe mnazipata ili barabara hii ya kiuchumi ya kutokea Mpanda kupita Kaliua mpaka Kahama iweze kukamilika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini la mwisho, pale Kaliua ni junction abiria wanaotumia treni kutoka Kigoma wakifika Kaliua wakishuka wanatumia treni inayokwenda Mpanda; eneo lile naomba waongeze muda wa treni kwa sababu muda wa kusimama treni Kaliua ni mchache, ni dakika kumi na ile ni junction ina abiria wengi sana. Kwa hiyo, naomba waboreshe pale kwa kuongeza muda ili uwe wa kutosha. Jambo la pili pale pale ni tiketi, Kaliua tiketi hazitoshi, naomba watupe tiketi za kutosha sisi bado tunatumia sana usafiri wa treni. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini la tatu hapo hapo, ni usimamizi kwenye vile vituo vidogo, kituo kama kilometa 34, kilometa 48 mpaka Mpanda. Naomba maeneo hayo toeni muda wa kutosha kwa sababu treni inasimama dakika moja unaona imeondoka, mnasababisha ajali. Kwa hiyo, naomba wananchi wa maeneo hayo waweze kuongezewa tiketi na muda wa kutosha kwa ajili ya kuhakikisha wanasafiri vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nashauri pia Wizara pamoja na kazi nzuri walizofanya, ile reli ya kutoka Kaliua kwenda Mpanda ni mbovu mno, wanatumia saa kumi. Sasa saa 10 kwa kilometa chache hizo karibu kilometa 180, naomba waiboreshe wakati tunasubiri hiyo Standard Gauge ambayo inakuja, waikarabati reli hiyo vizuri tupunguze hata muda wa kusafirisha mazao yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kuyasema hayo, nirudie kuipongeza sana Wizara hii kwa kazi nzuri wanazozifanya lakini nawaomba wasisahau kurekebisha zile kilometa 5 za Kaliua mjini pamoja na taa za barabarani, maana wale wananchi wakifika tu Urambo, wanaona Urambo bypass yao ipo safi na taa za barabarani wanauliza Mbunge yupo wapi nami napenda nirudi awamu ijayo. Ndugu zangu chondechonde nawaomba kabisa kwenye bajeti hii muendelee kuwa wasikivu na kunihakikishia mmeniwekea hizo kilometa 5. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kuyasema hayo, nawashukuru sana, naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Kilimo
MHE. ALOYCE A. KWEZI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Binafsi nakushukuru wewe kwa hekima na busara zako za kuongoza Bunge letu. Pia nichukue nafasi hii kuwapongeza sana Waziri, Naibu Waziri na timu nzima ya watendaji kwenye Wizara ya Kilimo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimesimama hapa kwa niaba ya wananchi wa Wilaya ya Kaliua hususani Mkoa wetu mzima wa Tabora kuhusiana na zao la tumbaku. Naomba Wizara hii itusaidie, kwanza kabisa kwenye zao la tumbaku kumejitokeza changamoto kwenye soko. Bei elekezi ya zao la tumbaku Serikali imetoa ni dola 1.61 lakini pia gharama ya mkulima kuzalisha anatumia dola 1.4, wanunuzi walipokuja wamenunua chini hata ya gharama ya wakulima; wamenunua chini ya dola 1.2. Haya yametokea siyo kwenye Jimbo la Kaliua peke yake pia yametokea kwenye maeneo ya Usimba, Kasungu, Kaliua Rural, Kamsekwa, Igwisi na maeneo mengine. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, zao hili la tumbaku limekuwa na changamoto, ambaye ananunua vizuri kabisa ni kampuni ya GTI, lakini kampuni ya Alliance One wamenunua tofauti kabisa wakati wale ma-valuer wa Serikali wamefika wakatathmini bei ikaonekana ni nzuri walipofika GTI wakanunua kwa bei nzuri lakini walipokuja kununua hawa Alliance One wamenunua kwa bei ya chini sana ambayo inaumiza wakulima. Naomba Wizara iingilie kati kuhakikisha masoko ambayo yamefanyika katika kipindi cha mwezi mmoja uliopita bei ya wakulima iweze kupanda kama tathmini ya Serikali ilivyokuwa imesema. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niongelee CSR kwenye kampuni hizi, kampuni ya GTI hii imetusaidia sana inatoa CSR, tunajua madhara pia ya tumbaku, wanatu-support madarasa, zahanati, vituo vya afya, hata mimi kwangu Usinge wameleta milioni 500. Huyu Allowance One ambaye ananunua sana tumbaku kule hata CSR kwa maana ya huduma za jamii ha-support. Sasa kwa nini yeye anakuwa tofauti na wanunuzi wengine? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuna kampuni ya Grand Tobacco Limited pamoja na Majestic, wamenunua tumbaku msimu wa 2019/2020 mpaka sasa hawajalipa wakulima wa tumbaku. Pale kwangu kuna chama kinaitwa Mwamko kinadai shilingi milioni mia moja na moja mpaka sasa hawajawalipa. Kibaya zaidi wamerudi kwenda kufunga mkataba yaani unamdai, hajalipa, halafu umefunga mikataba na vyama vya msingi. Naibu Waziri alikuja akatuahidi kulishughulikia lakini muafaka bado, naomba Bunge litusaidie kwenye zao hili la tumbaku. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwenye zao hili hili la tumbaku nashangaa sana tumewekewa ukomo wa kulima yaani wewe unaambiwa zalisha kilo mia mbili wakati wewe una uwezo wa kuzalisha zaidi ya kilo mia mbili, hii limit kwa nini wanaiweka? Ni kwa nini Wizara isiingilie kati na kuhakikisha tunapata masoko? Lazima tusimame pamoja kupata masoko ya kutosha. Naomba hii limit iondolewe kwa wakulima wazalishe kadri ya pembejeo wanazopata na uwezo walionao. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba pia Wizara itusaidie kuhusiana na kilimo cha alizeti katika Mkoa wa Tabora. Tabora alizeti inakubali, Singida na Tabora unaitofautishaje, hali ya hewa ya Kaliua, Urambo, Igalula, Nzega na Igunga inafanana na alizeti tunalima. Hizi mbegu ambazo zimesambaza kwenye mikoa mitano kama alivyokuwa analia wa Kilimanjaro tunaomba zifike Tabora. Kwa heshima zote nawaomba waingilie kati watusaidie. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini niwapongeze kwa jambo kubwa sana, jiografia ya Kigoma inafanana na ya Tabora, mmetusaidia kwenye Jimbo la Kaliua mmetuletea michikichi miche karibu laki moja na nusu. Naomba sambazeni miche ile katika mkoa wote wa Tabora kwa sababu haya mazao yanakubali kwenye Mkoa wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba nizungumzie suala la pembejeo na nina ushauri; CRDB Bank na mabenki mengine yanatusaidia lakini Benki yetu ya Kilimo kwa nini isitusaidie kwa sababu riba ya pembejeo ikitoka kwenye TADB itakuwa ni ya chini kuliko ambavyo ipo kwenye mabenki mengine. Asilimia nane ni kubwa, naamini hata kule wanako-support kama TADB akisimama vizuri tutakuwa na mchango mzuri sana na wananchi watanufaika sana kwa sababu asilimia 80 ni wakulima na sisi tumesimama hapa leo tumesomeshwa na wakulima, kama siyo alizeti basi ni kahawa, kama siyo tumbaku basi ni zao lingine. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ushauri wangu wa mwisho uende kwenye kilimo cha umwagiliaji. Yapo maeneo tunapoteza maji, mafuriko yanatokea hivi tumeshindwa ku-design mabwawa ya kutosha ili kila kiangazi tuzalishe nyanya, vitunguu na mazao mengine ya umwagaliaji. Hatuna sababu ya kudharau kilimo cha umwagiliaji. Nawaomba Kata ya Zugimlole tuwekeeni bwawa pale, Igwisi tumesha design bwawa tunaomba mtuletee fedha, lakini Igagala Namba Tano tume-design bwawa, tunaomba mtuletee fedha hizo ili ziweze kutusaidia.

Mheshimiwa Spika, nimalizie kwa kuwapongeza Wizara hii kwa umakini, unapowapa taarifa wanakuja haraka na wanatusaidia kutatua migogoro mbalimbali. Kwa hiyo, mimi nikuombe Mheshimiwa Waziri Profesa wangu na Naibu wako makini kabisa Mheshimiwa Bashe, msilale, hiki kilimo ndiyo kinatufanya sisi tuonekane tumetekeleza Ilani ya Chama cha Mapinduzi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mwisho kabisa siyo kwa umuhimu CSR nyingi sisi tunazipata kupitia mazao ambayo yanapatikana kwetu na hususani tumbaku. Halmashauri zetu mapato ya ndani zinategemea kwenye tumbaku, naomba hawa watu muwabane walipe, wanapolipa Halmashauri zikapata mapato ndiyo tunaweza kusaidia Serikali Kuu kwenye ujenzi wa vituo vya afya, barabara, kununua mitambo ya barabara na mambo mengine ya msingi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema haya, nashukuru kwa hekima na upendeleo ambao umenipatia mimi. Nakushukuru sana, Mungu akubariki, naunga mkono hoja asilimia mia moja. (Makofi)
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022
MHE. ALOYCE A. KWEZI: Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru kwa kunipatia nafasi hii ya kuweza kuchangia, lakini kwa nafasi ya pekee naomba tu nianze kwa kuwapongeza sana Wizara ya Fedha kwa maana ya uratibu mzuri wa bajeti kuu.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba pia nimpongeze sana Mheshimiwa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kwa nafasi ya pekee mama huyu kwa kweli ni msikivu sana na usikivu huo utauona kabisa, kwa mfano mimi katika bajeti iliyopita nilichangia sana kwenye masuala ya Utumishi nikaongelea stahili za Watendaji wa Kata pamoja na Wabunge wenzangu, tukaongelea stahili za Maafisa Tarafa na tukaongelea masuala ya promotion kwa watumishi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hivi ninavyokwambia karibu halmashauri zote wapo busy kuendelea na upandishaji wa vyeo kwa watumishi. Sio hilo peke yake utekelezaji tumeuona kwa ile laki moja moja ambayo inakwenda sasa kwa Maafisa Tarafa na pia kwa Watendaji wa Kata. Siyo hilo peke yake bado kwa wale wastaafu tulilalamika hapa, tumeona mkakati ambao amekuja nao, Mheshimiwa Waziri na usikivu wa Serikali unaonekana moja kwa moja. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo naomba nisimame nitembee kifua mbele na niwaombe wenzangu tutembee kifua mbele kwa kuamini kwamba, ushauri tunaoutoa ni shauri ambao unasikilizwa na unatekelezwa. Maana yake hakuna kitu kizuri unaposhauri halafu kikafanyiwa kazi na ndiyo maana ya Ubunge, tungekuwa tunashauri halafu msifanyie kazi, kwa kweli tungekuwa tunasema mbona ili tulilisema hakuna ambacho kimefanyika.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwaweli nimejisikia faraja sana, ndiyo maana narudia kumpongeza sana Mheshimiwa Rais kwa usikivu wake. Kwa namna hii naamini kabisa Watanzania wengi hata ukipita vijiweni wanajisikia furaha na amani kwa Serikali ya Awamu ya Sita imekuwa ni Serikali sikivu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niwapongeze kwa miradi ambayo inaendelea, ukifuatilia bajeti kuu miradi mikubwa yote ya kimkakati bado inaendelea na mama mpaka tunavyoongea yuko Mwanza ametoka kuzindua reli, lakini jana nimeona anazindua masoko ya dhahabu. Pakubwa zaidi ambapo amepalenga na ambapo ndiyo kilikuwa kilio kikubwa cha Wabunge ni suala kubwa la TARURA. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Mwigulu Nchemba sitaki nimpongeze kwa namna ya kuuma ulimi, nampongeza hapa akiwa ananiangalia kwamba kazi aliyoifanya na ushauri aliofikisha Mwenyezi Mungu ambariki sana, kwa sababu kwenye TARURA mazao ya wananchi wote wanafahamu yanauzwa bei ya chini kutokana na barabara. Mwananchi anatoka na mzigo wake kule wa mahindi, vitunguu, nyanya na alizeti, anakutana na barabara hakuna daraja, hakuna karavati na maji yapo kiunoni. Kwa hiyo matokeo yake yananunuliwa mazao yao kwa bei ya chini.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo kwa alternative hii ambayo waekuja nayo, naomba niwapongeze sana na wasimamie hilo. Wasimamie hilo ili waturahisishie sisi kujibu maswali, maana yake tukimaliza Bunge hapa tutakuwa kwenye majimbo yetu, tutakuwa kwenye mikoa yetu, kwa hiyo itakuwa ni fursa nzuri ya kuwaambia nini ambacho tumekisema na nini ambacho Serikali sikivu imetekeleza.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo kubwa lingine ambalo nimeliona hapa na ni lazima niliseme kwenye Kamati yetu ya Ardhi, Maliasili na Utalii. Pale kwenye utalii nimefurahishwa sana kwasababu tulikuwa tunapata wasiwasi kwenye Kamati kwamba utalii ni sekta ambayo inatuingizia fedha za kigeni, lakini baada ya kuondoa yale mapato yanaenda moja kwa moja kwenye Mfuko Mkuu ule, tukawa na wasiwasi watatuzoroteshea maendeleo ya utalii. Sasa niwaombe kwasababu wanatoa in advance labda miezi miwili, wamefanya akili ya ziada sana, kwa hilo nawashukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, bado nawaomba jambo kubwa kwenye mapato yetu ya ndani, ni lazima zaidi ya hapa tuimarishe sehemu gani kwenye utalii. Kwenye utalii, katika hifadhi zetu kuna maeneo au hifadhi wakati wa masika hazifikiki kabisa. Sasa tunahamasisha Watanzania waende kwenye maeneo ya hifadhi, naomba nitoe mfano wa Kitulo National Park, tulitaka kwenda pale Kitulo tukaambiwa kwa muda huu wa mvua, Kitulo barabara haifikiki. Pia tukataka kwenda kuna Ziwa moja linaitwa Ngosi ikashindikana, sasa hizo ni sample mbili, lakini nilikanyaga Biharamulo kuingia kule Burigi ikawa na yenyewe kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa naomba hapa tushauriane vizuri, tunahitaji fedha kwa ajili ya maendeleo ya nchi yetu na kwa ajili ya miradi, nashauri tu-inject fedha nyingi kwenye kuboresha miundombinu ile ya kwenye hifadhi zetu ili hata kama ni masika watu wanataka kwenda Christmas kupumzika mwezi wa Tatu wanataka kwenda mle, pamoja na sikukuu zetu hizi za kuchinja, wawe na uwezo wa kwenda kule kula vitu vyao vizuri wakati wa masika na wakati wa kiangazi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo ningeweza kuwashauri, kwenye sekta ya afya nafahamu kabisa ziko kata hatujakamilisha shule na zipo tarafa ambazo hatuna vituo vya afya, hebu tujaribu kwenye hizi fedha ambazo wameangalia, nafikiria tuwabane kidogo, unajua unapoenda kutoa fedha kwenye M-pesa, kwenye Halopesa, kwenye Tigo pesa na kwenye Airtel Money, kama unatoa milioni moja au unatuma milioni moja unakatwa labda 3,500 au 4,000. Unapokwenda kutoa unakatwa tena 8,000/=.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomb tujaribu kuangalia hapo je, hatuwezi kuongea na makampuni yetu, yalipe kodi kama kawaida maana yake tusichezee kodi, lakini bado tuangalie ile fedha ambayo ilikuwa inapotea pale kwenye zile transactions, naona ile fedha ni kubwa. Yaani muamala nimekutumia hapo Mheshimiwa unaupokea, mimi niliyetuma nakatwa, wewe ukinyanyuka kwenda kutoa unakatwa karibu 8,000 mpaka elfu 10,000 na zaidi. Sasa ile fedha ni nyingi, kwa nini tusiongee, kwa sababu ni suala la uzalendo na wana- exist nchini kwetu na tunafanya nao kazi, tuwashawishi kwamba if possible, basi angalau na wenyewe wajaribu kuachia shilingi elfu moja moja ziende kwenye TARURA, kwa sababu barabara za vijijini ndiyo mishipa ya uchumi wetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, tukitaka tuyapunguze maneno mengi ni hapo ambapo tumelenga kwenye TARURA, afya, elimu na maji. Haya maeneo tukibana vizuri, naamini kabisa mwelekeo wetu utaendelea kuwa vizuri na kama nchi tutaendelea kutembea kifua mbele kwa kuhakikisha tunawasaidia wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine kubwa naendelea kupongeza ni la Madiwani wetu, nawaambia kabisa by professional mimi ni Afisa Utumishi, kwa hiyo nimekaa halmashauri karibia miaka 15 ninachokiona…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. ALOYCE A. KWEZI: Mheshimiwa Naibu Spika, ndiyo ya kwanza?

NAIBU SPIKA: Malizia sentensi yako unachokiona…

MHE. ALOYCE A. KWEZI: Mheshimiwa Naibu Spika, ninachokiona ambacho ningekishauri, inawezekana kuna halmashauri ambazo wakawa na wasiwasi kuwalipa moja kwa moja, naomba kupitia ule Mfuko Mkuu wajaribu kuziangalia zenye uwezo mkubwa sana, ndiyo iwe hivyo kwa maana yale majiji makubwa yenye fedha, lakini hizi halmashauri zingine zote zinasuasua, wahakikishe wanawalipa kupitia hii Serikali Kuu moja kwa moja, kusiwepo kwamba hiki na hiki, zile za daraja A, zile halmashauri kama Kinondoni hapo sawa.

NAIBU SPIKA: Haya ahsante sana Mheshimiwa.

MHE. ALOYCE A. KWEZI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nikupongeze sana na naunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)