Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Agnesta Lambert Kaiza (15 total)

MHE. AGNESTA L. KAIZA: Mheshimiwa Spika, nikushukuru kwa nafasi hii ili niweze kuuliza maswali mawili ya nyongeza, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu na takwimu zilizotolewa na Serikali, ukweli ni kwamba kutoka ngazi ya Mkaguzi Msaidizi kwenda Mkaguzi kamili inapaswa kufanyika ndani ya mwaka mmoja mpaka miaka miwili. Je, Mheshimiwa Waziri anayo taarifa kwamba kuanzia mwaka 2015 mpaka muda huu ambapo nimesimama mbele ya Bunge hili Tukufu kuna Wakaguzi Wasaidizi ambao hawajapandishwa madaraja?

Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo, Mheshimiwa Waziri atueleze hapa ikiwa anazo hizo taarifa ni kwa nini basi hao Wakaguzi hawajapandishwa madaraja?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Agnesta Lambert Kaiza, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, si kweli kwamba tangu 2015 mpaka hapa tulipo watu hawajapandishwa madaraja. Kama ataangalia kwenye jibu langu la msingi nilitoa takwimu ambazo zinaonyesha kwamba kuna watu walipandishwa madaraja.

Mheshimiwa Spika, kingine nimfahamishe tu Mheshimiwa kwamba ni vizuri wakapata nafasi wakaipitia hii PGO (Police General Order) itawasaidia kujua baadhi ya taratibu ambazo zinatumika kupandisha madaraja. Kuna mambo ya msingi huwa yanaangaliwa, siyo kwamba watu wanapandishwa tu kwa sababu hawajapandishwa muda mrefu. Kwanza, lazima kipatikane kibali cha kupandisha majaraja. Pili, tunaangalia pia uwezo wa kiuongozi wa yule ambaye anatakiwa kupandishwa daraja. Tatu, tunazingatia zaidi vigezo vya kimaadili kwamba tunayekwenda kumpandisha cheo ana maadili gani katika kutumikia Taifa hili. Nne, tunaangalia kama hana mashtaka mengine. Tano, huwa tunaangalia na bajeti maana tukimpandisha cheo lazima tumpandishie na mshahara wake.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, Mheshimiwa afahamu kwamba utaratibu ndiyo huo lakini tumeanza na tumepandisha madaraja mbalimbali kwa watumishi wa Jeshi la Polisi kama ambavyo taratibu zimeeleza.
MHE. AGNESTA L. KAIZA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa ajili ya nafasi hii ili niweze kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Pamoja na majibu aliyoyatoa Mheshimiwa Waziri kwamba, hayaleti matumaini ya moja kwa moja kwa wakazi wa Butiama naomba nijielekeze kwenye maswali kama ifuatavyo; Swali la kwanza; kwa kuwa, miradi hii ambayo Mheshimiwa Waziri ameitaja hapa utekelezaji wake umekuwa ni wa kusuasua sana kwa lugha nyingine umekuwa na mwendo wa kinyonga. Je, nini kauli ya Serikali basi kuhusiana na bili zinazotolewa kwa wakazi wa Butiama bila kupatiwa huduma?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; kwa kuwa, kauli mbiu ya Serikali ya Awamu ya Tano ni kumtua mwanamke ndoo kichwani. Swali langu ni kwamba, ni lini basi Serikali itatekeleza kauli mbiu hii kwa matendo kukamilisha miradi yote ya Serikali nchi nzima ambayo imeonekana kusuasua mpaka sasa? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba majibu kutoka kwa Mheshimiwa Waziri.
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na masuala ya bills, maeneo mengi yalikuwa na tatizo hili, lakini tayari Wizara tunashughulikia kwa karibu kuona kwamba, mtu anakwenda kulipa bili kulingana na matumizi yake. Tunaendelea kuweka mbinu mbalimbali kama kumhusisha moja kwa moja mtumiaji maji kwa kushirikiana na msomaji mita wataangalia kwa Pamoja, watasaini kadi na hapo sasa yule mlipaji atakwenda kulipa bili kulingana na matumizi yake.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na kumtua mwanamke ndoo kichwani; hili suala sasa hivi ni tayari linatekelezeka. Maeneo mengi ya Tanzania sasa hivi akinamama wameshakiri hawabebi tena maji vichwani na tayari Wizara tunaendelea kufanya kazi usiku na mchana kuhakikisha maeneo yote ya pembezoni mwa miji kwa maana ya vijijini nao wanakwenda kukamilika katika mpango huu na kazi zinaendelea. Tayari tuna ari kubwa sana kama Wizara na watendaji wetu wametuelewa mwendo wetu ni mwendo wa kasi ya mwanga. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. AGNESTA L. KAIZA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. Changamoto ya kujaa kwa maji yanayotokana na mvua iliyoko Mkoa wa Mtwara haina tofauti kabisa na changamoto iliyopo Mkoa wa Dar es Salaam hususan eneo la Jangwani. Kujaa kwa maji katika eneo la Jangwani imekuwa ni changamoto ya muda mrefu na haijawahi kupatiwa tiba ya kutosha. (Makofi)

Mhesimiwa Spika, swali langu ni kwamba, je, Serikali ina mkakati gani au inatueleza nini kuhusiana na changamoto hii ya kujaa maji pale Jangwani hasa ikizingatiwa kwamba Jangwani ni kiunganishi kikubwa sana cha wafanyabiashara wanaoelekea Kariakoo eneo ambao limebeba uchumi mkubwa sana wa nchi? Naomba Serikali basi itoe majibu ni lini itaweza kukomesha changamoto hii ya kujaa maji Jangwani. Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana, naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Agnesta Kaiza, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Mbunge amejaribu kuoanisha eneo la Jangwani na maeneo yaliyoko kule Mtwara katika Manispaa ya Mikindani kwamba na lenyewe linajaa sana maji na anataka kufahamu mkakati gani ambao Serikali inao kuhakikisha tunatatua tatizo katika eneo hilo.

Mheshimiwa Spika, cha kwanza nimhakikishie kwamba Ofisi ya Rais, TAMISEMI tuna mradi mkubwa wa DMDP ambao unajenga miundombinu katika Jiji la Dar es Salaam. Sehemu ya miundombinu hiyo ambayo tumekuwa tukiijenga ni pamoja na mifereji mikubwa ambayo imekuwa ikihamisha maji kutoka katika mitaa mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam na kupeleka baharini.

Mheshimiwa Spika, lakini jambo la pili, sasa hivi tuna Mradi mkubwa wa Mabasi Yaendayo Kasi na moja ya jukumu lao kubwa ni kuhakikisha lile eneo la Jangwani linapandishwa tuta kubwa ambalo litahakikisha ile kero ambayo inawapata wananchi inaondolewa. Kwa hiyo, nimhakikishie kabisa Serikali ipo kazini na ile kazi itakamilika na wananchi wa Jiji la Dar es Salaam hawatajutia kuichagua Serikali ya Chama cha Mapinduzi. Ahsante. (Makofi)
MHE. AGNESTA L. KAIZA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, Tume ya Umwagiliaji imekuwa ikipata shida kubwa sana ya bajeti ili kuweza kuteleza majukumu yake yanayohusiana na skimu za umwagiliaji. Je, Serikali ina mkakati gani endelevu wa kuhakikisha Tume hii ya Umwagiliaji nchini inapata bajeti endelevu na si ya kusuasua kama ilivyo sasa?

Mheshimiwa Spika, swali langu la pili, soko la ndani pekee haliwezi kuwanufaisha wakulima wa mazao katika skimu ya umwagiliaji. Je, Serikali ina mpango gani madhubuti wa kuhakikisha mazao haya sasa yanayopatikana kwenye hizi skimu za umwagiliaji yanapata masoko nje ya nchi kuliko ilivyo sasa?

Mheshimiwa Spika, nakushuru sana.
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Agnesta, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba kumekuwa na upungufu wa rasilimali fedha katika maeneo mbalimbali lakini mkakati ambao Serikali unao na hili lilikuwa ni agizo la Mheshimiwa Rais Mama Samia Suluhu Hassan alilolitoa mwaka jana akiwa Makamu wa Rais katika Mkoa wa Simiyu ni kuzifanya subsector zilizoko ndani ya sekta ya kilimo kujiendesha. Wizara ya Kilimo hatua ya kwanza ambayo tumechukua na Bunge hili likituidhinishia bajeti, katika mwaka wa fedha ujao tunaanzisha kitu tunaita Irrigation Development Fund (Mfuko wa Kuendeleza Umwagiliaji).

Mheshimiwa Spika, suala la ujenzi wa miundombinu ya umwagiliaji ni wajibu wa Serikali. Serikali inaenda kujenga miundombinu ya umwagiliaji kwenye mashamba ya wananchi wa kawaida. Hivi karibuni tumefanya mradi kwenye skimu tano kwa zaidi ya dola milioni 22 katika Mkoa wa Morogoro, tunatengeneza utaratibu ambao umo kwenye sheria kwamba tunapowekeza katika eneo la umwagiliaji kunakuwa kuna kuzizungusha zile fedha ili zirudi katika Mfuko na ziweze kutumika katika eneo lingine.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo katika bajeti ijayo mtaona tunaanzisha Mfuko wa Umwagiliaji ambao utakuwa sustainable na revolving ambao utawezesha sekta ya umwagiliaji kuwa na uhakika wa fedha. Tunawashukuru wenzetu wa Wizara ya Fedha wameturuhusu part of that fund ziweze kuwa retained na Mfuko na hazitaenda katika Mfuko Mkuu wa Hazina ili tuwe na uhakika wa kuweza kujiendesha.

Mheshimiwa Spika, jambo la pili katika eneo la umwagiliaji badala ya miradi mingi kuendesha katika mfumo ambao tumekuwa tukiendesha sasa hivi, tunafanya miradi mipya kuanzia mwaka kesho kwa kutumia mfumo wa design and build na kutumia force account kama tunavyojenga shule, zahanati na vituo vya afya katika Halmashauri. Pia tutaiwezesha Tume ya Umwagiliaji kwa kuipatia vifaa ili iweze kufanya miradi yenyewe moja kwa moja badala ya kutegemea njia zingine. Kwa hiyo, hii nadhani itatusaidia sana kupunguza gharama za miradi lakini kuifanya Tume kuwa na uhakika.

Mheshimiwa Spika, kuhusu soko la mazao, siyo tu mazao yanayotokana na skimu za umwagiliaji, dhana yetu ya umwagiliaji mara nyingi tunaitazama katika mpunga tu, kila ukimsikiliza Mbunge au mtu yeyote anaitazama dhana ya umwagiliaji katika suala la mpunga. Sisi tunafanya jitihada ya kufungua masoko ya mazao yote, sasa hivi tunatumia Balozi zetu na hasa mazao ya nafaka, tunaanza communication na nchi ambazo zina masoko tuweze kujenga bonded warehouses kulekule ili wafanyabishara wetu waweze kupeleka mazao na kuyauzia sokoni badala ya kumsubiri mnunuzi atoke Kongo kuja Dar es Salaam au kuja Tanzania kununua. Kwa hiyo, hii ni njia nyingine ambayo tunaitumia, tunaamini kwa kutumia Mabalozi; kupunguza ukiritimba katika biashara ya mazao; kufungua mipaka; kupunguza gharama za biashara na kuongeza tija mazao yetu yatapata masoko ya uhakika.
MHE. AGNESTA L. KAIZA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Pamoja na utoaji na usambazwaji wa maji mijini na vijijini bado kuna malalamiko makubwa sana ya ankara za maji kutokuwa na uhalisia. Je, Serikali ina nini la kusema au kuna tamko gani la Serikali ili kuondoa mkanganyiko huu ambapo wananchi wanabambikwa ankara ambazo hazina uhalisia? Ahsante sana.
WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote nimshukuru Mheshimiwa Mbunge lakini niseme tu wazi ni haki ya mwananchi kupatiwa huduma ya maji na mwananchi ana wajibu wa kulipia bili za maji, lakini wajibu huo wa kulipia bili za maji zisiwe bambikizi. Kwa hiyo, maelekezo ya Wizara yetu ya Maji kwa Mamlaka zote za Maji nchini watoe bili halisia ambazo zimeidhinishwa na EWURA. Ikiwa kuna Mkurugenzi au msoma mita kwa makusudi anambakizia mwananchi bili ya maji tutashughulika naye.
MHE. AGNESTA L. KAIZA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ili nami niweze kuuliza swali dogo la nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukosefu wa dawa na vifaatiba imekuwa ni changamoto karibia nchi nzima. Je, ni kwa nini Serikali basi isihamasishe uwekezaji mdogo na mkubwa wa viwanda vya dawa na vifaa tiba ikiwa ni pamoja na kuondoa Kodi ya Forodha pamoja na masharti mengine ili basi viwepo viwanda vingi ambapo mwisho wa siku dawa hizi zitakwenda kuwasaidia Watanzania na hususani walio wengi huko vijijini?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Agnesta Lambert ameleta pendekezo kwamba ni kwa nini sasa Serikali isione haja ya kuongeza uwekezaji kwenye viwanda vya kuzalisha dawa na vifaa tiba nchini ili kupunguza hii adha? Jambo hili ni jema, ndiyo maana sasa hivi sera ya Serikali ni kuhimiza watu wote wanaotaka kuwekeza nchini waje, ikiwemo kwenye sekta hii ya dawa na vifaa tiba.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, sisi tunawaruhusu watu wote na katika kipindi sahihi kabisa cha kuwekeza ni
sasa, kwa sababu Serikali imeboresha mazingira bora ya kufanya biashara nchini ambayo yanaruhusu wawekezaji wote kuwekeza ndani ya nchi. Ninaamini hao watakaokuja kuwekeza kwenye maeneo ya dawa na vifaa tiba wanapewa kipaumbele zaidi. Kwa hiyo, mazingira ya Serikali yako sahihi na tunawaruhusu na Serikali itaendelea kuwekeza zaidi. Ahsante.
MHE. AGNESTA L. KAIZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Wafanyabiashara wengi wenye mitaji midogo hawana elimu ya kutosha kuhusiana na suala zima la kufanya makadirio yao wenyewe ya kulipa kodi. Jambo hili limepelekea wafanyabiashara hawa mara nyingi kuajiri wataalam wa kuja kuwasaidia jambo ambalo hupelekea wao kutozwa fedha nyingi kuanzia shilingi laki tano, milioni moja na kuendelea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo hili limekuwa ni changamoto sana kwa wafanyabiashara na mwisho wa siku wafanyabiashara wengi wameshindwa kuendelea na biashara kwa maana wamekata tamaa kwa kuwa mwisho wa siku wanajikuta hawapati chochote, kila wanachokifanya kinaishia katika kulipa wataalam.

Je, Serikali ina mpango gani madhubuti wa kutoa elimu sahihi kwa wafanyabiashara hawa hususan wafanyabiashara wa vijijini ambao kimsingi elimu kwao haipo kabisa? Naomba majibu ya Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, wafanyabiashara hawa wenye mitaji midogo walikuwa wamewekewa utaratibu maalum wa makadirio ya shilingi 20,000/= kwa mwaka, lakini mpaka sasa ninapoongea utaratibu huu upo kimya kabisa, ni kama haupo: Je, Serikali ina kauli gani kuhusiana na utaratibu huu ambao upo kimya kwa wafanyabiashara hawa ikiwa ni sambamba na kwa wafanyabiashara wenye maduka siyo tu kwa machinga. Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwanza naomba nimpongeze sana ndugu yangu Mheshimiwa Agnesta kwa namna anavyotetea Wafanyabiashara wadogo nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la taaluma, Serikali kupitia Mamlaka ya Mapato Tanzania imekuwa na utaratibu wa kutoa elimu kwa wafanyabiashara wadogo wadogo na hata wakubwa kupitia runinga, redio, na matamasha. Inawezekana baadhi ya vijiji elimu hiyo haijawafikia. Tutachukua ushauri huu kushuka chini vijijini kabisa kwa ajili ya kupeleka elimu ya kulipa kodi hasa kwa hiari. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili; kuhusu utaratibu wa wafanyabiashara wadogo kulipa ada ya shilingi 20,000/= kwa mwaka bado upo na unaendelea kwa wale wafanyabiashara wadogo wadogo kupitia vitambulisho vya Machinga. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. (Makofi)
MHE. AGNESTA L. KAIZA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili nami niweze kuuliza swali dogo la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, Jiji la Dodoma ni jiji kama yalivyo majiji mengine na hivyo linapaswa kuwa na hadhi zote za jiji. Sasa swali langu; ni lini Serikali itaanza ujenzi wa barabara za mitaani kwa kiwango cha lami kwa mitaa yote ya Jiji hili la Dodoma?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Lambert kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, nataka nimhakikishie kwamba jitihada kubwa sana zinafanyika kufanya kwamba barabara zote za Jiji la Dodoma zinafanyika. Tuna barabara za outer ring circuit na za inner ring circuit, lakini pia barabara zote ziko kwenye mpango kuhakikisha kwamba zinapanuliwa na kujengwa kwa kiwango cha lami ili kuhakikisha kwamba jiji linakuwa kweli na hadhi ya jiji, ahsante.
MHE. AGNESTA L. KAIZA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi. Barabara ya kutoka Kinyerezi kupitia Segerea hadi Tabata Relini ni barabara ambayo imekuwa na changamoto kwa muda mrefu; na Serikali wamekuwa wakiahidi mara kwa mara bila ya utekelezaji.

Mheshimiwa Spika, napenda kufahamu kauli sahihi kuhusiana na barabara hii. Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Lambert, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, barabara ya Segerea kwenda Relini niliijibu wiki iliyopita wakati Mheshimiwa Mbunge wa Jimbo la Segerea alipoliuliza. Nilichosema na bado naendelea kusema, barabara ilikuwa imefumuliwa na kulikuwa na changamoto ya Mkandarasi. Tunapoongea sasa hivi, Mkandarasi yupo site kukamilisha vipande vyote ambavyo vilikuwa vimefumuliwa.

Mheshimiwa Spika, nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba hiyo barabara inaendelea kutengenezwa. Ahsante. (Makofi)
MHE. AGNESTA L. KAIZA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi, naomba niende moja kwa moja kwenye swali langu dogo.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na uwepo wa viwanja vya ndege gharama au nauli za ndege zimekuwa juu sana nini kauliya Serikali kuhusiana na kuhakikisha nauli hizi zinakuwa himilivu kwa Watanzania hasa baada ya kuwa wamehamasika sana?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la nauli ni suala la kibiashara na nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba wenzetu wa ATCL kuna taratibu ukifanya booking mapema bei inashuka lakini kama utanunua tiketi utaratibu wa mashirika mengi ya ndege kama utachelewa kununua tiketi ya ndege siku zote bei inakuwa juu, lakini kama utafanya booking mapema basi nauli inakuwa ni ya chini.
MHE. AGNESTA L. KAIZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushuru kwa kunipa nafasi ili nami niweze kuuliza swali dogo la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa tatizo la uchakavu wa vituo vya polisi ni la nchi nzima; swali langu je, Serikali haioni umuhimu wa kuandaa mpango kabambe wa miaka mitatu kwa ajili ya maboresho ya vituo hivi kwa maana ya kurahishisha ulinzi na usalama wa raia na mali zao? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mbunge Mheshimiwa Lambert, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpe uhakikisho kwamba kwa kutambua umuhimu wa kuwa na mpango mkakati wa utekelezaji Wizara ya Mambo ya Ndani kushirikiana na vyombo vyake imeandaa mpango wa miaka kumi wa ujenzi na ukarabati wa vituo vya polisi. Kwa hiyo, ulilolisema tumeshalifanyia kazi, mpango ule tunaugawa katika vipindi vya miaka mitano/mitano na miaka mitatu mitatu kwa maana ya Medium Term Expenditure Framework (MTF) ili kuvigharamia, ndio maana tunaposema hapa kwamba tunaingiza, tunatoa kwenye ule mpango mkuu wa miaka kumi tulionao. Nashukuru.
MHE. AGNESTA L. KAIZA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Uraia pacha imekuwa ni kilio cha Watanzania walio wengi. Nini kauli ya Serikali rasmi kuhusiana na jambo hili? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba nimwombe Mheshimiwa Lambert swali hili ni mahsusi, liwasilishwe ili lifanyiwe utafiti hatimaye liweze kujibiwa ipasavyo hapa Bungeni. (Makofi)
MHE. AGNESTA L. KAIZA: Mheshimiwa Spika, nikushukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Mradi huu umechukua muda mrefu kutekelezwa na majibu ya Serikali muda wote yamekuwa ni haya; na kipindi kutoka sasa hadi Julai, ambapo Mheshimiwa Waziri amesema mradi huu utakuwa umetekelezwa ni takribani miezi mitatu tu. Sasa swali langu, Mheshimiwa Waziri analihakikishia Bunge hili Tukufu kwamba kufikia kipindi hicho, taratibu zote ikiwa ni pamoja na kulipa fidia wananchi watakaoguswa na mradi zitakuwa zimekamilika?

Mheshimiwa Spika, swali langu la pili; Bonde la Mto Msimbazi ni chanzo kikuu cha mafuriko katika barabara iendayo Kariakoo eneo la Jangwani. Barabara hii inaelekea katika kitovu cha uchumi wa nchi. Sasa, swali langu kwa Serikali;

Je, ni mkakati gani wa dharura umeandaliwa kwa kipindi hiki ambacho mvua zinaendelea kwa kasi katika Jiji la Dar es Salaam?

Mheshimiwa Spika, ahsante sana.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Mbunge, wa Viti Maalum, Mheshimiwa Agnesta Lambert Kaiza, maswali yake mawili ya nyongeza kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, tunapotaka kufanya jambo lolote, hasa jambo ambalo limezunguka kwenye maeneo ya makazi ya watu si kwamba tu tunaangalia kwenye fidia lakini kuna baadhi ya mambo ya msingi huwa tunaangalia. Kwanza katika mazingira kuna kitu kinaitwa EIA, Environment Impact Assessment; kwa hiyo kwanza tunaziangalia athari za kimazingira. Je, tutakapofanya hilo jambo tunaweza tukawaathiri vipi wananchi kwenye hilo. Lakini pia kuna kitu tunakiita PA property assessment, kwamba je, mali za wananchi wanavipando vyao, wana nyumba zao wana makazi mengine.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, kwa ufupi ni kwamba hili jambo tumeshalikali kitako na tayari tathmini inaendelea ni mtoe hofu Mheshimiwa, tunalithibitishia Bunge hili pamoja na hizo tathmini ambazo ambazo zinaendelea lakini bado tunaendelea na kama tulivyoeleza kwamba miezi michache inayofuata ujenzi huu unaanza.

Mheshimiwa Spika, lakini je, tunajuhudi au jitihada gani katika kuzuia mafuriko; nimwambie tu kwamba tumeshakaa pamoja, sisi Ofisi ya Makamu wa Rais, pamoja na maafisa wetu wa mazingira tumekaa na halmashauri tumekaa watu wa TARURA, tumekaa na watu wengine ili kuona namna ambavyo tunaweza tukapunguza angalau hizo athari za mafuriko, zikiwepo za kutengeneza vi-streams vidogovidogo vitakavyoyaondosha maji pale na kuyapeleka maeneo ya bahari ili pale yasituwame na yakapunguza athari kwa wananchi. Nakushukuru.
MHE. AGNESTA. LAMBERT KAIZA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuuliza maswali mawili madogo ya nyongeza.

Kwa kuwa sheria zetu siyo amri ya Mungu na kwa kuwa ndani ya Bunge hili tumekwisha rekebisha sheria mbalimbali. Je, Serikali inapata kigugumizi gani kuleta Muswada wa Marekebisho ya Sheria hii ya Uraia Pacha? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali langu la pili; kwa kuwa Katiba yetu ya nchi inakataza ubaguzi wa aina yoyote ile. Je, Serikali haioni kuwa kama raia wake ambao wamepata urai nchi nyingine kwamba huu nao ni ubaguzi kwao? (Makofi)
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu maswali mawili kwa pamoja ya nyongeza ya Mheshimiwa Agnesta Lambert, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli sheria siyo msahafu na sheria hizi zinatungwa kwa maslahi ya watu, lakini pia zinatungwa kwa matakwa ya watu. Bado Serikali haijajiridhisha kwamba uraia pacha ni takwa la wananchi walio wengi na ndiyo maana hata ukiangalia katika mchakato wa Katiba uliyokwama ambao ulihusisha maoni ya wananchi mbalimbali Serikali ilipendekeza hadhi maalum na siyo uraia pacha. Kwa sababu halikuwa takwa la wananchi waliyo wengi lakini ikitokezea haja hiyo Serikali italiangalia.

Mheshimiwa Spika, sheria hii na hili haina maana kwamba Serikali ina ubaguzi na ndiyo maana tupo katika hatua za mwisho mwisho kuanzisha utaratibu wa kuwa na hadhi maalum kwa ndugu zetu hawa ambao wananchi nje ambao utaweza kuwapa fursa mbalimbali, wataweza kupata fursa nyingi ambazo wenyewe wamependekeza kulingana na maoni waliyotoa. Kuna fursa kama kumi ambazo utaratibu huu utakapokamilika zitaweza kutolewa kwa ndugu zetu hawa Watanzania waliochukua uraia wa nchi nyingine.
MHE. AGNESTA L. KAIZA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili nami niweze kuuliza swali dogo la nyongeza.

Kwa kuwa eneo la makutano ya Mkwajuni, Kinondoni na Mto Msimbazi hukumbwa na mafuriko kipindi cha mvua kama ilivyo Jangwani na hivyo kusababisha adha kubwa sana kwa wananchi wa makazi hayo.

Mheshimiwa Spika, swali langu; je, Serikali ipo tayari kujenga daraja la kudumu ili kuondoa kero hii kwa wananchi ambayo imedumu kwa muda mrefu? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, ahsante, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Lambert Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, daraja alilotaja pia ni sehemu ya Bonde la Jangwani ambalo litafanywa pamoja kwenye Mpango wa DMDP ili kuboresha usafiri katika eneo hilo. Ahsante.