Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Agnesta Lambert Kaiza (14 total)

Hotuba ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyoitoa wakati wa Ufunguzi wa Bunge la Kumi na Mbili, Tarehe 13 Novemba, 2020
MHE. AGNESTA L. KAIZA: Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru sana kwa nafasi hii adimu ambayo umenipatia ili niweze kusema machache kuhusiana na hotuba ya Mheshimiwa Rais.

Mheshimiwa Naibu Spika, kabla ya kuchangia nitumie fursa hii kwanza kabisa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa uzima, lakini pia kwa kunipa afya njema na kuweza kusimama mbele ya Bunge lako tukufu ili niweze kujadili masuala mazima yanayohusiana na hotuba hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, miongoni mwa mambo mengi ambayo Mheshimiwa Rais alizungumza katika hotuba yake ni pamoja na nchi yetu kuingia katika uchumi wa kipato cha kati. Hii ni habari njema kwa Taifa na ni jambo la kujisifia kama Taifa.

Mheshimiwa Naibu Spika, ikiwa ni kweli Serikali yetu imetuingiza katika uchumi wa kipato cha kati, kuna mambo ya msingi sana ambayo yanapaswa au yalipaswa ku-reflect moja kwa moja kwamba sasa Tanzania tumeingia katika uchumi wa kipato cha kati. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba mbele ya Bunge lako tukufu nijikite katika masuala makuu manne ambayo yanaashiria moja kwa moja kwamba ni ama tumedanganywa kama nchi kwamba tumeingia katika uchumi wa kipato cha kati au Serikali imedanganya kwamba sasa hivi imekuwa ikikusanya mapato makubwa sana ambacho ni kiashiria cha ukuaji wa uchumi wa kati.

Mheshimiwa Naibu Spika, mosi, wewe ni shahidi kwamba Serikali imekopa pesa nyingi kutoka kwenye Mifuko ya Hifadhi ya Jamii. Mfano NSSF; Serikali imechukua, au imekopa fedha ambazo Serikali ilitarajiwa irudishe ile mikopo ndani ya ule muda ambao masharti yanasema ili mwisho wa siku sasa wastaafu, mama zetu, mashangazi zetu, wajomba zetu ambao walitumikia nchi hii kwa uaminifu mkubwa sana na baadaye wakastaafu sasa waweze kupewa…

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU (SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU): Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Kaiza, kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Jenista.

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU (SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba tu nimpe taarifa Mheshimiwa Mbunge anayezungumza. Anataka kujenga hoja kwamba Serikali bado haijalipa fedha ambazo ilikuwa inadaiwa na Mifuko ya Hifadhi ya Jamii.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nilipe taarifa Bunge lako Tukufu kwamba Serikali imeshafanya kazi hiyo na mpaka sasa zaidi ya trilioni 1.2 ambazo Mfuko wa PSSSF ulikuwa unaidai Serikali, fedha hizo zimekwisha kurudishwa na Mheshimiwa Mbunge ni shahidi wakati tulipokuwa kwenye kikao cha Kamati, mimi mwenyewe na watendaji wa Mfuko tulishatoa taarifa hiyo kwenye Kamati. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, yapo maeneo mengine ambayo Serikali bado inaendelea kufanya uhakiki. Utaratibu wa Serikali sasa hivi katika madeni yaliyobakia haiwezi kulipa bila kufanya uhakiki, kwa hiyo kila baada ya uhakiki Serikali imeendelea kuwa inalipa madeni hayo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu ya muda, labda nitakapokuja jioni ama wakati wa kuchangia Mpango tutatoa taarifa ya wastaafu wangapi wamekwishalipwa mafao yao na kwa nini labda kumekuwa na kuendelea kuwalipa wastaafu mafao kwa utaratibu mmoja na mwingine. Kwa hiyo maeneo haya tutayatolea maelezo lakini justification ya malipo ya Serikali tunayo na Serikali imelipa na tunaendelea kuhakiki na tunaendelea kulipa yale yaliyokwisha kuhakikiwa. (Makofi)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Agnesta Lambert Kaiza, unaipokea taarifa hiyo?

MHE. AGNESTA L. KAIZA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa nikiri kwamba mama yangu, dada yangu, rafiki yangu mpenzi, anafanya kazi nzuri sana, lakini itoshe kusema kwamba hayo aliyoyasema kwamba Serikali haijalipa ndiyo hayo ambayo nayaongelea mimi.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inasema tayari imetuingiza kwenye kipato cha kati. Kama tumeingia kwenye kipato cha kati na tayari kuna wastaafu ambao waliitumikia nchi hii kwa uaminifu mkubwa sana hawajalipwa, itoshe kusema kuna tatizo. Sasa nimshauri dada yangu na rafiki yangu achukue ushauri wangu huu, kwamba pamoja na kazi nzuri anayoifanya, hili linaitia doa Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niende moja kwa moja katika ajenda yangu ya pili inayohusiana na Serikali kuchelewesha malipo kwa makandarasi. Ikiwa kweli Serikali hii imetuingiza katika kipato hiki cha kati, ilipaswa moja kwa moja kitu cha kwanza kabisa iwe inalipa on time fedha za makandarasi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wewe umesikia jana, leo, juzi, wachangiaji wengi katika Bunge hili wamekuwa wakilalamika kuhusiana na ujenzi wa barabara. Kwa hiyo, unaposikia kuwa…

T A A R I F A

MHE. DKT. CHARLES S. KIMEI: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Kaiza, kuna taarifa.

Waheshimiwa Wabunge, hii itakuwa taarifa ya mwisho kwa sababu muda wetu ni mfupi. Mheshimiwa Charles Kimei.

MHE. DKT. CHARLES S. KIMEI: Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nimweleweshe msemaji kwamba hivyo vitu anavyovizungumza haviendani na hoja anayotaka kutoa ya kusema kwamba tuko kwenye kipato cha kati. Kipato cha kati hakiendani na mambo ya Serikali kukopa au Serikali kutokulipa, hayo ni mambo tofauti kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vigezo vinavyotumika ni wastani wa pato la mtu mmoja. Unachukua pato la Taifa unaligawanya kwa idadi ya watu, unapata huo wastani. Kwa hiyo, hiyo haihusiani na mambo ya Serikali kutokulipa au kufanya nini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka kumwelekeza kwamba hilo analozungumza ana hoja nyingine pengine lakini siyo hiyo. (Makofi)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Kaiza, unaipokea taarifa hiyo?

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. AGNESTA L. KAIZA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza taarifa hiyo siipokei, lakini nakuomba wewe na Kiti chako unilindie muda wangu wa dakika tano vizuri sana, nakuomba sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Mbunge anadai kwamba ninachokiongelea hapa siyo sehemu ya hiyo dhana nzima ambayo nimetoka kuisema. Hata hivyo, ikiwa pato la Taifa hali-reflect maisha ya wananchi ya kila siku, tusijidanganye kwamba tumeingia katika uchumi wa kati. Mfano, wakandarasi wanashindwa kwenda kulipa fedha kwenye…

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Kaiza, nilikupa sekunde 30 kwa sababu kengele ilishagonga. Ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto
MHE. AGNESTA L. KAIZA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipatia nafasi hii ili nami kwa uchache niweze kuchangia katika Wizara hii muhimu. Mchango wangu wa leo utajikita katika ripoti ya CAG ukurasa Na. 223 na ukurasa Na. 226.

Mheshimiwa Naibu Spika, nchi yetu imekumbwa na ugonjwa wa hatari ambao umeua watu wengi duniani kote wakiwemo ndugu zetu, jamaa zetu na marafiki zetu. Kila nchi imeweka mkakati madhubuti wa kupambana na ugonjwa huu wa corona; na nchi yetu Tanzania pamoja na mikakati mingine ambayo iliweka, ilijikita zaidi kuhakikisha Watanzania tunajikinga kwa kutumia barakoa na siyo tu kwa kunawa mikono.

Mheshimiwa Naibu Spika, mnamo mwezi Mei, 2020 Serikali kupitia MSD iliagiza mtambo wa kutengeneza barakoa hapa nchini. Mtambo huu umegharimu dola za Kimarekani 270,314 sawa na shilingi milioni 600 plus. Mtambo huu according to CAG ulitarajiwa kuzalisha barakoa milioni nne kwa mwezi. Hata hivyo, management ilikaa na kukubaliana kwamba badala ya kuzalisha barakoa milioni nne kwa mwezi, basi izalishe barakoa 504,000 tu kwa mwezi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimeyasema haya kwa mujibu wa CAG. Pamoja na kwamba management ilijipanga kuzalisha barakoa 504,000 malengo haya hayajatimia kabisa. Ukumbuke, nimesema kwamba uwezo wa mtambo huu ulipaswa kuzalisha barakoa milioni nne kwa mwezi. Mpaka sasa nimesimama mbele zako, mnamo mwezi Agosti mtambo huu umezalisha barakoa 76,500 tu. Mwezi Septemba mtambo huu umezalisha barakoa 244,000 tu which means hata yale malengo waliyojiwekea ya kuzalisha barakoa 504,000 yameshindikana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mujibu wa CAG, anasema katika ukurasa 223, kwamba changamoto hii ya mashine hii kushindwa kuzalisha milioni nne kwa mwezi ilitokana na compressor iliyokuwepo kutokufanya kazi vizuri na hivyo basi, ikabidi iletwe compressor nyingine ili kuongeza nguvu na hatimaye angalau uzalishaji ufikie malengo yale ya management iliyokuwa imejiwekea ya 504,000. Mpaka hivi sasa, kwa mujibu wa CAG mtambo huu wa kuzalisha barakoa umefanya uzalishaji kwa asilimia nne tu ya uwezo wa mtambo huu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimesema kwamba ilifungwa compressor nyingine ili iongeze nguvu kwamba sasa angalau uzalishaji uweze kuwa mkubwa. Cha kushangaza…

MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

T A A R I F A

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Agnesta Lambert, kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Musukuma.

MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Nimemsikiliza mzungumzaji, anazungumza kuhusu suala la uzalishaji wa barakoa. Nilitaka kumpa tu taarifa kwamba kitu chochote kinachotengeneza vitu kibiashara, kinategemea na mahitaji yanayotakiwa. Sasa ukiangalia hata humu Bungeni, namwona dada yangu Mheshimiwa Halima peke yake ndio amevaa barakoa. Sasa hata tungezalisha hizo milioni nne, yeye mwenyewe mwongeaji, yuko empty ingekuwaje? (Makofi)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Agnesta Lambert, unaipokea taarifa hiyo?

MHE. AGNESTA L. KAIZA: Mheshimiwa Naibu Spika, siipokea taarifa hiyo, lakini nadhani alikuwa hanisikilizi vizuri. Nilisema mchango wangu utajikita katika ripoti ya CAG. Haya siyo maneno yangu mimi Agnesta Lambert, ni maneno na ripoti ya CAG. Kwa hiyo, taarifa hiyo ingekuwa ni vyema kama ungemtafuta CAG ukampatia ili aweze kukupatia majibu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sasa niendelee. Nimesema mtambo huu siyo tu kwamba umeshindwa kukidhi matakwa ya kuzalisha milioni nne kwa mwezi, imeshindwa hata kukidhi matakwa ya kuzalisha barakoa 504,000 which means hapa kuna shida. Kuna utata! Ni wazi Watanzania tumeuziwa mbuzi kwenye gunia.

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Agnesta Lambert, kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Getere.

T A A R I F A

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Naibu Spika, nampa taarifa mzungumzaji kwamba suala la uzalishaji wa barakoa ni biashara inayoweza kufanywa, kwa sababu kuna demand na supply. Sasa demand ya biashara ya Tanzania ni kidogo sana, lakini pia tulisharuhusu badala ya Serikali kutengeneza barakoa, tutengeneze wenyewe. Kwa hiyo, yeye asihangaike na mambo ya CAG, atengeneze tu kwa njia yake. (Kicheko)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Agnesta Lambert, unaipokea taarifa hiyo?

MHE. AGNESTA L. KAIZA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza siipokei hiyo taarifa, lakini pili naomba niwe wazi, niko hapa kuwatetea Watanzania zaidi ya milioni 60. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika eneo hili nimalize kwa kusema hivi, lazima ufanyike uchunguzi kabisa wa moja kwa moja ili kuangalia mambo makuu mawili. Kwanza, tuhakiki kama kweli mtambo huu ulinunuliwa kwa thamani hiyo ya dola za Kimarekani 270…

(Hapa kengele ya kwanza ililia)

MHE. AGNESTA L. KAIZA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niendelee nimalize kwa kusema hivi, kwa mwaka mmoja mashine hii au mtambo huu ulipaswa kuzalisha barakoa milioni 48, lakini mpaka sasa hivi nimesimama mbele zako MSD wamezalisha barakoa 320,000 tu. It is a shame.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niende moja kwa moja ukurasa 226 wa ripoti ya CAG. Katika mchango wangu nilipokuwa nachangia katika Wizara ya Ofisi ya Waziri Mkuu niliongelea moja kwa moja juu ya usugu wa Serikali kutokulipa madeni ya MSD, jambo ambalo limesababisha MSD siyo tu kwamba imeshindwa kuagiza madawa, lakini Watanzania wengi wanakufa na wanakosa huduma kwa sababu tu ya madeni ya Serikali.

Mheshimiwa Naibu Spika, hiyo nimeweka tu kumbukumbu lakini hoja yangu ya msingi imejikita…

T A A R I F A

NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA (MHE. PASCHAL P. KATAMBI): Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

NAIBU SPIKA: Waheshimiwa Wabunge, hiyo itakuwa taarifa ya mwisho. Mheshimiwa Agnesta Lambert, kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Patrobas Katambi.

NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA (MHE. PASCHAL P. KATAMBI): Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nakushukuru. Napenda kumpa taarifa msemaji, suala la malipo ya MSD lilitolewa ufafanuzi na Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, kwamba liko kwenye hatua ya uhakiki wa madeni na taarifa na kama tunakumbuka katika Bunge la wiki iliyopita taarifa hiyo ilielezwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, zaidi katika eneo la uzalishaji wa barakoa; uzalishaji wa barakoa unaendana na kusudio kwa maana ya mahitaji. Zingezalishwa barakoa unazozihitaji kwa kipindi hicho, kungekuwa na query tena ya CAG kwa utaratibu ule ule. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, napenda tu kumpa taarifa kwamba awe anachunguza zaidi katika kuangalia haya mambo kabla hajaleta hoja mezani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. (Makofi)

NAIBU SPIKA: Ahsante sana. Mheshimiwa Agnesta Lambert, unaipokea taarifa hiyo?

MHE. AGNESTA L. KAIZA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kiti chako kilinde muda wangu, nafikiri umeona jinsi ambavyo Waheshimiwa Wabunge wame-interfere sana.

Mheshimwia Naibu Spika, naomba niende kwa point yangu ya pili. Hoja yangu ya pili ni kuhusiana na usugu wa Serikali uliokolea sasa kwa kutokupeleka bajeti iliyoidhinishwa na Bunge lako Tukufu kwenda MSD.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka wa fedha wa 2019/ 2020, Bunge lako hili Tukufu lilipitisha bajeti ya bilioni 200 kwenda MSD, lakini pesa hii haijaenda hata shilingi moja. Matokeo yake MSD wameshindwa kuagiza madawa pamoja na vifaa tiba venye thamani ya milioni 119, yote haya Serikali ni kwa sababu inashindwa kupeleka fedha bilioni 200 kwenye MSD kupambana kuhakikisha Watanzania wanakua na afya njema, lakini wanapata huduma bora…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Kengele ya pili imeshagonga Mheshimiwa, ahsante sana.

MHE. AGNESTA L. KAIZA: Mheshimiwa Naibu Spika, nipe sekunde moja ili ni-finalize wamechukua muda wangu.

NAIBU SPIKA: Sekunde 30.

MHE. AGNESTA L. KAIZA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Nimalizie kwa kusema kwamba kwa kipindi cha miaka mitano Bunge lako Tukufu limeidhinisha kiasi cha fedha za Kitanzania trilioni 1.04 kwenda MSD, lakini mpaka hivi sasa nimesimama mbele yako Serikali imepeleka bilioni 315 tu. This is the shame, hii ni asilimia 30 ya bajeti nzima ya MSD.
Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali (Na 2) wa Mwaka 2021 (Toleo la Kiingereza)
MHE. AGNESTA L. KAIZA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ili nami niweze kuchangia. Niseme kwamba ni Mjumbe wa Kamati ya Katiba na Sheria kwa hiyo nimeshiriki kwa asilimia 100 kupitia Muswada huu ambao uliletwa kwetu na Serikali.

Mheshimiwa Spika, nikiri kwamba Muswada huu haukuwa ni Muswada ambao ulikuwa una taswira ya maslahi mapana ya Taifa. Nasema hivyo kwa sababu ndiyo maana ukiangalia ripoti yetu Kamati unaona jinsi ambavyo tumeweza kufumua sheria nyingi ambazo zilipendekezwa na Serikali kwamba ziweze kufanyiwa marekebisho.

Mheshimiwa Spika, kwanza nipongeze kwa namna ambavyo Serikali imeweza kuyachukua mapendekezo yetu kama Kamati na kuyafanyia kazi na kukubali kutembea katika ushauri ambao tumeweza kuutoa. Kwa sababu nasema hivyo, nakumbuka wakati Serikali inawasilisha mswada huu nilikuwepo na kutokana na Sheria hizi ambazo zilikuwa ni sheria kumi na tatu kabla hatujaondoa ile Tafsiri ya Sheria Sura ya kwanza, mimi mwenyewe nilisimama nikasema ikiwa Serikali haitokubaliana na mapendekezo ambayo binafsi mwenyewe niliyatoa, nilisema nitakuja kusimama juu meza hapa.

Mwenyekiti wangu nishahidi na Wajumbe, nikasema nitasismama juu meza kusema kabisa kwamba hizi Sheria hazina maslahi kabisa, lakini nawashukuru kwamba wameyachukua na wamekubali kuyafanyia kazi.

Mheshimiwa Spika, haitoshi kabisa kusema kwamba nawapongeza kwa kuchukua mawazo yetu na ushauri wetu na kuufanyia kazi. Hiyo haitoshi, nasema haitoshi kwa sababu gani najaribu ku-imagine ikiwa Kamati hii ya Katiba na Sheria siku hiyo wakati tumekuwa tukipitia huu Muswada tungekuwa tumeamka vibaya, nikisema kuamka vibaya nafiri yaani tumeamka vibaya kama Kamati, halafu tukawa hatujaona haya ambayo tumeyaona na tukaleta mapendekezo na tukapitisha kama the way ambavyo Serikali ilikuwa inataka, ni wazi kabisa kwamba yangekuja tukukuta kama yale ya tozo.

Mheshimiwa Spika, sasa nilikuwa naushauri, niushauri, Serikali kabla haijaleta Muswada Bungeni, haijaleta Muswada kwenye Kamati ya Katiba na Sheria, wawe wanakaa kwanza wanakuwa makini, watafute wataalam, watafute wabobezi, wakae nao chini, wawashirikishe namna na jinsi ambavyo wamepanga kuleta Muswada na wapate ushauri kwamba je, huu Muswada, hii Sheria mnayotaka kuipeleka imebeba maslahi mapana ya Taifa? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa sababu haitoshi tu, haitoshi tu kusema kwamba tutarekebisha tayari tutakuwa tumeshatengeneza damage kubwa sana. Tupo hapa tunajadili mambo mbalimbali mfano, umesema kwamba siyo busara, siyo busara kuanza kuongelea yale mambo ambayo Serikali imekubali kuyafanyia kazi na mengine kuyaondoa.

Mheshimiwa Spika, lakini tujiulize kama wangekaa chini Serikali ikakaa chini na Wataalam wakaona namna gani wanakwenda kuleta Muswada wenye mantiki sisi tukafanya kuboresha boresha tu kidogo, tuboreshe tu kidogo siyo mnaleta Muswada, siyo tu unafumuliwa lakini mwingine tunautupa nje kabisa. mfano hii hapa ya Sheria ya Tafsiri ya Sheria, Sura ya Kwanza…

MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Spika, Taarifa.

SPIKA: Ngoja upokee taarifa halafu utaendelea Mheshimiwa Agnesta.

T A A R I F A

NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Spika, namshukuru mchangiaji anachangia vizuri na tunashukuru Kamati kwa kupokea maoni na mawazo ya Wanakamati. Kazi ya Bunge ni kutunga Sheria na Serikali inapoleta Muswada hapa inatarajia maoni na ushauri kutoka kwa watunga Sheria. Sasa hawezi akasema kwamba yeye hawezi kupongeza sijui, ni kazi yake, anapongeza nini? Kwa hiyo, asilaumu chochote imeletwa mahala husika kwa watunga sheria, waitunge Serikali ifanyie kazi. (Makofi)

SPIKA: Mheshimiwa Agnesta, unapokea taarifa hiyo kwamba usilaumu chochote. (Kicheko)

MHE. AGNESTA L. KAIZA: Mheshimiwa Spika, kwa kweli sipokei hiyo taarifa na niseme, ukiangalia katika ushauri wa jumla wa Kamati pamoja nashauri zingine Kamati imeishauri Serikali kwamba kabla haijaleta, haijaleta huo Muswada iwe inakaa chini, inatathmini, inajiridhisha that’s why tuna wataalam, sasa kama tumeweka watu ambao wanapaswa kufanya uchambuzi kabla ya mambo hajafika Bungeni then why tumewaka watu kama hao. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, siipokei lakini niseme pia ni nafasi yangu kama Mbunge lakini pia kama Mjumbe Kamati kuishauri Serikali kwamba iwe inakaa, inatulia, inajipanga vizuri kuleta Miswada kuanzia sasa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ukiniambia kwamba kazi yangu ni kutunga Sheria, yaani kwamba Serikali upo kwa kajili ya kuleta Miswada halafu mimi naifumua tu, naifumua tu, naifumua, what is it them!

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naomba niendelee na mchango wangu kuendelea kuishauri Serikali kama jinsi ambavyo Kamati imeshauri, kwamba siku nyingine mkae chini, muwaweke wataalam, mpate ushauri mbalimbali, mtafuta wadau kama jinsi ambavyo sisi kama Kamati tunaita wadau. Tuliwaita, wakaja wakapitia Muswada wenu huo huo, wakagundua vitu mbalimbali ambavyo haviko sawa that’s why tumewaletea Taarifa ambayo ipo sahihi na ninyi mmekwenda mmeifanyia kazi mmekubali kuifanyia marekebisho. Siyo tu kukubali mkanyofoa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ni kwa sababu umesema kwamba tusiongelee yale ambayo Serikali imeshayatoa kwa sababu tungesema yaliyojiri kwenye Kamati ni hatari tupu! (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ninapoendelea na mchango wangu ninapokuwa namalizana na suala zima la kuishauri Serikali katika marekebisho ya Kifungu cha 54 cha Sheria ya Tafsiri ya Sheria Sura ya Kwanza, pamoja na kwamba Kifungu hiki au Sheria hii tumeiondoa kabisa lazima ifike sehemu Serikali tuweze kujitathmini sana, kwamba sheria kama hii ambayo ilikuwa inapendekeza kwamba ile Bodi inapovunjwa yaani Bodi inapokuwa imeisha wakati wake mfano kwamba Katibu Mkuu akiwa peke yake…

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Spika, taarifa.

SPIKA: Mheshimiwa Chief Whip!

T A A R I F A

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Spika, naomba tu niweke vizuri jambo hili kwa sababu Watanzania wanaweza kuwa pia wakapata fursa ya kusikiliza huu mjadala wetu kwa hiyo, ni lazima tuliweke sawa.

Mheshimiwa Spika, ninakubali ushauri na maoni ya Waheshimiwa Wabunge, lakini Mbunge anaposema kwamba Kamati imeiondoa Sheria ya Serikali siyo sahihi. Muswada huu ulioletwa ni Muswada mmoja wenye sheria ndogo mbalimbali. Kwa hiyo, ndani ya Muswada huu mmoja, yaani sheria hii iliyoletwa kipengele fulani ndicho kilichoondolewa.

Kwa hiyo, nilikuwa nataka twende kwa muktadha huo. Isipeleke picha kwenye public kwamba ule Muswada au sheria iliyoletwa na Serikali Bunge imeiondoa, lakini sehemu ya sheria iliyoletwa kwenye Muswada huu Namba hii ambao ndiyo unaendelea ndani ya Bunge basi katika hatua ya Kamati Serikali ilishauriwa jambo hili liondolewe.(Makofi)

Mheshimiwa Spika, nilikuwa naomba kutoa hiyo taarifa ili kusudi tuchangie huku tukielewana kwa muktadha wa uelewa wa public na wenyewe humu ndani.

SPIKA: Mheshimiwa Agnesta Lambert Kaiza ‘nshomile’ unakubali ushauri huu? (Kicheko)

MHE. AGNESTA L. KAIZA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Labda nimuulize Mheshimiwa Jenista ni kweli kuna sheria zimefutwa au hazipo?

Mheshimiwa Spika, mfano hatutaki kusema, ipo sheria mbovu nafikiri itajadiliwa kesho, imefutwa inahusiana na Posta ambayo walitengeneza mazingira ya ku-hold kwamba vifurushi kusafirisha vifurushi huku na kule kwa maana ya Posta peke yao ndiyo waweze kufanya shughuli katika utandawazi wa sasa.

SPIKA: Mheshimiwa Agnesta, hapo unawahisha shughuli, kama unajua ni ya kwesho basi iweke mpaka kesho. (Kicheko)

MHE. AGNESTA L. KAIZA: Mheshimiwa Spika, unajua ukichokozwa wakati mwingine na wewe unachokonoa. (Kicheko)

Mheshimiwa Spika, nimechokonoa lakini itoshe tu kusema Mheshimiwa Jenista pamoja na Waheshimiwa Wabunge kwamba nia yangu ni njema sana tusitumie muda mwingi wa kufumua fumua hii Miswada mnayoileta ikiwa…

MHE. ABDULLAH ALI MWINYI: Mheshimiwa Spika, taarifa.

SPIKA: Mheshimiwa Agnesta kuna Taarifa nadhani inahusu kuchokonoa.. (Kicheko)

Mheshimiwa Abdallah Mwinyi tafadhali.

T A A R I F A

MHE. ABDULLAH ALI MWINYI: Mheshimiwa Spika, ningependa kumpa taarifa Mheshimiwa Agnesta kwamba hiyo sheria anayoizungumzia kesho siyo kwamba ni sheria nzima ni kipengele ndani ya sheria kama Mheshimiwa Jenista Mhagama alivyosema. Ahsante.

SPIKA: Mheshimiwa Mbunge na hilo nalo usiendelee nalo kwa sababu ni la kesho, Mheshimiwa malizia bado dakika moja tu kama unalo la kusema.(Kicheko)

MHE. AGNESTA L. KAIZA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. Naomba nimalize kwa kuendelea kuipongeza Kamati ya Katiba na Sheria chini ya Mwenyekiti wetu mahiri hakika tumeweza kufanya kazi kubwa kubwa isiyokuwa ya kifani na Mwenyekiti wetu anastahili pongezi kwa sababu Mheshimiwa Spika utakuwa shahidi, sheria 12 ambazo tulikuwa tunazifanyia marekebisho hakuna sheria hata moja ambayo tulisema kwamba Serikali walipoileta ilikuwa sawa kwamba sasa ipite kama ilivyo.

Mheshimiwa Spika, naomba sasa…

MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Spika, taarifa!

SPIKA: Ahsante sana. Muda umekwisha ni kengele ya pili.
THE WRITTEN LAWS (MISCELLANEOUS AMENDMENTS) (NO. 5) ACT, 2021
MHE. AGNESTA L. KAIZA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ili nami niweze kuchangia machache. Kabla sijakwenda katika Muswada naomba nitumie nafasi hii kwanza kabisa kumpongeza Mwenyekiti wangu wa Kamati ya Katiba na Sheria kwa jinsi ambavyo ametusimamia kwa weledi na hata tukaweza kufanikisha kudadavua na kuweka sawa Muswada huu.

Mheshimiwa Spika, ni wazi kwamba kwa weledi huu wa mwana mama unatuma ujumbe moja kwa moja kwamba wanawake tukiaminiwa na kukabidhiwa majukumu makubwa na mazito tuna uwezo wa kuyasimamia, kuyafanya na tukaleta matokeo chanya ambayo hayakutarajiwa.

Mheshimiwa Spika, niende moja kwa moja sasa katika mchango wangu kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Ibara ya 28 inapendekeza katika Kifungu kidogo cha 4 cha Sheria ya Uhamiaji Sura ya 54 kuitambua Idara hii ya Uhamiaji kuwa ni Jeshi kamili bila kubadilisha jina. Natambua nia njema kabisa ya Serikali juu ya jambo hili, lakini niseme kwamba yapo mambo kadha wa kadha ambayo sisi kama Bunge tunapaswa kuyatafakari kabla hatujapitisha Sheria hii.

Mheshimiwa Spika, suala la majeshi ni suala la Kikatiba. Ninaposema suala la Kikatiba ina maana tunapokuwa tunapitisha Sheria hii hatuna budi kuhakikisha kwamba Sheria hii haiendi kukinzana na Katiba. Kuanzisha au kufuta, kufuta au kuanzisha Jeshi jipya au kulipa hadhi, jambo hili linapaswa kuangaliwa kwa kina kwa maana ya Katiba yetu ya Nchi kwa sababu bila hivyo tunaweza kujikuta tuna-contradict Sheria pamoja na Katiba ya Nchi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania haitambui Idara ya Uhamiaji kuwa ni miongoni mwa Majeshi katika nchi yetu. Sasa tunapokuwa tunaletewa Muswada kama huu wa kuweza kuipa hadhi. (Makofi)

SPIKA: Nimeishaikamata, na Waheshimiwa Wabunge…

MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Spika, taarifa.

SPIKA: …kama wanazo katika vishkwambi vyao, unaposema Katiba lazima u-refer Katiba wapi na nini, halafu mtu taarifa utakuja baadaye kidogo, ili twende pamoja.

MHE. AGNESTA L. KAIZA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. Ibara ya 147 Kifungu kidogo cha Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania haitambui kabisa...

SPIKA: Twende polepole, na dakika zako zinalindwa kabisaa. 147 aah kidogo ili twende pamoja, ehee nimeshafika 147.

MHE. AGNESTA L. KAIZA: Mheshimiwa Spika, Kifungu kidogo cha 4.

SPIKA: Endelea kwa kuisoma.

MHE. AGNESTA L. KAIZA: Mheshimiwa Spika, sina Katiba, iko wapi Katiba.

SPIKA: 147(4) si ndiyo.

MHE. AGNESTA L. KAIZA: Mheshimiwa Spika, ndiyo.

SPIKA: Kwa madhumuni ya Ibara hii mwanajeshi maana yake ni askari aliyeajiriwa kwa masharti ya muda au ya kudumu katika Jeshi la Ulinzi, Polisi, Magereza au Jeshi la Kujenga Taifa. Mmmhm.

MHE. AGNESTA L. KAIZA: Mheshimiwa Spika, naweza kuendelea,

SPIKA: Mmmhm.

MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA: Mheshimiwa Spika, taarifa.

SPIKA: Yupo Msekwa au yupo humu humu ndani? Endelea Mheshimiwa na taarifa yako.

T A A R I F A

MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA: Mheshimiwa Spika, nilikuwa nataka nimpe taarifa mzungumzaji kwamba kama tutaridhia na kuifanya Idara ya Uhamiaji kuwa na hadhi ya Jeshi hatukiuki Katiba kwa sababu Ibara anayoisoma haisomwi peke yake, unaweza kuisoma na Ibara nyingine 2. Kwanza Ibara ya 147(2) inasema; Serikali ya Jamhuri ya Muungano yaweza kwa mujibu wa Sheria kuunda na kuweka Tanzania Majeshi ya aina mbalimbali kwa ajili ya ulinzi na usalama wa nchi na wananchi wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini ukisoma Ibara 151 ya Katiba yetu ambayo ni Ibara ya tafsiri inasema hivi; Jeshi maana yake ni lolote kati ya Majeshi ya Ulinzi na ni pamoja na Jeshi lolote jingine lililoundwa na Katiba hii au kwa Mujibu wa Sheria na linalotawaliwa kwa amri ya Jeshi.

Kwa hiyo Katiba hii Ibara hiyo imetaja lakini haisomwi peke yake maana majeshi haya yaliyotajwa kwenye Katiba lakini na lolote litaloundwa kwa mujibu wa Sheria ya Nchi yetu inayotungwa na Bunge hili. Nakushukuru. (Makofi)

SPIKA: Agnesta leo unapigwa asubuhi asubuhi tu. (Kicheko)

MHE. AGNESTA L. KAIZA: Mheshimiwa Spika, kama kawaida.

SPIKA: Jipange vizuri. Dakika zake mmemlindia enhee.

MHE. AGNESTA L. KAIZA: Mheshimiwa Spika, naomba niendelee, kwanza niseme kwamba Taarifa hiyo binafsi siipokei kwa sababu the way ninavyoendelea kuchangia nitamjibu Mheshimiwa Mbunge ni nani haswa na jambo gani linapaswa kufanyika ili tuweze kupitisha sheria hii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, narudia kusema suala zima la kijeshi ni la kikatiba. Sasa unaposema tunakwenda kupandisha Idara ya Uhamiaji kuipa hadhi ya kuwa jeshi kamili wakati katika Ibara 147 haiitambui which means yupo mtu…

T A A R I F A

MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Spika, taarifa.

MHE. HALIMA J. MDEE: Mheshimiwa Spika, Taarifa.

SPIKA: Unajua tuna pande mbili na Msekwa, sasa ni vizuri kusema ni nani, sasa nimekuona Mheshimiwa Massare.

MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Spika, ahsante. Ibara ya 47 kipengele anachosema Mheshimiwa…

SPIKA: Taratibu, umesema Ibara ya 47?

MHE. YAHAYA O. MASSARE: Ndiyo.

SPIKA: Twendeni taratibu, endelea.

MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Spika, angetakiwa arudi nyuma kidogo asome kifungu kidogo cha
(1) na (2) ambacho kinasema Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa mujibu wa sheria…

SPIKA: Umesema Ibara ya 47 au ngapi?

MHE. YAHAYA O. MASSARE: Ibara ya 47(2) ambayo inasema Serikali ya Jamhuri ya Muungano yaweza kwa mujibu wa sheria…

SPIKA: Ibara ya 47(2) inasema bila kuathiri masharti…

MHE. YAHAYA O. MASSARE: Ni Ibara ya 147(2).

SPIKA: Ibara ya 147?

MHE. YAHAYA O. MASSARE: Ndiyo.

SPIKA: Okay! Ile aliyoisoma Mheshimiwa?

MHE. YAHAYA O. MASSARE: Ndiyo, yeye ameruka kifungu anatakiwa arudi juu kidogo, yeye amekwenda chini, arudi kifungu cha (2).

SPIKA: Alishapewa taarifa hiyo tayari.

MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Spika, alipewa Ibara ya 151.

SPIKA: Alipewa na hiyo.

MHE. YAHAYA O. MASSARE: Haya sawa.

SPIKA: Mheshimiwa Agnesta, sasa endelea tu maana hiyo...

MHE. AGNESTA L. KAIZA: Mheshimiwa Spika, kabla sijaendelea nikuombe ulinde muda wangu maana hizi Taarifa zimekuwa nyingi sana. (Makofi)

SPIKA: Unaelimishwa tu usiwe na wasiwasi. (Kicheko)

MHE. AGNESTA L. KAIZA: Mheshimiwa Spika, aliyetoka kunipa taarifa amekiri kwamba Idara ya Uhamiaji haijatajwa katika Ibara hii ambayo nimeitaja which means ili tuweze kuipandisha hadhi Idara ya Uhamiaji kuwa jeshi kamili, yapo ya kufuata, yapo ya kuzingatia, ndiyo hayo ambayo nakwenda kuyaelezea.

T A A R I F A

MHE. NAJMA MURTAZA GIGA: Mheshimiwa Spika, taarifa.

MHE. AGNESTA L. KAIZA: Eeeee!

SPIKA: Unapewa taarifa Mheshimiwa Agnesta.

MHE. NAJMA MURTAZA GIGA: Mheshimiwa Spika, naomba nimtoe wasiwasi ndugu yangu Mheshimiwa Agnesta kwamba Bunge hili linaweza kuyarekebisha hayo kupitia Ibara ya 98(1) ambayo inasema: “Bunge laweza kutunga Sheria kwa ajili ya kubadilisha masharti yoyote ya Katiba hii kwa kufuata Kanuni zifuatazo:- (a) Muswada wa Sheria kwa ajili ya kubadilisha masharti yoyote ya Katiba hii (isipokuwa yale yanayohusika na aya ya (b) ya ibara hii ndogo) au masharti yoyote ya Sheria yoyote iliyotajwa katika Orodha ya Kwanza kwenye Nyongeza ya Pili utaungwa mkono kwa kura za Wabunge ambao idadi yao haipungui theluthi mbili ya Wabunge wote”.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nimtoe tu hofu kwamba hili jambo linawezekana kwetu wenyewe baada ya sheria kupita na sisi tukaweza kuwaingiza haya majeshi yatakayoongezeka…

MHE. HALIMA J. MDEE: Mheshimiwa Spika, taarifa.

MHE. NAJMA MURTAZA GIGA: Mheshimiwa Spika, …kwa mujibu wa Ibara ya 51 waweze kujumuika katika Ibara ya 147. (Makofi)

MHE. HALIMA J. MDEE: Mheshimiwa Spika, taarifa.

SPIKA: Haiwezekani kumpa taarifa mtoa taarifa.

MHE. HALIMA J. MDEE: Mheshimiwa Spika, sasa kuna taarifa anapotosha. (Kicheko)

SPIKA: Subiri! Inatakiwa kwanza niendelee na Mheshimiwa Agnesta kwanza ndiye aliyepewa taarifa.

MHE. AGNESTA L. KAIZA: Mheshimiwa Spika, kwa heshima kubwa niliyonayo ambayo nampa Mwenyekiti wangu naomba niendelee kuchangia hoja yangu.

MHE. HALIMA J. MDEE: Mheshimiwa Spika, taarifa.

MHE. AGNESTA L. KAIZA: Mheshimiwa Spika, nimesema na narudia kusema kwamba natambua nia njema ya Serikali juu ya jambo hili lakini…

T A A R I F A

MHE. HALIMA J. MDEE: Mheshimiwa Spika, taarifa.

SPIKA: Mheshimiwa Agnesta unapewa taarifa.

MHE. HALIMA J. MDEE: Mheshimiwa Spika, naomba nimpe taarifa Mheshimiwa Agnesta kwa kurejea Taarifa ya Kamati inayosema yafuatayo, naomba ninukuu, yasionekane ni maneno yangu.

SPIKA: Pale wamekosea.

WABUNGE FULANI: Aaaaa.

MHE. HALIMA J. NDEE: Mheshimiwa Spika, taarifa ya Kamati inasema yafuatayo…

SPIKA: Kamati walikosea Mheshimiwa Halima. (Kicheko)

MHE. HALIMA J. MDEE: Mheshimiwa Spika, naomba niruhusu…

SPIKA: Ni makosa ya uchapaji tu. (Kicheko)

MHE. HALIMA J. MDEE: Mheshimiwa Spika, naomba uniruhusu nitoe taarifa yangu. (Kicheko)

Mheshimiwa Spika, ukurasa wa…

SPIKA: Ni makosa ya uchapaji Mheshimiwa Halima, nimeshakupa mwongozo, kwa hiyo, hiyo achana nayo. Mheshimiwa Agnesta endelea.

WABUNGE FULANI: Aaaaaaaa. (Kicheko/Makofi)

SPIKA: Mheshimiwa Halima, kaa. Mheshimiwa Agnesta endelea. (Makofi/Kicheko)

Nimesikia vizuri, si niko hapa, wewe tulia. Mheshimiwa Agnesta endelea. (Kicheko)

MHE. AGNESTA L. KAIZA: Mheshimiwa Spika, naomba kuendelea na nimeipokea Taarifa. (Kicheko)

Mheshimiwa Spika, naomba sasa niende moja kwa moja katika mchango wangu. Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Katiba yetu inamtambua kama Amiri Jeshi Mkuu na Katiba inasema Amiri Jeshi Mkuu pale anapoona kwamba kuna hali ya hatari, dharura juu ya jambo fulani la kijeshi ataleta au atatoa kitu kinachoitwa hati idhini. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, uki-refer kwenye Taarifa yetu ya Kamati imeongelewa vizuri hati hii kwamba hati idhini kutoka kwa Amiri Jeshi Mkuu ilipaswa kuja kwetu ili ikapate kuwa mwongozo wa Bunge…

SPIKA: Nitajie kifungu cha Katiba kinachozungumzia hati idhini, kifungu namba ngapi? (Kicheko)

SPIKA: Kengele ya kwanza hiyo bado una muda.

MHE. AGNESTA L. KAIZA: Mheshimiwa Spika, ili kuukomboa wakati naomba niendelee kuchangia…

SPIKA: Mambo ya Kikatiba hayana kuokoa wakati, likishakuwa la Kikatiba lazima tuwe na uhakika. (/Kicheko)

MHE. AGNESTA L. KAIZA: Mheshimiwa Spika, naomba niendelee please…

SPIKA: Haya, hiyo umeifuta. Endelea basi.

MHE. AGNESTA L. KAIZA: Mheshimiwa Spika, sijaifuta kwa sababu kutokusema iko sehemu gani haimaanishi kwamba sijui na ndiyo maana nimeiongelea kwa sababu najua ipo. Sasa niseme tu ni wazi kwamba tunahitaji hiki kitu kinachoitwa hati idhini kutoka kwa Amiri Jeshi Mkuu.

SPIKA: Lakini umeshindwa kutuambia iko wapi.

MHE. AGNESTA L. KAIZA: Mheshimiwa Spika, nitakuambia kabla sijakaa. Naomba niendelee…

SPIKA: Haya mambo yanataka ujipange. (Kicheko)

MHE. AGNESTA L. KAIZA: Sawa.

Mheshimiwa Spika, sisi kama Kamati ya Katiba na Sheria wakati tunajadiliana pamoja na Mwanasheria Mkuu wa Serikali tulihoji ndiyo maana hata hawa wenzangu wanaonipa Taarifa najua mioyoni mwao ninachokisema ndicho wanachokiamini, tulisema na tulimuuliza kwamba tunahitaji kupata ile hati idhini ili iweze kutuongoza lakini…

SPIKA: Hiyo kitu yako umeshindwa kutuongoza ni wapi? Unapiga blah blah theory hapa, hatutaki theory, mradi una-refer jambo ambalo ni la Kikatiba unapaswa kutuambia wapi.

MHE. AGNESTA L. KAIZA: Mheshimiwa Spika, basi naomba niendelee katika jambo lingine.

SPIKA: Eeh! Hapo sawa.

MHE. AGNESTA L. KAIZA: Mheshimiwa Spika, lakini naona hilo limepokelewa na limesikika.

Mheshimiwa Spika, tunapokuwa tunajadili suala zima la kupandisha Idara ya Uhamiaji kwenda kuwa jeshi kamili lazima tujiulize mambo makuu mawili. Serikali inapaswa kujiuliza kwanza mahusiano yetu ya kimataifa na wenzetu kule wanatuonaje tunapokuwa tumeibadili Idara ya Uhamiaji kuwa jeshi kamili, tunakuwa tunatengeneza taswira gani kwa watalii na wawekezaji?

Mheshimiwa Spika, najaribu ku-imagine mtalii au mwekezaji anakuja au kule Ubalozini labda anatafuta documents au amekuja hapa Tanzania anakutana na Uhamiaji wako full …

T A A R I F A

WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, taarifa.

SPIKA: Mheshimiwa Agnesta, sasa wewe unataka wakute raia wamekaa kienyeji? Mheshimiwa Simbachawene tafadhali.

WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, pengine ili tusikupotezee muda tusichangie wengi nitumie nafasi hii kumuelewesha kwamba tutaonekanaje tukiifanya Idara ya Uhamiaji kuwa jeshi, nimueleze tu, Uingereza Uhamiaji ni jeshi na linaitwa UK Border Force, wanatumia silaha na iko chini ya Wizara ya Mambo ya Ndani. Marekani, India na Australia Uhamiaji ni jeshi. Kwa hiyo, watatuonaje, watatuona tunafanana na wao na tunajitahidi sana kuwa kama wao. (Makofi/Kicheko)

SPIKA: Mheshimiwa Waziri, Mheshimiwa Agnesta hajapitapita huko. Mheshimiwa endelea kuchangia. (Kicheko)

MHE. AGNESTA L. KAIZA: Mheshimiwa Spika, nimesikia Taarifa ya Mheshimiwa Waziri lakini ningepewa nafasi ya kuuliza pia na mimi ningeuliza, tulisubiri…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Ooh, bahati mbaya kengele ya pili imeshalia.

MHE. AGNESTA L. KAIZA: Mheshimiwa Spika, this is not fair.

SPIKA: Kengele ya pili imeshalia, tunaendelea na uchangiaji…

MHE. HALIMA J. MDEE: Mheshimiwa Spika, Mwongozo.

MHE. AGNESTA L. KAIZA: Mheshimiwa Spika, naomba dakika moja ni-wind up. (Makofi)

SPIKA: Tukifika mbele kule kwenye vifungu na nini nitakupa tu nafasi, endelea kujiandaa.
Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali (Na. 3) wa Mwaka 2022
MHE. AGNES L. KAIZA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili nami kwa uchache niweze kuchangia katika Muswada huu muhimu ulio mbele yetu.

Mheshimiwa Spika, mchango wangu utajikita katika marekebisho ya Sheria ya Benki na Taaisisi za Kifedha, Sura ya 342 kifungu cha 21 ambacho kinapendekeza marekebisho ya sheria katika kipengele cha 17 ambayo ni sheria mama kwa kukifuta na kukiandika upya ambacho kinapaswa kusomeaka kama ifuatavyo, naomba kunukuu: “Kila benki au taasisi ya fedha itatakiwa kuwa na kiwango cha chini cha mtaji na kuhakikisha kuwa nyakati zote kiwango hicho hakipungui kadiri itakavyoelekezwa na benki kuu.” Mwisho wa kunukuu.

Mheshimiwa Spika, kwanza ni-declare interest kwamba mimi ni Mjumbe wa Kamati ya Katiba na Sheria na nimeshiriki kuupitia huu Muswada pamoja na wenzangu na mwisho wa siku sasa upo mbele yako kwa ajili ya kujadiliwa.

Mheshimiwa Spika, mtazamo au maoni ya Kamati katika Muswada huu ilikuwa ni kwamba Muswada utaje moja kwa moja kiasi halisi ambacho Benki au taasisi za fedha zinapaswa kuwanacho wakati wanaendesha shughuli zao. Maoni haya au mtazamo wa kamati ulikuwa ni kwa nia njema ili mwisho wa siku kuondoa changamoto mbalimbali ambazo kwa njia moja ama nyingine zingeweza kujitokeza.

Mheshimiwa Spika, kwa masikitiko makubwa sana, nimepitia jedwali la marekebisho la Serikali, sijaweza kuona kifungu hiki cha 21 kikionesha marekebisho yoyote ambayo yatasababisha kifungu hiki sasa kutumika katika ustawi mzima wa Taifa letu.

Mheshimiwa Spika, katika Kamati Serikali kinagaubaga na ikasema kwamba kiwango hiki kitatajwa katika kanuni mbalimbali ambazo zitaenda kutungwa ili mwisho wa siku kiweze kutekelezeka. Serikali haikuona umuhimu wowote Muswada huu kuingizwa moja kwa moja kwenye sheria kwamba hiki kiwango kitajwe sasa kwa uwazi kwamba ni Shilingi ngapi exactly ambayo taasisi hizi zinapaswa kuwa nayo?

Mheshimiwa Spika, katika maelezo ya Serikali ndani ya Kamati, Serikali ilisema kinagaubaga kwamba, kiasi cha Shilingi bilioni 15 ndicho kiasi ambacho ni minimum capital ambayo taasisi na benki wanapaswa kuwa nacho.

Mheshimiwa Spika, sote tunafahamu na kutambua kwamba ziko benki ambazo zina sura ya kitaifa, lakini pia zipo taasisi za kifedha na baadhi ya benki ambazo zina-operate shughuli zake za kiuchumi kwa maana ya kukopesha fedha kwa wananchi pasipo kutumia dhamana au amana za wananchi.

Mheshimiwa Spika, kwa sababu hiyo, kuwawekea kiwango kimoja kwamba sasa wanapaswa kuwa na Shilingi bilioni 15 za Kitanzania. Kwa upande wangu naona kwamba hapa sio sahihi, kwa sababu tunatambua zipo taasisi za fedha na wengine tumo katika hizo taasisi, zinatuhudumia. Tunatambua kwamba hizi taasisi unakuta ni mtu binafsi kabisa, ametafuta Mtaji wake, amepambana huku na kule au ni kikundi kimeji-organize, kimefungua taasisi ya fedha kwa ajili ya kukopesha wananchi, lakini hakikusanyi amana yoyote kutoka kwa hao watu ambao anaenda kuwahudumia.

Mheshimiwa Spika, kupitia Muswada huu, ikiwa sasa tutasema na taasisi hizo zinapaswa kuwa na mtaji wa Shilingi bilioni 15, naona sasa tunapoelekea tunaenda kuondoa kabisa hizi taasisi ambazo kimsingi zimekuwa ni mkombozi kwa wananchi na hususan kwa Wabunge wenzangu ambao tunatoka vijijini. Taasisi hizi zimekuwa ni faraja na msaada mkubwa kwa wananchi wetu na wapiga kura wetu.

Mheshimiwa Spika, taasisi hizi kwanza hazina masharti magumu. Kama tunavyofahamu, Watanzania asilimia kubwa ni wanyonge, hawana dhamana, hawana nyumba, hawana viwanja wala magari. Sasa kupitia taasisi hizi wananchi wameweza kujikomboa kwa kukopa fedha kwa ajili ya kuendesha shughuli zao za kiuchumi.

Mheshimiwa Spika, tunapokuwa tunakwenda kukubaliana na mapendekezo ya Serikali kwamba utaenda kuwekwa kwenye Kanuni, mwisho wa siku tukipitisha Muswada huu, moja kwa moja taasisi zote za kifedha bila kujali hali zao za kiuchumi, bila kujali kwamba taasisi hizi hazichukui chochote kile kutoka kwa wananchi, bali zina-deliver service tu kwamba nina mtaji wangu, sasa nakopesha wananchi Shilingi laki moja, laki mbili au laki tatu.

Mheshimiwa Spika, ikumbukwe kwamba taasisi hizi ndogo mdogo za kifedha zina-operate kwa kuangalia nature ya watu zinaowahudumia. Mfano, kule kijijini ninakotoka, haiwezekani ukaenda kukutana na mteja ambaye anasema anahitaji Shilingi milioni 20, Shilingi milioni 30 au Shilingi milioni 50. Kwa hiyo, unapoilazimisha ile taasisi kwamba wewe ni lazima uwe na mtaji wa Shilingi bilioni 15 ili uweze ku-operate, hata hao wateja huko vijijini huwezi kuwapata. Pia tutakuwa tumefunga mlango na kufungua mlango wa wawekezaji wakubwa kutoka nje, au ndani ya nchi ambao ni wachache sana watakaokwenda kushikilia uchumi, jambo ambalo siyo jema kwa mustakabali mzima wa Taifa.

Mheshimiwa Spika, tunatambua kwamba uchumi imara ni ule ambao unamilikiwa na wananchi wote. Sasa ili uchumi huu umilikiwe na wananchi wote, hatuna budi kuangalia suala hili. Nikubaliane kwamba Benki zenye sura ya Kitaifa lazima zidhibitiwe kwa sababu zimebeba dhamana/amana za wananchi. Ila hizi taasisi ndogo ndogo na baadhi ya benki ambao zimejipambania zenyewe, zimejikwamua; mtu anakwambia sasa nina mtaji huu nakwenda kuwakopesha wananhchi, sheria hii isifanye kazi kwao na badala yake uangaliwe utaratibu mwingine ambao utaweza kutumika ili kuhakikisha taasisi hizi zinaendelea siyo tu kuwa msaada, bali kuhakikisha zinasaidia wananchi wetu huko vijijini ambao uhitaji wao ni wa fedha ndogo ndogo kwa ajili ya kuendesha shughuli zao za kila siku.

Mheshimiwa Spika, naomba sasa nieleze madhara ambayo naona yatatukumba kama nchi ikiwa tutaruhusu huu utaratibu wa kwenda kutunga hizi kanuni pembeni. Sote tunatambua kanuni zinatungwa nje ya uwepo wa Bunge na zinapotungwa nje ya uwepo wa Bunge, which means sisi kama Bunge tunakuwa tumekaa pembeni ili kuweza kudhibiti watunga hizo Kanuni wasiweze kutunga Kanuni ambazo mwisho wa siku haziangalii maslahi mapana ya Watanzania.

Mheshimiwa Spika, kwa sababu hiyo, niseme kwamba tukiruhusu huu utaratibu twende nao kama mapendekezo yalivyokuja, niseme kwamba, cha kwanza, taasisi zote ambazo hazina uwezo wa hizo Shilingi bilioni 15 automatically tutakuwa tumeziondoa katika uwanja wa huduma, jambo ambalo siyo jema sana kwa sababu mwisho wa siku huwezi ukakuta CRDB Bank, NMB, sijui Barclays ukazikuta huko interior kwako Mbeya ndanindani kule kabisa. Haiwezekani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kingine nilikuwa najaribu kutafakari jambo hili; mimi kama Mbunge au wewe mwenyewe, the way unavyowapenda watu wako wa Mbeya, ukaamua kwamba kuanzia sasa nataka nikafungue kitaasisi cha fedha kwa ajili tu ya kuwahudumia wapiga kura wangu wa Mbeya, halafu unaambiwa you need fifteen billion kwa ajili tu ya kuwakopesha wale akina mama wa mboga mboga Shilingi 50,000/=, Shilingi 100,000/= na vitu kama hivyo. Haiwezekani. Mwisho wa siku hata hizo fedha kama utakuwanazo hutaweza kuzifanyia kazi.

Mheshimiwa Spika, naweka angalizo kwamba tuangalie namna ya kudhibiti hizi Benki zenye sura ya Kitaifa, lakini turudi chini tuangalie hizi taasisi ambazo zimekuwa ni mkombozi wa Watanzania kwa kipindi chote, tuone namna ya kuweka moja kwa moja sheria kwenye Muswada huu ambayo itasema moja kwa moja kwamba taasisi hizi hazihitaji kubanwa ndani ya hii Sheria ya kwamba lazima wawe na shilingi bilioni 15.

Mheshimiwa Spika, vile vile tukubaliane kwamba taasisi hizi ndogo ndogo za kifedha zimesaidia kwa asilimia kubwa sana kuondoa umasikini kwa wananchi wetu hususan kule vijijini. Tukienenda na huu utaratibu, ina maana tunaenda kukaribisha umasikini zaidi kuliko umaskini tulio nao sasa kwa wananchi wetu ambao wengi wako kule vijijini. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimekuwa nikisikia hapa Waheshimiwa Mawaziri tukiwemo na sisi kwamba mama yetu Mheshimiwa Samia anaupiga mwingi, na nikubali kwamba Mama Samia anaupiga mwingi. Sisi kama wanawake pasipo kujali vyama vyetu, tunasema jambo la mwanamke ni jambo la kwetu sote. Kwa hiyo, hatuna budi kumuunga mkono mwanamke mwenzetu.

Mheshimiwa Spika, hata hivyo, kwa mfumo huu tunaokwendanao kwenye huu Muswada, kweli tutakuwa tunamsaidia mama yetu Mheshimiwa Samia? Tunapokwenda kudidimiza taasisi ndogo ambazo zimekuwa ni mwarobaini kwa wananchi wetu wanyonge huko chini, sidhani kama tutakuwa tunamsaidia Mheshimiwa Rais wetu. Pia kingine hii inaweza ikaenda kuwa ni bomu kubwa zaidi kuliko hata tozo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niendelee kuomba kupitia Bunge lako tukufu kwamba suala la minimum capital liangaliwe kwa hizi Benki zenye sura ya Kitaifa na siyo vinginevyo, lakini sheria ya hizi benki na taasisi ndogo ndogo iingizwe moja kwa moja kwenye hii sheria na iseme waziwazi kabisa kwamba watu hawa hawatabanwa kabisa na hii sheria ya Shilingi bilioni 15.

Mheshimiwa Spika, nakushukuru. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. AGNESTA L. KAIZA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii ili na mimi niweze kuchangia hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu.

Mheshimiwa Naibu Spika, siku chache zilizopita kupitia Bunge lako hili Tukufu tulikaa na kujadili na kupitisha Mpango wa Serikali wa Miaka Mitano. Yote ambayo tumeyapitisha, yote ambayo tumeyajadili na leo hii tupo kujadili na kupitisha bajeti za Wizara mbalimbali, tutambue kwamba ufanisi wa jambo hili hauwezi kabisa kupatikana ikiwa wananchi wetu hawana afya njema. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika Ripoti ya CAG inayohusiana na mashirika ya umma, ukurasa namba 128, utaona jinsi ambavyo CAG kwa uwazi kabisa ameweza kuonesha ukosefu wa mamlaka ya kudhibiti bei za dawa pamoja na vifaa tiba. Tunatambua na tunafahamu kwamba, Watanzania wote au niseme asilimia kubwa ni maskini, si wanyonge, lakini ni maskini. Watanzania hawa hawawezi kabisa kumudu bei ghali za dawa pamoja na vifaa tiba. Kutokuwepo kwa chombo hiki cha kudhibiti bei za dawa pamoja na vifaa tiba kumesababisha wafanyabiashara wanaouza dawa pamoja na vifaa tiba kujipangia bei kadiri wao wanavyoona inafaa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, zipo sababu kuu mbili zinazosababisha dawa na vifaa tiba kuwa na bei ya juu sana. Serikali yenyewe ambayo inapaswa kuwa namba moja kuhakikisha wananchi wake wanapata huduma nzuri za afya kwa bei nafuu ndiyo ambayo imekuwa ikisababisha wafanyabiashara kupandisha bei za dawa pamoja na vifaa tiba kwa sababu katika hospitali zetu hakuna dawa kabisa. Serikali hii ambayo siku zote inajinasibu kwamba imekuwa ikitekeleza yale ambayo imepanga imekuwa ni namba moja kusababisha wananchi wetu kushindwa kumudu dawa hizi ambazo nimezielezea. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa msingi huo basi, naomba niseme hivi, tunayo MSD ambayo kazi yake ni kununua na kusambaza dawa pamoja na vifaa tiba katika hospitali zetu, lakini kumekuwepo na upungufu mkubwa wa dawa hizi ambazo naelezea pamoja na vifaa tiba. Ni kwa nini basi kumekuwepo na huu upungufu? Ni kwa sababu Serikali imekuwa ikikopa fedha kutoka MSD na hairejeshi kwa wakati na wakati mwingine hairejeshi kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ukifuatilia Ripoti ya CAG ya mwaka 2017, 2018 na 2019, Serikali hii ilikuwa inadaiwa shilingi bilioni 53.63. Tungetegemea kwamba katika Ripoti ya CAG ya sasa tuone ni jinsi gani Serikali imeweza kupunguza, kama siyo kumaliza kabisa deni hilo ambalo ni kubwa sana. Hata hivyo, katika ripoti hii mpya ya CAG inasema, Serikali mpaka sasa inadaiwa kiasi cha shilingi bilioni 256. This is a shame kwa sababu huwezi kuwa inapoitwa leo wewe unazidi kuongeza madeni. Tulitegemea Serikali iwe ndiyo namba moja kuwa na huruma kwa Watanzania hawa. (Makofi)

T A A R I F A

MHE. ERIC J. SHIGONGO: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Eric Shigongo.

MHE. ERIC J. SHIGONGO: Mheshimiwa Naibu Spika, nilitaka tu kumkumbusha mzungumzaji aliyekuwa anazungumza kwamba Serikali ya Chama cha Mapinduzi imechukua hatua za kutosha kabisa za kuimarisha MSD. Kiongozi Mkuu wa MSD kwa sasa alitoka Jeshini. Chini ya uongozi wa Meja Jenerali huyu, MSD imefanya improvement kubwa sana ikiwemo kuanzisha kiwanda chake yenyewe cha kutengeneza paracetamol. MSD inatengeneza paracetamol zake yenyewe na imeweza kushusha cost za kufanya dialysis katika nchi yetu. Kwa hiyo, kusema kwamba, ni shame sio jambo sahihi, ahsante. (Makofi)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Agnesta Lambert, unaipokea Taarifa hiyo?

MHE. AGNESTA L. KAIZA: Mheshimiwa Naibu Spika, Taarifa hiyo siipokei kwa sababu nilichokitaja hapa kwamba Serikali inadaiwa shilingi bilioni 256 ni kutokana na Ripoti ya CAG.

Sasa Mheshimiwa Mbunge pale kama anadhani kusema kwamba wamejenga kiwanda cha kutengeneza Panadol ndiyo iwe sababu sasa ya kusema kwamba mna haki ya kukaa na shilingi bilioni 256, yet Waziri husika anakuja hapa mbele anatuambia kwamba tunazo dawa katika hospitali, it can’t be. (Makofi)

T A A R I F A

MHE. KHADIJA S. TAYA: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Mbunge, kuna Taarifa nyingine kutoka kwa Mheshimiwa Khadija Shaaban Taya.

T A A R I F A

MHE. KHADIJA S. TAYA: Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nimwambie mzungumzaji Mheshimiwa Agnesta kwamba sasa hivi tunajadili kuhusu Hotuba ya Waziri Mkuu, hatujaanza bado kujadili Hotuba ya CAG, nashukuru sana. (Makofi)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Agnesta Lambert.

MHE. AGNESTA L. KAIZA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niendelee kwa sababu nafahamu na kutambua kwamba Mheshimiwa Khadija anafahamu fika kabisa kwamba anachokisema sicho kabisa.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sasa niendelee kujikita katika ushauri kuhusiana na jambo hili kwa upande wa Serikali. Kwa sababu ikiwa tutakuwa hatuna chombo hiki maalum au mamlaka maalum ambayo itadhibidi bei za dawa pamoja na vifaa tiba, mwisho wa siku tutakuwa na Watanzania ambao usiku na mchana wanaumwa na magonjwa madogo lakini wanakosa dawa ambazo kimsingi dawa hizo zilipaswa kuwepo. Kauli mbiu ya Serikali ya sasa ni ushindani wa viwanda na maendeleo ya watu iende sasa ikajielekeze katika kulipa hizi shilingi bilioni 256 ili mwisho wa siku MSD waweze kuleta dawa kwa wingi kuliko ilivyo sasa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimesikia hapa wengine wanachangia, Waziri alikuwa anajibu anasema dawa zipo, hakuna kitu kama hicho. Ni knowledge ya kawaida tu MSD wanategemea Serikali ilipe madeni na wenyewe waende kuagiza dawa, lakini mwisho wa siku MSD inaonekana imekuwa na yenyewe ikikopa kule inakoagiza dawa. Kwa hiyo, inafika sehemu ambayo haiwezi tena kuagiza mpaka Serikali iweze kulipa madeni. Kwa kipindi hiki ambacho tunapitia katika mlipuko wa wimbi la pili la Covid-19 ni vema basi Serikali hii ikafanya kwa vitendo kulipa hili deni ili mwisho wa siku tuweze kuhakikisha kwamba tunaona hili suala la Covid-19 hatupati shida ya dawa katika hospitali zetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ukosefu wa hii mamlaka ambayo nimeisema mwisho wa siku Watanzania wanakwenda kununua dawa katika pharmacy wanakutana na bei ghali sana. Hii ni kwa sababu wafanyabiashara wa dawa hizi hawana kitu kinachowa-limit kwamba dawa hii inapaswa kuuzwa kwa bei kuanzia elfu moja mpaka elfu tano. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora
MHE. AGNESTA L. KAIZA: Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru na mimi niende moja kwa moja katika mchango wangu. Nitakwenda kuanzia walikoishia Waheshimiwa Wabunge wenzangu hususan Mheshimiwa Nape Nnauye.

Mheshimiwa Naibu Spika, sheria inataka watumishi wa umma wapandishwe madaraja kila baada ya miaka mitatu, hiyo ndiyo sheria inavyotaka. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kumekuwepo na watendaji wa taasisi mbalimbali ikiwemo utumishi wa umma wamekuwa wakishusha nyaraka mbalimbali ambazo zinakinzana moja kwa moja na sheria hii ambayo nimeitaja awali na nyaraka hizi zimekuwa zikielekeza kwamba watumishi wapandishwe madaraja kila baada ya miaka mitano. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa tunaye Waziri husika Mheshimiwa Mchengerwa, ningependa atakapokuja ku-wind up atueleze ni kwa nini basi Wizara imeamua kukiuka Sheria hii ya Watumishi wa Umma kwa nini wameamua basi kukiuka sasa sheria hii na sasa wametengeneza nyaraka tofauti kabisa ambazo zinapingana na haki za watumishi wa umma. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hivi nilivyosimama mbele yako wapo watumishi wengi ambao ni takribani miaka sita hawajapandishwa madaraja na nimesema kuna nyaraka ambayo inakinzana na sheria yenyewe ambayo inasema watumishi hawa wa umma wapandishwe madaraja ndani ya miaka mitano, lakini sasa hivi hata hilo ambalo haliendani na sheria wameshindwa kulitimiza.

Mheshimiwa Naibu Spika, wote tunafahamu kwamba watumishi wa umma ndiyo kiungo pekee cha Serikali katika utekelezaji wote wa bajeti tunazopitisha, mipango yote ambayo tunaipima, tunaipanga, lakini maslahi yao yamekuwa hayaangaliwi. Kama jinsi ambavyo nimesema watu walipaswa kupandishwa madaraja miaka sita iliyopita na watumishi hawa wanaendelea kuchapa kazi na watumishi hawa wanaendelea kutarajiwa kwamba wa-deliver vizuri kulingana na taratibu za utumishi jinsi zinavyosema. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna msemo unasema ukitaka kumtawala mtu unapaswa kuhakikisha anakula na kushiba. Ikiwa tunahitaji watumishi hawa wa umma waweze kufanya kazi kwa ufanisi hatuna budi kuangalia maslahi yao ikiwemo kupandishwa madaraja, ikiwemo kulipwa/ kuongezewa mishahara, lakini pia ikiwepo kulipwa malimbikizo yote ambayo watumishi hawa wa umma wanayadai. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ni jukumu la Serikali kuhakikisha inatoa mafunzo kwa watumishi wa umma na mafunzo siyo luxury, siyo kwamba ni starehe, hapana, tunaishi katika dunia ambayo inakwenda kwa kasi, teknolojia zinakwenda kwa kasi. Ninavyosimama hapa mbele yako ni miaka sita imepita hakuna mafunzo yaliyofanywa kwa watumishi wa umma hawa. Lakini watumishi hawa tunategemea na kuwatarajia waweze ku-deliver kulingana na jinsi teknolojia inavyokwenda jambo hili haliwezekani na haliendani na uhalisia kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ushauri wangu kwa Serikali ufanyike utaratibu wa haraka wa kuhakikisha watumishi hao wa umma wanapatiwa mafunzo na siyo tu suala la kupatiwa mafunzo; watumishi wetu wanapaswa kupata exposure, mtumishi unakuta yupo kazini zaidi ya miaka sita, lakini hajawahi hata siku moja kwenda nje angalau kupata mafunzo au hata kupata exposure tu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa jinsi dunia inavyokwenda lazima tukubali kwamba watumishi wetu wanapaswa kwenda sambamba na the way dunia inavyokwenda kwa kasi.

Kwa hivyo basi, ushauri wangu kwa Serikali na hususan kwa Wizara husika waangalie uwezekano mkubwa sana wa kufuta hii damage ya kuwa na watumishi ambao takribani miaka sita hawajapata mafunzo na mwisho wa siku ndiyo maana tunawakuta Wakuu wa Wilaya mfano Mkuu wa Wilaya tu anakwenda kwenye eneo lake la kazi, anakutana na watumishi wale ambao wako chini yake, badala ya kuwaelekeza namna ya kufanya kazi, hata akikuta wamekosea kidogo mwisho wa siku anawachapa viboko. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wakati mwingine tunaweza kudhani kwamba wanafanya makusudi, wakati mwingine hawajui hata wajibu wao, mwisho wa siku wanadhani hata kupiga viboko ni sehemu ya majukumu yao. Ndiyo maana nasema suala la mafunzo kwa watumishi wetu wa umma ni lazima na ni takwa la kisera. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo upande wa utumishi tunatambua au niseme natambua kwamba zipo taratibu na kanuni zinazotuongoza au zinazoongoza Wizara husika kuwajibisha watumishi wa umma pale ambapo wanakutwa na makosa mbalimbali. Lakini hivi ninavyoongea na wewe hapa kupitia Bunge lako Tukufu, wapo watumishi wengi ambao wamewekwa bench kwa masuala mazima ya nidhamu. Watumishi hawa wengine wamekaa zaidi ya miaka mitatu/minne mpaka mitano wako bench wanafamilia, wanatunza familia, wanapeleka watoto shule maisha yao yote yanategemeana na kazi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini watumishi hawa hawapewi hata ile nusu mshahara ambayo kikatiba kisheria na kikanuni unapokuwa umewekwa bench, haujakutwa na hatia lazima ulipwe nusu mshahara. Lakini mtumishi huyu yuko miaka minne na wakati yuko kazini alikopa, wote tunatambua mishahara ya watumishi wetu hawa siyo mikubwa, haiwezi ikawafanya wakaishi comfortable.

Kwa hiyo, watumishi hawa wamekuwa wakikopa walipokuwa kazini, wapeleke watoto shule, wale, walipe kodi za nyumba, wengine hata kujenga hawana uwezo wa kujenga. Lakini leo hii wamewekwa bench kwa takriban ya miaka minne hawapewi hata senti wanaishije. Je, unadhani wale ambao wapo wanaendelea na kazi wanapokuwa wanaona yanayowapata hawa waliopo bench watashindwa kuchukua rushwa, kweli watakuwa ni waaminifu? Haiwezekani.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo niombe kupitia Wizara na Mheshimiwa Mchengerwa nimekuwa chini ya uongozi wako ukiwa Mwenyekiti wangu wa Kamati ya Katiba na Sheria, nakujua utendaji kazi wako naujua, commitment yako naijua kwa Taifa hili, nikuombe chonde chonde uangalie ni namna gani sasa ya kwenda kufuatilia mambo haya wengine wamesimamishwa siyo kwa sababu wanamakosa, ni kwa sababu waliowasimamisha wana bifu na tu ni kwa sababu wanawasimamisha wanadhani wanawezafanya chochote as long as wao wako kwenye madaraka. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo ambalo nimelisema kuhusiana na Wakuu wa Mikoa Wakuu wa Wilaya pamoja na Wakurugenzi wote tunatambua hawa ni wateule wa Mheshimiwa Rais. Unapokuwa mteule wa Mheshimiwa Rais, ukaenda huko chini katika majukumu yako ya kila siku unakwenda kwa niaba ya Mheshimiwa Rais, sasa unapofika kule ukafanya vitu ambavyo haviendani na miongozo ambayo sisi wenyewe tuliisaini kama watumishi kwamba tutakuwa na maadili, tutaongoza kwa kuongozwa na miongozo hii ya maadili, mwisho wa siku Serikali ambayo inasimamiwa na Mheshimwia Rais inapata taswira mbaya kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ndiyo maana Mheshimiwa Waziri utakapokuja ku-wind up natamani nisikie angalau unatoa tamko kwa Wakuu wa Wilaya, kwa Wakuu wa Mikoa, Wakurugenzi ukiwaelekeza namna ya kufanya wakati tunaandaa mafunzo ambayo nimeweza kuyasema. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niseme jambo moja lingine niombe au niseme ushauri kwa mambo yote ambayo nimeelezea hapa kuhusiana na watumishi wa umma, kwa mambo yote ambayo nimeeleza hapa hususiana na utawala bora, Mheshimiwa Waziri nikuombe mambo makuu matatu; la kwanza chonde chonde waangalie watumishi hawa wa umma ambao waliwekwa bench ambao mpaka sasa hivi wengine wamekimbilia vijijini, vijijini na kwenyewe wamekuta matatizo ya wazazi wao hawawezi kabisa kujisaidia wao hata kusaidia familia zao, uchunguzi ufanyike haraka Mheshimiwa Waziri, ufanyike uchunguzi ambao hawana hatia warudi kazini na wakirudi kazini…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Kengele ya pili imeshagonga ahsante sana.

MHE. AGNESTA L. KAIZA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sekunde nimalize ushauri kwa Serikali. (Makofi)

NAIBU SPIKA: Utashauri kwa maandishi muda wetu hautoshelezi ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 –Wizara ya Katiba na Sheria
MHE. AGNESTA L. KAIZA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii ili nami kwa uchache niweze kuchangia katika Wizara hii muhimu ya Katiba na Sheria. Mchango wangu utajikita katika mafungu mawili tu, kwa maana ya Fungu la 59 na Fungu la 35.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika Magereza yetu nchini kumekuwepo na changamoto kubwa ya mlundikano wa wafungwa pamoja na mahabusu. Mlundikano huu siyo kwamba Tanzania tuna wahalifu wengi sana, siyo kwamba Watanzania hatutekelezi sheria ambazo tunaelekezwa. Sababu kubwa sana ya milundikano ni kwa sababu kesi au tuseme mashauri yanachukua muda mrefu sana kufanyiwa upelelezi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na mlundikano huu, wakati mwingine mahabusu yanazidiwa nguvu na kupelekea watoto wa chini ya miaka 18 kwenda kuungamanishwa au kuchanganywa katika Magereza au Mahabusu ya Watu Wazima. Inawezekana ikaonekana kwamba ni maajabu ninaposema kwamba inafika wakati watoto wa chini ya miaka 18 wanawekwa pamoja na mahabusu watu wazima, lakini hii inatokea kwa sababu kama mahabusu yamezidiwa na kuna watoto ambao wanapaswa kuingia mle ndani, automatically kwa sababu mabweni hayatoshi, tutajikuta watoto wetu wanaingizwa, wanachanganywa na watu wazima na mwisho wa siku wanajifunza tabia mbaya ambazo hawakuingia nazo katika yale Magereza au Mahabusu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sababu nyingine inayopelekea mlundikano mwingi katika Magereza haya ni kwa sababu kumekuwepo na kubambikiziwa kesi nyingi sana za jinai, yaani kila inapoitwa leo unasikia fulani ana kesi ya uhujumu uchumi. Ukisikia mtu fulani amepigana tu na mwenzake; ni mke na mume wamepigana nyumbani wakifikishwa tu kule Mahakamani unaambiwa umehujumu uchumi. Kwa sababu mambo haya yapo katika jamii na tunayaishi, ni wazi kabisa kwamba mlundikano hauwezi kumalizika katika Magereza na Mahabusu zetu. (Makofi/ Kicheko)

Mheshimiwa Naibu Spika, sababu nyingine na mlundikano katika Magereza zetu inatokana na uwepo wa masharti magumu ya upatikanaji wa dhamana. Najaribu kuangalia au kuwaza huko vijijini, tuachie kwanza mjini; huko vijijini ambapo changamoto hizi za watu kubambikiwa kesi, hivi na vile, zimeshika kasi sana kuliko mjini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, najaribu kuwaza kwamba ili mtuhumiwa aweze kudhaminiwa, anapaswa kuwa na watumishi wawili wa Serikali kwenda kumdhamini; na ikumbukwe kule vijijini ni ngumu sana, siyo rahisi sana kama mjini kwamba utapata Watumishi wa Umma, ni ngumu sana. Hata ukiwakuta hao wachache, hawana utayari wa moja kwa moja wa kudhamini watuhumiwa, kwa sababu unakuta mtu ametolewa Tanga anakwenda kufanya kazi huko Kagera kwetu huko ndani kabisa, hafahamiani na mtu, hana ushiriki mzuri wa moja kwa moja na wale watu, kwa hiyo, ni ngumu sana kumdhamini mtu ambaye hamfahamu vizuri kabisa. Hili linakuwa ni changamoto sana, nimesema zaidi sana vijijini kwa sababu mjini unaweza ukapata kidogo unafuu wa kumpata mdhamini kwa sababu Watumishi wa Umma wapo wengi ukilinganisha na vijijini. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Naibu Spika, tukiweka pembeni hilo la uhaba wa watumishi vijijini kwenda kuwadhamini watuhumiwa, sheria inamtaka mtuhumiwa aweke dhamana ya hati ya nyumba, kwa maana ya mali isiyohamishika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, unapowaambia watuhumiwa hao kwamba wanapaswa kuwa na hati ili waweze kujidhamini wakati tunafahamu kwamba hati hizi siyo tu vijijini, hata mijini ni less than fifty percent ya watu ambao wana hati za nyumba. Kwa hiyo, unaweza kuona mlolongo huu ambao nimeweza kuulezea, sababu hizi chache kati ya nyingi ambazo nimeweza kuzielezea zinazopelekea mlundikano mwingi katika Magereza yetu unatokana moja kwa moja na kuwepo kwa masharti magumu ya dhamana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ushauri wangu katika hili, Tume ya Kurekebisha Sheria ilete maboresho hapa Bungeni; kwanza, tupitishe sheria ya kuwepo na ukomo wa upelelezi wa hizi kesi ambazo zinachukua muda mrefu. Tukifanya hivyo, tutapunguza moja kwa moja mlundikano usiokuwa wa lazima katika Magereza. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niende moja kwa moja sasa...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023
MHE. AGNESTA L. KAIZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili nami kwa uchache niweze kuchangia katika Mpango huu. Ili Mpango wowote wa maendeleo uweze kutekelezeka kunahitaji nguvukazi yenye afya bora. Chombo pekee kinachoshughulika na masuala mazima ya kununua na kusambaza dawa na vifaatiba ni bohari kuu ya dawa yaani MSD. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa ya PAC ya tarehe 18 Agosti, 2021 imeweka bayana jinsi ambavyo deni la Serikali kwa MSD imekuwa ni changamoto kubwa sana inayopelekea MSD ishindwe kutekeleza wajibu wake kwa ufanisi. Deni la Serikali mnamo tarehe 18 Agosti kama nilivyosema, ilikuwa imefikia shilingi bilioni 269. Baada ya PAC kuikaripia Serikali kwamba sasa inazorotesha ufanisi wa MSD, mnamo mwezi Septemba Serikali ililipa shilingi bilioni 39 tu kutoka katika deni la shilingi bilioni 269. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ikumbukwe mnamo mwaka 2018 na 2019 deni la Serikali kwa MSD ilikuwa ni shilingi bilioni 53.63 na kwa kipindi kile kwa mujibu wa CAG, alisema MSD ilikuwa na hali mbaya, mbaya, mbaya sana. Sasa linganisha deni lile la shilingi bilioni 53.63 na deni la sasa la shilingi bilioni 269; unaweza kuona namna gani MSD wana hali mbaya. Kama MSD ina hali mbaya, basi Watanzania tuna hali mbaya sana. Nimesema Serikali imelipa shilingi bilioni 39 tu mpaka sasa na kufanya balance ya deni liwe ni shilingi bilioni 230 mpaka wakati huu ninapokuwa naongea mbele ya Bunge lako Tukufu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wote tunatambua, bila ya kuwa na nguvu kazi yenye afya bora, Mipango yote tunayoipanga hapa kamwe haiwezi kutekelezeka kwa ufanisi. Tumesikia au niseme nimesikia na nimesoma taarifa ya Kamati ya Bajeti na niseme naipongeza sana Kamati hii kwa sababu imefanya kazi nzuri sana, kwa msemo wa sasa wanasema Kamati hii imeupiga mwingi sana. (Makofi/ Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa ya Kamati ya Bajeti inasema, MSD ina hali mbaya na hivyo basi, inahitaji shilingi bilioni 363.39 ili iweze kufanya majukumu yake kwa ufanisi. Yaani hapo MSD wanahitaji mtaji. Kwa lugha nyingine MSD hivi tunavyoongea haina mtaji kabisa na tupo hapa tunapanga mipango ya maendeleo ambayo wanaokwenda kuitekeleza hawana uhakika wa afya bora. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa ya bajeti inasema, bajeti inaelekeza kwamba Serikali itenge shilingi bilioni 150 ipeleke MSD. Hiyo ni sehemu ndogo angalau ya bajeti halisi ya shilingi milioni 363.93. Ni wazi kabisa, kwa changamoto ya MSD jinsi ilivyo, hata leo hii tukisema tupeleke shilingi bilioni 150, chombo ambacho hakina mtaji kabisa, shilingi bilioni 150 haiwezi kutosha kabisa, kabisa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mawazo yangu, shilingi bilioni 150 haiwezi kutatua changamoto zilizopo MSD. Ni kwa nini nasema hivi? Tumesema MSD inahitaji mtaji wa shilingi bilioni 363.93 lakini inaidai Serikali shilingi bilioni 269 na kwa sasa imebaki shilingi bilioni 230 kama balance ya deni. Kwa hiyo, leo hii ukipeleke shilingi bilioni 150 MSD, kwanza unawaongezea stress tupu, kwa sababu hazitoshi kuagiza dawa, hazitoshi kulipa madeni na mwisho wa siku sasa wanabaki wanajiuliza, hizi fedha tuzifanyie jambo gani?

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hotuba ya Waziri wa Fedha inayohusu Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo 2022/2023 kwa maana ya Mheshimiwa Dkt. Mwigulu, ameeleza katika ukurasa wa 14 mpaka ukurasa wa 15, naomba nimnukuu, anasema: “Upatikanaji wa dawa muhimu katika vituo vya kutolea huduma za afya umefikia asilimia 94.”

Mheshimiwa Mwenyekiti na Waheshimiwa Wabunge katika Majimbo yetu tujiulize, ni kweli tumefikiwa kwa asilimia 94? Kama haitoshi, Mheshimiwa Waziri wa Fedha akaenda mbali akasema, “shilingi bilioni 234 zilitolewa kwa ajili ya kununua dawa na shilingi bilioni 26.3 kwa ajili ya vifaa tiba.”

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii siyo realistic. Nayasema haya kwa sababu kuu mbili; kwanza, PAC imesema, Kamati ya Bajeti imesema na Waziri Mkuu Mheshimiwa Kassim Majaliwa mnamo tarehe 10/10/2021 aliongea na Waandishi wa Habari akiwa na Mkurugenzi Mkuu wa MSD pamoja na Naibu Waziri wa Afya, akawaelekeza na akasema baada ya kutoka kwenye ziara aliyokuwa anaifanya, alikuta kule chini kwenye Mikoa, kwenye kanda kwenye Wilaya, kote kabisa hali ni mbaya. Hali ilikuwa ni mbaya kweli kweli, na Mheshimiwa Waziri aliwaelekeza na kuwapa wiki moja wawe wametekeleza jukumu la kushusha dawa. Sasa hii asilimia 94 inatokea wapi? (Makofi/Kicheko)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Malizia.

MHE. AGNESTA L. KAIZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, inatokea wapi? Je, tuamini Mpango, tumwamini Mheshimiwa Waziri Mkuu, tuiamini PAC au Kamati ya Bajeti? Where? Wapi? Ni nani tuweze kumwamini?

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu sasa…(Makofi/Kicheko)

MWENYEKITI: Nusu dakika.

MHE. AGNESTA L. KAIZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu, nafahamu hivi karibuni tumepokea mkopo wa shilingi trilioni 1.3. Ili kuondokana na aibu hii iliyopo ya MSD nashauri mambo makuu mawili. Kwanza itengwe shilingi bilioni 600 zipelekwe MSD kwa sababu ya mambo makuu mawili; mosi, ikamalize balance ya deni la Serikali ya shilingi bilioni 230. Iikisha-clear hiyo shilingi bilioni 230, ina maana kwenye hiyo shilingi bilioni 600 tutakuwa tumebaki na shilingi bilioni 363.93 ambayo ndiyo mtaji halisi wa MSD wanaouhitaji waweze kufanikisha majukumu yao. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Agnesta. Najua muda hautoshi. Ahsante sana, muda haupo upande wako.

MHE. AGNESTA L. KAIZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakuomba wakati nakaa, Waziri anapokuja ku-wind up atuondolee mkanganyiko huu wa taarifa tatu; atuambie tuuamini Mpango, tumwamini Mheshimiwa Waziri Mkuu, tuiamini PAC au tuiamini Kamati ya Bajeti?

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. (Makofi)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2022
MHE. AGNESTA L. KAIZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru kwa kunipa nafasi ili nami kwa uchache niweze kuchangia katika Kamati ya Katiba na Sheria, Kamati ambayo mimi mwenyewe ni Mjumbe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza niipongeze Kamati ya Katiba na Sheria kwa kazi nzuri iliyotukuka ambayo imeweza kuifanya chini ya Mwenyekiti wetu na niseme kwamba naunga mkono kwa asilimia 100 kile ambacho kimewasilishwa hapa katika Bunge lako tukufu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitajikita leo katika kuchangia suala zima la ushirikishwaji wa wadau katika kutunga sheria. Taarifa ya Kamati imeweka bayana umuhimu wa kutanua wigo kwa ajili ya wadau kushiriki vyema kabisa katika kutoa maoni yao katika utungwaji wa sheria, na tunafahmu vyema kabisa kwamba zipo faida nyingi sana ambazo tunazipata kama Taifa pale ambapo ushiriki wa wadau unakuwa ni ushiriki uliokamilika kwa maana ya kupata muda mzuri, muda wa kutosha kudadavua, kupitia sheria zote ili hata wanapokuwa wanatoa maoni basi, watoe maoni ambayo yanaendana na uhalisia wa wananchi ambao wanakwenda kutekeleza sheria hizo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na mapendekezo hayo mazuri ya Kamati, niseme kwamba lipo tatizo moja kwa upande wa Serikali na tatizo hilo ni kuleta miswada kwa Hati ya Dharura hapa Bungeni, miswada ambayo mara nyingi inakuwa haina udharura ndani yake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, unapokuwa unaleta muswada Bungeni kwa Hati ya Dharura, wote tunafahamu kwamba, lazima kuwepo na udharura kweli kweli, na tunafahamu kwamba, udharura wenyewe ni pale ambapo huenda nchi ipo hatarini au nchi iko katika vita au kuna udharura mkubwa kiasi kwamba jambo hilo lisipotungiwa sheria kwa Hati ya Dharura nchi itakuwa katika hatari. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa sisi ni mashahidi katika Bunge lako hili tukufu, ipo mifano mingi sana ya miswada ambayo imeletwa hapa Bungeni kwa Hati ya Dharura, lakini haikuwa na huo udharura, na kwa sababu, ililetwa bila wadau kuwa wametoa maoni yao kikamilifu sheria hizi zilivyopitishwa tu kwa muda mfupi zilirudi Bungeni kwa ajili ya marekebisho. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti sisi ni mashahidi katika Bunge lako hili tukufu, ipo mifano mingi sana ya miswada ambayo imeletwa hapa Bungeni kwa hati ya dharura lakini haikuwa na huo udharura na kwa sababu ililetwa bila wadau kuwa wametoa maoni yao kikamilifu, sheria hizi zilivyopitishwa tu kwa muda mfupi zilirudi Bungeni kwa ajili ya marekebisho na unapoona kwamba Bunge ambalo linaaminiwa na nchi kwamba Wabunge tumepewa jukumu la kutunga sheria tunatunga sheria ambayo inakwenda kwa wananchi na muda mfupi inarudi kuonekana kwamba kile tulichokitunga hakikuwa na uhalisia hii inakuwa ni aibu kwa Taifa, lakini pia tunakuwa tunachonganisha sasa Bunge na wananchi, lakini pia tunakuwa tunamchongea Mheshimiwa Rais ambaye lazima asaini zile sheria sasa zianze kwenda kutumika. Sasa zinakuwa zimetumika na zimerudi kwamba hazina tija, Mheshimiwa Rais naye tunakuwa tumemweka katika wakati mgumu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nitoe mifano ya baadhi ya sheria ambazo tulizitunga na muda mfupi tu zikarudishwa hapa Bungeni. Sheria ya kwanza ni Sheria ya Habari; sisi ni mashahidi sheria hii ilirudi na ni kwa sababu hatukutoa mwanya wa wadau kudadavua na kutoa maoni yao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sheria nyingine ni Sheria ya Vyama vya Siasa; Serikali ilileta muswada huu wa Sheria ya Vyama vya Siasa kwa hati ya dharura na haikuwepo udharula wowote ule na kimsingi muswada huu ndio muswada pekee ambao ulipaswa kutoa wigo mpana wa wadau kuweza kuchangia, kudadavua kuweka mpaka midahalo ili tunapokuja Bungeni kupitisha tuwe tumepitisha jambo ambalo ni sahihi, lakini nao pia ulirudishwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sheria nyingine ni Sheria ya Takwimu; huko nje kwa wananchi, wananchi tunaowaongoza wanatuamini sisi Wabunge waliotuchagua wakiamini kwamba sisi ndio wanasheria wao ambao tunakuja kuwatungia sheria ambazo zitakuwa ni rafiki ili ziweze kutekelezeka, lakini matokeo yake tunatunga sheria ambazo mwisho wa siku zinakuwa ni mzigo, zinakuwa hazitekelezeki na ni kwa sababu ya Serikali kuleta miswada kwa hati ya dharura ambayo haina udharura wowote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hili naomba nishauri sasa; Serikali nafahamu kwamba inatambua nini maana ya neno udharura inajulikana na wote tunafahamu. Ituletee miswada ya hati ya dharura ambayo kweli kweli ina hati ya udharura, I mean ina uhitaji wa haraka wa kutungiwa sheria kwa hati ya dharura. Lakini kama si hivyo basi Serikali inapaswa kuleta hii miswada ya sheria kwa maana kuhakikisha wadau wote wameshiriki kikamilifu na ikibidi sisi Wabunge ambao ndio wadau namba moja, sisi ndio watunga sheria, sisi ndio wapitisha sheria, sisi wenyewe nje ya wadau wengine tunapaswa kudadavuliwa moja kwa moja hii miswada kabla hata haijaja Bungeni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, na…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana.

MHE. AGNESTA L. KAIZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja, ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Katiba na Sheria
MHE. AGNESTA L. KAIZA: Mheshimiwa Spika, nikushukuru kwa kunipa nafasi ili namimi niweze kuchangia machache katika Wizara hii ya Katiba na Sheria. Kabla sijaenda katika mchango wangu wa leo, naomba nitumie nafasi hii kwanza kabisa kumpongeza Waziri wa Katiba na Sheria, Naibu Waziri Mheshimiwa AG pamoja na Mtendaji Mkuu wa Mahakama kwa kazi nzuri kwa kweli ambayo wanaifanya. Mimi ni Mjumbe wa Kamati ya Katiba na Sheria, nimeshiriki katika ziara kwenda kukagua miradi ya maendeleo iliyopo chini ya Mahakama.

Mheshimiwa Spika, nikiri kwamba kwa macho yangu nimeona value of money na nichukue nafasi hii kuwapongeza kwamba fedha ambazo zimetengwa, hakika Mahakama wamezitendea haki na value for money inaonekana kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya hapo sasa, niende kwenye mchango wangu ambao utakijita kwenye Fungu namba 55 kwa maana ya Tume ya Haki za Binadamu. Tume ya Haki za Binadamu ndicho chombo pekee ambacho kimeundwa na Serikali ili kuhakikisha kinalinda, kinasimamia haki zote za binadamu nchini. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa lugha nyingine ikiwa kuna namna yoyote ya haki za binadamu kutokufuatwa au kuvunjwa, nchi haiwezi kuwa katika hali ya usalama. Nayasema haya ili kuonesha namna gani ambavyo chombo hiki au Tume hii ya Haki za Binadamu ni chombo muhimu sana, lakini kwa masikitiko makubwa sana niseme Tume hii imekuwa ni Tume mfu. Nayasema haya na niliyasema hata ndani ya Kamati yangu ya Katiba na Sheria, nikasema Tume hii ni Tume ambayo imekuwa ikionekana au naweza nikasema imekuwa ikifufuka wakati wa bajeti kama hizi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Tume hii haisikiki kabisa huko kwa wananchi ambapo inapaswa kusikika. Tume hii imeshindwa kutekeleza wajibu wake wa msingi ambao umeidhinishwa au ni jukumu lake la kimsingi kikatiba kuhakikisha wanasimamia na wanalinda haki za binadamu zisivunjwe. Pamoja na majukumu mengine Tume hii ina wajibu wa kutembelea katika magereza, kutembea shuleni, kutembea katika vituo vya Polisi kuhakikisha wanalinda na wakati wanalinda wanaangalia, je, haki za Watanzania zinalindwa? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niseme kwamba Tume hii haifanyi kazi na naweza kusema kwamba haifanyi kazi kabisa kwa sababu hatuisikii. Nayasema hayo kwamba ni mfu, ukiangalia bajeti ya mwaka wa fedha ya maendeleo ya mwaka 2021/ 2022, bajeti ya maendeleo ilitengwa Sh.373,000,000 tu na fedha hizi hazitokani na mapato ya ndani, ni fedha ambazo zinatoka kwa donors. Sasa inasikitisha kwamba haki za watu wetu zinalindwa na watu wa kutoka nje, yaani Serikali haioni kama ina wajibu wa kutenga bajeti tena bajeti ya kutosha kuhakikisha Tume hii sasa inakwenda kufanya kazi yake kwa uaminifu, kwa uadilifu, lakini pasipokuwa na kikwazo cha bajeti. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mimi natokea Mkoa wa Dar es Salaam, Mkoa wa Dar es Salaam tukihesabu kuna shule ngapi, tukihesabu kuna vituo vya Polisi vingapi, tukayahesabu na magereza ukiangalia hii bajeti ya Sh.373,000,000 haiwezi kutosha hata kwa mkoa mmoja! Kama kweli Tume inafanya kazi fedha hizi sio tu kwamba hazitoshi nchi nzima hata mkoa mmoja hazitoshi. Hata hivyo, kuonesha kwamba Tume hii ni mfu mwaka huu wa bajeti imetengwa Sh.260,000,000 tu na hizi fedha ni kutoka nje, hakuna mpango mkakati wa Serikali kuona umuhimu wa kulinda haki za watu wake au wananchi wake ni mpaka tusaidiwe na donors kutoka nje. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa najiuliza inawezekana kweli umezaa mtoto, mtoto wako unampenda sana, unalala naye nyumba moja mlango haufungi, unategemea jirani aje kumfungia mlango mtoto wako na bado unaamini mtoto wako yupo salama, ni jambo ambalo haliwezekani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naendelea kuonesha namna gani ambavyo Tume hii ya Haki za Binadamu ni mfu na huwa inafufuka wakati wa bajeti kama hii, tunafahamu, tunatambua kwamba yamekuwepo matukio mbalimbali ya watu kutekwa, watu kuuawa na wengine mpaka leo hawajawahi kuonekana, mfano wa Azory Gwanda, Mfano Benny Saa Nane, alitekwa mpaka leo hajaonekana, hatukuwahi kusikia Tume hii ikisimama kutekeleza wajibu wake wa kukemea, wa kulaani na hata kushtaki angalau taasisi au watu wanaosadikiwa kwamba walishiriki katika uvunjaji wa haki za binadamu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sio tu hilo lakini wapo Watanzania wenzetu ambao walitekwa lakini wakapatikana, yaani mtu anatekwa halafu anarudi, ana uwezo wa kuelezea wapi alikuwepo nani alimkamata, kilikwenda kilirudi, watu hao wakaonekana, mfano Mo Dewji, lakini tunaye mwingine Roma Mkatoliki, walitekwa wakarudi wakapatikana, Tume hii haijawahi kusikika inalaani, haijawahi kusikika angalau inatoa tamko au basi angalau kufuatilia hata kwenda kufungua kesi, kwa sababu ni wajibu wa Tume hii inapobidi kufungua kesi against taasisi au mtu ambaye inasemekana amefanya uvunjifu wa haki za binadamu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sababu nyingine kuonesha kwamba hii ni Tume mfu, hivi karibuni yametokea matukio makubwa katika Mkoa wa Mtwara na Mkoa wa Tanga, Jeshi la Polisi linatuhumiwa kuua Watanzania. Ni kiongozi wa nchi Mheshimiwa Rais Mama yetu Samia Suluhu Hassan ambaye alisimama juu ya mlima akapiga kelele, kwanza akalaani, akakemea na akatoa maelekezo nini kifanyike kwa ajili ya uvunjwaji wa haki za binadamu, lakini Tume hii ambayo leo hii ipo hapa inahitaji tupitishe bajeti iko kimya imekufa…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Katiba na Sheria
MHE. AGNESTA L. KAIZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru kwa kunipa nafasi ili nami kwa uchache niweze kuchangia katika Wizara hii nyeti Wizara ya Katiba na Sheria.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu leo utajikita katika Tume ya Haki za Binadamu, Fungu 55. Katika Ibara ya 130 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, katiba imeweka wazi kabisa majukumu inayopaswa kutekelezwa na Tume hii ya Haki za Binadamu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukisoma majukumu haya kwa umakini na kwa umakini utaona namna ambavyo tume hii imepewa majukumu mazito sana, majukumu nyeti, majukumu ambayo yasipotekelezwa kwa ufanisi wake Taifa hili litajikuta liko katika hatari kubwa sana ya ukiukwaji wa Haki za Binadamu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, chombo hiki kwa maana ya Tume ya Haki za Binadamu pamoja na majukumu mengine tume hii ina wajibu wa kumulika taasisi zote za Kiserikali kuangalia kama misingi ya Haki za Binadamu na Utawala Bora vinasimamiwa, vinatekelezwa kwa ukamilifu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jukumu hili ni kubwa sana na ukiangalia ukubwa wa majukumu ya tume hii utakubaliana na mimi kwamba Bajeti ya Tume hii inapaswa kwenda sambamba na uzito wa majukumu yaliyoainishwa katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa kabla sijaendelea mbele naomba nilipitishe Bunge lako Tukufu katikati ya Bajeti za miaka mitatu mfululizo ya Tume hii ya Tume ya Haki za Binadamu ili kwa pamoja tuangalie kama kweli bajeti hii inaendana sambamba na majukumu mazito ambayo tume hii imekabidhiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2021/2022 tume hii iliomba kuidhinishiwa kiasi cha shilingi milioni 373.6. Nafahamu wewe ulikuwa ni Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Katiba na Sheria, unafahamu vizuri majukumu haya. Katikati ya majukumu haya tume inaomba kuidhinishiwa kiasi cha shilingi milioni 373.6 pekeyake. Hiyo kama haitoshi, fedha hizi kwa 100% ni fedha za kutegemea wahisani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapofika hatua Taifa lianweka rehani haki za Watanzania kwamba sasa wahisani ndiyo waje sasa kulinda haki zetu nchini, tunapotea na tunazidi kupotea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka wa Fedha wa 2022/2023, tume hii iliomba kuidhinishiwa kiasi cha shilingi milioni 115 tu. Kumbuka mwaka uliopita ilikuwa ni shilingi milioni 373 nayo ilikuwa ni ndogo tulipiga kelele. Sasa ikaenda mwaka unaofuata ikasema sasa hatuhitaji hata hiyo mia tatu sabini na kitu. Ikasema tunahitaji shilingi milioni 115 tu ambazo fedha hizi kwenye Wizara zingine hata kwenye baadhi ya mafungu ya Katiba na Sheria ni fedha za viburudisho tu, chai yaani chai na korosho, lakini tume inatuambia inahitaji milioni 115 kutekeleza wajibu wake wa kikatiba wa kulinda haki za Watanzania, this is a joke. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, milioni hii 115 iliyoombwa mpaka Februari mwaka huu haijatoka hata shilingi moja. Ina maana gani hii? Ina maana ndani ya mwaka wa fedha wa 2022/2023 Tume hii ya Haki za Binadamu ilikuwa ofisini kabisa inakula bata. Kwa sababu fedha hizi ni fedha za maendeleo na tume hii ili uweze kutoka na kwenda kutekeleza wajibu wake lazima fedha ya maendeleo iwepo kwa 100%. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kituko kingine sasa mwaka huu wa fedha ambao sasa tuko hapa tunajadili bajeti ya Tume hii ya Haki za Binadamu, tume hii imesema yenyewe haina kazi kabisa ya kufanya. Yaani haiihitaji hata shilingi mia kutimiza wajibu wake na kwa lugha nyingine tume hii inataka kulieleza taifa au inataka kulieleza Bunge lako Tukufu kwamba uvunjwaji wa Haki za Binadamu nchini umeisha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, haujaisha na ndiyo maana Mama yetu Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama Samia Suluhu Hassan amekuwa mstari wa mbele kila anapokutana na watu kila anapokwenda anakemea juu ya uvunjifu wa Haki za Binadamu. Wabunge wengine wamesema lakini hata vyombo vingine vinavyosimamia ambavyo siyo vya Kiserikali ambavyo vinasimamia vinafuatilia mwenendo mzima wa Haki za Binadamu nchini wanasema ukiukwaji wa Haki za Binadamu nchini kwa sasa ni mkubwa kuliko wakati mwingine ule. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesema kwamba fedha hizi kwa 100% ni fedha za wahisani. Utakumbuka kwa sasa taifa au niseme dunia kila nchi sasa hivi inapambana na hali yake kupambana na mapenzi ya jinsia moja kwa maana ya ushoga. Asilimia kubwa ya wahisani ambao wanasaidia nchi mbalimbali ikiwemo Tanzania ni wale ambao wanaamini kwamba mapenzi ya jinsia moja ni Haki namba moja ya Binadamu; which is not true.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukiendelea kutegemea fedha za wahisani matokeo yake ndiyo haya tume inakaa ofisini haina kazi ya kufanya, ni watumishi ambao wana ajira za kudumu, wanalipwa mishahara inayotokana na kodi za Watanzania ambao ndiyo wanyonge hao hao ambao haki zao zimebinywa, zimepokwa na wanalia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo hili halikubaliki na niseme kabisa Waziri atakapokuja ku-wind up hapa atueleze hivi anadhani tume hii inapaswa kuendelea kuwepo? Tume ya kukaa ofisini, tume inayokuja leo inasema tunahitaji mtupitishie bajeti tu ya mshahara na viburudisho, sisi hatuna kazi ya kufanya. Waziri asiponipa majibu yanayojitosheleza, siku ya leo nitakwenda kukamata shilingi yake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sasa niendelee kusema katikati ya changamoto za Tume ya Haki za Binadamu, tume ambayo haifanyi kazi kabisa kwa sababu kwanza haina fedha inahitaji uwe na kiongozi mwenye moyo wa kujali na kulinda Haki za Binadamu kama Mama yetu Mama Samia Suluhu Hassan ambaye aliona kwa jicho la pembeni kwamba tume hii siyo tu imelala, yaani imeshajivua wajibu wake kabisa wa kikatiba ndipo alipoamua baada ya kusikia kelele za Watanzania kutokana na haki zao kupokwa akaamua kuunda Tume Maalum, Tume Maalum ambayo kazi yake ni kuchunguza mwenendo wa Haki za Binadamu nchini. Jukumu ambalo kikatiba wamekabidhiwa tume ya haki za binadamu na kwa lugha nyingine kuwa na tume nyingine hii ambayo Mama yetu Samia Suluhu Hassan ameiona na huenda asingeiweka tungekuwa katika hali ya hatari sana ya ukiukwaji wa haki za binadamu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa lugha nyingine ni kwamba kwa sasa hivi Tume hii ya Haki za Binadamu imeisababishia Serikali kuingia gharama nyingine ya kuunda tume nyingine ya kufanya majukumu yake yale yale wakati tume yenyewe iko ofisini na mshahara unaotokana na kodi za Watanzania wanachukua kama kawaida. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niendelee. Nimekuwa nikijiuliza na niliwahi kumuuliza Mheshimiwa Waziri kwenye kamati, nikasema; Tume ya Haki za Binadamu ina jukumu la kumulika taasisi za Kiserikali ili kuona kama Haki za Kibinadamu zinatendeka na nikasema kama ndiyo hivyo, tumekuwa tukimwona CAG akileta taarifa zake hapa Bungeni za kila mwaka na tumekuwa tukiona vituo vingine visivyo vya kiserikali viantaoa taarifa zake mfano kama hii hapa nikipata muda wa kuielezea nitaielezea ni kwa nini basi tume hii yenye wajibu wa kikatiba isiwe inaleta ripoti yake ya uchunguzi wa mwenendo wa haki za binadamu hapa Bungeni? (Makofi)

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Agnesta.

MHE. AGNESTA L. KAIZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba dakika moja tu.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Agnesta muda wako umekwisha.

MHE. AGNESTA L. KAIZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
MHE. AGNESTA L. KAIZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru kwa kunipa nafasi ili na mimi niweze kuchangia Wizara hii ya Mambo ya Ndani. Kabla sijaenda katika mchango wangu kwa moyo kabisa wa dhati naomba nimpongeze Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan. Pamoja na mambo mengine mazuri sana ambayo anaendelea kuyafanya, Mheshimiwa Rais ameweza kuweka utulivu katika nchi, ameweza kuweka amani na ametengeneza mshikamano. Lakini zaidi sana Mheshimiwa Rais ametufanya Watanzania kuwa wamoja bila kujali itikadi zetu za vyama lakini pia bila kujali itikadi zetu za dini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu wa leo nitakwenda kujikita katika hoja moja inayohusiana na uraia pacha. Mnamo tarehe 15 mwezi wa tano, 2023 nilisimama mbele ya Bunge lako tukufu nikihitaji kupata ufafanuzi kutoka kwa Serikali ni kwa nini inapata kigugumizi kuhusiana na suala zima la kuwapatia wenzetu diaspora haki yao ya msingi kwa maana ya uraia pacha. Majibu ya Mheshimiwa Waziri wa Mambo ya Ndani ndiyo yanayonisababisha hivi leo nisimame kuchangia kuhusiana na suala hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, natambua hoja yangu ya leo itakwenda kugusa Wizara ya Mambo ya Ndani lakini pia itakwenda kugusa Wizara ya Mambo ya Nje. Sasa kwa sababu Wizara ni moja kila Waziri atanisikiliza kinacho muhusu basi atakwenda kukijibia katika eneo lake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesema nitakwenda kuchangia suala zima la uraia pacha. Tunafahamu na tunatambua wazi wazi kwamba wapo watanzania wenzetu ambao tunawaita ma diaspora ambao walizaliwa katika nchi hii ya Tanzania, wamezaliwa katika Mikoa hii ya Tanzania katika vijiji na vitongiji ndani ya Tanzania. Diaspora hawa, hawa Watanzania wenzetu wazazi wao uhalisia wao ni Utanzania ni Watanzania na kwa lugha nyingine Watanzania hawa na wenyewe ni Watanzania kwa kuzaliwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tunatambua kwamba wapo diaspora ambao wamekulia ndani ya nchi hii kwa maana ya kukulia, wamelelewa lakini Watanzania hawa wamepata elimu zao ndani ya Tanzania, na wengine wamesomeshwa na kodi za Watanzania wanyonge wakiwa ndani ya nchi hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunatambua na tunafahamu kwamba hata sisi tulio katika Bunge hili tumeacha mikoa yetu, vijiji vyetu tunakwenda katika miji mingine kama ni Dar es Salaam Mbeya au ni wapi kwa lengo moja la kutafuta maisha kwa sababu Mtanzania yeyote ana haki ya kwenda popote kwa ajili ya kutafuta maisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Watanzania hawa waliondoka ndani ya Tanzania wakiwa wamepitia process zote za kiusalama kwa maana ya uhamiaji. Watanzania hawa walipewa passport na uhamiaji. Na kwa lugha nyingine, watanzania hawa Serikali iliwathibitisha kwamba ni Watanzania safi, ni Watanzania wazalendo, na ikawapa kibali cha kwenda kutafuta ng’ambo ili mwisho wa siku waje kuifaidisha nchi yao au Taifa lao la Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunatambua suala zima la ajira nchini ni changamoto sugu. Kwa hiyo tunapopata Watanzania wenye elimu, wenye uwezo wa kwenda kule kwenye mataifa mengine ili waweze kutafuta tunapaswa kama Taifa kuhakikisha watu hawa tunalinda uraia wao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunatambua kwamba zipo nchi ambazo ili uweze kupata kazi, ili uweze kufanya biashara, ili uweze kufanya lolote ndani ya nchi hiyo huna budi kuwa na uraia wa pale. Wakati naongelea hili naomba tujikumbushe. Nimesema Watanzania hawa walitoka nchini wakiwa ni salama salimini, kwa maana ya vyombo vyote vya usalama vilithibitisha kwamba hawa watu ni safi kabisa. Sasa, walipofika katika mataifa yale, kwa sababu wameingia katika nchi hizo na wanaonekana ni watu safi na wana passport za Tanzania na ni wazalendo wakaamua wawape uraia ili waweze kufanya maisha yao kuwa mazuri zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukubaliane jambo moja; kwamba hakuna sababu yoyote ile ya kisheria inayopaswa kumwondolea Mtanzania uhalisia wake wa kuzaliwa. Nayasema haya kwa sababu gani? Mnamo mwaka 1995 ndani ya Bunge hili ilitungwa sheria kandamizi inayohusiana na uraia…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Mheshimiwa ahsante sana muda wako umeisha.

MHE.AGNESTA L. KAIZA: How can it be?
THE WRITTEN LAWS (MISCELLANEOUS AMENDMENTS) (NO. 4) ACT, 2021
MHE. AGNESTA L. KAIZA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia machache.

Mheshimiwa Spika, naomba niende moja kwa moja katika Sehemu ya Nne ya Muswada huu inayoongelea Bohari ya Madawa, katika Muswada huu bohari wanahitaji au wanataka kufanya production ya madawa pamoja na vifaatiba. Sasa natambua kwamba, siku ya leo…

SPIKA: Uko kipengele gani? Ukurasa wa ngapi?

MHE. AGNESTA L. KAIZA: Mheshimiwa Spika, niko katika Sehemu ya Nne ya Muswada. Naomba niendelee.

SPIKA: Part four.

MHE. AGNESTA L. KAIZA: Mheshimiwa Spika, nimesema kwamba, bohari ya dawa inahitaji kuanza production ya madawa…

SPIKA: Yaani wapi?

MHE. AGNESTA L. KAIZA: Mheshimiwa Spika, Sehemu ya Nne ya Muswada huu.

SPIKA: Yaani kwa hiyo, unajadili zote kuanzia 11 mpaka 21 kwa ujumla wake?

MHE. AGNESTA L. KAIZA: Mheshimiwa Spika, ndiyo.

SPIKA: Kama ni zote haya endelea.

MHE. AGNESTA L. KAIZA: Mheshimiwa Spika, nimesema Bohari ya Madawa inahitaji kufanya production ya madawa plus vifaatiba. Siku ya leo kwanza tuko hapa kwa ajili ya kujadili ili tuweze kupitisha sheria hii, lakini mpaka naongea hapa mbele ya Bunge lako Tukufu MSD tayari kwa tetesi zilizopo kwamba…

SPIKA: Aah, ngoja. Yaani hapa tunatunga sheria, ndio maana jana Wanasheria walijiita wasomi, tofauti iko hapo. Tunapotunga sheria habari ya tetesi, sijui nini, yaani hapa tunaenda moja kwa moja wapi? Panasemaje? Sentensi gani ifutwe? Koma ihame kutoka wapi iende wapi? Isisomeke hivi ila isomeke namna hii, katika hatua hii hatuchangii hoja tena ya ile, hapa tunatunga sheria. Kwa hiyo, tuambie kabisa wapi pakibaki palivyo itakuwa hivi, lakini ukituambia tetesi hapa haiingii.

MHE. AGNESTA L. KAIZA: Mheshimiwa Spika, nimeshaelewa naomba niendelee. Nimesema kwamba, bohari ya madawa inahitaji kufanya production…

SPIKA: Huendelei mpaka uniambie ni wapi? (Kicheko)

MHE. AGNESTA L. KAIZA: Mheshimiwa Spika, Section 12 ya Muswada huu inaongeza neno production kwa maana ya uzalishaji.

SPIKA: Enhee.

MHE. AGNESTA L. KAIZA: Mheshimiwa Spika, sasa nimesema bohari inahitaji itoke kwenye usambazaji, I mean, iwe na usambazaji at the Same time inafanya production. Wote tunatambua na tunafahamu na nilisema wakati tuko kwenye Bunge la Bajeti, MSD ime-fail big time katika suala zima la usambazaji wa madawa, lakini leo hii inahitaji ijiongezee tena kazi nyingine ya kufanya production.

Mheshimiwa Spika, kwa mawazo yangu sioni kama MSD ina capacity ya kufanya production at the Same time ikafanya usambazaji, lakini natambua kwamba, hata nikisema namna gani, nikipinga hii sheria namna gani, sheria hii itakwenda kupita. Sasa niseme jambo moja…

SPIKA: Kwa sababu hujaelewa tu, lakini ukieleweshwa vizuri utaelewa jinsi ambavyo MSD kwa kwenda kuzalisha baadhi ya madawa ambayo tunayaagiza nje na mahali pengine kwa bei kubwa itaokoa billions of shillings. Endelea tu. (Makofi)

MHE. AGNESTA L. KAIZA: Mheshimiwa Spika, nakuelewa na kwa upande mwingine uko sahihi kwamba, MSD kama ingekuwa na capacity kwa sababu, tuna sehemu ya kuwaangalia kwanza walikuwa wanafanya usambazaji, wame-fail. Wewe ni shahidi na uliwahi kusema katika Bunge hili kwamba mdawa ni shida…

SPIKA: Hawatazalisha kila dawa. Kuna baadhi ya dawa ambazo wana capacity ndio wataenda kuzalisha.

MHE. AGNESTA L. KAIZA: Mheshimiwa Spika, sasa naomba niseme hivi kwa kuwa, inaonekana kwamba, MSD wanaweza kufanya production at the Same time wakafanya…

MHE. JOSEPH A. TADAYO: Mheshimiwa Spika, Taarifa.

Mhe. HALIMA J. MDEE: Mheshimiwa Spika, Taarifa.

SPIKA: Iko Msekwa au iko wapi?

MHE. HALIMA J. MDEE: Mheshimiwa Spika, Taarifa iko hapa. Niko hapa.

MHE. JOSEPH A. TADAYO: Mheshimiwa Spika, Taarifa, Msekwa. Niko hapa Msekwa.

SPIKA: Ndio mwenye Taarifa? Msekwa, endelea Taarifa, hapa ndani subiri Ukumbi wa Msekwa kwanza.

T A A R I F A

MHE. JOSEPH A. TADAYO: Mheshimiwa Spika, naomba tu nimpe taarifa mzungumzaji kwamba, MSD isingeweza kuanza production kabla hatujaitungia sheria. Tunaitungia sheria ili iweze kuanza kufanya hiyo kazi kabla ya hapo ingafanya production bila sheria ingekuwa inafanya kitu cha ajabu, ingewekwa hata ndani. Ahsante.

SPIKA: Ahsante Mheshimiwa Tadayo. Kwamba tusiwahukumu kabla hatujawapa uwezo wa kufanya. Mheshimiwa Agnesta taarifa hiyo ni kwako, hapana siyo kwenu ninyi wawili. Taarifa hiyo inakwenda kwa Mheshimiwa Agnesta Lambert.

MHE. AGNESTA L. KAIZA: Mheshimiwa Spika, naomba niseme kwamba, Taarifa hii siipokei.

MHE. HALIMA J. MDEE: Mheshimiwa Spika, Taarifa.

SPIKA: Bahati mbaya muda umeisha.