Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Ahmed Yahya Abdulwakil (3 total)

MHE. AHMED YAHYA ABULWAKIL: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Pamoja na majibu mazuri na yenye tija, naipongeza Serikali kwamba hivi karibuni itapata kituo kile na kuondokana na gharika ya majambazi waliovamia miaka ya nyuma. Kwa sababu hiyo, nashawishika kumwuliza maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa Kituo cha Polisi cha Kwahani Eneo la Ng’ambo Jimbo la Kwahani ni Kituo cha Polisi cha muda mrefu tangu ukoloni; na kwa sasa hakikidhi mahitaji kuhudumia wananchi wakati huu: Je, Serikali ina mpango gani wa kukitanua ili maofisa wetu waweze kufanya kazi kwa utulivu na ufasaha? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili ni kwamba, hivi karibuni Mheshimiwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi amezindua soko jipya la kisasa eneo la Kibanda Maiti au tunaweza kusema Kibanda cha Demokrasia; linahudumia zaidi ya watu 10,000 usiku na mchana: Je, Wizara yako ina mpango gani kulinda usalama wa raia na mali zao? (Makofi)
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Spika, kwanza uniruhusu nimpongeze Mheshimiwa Mbunge, kwa sababu Mheshimiwa Mbunge anafanya kazi kubwa na wananchi wake hawakukosea kumchagua. Ninafahamu Mheshimiwa Mbunge amekuwa mstari wa mbele kwenye kuchangia maendeleo iwe kwenye elimu au vituo hivi vya Polisi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika kujibu swali lake, ninafahamu pia kwamba hii miji inapanuka na ongezeko la watu linakuwa kubwa. Ongezeko hili linaendana na changamoto mbalimbali zikiwemo za ulinzi. Kwa hiyo, niendelee tu kumsihi Mheshimiwa Mbunge na Waheshimiwa Wabunge kwa ujumla tuendelee kuhamasisha wananchi kwamba jukumu la ulinzi ni letu wote ili tuweze kushirikiana kwanza kuhakikisha kwamba tunafanya maboresho makubwa katika maeneo yetu.

Mheshimiwa Spika, kazi kubwa ya Serikali imefanyika; yako maeneo mbalimbali ambayo ujenzi umeendelea kukamilishwa na kama nilivyosema katika jibu la msingi ni kwamba Mfuko huu wa Tuzo na Tozo umefanya kazi kubwa. Katika mwaka 2020/2021 peke yake zaidi ya nyumba 431 zimekamilishwa ili kuhakikisha kwamba tunaweka mazingira mazuri ya askari wetu kufanya kazi. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge tuendelee kuhamasisha wananchi na Serikali kupitia mfuko huu tutaendelea kufanya maboresho makubwa.

Mheshimiwa Spika, mkakati tunaoufanya katika eneo hili la Kibanda Mauti, ni kweli kwamba kuna doria zinafanyika, wale wanaojihusisha na uhalifu wanaendelea kukamatwa na kufikishwa kwenye taratibu zetu za kisheria, lakini pia tunaendelea kutoa elimu kwa wananchi, tunaendelea kuwashirikisha wananchi ili waweze kusaidia katika ulinzi na tunaendelea pia kushirikiana na vyombo vingine. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nitoe maelekezo kwa Jeshi la Polisi kule Zanzibar, washirikiane na Uongozi wa Soko katika eneo Mheshimiwa Mbunge amelitaja ili tupate eneo ambalo sasa tutaanza mkakati wa kujenga kituo katika eneo hili kwa sababu changamoto zimeongezeka na idadi kubwa ya watu katika maeneo haya na kuwepo kwa soko kunahitaji ulinzi madhubuti. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. AHMED YAHYA ABDULWAKIL: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kuniona. Naomba nimuulize swali Mheshimiwa Naibu Waziri; kwa kuwa Jimbo la Chukwani wananchi wamejenga kituo kipya cha ghorofa moja na mpaka sasa kimefikia asilimia 85, bado asilimia 15 kimalizike.

Naomba Serikali itoe kauli lini kituo kile kitamalizika na kuanza kutumika na hasa ukitia maanani kwamba lilitokea wimbi kubwa la mauaji katika eneo lile? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Yahya, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, napokea ombi au swali lenye mwelekeo wa ombi la Mheshimiwa Yahya, kwamba katika vitu ambavyo tutaviangalia kule ambako wananchi wamejitokeza wakachangia nguvu zao na rasilimali zao nyingine kupitia Mfuko wetu wa tozo tunaweza kuwasaidia ili kukamilisha vituo hivyo. Kwa hiyo katika tathmini itakayofanyika kwa Mheshimiwa Mbunge pia tutapazingatia. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. YAHYA ABDULWAKIL AHMED: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Pamoja na majibu mazuri na ya kutia moyo katika ununuzi wa meli hii, naipongeza Serikali kidogo, nina swali moja la nyongeza.

Kwa vile ununuzi wa meli hizi utashirikisha Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, watafaidika wa meli mbili na mbili itafaidika Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambayo Tanzania Bara, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeshirikishwa katika hatua hizi za awali za manunuzi haya? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, ushirikishwaji wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar upo wa kiwango kikubwa kabisa na jambo hili linaratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu ikishirikiana na Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais upande wa Zanzibar na Wizara zetu pia vilevile ya Mifugo na Uvuvi na Wizara ya Uchumi wa Bluu lakini na Mashirika yetu vilevile ya TAFCO na ZAFCO yote yanafanya kazi hii kwa pamoja. Kwa hiyo, nimtoe wasiwasi Mheshimiwa Abdulwakil kwamba Serikali inashirikishwa ipasavyo. Ahsante.