Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Ahmed Yahya Abdulwakil (10 total)

Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022
MHE. AHMED YAHYA ABDULWAKIL: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Natumia fursa hii kukushukuru wewe binafsi na kumshukuru Mwenyezi Mungu ambaye amenijalia mara yangu ya kwanza kusimama katika Bunge lako hili tukufu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapohapo nawashukuru sana wananchi wa Jimbo la Kwahani kule Zanzibar ambao kwa imani moja wamenileta hapa niwe mwakilishi wao. Walikuwa na simanzi kwa vile wanaona kama wameondokewa na Mbunge mwaminifu, mtiifu na mwenye bidii, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi. Nawahakikishia kwa nafsi yangu kwamba mimi naweza na nitawapa utumishi uliotukuka na kufuta machozi madogo madogo ambayo walikuwa wanayatoa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ni Mjumbe wa Kamati ya Miundombinu na Mawasiliano na kwa kiasi fulani nitajikita zaidi katika kuuchangia Mpango huu wa Miaka Mitano. Nchi yetu kama hii kwa kitendo cha Rais wetu mpendwa kuanzisha reli iendayo kasi kwa kutumia fedha zetu za ndani kwa kipindi hiki ni suala la kumpongeza na kumtakia mafanikio mema katika safari hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nilibahatika kidogo kusafiri (mtundu wa kusafiri), ninakona reli kama hii ya Shirika la Reli la Marekani linaitwa Acela inayochukua abiria na mizigo kutoka Washington DC mpaka New York kwa mwendo wa saa nne na nilipanda shirika hilo. Leo nchi kama yetu ya Tanzania hili ni jambo la mfano, Rais wetu mpendwa ameidhinisha zaidi ya shilingi trilioni saba na kuendelea na reli inaendelea. Kwa hiyo, hili ni jambo la kuigwa na huyu ni Rais wa kuombewa dua kila siku kwa madhehebu yote ili aweze kuishi na aweze kutufikisha salama. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile napenda kuchangia kuhusu Shirika la Ndege la ATC. Shirika la Ndege la ATC kila mmoja leo anaona mafanikio yake na limeweza kwa mara ya kwanza katika utawala wa Dkt. John Pombe Magufuli kutoa gawio (dividend) kwa Serikali. Kwa hiyo, hili ni jambo la mfano; amefufua shirika hili na leo lina ndege zaidi ya tisa na nyingine za mizigo ziko mbioni zinakuja. Kwa hiyo, hili ni jambo la mfano katika nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi karibuni ilivyoingia COVID tumeona deterioration ya bidhaa kuja kwetu Tanzania. Shirika la Ndege la Ethiopia limetumia nafasi ya kuchukua mizigo ya wafanyabiashara kuleta Tanzania. Ni jambo la faraja kusikia kwamba ndege ya mizigo inakuja na iko njiani. Kwa hiyo, uchumi wetu utazidi kuhuika kwa kuwa sasa hivi tunatumia ndege yetu wenyewe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini si hivyo tu, nadokeza kwamba hivi karibuni shirika hili baada ya hii COVID kuondoka, lina mpango wa kuazisha safari za kuelekea Gatwick pamoja na London, Heathrow. Kwa hiyo, Watanzania hapa watakuwa wanapanda direct flight kutoka Julius Kambarage Nyerere Airport mpaka Gatwick. Kwa hiyo, hili ni jambo la mfano kwa Shirika la Ndege na hizi zote ni juhudi za Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli; hongera sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho katika uchangiaji wangu, natoa ushauri kwamba uvuvi wa Bahari Kuu ambao unachochea uchumi wetu uangalie ofisi za Zanzibar. Hapa katikati utoaji wa leseni ulisababisha ofisi ya Zanzibar kidogo kutikisika. Wavuvi wenye meli walikuwa wengi lakini alibakia mvuvi mmoja tu ndiye aliyepewa leseni. Kwa hiyo, zipo dalili za kuwasaili ikiwa hali imetengemaa na wakati wa utoaji wa leseni za meli za uvuvi wakaangalie kwa makini sana kutoa leseni kwa wakati na fair ili kusudi ile shake ya ofisi isije ikatokea tena.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa jumla mimi naunga mkono mpango huu kwa asilimia 100 ili mambo yaende.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. (Makofi)
Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2021/2022 – 2025/2026
MHE. AHMED YAHYA ABDULWAKIL: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa fursa hii ya kuchangia Mpango huu ambao ni dira kubwa, mimi naita ni jahazi litakalotuvusha kama kuna upepo au hakuna upepo kama alivyosema Rais wetu mpendwa, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan. Wabunge wengi walipokuwa wanachangia walizungumzia habari za markets yaani masoko, kwamba uzalishaji ni mkubwa lakini tuna upungufu wa masoko katika kuuza bidhaa zetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, nashauri ndugu yangu Mheshimiwa Mwigulu pamoja na Naibu kwamba duniani au Serikali ya Marekani imetoa fursa kwa nchi za kiafrika ambao Mpango huu unaoitwa AGOA (African Growth and Opportunity Act)nadhani katika utawala wa Bush ameamua Afrika iweze kuuza bidhaa zaidi bila ushuru wa aina yoyote. Sasa ni vema zaidi tukajikita na masoko ya nje, nchi yetu ina utajiri wa bidhaa mbalimbali tunazalisha, kuna maparachichi, kuna aina ya bidhaa mbalimbali.

Mheshimiwa Naibu Spika, nilikuwa nikifuatilia kwa karibu sana, kila Mbunge anayesimama anasema kwamba soko hatuna bidhaa zinaharibika, kwa hiyo naishauri Serikali kwamba soko la AGOA nalo likapiga hodi Marekani. Hili ni soko zuri na halina ushuru maadamu tu ile bidhaa iliyozalishwa iwe brand yake made in Tanzania na iko katika hali ya ubora. Tusiwe waoga, wakati umefika tutumie fursa za ulimwengu, tutumie madirisha ya ulimwengu kusudi na sisi tuweze kuuza bidhaa zetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hayo machache, naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja, ipite. Ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira
MHE. AHMED YAHYA ABDULWAKIL: Mheshimiwa Spika, ahsante sana, asubuhi ya leo baada ya kumshukuru Mwenyezi Mungu ambaye tupo katika mfungo, mimi naheshimu sana heshima hii ya kupewa kuwa mchangiaji wa mwanzo katika wizara hii ambayo ni ya uhai wa maisha yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kikawaida sina uchangiaji mkubwa sana maisha yote na nitatumia haitozidi dakika tatu, nne mpaka tano. Kwa hiyo nitasevu muda kusudu ajaye apate nafasi ya kuongea zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nitaongea upande wa Mazingira (Environment). Katika hotuba ya Mheshimiwa Rais, hapa alitumia dakika tatu, jinsi anavyojali na kuthamini mazingira. Kwa njia hii alipitia kiatu hiki kabla ya leo kufikia kuwa Rais wa Tanzania, kwa hiyo tumpongeze sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa upande wa ufadhili hapa kidogo ndiyo nataka Mheshimiwa Waziri atakapokuja ku-wind up hotuba yake, dunia imekuwa sana katika upande wa mazingira na mikutano mbalimbali inafanyika ulimwenguni kwa sababu ya kuhifadhi mazingira. Kwa hiyo, kwa upande wa Zanzibar kuna PECCA ukanda wa PECCA ni ukanda mali sana huu, ambao kwa namna moja au nyingine umeingia katika ramani ya dunia pamoja na kisiwa cha Misali. Misali kuna kisiwa, kuna bahari na kuna bustani chini ya ulimwengu ambayo si nchi nyingine ni natural. Sasa lazima yalindwe kimazingira kwa hiyo tulikuwa na wasiwasi kama nchi kwamba vipi hali ya ufadhili wa kimazingira katika hizo sehemu ambazo kubwa zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ukiangalia katika uchumi, Tanzania tunakusudia kununua meli nane (8) za uvuvi; meli nne (4) Tanzania Bara na nne(4) Tanzania Visiwani.

Katika uvuvi, kuna siri kubwa sana ya kupata harvest yaani mavuno kwa kutumia matumbawe. Haya kama hayakuhifadhiwa kimazingira, mara nyingi samaki wanahama na kutakuwa hakuna pia samaki wenyewe tunaokusudia, meli itakuja na hatutavua. Sasa napenda kujua wakati Mheshimiwa Waziri akija ku-wind up, atueleze hali ya kimazingira ya matumbawe, nchi zote baina ya Zanzibar na Tanzania Bara ikoje kusudi tuweze kufaidi neema hii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nyuma kuna mfuko ukiitwa, Mfuko wa Kusaidia Nchi Masikini katika Kuokoa Mazingira (LDCF). Sasa wakubwa duniani wana hiari yao kutusaidia au kutosaidia hali ikoje katika kupambana na hali hii na ufadhili, ili kusudi tuweze kuishi katika ustahi mazingira mazuri kwa nchi yetu? Ahsante sana. (Makofi)

SPIKA: Ahsante sana Ahmed, lakini jina lako huwa linanipa tabu kidogo, unauhusiano gani na Mzee Abdulwakil?

MHE. AHMED YAHYA ABDULWAKIL: Mheshimiwa Spika, jina langu kamilifu naitwa Ahmed Yahya Abdulwakil Mbunge wa Kohani. Tunao uhusiano wa kijomba wa huko nyumbani. (Makofi/Kicheko)

SPIKA: Ahsante sana Ahmed.

MHE. AHMED YAHYA ABDULWAKIL: Sikutaka kuweka sawa ehe! Kusudi watu wakatishika, hamna! (Kicheko)

SPIKA: Kiti changu kimekuwa kikipata tabu kidogo. Nashukuru kwa ufafanuzi huo, Ndugu yangu Ahmed.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi
MHE. AHMED YAHYA ABDUWAKIL: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii ili kuchangia bajeti hii ya Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi, ambayo ni bajeti mkombozi na Wizara ambayo inaweka ustawi mzuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikienda mbele zaidi napenda kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan na namna anavyotupendezesha na kutufurahisha katika uongozi wake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mara ya mwanzo nilivyosimama kuongea kwenye kiriri hiki nilisema maajabu ya Reli ya SGR, leo Tanzania tunakuwa kama Marekani. Tunakuwa na reli ya kisasa ambayo ni sawasawa na Shirika la Reli la Marekani linaloitwa FELA na kama nasema uongo Balozi Mulamula analijua vizuri shirika hili. Kwa hiyo na sisi Tanzania tunaingia katika historia mpya kwa hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikiingia kwenye nukta ya pili tuseme tu kwamba nchi inasonga mbele, ndugu yangu Profesa Mbarawa na timu yake na Engineers wake wanafanya kazi usiku na mchana. Nimewahi kushuhudia daraja la Wami, kazi imemalizika kabla ya muda ambayo si rahisi kwasisi tunaoshughulika na shughuli za ujenzi, lakini Daraja la Wami limeokoa vifo kabla muda na limefunguliwa kabla ya muda. Hili niseme tu ni kwa sababu ya kuwa na watendaji wazuri na aliyevaa kiatu cha TANROADS Engineer Mativila lazima apongezwe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikienda mbali zaidi kwa shukurani kwamba kwa sisi watu wa Kusini Zanzibar tunaitwa kwamba Profesa na timu yake “hawana lala” kucha kutwa “wa kazini” maana yake wao kutwa muda wote wako kazini. Kwa hiyo nampa hongera sana sana Profesa, anafanya kazi nzuri na timu yake yote, Engineers wote hapo Mwakibete na wenzio. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mara nyingi humu katika Bunge imezungumzwa Air Tanzania ambayo inafanya kazi kubwa. Pamoja na matatizo madogo madogo yaliyokuwepo lakini Air Tanzania wanafanya kazi kubwa sana. Mashirika ya Ndege kama Ethiopia, Alitalia American Air na mengineyo hayakuanza hivyo, walianza kwa kusuasua mpaka yakatengemaa. Yapo matatizo madogo madogo ya kiutendaji na CEO Matindi anachukua juhudi kubwa sana kuweka sawa. Kwa hiyo tuwapongeze, tungepata wapi kama si juhudi za Mama? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Timu ya Yanga Africans inakwenda Algeria kwa ndege yetu, tungepata wapi? Kwa jeuri tunaipeleka na kuirejesha, kwa hiyo kwa sifa hizo, naunga mkono bajeti hii kwa asilimia mia moja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi. (Makofi)
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022
MHE. AHMED YAHYA ABDULWAKIL: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii asubuhi ili nami niweze kuchangia bajeti hii ya Serikali, ambayo mimi ninaiita bajeti mkombozi na ufunguzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kumshukuru Mwenyezi Mungu, kwanza inafurahisha mno, kwamba bajeti hii ina malengo mazuri ya kututoa hapa tulipo na kwenda katika hatua nyingine, hili ni jambo la kupongezwa. Vijana wetu, Mawaziri wote, Naibu Waziri pamoja na timu yote imefanya kazi kubwa sana kuandaa bajeti hii ambayo leo mmetuletea mbele yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kukuza uchumi lazima kuwe na vichocheo vya uchumi ambavyo vitaufanya uchumi ule ustawi na uendelee. Dalili zinaonesha kwamba katika kipindi kifupi tu cha mama yetu Pato la Taifa limekuwa na mama yetu ameweza kujiamini kwa kutoa fedha nyingi katika miradi mikubwa ya uchumi, ambayo italeta ufufuaji wa uchumi mzuri zaidi katika siku za usoni, hongera sana, hongera sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi na-declare interest kama ni mfanyabiashara na muwekezaji, na kwa bahati niliwahi kuwa Mjumbe wa Baraza la Wawakilishi kwenye sekta ya biashara, viwanda na kilimo. Ni ukweli usio wazi, na niko tayari hata na Naibu Waziri kwenda kuangalia ripoti ya fedha ya urari wa biashara baina ya Bara na Zanzibar kuwa ni mbovu mno! mbovu mno! Na niko tayari wowote kwenda, kwamba asilimia 75 ya biashara iliyokuwa ikifanywa baina ya Bara, imepungua mpaka asilimia 15 na imeweza kuathiri bajeti ya SMZ kwa kipindi cha miaka mitatu mfululizo, hiyo iko wazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, na ndugu yangu tunapendana sana, Mheshimiwa Naibu Waziri tunaweza tukaenda tukaangalia namna hali ilivyoathiri biashara. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, na kwa nini basi, Tanzania Bara wana-influence kubwa ya kuuza bidhaa kwetu Zanzibar; kwa mfano mbao, nondo, maji, cement na biashara nyingine zozote; hiyo ni free na hiyo ni free trade markets. Nchi ndogo kama yetu, ya Zanzibar yenye population ya watu 1,500,000 tu, sisi ukitaka tusitake tunategemea soko la Tanzania Bara. Na ukiangalia kwa upevu niliokuwa nao kwamba, hata miaka 100 nyuma, Zanzibar ilikuwa inategemea biashara (trade).

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hii bajeti iliyokuja ya kuondoa ondoa vikwazo vidogo vidogo tumeifurahia na tunaipongeza. Lakini la msingi, Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri naomba na hapa kidogo unitolee macho. Umefika wakati kwa makusudi na kwa malengo mazuri, iundwe tume ya fedha ya pamoja, jambo ambalo mama nalo amelisisitiza hilo. Hii yote itaondoa minong’ono midogo midogo baina ya Zanzibar na Tanzania Bara, na unalijua. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, basi mimi kwa jumla naunga mkono. Lakini la mwisho ni kwamba, katika ufanyaji wa biashara, nchi yoyote duniani haiogopi wafanyabiashara. Kwa mfano kampuni kubwa za Marekani kama vile Amazon, Boeing na nyingine zote, hizi zote zipo karibu na nchi au Serikali husika. Muhimu tu zile kodi zinalipwa na wale watu wathaminiwe, pasiwe na woga baina ya wafanyabiashara na Serikali, hawa ndio wenye engine ya uchumi wa nchi husika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hayo machache mimi naunga mkono hoja kwa asilimia 100. Mama amejizatiti na yuko kazini, na yote haya yatafanikiwa ikiwa tutakuwa tuna umoja na umoja wetu inshallah, Mwenyezi Mungu ataujaalia udumu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
MHE. AHMED YAHYA ABDULWAKIL: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Awali ya yote nakushukuru kwa udhati wa nafsi yangu kunipa nafasi hii adhimu ambayo nilikuwa naamini nitaipata. Baada ya kumshukuru Mwenyezi Mungu, napenda sana kumshukuru Rais wetu, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa namna usukani alivyoukamata barabara kutuongoza katika nchi yetu. Nchi imetulia, nchi ina amani wawekezaji wanakuja, hakuna longolongo ndogondogo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya hapo kwamba Zanzibar nimewahi kusikia hotuba moja ya Mheshimiwa Dkt. Samia kwamba ni eneo maalum tengefu kwa kuwa limezungukwa na square mita 2,800 za mraba na zote hizi square mita zimezungukwa na bahari yote. Kwa hiyo, nikawahi kumsikia kwamba linahitaji kupata zana za kisasa ili liwe na ulinzi wa kisasa kuepukana na maharamia ambao wanaidowea nchi yetu. Kwa hiyo, naamini timu nzuri inayoongozwa na Ndugu yangu Mheshimiwa Masauni na Mheshimiwa Jumanne wanaweza wakakidhi haja ya nchi yetu kupata ulinzi imara ndani ya bahari.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hali ni mbaya mno, walishawahi kunyemelea nyemela eneo la Kaskazini Pemba lakini Majeshi yetu ya Ulinzi yalikuwa imara na yakawafukuza wale maharamia. Kwa hiyo, ipo haja kupata mgao maalum wa zana za baharani pamoja na zana za nchi kavu ili shughuli za Jeshi la Polisi ziweze kuimarika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tangu niingie katika Bunge hili nilizungumza kuhusu Kituo cha Polisi cha Chukwani ambacho ni cha ghorofa, nikapata matumaini katika bajeti iliyopita kwamba kitajengwa au kitamaliziwa maana yake wananchi wamechangia milioni 60 wenyewe kukijenga. Nikapata matumaini kwamba katika bajeti tunayoendelea nayo, ziko zimetengwa milioni 60. Nimekwenda panda shuka Makao Makuu ya Jeshi la Polisi nimeonana na Kamishna wa Polisi, sijapata matumaini ya aina yoyote kiasi kwamba nimeanza kuvunjika moyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo natumia nafasi hii kuwaambia kwamba mimi sina nia hata siku moja ya kuzuia shilingi ya mtu yeyote, hata mia! Naomba nipate maelezo kamili ya kituo kile juu ya wananchi waliochangia milioni 60 nguvu zao na baadhi ya wengine ni wageni baada ya matokeo makubwa ya uvunjifu wa amani. Wameshakufa watu watatu na akitaka nani na nani nitamuambia, Wazungu wawili wamekufa mwaka jana, kwenye uchaguzi kuna Mzungu alivamiwa na mmoja Mwanasheria ambae alikuwa anashughulikia uchaguzi, mwanae Mwanasheria Hamili kadhalika alivyamiwa. Kwa hiyo, hali ni mbaya mno. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya hayo machache naomba sana nipate jibu rasmi ya kuwa kile kituo ni lini kitamalizika lakini yote kwa yote naunga hoja mkono asilimia 100. Ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
MHE. AHMED YAHYA ABDULWAKIL: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii ya kuweza kuchangia bajeti hii ya Wizara ambayo inatupeleka katika uso wa Dunia. Zaidi namshukuru Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Chief Hangaya, kwa namna alivyopata nafasi hii alikwenda moja kwa moja kuifungua nchi kwenye diplomasia ya uchumi ambapo sasa nchi inasonga mbele tunaelekea kwenye kipato cha kati na huenda tukaingia kwenye kipato cha kwanza. Inshaallah Mwenyezi Mungu atujalie.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa kitu Balozi ni kitu chenye hadhi kubwa sana, nchi yetu ina hadhi kubwa sana nchi za nje tofauti na tunavyoifikiria. Jina Tanzania ni Tanzania kweli. Nchi yenye ufahari, utulivu, mito, mimea na nchi yenye mali kila siku nchi hii inavumbua mali mbalimbali. Sasa, lazima tujitafaharishe na tujifaharishe zaidi kwamba hii ni nchi tamu na nchi ya kuishi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumebatika kutemebea nchi mbalimbali kama Amerika, Bara la Ulaya na nchi mbalimbali, nilipata bahati ya kutembea Marekani katika Mji wa Seattle kwenye ujumbe na Makamu wa Rais wa Zanzibar. Jinsi ya utamu wa nchi hii kuna Mmarekani alitusimamisha aliuliza naomba msimame nikuulizeni maswali, ninyi mnatoka wapi, tukamwambia sisi tunatoka Tanzania akasema na mimi ni Mtanzania na kwa Kichaga akasema yeye alikuwa na Kihamba kwamba ana kijishamba chake cha Tanzania. Kwa hiyo, akasema ninyi mna nchi nzuri, utulivu wenu umefanya nchi ifunguke na nchi yenu imetulia na ina amani. Kwa hiyo, hongereni sana kuja hapa America. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, haya hayakuja tu lazma niwampongeze Mheshimiwa Waziri na timu yako Mheshimiwa Dkt. Mbarouk kwa kuisimamia vizuri, mnafanya kazi nzuri, hamlali na hamchoki, Mwenyezi Mungu akupeni afya na muihudumie zaidi nchi hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa katika diplomasia ya kiuchumi kuna mambo na fursa mbalimbali zinapatikana hasa za uchumi. Mashirika yafuatayo yameweka mkono wazi kwetu Tanzania, kama vile World Bank, IFAD, FAO, UNDP, African Bank, BADEA, Kuwait Fund na mashirika mengine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa unapochukuliwa Balozi iwe unapata ripoti ya kila siku kwamba neno gani au jambo gani Tanzania lina manufaa nchi iko wazi. Kwa utundu wangu kuna siku nilikaa mgongoni kidogo World Bank kwenye corridor zile mbili, nikapata na bahati nikakaa kidogo nikachukuliwa nikaona kwamba World Bank corridor mashirika makubwa ya dunia yamekaa yanagojea tuende tukawaombe au tukakape pesa zetu. Kwa mfano, Zanzibar mradi wa PADEP, mradi wa MANCEP hii ni juhudi binafsi za Makatibu Wakuu kwa wakati ule na viongozi, mradi ule leo unawafaa Wazanzibari.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, mimi kwa hapo tu naomba Balozi zetu zichangamke fursa zipo, zituletee maendeleo ili nchi iwe na neema kwa hii fursa ya uchumi wa Bluu. (Makofi)

MHE. ENG. MWANAISHA N. ULENGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Engineer Mwanaisha.

TAARIFA

MHE. ENG. MWANAISHA N. ULENGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naomba kumpa taarifa mzungumzaji kwamba, anayoyazungumza kuhusiana na Balozi zetu kuiendea kwa kasi dhana nzima ya diplomasia ya uchumi, Balozi zinapaswa kukumbuka pia zitafute uwekezekano wa nchi zetu kuanzisha benki katika zile nchi ambazo tunafanya nazo biashara kwa karibu. Kwa sababu tunaingiza intermediate currency ambayo inampotezea Mtanzania fedha nyingi anapokwenda kununua mizigo kama China na nchi za namna hiyo, ahsante sana.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Yahya, unaipokea taarifa hiyo?

MHE. AHMED YAHYA ABDULWAKIL: Mheshimiwa Mwenyekiti, naipokea taarifa ya Mheshimiwa Engineer Ulenge kwa mikono yote miwili. Basi mimi taarifa yangu ni hiyo Balozi zichangamke fursa zipo nyingi, nchi iendelee mbele ili lengo la Rais wetu litimie la diplomasia ya uchumi, ahsante sana kwa kunipa nafasi. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
MHE. AHMED ABDUL WAKIL: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya mtu wa kwanza kuchangia kwenye Wizara hii muhimu sana ambayo inatuunganisha na dunia ya kisasa. (Makofi)

Awali ya yote napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuamka salama na kwa utulivu mkubwa katika Bunge letu na hapo hapo nikimshukuru Rais wa Tanzania Mama yetu Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa na ya gear kubwa aliyoanza kwenye Wizara hii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nawapongeza sana Mheshimiwa Waziri Balozi Libarata pamoja na mkongwe Balozi Mbarouk kwa kazi kubwa ya kumsaidia Rais katika diplomasia ya uchumi. Timu yako ya Wizara inafanyakazi kubwa sana kwenda na kasi ya mama katika kuweka diplomasia ya uchumi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo kubwa ambalo nalipongeza kwamba dunia si kijiji au dunia ni Kijiji, mama amekifanya kijiji kiwe chini ya mikono yetu hivi sasa na hakuja na diplomasia ya kuzungumza tu, lakini amekuja na diplomasia ya uchumi ambayo uchumi ni kila kitu katika dunia. Kwa hiyo, uteuzi wa balozi alioufanya karibu nchi 45 na umekiri kwamba hivi karibuni amefungua Balozi mpya ya Indonesia imeleta faraja kubwa sana katika nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Balozi hizi tunaziona zinavyofanyakazi katika mitandao mbalimbali kama Italy, USA, China, Korea na Balozi nyingine nyinginezo zinakwenda moja kwa moja katika kutekeleza diplomasia ya uchumi.

Mimi nitazungumzia uchumi tu, kwa hiyo ipo haja na hoja kwamba Balozi hizi Mheshimiwa Waziri zije na mpango kazi ambao tutahakikisha sasa kwa mfano nchi ya Turkey ni mzalishaji wa chuma, mzalishaji wa bati, vifaa vya uvuvi na vifaa vya marine. Kwa hiyo, tujikite kutafuta fursa zile pale kwa nchi yetu kusudi tuweze kufaidika.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukija na balozi nyingine kadhalika wakija na mpango kazi madhubuti tutakuwa tunajua focus gani tunaweza tukapata maendeleo na kufaidika katika nchi zetu. Kwa jumla mimi sina mengi sana ya kuzungumza nakushukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho kwamba ipo haja na hoja Zanzibar tusiishie ukarabati wa Wizara, ipo haja sasa hivi kwa miaka hii karibu 60 ya Uhuru lijengwe jengo la kisasa, wageni wakija tuachane na vichochoro vidogo vidogo viliopo ili kusudi Zanzibar nayo kuwe kuna jengo walau lenye hadhi ya kibalozi, (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hayo machache ahsante sana na naunga hoja mia dhul mia ahsante sana. (Makofi)
Muswada wa Sheria ya Uwekezaji Tanzania wa Mwaka 2022
MHE. AHMED YAHYA ABDULWAKIL: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii jioni ya leo na mimi nikiwa ni miongoni mwa wachangiaji wa sheria hii.

Kwanza niseme tu mimi ni miongoni mwa Wajumbe wa Kamati ambao tulijadili kwa kina huu Muswada wa Ulinzi wa Taarifa Binafsi. Mimi nasema hatujachelewa, tumekuja muda mzuri na muda muafaka kwa ajili ya kujadili na kupitisha sheria hii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hakika sheria hii tulipata wadau wengi kwa mara ya kwanza, walifurika kwenye chumba chetu na kwa muda wote kulikuwa hakuna mizozo ya kisheria na kanuni na miongozo yao, walitukubalia na sisi tukawakubalia, lakini katika kujadili suala hili kuna neno lilijitokeza, kuongezwa neno faragha ili kutia nyama kwenye sheria hii na ndio maana wajumbe wengi ukiona waliosimama hapa kitu faragha imo, ingawa muswada ndani yake humo ndani kuna neno linaitwa faragha.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, mimi nakubaliana na neno faragha na liangaliwe vizuri kwenye kamusi ya Kiswahili ya Oxford, lina maana yake. Kamusi ya Kiswahili ya Oxford neno faragha lina maana yake, sitaki kuendelea sana, lakini nasema kwamba sheria hii ikipitishwa itajenge utu wetu, heshima yetu na faragha yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii ndogo, ahsante. (Makofi)
Muswada wa Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi wa Mwaka 2022
MHE. AHMED YAHYA ABDULWAKIL: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii jioni ya leo na mimi nikiwa ni miongoni mwa wachangiaji wa sheria hii.

Kwanza niseme tu mimi ni miongoni mwa Wajumbe wa Kamati ambao tulijadili kwa kina huu Muswada wa Ulinzi wa Taarifa Binafsi. Mimi nasema hatujachelewa, tumekuja muda mzuri na muda muafaka kwa ajili ya kujadili na kupitisha sheria hii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hakika sheria hii tulipata wadau wengi kwa mara ya kwanza, walifurika kwenye chumba chetu na kwa muda wote kulikuwa hakuna mizozo ya kisheria na kanuni na miongozo yao, walitukubalia na sisi tukawakubalia, lakini katika kujadili suala hili kuna neno lilijitokeza, kuongezwa neno faragha ili kutia nyama kwenye sheria hii na ndio maana wajumbe wengi ukiona waliosimama hapa kitu faragha imo, ingawa muswada ndani yake humo ndani kuna neno linaitwa faragha.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, mimi nakubaliana na neno faragha na liangaliwe vizuri kwenye kamusi ya Kiswahili ya Oxford, lina maana yake. Kamusi ya Kiswahili ya Oxford neno faragha lina maana yake, sitaki kuendelea sana, lakini nasema kwamba sheria hii ikipitishwa itajenge utu wetu, heshima yetu na faragha yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii ndogo, ahsante. (Makofi)