Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Asya Mwadini Mohammed (6 total)

Hotuba ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyoitoa wakati wa Ufunguzi wa Bunge la Kumi na Mbili, Tarehe 13 Novemba, 2020
MHE. ASYA MWADINI MOHAMED: Mheshimiwa Spika, nikushukuru kwa kuweza kunipa nafasi jioni ya leo nami kuchangia hoja ya Mheshimiwa Rais ambayo aliutubia siku ya uzinduzi wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini hapa Dodoma.

Mheshimiwa Spika, awali ya yote kwanza napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuweza kunipa pumzi na mimi leo nikasimama mbele yako ili kuweza kuchangia hayo ambayo yanakuja juu yako. Katika hotuba ya Mheshimiwa Rais nimeipitia, amezungumza vitu vingi, lakini mimi ninaomba kurudia ukurasa wa 13 na 14 ambao Mheshimiwa Rais alisisitiza zaidi kuhusu ulinzi wa amani, umoja, kuyalinda Mapinduzi matukufu ya Zanzibar, lakini vile vile suala zima la Muungano.

Mheshimiwa Spika, mimi nataka kuzungumza kipengele kidogo kuhusiana na kero kubwa za Muungano ambazo zinakumba Taifa hili. Tangu ninapata ufahamu na kulifahamu Bunge lako tukufu na nikiwa nikilifuatilia vipindi mbalimbali nimesikia watu sana Wabunge waliopita walikuwa wakilalamika juu ya mustakabali mzima wa kero za Muungano, lakini bado kero zinaendelea na hadi sasa tunaona kwamba kuna changamoto hizi zinaweza kuondoka kwa haraka.

Mheshimiwa Spika, vikao vinakaliwa mbalimbali kujadili mustakabali mzima wa kero za Muungano lakini bado kuna kero ambazo tunakutana nazo asubuhi na jioni, na niweze kutoa mfano, kwenye kero kubwa ya masuala mazima ya biashara. Wazanzibari tunafahamu kwamba tumelelewa na utamaduni mkubwa wa masuala mazima ya ufanyaji wa biashara. Suala hili kwenye kero za Muungano linaudhi sana kwa sababu ndugu zetu kutoka Tanzania Bara hawawezi kuja kununua vitu kutoka Zanzibar, wakisafirisha kufika bandarini wanadaiwa malipo (charged) wanaambiwa hiyo ni mali ya Wazanzibari.

Sasa tunaona hapa ni jinsi gani kunakuwa na stofahamu kati ya bande hizi mbili wakati Mheshimiwa Rais kwenye hotuba yake amesema anasisitiza kuweka sawa suala hili nzima na kusema kwamba hatahakikisha usawa na maendeleo yatapatikana.

Mheshimiwa Spika, lakini maendeleo pia yawezi kupatikana bila kuwa na elimu, tunaziona changamoto za elimu kati ya Tanzania Visiwani na Tanzania Bara kitu ambacho ukiangalia syllabus ya msingi wa Tanzania Bara ambao unakuwa umetengenezwa na Wizara ya Elimu ya Tanzania bara lakini syllabus ya elimu ya msingi kwa upande wa SMZ syllabus hii pia inatengenezwa maana yake iko tofauti. Lakini syllabus hiyo hiyo ukienda kwenye sekondari wanatumia syllabus moja, lakini inapelekea kwamba bara wanasoma vitabu vyao na Tanzania Visiwani wana vitabu vyao. Hii ni changamoto kubwa kwa watoto wetu wa Kizanzibari inawapelekea sana na siku zote katika drop failure ya school huwa tunawaona watoto wa Kinzanzibari wana- fail sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo Wizara husika inayosimamia masuala mazima ya Muungano naomba walichukue na walifanyie kazi kiukweli ni kero kubwa na inawaumiza sana Wazanzibari.

Kwa kuwa ni muda ni mchache sana naomba nichangie hotuba ya Mheshimiwa Rais ukurasa wa 46 unaozungumzia issue nzima za utalii. Mheshimiwa Rais alituambia kwamba mwaka 2015 kulikuwa na wageni ambao wanaingia 1,137,182 lakini kutoka gap ya mwaka 2015 mpaka 2019 ametuambia tena kuna gap ya wageni ambao waliokuwa wanaingia 1,510,051.

Mheshimiwa Spika, hapo unaoiona hii distance ambayo inaonekana bado miaka mitano yaani interval ya wageni kuongezeka ndani ya Tanzania imekuwa ndogo sana. Nishauri kwa Wizara husika ambazo zinasimamia masuala ya utalii waweze kuongeza nguvu za ziada kuweza kukaribisha wageni, waweze kufika ndani ya Tanzania, lakini vilevile tuna vivutio vingi ndani ya Tanzania yetu, kitu ambacho vitu hivi havisimamiwi ipasavyo na havitengenezwi vizuri, kwa hiyo, tunakosa wageni kufika. Mimi mwenyewe nimefika katika Makumbusho ya Bagamoyo na nimekwenda, hali ilikuwa hainiridhishi. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Mheshimiwa Asya, dakika zako zimeshakwisha.

MHE. ASYA MWADINI MOHAMED: Mheshimiwa Spika, naomba nimalizie…

SPIKA: Unga mkono hoja.

MHE. ASYA MWADINI MOHAMED: Mheshimiwa Spika, suingi mkono hoja. (Kicheko)

SPIKA: Mheshimiwa Vedastus Mathayo Manyinyi.

MHE. ASYA MWADINI MOHAMED: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira
MHE. ASYA MWADINI MOHAMMED: Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa nakushukuru kwa kuweza kunipa nafasi, na mimi nichangie hotuba hii ya bajeti ya Wizara ya Muungano.

Mheshimiwa Spika, nachukua nafasi ya kwanza kumpongeza Mheshimiwa Rais mama Samia Suluhu Hassan kwa juhudi zake za makusudi kwa kuweza kuuheshimisha Muungano huu.

Mheshimiwa Spika, ikiwa jana ni siku ya Muungano, aliweza kutoa fedha za Sherehe ya Muungano na kuzigawa kwa nchi mbili hizi. Kwa hiyo, nampongeza sana na ametutia moyo, ameonesha kweli ana nia ya kwenda kuusaidia Muungano huu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, la pili, mama huyu, Rais wetu pia anaboresha mawasiliano ya kidemokrasia, ameweza kumpa nafasi Mheshimiwa Rais wa Zanzibar Dkt. Hussein Mwinyi kwenda kumwakilisha katika Mkutano wa SADC. Imetoa faraja sana na ninampongeza sana, tunaona kweli njia iliyokuwa na magugu sasa inakwenda kuwa safi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pamoja na mazuri ambayo yameanza, napenda kulieleza Bunge lako Tukufu, kumekuwa na changamoto nyingi kupitia Muungano huu, hususan Wazanzibari wakilalamika kupitia mitandao mbalimbali na maeneo mengi. Mengi yanazungumzwa, lakini mimi napenda kulizungumza suala zima la mfuko wa pamoja wa Jamhuri ya Muungano wa Zanzibar. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, leo imezungumzwa hotuba…

SPIKA: Mheshimiwa Asya, umesema mfuko…

MHE. ASYA MWADINI MOHAMMED: Mheshimiwa Spika, mfuko wa pamoja wa Muungano. Umenielewa? (Kicheko)

Mheshimiwa Spika, leo imekuja hotuba ya Bajeti ya Wizara hii, lakini hatukuona kwamba kuna kipengele ambacho kina uwezo wa kuuchambua mfuko huu ili kuyaweka mambo haya sawa kuutambua kwanza mfuko huu una kiasi gani? Pia mfuko huu mgawanyo wake uko vipi? Wazanzibari wana haki ya kupata asilimia ngapi? Wanadai kiasi gani? Tunaomba mfuko huu uwe unaletwa katika Bunge lako Tukufu na uwe unajadiliwa ili kuyaweka mambo haya wazi na kupunguza kelele za mitaani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, napenda pia kuchangia katika kipengele cha mazingira. Yamezungumzwa mengi; kumekuwa na Idara ya Mazingira, mimi nitakwenda kujikita zaidi kwenye issue nzima ya mifuko ya plastiki. Serikali ilitoa tamko la kuzuia uingiaji wa mifuko ya plastiki hasa kwa watumiaji na wafanyabiashara ambao wapo ndani ya nchi yetu. Kwa masikitiko makubwa, mifuko inaendelea kutumika na watu wanaitumia, lakini kinachoniumiza, Serikali huwa inachukua hatua kwa wafanyabiashara wadogo wadogo ambao wako chini, wao kazi yao kuuza mboga za majani pamoja na nyama na vitu vingine, wanawakamata, wanawapiga fine, na kuwafanyia mambo mengi ambayo huwa siyo mazuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika jambo hili, wako vigogo ambao ndio wanaoingiza mifuko. Tukiendelea kuwakandamiza wananchi wa chini, hatujaweza kuwasaidia. Tunatakiwa twende tukawatafute wahusika na wanajulikana; waweze kusema na kutoa hili tamko ambalo limetoka kwamba lisifanyiwe implementation kwa wafanyabiashara wadogo, wakatafutwe ambao wamewekeza na wanaoingiza mifuko hiyo ndani ya nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tumekuwa tukiona mambo mengi, ni kwa sababu hao ambao wanaleta mifuko hii wanahifadhiwa kwenye kwapa, lakini wanaumizwa hawa ambao wako chini. Suala hili kama tunahitaji kweli kuwasaidia Watanzania, basi Serikali hii ikaanze kuwashika hawa ambao wanaingiza mifuko hii ndani ya nchi yetu, ndipo wakamalizane na watu wa chini kwa sababu muuza mboga kama hajapewa yeye kifungashio cha mfuko wa plastiki, anakitoa wapi? Mtaji wa mboga ni shilingi 200,000/=. Kwa hiyo, lifanyiwe kazi kweli kweli. (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Spika, la pili, ni kweli tumeamua kuondoa vifungashio vya plastiki ndani ya nchi yetu, lakini tumekuja na mbadala? Tunatoa vifungashio vya plastiki, je, tumeweza kuwapa mbadala hawa akina mama wanaouza mboga mboga au wauza nyama? Leo mtu anakwenda sokoni na shilingi 2,000/= yake anasema anataka kununua mchicha wa shilingi 500/=, dagaa zake za shilingi 500/= na kitu kingine. Mfuko wenyewe unauzwa shilingi 500/=. Kweli wataweza kuumudu? Kwa hiyo, Serikali inapoamua kupiga marufuku ya kitu fulani, kwanza wafanye utafiti, waje na solution ya kuweza kulisaidia Taifa hili ndipo wapangue hiyo mifuko. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, vile vile elimu inahitajika sana na watu lazima waelimishwe kwamba tunaondoa mifuko ya plastiki kwa sababu ni hatarishi, wanyama wetu wanaweza wakala, lakini na hawa wanyama sisi tunakula nyama yake na vitu vingine vingi ili kuweza kulisaidia Taifa hili; lakini kutoka tu kusema kwamba tunaondoa mifuko bila kuwatafutia mbadala, bila kutoa taaluma, bila kuwakamata vigogo wanaotuingizia, jambo hili haliwezi kusaidia. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. ASYA MWADINI MOHAMMED: Mheshimiwa Spika, unanipa dakika mbili? (Makofi/Kicheko)

SPIKA: Malizia dakika moja.

MHE. ASYA MWADINI MOHAMMED: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana.

Mheshimiwa Spika, la tatu,…

MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Spika, Taarifa.

SPIKA: Ah, unaona sasa Mheshimiwa Asya unanitia katika matatizo. (Kicheko)

Taarifa inatoka wapi Mheshimiwa? Ahsante, endelea. Mheshimiwa Asya ukae chini ili uandike hiyo taarifa vizuri, uzime hapo, maana taarifa nyingine hizi ni muhimu.

T A A R I F A

MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Spika, napenda kumpa taarifa mchangiaji kwamba siyo jukumu la Serikali kumwelekeza mwananchi alternative. Zipo alternatives nyingi, tulikuwa nazo tangu zamani. Tuna mifuko ya kushona, tulikuwa tunashona tangu tuko watoto, ipo inatumika. Kwa hiyo, wananchi watumie hizo alternatives. Siyo lazima Serikali iwaoneshe alternatives, Mifuko ya plastiki haitakiwi, ni kazi ya Serikali kuizuia na wananchi watafute njia rahisi kwa ajili ya kupata vifungashio mbadala. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, napenda kumpa taarifa hiyo mchangiaji. (Makofi)

SPIKA: Ahsante sana. Mheshimiwa Asya Mwadini Mohammed, taarifa hiyo unaipokea? (Makofi)

MHE. ASYA MWADINI MOHAMMED: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Mimi leo nimefunga na huu ni mwezi Mtukufu wa Ramadhani. Nadhani nilikuomba dakika mbili kwa ajili ya kulisaidia Taifa hili. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Spika, Katiba yetu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ukurasa wa 128 umezungumza mambo mengi ambayo yanapaswa kusimamia katika Muungano huu. Kuna suala la ulinzi na usalama, lakini kwenye ulinzi na usalama kuna Wizara ambayo inahusika katika kitengo hiki. Wizara hii kwa upande wa Zanzibar haina Ofisi, hivyo inasababisha wastaafu wanajeshi ambao ni mama zetu na bibi zetu ambao wanasubiri viinua mgongo, wanalazimika kusafiri kuja bara, kwenda Dodoma na sehemu nyingine kwa ajili ya kufuatilia mafao hayo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naishauri Serikali iweze kuwasaidia wastaafu hao maana waliitumikia nchi hii. Hivyo, kama waliitumikia wana haki zao sawa na wengine.

Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. ASYA MWADINI MOHAMED: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kuweza kunipa nafasi ili niweze kuchangia hotuba hii muhimu ya Wizara ya Maliasili na Utalii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa naomba nilieleze Bunge lako Tukufu kwamba Utalii ni Sekta muhimu sana katika uchumi wa Tanzania lakini sekta hii inachangia Pato la Taifa asilimia 17. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mujibu wa Taarifa ya Bodi ya Utalii Tanzania, Tanzania inatembelewa na wageni wapato milioni moja kwa mwaka. Pia, Bodi hiyo ya Utalii imesema kwamba hao wageni milioni moja asilimia 60 ni wageni kutoka nje ya nchi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hili linanisikitisha sana ukizingatia kwamba tunawategemea sana wageni kutoka nje ya nchi kuliko sisi ambao tupo ndani ya Taifa letu. Kwa hiyo, faida inayopatikana kwa utalii wa ndani, kuna nchi kwa mfano Brazil wao wana wageni wa ndani ya nchi wanaotembelea katika vivutio vyao ni asilimia 68. Wanategemea asilimia 32 tu, wageni kutoka Mataifa mbalimbali kwa ajili ya kwenda Brazil. Hii inaonesha kwamba unapokuwa umejipanga vizuri katika utalii wa ndani huwezi kutegemea sana ule utalii wa nje. Hilo la kwanza. La pili, pato lile unakuwa na uhakika nalo kwa sababu liko ndani ya nchi. Kwa hiyo, haliwezi kutoka nje ya nchi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hivyo, naishauri sana Serikali kwanza kabisa masoko yetu yajikite zaidi kufahamisha Watanzania; kwanza kuhusiana na masuala mazima ya utalii. Pili, hata hawa wanafunzi wetu shuleni tungewatengenezea mtaala au vitabu wakaanza kukua na utamaduni wa kufanya utalii ili iweze kusababisha, maana wanavyokuwa wakubwa wanajua utalii ni suala muhimu na linaweza kuwaletea tija wao wenyewe binafsi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tusiwategemee sana wageni kutoka nje ya nchi kuja kututembelea. Kwa mfano, tumeona mwaka jana 2019/2020 kulivyokuwa na janga kubwa la corona. Kwa hiyo, utalii ulitetereka. Tuna watoto wetu na ndugu zetu walikosa kazi wengi sana wakaendelea kukaa nyumbani. Kama tungekuwa tumeimarisha vizuri Sekta ya Utalii hapa kwetu hivyo wale watu wangeendelea kufanya kazi na masuala mengine yangeendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia, naomba niende kwenye kipengele kidogo tu, labda niseme, nimeipitia Sera ya Utalii ya Tanzania inanisikitisha sana. Tunavyosema tunahitaji kupiga hatua kwenye utalii lakini sera yetu bado ni ya mwaka 1999. Kwa hiyo, sera hii haikidhi mahitaji ya utalii wa sasa ambao tuko nao. Kwa hiyo, tunahitaji kwanza tuboreshe sera yetu pamoja na sheria za utalii ili tuweze kuinua utalii wetu na pia waweze kuingiza Pato letu la Taifa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye utalii wa ndani tusiwategemee sana japo tunapiga kelele Wabunge humu, ofisi mbalimbali, lakini, kwa nini hata hawa Wabunge ukiwauliza humu ndani wangapi wameweza kutembelea vivutio vyetu itakuwa ni mtihani kwa kweli. Wengine wanaweza kukuambia wamefanikiwa tu kwenda kwenye Kamati ndiyo wameweza kuona tembo na chui. Sasa hili halileti tija, maana tunapokaa tunapiga kelele haileti tija, tuoneshe mfano sisi wenyewe viongozi kwanza. Twende kwenye vivutio, tuwape support Wizara ili na hawa watoto wetu tukiwachukua, watoto wakienda kwenye vivutio, unajua watoto wana story, wakirudi shuleni wanahadithia watoto wenzao. Kwa hiyo, watoto nao wanaenda kuhadithia wazazi. Kwa hiyo, tunakuwa na jopo kubwa la mwingilio wa utalii wa ndani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba pia nichangie kwenye masuala mazima ya vivutio vya utalii. Mwanzo nilisema kwamba tunategemea sana wageni wapato milioni moja. Average inaonesha kutokana na vivutio ambavyo tunavyo, hawa wageni bado ni kidogo sana. Ni kidogo kwa sababu vivutio vyetu ni vingi, maana yake vivutio vimewakumbatia wageni kwa hiyo, maana yake vinabaki vinahitaji watu. Kwa hiyo, niishauri Serikali kwenye suala hili.

Mheshimiwa Naibu Spika, la kwanza, tuweze kuwapa wawekezaji vivutio vingine ambavyo hatuviwezi. Suala la pili, nakumbuka nilichangia kwenye uvuvi, nilizungumza sana issue ya marine park na nikaomba Wizara ya Uvuvi hili suala la marine conservation wawapelekee Idara ya Utalii, kwa sababu ukipitia takwimu inaonekana wageni kuanzia 45,000 kwenda 70,000, wageni hawa wanavyokuja Tanzania wanafanya diving. Wanaenda kuangalia matumbawe na masuala mengine kwenye bahari.

Mheshimiwa Naibu Spika, hata ukiangalia kwenye mitandao wageni ambao wanatoka Scandinavia yaani kule kwetu Zanzibar wanavyokuja lazima wakifika waombe kwenda kuangalia coral reef na vitu vingine. Kwa kuwa watu wa utalii ni wataalam zaidi kwenye masuala ya uhifadhi, naishauri Serikali hii Idara ya Marine Park iende moja kwa moja kwenye Wizara ya Utalii na tutaweza kupata pato kubwa zaidi kupitia hii tour moja tu, sikwambii hizo zingine. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niende pia zaidi kwenye masuala mazima ya kumshirikisha mwanamke katika utalii wa Tanzania. Tunaona kwamba tunazungumza utalii, nimepitia hotuba na vitu vingine vingi lakini hatuoni mwanamke anatajwa kama ana sehemu kwenye utalii na anafaidika vipi. Namzungumzia zaidi mwanamke ambaye yuko chini grassroot ambaye amepakana na border, hifadhi, yuko kwenye maziwa, yuko chini ya fukwe na yuko katika sehemu pengine nyingi za utalii. Kwa hiyo, mwanamke huyu utaona kwamba yeye yupo amepakana na hifadhi au amepakana na msitu lakini wanaofaidika ni watu labda wanaotokea mkoa mwingine kwa sababu analeta wageni. Yeye yuko pale tu na ule msitu, atafaidika labda kupata hewa safi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa niishauri Serikali kwamba; kwanza, tuweze kutengeneza mkakati maalum kuweza kuwasaidia wanawake hawa kupitia miradi mbalimbali midogo midogo ambayo itaweza kuwainua akinamama. Kwa mfano, tuna utalii tunaita culture tourism. Huu utalii, mgeni anaweza akaja mimi mwenyewe binafsi napenda pia kujifunza. Niliwahi kwenda Kagera lakini nilifika nilitumia masaa matatu kuangalia Wanabukoba wanapika chakula chao cha ndizi kwa mtazamo upi. Kwa hiyo, huu ni utalii. Tuwape nafasi akinamama waweze kile kidogo ambacho wako nacho kule majumbani wanafua, wanapika, wanatwanga, lakini mgeni ana-appreciate sana na anajifunza vitu vingi zaidi pale kwa kuona. Kwa hivyo, akinamama watapata pato, lakini vile vile na Serikali nayo itaongeza uchumi. Tusiuache utalii wa utamaduni, ni utalii ambao unaleta pato kubwa ndani ya Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano ukienda India, Wahindi hawakubali ukifanya utalii usipite katika street zao, usipite kwenye vichochoro vyao ili ujifunze bajia na kachori zinatengenezwa vipi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niendelee zaidi nilizungumza suala zima la masoko na tunahitaji bado masoko yetu yako chini kwenye suala zima la utalii na tunahitaji zaidi Serikali kupitia Idara ya Utalii waweze kutengeneza mechanism ambayo iko strong itakayo-deal na marketing on tourism only ili tuweze kupata pato lakini na kuleta wageni. Narudia tena, tusitegemee zaidi wageni kutoka nje ya nchi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile, nishauri labda kwa sababu tunatumia TV, magazeti, vipeperushi lakini kuna mitandao. Sasa hivi, dunia iko kwenye mkono, kuna hawa akina Ayo na wengineo, kwa nini tusingetengeneza vitu kama hivi mtu akiingia tu anapofungua simu yake akiingia kwenye mtandao anakutana na kitu kwamba Visit Tanzania, kuna one, two, three, four ili iweze ku-motivate na nilishazungumza kwamba tutaenda kuwahamasisha watoto wa shule, vyuo vikuu, maana hapa tunakuja Bungeni tunawaleta watoto wa shule, tunawaleta watu kutoka vyuo vikuu, wanahamasika. Kwa hiyo na hiyo itatumika zaidi ili kuweza kukuza utalii wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho kabisa nisisahau, ni suala zima la uhifadhi na usimamizi wa mazingira kwa pamoja. Kwenye mazingira hasa masuala ya takataka na mambo mengine tumeukaribisha utalii Tanzania, kwa hiyo, Serikali nayo inapaswa kuanza kufahamu kwamba tayari tunavyoleta wageni nje ya nchi wanakuja na vifungashio vyao tofauti, wanakuja na material yao tofauti ambayo sisi kama utamaduni wetu yalikuwa hayapo.

Kwa hiyo, hatuna budi kwanza pia ku-focus na kwenye masuala mazima ya uhifadhi wa mazingira ili takataka ambazo zipo zinazalishwa kwenye upande wa utalii zisiwe zinachomwa, zisiwe zinapelekwa baharini na zisiwe zinafanyiwa mambo mengine.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba tujifunze pia masuala mazima ya recycling, tutumie akinamama, tutumie vijana wetu ambao hawana kazi, wajifunze kwenye utengenezaji wa mbolea na masuala mazima mengi kwa ajili ya kukuza uchumi wetu, lakini na kutengeneza step ya kutoka hapa tulipo na twende kwenye hatua ambayo tunataka utalii ukue. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi
MHE. ASYA MWADINI MOHAMED: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kuweza kunipa nafasi nami niweze kuchangia hotuba hii ya Wizara muhimu kwa maendeleo ya Taifa letu.

Mheshimiwa Spika, naomba ninukuu Taarifa ya Kamati ya Bunge ya mwaka 2018 ambayo inasema kuhusiana na shughuli za uvuvi wa Bahari Kuu, kama utasimamiwa vizuri ipasavyo, basi Serikali tunaweza kuiingia pato la moja kwa moja shilingi bilioni 352. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hali kadhalika, Kamati ya Bunge leo hapa ilipokuja, imehakikisha na imezungumza pia bado Serikali haijafanya uwekezaji wa kutosha katika Sekta hii ya Uvuvi, hasa katika Bahari Kuu. Hili nimeliamini na limejidhihirisha pia; kwenye hotuba ya Waziri amesema pia kuwa wapo katika mchakato wa hatua ya kufufua Shirika la Uvuvi TAFICO ambalo Mheshimiwa Waziri ameliongelea zaidi kwenye ukurasa wa 119. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa masikitiko makubwa sisi tumezaliwa na bahari tumeikuta, lakini leo ndio kwanza tunazungumza ufufuaji wa shirika. Kweli tumekuwa tuko tayari kwenye uwekezaji wa bahari?

Mheshimiwa Spika, ukiangalia bahari hii inaambiwa ina iwezo wa kuleta mapato shilingi bilioni 352. Sioni Serikali inakwama wapi kwa ajili ya kwenda kuwekeza, lakini kama Serikali nguvu hazitoshi kuna wadau wako tayari kuwekeza ambao tunawasema wawekezaji. Nadhani, nishauri, Wizara itoe wazo na iseme kwa bayana wawakaribishe wawekezaji kwenye bahari kuu waweze kuwekeza, ili tuweze kusaidia vijana wetu kupata ajira, lakini halikadhalika tuongeze pato la Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, unapozungumza bahari huwezi kuacha kuzungumza uhifadhi wa maeneo ya mazalia ya samaki, nikimaanisha matumbawe. Haya matumbawe ambayo yapo yanazunguka ndani ya bahari yetu ndio sehemu salama na ndio muhimu kwa samaki wetu ambao wana uwezo wa kuzaliana, lakini pia samaki wanapata chakula kupitia hifadhi hizi muhimu za matumbawe. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa masikitiko makubwa matumbawe yetu yanapotea na yanaathirika kweli, kwa ambao wale wataalamu wa bahari wanakwenda baharini, nikiwemo mwenyewe nilishawahi kuangalia hayo matumbawe, unakuta matumbawe ambayo tayari yamefariki. Ukiwauliza wataalamu wanakwambia haya matumbawe yamefariki kwa sababu ya uchafuzi wa mazingira. Bahari inajaa joto kutokana na uchafuzi mbalimbali ambao unafanywa wa kimazingira hivyo husababisha matumbawe yale kufariki. Yanapofariki yale matumbawe na kuondoka kabisa itabidi samaki hawa waweze kuhama sehemu ile ambayo hawawezi kuzaliana wala kupata chakula na kwenda kutafuta hifadhi mbali. Sasa maana yake wanavyokwenda mbali wana uwezo wa kutoka ndani ya bahari yetu ama kutoka ndani ya Tanzania na kwenda nchi jirani. Je, Serikali ina mkakati gani wa kuwadhibiti samaki hawa ambao wanatoka? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, la pili, Serikali je, ilishawahi kukaa na nchi jirani na kutengeneza mikataba ya makubaliano juu ya usimamizi wa hifadhi za bahari na hasa samaki wetu wanavyotoka na kwenda kuhamia katika nchi jirani? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuna samaki wanaitwa Tuna, hao wana tabia kama ya nyumbu. Kuna msimu wanaondoka Tanzania, wanaondoka ndani ya bahari wanakwenda katika nchi jirani, wanakwenda kustarehe huko then wanarudi wanapenda kufanya tour. Kwa hiyo, samaki hawa wana uwezo wa kutoka na kwenda, lakini wakifika kule wakavuliwa then tunarudishiwa samaki hawa wanauzwa kwenye vikopo tunaambiwa nunueni Tuna kwenye makopo, lakini kumbe tunauziwa mali yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa sababu tunahitaji Serikali, nishauri, iwekeze zaidi ifanye mashirikiano na nchi jirani kuhakikisha wanasaini mikataba ambayo halali ya kusimamia samaki tuna na wengineo, ili kuweza kusaidia pato la nchi hii lisiweze kupotea. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, halikadhalika kwenye uhifadhi, naomba niishauri tena Serikali, kuna kisiwa Zanzibar kinaitwa Chumbe Island, hiki kisiwa kwa wale wanaosafiri kwa boti mara kwa mara utakutananacho utakuta mnara pale wakati unaelekea Zanzibar. Hiki kisiwa kimepata tuzo ya uhifadhi wa utalii wa kimazingira mwaka 2019 kwa East Africa kimekuwa cha kwanza. Ni kwa sababu, kisiwa hiki kina muwekezaji kwa hiyo, wamewekeza vizuri, wana wataalamu wa kutosha na wanahifadhi vizuri yale matumbawe kwa kushirikiana na Serikali ya Zanzibar. Kwa hiyo, wamefikia kupata hiyo tuzo, lakini pia sio hiyo tu, wamepata tuzo nyingine kuwa Wanautalii wa kihifadhi bora ndani ya miji ya kidunia yote wapo ndani ya namba 10. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, lisiwe tu kwa Chumbe na ukienda Chumbe kweli ni kweli hata kama hujui kuogelea wewe unaweza ukavishwa mask na ukasaidiwa na ukaona hayo matumbawe na jinsi roho yako itakavyoburudika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nishauri, matumbawe kwa jina jingine yanaitwa coral reef jamani. Niishauri Serikali kama Wizara ya Uvuvi imeona pia ni mzigo wa kuhifadhi kuna Wizara ya Utalii na Maliasili hawa ndio makonkodi wa uhifadhi. Kwa nini wasii-move hii marine park wakawapelekea Wizara ya Utalii na utalii ukaweza kuhifadhi vizuri? lakini nje na kwamba, tunatumia kupata samaki haya matumbawe, lakini vilevile ni utalii wa kimazingira ambao wageni walio wengi wanapenda kufanya utalii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ukifika pale kwenye Kisiwa cha Chumbe unafanya booking mwezi mmoja kabla ukiwa unataka kwenda kuyaona matumbawe. Kwa hiyo, unaona jinsi gani pato linaongezeka na wageni wanapenda kwa hiyo, nishauri Serikali kama wao mzigo umekuwa mzito wawape Wizara ya Utalii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, la mwisho, pia nishauri hapo waongeze juhudi ya kuwatafuta wataalamu zaidi kwa sababu, tunahitaji samaki na bado samaki hawatutoshi wanakwenda mbali kwa hiyo, imekuwa ni shida na hasa kwa hawa Ndugu zetu ambao wanafanya kazi za bahari kila siku. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niendelee kwenye mafunzo kwa wavuvi wetu, tuna wavuvi ambao wanaamka asubuhi majumbani wanakwenda baharini, na wanakwenda kwa sababu ya njaa ya maisha, lakini hawaendi kwa sababu hii kazi wanataaluma nayo. Mwingine anakwenda kwa sababu ameirithi, labda babu yake alikuwa mvuvi, leo atamchukua apige kasia, kesho wataingia baharini kwa hiyo na yeye anakwenda kwa kufikiri babu hapa alikuwa akitupa ndoana ndio wanapatikana samaki, lakini sivyo dunia imebadilika. Mabadiliko ya tabia ya nchi yapo mengi, halikadhalika bahari imekuwa na kina kikubwa cha maji, matumbawe ndio kama hivyo yanapotea kipindi hicho kulikuwa hakuna uchafuzi wa mazingira. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa wavuvi wetu wanakwenda kuvua wanarudi hakuna. Na wanarudi maisha yanaendelea kuwa magumu sana, lakini la pili pia wakipatiwa mafunzo wavuvi wetu itawasaidia watakwenda sehemu salama za kuweza kuvua, lakini la mwisho kabisa wakipatiwa mafunzo watakwenda sehemu ambazo wana uhakika leo tukienda siku ya leo tunapokwenda sehemu kadhaa basi hatuwezi kukutwa na changamoto yoyote ya kiuvuvi, lakini na watasikia moyo watasema kwamba, leo kama fulani ni mvuvi na mwingine atakwenda. (Makofi/Vigelele)

SPIKA: Ahsante Mheshimiwa Asya.

MHE. ASYA MWADINI MOHAMED: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi. (Makofi)
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022
MHE. ASYA MWADINI MOHAMMED: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kuweza kunipa nafasi nami jioni hii ya leo niweze kuchangia hotuba hii ya Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Mipango.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kwanza kabisa nianze kunukuu hotuba ya Mheshimiwa Waziri aya ya 77 ukurasa wa 65 unaosema kuhusu Zanzibar. Kwa maneno aliyoweka ya kunukuu, napendekeza kutekeleza utaratibu wa kuruhusu mapato yanayotokana na kodi na tozo za Muungano kwenye mapato yanayotokana na viza ili yaweze kutumika pale yanapokusanywa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mapato yanayotokana na tozo na viza za Zanzibar yaonekane kwenye bajeti upande wa Zanzibar kuidhinishwa na kutumika kwa upande wa Zanzibar. Hii kwa Wazanzibari imekuwa ni jambo jema sana na inakwenda kuendelea kutatua zile kero mbalimbali zinazogusa Muungano wetu. Naiomba Serikali, maana maneno siyo vitendo, kwa hiyo, linapozungumzwa, tunaomba sana liende kwenye utekelezaji. Tuone kama bajeti inaanza kutumika Julai, basi utekelezaji huu na makusanyo kuanzia Julai yaanze kutekelezwa na yakaweze kutumika kwa upande wa Zanzibar. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika kuisaidia Serikali ili tuweze kupata mapato, najikita katika Sekta ya Uvuvi. Sekta hii inachangia pato la Taifa asilimia 1.8, lakini mapato yanayotokana na mauzo mbalimbali ya bidhaa za uvuvi ni 3%. Kwa masikitiko makubwa sana, hii sekta ni kubwa na pana, lakini pato ambalo limetajwa hapa la asilimia 1.8 ni dogo kulinganisha na rasilimali zinazotokana na bahari.

Mheshimiwa Naibu Spika, bahari yetu Mungu ametujaalia neema kubwa sana kwa kweli, ina rasilimali nyingi sana za kutosha. Kama Serikali itajiwekeza zaidi, basi tuna uwezo wa kupata pato kubwa ndani ya Taifa letu na tutapunguza hata hizi kodi mbalimbali ambazo zinawagusa wananchi wanyonge wakipunguziwa mzigo huu, mapato yataongezeka kupitia sekta hii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ukipitia bajeti ya utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano iliyokwisha, Wizara hii ya Uvuvi imekuwa ikipatiwa asilimia 21 tu ya bajeti katika utekelezaji wake. Hii inaonekana wazi kwamba Serikali bado haijaamua kujiwekeza vizuri katika Wizara hii, ikiwa miradi ya maendeleo inapewa asilimia 21 kwa miaka mitano, tusitegemee kama kuna mabadiliko wala kupata mapato katika Sekta hii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika rasilimali ambazo zipo ndani bahari, nakumbuka nilizungumza suala zima la uhifadhi wa matumbawe kama kivutio na nikatoa mfano wa baadhi ya wageni ambao huwa wanatembelea na tunapata mapato mengi kama Serikali. Nje na matumbawe, kuna kilimo cha mwani. Cha kushangaza ni kwamba Serikali yetu bado haijatupa jicho na wala haioni kama kuna umuhimu wa kuwekeza zaidi kwenye kilimo cha mwani. Ni kilimo ambacho kinalimwa kwa muda wa wiki sita tu na watu wanavuna. Kwanza kilimo chake ni cha muda mfupi lakini tumepewa bahari ambayo ndiyo sehemu sahihi tuna uwezo wa kupanda mwani wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile faida ambayo inapatikana katika kilimo cha mwani kwanza tutatengeneza ajira pana, maana watu watajiajiri kwenda baharini na tutakuwa na viwanda nje. Tunazungumza kila siku tunahitaji kuwa na Tanzania ya viwanda, lakini tutakuwa na viwanda ambavyo mwisho wa siku hatutakuwa na rasilimali kwenye hivyo viwanda ambavyo tunavyo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nje tu na ajira, mwani ni chakula. Tuna uwezo wa kutengeneza vitu mbalimbali ambavyo binadamu tunavitumia, ni vyakula vya kila siku. Vile vile, mwani hutumika kama vipodozi. Akina mama wengi wa Kitanzania tunatumia cosmetics kutoka nje ya nchi wakati tuna rasilimali zetu nyingi. Ukianza na huu mwani, tuna uwezo wa kutengeneza sabuni na vitu vingi tukavitumia wenyewe. Kwa hiyo, kuna haja Serikali nayo kutupa jicho kwenye kilimo hiki cha mwani ili tuweze kuokoa Taifa letu na kupata mapato. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile kilimo hiki cha mwani tukizungumza kwa dunia, tuchukue mfano nchi ya Indonesia ndiyo imekuwa ya kwanza ikilima mwani na ndiyo nchi ambayo inafanya vizuri kwenye Sekta hii ya Mwani. Mheshimiwa Rais alisema kwamba tuwe tunajaribu kuwaiga watu wanaofanya vizuri, siyo dhambi. Kwa hiyo, nasi nadhani ni wakati wetu sasa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, watu wa Indonesia walio wengi wametajirika kupitia kilimo cha mwani. Vile vile wana viwanda vingi vya kutengeneza dawa, vipodozi, wanatumia mwani kama chakula na bado maisha yao yamenyanyuka vizuri sana. Kwa hiyo, naishauri tu Serikali kwanza tuwekeze kwenye mwani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kama Serikali imeona labda imekuwa mzigo mzito au tunaona ni jambo ambalo haliwezekani, wawekezaji wako tayari na wanahitaji hii bahari. Wanaiangalia kwa jicho la huruma sana na wanaitamani kama leo waipate na waweze kuwekeza ili tuweze kutengeneza ajira pana kwa Taifa hili na ili tuweze kutengeneza pato la Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niende katika Sekta ya Utalii. Sekta hii nayo imekuwa ni chachu ya uongezaji wa pato letu, tunaizungumza kila siku lakini ukiangalia sekta hii, utalii ambao umejikita zaidi ni utalii wa wanyamapori maana tumekuwa hatu-focus kwenye utalii mwingine, yaani tumeganda tu kwenye wanyamapori, sisi kila siku kazi yetu ni kutangaza, tuna Ngorongoro na sehemu nyingine. Sasa tunahitaji pia kupanua wigo zaidi. Vile vile, kama sisi hatuwezi wawekezaji wapo, wa ndani na wa nje wako tayari, wanahitaji hii nchi kwa ajili ya kuwekeza. Wao watatengeneza pesa lakini na sisi tutatengeneza mapato, ndiyo kinachotafutwa ili tuweze kuiokoa nchi yetu kwenye masuala mazima ambayo yanaleta maendeleo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hata ukipitia ripoti ya CAG, naye alishauri kwamba utalii wa Tanzania, kuna haja sasa ya kwenda kuingiza katika utalii mwingine na kuanza kuutangaza. Tusing’ang’anie tu kwa wanyamapori. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naishauri tena Serikali iweze kutengeneza mikakati iliyokuwa bora ili tuweze kusimamia Sekta hii vizuri sana. Halikadhalika unapopitia hii hotuba, Mheshimiwa Waziri alisema kwamba watapunguza ada ya leseni za biashara za utalii kutoka Dola 2,000 hadi Dola 500. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kupunguza tu ada kwenye leseni bado hatujasaidia kwenye hii Sekta, kwa sababu tuna changamoto nyingi ambazo zinaikabili Sekta hii. Ukiangalia miundombinu yetu ni mibovu sana. Sehemu ambazo zina vivutio hazifikiki. Kwa hiyo, naishauri Serikali waanze kwanza kuboresha sehemu zenye vivutio vya utalii, watengeneze barabara, viwanja vya ndege ili watalii wawe wana uwezo wa kufika vizuri na kuweza kuingiza pato ndani ya Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia kuwe kuna mazingira Rafiki; tupunguze sintofahamu kwa wawekezaji wetu, maana Uhamiaji anamganda mwekezaji; sijui Halmashauri anamganda mwekezaji na wengine wengi. Imekuwa harassment kubwa sana. Kwa hiyo, tupunguze hizo harassment kwa wawekezaji wetu ili nao waweze kuwekeza kwa kujiachia na kuweza kulisaidia Taifa hili kwa kuwapa ndugu zetu ajira na kulisaidia Taifa hili kwa kuweza kutuingizia mapato.

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Ahsante sana. (Makofi)
Taarifa za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii na Kamati ya Kudumu Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama kuhusu shughuli za Kamati hizo kwa Mwaka 2021
MHE. ASYA MWADINI MOHAMMED: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kuweza kunipa nafasi nami niweze kuchangia michango ya Kamati kutokana na taarifa ambayo imewasilishwa hapa Mezani.

Mheshimiwa Spika, kuhusiana na suala la Ngorongoro mimi itabidi niliruke, naona wadau wenzangu wamelichangia vizuri vya kutosha. Sasa ni kazi kwa Serikali kulichukulia hatua na kwenda kulifanyia kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba nijielekeze zaidi katika sekta ya utalii na hapa nitazungumzia kuhusiana na Serikali yetu kujikita na utalii wa aina moja, nao ni utalii wa wanyamapori. Tunaona utalii wa wanyamapori unatuletea mapato mengi ndani ya Taifa letu, lakini kwa nini tunajisahau kuwekeza zaidi katika sekta nyingine? Maana yake kuna utalii wa masuala ya bahari ambapo nakumbuka kwenye Bunge la Bajeti nilisimama hapa na nikachangia vizuri sana. Tuna utalii wa malikale ambapo leo malikale zetu ukizitembelea kwa kweli ni masikitiko makubwa sana kama Taifa. Ninaumia kama mdau wa Taifa hili. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ni ushauri; ukipitia ripoti ya CAG, ameshauri kwamba sasa kama Taifa tuna haja ya kwenda mbele kujiwekeza zaidi katika sekta ya utalii na tuachane na sekta ya wanyamapori, twende na sekta nyingine. Kwa sababu tunategemea sekta hii ya wanyamapori peke yake, leo ikitokea janga la Taifa, Mungu aliepushe, wanyama wamepata magonjwa ama wamepoteza maisha, maana yake hatuna utalii Tanzania. Kwa hiyo, kuna haja kama Serikali kujiwekeza zaidi katika sekta nyingine. Tuna utalii wa kiutamaduni, utalii wa masuala mazima ya bahari, lakini kuna utalii wa wafuga nyuki. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hizi sekta za utalii wa utamaduni pamoja na wafuga nyuki nimekuwa interested nazo sana kwa sababu ni sekta pekee ambazo wanaweza kupewa akina mama na wakaziendesha vizuri. Kwanza wataisaidia Serikali kupata mapato na akina mama hawa watatengeneza fedha kupitia sekta hizi. Utamaduni ni muhimu sana. Sasa hivi katika Taifa letu watu wanaiga sana utamaduni wa nje, itafika kipindi hapa wajukuu zetu watasahau asili ya Mtanzania. Sasa tukiwekeza zaidi katika sekta ya utamaduni tunaweza kulisaidia Taifa hili. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia nishauri, kama haitoshi, Serikali kama inaona ni mzigo mkubwa kutumia nguvu katika sekta nyingine, kuna haja pia ya kuita ama kuwapa nafasi wawekezaji aidha wa ndani, ama wa nje, kwa ajili ya kuendeleza utalii wetu katika nafasi mbalimbali.

Mheshimiwa Spika, naomba nizungumzie sera. Kamati yangu pendwa ya Ardhi na Maliasili imeshauri hapa na ikawaambia kwamba kama Taifa linahitaji kupeleka mbele utalii wetu, kuna haja sasa ya kubadilisha sera zetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ukiipitia Sera ya Utalii ya mwaka 1999, hebu tuangalie kuna gap ya miaka mingapi mpaka kufikia 2022 leo tunapouzungumza utamaduni wa 1999 na 2022? Hapo tunaweza kupata picha kwamba bado tuna safari ndefu. Kwanza tubadilishe sera zetu. Hata hivyo nishauri katika kubadilisha sera; tusikimbilie kama Wizara tu na department ya utalii wakajifungia peke yao kuanza kuzichambua sera. Ni lazima wajaribu kuwaalika wadau wengine wa Wizara nyingine. Kwa sababu sekta ya utalii ni sekta mtambuka, ukizungumza; uvuvi inaikuta ndani ya sekta ya utalii, ukizungumza mazingira utakuta ndani ya utalii, ukizungumza maji, unakuta ndani ya utalii na Wizara nyingi kama ardhi na kadhalika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nashauri kwamba Wizara ya Utalii ikae sambamba na Wizara nyingine wakati wanatengeneza hii sera, iwe ya utalii ama ya nyuki kwa maslahi mapana ya Taifa ili tupunguze zile contradiction zinavyokuja hapa. Maana yake wakati mwingine unakuwa na swali hujui ulipeleke kwenye Wizara ipi? Kwa hiyo, Mawaziri wakikubaliana kwamba hiki ni kitu cha utalii, lakini kinamhusu wa maji au wa kilimo, au mfugaji, ama mazingira, watakubaliana kwa pamoja ili tuweze kwenda mbele kama Taifa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niendelee kujikita zaidi kwenye suala zima la masoko na utalii. Sekta yetu ya utalii bado hairidhishi ama haturidhiki na masoko ambayo yanafanywa ndani ya sekta hii. Kamati imeshauri, nami pia nashauri zaidi waweze kujiwekeza zaidi katika matangazo. Kwa sababu kuna msemo unasema, “biashara itakangazwayo ndiyo itokayo.” Kwa hiyo, wajiwekeze zaidi kwenye matangazo kwa njia mbalimbali ili tuweze kuisaidia sekta hii iweze kukua zaidi.

Mheshimiwa Spika, kwa mfano, sekta hii ya utalii kuna TV wanaita Safari Channel. Ukiifungua hii TV sometime ina- bore, kwa sababu ukifungua tu unakutana na wanyamapori tu. Yaani dakika kumi, ishirini wanyamapori; baada ya dakika kumi, ishirini, wanyamapori. Kwa hiyo, mtu ataangalia wanyamapori, kesho akifungua akikuta tena wanyamapori, hawezi kufungua tena hiyo TV. Ataangalia vitu vingine. Kwa hiyo, tunatakiwa tubadilishe zile ladha ili tuweze kulisaidia Taifa na kutangaza vyema utalii wetu na vivutio vyetu kwa maslahi mapata ya Taifa hili ili tuweze kupata mapato ya Serikali kuweza kupiga hatua. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. ASYA MWADINI MOHAMMED: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana.