Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Prof. Shukrani Elisha Manya (3 total)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Madini
NAIBU WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kujibu baadhi ya hoja ambazo zimechangiwa na Waheshimiwa Wabunge. Pia, nawashukuru Waheshimiwa Wabunge wote waliotoa mchango wao.

Mheshimiwa Spika, utaona kwamba, wengi wa Waheshimiwa Wabunge wametoa michango ya kujaribu kuboresha na kuendeleza sekta yetu ya madini, wakitambua kwamba ni moja ya sekta ambazo kama ikisimamiwa vizuri ni kweli kwamba itachangia pato la Taifa kwa kadiri ya malengo yaliyo katika sera. Pia ni sekta ambayo katika nyakati ambazo hazitabiriki inaweza ikawa ndiyo sekta mkombozi kwa ajili ya kuchangia uchumi wa Taifa letu.

Mheshimiwa Spika, nitaanza na hoja ya Mgodi wa WDL ambao ni kweli kwamba umeacha uzalishaji kwa muda. Pia ni kweli kwamba kuacha uzalishaji kwa Mgodi huu wa WDL ambao Serikali ina hisa, inatokana na sababu ambazo ziko nje ya uwezo wetu. Kwa sababu, janga la Covid 19 ndilo ambalo lilisababisha kuanguka kwa soko la almasi kwa sababu walaji wengi wa madini haya ya almasi walikuwa wako katika lock down na kwa jinsi hiyo wakawa wameshindwa kununua almasi na soko la almasi likaanguka. Hata hivi tunavyoongea, ni kweli kwamba soko hili halijatengemaa sana na hivyo linakuwa ni sababu ambazo ziko nje ya uwezo wetu.

Mheshimiwa Spika, napenda kupokea maoni ya Mheshimiwa Mbunge kwamba Wizara ya Madini itakuwa bega kwa bega na kusaidia kuwezesha WDL ili kuweza kupata fedha katika benki zetu.

Mheshimiwa Spika, tukupe tu taarifa kwamba katika siku za karibuni benki zetu za ndani zimepata mwamko mkubwa sana wa kuona kwamba, biashara ya madini ni biashara inayolipa nao wameanza kuwekeza fedha katika sekta ya madini. Hili jambo halikuwa huko nyuma na tukubali kwamba, maisha ni dynamic, maisha yanakwenda, hatimaye benki zetu zimeelewa kwamba wanaweza wakakopesha wachimbaji nao pia wakapata faida na Wizara ya Madini iko nyuma ya Mgodi wa WDL na tunaamini kwamba wataweza kufanikiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, napenda kuongea pia hoja ya Geological Survey ambayo imechangiwa na Wabunge wengi pia, kwamba Geological Survey ndiyo taasisi ya Serikali ambayo inaweza ikafanya utafiti na hatimaye kutoa takwimu na ramani za kuonesha wapi madini yalipo.

Mheshimiwa Spika, napenda kusema tu kwamba pia Serikali imeendelea kutambua umuhimu wa GST. Katika mwaka wa 2020/2021 GST ilipewa fedha maalum kiasi cha shilingi bilioni 3.3 na fedha hizi zilielekezwa katika kuboresha miundombinu ya maabara, vifaa vya ugani, ilipewa magari sita na pia vifaa vya kuratibu matetemeko ya ardhi na vifaa vya jiofizikia. Kwa mtindo huo basi, GST imeendelea kujizatiti kuona kwamba itaendelea kufanya utafiti na kutoa taarifa za awali na kutoa ramani ambazo kimsingi zinapatikana pale GST.

Mheshimiwa Spika, wawekezaji wakubwa wale ambao sasa wanaweza wakaja kuleta taarifa zinazotaka feasibility study wanaweza wakatumia taarifa hizo za awali na wana ramani na hatimaye kuwapa wawekezaji wakubwa ili tuendelee kupata madini mengine yaliyotafitiwa vizuri kama ambavyo Mheshimiwa Mbunge wa Ngara amesema kwa ajili ya Tin, Tungsten, Iron pamoja na madini mengine.

Mheshimiwa Spika, pia katika habari ya utafiti wa GST ni kweli kwamba utafiti katika hifadhi zetu umeshafanyika mahali mahali na hivi tunajua kabisa mahali ambapo kuna madini katika hifadhi za Selous, Rungwa, Moyowosi, Lukwati, Kigosi. Hivyo, Wizara itawasiliana na Wizara ya Maliasili na Utalii ili kuweka utaratibu bora wa kuendelea kutekeleza agizo la Mheshimiwa Rais ili tuweze kufanya uchimbaji katika maeneo haya ya hifadhi huku tukizingatia usalama wa mazingira ya hifadhi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nipende pia kusema kwamba tayari GST imeona umuhimu wa changamoto za wachimbaji wadogo kwama sio wote wanaoweza kufika Dodoma na kuleta sample zao kwa ajili ya kufanya analysis katika maabara. Kutokana na hali hiyo, tayari GST imeanza kupeleka huduma za maabara na jiolojia katika maeneo ya Geita na Chunya kwa kuanzisha ofisi za muda, na zoezi hili litakuwa endelevu ili kuendelea kupeleka huduma katika maeneo ya uchimbaji.

Mheshimiwa Spika, napenda pia niongee hoja iliyoletwa na Mbunge inayohusu helium gas; ni kweli kwamba katika Ziwa Rukwa tunao wingi wa gesi ya helium na wakati mwingine tujue tu kwamba ipo katika hatua ya utafiti wa kina, maana utafiti hadi kufikia uzalishaji lazima upitie hatua. Kwa hiyo tunapoongelea geli ya helium ni kweli kwamba mwekezaji yupo, Kampuni ya Helium One ipo na walishafanya utafiti ule ya preliminary na sasa wapo katika infill drilling. Infill drilling ni kuonyesha kwamba baada ya kuona kwamba mashapo yapo, sasa wanakwenda katika hatua ya kuthibitisha. Sasa wakimaliza hapo ndipo wanapoweza wakaja na feasibility study ambayo sasa ndio itatuonesha jinsi uzalishaji utakavyofanyika.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo ni kweli kwamba helium gas ipo, uzalishaji haujaanza na kabla ya uzalishaji kuanza ni kweli kwamba Wizara itatoa semina elekezi kwa watu wanaozunguka maeneo ya uzalishaji ili kwamba waweze kunufaika na gesi hii ya helium.

Mheshimiwa Spika, pia Wabunge wameongelea juu ya kwamba hatujaanzisha migodi mipya siku za karibuni, ni kweli na kwamba pia tumekuwa na utegemezi sana juu ya madini ya dhahabu; naomba nitoe mfano kidogo ambao unaweza ukaleta perspective katika eneo hili. Tuna Madini ya aina nyingi, makaa ya mawe tani moja ni Dola 45, kilo moja ya dhahabu ni Sh.140,000,000, kwa vyovyote vile wawekezaji watapeleka fedha zao katika madini yanayolipa. Kwa hiyo, kwa msingi huo ndio maana dhahabu imeendelea ku-attract investment kwa sababu ni madini yatakayolipa na kurudisha fedha haraka. Kutokana na hilo ndio maana yameendelea kuchangia kwa wingi katika pato letu linalotokana na madini. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, napenda kuamini kwamba kwa kuingia ubia na Tembo Nickel tukaiingiza aina mpya ya madini katika uzalishaji wa nchi yetu, lakini pia napenda kuamini kwamba Serikali inafanyia kazi utoaji wa leseni mpya mbili siku za karibuni, ambazo ni Mradi ya Nyanzaga uliopo Sengerema kwa Mheshimiwa Tabasam lakini pia na Mradi wa Rare Earth uliopo Songwe. Kwa kuingiza miradi hii pia tutaanza kuingiza maingizo mapya ya uchimbaji na uzalishaji katika nchi yetu…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Ahsante Mheshimiwa Profesa.

NAIBU WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Spika, naomba kuunga hoja mkono. Ahsante sana. (Makofi)
Taarifa ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira Kuanzia Januari, 2021 hadi Februari, 2022 pamoja na Taarifa ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji kwa Kipindi cha Januari 2021 hadi Januari 2022
MHE. PROF. SHUKRANI E. MANYA: Mheshimiwa Naibu Spika, nami nichukue nafasi hii kukupongeza kwa kuchaguliwa kwa kura nyingi kushika wadhifa huo na nikutakie kila la kheri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika Kamati yetu ya Kilimo, Mifugo na Maji napenda kujikita katika hoja ambayo inazungumzia dhana ya muunganiko pamoja na mwendelezo katika utoaji huduma ili kukuza uchumi. Lugha rahisi ni connectivity and linkages.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika sekta ndogo hiyo ya kilimo ya mazao ya bustani, maua, mbogamboga pamoja na matunda; kwanza ni sekta ambayo inakua kwa kasi, imeonekana ikikua kwa asilimia saba kulinganisha na kilimo chote kwa ujumla kikikua kwa asilimia nne, pia kinachotoa ajira nyingi kwa Watanzania na sasa inakadiriwa kwamba at least Watanzania milioni 6.5 katika mnyororo mzima wanashughulika na sekta hiyo ndogo.

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuweka mkazo kwamba sekta hii ndogo ya maua, mbogamboga pamoja na matunda ni sekta ambayo ni logistic sensitive. Ninasema hivi kwa sababu tunahitaji usafirishaji kutoka kwa wazalishaji lakini je, ni wote katika mnyororo ule wanajua kwamba tuna- deal na perishable goods? Je, askari wetu barabarani wanajua kwamba hili ni kontena la maparachichi ambayo yanapaswa yafikie soko mapema? Je, tunapofika kwenye ports kuna handling facilities ambazo zitasaidia kutooza mapema kwa ajili ya bidhaa hizi? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, unagundua kwamba kama hii ni emerging market kwa sasa, lakini je, watu wote katika mnyororo mzima unaotaka tutoe kutoka uzalishaji kufikisha bidhaa yetu sokoni ikiwa katika hali njema wana ufahamu huo? Je, pale Mamlaka ya Bandari tutachukua siku chache kuliko msafirishaji wa copper kwa sababu hizi ni perishable goods? Je, ufahamu huo upo? Je, kuna facilities za ku-handle kwa sababu hiki ni kitu ambacho kinahitaji uharaka?(Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nadhani tunahitaji kuwa na connectivity katika sekta hii kwa sababu tusipofanya hivyo tutagundua kwamba tija yake inaweza isionekane mapema na ndiyo maana huenda hata takwimu za nini tunapeleka nje ya nchi kutoka kwenye hii sekta ndogo imesababishwa na kutokuwa na facilities, lakini wakati mwingine pia kutokuwa na wadau wote kuhusishwa ili tuweze kufikia malengo yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa msingi huo ninapenda kuiomba Serikali pamoja na Wizara husika kwamba tunapokuwa na kitu ambacho ni emerging market kama hii hapa ili tuweze kupata tija maana yake ni kwamba lazima tuwahusishe wadau wote wanaohusika, kwanza kuwapa elimu hiyo, lakini pia kuwapa tahadhari kwamba hebu tusifanye yale mazoea, maana yake ni kwamba tusije tukawa tunachelewesha bidhaa zetu hatimaye zikaoza au zikaharibika ubora kwa sababu tu watu fulani anadhani kwamba anapaswa kwenda kama ambavyo nafanya bidhaa nyingine.

Mheshimiwa Naibu Spika, hii mara nyinge imetokea katika bandari zetu, lakini pia katika airports zetu japo ni kweli kwamba kuna improvement sana kuwepo na standard cold rooms katika airport zetu kwa ajili hiyo, nadhani kwamba bado kunahitaji kuwa na sensitivity juu ya jambo hili ili tuweze kupata tija. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hoja yangu naelewa dakika zangu siyo nyingi niliamua niongelee jambo hili tu kwamba hebu sasa Serikali kwa maana ya Wizara ya Kilimo ijue kwamba wateja wake ni wengi sana, iwape elimu, iwape msukumo ili kwa pamoja kusiwe na vikwazo katika kufikia soko ambalo tunalihitaji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia tuliweka mkazo juu ya yale mashamba ya Arusha ambayo hayafanyi kazi kwa sasa, Serikali ifikie kuleta suluhisho la jambo hilo ili tuweze kupata tija. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana ninaunga mkono hoja. (Makofi)
The Water Resources Management (Amendment) Act, 2022
MHE. PROF. SHUKRANI E. MANYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa nafasi ya kuchangia Muswada ulioko mbele yetu, Muswada wa Sheria ya Usimamizi wa Rasilimali za Maji ya Mwaka 2022. Pia kama sehemu ya Wajumbe wa Kamati tunaunga mkono mapendekezo ya Serikali yaliyoletwa na tungetamani kuona kwamba yale ambayo wanayapendekeza katika Muswada huu, waende kuyasimamia vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu gani tunaunga mkono mapendekezo ya Serikali na pia nitumie nafasi hii kuliomba Bunge lako Tukufu yaani Wabunge waweze kuunga mkono hoja iliyoletwa na Waziri, ni kwa sababu moja mapendekezo haya yanabeba maudhui ya kulinda vyanzo vya maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili ni jambo la msingi sana kama tusipolinda vyanzo vya maji vya asili vilivyopo gharama za kupata maji kwa ajili ya domestic use, lakini pia tunakwenda kupanua mahitaji ya maji katika nchi hii katika kilimo na umwagiliaji, itakuwa shida sana kama vyanzo vya maji havitalindwa. Kwa hiyo ni hoja ya kwanza kwa nini tunaunga hoja mkono, kwa sababu inaenda kuimarisha udhibiti na usimamizi wa vyanzo vya maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme tu kwamba, Wizara iendelee kuongeza jitihada za kuwafikishia maji Watanzania, wakishakuwa wamepata maji kwa ajili ya matumizi, maana yake kuvilinda vyanzo vya maji inakuwa ni rahisi, lakini kama mtu hana maji ya kutumia kwa vyovyote atayatafuta kwa njia anayoiona. Kwa hiyo kuwafikishia wananchi maji ili wapate maji ya kutumia itakuwa pia ni ulinzi kwa vyanzo vya maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kwa nini tuunge hoja mkono? Hoja hii imebeba maudhui ambayo pia wadau wametia maoni yao kwa maana kwamba wadau muhimu katika sekta ya maji pia wamekubaliana na mapendekezo haya na kuweka maboresho yao ambayo Serikali imeyapokea. Vile vile kwa nini tuunge hoja mkono? Ni kwa sababu inapendekeza adhabu na faini kwa mtu au taasisi ambayo itajihusisha na uharibu wa vyanzo vya maji pamoja na kuharibu mfumo wote wa udhibiti wa vyanzo vya maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa katika Kamati msisitizo wetu ulikuwa kuwa, elimu na ushirikishwaji wa wananchi katika ulinzi na usimamizi ndiyo iwe nyenzo kubwa ya ulinzi. Kwa sababu gani tunasema hivi? Kama unapendekeza adhabu na faini lakini mtu hajui kwamba hata anakosa, siyo sawa. Kwa hiyo Serikali yaani Wizara itumie muda wa kutosha kwa vyombo vya habari kwa namna yoyote inayoweza kupeleka elimu na kuwashirikisha wananchi. Huo ndiyo utakuwa ni ulinzi unaojitosheleza, lakini ukienda na nguvu ya adhabu na faini zilizopendekezwa, watu watatoa faini lakini hutakuwa umelinda vyanzo vya maji, kwa hiyo ndiyo maana tukasema kwamba Wizara itoe elimu na iwashirikishe sana wananchi ili wao wenyewe baada ya kupata elimu waweze kuwa ni walinzi wazuri wa vyanzo vya maji na usimamizi utakuwa ni bora.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, watu wengi sana nchini Tanzania tumechimba visima vya maji kwa ajili ya matumizi ya nyumbani, lakini hatukujua kwamba tunahitaji vibali na kwamba kuna faini katika hilo. Ni ukweli usiopingika kwamba katika sasa sijui Kiswahili cha aquifer ni nini, lakini katika aquifer moja ukitoboa mashimo mengi sana ya visima, utaharibu kabisa mfumo wa maji, lakini hatujui. Sasa ndiyo maana kwamba lazima hiyo elimu wananchi waipate, kwamba jamani nyinyi katika mkondo huu hapa mko katika aquifer moja, geological formation ya aquifer moja hatuhitaji visima 20 hapa, la sivyo tutaharibu, elimu hiyo hatuijui, ni lazima tuipate ili tuweze kulinda hivyo vyanzo vya maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati mwingine watu huchimba visima akipata maji katika yale maji ya juu juu ambayo siyo aquifer anaamini amepata maji, baadaye kisima kinakauka elimu hiyo hatuijui. Kwa hiyo ndiyo maana Wizara hii inahitaji kufanya sana uhamasishaji na ushirikishwaji ili hata visima vilivyochimbwa vionekane kwamba vina ubora wa kutosha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, watu pia wamekuwa wakitumia chemchem yao siku zote, Waziri hajawapelekea maji ya bomba, wanaitumia kwa jinsi wanavyoweza, wakati mwingine anamwagilia ili apate kabichi ya kula. Mheshimiwa Waziri asiende akampiga faini mtu yule amweleweshe kwanza na amsaidie namna ya ambavyo atapata maji kwa ajili ya kukidhi mahitaji yake, kwa sababu maji ni hitaji la msingi. Sasa Waziri akifika akampiga faini kwa sababu anatumia maji ya chemchem hajampa maji, nadhani Waziri anaelewa kabisa kwamba maji ni haki ya msingi, anayahitaji kwa matumizi, kwa hiyo tusitangulize faini kabla ya kutoa elimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika ibara ya 13 inapendekezwa Waziri aweze kuanzisha maabara kwa ajili ya ubora wa maji. Hili jambo ni la kupongezwa na Mheshimiwa Waziri atafute vyanzo vya fedha kokote anakoweza kupata aanzishe maabara za kupima ubora wa maji. Kwa nini nadhani kwamba hili ni jambo la msingi? Watanzania wanaotoka baadhi ya maeneo sasa siyo kwamba na-abuse lakini tunaona kwamba wana meno ambayo yana rangi ya kahawia kwa sababu ya fluorine. Mara nyingi tunadhani kwamba hiyo ndiyo athari peke yake ya fluorine nyingi katika maji, lakini florine ikizidi inaleteleza hadi osteoporosis, ugonjwa wa kukonda mifupa inakwenda mpaka kukuharibu joints, inazi-damage fluorine nyingi, lakini watu wengi katika maeneo ambayo tunatoka wanatumia maji, tunaona tu meno yao yamekuwa kahawia tunasema anatoka Singida, huyu anatoka Moshi huyu. Kwa hiyo lazima Waziri aweke maabara ili zipime ubora wa maji kabla ya kutumiwa kwa sababu athari za elements nyingi katika maji ni kubwa zaidi ya zinazoonekana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano wa uchafuzi wa maji ambao ni mbaya zaidi na huwa hatuiongelei ni nitrate. Nitrate inaingia katika maji kutoka kwenye vyoo na maji ya viwandani mara nyingi visima vile vilivyochimbwa vifupi wanatumia yale maji kukiwa na nitrate nyingi sana. Sasa unashangaa kwa nini tuna saratani nyingi na kuna birth defects yaani kizazi kinaharibika kwa sababu ya too much nitrate katika maji. Kwa hiyo water quality laboratories ni za msingi sana ili Watanzania watumie maji ambayo yako quality, tutamsaidia sana Mheshimiwa Ummy Mwalimu kutojadili kwamba vyanzo vya kansa vinatoka wapi kumbe vingine ni kwa sababu ya too much nitrate. Kwa hiyo Water Quality Laboratories ni za msingi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, sera tunajadili Sera ya mwaka 2002 ambapo population ya Watanzania ilikuwa ni 34,000,000 sensa itatwambia lakini tuko almost doubled, sasa una sera ya population ya watu ambao wame-double, yawezekana ikawa haikidhi mahitaji ya sasa. Kwa hiyo tunaomba Wizara iharakishe mchakato wa kuwa na sera mpya ambayo ita- take on both, Dira ya Maendeleo ya miaka 25 mingine, lakini pia kuangalia maendeleo ya kisasa, miji yetu imekua na kila maendeleo mengi yamefanyika Tanzania baada ya miaka hii 20, tupate Sera mpya ya Maji ambayo itakuwa inakidhi mahitaji ya sasa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mchango huo, naunga mkono hoja na tumwombe sana Waziri akayasimamie haya na atafanikiwa sana katika Wizara ambayo amepewa dhamana kuisimamia. Ahsante sana.