Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Answers to supplementary Questions by Hon. Dr. Dorothy Onesphoro Gwajima (1 total)

SPIKA: Mheshimiwa Naibu Waziri hujamsikia swali lake naomba ukae ulisikie tena swali lake. Mheshimiwa Hawa Mchafu nakupa nafasi uulize tena swali lako. Ngoja aulize tena swali ili wamsikie,issue siyo majibu,issue ni kumjibu swali ambalo mtu ameuliza. (Makofi)

MHE. HAWA M. CHAKOMA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa hii nafasi tena. Mheshimiwa Waziri mgao wa fedha wa kununulia madawa kwa mwaka huu wa bajeti tuliokuwa nao, umeenda mara moja tu kwenye vituo vyetu vya afya na zahanati zetu na isitoshe fedha hizo zinakatwa juu kwa juu kwenda kulipa deni sugu lililopo Bohari ya Madawa.Nataka kujua sasa mkakati wa Serikali juu wa ulipaji wa deni lililopo MSD na dawa ziendelee kuwepo katika vituo vyetu vya afya na zahanati zetu.

Mheshimiwa Spika, la pili, wanampango gani kuhakikisha mgao wa fedha unaopangwa kwenda kununulia madawa haukatwi juu kwa juu kwenda kulipia deni?
WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Spika, kwa sababu ni mara yangu ya kwanza kusimama kwenye Bunge lako tukufu kujibu swali naomba kwanza nichukue fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema kwa kuifanya siku ya leo iwepo katika ramani ya mipango yake.

Mheshimiwa Spika, pili naomba kumshukuru sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwa kuniamini na kuona kwamba natosha kuwa sehemu ya chombo hiki tukufu cha kuleta maendeleo katika nchi yetu. Tatu naomba nimshukuru sana familia hususani mume wangu Advocate, wakili msomi Metusela Gwajima Mpenzi wangu sana pamoja na watoto wetu…(Makofi)

SPIKA: Mheshimiwa Waziri, sasa majibu ya maswali ya nyongeza.

WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Spika, Evelyn, Mary Mkubwa, Mary Mdogo na Victoria Gwajima.

Sasa Mheshimiwa Naomba nijielekeze kwenye swali la Mheshimiwa Hawa Mchafu kuhusu dawa.

Mheshimiwa Spika, kweli dawa katika kipindi cha mwaka huu wa fedha zimekwenda mara moja, lakini katika mfumo huu wa sekta ya afya tunapopeleka dawa kutoka MSD, sheria ni cash na carry kwamba ulipe ndiyo upewe hizo dawa, kwa kipindi kirefu vituo vyetu vimekuwa havitekelezi vizuri usimamizi wa cost sharing ile user fees pamoja na bima ili zirejeshe zile pesa huko. Hata hivyo, Serikali imeendelea kupeleka hizi dawa kule kwao, baada ya kuona kwamba wana madeni tukaweka utaratibu kwamba wao sasa wanaruhusiwa kwenda pale MSD wakasaini contract kwamba hizi pesa zisikatwe kwanza tupeleke kule tukafanye ule mzunguko turejeshe. Wengine wamefanya hivyo wanapelekewa hizo dawa kwa utaratibu huo wa makubaliano watalipaje deni, wengine hawafanyi hivyo. Kwa hiyo, nimelipokea, nimelichukua naomba nikawasiliane huko kwenye halmashauri tukaone tatizo liko wapi wa kutekeleza hiyo offer.

Mheshimiwa Spika, kuhusu swali la pili la nyongeza la kwamba tutaendeleaje kuhakikisha kwamba pesa zinaenda na Serikali inaendelea kulipa hilo deni. Serikali inampango na mipango yake ni mipana kuimarisha makusanyo ambayo yamekuwa yakivuja sana kule kwenye hivi vituo, lakini pia kufuatilia matumizi ya zile bidhaa tunazopeleka kule. Hivi sasa ninavyosema kuna timu zetu ziko kule zinafanya ukaguzi. Kwa hiyo, msingi mkubwa hapa ni kwamba tunavitaka vituo viende MSD viingie makubaliano lile deni halitakatwa kiasi cha kuwanyima zile bidhaa zao, watachukua bidhaa tutaendelea kuimarisha ili nao watekeleze sheria ya cash and carry.