Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Ndaisaba George Ruhoro (29 total)

MHE. NDAISABA G. RUHOYO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Napenda kwanza nimshukuru sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri na aliyoyasema yakitekelezeka basi Tanzania ndani ya kipindi cha miaka mitatu itakuwa inaongoza kwa uzalishaji wa kahawa ukiachia Ethiopia, Uganda, Cote d’lvoire pamoja na Kenya.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sasa niulize swali langu la nyongeza.

Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha miche milioni 20 inayotarajiwa kuzalishwa inawafikia wakulima wa Tanzania wakiwemo wananchi wa Wilaya ya Ngara kwenye Tarafa za Kanazi, Nyamiaga, Rulenge pamoja na Murusagamba?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, mwezi Februari mwaka huu tutagawa katika Mkoa wa Kagera kuanzia tarehe 27 Februari, 2021, tutagawa jumla ya miche 1,000,000 kwa wakulima bure. Kwa hiyo hiyo ni sehemu na malengo tuliyojiwekea ni ugawaji wa jumla ya miche milioni 20.
MHE. NDAISABA G. RUHORO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa fursa hii ya kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, liko kundi kubwa sana la wanafunzi wa vyuo vikuu ambao wanakosa mkopo licha ya kuwa na sifa zote alizozitaja Mheshimiwa Naibu Waziri, na baada ya kukosa mkopo hupitisha bakuli maeneo mbalimbali wakichangisha fedha na wanabahatika kwenda vyuo vikuu lakini baadaye wanakatisha masomo yao kwa kushindwa kupata fedha za kuendelea.

Je, Serikali ina mpango gani wa kuwatambua wanafunzi hao ambao wame-drop out na kuweza kuwasaidia ili waweze kuhitimisha elimu yao na kufikia ndoto zao? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyoeleza awali kwamba Serikali tunaendelea na kuongeza wigo wa bajeti ili kuweza kuwafikia walengwa wengi zaidi. Kama nilivyojibu katika jibu langu la msingi, katika mwaka 2020/2021 waliojaza fomu ni zaidi ya 66,000 lakini tulioweza kuwapa mikopo ni 55,000.

Mheshimiwa Naibu Spika, jawabu kwamba kuna zaidi ya wanafunzi 11,000 ambao walikidhi vile vigezo lakini hatukuweza kuwapa. Majawabu ya Wizara kupitia Serikali tunakwenda kuongeza wigo wa bajeti ili kuweza sasa kuwafikia walengwa wengi zaidi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimeeleza hapo mwanzoni kwamba bajeti yetu ya mwaka 2017/2018 ilikuwa ni bilioni
427. Bajeti ya 2020/2021 ilikuwa 464, lakini bajeti yetu ya mwaka 2021/2022 inakwenda kuwa bilioni 500. Tunaamini kwa kadri tutakavyokuwa tunaongeza bajeti yetu itaweza kuwafikia walengwa wengi na vijana wetu wengi wataweza kunufaika na mikopo hii.
MHE. NDAISABA G. RUHORO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii ya kuuliza swali la nyongeza. Changamoto iliyopo Mara ya wazee kutokutibiwa bure ipo kwenye Jimbo la Ngara ambapo hata wale wazee waliokuwa na vitambulisho walinyang’anywa walipofika kwenye vituo vya kutolea huduma za afya:-

Je, Mheshimiwa Naibu Waziri yupo tayari kufika kwenye Jimbo la Ngara kushuhudia namna ambavyo Sera ya Matibabu Bure haitekelezwi kwa hao wazee na kutoa muafaka wa namna nzuri ya hao wazee kupata huduma za matibabu bure? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, Sera ya Matibabu Bila Malipo kwa Eazee inahusika katika mamlaka zote nchini kote, ikiwepo Halmashauri ya Ngara. Kwa hiyo, naomba kwanza nipokee taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Mbunge kwamba katika Jimbo la Ngara kuna baadhi ya wazee wenye vitambulisho walinyang’anywa. Suala hilo halikubaliki na wala siYo maelekezo ya Serikali.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza naomba nimwelekeze Mkurugenzi wa Halmashauri ya Ngara na Mamlaka za Serikali za Mitaa za Ngara kuhakikisha wanalifanyia kazi suala hili mapema. Serikali inaelekeza kutoa vitambulisho vya matibabu kwa wananchi, wazee wenye umri wa miaka 60 na kuendelea wasio na uwezo. Kwa hiyo, hakuna sababu ya kunyang’anya vitambulisho vile kwa sababu ni kuwanyima haki wazee hao ambao sera inawatambua kwamba wanahitaji kupata vitambulisho hivyo kwa ajili ya matibabu.

Mheshimiwa Naibu Spika, niko tayari kufuatana na Mheshimiwa Mbunge kwa ajili ya kulitekeleza hilo, lakini kabla sijaenda, lazima Halmashauri ya Ngara itekeleze maelekezo haya ya Serikali kuhakikisha inaendelea kutoa vitambulisho kwa wazee na hakuna ruksa ya kumnyang’anya mzee yeyote kitambulisho kwa ajili ya matibabu. (Makofi)
MHE. NDAISABA G. RUHORO: Mheshimiwa Spika, ninashukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; kwa kuwa eneo hili la Kabanga Nickel kuna leseni nyingi zimechukuliwa hivi karibuni kuzunguka eneo hili. Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha kwamba leseni hizi zilizochukuliwa hazitazuia uwekezaji wa msingi wa Tembo Nickel?

Mheshimiwa Spika, swali la pili; kwa vile kuna tathmini ilifanyika hapo awali kwa ajili ya kutoa fidia kwa wananchi wanaoishi kuzunguka mgodi huu na kwa vile tathmini hii ambayo ilishafanyika, ilifanyika kipindi kirefu na hivyo imeshapoteza uhalali; je, Serikali ina mpango gani wa kurudia kufanya tathmini ili wananchi wanaounguka Mgodi huu wa Kabanga ambao kwa sasa unaitwa Tembo Nickel waweze kupata fidia? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Ndaisaba, Mbunge wa Jimbo la Ngara, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, uwepo wa leseni zinazozunguka mradi tarajiwa wa uchimbaji wa Tembo Nickel, ni kwamba mtu anapokuwa amepewa leseni ana eneo ambalo lipo katika coordinates na kwa maana hiyo anachimba katika eneo lake na uwepo wa leseni nyingine zozote zinazozunguka eneo la mradi hauna uhusiano wa kuzuia uchimbaji wa mtu aliye na leseni yake. Ni sawa na upangaji tu wa nyumba mtu ana kiwanja chake utaingia nyumbani kwako na mimi nitaingia nyumbani kwangu.

Mheshimiwa Spika, nimhakikishe Mbunge kwamba kuwepo kwa leseni nyingine zozote zilizotolewa siku za karibuni hazitazuia kamwe uchimbaji unao tarajiwa wa mradi wa Nickel.

Mheshimiwa Spika, swali lake la pili ni kuhusu tathmini; ni kweli kwamba tathmini ilishafanyika siku za nyuma na ikipita miezi sita mara nyingi tathmini hiyo kisheria inaonekana kwamba haifai na hivyo inabidi kurudiwa. Katika miradi yote ya uchimbaji mkubwa hakuna mradi ulioanza bila kufanya tathmini na wananchi kulipwa malipo stahiki. Siku zote tunawaelekeza watu hawa wanaofanya miradi mikubwa ya uchimbaji waweze kuwa na social license, kwamba waweze kuwa na mahusiano mazuri na jamii inayowazunguka.

Kwa hiyo tutawaelekeza Tembo Mineral Corporation kwamba warudie kufanya tathmini na walipe fidia ili hatimaye mradi uweze kuanza. (Makofi) Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha kwamba Wananchi wa Jimbo la Ngara wananufaika na uchimbaji wa Madini ya Nickel unaotarajia kuanza katika eneo la Kabanga.
MHE. NDAISABA G. RUHORO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa, Mto Ruvuvu una tabia ya kujaa, hali inayoweza kusababisha kivuko hiki kutofanya kazi, hasa nyakati za masika; na kwa kuwa vivuko hivi vina tabia pia ya kupata hitilafu, hali ambayo inasababisha huduma ya kuvusha wananchi isiwepo. Swali la kwanza; je, Serikali iko tayari kutuletea mtumbwi wa kisasa ili uweze kutoa huduma pindi ambapo kivuko kitakuwa hakiwezi kufanya kazi?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, je, Mheshimiwa Waziri yupo tayari kuambatana na mimi twende kwenye Jimbo la Ngara akashuhudie changamoto zetu za vivuko pamoja na miundombinu mingine, ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza ninampongeza kwa swali lake zuri kwa sababu anatu-alert kwamba tunapojenga vivuko tuweke pia na mitumbwi kama backup ikitokea tatizo tuweze kupata huduma katika maeneo hayo. Naomba nimuelekeze Katibu Mkuu Sekta ya Uchukuzi atume wataalam wetu waende katika eneo hili la Mto Ruvuvu akafanye tathmini tujue aina ya mtumbwi na gharama zake ili tuweze kupeleka huduma hii muhimu katika eneo hili.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Ndaisaba kwamba kwakuwa ni mjukuu wangu nitaenda pale Kagera kutembelea Ngara katika eneo hili baada ya Bunge hili kumaliza Bunge la Bajeti, ahsante.
MHE. NDAISABA G. RUHORO: Mheshimiwa Spika, ninakushukuru sana. Kwa kuwa, ukosefu wa vitalu vya kufugia mifugo na maeneo ya malisho ndio sababu kubwa ya kupeleka mifugo hifadhini na kwa kuwa, elimu inayotolewa na Wizara ya Maliasili inatolewa kwa binadamu na siyo ng’ombe na kwa vile ng’ombe wao wanataka kula majani na wakati wa kiangazi hakuna sehemu ya majani na majani yako porini.

Je, Wizara ina utaratibu gani ama ina mpango gani wa kuhakikisha eneo lile la hifadhi linamegwa, tunapata vitalu kwa ajili ya kufugia mifugo yetu ng’ombe kwa upande wa Biharamulo na Ngara? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Ndaisaba, kama ifuatavyo.

Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba kumekuwa na changamoto ya ukosefu wa malisho na imepelekea kuwepo na migogoro baina ya Wahifadhi na Wafugaji. Serikali inatambua changamoto za ukosefu wa maeneo ya mifugo, lakini kupitia Kamati ya Mawaziri Nane ambao tumekuwa tukizunguka nchi nzima, tayari Serikali imetoa maeneo ambayo yatamegwa kwa ajili ya wananchi kutumia. Hivyo tunaendelea kuelekeza wananchi wayatumie vizuri ikiwemo kutenga maeneo hayo kwa ajili ya malisho na kuandaa matumizi bora ya ardhi kwa ajili ya wafugaji na matumizi kwa ajili ya kilimo. Hivyo, Serikali imeshaliona hili na tumeendelea kutoa elimu lakini pia kumega maeneo ya hifadhi. (Makofi)
MHE. NDAISABA G. RUHORO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Changamoto ya wakulima wa Lupembe kwenye eneo la chai ni sawa na changamoto inayowakabili wakulima wa parachichi kwenye Wilaya ya Ngara. Mathalani upatikanaji wa miche bora ya parachichi, masoko pamoja na bei.

Je, Serikali ina mpango gani wa kuwatambua wakulima wa parachichi Ngara lakini pia na kuboresha zao la parachichi Ngara? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kumjibu Mheshimiwa Ndaisaba, Mbunge wa Ngara kama ifuatavyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza yeye ni mdau wa mazao ya horticulture na amekuwa akishirikiana na Wizara katika maeneo mbalimbali. Pili, parachichi ni moja kati ya mazao ambayo kama Wizara ya Kilimo tunayapa priority kubwa kama ni zao ambalo linaweza likabeba sekta nzima ya mbogamboga na matunda. Nataka nimuhakikishie tu kama ana special case zinazohusu Ngara aje Wizarani tukae, tuweze kutatua kama ambavyo tumekuwa tukitatua matatizo ya wakulima wa chai. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu miche ya parachichi sasa hivi kama Wizara kupitia TOSCI na TARI, tumeanza mpango wa kutambua wazalishaji wa miche binafsi ambao wanazalisha miche ya parachichi na kuwasajili ili kuweza kulilinda zao hili siku ya mwisho lisiweze kujikuta tunaingia kwenye matatizo kama nchi. Kwa hiyo, nataka nimuombe kama ana jambo specific aje tukae tuweze kujadiliana. (Makofi)
MHE. NDAISABA G. RUHORO: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kwa kuwa utekelezaji wa miradi ya maji umekuwa ukitumia wakandarasi; na kwa kuwa wakandarasi hawa wanachukua muda mrefu sana kukamilisha miradi hii ya maji; na kwa kuwa yuko mkandarasi alipewa mradi aumalize ndani ya mwaka mmoja na sasa ni mwaka wa sita unakwenda wa saba hajakamilisha mradi huo; na kwa kuwa mimi nia yangu ni kuhakikisha miradi yote ya maji niliyoshiriki kupitisha fedha Bungeni hapa inakamilika ndani ya kipindi cha miaka mitano. Je, Serikali inaweza kuturuhusu kutumia force account kutekeleza Mradi huu wa Maji wa Ngara Mjini na miradi mingine ili miradi hii ikamilike kwa wakati, tena ndani ya kipindi cha miaka mitano? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Ndaisaba George Ruhoro kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, awali ya yote, napenda kumpongeza sana Mheshimiwa Ndaisaba Ruhoro, amekuwa ni mfuatiliaji na yeye mwenyewe amekuwa akienda mbele zaidi katika shughuli hizi za miradi ya maji. Hata nilipomtembelea pale jimboni, alionesha jitihada kubwa sana ya kuona kwamba miradi inakamilika.

Mheshimiwa Spika, kutumia force account ni moja ya namna ambavyo tunatekeleza miradi yetu sisi Wizara ya Maji. Hivyo, katika miradi hii ambayo imechukua muda mrefu, tayari miradi zaidi ya 100 tumeweza kuruhusu force account na imekamilika. Hivyo na huu nao tunaupokea, tutahakikisha wenzetu waliopo pale Ngara na wao wanafanya jitihada ya kuona mradi unakamilika. Ahsante.
MHE. NDAISABA G. RUHORO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Changamoto iliyopo Manyoni Mashariki ni sawa na changamoto iliyopo kwenye Jimbo la Ngara ambapo Serikali ilituahidi miaka 15 iliyopita kutujengea barabara ya Murugarama, Rulenge na Rusahunga kilomita 85 kwa kiwango cha lami. Kwa masikitiko makubwa miaka 15 iliyopita hakuna kilichofanyika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujua sasa: Ni lini; kwa maana ya dakika, saa, siku, mwezi na mwaka ambapo Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi itaanza kujenga barabara yetu kwa kiwango cha lami?

Mheshimiwa Mwenyekiti, Naibu Waziri alikuja mwaka 2021, tukaahidi wananchi kwamba barabara hii inaenda kuanza kujengwa kwa kiwango cha lami. Naomba niambiwe saa, siku, mwezi na mwaka ambapo barabara hii inaanza kujengwa kwa kiwango cha lami.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GEOFREY G. MSONGWE): Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Ndasaba, Mbunge wa Ngara kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli nilitembelea Jimbo la Ngara na moja ya eneo ambalo tulilitembelea ni hii barabara. Naomba nimhakikishie Mheshimiwa Ndaisaba, Mbunge wa Ngara, pamoja na wananchi wa Ngara kwamba dhamira ya Serikali bado ni kuijenga barabara hii kwa kiwango cha lami.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Mbunge atakubaliana nami kwamba bajeti tunayoendelea kuitekeleza tulitenga fedha. Kwa hiyo, mara fedha itakapopatikana, ujenzi wa barabara hii utaanza kwa kiwango cha lami. Ahsante. (Makofi)
MHE. NDAISABA G. RUHORO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kuniona, lakini pia na kwa kutoa fursa nyingi kwa Waheshimiwa Wabunge kuuliza maswali mengi ya nyongeza, tunakushukuru sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ilitenga fedha kwa ajili ya kujenga minara tisa ya mawasiliano kwenye Jimbo la Ngara. Naomba kuiuliza Serikali ni lini ujenzi huu wa minara tisa utaanza ili kutatua changamoto ya mawasiliano kwenye jimbo la Ngara? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Ndaisaba, Mbunge wa Ngara kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kabisa Serikali ilitangaza kujenga minara tisa katika Jimbo la Ngara katika awamu iliyopita iliyokuwa imetangazwa. Lakini naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, Mheshimiwa Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, mwezi huu anakwenda kusaini mkataba wa ujenzi wa minara 90 ambayo ni pamoja na minara ambayo itakuwa hapo katikati Jimbo la Ngara.

Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge awe na subira ili Mheshimiwa Waziri akishakamilisha jambo hili tayari utekelezaji utaanza mara moja. Ahsante.
MHE. NDAISABA G. RUHORO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa fursa ya kuuliza swali la nyongeza. Naomba kuuliza Serikali ni lini italeta fedha za awamu ya pili kuwezesha ujenzi wa hospitali ya Wilaya ya Ngara?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Ndaisamba, Mbunge wa Jimbo la Ngara, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, hospitali ya Wilaya ya Ngara ilipelekewa shilingi Milioni 500 mwaka wa fedha uliopita na nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tunajenga hospitali zetu hizi kwa awamu, sasa tunakwenda awamu ya pili ambapo katika mwaka wa fedha huu hospitali hii pia imetengewa Shilingi Milioni 500 na zitakwenda wakati wowote ndani ya mwaka huu wa fedha.
MHE. NDAISABA G. RUHORO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana kwa fursa hii ya kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuiuliza Serikali ni lini itaisaidia Wilaya ya Ngara kuweza kujenga stendi mpya na ya kisasa? Ahsante.
NABU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Ndaisaba George, Mbunge wa Ngara kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, anachotaka kujua tu ni lini tutawasaidia kujenga stendi mpya na naamini kwamba moja ya miradi ya kimkakati katika Halmashauri nyingi ni pamoja na kuwa na stendi mpya. Kwa hiyo, kama Halmashauri yake itakuwa imewasilisha andiko maana yake kazi kubwa ambayo tunaifanya sasa ni kutafuta fedha, mara tutakapopata fedha maana yake ujenzi huo na wenyewe utaanza. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. NDAISABA G. RUHORO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. Kwa kuwa maeneo yote aliyoyataja hayana vituo vya Polisi: Je, Mheshimiwa Naibu Waziri yupo tayari kutupatia gari liendelee kuimarisha ulinzi eneo hilo huku tukiwa tunasubiri kujengwa kwa vituo hivyo? Hilo ni namba moja.

Mheshimiwa Spika, swali la pili; kwa kuwa eneo la Ngara liko mpakani na changamoto ya ulinzi na usalama ni kubwa, Mheshimiwa Naibu Waziri yuko tayari kuambatana nami tukaone changamoto hizo sambamba na kutatua mgogoro wa Rusumo Magereza na wananchi wa kijiji cha Magereza? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Ruhoro kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kuhusu kusaidia gari kwa ajili ya kuimarisha usalama na ulinzi wa raia na mali zao, kama ilivyojibiwa siku tatu zilizopita na Mheshimiwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi hapa, Wizara kweli itapata magari 78 mwishoni mwa mwezi huu ambapo tathmini itafanyika kuona Halmashauri yenye changamoto kubwa iweze kuzingatiwa ikiwemo Halmashauri ya Wilaya ya Ngara na hasa ukizingatia iko mpakani.

Mheshimiwa Spika, kuhusu kuambatana naye, niko tayari kuongozana naye wakati wowote nafasi itakapopatikana hususan baada ya Bunge hili ili kuweza kuona changamoto zake na kuzifanyia kazi. (Makofi)
MHE. NDAISABA G. RUHORO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana kwa kunipa fursa ya kuuliza swali la nyongeza.

Kwa kuwa, uwanja wa ndege wa Ruganzo umejengwa muda mrefu umechoka na sasa unahitaji ukarabati. Na kwa kuwa, sasa Ngara imefunguka, wageni ni wengi, Nickel inatakiwa kuchimbwa na biashara mpakani imeshamiri.

Je, ni lini Serikali itakuja kukarabati uwanja wa ndege wa Ruganzo?
NAIBU WAZIRI UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Ndaisaba, Mbunge wa Ngara kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba suala lake limepokelewa na tunajua wageni wengi wanaenda Ngara ambapo ni mbali kutoka viwanja vyote vya ndege ambavyo viko karibu. Kwa hiyo, suala lake tumelichukua na Serikali itatafuta fedha ili kuweza kukikarabati kiwanja hiki ili wageni na watu mbalimbali waweze kufika kwa urahisi kwa ndege katika Wilaya ya Ngara.
MHE. NDAISABA G. RUHORO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana.

Kwanza naishukuru Serikali kwa kuweza kutupatia fedha hiyo na ujenzi unaendelea. Ila sasa kwa kuwa fedha hii inakuja kwa mafungu ya shilingi milioni 500, na kwa kuwa fedha inayotakiwa kukamilisha ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Ngara ni shilingi bilioni tatu na zaidi.

Je, Serikali ipo tayari kuongeza muamala kutoka shilingi milioni 500, mpaka shilingi bilioni moja ili tuweze kujenga hospitali yetu kwa wakati na tuimalize? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Ndaisaba George Ruhoro, Mbunge wa Jimbo la Ngara kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli, kama alivyosema Mheshimiwa Mbunge Mheshimiwa Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan ameendelea kupeleka fedha kwenye Halmashauri hii ya Ngara kwa ajili ya ujenzi wa hospitali. Tayari wana bilioni moja; shilingi milioni 500 bado hawajaanza kuitumia. Kwa hiyo nimhakikishie kwamba mara watakapotumia fedha hiyo kwa wamu ya pili, Mheshimiwa Rais na Serikali yetu itaendelea kupeleka fedha hiyo ili kuhakikisha Hospitali ya Halmashauri ya Ngara inakamilika.
MHE. NDAISABA G. RUHORO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa fursa ya kuuliza swali la nyongeza kwa niaba ya wananchi wa Jimbo la Ngara. Jimbo la Ngara ni miongoni mwa majimbo ambayo bado yana kata hazijawahi kuona hata nguzo moja ya umeme. Mathalan kata ya Bugarama, Keza, Kibogora pamoja na Muganza wananchi hawa hawajafikiwa na miundombinu ya umeme. Naomba sasa kuiuliza Serikali, je, ni lini wananchi wangu hawa watapelekewa huduma ya umeme? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ndaisaba George Ruhoro, Mbunge wa Jimbo la Ngara, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, maeneo yote ya kata na vijiji ambayo hayajapata umeme yako katika mpango wa REA awamu ya tatu, mzunguko wa pili ya upelekaji wa umeme katika maeneo hayo na mradi huo tunatarajia mwishoni mwa mwaka huu uwe umekamilika. Ni kweli kuna maeneo yamesuasua kwa muda mrefu katika upelekaji wa umeme na Mkoa wa Kagera ikiwa ni mmojawapo. Tumechukua jitihada za makusudi za kukaa na Wakandarasi hao na kuwasimamia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba katika muda mfupi sana ataona Wakandarasi wakirudi kwenye maeneo hayo kuweza kufanya kazi na kutimiza ndani ya muda na tulipeana hadi muda mfupi wa miezi mitatu kuhakikisha maeneo ambayo hayajafikiwa kabisa sasa miundombinu imefika. Kwa hiyo tutapeana taarifa na Mheshimiwa Mbunge ya ufikaji wa Mkandarasi kwenye maeneo hayo na utekelezaji wa mradi kwa mujibu wa mkataba.
MHE. NDAISABA G. RUHORO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa fursa hii ya kuuliza swali la nyongeza. Naomba sasa Serikali inijibu, ni kwa nini mkandarasi wa REA Ngara amepotea site, haonekani kwa takribani kipindi cha miezi mitatu? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ndaisaba, Mbunge wa Ngara, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, awamu ya upelekaji wa umeme vijijini iko na awamu tofautitofauti, kama nilivyosema kwenye jibu la msingi kuna upembuzi yakinifu, ku-survey yake maeneo, uagizaji wa vifaa na hatua ya mwisho ya uwekaji wa miundombinu yenyewe. Maeneo hayo na mazingira hayo ya hatua hizo yanaweza kufanya mkandarasi asionekane site kwa muda na hasa pale anapokuwa kwenye hatua ya kuagiza vifaa. Naamini maeneo mengi wengine vifaa vimefika, wengine bado, kwa hiyo sehemu ambapo hajafika, naamini itakuwa labda alichelewa kwenye kuagiza vifaa, lakini vifaa vitafika, kwa sababu maelekezo yetu ni kabla ya Desemba mwaka huu miradi iwe imekamilika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi hii kuwaelekeza wakandarasi wote kuendelea na kazi katika site zao kulingana na schedule walizoziweka na vifaa vilivyopo ili tuweze kufikia deadline ya Desemba kuweza kufikisha umeme kwenye maeneo hayo.
MHE. GEORGE N. RUHORO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa fursa ya kuuliza swali la nyongeza. Jimbo la Ngara bado lina kata nyingi hazina vituo vya afya, je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha tunapata vituo vya afya kwenye kata hizo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA- (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Ndaisaba George, Mbunge wa Jimbo la Ngara kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali imeshafanya tathmini na kuainisha maeneo ya kimkakati ya kujenga vituo vya afya ikiwemo katika Kata za Jimbo la Ngara.
MHE. NDAISABA G. RUHORO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana; pamoja na majibu mazuri ya Naibu Waziri mimi nina maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza, mkandarasi wa mradi huo wa Kabanga hajalipwa fedha zake kwa mwaka mzima. Naomba kujua ni sababu gani zimesababisha mkandarasi huyu asilipwe fedha yake kwa mwaka mzima?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; naomba kujua, Wizara ya Maji na Serikali wana mfumo wa kuweza ku-track status ya miradi ya maji ili kuepukana na changamoto hizi za miradi kusimama na mkandarasi kutokuwa site kwa mwaka mzima? Naomba kupata majibu ya Serikali ya maswali hayo mawili.
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Ndaisaba George Ruhoro, Mbunge wa Ngara kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza niendelee kuwaomba tu wakandarasi ambao wanaidai Serikali kwamba kwa sasa Serikali imeshaanza kulipa na tayari fedha zimeshaanza kupelekwa katika maeneo husika. Kwa hiyo wakae mkao wa kupokea fedha hizo ili waweze kuendelea na kazi ambazo ziko katika site hizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye upande wa strategy, tunaamini kwamba lengo la Serikali ni kumtua ndoo mama kichwani, na strategy mojawapo ni kuhakikisha huduma ya maji inawafikia wananchi kwa ukaribu zaidi. Hivyo nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba kwa kuwa Serikali imeshaweka mikakati mahususi ya kuhakikisha maji haya yanawafikia wananchi tutaendelea kusimamia kwa ukaribu zaidi ili miradi hii iweze kukamilika na wananchi waweze kupata huduma iliyo bora.
MHE. NDAISABA G. RUHORO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa fursa ya kuuliza swali la nyongeza. Naomba sasa kuiuliza Serikali swali la nyongeza. Je, Wizara ya Kilimo ina mkakati gani wa kuhakikisha wakulima wa kahawa wa Wilaya ya Ngara wanaendelea kuuza kahawa yao kwa bei nzuri kama ilivyokuwa kwenye msimu uliopita? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, nimpongeze Mbunge kwa kazi nzuri ambayo anaifanya kwenye zao hili la kahawa, nataka tu nimhakikishie kwamba utaratibu ambao tulioanza nao ulimpa mkulima bei nzuri, tutaendelea nao. Vilevile tutahakikisha kwamba tunamsaidia mkulima kupata masoko ya uhakika na azalishe kahawa yenye ubora ili iweze kumpatia bei nzuri sokoni. Kwa hiyo nimwondoe hofu Mheshimiwa Mbunge kwamba wakulima wa kahawa Mkoa wa Kagera na maeneo mengine wataendelea kunufaika na utaratibu ambao tumeuweka hivi sasa.
MHE. NDAISABA G. RUHORO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana, kwa kuwa Serikali ilikuja kujenga miundo mbinu ya umwagiliaji kwenye bwawa kwenye Bonde la Bigombo liliko Ngara mwaka 2013 na kwa kuwa Serikali ilitelekeza bwawa hilo na miundombinu yake mwaka huo huo wa 2013;

Je, ni upi mkakati wa Serikali wa kuja kujenga lile bwawa na kulikamilisha?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, nimesikia kilio cha Mheshimiwa Mbunge juu ya mradi wa scheme ya Bigombo ambayo ameutaja. Namwelekeza Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji na timu yake nzima kwenda kuliangalia bwawa hilo na scheme hiyo ili kujua changamoto iliyopo tuweze kuitatua. Kwa hiyo nimwondoe hofu Mheshimiwa Mbunge, timu yangu itaelekea huko kwenda kuangalia,
lengo letu ni kuhakikisha kwamba wananchi wetu wanafanya kilimo cha umwagiliaji.
MHE. NDAISABA G. RUHORO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Nimefurahishwa na majibu ya Serikali nina swali moja la nyongeza. Kwa kuwa eneo lile la Rusumo limewahi kukumbwa na majanga ya moto hasa eneo lile ambalo bwawa lenyewe limejengwa. Na kwa kuwa ulipotokea moto tulilazima kuomba ndege ya kuzima moto kutoka Taifa Jirani. Ni upi mkakati wa Wizara wa kuhakikisha tunakuwa na gari la zimamoto ili kulinda miundombinu yetu tuliyowekeza pale, pale itakapotea majanga ya moto kama ilivyotea huko nyuma? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nishukuru kwa niaba ya Serikali kwa kufurahishwa na majibu haya na ukamilikaji wa mradi. Nimpongeze Mheshimiwa Mbunge kwa kufatilia mradi wote lakini hasa suala la kuzima moto. Nimuahidi Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali inalichukua tunaamini mradi utakapo kamilika kuna serving ambayo itatafanyika. Tutahakikisha basi tunawashawishi ili waombe katika mahitaji yao muhimu ya matumizi ya ile pesa itakayobaki.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia katika Miradi ya CSR ambayo itaanza kufanyika baada ya mradi kukamilika tutawashauri pia walilete kama moja wapo ya hitaji lao ili tuweze kulifanyia kazi na Serikali itahakikisha kwamba linafanyika kwa ajili ya ku–safe guard maisha ya watu wanayo tumia maeneo hayo.
MHE. NDAISABA G. RUHORO: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Ninaomba kumuuliza Mheshimiwa Naibu Waziri kwamba ni kwa nini Serikali wanaendelea kufanya utafiti wa mbegu za asili ambazo zimetukuza wote mpaka hapa tulipo badala ya kuzalisha kwa wingi na kuzisambaza? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, katika majibu yangu nimezungumza kwamba tayari Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu pale Arusha wanayo benki na wanaendelea kuzitunza mbegu hizi kwa ajili ya usambazi. Kwa hiyo, zoezi la usambazi na kwenye kilimo utafiti haukomi vitakwenda sambamba lakini mwisho wa siku ni kuhakikisha kwamba mbegu hizi zinawafikiwa wakulima kwa wakati. Kwa hiyo, mamlaka inafanya kazi hiyo vilevile utafiti hauwezi kukoma kwa sababu ni kila siku mambo mapya yanajitokeza.
MHE. NDAISABA G. RUHORO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Serikali kupitia Wizara ya Kilimo mradi wake wa DASP walifika Ngara mwaka 2015, wakaanza kujenga Skimu ya Umwagiliaji ya Vigombo, wakaitelekeza ikiwa imefika katikati kwa zaidi ya miaka nane iliyopita. Je, ni lini Wizara ya Kilimo itafika Ngara na kuja kukamilisha Mradi wa Skimu ya Umwagiliaji ya Vigombo? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, ni dhamira ya Serikali kuhakikisha miradi yote ya umwagiliaji inakamilika na ndiyo maana tumewekeza fedha nyingi kwa ajili ya ukarabati na kuipitia. Nichukue fursa hii kumuahidi Mheshimiwa Mbunge ya kwamba nitampa maelekezo Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji aelekee katika eneo la Rulenge pale Vigombo ili aangalie mradi huu na tuone namna ya kuweza kuwakwamua wananchi ili wafanye kilimo cha umwagiliaji.
MHE. NDAISABA G. RUHORO: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Serikali iliahidi kujenga minara ya mawasiliano kwenye Kata ya Bugarama na Kata ya Kibogora lakini kazi haijaanza hadi sasa. Ni lini Serikali itakuja Ngara kwenye Kata hizo kujenga minara ya mawasiliano? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Ndaisaba George Ruhoro Mbunge wa Ngara kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, mwenyewe na Mheshimiwa Ndaisaba George Ruhoro tulishatembelea jimbo lake na tulizunguka katika maeneo yote ambayo yana changamoto ya mawasiliano na baada ya kugundua changamoto hiyo Serikali ikaingiza katika mpango wa utekelezaji.

Mheshimiwa Spika, katika mpango huo wa utekelezaji, tayari watoa huduma wameshapatikana lakini utoaji wa huduma hii una mchakato kidogo unaposaini, lakini kuna masuala ya vibali kwenda kupata ardhi kuingia mikataba na wenye ardhi, lakini nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba maeneo haya kwa kuwa Serikali imeshaahidi hakuna eneo ambalo litaachwa bila kujengwa mnara, ahsante sana.
MHE. NDAISABA G. RUHORO: Mheshimiwa Spika, ahsante sana pamoja na majibu mazuri ya Serikali ninayo maswali mawili ya nyongeza.

Swali la kwanza; kwa kuwa kuna Wakandarasi wengi wamesaini mikataba na Serikali hasa mikataba ya ujenzi; na kwa kuwa Mikataba hiyo imeathiriwa sana na mabadiliko makubwa ya viwango vya kubadilisha fedha za kigeni hasa dola za Kimarekani. Je, Serikali ina mkakati gani wa kuwasaidia Wakandarasi hawa ili wasishindwe kutekeleza miradi hiyo hasa miradi ya ujenzi?

Mheshimiwa Spika, swali la pili; kwa kuwa mabadiliko ya viwango vya kubadilishia fedha za kigeni kabla hatujapitisha bajeti ya nchi ilikuwa shilingi 2,350, hiyo ni dola ya Kimarekani na sasa ni shilingi 2,500 hadi shilingi 2,600 na mabadiliko haya yameathiri bajeti ya nchi tuliyoipitisha hapa Bungeni hasa kwenye maeneo ambapo Serikali inahitaji kununua bidhaa nje ya nchi.

Je, Serikali ina mkakati gani wa kuinusuru bajeti yetu tuliyoipitisha hapa Bungeni ili iweze kutekelezeka vizuri? Ahsante sana. (Makofi)
WAZIRI WA FEDHA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa maswali mazuri aliyouliza Mheshimiwa Ndaisaba; kuhusu swali la kwanza ambalo linahusisha Wakandarasi ambao watakuwa wameathirika na mabadiliko ya bei za kubadilishia fedha huku Mikataba yao ikiwa imeshasainiwa, nimwombe Mheshimiwa Mbunge na niwaombe Wakandarasi wa aina hiyo kufanya engagement, kufanya mashauriano na sekta zinazohusika kwa sababu masuala ya kimkataba ni ya sekta kwa sekta ili jambo hili liweze kusogelewa kwa umahususi wake katika eneo husika.

Mheshimiwa Spika, tunazo taarifa katika baadhi ya miradi ambako tayari walishafanya mashauriano ya aina hiyo kutokana na mabadiliko haya ambayo yalikuwa yanajitokeza ya kiuchumi. Kwa hiyo hata hawa ambao watakuwa wamekumbwa na jambo hilo, ni vizuri kufanya majadiliano katika maeneo husika.

Mheshimiwa Spika, kuhusu jambo la pili la kunusuru bajeti, Serikali inachukua hatua ambapo mpaka hivi sasa tumefanya utaratibu wa kuona namna ambavyo tunaweza tukabana matumizi ya ndani ya Serikali hasa katika maeneo ya matumizi ya kawaida ili kuweza kutoa fursa miradi ya wananchi isiathirike. Hilo ndiyo lilikuwa agizo la Mheshimiwa Rais kuhakikisha kwamba, tunafanya utaratibu wa kuangalia matumizi ambayo siyo ya lazima ili fedha ambayo inapatikana iweze kutekeleza miradi ya maendeleo ili bajeti ya miradi ya maendeleo isiathirike.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Rais ameendelea kutuongoza katika baadhi ya maeneo kuweza kuhakikisha kwamba tunapata fedha nyingi za kigeni ili ziweze kupunguza tatizo la uhaba wa dola ndani ya nchi na kuruhusu uhimilivu ama ustahimilivu, uimara wa bei ya kubadilishia fedha na uimara wa shilingi yetu ya Tanzania. (Makofi)
MHE. NDAISABA G. RUHORO: Mheshimiwa Spika, ninakushukuru sana, nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, kwanza nashukuru Serikali, majibu ni mazuri sana. Sasa swali la kwanza, kwa kuwa ujenzi umefanyika kwa muda mrefu na sasa kuna cracks nyingi zimetokea pale. Je, Wizara iko tayari kwenda kufanya ukarabati eneo lile ili uzinduzi utakapofanyika eneo lile liwe linafaa kwa ajili ya mnada, swali la kwanza.

Mheshimiwa Spika, swali la pili, naomba kukuuliza Mheshimiwa Waziri uko tayari kuambatana na mimi baada ya Bunge hili twende pale Ngara, Murusagamba tukazindue huo mnada? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana; cha kwanza nimuondoe hofu Mheshimiwa Mbunge kwamba pamoja na kwamba mnada umekamilika na hayo mapungufu machache ambayo Mheshimiwa Mbunge ameainisha tutayarekebisha kabla ya kuzindua na mimi niko tayari kwenda mara baada ya Bunge lako tukufu kuahirishwa, ahsante sana.
MHE. NDAISABA G. RUHORO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa fursa ya kuuliza swali la nyongeza. Kwa kuwa Kata ya Nyamagoma ni miongoni mwa Kata za Wilaya ya Ngara ambazo hazina shule ya sekondari. Je, ni lini Serikali itaanza ujenzi wa Shule ya Sekondari ya Nyamagona? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana, naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Ndaisaba George, Mbunge wa Jimbo la Ng’ara, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Kata ya Nyamagona ipo katika mpango ambao tunakwenda kujenga katika mwaka wa fedha unaokuja. Kwa hiyo nimwondoe shaka kwamba itajengwa katika mwaka wa fedha unaokuja wa 2022/2023.
MHE. NDAISABA G. RUHORO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana, kwa kuwa kivutio chetu pekee cha maporomoko ya Rusumo sasa kimepunguza mvuto baada ya uwekezaji wa mradi wa umeme pale Rusumo, Serikali haioni kuna haja sasa ya kuisaidia Ngara kuendeleza vivutio vingine ili Ngara isiondoke kwenye ramani ya kupata watalii, ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, nakushukuru naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ndaisaba kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Kivutio cha Rusumo siyo kivutio pekee kilichopo katika ukanda huu tunazo mbuga za wanyama zilizoko katika ukanda huu. Vilevile, kama nilivyosema kwenye jibu langu la msingi tunaangalia kutumia uwepo wa mradi wa umeme kuufanya kama sehemu ya kivutio. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba katika kuendeleza utalii katika ukanda huu tutaunganisha vivutio vingine vyote vilivyopo ili Sekta ya Utalii iweze kunufaisha ukanda huu na nchi yetu kwa ujumla.