Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Ndaisaba George Ruhoro (3 total)

Hotuba ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyoitoa wakati wa Ufunguzi wa Bunge la Kumi na Mbili, Tarehe 13 Novemba, 2020
MHE. NDAISABA G. RUHORO: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii. Nami nianze kuwashukuru wananchi waJimbo la Ngara kwa kunichagua kwa kishindo kikubwa na siku ya leo nipo hapa Bungeni kama Mbunge miongoni mwa Wabunge wa Bunge la Kumi na Mbili. Vilevile naomba nishukuru Chama changu Cha Mapinduzikwa kuniteua, bila Chama Cha Mapinduzi kuniteua leo hii nisingekuwepo hapa.

Nimesoma sana kwa umakini mkubwa hotuba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ukiondoa vitabu vya dini kwa maana ya Biblia, hii hotuba ya Mheshimiwa Rais ni Biblia yangu ya pili. Ukiangalia namna hotuba hii ilivyopangiliwa maudhui yaliyomo utagundua kabisa ndiyo maana Taifa letu linasonga mbele kwa sababu Jemedari wetu Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania yuko vizuri na mipango ipo vizuri.

Mheshimiwa Spika, naomba nichangie hotuba ya Rais kwenye maeneo matatu: Eneo la kwanza ni kuwezesha wananchi kiuchumi; eneo la pili, ni ufugaji; na eneo la tatu, ni upande wa sekta za maji, umeme pamoja na barabara.

Mheshimiwa Spika, naomba nianze na sehemu ya kwanza ya uwezeshaji wananchi kiuchumi. Ukisoma hotuba ya Mheshimiwa Rais ukurasa wa11 imeelezea kwamba kuna mifuko ya kukopesha wananchi zaidi ya 18 na mifuko hiyo inaonekana haileti tija kwa sababu ya gharama za kuendesha mifuko hiyo, suala la uratibu, lakini ukiangalia na namna ya kupima matokeo inaleta changamoto kunapokuwepo na mifuko mingi.

Mheshimiwa Spika, ukisoma hotuba hiyo ukurasa huo wa11 utaona kuna ombi ambalo linamwomba Mheshimiwa Waziri Mkuu kuangalia uwezekano wa kuunganisha mifuko hii ili iweze kuleta tija kwa Watanzania. Mimi mwenyewe nilisikia baadhi ya mifuko kwa mara ya kwanza alipokuwa anaisoma Mheshimiwa Rais. Nataka nikueleze Watanzania hawajui hii mifuko tena ukiangalia, Mheshimiwa Rais amesema kwenye hotuba yake hapa kwamba mikopo hii ni ile isiyokuwa na riba na ile yenye riba nafuu.

Mheshimiwa Spika, hata sisi Wabunge tungependa kwenda kukopa kwenye mifuko hii tukaachana na kukopa hadi kwenye gratuity za kwetu, naomba niiombe Serikali hasa Ofisi ya Waziri Mkuu iweke utaratibu mzuri kwanza wa utoaji taarifa kwa Watanzania juu yahii mifuko. Vile vile iweke utaratibu mzuri hii mifuko iweze kusaidia wananchi na wananchi wote nchi nzima waweze kupata taarifa sahihi za mifuko hii na utaratibu wa kuweza kupata fedha kutoka kwenye mifuko hii ya kuwezesha wananchi kiuchumi.

Mheshimiwa Spika, naomba niende kwenye upande wa ufugaji na hapa najikita kwenye kitu kinaitwa uhimilishaji, huduma ya uhimilishaji ni huduma inayomfanya mfugaji ahamuwe muda na siku ambapo na siku ambapo mfuko wake utapata mimba, huduma ya uhimilishaji inamwezesha mwananchi kupanga akitaka ng’ombe wake apate mimba kesho yake anamwita Daktari wa Mifugo, anaweka homoni pale anaweka mbegu na ng’ombe wake anapata mimba.

Mheshimiwa Spika, huduma hii inaweza kumfanya mfugaji kuamua idadi ya mifugo anayoitaka kila mwaka na hivyo tunaweza kuzalisha mifugo mingi na hivyo kukuza uchumi wa kaya moja moja na Taifa kwa ujumla. Naiomba Serikali kwenye eneo hili la uhimilishaji iweze kutenga fedha za kutosha kununua zana za uhimilishaji na kupeleka Madaktari wa Mifugo kwenye chuo kilichopo Arusha kinachofundisha masuala ya uhimilishaji ili kuweza kuleta tija kwenye eneo hili la ufugaji.

Mheshimiwa Spika, naomba niende kwenye upande wa miundombinu hasa specifically kwenye sekta za maji, umeme pamoja na barabara. Jimboni kwangu na maeneo mengine nimesikia Watanzania wengi sana wanalalamika hasa vibarua pamoja na kampuni za Kitanzania zinazofanya kandarasi kama sub-contractors na makampuni ya nje. Mimi mwenyewe nimewahi kuwa sub kwenye tenda ambayo walipewa Wajerumani. Nataka nieleze wazi kwamba tunapigwa sana kwenye eneo hili, mzungu anasaini mkataba wa dola milioni tatu anakupatia kazi kama sub tunafanya kazi yote asilimia 98, inapokuja kwenye malipo kipindi kingine anatuzungusha, kipindi kingine bargaining power inakuwa ni ndogo na hata kipindi kingine Watanzania tunadhulumiwa.

Mheshimiwa Spika, achilia mbali sisi ambao niConsultants, njoo upande wa vibarua takribani maeneo mengi sana nchi nzima, wananchi vibarua wanalia. Hapa ninaombi kwa Serikali hasa kwenye idara zote hizi upande wa sekta ya maji, umeme na barabara, naomba Wizara ziweke utaratibu mzuri wa wananchi hawa wa Tanzania kulipwa moja kwa moja kutoka kwenye Wizara husika. Tukifanya hivyo, Watanzania watalipwa moja kwa moja na ile dhuluma ambayo tunadhulumiwa haitakuwepo, ni suala la Serikali kuweka utaratibu mzuri, mkandarasi mkubwa anatoa taarifa kwa aliyetoa kazi za vibarua ama aliyefanya naye sub-contractors, then Serikali inalipa moja kwa moja, tunadhulumiwa sana kwenye eneo hili.

Mheshimiwa Spika, mwisho kabisa,naomba nieleze changamoto iliyopo kwenye upande wa barabara. Barabara nyingi hasa za mjini ni chafu kwa maana ya kwamba zimejaa mchanga. Utaratibu uliopo wa kusafisha barabara nimeshindwa kuelewa vizuri, nilikuwa najiuliza, barabara inajengwa nzuri ya lami lakini baada ya muda mfupi unakuta michanga imejaa na kaeneo ka kupita ni kadogo katikati ya barabara na ile michanga inamomonyoa barabara. Naomba Serikali iangalie utaratibu mzuri iuandae wa kusafisha hizo barabara kutoa michanga kwenye lami. Najiuliza jukumu la kusafisha barabara wakipewa TAMISEMI, akapewa Mheshimiwa Jafo, mtaa husika ukahusika kusafisha zile barabara ile michanga itaondoka maeneo yale na barabara zitakuwa safi.

Mheshimiwa Spika, zile barabara za mijini zilizotengenezwa kwa gharama kubwa hata ukipita wewe jaribu kuchungulia kwenye kioo cha gari yako utakuta michanga imesogea kabisa mpaka inataka kumaliza barabara.

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja. Ahsante sana.(Makofi)
Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2021/2022 – 2025/2026
MHE. NDAISABA G. RUHORO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Miaka Mitano. Naomba nianze kwa pongezi. Wapo Mawaziri wanne ambao wamegusa maisha ya wananchi wa Jimbo la Ngara na ninapenda nitumie nafasi hii kuweza kuwapongeza. Naomba kumpongeza Mheshimiwa Prof. Adolf Mkenda na Mheshimiwa Hussein Bashe kwa kugusa maisha ya wananchi wa Jimbo la Ngara.

Mheshimiwa Naibu Spika, nilipomwomba Mheshimiwa Prof. Mkenda miche ya michikichi ndani ya siku saba, alituma watu wa TARI, walifika Ngara na kuotesha vitalu vya miche ya mchikichi. Ahsante sana. Nilipoomba miche ya kahawa, Mheshimiwa Hussein Bashe ndani ya mwezi mmoja amenipatia miche 300,000 na wananchi wangu wa Jimbo la Ngara wameshaipanda. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, speed hii ya Wizara ya Kilimo ni speed ya dream-liner naomba muweze kuindeleza. Vile vile, naomba nimpongeze Mheshimiwa Dorothy Gwajima pamoja na Mheshimiwa Godwin Mollel kwa kuendelea kuimarisha huduma za afya na hasa kwa kufika kwenye jimbo langu la Ngara na kuhakikisha kwamba changamoto zile za ukosefu wa madawa wamezifanyia kazi na sasa zile simu nilikuwa ninapigiwa kwamba hakuna madawa kabisa kwenye vituo vya kutolea huduma za afya, zimepungua. Ahsanteni sana kwa kuja Ngara, naomba kazi mnayoifanya ya kuboresha huduma za afya muweze kuendelea nayo na mtu yeyote asiwakatishe tamaa, mimi na wananchi wa Jimbo la Ngara nipo pamoja nanyi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimalizie kwa kumpongeza Mheshimiwa Maryprisca na Mheshimiwa Aweso kwa kuja Ngara pia kugusa maisha ya wananchi wa Jimbo la Ngara. Walikuja Ngara na wakati Mheshimiwa Maryprisca anafika pale, alikuja na barua mkononi ambayo ilikuwa na taarifa za kupewa kibali cha kuruhusiwa kujenga mradi wa maji mpya ambao unaenda kutatua matatizo ya maji kwenye Mji wa Ngara Mjini pamoja na viunga vyake. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kuwapongeza Waheshimiwa Mawaziri hao waliogusa maisha ya wananchi wa Jimbo la Ngara, naomba niseme kwamba Wizara yote itakayotugusa kabla sijaendelea na mchango, nitakuwa nawapongeza hapa hivyo, nikija kuwaomba msaada kutokea Ngara Waheshimiwa Mawaziri, basi ujue kabisa kwamba ukinisikiliza haraka haraka utakula pongezi ndani ya hili Bunge. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niende moja kwa moja kwenye eneo la kilimo na ninaomba nichangie kwenye upande wa kilimo cha zao la alizeti. Mahitaji ya mafuta ya kula Tanzania kwa mwaka mmoja tunaitaji metric tani 400,000 mpaka 500,000 za mafuta ya kula. Uwezo wa kuzalisha mafuta ya kula kama Taifa ukijumlisha michikichi, alizeti na kadhalika, tunazaliza metric tani 200,000 mpaka 250,000 kwa mwaka. Hii inafanya tuweze kuagiza mafuta nje ya nchi kwa kutumia fedha za Kitanzania zenye dhamani ya Dola za Kimarekani milioni 80. Tunatumia fedha hii wakati Watanzania wapo na wana uwezo wa kulima alizeti na hayo mazao mengine tukazalisha mafuta ya kula hapa nchini.

Mheshimiwa Naibu Spika, Watanzania tuko tayari kuzalisha mafuta ya kutosheleza mahitaji ya Taifa. Wapo wakulima wa kutosha, wako wasindikaji wa mafuta ambao kwa Mkoa wa Manyara peke yake, nikitolea mfano, kuna viwanda vya kukamua na kusindika mafuta ya alizeti 234; na kwenye Jimbo la Ngara kipo kiwanda kimoja ambacho ni changu mwenyewe na chenyewe kina uwezo wa kuzalisha mafuta ya kula ya alizeti yanayotosheleza wakazi wa Jimbo la Ngara. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, changamoto kubwa inayofanya tushindwe kuzalisha mafuta ya kula ya kutosha, ipo kwenye upatikanaji wa mbegu bora ya kisasa. Taasisi za utafiti za Tanzania tulizonazo hazijawahi na sijui kama wana mpango wa kuanza uzalishaji wa mbegu bora ya alizeti aina ya high breed. Teknolojia wanayoitumia kwa sasa kuzalisha mbegu ya alizeti inaitwa Open Pollinated Varieties (OPV), maana yake wanazalisha mbegu yenye daraja la kati ambayo haiwezi kuzalisha mafuta ya kutosha kutosheleza mahitaji ya nchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mantiki hiyo, naomba nitumie nafasi hii kuweza kumwomba Waziri wa Fedha kufanya mambo yafuatayo; kaka yangu Mheshimiwa Mwigulu, mwana wa Nchemba, naomba utusaidie mambo yafuatayo: moja, Wizara yako isaidie kulinda viwanda vya ndani hususani vile vinavyomilikiwa na wasindikaji wadogo, viwanda vya kati na vile vidogo hususani kwa kuzielekeza mamlaka, hasa TRA kujitafakari inapokwenda kwenye viwanda hivi na kuviathiri kupitia makusanyo ya kodi kwenye usajili, lakini pia na kodi za ukaguzi.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia zipo mamlaka nyingine zinazoathiri viwanda hivi vidogo vidogo. NEMC, hitaji la kufanya Environment Impact Assessment ambalo linataka ukiwa na kiwanda uweze kutoa shilingi milioni 10, hiyo una- depots benki, umekopa huku kuanzisha kiwanda; hii nayo inatuathiri kwenye viwanda vidogo vidogo. Hivi vitu Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Mipango viangaliwe ili athari inayopatikana kutokana na vitu hivyo ipunguzwe ili viwanda hivi viweze kufanya kazi vizuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la pili ambalo ni muhimu, ninaomba Vituo vya Utafiti vya Serikali vya Mbegu viwezeshwe ili vianze kuzalisha mbegu bora za kisasa. Narudia tena kwa msisitizo na herufi kubwa, VITUO VYA UTAFITI VYA SERIKALI VIWEZESHWE KUZALISHA MBEGU BORA ZA ZAO LA ALIZETI ZA KISASA MBEGU ZA HIGH BREED.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye soko, mbegu la zao la alizeti inanunuliwa shilingi 35,000/=. ukienda Mbeya Vijijini, ni mwananchi gani ana uwezo wa kumudu gharama hii ya mbegu shilingi 35,000/= kwa kilo moja? Hayupo! Ndiyo maana mimi kule kwenye Jimbo langu la Ngara nimenunua mbegu na nikatoa mikopo nikawagawia wakulima. Ninaomba watu wa kilimo waje wajifunze, tume-pilot na inaenda vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine ambalo ni muhimu sana ninaiomba Wizara ya Fedha iweze kusaidia Pamoja na Wizara ya Kilimo ni utolewaji wa mikopo ya mbegu kwa wakulima. Wakulima wawezeshwe kununua mbegu ili waweze kupanda zao la alizeti kwenye mashamba yao.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika hali ya kawaida, mwananchi ana shamba lake amelilima, mbegu sokoni inauzwa shilingi 35,000/=, hata kama tukiwezesha kwenye Taasisi zetu za Utafiti, sidhani kama itashuka shilingi 10,000/=. Bila kumwezesha mkulima huyu kwa kumpatia mkopo aweze kununua ile mbegu na kupata nguvu ya kupalilia shamba zima na baadaye kuvuna, hawezi kulima mashamba makubwa kibishara. Hivyo wakulima wawezeshwe.

Mheshimiwa Naibu Spika, tukifanya hayo mambo matatu tutakuwa tumepata faida zifuatazo: moja, tutawezesha Watanzania kupata mbegu za kutosha tena mbegu bora za zao la alizeti, ambapo endapo tutawezesha Taasisi zetu za Utafiti kuzalisha; na hii haina chenga chenga.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama hatuwezi kutenga fedha za kuwezesha taasisi zetu zizalishe mbegu ya kisasa na badala yake tukawa tunasubiria Mataifa ya nje ambayo yana kampuni zao zinazozalisha mbegu za kisasa, wao ndio waje watuuzie, tena wanatupiga kweli kweli, kilo moja shilingi 35,000/=; bila hivyo tutakuwa hatujawatendea haki wananchi wangu wa Jimbo la Ngara, Shubi pamoja na Wahangaza na Wasukuma wa Nyamagoma pamoja na Wahaya wa Benagu. Tutakuwa hatujawatendea haki wananchi wa Dodoma wanaolima alizeti, Wagogo pamoja na wengine wa Singida, Wanyiramba na kadhalika.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kufanya hivyo, tutapunguza gharama ya kununua mbegu ya zao la alizeti sokoni iliyopo kwa sasa. Kama tutawekeza kwenye viwanda vyetu vya kuzalisha mbegu, tutawezesha upatikanaji wa chakula cha mifugo cha kutosha. Yale mashudu yanatumika kwa ajili ya kulishia mifugo.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. NDAISABA G. RUHORO: Mheshimiwa Naibu Spika, namalizia.

NAIBU SPIKA: Kengele ya pili imeshagonga Mheshimiwa.

MHE. NDAISABA G. RUHORO: Mheshimiwa Naibu Spika, namalizia kabisa sekunde tano.

Mheshimiwa Naibu Spika, tukiwekeza hivi kwa kuwezesha taasisi zetu tunaenda kuondoa tatizo la mafuta kwenye nchi yetu ndani ya kipindi cha miaka miwili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, naunga mkono hoja. (Makofi)
Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022
MHE. NDAISABA G. RUHORO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi nami ya kuchangia kwenye Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nijikite kwenye vitu vitatu na vyote viko kwenye eneo la kilimo. Nitatumia lugha mchanganyiko. Eneo la kwanza ni effective utilization of labour force, post-harvest loss na productivity kwenye agriculture.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikija kwenye effective utilization of labor force; ukiangalia Tanzania majority age group ni vijana ambao ndiyo tunawategemea waweze kuzalisha. Hawa vijana kama ambavyo nimechangia mchana wakati mzungumzaji alipokuwa anachangia pale walio wengi ni wale waliomaliza kidato cha nne, wengine darasa la saba na wengine wametoka vyuo vikuu. Hawa vijana kama nilivyokuwa nimegusia mwanzoni wanaposikia shughuli za kilimo, ufugaji, iwe ni kulima ni kama vile hiyo kazi ni ya watu fulani ambao sio wao wenyewe. Kwanza wanaumia, hawako tayari kwenda kufanya hizo kazi, kwa hiyo kama Taifa hatuja-harness vizuri ile nguvu ya wale vijana katika kuzalisha mali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, angalia China, Wachina wanafanya kazi kama nyuki, angalia Vietnam, Vietnam wanafanya kazi kama nyuki, njoo Tanzania. Saa tatu kamili za asubuhi, mtu ameshatoka shambani yuko nyumbani amekula kishoka. Saa nne kamili za asubuhi tayari ameshakunywa aina ya maji, ameshaanza kuchangamka mpaka saa sita anazungumza Kiingereza. Matokeo yake kama Taifa hatujanufaika vizuri na matumizi ya nguvu za vijana katika kuzalisha ili tuweze kupata mafanikio tunayoyataka kama Taifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, matokeo ya haya, vision na mission tuliyonayo kama Taifa huko tunakoelekea kwa spidi, sisi tunaelekea huku, wananchi ambao ni wazalishaji tumewaacha huku. Hivyo kama Taifa nina ushauri sasa, kwenye eneo hili la matumizi sahihi ya nguvu kazi za vijana kwenye kujenga Taifa nashauri mambo yafuatayo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, pendekezo la kwanza, vileo vipigwe marufuku kuuzwa na kunywewa mida ya kazi. Ni rahisi sana, kama Mheshimiwa Waziri Mkuu alisimama akakataza viroba na vikapotea, vivyo hivyo katazo linaweza likatolewa wananchi wakabaki wanakunywa muda wa weekend.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pendekezo la pili, nashauri turejeshe mfumo wa kufundisha vijana wetu uzalishaji wakiwa shuleni, nenda sekondari, ukienda sekondari mwanafunzi anasoma kuanzia form one hadi kidato cha sita hajawahi ku-practise ufugaji wala kilimo. Naishauri Serikali kwenye Mpango huu unaokuja wa miaka mitano turejeshe haya mashamba darasa kwenye shule zetu. Hawa ambao wameshamaliza muda wao umepita tuwaache, lakini hawa ambao wako kwenye shule zetu tuwafundishe kulima na tuwafundishe ufugaji. Wale watakaobahatika kuendelea na Vyuo Vikuu, wataendelea. Wale ambao hawatabahatika waweze kuona hizi shughuli za kilimo kama sehemu ya ajira.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nihamie upande wa kuongeza uzalishaji (increasing productivity). Tanzania tumebahatika kuwa na mito, mabonde na ardhi nzuri yenye rutuba. Eneo linalolimwa ni dogo, mkuu wa kaya ambaye mara nyingi ni baba, unakuta kwenye kaya zetu ukienda vijijini hata hapa Dodoma mtu amelima nusu eka, amelima eka moja, ana vimbuzi viwili nyumbani, akiongeza na ng’ombe watatu amemaliza, watu wameridhika. Hii kasi tuliyonayo sisi kama Serikali kwamba watu tufanye kazi people are relaxing, hawana haraka, ameridhika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naishauri Serikali, kupitia mifumo iliyopo ya kuhudumia na kusimamia maendeleo tutoe maelekezo. Tutoe target kwa kila mkoa, wilaya na kijiji, ili familia zote za vijijini ziweze kuzalisha. Badala ya kulima eka moja au mbili ziweze kuwa eka nyingi ili nguvu ya Serikali inayoenda kuwekezwa kwenye kilimo iweze kuonekana ndani ya kipindi cha miaka mitano. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la post harvest loss sijaweza kulizungumzia, ila niseme tu kwamba naunga mkono hoja. Ahsanteni sana. (Makofi)