Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Jerry William Silaa (2 total)

Hotuba ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyoitoa wakati wa Ufunguzi wa Bunge la Kumi na Mbili, Tarehe 13 Novemba, 2020
MHE. JERRY W. SILAA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii kuchangia hotuba ya Rais aliyoitoa Bungeni akifungua Bunge letu hili la Kumi na Mbili.

Kwanza na mimi kwa sababu ni mara ya kwanza, nitumie fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa fursa mimi kuwa mmoja wa Wabunge wa Bunge lako hili tukufu. (Makofi)

La pili, nikishukuru Chama changu cha Mapinduzi, chama ambacho nimekitumikia kwa zaidi ya nusu ya uhai wangu, kwa kunipa fursa, namshukuru sana Mwenyekiti, navishukuru vikao vya uteuzi na wanachama wenzangu.

Mheshimiwa Spika, naomba kuungana na wenzangu kuunga mkono hoja, lakini vilevile naomba sana kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa hotuba hii iliyobeba dira na maelekeo ya nchi yetu kwa miaka mitano. Hotuba hii ukiisoma na ile ya Bunge la Kumi na Moja, ukisoma utekelezaji wa Ilani, ukisoma machapisho mbalimbali ya taarifa ya uchumi, utaona jinsi gani Rais wetu amefanya kazi kubwa kwa miaka mitano, tunampongeza sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, maeneo ya uchumi, uchumi wa nchi yetu umekua, Pato la Taifa limekuwa, mfumuko wa bei umekuwa uko katika hali nzuri, haujazidi asilimia 4.4, akiba ya fedha za kigeni kwa mara ya kwanza iko juu na inaendelea kuongezeka, thamani ya shilingi imeimarika sana, pongezi kubwa kwa Rais wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika huduma za jamii, kazi kubwa imefanyika, vituo vya afya, zahanati zimejengwa nchi nzima na tumeona kwenye hotuba hii tunayoijadili.

Mheshimiwa Spika, lakini labda kwa kifupi sana ni kuomba Bunge lako tukufu kwamba tuna kazi kubwa baada ya kumpongeza Rais kumsaidia ili malengo aliyoyaweka kwenye miaka hii mitano yatimie na katika kumsaidia wote tuna wajibu wa kumsaidia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wa kwanza ni wasaidizi wake, na bahati nzuri tunaye Waziri Mkuu mchapakazi, mpenda watu, anafikika na Waheshimiwa Wabunge mtakuwa ni mashahidi. Lakini wako wasaidizi wake wengine, watendaji wa Serikali nao wanafanya kazi nzuri, tumeanza vizuri. Sisi kule Dar es Salaam katika Jimbo langu la Ukonga, Mkurugenzi wetu Jumanne Shauri na watendaji wenzake wanatupa ushirikiano. Ingawa hatuwezi kuacaha kusema wako watendaji ambao inabidi wabadilike kuendana na kasi ya Rais wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, binafsi sina taabu na wewe na ninaamini Wabunge wenzangu hawana shida na wewe, tunafahamu kasi yako. Tumeona juzi hapa Mawaziri walivyokuwa wanajibu maswali ukisimamia Serikali kutoa majibu yanayoendana na shida za wananchi. Niwaombe Wabunge wenzangu, sisi tuna kazi kubwa ya kusaidia Mheshimiwa Rais kufikia malengo haya ya miaka mitano. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Wabunge hawa wamefanya kazi kubwa ya kampeni. Ukiingia hapa asubuhi Wabunge wengi wakiweka sura zao zile mashine zinakataa, siyo kwamba mashine ni mbovu ila sura walizokuja nazo hapa Novemba siyo sura walizonazo leo. (Makofi/Kicheko)

Tumefanya kazi kubwa, Waheshimiwa Wabunge wengine hapa wameosha vyombo, wengine wamepaka rangi kucha, tunayoyasema hapa ndiyo reflection ya matatizo ya wananchi wetu kule tunakotoka, tunaomba tusikilizwe na Waheshimiwa Wabunge, niwaombe tuseme, na wasiposikia tuwafokee. Tufoke kwa niaba ya wananchi tunaowawakilisha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mimi niliwahi kuwa mmoja wa watu tuliokuwa tunaishauri Serikali kuanzisha TARURA. TARURA imekuja kuondoa matatizo ya urasimu ule wa kihalmashauri wa ujenzi wa barabara, ilikuja kuleta tija kwenye utendaji wa kihandisi, lakini matokeo yake, tulianza vizuri na mameneja wa TARURA wa wilaya, akawa kuna coordinator wa mkoa, leo kumetengenezwa Meneja wa Mkoa, Mhandisi wa TARURA yule Meneja wa Wilaya amegeuka kuwa karani. Hana fedha, hatafuti zabuni, hamlipi mkandarasi, nimshukuru Mheshimiwa Jafo ameanza kulifanyia kazi. (Makofi)

Tulileta jambo lile…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa Jerry Silaa.

MHE. JERRY W. SILAA: Mheshimiwa Spika, naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)
Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022
MHE. JERRY W. SILAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nitoe shukrani kwa kunipa nafasi kuchangia kwenye Mpango wa Serikali wa Miaka Mitano na wa mwaka mmoja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niipongeze Serikali,k hotuba ya Waziri ameonesha kazi kubwa iliyofanyika kwa miaka mitano. Tunaipongeza sana Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukisoma rasimu hii ya Mpango wa Miaka Mitano, naomba kuchangia kwenye Sura ya Tano; 5.4.10 ukurasa wa 102 kwenye miundombinu ya barabara. Kwenye miaka mitano iliyopita kazi kubwa sana imefanyika kwenye miundombinu ya barabara. Nchi nzima barabara zimejengwa, madaraja yamejengwa na sisi wa Dar es Salaam tumeona ujenzi mkubwa wa miundombinu kwenye Daraja la Mfugale, Ubungo interchange na interchange zingine zinaendelea kujengwa pale Chang’ombe na ujenzi unakaribia kuanza pale Morocco na maeneo mengine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukisoma Rasimu hii ya Mpango inaonesha jinsi gani Serikali imejipanga kwa miaka mitano hii inayokuja kukamilisha ujenzi wa barabara za lami lakini vilevile kuondoa msongamano wa magari katika majiji. Mimi naamini Waheshimiwa Wabunge watakubaliana na mimi kwamba unapoongelea mafanikio haya makubwa ya miudnombinu mikubwa ya barabara lazima uoanishe na barabara za ndani ambazo ndiyo zinamhudumia mwananchi katika maeneo yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, unapozungumzia barabara hizi za mijini na vijijini, unaizungumzia TARURA. Naomba sana kuishauri Serikali kwamba lazima kwenye mpango huu kuwe na mipango inayotekelezeka ya kuisaidia TARURA iweze kutatua changamoto ya miundombinu kwenye maeneo yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo wakazi wa Jimbo la Ukonga tunamshukuru Rais, ile foleni ya TAZARA pale haipo tena. Hata hivyo, leo wakazi wangu akiwemo Mheshimiwa Waitara, akishavuka TAZARA kutoka pale Banana kuitafuta Kivule ama Kitunda kuna kazi kubwa sana. Ukienda TARURA mfumo mbovu lakini na fedha hazitoshi. Leo Dkt. Ndumbaro na wakazi wenzake wa Majohe atavuka vizuri TAZARA lakini nyumbani hapafikiki. Simu zetu hizi ukiona simu yoyote inatoka maeneo hayo unaanza kuomba dua. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kifupi yako mambo mawili ambayo Serikali ikijipanga vizuri itafikia malengo haya yaliyowekwa kwenye Rasimu ya Mpango. La kwanza, ni muundo wa TARURA. Tulianza vizuri, tulikuwa na Regional Coordinator na na Meneja wa Wilaya. Kazi ya Meneja wa Wilaya ilikuwa ni kutekeleza miradi ya barabara kule kwenye Wilaya na Majimbo yetu. Hata hivyo, mfumo umebadilika, tumemgeuza yule Regional Coordinator amekuwa Regional Manager na yule Manager wa Wilaya sasa hata ile kazi aliyokuwa anafanya ya kulipa wakandarasi wanaofanya kazi kwenye maeneo yake imehamishiwa mkoani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo kumpata mkandarasi wa kufanya kazi Nachingwea anatafutwa Lindi Mjini, mazingira haya ni tofauti sana. Huwezi ukampata mtu kufanya kazi Ngara kwa kumtafutia pale Bukoba Mjini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimshukuru Mheshimiwa Waziri ameliona hili kwenye ziara zake, ameahidi kuanza kulifanyia kazi na mimi naomba kuishauri Serikali. Ili Mpango huu uweze kutekelezeka lazima tuwe na muundo wa uhakika wa TARURA. Yule Meneja wa Wilaya awezeshwe, aweze kupata wakandarasi, fedha zifike, aweze kusimamia miradi yake na aepuke kuwa karani wa kutujibu sisi maswali yetu Waheshimiwa Wabunge ambayo hana utendaji wake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakii la pili, ni fedha. Ipo dhana na naendelea kuliomba Bunge lako na Serikali ijenge dhana ya kusikiliza michango ya Wabunge kwa sababu Waheshimiwa Wabunge hawa wanayoyasema hapa siyo mawazo yao ni mawazo ya wananchi wanaowaongoza. Ipo dhana kwamba ukiongeza tozo ya barabara kwa mfano, leo Bunge likashauri kuongeza tozo ya barabara za mjini na vijijini kwenye mafuta, iko dhana kwamba gharama ya usafirishaji itaongeza. Leo kwa miundombinu isiyopitika kwenye maeneo yote ya pembezoni ya mijini na vijijini ya nchi yetu gharama za usafirishaji ziko juu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo mwananchi wa kule Majohe Bomba Mbili kuitafuta Mombasa analipa nauli Sh.700 mpaka Sh.1,000. Naamini barabara ya uhakika ingejengwa leo kungekuwa na daladala zinatoka kuanzia Bomba Mbili mpaka Kariakoo na gharama ya usafirishaji itashuka badala ya kuongezeka kwa kuongeza tozo kwenye mafuta. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Waziri anapokuja ku-wind up Mpango na wewe mwenyewe umesema kwamba Mpango huu ni Rasimu, basi mawazo haya tunayoyatoa yaweze kuchukuliwa kwa uzito na yahusishwe kwenye Mpango huu wa miaka mitano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, iko miradi ya TASAC, miradi ya DMDP Phase II, kule kwetu ni kizungumkuti, inasemekana imekwama kwenye maamuzi kwenye meza za watendaji wa Serikali lakini matatizo kule chini ni makubwa sana. Ni vyema tunavyotengeneza Mpango ukaongeza na kasi ya utendaji kwa watendaji wetu hasa kwenye miradi hii inayowagusa wananchi wa hali ya chini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, katika dhana hii hii ya kusikilizwa na leo wewe nikupongeze kwenye swali lile la Mheshimiwa Gambo asubuhi lazima Serikali ijifunze kusikiliza yale yanayosemwa na Waheshimiwa Wabunge. Ukiingia sasa hivi kwenye mitandao comments za wananchi wa Arusha wanaoathirika na utalii wanasikitishwa sana na majibu yale yaliyotolewa na Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nirudie kuiomba Serikali hii sikivu kwa sababu tunafahamu jinsi gani Rais wetu alivyokuwa msikivu, tunaona anavyotatua matatizo ya wananchi kule anakopita, tuombe na Mpango huu na wenyewe ujipange katika kutatua matatizo ya wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naskuhukuru sana, naunga mkono hoja. (Makofi)