Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon Toufiq Salim Turky (3 total)

Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022
MHE. TOUFIQ SALIM TURKY: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Awali ya yote, naomba nimshukuru Mwenyezi Mungu Subhana Wataala kwa kunijalia kufika hapa, lakini pia kumtakia Rehema mzee wangu aliyekwishakutangulia mbele ya haki Mheshimiwa Salim Turky, Mr. White. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia naomba nichukue fursa hii nikishukuru chama changu, Chama cha Mapinduzi kwa kuona ninafaa na kuweza kuwakilisha wananchi wetu wa Jimbo la Mpendae. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi naomba nianze na kuunga mkono hoja, kwa kweli Mpango huu ni mpango kazi. Kusema kweli nchi yetu inavyoelekea imetuletea hamasa kubwa mno ndani ya miaka mitano hii. Mheshimiwa Rais wetu kafanya makubwa sana, ile hamasa imekuja mpaka Visiwani. Kwa mara ya kwanza katika historia CCM kushinda kwa asilimia 74 Zanzibar, imeonesha kwa namna gani Awamu ya Tano ilivyofanya kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika suala la uchumi, nataka kuongelea masuala mawili tu, hatuwezi kuongelea uchumi kama hatuongelei mtaji. Mtaji tukisema inaingia katika masuala ya ajira, lakini muhimu sana namna gani unaweza kuipata ile capital.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika suala la ajira tunatafuta ajira milioni 8, namna gani tutazipata hizi ajira? Ni kwa kupitia private sector lakini pia watu kuweza kujiajiri wenyewe. Tukitizama mabenki yetu wanawapatia mtaji matajiri zaidi kuliko wanyonge, sasa namna gani wale wanyonge wanaweza kupata mtaji?

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tuitazame katika taswira mbili; uchumi wa pande hizi mbili uko tofauti, tukifuata uchumi wa Bara uko tofauti na wa Zanzibar. Zanzibar kitu gani tunaweza tukafanya ambacho kinaweza kusaidia kwa pande zote mbili, kupitia Benki Kuu (Bank of Tanzania), tunaweza tukaongeza wigo wa kuanzisha offshore banking. Hii off shore banking itasaidia vipi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia visiwa vyote vilivyoendelea duniani, mfano Singapore, Dubai, Hongkong, Mauritius, Panama masuala yote wanayofanya ni offshore banking, wanahakikisha watu wanaleta fedha ndani ya nchi zao. Sasa zikipatikana zile hela ndipo yale mabenki wanakuwa na excess funds za kuweza kuwapatia wajasiriamali wadogowadogo watakuwa na appetite. Sasa kwa kwa nini tusianzishe offshore banking katika kusaidia uchumi wa Zanzibar lakini BoT ikawa ni msimamizi mkuu kupitia Bank of Tanzania branch ya Zanzibar? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili ni kuhusu Zanzibar kuendelea katika real estate. Uchumi wa visiwa ni fedha na real estate, hiyo ndiyo ukitizama karibu visiwa vyote vilivyoendelea. Sasa tukitizama katika suala la real estate kuna changamoto moja kubwa nayo ni suala la immigration. Dubai leo ukitaka kununua nyumba zaidi ya milioni 1 Dirham, sawasawa na Dola 270,000 unapatiwa resident permit ya miaka mitatu. Leo kuna nyumba ya Dola 600,000 imejengwa pale na Mzee Bahresa, wako wengine wamejenga hata resident permit ya mwaka mmoja hupati. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ukitizama ule mradi wametumia tayari almost 150 million dollars, lakini hauwezi ku-take off. Miradi ya namna ile iko mingi sana Zanzibar. Zanzibar kuendelea ni suala zima la tourism na real estate, sasa ni namna gani tunaweza kusaidia? Tunaweza kutizama katika wigo huo, namna gani immigration kupitia Zanzibar ikawa na wigo fulani sasa wa kuwawezesha Wazanzibar kule katika uwekezaji wao. Tutaweka cealing, mtu aki-invest dola laki tatu anaweza kupata resident permit, pengine inamruhusu kubakia Zanzibar au akitaka kuja mpaka Bara kuwe na namna fulani ya kuweza kuwekeza watu wasiweze kutumia vibaya ile mianya ya uwekezaji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini ni muhimu sana tufanye hivyo kama kweli tunataka maendeleo yafanyike, hususan kwa uchumi wa Zanzibar. Tukitizama rasilimali zetu sisi zaidi ya uchumi wa blue ambapo tunaongelea bahari ni mdogo mno tofauti na Bara; kuna rasilimali watu, rasilimali nguvu na minerals. Kwa hivyo, naombeni sana tulitizame suala hili na muhimu suala la BoT kwenda offshore na immigration hususan katika masuala ya resident permit. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja asilimia mia moja. Ahsanteni sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. TOUFIQ SALIM TURKY: Mheshimiwa Spika, awali ya yote, naomba nichukue fursa hii nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujalia Mwezi huu Mtukufu wa Ramadhan tungali sote salama. Pia tuwatakie rehema waliotutangulia mbele za haki wazee wetu hususan Hayati Rais mpendwa wetu Magufuli.

Mheshimiwa Spika, haijapata kutokea mabadiliko ya Serikali ya namna hii na sisi wananchi na Serikali kwa ujumla, sote tukawa kitu kimoja. Lazima tumshukuru Mwenyezi Mungu Subhanah-Waatalah. Pia na Waheshimiwa wengine tukawa tunajiuliza, Hayati Dkt. Magufuli Waziri Mkuu alimtolea wapi? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa kweli katika kubarikiwa huku, tumebarikiwa kupata kiongozi aliyekuwa mtumishi mtiifu mno. Katika kubadilika kwa Serikali hii, kiungo kikubwa bado kingalipo. Kwa hiyo, tuendeleeni, ilikuwa Bunge hili hili tukampitisha kwa kura zote kabisa, kwa heshima zote kabisa, kwa hiyo, tuendelee kushikamana na Serikali yetu kuhakikisha uchumi wetu unaendelea kuwa mbele. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tumwombee sana Rais wetu wa sasa Mheshimiwa Mama Samia Suluhu Hassan, Mwenyezi Mungu ampe hekima, busara na maono (maana viongozi huwa wanapata maono) yale ya kuipeleka Tanzania yetu mbele kama waasisi wa nchi hii walivyokusudia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, napenda sana kuongelea kwa uchache katika suala zima la uwekezaji. Uwekezaji hauwezi kupatikana ndani ya nchi yetu kama elimu hatujaipa kipaumbele. Hivi karibuni nilipata bahati ya kwenda Kenya nikakaa na viongozi wa pale, katika masuala waliyokuwa wanaongelea wakasema Tanzania sisi tunaionea wivu sana, kwa sababu wana rasilimali za kila aina kuliko sisi; lakini sisi tuna rasilimali moja ambayo Afrika nzima hawana, ni rasilimali nguvu watu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, literate level ya Kenya ni 93%. Vile vile elimu yao wanasema ni tofauti na elimu ya watu wengi sana. Afrika watu husoma kwa ku-pass, sisi tunasomesha vijana wetu kwa kufahamu. Mara nyingi sana, ndiyo maana utaona Tanzania hapa tuna ma-degree, wengine wana Masters, wengine Ma-professor, lakini inapokuja katika uelewa na katika suala zima la dunia inavyoenda, exposure ni tofauti. Attitude yetu iko mbali. Ndiyo maana katika suala zima la uwekezaji, watu wanatafuta ma-expatriates. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niliona Wabunge tunavutana sana katika suala la kwa nini tunachukua watu kutoka nje? Hakuna mtu anataka kutoa gharama mara tatu, mara nne, mara tano kuwalipa watu wa nje na wakati Watanzania wapo, lakini bado vijana wetu wako nyuma mno kielimu. Tunafanyaje sasa katika suala hili? Ni lazima turudi tena, tutazame namna gani tunaweza kuwasaidia wanafunzi wetu kuhakikisha wanaendana na matakwa ya dunia ya sasa? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Armania ni Eastern Europe Country, sasa hivi kuanzia Darasa la Sita wanafundisha subject ya coding; masuala ya software. Miradi yote karibu sasa hivi watu wanasema tunataka sisi tuwe na mfumo, lakini mifumo yote inatoka nje ya nchi. Hizo ndio ajira za baadaye. Watu duniani wanakadiria, ndani ya miaka 10 ijayo akili zetu zitakuwa hazifanyi tena kazi, itakuwa ni suala zima la artificial intelligence. Vijana wetu tumewatayarisha vipi kuhakikisha ajira za baadaye hatuzikosi? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ajira za mwanzo zilikuwa za viwanda, tunatafuta watu wa kulima. Ajira za pili zikaja kuwa ni masuala mazima ya vibarua kwa ajili ya viwanda. Ajira za tatu zimekuja katika kutengeneza viwanda. Ajira zijazo ni namna gani dunia itaenda ki-ICT only; Artificial intelligence? Vijana wetu tuwatayarisheni katika ajira za baadaye. Hizo milioni nane zitakuwa ndoto. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022
MHE. TOUFIQ SALIM TURKY: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa nafasi hii. Awali ya yote, naomba nimshukuru Mwenyezi Mungu Subhanahu Wataala kwa kutujaalia uzima tukafika katika Bunge hili. Halikadhalika naomba tumwombee dua Mbunge mwenzetu Mheshimiwa Ghati amepata ajali na yuko mahututi, lakini tumwombe Mungu amjaalie shufaa aweze kurudi katika Bunge hili tuwe nae pamoja. [Maneno Haya Siyo Sehemu ya Taarifa Rasmi za Bunge]

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Turky, ngoja tuelewane vizuri. Taarifa kuhusu wagonjwa na vifo hutolewa na Kiti. Kabla Kiti hakijatoa maelezo usije ukasema hapa mgonjwa yuko mahututi kumbe sio mgonjwa. Kwa hiyo tafadhali, hayo maneno yaondoke, madam Kiti hakijatoa bado Taarifa.

MHE. TOUFIQ SALIM TURKY: Mheshimiwa Naibu Spika, nafuta hayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichukue fursa hii tumuombee mzee wetu Hayati Kenneth Kaunda alikuwa katika waasisi wa Bara letu hili la Afrika. Alikuwa pamoja na mzee wetu Mwalimu Nyerere katika kuwakomboa Waafrika wenzetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nichukue fursa hii kuipongeza Wizara ya Fedha na Mipango kwa kuja na bajeti ya namna yake. Kwa kweli bajeti hii imewagusa karibu Watanzania wote, tukisema wote pamoja na wa visiwani. Kwa kweli, mwenyewe nimeshaenda kwenye vikao tofauti katika Baraza la Biashara Zanzibar, Baraza la Biashara la Taifa la Bara na katika kilio kikubwa sana kilikuwa ni kilio cha VAT. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru sana Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan pamoja na Wizara ya Fedha kwa kuona kilio cha Watanzania. Watanzania sisi ni ndugu tuna ushemeji kila mkoa kutokana na kwamba, kuna Wasukuma wako Zanzibar, wako Wagogo Zanzibar, wanakuja kule kutembelea kwetu, wanaona TV, wanaona blender, wakichukua wanalipishwa VAT, wakija zao bara wanalipishwa VAT Bara, lakini hiki kilio cha Watanzania kimeonekana. Hongereni mno. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, halikadhalika tunafahamu Watanzania wengi waliokuwepo ni wajasirimali na wafanyabiashara wadogo wadogo. Kama hatujabuni miradi tofauti basi Watanzania tutabakia kuwa na vibaka au wakawa waporaji. Leo kwa kupitia punguzo la bodaboda hizi faini peke yake, basi imeleta hamasa ndani ya nchi watu wameweza kufanya kazi zao ipasavyo. Ilikuwa ni juzi wakati inasomwa bajeti nilikuwa na Mheshimiwa Shabiby wakati linaongelewa suala la kupandisha mafuta bei, akasema sasa haya mafuta yameshapandishwa, nikamwambia kwani unadhani zile pesa za TARURA za 500 zingetoka wapi? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naipongeza sana Wizara ya Fedha na Mipango kuja na ubunifu wa kutafuta vyanzo tofauti vya kuleta maendeleo ndani ya Tanzania yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nitapenda sana kuongelea suala zima la forodha ndani ya Afrika Mashariki. Hivi karibuni nilimwona rafiki yangu, Mheshimiwa Bashe akienda zake Namanga kwenda kupigania masuala ya mahindi. Tukajiuliza, kwani hii kazi ya Waziri au ya Wizara? Kulikuwa kuna itifaki ya Forodha ya Afrika Mashariki. Katika itifaki hii ilipaswa kila mwanachama atoe wajumbe watatu. Mjumbe mmoja ni Mwanasheria, anatakiwa Afisa wa Forodha halafu pia anatakiwa na Afisa wa Biashara. Toka 2005 itifaki hii kupitia Ibara ya 24 ya Biashara inatakiwa kuwe na Kamati ya Biashara ambayo inatatua changamoto hizi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa bahati mbaya au nzuri wakaongezeka wanachama wawili wengine Burundi na Rwanda, ikabidi ifanyike amendment. Miaka 15 imechukua kubadilisha amendment. Kwa bahati nzuri amendment imekamilika, kinachohitajika sasahivi ni kupitisha katika Mabunge yetu kuhakikisha hii Itifaki ya Forodha inafanya kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hivyo naomba sana kupitia Bunge hili la Kumi na Mbili kuweka historia kuwa Itifaki ile ya Forodha tumeweza kuipitisha na tukawa katika mstari wa mbele kidiplomasia kushawishi wanachama wenzetu wa Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi kupitia Mabunge yao kuhakikisha ile itifaki inapitishwa. Baada ya hapo tutakuwa na Kamati sasa inayotatua haya masuala ya NTBs. Haiwezekani leo kuona tuna changamoto ya bidhaa fulani mtu anatoka katika Wizara yake anakwenda kutatua, anaenda mipakani na wakati tayari tumeshajipangia inawezekana kuwa na Kamati ya Biashara kutatua changamoto hizi.

Mheshimiwa Naibu Spika, leo tunaelekea katika AfCFTA ukanda wa Afrika nzima kuwa na biashara huru wakati East Africa pekee mpaka sasa hivi tunatafuta Mawaziri, Naibu Mawaziri na Makatibu waende kutatua matatizo haya. Kusema ukweli ile ndoto ya kuwa na Ukanda wa Afrika ya Biashara Huru, basi itakuwa ni ndoto tu. Kwa hivyo, nawaomba sana tuipitishe itifaki hii kuhakikisha Kamati ya Biashara inafanya kazi yake. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kumalizia nataka niongee kidogo kwenye suala la ufugaji. Tanzania sisi ni wa pili katika kuwa na wanyama (cattle) wengi. Hata hivyo, ukitazama value katika wanyama hao, yetu iko chini mno.

Nimetazama kuna Mabara ya Japan wana steak inaitwa Wagyu, kuna wenzetu kupitia Scotland wanaitwa Angus. Ile nyama kilo moja inaweza kufika mpaka dola 200 sawasawa na ng’ombe mzima tunayeuza sisi. Sasa hebu tuwasaidie wakulima wetu kuhakikisha tunakuwa na prime steak pia. Leo katika hoteli zote za nyota tano nyama zinatoka Afrika Kusini, Argentina, New Zealand na sisi bado nyama zetu haziko katika quality za kuwepo katika five Star properties. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, haiwezekani hata siku moja tuwe wa pili katika Bara la Afrika na nyama zitoke nchi nyingine kwa sababu kiwango chake bado hakijafikiwa. Naiomba sana na naishauri Wizara husika kuhakikisha tunaelimisha wafugaji wetu kuweza kuwalea ng’ombe, mbuzi na wanyama wetu kuhakikisha wanakuwa wa kiwango, sio tu kwa kutumika kwenye hoteli zetu lakini kupitia ukanda mzima wa Afrika na dunia kiujumla. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)