Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon Abubakar Damian Asenga (44 total)

MHE. ABUBAKARI D. ASENGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Nami naomba kuuliza Wizara ya Mawasiliano swali la nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuwa vijiji vitatu katika Kata ya Ziginali, Kisawasawa na Kiberege havina mawasiliano ya simu kabisa. Je, ni lini Serikali itawasaidia wananchi hawa huduma ya mawasiliano ya simu?
NAIBU WAZIRI WA MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Naibu Spika, kama ambavyo nilijibu katika majibu yangu ya msingi, ni kwamba Serikali iko katika mpango wa kufanya tathmini katika Kata nyingine 1,392 ambazo zimebaki Tanzania Bara ili tuweze kuona namna gani tutaziingiza katika Mpango wa Utekelezaji katika Bajeti ya 2020/2021. Hivyo namhakikishia Mheshimiwa Mbunge, sambamba na hilo tutahakikisha kwamba tunawasiliana naye kwa ukaribu sana ili kujua changamoto ziko katika maeneo gani ili tuhakikishe kwamba mawasiliano katika Kata hizo yanafika kwa ukamilifu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. (Makofi)
MHE. ABUBAKARI D. ASENGA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Kwa kuwa wewe ni miongoni mwa watu waliofika Jimboni kwetu na kuona namna ambavyo tunalima miwa kwa bidii kwa kufuata kauli ya Mheshimiwa Rais ya nchi kujitegemea katika suala zima la sukari; na kwa kuwa hao wenye viwanda ndio waliopewa vibali vya kuingiza sukari inayopungua katika nchi yetu, je, Serikali haioni umuhimu wa kuweka mwekezaji mwingine wa kiwanda ili kuondoa monopolism ya kiwanda ambacho kipo?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, je, Mheshimiwa Waziri na Mawaziri husika katika sekta hii ya kilimo na viwanda na biashara, watakuwa tayari kuambatana nami baada ya Bunge hili, kwenda kuwasikiliza wananchi hasa wakulima wa miwa Jimboni kwangu?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Abubakari, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kama nilivyojibu kwenye swali langu la msingi, Serikali inaona umuhimu wa kuongeza uwekezaji wa viwanda vya sukari nchini hasa katika Kiwanda cha Kilombero ili kuongeza uzalishaji wa sukari nchini. Kwa upande wa Kiwanda cha Sukari cha Kilombero, Serikali na mbia mwenza, iko katika majadiliano ya kupanua kiwanda hiki na hatimaye kuongeza uzalishaji wa sukari ili miwa yote inayolimwa iweze kutumika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali lake la pili, napenda kumwahidi Mheshimiwa Abubakari kwamba niko tayari kuongozana naye pamoja na wataalam wangu kutoka Ofisi ya Msajili wa Hazina ili kujionea hali halisi ya uzalishaji katika kiwanda hicho, pale tutakapopata nafasi mara baada ya mkutano huu wa Bunge kuahirishwa. (Makofi)

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS (UWEKEZAJI): Mheshimiwa Spika, ahsante na naomba kuongezea majibu kwa majibu mazuri sana ya Mheshimiwa Naibu Waziri kwamba Serikali iko kwenye mazungumzo na wawekezaji kadhaa angalau watatu ambao wana nia ya kuwekeza katika kujenga viwanda vipya vya sukari. Naamini kwa mazungumzo hayo, tukiwapata tutapunguza sana tatizo la sukari na nia ya Serikali ni kuona kwamba katika mwaka mmoja ujao tunajitosheleza kwa mahitaji ya sukari hapa nchini. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, la pili ni kwamba, wiki ijayo baada ya Bunge hili mimi na Mheshimiwa Waziri wa Kilimo tuna ziara katika Mkoa wa Morogoro na tutajitahidi tufike pia jimboni kwa Mheshimiwa ili kuweza kuona changamoto. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. ABUBAKARI D. ASENGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali madogo mawili ya nyongeza.

Nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali, lakini bado specifically ninataka kusikia angalau kwenye takwimu jinsi ambavyo Serikali inawekeza haraka kutumia pumba hizi kwa sababu zinaharibu mazingira na hivi ninavyozungumza na wewe zimesababisha Mto Kilombero kujaa maji na kusababisha mafuriko kwa wananchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la kwanza ni kwamba ni kiasi gani Serikali inawekeza haraka iwezekanavyo kutumia pumba hizi ambazo Mheshimiwa Naibu Waziri amesema ni tani 11,000; zinakwenda wapi pumba hizi? Ni kwamba uwekezaji wa haraka unatakiwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; hawa wakulima wadogo wadogo wa kilimo cha uyoga tayari Halmashauri yetu imewakopesha katika vikundi na wanaendelea kulima, changamoto kubwa wanayoipata ni katika vifungashio, mifuko ile ya kupandia.

Je, Serikali haiwezi kutafuta wawekezaji watakaoruhusu mifuko hii ya kupandia ipatikane kama ambavyo imefanyika kwa wauza mikate kwa sababu sasa hivi kuna katazo la Serikali la mifuko ya nylon?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU (UWEKEZAJI): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Asenga kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu kwamba kwa nini Serikali haijawekeza; naomba nimfahamishe Mheshimiwa Mbunge kwamba zao la uyoga ni zao ambalo ni kama ndiyo linaanza. Kwa hiyo, bado tunahitaji kufanya utafiti na kutoa hamasa kubwa ili wananchi waweze kufahamu umuhimu wa kulima hilo zao, lakini pia tuweze kuwa na elimu basi hata ya namna ya kulipanda na kulihudumia.

Kwa hiyo, Serikali imeanza kwa kutoa uhamasishaji na kufanya tafiti mbalimbali. Sasa huko mbele ya safari tunaamini kwamba taarifa ambayo itatokana na tafiti hizo, na wananchi wakihamasika basi inakuwa ni rahisi kuvutia wawekezaji wengine na hata kutoka nje.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na upatikanaji wa vifungashio; ni swali zuri na sishangai kwa sababu ni Mbunge makini, namfahamu tokea siku nyingi. Lakini naomba nilibebe ili tushirikiane na Ofisi ya Makamu wa Rais, Mazingira pamoja na wenzetu wa Wizara ya Kilimo, tuangalie ni namna gani tunaweza tukapata vifungashio vizuri zaidi kwa ajili ya kuzalisha vimeng’enya kwa ajili ya uzalishaji wa uyoga.
MHE. ABUBAKARI D. ASENGA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa nafasi, japokuwa ntaendelea kubakia kuwa mwananchi mtiifu wa Jangwani, na chini ya GSM naamini kwamba tutavuka salama. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri Mkuu alipokuja katika Jimbo la Kilombero na Mheshimiwa Job Ndugai akiwa Mjumbe wa Kamati Kuu alipokuja katika Jimbo la Kilombero, waliwaahidi wananchi wa Jimbo la Kilombero juu ya ujenzi wa Hospitali ya Jimbo la Kilombero. Namshukuru Mheshimiwa Waziri, dada yangu, Mheshimiwa Ummy, ametuahidi kwamba tutapata milioni 500 za kuanza ujenzi huu.

Mheshimiwa Spika, swali langu; je, ni lini ujenzi huu utaanza?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, nimhakikishie kabisa katika bajeti inayokuja ya mwaka 2021/ 2022, Serikali imehakikisha kuanza hospitali mpya katika halmashauri zote nchini ambazo hazina hospitali za wilaya.
MHE. ABUBAKARI D. ASENGA: Mheshimiwa Naibu Spika, naishukuru Serikali kwa majibu mazuri, na kwa niaba ya Mbunge wa Ulanga Mheshimiwa Salim, naomba kuuliza maswali madogo mawili ya nyongeza kama ifutavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa lazima ukitaka kwenda Ulanga upite Jimbo la Kilombero na kwa kuwa Wilaya ya Malinyi, Ulanga, Jimbo la Mlimba na Jimbo la Kilombero ni ukanda mmoja.

Mheshimiwa Naibu Spika, je, Mheshimiwa Waziri haoni kwamba ni muhimu kuwa na timu ya dharura ya TARURA ikaenda kwenye eneo hilo kwa sababu Wilaya ya Kilombero, Jimbo la Mlimba, Ulanga na Malinyi hakuendeki?

Mheshimiwa Naibu Spika, pili: Je, Mheshimiwa Waziri pia haoni kwa udharura huo akatafuta haraka iwezekanavyo gari la kuwapelekea wananchi wa Wilaya ya Ulanga kwa maana ya timu ya TARURA ikapata gari la dharura wakati huu wa mvua ambapo njia hazipitiki? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Jambo la kwanza ameiomba Serikali kupeleka timu ya dharura kwa ajili ya kwenda kupitia zile barabara ambazo zimebadilika na kufanya tathmini. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, hivi ninavyozungumza sasa hivi kuna timu zipo huko kwa ajili ya kuangalia zile barabara zote mbovu ambazo zilipitiwa na hili janga la mvua yakiwemo maeneo ya kule Malinyi. Kwa hiyo, watu wapo kazini na hiyo timu inaendelea.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu katika Bunge hili wengi huwa wanatusikiliza sasa hivi, ninaagiza wapitie tena upya waangalie hiyo tathmini ya barabara ya Kilombero kupitia Ulanga inafanyiwa kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili ameomba kwamba tuwe na gari la dharura kwa ajili ya Ulanga. Kama nilivyoeleza katika jibu la msingi kwamba, tumeshatengewa fedha na katika hizo fedha tutanunua magari 30 na miongoni mwa maeneo ambayo tumeyapa kipaumbele, tutapeleka gari kwa ajili ya TARURA ni katika Jimbo la Ulanga. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshmiwa Mbunge, Ulanga watapata hilo gari.
MHE. ABUBAKARI D. ASENGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Kwa niaba ya wananchi wa Jimbo la Kilombero, napenda kushukuru kwa majibu mazuri ya Wizara na tunaombea kweli huu mkopo upatikane na mradi huu ufanyike.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuuliza maswali madogo mawili ya nyongeza, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, je, ni lini Mheshimiwa Waziri atakuwa tayari kutembelea Jimbo la Kilombero ili apite angalau kuzungumza na wananchi wa Zinginai, Magombera, Kanyenja, Mpanga na Muhelule ambao wana shida kubwa ya maji?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kutokana na hali ya udharura wakati tukisubiri mradi huu wa maji tayari Serikali ilishachimba kisima kikubwa katika Kata ya Lumemo ambapo kinatoa lita 30,000 kwa saa. Changamoto ni tenki la kuhifadhi maji yale kuwasambazia wananchi. Katika hali hii ya udharura, je, Serikali haiwezi kutujengea tenki wakati tunasubiri mradi wa maji wa Kiburubutu - Ifakara? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naomba kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Abubakari Damian Asenga, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, hili la kwenda Kilombero ni moja ya majukumu yangu. Mheshimiwa Mbunge mara baada ya Bunge hili tutaweka utaratibu mzuri ili niweze kufika hapo. Naamini mpaka mwisho wa Bunge hili hata mradi huu utekelezaji utakuwa umeanza, kwa hiyo, nitakuja nikiwa na bashasha.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na ujenzi wa tenki kwa kisima kile ambacho tumekichimba, nia na dhamira kabisa ya Wizara ni kuona wananchi wanapata maji kwa umbali mfupi. Tumeshaweza kutoa fedha ya kuchimba kisima ni dhahiri lazima tutoe fedha ya ujenzi wa tenki. Nimuahidi Mheshimiwa Mbunge, kabla ya mwaka huu wa fedha kuisha, ujenzi wa tenki utaanza kufanyika. (Makofi)
MHE. ABUBAKARI D. ASENGA: Mheshimiwa Spika, ninakushukuru sana, Kituo cha Afya cha Kidatu Nyandeo kina uhaba mkubwa sana wa jokofu la kuhifadhia miili ya marehemu na mara ya mwisho tuliwasiliana na MSD wakasema kwamba wangepeleka jokofu hilo lakini mpaka sasa hawajapeleka.

Je, lini Serikali itapeleka Jokofu katika Kituo cha Afya cha Nyandeo Tarafa ya Kidatu Jimbo la Kilombero?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Abubakari Asenga, Mbunge wa Kilombero kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuweka mipango ya kupata vifaa tiba na vifaa mbalimbali yakiwemo majokofu ya kuhifadhia maiti, lakini pamoja na jitihada za Serikali tumeendelea pia kuhakikisha tunawaelekeza Wakurugenzi wa Mamlaka za Serikali kuona umuhimu wa kutenga fedha katika mapato ya ndani kununua baadhi ya vifaa tiba na baadhi ya vitendea kazi katika hospitali zetu yakiwemo majokofu ya kuhifadhia maiti.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, ninaomba nichukue nafasi hii kumwagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilombero kwa sababu majokofu haya ni kati ya Milioni 12 hadi Milioni 30; fedha hii ipo ndani ya uwezo wa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Kilombero na hivyo ninamuelekeza katika mwaka ujao wa fedha wahakikishe wanaweka provision ya kununua jokofu la kuhifadhia maiti katika kituo cha afya. Nakushukuru sana.
MHE. ABUBAKARI D. ASENGA: Mheshimiwa Spika, ninakushukuru sana, Kituo cha Afya cha Kidatu Nyandeo kina uhaba mkubwa sana wa jokofu la kuhifadhia miili ya marehemu na mara ya mwisho tuliwasiliana na MSD wakasema kwamba wangepeleka jokofu hilo lakini mpaka sasa hawajapeleka.

Je, lini Serikali itapeleka Jokofu katika Kituo cha Afya cha Nyandeo Tarafa ya Kidatu Jimbo la Kilombero?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Abubakari Asenga, Mbunge wa Kilombero kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuweka mipango ya kupata vifaa tiba na vifaa mbalimbali yakiwemo majokofu ya kuhifadhia maiti, lakini pamoja na jitihada za Serikali tumeendelea pia kuhakikisha tunawaelekeza Wakurugenzi wa Mamlaka za Serikali kuona umuhimu wa kutenga fedha katika mapato ya ndani kununua baadhi ya vifaa tiba na baadhi ya vitendea kazi katika hospitali zetu yakiwemo majokofu ya kuhifadhia maiti.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, ninaomba nichukue nafasi hii kumwagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilombero kwa sababu majokofu haya ni kati ya Milioni 12 hadi Milioni 30; fedha hii ipo ndani ya uwezo wa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Kilombero na hivyo ninamuelekeza katika mwaka ujao wa fedha wahakikishe wanaweka provision ya kununua jokofu la kuhifadhia maiti katika kituo cha afya. Nakushukuru sana.
MHE. ABUBAKARI D. ASENGA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru, napenda kumshukuru Mheshimiwa Waziri wa Maliasili na Naibu wake, walipokuja jimboni kwetu walichukua hatua kuhusu askari wa TAWA, baadhi ambao walikuwa wakiwaonea wananchi wetu. Na kuwa Mheshimiwa Waziri aliahidi pale katika mkutano ule kwamba atatujengea soko la samaki, Ifakara, Kilombero. Naomba kuiuliza Serikali ni lini ahadi ile nzuri ya Mheshimiwa Waziri wa Maliasili na Utalii itaanza?
WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, nimpongeze Mheshimiwa Asenga kwa kuuliza swali hilo na kujali wananchi wake:-

Mheshimiwa Spika, mpango wa kujenga soko katika Daraja la Mto Kilombero upo katika bajeti ya Wizara katika mwaka huu 2021/2022. Kwa hiyo, mara baada ya bajeto hiyo kupitishwa mkakatin huo utaanza.
MHE. ABUBAKARI D. ASENGA: Mheshimiwa Naibu Spika, japokuwa majibu ya Serikali zijaridhika nayo sana, lakini kwa kuzingatia kuwa Kassim Faya Nakapala Mwenyekiti wa Halmashauri na Ebeneza Emmanuel Katibu wa CCM wa Wilaya wako hapa kufuatilia miongoni mwa mambo mengine jambo hili na Diwani wa Kata husika Fatma Mahigi wa Mang’ula “B” kwamba eneo hili sasa limekuwa hatarishi sana ni eneo ambalo lina ekari takribani 250 na akina mama wameshaanza kubakwa. Naomba kuiuliza Serikali maswali mawili madogo ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, la kwanza Serikali ipo tayari kuweka ulinzi wakati huu inatafuta mwekezaji wa kuwekeza katika Kiwanda hiki cha Machine Tools?

Lakini pili naomba kuiuliza Serikali sasa hivi tunajenga reli ya kisasa ya SGR na hii reli ya kisasa itahitaji mataruma na kadhalika, kwa nini wasikabidhi eneo hili na kiwanda hiki kwa SGR ili iendelee kutumia kuzalisha vifaa vya reli? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Abubakari Damian Asenga, Mbunge wa Kilombero kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nichukue nafasi hii kumpongeza sana ndugu yangu Asenga kwa ufuatiliaji kwa ajili ya maendeleo ya Jimbo lake na hasa katika sekta ya viwanda na kwa ajili ya ufufuaji wa kiwanda hiki cha Mang’ula Machine Tools.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli eneo hili limekuwa kwa muda mrefu halitumiki kama nilivyosema kwa sababu mwekezaji aliyepewa eneo hili kuliendeleza hajaliendeleza kwa muda mrefu, nichukue nafasi hii kumuahidi kwamba tutashirikiana na Halmashauri kuona namna bora ya kuweka ulinzi ili eneo hili lisiwe hatarishi kwa sasa ambapo bado hatujapata mwekezaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini swali la pili kama nilivyosema tunaangalia matumizi bora ikiwa ni pamoja na kutafuta wawekezaji ambao wataweza kutumia eneo hili kwa ajili ya kuwekeza viwanda, tuchukue pia hoja ya Mheshimiwa Mbunge kwamba kama wenzetu wa reli ya kisasa watataka kutumia eneo hili kwa ajili ya kuzalisha bidhaa mbalimbali kwa ajili ya kutumika katika SGR basi nao tutawakaribisha, ahsante sana.
MHE. ABUBAKARI D. ASENGA: Mheshimiwa Spika ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, pia Halmashauri ya Mji wa Ifakara Jimbo la Kilombero imekuwa ikikosa umeme kila Jumanne na Alhamis; na tunamradi mkubwa sana wa Serikali wa zaidi ya shilingi bilioni 20 wa kituo cha kukuzia umeme. Ujenzi huo wa mradi unasuasua kwa muda mrefu sana: -

Je, Naibu Waziri atakuwa tayari kutembelea pale kutazama changamoto za kusuasua za mradi ule?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Asenga kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwa ruhusa yako nipo tayari kwenda kuangalia changamoto hizo, lakini niseme kwamba kama anasema ni Jumanne na Alhamis, basi nitafanya mawasiliano na wenzangu tufahamu shida ni nini?

Mheshimiwa Spika, niwahakikishie Watanzania kwamba hatuna mgao kwa nchi yetu ya Tanzania kwa sasa. Tunao umeme ambao unatosheleza mahitaji tuliyokuwa nayo kwa kile kiasi tunachoweza kupeleka, lakini tutaenda kuangalia tatizo ni nini ili tuweze kulitatua.
MHE. ABUBAKARI D. ASENGA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru, napenda kuishukuru Serikali kwa majibu mazuri ya kutelekeza ahadi hii ya Mheshimiwa Waziri Mkuu maana Waziri Mkuu mwenyewe alilitembelea eneo hili na aliona ufinyu wa eneo hili. Napenda pia kuishukuru Serikali kwa Waziri wa Ardhi Mheshimiwa Lukuvi kutupatia ardhi Kata ya Kiberege kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali hii ya Halmashauri.

Mheshimiwa Spika, naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Kwa sasa hivi wakati mchakato wa ujenzi wa Hospitali ya Halmashauri ukiendelea Wananchi wa Halmashauri ya Mji wa Ifakara wanategemea sana kituo cha afya cha Kibaoni, kituo hiki kinakabiliwa na upungufu mkubwa sana wa watumishi.

Je, Serikali haioni kuchukua hatua za haraka kuongeza watumishi katika kituo cha afya cha Kibaoni? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili; kutokana na ufinyu wa ardhi na eneo la ekari takribani kumi za kujenga Kituo cha Afya cha Kata ya Ifakara Mjini, Ifakara Mjini mpaka sasa hivi haina Kituo cha Afya eneo lililopo ni dogo. Je, Serikali ipo tayari kutupatia ramani maalumu ya ujenzi wa ghorofa ili tufanye mchakato wa kuanza Kituo cha Afya cha Kata ya Ifakara Mjini?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Abubakari Damian Asenga Mbunge wa Kilombero kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwanza nipokee shukrani zake nyingi kwa Serikali yetu ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa kazi ambayo imeendelea kuifanya ya kujenga vituo vya afya, hospitali na zahanati nchini kote na nimuhakikishie kwamba mpango huo ni endelevu tutaendelea kujenga vituo vya afya, zahanati, lakini na hospitali zetu za halmashauri kuhakikisha tunasogeza huduma za afya kwa wananchi.

Mheshimiwa Spika, kuhusiana na kituo cha afya cha Kibaoni kuwa na watumishi wachache nimuhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba ujenzi wa vituo hivi unakwenda sambamba na mipango ya kuajiri watumishi kwa awamu kwa kadri fedha zitakapopatikana, lakini pia kwa kadri ya vibali vya ajira vitakavyotolewa. Kwa hiyo, naomba nichukue suala hilo na tutakipa kipaumbele kituo cha afya cha Kibaoni ili kiweze kupata wahudumu kwenye awamu za ajira zinazofuata ili tutoe huduma bora kwa wananchi.

Mheshimiwa Spika, kuhusiana na kituo cha afya Ifakara Mjini utaratibu upo wazi kama tunahitaji kujenga jengo la kwenda juu kwa maana ya ghorofa. Tunaomba kibali rasmi Ofisi ya Rais, TAMISEMI tunawasilisha michoro na Ofisi ya Rais, TAMISEMI kupitia watalaamu tunapitia na kuwashauri namna ya kujenga. Kwa hiyo tunakukaribisha kuwasilisha maombi hayo ili tuweze kuona uwezekano wa kujenga kituo hicho. Ahsante. (Makofi)
MHE. ABUBAKARI D. ASENGA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru na mimi nitoe pongezi kwa Wizara ya Kilimo kwa kufuatilia kilimo cha miwa katika Jimbo la Kilombero, na hivi karibuni Mheshimiwa Naibu Waziri alikuwa kule.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na Serikali kuendelea kuboresha ushirika bado kuna baadhi ya watu wa ushirika ambao wanalalamikiwa na wakulima, hususan katika Jimbo la Kilombero.

Je, Waziri ama Naibu Waziri atakuwa tayari sasa kuja Kilombero ili kufanya mkutano maalum na wakulima wa miwa na kuwasikiliza kuhusu malalamiko yao kuhusiana na ushirika?
WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri.

Mheshimiwa Spika, nataka nimhakikishie Mheshimiwa Abubakari na Wabunge wote wa ukanda wa Kilombero, Mtibwa pamoja na maeneo yote hayo, nitakuja mwenyewe binafsi, nitakuja kufanya mikutano na wakulima, nitafanya mikutano na viongozi wa Ushirika na makampuni ili tuweze kuyaondoa matatizo yaliyoko kwenye eneo hilo. (Makofi)
MHE. ABUBAKARI D. ASENGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Wilaya ya Kilombero ni miongoni mwa wilaya kongwe sana, lakini haina Kituo cha Polisi cha Wilaya, hali inayopelekea OCD na askari wake kutumia Kituo Kidogo cha Ifakara kama Kituo cha Polisi cha Wilaya. Sasa swali langu dogo tu. Je, Mheshimiwa Naibu Waziri atakuwa tayari kutembelea Kilombero kujionea Kituo Kidogo cha Polisi Ifakara kinavyozingirwa na mafuriko kupelekea polisi wetu kwenda kazini wakiwa wamekunja suruari na kuvua viatu ili apandishe morali ya Serikali kusaidia juhudi ya Mkuu wa Wilaya, Mkurugenzi na Mbunge kujenga kituo cha polisi kipya?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Abubakari Asenga, Mbunge wa Kilombero, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati wote nipo tayari kuungana na Mheshimiwa Mbunge kufuatilia jambo hili. Nilikwenda kutembelea gereza kule Kilombero alizungumza juu ya jambo hili, muda haukuruhusu. Hivyo, nipo tayari baada ya Bunge hili kuongozana ili tukatatue tatizo lake lililotajwa. Ahsante. (Makofi)
MHE. ABUBAKARI D. ASENGA: Mheshimiwa Spika, ninakushukuru; kwa kuwa mmoja wa Wabunge mwenzetu aliwahi kuuliza humu Bungeni kuhusu ukarabati wa viwanja vya michezo na Serikali ikachukua jukumu la kukarabati.

Je, ni lini Serikali itafanyia kazi ombi la ukarabati wa Uwanja Mkuu wa Tanganyika - Ifakara ambao unatumika na Wilaya tatu?
NAIBU WAZIRI WA UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Spika, nikushukuru na naomba nijibu swali la Mheshimiwa Abubakari kuwa sisi kama Wizara hatuna tatizo kabisa kushirikiana na Serikali za Mitaa, atakapotuletea maombi haya kwenye Mfuko wa Maendeleo ya Michezo pale tutakapoweza pia tunaweza tuka-support. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ninaendelea kutoa rai kwa Halmashauri zetu kwamba hili jambo ni serious, tumekuwa tukitenga asilimia 10 ya mikopo, ujenzi wa hospitali, shule zetu, lakini suala la michezo imekuwa siyo kipaumbele. Ninawaomba Waheshimiwa Wabunge tushirikiane na ninawapongeza kwa dhati Wabunge ni wadau wakubwa sana wa michezo. (Makofi)
MHE. ABUBAKARI D. ASENGA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Ujenzi wa Hospitali ya Halmashauri au Wilaya katika Jimbo la Kilombero unaenda kwa kusuasua: Je, Serikali inawahakikishia nini wananchi wa Jimbo la Kilombero kwamba hospitali hiyo ya Halmashauri itakamilika?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Asenga ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, naomba nitoe maelekezo kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Kilombero kuhakikisha anatumia fedha za Serikali zilizoletwa kwa ajili ya kujenga hospitali hiyo, na hospitali hiyo ikamilike kwa wakati kama mpango kazi ulivyo. Nasi Ofisi ya Rais, TAMISEMI, tutafuatilia kuona utekelezaji huo. Ahsante. (Makofi)
MHE. ABUBAKARI D. ASENGA: Mheshimiwa Naibu Spika, Mji wa Ifakara ni mji unaokuwa kwa kasi sana na uwanja wake wa ndege ni dhoofu. Ni lini Serikali itakarabati Uwanja wa Ndege wa Ifakara ili ndege kubwa ziweze kutua?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Asenga Mbunge wa Kilombero kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba tulichukue. Hata hivyo niwaagize watu wa TAA na TANROADS wautembelee uwanja huo kwa ajili ya kuufanyia ukarabati. Ahsante.
MHE. ABUBAKARI D. ASENGA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Tunaishukuru Serikali kwa kuendelea na ujenzi wa Barabara ya Ifakara – Kidatu na hasa tunaishukuru Wizara ya Ujenzi na TANROADS kwa usimamizi wa barabara hii. Je, Serikali ina mpango gani wa uwekaji wa taa za barabarani katika Barabara hii ya Ifakara – Kidatu kama Mheshimiwa Waziri Mkuu alivyoelekeza kwa zile barabara zinazopita katika vijiji?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, ahsante, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Asenga, Mbunge wa Kilombero, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwanza nimshukuru na kumpongeza kwa kutambua jitihada za Serikali kuhakikisha kwamba barabara hii inaendelea kujengwa sasa hivi kwa kasi tofauti na ilivyokuwa. Naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba kwa sasa barabara zote zinazojengwa na hasa kwa kiwango cha lami, pale ambapo kuna miji mikubwa na midogo taa za barabarani zinatakiwa ziwekwe.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba utaratibu huo upo na itakapokamilika basi awamu itakayofuata itakuwa ni kuweka taa za barabarani. Ahsante.
MHE. ABUBAKARI D. ASENGA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa nafasi. Takribani wananchi Elfu Sita wa Kijiji cha Katurukira Kata ya Mkula na Kijiji cha Sururu Kata ya Signari hawana mawasiliano mazuri ya simu. Je ni lini Serikali itawasaidia wananchi miundombinu ili waweze kupata mawasiliano mazuri ya simu?
NAIBU WAZIRI HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge wa Kilombero kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali ina mradi wa Tanzania ya Kidigitali (Digital Tanzania) na tayari mradi huu tenda yake imeshatangazwa tarehe 20 Oktoba na tarehe 2 Disemba tayari mradi utafunguliwa ambapo Kata na Vijiji vya Jimbo la Kilombero vimeingizwa katika mradi huo. Hivyo, Mheshimiwa Mbunge asiwe na wasiwasi pindi mchakato huu utakapokamilika basi ujenzi wa minara utaanza kufanyika rasmi katika Jimbo lake.
MHE. ABUBAKARI D. ASENGA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru na kwa kuzingatia maelekezo yako ya maswali ya nyongeza yawe mafupi, nakushukuru sana swali langu kuwa la kwanza katika Bunge lako hili la kwanza ikiwa Simba imeshafanya yake. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Spika, wakati Simba ikifanya yao tayari Yanga Sport Club ikiwa inaongoza ligi ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Sasa naomba kuuliza maswali yangu mafupi madogo mawili ya nyongeza.

Kwanza, kwa kuzingatia majibu ya Mheshimiwa Waziri ni kwamba tumekosa fedha kutokana na ripoti ya wataalam wetu au andiko la wataalam wetu kutokukidhi vigezo. Je, Mheshimiwa Waziri anatuhakikishia kwamba ataweza kutupatia wataalam ili tuandike upya andiko hili?

Swali la pili, wananchi wa Mji wa Ifakara wanateseka sana kutokana na soko hasa msimu huu wa mvua. Je, Mheshimiwa Waziri mwenyewe wa TAMISEMI atakuwa tayari katika Bunge hili kutafuta hata siku moja kutembelea soko hili na kuzungumza na wananchi wa Mji wa Ifakara?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naomba kujibu maswali madogo mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Abubakari Damian Asenga, Mbunge wa Jimbo la Kilombero kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza aliuliza kwamba kama Ofisi ya Rais, TAMISEMI tunaweza kuwapatia wataalam. Tuko tayari kuwapatia wataalam ambao watashirikiana na Halmashauri ya Mji wa Ifakara kuhakikisha wanakamilisha andiko lao, kwa hiyo hilo tuko tayari.

Mheshimiwa Spika, swali la pili kuhusu kwenda Ifakara. Mheshimiwa Mbunge mimi niko tayari hususani wakati wa weekend tunaweza tukaongozana kwenda kushuhudia hiyo kero ya wananchi katika eneo lako. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. ABUBAKARI D. ASENGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Kwa kuzingatia ushauri wa Mheshimiwa Waziri wa Elimu, tayari Kijiji cha Mpanga, Kata ya Kisawasawa, Halmashauri ya Mji wa Ifakara, Wilaya ya Kilombero, imepata eneo la ujenzi wa Chuo cha VETA.

Je ni lini ujenzi wa chuo hicho utaanza?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Naomba kujibu swali dogo la Mheshimiwa Asenga, Mbunge wa Kilombero kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spiuka, kama nilivyojibu kwenye majibu yangu ya swali la msingi kwamba Wilaya ya Kilombero ni miongoni mwa Wilaya 63 ambazo zipo kwenye mpango huu wa ujenzi wa vyuo vya VETA. Nimwondoe wasiwasi Mheshimiwa Mbunge, tunasubiri fedha kutoka Wizara ya Fedha. Mara tu fedha zitakapopatikana, basi Wilaya ya Kilombero ni miongoni mwa Wilaya 63 ambazo ujenzi utaanza rasmi.
MHE. ABUBAKARI D. ASENGA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana, napenda kuishukuru Serikali ya Awamu ya Sita kwa kujenga Mahakama mpya nzuri ya Wilaya ya Kilombero. Swali, je, ni lini Mahakama ile itazinduliwa katika Kata ya Kibaoni pale ili wananchi wawenze kupata huduma za Mahakama Mpya?
NAIBU WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Spika, nipende kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge kutoka Kilombero. Ni kwamba wakati wowote atajulishwa utaratibu wa uzinduzi wa ile Mahakama kwa sababu haijaisha muda mrefu sana. Sasa hivi tunaharakisha uzinduzi wa Mahakama zote ambazo zimekamilika hapa nchini kwa ajili ya kuzizindua. Ahsante.
MHE. ABUBAKARI D. ASENGA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Naomba kumwuliza Mheshimiwa Waziri kuwa Kata ya Kidatu kuelekea Kata Msola Stesheni katika Halmashauri ya Mji wa Ifakara, barabara haipitiki kwa sasa: -

Je, Serikali ina mpango gani wa dharura wa kutengeneza barabara ile angalau kwa kiwango cha changarawe ili iweze kupitika?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naomba kujibu swali la Mheshimiwa Abubakari Asenga, Mbunge wa Kilombero, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, barabara aliyoanisha Mheshimiwa Mbunge ipo katika mipango ya Serikali ya kuhakikisha kwamba inajengwa. Kwa hiyo, tusubiri tu muda utakapofika na barabara hiyo itafanyiwa kazi.
MHE. ABUBAKARI D. ASENGA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Kwa majibu haya, dah, hadi maswali ya nyongeza yanakuwa na utata. Kwa ruksa yako nilikuwa naomba Mheshimiwa Waziri wakati Serikali inaendelea na mchakato wa kuboresha huduma za afya nchini; katika Jimbo la Kilombero chini ya Kanisa Katoliki imejengwa Hospitali kubwa sana ya Kansa. Hospitali hiyo mpaka leo haijafunguliwa. Baba Askofu anaomba Viongozi Wakuu wa nchi yetu wakafungue Hospitali hiyo. Mheshimiwa Waziri ana majibu gani?

Mheshimiwa Spika, swali la pili. St. Francis Hospital ni hospitali ya kanda, inatibu zaidi ya mikoa 10. Gharama zimekuwa kubwa na wananchi wanalalamikia kwa sababu Serikali imeondoa ruzuku iliyokuwa inatoa zamani: -

Je, Waziri anaweza kusema chochote kwamba wanaweza kukaa na Uongozi wa St. Francis Hospitali ya Ifakara ili kuzungumza namna ya kurejesha ruzuku ya awali?
NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mbunge kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwanza amezungumzia hospitali ambayo imefunguliwa, mimi na yeye tutakwenda Kilombero kuiangalia hospitali hiyo na kukagua halafu tuje tushauri mamlaka husika ili taratibu anazozisema ziweze kuchukuliwa hatua.

Mheshimiwa Spika, pili, suala la ile ruzuku ambayo alikuwa anaipata, nafikiri hata juzi tulikuwa tunazungumza hapa na Mheshimiwa Jenista Mhagama kuhusu hata masuala ya watumishi na mambo mengi. Nalo hili tunaenda kulifikiria kwenye bajeti hii na wakati wa bajeti tutawajibu.
MHE. ABUBAKARI D. ASENGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru na ninashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali.

Kwa kuwa jana Katibu Mkuu wa CCM, Comrade Daniel Chongolo alipita kwenye ziara katika Jimbo la Kilombero na aliviona vituo hivi na akanielekeza Mheshimiwa Mbunge nije niongee na Waziri wa Mambo ya Ndani kwa ajili ya kuanza ujenzi wake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza; je, nikileta nakala ya hati ya ardhi hizo ambazo Mheshimiwa Naibu Waziri amesema, Serikali itakuwa tayari kuanza ujenzi wa vituo hivyo vya Tarafa ya Mang’ula na Tafara ya Kidatu?

Swali la pili; kwa kuwa tayari Tarafa ya Ifakara lipo eneo linalomilikiwa na Jeshi la Polisi na Wizara ya Mambo ya Ndani; je, Serikali iko tayari kuanza kwa haraka kujenga Kituo cha Polisi cha Ifakara?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Meshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, naomba kujibu maswali ya nyongeza ya Mheshimiwa Mbunge Asenga, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba maeneo hayo mawili ni ngazi ya Tarafa yanahitaji Vituo vya Polisi, lakini majengo yaliyopo yamechakaa sana, lakini mojawapo ya jengo la JWTZ liko kwenye hifadhi ya barabara, na barabara inayojengwa italiondoa.

Kwa hiyo, ni ahadi yetu kwamba tunaweka katika bajeti ya mwaka 2023/2024 tutakayoipitisha mwezi Juni ili tuweze kuanza mipango ya ujenzi, la msingi tupate hizo hati miliki ili kuhakikisha kiwanja kiko ndani ya mikono ya Jeshi letu la Polisi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu Kituo cha Ifakara naomba nimuahidi Mheshimiwa Mbunge, nilitembelea eneo lile kwa kweli wanachangamoto ya kituo, wanahitaji kujengewa kituo kipya cha Polisi ngazi ya Mji wa Ifakara.

Kwa hiyo, ni ahadi yetu pia kwamba tutakipa kipaumbele katika bajeti inayokuja, nashukuru sana.
MHE. ABUBAKARI D. ASENGA: Mheshimiwa Spika, katika hayo magari yatakayokuja yananunuliwa na Serikali; je, Serikali iko tayari kupeleka gari moja katika Mji wa Ifakara?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, kwa sababu baadhi ya mikoa haina magari, siwezi kutoa ahadi hapa kwamba Ifakara watapata gari, lakini kadri tutakavyoongeza uwezo wetu wa kununua magari Wilaya zenye changamoto kubwa pia zitazingatiwa, nashukuru.
MHE. ABUBAKARI D. ASENGA: Mheshimiwa Spika, Je, ni lini Wizara itatekeleza maelekezo ya Mhesimiwa Waziri January Makamba kwa kurejesha bei ya kuunganisha umeme kwa Tarafa ya Ifakara mathalani maeneo yote yale ambayo yana asili ya vijiji 27000 kwa mfano Katinduka B na C.
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Asenga, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, utaratibu wa kubaini maeneo ya kupelekea umeme kwa gharama ndogo ulifanyika lakini haukuwa makini vya kutosha kwa hiyo tumewaelekeza wenzetu wa TANESCO warudie zoezi hilo tena kwa kuwa - consult Waheshimiwa Wabunge wote ili tupate maeneo hayo na kuyafanyia kazi sahihi.
MHE. ABUBAKARI D. ASENGA: Mheshimiwa Spika, swali langu linataka kufahamu kimsingi kwamba taasisi kubwa za nchi yetu, kwa maana ya Mahakama, Bunge na executive ya president, wale viongozi wakuu na wenza wao wanapokuwa madarakani wanaanzisha taasisi ambazo zinafanya makubwa katika nchi yetu. Taasisi hizo zinaaminika duniani zinapata fedha nyingi katika nchi yetu. Wanavyoondoka madarakani hakuna mfumo mzuri wa kiserikali wa kuziendeleza taasisi hizi. Kwa mfano Mkapa Foundation, WAMA, Tulia Trust leo inafanya makubwa lakini ukiondoka inapotea, Mama Magufuli alikuwa na taasisi ya wazee hatumwoni Mama Magufuli akiendeleza taasisi ya wazee.

Mheshimiwa Spika, swali langu kwa Serikali viongozi hawa wanapotoka madarakani kuna utaratibu gani wa kuendelea kusaidia taasisi hizi kubwa kama nchi zilizoendelea, tunavyoona Jimmy Carter leo inaweza kuwa January Makamba. Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Spika, swali alilouliza Mheshimiwa Abubakari Asenga Mbunge ni swali zuri; lakini kwa kuwa hadi hapa tunapozungumza sasa hakuna sheria wala mwongozo wowote unaotutaka sisi kufanya kazi au kupeleka kibajeti juu ya hizo taasisi za wenza wa viongozi naweza kusema kwa namna moja au nyingine kwamba hatuna la kufanya kwa sasa hivi. Hata hivyo, kama mawazo yako yatakuwa mazuri tutaangalia, lakini kuchukua fedha za umma kupeleka kwenye taasisi za watu binafsi hili jambo halijakaa sawa.
MHE. ABUBAKARI D. ASENGA: Mheshimiwa Spika, ahsante nakushukuru. Serikali mwaka 2021 iliahidi kujenga Chuo cha VETA katika Halmashauri ya Mji wa Ifakara Kata ya Kisawasawa. Sasa hivi tunapewa taarifa kwamba chuo hakitajengwa katika Halmashauri hiyo kwa sababu kuna Chuo cha Ufundi cha FDC. Chuo kinaenda kujengwa katika Halmasahuri ya Mlimba: -

Mheshimiwa Spika, nataka kujua: Je, kuwepo kwa Chuo cha Ufundi cha FDC ni sababu ya kukosa vyuo vya VETA? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Spika, ahsante, naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Asenga, Mbunge wa Ifakara, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kama nilivyoeleza kwenye majibu ya swali la msingi, vyuo hivi tunajenga katika ngazi ya Wilaya, havijengwi katika ngazi ya Halmashari. Ni jukumu la Wilaya kuangalia kwamba vinakwenda kujengwa wapi? Kwa zile Wilaya ambazo zina Halmashauri zaidi ya moja, ni lazima wakae chini Wakuu wa Wilaya pamoja na Wakurugenzi ili waweze kuamua wapi chuo hiki kinakwenda kujengwa? Kwa hiyo, sisi jukumu letu ni kwenda kujenga Chuo cha VETA lakini majukumu au wajibu wa kuchagua eneo gani la kwenda kujenga linabakia katika Wilaya husika.

Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana.
MHE. ABUBAKARI D. ASENGA: Mheshimiwa Spika, ni zaidi ya miaka mitano sasa daraja la kuunganisha Kata ya Msolwa Station na Mang’ula limekatika sambamba na kivuko cha Chikago – Kidatu na kivuko cha pale Kiberege. Je, ni lini Serikali itajenga madaraja haya?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA – (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Asenga: -

Mheshimiwa Spika, naomba nichukue nafasi hii mbele ya Bunge lako Tukufu kumuelekeza Meneja wa TARURA wa Mkoa wa Morogoro na Meneja wa TARURA wa Wilaya anakotoka Mheshimiwa Asenga, kuhakikisha wanafika kwenye barabara hiyo ambayo ameitaja Mheshimiwa Asenga, ili kufanya tathmini na kujua ni kiasi gani kinahitajika kwa ajili ya kuweza kuunganisha kata hizo mbili.
MHE. ABUBAKARI D. ASENGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, natoa pole kwa wananchi wetu wa Halmashauri ya Mji wa Ifakara kwa mafuriko makubwa ambayo wameyapata, na tunashukuru Mungu mpaka sasa hakuna kifo kilichotokea, tunapambana kupeleka misaada kwa wananchi ambao wameathirika sana. Mafuriko haya yamethibitisha kwamba kuna miundombinu ya TANROADS katika Kalavati la Sheli ya Madinga kwenda Rumomo na Kalavati la Kwa Shungu kwamba ni madogo na ndio yalichangia kupatikana kwa mafuriko.

Je, Serikali ina hatua gani za haraka za kurekebisha makalavati haya kama tulivyotembea na Mheshimiwa wa Wilaya na kujionea?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante naomba nitumie nafasi hii kumwagiza Meneja wa Mkoa wa Morogoro aende hilo eneo ambalo makalavati ni madogo atafute namna ambavyo anaweza akaongeza hayo makalavati kwa haraka ili kuondoa changamoto ambayo inawakuta wananchi wa Jimbo la Kilombero kwa Mheshimiwa Asenga, ahsante.
MHE. ABUBAKARI D. ASENGA: Mheshimiwa Spika, tunaishukuru Serikali walau Wilaya ya Kilombero sasa inapata chou cha VETA. Swali la kwanza, mtalifanyia nini eneo Kata ya Kisawasawa mlilopewa na wananchi na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Ifakara, maana wataalam wameshaenda na wameshalichukua hilo eneo?

Swali la pili, kule shamba Nakaguru Mchombe ambako mnakwenda kujenga hicho chuo cha VETA hakuna hata barabara, na fedha milioni 45 ni ndogo sana. Je, ni lini fedha zingine zitaongezwa?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Asenga kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kama nilivyokwisha eleza kwenye majibu ya swali la msingi, wajibu wa kutambua au kuamua ni eneo gani chuo kiende kujengwa ni mamlaka za wilaya pamoja na mikoa. Kwa hiyo nimwondoe wasiwasi kwanza Mheshimmiwa Asenga na Bunge lako Tukufu, kwamba eneo hili la Kisawasawa alilolitaja ambalo labda lilitengwa awali na mamlaka za wilaya au na mkoa na kukabidhiwa Wizara ya Elimu nimwondoe shaka na wasiwasi, Serikali bado ina mipango mingi na mikubwa eneo hili bado tuna uhitaji nalo na tutapanga utaratibu mwingine na miradi mingine ya kimaendeleo inaweza kupelekwa katika eneo hilo.

Mheshimiwa Spika, kuhusiana na swali lake la pili, kwamba fedha iliyopelekwa ni ndogo ni kweli, tumepeleka fedha milioni 45 kwa ajili ya kazi zile za awali ambayo ilikuwa ni masuala ya geotechnical survey, topographical survey pamoja na environmental and social impact assessment. Hivi sasa tayari fedha kwa ajili ya kazi zile za substructure pamoja na superstructure ela zake tayari tumeshazipata. Nadhani ndani ya wiki hii au wiki ijayo fedha hizo zitakwenda kule kwa ajili ya kuanza rasmi ujenzi huo wa majengo yale tisa kama tulivyoweka kwenye mpango wetu.
MHE. ABUBAKARI D. ASENGA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Nashukuru sana Serikali kwa kuanza mchakato wa barabara hizi za kufungua Mkoa wa Morogoro. Sasa kipande cha Ifakara - Lupilo kimetangazwa.

Sasa swali langu la kwanza, je, ni lini kipande cha Lupilo – Mahenge – Liwale kitaanza ujenzi?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa kuwa kipande hiki cha Ifakara – Lupilo kitapita by pass ya Ifakara Mjini ambako wananchi wa Kata ya Mbasa na Katindiuka wamesubiri kwa muda mrefu sana, zaidi ya miaka minne kulipwa fidia na Serikali yao.

Je, ni lini Serikali itawalipa fidia wananchi hawa pamoja na hasara ya kusubiri zaidi ya miaka minne? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kipande cha Barabara ya Lupilo – Mahenge - Liwale kina sehemu mbili. Kwanza kuanzia Lupilo hadi Mahenge ni barabara kuu ambayo itakuwa ni sehemu ya ujenzi kwenye barabara hii kubwa ambayo nimeitaja kwa mpango wa EPC, lakini kuanzia Mahenge kwenda Ilonga hadi Liwale tumesema mwaka huu tumeingiza kwenye mpango wa kuanza kuifanyia upembuzi yakinifu na usanifu, maana hiyo barabara haipo lakini Serikali kwa sababu ya maombi ya muda mrefu kuunganisha Mkoa wa Morogoro na Lindi tumeshaweka kwenye mpango wa kuanza kuifanyia kazi.

Mheshimiwa Spika, kuhusu by pass ya Ifakara; hii by pass ya Ifakara ni sehemu ya huo mpango mkubwa na kitakachofanyika sasa ni pamoja na kuhuisha zile tathmini zilizofanyika kwa wananchi ambao wataathirika na mradi huu kwa ajili ya kuwalipa fidia. Kwa hiyo watakuwa ni sehemu ya huo mradi mkubwa ambao tunaenda kuutekeleza, ahsante.
MHE. ABUBAKARI D. ASENGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Kwa kuwa Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan analeta fedha nyingi sana za miradi katika Halmashauri ya Mji wa Ifakara, na kwa kuwa miradi hiyo mingi haiendi vizuri na sababu moja wapo ni kukosekana kwa mtumishi Mkuu wa Idara ya Ujenzi;

Je, ni lini Serikali inapeleka injinia mzoefu wa majengo ya ujenzi Halmashauri ya Mji wa Ifakara ili kunusuru miradi hii?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imekuwa ikiajiri mainjinia, kulitokea changamoto ya kuwa na upungufu wa mainjinia katika halmashauri zetu nchini, baada ya kuanzishwa TARURA; mainjinia wengi wa halmashauri walihamia wakala wa TARURA. Mwaka wa fedha uliopita Serikali iliajiri mainjinia zaidi ya 265 ambapo kila halmashauri nchini ilipata injinia mmoja, na hivi sasa Serikali ipo katika mchakato wa kuajiri tena mainjinia kwa ajili ya kutoa upungufu huu ambao upo ikiwemo kule kwa Mheshimiwa Asenga na tutaangalia pale ambapo ajira hizi zitapatikana basi kule kwa Mheshimiwa Asinga nao watapata injinia.
MHE. ABUBAKARI D. ASENGA: Mheshimiwa Spika, tarehe 5, mwezi wa Nane Wizara ilisaini barabara ya kutoka Ifakara kwenda Mbingu na baadaye Mlimba. Je, ni lini ujenzi wa barabara hiyo utaanza?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, barabara hiyo itaanza kujengwa mara tu tutakapokuwa tumekamilisha taratibu zote ikiwa ni pamoja na mkandarasi kuanza kufanya mobilization, yaani kuandaa vifaa kwa ajili ya kuanza kuijenga hiyo barabara. (Makofi)
MHE. ABUBAKARI D. ASENGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Naomba kuuliza maswali madogo mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza namshukuru sana Mheshimiwa Waziri kwa kufanya ziara jimboni karibu mara mbili, ametembelea kiwanda cha Kilombero Sugar na Mang’ula Machine Tools pamoja na shamba hili la rubber.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza. Shamba hili ambalo lina ukubwa wa karibu hekari 1,678; sasa hivi kuna watu wachache kwa manufaa yao wanalikodisha kwa wananchi: Kwanini Serikali kupitia Serikali ya Kata isitoe uwazi eneo la shamba ambalo halijapandwa rubber, lilimwe na wananchi mpunga au miwa kwa uwazi tofauti na ilivyo sasa?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili. Ili kuweka ulinzi wa shamba hilo, tuliwasilisha ombi letu kwa Mheshimiwa Waziri kutoa sehemu ya shamba kwa maslahi ya maendeleo ya wananchi kwa ujenzi wa kituo cha polisi, high school na kituo cha afya: Je, ombi letu limefikia wapi?
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Ni kweli kulikuwa na changamoto hizi za uvamizi katika shamba hili la mpira. Namshukuru sana Mheshimiwa Mbunge kwa kuleta taarifa hii ambayo kimsingi hairuhusiwi watu kufanya shughuli nyingine nje ya shughuli tarajiwa katika shamba hili la mpira.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama kuna uvamizi huo, naomba niielekeze NDC waweze kufuatilia ili kama kweli kuna haja ya wananchi kutumia maeneo ambayo hayajaanza kuendelezwa kwa kupanda miti ya mpira, basi tuone namna ya utaratibu mzuri kama ambavyo ameshauri Mheshimiwa Mbunge kupitia viongozi wa Kata na eneo husika ili wananchi wa pale waweze kufaidika na kutumia eneo hilo ambalo ni la Serikali, kwa utaratibu kamili. Kimsingi, eneo hili ni la kuzalisha miti kwa ajili ya mpira.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili kama alivyosema Mbunge, Mheshimiwa Waziri amepitia katika shamba hili, tunaendelea kujadiliana tuone namna gani tunaweza kuwezesha huduma hizi za kijamii kwa maana ya shule, vituo vya afya au kituo cha polisi, tuone kama vinaweza kujengwa katika eneo hili la shamba ambapo kimsingi ni kwa ajili ya uzalishaji wa mpira, nakushukuru.
MHE. ABUBAKARI D. ASENGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Naipongeza Serikali kwa nia yake ya kuwa tayari kwa mafunzo haya, na Wabunge wengi tulioenda katika yale mafunzo tulikuwa tunapata maswali mengi sana ya Wakuu wa Idara na baadhi ya Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi wanaotaka kwenda kwa kujitolea, walikuwa wanauliza ni utaratibu gani ambao wanaweza kuufuata ili kushiriki mafunzo haya? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaishukuru sana Kambi ya Makutupora hapa, imetupa mafunzo mazuri sana na tunatoa ombi kwa Wabunge ambao hawajaenda waende kwa sababu kila siku wanatuambia kwenye group kwamba vifaa vyao viko pale. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, maswali yangu mawili ya nyongeza. La kwanza: Je, ni lini intake nyingine ya Wabunge na viongozi wa wilaya ambao wako tayari itaenda? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili. Kama nilivyosema, Kambi ya Makutupora iko hapa Dodoma, ni kaibu: Je, Serikali ina mpango gani wa kuongeza fedha ya bajeti kwa sababu JKT ni taasisi ya Kiserikali ili Kambi ile jirani ya Makutupora iweze kutoa mafunzo vizuri zaidi na kwa ufanisi zaidi, ikiwemo kujenga mabweni, vitanda na kadhalika?

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA K.n.y. WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Abubakari Damian Asenga, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba Waheshimiwa Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mara kadhaa wamekuwa wakienda kwenye kambi hizi kwa ajili ya kushiriki kwenye mafunzo haya ambayo yana nia ya kuwajenga Waheshimiwa Wabunge. Ni kweli kwamba wapo baadhi ya Waheshimiwa Wabunge hawajapata fursa hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kikubwa niwaambie tu kwamba mara nyingi sababu zinazosababisha hizi, kwanza ni nafasi yetu sisi kama Waheshimiwa Wabunge kwa sababu ya majukumu ambayo tunayo. Lingine kubwa ni kutokana na utaratibu. Nawaomba Waheshimiwa Wabunge kupitia Bunge hili, kama tulivyoeleza katika jibu la msingi, iombwe ruhusa, kwa maana ya kwamba tuombwe kibali maalum ili Jeshi la Kujenga Taifa liweze kutoa fursa hiyo ya Wabunge wengine kuweza kuendelea ama kupata mafunzo hayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine niseme tu kwamba, kwa kuwa mafunzo haya yamelenga katika kuwajengea uzalendo, kuwajengea utayari, ukakamavu na ujasiri Waheshimiwa Wabunge na viongozi wengine wa taasisi nyingine, nimwambie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba tutajitahidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ilivyoelezwa katika jibu langu la msingi, kwamba suala la uchangiaji gharama ni jambo la msingi; na kwa sababu tunatakiwa tuchangie gharama hizi kwa sababu ya mahitaji maalum yakiwemo afya, matibabu, chakula na vifaa vingine, lakini nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba katika bajeti inayofuata tutajitahidi tuongeze fungu maalum kwa ajili ya kutoa huduma hizi za mafunzo kwa Waheshimiwa wengine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru.
MHE. ABUBAKARI D. ASENGA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Barabara ya kutoka Ifakara – Lumemo – Michenga – Idete mpaka Mlimba imeshatangazwa; je, ni lini ujenzi wa barabara hiyo utaanza?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, ahsante ni kweli kwamba barabara hiyo imeshatangazwa na nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tutajenga kilometa 100 na tuna lots mbili. Kinachosubiriwa sasa hivi ni kusaini mikataba na wakandarasi ambao wamepatikana kwa ajili ya kuanza ujenzi huo wa barabara, ahsante.
MHE. ABUBAKARI D. ASENGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Naishukuru Serikali kwa kututengea fedha kwa ajili ya mradi huu. Kwa kuwa Mkurugenzi wa Umwagiliaji aliahidi kwenda yeye mwenyewe, nataka kujua: Je, Mheshimiwa Naibu Waziri, atamwelekeza lini aende kutembelea mwenyewe mradi huu wa Kisawasawa kwa sababu aliahidi wakati wa Bunge hapa?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili. Kwa kuwa Kijiji cha Lungongole Tarafa ya Ifakara nako wana eneo linalofaa kwa umwagiliaji hasa wakati wa kiangazi: Je, ukimwagiza aende Kisawasawa, uko tayari kumwagiza aende na Lungongole ili tathmini pia ianze? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu maswali ya Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, nitamwelekeza Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji kufika Kilombero mapema kadiri iwezekanavyo. Kuhusu eneo lake la pili, bahati nzuri tulisaini mkataba hapa wa kuajiri Washauri Waelekezi kwa ajili ya kuyapitia mabonde yote nchini likiwemo Bonde la Ifakara - Idete. Kwa hiyo, nimwondoe hofu Mheshimiwa Mbunge kwamba tayari tunayo Kampuni pale ya Clemence na Vibe International Company Limited wako tayari na wako 13% ya kufanya usanifu katika eneo hilo. Kwa hiyo, mradi huo pia utajumuishwa katika skimu ambayo itatengenezwa hapo katika Bonde la Ifakara.
MHE. ABUBAKARI D. ASENGA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru na ninashukuru Serikali kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri.

Mheshimiwa Spika, kuna academies za mchezo wa mpira wa miguu kama vile Kilombero Soccernet Academy ambazo zimesajiliwa rasmi na ziko pale Wilaya ya Kilombero, lakini zina uhaba mkubwa wa vifaa.

Je, kwa dharura, Wizara haioni kwamba inaweza ikachukua hatua za kutafuta vifaa, hata kama ni mipira, jersey, ikazipelekea hizi academies ambazo zimesajiliwa rasmi na TFF?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, nilimwomba Mheshimiwa Naibu Wazri mipira 100 ya vijijini na aliniahidi atanipatia; je, lini tunakwenda kukabidhi mimi na yeye mipira hiyo Ifakara na kukiamsha pale Ifakara Mjini? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Spika, ahsante, kama nilivyosema kwa sasa Serikali inachoweza kufanya kutokana na upatikanaji wa fedha ni kupunguza kodi kwenye vifaa vya michezo kama vile nyasi bandia na viambata vyake. Haya mengine kwa kadri fedha zitakavyopatikana tutaendelea kuvi-support vituo hivi na kuhakikisha vinapata nguvu kupitia Serikalini vilevile, ahsante.

MHE. ABUBAKARI D. ASENGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru, na ninaishukuru Serikali kwa majibu hayo, lakini swali la kwanza; kwa kuwa Ifakara ni katikati ya Wilaya za Kilombero, Malinyi na Ulanga, na mahitaji ya kuwepo kwa tawi ama kituo cha mitihani ni makubwa mno: -

Je, Serikali ina mkakati gani wa kuanzisha Tawi dogo la Chuo Kikuu Huria?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; endapo halmashauri itatoa eneo kwa sasa: -

Je, Serikali iko tayari kujenga Tawi la Chuo Kikuu Huria ama tawi la chuo kikuu kingine chochote? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Abubakari Damian Asenga, Mbunge wa Kilombero, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyokwisha jibu katika majibu ya swali la msingi, lakini Mheshimiwa Asenga anataka kufahamu, japo kuwa pale tuna Kituo cha Chuo Kikuu Huria ambacho wanafanyia mitihani bado ana msisitizo huo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimwondoe wasiwasi Mheshimiwa Asenga; Chuo Kikuu Huria kinao utaratibu wa kuwa na vituo vya mitihani katika ngazi za wilaya pamoja na kata kulingana na uhitaji wa maeneo hayo. Lakini vilevile kina utaratibu wa kuweza kuanzisha matawi au vituo hivyo vya kuratibu mitihani katika makambi yetu ya majeshi pamoja na kambi mbalimbali za wakimbizi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo Mheshimiwa Asenga naomba tu nikuhakikishe kwamba Serikali itaendelea kufanya tathmini ya kina katika eneo hilo ulilolitaja la Kilombero, Ulanga na kule Malinyi na maeneo mengine nchini, na kuweza kuona kama uhitaji huo upo ili tuweze kuanzisha ama vituo au matawi ya Chuo Kikuu Huria.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika eneo la pili, kwanza tuishukuru Halmashauri ya Ifakara, lakini tukushukuru wewe binafsi kwa jitihada zako za kutenga eneo kwa ajili ya Chuo Kikuu Huria. Naomba nikuhakikishie kwamba Serikali itaendelea kufanya tathmini, pamoja na uwepo wa maeneo haya, lakini vilevile kuna uhitaji wa rasilimali fedha pamoja na uhitaji wa rasilimali watu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, hivi vyote vikichanganywa ndipo tunakwenda kuanzisha matawi haya ya chuo kikuu, lakini vilevile uhitaji wa hilo tawi katika eneo hilo. Kwa hiyo, baada ya tathmini hii tutajihakikishia sasa kama upo umuhimu wa kwenda kuanzisha tawi katika eneo la Ifakara au la, nakushukuru.
MHE. ABUBAKAR D. ASENGA: Mheshimiwa Spika, nashukuru. Ukizingatia majibu mazuri ya Serikali ni kwamba tumebakiwa takribani na mwezi mmoja mpaka kufikia mwisho wa mwaka wa Serikali.

Swali la kwanza je, ni lini tutaenda kusaini mkataba huo kwa ajili ya kuanza mradi huo wa miji 28 wa Kiburubutu?

Mheshimiwa Spika, swali la pili je, Serikali itakuwa tayari kwenda kusainia mikataba ya miradi ya miji 28 site maeneo ya matukio ilikuwathibitishia wananchi wa Jimbo la Kilombero kuwa Serikali ya CCM inaendelea kuupiga mwingi sana?

NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, ahsante; naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Abubakari kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, wakati wowote mradi huu utakwenda kusainiwa kwa umuhimu wake na heshima kubwa na kazi kubwa aliyoifanya Mheshimiwa Rais wa kuhakikisha mradi huu sasa unaenda kwenye utekelezaji wakati wowote Mheshimiwa Rais akipata nafasi naamini tutakwenda kusaini mkataba huu kwa wingi wake.

Mheshimiwa Spika, swali lako namba mbili sasa Wizara tumejipanga tutaelekea kwenye hii miji 28 yote tutatawanyika na kila eneo husika tutasaini mkataba hapo.
MHE. ABUBAKAR D. ASENGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naomba kumuuliza Mheshimiwa Naibu Waziri kwamba kwa kuzingatia kuwa Mkoa wa Morogoro ni ghala la Taifa na katika Jimbo letu la Kilombero kuna miradi mingi ya umwagiliaji; Mradi wa Kisawasawa, Mkula na Sanje inasuasua. Je, Mheshimiwa Naibu Waziri atakuwa tayari kuambatana na mimi angalau weekend moja akajionee kusuasua kwa miradi hii ili Serikali ichukue hatua haraka za kuinusuru?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Abubakar Asenga, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, niko tayari kuongozana naye, tutakwenda kuangalia ili tuone namna ya kuweza kukamilisha miradi hii.
MHE. ABUBAKARI D. ASENGA: Mheshimiwa Spika, pamoja na furaha tuliyonayo wananchi kuhusu mambo yaliyotokea Jumamosi huko Mwanza naomba kuuliza swali dogo la nyongeza. (Makofi)

Wakati wenzetu wanang’ang’ania vituo vya Kata vya Tarafa Wilaya ya Kilombero ina Kata 35 na haina Kituo cha Polisi cha Wilaya; je, ni lini Serikali itajenga Kituo cha Polisi cha Wilaya ya Kilombero?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Asenga, Mbunge wa Kilombero kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, tumeshazungumza na Mbunge hiyo changamoto yake ya kituo, lakini tumesema katika maeneo yatakayopewa kipaumbele katika miaka ijayo tukianza na mwaka wa fedha 2022/2023 ni maeneo ya Wilaya ambayo hayana kabisa Vituo vya Polisi. Kwa hiyo matarajio yangu ndani ya mwaka mmoja miwili ijayo tutakuwa tumeanza ujenzi wa Kituo cha Polisi cha Wilaya ya Kilombero kama ilivyoombwa na Mheshimiwa Mbunge.