Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Juliana Didas Masaburi (5 total)

MHE. JULIANA D. MASABURI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, napenda kuwashukuru Serikali kwa majibu yao mazuri, lakini je, Serikali imejipangaje hasa kuwachukulia hatua hawa wawekezaji ambao wanapewa hivi viwanda na wanavitelekeza na wanaenda mbali zaidi wanavichukulia mikopo na kuviacha hapo? Serikali imejipangaje kisheria kuwabana aina hii ya wawekezaji? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Juliana Didas Masaburi kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeshaanza kuchukua hatua na ndiyo maana tumeona katika viwanda vile 68 ambavyo vilikuwa haviendelezwi tayari hivi 20 vimesharejeshwa Serikalini. Lakini pia tunaendelea kuvitathimini na hivyo vingine.

Kwa hiyo niwahakikishie watanzania na Mheshimiwa Juliana Masaburi na Wabunge wote kwamba Serikali ipo makini kuona sasa wawekezaji wote watakaoingia mikataba ya kuviendeleza viwanda katika sekta zote pale ambapo watakiuka masharti ya mikataba tutakayoingia nayo sheria zitachukuliwa na hatua mahsusi ikiwemo kuwanyang’anya viwanda hivyo vitachukuliwa ili kuhakikisha sasa tunapata wawekezaji makini ambao kweli wataleta tija katika uendelezaji wa sekta ya viwanda nchini. Ahsante sana.
MHE. JULIANA D. MASABURI: Mheshimiwa Spika, namshukuru Mheshimiwa Waziri kwa majibu yake mazuri, lakini nina swali moja la nyongeza. Inasemekana samaki na dagaa za Ziwa Victoria zina madini ya zebaki: -

Je, Serikali imefanya tafiti juu ya hili? (Makofi)
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Spika, awali ya yote naomba kumpongeza sana dada yangu Mheshimiwa Juliana, kwa kweli yeye ni mwanamazingira mzuri sana. Katika upande huo kuhusu samaki na dagaa wanaopatikana katika Ziwa Victoria kwamba inasemekana wana madini ya zebaki, jambo hilo tuseme kwamba si sawasawa kwa sasa hivi, kwa sababu tunafahamu kwamba tuna-export samaki wengi nje ya nchi na samaki hao wamekuwa wakinufaisha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wataalamu wetu hivi sasa wanaendelea kufanya kazi kubwa ya kuhakikisha kwamba katika suala la kanda ya ziwa matumizi mbalimbali ya kemikali yanadhibitiwa, lakini hata hivyo mpaka hivi sasa tafiti mbalimbali zimefanyika na hazijaonyesha kwamba samaki hawa wanaathirika.

Kwa hiyo, kikubwa zaidi tuwaombe wananchi katika maeneo mbalimbali kuendelea kuzingatia masuala mahususi ya kimazingira kwa lengo kubwa la kuendelea kulinda Taifa letu kwa ujumla wake.

Mheshimiwa Spika, ahsante sana. (Makofi)
MHE. JULIANA D. MASABURI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Pamoja na majibu hayo ya Serikali ambayo bado hayaridhishi napenda kuiuliza Serikali; tangu nimeandika hili swali najua kuna shirika la TBS najua kuna Tume ya Ushindani; lakini bidhaa fake hasa vipodozi, vyakula vimezidi kuzalishwa nchini na kuingizwa kwa kasi ya juu. Naomba majibu sahihi ya Serikali nini wanapanga kudhibiti bidhaa fake? (Makofi)
NAIBU WAZIRI UWEKEZAJI, VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. Napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Juliana Didas Masaburi Mbunge kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli changamoto ya bidhaa fake ni ya kudumu. Na kwa namna ambavyo tunajua lazima tuendelee kudhibiti. Serikali inaendelea kufanya juhudi mbalimbali.

Mheshimiwa Spika, mojawapo ya changamoto tuliyonayo ni upungufu wa watumishi katika taasisi zetu hizi za TBS na FCC. Hata hivyo tunaendelea kuboresha ili kupata watumishi wa kutosha. vilevile tunaweka nguvu au mkazo kwenye elimu kwa umma, kwasababu bidhaa fake au bidhaa hizo au vipodozi hivi vinavyoingizwa ni kwasababu ya mahitaji ambayo Watanzania wanahitaji. Kwa hiyo, tukiwapa elimu sahihi maana yake vitakosa soko au uhitaji wa bidhaa hizo. Kwa hiyo tutaendelea kutoa elimu pamoja kuimarisha zaidi kwa kuhakikisha tunapata watumishi wa kutosha ili wasaidie kudhibiti mianya ambayo inatumika kuingiza bidhaa hivi fake na vipodozi ambavyo vinakosa sifa za kutumika kwa ajili ya kudhibiti soko la Tanzania.

Mheshimiwa Spika, nakushukuru.
MHE. JULIANA D. MASABURI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kumekuwa na wimbi kubwa la wazazi kuwafanyia vitendo vya kikatili watoto. Je, Serikali inampango gani wa kuwajengea watoto uwezo au uelewa mashuleni wa kujitetea pindi wanapopitia ukatili wa kijjinsia?
NAIBU WAZIRI WA MAENDELEO YA JAMII, JINSIA,WANAWAKE NA MAKUNDI MAALUM: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, katika kukubaliana na hili, Serikali inatekeleza afua mbalimbali za kutoa elimu za malezi na makuzi, pamoja na elimu ambayo inakabiliana na ukatili dhidi ya watoto. Aidha, kuimarisha Kamati ya Ulinzi na Usalama wa Wanawake na watoto zilizopo ngazi zote nchini kwa ajili ya kuwa elimu wananchi wa jamii yetu.
MHE. JULIANA D. MASABURI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Swali langu ni dogo. Je ni lini mradi wa kilomita mbili za nyongeza katika mradi wa REA III round two utaanza kutekelezwa katika Mkoa mzima wa Mara?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema kwa Mheshimiwa Getere nipende kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Masaburi kwamba tunatarajia Ijumaa ya wiki hii wenzetu wa REA watakaa na wakandarasi. Tayari wameshapewa idhini ya kuendelea na maeneo hayo ya kutekeleza kilomita mbili na wakishasaini mikataba mwishoni mwa wiki hii tunatarajia mwanzoni mwa mwezi unaokuja kazi itaanza na kwa kuwa ni kazi ndogo tunatarajia itakamilika pamoja na kazi kubwa mwezi Desemba mwaka huu kwa sababu ni kupeleka line ndogo za kuwasha umeme katika vijiji vyote ambavyo vilikuwa katika REA III round two kwa maana ya kuongeza kilomita mbili kwa kila kitongoji. Nakushukuru.