Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Juliana Didas Masaburi (4 total)

Hotuba ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyoitoa wakati wa Ufunguzi wa Bunge la Kumi na Mbili, Tarehe 13 Novemba, 2020
MHE. JULIANA D. MASABURI: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi hii name niweze kuchangia hotuba ya Mheshimiwa Rais alipofungua Bunge letu la Kumi na Mbili.

Mheshimiwa Spika, kwanza na mimi kwa vile ni mara ya kwanza kusimama hapa kwenye Bunge lako tukufu napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema kwa kunipa kibali kuwa mmoja wa Wabunge. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pili, nikishukuru Chama changu cha Mapinduzi, kwa kutupa nafasi za upendeleo hasa sisi mabinti vijana kuja kwenye Bunge lako kuwawakilisha vijana wote Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba niende moja kwa moja kwenye kuchangia hotuba ya Mheshimiwa Rais, kwenye hotuba ya Mheshimiwa Rais wakati anafungua Bunge aliongelea kuhusu ukuzaji wa uchumi, katika ukuzaji wa uchumi aligusia kuhusu Serikali kuongeza jitahada za kuwezesha wananchi wake kiuchumi, lakini pia alisema kuwapatia mikopo ambayo haina riba au yenye riba nafuu. Hii mikopo napenda kuwapongeza Serikali kwamba Halmashauri zetu kote nchi inatoa hii mikopo ya asilimia 10 kwa vijana, akinamama na walemavu, na inafanya vizuri sana kusema kweli. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini bado hii mikopo haitoleta matokeo chanya kama tuvyotarajia, kwa sababu kwanza zile pesa ambazo zinatolewa na Halmashauri ni ndogo lakini pia Halmashauri au Serikali imesema kwamba mikopo hii itolewe kwa vikundi mbali za vijana, akinamama na walemavu, kwenye vikundi sio kila kijana wana idea ya kuwa pamoja na jinsi gani ya kufanya biashara. kwa hiyo, wanajikuta wanachukua hii mikopo baada ya kuchukua hii mikopo wanaanza kugombana kwa sababu kila mtu ana idea yake na kikundi kinavunjika. Vikundi vinavyovunjika pia mikopo ile iliyochukuliwa kwenye Halmashauri haiwezi kurejeshwa kwa wakati, kwa hiyo, inapelekea hii mikopo kutoonekana faida yake kubwa kwa vikundi ambavyo vinachukua mikopo na hasa vijana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ningependa pia kuishauri Serikali ingeangalia ni jinsi gani inaweza kumwezesha kijana mmoja mmoja kuchukua hii mikopo amesema Mbunge mwenzangu wa vijana pale Mheshimiwa Asia kwamba kijana mmoja akiji- commit akachukua mkopo akaaminiwa akachukua mkopo ni rahisi kurejesha kwa wakati ili kijana mwingine au watu wengine waweze kukopa zaidi. Lakini yule kijana pia ataajiri vijana wengine nyuma yake, watano au kumi atakuwa ameongeza ajira kwa vijana zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ningependa kuishauri Serikali iangalie jinsi gani inamsaidia sasa kijana benki zetu nchini Tanzania hazi-support vijana sana. Unakuta benki wanakwambia ukienda na business idea wanakwambia kwamba ni lazima uwe na collateral au uwe na bank statement kuanzia miezi sita, mwaka au miaka mitatu. Sasa kijana kama mimi nimetoka kwenye chuo VETA nina ujuzi, nina kila kitu, sina hiyo collateral, sina hiyo bank statement sina cash flow nitawezaje kuanzisha biashara bila kuangalia mfumo mzuri wa kutu-support vijana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia benki zetu zimekuwa rahisi sana kukopesha wafanyabiashara wakubwa, sisi Wabunge na wafanyakazi wa Kiserikali, lakini vijana imeweka kwamba ni lazima wawe na security. Ningependa kuishauri Serikali iangalie ni jinsi gani itakaa na hizi taasisi za kifedha itaangalia ni jinsi gani inaweza kumsaidia kijana mwenye idea nzuri ya kibiashara iweke tu uaminifu, kijana ana business idea nzuri, anachokiongea anakijua, anaweza kufanya biashara imuamini imwezeshe afanye biashara. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Rais wakati anafungua hili Bunge…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha muda wa Mzungumzaji)

MHE. JULIANA D. MASABURI: Mheshimiwa Spika, ahsante naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. JULIANA D. MASABURI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kunipa nafasi hii niweze kuchangia hotuba hii ya Mheshimiwa Waziri Mkuu. Sote tunafahamu kwamba kuna ongezeko kubwa sana nchini la mashine za kamari almaarufu kama beting za kachina na mashine hizi zinafungwa sana kwenye mikusanyiko ya masokoni, kwenye vituo vya daladala, vituo vya taksi bajaji na bodaboda. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mashine hizi za kamari sasa hivi zinaingizwa hapa nchini kama spear parts na zinakuja kuwa-assembled hapa hapa nchini kwa hiyo, nina wasiwasi kwamba TRA haina idadi Kamili za mashine hizi za kamari ambazo zipo nchini. Hii inawezesha TRA kukosa mapato yake kihalali. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mashine hizi za kamari zipo hapa nchini kwenye maduka mpaka ya Mangi ambazo TRA kule kwenye maduka ya Mangi hawana ofisi zake. Kwa hiyo, inashindwa kuhakiki na inashindwa kukusanya kodi zake ipasavyo ninaushauri kwa Serikali kwenye suala hili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza naomba Serikali ifanye uhakiki upya wa kutoa leseni kwenye mashine hizi za kamari leseni kwa mashine moja moja mashine moja inapewa leseni moja hii itasaidia Serikali kupata idadi kamili za mashine zilizopo lakini na kukusanya kodi yake ipasavyo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini sote tunajua kama kamari ni kitu haramu na baadhi ya nchi haziruhusiwi kabisa lakini naomba kushauri Serikali pia kuweka sheria kali ambazo zitamlinda kijana zitamlinda mtoto mwanafunzi siyo tu wanavyosema kuanzia miaka 18, ningeshauri Serikali iweke hata kuanzia miaka 25 kwasababu kijana wa miaka 18 bado hajaweza kujipambanua na wanaingia kwenye huu mtego wa kamari hizi tunaenda kupoteza nguvu kazi ya Taifa. Unakuta mwanafunzi sasa hivi haendi darasani anatoka nyumbani anaenda shule lakini anaishia hapo katikati kwenye kucheza hizi kamari. Kwa hiyo, naomba Serikali iliangalie hili suala kwa umakini zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kama Serikali itaona kuna haja ya kuendeleza hii kamari za mtaani lakini haikusanyi kodi yake ipasavyo. Kwa mwezi TRA inawatoza hawa wafanyabiashara ya kamali shilingi 100,000 lakini wao kwa siku wanafunga Sh.300,000 mpaka shilingi 700,000 na kwa mwezi wanafunga shilingi 9,000,000 mpaka Sh.21,000,000. Napenda kuishauri Serikali iangalie suala hili kwa makini zaidi, kwanza ni vitu ambavyo vinaenda kuharibu vizazi vyetu huko nje, kwa hiyo, kama kodi wa wachatozwe kodi kweli kweli. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, yangu ni hayo, naunga mkono hoja. (Makofi)
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2022 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024
MHE. JULIANA D. MASABURI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante na mimi niungane na wenzangu Wabunge wenzangu kwanza kumpongeza Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan lakini kipekee pia kumpongeza Waziri wa Fedha Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba. Kusema ukweli wote mnastahili maua. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitaenda kwa haraka haraka kwa ajili ya muda. Kwanza napenda kuchangia kwenye mambo matatu. Jambo la kwanza ni cargo consolidation na deconsolidation kusajiliwa kwa store na mfumo wa EFD Machine. Nikianza kwenye consolidation na deconsolidation. Kuna tatizo hasa kwenye hawa wasafirishaji wa mizigo ambao wafanyabiashara wakienda kwa mfano China, Uturuki, Marekani nchi yoyote wanaenda kununua mizigo kwa ajili ya kuleta nchini kwa ajili ya mauzo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hawa wafanyabiashara wengi wanatumia wasafirishaji wa mizigo ambao kitaalam kwa lugha yao TRA wanaitwa consolidation na hao consolidation kazi yao kubwa inakuwa kukusanya mizigo ya wafanyabiashara wengi na kuweka kwenye cover moja au container moja. Sasa nachangia kuhusu hili kwa sababu gani? Kwa ajili ya mgogoro mkubwa uliotokea kama mwezi uliopita pale Kariakoo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hawa consolidators ambao wanafanya biashara ya kukusanya mizigo ya wafanyabiashara wadogo wadogo na kuingiza nchini mfumo huu Serikali ilikuwa na nia njema kabisa kwa ajili ya kuandaa mfumo huu wa hawa wasafirishaji kukusanya mizigo ya wafanyabiashara. Walikuwa na nia njema kabisa na walikuwa sahihi lakini Mheshimiwa Waziri wa Fedha mfumo huu ndiyo unawasababishia kukosa kodi halisi, kwa sababu gani?

Mheshimiwa Mwenyekiti, mfanyabiashara anapoenda Guangzhou au nchi yoyote ile anaenda kununua mzigo anapewa risiti kwenye manunuzi yake. Anaenda kwenye maghala kule Guangzhou au Beijing au popote, consolidator anachukua ule mzigo kwa nia ya kumsafirishia mpaka nchini kwake na consolidator anapofika hapa nchini anaingiza ule mzigo kwanza kwenye forodha anaingiza ule mzigo anasema yeye ni consolidator, anaingiza kwa pamoja lakini kwenye ulipaji wa kodi Mheshimiwa Waziri wa Fedha hawa consolidators wanatumia mbinu za kukwepa kulipa kodi halisi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda pale kwa kamishna wa TRA wa kodi za ndani wakiwa wanakaguliwa wanaingiza hii mizigo kwa majina yao au kwa kampuni zao na remind you Mheshimiwa Waziri wa Fedha wakishaingiza hii mizigo kwa majina yao kwa kampuni zao wanalipia ile mizigo wao wenyewe pale TRA. Wakishailipia ile mizigo wanaenda sasa nje kwenye maghala yao mizigo ikishatoka wanawapa wafanyabiashara wale mizigo yao bila kuwapa risiti zao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo linakuja sasa afisa TRA anapoenda Kariakoo kukagua mahesabu ya wafanyabiashara au mizigo tatizo linakuja wale wafanyabiashara wanakuwa hawana risiti halisia kabisa na ndiyo maana wanapokuwa wanakisiwa kodi wanasema wanaonewa kwa sababu kiukweli wanakuwa hawana kumbukumbu ya risiti na risiti zinabaki kwa msafirishaji. Nia ilikuwa njema lakini naona inafanyika vibaya sana sasa hivi.

TAARIFA

MHE. TARIMBA G. ABBAS: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Tarimba taarifa.

MHE. TARIMBA G. ABBAS: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze sana kwa mchango mzuri Mheshimiwa Mbunge. Nataka nimwambie sababu hiyo ndiyo inayofanya ulipaji wa VAT uwe mgumu kwa sababu kodi ya VAT ni input tax na output tax. Sasa bila kuwa na VAT uliyolipa wakati ukiingiza mzigo huwezi ukatoa risiti kwa minajili ya kulipia VAT wakati ukiuza na ndiyo maana kuna bei ya bila risiti na bei ya risiti. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Juliana Masaburi, unaipokea hiyo taarifa?

MHE. JULIANA D. MASABURI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napokea taarifa hiyo ahsante sana Mheshimiwa Mbunge wa Kinondoni Mheshimiwa Abbas Tarimba. Sasa kama Mheshimiwa Abbas Tarimba alivyosema kwa hiyo hapa kuna tatizo Mheshimiwa Waziri na ninakuomba sana ili pia uwaziri wako siku ukiondoka uache legacy hili suala linatakiwa kushughulikiwa haraka na ipasavyo na hili suala la hawa consolidators unawaona hata wafanyabiashara wenyewe hawalalamiki kwa sababu kwanza wanapata faida. Wanapata faida sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pale Kariakoo nilienda kuhudhuria sijamsikia mtu kulalamikia kuhusu hawa wasafirishaji consolidators kwa sababu they know wanapata profit, I mean triple. Umeona Mheshimiwa Waziri wa Fedha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ushauri wangu ni nini? Ushauri wangu sawa kuwe na hawa consolidators wasafirishaji hawawezi kuepukika kwa ajili ya urahisi wa kusafirisha mizigo ya wafanyabiashara lakini Wizara yako na TRA waone njia sahihi ya ku-accommodate hawa wasafirishaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependekeza mfanye kama ile bonded warehouse ya magari. Mizigo ikishafika ikae waipeleke kwenye bonded warehouse kila mfanyabiashara akafutae mzigo wake apewe risiti zake, akalipe kodi mwenyewe. Hii itasababisha kwanza Serikali nyinyi kupata kodi zenu halisi lakini pia wafanyabiashara kutoogopa kwamba kuwe na point kwamba kuna mlolongo wa watu au foleni au nini lazima kila mfanyabiashara alipe kodi kwa sababu ya mahesabu ya kampuni yake au biashara yake kuwa safi na sahihi. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. JULIANA D. MASABURI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Makadirio na Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi
MHE. JULIANA D. MASABURI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi hii nami niweze kuchangia bajeti hii ya Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ningependa kumpongeza Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mama yetu Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kufanyakazi njema kwa Taifa letu, lakini pili ningependa kupongeza Chama changu cha Mapinduzi kwa kuendelea kusimamia Ilani ya Chama cha Mapinduzi kwa viwango vya hali ya juu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa niende moja kwa moja kwenye mchango, nitaanza kuchangia kuhusu barabara. Pale Musoma tuna barabara ambayo inaanzia Musoma Mjini kupitia Makojo mpaka Busekera ambayo ina urefu wa kilometa 92. Lakini nimesoma hotuba ya Mheshimiwa Waziri wameanza kujenga kilometa tano tu kwa kiwango cha lami, kilometa takribani 87 hawajazieleza zitajengwa lini. Sasa Mheshimiwa Waziri akija ku-windup hoja yake ningependa kujua commitment ya Serikali ni lini watamalizia kujenga hizi kilometa zilizobaki kwa kiwango cha lami, kwani barabara hii ni muhimu sana kwa wananchi wa Musoma Mjini mpaka Musoma Vijijini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili; ningependa kuongelea kuhusu airport yetu ya pale Musoma, kwanza naishukuru Serikali kwa kufanya ukarabati wa ile airport, lakini Mheshimiwa Waziri utakubaliana na mimi ile runway ambayo ndiyo uwanja wa ndege wenyewe ni ndogo sana. Kwa hiyo, itasababisha ndege kubwa kutoweza kutua. Ningependa kuishauri Serikali iweze kwenda pale kuongea na wananchi ambao wanakaa karibu na maeneo yale na kuyanunua yale maeneo ili kupanua ile airport ili ndege kubwa ziweze kutua. (Makofi)

MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.

MWENYEKITI: Taarifa.

T A A R I F A

MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nampa taarifa mdogo wangu kwa mchango wake mzuri, uwanja wa ndege wa Musoma ni muhimu sana kwa wananchi wa Mkoa wa Mara na Serikali imekuwa ikiahidi mara nyingi lakini hawaujengi huo uwanja wa ndege na hasa ukizingatia Mkoa wa Mara unahistoria ya kumtoa mpiganaji wa uhuru wa nchi hii, lakini uwanja wa Musoma haupo kwenye hadhi yake. (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Juliana Masaburi unaipokea taarifa hiyo.

MHE. JULIANA D. MASABURI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naipokea taarifa hiyo kutoka kwa dada yangu, senior, Mheshimiwa Ester Bulaya.

Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri tungependa sana huu uwanja uwe ni uwanja wa viwango vya hali ya juu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la tatu; ningependa kuongolea bandari kuu ya pale Musoma Mjini; Mkoa wa Mara ni moja ya mkoa mkongwe sana lakini maendeleo yake ni maendeleo hafifu na duni, yote hii inasababishwa kwasababu hakuna mzunguko mkubwa wa kibiashara. Mheshimiwa Waziri kwenye hotuba yako hapa sijaona umeongelea kuhusu ile bandari, ningependa ukija kuhitimisha hoja yako pia uniambie mkakati wako wakuifufua ile bandari kwani bandari ile ni muhimu hasa kwa vijana italeta ajira, lakini ita-stimulate… (Makofi)

MHE. JAFARI W. CHEGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.

MWENYEKITI: Taarifa.

T A A R I F A

MHE. JAFARI W. CHEGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na mchango mzuri sana wa mdogo wangu wa Mheshimiwa Juliana Masaburi, ni kweli kabisa hii bandari ile kipindi cha miaka ya nyuma Wakenya, Waganda walikuwa wanakuja kuchukua samaki zinazovuliwa na maeneo ya wavuvi wote wa Mkoa wa Mara, lakini si hivyo tu, tulikuwa tunamali ambayo ilikuwa ikitoka Mwanza, Bukoba inapita pale Musoma inatua kwenye bandari ile kwenda Kenya. (Makofi)

Kwa hiyo, anachochangia Mheshimiwa Juliana ni kwamba bandari ile ni muhimu sana katika ukuaji wa uchumi wa Mkoa mzima wa Mara. Kwa hiyo nafikiri nataka nimuongozee kwenye hilo ili Mheshimiwa Waziri naye ali-consider hili kama mchango wa Mheshimiwa Mbunge.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Juliana Masabauri unaipokea taarifa hiyo?

MHE. JULIANA D. MASABURI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kaka yangu, Mheshimiwa Chege, napokea taarifa yako. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, najua Mheshimiwa Waziri anajua umuhimu wa hii bandari nanaomba ukija kuhitimisha hoja yako utuambie mkakati wako watu wa Mara ni nini unategemea kufanya kufufua bandari hii? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho, nianzie alipoishia kaka yangu Mheshimiwa Jerry kuhusu Kampuni ya Sinohydro. Mheshimiwa Waziri Mbarawa hii kampuni ni thuma amanu, thuma kafaru, haitufai Watanzania, hii kampuni ni danganyifu, haimalizi miradi, hailipi madeni yaani sijui hata ipo akhera, sijui wapi mimi hata sielewi, lakini hawa Wachina hawatufai na kwa ufupi hii kampuni inahujumu nchi yetu na bado tunaendelea kuipa kazi nyingi.

Kwa hiyo, Mheshimwia Waziri mimi ningependa ulichukulie hili suala serious na una vyombo vya kuchunguza, mchunguze hii kampuni kwa nini mnaing’ang’ania? Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbarawa kwa kipekee kabisa ningependa pia ukija kuhitimisha hoja yako nadhani utakuwa umeshachunguza na umeshaambiwa. Utuambie nini mpango na hii kampuni? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante na naunga mkono hoja. (Makofi)