Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Aloyce John Kamamba (1 total)

MHE. ALOYCE J. KAMAMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, lengo la Serikali ni kupeleka huduma kwa wananchi. Tatizo lililojitokeza hapa ni baadhi ya vitongoji hasa katika Mji wa Kakonko kurukwa. Mfano, vitongoji vya Itumbiko, Mbizi, Kizinda, Cheraburo zikiwemo taasisi kama shule za makanisa. Kwa nini taasisi na vitongoji hivi vinarukwa? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, lini sasa haya maeneo ambayo yamerukwa yatapewa huduma hiyo ya umeme? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Aloyce Kamamba, Mbunge wa Kakonko, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, vitongoji vya Jimbo la Kakonko havijarukwa isipokuwa Serikali inaendelea kupeleka umeme katika vijiji na vitongoji vyetu kwa awamu. Kwa hiyo, kadri ya upatikanaji wa fedha vitongoji vimekuwa vikipatiwa umeme kulingana na mazingira yalivyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, tayari umeme umepelekwa katika vijiji 40 vya Jimbo la Kakonko na wakati tunapeleka umeme katika vijiji hivyo baadhi ya vitongoji vilifikiwa katika awamu ya pili ya REA na awamu ya tatu mzunguko wa kwanza. Sasa awamu ya tatu mzunguko wa pili itapeleka umeme katika vijiji lakini na baadhi ya vitongoji pia.

Mheshimiwa Naibu Spika, Jimbo la Kakonko lipo katika awamu ya pili (b) ya mraji jazilizi wa umeme katika vitongoji. Jumla ya vitongoji 49 vitapatiwa umeme katika Jimbo la Kakonko na mradi huu wa jazilizi unaanza kuanzia mwezi Aprili. Kwa hiyo, kadri ya upatikanaji wa fedha, vitongoji vya Jimbo la Kakonko lakini na vitongoji vingine vingi nchini vitaendelea kupelekewa umeme taratibu ikiwa ni pamoja na taasisi za umma. (Makofi)