Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Aloyce John Kamamba (14 total)

MHE. ALOYCE J. KAMAMBA Aliuliza:-

(a) Je, ni kwa nini vijiji vyote vya Wilaya ya Kakonko havijapata umeme?

(b) Je, ni lini vijiji hivyo vitapata umeme?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI Alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nishati, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Aloyce John Kamamba, Mbunge wa Buyungu, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-

(a) Mheshimiwa Naibu Spika, Jimbo la Buyungu lina jumla ya vijiji 44, vijiji 40 tayari vinapatiwa umeme kupitia awamu ya pili na ya tatu ya utekelezaji wa Mradi wa Kusambaza Umeme Vijijini. Kazi inayoendelea sasa ni kuunganisha umeme katika vijiji 22 kwa wateja ambavyo vilipata umeme tayari ili kukamilisha mpango kazi aliyopewa mkandarasi katika eneo hilo. Kazi hiyo, inatarajia kukamilika ifikapo mwezi Aprili, 2021.

(b) Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa usambazaji wa umeme vijijini umekuwa unafanyika kwa awamu, vijiji vinne vilivyobaki ambavyo ni Kijiji vya Rumashi, Nyamtukuza, Nyabibuye na Kinyinya viko katika mpango wa REA awamu ya tatu mzunguko wa pili utakaoanza mwezi Februari 2021 na kukamilika Septemba, 2022.
MHE. ALOYCE J. KAMAMBA aliuliza:-

Mwaka 2015 wakati wa Kampeni, Mhe. Rais aliahidi kujenga barabara ya kilometa tatu katika Mji wa Kakonko ambao ndiyo Makao Makuu ya Wilaya.

Je, kwa nini ahadi hiyo haijatekelezwa na ni lini sasa itatekelezwa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Aloyce John Kamamba, Mbunge wa Jimbo la Buyungu, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali imeanza kutekeleza ahadi ya aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tano, Hayati Dkt. John Joseph Pombe Magufuli kwa awamu. Katika mwaka wa fedha 2020, Serikali imeanza ujenzi wa barabara yenye urefu wa mita 630 kwa kiwango cha lami katika Mji wa Kakonko itakayogharimu shilingi milioni 500. Ujenzi huu umefikia asilimia 80 na unatarajiwa kukamilika mwezi Mei 2021.

Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kutenga fedha kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya barababara nchini ikiwemo Wilaya ya Kakonko kwa kadri ya upatikanaji wa fedha.
MHE. ALOYCE J. KAMAMBA aliuliza:-

(a) Je, ni kwa nini miradi ya maji katika Mji wa Kakonko kwa muda mrefu haijakamilika?

(b) Je, ni lini Mji wa Kakonko na vitongoji vyake vitapata maji safi na salama ya kutosha?
NAIBU WAZIRI WA MAJI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Aloyce John Kamamba, Mbunge wa Buyungu kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, hadi Desemba, 2020 miradi 15 ilikuwa inatekelezwa katika Wilaya ya Kakonko ambapo miradi 14 imekamilika na inatoa huduma ya maji kwa wananchi, mradi mmoja uliobaki ni mradi wa Kakonko ambao utekelezaji wake umefikia asilimia 65 na unatarajiwa kuhudumia Mji wa Kakonko pamoja na kijiji cha Kasuga.

Mheshimiwa Spika, Mradi wa Maji wa Kakonko unatekelezwa na RUWASA kwa kutumia Wataalam wake wa ndani kwa ajili ya kuukamilisha. Utekelezaji wa mradi huu unafanyika kwa awamu ambapo awamu ya kwanza ambayo inahusisha ulazaji wa bomba kilometa 35 na ujenzi wa matanki mawili yenye ujazo wa lita 500 kila moja utakamilika mwezi Desemba mwaka 2021 na kunufaisha Mji wa Kakonko pamoja na vijiji jirani vya Kasuga, Mbizi, Kanyonza pamoja na Kata ya Kiziguzigu yenye Vijiji vya Kiziguzigu, Kibingo, Kiyobera na Ruyenzi.

Mheshimiwa Spika, awamu ya pili itahusu kufanya upanuzi kwa kulaza mabomba urefu wa kilometa 78 kuelekea vijiji vya Njoomlole, Muganza, Kihomoka na Nyakayenzi ambapo itakamilika mwezi Juni, mwaka 2022.

Aidha, katika mwaka wa fedha 2021/2022 Serikali pia imepanga kujenga miradi mipya katika Vijiji vya Chilambo na Kinonko, ukarabati na utanuzi wa mradi wa Muhange kwenda Muhange Juu na Shule ya Sekondari Ndalichako pamoja na kuchimba visima virefu viwili katika Vijiji vya Chilambo na Nyakiyobe.
MHE. ALOYCE J. KAMAMBA aliuliza:-

(a) Je, ni kwa nini miradi ya maji katika Mji wa Kakonko kwa muda mrefu haijakamilika?

(b) Je, ni lini Mji wa Kakonko na vitongoji vyake vitapata maji safi na salama ya kutosha?
NAIBU WAZIRI WA MAJI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Aloyce John Kamamba, Mbunge wa Buyungu kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, hadi Desemba, 2020 miradi 15 ilikuwa inatekelezwa katika Wilaya ya Kakonko ambapo miradi 14 imekamilika na inatoa huduma ya maji kwa wananchi, mradi mmoja uliobaki ni mradi wa Kakonko ambao utekelezaji wake umefikia asilimia 65 na unatarajiwa kuhudumia Mji wa Kakonko pamoja na kijiji cha Kasuga.

Mheshimiwa Spika, Mradi wa Maji wa Kakonko unatekelezwa na RUWASA kwa kutumia Wataalam wake wa ndani kwa ajili ya kuukamilisha. Utekelezaji wa mradi huu unafanyika kwa awamu ambapo awamu ya kwanza ambayo inahusisha ulazaji wa bomba kilometa 35 na ujenzi wa matanki mawili yenye ujazo wa lita 500 kila moja utakamilika mwezi Desemba mwaka 2021 na kunufaisha Mji wa Kakonko pamoja na vijiji jirani vya Kasuga, Mbizi, Kanyonza pamoja na Kata ya Kiziguzigu yenye Vijiji vya Kiziguzigu, Kibingo, Kiyobera na Ruyenzi.

Mheshimiwa Spika, awamu ya pili itahusu kufanya upanuzi kwa kulaza mabomba urefu wa kilometa 78 kuelekea vijiji vya Njoomlole, Muganza, Kihomoka na Nyakayenzi ambapo itakamilika mwezi Juni, mwaka 2022.

Aidha, katika mwaka wa fedha 2021/2022 Serikali pia imepanga kujenga miradi mipya katika Vijiji vya Chilambo na Kinonko, ukarabati na utanuzi wa mradi wa Muhange kwenda Muhange Juu na Shule ya Sekondari Ndalichako pamoja na kuchimba visima virefu viwili katika Vijiji vya Chilambo na Nyakiyobe.
MHE. ALOYCE J. KAMAMBA aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga Zahanati na Vituo vya Afya katika Wilaya ya Kakonko?
NAIBU WAZIRI OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Aloyce John Kamamba, Mbunge wa Jimbo la Buyungu, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea kutenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa Zahanati na Vituo vya vya Afya vya kimkakati nchini, ambapo katika mwaka wa fedha 2021/2022 Serikali imetenga shilingi bilioni 38.15 kwa ajili ya ukamilishaji wa maboma ya zahanati 758 kote nchini. Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko imetengewa shilingi milioni 150 kwa ajili ya ukamilishaji wa zahanati tatu.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2021/2022 Serikali imetoa fedha za makato ya tozo za miamala ya simu shilingi bilioni 55.25 kwa ajili ya ujenzi wa Vituo vya Afya 221 kwenye Tarafa zisizo na Vituo vya Afya vyenye uwezo wa kutoa huduma ya upasuaji, ambapo Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko imepokea shilingi milioni 250 kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Afya katika Tarafa ya Nyaronga kata ya Gwalama.

Mheshimiwa Spika, mpango wa Serikali ni kuendelea kujenga zahanati na vituo vya afya katika Wilaya ya Kakonko na nchini kote katika maeneo ya kimkakati kulingana na vigezo vilivyowekwa badala ya kila Kijiji na kila Kata. Ahsante.
MHE. ALOYCE J. KAMAMBA aliuliza: -

Je, Serikali ina taarifa juu ya madini yanayopatikana Kakonko na wananchi wananufaikaje nayo?
NAIBU WAZIRI WA MADINI alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Madini naomba kujibu swali la Mheshimiwa Aloyce John Kamamba, Mbunge wa Jimbo la Buyungu, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mujibu wa tafiti zilizofanywa na Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (Geological Survey of Tanzania - GST), Wilaya ya Kakonko ina madini yafuatayo; dhahabu katika Kata za Nyamtukuza, Gwanumpu, Muhange na Kasuga. Pia ina madini ya vito aina ya Agate katika Kata za Gwanumpu na Kasanda na ina madini ya ujenzi katika Kata zote za Wilaya ya Kakonko.

Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, Wizara imetoa leseni 27 za wachimbaji wadogo wa madini katika maeneo tofauti ya Kakonko kama ifuatavyo:- Dhahabu leseni 21, mawe ya chokaa leseni Mbili, shaba leseni Moja, kokoto leseni Tatu, mchanga leseni Moja, chuma leseni Moja na mawe leseni Moja.

Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na uwepo wa leseni za uchimbaji mdogo wa madini ambapo migodi huhitaji watu wengi wa kuzalisha, hivyo kwa njia hiyo wananchi wananufaika na ajira za moja kwa moja katika migodi kwa kutoa huduma mbalimbali kama chakula, malazi, usafirishaji na kadhalika, hivyo kuongeza manufaa ya kiuchumi kwa wananchi wa Wilaya husika na hususani kwa Wilaya ya Kakonko. Ahsante sana.(Makofi)
MHE. ALOYCE J. KAMAMBA aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kupeleka Watumishi wa Afya wa Kada mbalimbali katika Wilaya ya Kakonko?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE) alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Aloyce John Kamamba, Mbunge wa Jimbo la Buyungu, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka wa fedha 2020/2021 Serikali iliajiri Watumishi wa kada za afya 2,726 ambapo Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko ilipelekewa watumishi 24 waliopangwa kwenye vituo vya kutolea huduma za afya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali katika mwaka wa fedha 2021/2022 imepanga kuajiri watumishi wa kada mbalimbali za afya kwa ajili ya kuboresha hali ya utoaji huduma za afya nchini kote ikiwemo Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko. Aidha, Serikali kwa kushirikiana na wadau itaendelea na mpango wa kuajiri watumishi wa kada za afya kwa awamu kulingana na upatikanaji wa fedha. (Makofi)
MHE. ALOYCE J. KAMAMBA aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itatekeleza ahadi yake ya kujenga kwa kiwango cha lami barabara inayoanzia Mji wa Kakonko hadi Muhange?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Aloyce John Kamamba, Mbunge wa Jimbo la Buyungu, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, barabara ya Kakonko kupitia Vijiji vya Kinonko, Ruhuru, Nyakiyobe, Gwarama, Kabane hadi Muhange inasimamiwa na mamlaka mbili kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kipande cha barabara kutoka Kakonko – Kinonko – Ruhuru – Nyakiyobe – Gwarama yenye urefu wa kilometa 26 inasimamiwa na TANROADS na kipande cha barabara kutoka Gwarama – Muhange yenye urefu wa kilomita nane inasimamiwa na TARURA.

Mheshimiwa Spika, kipande cha barabara inayosimamiwa na TARURA yenye urefu wa kilomita nane ipo katika hali nzuri kufuatia matengenezo yaliyofanyika katika mwaka wa fedha 2019/2020 kwa gharama ya shilingi milioni 40.88.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2022/2023, kipande cha barabara hii yenye urefu wa kilomita tano, kiasi cha shilingi milioni 10 imetengwa kwa ajili ya matengenezo ili kuhakikisha huduma za kiuchumi na kijamii zinaendelea kufanyika kwa wananchi kwa kipindi chote cha mwaka.

Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kuboresha miundombinu ya barabara za Jimbo la Buyungu kulingana na upatikanaji wa fedha.
MHE. ALOYCE J. KAMAMBA aliuliza: -

Je, lini minara ya mawasiliano itapelekwa Kata za Nyamtukuza, Nyabibuye, Gwarama, Kasuga, Rugenge, Gwanumpu, Katanga na Magunzu?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI, alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Aloyce John Kamamba, Mbunge wa Buyungu, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kwa kushirikiana na Kampuni ya Vodacom imetekeleza miradi ya kufikisha huduma za mawasiliano ya simu katika Kata za Nyamtukuza, Nyabibuye, Gwarama, Gwanumpu, Rugenge na Mugunzu. Miradi hii imetekelezwa kati ya mwaka 2016 na 2019 ambapo ujenzi wa minara katika Kata hizi umekamilika na inatoa huduma kwa teknolojia ya 2G na 3G.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa Kata ya Katanga na Kasuga, Serikali itafanya tathmini ya hali halisi ya upatikanaji wa huduma za mawasiliano Kata hizi katika mwaka wa fedha 2023/2024, ahsante.
MHE. ALOYCE J. KAMAMBA aliuliza: -

Je, ni Wazee wangapi wamepewa Bima ya Wazee na waliobaki ni lini watapewa Bima hizo Wilayani Kakonko?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Aloyce John Kamamba, Mbunge wa Jimbo la Buyungu, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko inatekeleza afua mbalimbali za afya ikiwemo huduma za afya kwa wazee, kwa kuwapatia vitambulisho vya matibabu bila malipo wazee wenye umri wa miaka 60 na kuendelea wasio na uwezo, kama ilivyo katika Sera ya Wazee ya mwaka 2003, Sera ya Afya ya mwaka 2007 na Mwongozo wa uchangiaji wa huduma za afya nchini.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha wa 2022/2023 Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko iliwatambua wazee wa miaka 60 na kuendelea wasio na uwezo wapatao 11,524. Kati yao wazee 6,084 walipewa vitambulisho vya matibabu bila malipo, wazee 2,000 walikatiwa bima ya mfuko wa afya ya jamii ulioboreshwa kupitia mapato ya ndani.

Mheshimiwa Spika, katika Mwaka wa Fedha wa 2023/2024, Serikali kupitia mapato ya ndani itatenga bajeti kwa ajili ya kuwapatia vitambulisho wazee 3,440 waliobaki katika Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko.

Mheshimiwa Spika, nitumie fursa hii kuwakumbusha viongozi wote wa mikoa na halmashauri kutekeleza maelekezo ya kuwapa vitambulisho vya matibabu bila malipo wazee wote wenye umri wa miaka 60 na kuendelea wasio na uwezo. ahsante.
MHE. ALOYCE J. KAMAMBA aliuliza: -

Je, lini shule za Sekondari Nyamtukuza, Muhange, Shuhudia, Kasanda na Gwanumpu zitakuwa za kidato cha tano na kidato cha sita?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Aloyce John Kamamba, Mbunge wa Jimbo la Buyungu, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Shule ya Sekondari ya Muhange imekaguliwa na wadhibiti ubora wa shule ikaonekana ina mapungufu ya mabweni mawili, mapungufu hayo yakikamilishwa itapandishwa hadhi ya kuwa kidato cha tano na sita.

Mheshimiwa Spika, Shule za Nyamtukuza, Shuhidia, Kasanda na Gwanumpu zinaendelea kuongezewa miundombinu ya majengo, ikikamilika zitakaguliwa na wadhibiti ubora wa shule na kuombewa kupandishwa kuwa za Kidato cha Tano na Sita. Hata hivyo, shule moja mpya ya kidato cha tano na sita imesajiliwa ambayo inaitwa Amani Mtendeni.
MHE. ALOYCE J. KAMAMBA aliuliza: -

Je, lini Serikali itakarabati Skimu za Umwagiliaji za Katengera, Ruhwiti na Muhwazi ili kuboresha kilimo cha umwagiliaji Kakonko?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, ninapenda kujibu swali la Mheshimiwa Aloyce John Kamamba, Mbunge wa Buyungu, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Skimu za Umwagiliaji Katengera, Ruhwiti na Muhwazi ni miongoni mwa skimu zilizoko katika Wilaya ya Kakonko zinazounda mabonde 22 ya kimkakati. Katika mwaka wa fedha 2022/2023 Wizara ya Kilimo kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji imepanga kufanya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina kupitia mshauri elekezi katika Skimu za Buyungu, Nyakanyezi, Mgunzu, Kayonza, Muhwazi, Ruhuru na Chulanzo zilizoko katika Wilaya ya Kakonko.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2023/2024 Wizara ya Kilimo kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji imetenga fedha za kuanza ujenzi wa skimu zinazounda mabonde 22 ya kimkakati ambapo Skimu za Katengera, Ruhwiti na Muhwazi ni miongoni mwa skimu hizo.
MHE. ALOYCE J. KAMAMBA aliuliza:-

Je, lini zoezi la kufikisha umeme katika vitongoji, vijiji na mitaa ambayo haina umeme litakamilika Wilayani Kakonko?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Nishati napenda kujibu swali la Mheshimiwa Aloyce John Kamamba, Mbunge wa Buyungu kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali inatekeleza Mradi wa Kusambaza Umeme Vijijini Awamu ya Tatu, Mzunguko wa Pili ambapo vijiji vyote visivyokuwa na umeme vitafikiwa na huduma hiyo. Aidha, vijiji saba tu vya Wilaya ya Kakonko visivyokuwa na umeme vitakamilika kuwashiwa umeme ifikapo tarehe 30 Juni, 2023.

Mheshimiwa Spika, Serikali imekamilisha uhakiki wa vitongoji 36,101 visivyo na huduma ya umeme na kuandaa mradi kabambe wa kusambaza umeme katika vitongoji vyote unaoitwa Hamlet Electrification Project (HEP) vikiwemo vitongoji 196 vya Wilaya ya Kakonko. Mradi huu utatekelezwa kuanzia mwaka wa fedha 2024/2025. Kwa mwaka 2023/2024 Jimbo la Buyungu Wilayani Kakonko litapatiwa fedha kwa ajili ya kupeleka umeme katika vitongoji 15 vya kuanzia, nakushukuru.
MHE. ALOYCE J. KAMAMBA aliuliza: -

Je, lini Serikali itajenga Chuo cha VETA Wilayani Kakonko?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Waziri, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Aloyce John Kamamba, Mbunge wa Jimbo la Buyungu, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali inayo azma ya kujenga Chuo cha Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) katika kila mkoa na wilaya nchini. Katika mwaka wa fedha 2022/2023, Serikali ilitenga kiasi cha shilingi bilioni 100 kwa ajili ya kujenga Vyuo vya VETA katika wilaya 64 ambazo zilikuwa hazijajengewa vyuo hivyo. Aidha, Wilaya ya Kakonko ni miongoni mwa wilaya hizo 64 ambazo zinajengewa vyuo hivyo.

Mheshimiwa Spika, kwa sasa Serikali imeshapeleka kiasi cha shilingi 228,000,000 pamoja na vifaa vya ujenzi ikiwemo nondo na sementi kwa ajili ya kuendelea na ujenzi wa Chuo cha VETA cha Wilaya ya Kakonko ambapo ujenzi upo katika hatua ya kujenga misingi ya majengo. Ahsante sana.