Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon Norah Waziri Mzeru (13 total)

MHE. DENNIS L. LONDO K.n.y. MHE. NORAH W. MZERU aliuliza:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kuweka mashine za incubator za kutosha nchini ili kuzuia vifo vya watoto?
WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu: -

Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naomba kujibu swali la Mheshimiwa Norah Waziri Mzeru, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kabla sijaanza naomba nimpongeze sana Mheshimiwa Norah Waziri Mzeru kwa kuwa na utashi wa kuangalia afya za watoto wachanga katika Taifa letu kama sehemu ya changamoto tuliyonayo sekta ya afya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali lake kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kifaa cha incubator hutumika kuwasaidia watoto wachanga waliozaliwa kabla ya wakati au wenye uzito pungufu ili kuwapatia joto na kuzuia wasipoteze maisha. Hadi sasa tuna incubators 214 nchi nzima kwenye hospitali mbalimbali.

Mheshimiwa Spika, hata hivyo tafiti zimeonesha kuna changamoto nyingi sana za kutumia incubators kuliko faida zenyewe. Incubators zimesababisha kusambaa kwa magonjwa kutoka mtoto mmoja kwenda kwa mwingine atakayefuatia kulazwa hapo. Aidha, hakuna ukaribu wa mama aliyejifungua na mtoto aliyewekwa kwenye incubator.

Mheshimiwa Spika, matumizi ya incubator katika mazingira ambayo umeme siyo wa uhakika nayo inakuwa changamoto. Hivyo, katika mazingira hayo, incubator inaweza kuwa chanzo cha uambukizo na vifo badala ya kusaidia. Hata hivyo incubators chache zilizopo zinatumika kwa ajili ya watoto waliozaliwa na uzito pungufu sana (extreme low birth weight) kwa kuzingatia kanuni za usafi wa hali ya juu.

Mheshimiwa Spika, hivyo, Wizara inasisitiza kuwa kila hospitali ianzishe vyumba maalum kwa ajili ya matibabu ya watoto wachanga ili kuendana na mwongozo wa Kitaifa wa Matibabu ya Watoto Wachanga. Vyumba hivyo ni chumba cha huduma ya Mama Kangaroo, yaani mtoto anakaa na mama kifuani kwake muda mwingi kwa watoto waliozaliwa na uzito pungufu, lakini pia na chumba cha matibabu ya mtoto mchanga mgonjwa. Kufikia Julai, 2021, jumla ya hospitali 159 zilishaanzisha vyumba hivyo na kazi inaendelea kwenye hospitali nyingine. Ahsante.
MHE. NORA W. MZERU aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kuwasaidia wafugaji wa Mkoa wa Morogoro kufanya ufugaji wa kisasa na wenye tija kwa kuwa Mkoa huu una wafugaji wengi?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Nora Waziri Mzeru Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Wizara imekuwa ikifanya jitihada mbalimbali, ili kufanya ufugaji katika Mkoa wa Morogoro kuwa wenye tija na wa kisasa. Juhudi hizo ni pamoja na uboreshaji wa mbari za mifugo kwa kuhimilisha ngómbe, kuwezesha upatikanaji wa kuku wazazi walioboreshwa, mafunzo rejea juu ya teknolojia za ufugaji bora kwa wafugaji na maafisa ugani. Vipindi vya elimu kwa umma vya redio, televisheni, maonyesho mbalimbali yakiwemo ya sabasaba na nanenane.

Mheshimiwa Spika, kutokana na juhudi hizi, hadi mwaka 2020 mifugo iliyoboreshwa katika Mkoa wa Morogoro imefikia ng’ombe 28,582 sawa na asilimia 3 ya ng’ombe wote na mbuzi 19,899 sawa na asilimia 11 ya mbuzi wote na kuku millioni 2.5 sawa na asilimia 69 ya kuku wote.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2021/2022 Wizara kwa kushirikiana na wadau na Mamlaka za Serikali za Mitaa, inatarajia kuhimilisha ng’ombe 32,606 Mkoani Morogoro, kwa kutumia mbegu bora za mifugo za ruzuku kutoka katika Kituo cha Taifa cha Uhimilishaji cha NAIC Arusha. Ahsante sana.
MHE. NORAH W. MZERU aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kuufanya Mkoa wa Morogoro kuwa moja ya kitovu kikuu cha utalii duniani kwa kuwa ni Mkoa wenye vyanzo vingi vya utalii?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu: -

Mheshimiwa Spika, ahsante sana, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Norah Waziri Mzeru, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, katika kuongeza kasi ya ukuaji wa sekta ya utalii katika Mkoa wa Morogoro, Serikali ilipandisha hadhi sehemu ya Pori la Akiba la Selous kuwa Hifadhi ya Taifa ya Nyerere. Sambamba na jitihada hizo, Serikali kupitia Mradi wa Kukuza Maliasili na Kuendeleza Utalii (REGROW), barabara zenye urefu wa takribani kilometa 996, njia za watembea kwa miguu kilometa 132.5, viwanja vya ndege saba, malango ya kuingilia wageni nane, vituo vya askari nane na vituo vya kutolea taarifa kwa wageni vitatu vitajengwa katika Hifadhi za Taifa za Mikumi, Udzungwa na Nyerere Mkoani Morogoro. Juhudi hizi zitaendelea kuchochea hali ya utalii katika Mkoa huo.

Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo katika hatua nyingine Serikali imeendelea kupandisha hadhi maeneo mbalimbali ikiwemo Hifadhi ya Wanyamapori ya Jamii ya Wami Mbiki kuwa Pori la Akiba. Vilevile kukamilika kwa reli ya mwendokasi (SGR) pamoja na kutumika kwa reli ya TAZARA kutaongeza wigo wa shughuli za utalii katika mikoa ya Morogoro na Pwani. (Makofi)
MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI K.n.y. MHE. NORAH W. MZERU aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kuboresha Wodi za Wazazi nchini pamoja na kuongeza huduma hizo kwa Wananchi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-TAMISEMI naomba kujibu swali la Mheshimiwa Norah Waziri Mzeru Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kati ya mwaka 2018/2019 mpaka sasa, Serikali imejenga Hospitali mpya za Halmashauri 127 kati ya hizo Hospitali 70 zimeshasajiliwa na kuanza kutoa huduma kwa wananchi ikiwemo huduma za dharura, upasuaji na wodi za Wazazi.

Mheshimiwa Spika, katika kipindi hicho, Vituo vya Afya 822 vimekarabatiwa na kujengwa ambapo kati ya hivyo 476 vinatoa huduma za dharura, upasuaji na wodi za wazazi. Wodi za Wazazi zimeboreshwa kwa kuweka maeneo yote muhimu kwa huduma za uzazi salama.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2022/2023 Serikali imetenga shilingi bilioni 12.5 kwa ajili ya kujenga hospitali 25 zitakazokuwa na Wodi za Wazazi.
MHE. ABUBAKARI D. ASENGA K.n.y. MHE. NORAH W. MZERU aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kuwajengea wahudumu wa kada mbalimbali za afya nyumba bora ili kuboresha makazi yao?
NAIBU WAZIRI WA AFYA alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Norah Waziri Mzeru, Mbunge Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2021/2022 Serikali imejenga nyumba 176 na katika mwaka wa fedha 2022/2023 itajenga nyumba 300 za kukaa familia tatu kwa kila nyumba. Ahsante.
MHE. NORAH W. MZERU aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kupunguza gharama ya gesi ili kuepuka matumizi ya mkaa na kuni?
WAZIRI WA NISHATI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Norah Waziri Mzeru, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Tanzania hatuzalishi gesi iliyosindikwa kiwandani (LPG) ambayo pia hutumika kama nishati ya kupikia. Gesi ya LPG huagizwa kutoka nchi za nje. Kama ilivyo kwa bidhaa nyingine zinazotokana na mafuta ya petroli, gharama za LPG pia hutegemea bei katika soko la dunia.

Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea kuhamasisha na kushirikiana na sekta binafsi kuwekeza katika miundombinu ya kupokea na kuhifadhi LPG ili kuwa na uwezo mkubwa zaidi ya tani 16,000 za sasa. Hii itatuwezesha kuanza kuagiza LPG kwa mfumo wa uagizaji wa pamoja na hivyo kupungua kwa gharama za uagizaji na kupata nafuu katika gharama ya gesi.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2022/2023 Serikali kupitia TPDC imetenga fedha Shilingi bilioni 10 kwa ajili ya kutekeleza mradi wa kusambaza gesi asilia ambayo ipo hapa nchini na kuwaunganisha wateja kwa maeneo yaliyopitiwa na mradi wa Bomba la Gesi Asilia kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam kwa ajili ya matumizi mbalimbali ikiwemo kupikia. Gesi hiyo inayotumika kwa kupikia ni nafuu kwa kiasi kikubwa ukilinganisha na vyanzo vingine vyanzo vingine vya nishati ya kupikia. (Makofi)
MHE. NORAH W. MZERU aliauliza: -

Je, ni lini Kiwanda cha Mazava Winds Group – Morogoro kitapatiwa eneo kubwa la uwekezaji?
NAIBU WAZIRI WA UWEKEZAJI, VIWANDA NA BIASHARA alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Norah Waziri Mzeru, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Kiwanda cha Mazava Fabrics and Production East Africa Limited kinajishughulisha na uzalishaji wa nguo. Kiwanda hiki kipo chini ya mamlaka ya EPZ na kinafuata taratibu za uwekezaji zilizowekwa na Mamlaka hiyo. Kiwanda hiki kinatumia majengo ya kupanga kwa sasa.

Mheshimiwa Spika, Mamlaka ya EPZ kwa kushirikiana na Mkoa wa Morogoro waliwezesha kupatikana kwa eneo la uwekezaji linalofahamika kwa jina la Star City lililopo Manispaa ya Morogoro, lenye ukubwa wa mita za mraba 20,000. Mwekezaji alikubaliana na eneo hili kuwa linafaa kwa ajili ya uwekezaji.

Mheshimiwa Spika, vilevile Mkoa wa Morogoro umetenga eneo la uwekezaji ambalo pia linafaa kwa ajili ya uwekezaji wa viwanda liitwalo Kiyegera. Eneo hili linafaa kwa uwekezaji Mkubwa na Mdogo.
MHE. NORAH W. MZERU aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itaweka miundombinu katika kivutio cha utalii cha Mount Uluguru Waterfall?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Nora Waziri Mzeru, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeanza kujenga miundombinu mbalimbali ikiwemo ngazi kuelekea kwenye Maporomoko ya Hululu, ujenzi wa choo, kuweka miundombinu ya maji, mfumo wa umeme wa jua na mashine ya kusukumia maji na kujenga daraja la mbao kuvuka mto Mgeta. Aidha, Serikali kupitia mradi wa kupunguza athari za UVIKO -19 ilikarabati barabara ya kuelekea kwenye msitu huo wenye urefu wa Kilometa nane kutoka Kijiji cha Kibaoni hadi Bunduki kwenye kivutio cha Maporomoko ya Hululu. Ukarabati huo umewezesha kufikika kwa urahisi kwenye kivutio hicho kwa shughuli za utalii na uwekezaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, Serikali inaendelea kuhamasisha wawekezaji kuwekeza miundombinu ya utalii katika msitu huo. Miundombinu ya utalii inayoweza kuwekezwa na sekta binafsi ni pamoja na makambi (camp sites), lodge, hotel na maeneo ya burudani, nakushukuru.
MHE. NORAH W. MZERU sliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kutatua tatizo la uhaba wa Hosteli kwa wanafunzi wa Elimu ya Juu wanaosoma katika Vyuo vya Mkoa wa Morogoro?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA, Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia napenda kujibu swali la Mheshimiwa Norah Waziri Mzeru Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali inafanya juhudi mbalimbali katika kutatua tatizo la uhaba wa hosteli kwa wanafunzi wanaosoma katika vyuo vikuu hapa nchini vikiwemo Vyuo vya Mkoa wa Morogoro. Kwa sasa hosteli zilizopo katika vyuo vikuu vya Mzumbe na Sokoine zina uwezo wa kulaza jumla ya wanafunzi 7571. Ikiwa Mzumbe ni wanafunzi 3742 na Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo ni wanafunzi 3829.

Mheshimiwa Spika, hata hivyo wanafunzi ambao hawapati nafasi za malazi katika hosteli za vyuo wamekuwa wakipata malazi katika hosteli zinazomilikiwa na watu binafsi katika maeneo yaliyokaribu na vyuo.

Mheshimiwa Spika, kwa kutambua ongezeko la uhitaji wa malazi kwa wanafunzi katika vyuo vikuu vya serikali vikiwemo vyuo vya Mkoa wa Morogoro, Serikali imekamilisha ujenzi wa hosteli 4 zenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 1024 katika Chuo Kikuu cha Mzumbe na zimeanza kutumika kuanzia mwaka 2021.

Mheshimiwa Spika, aidha kwa mwaka wa fedha 2023/2024 Serikali kupitia Mradi wa Higher Education for Economic Transformation yaani HEET imetenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa Hosteli moja yenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 600 katika Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo Kampasi ya Mazimbu Morogoro. Nashukuru.
MHE. ABUBAKARI D. ASENGA K.n.y. MHE. NORAH W. MZERU aliuliza:-

Je, kuna mpango gani wa kuwawezesha wadau wa michezo kuwekeza katika kuzalisha vipaji vya michezo hasa mpira wa miguu?

NAIBU WAZIRI WA UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO alijibu:-

Mheshimiwa Spika, nakushukuru, na kwa ridhaa yako, naomba nitumie sekunde chache kuwapongeza vijana wetu wa Timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars) kwa ushindi wa goli moja kwa bila walioupata dhidi ya Niger jana, ushindi ambao unatuweka katika nafasi nzuri na uwezekano mkubwa wa kuweza kupata nafasi ya kushiriki katika Fainali za Mataifa ya Afrika zitakazochezwa mwakani kule Senegal. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kama ambavyo niliwaahidi jana ile milioni 10 yao ya goli la mama kutoka kwa shabiki na mwezeshaji namba moja wa timu ya Taifa itawafikia leo kwa sababu mama hana kona kona, akishaahidi lazima litekelezwe, ahsante. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo naomba kujibu swali la Mheshimiwa Norah Waziri Mzeru, Mbunge wa Viti Maalum lililoulizwa kwa niaba yake na Mheshimiwa Abubakari Asenga kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali katika kuwezesha wadau kuwekeza kwenye uzalishaji wa vipaji vya michezo hasa mpira wa miguu imefanya jitihada mbalimbali ikiwemo kuweka miongozo mahususi ya uanzishwaji na uendeleshaji wa shule maalum za kuibua; kukuza na kuendeleza vipaji (sports academies); kuweka mfumo madhubuti wa usajili wa academia na vituo vya michezo; kupunguza kodi kwenye vifaa vya michezo kama vile nyasi bandia na viambata vyake; kutoa utaalamu na ushauri katika ujenzi wa miundombinu ya michezo; na kuandaa mashindano ya UMISETA kwa shule za sekondari na UMITASHUMITA kwa shule za msingi ili kuwashindanisha, kuibua na kuendeleza vipaji vyao, ahsante.
MHE. NORAH W. MZERU aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itaanza ujenzi wa barabara ya Morogoro – Malinyi – Namtumbo kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Norah Waziri Mzeru, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inaendelea kutafuata fedha kwa ajili ya kuanza ujenzi kwa ajili ya kuanza ujenzi wa barabara ya Ifakara – Malinyi – Kilosa kwa Mpepo - Londo hadi Lumecha (Namtumbo) kwa kiwango cha lami. Kwa sasa maeneo yote korofi yataainishwa na kujengwa ili barabara hii ipitike mwaka wote, ahsante.
MHE. DKT. CHRISTINE G. ISHENGOMA K.n.y. MHE. NORAH W. MZERU aliuliza:-

Je, lini Serikali itamalizia ujenzi wa zahanati ya Uwanja wa Ndege katika Kata ya Mafisa Mkoani Morogoro?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Norah Waziri Mzeru, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kusogeza huduma za afya kwa wananchi wa Uwanja wa Ndege, mwaka wa fedha 2017/2018, Serikali ilipeleka shilingi milioni 70 kwa ajili ya ujenzi wa Zahanati ya Uwanja wa Ndege iliyopo katika Kata ya Kiwanja cha Ndege Manispaa ya Morogoro. Ujenzi umekamilika na huduma zimeanza kutolewa mwezi Mei, mwaka 2022. Zahanati hii kwa wastani huhudumia wagonjwa wapatao 750 kwa mwezi na wagonjwa 9,000 kwa mwaka, ahsante.
MHE. DKT. CHRISTINE G. ISHENGOMA K.n.y. MHE. NORAH W. MZERU aliuliza:-

Je, lini Serikali itamalizia ujenzi wa zahanati ya Uwanja wa Ndege katika Kata ya Mafisa Mkoani Morogoro?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Norah Waziri Mzeru, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kusogeza huduma za afya kwa wananchi wa Uwanja wa Ndege, mwaka wa fedha 2017/2018, Serikali ilipeleka shilingi milioni 70 kwa ajili ya ujenzi wa Zahanati ya Uwanja wa Ndege iliyopo katika Kata ya Kiwanja cha Ndege Manispaa ya Morogoro. Ujenzi umekamilika na huduma zimeanza kutolewa mwezi Mei, mwaka 2022. Zahanati hii kwa wastani huhudumia wagonjwa wapatao 750 kwa mwezi na wagonjwa 9,000 kwa mwaka, ahsante.