Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon Norah Waziri Mzeru (2 total)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto
MHE. NORAH W. MZERU: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii. Kwanza nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa siku ya leo pili nikushukuru wewe kwa kunipa nafasi hii muhimu na adhimu kwangu kwa kuweza kusimama kwa mara ya kwanza katika Bunge lako hili tukufu na kuchangia Hotuba ya Bajeti ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Watoto na Wazee.

Mheshimiwa Naibu Spika, pili, nichukue nafasi hii kumshukuru Mheshimiwa Waziri pamoja na timu yake kwa kazi nzuri wanayoifanya. Tatu, nichukue fursa hii kuishukuru Serikali kwa kazi nzuri wanayoifanya katika kutatua kero na changamoto za wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wote ni mashahidi kutokana na kazi nzuri aliyoifanya Hayati Dkt. John Pombe Magufuli katika kipindi cha mwaka 2015/2020. Wakati akilihutubia Bunge Novemba, 2020 alielezea mafanikio kadhaa wa kadha ambayo yote ukiyatilia maanani yamewagusa kwa asilimia mia moja Wanawake, Vijana na Watoto, Kiuchumi, Kijamii, Kisiasa, wote tulikuwa mashahidi tulisisimkwa kwa furaha kuona namna gani Taifa letu limepiga hatua kubwa za kimaendeleo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mwelekeo huu wa Bajeti ya Serikali tunajadili kwa mwaka 2021/2022 unaelekea katika maandalizi ya bajeti ya sita tangu Rais Mama Samia Suluhu aingie madarakani. Ambapo ukifuatilia kwa umakini utaona namna gani bajeti zote zilivyojikita katika kugusa maendeleo ya wananchi lakini zaidi kwa namna moja ama nyingine kugusa zaidi wanawake na Watoto nchini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, siku zote wanafalsafa utuambia Uongozi Bora ni kupigania maslahi ya wengi lakini ili uwe Kiongozi Bora lazima ujielekeze kwenye utayari. Kujiandaa katika upeo na uwezo wa kiuongozi kadri unavyotafakari, katika kuwafanyia mambo mema unaowaongoza, aina hiyo ya uongozi siku zote hutoa majawabu ya utatuzi wa shida na kero za wananchi bila kujali maneno, maneno ya upotoshaji wa wachache. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nishauri Serikali katika bajeti ijayo ya mwaka 2022,2023 kuendelea kuwekeza katika kusomesha, kuajiri na kupeleka waganga, wauguzi na wakunga katika maeneo ya vijijini ili kuokoa Maisha ya akinamama Wajawazito sambamba na kutoa huduma bora za afya na tiba. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ili kufikia malengo ya millennium kuna ulazima wa kuhakikisha Maisha ya akinamama wajawazito yanawekewa utaratibu bora wa kiuhuduma kwa kupewa ushauri na maendeleo yao nyakati za ujazito. Wakipata huduma bora katika vituo vya huduma ya afya.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya wanawake wote wa Mkoa wa Morogoro nimpongeze sana Rais wetu, Mama yetu kipenzi, Mama Samia Suluhu Hassan kwani jinsi alivyojipanga na Serikali yake ya Awamu ya Sita kwa ajili ya kuendelea kushamirisha maendeleo nchini ambayo yametugusa moja kwa moja Wanawake, Vijana na Watoto. Katika Taifa lolote ulimwengu huu tulionao huwezi kuzungumzia maendeleo hayo bila kuwagusa wanawake. Nashauri bajeti hii tuendelee kukumbukwa kinamama hasa katika masuala ya elimu, afya uwezeshaji wa kiuchumi ili tuweze kujiajiri na fursa za kiuongozi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niseme tu uongozi wa Rais Mama Samia Suluhu umetuhemisha sana wanawake na tunaamini kuwa ataendelea kutuheshimisha zaidi kutokana na dhamira yake njema kwetu. Kipaumbele ni kuweka mazingira bora kuanzia Halmashauri ya Wilaya hadi Serikali Kuu ili kusomesha, kuajiri na kupeleka Wakunga, Waganga na Wauguzi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mikakati ya maendeleo, uimarishaji huduma za msingi za kijamii lakini lazima sasa iibuliwe katika ngazi za halmashauri za Wilaya kabla ya Serikali Kuu haijaweka mkono wake. Viongozi tushirikiane kutenga muda wa kushughulikia na kuondosha kero mapema katika maeneo yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali Kuu haiwezi kufanya kitu katika Vitongoji, Vijiji, Kata na Wilaya kwenye wilaya kazi hiyo lazima ifanywe na halmashauri zetu, wakiwemo watalaam na usimamizi ili liende sambamba na usimamizi mzuri wa matumizi bora ya fedha. Tukifanya hivyo maendeleo na mafanikio kila Kijiji tutayaona na Taifa litaendelea kupiga hatua kubwa za maendeleo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali kwa Wizara ya Afya, Wazee, Jinsia na Watoto tumekuwa tukishuhudia jitihada za Serikali katika kuboresha makazi ya wahudumu wa kada mbalimbali, lakini katika kada hii ya afya tuna wataalam wengi sana Waganga, kama vile Waganga wa Kinga, Wakunga na Wauguzi ambapo katika mazingira wanayoishi wengine wapo vijijini ambapo ndipo kwenye changamoto nyingi. Serikali inamkakati gani wa kujenga nyumba bora za kisasa? Ghorofa?

MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

MHE. NORAH W. MZERU: Ambazo Waganga Wakunga na Wauguzi wataishi na kuridhika hasa maeneo ya vijiji ambapo miji inapanuka.(Makofi)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Norah Mzeru kuna taarifa.

MHE. NORAH W. MZERU: Mheshimiwa Naibu Spika, ok.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Nora Mzeru kaa kidogo, kaa kidogo Mheshimiwa.

T A A R I F A

MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimpe taarifa mchangiaji kwa mujibu wa kanuni haitakiwi anapochangia asome anachangia vizuri lakini anasoma. Ahsante. (Kicheko)

NAIBU SPIKA: Waheshimiwa, ngoja ngoja Waheshimiwa Wabunge msiwe na haraka. Kwanza taarifa si jambo la kuvunjwa kwa kanuni kwa hiyo kama kanuni imevunjwa unasimama kwa kanuni zinazohusu utaratibu, kwamba kuna kanuni imevunjwa humu ndani. Mheshimiwa Nora Mzeru hasomi anachangia lakini anaangalia sehemu ambayo ameweka ule mchango wake. Mheshimiwa Norah Mzeru. (Makofi)

MHE. NORAH W. MZERU: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Mwisho napenda kumpongeza Rais Mama Samia Suluhu Hassan pamoja na uongozi wake wa juu ikiwemo Makamu wa Rais, Waziri Mkuu na timu nzima ya utawala kwa jinsi wanavyofanya kazi kubwa ya maendeleo kwa kushirikiana Bunge lako Tukufu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuunga mkono hoja. (Makofi/Kicheko)
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022
MHE. NORAH W. MZERU: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuchangia hotuba ya Bajeti Kuu ya Serikali. Kwa dhati ya moyo wangu nampongeza Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mama yetu kipenzi Mama Samia Suluhu Hassan, nampongeza Rais kwa juhudi zake anazozichukua siku hadi siku pamoja na kutupa kipaumbele hasa sisi wakina mama wa Taifa hili.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia nampongeza tena Mama Samia Suluhu Hassan kwa kumuamini na kumteua Dkt.r Philip Mpango kuwa msaidizi wake Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; ninampongeza Mheshimiwa Spika pamoja na Naibu Spika pamoja na Wenyeviti wa Bunge hili kwa kutuendesha vizuri katika shughuli zetu za Bunge.

Nampongeza pamoja na kumshukuru Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa umahiri wake wa utekelezaji wa majukumu yake ya kila siku, namuombea kwa Mwenyezi Mungu aangalie uzima wa afya yake na amani katika maisha yake ya kila siku pia nampongeza Waziri wa Fedha – Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Nchemba na Naibu wake Engineer Masauni pamoja na Katibu Mkuu na viongozi wote waandamizi wa Wizara hii ya Fedha na Mipango na pia naipongeza Kamati ya Kudumu ya Bunge kwa kushirikiana na Wizara kwa kutuleta bajeti ambayo imekidhi kiwango.

Mheshimiwa Naibu Spika, bajeti hii imegusa maslahi mapana ya Taifa letu, naamini itawanufaisha Watanzania kwa ujumla, sina budi ya kumpongeza Mheshimiwa Rais na Serikali yake kiujumla, lakini naomba kuchangia kwa ufupi kuhusu upatikanaji wa maji safi na salama mijini na vijijini bado hairidhishi. Maji hayana mbadala, maji ni uhai, maji ni maisha kwa viumbe hai vyote, bado vipo vijiji ambavyo havina kisima hata kimoja cha maji safi na salama na badala yake hutumia maji ya mapalio, maji ya madimbwi, maji ya mito wanayochangia na Wanyama.

Mheshimiwa Naibu Spika, Tanzania ina vyanzo vingi vya maji mfano Mkoa wa Morogoro kuna changamoto kubwa ya upatikanaji wa maji safi na salama, lakini vyanzo vingi vya maji vimeanzia Mkoa wa Morogoro na kutumika katika baadhi ya mikoa mingine na si kuwasaidia wakazi waliopo vijijini ndani ya Mkoa wa Morogoro; kwa mfano Bwawa la Kidunda liliopo Wilaya ya Morogoro Vijijini nalo lingekuwa msaada mkubwa kwa wanakijiji.

Mheshimiwa Naibu Spika, ushauri wangu iweke nguvu katika sekta ya maji ili tuweze kumtua ndoo ya maji mama kichwani.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kwa ufupi niongezee katika upande wa elimu; kuna changamoto kubwa katika upande wa madarasa na madawati, madarasa mengi yamekuwa chakavu na mlundikano wa watoto katika darasa moja linakuwa na wanafunzi zaidi ya 100 na Serikali imeona muitikio mkubwa wa wanafunzi kusoma kutokana na elimu bila malipo.

Mheshimiwa Naibu Spika, ombi langu naomba kuwe na mkakati maalum kwa watoto wanaohitimu darasa la saba kwenda kidato cha kwanza kuhakikisha wanakuwa na madarasa na si kuanza ujenzi wa madarasa kipindi watoto wanataka kuingia shuleni.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuwasilisha na ninaunga mkono hoja Ahsante.