Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Answers to supplementary Questions by Hon Sagini Jumanne Abdallah (399 total)

MHE. FLORENT L. KYOMBO: Mheshimiwa Spika, nikushukuru tena kwa nafasi. Ni mara ya pili nauliza swali kama hili katika Bunge lako Tukufu, lakini kwa imani kubwa niliyonayo kwa Waziri wa Mambo ya Ndani, ndugu yangu, Mheshimiwa Engineer Masauni na Mheshimiwa Sagini, naamini sasa hili suala litakwenda kutafutiwa ufumbuzi wa kudumu.

Mheshimiwa Spika, wananchi wa Jimbo la Nkenge, Wilaya ya Misenyi, hasa Kata za Mutukura, Kakunyu, Minziro na maeneo mengine wamekuwa na mila na desturi zinazofanana kabisa na Nchi ya Uganda. Sisi tunaongea Ruganda lakini majina unayoyakuta upande wa Tanzania ni sawasawa na unayoyakuta upande wa Uganda. Wataalam wetu wa Uhamiaji wamekuwa wanatumia kigezo hicho kuwa-judge kwamba siyo raia kwa sababu ya lugha na majina yale.

Mheshimiwa Spika, swali langu; je, ni lini Serikali itatambua hayo mahusiano ya ukaribu ya mila na desturi wananchi wakapewa haki yao ya uraia na waweze kupata pia vitambulisho vya NIDA? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali langu la pili; kwa kuwa sheria, kama aliyoitaja Naibu Waziri ya mwaka 1995 ya Uraia inaruhusu mwananchi ambaye amekaa katika nchi yetu kwa muda wa takribani miaka saba hadi kumi kwa tabia njema aweze kupata uraia wa Tajnisi. Sasa Mheshimiwa Waziri au Naibu Waziri, hamuoni ni muda muafaka twende wote katika kata hizo tukae na wananchi tuwaongoze wajaze fomu waweze kupata uraia na kuishi kwa amani katika nchi yao? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, nimshukuru sana Mheshimiwa Kyombo kwa namna anavyofuatilia kwa karibu maslahi ya wananchi wake, hususan anaoona wanakosa uraia ambao wanastahili.

Mheshimiwa Spika, kama alivyosema, bahati nzuri vigezo anavifahamu, ametaja uraia mwema lakini viko vigezo vingine ambavyo vipo kwa mujibu wa sheria, kwa haraka nitaje vichache: -

Mheshimiwa Spika, tunasema kabla ya tarehe ya kuwasilisha maombi yake ya uraia awe alikuwepo ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa miezi 12 mfululizo; kwamba katika kipindi cha miaka kumi kabla ya muda wa miezi 12 awe ameishi ndani ya Jamhuri ya Muungano kwa kipindi kisichopungua miaka saba; awe na ufahamu wa kutosha wa Lugha za Kiswahili na Kiingereza au Kiingereza; awe mwenye tabia njema. Hiyo ni moja, lakini mbili za mwisho, awe amechangia au ameshiriki katika kukuza uchumi wa Taifa na mwisho aahidi kwamba akipata uraia anayo nia ya kuendelea kuishi ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kwa hiyo ikiwa amekidhi vigezo hivi kwa kweli ana haki ya kupewa uraia.

Mheshimiwa Spika, ombi lake la pili, mimi na Waziri wangu, tuko tayari kuongozana naye na wataalam wetu ili kuona changamoto ambayo wanakabiliana nayo wananchi hawa walioko mpakani. Kuzungumza lugha ya nchi jirani hakiwezi kuwa kigezo cha kumnyima mtu uraia kwa sababu hali ya mipakani iko hivyo katika maeneo yote. Nashukuru.
MHE. HAJI AMOUR HAJI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwa vile Serikali inatambua umuhimu wa kuwepo kwa sheria ya makampuni ya ulinzi binafsi, swali langu ni hili; je, sheria gani kwa sasa hivi inayotumika kuwapatia vibali hayo makampuni binafsi ya ulinzi?

Mheshimiwa Spika, ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwa sasa hakuna sheria mahususi kwa ajili ya kazi hiyo, badala yake inatumiwa miongozo inayotolewa na Mkuu wa Polisi Nchini (IGP).
MHE. AMINA DAUD HASSAN: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi hii. Kwa kuwa tunayo makampuni mengi ya binafsi katika nchi yetu: -

Je, ni lini Serikali italeta Muswada wa kuwa na Sheria ya Makampuni Binafsi ya ulinzi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, kama nilivyojibu kwenye swali langu la msingi ni kwamba mashauriano yanaendelea baina ya Serikali zetu mbili; Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ili turidhiane. Kwa sababu suala hili linagusa Muungano, hatuwezi kulifanya upande mmoja wa Muungano tukasema tumekamilisha.

Mara taratibu hizo zitakapokamilika, then tutapeleka Muswada kwa ajili ya kupitiwa na kuridhiwa na Bunge.

Mheshimiwa Spika, nashukuru. (Makofi)
MHE. USSI SALUM PONDEZA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kwanza napenda nimpongeze Mheshimiwa Waziri kwa majibu yake mazuri, lakini nina swali dogo kabisa la nyongeza la kumuuliza.

Mheshimiwa Spika, tathmini hiyo ambayo imefanywa ya vituo vibovu na nyumba chakavu za askari, lakini katika Jimbo langu la Chumbuni nina vituo viwili ambavyo ni vibovu ambavyo vimefungwa zaidi ya miaka minne. Nataka nimuulize Mheshimiwa Waziri; yuko tayari kuambatana na mimi kwenda katika jimbo langu kwa ajili ya ukarabati wa vituo vyangu ambavyo nimekuwa navidai sasa ni awamu ya pili? Ni lini na yeye yuko tayari nami niko tayari naomba, anisaidie kwa jambo hili. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Ussi Salum Pondeza, Mbunge wa Chumbuni, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, najua katika jimbo lake Kituo cha Kiwanda cha Soda Maruhubi na Kituo cha Chumbuni ndivyo ambavyo vimeathirika sana. Nimwahidi mbele yako kwamba tarehe 22 na 23 mwezi huu wa Februari nitakuwa Zanzibar. Pamoja na mambo mengine nitakayofanya ni kutembelea Vituo vya Chumbuni. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. JUMA USONGE HAMAD: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naitwa Juma Usonge.

Mheshimiwa Spika,Mkoa wa Kaskazini Unguja ni mkoa ambao unaongoza kwa shughuli za kitalii kwa Zanzibar, lakini pia population ya watu ni kubwa sana. Naiomba sana Serikali kupitia Mheshimiwa Waziri; wamejipangaje Wizara hii ili kuhakikisha Mkoa wa Kaskazini Unguja unakuwa na idadi kubwa ya Vituo vya Polisi, ingawa sasa hivi kuna Vituo vitano tu vya Polisi? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Juma Usonge Hamad, Mbunge wa Chaani, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kama nilivyosema kwenye jibu langu la msingi, tumefanya tathmini ili tuweze kuona uchakavu wa vituo vilivyopo kwa madhumuni ya kuvifanyia ukarabati. Kwa hiyo baada ya kumaliza zoezi hilo, kwa kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar tutaona maeneo mengine yanayohitaji kuimarishwa ulinzi ili tuweze kuona namna ya kuviongezea nguvu. Ahsante. (Makofi)
MHE. ZUENA A. BUSHIRI: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kuniona ili niweze kuuliza swali la nyongeza. Kwa kuwa matatizo yaliyopo Unguja na Pemba yanafanana sawa na matatizo yaliyopo katika Kituo cha Polisi cha Gonja Maore. Kituo hiki kilijengwa tangu mwaka 1958, kilijengwa kipindi cha Mkoloni. Nyumba zake zote zimechakaa sana, Kituo cha Polisi kimechakaa sana, miundombinu yake hasa maeneo ya toilets hayafai. Je, ni lini sasa Serikali itakwenda kufanya ukarabati katika nyumba hizo? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Zuena Bushiri, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwa kweli naomba nitumie nafasi hii kusema kwamba Wizara inatambua uchakavu wa vituo na makazi ya askari katika maeneo mbalimbali nchini. Ndiyo maana tumesema tunafanya tathmini ili kuona kiwango cha uchakavu, tuandae mpango kabambe wa kukarabati vituo hivi. Kwa hiyo, Kituo cha Mheshimiwa Mbunge cha Gonja Maore tutakifuatilia ili kuona katika mwaka ujao nini tunaweza kufanya kukirekebisha kiweze kutoa huduma kwa wananchi wa Gonja. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. AHMED YAHYA ABDULWAKIL: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kuniona. Naomba nimuulize swali Mheshimiwa Naibu Waziri; kwa kuwa Jimbo la Chukwani wananchi wamejenga kituo kipya cha ghorofa moja na mpaka sasa kimefikia asilimia 85, bado asilimia 15 kimalizike.

Naomba Serikali itoe kauli lini kituo kile kitamalizika na kuanza kutumika na hasa ukitia maanani kwamba lilitokea wimbi kubwa la mauaji katika eneo lile? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Yahya, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, napokea ombi au swali lenye mwelekeo wa ombi la Mheshimiwa Yahya, kwamba katika vitu ambavyo tutaviangalia kule ambako wananchi wamejitokeza wakachangia nguvu zao na rasilimali zao nyingine kupitia Mfuko wetu wa tozo tunaweza kuwasaidia ili kukamilisha vituo hivyo. Kwa hiyo katika tathmini itakayofanyika kwa Mheshimiwa Mbunge pia tutapazingatia. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Mwenyekiti nakushukuru, nimesikiliza majibu ya Serikali.

Mheshimiwa mwenyekiti, swali langu la msingi lilijikita mpakani tukiamini kwamba Wilaya ya Nkasi inapakana na nchi ya Congo na nchi ya Burundi, Kituo cha Polisi ambacho Mheshimiwa Naibu Waziri anajibu anazungumzia Daraja C, Daraja C hilo ambalo unalizungumza katika kata 10 za mwambao unazungumzia kata tano, na hao askari kila kituo ni askari watano, hakuna pikipiki, hakuna gari, hakuna usafiri wa majini wala wa nchi kavu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa maeneo hayo yamekuwa yanavamiwa mara kwa mara Serikali haioni haja kwa kuwa shida yetu sio majengo ya kituo cha polisi, tunataka vituo vya Polisi vyenye hadhi ya kupambana ikitokea uvamizi kwenye maeneo ya mpaka. Hamuoni haja sasa ya kujenga vituo hivyo kwenye maeneo ya mpakani?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa kuwa katika kata 10 za mwambao ambazo ndio zimekuwa zinatumiwa na hao maadui. Kata tano zina vituo; kata tano hazina.

Je, tunaomba kujua Serikali ina mpango gani wa haraka kwa kuwasaidia ulinzi wa wale watu kwa sababu sio ulinzi wa Nkasi ni ulinzi wa nchi nzima, ni lini mtajenga vituo hivyo vya polisi kwenye kata ya Korongwe, Nkinga na kata ya Kala ambayo wanavamiwa kila wakati? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Aida Joseph Khenani Mbunge wa Nkasi Kaskazini kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua umuhimu wa uwepo wa vituo vya Polisi hasa maeneo yaliyo katika mipaka, na sio uwepo tu wa Jeshi la Polisi lakini kupitia Wizara ya mambo ya ndani Serikali inatambua umuhimu wa kuwepo hata vyombo vyengine, ili lengo na madhumuni mipaka yetu iendelee kubakia kuwepo salama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, Mheshimiwa nimwambie tu kwamba katika mipaka mingi ambayo nimeizunguka wakati ule hasa nilipokuwa nipo katika Wizara ya Mambo ya Nchi, ambao naamini na Waziri huyu ambae sasa hivi ndio Waziri wa Mambo ya Ndani alikuwepo kule aliizunguka mipaka mingi. Maeneo mengi vituo vya Polisi vipo, lakini vituo hivi vipo distance kidogo na maeneo ya mipaka. baada ya kuona kwamba kwenye ile mipaka yenyewe Polisi na vyombo vyengine wapo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nimawambi tu Mheshimiwa asiwe na wasiwasi, Serikali itaendelea kujenga vituo vya Polisi, ili lengo na madhumuni wananchi waweze kuishi kwa amani na uatulivu ikiwa mipakani, ikiwa ndani ya miji, ikiwa pembezoni, ikiwa popote lengo na madhumuni watanzania waishi kwa amani na utulivu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia Serikali itaendelea kuhakikisha kwamba inapeleka vitendea kazi ili lengo na madhumuni zile huduma za doria na mambo mengine yapatikane katika maeneo ya wananchi, ninakushukuru.
MHE. FAKHARIA SHOMAR KHAMIS: Mheshimiwa Mwenyekiti ahsante, kwa kuwa kituo cha Polisi cha Ng’ambo ambacho kipo Wilaya ya Mjini Unguja kina tataizo kama vituo kituo cha Polisi kilichozungumzwa. Na tatizo letu hasa ni uzio. Kwa sababu kituo hicho kipo katikati ya barabara pande zote, pia kimezungukwa na mitaa hatari ya magari yanaweza yakaingia ndani yakagonga kituo, au wanyama wanaofugwa mtaani wakaingia ndani na kituo hicho kipo tokea wakati wa ukolono, hakijaongezwa uzio, ulikuwa uzio wa senyenge umezungushwa na majani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Naibu Waziri aliwahi kuzungumza kwenye baraza hili tukufu kwamba wakati wowote utawekwa uzio toka bajeti tuliyoimaliza na tunaenda kwenye bajeti mpya hali hiyo haijatengamaa. Je, uzio huo utawekwa lini ili watu wa pale wapate amani? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante nakushukuru, naomba sasa kujibu swala la nyongeza la Mheshimiwa bi Fakharia Mbunge wa viti maalum kutoka Mkoa wa Mjini kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kituo hichi ni moja ya miongoni mwa vituo vya Polisi ambavyo nimevifanyia ziara, na moja ya miongoni mwa vitu ambavyo tayari vimeshafanyika ni tathmini kwa ajili ya ujenzi wa uzio wa kituo kile, kalini wakati huo tunafanya tathmini tunaangali namna kwa sababu kile kituo ukikitazama unakuta kwamba kila pembe kimezungukwa na barabara. Kwa hiyo, the way utakavyojenga uzio kuna hatari ukaja ukajikuta kwamba unaila ile barabara. Sasa kula chote lakini usiile barabara kwasababu unaweza ukatengeneza mazingira mengine ambayo yanaweza kusababisha ajali za barabarani ambazo hazina sababu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kikubwa nimwambie Mheshimiwa kwamba tathmini imeshafanyika na sasa tunatafuta fedha kwa ajili ya ujenzi wa kituo kile, Mheshimiwa wewe kwa niaba ya wananchi muwe na subra kidogo mtusubirie na sisi tumo mbioni kuhakikisha kwamba uzio unajengwa katika kituo kile. Ahsante.
MHE. AGNES E. HOKORORO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali dogo la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya za Mkoa wa Mtwara takriban zote ziko mpakani. Je, Serikali iampango gani wa kujenga kituo cha Polisi katika Wilaya Masasi katika kata za mpakani kabisa za Mnadhira, Mchauru, Sindano na Chikoropola ambapo kwa sasa kunaonekana kuna vuguvugu za vurugu kati ya wakulima na wafugaji? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Agnes Hokororo Mbunge wa Viti maalum kutoka Mtwara kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati tunapitisha ile bajeti yetu ya 2021/2022 moja ya miongoni mwa mambo ambayo tunakwenda kuyafanya katika bajeti ile ni kujenga vituo vingi vya Polisi na hasa yale maeneo ambayo yanautauta kiulinzi, maeneo ya mipakani na maeneo mengine ambayo tunahisi yana sababu za zaidi asilimia moja kuwepo kwa vituo vya Polisi kwa ajili ya kulinda Maisha ya wananchi na mali zao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nimwambie Mheshimiwa kwamba awe na subra Serikali itahakikisha kwamba inajenga vituo vya Polisi maeneo mengi lakini hasa katika maeneo ambayo wameyataja ili liengi na madhumuni wananchi waweze kuishi katika Maisha ya ulinzi na usalama zaidi, Nashukuru.
MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Wilaya ya Lushoto ina tarafa 8 lakini tuna vituo 5 tu vya Polisi, lakini katika Kata ya Lukozi na Lunguza ambazo ni miji midogo na hii Lunguza ipo karibu kabisa na mpaka wa nchi jirani ya Kenya, wananchi wale wametenda maeneo na wanataka kulikabizi Jeshi la Polisi ili kwa kushirikiana nao tuweze kujenga vituo vya Polisi. Je, Waziri yuko tayari kumuagiza Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Tanga aje akabaini yale amaeneo na shughuli za ujenzi zianze? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Rashidi Shangazi Mbunge kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, moja ya miongoni mwa azma kubwa ya Serikali ni kuhakikisha kwamba wananchi wanaishi kwa amani na utulivu katika maeneo yao hasa baada ya kupata ushirikiano kutoka kwa Jeshi la Polisi na vyombo vyengine vya ulinzi na usalama, na zaidi pale wananchi wanapoamua kwamba wao wenyewe wameshajitolea wako tayari kujenga kituo cha Polisi, sisi kama Serikali kama Wizara kama Jeshi la Polisi tupo tayari kutoa ushirikiano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa nichukue fursa hii kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi nimuagize RPC Mkoa wa Tanga kwa kushirikiana na OCDs wake na baadhi ya mastafu wake, wahakikishe kwamba wanakwenda kutoa ushirikiano kwa wananchi ili lengo namadhumuni kituo hiki cha Polisi kijengwe ili wananchi waweze kupata huduma ya ulinzi na usalama. Nakushukuru.
MHE. PROF. KITILA A. MKUMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa nafasi hii. Wananchi wa mtaa wa Mavurunza Kata ya Kimara na mtaa Kibo kata ua Ubungo, tumechangishana tumejenga vituo 2 vya Polisi lakini hatujamalizia kwa sababu nguvu zimeisha. Je, Serikali inaweza ikaahidi kuingiza katika bajeti ijayo ili vituo hivi vikamilike? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Profesa Kitila Mkumbo Mbunge wa Jimbo la Ubungo kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, narejea tena azma ya Serikali ni kuhakikisha wananchi wanajengewa vituo vya Polisi ili lengo na madhumuni waweze kupata pahala pa kupeleka matatizo yao, lakini pia waweze kulindwa wao na mali zao. Nimwambie tu kwamba tupo tayari kuhakikisha kwamba tunaingiza fungu maalum kwa ajili ya ujenzi wa hicho kituo ili lengo na madhumuni wananchi wa Ubungo na maeneo ya Jirani waweze kunufauika na kituo hicho. Nakushukuru sana.
MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. pamoja na majibu ya Serikali, na kwa kuwa amekiri kwamba Muswada huu umeshasomwa kwa mara ya kwanza Bungeni, ni commitment gani anatoa kwa maana Muswada huu uweze kuja kwa mara ya pili, hatimaye mara ya tatu ili hii sheria iweze kuboreshwa?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; Sheria ya Usalama Barabarani ya mwaka 1973 ilikuwa haitambui usafiri wa pikipiki, almaarufu kama bodaboda, kama ni chombo rasmi cha kusafirisha abiria na chombo hiki sasa hivi kinatumika kwa Watanzania walio wengi nchini. Kama sheria hii itaendelea kuchukua muda, Serikali haioni umuhimu wa kuleta kwa hati ya dharura hata katika sheria ya mabadiliko mbalimbali ili jambo hili liweze kuwa katika sheria zetu za nchini?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali ya nyongeza ya Mheshimiwa Rashid Abdallah Shangazi, Mbunge wa Mlalo, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu commitment ya Serikali, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba katika vikao vijavyo ambavyo tutaruhusu marekebisho ya sheria tutaangalia uwezekano wa kuileta sheria hiyo ili iweze kupitishwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu hili suala la usafiri wa pikipiki, hili ni pamoja na mambo mengine ambayo yalijitokeza na hususan maoni ya Kamati ya NUU, yalibaini kwamba pana mambo mengine ya kuhitaji kuzingatiwa ukiwemo usafiri wa pikipiki. Kwa hiyo ni ahadi yetu kwamba muswada huo utakapoletwa humu utakuwa pia umezigatia masuala ya usafiri wa bodaboda. Ahsante. (Makofi)
MHE. TARIMBA G. ABBAS: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi. Ni kweli kuna haja ya kuweza kuifanyia marekebisho sheria hii ya mwaka 1973, lakini kama ilivyo sheria hii, bado ina nguvu ya kuweza kusimamia matatizo ya usalama barabarani kama askari wa polisi wa usalama barabarani watakuwa wanafanya kazi yao inavyostahiki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu bodaboda zinapita taa nyekundu, zinapita no entry, zinapita barabara za mwendokasi; ni nini kauli ya Serikali wakati tunasubiri kwenda kurekebisha sheria kwenye suala hili linalohusiana na matumizi mabaya ya barabara? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba swali la nyongeza la Mheshimiwa Abbas Tarimba, Mbunge wa Kinondoni, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakubaliana naye, kwamba sheria ilivyo bado inaweza ikadhibiti usalama barabarani ikisimamiwa ipasavyo. Lakini hawa vijana wetu wanaoendesha bodaboda matendo wanayofanya ni hatarishi, siyo kwao tu, bali hata wale abiria wanaowabeba kama wataendelea kutumia barabara kama wanavyofanya inavyozungumzwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitumie Bunge lako Tukufu kuviomba vyombo vyote vya dola vishirikiane na hawa polisi wa usalama barabarani kuwadhibiti vijana hawa, lakini pia kutumia nafasi hii kuwaelimisha wazingatie Sheria ya Usalama Barabarani kama ambavyo imeanza kufanyika kwenye maeneo mengine. (Makofi)
MHE. MWANTATU MBARAK KHAMIS: Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yake mazuri na yenye kuleta matumaini. Lakini pia niwapongeze kwa kuona umuhimu wa kukifungua Kituo cha Jang’ombe kwa kuweza kuwasaidia wananchi wa eneo hili. Lakini nina swali moja la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na kufungwa kwa vituo hivi kwa muda mrefu vinaonekana kuchakaa, na Mheshimiwa Waziri amesema kwamba pindi tu askari watakapotoka shule Moshi vituo vile vitafunguliwa. Je, wana mpango gani wa kuvifanyia ukarabati vituo vile ambavyo vimefungwa kwa muda mrefu ili viweze kuwa na mwonekano mzuri wa kiofisi? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mwantatu Mbarak Khamis, Mbunge wa Kotoka Baraza la Wawakilishi kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba vituo hivi ambavyo vimefungwa muda mrefu kwa vyovyote vile haviwezi kwenda kuanza bila angalau kufanyiwa ukarabati. Nitumie nafasi hii kumuomba Kamishna wa Polisi Zanzibar aweze kufanya marekebisho ya vituo hivi kabla ya kupangiwa askari baada ya kuhitimu mafunzo yao. Nashukuru.
MHE. REGINA N. QWARAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kuniona niweze kuuliza swali la nyongeza. Katika Tarafa ya Bashnet tuna vituo viwili vya polisi; Kituo cha Bashnet na Kituo cha Dareda, lakini huduma hutolewa kwa saa 12 tu. Je, Serikali haioni sasa kutokana na ongezeko kubwa la uhalifu katika maeneo yale kuanzisha huduma kwa saa 24 ili kuboresha ulinzi katika maeneo hayo? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Regina Qwaray kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunatambua, na kama nilivyoeleza majuzi, maeneo yote ambayo yana vihatarishi vya usalama ni wajibu wa viongozi wetu wa Jeshi la Polisi ngazi ya wilaya kwa maana ya ODC na RPC ngazi ya mkoa kuona wapi tuwekeze nguvu. Na kwa kushirikiana na Mamlaka zetu za Serikali za Mitaa kama wananchi wanaona upo umuhimu wa kufungua kituo kile, tuko tayari kushirikiana nao kuona uwezekano wa kuvianzisha kudhibiti matendo ya uhalifu katika maeneo hayo. Nashukuru. (Makofi)
MHE. ABUBAKARI D. ASENGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Wilaya ya Kilombero ni miongoni mwa wilaya kongwe sana, lakini haina Kituo cha Polisi cha Wilaya, hali inayopelekea OCD na askari wake kutumia Kituo Kidogo cha Ifakara kama Kituo cha Polisi cha Wilaya. Sasa swali langu dogo tu. Je, Mheshimiwa Naibu Waziri atakuwa tayari kutembelea Kilombero kujionea Kituo Kidogo cha Polisi Ifakara kinavyozingirwa na mafuriko kupelekea polisi wetu kwenda kazini wakiwa wamekunja suruari na kuvua viatu ili apandishe morali ya Serikali kusaidia juhudi ya Mkuu wa Wilaya, Mkurugenzi na Mbunge kujenga kituo cha polisi kipya?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Abubakari Asenga, Mbunge wa Kilombero, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati wote nipo tayari kuungana na Mheshimiwa Mbunge kufuatilia jambo hili. Nilikwenda kutembelea gereza kule Kilombero alizungumza juu ya jambo hili, muda haukuruhusu. Hivyo, nipo tayari baada ya Bunge hili kuongozana ili tukatatue tatizo lake lililotajwa. Ahsante. (Makofi)
MHE. KASALALI E. MAGENI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Katika Jimbo la Sumve, jimbo zima hakuna Kituo cha Polisi ambacho kina sifa ya kutunza silaha. Serikali kupitia Mawaziri mbalimbali wa Mambo ya Ndani imeshaahidi kuboresha Kituo cha Polisi cha Nyambiti ili kiweze kujengewa jengo la kutunza silaha.

Je, Serikali haioni kwamba umefika wakati sasa wa kuhakikisha kwamba Jimbo la Sumve na lenyewe linakuwa na Kituo cha Polisi chenye sifa ya kuwalinda watu wa Sumve muda wote? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Kasalali Mageni, Mbunge wa Sumve, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati wowote Serikali ya Chama cha Mapinduzi iko tayari kuwahudumia wananchi wake kwa njia zote za kiusalama. Jimbo la Sumve ni Jimbo moja katika Wilaya ya Kwimba, kwa hiyo, matarajio yangu ni kwamba kama pana haja ya kuanzisha Kituo cha Polisi cha hadhi ya Tarafa na kikawa na majengo stahiki kinaweza kutunza silaha. Naomba kupitia Bunge lako Tukufu nimwahidi Mheshimiwa Kasalali kwamba baada ya Bunge hili katika ziara yangu Kanda ya Ziwa nipo tayari kutembelea eneo lake ili kuona namna ambavyo tunaweza tukashughulikia suala la kuimarisha usalama katika eneo lake. Ahsante. (Makofi)
MHE. AMINA DAUD HASSAN: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kwa kuniona na kunipa nafasi hii. Kwa kuwa Kituo cha Polisi cha Uzing’ambwa kipo ndani ya kisiwa ambacho kimejitenga na vijiji vingine na kufungwa kwa kituo hiki kumeleta kero kubwa kwa wananchi wa eneo hili pindi wanapohitaji msaada wa Kituo cha Polisi. Je, Serikali haioni kuna haja ya dharura ya kufungua kituo hiki kwa lengo la kuwasaidia wananchi wa vijiji hivi viwili? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Amina Daudi Hassan, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyoahidi majuzi kwamba tarehe 22 na 23 nitakuwa Zanzibar pamoja na mambo mengine kukagua Vituo vya Polisi vya Chumbuni, niko tayari kuungana na Mheshimiwa Amina kuangalia kituo chake hiki ili kuona uwezekano wa kukifanyia matengenezo. Nashukuru. (Makofi)
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Wilaya ya Bunda ina majimbo matatu, Bunda Mjini, Bunda na Mwibara. Tuna kituo kimoja ambacho ni chakavu hakiendani na hadhi ya Kituo cha Wilaya. Mheshimiwa Naibu Waziri anakijua, anapita pale akienda jimboni kwaeo, nimeuliza zaidi ya mara tatu swali hili.

Lini Serikali itakifanyia ukarabati Kituo cha Polisi cha Wilaya ya Bunda kiendane na hadhi ya wilaya? Nilipokuwa Mbunge nilitengeneza Ofisi ya Upelelezi. Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Ester Bulaya, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba Kituo cha Polisi cha Wilaya ya Bunda nakifahamu na kama zilivyo wilaya nyingi na hasa wilaya mpya kinahitaji kuimarishwa.

Sasa hivi tunaendelea na ujenzi wa Vituo vya Polisi vya ngazi ya mikoa maana tunayo baadhi ya mikoa ambayo haina Makao Makuu ya RPC; na wilaya mpya ambazo zimeanzishwa tangu mwaka 2012. Naomba kumuahidi Mheshimiwa Bulaya katika mpango wetu wa ukarabati wa vituo hivyo Bunda pia itazingatiwa. Nashukuru. (Makofi)
MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Kwanza niseme nasikitishwa na majibu ya Serikali: -

Mheshimiwa Naibu Spika, sote tunafahamu jinsi Taifa letu linavyokumbwa na majanga mbalimbali ya moto, kama kuungua kwa masoko, shhule, nyumba binafsi na hata kwenye biashara mbalimbali kama hoteli na vinginevyo, ambayo inasababisha hasara kwa mali za raia, lakini hata uhai wao.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa, magari ya kisasa, on average, ni kuanzia milioni 500 na kuendelea. Na bajeti ya Serikali imeonesha kutenga bilioni mbili tu kwa maana ya kwamba, watanunua walao magari manne tu tena hayo ni ya wastani. Ni kwanini sasa Serikali isione umuhimu wa kutenga fedha kwa udharura, ili waweze kununua magari walao mawili katika kila halmashauri, kama ambavyo wanafanya kwenye magari ya washawasha? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili, sote tumeshuhudia wakati wa chaguzi ambazo zinafanyika kila baada ya miaka mitano kwenye majimbo yetu kunakuja magari ya washawasha zaidi ya mawili matatu, ambayo gari moja la washawasha ni takribani milioni 500, kama ilivyo kwa gharama za gari la zimamoto. Je, kipaumbele cha Serikali ni kipi kati ya kulinda mali ya raia na uhai wao dhidi ya kudhibiti wapinzani wakati wa uchaguzi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Esther Nicholas Matiko, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema kwenye jibu langu la msingi. Serikali inatenga fedha mwaka huu, imetenga mwaka jana bilioni mbili na nusu, mwaka huu imetenga bilioni mbili. Tutaendelea kutenga fedha hizo au zaidi kutegemea upatikanaji wa fedha ili kuimarisha jeshi hili.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia nikumbushe. Jeshi la Zimamoto na Uokoaji halifanyi kazi peke yake, hushirikisha majeshi mengine na vituo vingine kama viwanja vya ndege, bandari na kadhalika.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili, tunathamini mali na wananchi wetu kwa hiyo, mfano anaoutoa wa washawasha hauna uhusiano wa moja kwa moja na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji.nashukuru sana. (Makofi)
MHE. SEBASTIAN S. KAPUFI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa nafasi.

Mheshimiwa Naibu Spika, Halmashauri ya Manispaa ya Mpanda ilikuwa na gari zuri la zimamoto, gari ambalo lilikuwa ni la kisasa. Kwa bahati mbaya lilipata ajali mwaka 2015, toka Serikali imelichukua kwa ajili ya matengezo, gari hilo halijaweza kurejeshwa Mpanda. Swali langu, ni lini Serikali itaturejeshea gari hilo zuri na la kisasa?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nijibu swali la Mheshimiwa Mbunge, la nyongeza, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, tuna interest na Tanga kutokana na miradi mingi mliyonayo ya kiuchumi ikiwemo bandari na bomba la mafuta linalopita pale. Tutafuatilia baada ya Bunge hili kuona kwamba, matengenezo ya gari hilo yanakamilika lirejeshwe Tanga kwa ajili ya kuendelea kutoa huduma kwa wananchi. Ahsante sana.
MHE. SAASHISHA E. MAFUWE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali: -

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na uchakavu wa Kituo cha Polisi cha Wilaya ya Hai, lakini Wilaya ya Hai ina watumishi 149, hakuna nyumba hata moja ya watumishi hawa, kiasi kwamba, OCD, OC-CID na Mkuu wa Kituo cha Polisi Wilaya ya Hai anakaa mbali sana kwa hiyo, wanashindwa kutoa huduma pale. Ni lini sasa Serikali itajenga walao hata nyumba moja tu ya Mkuu wa Kituo Wilaya ya Hai?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Saashisha Mafuwe, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, ni nia ya Serikali kuweka mazingira bora ya utendaji wa kazi wa vyombo vyetu vya ulinzi, hasa vya usalama, ikiwemo Polisi, Zimamoto, Magereza,
n.k. Kama nilivyosema katika jibu nililotoa juzi, tunaendelea kutenga fedha na mwaka huu zipo fedha zimetengwa kwa ajili hiyo. Lengo ni kuhakikisha kwamba, maeneo yote ambayo hayana nyumba yanapewa kipaumbele ikiwemo wilaya yako ya Hai. Ahsante sana
MHE. DOROTHY G. KILAVE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, swali langu mimi ni, kule Temeke Kata ya Sandali, kuna jengo kubwa sana ambalo mmelijenga la zimamoto, lakini mpaka sasa halijamaliziwa wala hakuna vifaa vyovyote ambavyo vimeingizwa kwa ajili ya zimamoto.

Je, ni lini sasa vifaa hivi pamoja na jingo lile litamalizika kwa ajili ye Serikali yetu?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Kilave, Mbunge wa Temeke, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, nalifahamu amelizungumzia suala hilo la eneo la Mchicha majuzi, tutalipa kipaumbele kwa interest ya watu wa Dar es Salaam, uchumi wao na shughuli nyingi za kiviwanda zinazotekelezwa ili kuwawezesha Fire kutimiza majukumu yao kwa ufanisi.
MHE. DKT. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi na nishukuru sana majibu ya Naibu Waziri japokuwa yamekuwa ni hayo hayo muda mrefu.

Mheshimiwa Spika, changamoto iliyopo katika muingiliano huu wa hospitali na magereza kwa kweli unatesa sana wananchi wa Mkoa wa Iringa. Kiasi kwamba barabara ile imefungwa ambayo inaingilia hospitali kuna wakati wafungwa wakitolewa, ambulance inashindwa kupita inazunguka mzunguko mrefu sana kumuwahisha mgonjwa hospitali. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini kwa kuwa tulipokaa katika kikao cha Mkoa - RCC iliazimia kwamba kwa sababu hii changamoto haitatuliki basi tuiombe Serikali either ibadilishe kwamba majengo yaliyopo katika hospitali hii yawe hospitali ya wilaya na eneo ambalo lipo Frelimo kwa sababu ni kubwa sana linaweza likajengewa hata nyumba za madaktari basi iwe ndio hospitali yajengwe majengo ya hospitali ya mkoa. (Makofi)

Je, sasa Mheshimiwa Waziri yupo tayari kushirikiana na Wizara ya Afya ili kuona changamoto hii iweze kuondoa tatizo lililopo katika Mkoa wetu wa Iringa? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali langu la pili; sambamba na hilo kwa kuwa katika Mkoa wetu wa Iringa pia lipo Gereza Kihesa Mgagao, Wilaya ya Kilolo, hili eneo ni eneo ambalo walikaa wapigania uhuru wa South Africa - ANC lakini utaona wenzetu walipokaa…

SPIKA: Mheshimiwa Ritta uliza swali.

MHE. DKT. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Spika, ndio.

Mazimbwi, Dakawa wamejenga vituo vya maendeleo kama shule hospitali lakini eneo hili bado kuna Gereza…

SPIKA: Uliza swali Mheshimiwa Ritta.

MHE. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Spika, je, Serikali sasa kwa sababu tulikuwa tumeomba pia hilo Gereza lihamishwe ili kijengwe hata Chuo cha VETA… (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Dkt. Kabati kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwanza Wizara yangu iko tayari kuwasiliana na Wizara ya TAMISEMI na Wizara ya Afya ili kuona uwezekano wa kuhamisha mojawapo ya huduma kutoka Hospitali ya Mkoa iwe Hospitali ya Wilaya halina tatizo kabisa.

Mheshimiwa Spika, lakini hili la pili nadhani halikukamilika swali lenyewe kwa hiyo, nashukuru sana. (Makofi/Kicheko)
MHE. NICHOLAUS G. NGASSA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, nyumba hizi tunazoziongelea kama alivyosema Naibu Waziri zipo nne na zinakaa familia 20 zilijengwa mwaka 1993 nakumbuka mimi nilikuwa darasa la kwanza; sasa zimechakaa sana na zinahatarisha usalama wa askari wetu. Mimi ninachoomba ni commitment ya Serikali na mwaka jana kwenye bajeti niliongelea. (Makofi)

Ni lini watatuweka katika kipaumbele cha kuzijenga nyumba hizi ili tusihatarishe maisha ya askari wetu? Hilo la kwanza. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, la pili Naibu Waziri je, atakuwa tayari baada ya hili Bunge kuahirishwa apite Igunga, tuweze kwenda kuona hali halisi ambayo naiongelea hapa kabla maafa hayajatokea kuathirisha maisha? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawii ya nyongeza ya Mheshimiwa Ngassa kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kuhusu commitment tunayo kama nilivyokwisha eleza tumefanya tathmini gharama zinajulikana, tutaanza awamu kwa awamu kukarabati nyumba ambazo zina hali mbaya sana. Kwa maana hiyo tutakapokuwa tunamaliza shughuli za Bunge katika ziara yangu niliyokwisha ahidi kutembelea Sumve - Mwanza, tutapita Igunga kuona kiwango cha uchakavu ili kuipa kipaumbele katika ukarabati wa nyumba hizo. Nashukuru. (Makofi)
MHE. OMAR ISSA KOMBO: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Je, ni lini Serikali itamalizia na kukarabati ujenzi wa nyumba za polisi katika kituo cha polisi Wilaya ya Micheweni? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, kama nilivyokwisha jibu katika swali langu la msingi, Micheweni ambako kunahitajika pia ujenzi wa nyumba na kuboresha kituo ni miongoni mwa vituo ambavyo vitaimarishwa kulingana na mpango wetu wa kukarabati nyumba na vituo chakavu. Nashukuru. (Makofi)
MHE. MARIAM N. KISANGI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kunipa nafasi na mimi niweze kuuliza swali la nyongeza.

Je, Serikali ina mpango gani wa kukarabati makazi ya askari polisi Wilaya ya Mbagala ambayo yana hali mbaya sana, sana, sana pamoja na kituo cha polisi cha Wilaya ya Mbagala? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mariam Kisangi kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, niliahidi tarehe 22 Februari nitakuwa Dar es Salaam naomba Mbunge awe tayari tuzunguke naye kwenye maeneo ya Mbagala, kuona kiwango cha uchakavu ili kwa pamoja tutafakari namna ya kuboresha majengo hayo kupitia bajeti yetu tunayotoa kila mwaka. Ahsante. (Makofi)
MHE. RAMADHAN SULEIMAN RAMADHAN: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Ingawa Mheshimiwa Naibu Waziri amejibu vizuri kwenye swali lake la msingi, naomba nimwulize maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza ni kwamba, wakati tunasubiri fedha zitengwe kwenye bajeti ya mwaka 2023/2024 kwa ajili ya ujenzi wa Kituo kikubwa.

Je, Serikali haioni haja ya kujenga vituo vidogo vya Polisi (Police Post) kwenye maeneo tofauti ya Mji wa Chakechake? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, la pili je, Mheshimiwa Naibu Waziri yuko tayari kufuatana nami twende kwenye eneo la Chakechake akaone jiografia na kama ujenzi wa Kituo cha Vitongoji ndiyo ingekuwa suluhisho la wananchi kufuata huduma za kipolisi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Ramadhan Suleiman Ramadhan, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, moja, ni kweli kwamba pale ambapo pana umuhimu Serikali inaweza ikasaidiana na wananchi kujenga Police Post kwa maana ya vituo vidogo vya Polisi panapohitajika. Hata hivyo, kwa sababu Kituo cha Chakechake kwa sasa kimechakaa, kinahitajika kujengwa kituo kipya, kipaumbele tumeweka kwenye kujenga kituo kipya katika mwaka wa fedha ujao. Namwomba Mheshimiwa Mbunge akubaliane nasi tulitekeleze hilo kwanza.

Mheshimiwa Spika, jambo la pili juu ya umuhimu wa kuongozana naye kwenda vitongojini, niko tayari, hakuna kikwazo chochote. Wakati utakapofika tukaambiana basi tutaongozana. Nashukuru. (Makofi)
MHE. USSI SALUM PONDEZA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii nami niulize swali dogo la nyongeza. Kama ilivyo Jimbo la Chakechake kuhusu kujengewa kituo; nami nimekuwa nikiuliza sana katika Jimbo langu la Chumbuni; na nimekuwa nikipewa ahadi zaidi ya mara sita, saba kwa vituo vyangu viwili vya Marubi na Chumbuni kuwa nitapata msaada kutoka Jeshi la Polisi na kujengewa; na tuliwahi kuuliza ikiwa Serikali iko tayari kuvirasimisha kwetu, kwa wananchi wa Jimbo la Chumbuni? Basi wafanye hivyo, halafu watupe kibali, nasi tunaweza kuendelea wenyewe. Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Pondeza, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli amekuwa akiuliza maswali ya Chumbuni na nilimwahidi katika kipindi cha bajeti cha Aprili – Juni. Niliweza kwenda Zanzibar na nilitembelea kituo chake. Kinachogomba ni upatikanaji wa fedha ndiyo maana tunaweka vipaumbele. Mheshimiwa Mbunge avumilie na akubaliane nami kwamba pale tutakapopata fedha, Chumbuni itapewa kipaumbele kama tunavyofanya kwenye maeneo mengine ya Chakechake na kwingineko. Nashukuru. (Makofi)
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Wilaya ya Liwale ina umri wa miaka 47 sasa, haijawahi kuwa na jengo la Kituo cha Polisi ukiacha lile jengo ambao wamepanga lililokuwa la benki. Nini, kauli ya Serikali kuipatia Wilaya ya Liwale jengo la Polisi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge wa Liwale, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, tunafahamu Wilaya kongwe hizi zimekuwa na vituo lakini chakavu sana. Sasa kwa bahati mbaya Liwale hawajawahi kuna nacho. Namwahidi kwamba katika bajeti ijayo tutaweka kipaumbele ili Wilaya yake ianze mchakato wa kujenga kituo chake cha Polisi kama zilivyo Wilaya nyingine za Tanzania Bara. Nashukuru. (Makofi)
MHE. KHALIFA MOHAMED ISSA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Nami nimwulize swali moja dogo la nyongeza Mheshimiwa Naibu Waziri. Kituo cha Wete ndiyo Makao Makuu ya Polisi Mkoa wa Kaskazini Pemba. Kituo kimechakaa, hakina hadhi: Ni lini Serikali itakikarabati kituo kile? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mbunge wa Wete, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, nafahamu na Mheshimiwa Mbunge anafahamu kwamba vituo vingi vilivyojengwa siku nyingi vimechakaa sana. Kama atafuatilia, tumeanza kukarabati vituo vya Polisi vikianzia Makao Makuu pale Zanzibar na makazi yao. Tutaendelea kufanya hivyo maeneo ya Pemba kutegemea upatikanaji wa fedha.

Mheshimiwa Spika, tumeshakubaliana na Mheshimiwa Mbunge kwamba awamu ijayo nitatembelea Pemba na eneo la Wete ni eneo nitakalolipa kipaumbele katika ziara yangu. Nashukuru.
MHE. MOHAMED SAID ISSA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naomba kuuliza swali dogo la nyongeza. Katika Bunge lililopita la bajeti, Wizara ya Mambo ya Ndani iliniahidi kituo cha Konde kutengenezwa kwa thamani ya shilingi 41,500,000 na bajeti tayari tumeshapitisha.

Je, ni lini Wakandarasi watafika kwenye Kituo cha Konde na kuanza matengenezo? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika,
naomba kumjibu Mheshimiwa Mbunge wa Konde, swali lake la nyongeza kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, maadamu bajeti imepitishwa na ipo na anachosubiri ni Mkandarasi, tutawasiliana na Kamishna wa Polisi Zanzibar ili mipango ya kumpa Mkandarasi, kwa sababu tunatumia force account, aweze kuelekezwa engineer wa Polisi Zanzibar ili ukarabati wa jengo hilo uweze kuanza. Nashukuru. (Makofi)
MHE. PROF. SHUKRANI E. MANYA: Mheshimwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Janejelly Ntate, nipende kuuliza swali la nyongeza – na kwanza ninashukuru kwa majibu ya Serikali – kwamba sasa baada ya kukamilisha kituo hicho, ni lini sasa watumishi wataletwa ili kuimarisha hali ya usalama katika maeneo hayo?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru baada ya kituo hiki kukamilishwa nampa assurance Mheshimiwa Mbunge kwa niaba ya Mheshimiwa Janejelly kwamba Serikali kupitia Jeshi la Polisi Kanda Maalum Mkoa wa Dar es Salaam na Mkoa wa Kipolisi wa Temeke, mara moja watapelekwa Askari kwa ajili ya kuanza kutoa huduma. Ikumbukwe kwamba sasa hivi tunao Askari mpaka ngazi ya Kata na eneo hili lipo kwenye utawala wa Kata na Inspectors wameshapangwa kule wameshapangwa kule kwa ajili ya kutoa huduma za ulinzi. Kituo kikikamilika tutapeleka askari wa kutosha ili kutekeleza majukumu ya usalama kwenye eneo hilo. (Makofi)
MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wote tunajua usalama ulivyo, Kituo cha Polisi Mgeta ni kituo kiko Makao Makuu ya Tarafa ya Chamuriho, toka mwaka jana nimeahidiwa kwamba fedha zitakwenda kumalizia boma la kituo hicho Waziri wa Mambo ya Ndani alishaahidi, wewe Naibu Waziri ulishaahidi. Je, ni lini hela zitakwenda kwenye kituo hicho?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kumjibu Mheshimiwa Getere kwamba ni kweli kwamba kwa mara kadhaa tumeahidi kwamba kituo hicho kitakamilishwa na ndiyo tumeanza tu Mheshimiwa Getere, ni mwezi wa tatu tangu tulipoanza utekelezaji wa bajeti, ninakuahidi tu katika robo inayokuja tutahakikisha kupitia Jeshi la Polisi fedha inapelekwa ili kukamilisha ujenzi wa kituo cha Mgeta ambacho ni muhimu sana kwa usalama wa wananchi wa eneo la Mgeta na Tarafa nzima ya Wilaya ya Bunda Vijijini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru.(Makofi)
MHE. BUPE N. MWAKANG’ATA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza. Kituo cha Polisi cha Sumbawanga Mjini ni cha toka enzi za mkoloni.

Je, ni lini Serikali itaanza ujenzi wa kituo hicho? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza Mheshimiwa Mbunge kwamba vituo vyote ambavyo ni chakavu, wakati fulani tuliwahi kusema hapa Bungeni vimefanyiwa tathmini na kinachosubiriwa ni upatikanaji wa fedha tu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kipaumbele kikubwa tulikielekeza kwenye maeneo ambayo hayakuwa na vituo vya Polisi kabisa, ndiyo maana ukarabati kidogo tumekuwa tukienda taratibu ili kuhakikisha wale ambao hawana huduma za usalama wa raia kabisa angalau waweze kupata. Ninakuahidi Mheshimiwa Mbunge tunajua eneo unalolitaja linakaribia kupakana na mpakani na kuna matukio mengi ya uhalifu. Kwa hiyo tutahakikisha kwamba katika mipango yetu ya ukarabati jicho linaelekezwa kwenye kituo hicho ili kiweze kufanyiwa ukarabati. (Makofi)
MHE. DANIEL B. SILLO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali moja la nyongeza.

Kwa kuwa, Mheshimiwa Waziri wa Mambo ya Ndani aliahidi kumalizia ujenzi wa Kituo cha Polisi cha Galapo katika mwaka wa fedha 2022/2023. Je, ni lini Serikali itatoa fedha ili kazi hiyo iweze kukamilika?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kumjibu Mheshimiwa Sillo kwamba mpango wa ukamilishaji wa vituo vya Polisi kwa kweli inategemea upatikanaji wa fedha. Ninafahamu wakati wa bajeti yetu iliyosomwa mwaka huu, Waziri aliainisha maeneo mbalimbali ambayo yatapelekewa fedha kwa ajili ya kukamilisha ujenzi huo. Ninamuomba tu Mheshimiwa Mbunge awe na Subira, miongoni mwa maeneo ambayo yatapewa kipaumbele ni haya ambayo yana matukio mengi ya uhalifu ikiwemo eneo la Galapo ambalo limekuwa ni kituo kikubwa cha kibiashara na tutakipa pia kipaumbele. Ninakushukuru sana. (Makofi)
MHE. HUSNA J. SEKIBOKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kuniona.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kata ya Lukozi Wilaya ya Lushoto ni moja ya Kata kubwa yenye idadi kubwa ya watu na mwingiliano mkubwa wa kibiashara lakini kata hiyo haijapata kabisa huduma ya Polisi.

Je, ni lini sasa Serikali itaanzisha Kituo cha Polisi kwenye Kata hiyo?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kumjibu Mheshimiwa Husna, Mbunge wa Viti Maalum Tanga, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba kipaumbele chetu ni kuhakikisha kwamba Kata zote zinapata huduma za Polisi hususan Polisi Shirikishi. Ndiyo maana katika bajeti ya mwaka uliopita tulieleza bayana, kwamba watumishi wapya Askari, Inspectors zaidi ya 4,200 waliopatikana wamepangwa kwenye Kata zote ili kuimarisha huduma za ulinzi. Ninamuomba Mheshimiwa Mbunge kupitia Halmashauri ya Wilaya Lushoto wawahamasishe wananchi waanze angalau zile shughuli za awali za ujenzi wa kituo hicho ili Serikali ije iunge mkono nguvu zao kukamilisha ujenzi huo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wale ambao wameweka kipaumbele na wakaanza ujenzi Wizara ya Mambo ya Ndani kupitia Jeshi la Polisi inawaunga mara moja mkono, lakini wale ambao wanataka Wizara ianze moja, uwezekano huo hautakuwepo kutokana na changamoto ya kibajeti. Nimuombe tu tuvianzishe na Wizara tutaunga mkono.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru. (Makofi)
MHE. ABDUL-HAFAR IDRISSA JUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali lakini ni lini hasa Serikali itaanza kugawa vitambulisho vya Taifa kwa wale ambao wameshasajiliwa hasa waliosajiliwa zaidi ya miezi sita ama zaidi ya miaka miwili? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa
Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo: -

Ninafahamu Bungeni hapa tumesema tumejadili changamoto ya Vitambulisho vya Taifa tukaeleza, lakini tukasema changamoto ile imeshakwamuliwa baada ya ku-review ule mkataba na kuuhuisha, tukasema kinachosubiriwa ni mzalishaji kuanza kutengeneza vitambulisho hivi. Kwa hiyo, nimuombe Mheshimiwa Mbunge ni kweli wananchi ambao kwa miezi Sita iliyopita wamesajiliwa na kutambuliwa na wakapewa namba baada ya Mkandarasi kuanza kuzalisha vitambulisho hivyo watapewa kipaumbele watu hawa ambao wamekaa muda mrefu bila kupewa kadi zile za vitambulisho. Ninashukuru. (Makofi)
MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Ninataka kujua Serikali ina mkakati gani wa kuboresha vitambulisho hivi vya Taifa ili viweze kubeba taarifa muhimu zote za mhusika?(Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa
Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Esther Matiko, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli baada ya kuanza kutumika kwa Vitambulisho vya Taifa ambavyo vimeonekana vimekuwa na matumizi mengi Zaidi, imeonekana umuhimu wa kuvihuisha vitambulisho hivyo ili vibebe taarifa nyingi na kumpunguzia Mtanzania utaratibu wa kubeba vitambulisho hiki, Leseni na nini. Tunaendelea kuzungumza na wenzetu wa mamlaka nyingine ambazo zina vitambulisho hivyo ili kuweza kuhuisha Kitambulisho hiki cha Taifa kiweze kubeba taarifa hizo kumpunguzia mwananchi kuwa na makadi au vitambulisho vingi. Kwa hiyo, mazungumzo yatakapokamilika Mheshimiwa Esther jambo hilo litafanyika. Ninakushukuru sana. (Makofi)
MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa majibu ya Serikali na kupata nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa sekta ya uchukuzi ina mchango mkubwa sana katika uchumi wa nchi yetu na madereva ndio wahusika wakubwa: Je, Serikali haioni umuhimu wa kuleta mabadiliko haya ya sheria ili hili kundi maalum likapata hizo hati za dharura walau kwa muda wa miezi sita hadi mwaka mmoja? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili: Kwa kuwa kupata Passport ni mchakato unaochukua siku kadhaa; je, Serikali iko tayari kuwa na dawati maalum kwa ajili ya kuwahudumia madereva ambao wako tayari kupata Passport za kudumu wapate huduma kwa haraka? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, naomba kujibu maswali mawili nya nyongeza ya Mheshimiwa Chumi, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli upo umuhimu wa hawa madereva kuwa na passport, lakini kwa sababu mchakato wa kutoa Passport kwa maana ya kuongeza muda wa Passport za dharura kuzidi mwezi mmoja uliopo sasa unahitaji mchakato wa mabadiliko ya sheria, ni ushauri wetu; kwa sababu hizi safari wanazifanya mara kwa mara, hakuna sababu za kwa nini wasipate hizi passport. Akiipata Passport kwa miaka 10 watakuwa wanazitumia hizi passport. Kwa hiyo, huenda kukawa na nafuu kuliko kupata Passport za dharura mara kwa mara.

Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo kwa sababu ya kujua umuhimu wa madareva na safari zao, Wizara ya Mambo ya Ndani kupitia Idara ya Uhamiaji imeweka dirisha maalum la kuwahudumia madereva hawa ili pindi wafikapo wasikae foleni muda mrefu.

Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru.
MHE. FAKHARIA SHOMAR KHAMIS: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa taarifa aliyoitoa Mheshimiwa Waziri, lakini nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, kwanza ningependa kujua TANROADS pamoja na polisi wanashirikiana vipi ili kuweka usalama wa raia barabarani?

Mheshimiwa Spika, la pili, baadhi ya bodaboda, pamoja na wapakia wateja wao wanapopita barabara huwa hawavai helmet.

Je, Wizara yako inaangalia vipi sheria wakati askari wa barabarani hawawajibiki na kutenda majukumu yao wakati wanatembea watu bila helmet?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Fakharia Shomar kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, namna tunavyoshirikiana na TANROADS kudhibiti usalama barabarani ni pamoja na kuimarisha miundombinu, ambayo ni shughuli ya TANROADS kwa pande barabara kuu za mikoa na barabara kuu za kitaifa, lakini kwa upande wa TAMISEMI ni TARURA, na hawa wote ni wajumbe wa Baraza la Taifa la Usalama Barabara. Na Naibu Waziri, wa Wizara yenye dhamana na uchukuzi ni Makamu Mwenyekiti wakati ni Naibu Waziri Mambo ya Ndani ni Mwenyekiti. Kwa hiyo tuna ushirikiano mkubwa sana kuhakikisha kwamba kwa pamoja inapotokea ajali tunafanya uchunguzi kujua sababu na kama sababu ni za kimiundombinu, TANROADS wanahusishwa, kama sababu ni za kisheria basi polisi kwa maana ya Wizara ya Mambo ya Ndani inachukua hatua.

Mheshimiwa Spika, kuhusu swali la pili, bodaboda kutokuvaa helmet, hili nalo ni moja ya makosa ambayo vyombo vyetu vya usalama barabarani hususan askari wa usalama barabarani traffic police wanawaelimisha hawa vijana wanaoendesha bodaboda mara kwa mara kwa sababu kwa kweli kutovaa kofia ngumu ambazo ndizo zinaitwa helmet ni chanzo kikubwa cha vifo ambavyo vijana wetu wanaoendesha bodaboda wanapata. Kwa sababu wanapogongwa au kichwa kikigonga barabara ya lami hupasuka, au kinapogongwa na chombo kingine ama gari na kadhalika. Kwa hivyo, kuepusha madhara mkubwa haya tunawahimiza wazingatie sheria pamoja na kuvaa hii helmet.
MHE. TARIMBA G. ABBAS: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana. Kwa maelezo ya Mheshimiwa Waziri, na kwa changamoto za matumizi ya barabara kwa bodaboda kuongezeka na kuhatarisha Maisha kila siku; sasa Serikali haioni leo kutoa tamko kwamba bodaboda wote wanaopita kwenye taa nyekundu, no entries pamoja na kupakia mishikaki wakamatwe na kuchukuliwa hatua za kisheria?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali ya nyongeza ya Mheshimiwa Tarimba Abbas kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba ni kosa kubwa sana si bodaboda tu hata magari kukatisha wakati taa nyekundu zimewaka, zikawazuia kwenda wao wakapita; kwa sababu wakati taa nyekundu zimekuzuia wewe za kijana zimeruhusu gari nyingine kupita. Kwa hiyo, unapojaribu kukatisha kwa kweli unajiweka kwenye hatari kubwa sana.

Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba polisi wetu wa usalama barabarni huchukua hatua, lakini mara nyingine imekuwa changamoto kwa upande wa viongozi wa kisiasa kuwatetea vijana hawa. Kwa hiyo, niombe tushirikiane sote. Elimu tunatoa, sheria huchukuliwa, lakini wote tuwe na utashi wa kisiasa, kwa maana ya mabaraza ya madiwani, ngazi zetu sisi Wabunge, Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya ili wote tuzungumze lugha moja kuhusu usalama wa barabarani, hususan hawa vijana wa boda boda nashukuru sana.
MHE. GRACE V. TENDEGA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi kuweza kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Wilaya ya Mkalama ina gari mmoja ambalo pia ni bovu.

Je, Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha kwamba, wanapomaliza ujenzi wa kituo hicho wanawapa na nyenzo kama magari na pikipiki maalum?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, katika Jimbo la Kalenga pia kuna kituo cha Polisi cha Kata ya Ifunda lakini hawana nyumba Askari hao na pia hawana magari, je, ni mkakati gani wa Serikali unao ili kuhakikisha kwamba kituo hiko kinapata nyumba za watumishi pamoja na magari? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Tendega, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, moja, kuhusu Kituo cha Mkalama baada ya kukamilika kupewa nyenzo za kutendea kazi ikiwemo magari, hilo ni wazi, gari lililopo kama ni bovu, kituo kitakapokamilika tutawapa gari ili waweze kutimiza majukumu yao vizuri. Kwa bahati nzuri tumeanza kupokea magari hayo na yameanza kugawiwa kule ambako kuna mahitaji makubwa sana.

Mheshimiwa Spika, kuhusu Kalenga, hii Kata ya Ifunda, kuwa na kituo ambacho hakina nyumba wala magari; tutawasiliana na uongozi wa Polisi wa Mkoa, nadhani ni Iringa hii, ili kuona kama wanalo eneo la kutosha basi waingize kwenye mpango wa ujenzi waweze kufikiriwa kujengewa. Nashukuru. (Makofi)
MHE. FRANCIS I. MTINGA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi. Wilaya ya Mkalama pamoja na kuwa Kituo hicho kimekuwa gofu muda mrefu lakini pia Askari ni wachache sana, katika Kata zote 17 ambazo zinamtawanyiko mkubwa, sehemu kubwa tunatumia mgambo. Serikali inatuambia nini kuhusu kutupatia Askari wapya katika mgao unaokuja. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Francis Mtinga, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba Wilaya nyingi hasa ambazo hazikuwa na Vituo vya Polisi, wamekuwa na Askari kulingana na uwezo wa vituo vilivyopo kuwabeba. Tunashukuru baada ya kupata ajira ya zaidi ya Askari 4,200 waliotoka kwenye mafunzo mwanzoni mwa mwaka huu, wameweza kugawiwa kwenye vituo hivi, vikiwemo mpaka ngazi za Kata. Naamini Mheshimiwa Francis anafahamu kwamba sasa hivi tunao Askari Kata ngazi ya Cheo cha Mkaguzi Msaidizi wa Polisi kwa ajili ya kusimamia usalama katika ngazi hizo. Kwa hiyo, naamini atakuwa amepata Askari hao kwenye Jimbo lake la Mkalama. Nashukuru.
MHE. DANIEL B. SILLO: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali moja la nyongeza.

Je, ni lini Serikali itamalizia Kituo cha Polisi cha Galapo ambacho iliahidi kwamba itatekeleza katika mwaka huu wa fedha 2022/2023?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Daniel Sillo, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwa kweli tumeshazungumza juu ya jambo hili na Mheshimiwa Sillo, nimeahidi baada ya Bunge hili kutembelea eneo lile la Galapo kwa sababu ni eneo ambalo ni kubwa sana kibiashara linahitaji Kituo cha Polisi. Tumeingiza kwenye mpango wa kukamilisha ujenzi wa kituo hicho ili wananchi wa eneo hilo waweze kupata huduma za usalama wa raia na mali zao.
MHE. ALLY M. KASSINGE: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipatia nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Wananchi wa Kata ya Nanjilinji katika Jimbo la Kilwa Kusini, wamekamilisha ujenzi wa Kituo cha Polisi wakishirikiana nami Mbunge wao. Je, Serikali iko tayari kutoa maelekezo kupitia Bunge hili kwa Uongozi wa Polisi Mkoa wa Lindi ili wakakague kituo hicho na hatimae kupeleka Askari Polisi pale Nanjilinji?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Kassinge, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwanza niwapongeze kwa kukamilisha ujenzi wa kituo hicho, hivyo ni wajibu wetu Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi hususan Jeshi la Polisi, kupeleka Askari. Kupitia Bunge lako naomba kuelekeza Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Lindi wafanye ukaguzi kama kinakidhi wa wapangie Askari ili waweze kutoa huduma za usalama wa raia kwenye eneo hili la Nanjilinji. Nashukuru sana.
MHE. SAADA MANSOUR HUSSEIN: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Je, ni hatua gani zilizochukuliwa na Serikali hadi sasa kwa wote waliohusika?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YANCHI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Saada Mansour Hussein kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, watuhumiwa wa mauaji haya yaliyotokea Zanzibar, wote walikamatwa na kesi zao zinaendelea mahakamani. Nakushukuru sana.
MHE. REHEMA J. MIGILLA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Tarafa ya Ulyankulu yenye kata saba haina kabisa Kituo cha Polisi, hali ambayo inapelekea vitendo vya kihalifu kuwa ni vingi: Je, ni lini Serikali itatujengea Kituo cha Polisi kwenye hii Tarafa ya Ulyankulu?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Rehema Migilla kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba Tarafa ya Ulyankulu haina Kituo cha Polisi chenye hadhi ya tarafa, lakini ni suala la kuweka katika mipango yetu ili kiweze kufikiriwa kujengewa Kituo cha Polisi. Kwa hiyo, bajeti itakaporuhusu tutaliingiza hili na kituo kitajengwa kwenye hiyo Tarafa ya Ulyankulu.

Mheshimiwa Spika, nashukuru sana.
MHE. USSI SALUM PONDEZA: Mheshimiwa Spika, nami nakushukuru kwa kunipa nafasi hii. Nilikuwa nataka tu nami nipate majibu ya Mheshimiwa Waziri ya swali langu dogo la nyongeza. Nimekuwa nikiahidiwa mara nyingi sana, zaidi ya mara sita, saba juu ya vituo vyangu katika Jimbo langu la Chumbuni, lakini sijapata mwendelezo wala kujengewa vituo hivi na hali ya kiusalama kila siku zikivyoenda imekuwa siyo nzuri na wananchi wanafuata huduma mbali kiasi ambacho kama kuna mhujumu ametokea, basi watu kupata usaidizi inachukua muda mrefu sana.

Mheshimiwa Spika, nilikuwa naomba majibu ambayo yataeleza ni lini tutapata huduma hii katika Jimbo letu la Chumbuni?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Ussi Pondeza kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Ussi anafahamu nilitembelea Zanzibar na kwenye jimbo lake nilifika nikaona hali ya vituo vidogo vya polisi vilivyopo na kwa kweli kwenye eneo lake anastahili kujengewa Kituo cha Polisi.

Mheshimiwa Spika, naomba tu upande wa Kamisheni ya Polisi ya Zanzibar iingize mahitaji ya Kituo cha Polisi eneo la Chumbuni ili iweze kupangiwa bajeti kwa ajili ya kuanza kujengwa kwenye bajeti itakayofuata.

Mheshimiwa Spika, ahsante sana.
MHE. JUMA USONGE HAMAD: Mheshimiwa Spika, nishukuru sana Serikali kwa commitment ya kutaka kukijenga Kituo hicho cha Lungalunga. Sasa naomba niulize swali langu la nyongeza.

Je, ni lini Mheshimiwa Waziri atapanga ziara ya kuja kutembelea kwenye eneo hilo ili wananchi wale wawe na matumaini makubwa kwamba kweli Serikali ina commitment ya kutaka kujenga kituo hiki cha polisi?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Juma Usonge Hamad, Mbunge wa Chaani, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kabla ujenzi wa kituo hicho haujafanyika, nampa ahadi Mheshimiwa Mbunge kwamba tutakwenda kutembelea eneo hilo tukiwa pamoja naye ili kuweza kujiridhisha kwamba kazi itafanyika. Nashukuru.
MHE. ASYA SHARIF OMAR: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali moja la nyongeza na kwanza naomba nimshukuru Naibu Waziri kwa majibu yake mazuri. Lakini nataka kuuliza, je, kuna mkakati gani mahususi la kuongeza suala hili la usafiri katika Makao Makuu ya Polisi Mkoa wa Kaskazini Pemba, kwa sababu bado changamoto ni kubwa na hasa ukizingatia na vituo vidogo ambavyo vina mahitaji makubwa ya usafiri ikiwemo Kituo cha Mchangamdogo, lakini pia Kituo cha Mapana Kifuani ambacho nimekuzungumzia juzi? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali moja la nyongeza la Mheshimiwa Asya Sharif Omar kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kama nilivyosema kwenye jibu la msingi, hivi sasa wamegaiwa magari matatu, tutaendelea kuwapatia magari ili wamudu kutekeleza majukumu ya ulinzi, usalama wa raia mali zao kadri tutakavyopata bajeti na kama anavyofahamu Mheshimiwa mwaka huu tumepitishiwa bajeti ya shilingi bilioni 15, yakanunuliwa magari, miongoni mwa maeneo yatakayopata magari ni pamoja na mikoa ya Pemba. Nashukuru.
MHE. KHALIFA MOHAMED ISSA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana, naomba nimuulize swali la nyongeza Mheshimiwa Waziri.

Mheshimiwa Spika, Zanzibar kuna polisi jamii, na polisi jamii hawa wanapelekwa kila Shehia katika Shehia za Zanzibar na shida yao kubwa ni mafuta.

Je, Serikali inatuambiaje kuwapatia walau mafuta, japo hawakupatiwa pikipiki lakini au maufta yakuwafikisha katika vituo vyao vya kazi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Khalifa Mohamed Issa, Mbunge kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli sio Zanzibar tu maeneo mbalimbali nchini Tanzania tunao utaratibu wa kuwa na polisi jamii kwa ajili ya kusaidia ulinzi shirikishi pale ambapo polisi wetu wanakuwa mbali na kwa sababu kama inavyoitwa polisi jamii uendeshaji wake kwa muda imekuwa ukichangiwa na wan jamii wenyewe. Sasa suala hili la kuzingatia kwenye upande wa mafuta ni suala kibajeti, tutalitafakari pale hali ya fedha na bajeti itakavyoruhusu tutaanza kuona uwezekano wa kuwafikiria mafuta na vyombo vya usafiri kama alivyotaja pikipiki. Nashukuru.
MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali dogo la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa Wilaya ya Nyang’hwale ina vijiji 62 kata 15 na OCD wetu pale Wilayani ana gari moja na si zuri sana; je, Wizara ina mpango gani wa kutuongezea gari nyingine polisi Nyang’hwale?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Amar, Mbunge wa Nyang’hwale kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kama alivyosema angalau yeye analo gari haliko vizuri sana lakini at least linatumika. Ushauri wetu gari hilo liendelee kukarabatiwa, lakini kama nilivyokwishasema wakati namjibu Mheshimiwa Asya, tunao utaratibu wa kununua magari na kuyapeleka kule ambako yanahitaji sana.

Kwa hiyo, Nyang’hwale, kama sehemu ya Mkoa wa Geita tutauangalia kulingana na upatikanaji wa hayo magari ili waweze kupata gari linawezesha OCD wetu kufanya kazi yake vizuri. Nashukuru.
MHE. BONIPHACE N. BUTONDO: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, Wilaya ya Kishapu ina jumla ya kata 29 na ina vijiji 128 na Wilaya hii sasa haina gari hata moja, magari yote ni mabovu na kwa sasa hivi tumekuwa tukitumia gari moja ambayo tumeazimwa na Mgodi wa Williamson Diamond Limited.

Sasa Serikali inafanya jitihada gani za haraka kuhakikisha kwamba inapeleka angalau gari moja ya dharura kwa ajili ya kuokoa wananchi kupata huduma za msingi?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Butondo, Mbunge wa Kishapu kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba Wilaya ya Kishapu inayochangamoto ya magari kama alivyosema Mheshimiwa Mbunge, gari walilonalo ni chakavu, linahitaji matengenezo ya mara kwa mara. Nimpe matumaini Mheshimiwa Mbunge pale ambapo tutapata magari yanayotokana na bajeti hii tunayoitekeleza kipaumbele kitawekwa kule ambako hawana magari kabisa.

Kwa hiyo, kama Kishapu watakuwa hawana gari tutaelekeza IGP aipe Kishapu kipaumbele katika ugawaji wa magari hayo. (Makofi)
MHE. NDAISABA G. RUHORO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. Kwa kuwa maeneo yote aliyoyataja hayana vituo vya Polisi: Je, Mheshimiwa Naibu Waziri yupo tayari kutupatia gari liendelee kuimarisha ulinzi eneo hilo huku tukiwa tunasubiri kujengwa kwa vituo hivyo? Hilo ni namba moja.

Mheshimiwa Spika, swali la pili; kwa kuwa eneo la Ngara liko mpakani na changamoto ya ulinzi na usalama ni kubwa, Mheshimiwa Naibu Waziri yuko tayari kuambatana nami tukaone changamoto hizo sambamba na kutatua mgogoro wa Rusumo Magereza na wananchi wa kijiji cha Magereza? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Ruhoro kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kuhusu kusaidia gari kwa ajili ya kuimarisha usalama na ulinzi wa raia na mali zao, kama ilivyojibiwa siku tatu zilizopita na Mheshimiwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi hapa, Wizara kweli itapata magari 78 mwishoni mwa mwezi huu ambapo tathmini itafanyika kuona Halmashauri yenye changamoto kubwa iweze kuzingatiwa ikiwemo Halmashauri ya Wilaya ya Ngara na hasa ukizingatia iko mpakani.

Mheshimiwa Spika, kuhusu kuambatana naye, niko tayari kuongozana naye wakati wowote nafasi itakapopatikana hususan baada ya Bunge hili ili kuweza kuona changamoto zake na kuzifanyia kazi. (Makofi)
MHE. STANSLAUS H. NYONGO: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Wilaya ya Maswa hasa katika Mji wa Maswa hatujawahi kujengewa Kituo cha Polisi toka tumepata uhuru mwaka 1961: -

Je, ni lini Serikali itajenga kituo chake katika Wilaya ya Maswa na nyumba za maaskari?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Stanslaus Nyongo kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, tunatambua kwamba kweli ziko wilaya hasa Wilaya kongwe kama Maswa hazina vituo vya polisi kwa maana ya ngazi ya OCD. Wizara ina mpango wa kuzijengea vituo vya polisi vya ngazi ya wilaya, wilaya zote ambazo hazina vituo hivyo kwa kutegemea upatikanaji wa fedha. Nami nafahamu wilaya hii kwa sababu pia ina mapori kule na hifadhi, wanahitaji kituo hiki, hivyo tutaipa kipaumbele katika mpango huo. (Makofi)
MHE. FLORENT L. KYOMBO: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa nafasi. Wananchi wa Kata Kakunyu, Wilaya ya Misenyi ambapo ni mpakani mwa nchi yetu na Uganda, wamejenga kituo cha polisi mpaka kuezeka.

Je, ni lini sasa Serikali itawaunga mkono kumalizia kituo hicho wapate huduma za kipolisi? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Kyombo kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kama alivyosema, wananchi wamejenga kituo, wanahitaji msaada wa kumalizia. Hatua watakayoanza ni kutathmini kiwango gani cha fedha kinatakiwa ili kukamilisha kituo hicho ili kuona kama tunaweza tukatumia sehemu ya fedha ya tuzo na tozo kwa ajili ya ku- support vituo hivi ambavyo viko mpakani. (Makofi)
MHE. TARIMBA G. ABBAS: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi. Kwa kuwa Jimbo la Kinondoni lina watu wengi sana na mahitaji ya usalama wa watu hao pamoja na mali zao ni mkubwa, hasa ikitiliwa maanani nyumba ziko karibu karibu sana: -

Je, Serikali haioni kwamba sasa ni wakati muafaka kuruhusu vituo vidogo vya Polisi vinavyofungwa saa 12 vifanye kazi masaa 24 ili kuweza kusaidia usalama katika maeneo hayo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Abbas kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, tunatambua wingi wa watu kwa wananchi wa Kinondoni na umuhimu wa kuwa na vituo vidogo vya Polisi katika maeneo mbalimbali. Tutatathmini kwa sababu ili Kituo Kidogo cha Polisi kiweze kufanyakazi saa 24, vinahitaji rasilimaliwatu; na muundo wa kituo kile kuweza kuhifadhi silaha na mambo kama hayo. Kwa hiyo, tutatathmini kuona mahitaji, tutashauriana na Mheshimiwa Abbas kuona namna gani tuvifanye viweze kutoa huduma saa 24. (Makofi)
MHE. ENG. MWANAISHA N. ULENGE: Mheshimiwa
Spika, ahsante sana kwa nafasi ya swali la nyongeza. Kwa kuwa Jiji la Tanga limetanuka na lina makazi mapya mengi, sasa ni lini Serikali itajenga vituo vya Polisi katika maeneo ya Kange Uzunguni, Kange Mbugani, Mwahako na Mwakidila? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mwanaisha Ulenge, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, tunatambua ukubwa wa Jiji la Tanga na kwa kweli limepanuka sana na umuhimu wa kuimarisha ulinzi na usalama katika maeneo hayo ni mkubwa, kwa hiyo tutashauriana na uongozi wa Polisi wa Mkoa ili kuwajumuisha wadau akiwemo Mheshimiwa Ulenge na wengine wadau wema kuanza kujenga Vituo vya Polisi kwenye maeneo haya yaliyopanuka ili kuimarisha ulinzi kwenye maeneo hayo. (Makofi)
MHE. ASSA N. MAKANIKA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Tuna Kituo cha Polisi katika Wilaya yetu ya Kigoma DC, Kituo cha Polisi cha Mkuti, ukiangalia matukio mengi sana ya kihalifu yanafanyika katika eneo lile.

Je, ni lini Serikali itaweza kumalizia Kituo kile cha Polisi katika hali iliyopo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Makanika, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, nipo tayari kufuatana na Mheshimiwa Makanika baada ya Bunge hili ili kuona mahitaji ya kituo hicho kwa maana ya kufanya tathmini, kuona fedha zinazohitajika ziweze kutengwa katika bajeti zetu zinazofuata. (Makofi)
MHE. MICHAEL C. MWAKAMO: Mheshimiwa Spika, Mji wa Mlandizi unakua kwa kasi na pale Mlandizi kuna majengo kwenye Kituo cha Polisi yaliyojengwa kwa nguvu za wananchi. Je, ni lini Serikali itaweka nguvu za Serikali kusaidia nguvu za wananchi kumaliza nyumba zile? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Michael, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, tutaomba uongozi wa Polisi wa Mkoa ilipo Wilaya ya Mheshimiwa ili iweze kufanya tathmini kujua kiwango cha fedha zinazohitajika kwa ajili kukamilisha ili tuweze kuingiza kwenye mpango na hatimaye kiweze kumaliziwa. (Makofi)
MHE. SALOME W. MAKAMBA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Katika Jimbo la Shinyanga mjini Kituo Kikuu cha Polisi kilikuwa na hali mbaya jambo ambalo uongozi wa Polisi waliamua kujenga kwa fedha zao za ndani, lakini kituo hicho kipya kilichojengwa bado hakijakamilika. Je, Serikali ina mpango gani wa kuongeza fedha katika kituo hicho ili kiweze kukamilika? Nashukuru. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Salome Makamba, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kuhusu uchakavu wa Kituo cha Polisi Shinyanga Mjini kinachohitaji ukarabati, tutafanya tathmini ili kuona kiwango cha fedha zinazohitajika kuwezesha ukarabati huo kufanyika, tuingize kwenye mpango wa bajeti katika miaka inayofuata.
MHE. DKT. JOHN D. PALLANGYO: Mheshimiwa Spika, nakushuru sana kwa kunipa nafasi na mimi niulize swali la nyongeza. Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga Kituo cha Polisi katika Kata ya King’ori?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Pallangyo, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, tupo tayari kushirikiana na Mbunge na wadau wengine wa Kata ya King’ori kuona kiwango cha ujenzi kinachotakiwa kumaliziwa ili tuweze kutengea fedha kituo hicho kiweze kukamilishwa. (Makofi)
MHE. MOHAMED SAID ISSA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana nina maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza, kwanza, niishukuru Wizara kwa kuweza kutenga fedha kwa ajili ya matengenezo ya Kituo cha Konde, lakini swali langu la nyongeza ni kwamba katika Kituo cha Polisi cha Konde pia kuna nyumba za askari ambazo wanatumikia katika kituo kile. Je, Serikali ina mpango gani wa kuweza kuzikarabati?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, pia katika maeneo ya Konde mbele kuna Kituo cha Polisi kinaitwa Matangatuani ambacho ni kituo muhimu sana kinatumika kwa ajili ya ulinzi wa mali, lakini pia na uhalifu kwa sababu Jimbo la Konde ni la mpakani, Je Serikali ina mpango gani wa kuweza kukikarabati Kituo hicho cha Matangatuani?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Mohamed Saidi Issa, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kuhusu kukarabati nyumba za askari zilizo kwenye kituo hicho, hili ni jambo muafaka kabisa tunapokuwa tunafanya tathmini hizi gharama zinazohitajika kwa ajili ya ukarabati wa kituo tutazingatia nyumba hizo ili ziweze kuingizwa katika mpango wa ukarabati.

Mheshimiwa Spika, kuhusu swali la pili la kuboresha kituo cha polisi kilicho mpakani, Matangatuani, tutakifanyika tathmini kituo hicho ili kuona kiwango cha fedha zinazohitajika kwa ajili ya ukarabati wake, tuweze kukiingiza katika mpango wetu wa ukarabati. Nashukuru. (Makofi)
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Wilaya ya Liwale haina Kituo cha Polisi na kwa kuliona tatizo hilo nimetoa fedha shilingi 10,000,000 kutoka kwenye Mfuko wa Jimbo kwa ajili ya kuanza ujenzi. Je, Serikali inatusaidiaje ili kuimarisha kituo cha Polisi cha Wilaya ya Liwale? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Kuchauka, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwanza nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Mbunge Kuchauka kwa kuchangia shilingi 10,000,000 kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Polisi Liwale, naomba nitoe ahadi kama nilivyosema katika swali lililopita kwamba maeneo yote ya Wilaya ambayo hayana Vituo vya Polisi ni mpango wa Serikali kuona kwamba Wilaya hizo zinapata Vituo vya Polisi, hivyo tutafanya tathmini kuona kiwango cha fedha kinachohitajika ili kushirikiana nae tuweze kukamilisha Kituo cha Polisi Liwale. (Makofi)
MHE. MUSSA R. SIMA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. Singida Mjini ni Mji ambao unakuwa kwa kasi sana na maeneo mengi hayana vituo vya Polisi hali inayopelekea askari wetu kusafiri kwa umbali mrefu. Je, Serikali haioni haja sasa umefika wakati wa kuwaongezea walau fedha ya mafuta ili waweze kufanya kazi yao vizuri ya usalama wa raia?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mussa Sima, Mbunge wa Singida Mjini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, tunatambua kwamba Makao Makuu ya Mikoa yetu mingi kwa kweli yanapanuka sana na kuhitaji huduma za kipolisi kwa maana ya kuwa na magari, kuelekea kwenye maeneo hayo kuwahudumia wananchi. Niseme kama itakavyokuja kusomwa bajeti yetu hapa mwaka huu Rais wa Awamu ya Sita, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, ameongeza fedha kwenye majeshi yetu ikiwemo Jeshi la Polisi ili kuimarisha shughuli za kiulinzi ikiwemo doria na mambo kama hayo. Kwa hiyo Wilaya ya Singida na Manispaa ya Singida ni moja ya Wilaya zitakazonufaika na ongezeko hilo la Bajeti. (Makofi)
MHE. CHARLES M. KAJEGE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Nina swali moja; kwa vile Vituo vya Polisi vya Kibara, Bulamba na Kisorya vinatumia nyumba za wenyeji kufanyia kazi zake. Je, ni lini Serikali itajenga vituo hivyo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Kajege, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, naomba kwanza nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Kajege kwa juhudi zake za kuimarisha huduma za ulinzi wa wananchi ikiwemo kuhamasisha wananchi kushiriki kujenga vitu vya Polisi vya Bulamba na Kisorya. Napenda kumuahidi Mheshimiwa Mbunge kwamba tutafanya tathmini ya kiwango cha fedha zinazohitajika kukamilisha vituo hivyo ili viweze kuingizwa katika mpango na bajeti itakayosomwa siku zijazo. Nashukuru.
MHE. HAWA S. MWAIFUNGA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru Je, Serikali ina mpango gani wa kufanya ukarabati mkubwa katika Kituo cha Central kilichopo Jimbo la Tabora Mjini? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Hawa Mwaifunga, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Vituo Vikuu vya Polisi vya Mikoa kama anavyosema Central Tabora vinahitaji kufanyiwa tathmini kwa ajili ya kuona mahitaji ya fedha yanayohitaji kwa ajili ya kuwezesha ukarabati huo kufanyika. Naomba nimuahidi Mheshimiwa Mwaifunga na bahati nzuri Tabora ni eneo nililoanzia kazi, tutashirikiana na Mheshimiwa Mbunge na Mbunge wa Jimbo ili kufanya tathmini ya kiwango cha fedha zinazohitajika ili ukarabati huo uweze kufanywa. (Makofi)
MHE. TWAHA A. MPEMBENWE: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ili kuuliza swali la nyongeza. Wilaya ya Kibiti inafahamika maarufu sana kwa jina la Kanda Maalum, sasa ni upi mpango wa Serikali kujenga Kituo cha Polisi ambacho kina hadhi ya Kanda Maalum katika Wilaya ya Kibiti? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Twaha, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, tunatambua ulianzishwa Mkoa wa kipolisi Kanda Maalum ya Kibiti, ukaanza kwa utaratibu wa dharura kwa kutumia ofisi ya OCD zilizokuwepo miongoni mwa Mikoa mipya ya kipolisi ambayo itajengewa majengo yake ni pamoja na Mkoa huu wa Kanda Maalum ya Kibiti. Kwa hivyo Mheshimwia Mbunge asubiri kadri tutakapokuwa tunapata fedha, Kibiti itapewa msisitizo maalum. (Makofi)
MHE. MOHAMED ABDULRAHMAN MWINYI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali naomba kuuliza swali moja la nyongeza. Kwa kuwa kuna vitendo vya uhalifu vinavyojitokeza katika Jimbo langu la Chambani, kama vile uwingizaji na utumiaji wa madawa, wizi wa mifugo na mazao.

Je, nili Serikali itaanza doria kwa kupambana na wahalifu hao?
NAIBU WAZIRI MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Abdulrahman Mwinyi Mohamed, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Abdulrhman Mwinyi kwa kujali utulivu usalama na amani kwenye Jimbo Lake la Chambani. Hata hivyo, kwa kuwa ujenzi wa vituo hivi utachukua muda nitoe maelekezo kwa RPC Mkoa wa Kusini Pemba kuimarisha doria kwenye maeneo korofi ambayo ni pamoja na Dodo, Chambani Pamoja na eneo la Chonga ili wenye vitendo vya wizi wa mifugo na mazao waweze kukoma. Ahsante.
MHE. ESTHER L. MIDIMU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, ujenzi wa kituo cha Polisi Wilaya ya Itilima tayari umeshaanza na jengo limesimama, na Mheshimiwa Waziri kipindi kile alikuwa Naibu Waziri wa Fedha alikuja kutembelea, Waziri wa Mambo ya Ndani alikuja kutembelea.

Je, ni lini Serikali itatoa pesa za kumalizia ujenzi huo? Na Mheshimiwa Waziri nikuombe uje utembelee katika Wilaya yetu ya Itilima. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Esther Midimu kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, natambua juhudi za wananchi wa Itilima pamoja na Mbunge wao Mheshimiwa Njalu Silanga katika kufuatilia ujenzi wa kituo hiki. Na kuhusu ombi lake, kwamba nitembelee Itilima, niko tayari kutembelea Itilima ili kuweka msukumo wa kupata fedha kutoka tunzo na tozo ili ukamilishaji wa kituo hiki uweze kufanyika.
MHE. SIMAI HASSAN SADIKI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kuweza kunipa nafasi hii ya kuuliza swali la moja la nyongeza.

Ni lini Serikali itajenga uzio kuzunguka eneo la Kituo cha Polisi lilolokuwepo Nungwi ili kuepusha uvamizi eneo hilo?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Simai kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, tutatathimini mahitaji ya gharama za ujenzi wa uzio huo ili kuweza kuanza mkakati wa ujenzi kupitia juhudi za mfuko wa tunzo na tozo kama ambavyo tumefanya kwenye maeneo mengine.
MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Serikali imekuwa ikiahidi mara nyingi kujenga Kituo cha Polisi Itigi ambacho wanatumia majengo chakavu ya reli, angalau kituo cha daraja C. Sasa, je, ni lini?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Massare Mbunge wa Itigi kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu uchakavu wa kituo kilichopo, tutafanya tathimini kuona kiwango cha uchakavu; na kama eneo hili halitoshi tuko tayari kushirikiana na Mheshimiwa Mbunge ili eneo lipatikane la kutosha kwa ajili ya kujenga kituo chenye hadhi ya Wilaya ya Itigi.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninashukuru.
MHE. VENANT D. PROTAS: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Wananchi wa Kata ya Tula na Goweko wameanza ujenzi wa vituo vya afya. Ni lini Serikali itapeleka fedha kuungana na wananchi kumalizia vituo hivyo?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge wa Igalula kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, tutafanya tathimini ya kuangalia kiwango cha ujenzi uliofikiwa ili kuona kiasi cha fedha ambazo zinahitajika kumalizia ujenzi wa kituo hicho, na gharama zitakapojulikana zitajumuishwa kwenye mapango wetu wa umaliziaji wa vituo vya polisi vikiwemo hivyo vya Goweko na Igalula.
MHE. NEEMA G. MWANDABILA: Mheshimiwa Naibu Spika, Neema Mwandabila.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Mji wa Tunduma upo mpakani na kituo kilichopo pale hakina hadhi ya kuweza kuhudumia katika eneo lile; wahalifu ni wengi kiasi kwamba kinalemewa.

Ni lini Serikali itaona umuhimu wa kujenga kituo cha chenye hadhi ya Wilaya katika eneo la Tunduma?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Neema Mwandabila kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyojibu hivi majuzi kwamba Wilaya zote ambazo hazina vituo vya polisi ni mpango wa wizara kuanza ujenzi kwenye maeneo hayo. Kwa hiyo, eneo analolitaja hili ni moja ya maeneo ambayo yatazingatiwa katika ujenzi wa vituo vya polisi.
MHE. NASHON W. BIDYANGUZE: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niulize swali la nyongeza.

Ni lini Serikali itajenga kituo cha polisi cha Wilaya Uvinza?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, nafahamu Wilaya ya Uvinza ni miongoni mwa wilaya mpya ambazo hazina vituo vya polisi, na kwa hiyo katika mkakati wetu wa kuhakikisha mikoa na wilaya zote ambazo hazina vituo vinajengewa vituo hivyo Uvinza ni eneo mojawapo litakalo zingatiwa katika ujenzi wa vituo vipya vya polisi.
MHE. HAWA S. MWAIFUNGA: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu ya Naibu Waziri, naomba nimuulize maswali mawili madogo ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mkoa wa Tabora ni moja kati ya mikoa mikubwa na yenye watu wengi lakini kumekuwa na changamoto kubwa sana ya usafiri kwa askari wetu katika vituo mbalimbali. Serikali inampango gani wa kupeleka magari ili kuweza kurahisisha kazi za askari wetu wanapokutana na matukio?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili. Jimbo la Tabora mjini lina kituo cha Central Police, lakini kumekuwa na changamoto kubwa sana, na nimekuwa nikiliuliza sana swali hili la usafiri, hata gari lililopo ni tia maji tia maji. Serikali ina mpango gani basi angalau katika bajeti hii kupeleka magari machache katika Mkoa wa Tabora, hususani Jimbo la Tabora Mjini ili kurahisisha kazi za askari wetu?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali ya nyongeza ya Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, tunafahamu kwamba kweli Mkoa wa Tabora ni mkubwa na uhitaji wake wa magari hauhitaji kupingwa, iko wazi. Kwa kulitambua hilo, Mkoa wa Tabora umepata mgao wa magari. Katika magari 78 tuliyoyapokea mwezi uliopita Tabora wamepata magari mawili. Moja limepelekwa kwa RPC Tabora na jingine limekwenda FFU Tabora. Kuhusu manispaa ya Tabora Mjini niahidi, kadri tutakapokuwa tunapata fedha, kama ambavyo mwaka huu tumetengewa Shilingi bilioni 15. Fedha zitakazopatikana tutanunua magari na Tabora kwa uhitaji wake pia watafikiriwa kupewa gari. Nashukuru.
MHE. EMMANUEL P. CHEREHANI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwenye Bunge la Bajeti lililopita Mheshimiwa Naibu Waziri aliniahidi kupeleka fedha kwenye ujenzi wa Kituo cha Polisi kilichopo katika Halmashauri ya Ushetu; na wananchi wale walishajichanga pamoja na wadau mbalimbali wakajenga msingi. Sasa nataka nijue, ni lini Serikali inapeleka fedha hizi ili kuanza ujenzi wa Kituo cha Polisi katika Halmashauri ya Ushetu?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Cherehani kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, tunafahamu maeneo ya Wilaya mpya kama ilivyo ya Ushetu wanahitaji kuwa na vituo vya polisi ili kusogeza huduma za usalama wa raia karibu zaidi na wananchi. Ni ahadi yetu kwamba kwa vyovyote vile kwa sababu wananchi wameshajitokeza, wamechangia nguvu zao na jitihada wakafikia mpaka kiwango cha msingi, nimtie moyo Mheshimiwa Mbunge, kwamba pale ambapo tutapata fedha kwa ajili ya ujenzi, Wilaya ya Ushetu itazingatiwa pia. Nashukuru.
MHE. CHARLES J. MWIJAGE: Mheshimiwa Naibu Spika, nina maswali mawili ya nyongeza: -

Mwaka jana Oktoba, Bibi yangu Ndugu Juliana Leo Gaesha, aliitwa kituo cha Polisi na kupelekwa Mahakama Kamachumu, Hakimu alimueleza mlalamikaji kwamba Bibi huyu apandishwe pikipiki na mlalamikaji akalipa fedha, Bibi yangu na watu wawili wakafungwa mshikaki kwenye pikipiki wakaenda Muleba, kufungwa Muleba magereza. Sasa kwa majibu yako Waziri ni lini mamlaka yako Wizara ya Mambo ya Ndani, Wizara ya Sheria na TAMISEMI, mtatengeneza Tume ya Kitaifa, yaani ngazi ya Taifa muende mpeleleze tukio hili la Juliana Gaesha? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa tukio hili lililotokea Muleba, kwa kweli hatuhitajiki kuunda Tume, badala yake wale ambao wako kule wanaosimamia utekelezaji wa sheria wazingatie sheria, labda kama jambo lingekuwa limepitiliza sana hiyo ipo haja ya kufanya hivyo. Lakini kwa kiwango hiki ninaamini wasaidizi wetu walioko ngazi hizo watazingatia na kuanza kutekeleza. Kama linaigusa Mahakama, wenzangu wa Mahakama wapo wamesikia litatekelezwa Mheshimiwa. Ahsante sana.
MHE. EDWARD O. KISAU: Mheshimiwa Naibu Spika, nina swali dogo tu. Kijiji cha Magungu wamejenga jengo la Kituo cha Polisi tangu mwaka 2016, nini kauli ya Serikali katika kuwasadia kumaliza lile jengo?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mhesimiwa Olelekaita kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza niwapongeze wananchi wa Kijiji hicho cha Magungu, kwa kufanya jitihada na juhudi kujenga Kituo cha Polisi. Tutakachofanya ni kufuatilia kiwango kilichofikia hilo jingo, linahitaji kiasi gani ili liweze kukamilishwa na tuone uwezekano wa kuingiza kwenye mpango wa ujenzi kutegemea upatikanaji wa fedha. Kama tulivyoongea juzi wakati wa ziara yangu nitafikia kwenye kituo hicho ili kuweza kuona hatua iliyofikia.(Makofi)
MHE. DKT. CHARLES S. KIMEI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.

Je, ni lini Serikali itatoa fedha kuwasaidia wananchi wa Kata ya Mwika Kaskazini kumalizia kituo muhimu sana kwenye Soko Kuu la Mwika?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Dkt. Kimei, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kama wananchi wa Kata hiyo wameshajenga kituo wanahitaji kupata msaada wa Serikali kukamilisha tutahitaji tu uongozi wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro waweze kufanya tathmini kuona jengo limefika kiwango gani ili waweze kuliingiza kwenye mpango wa ujenzi kama tunavyofanya kwenye maeneo mengine.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Dkt. Kimei, tukupongeze kwa kuhamasisha wananchi na sisi tutakuunga mkono baada ya kupata uthamini huo.
MHE. ASYA SHARIF OMAR: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali lakini bado naona iko haja ya Mheshimiwa Naibu Waziri kulipa kipaumbele suala la kwenda kukiona kituo kile kwa sababu Askari wale wanafanya kazi katika mazingira magumu.

Je, Naibu Waziri yuko tayari kuongozana na mimi kwenda katika eneo hilo la Kituo cha Polisi cha Matangatuani ili kuweza kutoa msukumo zaidi katika bajeti hiyo 2023/2024 kufanikisha ujenzi huo wa kituo kipya lakini pia na nyumba za makazi ya Askari Polisi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ambayo kwa kweli yanakaribia kufanana ya Mheshimiwa Asya kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, natambua kwamba eneo hilo halina Kituo cha Polisi lakini jambo kutia moyo wananchi hawa tayari wametenga eneo la kutosha kujenga kituo na nyumba za watumishi upande wa Polisi.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaahidi kwamba niko tayari kukitembelea ili kuona kiasi gani kinahitajika na pia kuweka msukumo ili jengo hilo likamilishwe kwa haraka baada ya kutolewa kwa fedha hizi. Kwa hiyo, kuongozana naye wala halina tatizo. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. MARYAM AZAN MWINYI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa kituo cha Polisi kilichopo wilaya ya Mkoani mkoa wa Kusini Pemba kipo katika hali mbaya.

Je, ni lini Serikali itakifanyia ukarabati kituo hicho japo kwa dharura?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Maryam Mwinyi Kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba maeneo ya Pemba vituo vyake vingi vya Polisi vimechakaa vinahitaji kufanyiwa marekebisho au kiujengwa vipya. Tumeanza na majengo ya Kamanda wa Polisi wa mikoa miwili ya Pemba, lakini tutaendelea kujenga hivi vya ngazi ya wilaya na vingine vidogo ili hatimaye maeneo yote yaweze kupata vituo vinavyostahiki. Nimuahidi Mheshimiwa Mbunge kwamba katika ziara nitakayoifanya huko Pemba, moja ya maeneo ni kuzingatia maeneo haya ambayo hayana kabisa vituo vya Polisi ili na wao waweze kupatiwa vituo hivi kwa ajili ya usalama wa raia na mali zao.
MHE. DKT. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ili niulize swali dogo la nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, wakati maeneo mengine wanazungumzia habari ya ukarabati wa vituo vya Polisi, kwenye Mkoa wetu wa Iringa katika wilaya ya Kilolo bado Serikali haijajenga Makao Makuu ya Jeshi la Polisi ngazi ya wilaya ilhali ni zaidi ya miaka ishirini sasa Serikali imekuwa ikitoa ahadi.

Je, ni lini sasa Serikali itajenga makao makuu ya polisi Wilaya ya Kilolo?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Ritta Kabati kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema kwenye majibu yaliyotangulia, ni nia ya Serikali kuhakikisha kwamba wilaya zote zinapata vituo vya polisi vyenye hadhi ya wilaya. Hivyo kutokana na upatikanaji wa fedha tunakwenda kwa awamu. Nimuahidi tu Mheshimiwa Ritta kwamba Wilaya ya Kilolo ni miongoni mwa wilaya zitakazozingatiwa hasa ukizingatia kwamba kuna uharibifu mkubwa wa mazingira yanayohitaji usimamizi wa sheria kwenye maeneo hayo. Kwa hiyo itapewa kipaumbele katika bajeti zetu.
MHE. DKT. TECLA M. UNGELE: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa umbali kutoka Nachingwea – Liwale ni zaidi ya Kilometa 130 na Kilwa – Liwale ni zaidi ya kilometa 260.

Je, ni lini Serikali itajenga vituo vya polisi pale Kibutuka Wilaya ya Liwale na Njinjo kule Wilaya ya Kilwa? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Tecla Ungele kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa umbali alioutaja Mheshimiwa Mbunge kwamba kutoka eneo moja hadi kituo cha Polisi ni zaidi ya kilometa 100 ina-justify kabisa umuhimu wa uwepo wa kituo cha Polisi. Nimuahidi tu Mheshimiwa Mbunge, kwamba tutaelekeza Kamanda wa Polisi Mkoa na Jeshi la Polisi kwa ujumla wake kufanya tathimini ya uhitaji wa kituo cha Polisi maeneo hayo uliyoyarejea ili mpango wa ujenzi wa vituo hivyo uweze kutekelezwa. Ahsante sana.
MHE. ATHUMAN A. MAIGE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, Je, Serikali inakiri kuwa muda wa miaka sita tangu ichukue Muswada huu ni mrefu sana kutoletwa Bungeni?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, wakati tunajadili kupata maoni ya Muswada huu tuligundua kwamba kipengele kile cha kubeba silaha Upande wa Zanzibar kisingekubaliwa. Je, tukiongeza maneno “isipokuwa Zanzibar” katika kipengele kile kitafanya Muswada huu uamke na kuletwa Bungeni?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu mawali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Maige kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, uandaaji wa sheria, hasa hizi ambazo zinahitaji ushirikishwaji mpana wa jamii hususani kwenye hili ambalo linahusu pande mbili za Muungano ni jambo ambalo miaka sita huwezi ukasema ni muda mrefu sana. Ni muda mrefu lakini ili tupate sheria itakayokubalika kwa pande zote na wadau wote tunaomba Mheshimiwa atuvumilie tuweze kulikamilisha.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu maoni ya kubeba silaha upande wa Zanzibar kwamba kuna changamoto pengine hicho kipande kiondolewe, naomba Mheshimiwa asubiri michakato ya Baraza la Mapinduzi Zanzibar na Baraza la Mawaziri wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania yaweze kukamilisha kazi yake tuweze kuwasilisha Muswada huo.

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana.
MHE. JOSEPHINE J. GENZABUKE: Mheshimiwa Spika, ahsante, naomba kumuuliza Mheshimiwa Naibu Waziri. Je, ni lini Serikali itajenga Kituo cha Polisi katika Wilaya ya Uvinza?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Josephine Genzabuke, Mbunge, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, tunafahamu Uvinza ni Wilaya mpya na kama zilivyo Wilaya nyingine hazijawa na Vituo vya Polisi vya ngazi ya Wilaya. Nimpe matumaini Mheshimiwa Mbunge kwamba tumeanza ujenzi wa Vituo vya Polisi kwenye hizi Wilaya zote mpya kadri tunavyoendelea kupata bajeti tutaifikia Wilaya ya Uvinza ambayo tunatambua iko mpakani itapewa kipaumbele katika ujenzi huo. (Makofi)
MHE. CATHERINE V. MAGIGE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Nini mpango wa Serikali kuwasaidia wananchi wa Kata wa Kamwanga, Wilayani Longido Mkoa wa Arusha, kumalizia Kituo cha Polisi ambacho walianza kukijenga kwa juhudu zao wenyewe?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Catherine Magige, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwanza tuwapongeze wananchi ambao wamejitokeza kujenga Kituo cha Polisi huko Longido, niuelekeze Uongozi wa Polisi, Mkoa wa Arusha waweze kufuatilia kufanya tathmini kituo hicho kimefikia hatua gani na kinahitaji kiasi gani cha fedha ili kukamilisha ili tuweze kuingiza kwenye mpango wetu kutegemea upatikanaji wa fedha. Hilo jambo likishafanyika, basi tutakamilisha kituo hicho.
MHE. MIRAJI J. MTATURU: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi. Naomba nimuulize Mheshimiwa Naibu Waziri kwamba tulipitisha bajeti ya Bilioni Moja na Milioni Mia moja kwa ajili ya kujenga Kituo cha Polisi pale Ikungi na leo ni mwezi wa Novemba. Je, ni lini sasa Serikali italeta fedha kwa ajili ya ujenzi wa kituo hicho kama bajeti ilivyopitishwa?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mtaturu, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba bajeti hiyo ilipitishwa kwa ajili ya ujenzi wa kituo hicho kinachofanyika ni Jeshi la Polisi limewasilisha mpango wa ujenzi ambao utakapopitishwa na Wizara utawasilishwa Hazina kwa ajili ya kutoa fedha. Ni matarajio yetu fedha za maendeleo kwa ajili ya ujenzi wa kituo hiki kwa vile zinatoka kwenye Mfuko ambao tunauzungumzia kwa ukamilifu wiki iliyopita zitatoka kwa ajili ya kuwezesha ujenzi wa kituo hicho kuanza. Ninaashukuru. (Makofi)
MHE. DKT. PIUS S. CHAYA: Mheshimiwa Spika, kwanza nashukuru sana kwa majibu mazuri kwa Mheshimiwa Naibu Waziri, lakini nina maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; kwa kuwa tayari wananchi wa Tarafa ya Kintinku wameshatenga eneo la zaidi ya hekari nne katika Kijiji cha Lusilile kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Polisi. Je, Naibu Waziri yuko tayari kuambatana nami kwa ajili ya kuona hilo eneo kama linafaa kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Polisi?

Mheshimwa Spika, swali la pili; katika Makao Makuu ya Polisi ya Wilaya ya Manyoni, tuna upungufu mkubwa sana wa nyumba za watumishi hususani OCD na Mpelelezi wa Wilaya.

Je, nini commitment ya Serikali kuhakikisha kwamba tunawajengea watumishi hawa nyumba za kuishi? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Chaya, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwanza niwapongeze wananchi wa Tarafa ya Kintinku kutenga hizo hekari nne ili kujenga Kituo chao cha Polisi, nami nitaungana na Mheshimiwa Mbunge wakati wowote atakapokuwa tayari kwenda kujiridhisha juu ya kituo hicho. Hata hivyo, hata kabla mimi sijaenda, niutake Uongozi wa Polisi Mkoa wa Singida waanze kutembelea eneo hilo na kama wanaona linafaa waweze kuwashauri ipasavyo wananchi hawa ili nitakapofika basi ni uamuzi uwe unafanyika.

Mheshimiwa Spika, kuhusu swali la pili la ukosefu wa nyumba za watumishi akiwemo OCD Manyoni, nimuahidi Mheshimiwa Mbunge, tumeripoti hapa wakati wa bajeti kwamba tunao mpango wa ujenzi wa vituo vya polisi na makazi ya askari na tutakwenda kujenga kwa awamu kwa kutegemea upatikanaji wa fedha. Ni matarajio yetu kabla ya mwaka 2025 Manyoni pia watakuwa mmefikiwa. Ahsante sana.
MHE. PROF. PATRICK A. NDAKIDEMI: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa kunipa fursa. Wananchi wa kata za Mbokomu na Uru-Shimbwe katika Jimbo la Moshi Vijijini wamejenga Vituo vya Polisi na bado havijakamilika.

Je, Serikali ina mpango gani wa kuwasaidia wananchi hawa waliotumia nguvu zao kujenga hivi vituo na kuwajengea nyumba Polisi wa Kata?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Prof. Patrick Ndakidemi, Mbunge kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwanza nimpongeze yeye na wananchi wake kwa kuanza ujenzi wa vituo hivi kwa kutumia nguvu zao na jitihada zao Mbokomu na Uru. Kama nilivyojibu kwenye swali lililoulizwa na moja ya Wabunge hapa tutawatuma Askari wetu upande wa Kilimanjaro ili wafanye assessment ya kiwango kilichofikiwa, kiasi gani kinatakiwa ili vituo hivi viweze kukamilishwa hatimaye tuviingize kwenye mpango wa ujenzi. Nashukuru. (Makofi)
MHE. ABDALLAH J. CHAUREMBO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Hivi karibuni kumekuwa na wimbi la uhalifu katika Mikoa mbalimbali nchini. Je,Serikali ina mkakati gani wa kuunga mkono juhudi za wananchi nchi nzima ambao wameanzisha ujenzi wa Vituo vya Polisi ili kuweza kuvimalizia na hatimaye ulinzi uweze kuwa imara?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Chaurembo, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwanza uwepo wa wimbi la uhalifu ambao tumekuwa tukisema hapa uhalifu ni matokeo ya tabia na mwenedo wa jamii tunaupiga vita kwa nguvu zetu zote. Ndiyo maana yalivyojitokeza matukio haya ya panya road, ni jeshi halikulala hatimaye nchi imekuwa tulivu pia niwapongeze wananchi kwa kujenga Vituo vya Polisi mahala vinakohitajika ili mapolisi wawe karibu na wananchi.

Mheshimiwa Spika, kama nivyosema kwenye majiibu yangu ya msingi ya maswali yaliyopita, pale ambapo wananchi wamefanya kazi niwaombe Waheshimiwa Wabunge tuwasiliane na ma-OCD wetu na ma-RPC kwenye Mikoa yetu waweze kufanya tathmini kwenye kiwango cha ujenzi kilicho fikiwa na nini kinatakiwa kukamilisha, ili tuweze kuingiza kwenye mpango wa ugaramiaji kitaifa. Tukilifanya hilo itakuwa rahisi kuingizwa kwenye mipango. Nashukuru. (Makofi)
MHE. IDDI K. IDDI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Ni lini sasa Serikali itaanzisha ujenzi wa Kituo cha Polisi cha Wilaya katika Halmashauri ya Msalala?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Iddi Kassim Iddi, Mbunge wa Msalala, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Msalala ni Wilaya mpya kama ilivyo Wilaya nyingine, tumeanzisha mpango wa ujenzi wa Vituo vya Polisi kwenye maeneo mapya ambayo hayakuwahi kuwa nayo, ni matarajio yetu kulingana na upatikanaji wa fedha Wilaya ya Msalala pia itafikiwa muda siyo mrefu ujao. Nashukuru. (Makofi)
MHE. SALMA R. KIKWETE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Hali ya Kituo cha Polisi cha Mchinga ambapo ndipo Makao Makuu ya Jimbo ni mbaya sana. Je, ni lini kitafanyiwa ukarabati Kituo hicho?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Salma Rashid Kikwete, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, tunatambua Mchinga ndiyo Makao Makuu ya Jimbo na Wilaya. Niombe Mheshimiwa Mbunge uridhie nilishaahidi kufanya ziara katika Mkoa wa Lindi, moja ya maeneo nitakayopitia ni Mchinga ili kuona kiwango cha uchakavu wa kituo hiki tuweze kufanya mpango wa ukarabati ili kikamilike kiwe kituo stahiki kufaa kukaliwa na Askari wetu. Nashukuru. (Makofi)
MHE. NAGHENJWA L. KABOYOKA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza pia nikushukuru kwa kunipa nafasi kwamba swali hili lirudiwe leo kwa mara ya tatu.

Kwa kuwa, Kata ya Bombo lijenga Ofisi yake ya Kata na ikaweka nafasi ya Polisi pamoja na chumba cha mahabusu. Kwa kutambua kwamba hizi sehemu zote ulizoongelea ziko tambarare na hawa wakazi wa Kata Tisa zote wako milimani ambako usafiri ni shida sana. Je, Serikali haioni ianzishe kituo mnaita Police post ili angalau katika Kata hii ya Bombo kiwepo kusaidia wananchi walioko huko milimani?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, kwanza nianze kwa kuwapongeza wananchi wa eneo hilo kwa kujenga jengo la utawala ngazi ya Kata na kutenga eneo kwa ajili ya huduma za Kipolisi. Nitumie nafasi hii kuelekeza Jeshi la Polisi hususani Mkoa wa Kilimanjaro kutembelea eneo hilo kuona kama ujenzi ule unakidhi kuwa Kituo cha Polisi basi huduma za kipolisi zianze kutolewa kwenye eneo hilo. Nashukuru. (Makofi)
MHE. ANNE K. MALECELA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kupata nafasi hii. Kwa kuwa, Tarafa ya Gonja na Tarafa ya Mambavunta ni Tarafa ambazo ziko kwenye milima mikubwa sana na hiki Kituo cha Polisi cha Gonja wanapata shida sana kuwafikia wananchi kule milimani.

Je, Serikali haioni umuhimu mkubwa sana wa kupeleka gari lenye uhakika kwenye Kituo cha Afya cha Gonja ili waweze kuwahudumia wananchi wangu walioko kwenye Tarafa zile ambazo ni ngumu sana.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Anne Kilango Malacela, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli hii Kata aliyoitaja ya Gonja iko milimani na ni changamoto kubwa kutoka maeneo ya tambarare kuwahudumia wanachi kule milimani. Tunatambua umuhimu wa gari tumeeleza hapa juzi hivi sasa tulipata magari 78, na tumeweza Mkoa wa Kilimanjaro kuupatia magari mawili, ni ahadi yetu kwa Mheshimiwa Mbunge kulingana na changamoto ya usafiri wa eneo hilo tutakapo pata magari eneo hilo litafikiriwa na kupewa kipaumbele. Nashukuru. (Makofi)
MHE. GRACE V. TENDEGA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kuniona. Ni lini Serikali itajenga Kituo cha Polisi katika Tarafa ya Kalenga katika Jimbo la Kalenga Mkoani Iringa?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Grace Tendega, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli sasa hivi mwelekeo tumekwenda mpaka ngazi ya Kata tumepeleka maofisa wetu wakaguzi na wakaguzi wasidizi kwa ajili ya kusomamia Shughuli za polisi. Sasa iwapo Kata ya Kalenga haina tutaipa kipaumbele ili kata hii iweze kingatiwa hatimaye vijana wetu waweze kufanya kazi kwenye mazingira stahiki ya kutoa huduma za usalama wa raia na mali zao. Ahsante.
MHE. DAIMU I. MPAKATE: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi hii. Jimbo la Tunduru Kusini lina Tarafa Tatu. Tarafa ya Namasakata haina Kituo cha Polisi na ndiyo iliyopo mpakani na Msumbiji.

Je, ni lini Serikali itapeleka Kituo cha Polisi katika Tarafa hii ya Namasakata?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mpakate, Mbunge, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ninamshauri Mheshimiwa Mbunge ikiwa Tarafa hii haina kituo cha kwanza tutafute ardhi. Ardhi ikishapatikana tuipime tukabidhi Jeshi la Polisi hatimaye tuweze kuingiza eneo hilo kwenye mpango wetu wa ujenzi wa Kituo cha Polisi. Kwa vile anasema kiko mpakani inahitaji kwa kweli ulinzi eneo hilo na tutakupatia kipaumbele iwapo upatikanaji wa ardhi utatekelezwa mapema. (Makofi)
MHE. SIMAI HASSAN SADIKI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali nitakuwa na maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; kwa kuwa sasa Nungwi imebadilika hadhi kutoka kijiji kuelekea mji na kwa kuwa sasa kumekuwa na ongezeko kubwa la watu pamoja na wawekezaji katika sekta ya utalii wa Kimataifa.

Je, Serikali haioni haja ya kuongeza majengo na watendaji ili kukiongezea daraja Kituo cha Polisi Nungwi kutoka daraja C kwenda B?

Mheshimiwa Spika, swali la pili; kwa kuwa Nungwi kumekuwa na changamoto kubwa mno ya upatikanaji wa maji jambo ambalo limewapelekea maaskari wengi kuondoka kituoni kwenda sehemu za mbali kutafuta maji hayo.Je, Serikali haioni haja ya kuwachimbia kisima au kutafuta njia mbadala ili kuhakikisha kuna upatikanaji wa maji ya kudumu katika eneo lile? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Simai, Mbunge wa Nungwi, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, moja tunatambua kweli maeneo mengi ya vijijini ikiwemo Kijiji cha Nungwi kimekua na kuwa Mji Mdogo na watu wameongezeka, lakini kama nilivyosema kwenye jibu la msingi, eneo hili ni dogo, kama tuna dhamira ya kupanua, basi Mheshimiwa Mbunge atusaidie kushirikiana na Mamlaka ya Wilaya pale ili tupate eneo la kutosha kuweza kujenga kituo kinachokidhi mahitaji.

Mheshimiwa Spika, kuhusu suala la upatikanaji wa maji, naomba nishauri kwamba, kazi ya Jeshi la Polisi sio kuchimba visima, lakini kule kuliko na polisi kama walivyo wananchi wengine mamlaka za ugawaji wa maji ziwafikie kwa ajili ya kuangalia uwezekano wa kuwachimbia kisima. Tutawasiliana na wenzetu wa upande wa Zanzibar ili kuona uwezekano wa kuwapatia kisima wenzetu hawa ili wasiende umbali mrefu kutafuta maji. (Makofi)
MHE. JUMA USONGE HAMAD: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipatia fursa ya kuuliza swali la nyongeza. Mwaka, 2013 Kituo cha Polisi cha Mkokotoni kilipata majanga ya kuungua kwa moto na hadi kufikia tarehe 29 Machi, kituo hicho tayari kimekamilika kwa asilimia 95. Je, ni ipi kauli ya Serikali ili kukamilisha asilimia hizi tano ili kituo kile cha polisi kiweze kufanya kazi vizuri kama inavyotakiwa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Usonge, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ikiwa wananchi wamejitahidi kukamilisha kituo kwa kiwango cha asilimia 95, nachukua dhima ya kuwasiliana na wenzetu wa Jeshi la Polisi kupitia Mfuko wao wa Tunzo na Tozo kukamilisha asilimia tano zilizobaki ili kituo hicho kiweze kukamilishwa. (Makofi)
MHE. DKT. THEA M. NTARA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Licha ya juhudi kubwa anazofanya Mbunge wa Jimbo la Peramiho, je, ni lini Serikali itajenga Kituo cha Polisi pale Peramiho?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Thea Ntara, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, hitaji la kuwepo Kituo cha Polisi katika eneo la Peramiho ni kubwa kutokana na kukua kwa kasi ya shughuli za kibinadamu kwenye eneo hilo la Peramiho. Namwahidi Mheshimiwa Mbunge kwamba kwa kushirikiana na uongozi wa Mkoa wa Ruvuma, tutaona uwezekano wa kuingiza eneo la Peramiho katika mpango wa ujenzi wa kituo cha polisi. (Makofi)
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza, pamoja na majibu mazuri ya Serikali ya kutoa elimu ninalo swali hili: -

Mheshimiwa Spika, kwa sababu matukio haya ya uvunjifu wa sheria kwa vitendo hivi ambavyo nimevieleza katika swali la msingi vimeanza kuwa na matukio mengi, na sasa hivi yanapelekea matishio hata kwenye shule zetu za msingi na sekondari: Je, kwa nini Serikali isianzishe kampeni ya kutoa elimu ambayo itakwenda kila maeneo kunusuru Taifa hii na vitendo hivi vya uvunjifu wa sheria?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Massay, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli anachokisema tumepata malalamiko kwamba baadhi ya matendo yanayokiuka maadili ya Taifa na jamii zetu yameingia hadi kwenye shule, siyo msingi, sekondari na pengine hata vyuo. Wizara ya Mambo ya Nchi kama Wizara yenye dhamana ya kusimamia sheria, ulinzi wa mali, watu na mali zao, na kukabiliana na makosa ya kijinai yakiwemo haya, inaendelea kuhimiza jamii nzima, kama tulivyosema mara kwa mara, makosa mengi ni matokeo ya vitendo vilivyoko kwenye jamii zetu. Kwa hiyo, tunapaswa kuwa na ushirikiano kwa maana ya wazazi walezi jamii, shule, taasisi za dini na makundi mbalimbali kupigia kelele maeneo haya ili kuyatokomeza.

Mheshimiwa Spika, upande wa Jeshi la Polisi yeyote anayekiuka sheria ikiwemo kutenda makosa haya yanayobainika, uchunguzi unafanywa, tukithibitisha, wanapelekwa mahakamani ili sheria ichukue mkondo wake. Kwa maana ya jamii nzima, nimeona juhudi zinafanywa na Wizara mbalimbali ikiwemo Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto na Wizara ya Elimu hili liwe jukumu letu sote kukemea matendo kama haya.

Mheshimiwa Spika, naungana na Mheshimiwa Mbunge kuhusu kutoa elimu kwa ujumla kwa nchi nzima ili kukomesha vitendo hivi ambavyo vinakiuka kwa kiwango kikubwa maadili ya nchi yetu, ahsante. (Makofi)
MHE. ISSA OMAR KOMBO: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa nafasi, kwanza naomba nikumbushe tu kwamba kwa Zanzibar tunatumia Wadi siyo Kata. Kwa hiyo, hii ni Wadi ya Kiuyu.

Mheshimiwa Spika, naomba niulize swali moja la nyongeza kama ifuatanyo; ni miaka miwili sasa tumekuwa tukipata matumaini haya ya Serikali kwamba tutajengewa ofisi, lakini kiukweli hali ni mbaya. Kwa NIDA Micheweni wanatumia vyumba viwili walivyoazimwa na Wizara ya Afya ambapo vyumba hivyo viwili wanatumia Ofisi ya DRO, Ofisi ya Picha, store na jiko. Kwa kweli hali mbaya sana, hata ufanisi unakuwa ni mdogo sana.

Mheshimiwa Spika, tunaomba commitment ya Serikali; je, ni quarter gani ya mwaka wa fedha husika tutaanza kujengewa ofisi hii wananchi wa Wilaya ya Micheweni? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Kombo, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kweli narekebisha, badala ya kuita Kata ya Kiuyu, ni Wadi ya Kiuyu, ahsante sana.

Kuhusu kuwapa matumaini na kwamba hali ya ofisi hizo ni mbaya sana, nakubaliana naye. Ndiyo maana tunasema katika mwaka 2023/2024 tutaweka fedha kwa ajili ya ujenzi wa ofisi hii.

Mheshimiwa Spika, commitment ninayoitoa, ni kazi ndogo tu. Bunge lako tukufu likiidhinisha bajeti hii ambayo itakuwa imebeba pia dhima ya kujenga hizo ofisi 31, ni kwa uhakika kabisa jimbo lake litanufaika na ujenzi huo, ahsante.
MHE. JUMA USONGE HAMAD: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipatia fursa ya kuuliza swali la nyongeza.

Wilaya ya Kaskazini B - Unguja ni miongoni mwa wilaya ambazo zimekosekana ofisi hiyo ya NIDA; je, ni lini Serikali itawahakikishia wananchi wa Wilaya ya Kaskazini B kuwajengea kituo hicho cha Ofisi ya NIDA? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Juma Usonge kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, natambua uwepo wa changamoto za ofisi maeneo mbali mbali ikiwemo wilaya aliyoitaja ya Kaskazini B, Unguja. Ni ahadi yetu tutaendelea kujenga hatua kwa hatua kulingana na upatikanaji wa fedha. Kama muda ungeruhusu, ningeweza kusoma hizo ofisi 31 ambazo zitapata fedha, lakini niko tayari kuzi-share na Waheshimiwa Wabunge wajue lakini kadri tunavyopata fedha, kila kusipokuwa na ofisi tutajenga ofisi hizo. Nashukuru.
MHE. ABUBAKARI D. ASENGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru na ninashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali.

Kwa kuwa jana Katibu Mkuu wa CCM, Comrade Daniel Chongolo alipita kwenye ziara katika Jimbo la Kilombero na aliviona vituo hivi na akanielekeza Mheshimiwa Mbunge nije niongee na Waziri wa Mambo ya Ndani kwa ajili ya kuanza ujenzi wake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza; je, nikileta nakala ya hati ya ardhi hizo ambazo Mheshimiwa Naibu Waziri amesema, Serikali itakuwa tayari kuanza ujenzi wa vituo hivyo vya Tarafa ya Mang’ula na Tafara ya Kidatu?

Swali la pili; kwa kuwa tayari Tarafa ya Ifakara lipo eneo linalomilikiwa na Jeshi la Polisi na Wizara ya Mambo ya Ndani; je, Serikali iko tayari kuanza kwa haraka kujenga Kituo cha Polisi cha Ifakara?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Meshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, naomba kujibu maswali ya nyongeza ya Mheshimiwa Mbunge Asenga, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba maeneo hayo mawili ni ngazi ya Tarafa yanahitaji Vituo vya Polisi, lakini majengo yaliyopo yamechakaa sana, lakini mojawapo ya jengo la JWTZ liko kwenye hifadhi ya barabara, na barabara inayojengwa italiondoa.

Kwa hiyo, ni ahadi yetu kwamba tunaweka katika bajeti ya mwaka 2023/2024 tutakayoipitisha mwezi Juni ili tuweze kuanza mipango ya ujenzi, la msingi tupate hizo hati miliki ili kuhakikisha kiwanja kiko ndani ya mikono ya Jeshi letu la Polisi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu Kituo cha Ifakara naomba nimuahidi Mheshimiwa Mbunge, nilitembelea eneo lile kwa kweli wanachangamoto ya kituo, wanahitaji kujengewa kituo kipya cha Polisi ngazi ya Mji wa Ifakara.

Kwa hiyo, ni ahadi yetu pia kwamba tutakipa kipaumbele katika bajeti inayokuja, nashukuru sana.
MHE. ALOYCE J. KAMAMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kituo cha Polisi cha Tarafa ya Nyalonga kilichopo katika Kijiji cha Nyadibuye majengo yake yamechoka sana, na hivi wakati wa mvua yanavuja tena sana.

Swali; lini Serikali itafanya ukarabati wa kituo hicho cha polisi? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Aloyce Kamamba, Mbunge wa Buyungu, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli tulishazungumza na Mbunge na moja ya ziara yangu ilikuwa nifike, lakini sikuweza kufika kwamba kuna changamoto kwenye kituo hiki na ukanda ule ni ukanda wa mvua kubwa, ni kweli changamoto tunaiona.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpe ahadi Mheshimiwa Mbunge kwamba tutawasiliana na OCD na RPC wa Mkoa wa Kigoma ili katika vipaumbele vyake vya ukarabati wa majengo chakavu ya polisi hiki kipewe kipaumbele, ili hatimaye fedha zitakapotoka kiweze kukarabatiwa, nashukuru.
MHE. IDDI K. IDDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante; kwa kuwa wananchi wa Jimbo la Msalala hasa Kata ya Ngaya na kata ya Isaka tayari wana eneo na tayari tumeshajenga vituo vya polisi viko kwenye hatua ya renta; sasa ni lini Serikali itatenga fedha ili ije imalizie vituo hivi viwili ili wananchi waweze kupata huduma hiyo haraka? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Iddi, Mbunge wa Msalala kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Mbunge kwa juhudi anazofanya za kuhamasisha wananchi wake kuchangia ujenzi wa vituo hivi ikiwa ni pamoja na Halmashauri ya Msalala. Nimuahidi tu Mheshimiwa Mbunge kwamba kadri hali ya fedha itakavyoruhusu vituo hivi vya kata mbili ambavyo vimeshajengwa kiwango cha renta tutaviunga mkono kwa kumalizia baadhi ya vifaa vinavyopatikana madukani/viwandani sorry ili ujenzi wake uweze kukamilishwa, nakushukuru.
MHE. AGNESTA L. KAIZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushuru kwa kunipa nafasi ili nami niweze kuuliza swali dogo la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa tatizo la uchakavu wa vituo vya polisi ni la nchi nzima; swali langu je, Serikali haioni umuhimu wa kuandaa mpango kabambe wa miaka mitatu kwa ajili ya maboresho ya vituo hivi kwa maana ya kurahishisha ulinzi na usalama wa raia na mali zao? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mbunge Mheshimiwa Lambert, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpe uhakikisho kwamba kwa kutambua umuhimu wa kuwa na mpango mkakati wa utekelezaji Wizara ya Mambo ya Ndani kushirikiana na vyombo vyake imeandaa mpango wa miaka kumi wa ujenzi na ukarabati wa vituo vya polisi. Kwa hiyo, ulilolisema tumeshalifanyia kazi, mpango ule tunaugawa katika vipindi vya miaka mitano/mitano na miaka mitatu mitatu kwa maana ya Medium Term Expenditure Framework (MTF) ili kuvigharamia, ndio maana tunaposema hapa kwamba tunaingiza, tunatoa kwenye ule mpango mkuu wa miaka kumi tulionao. Nashukuru.
MHE. MWANTUMU DAU HAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana; pamoja na majibu mazuri ya Serikali naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa shehia yangu ya Fuoni ina matatizo makubwa katika eneo hilo, matatizo ya wizi na vibaka pamoja na wabakaji, maana kuna vibaka na wabakaji masuala mawili hayo muyaone.

Je, Serikali haioni haja kujenga Kituo cha Polisi katika eneo hilo? (Makofi)

Je, ni lini Serikali itaanza huo ujenzi katika maeneo hayo? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Mwantumu Dau, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, umuhimu wa kujenga Vituo vya Polisi kwa kweli unaanzia kwa wananchi na mamlaka zao za Serikali za Mitaa. Kwa maana ya uwepo wa matukio ya wizi, udokozi kwenye shehia aliyoibainisha, nimwombe Mheshimiwa Mbunge kwamba katika vikao vya Kamati za Usalama watakapojadili na kuona umuhimu wa kujenga Kituo cha Polisi, basi sisi Polisi Makao Makuu kwa maana ya IGP atatenga fedha kwa ajili ya kusaidiana na nguvu za wananchi kujenga vituo hivyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo kama Kamati ya Usalama ya Wilaya na Mkoa wataona umuhimu tuko tayari kuungana nao. Ni lini? Wakati wowote tutakapopata maombi hayo tutatekeleza mpango wa ujenzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana.
MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa nafasi. Ipo ahadi ya Serikali ya kujenga Kituo cha Polisi Itigi. Kwa muda mrefu, majengo wanayotumia polisi sasa ni ya reli na ambayo reli sasa wanajenga. Je, ni lini Serikali itatekeleza ahadi yake ya kujenga Kituo cha Polisi daraja B Itigi?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunatambua kweli Itigi ulikuwa Mji Mdogo lakini sasa unakua kwa kasi na unahitaji Kituo cha Polisi na ndio maana tayari tumeshamtuma Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida ili kufanya uhakiki wa uwepo wa kiwanja, ukubwa wake ili kuleta mahitaji na michoro iweze kuandaliwa kwa ajili ya ujenzi wa kituo hicho. Kwa hiyo Mheshimiwa niko tayari kufuatilia jambo hilo ili kuona kwamba linatekelezwa ili Mji wa Itigi uweze kupata Kituo cha Polisi kama alivyoomba cha daraja B.
MHE. FAKHARIA SHOMAR KHAMIS: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwa kuwa Mmtaa wa Mlandege ulioko Mjini Unguja kulikuwa na Kituo cha Polisi toka wakati wa ukoloni na pana maduka mengi ya wananchi, lakini kituo hicho sasa hivi kimekufa. Naomba Wizara iangalie tena kukifufua kituo kile kwa sababu ni mtaa wa maduka na umezungukwa na wananchi na maduka.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni ushauri nimeupokea na tutaangalia. Ahsante sana.
MHE. ORAN M. NJENZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana. Kwa kuwa wananchi wa Kata ya Igoma, Wilaya ya Mbeya wameanza kujenga kituo cha kimkakati kwa kuhudumia kata jirani za Wilaya Rungwe, Wilaya ya Mbeya na Wilaya ya Makete ikiwemo Kitulo pamoja na TFC. Je, Serikali ina mpango gani wa kuweza kuwaunga wananchi waliojenga mpaka Mtamba wa Panya ili wamalizie hicho kituo cha kimkakati angalau milioni 100 tu? Kama Serikali inaweza kuwapelekea hicho kituo kitafika hatua nzuri. Nashukuru sana.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge wa Mbeya Vijijini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza tunawapongeza wananchi wa Mbeya Vijijini pamoja na Mheshimiwa Mbunge wao kwa ushirikiano walioufanya na kuanza ujenzi wa Kituo cha Polisi Kata ya Igoma kama ilivyoelezwa na Mheshimiwa Mbunge. Ombi langu kwa uongozi wa Wilaya ya Mbeya wawasilishe maombi kwa Mkuu wa Jeshi la Polisi ili kituo hiki kiingizwe kwenye mpango wa ujenzi kama ambavyo tumefanya kwenye maeneo mengine. Nashukuru.
MHE. AMOUR KHAMIS MBAROUK: Mheshimiwa Spika, ahsante, nina swali moja la nyongeza; kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri kwa majibu yake mazuri.

Je, Mheshimiwa Naibu Waziri, yupo tayari baada ya Bunge hili kwenda kukitembelea kituo hicho?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza kwamba niko tayari ratiba itakavyoruhusu tutatembelea eneo hilo ili kuona kiwango cha uchakavu hicho kilichofikiwa.
MHE. USSI SALUM PONDEZA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii kuuliza swali la nyongeza. Ningependa nimuulize Mheshimiwa Waziri, nimekuwa nikisimama mara nyingi kuhusu matatizo ya vituo vyangu vya Chumbuni. Je, sasa nataka kauli yake, yuko tayari kuongozana na mimi mpaka kwenye jimbo langu kutokana na uhalifu umekuwa ukiongezeka na zaidi ya mara sita nimekuwa nikiuliza bila kupata majibu sahihi?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Pondeza kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kama nilivyokwishasema, tutakapokuwa tunakwenda kwa Mheshimiwa Amour kwa sababu kote ni Zanzibar niko tayari pia kupita kwenye jimbo lake ili kuona kiwango cha uhalifu anachozungumza.
MHE. JANET E. MAHAWANGA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Kufuatia changamoto ya Mkoa wa Dar es Salaam maeneo mengi kukosa vituo vidogo vya polisi hususan kata ya Makongo ambayo Serikali ilishaahidi kukamilisha ujenzi huo. Je, ni lini Serikali itatekeleza ahadi yake?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Janet kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba Serikali kwa nyakati tofauti ilishasema iko tayari kushirikiana na mamlaka za Serikali za Mitaa na Waheshimiwa Wabunge kukamilisha vituo vya polisi vilivyojengwa kwa nguvu za wananchi. Sasa kupitia Bunge lako tukufu nimuombe Kamanda wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, labda niseme IGP, kubaini vituo vyote vya Dar es Salaam ambavyo viko njiani havijakamilika kufanya tathmini ya kiwango cha ukamilifu unaohitajika ili viweze kutengewa fedha za kukamilisha vituo hivyo.
MHE. SYLVIA F. SIGULA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali la nyongeza, Kituo cha Polisi cha Wilaya ya Kibondo hakina hadhi ya kituo cha wilaya maana ni kidogo sana lakini pia ni chakavu mno. Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga kituo hicho ili kiwe na hadhi ya wilaya?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli tunafahamu kituo cha Kibondo ni kidogo kwa size lakini pia ni chakavu kinahitaji kufanyiwa ukarabati. Nimuahidi tu Mheshimiwa Mbunge kwamba kupitia Jeshi la Polisi mpango wa kukarabati kituo hicho kimewekwa katika Bajeti ya Serikali ya Mwaka 2023/2024 kwa hiyo ukae kwa subira kwamba mwaka ujao tukipitisha bajeti hapa kituo hicho pia kitakuwa kimezingatiwa.
MHE. MARYAM AZAN MWINYI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali moja la nyongeza. Je, ni lini Serikali itajenga Kituo cha Polisi Kengeja ambacho kipo Mkoani Pemba?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Maryam Azan Mwinyi kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kituo hiki cha Kengeja kipo isipokuwa ni chakavu sana. Nimekitembelea katika ziara yangu ya mwezi uliopita nikajiridhisha kwamba ni kituo chakavu na Wizara kupitia Jeshi la Polisi imekiweka kwenye mpango wa ukarabati katika bajeti ya mwaka 2023/2024.
MHE. ASIA A. HALAMGA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Je, ni lini Serikali itakamilisha ujenzi wa Jengo la Polisi Mkoa wa Manyara kwa kuwa takribani ni miaka 10 sasa lipo katika hatua ya msingi?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Asia Halamga, Mbunge wa Viti Maalum Manyara kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli nasi tumebaini kwamba jengo hilo limekaa muda mrefu na lilikuwa halijapangiwa bajeti lakini nimuhakikishie Mheshimiwa Mbunge katika bajeti ya mwaka 2023/2024, Jeshi la Polisi limeweka kituo hicho katika mpango wake wa ujenzi.
MHE. GODWIN E. KUNAMBI: Mheshimiwa Spika, ahsante, Kituo cha Polisi cha Mlimba ni kituo ambacho kinatumia majengo ya Shirika la Reli (TAZARA) na majengo yenyewe ni chakavu. Nini sasa mpango wa Wizara kujenga kituo cha polisi pale Mlimba?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Kunambi, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, bahati nzuri swali hili tumelijibu jana lilikuwa limeulizwa na Mbunge mwingine anayetoka Ifakara. Tunatambua uchakavu wa kituo hicho, ahadi ya Serikali ni kwamba kadiri tutakavyopata fedha katika bajeti ya mwaka 2024/2025, vituo hivi tena viwili, Ifakara na Mlimba vitawekwa kwenye mpango wa ujenzi.
MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru, nimshukuru pia Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani kwa majibu yenye kutia matumaini kiasi, lakini nina maswali madogo mawili ya nyongeza. Kama alivyosema Mheshimiwa Naibu Wazari kwamba Halmashauri ya Wilaya ya Kilindi imetenga eneo kwa ajili ya Kituo cha Polisi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza; kwa sababu eneo hilo limetengwa takribani miaka ishirini iliyopita je, ni utaratibu upi au mipango ipi au ni parameter zipi ambazo zinatumika kuhakikisha kwamba mnajenga Vituo vya Polisi kwa kuangalia uhalisia wa mahitaji ya eneo husika? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili; Mheshimiwa Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ambaye sasa hivi ni Waziri wa Mambo ya Ndani alikwishatembelea Wilaya ya Kilindi na kujionea uhalisia wa changamoto ya Kituo cha Polisi jinsi kilivyo.

Je, Mheshimiwa Naibu Waziri, yuko tayari kutoa commitment kwa wananchi wa Wilaya ya Kilindi kwamba mwakani watajenga Kituo cha Polisi? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Kigua, Mbunge wa Kilindi, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba kumekuwa na ahadi zinatolewa na zimechukua muda mrefu, hususan kituo hiki, eneo limetengwa muda mrefu kama alivyosema miaka 20, na ametaka tuseme tutazingatiaje uhalisia wa maeneo husika?

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba, tunapotaka kujenga eneo lolote lazima tuzingatie uhalisia wa eneo. Ndiyo maana wataalam wetu wanakwenda kule kufanya tathmini ya udongo ili kuweza kujiridhisha vifaa na kiwango gani cha ujenzi utakaohitajiwa. Kwa hiyo, watakapokuwa wanaanza ujenzi, mahitaji halisi ya eneo la Mheshimiwa Mbunge yatazingatiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia hili la commitment nimesema, tutatenga kwenye bajeti ya 2023/2024. Sasa bajeti yetu ikishapita hapa, namwomba Mheshimiwa Kigua asome maeneo yatakayojengewa vituo, atajiridhisha kwamba eneo lake litakuwa na mpango huo wa ujenzi. Nashukuru. (Makofi)
MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Katika Jimbo la Mlalo, Vituo vya Polisi vya Mlalo na Mtae vipo katika majengo ambayo ni ya Serikali za Vijiji: Je, Serikali ina mpango gani sasa kujenga majengo ya Polisi katika tarafa hizi mbili?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Shangazi, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nampongeza Mheshimiwa Shangazi, moja, kwa kujenga mahusiano mema na Serikali za Vijiji hata wakapata majengo ya kuazima. Pia, nikiri kwamba majengo yale hayakidhi haja ya vituo vya kisasa vya Polisi. Nimuahidi tu Mheshimiwa Mbunge kwamba kwa vile yeye analo fungu kidogo kwenye Mfuko wa Jimbo, nimshauri aweze kutenga kidogo kwa sababu, tumesema vituo vilivyoko kwenye maeneo ya kijamii kadiri wanajamii wanavyoanza kutoa na Serikali inawaunga mkono kumalizia. Kwa hiyo, akianza tu anipe taarifa na sisi Wizarani tutajipanga ili Jeshi la Polisi liweze kuongezea, vituo hivi vya Mlalo na Mtae viweze kukamilika, nashukuru.
MHE. SALMA R. KIKWETE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, naomba niulize swali la nyongeza kwa niaba ya Jimbo la Mchinga. Kituo cha Polisi cha Mchinga kina ukubwa wa kilometa 30 kwa 40 na bahati nzuri kiwanja kimepimwa, lakini kinakabiliwa na changamoto kadhaa nyingi tu. Changamoto ya kwanza ni uchakavu wa jengo, ikiwa na maana kwamba, paa linavuja kabisa, ukosefu wa usafiri na nyumba za watumishi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kujua, nini kauli ya Serikali juu ya kuboresha Kituo hiki cha Jimbo la Mchinga? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Salma Kikwete, Mbunge wa Mchinga, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakiri kwamba vipo Vituo vya Polisi vina hali mbaya sana. Kwa kuwa tulishatoa ahadi hapa ya kutembelea Jimbo lile na Wilaya ya Lindi kwa ujumla ili kuangalia uchakavu wa vituo vya Magereza, niahidi kwamba baada ya Bunge hili, nitatimiza ahadi hiyo ya kutembelea Lindi, Mchinga kwa madhumuni ya kuona kiwango cha uchakavu na hatimaye Mkuu wa Jeshi la Polisi aelekezwe kutenga fedha kwa ajili ya ukarabati wa kituo hicho.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, namwomba Mheshimiwa Mbunge, kama atapata nafasi niko tayari kuongozana naye, ahsante.
MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kunipa nafasi. Wilaya ya Tanganyika ni miongoni mwa Wilaya ambazo hazina Kituo cha Polisi, wanatumia Kituo cha Polisi kwenye jengo la Ofisi ya Kata. Halmashauri ya Wilaya la Tanganyika kupitia Ofisi ya Mkuu wa Wilaya wameomba wadau kuchangia, nami nikiwa miongoni mwa wadau kujenga Kituo cha Polisi. Serikali ina mpango gani wa kuwasaidia wananchi ambao wamejitolea ili waweze kukamilisha hicho Kituo cha Polisi ambacho kipo katika hatua ya awali ya msingi?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Kakoso, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, moja tumpongeze kwa kazi nzuri aliyofanya kama mmoja wa wadau na wadau wengine walioanza ujenzi wa Kituo hiki cha Polisi pale Tanganyika. Kwa niaba ya Waziri wangu, niahidi tu kwamba, tunamwelekeza IGP kupitia Makamanda wake waweze kufanya tathmini ya kiwango kilichofikiwa na kiasi gani kinatakiwa kama pungufu ili waweze kuingiza kituo hiki cha Tanganyika kwenye mpango wao wa ujenzi, nashukuru.
MHE. EMMANUEL A. MWAKASAKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipatia nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Katika kata 29 zilizopo katika Jimbo la Tabora Mjini kuna upungufu mkubwa kwenye vituo vya Polisi vilivyoko kata za nje. Kata ya Kazima haina kabisa Kituo cha Polisi na uhalifu mwingi unafanyika maeneo yale katika Jimbo la Tabora Mjini: Ni lini Serikali itaweza kuweka mkakati wa kujenga Kituo cha Polisi katika kata hiyo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mwakasaka, Mbunge wa Tabora Mjini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nampongeza Mheshimiwa Mbunge Mwakasaka kwa dhamira yake ya kujenga vituo vya Polisi kwenye maeneo ya Tabora. Unajua Tabora wakati fulani ilikuwa na wimbi kubwa sana la uhalifu, hapo katikati wakapoa sana, tukaamini pamekuwa eneo lenye utulivu. Sasa kama wameanza matukioya uhalifu, namwomba Mheshimiwa Mbunge, kupitia Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Tabora, waangalie maeneo yanayoweza kuwekwa vituo vya kimkakati kama Kazima, basi wayaingize kwenye mpango wao ili Serikali Kuu kupitia Jeshi la Polisi iweze kuwasaidia kukamilisha vituo hivyo. Wakifanya hivyo, tutawaunga mkono, nashukuru sana.
MHE. FATMA H. TOUFIQ: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa fursa ya kuuliza maswali ya nyongeza. Niishukuru sana Serikali kwa majibu mazuri, nina maswali mawili ya nyongeza: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza. Je, Serikali haioni umuhimu wa kuwa na program maalum hasa kwa kutumia mapolisi kata ili waweze kutoa elimu kwa jamii kuweza kupunguza masuala ya ukatili?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili. Kwa kuwa kuna baadhi ya wananchi wamekuwa wakisambaza picha ambazo zinaonesha matukio mbalimbali ya ukatili katika mitandao ya kijamii na picha nyingine zimekuwa zikikiuka haki za binadamu na kutweza utu wa wale ambao ni wahanga wa ukatili: Je, Serikali haioni upo umuhimu wa kuwa na namba maalum ya Serikali ambayo matukio yale yatapelekwa kule badala ya watu wachache kusambaza picha hizi katika mitandao?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Fatma Toufiq, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunatambua umuhimu wa kuendelea kuimarisha elimu kwa ajili ya jamii nzima kupitia Polisi wetu wa Kata. Kwa kutambua hilo, ndiyo maana kuanzia mwaka 2022 Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan imeridhia kutoa ajira zaidi ya Askari Wakaguzi Sasaidizi 3,200 na kupangiwa kwenye kata. Tumeanza kuona baadhi ya kata wameanza kufanya vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nawaomba Waheshimiwa Wabunge na viongozi wetu kwenye Wilaya na Halmashauri kuwatumia Polisi Kata hawa, hasa wanapokuwa na vikao vyao, mikutano ya hadhara ili waendelee kutoa elimu. Hii itasaidia kupunguza uhalifu kwenye maeneo mbalimbali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, juu ya ushauri alioutoa wa udhibiti wa usambazaji wa picha zinazokiuka haki na maadili, tunapokea ushauri huo ili tuweze kuufanyia kazi. Ni kweli, baadhi ya picha zinazooneshwa kwenye mitandao ya kijamii nyingine ziko vibaya sana, badala ya kusaidia zinaharibu kabisa. Kwa hiyo, tunaupokea ushauri huo ili tuweze kuufanyia kazi, ahsante sana.
MHE. DKT. THEA M. NTARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hili wimbi kubwa la ukatili na tabia zote mbaya katika jamii: Je, Serikali haioni sasa iko haja ya kuimarisha Polisi Jamii kwenye vijiji ili angalau huo ukatili uweze kutambulika kwa haraka zaidi? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Dkt. Thea Ntara, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwamba swali hili linakaribiana sana na swali lililoulizwa na muuliza swali la msingi. Ni kweli, sasa hivi tumeweka hawa Wakaguzi wa Polisi kama viongozi kwenye ngazi hizo za kijamii, lakini pia wapo Polisi wa kawaida wenye vyeo vya chini ili kushirikiana na hawa Polisi Kata. Kwa hiyo, ushauri alioutoa Mheshimiwa tunauzingatia na ndiyo maana tutaendelea kuimarisha eneo la Polisi Kata kweye kata zetu zote ili waweze kutimiza wajibu wao huu wa msingi, ahsante sana.
MHE. YAHYA A. MHATA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kuniona. Jimbo la Nanyumbu liko mpakani mwa Tanzania na nchi ya Msumbiji. Sisi sote ni mashahidi kwamba hali ya usalama sisi na ndugu zetu wa Msumbiji siyo nzuri kwa wakati huu. Majibu ya Serikali nayashukuru sana. Sasa swali kwa Mheshimiwa Waziri: -

Je, ni commitment gani ambayo unaitoa kwa wananchi wa Jimbo la Nanyumbu kuwahakikishia kwamba katika mwaka huo ujao wa fedha 2023/2024 watapata Kituo cha Polisi ili kuwa na uhakika na usalama wao na mali zao? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, commitment ni kiwango cha asilimia mia moja. Kama bajeti yetu itapitishwa mwezi Juni, uhakika ni kwamba Kituo cha Mangaka ni moja ya vituo vilivyopangwa kujengwa katika mwaka wa 2023/2024. Kwa hiyo, huo ni uhakika, naomba Mheshimiwa Mbunge asiwe na wasiwasi, ahsante sana. (Makofi)
MHE. AGNES E. HOKORORO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. naomba kuuliza swali dogo la nyongeza: -

Je, ni lini Serikali itaongeza majengo na kukarabati Kituo Polisi Masasi ambacho kilijengwa wakati wa ukoloni 1959?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongea la Mheshimiwa Hokororo, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, natambua vituo vilivyojengwa kabla ya uhuru kama hiki cha Masasi ni vya muda mrefu, vimechakaa, vinahitaji ukarabati. Kupitia Bunge hili namwomba IGP kupitia wasaidizi wake walioko mikoani waweze kufanya tathmini ya kiwango cha uchakavu wa Kituo cha Polisi ngazi ya Wilaya pale Masasi ili baada ya kubaini kiwango cha uchakavu kiweze kutengewa bajeti kwa ajili ya matengezo kulingana na mpango wetu wa matengezo na ujenzi wa vituo vyetu vya Polisi, nashukuru.
MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali dogo la nyongeza: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa, Tarafa ya Nyijundu tuna ujenzi wa Kituo cha Polisi, nami kama Mbunge nimeweza kushirikiana na wananchi hao kwa kuchangia matofali zaidi ya 2,000: Je, Serikali iko tayari kuchangia nguvu za wananchi ili tuweze kukamilisha kituo hicho?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge wa Nyanghwale, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo spirit ya Wizara kwamba pale ambapo wananchi na wadau wao wamejitokeza kuanza ujenzi wa vituo hivi vya Polisi kwa ajili ya usalama wetu, sisi tutawaunga mkono. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge kama ametoa matofali 2,000 na wadau wengine wametoa na ujenzi umeanza, basi katika ukamilishaji tutawanga mkono. Wakati wowote mtakapokuwa mmefikia hatua ya ukamilishaji, tafadhali tuwasiliane ili tuweze kukuunga mkono kituo hicho kikamilike na kuanza kazi, ahsante.
MHE. DEODATUS P. MWANYIKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru saba kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Kwa mikoa ambayo inategemea sana uchumi wa misitu; mikoa ya nyanda za juu Kusini na hasa Mkoa wa Njombe, wananchi wamepata umasikini mkubwa sana kutokana na moto ambao unatokea mwaka baada ya mwaka. Serikali ina mpango gani wa kuwa na mkakati wa kusaidia kwa kuleta vifaa vya kisasa kwenye maeneo hayo ambayo yanashambuliwa sana na moto?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Deo Mwanyika kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli anayoyasema hutokea kwenye mikoa na wilaya nyingi zenye misitu. Kwa kutambua hilo ndiyo maana Mkoa wa Njombe hadi sasa wanayo magari mawili, moja liko Njombe Mjini na lingine liko Makambako. Ni dhamira ya Serikali kadiri uwezo wetu utakavyoongezeka wa kununua magari ya kuzimia moto, Mkoa wa Njombe pia utazingatiwa.
MHE. INNOCENT S. BILAKWATE: Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa maelezo ambayo ameyaeleza Mheshimiwa Waziri inaonesha Ofisi ya NIDA imeshindwa kuwapatia Wanakyerwa vitambulisho, kwa sababu wananchi waliojitokeza ni 112,518. Wananchi waliopatiwa vitambulisho ni 31,897 ambayo ni asilimia 28. Kwa hiyo asilimia 71.7 bado hawajapatiwa vitambulisho.

Je, nani ambaye atalaumiwa kwa sababu wananchi hawa kutopatiwa vitambulisho hawawezi kusajili simu zao, wananchi hawa hawawezi kusajili hata kampuni, ni nani wa kulaumiwa katika hili?

Mheshimiwa Spika, swali lingine la pili kwa sababu inaonesha NIDA wameshindwa kutoa vitambulisho, kwa nini zoezi hili la NIDA lisisitishwe nchi nzima ili wakajipanga upya kuja kuwahudumia wananchi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu maswali ya nyongeza ya Mheshimiwa Bilakwate kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, moja; wa kulaumiwa nani? Nadhani hilo tumeshapata suluhisho Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan imeridhia kutoa fedha ambazo zilikwamisha kwa muda mrefu kutomlipa mzabuni zaidi ya bilioni 17. Baada ya kumlipa mzabuni mkataba umehuishwa na uzalishaji wa vitambulisho unaendelea. Na tuishukuru Wizara ya Fedha imeanza kutoa katika bajeti fedha iliyopitishwa katika bajeti bilioni 42 imeshatoa zaidi ya bilioni 10 ili kumlipa mkandarasi aanze kuzalisha vitambulisho hivyo. Kwa mwenendo huu nina uhakika wananchi wote watapata vitambulisho kama ilivyokusudiwa.

Mheshimiwa Spika, ili suala la kwamba wameshindwa sasa tusitishe; sasa tuko kwenye mkataba na Serikali imeshaji- commit kutoa fedha sasa unasitisha ili u-achieve nini wakati vitambulisho bado ni muhimu. Jambo la msingi watekelezaji wetu wa Serikali maeneo mbalimbali kama mtu ana namba ya utambulisho tumeshatoa mwongozo kwamba namba ile itumike kama kitambulisho, kama kuna mahali mtu anakwamisha tupeane taarifa ili hatua ziweze kuchukuliwa, nashukuru.
MHE. PRISCUS J. TARIMO: Mheshimiwa Spika, ahsante sana, kwa kuwa matukio haya yamekuwa yanajitokeza mara kwa mara na inaonekana uwezo wa Wizara kupambana nayo bado ni mdogo.

Je, hawaoni umuhimu wa kurudisha huduma hii ya zimamoto kwa Halmashauri?

Mheshimiwa Spika, swali la pili kwa sababu Mkoa kama wa Kilimanjaro una gari moja tu la zimamoto ambalo ni vigumu kuweza kufika mahali kwa muda mfupi. Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha angalau tunakuwa na gari la zimamoto kila Wilaya? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, kuhusu kurejesha suala hili la zimamoto kwenye local governments, naomba nimkumbushe Mheshimiwa Mbunge kwamba lilikuwa hivyo kabla ya mwaka 2010 ikaonekana uwezo wa Serikali za Mitaa kumudu jukumu hilo ni mdogo sana na ikaelekezwa Serikali Kuu ichukue jukumu hilo na ndio sheria ikabadilishwa Serikali za Mitaa zikarejesha jukumu hilo ngazi ya kitaifa.

Mheshimiwa Spika, sasa tunachoweza kufanya ni kuimarisha na bahati nzuri kupitia bajeti ijayo tuna zaidi ya magari ya zimamoto 12 yatanunuliwa na uokozi yakiwemo magari yenye ngazi, lakini vilevile tumepata mkopo kutoka Austria ambao utasaidia kuimarisha uwezo wetu wa kupata vifaa kwa ajili ya kuzimia moto.

Kwa hiyo, tusikate tamaa tunaendelea kuimarisha jeshi hili bila shaka baadaye litaongeza weledi katika eneo hilo, nashukuru.
MHE. NEEMA G. MWANDABILA: Mheshimiwa Spika, barabara ya Tanzam ni muhimu sana na imekuwa magari ya mafuta yanawaka moto na Mkoa wa Songwe hatuna gari la zimamoto. Ni lini Serikali italeta gari ya zimamoto katika Mkoa wa Songwe?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, ni lini Serikali itapatia Songwe; tumeweka kwenye bajeti katika magari 12 yatakayonunuliwa mwaka huu mikoa isiyokuwa na magari kabisa ikiwemo Songwe itapata gari hilo, ahsante.
MHE. ABUBAKARI D. ASENGA: Mheshimiwa Spika, katika hayo magari yatakayokuja yananunuliwa na Serikali; je, Serikali iko tayari kupeleka gari moja katika Mji wa Ifakara?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, kwa sababu baadhi ya mikoa haina magari, siwezi kutoa ahadi hapa kwamba Ifakara watapata gari, lakini kadri tutakavyoongeza uwezo wetu wa kununua magari Wilaya zenye changamoto kubwa pia zitazingatiwa, nashukuru.
MHE. SAASHISHA E. MAFUWE: Mheshimiwa Spika, kwenye hayo magari 12 ambayo Serikali imenunua; je, Wilaya ya Hai imo?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, kwa sasa haimo, lakini mpango wa Serikali kadri utakavyoongeza uwezo wetu maeneo kama haya ambayo yamekuwa na usumbufu wa kuwaka moto msitu wetu unaozunguka Mlima Kilimanjaro kuwaka moto mara kwa mara yatazingatiwa katika bajeti zetu zijazo.
MHE. TABASAM H. MWAGAO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru, kwa kuwa Sengerema ni sehemu ambayo ni ng’ambo ya Mwanza na tuna gari dogo sana ambalo lina uwezo wa kuchukua maji lita 500.

Je, Serikali iko tayari kutubadilishia tupate gari kubwa kwa sababu tuna-cover eneo kubwa mpaka Geita, ukichukua Buchosa na sasa hivi tuna mgodi?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba Sengerema inachukua eneo kubwa, lakini angalau wao wanalo gari moja japo dogo wengine hawana kabisa. Kwa hiyo, tutaendelea kuimarisha uwezo wetu ili baadaye Wilaya zote zikishapata then tutaingia uwezo wa kuongezea Wilaya ambazo zina magari madogo kama hayo.
MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Spika, kwa nini Serikali isiweke kipaumbele ya kununua hayo magari ya zimamoto kwenye mikoa yote ambayo haina pamoja na Wilaya zote nchini?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, nimejibu katika majibu ya swali la msingi kwamba katika bajeti ya mwaka huu tunaoendelea kutekeleza tutaanza kununua magari ambako mikoa isiyokuwa nayo itapewa kipaumbele baada ya hapo tutaingia kwenye Wilaya, nashukuru.
MHE. ABEID R. IGHONDO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru natambua juhudi hizo za Serikali, lakini kituo hicho cha polisi cha Kinyagigi ni kidogo, lakini pia kiko umbali mrefu kutoka yalipo majengo ya Serikali ikiwemo jengo la halmashauri, hospitali ya wilaya, benki pamoja na huduma za mahakama.

Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga kituo cha polisi chenye hadhi ya wilaya katika mji wa Ilongero?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, kituo cha polisi kilichopo katika Mji wa Ilongero ni chakavu, hakina gari wala nyumba za watumishi. Je, Serikali ina mpango gani sasa wa kuboresha huduma za kipolisi katika kituo hiki? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, kituo cha polisi hadhi ya wilaya nadhani ni jambo la kuhitaji tafakuru na niko tayari kuzungumza na Mheshimiwa Mbunge kwa sababu tayari Wilaya ya Singida ina kituo cha ngazi ya wilaya, kinachotafutwa hapa ni kituo cha ngazi ya halmashauri. Sisi tunafahamu sote huwezi ukawa na OCD wawili ndani ya wilaya moja, lakini pale ambapo halmashauri ile itakuwa wilaya itakuwa rahisi ku- determine kwamba tunampeleka OCD and therefore anakuwa na ofisi yake, lakini tunatambua umuhimu wa kujenga kituo chenye hadhi kuliko hiki cha Daraja la C kwa sababu ni kituo kidogo.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Mbunge tutawasiliana kupitia Jeshi la Polisi tuone uwezekano wa kujenga kituo kikubwa kidogo kinachoweza kutekeleza majukumu zaidi ya kituo cha Daraja C.

Mheshimiwa Spika, kuhusu uchakavu tumesema tutaendelea kufanya ukarabati wa vituo vilivyo katika hali mbaya kutegemea uwepo wa fedha. Kwa mwaka huu nitaja juzi hapa baadhi ya vituo na kadri ya hali ya fedha itakavyoruhusu eneo hili la Ilongero litazingatiwa katika bajeti zetu, ahsante.
MHE. REHEMA J. MIGILLA: Mheshimiwa Spika, nianze kwanza kuishukuru Serikali kwa kukubali maombi ya hawa raia wangu, lakini swali langu lilitaka ni lini huu mchakato utakamilika na kwenye majibu hawajaonesha. Sambamba na hilo nina maswali madogo mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, swali langu la kwanza; Jimbo langu la Ulyankulu katika hizo Kata tatu asilimia 99 ya mwananchi hao kwa sasa ni raia wa Tanzania. Ikijumlisha raia tajinisi na raia wazawa kabisa wa Tanzania lakini wananchi hawa wanaishi chini ya Sheria Na.9 ya wakimbizi ambayo sheria hii sasa inazuia kufanya shughuli zozote za maendeleo ikiwa sambamba na uwekezaji na kufanya shughuli nzuri za kuleta maendeleo kwa wananchi wetu. Sasa je, kwa sasa Serikali haioni kuna kila sababu ya kufuta hii Sheria Na.9 ambayo inazuia maendeleo na uwekezaji kwa wananchi wetu wakati huo Serikali inakwenda kujipanga kwenye zoezi zima la sensa ili kupanga shughuli za kimaendeleo? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali langu la pili, Waziri amesema kwamba hawa raia 6,620 ni watoto wa raia wa Tanzania, yaani wazazi wao kwa sasa ni raia wa Tanzania halafu watoto ni wakimbizi. Sasa je, kwa sababu mchakato haueleweki utakamilika lini, kwa nini sasa hatuoni haja ya UNHCR kuwahudumia hawa wananchi kwa kuwapatia package inayowapatia wakimbizi kwenye makambi mengine ya wakimbizi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Migilla, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, la kwanza, kuhusu umuhimu wa kufuta Sheria Na.9 ili waruhusiwe kufanya vitu vya maendeleo kwenye makazi yale nadhani Mheshimiwa asubiri tutakapokamilisha kuwapatia uraia wote then hatua za marekebisho ya sheria husika zitafuata. Lakini kama tunakiri kwamba bado watu wengine hawajapewa uraia itakuwa ngumu sana hilo kulitekeleza.

Mheshimiwa Spika, kuhusu swali la pili, watoto hawa wapate package kutoka UNHCR, hilo tutalizungumza, lakini nadhani Mheshimiwa Mbunge jambo la msingi ilikuwa kuharakisha wapate uraia wao ili wa-enjoy haki nyingine kama raia kuliko hilo la package lakini maadam Mheshimiwa Mbunge ameliuliza hapa, tutafanya mawasiliano na wenzetu wa UNHCR kuona uwezekano wa kuzingatia hili ombi lake. Nashukuru. (Makofi)
MHE. AGNESTA L. KAIZA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Uraia pacha imekuwa ni kilio cha Watanzania walio wengi. Nini kauli ya Serikali rasmi kuhusiana na jambo hili? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba nimwombe Mheshimiwa Lambert swali hili ni mahsusi, liwasilishwe ili lifanyiwe utafiti hatimaye liweze kujibiwa ipasavyo hapa Bungeni. (Makofi)
MHE. SOUD MOHAMMED JUMAH: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali nina maswali mawili ya nyongeza. Kwa kuwa wananchi wa Jimbo la Donge wanatembea masafa marefu kufuata huduma za kipolisi katika Vituo vya Polisi vya Mkokotoni na Kituo cha Polisi cha Mahonda na kwa kuwa uhalifu na halikadhalika idadi ya watu wameongezeka katika maeneo mbalimbali ya Jimbo la Donge. Je, Serikali haioni haja ya kufanya kazi na wananchi wa Jimbo la Donge kuweza kujenga kituo katika maeneo hayo?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa kuwa Kituo cha Polisi cha Mahonda ni kituo kikongwe toka kipindi cha ukoloni na kituo hiki hakijafanyiwa ukarabati mkubwa kwa kipindi kirefu. Je, Serikali ina mpango gani wa kukifanyia marekebisho makubwa Kituo cha Polisi cha Mahonda pamoja na nyumba za wafanyakazi ili kuweza kukidhi kupambana na masuala ya uhalifu ambayo yanaongezeka siku hadi siku? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Soud, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kuhusu umuhimu wa kujenga Kituo cha Polisi eneo la Donge ambalo ametaja vigezo vitatu vya masafa marefu lakini kuwepo kwa uhalifu, kujenga kituo pale tutawasiliana na Kamisheni ya Polisi Zanzibar wafanye utafiti kuona umuhimu wa kujenga pale ili iweze kuingizwa kwenye bajeti hatimaye ujenzi uweze kufanyika.

Mheshimiwa Spika, kuhusu swali lake la pili la kuchakaa kwa Kituo cha Polisi Mahonda, namwomba Mheshimiwa Mbunge, tutaituma Polisi Kamisheni Zanzibar kwa kauli yangu niombe Polisi Zanzibar wafanye uthamini wa Kituo cha Polisi Mahonda kwa madhumuni ya kubaini mahitaji ili tuweze kuingiza kwenye mpango wa ukarabati. Nashukuru.
MHE. KUNTI Y. MAJALA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa nafasi. Kata ya Soya, Wilaya ya Chemba ni kati ya Kata ambayo inahudumia wafanyabiashara wa mazao pamoja na wafanyabiashara wa mifugo, lakini Kata hii haina kituo cha polisi pamoja na kwamba kutokuwepo kwa kituo cha polisi michakato aliyoisema Naibu Waziri hapo tulishaikamilisha. Je, ni lini sasa Serikali itapeleka kituo cha afya, samahani, Kituo cha Polisi kwenye Kata ya Soya ili kukidhi mahitaji na matakwa ya usalama wa Jeshi la Polisi ya kulinda raia na mali zao? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, nashukuru maana mwanzoni afya ilinichanganya kidogo. (Kicheko)

Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Kunti Majala kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ikiwa kuna mahitaji makubwa ya kujenga Kituo cha Polisi Kata ya Soya, nishauri mamlaka za utawala, kwa maana ya Serikali ya Mtaa Chemba lakini na uongozi wa Wilaya kupitia Kamati yao ya Usalama wajenge hoja hii kama nilivyoeleza, wanyambue mahitaji yao ili wawasilishe kwa IGP, then taratibu ya kuingiza kituo hiki katika mpango wa ujenzi iweze kufikiriwa. Hata hivyo, kama tulivyokwishasema kwenye majibu ya maswali yaliyotangulia, tunahamasisha ushiriki wa Serikali za Mitaa ikiwa ni pamoja na wananchi waanze ujenzi ili Serikali isaidie kukamilisha vituo hivi wakiwa na haja ya kuwa na kituo cha polisi. Ahsante.
MHE. ANGELINA ADAM MALEMBEKA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa fursa ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Kwanza nimpongeze Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri yenye ufasaha zaidi, lakini nina maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza, katika majibu yake ameelezea uwezo wa gari pia uzima na usalama wa gari. Sasa hivi kuna magari mengi yanayobeba vinywaji baridi kusambaza madukani kumekuwa na utaratibu wa makusudi kuyapanua na kuyatanua magari yale kiasi kwamba hata dereva inabidi aweke nondo ili aweze kuipata ile site mirror vizuri. Je, Serikali ina kauli gani kuhusiana wamiliki wa magari hayo ambao wanapanua kwa makusudi magari hayo? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali langu la pili kwa kuwa pia ameelezea uzima na usalama wa magari, tuna magari mengi yanayobeba takataka lakini magari yale yenyewe ni sehemu ya takataka. Kama ni kweli yanakaguliwa kuangalia uzima wake na usalama, Serikali ina kauli gani kuhusiana na magari yanayobeba takataka ambayo yenyewe pia ni takataka? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Malembeka, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, moja kuhusu magari ya vinywaji baridi kupanuliwa kwa maana ya kuzidi uwezo wake wa kawaida, nadhani hili ni suala ambalo ni la viwango, tutashauriana na Wizara yenye dhamana ya Uchukuzi, na Wizara yenye dhamana ya Viwanda hili wanapokagua kwa maana ya TBS, magari yanavyoingia basi yazingatie uwezo na sura ya gari, sio ya upanuzi ambao unaathiri watumiaji wengine wa magari, kama alivyoeleza inatanuliwa mpaka site mirror zinaongezwa kiasi ambacho kinaleta usumbufu, ili watakapotoa viwango vile basi askari wetu wa usalama barabarani wanapotimiza wajibu wao wa kuona magari yanayostahili kuwa barabarani basi watasimamia kwa mujibu wa miongozo hiyo.

Mheshimiwa Spika, kuhusu magari ya taka, ambayo amesema yenyewe ni takataka, nadhani nizielekeze mamlaka zinazoyaajiri magari haya kwa Mamlaka za Miji na Majini, wahakikishe kwamba wanateuwa wakandarasi wenye uwezo wa kutoa magari yanayofaa badala ya magari haya ya kubeba taka yenyewe yanakuwa sehemu ya uchafuzi wa miji yetu. Nashukuru.
MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi, pamoja na majibu ya Serikali nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, majibu ya Serikali yanasema kwamba katika mwaka 2020/2021 ni wafungwa 70 tu waliopata msamaha kupitia Bodi za Parole. Sheria ilikuja ili kupunguza mzigo na mrundikano wa wafungwa katika magereza yetu ambapo mpaka sasa takribani wafungwa ni 15,000. Sasa ikiwa kwa mwaka tu bodi inatusaidia kusamehe wafungwa 70. Je, Serikali inaona kweli bodi ziko kazini?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili matokeo haya ya kusamehe wafungwa 70 tu inawezekana kabisa ni kutokana na kwamba vikao hivi vya bodi vya kimikoa ambavyo vinakaa mara nne kwa mwaka yawezekana kabisa iko mikoa vikao hivi havikaliwi.

Je, Serikali inatoa kauli gani kuwezesha vikao hivyo viwe vinakaa mara nne kwa mwaka kama sheria inavyoelekeza?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Chumi kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba Sheria ya Bodi za Parole iliwekwa ili kusaidia kupunguza msongamano wa wafungwa gerezani kwa kuwapa msamaha wale wanaokidhi vigezo. Nikiri kwamba kwa mwaka uliopita 2020/ 2021 vikao vingi havikukaa kwa sababu bodi ziliisha muda wake na bahati mbaya sana mapendekezo yale yalichelewa kumfikia Waziri wa Mambo ya Ndani. Lakini hivi tunavyozungumza bod izote zimeshaundwa mikoa yote, kwa hivi maelekezo yaliyotoka ni kuhakikisha kwamba vikao vinakaa kwa mujibu wa mwongozo ili wafungwa wanaokidhi vigezo waweze kunufaika na uwepo wa bodi hizi.
MHE. DKT. PAULINA D. NAHATO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika mahabusu kuna wanawake ambao wanakuwa wamewekwa mle wakiwa na matatizo mbalimbali na ni wajawazito, sasa wanajifungua wakiwa bado kesi zao hazijasilikizwa.

Je, Serikali ina utaratibu gani wa kuhakikisha wale watoto wanaozaliwa mama zao wakiwa mahabusu hawapati changamoto za kisaikolojia mama zao wanapokuwa pale ndani?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba kuna wakati baadhi ya wafungwa wanakuwa na changamoto, wanakuwa na hali ya ujauzito na kujifungua watoto wakiwa magerezani. Upo utaratibu unaowawezesha wafungwa wa namna hii kupata huduma stahiki ikiwa ni pamoja na hao watoto wanatengwa na kupewa nafasi ya kunyonyeshwa na mama zao kama miongozo ya sekta ya afya inavyoelekeza. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge usiwe na wasiwasi juu ya watu hawa kwa sababu taratibu za kuwalinda zipo. Nakushukuru.
MHE. JONAS W. MBUNDA: Mheshimiwa Spika, namshukuru Naibu Waziri kwa majibu mazuri ya Serikali. Vitendo vya ukatili na unyanyasaji wa kijinsia unaendelea katika nchi yetu, kuna umuhimu mkubwa wa Serikali kuweka mikakati ya kuhakikisha kwamba vituo hivyo vinajengwa kwa nchi nzima.

Mheshimiwa Spika, jengo la dawati la jinsia lililoanza kujengwa katika Wilaya ya Mbinga sehemu kubwa limejengwa kupitia michango ya wadau mbalimbali. Swali langu: Je, Serikali ni lini italeta fedha kuhakikisha kwamba inakamilisha ujenzi wa jengo hilo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunda, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kama nilivyosema katika jibu la msingi, vyanzo vya fedha kwa ajili ya ujenzi wa vituo vya Polisi vikiwemo maeneo ya jinsia na watoto zinatoka Serikalini, kwa wadau wa ndani na wa nje na mashirika mbalimbali. Kwa hiyo, nampongeza Mheshimiwa Mbunda kwa wadau wake kushiriki, lakini tumesema pale ambapo watakuwa wamefika kiwango cha umaliziaji kupitia Mfuko wa Tuzo na Tozo ya Jeshi la Polisi, tutasaidia kukamilisha.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, niko tayari kuwasiliana nawe ili kuona nini kinahitajika kukamilisha kituo hicho alichokirejea.

Mheshimiwa Spika, ahsante.
MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuuliza maswali madogo mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; kwa kuwa matukio haya ya kuungua masoko yamekuwa yakitokea kwa masoko haya ambayo hayajajengwa kisasa kwa sababu ya ukosefu wa miundombinu hiyo ya uzimaji wa moto na kwa kuwa Serikali wamekuwa wakichukua kodi au tozo katika haya masoko kwa sababu kuna wafanyabiashara humo.

Je, sasa Serikali haioni ni muhimu kufikiria namna ya kuwalipa fidia wale wananchi ambao waliumizwa na matukio haya? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili; kwa kuwa hayo masoko ya zamani hayana miundombinu, je, Serikali haioni umuhimu wa kuwa-train vijana miongoni mwao wanaofanya biashara na kuwawezesha wawe na vifaa vyote ili inapotokea majanga haya basi iwe ni raihisi wao wenyewe waweze…

SPIKA: Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Paresso, kama ifuatavyo: -

Mhehimiwa Spika, kuhusu suala la kulipa fidia hili ni suala la kisheria kwa mujibu wa sheria tulizonazo, sasa hatuwezi kusema lolote kwa sababu Bunge lako halijatoa utaratibu kama huo. Hata hivyo, nadhani lililo la umuhimu ni elimu ya kinga dhidi ya majanga haya ili yasitokee kwenye maeneo yetu.

Mheshimiwa Spika, kuhusu swali la pili la mafunzo hilo ni jambo jema na tumeanza kutoa kupitia kwa Scout, lakini vilevile na mifumo yetu ya Serikali za Mitaa ili kuwawezesha watu hawa kujikinga na majanga ya moto au kuzima yanapotokea katika hatua za awali. Nashukuru.
MHE. ZUENA A. BUSHIRI: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Katika Manispaa ya Moshi kumekuwa na matukio mengi sana ya kuungua masoko, lakini jambo la kusikitisha ni kwamba manispaa haina ya magari ya kutosha ya kuzimia moto tunategemea magari kutoka TPC. Hivyo basi husababisha mali za wananchi kupotea. Je, ni lini Serikali itanunua magari ya kuzimia moto katika Manispaa ya Moshi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, nashukuru, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Zuena Bushiri kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Bushiri amekuwa akifuatilia kwa karibu masuala ya Kilimanjaro kuhusiana na Zimamoto, Polisi na mambo yote yaliyo chini Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.

Mhehimiwa Spika, tunafahamu kama tulivyosema katika hotuba yetu iliyosomwa na Waziri wiki iliyopita maeneo mengi yana changamoto ya magari, lakini katika bajeti ijayo tumetenga fedha kwa ajili ya ununuzi wa magari, tutayapeleka kwenye maeneo strategic maeneo ya kimkakati ambayo yamekuwa yanakumbwa na tatizo la namna hii. Hata hivyo, uwepo wa magari tu si suluhisho la kudumu, bali utayari wa wananchi kukabiliana na mambo haya, lakini vile vile kinga dhidi ya majanga ya moto.

Mheshimiwa Spika, nashukuru.
MHE. ASKOFU JOSEPHAT M. GWAJIMA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kuniruhusu niulize swali la nyongeza. Matukio ya ujambazi, watu kupigwa, panya roads kwenye maeneo ya Kawe, Kunduchi na maeneo mengine yamezidi sana. Sasa ni nini tamko la Serikali?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali ya nyongeza la Mheshimiwa Josephat Gwajima, Mbunge wa Kawe, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwanza nimpongeze kwa namna anavyofuatilia suala hili, kuna wakati ameongea kwenye YouTube tumeona, lakini baadhi ya taarifa hazikuwa kweli sana.

Mheshimiwa Spika, kuhusu ujambazi nakupigwa ni ni jukumu la msingi la Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi na hususani Jeshi la Polisi. Nadhani mmemsikia Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, IGP na Kamanda wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam. Tumeahidi kushughulika na vijana hawa, tumesema wakitu-beep sisi tutawapigia. Kwa hiyo, kwa tahadhali hiyo, tunaomba watafute kazi nyingine ya kufanya badala ya uhalifu wanaofanya dhidi ya binadamu kwani hatutauvumilia. Ahsante.
MHE. BAHATI KHAMIS KOMBO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, naomba kuuliza swali moja la nyongeza. Mheshimiwa Waziri kwa nini sasa hatuoni umuhimu wa kuweka kambi ya kudumu katika eneo hili hasa tukizingatia miundombinu iliyopo ni rafiki? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyokwishajibu katika jibu la msingi, eneo hilo ni mahsusi kwa ajili zaidi ya mafunzo ya medani na kwamba kikosi nilichokitaja cha 14KJ, hakiko mbali sana kutoka kwenye eneo hili.

Kwa hiyo haja ya kuanzisha kikosi mahsusi kwenye eneo hilo bado labda pale ambapo itabainika kufanyika hivyo katika siku za mbeleni. Ahsante.
MHE. JUMA OTHMAN HIJA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali na nimeridhika na majibu hayo ya Serikali, lakini nimepata wasiwasi juu ya ufuatiliaji wa kazi hii. Barua ya hati miliki tu imechukua miaka miwili tangu Aprili, 2020 mpaka leo 2022 hakuna majibu yoyote. Je, Mheshimiwa Waziri ananiahidi nini kunitoa wasiwasi huu juu ya ufuatiliaji wa kazi hii?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali moja la nyongeza la Mheshimiwa Hija, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, nakubaliana naye kwamba si kawaida kuchukua muda mrefu namna hii hasa baada ya Jeshi la Polisi kuwa wamelipa Sh.2,200,000 kwa ajili ya kupata hati ya kiwanja hicho. Tutafuatilia kwa karibu na kupitia hadhara hii, nimwombe Kamishna wa Polisi Zanzibar afanye ufuatiliaji yeye binafsi ili kuhakikisha kwamba hati inapatikana, hatimaye ujenzi kwenye eneo hili uweze kuanza. Nashukuru.
MHE. MARYAM A. MWINYI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Kijiji cha Vujini, Wilaya ya Mkoani kina matokeo ya uhalifu sana. Je, ni lini Serikali itajenga kituo cha Polisi katika kijiji hicho ili kupunguza matukio hayo?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimshukuru Mheshimiwa Mbunge kwa ufuatiliaji wa hali ya usalama Zanzibar. Niombe tuendelee kushirikiana ni kweli kwamba baadhi ya maeneo ya Zanzibar ikiwemo kijiji alichokitaja kina hayo matukio ya uhalifu, lakini Jeshi la Polisi linafanya misako na doria kule ambako hakujawa na kituo ili kuhakikisha kwamba usalama unakuwepo. Kwa hiyo tutawasiliana na wenzetu wa upande wa Zanzibar kama maeneo yamepatikana na wananchi wako tayari kutoa ushirikiano, basi kituo hicho kinaweza kuanza kujengwa kwa siku za usoni.
MHE. KABULA E. SHITOBELO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Wilaya ya Ilemela inajenga Kituo cha Polisi kwa nguvu za wananchi eneo la Nyamuhongolo. Aliyekuwa Waziri wa Mambo na Ndani Mheshimiwa Kange Lugola alitoa ahadi ya mifuko 100 ya cement. Je, ni lini Wizara ya Mambo ya Ndani itatimiza ahadi hiyo? (Makofi/Kicheko)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge wa Viti Maalum kutoka Mkoa wa Mwanza kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza niwapongeze wananchi wa Ilemela pamoja na halmashauri yao kwa kuanza ujenzi wa kituo cha Polisi eneo la Nyamuhongolo tunawaunga mkono. Tutafuatilia ikiwa kweli Waziri wetu alitoa ahadi hiyo kuona uwezekano wa kuitekeleza ili isionekane kwamba Serikali inadanganya raia wake. Ahsante. (Makofi)
MHE. ESTHER L. MIDIMU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuuliza swali la nyongeza. Wilaya ya Maswa ni wilaya kongwe, lakini mpaka sasa haina Kituo cha Polisi.

Je, ni lini Serikali itajenga Kituo cha Polisi Wilaya ya Maswa?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Esther Midimu, Mbunge Viti Maalum, Mkoa wa Simiyu, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli tunatambua kwamba Maswa ni wilaya kongwe katika Mkoa wa Simiyu lakini inacho kituo cha polisi ambacho ni chakavu na kwa kweli ni majengo ya kuazima. Tutawasiliana na uongozi wa mkoa ili kupata eneo, hatimaye kuweka mipango ya ujenzi wa vituo vya polisi kwenye maeneo ambayo hayana ikiwemo Wilaya ya Maswa. Nashukuru.
MHE. USSI SALUM PONDEZA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii ya kuuliza swali dogo la nyongeza. Kutokana na kadhia ambayo ipo katika swali la msingi ambalo lililoulizwa, Jimboni kwangu katika Jimbo la Chumbuni nimekuwa nikiahidiwa ahadi kama hizi zaidi ya mwaka wa nne huu sasa hivi na Bunge lililopita Naibu Waziri alisema akija Zanzibar atakuja kwangu, lakini hakuweza kufika. Je, leo hii ananiahidi nini ili tukimaliza Bunge hili aweze kushughulikia vituo vyangu vya Chumbuni? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Nyongeza la Mheshimiwa Pondeza, kama ifuatavyo na kwa kweli kama nimemsikia vizuri: -

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli niliahidi kwenda Zanzibar na moja ya maeneo ambayo ningetembelea ni eneo alilolibainisha, lakini kutokana na ratiba kuwa finyu, nilishindwa kufika. Ipo ahadi ambayo niliitoa kuhusu kumalizia Kisiwa cha Pemba. Nitakapokwenda kule, eneo lako pia nitalitembelea ili kuona changamoto iliyopo. Nashukuru. (Makofi)
MHE. MOHAMED L. MONNI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali. Nina swali moja tu la nyongeza. Kwanza nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali kwa sababu mradi huu umeanza muda mrefu sana. Wilaya yetu ya Chemba miji yake mingi ipo pembezoni na ni ukweli kwamba eneo la mjini lina watu wachache sana. Sasa nataka kujua nini mpango wa Serikali wa kupeleka hii huduma ya Vituo vya Polisi kwenye miji hiyo mikubwa? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Monni, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli Wilaya ya Chemba sehemu kubwa ni Wilaya ya Vijijini na ina miji inayozunguka mji wenyewe wa Chemba, pale panahitajika pia utaratibu wa kuimarisha ulinzi kwenye maeneo haya.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo nimwahidi tu Mheshimiwa Monni kwamba tulikubaliana nitafanya ziara, moja ya lengo ni kuangalia maendeleo ya ujenzi huu, lakini la pili ni kuangalia maeneo ambayo kimkakati yanastahili kupewa huduma za kipolisi ili kuimarisha usalama wa raia na mali zao. Tutakapofika huko Mheshimiwa tutakubaliana ni maeneo gani yapewe kipaumbele. Ahsante.
MHE. BONIPHACE N. BUTONDO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. Wananchi wa Kishapu, Mfuko wa Jimbo wa Mbunge wa Jimbo la Kishapu, lakini pia na wadau wa maendeleo kama Mwadui na wengine wameweza kuchangia jumla ya Sh.53,000,000 kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Polisi cha Wilaya. Je, Serikali ina mpango gani kuhakikisha kwamba inaunga mkono nguvu na jitihada za wananchi na wadau wa maendeleo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa
Spika, naomba kumjibu Mheshimiwa Butondo, Mbunge wa Kishapu kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwanza tumpongeze Mheshimiwa Butondo kwa kufuatilia kwa karibu masuala yanayohusu usalama wa raia na mali zao na uhamasishaji wa wadau kuchangia hizi fedha. Nimwahidi tu kwamba Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kupitia Jeshi la Polisi tuna mpango mkakati wa kuimarisha ujenzi wa Vituo vya Polisi vya Mikoa na Wilaya ambazo hazina kabisa. Kwa hiyo hali ya fedha itakaporuhusu, Wilaya ya Kishapu ni moja ya maeneo yatakayopewa kipaumbele.

Mheshimiwa Spika, nashukuru.
MHE. KILUMBE S. NG’ENDA Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Ujenzi wa Vituo vya Polisi unakwenda sambamba na ujenzi wa makazi ya askari ili kuwawezesha Askari Polisi kupata makazi mazuri na kuweza kufanya kazi zao vizuri. Je, ni upi mpango wa Wizara kusaidia suala la nyumba za askari polisi katika eneo la Kigoma Mjini ambazo ziko katika hali mbaya sana?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Ng’enda,
Mbunge wa Kigoma, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba askari wanahitaji makazi hususan yawe karibu na vituo vya polisi, lakini tunajua pia kwamba makazi mengi hasa vituo vya zamani ni mabovu, ndio maana kipaumbele kimewekwa kwenye ukarabati wa majengo yaliyochakaa. Hata hivyo, tutaendelea kuimarisha ujenzi wa nyumba kwa ajili ya makazi ya askari kadiri tutakavyoweza kupata fedha kutoka Serikalini.

Mheshimiwa Spika, nashukuru.
MHE. NEEMA W. MGAYA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi. Kwa kuwa wananchi wa Kata ya Saja, Kijombe, Uhenga ndani ya Wilaya ya Wanging’ombe wako mbali sana na huduma za kipolisi. Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga Kituo cha Polisi ndani ya Kata ya Saja ili kuwapa unafuu wananchi hawa?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Neema Mgaya, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli Mheshimiwa Neema amekuwa mara kwa mara anaulizia masuala ya ulinzi, lakini jambo moja analonivutia ni kwamba kiwango cha uhalifu Njombe hakilingani na maeneo mengine hasa ile ya mipakani. Kwa hiyo niwapongeze wananchi kwa kuzingatia hilo. Kwa hivyo kadri hali ya fedha itakavyoruhusu tutaendelea kuimarisha kujenga vituo vya polisi katika maeneo yanayohitajika ikiwemo hii Kata aliyoitaja ya Saja kule Njombe.

Mheshimiwa Spika, nashukuru.
MHE. DKT. CHRISTINA C. MNZAVA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Kwa kuwa Kituo cha Polisi cha Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga kilichopo Selamagasi kimejengwa toka enzi ya mkoloni na kimechakaa sana. Je, ni nini mpango wa Serikali kukarabati kituo kile?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa
Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Dkt. Christina Mnzava, Mbunge wa Viti Maalum, Shinyanga, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kama nilivyosema katika majibu ya baadhi ya maswali ya Wabunge, tunatambua uwepo wa uchakavu mkubwa kwa baadhi ya Vituo vya Polisi kikiwemo hiki alichokitaja.

Mheshimiwa Spika, kama tulivyosema alivyosoma hotuba ya bajeti ya Wizara hii mpango wa Serikali kuanza ukarabati wa Vituo vya Polisi na makazi katika mwaka ujao na fedha zimepitishwa, tutaangalia kiwango cha uchakavu ili kuweza kuweka kipaumbele vikiwemo hivi vya Wilaya ya Shinyanga.
MHE. JANETH M. MASSABURI: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu ya Serikali, nina maswali mawili ya nyongeza. Kwa kuwa moja ya sababu inayosababisha ajali nyingi hapa nchini ni wembamba wa barabara zetu, Je, Serikali haioni haja ya kuruhusu magari makubwa ya mizigo kutembea nyakati za usiku? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili; je, ni umri upi unaoruhusiwa kutoa leseni kwa madereva wa magari makubwa? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali ya nyongeza ya Mheshimiwa Janeth Massaburi, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, moja, kuhusu wembamba wa barabara; ni kweli taarifa za utafiti zinaonesha wembamba wa barabara ni moja ya sababu inayosababisha ajali na hili linafanyiwa kazi na wenzetu wa Uchukuzi na Usafirishaji, ambao ni Wajumbe wa Baraza la Taifa la Usalama barabarani na ndio maana mtaona wakati mwingine tunapanua barabara kule upande wa Mbeya na maeneo mengine inavyoonekana imekuwa changamoto.

Mheshimiwa Spika, kuhusu swali la pili, magari ya mizigo yatembee usiku; nadhani sio suluhisho la kudumu kwa sababu tunataka nchi yetu ichangamke kwenye biashara, hatuwezi kuacha kusafirisha wakati wote tukisubiri wakati wa usiku tu.

Mheshimiwa Spika, tunachotakiwa kufanya ni kuimarisha usimamizi wa sheria za usalama barabarani na kuboresha miundombinu ya barabara ili kuwe na usalama wakati wote.

Mheshimiwa Spika, kuhusu umri unaofaa kwa mtu kupewa leseni ya kuendesha magari ya mizigo ni mtu mzima, na kwa Tanzania mtu mzima baada ya miaka 18 amefanya mafunzo na amefuzu kwa vigezo vyote anaweza akapewa leseni ya kuendesha magari.
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Katika Mji wetu wa Dar es Salaam kumejengwa barabara ya njia nane, lakini madereva wengi hawajui matumizi ya barabara ile.

Je, ni lini Serikali itaendesha mafunzo ya kutumia ile barabara kwa sababu unakuta guta limekaa kwenye highway badala ya kukaa kwenye barabara ya upande wa kushoto. Je, Serikali ni lini itatoa mafunzo rasmi?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Zuberi Kuchauka kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kama Wabunge wanafuatilia na wananchi kwa ujumla kazi inayofanywa na chombo chetu cha usalama barabarani (traffic police) wanatoa elimu kupitia vyombo vya habari kuhusu usafiri kwenye kipindi cha UBA, usafiri na uraia Tanzania. Pale hutoa mafunzo mbalimbali juu ya namna barabara zile zinavyotakiwa kutumika. Kwa gari yoyote inayokwenda mwendo mdogo au inaelekea kusimama inatakiwa itembee kushoto zaidi na gari ambayo inakwenda haisimami kwenye vituo vya karibu inatakiwa ipite kule kule ambako wanaita highway. Kwa hiyo elimu hii itaendelea kutolewa ili kuwe na matumizi sahihi ya barabara hizi, nashukuru.
MHE. BAHATI KHAMIS KOMBO: Mheshimiwa Spika, ahsante, kwa kuwa Mheshimiwa Waziri amekiri kuwa kituo hiki hakiwezi kutoa huduma; je, ni mpango gani wa dharura ambao wameuweka ili kulinusuru lile jengo pamoja na wafanyakazi walioko pale?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Bahati Khamis Kombo kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, mpango wa dharura ambao tumekuwa nao ni kutumia Kituo cha Polisi cha jirani cha Mtambile iwapo wataona jengo lile linazidi kuwa hatarishi kwa watumiaji.

Mheshimiwa Spika, lakini tumebaini kuwa kituo hiki kiko umbali wa kilometa nane kutoka pale mkoani; kwa hiyo tutakachofanya ni kuharakisha kujenga kituo hiki mara baada ya bajeti yetu kupitishwa mwezi Julai ili huduma zianze kutolewa kwenye kituo ambacho ni salama zaidi.
MHE. MINZA S. MJIKA: Mheshimiwa Spika, ahsante, je, ni lini Serikali itakarabati majengo ya Kituo cha Polisi Maswa ili yaweze kuendana na hadhi ya Wilaya?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge kutoka Mkoa wa Simiyu kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba Kituo cha Polisi cha Wilaya ya Maswa kweli ni cha siku nyingi na kimechakaa. Maelekezo yetu kwa IGP na wasaidizi wake kule mikoani wafanye tathmini ya kiwango cha uchakavu na kubaini gharama zinazohitajika ni kiasi gani ili kiweze kupangiwa matengenezo kadiri tutakavyopata fedha.
MHE. SALMA R. KIKWETE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana, kwa kuwa Mheshimiwa Naibu Waziri alikuja Jimboni kwangu Mchinga na kuona hali halisi ya Kituo kile cha Mchinga na Gereza la Kingurungundwa; je, ni lini vituo vile vitajengwa?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Salma Rashid Kikwete kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, tunakiri kwamba Kituo cha Mchinga na Gereza la Kingurungungwa kama alivyotaja ni chakavu sana na tayari tumeingiza kwenye mpango wa bajeti wa mawaka 2023/2024. Mara tutakavyoidhinisha bajeti, fedha zimetengwa kwa ajili ya ukarabati wa Kituo cha Mchinga na ujenzi actually wa kituo kipya na ukarabati wa Gereza la Kingurungundwa.
MHE. OMAR ALI OMAR: Mheshimiwa Spika, ahsante sana; nami nataka niulize swali moja la nyongeza.

Mkoa wa Kaskazini Pemba kituo cha polisi kiko katika hali mbaya; je, Serikali inampango gani wa kukitengeneza kituo hicho?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Omar Omar kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli nilitembelea Pemba na nilibaini kituo kile kweli ni chakavu. Kinachotia faraja ni kwamba mkoa umeshabaini eneo la kujenga kituo kipya cha ngazi ya mkoa. Katika bajeti yetu ya mwaka ujao ni mpango wa Serikali kuanza ujenzi wa Kituo kipya cha Polisi cha Mkoa wa Kaskazini Pemba.
MHE. VINCENT P. MBOGO: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali la nyongeza. Kwanza niishukuru Serikali kwa sababu niliomba fedha kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Polisi Kala Kijiji cha Mpasa ambapo kuna biashara kubwa sana ya Samaki inafanyika. Ukanda wa Ziwa Tanganyika kuna uhalifu wa mara kwa mara hasa Kata ya Kizumbi;

Je, ni lini Serikali itajenga kituo cha polisi Kata ya Kizumbi?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Vincent Paul Mbogo Mbunge wa Nkasi Kusini kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, tunashukuru kwamba Mheshimiwa Mbogo amekuwa akitoa ushirikiano kwa Wizara yetu na wakati mwingine kupitia halmashauri yake amekuwa akitenga maeneo kwa ajili ya ujenzi wa kituo hiki. Nimuahidi tu, baada ya kumaliza kituo hiki kadri hali ya fedha itakavyoruhusu maeneo tete kama ya Kizumbi tutaweza pia kuyajengea kituo cha polisi ngazi ya kata. Nashukuru.
MHE. RAMADHAN SULEIMAN RAMADHAN: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kutokana na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri kwenye swali langu la msingi nina swali moja la nyongeza.

Kwenye jibu lake la msingi amekiri kwamba upo uhaba wa Askari Polisi katika Mkoa wa Kusini. Je, ni ahadi gani ya Serikali kwamba watatoa kipaumbele kwenye hizo ajira 4,103 alizozitaja maalum kwa ajili ya Mkoa wa Kusini Pemba? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Ramadhan Suleiman Ramadhan Mbunge wa Chakechake kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kama nilivyosema kwenye jibu la msingi ahadi yetu ni kwamba hawa wahitimu wa mafunzo ya Jeshi la Polisi 4,103 watagawiwa maeneo yote yenye upungufu ikiwemo Mkoa wa Kusini Pemba. Kama tulivyokubaliana Mheshimiwa Ramadhan nitakwenda huko baada ya Bunge hili ili kuangalia pamoja na mambo mengine upungufu huo na kiwango kinachohitajika kusaidiwa. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. HAJI MAKAME MLENGE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Mbali na majibu mazuri ya Serikali naomba niulize masuala mawili ya nyongeza. Kwa kuwa watoa hati ni wanadamu na wanadamu wana kawaida ya wakati mwingine kukosea. Inapotokea kukosea wakati wa kutoa hati (printing error) na wakati huo wale wapewa hati wanakuwa wameshalipa. Kwa nini idara inawalipisha tena watu wale wakati wao Uhamiaji ndiyo wamekosea?

Mheshimiwa Spika, swali la pili Je, Serikali ipo tayari kutoa tamko kupitia Waziri la kwamba suala hili wapewa hati hawatalazimika kulipishwa mara ya pili badala yake gharama hizi wachukue Idara? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Haji Makame Mlenge, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba kuna wakati makosa hufanyika lakini makosa yakichunguzwa yakionekana aliyechangia kufanya makosa haya ni yule mwombaji kwa sababu ya taarifa alizojaza basi mwombaji huyo lazima atalipa. Lakini ikiwa itathibitika kwamba makosa hayo yanatokana na waandaaji ambao ni watumishi wa Idara ya Uhamiaji basi tutaangalia uzito wake ili waweze kufidia wenyewe utoaji wa hati hizo mpya. Nashukuru.
MHE. OMAR ISSA KOMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri, lakini nina swali dogo tu la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni awamu ya pili hii kuambiwa tumetengewa fedha kwa ajili ya ukarabati wa kituo hiki. Na kwa kuwa Mheshimiwa Naibu Waziri amekiri kwamba kwa kweli uchakavu ni wa hali mbaya sana. Tunaomba commitment ya Serikali; kama ni kweli kituo hiki kitajengwa kwenye bajeti ya mwaka unaokuja, ni quarter ipi wamepanga kufanya ukarabati wa kituo hiki?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Kombo kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, atakumbuka Mheshimiwa Kombo kwamba nilitembelea Kituo hiki cha Micheweni nikajionea hali halisi; na kwa msingi huo tukakubaliana ndani ya Wizara na Jeshi la Polisi kutenga fedha. Atakumbuka kwamba miaka iliyopita hata kama alipewa ahadi hakuna fedha iliyotengwa lakini mwaka ujao namhakikishia fedha imetengwa na tutahakikisha tutakapopata fedha za maendeleo basi kituo hiki tutakipa kipaumbele, nashukuru.
MHE. DEUS C. SANGU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Kituo cha Polisi Mji Mdogo wa Mpui na Kaengesa vimechakaa sana na vinahudumia kata 11.

Je, ni lini Serikali inakarabati vituo vya polisi katika mji mdogo wa Kaengesa na Mpui?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Deus kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake ameliuliza kwa ujumla, kwamba ni lini Serikali itakarabati vituo vilivyochakaa kama ilivyo cha kwakwe cha mji mdogo alioutaja. Nimuahidi tu kwamba pale tutakapokuwa tunapata fedha na vituo hivi vikiingizwa kwenye bajeti basi vitafanyiwa ukarabati. Atakumbuka kwamba mwaka huu maeneo mengi ikiwemo hata Zanzibar na Bara baadhi ya vituo vimekarabatiwa. Kwa hivyo nimwahidi tu kwamba kadri hali ya fedha itakavyoruhusu kituo chake pia kitafanyiwa ukarabati, nashukuru.
MHE. ALLY M. KASSINGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipatia nafasi ya swali la nyongeza. Wananchi wa Kata ya Nanjirinji wakishirikiana na mimi Mbunge wao wamejenga na kukamilisha kituo cha polisi ili kupunguza uhalifu mkubwa katika eneo la Nanjirinji. Je, Serikali iko tayari sasa kupitia Wizara ya Mambo ya Ndani kuelekeza uongozi wa polisi Mkoa wa Lindi wakakague kituo hiki wafanye tathmini na hatimaye kupanga askari wakafanye kazi pale?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Ally Kassinge kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Kassinge kwa kujumuika na wananchi wake wakajenga na wakakamilisha kituo cha polisi kama ilivyoelezwa hapa Bungeni. Ni maelekezo yangu kwa IGP kupitia Kamanda wake wa Polisi wa Mkoa wafanye ukaguzi wa kituo hiki ili kama kina kidhi haja kiweze kupangiwa askari na kuanza kuwahudumia wananchi wa eneo hilo, nashukuru.
MHE. JOSEPH G. KAKUNDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana; Wilaya ya Skonge tangu ianzishwe mwaka 1996 OCD amejibanza kwenye vijumba ambavyo vilianzishwa na Mtemi Haruna Msagila Lugusha, 1957, havitoshi na havifai;

Je, Wilaya ya Skonge itajengewa lini kituo cha polisi cha Wilaya chenye hadhi?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Joseph Kakunda kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza tuungane naye kwamba baadhi ya majengo yanayotumika na polisi si yale yaliyojengwa na Serikali bali ni yale yaliyotolewa na wadau waliokuwa kwenye maeneo hayo miaka kadhaa iliyopita. Sasa kupitia Bunge lako Tukufu nimwombe IGP kupitia RPC wake wa Mkoa wa Tabora waweze kufanya tathmini ya eneo hilo la kibanda anachosema kinakaliwa na OCD wa Sikonge kuangalia kiwango gani cha ukarabati tunahitajika kufanyika ili tukitengee fedha kikarabatiwe kikidhi mahitaji ya OCD, nashukuru.
MHE. STANSLAUS S. MABULA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru, naomba kumuuliza Mheshimiwa Naibu Waziri, kwamba maeneo mengi yaliyojengwa vituo vya polisi ikiwemo kituo kikuu cha polisi pale Nyegezi ambacho kitasaidia maeneo mengi sana, kwa maana ya ukanda wa kata za Buhongwa, Mkolani, Ruanima, Nyegezi, Luchelele pamoja na Mkolani yenyewe.

Je, ni lini sasa Serikali itafanya ukamilishaji wa kituo hiki?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mabula kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, nielekeze Mkuu wa Polisi Nchini (IGP) Wambura kupitia Kamanda wake wa Mkoa wa Mwanza wapiti kituo hiki cha Nyegezi alichokieleza Mheshimiwa Mbunge kuona kiasi gani cha umaliziaji unaotakiwa kufanyika ili gharama zake ziweze kutengewa fedha na kikamilishwe ili kiweze kuwanufaisha wananchi wa maeneo yaliyotajwa.
MHE. ABDUL-HAFAR IDRISSA JUMA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa majibu mazuri. Kwa niaba ya Mheshimiwa Kassim sasa mawasiliano haya ya Serikali yatakwisha lini, ikizingatiwa Serikali yote ipo Dodoma, ili mchakato huu uanze kufanya kazi. Ninashukuru.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Abdul-hafar kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba Serikali ipo Dodoma lakini taasisi zenye kutoa vitambulisho siyo zote ziko Dodoma, ambacho tunaweza kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge ni kwamba mazungumzo yanaendelea Wizara itafuatilia na ple ambapo kutakuwa na mkwamo basi ngazi za Wizara tutazungumza kwa sababu imeonekana nia ya Watanzania ni kupunguza idadi ya vitambulisho ambavyo mtu anabeba ili kuwa na kitambulisho kimoja chenye taarifa zote. Ninakushukuru.
MHE. SIMAI HASSAN SADIKI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, haki ya Kitambulisho cha Mtanzania ni haki ya kila raia wa nchi hii.

Je, Serikali haioni haja ya kuambatanisha kitambulisho cha Mtanzania na cheti cha kuzaliwa mara tu baada ya mtoto kuzaliwa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, katika swali la msingi tumesema umuhimu huo upo lakini kuhusu cheti cha kuzaliwa hili litakuwa la kisheria lazima sheria yetu ya NIDA irekebishwe Sheria ya Kitambulisho cha Taifa kwa sababu sheria ile inatambua mtu anayestahili kupewa kitambulisho ni yule aliyefikisha miaka 18 na kuendelea, lakini anayezaliwa leo anastahili kupata kitambulisho cha kuzaliwa. Kwa hivyo tutajitahidi katika marekebisho hayo kuweza kulijumuisha suala ambalo Mheshimiwa Mbunge amelihoji. Nashukuru.
MHE. VENANT D. PROTAS: Mheshimiwa Spika, ahsante. Je, Serikali haioni haja ya kuondoa matumizi ya Kitambulisho cha Taifa wakati Serikali haijajipanga kuwapa wananchi wake vitambulisho na kuondoa usumbufu unaowapata wananchi wake?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Venant Daud kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, hoja anayojaribu kuihoji inatokana tu na changamoto tulizozipata. Jambo linalotia faraja ni kwamba katika bajeti hii tunayoendelea kuitekeleza, Serikali imeweza kutoa fedha zote zaidi ya Bilioni 40 zilizokuwa zinahitajika ili kumlipa Mkandarasi na hatimaye aweze kuzalisha vitambulisho.

Mheshimiwa Spika, nimpe assurance Mheshimiwa Mbunge kwamba mara vitambulisho vitakapozalishwa Watanzania wote ambao walikuwa wako kwenye backlog hawajapata vitambulisho watapata vitambulisho vyao. Ninakushukuru.
MHE. REHEMA J. MIGILLA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kuniona.

Mheshimiwa Spika, wananchi wa Ulyankulu ambao walipatiwa uraia wana cheti cha NIDA, mara kwa mara wamekuwa wakiambiwa watanyang’anywa vitambulisho vyao vya NIDA.

Je, ni sababu zipi ambazo zinapelekea wananchi hawa kutishiwa kunyang’anywa vitambulisho vyao vya uraia?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Migilla kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, hatuna utaratibu wa kumnyang’anya kitambulisho mtu aliye na sifa za kupata kitambulisho hicho, sasa kama pana mamlaka au Afisa yeyote wa Serikali anawatishia kwamba atawanyang’anya, tuombe tu Mheshimiwa Mbunge atupatie hizo taarifa ili tuweze kuzifuatilia kwa umakini kuona sababu na nini kilizosababisha watishiwe hivyo, lakini utaratibu huo haupo. Ninashukuru. (Makofi)
MHE. MOHAMED ABDULRAHMAN MWINYI: Mheshimiwa
Mwenyekiti, kwanza niipongeza sana Serikali kwa hatua ambayo wamechukua na nina masuala mawili tu ya kuuliza.

(a) Kwa kuwa fecha zilitolewa Desemba, 2022 na mpaka leo imefika hatua ya kusafisha kiwanja hicho, je, ni tatizo gani ambalo linasababisha hilo?

(b) Ni lini Mheshimiwa Waziri atakwenda kuangalia ujenzi huo?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Mohabed Mwinyi kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, moja kuhusu tatizo la kuchelewa, ni kweli umetokea uchelewaji baada ya kubaini kwamba utaratibu uliokuwa umewekwa wa kutumia force account ulikosewa na baadhi ya watekelezaji wa jukumu hili. Serikali kupitia Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi alianza mfumo wa kuwaelimisha Makamanda wote wa Polisi wa Mikoa juu ya mfumo huo unaofanya kazi ili wauzingatie wakati wa utekelezaji, kwa hiyo ndio sababu ya kuchekelewesha. Sasa hivi wote umeshapitishwa ndiyo maana utekelezaji unaendelea.

Mheshimiwa Mwenyekiti,kuhusu lini nitakwenda, nimuahidi tu Mheshimiwa Mbunge kwamba tunao utaratibu wa kufatilia utekelezaji wa miradi ya maendeleo unaofanywa na maofisa wetu lakini na sisi viongozi wa kisiasa tunapata nafasi tunaenda huko. Kwa hiyo itakapokuwa pengine Bunge hili linamalizika kabla ya mwezi Agosti Mbunge akiwa tayari niko tayari kuongozana nae kuangalie maendeleo ya ujenzi huo. Nashukuru sana.
MHE. FRANCIS K. NDULANE: Mheshimiwa Mwenyekiti, kituo chetu cha Polisi cha Somanga kimechakaa sana.

Je, ni lini Serikali itajenga Kituo kipya katika eneo hilo?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Ndulane kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunatambua kwamba ni kweli kituo cha Somanga ni cha muda mrefu na kimechakaa kama ilivyokuwa vituo vingi maeneo mbalimbali nchini. Tutakachofanya kabla ya kuki-condemn kituo hiki kwamba hakifai kwa matumizi ya binadamu tutaenda kufanya tathmini ya uchakavu wa kituo hiki. Iwapo itaonekana kuwa gharama za ukarabati ni kubwa au zinakaribia kulingana na gharama za ujenzi kitaingizwa kwenye mpango wa ujenzi wa kituo kipya, nashukuru.
MHE. DEO K. SANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kuniona. Kwa kuwa Kituo cha Makambako kimewakuta wananchi na wananchi walitoa eneo hilo kwa roho nyeupe;

Je, ni lini sasa Wananchi hao watalipwa ela zao kwa sababu mwaka jana Rais alipopita mwezi wa nane aliahidi na Mheshimiwa Naibu Waziri na Waziri alikuwepo, ni lini watalipwa wananchi hao ili wasiteseke fedha zao?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Deo Sanga kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, natambua kweli kwamba kituo cha Makambako kimekuta wananchi na uthamini ulishafanywa, na kuna takriban shilingi milioni 240 kwa ajiri ya kuwalipa fidia na kwa maagizo ambayo yameshatolewa na Mheshimiwa Rais wetu. Maelekezo ya Mheshimiwa Rais ni ahadi ambayo lazima itekelezwe. Nimuahidi tu Mheshimiwa Mbunge kwamba tutafatilia Wizara ya Fedha ili kupata fecha hizo za kulipa fidia ili wananchi hawa waweze kupata haki yao wapishe ujenzi wa kituo hiki, nakushukuru sana.
MHE. MICHAEL C. MWAKAMO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. pamoja na majibu mazuri ya Serikali, naomba niulize maswali mawili madogo ya nyongeza.

Swali la kwanza, kwa kuwa gari analolizungumza Mheshimiwa Naibu Waziri ni gari aina ya lori na kituo kile kina shughuli nyingi za kipolisi kwa sababu eneo la Mji wa Mlandizi limejengeka. Je, Serikali haioni iko haja sasa ya kuwapelekea gari dogo litakaloendana sawa na kasi ya kukabiliana na uhalifu katika Mji ule?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili jengo la Kituo cha Polisi Mlandizi linatumika kwa ajili ya OCS pamoja na OCD, sasa kwa kuwa jengo hili ni dogo hawaoni sasa ni muda muafaka wa kutafuta eneo lingine kuzitofautisha ofisi hizi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Mwakambo Michael, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, mosi, tunatambua kwamba lori kwa kweli lina changamoto kwenye ufuatiliaji wa doria hasa kwenye vichochoro na njia kama hizo, lakini kwa shughuli nyingi za kiuchumi zinazoendelea pale Mlandizi wanayo kweli haki ya kupata gari ndogo. Naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mwakambo pamoja na Wabunge wote kwamba Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kupitia Jeshi la Polisi, karibuni itapata magari kwa ajili ya kuwezesha ofisi zote za ma OCD kupata gari ndogo kuwezesha kufanya kazi zao kwa ufanisi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu jengo hili, tumeeleza ofisi zitakazoongezeka kama kwenye jibu langu la msingi tulivyosema lakini kutokana na hoja kwamba eneo ni dogo, namwomba Mkurugenzi, kwa maana ya Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha, kutafuta eneo, na pale litakapokuwa limepatikana, sisi always tutakuwa tayari kushirikiana na Halmashauri hiyo kuimarisha majengo yanayotakiwa kwenye kituo kile, nashukuru.
MHE. MARYAM AZAN MWINYI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi niulize swali la nyongeza, nina swali moja la nyongeza. Kwanza napenda niipongeze Serikali kwa majibu yake mazuri. Je, Waziri yuko tayari kwenda kukikagua Kituo hicho cha Polisi ambacho Waziri amesema kitamalizika Agosti, 2023?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa
Spika, nimewahi kukitembelea kituo hiki na kuona kasi ya ujenzi unavyoendelea, inanitia moyo kwamba inaweza ikamalizika. Hata hivyo, kwa vile hakuna zida mbovu, niko tayari kuongozana na Mheshimiwa Mbunge baada ya Bunge kukamilika ili kwenda kuangalia maendeleo ya ujenzi na kujiridhisha kwamba kitakamilika katika muda uliopangwa, nashukuru.
MHE. ESTHER L. MIDIMU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuuliza swali la nyongeza. Wilaya ya Maswa ni wilaya Kongwe katika Mkoa wa Simiyu, lakini haina Kituo cha Polisi kabisa. Ni lini Serikali itajenga Kituo cha Polisi katika Wilaya ya Maswa?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa
Spika, tunatambua uwepo wa baadhi ya wilaya kongwe kama ilivyo Maswa ambazo hazina Kituo cha Polisi. Mara kadhaa tumetoa ahadi hapa, naomba nimuahidi Mheshimiwa Mbunge kwamba katika bajeti zetu zinazofuata tutaangalia uwezekano wa kutenga fedha kwa ajili ya kuanza wa ujenzi wa Kituo cha Polisi ngazi ya wilaya katika Wilaya ya Maswa, nashukuru.
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Wilaya ya Liwale pamoja na kwamba ni ya mwaka 1975 haijawahi kuwa na jengo la Kituo cha Polisi, lakini Serikali walituahidi kutujengea Vituo vya Polisi katika Kata za Kimambi, Lilombe na Kibutuka. Je, ni lini Serikali itatekeleza ahadi hii?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa
Spika, tumewahi kueleza hapa na naomba nirudie kwamba katika wilaya zetu hasa kwenye kata, mpango wa Serikali ni ku- support pale ambapo juhudi zimeoneshwa na wananchi na halmashauri zao za ujenzi wa vituo hivyo. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge akitusaidia kupitia Mfuko wa Jimbo, akaanzisha ujenzi, kwa vyovyote vile IGP kupitia fungu lake atatoa fedha za kusaidia kukamilisha vituo vyake. Kwa hiyo, nimtie moyo, hizi kata tatu ambazo zina changamoto za uhalifu, tuanze kwenye ngazi ya halmashauri na Mfuko wa Jimbo ili ngazi ya wizara kupitia Jeshi la Polisi liweze kusaidia kukamilisha, nashukuru.
MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA: Mheshimiwa Spika, nakushuru. Wananchi wa Kata ya Mazinde kwa kushirikiana nami Mbunge wao tumeshirikiana kujenga Kituo cha Polisi mpaka boma limekamilika. Je, ni lini Serikali itatusaidia kumaliza Kituo hicho cha Polisi?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa
Spika, kupitia bajeti ya mwaka 2023/2024, tutaona uwezekano wa kupata fedha kutoka Mfuko wa Tuzo na Tozo kukamilisha Kituo cha Mazinde ambacho Mheshimiwa Mbunge amekizungumzia.
MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Spika, ahsante. Polisi wote nchini wanapitia Shule ya Polisi Moshi inayojulikana kama CCP, shule hiyo ni chakavu, mbovu, barabara hazipitiki na wakija wageni wanapitishwa kwenye geti kubwa na sio hili la Moshi Sekondari. Je, ni lini sasa Serikali itakarabati chuo hicho?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa
Spika, nimekitembelea Chuo cha Polisi Moshi na kubaini uchakavu anaousema na kupitia ziara yangu tulikubaliana na uongozi wa Manispaa ya Moshi kupitia Mamlaka ya Barabara za Mjini na Vijijini (TARURA) kwa sababu chuo hiki kipo kwenye himaya yake waanze kutenga fedha. Nimtie moyo Mheshimiwa Mbunge kwamba, barabara kuu inayoingia tayari ukarabati umefanyika na tutaendelea kufanya ukarabati huo kwenye barabara zote nyingine zilizopo kwenye chuo hicho, nashukuru.
MHE. KUNTI Y. MAJALA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa nafasi. Kituo cha Polisi Kwamtoro ni kituo cha majengo ya mkoloni, kimechakaa, hakitamaniki, hakithaminiki. Je, ni lini Serikali itatenga fedha kwa ajili ya ukarabati wa kituo hicho?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa
Spika, kulingana na upatikanaji wa bajeti tunaendelea kuvikarabati Vituo vyote vya Polisi vilivyochakaa. Hiki cha Kwamtoro pia tutakiingiza kwenye mpango wa matengenezo kadri tutakavyopata fedha kutoka Serikalini, nashukuru.
MHE. DAVID M. KIHENZILE: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa fursa. Kutoka Makambako mpaka unaingia Mafinga hali ya usalama sio nzuri kwa sababu hakuna Kituo cha Polisi na tayari jitihada zimekwishaanza kufanywa na wananchi kwa kutenga eneo na hata mimi mwenyewe Mbunge kupeleka cement. Je, Wizara iko tayari kupeleka fedha kuhakikisha kwamba Kituo cha Polisi cha Nyololo kinakamilika?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa
Spika, kwa jitihada ambazo zimekwishafanywa na Mheshimiwa Mbunge pamoja na wananchi wake wizara itamuunga mkono kukamilisha kituo hicho, nashukuru.
MHE. REGINA N. QWARAY: Mheshimiwa Spika, ahsante. Gari lililopo katika Kituo cha Polisi Magugu ni chakavu. Je, ni lini Serikali itawapatia kituo hicho gari ili kurahisisha utendaji kazi?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa
Spika, tunao mpango katika Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kupitia Jeshi la Polisi kununua magari na kuzipatia Wilaya zote za Kipolisi nchini Tanzania. Naamini gari hiyo itakapopatikana, basi magari yaliyopo kwenye ngazi ya wilaya yanaweza kupelekwa kwenye kituo hicho kama kutaonekana kuna uhitaji mkubwa wa gari, nashukuru.
MHE. HASSAN S. MTENGA: Mheshimiwa Spika, Jimbo la Mtwara Mjini ndio kwenye Kituo Kikuu cha Polisi. Kituo hicho kilijengwa toka mwaka 1962, kwa sasa kituo hicho ni chakavu mno na inapelekea Askari kufanyia kazi kwenye mwembe. Je, ni lini Serikali itakwenda kufanya ukarabati kwenye kituo hicho?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa
Spika, tunatambua hali ya uchakavu wa Kituo cha Polisi ngazi ya Wilaya Mtwara. Hata hivyo, katika bajeti yetu ya mwaka 2023/2024, fedha zimetengwa za kuanza kufanya ukarabati kwenye kituo hicho. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge awe na matumaini kwamba mwaka 2023/2024 kituo hicho kitakarabatiwa, nashukuru.
MHE. JONAS V. ZEELAND: Mheshimiwa Mwenyekiti ahsante. Naomba niulize maswali mawili madogo ya nyongeza.

Swali la kwanza; kwa kuwa yapo malalamiko kwa baadhi ya askari wako kutotenda haki ikiwemo kuchukua rushwa na kuziharibu hizi kesi za migogoro ya wakulima na wafugaji, Mheshimiwa Waziri yupo tayari kuongozana nami baada ya Bunge hili la Bajeti kwenda kuwasikiliza wananchi wa Mvomero? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; kutokana na jiografia yetu ya Mvomero, tuna uhaba mkubwa wa vituo vya polisi. Je, Serikali ina mpango gani sasa wa kutuongezea Vituo vya Polisi lakini pia kuvimalizia Vituo vya Polisi vilivyoanza kujengwa kwa nguvu za wananchi kikiwemo Kituo cha Polisi Turiani na Kituo cha Polisi Mvomero? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu uwepo wa madai ya rushwa na kwamba Mheshimiwa amependekeza niende Mvomero pamoja naye kuwasilikiliza wananchi, hilo halina shida Mheshimiwa tutaongozana. Hata hivyo pale zinapokuwepo tuhuma za rushwa ushauri wangu wananchi waelekezwe kwenda kwenye vyombo vinavyosimamia sekta hiyo. Tunayo TAKUKURU kila Wilaya, kila Mkoa na Taifa, lakini kama inashindikana kuna Kamati ya Usalama inayoongozwa na Mkuu wa Mkuu wa Wilaya wanaweza wakapeleka manung’uniko huko.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia wapo Wakuu wa Mapolisi hawa wadogo wanaokuwa kwenye site kama OCD wanaweza pia kuwasikiliza, lakini nipo tayari kuungana naye kwenda kuwasikiliza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, juu ya swali la pili la kuongeza Vituo vya Polisi kwa sababu Wilaya ni pana, nitakapokwenda kwenye kikao hicho tutaweza kuviangalia vituo viwili vinavyoendelea kujengwa na kupata mapendekezo yako ni wapi kwingine wanapenda viongezwe ili viweze kuingizwa kwenye mipango yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru.
MHE. ALLY M. KASSINGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipatia nafasi ya swali la nyongeza katika Jimbo la Kilwa Kusini, Kata za Nanjilinji, Kikole na Kiranjeranje bado migogoro ya wakulima na wafugaji inaendelea. Je, ni nini jukumu la Jeshi la Polisi kuzuia na kukomesha kabisa migogoro hii badala ya kuendelea na kesi ambazo hatima yake inakuwa si nzuri sana? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu uwepo wa migogoro katika eneo la Kilwa alilotaja Mheshimiwa Mbunge ni kweli tunafahamu na kuna maelekezo yalitolewa na Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa Wakuu wote wa Mikoa ambao ni Wenyeviti wa Kamati za Usalama na wadogo zao kwa maana ya Wakuu wa Wilaya, Wenyeviti wa Kamati za Usalama ngazi ya Wilaya kuwa na mipango ya usimamizi wa matumizi bora ya ardhi pamoja na kuwapanga wakulima na wafugaji kuepuka mwingiliano unaosababisha migogoro.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kwa Jimbo la Kilwa na hizo kata tatu alizozitaja Mheshimiwa Mbunge nishauri tutumie infrastructure kwa maana ya miundombinu iliyopo ya upatanisho, Jeshi la Polisi kupitia Kitengo cha Polisi Jamii wanaendelea kuelimisha wananchi juu ya kupunguza migogoro isiyokuwa ya lazima kama hii. Hata hivyo, tuwaombe wataalam wetu wa ngazi za Serikali za Mitaa ambao hufanya uthamini wa uharibifu wa mazao kabla Polisi hawajachukua hatua za kurejesta kesi Mahakamani ili watimize wajibu wao ipasavyo, kwa sababu wakati mwingine wanaona inachelewa kumbe ni kutokana na kuchelewa kwa zile tathmini za wenzetu. Vinginevyo tuendelee kuwaelimisha wakulima na wafugaji, wote ni Watanzania, waishi kwa maelewano kila mmoja akitimiza wajibu wake, ahsante sana.
MHE. NICHOLAUS G. NGASSA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi. Naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mji wa Igunga ni moja ya miji inayokua kwa kasi kubwa sana kutokana na kuongezeka kwa shughuli za kiuchumi na kuongezeka kwa idadi kubwa ya watu.

a) Je, Serikali, kwa kutowapatia mpaka sasa gari la zimamoto haioni ni kuhatarisha maisha ya raia na mali zao endapo itatokea janga la moto?

Mheshimiwa Naibu Spika, mafuta ni moja ya kimiminika hatarishi sana duniani, na sisi Igunga tunashughuli za bomba la mafuta zinaendelea pale na kuna camp kubwa sana ambapo tunaona itakuwa hatari sana endapo shughuli hizi zitaendelea na hatutakuwa na gari la Zimamoto endapo kutatokea na changamoto yoyote ya mlipuko au maafa.

b) Je, Serikali inachukua hatua gani au mkakati gani kwa ajili ya kukabiliana na jambo hili?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika,napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika,kwanza tunatambua kwamba kuna uhaba wa magari ya zimamoto, tumekiri hapa ; na kwamba tumeanza utekelezaji wa bajeti kwa kupunguza tatizo hili kwenye maeneo ambayo hayana, lakini yote yanategemea upatikanaji wa fedha. Hata hivyo, tumesema kwenye jibu la Msingi. Igunga kutokana na hizo shughuli nyingi za kiuchumi pamoja na hilo bomba la mafuta linalopita kwenye eneo lake, tunalipatia kipaumbele kwa mwaka ujao ili wapate gari la kuzimia moto, nashukuru.
MHE. FESTO R. SANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Swali langu, Mkoa wa Njombe na halmashauri mbalimbali nchini ikiwemo Makete wanalipa ushuru wa fire lakini maeneo haya hayana gari za fire. Ni ipi kauli ya Serikali kwa halmashauri zote nchini ambazo haziona gari za fire na wanalipa ushuru wa fire iktu ambacho kwa wnanchi kimekuwa ni kero na wamekuwa wakituuliza maswali mengi?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika,ushuru unaolipwa si kwamba ndio unaokwenda kununua gari za zimamoto kwa sababu ni ushuru kidogo sana ukilinganisha na gharama za gari hizi; gharama za gari hizi hutegemea bajeti ya Serikali. Hata hivyo fedha zile zinalipwa kuwezesha Jeshi la Zimamoto na Ukoaji kutoa elimu ya namna ya kujikinga na majanga ya moto na majanga mengine ya kibinadamu kwenye maeneo hayo. Nikuahidi Mheshimiwa Mbunge na Wabunge wote, kwamba kipaumbele cha Serikali kuanzia mwaka ujao ni kupata fedha ili kuweza kuzipatia wilaya zote gari za zimamoto kwa kadri fedha zitapopatikana, ahsante.
MHE. DEODATUS P. MWANYIKA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kunipa nafasi. Mkoa wa Njombe una majanga makubwa sana upande wa misitu, na misitu ndio uchumi. Anaweza kutoa kauli ya Serikali kuhusiana na kutoa kipaumbele kwa mkoa huu muhimu na Mji wa Njombe? (Makofi)
NAIB WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, nimuahidi kwamba itaendelea kutoa kipaumbele kama ambavyo sasa hivi ina gari mbili, moja iko Njombe Mjini nyingine liko Makambako.

Tutaendelea kuimarisha utoaji wa gari hizi ili hatimaye kua- address matatizo ya majanga yakijitokeza katika mkoa huo, nashukuru.
MHE. MARTHA F. MARIKI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Zaidi ya miaka kumi Mkoa wa Katavi umekuwa hatuna gari la Zimamoto.

Je ni lini Serikali italeta gari la Zimamoto katika Mkoa wa Katavi?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika,Mkoa wa Katavi unalo gari moja la zimamoto lakini tunatambua kwamba ni bovu na liko kwenye matengenezo. Tutakachofanya ni kuharakisha matengenezo ya gari hili, ili angalau liweze kurejeshwa Katavi liweze kutoa huduma stahiki, nashukuru.
MHE. MASACHE N. KASAKA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali, lakini kiasi cha fedha ambacho kimetengwa takribani Milioni 50 tunashukuru, isipokuwa kiasi hiki ni kidogo sana kuweza kumaliza gereza hili. Swali la kwanza; kwa kuwa Bajeti ya Wizara ya Mambo ya Ndani bado haijasomwa, je, hatuwezi tukaongeza hizi fedha ili gereza hili liishe kwa wakati?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; kwa kuwa gereza hili linakwenda kuisha, sasa ni muda muafaka kuweza kupata vitendea kazi vya ofisi pamoja na gari. Je, Serikali inatuahidi nini ili tuweze kupata vitendea kazi hivyo?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli tunatambua ni kiasi kidogo Mheshimiwa Mbunge, lakini tulisema pamoja na ufinyu wa bajeti angalau gereza lile uendelezaji wake usisimame. Hata hivyo, nimuahidi tu kwamba kipaumbele baada ya mwaka huu 2023/2024 mwaka unaofuata 2024/2025, tutaongeza fedha za kutosha ili angalau ujenzi wake uwe wa kasi kubwa zaidi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu umuhimu wa kuwepo vitendea kazi, ofisi tumesema inaendelea kujengwa na gari tutapeleka kutokana na bajeti yetu itakavyoruhusu, ahsante sana.
MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Gereza la Karanga lililopo Mkoani Kilimanjaro ni katika yale magereza ya awali sana Tanzania. Miundombinu yake ni chakavu na hasa nyumba za wafanyakazi. Je, ni lini Serikali itatupa kipaumbele kukarabati gereza hilo?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, Gereza la Karanga tunatambua ni chakavu na ni la muda mrefu, lakini ni gereza ambalo angalau lina miradi ya maana ikiwemo hiki Kiwanda cha Viatu. Jambo moja ambalo namuahidi Mheshimiwa Mbunge, ni kwamba kupitia mapato yao ya ndani ikiwemo ya uuzaji wa viatu, waanze ukarabati lakini ngazi ya Serikali Kuu wataenda kutenga fedha kwa ajili ya kukrabati magereza makongwe ikiwemo Gereza la Karanga kadri bajeti ya Serikali itakavyoruhusu.
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Gereza la Liwale pamoja na kwamba lina uzio wa miti, Mkuu wa Gereza amejenga nyumba tano za two in One na bado nyumba zile zimeishia kwenye linta. Je, Serikali haioni umuhimu wa kumwongezea fedha Askari yule ili wamalizie nyumba zile za maaskari?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, nimuahidi Mheshimiwa Mbunge, kwa wale wanaofanya juhudi kama Mkuu wa Gereza wa Liwale pamoja na juhudi za Mbunge ambaye anatoa fedha kwenye fungu lake kwa ajili ya kuliwezesha gereza hili, tutaendelea kuwa-support kwa kuwapa bajeti ili miradi kama hiyo iweze kukamilishwa ndani ya muda mfupi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru.
MHE. OMAR ALI OMAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa fursa ya kuuliza maswali mawili madogo ya nyongeza. Swali la kwanza, kwa taarifa nilizokuwa nazo kwamba magari ya polisi yaliyoko Mkoa wa Kaskazini Pemba ni mawili tu. Je, hili gari moja limekwenda sehemu gani?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili; Jeshi La Polisi Mkoa wa Kaskazini Pemba lina magari machakavu mengi. Je, Serikali ina mpango gani wa kuyatengeneza magari haya au kuyapiga mnada?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Omar kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa alizonazo yeye ni magari mawili, lakini taarifa nilizopewa na IGP ni magari matatu. Tutafuta hilo la tatu liko wapi, kama limepelekwa mahali fulani tutahakikisha linapelekwa Pemba ili magari matatu yaweze kutimia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu uchakavu wa magari, tutafanya tathmini kama kawaida ilivyo kwa mali za Serikali, magari yaliyochoka yanafanyiwa tathmini, yanayoweza kufanyiwa ukarabati au matengenezo yakarejea barabarani yanafanyika, yale yanayoshindikana huuzwa kwa utaratibu unaosimamiwa na Wizara ya Fedha. Kwa hiyo, tutafanya tathmini ya haraka ili yale yaliyo machakavu kabisa tuyaondoe kwenye daftari kwa kuyauza na yale yanayoweza kutengenezeka yafanyiwe matengenezo, yasaidie usafiri wa vijana wetu, nashukuru.
MHE. EMMANUEL P. CHEREHANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Wilaya ya Kahama ina mwingiliano mkubwa sana wa raia wa kigeni lakini Ofisi ya Immigration katika Wilaya ya Kahama haina gari kabisa na haina kabisa usafiri. Inafikia hatua mpaka viongozi wa uhamiaji wanakimbizana na raia wa kigeni kwa kutumia pikipiki ambayo ni hatari sana kwenye maisha yao. Je, Serikali itapeleka lini gari la Uhamiaji katika Wilaya ya Kahama?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba Serikali inaendelea kuimarisha kuviwezesha vyombo vyake vya usalama ili viweze kutekeleza majukumu yake vizuri. Bahati mbaya katika swali la msingi huwa tunauliza polisi na hili limekuja kwa Immigration. Tutafuatilia Idara ya Immigration kuona uwezekano wa kuwapatia watu wa Kahama gari kulingana na changamoto ya wageni na shughuli za kibiashara nyingi zilizopo katika Mji wa Kahama. Kwa hiyo tutawasiliana na Mheshimiwa Mbunge ili kuona namna ya kutanzua tatizo hilo, nashukuru.
MHE. ANNE K. MALECELA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Mwaka 2015 nilipata msaada wa gari la Polisi kutoka Japan, nikalipeleka kwenye Kituo cha Afya cha Gonja ambacho kiko Kata ya Maole. Mimi mwenyewe nilifuatilia, Serikali ilikuwa hailiangalii lile gari mpaka sasa hivi sijui lina hali gani. Je, Waziri ataniambia leo Serikali itakwenda kuliangalia lile gari lirudi barabarani kama nilivyolileta kutoka Japan?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimuahidi Mheshimiwa Malecela Anne Kilango, kwamba binafsi nitalifuatilia kuona hilo gari liko wapi na ni changamoto gani inayosababisha lisiende kuwahudumia watu wa Gonja kama ilivyokusudiwa na Mheshimiwa Mbunge katika jitihada zake za kutafuta gari hilo. Namuahidi Mheshimiwa nitalifuatilia kwa kina baada ya kikao hiki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru.
MHE. FRANCIS K. NDULANE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Katika wilaya ya Kilwa Jeshi letu la Polisi lina gari chakavu sana. Je, ni lini Serikali itapeleka gari jipya kwa ajili ya matumizi ya Jeshi letu la Polisi, Wilayani Kilwa?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesema kwenye jibu langu la msingi kwamba katika mwaka huu wa bajeti tunaoendelea nao, Serikali imetutengea bilioni 15 kwa ajili ya ununuzi wa magari na ahadi yetu ni kwamba ma-OCD wote watapata mgao wa magari haya. Kwa hiyo, Mheshimiwa Ndulane kule Kilwa pia watapata mgawo wao, nashukuru.
MHE. MARYAM AZAN MWINYI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Je, Serikali itapeleka lini magari katika Mkoa wa Kusini, Pemba ambao una uhaba wa magari hayo?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kurejea jibu langu la msingi kwamba, mara tutakapopokea magari yatakayonunuliwa kwa bilioni 15 tulizopewa na Serikali ya Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Mkoa wa Kusini Pemba pia ni moja ya maeneo yatakayogawiwa magari hayo. Namwondoa mashaka Mheshimiwa Maida kwamba Mkoa wake pia utapata gari, ahsante.
MHE. SOUD MOHAMMED JUMAH: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa majibu ya Mheshimiwa Waziri, lakini pamoja na kwamba takwimu haziko vema na ningeomba Mheshimiwa Naibu Waziri apate muda akajiridhishe na hizo data au takwimu zilivyochukuliwa, lakini nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza; kwa kuwa magari ya mchanga yanasababisha sana ajali za daladala pamoja na ajali za bodaboda hasa katika maeneo ya Kaskazini A Kule Nungwi na maeneo ya Donge kwa ujumla wake. Je, Mheshimiwa Naibu Waziri ana mpango gani wa kukaa na Wizara za Mawasiliano pamoja na Wizara husika kule Zanzibar ili kuweza kutatua tatizo hili?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; kwa kuwa tatizo la magari ya mchanga kwenda mwendo wa kasi ni tatizo sugu hivi sasa. Je, Mheshimiwa Naibu Naibu Waziri haoni haja ya kukaa na taasisi inayoshughulikia masuala ya usafirishaji wa mchanga pamoja na maliasili isiyorejesheka ili kukaa na kuratibu utaratibu mzima wa leseni pamoja na utaratibu wa kusafirisha hizi rasilimali za mazao yasiyorejesheka? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Soud, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza takwimu hizi nimeletewa na Kamisheni ya Polisi Zanzibar, kwa hiyo nina Imani zimetoka kwenye mamlaka sahihi. Hata hivyo, kwa vile amesema tujiridhishe, mimi na yeye tutashirikiana kuzifuatilia, kama ana source nyingine yenye takwimu tofauti na hizi tutasaidiana kuona ni zipi ni sahihi zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kuhusu magari haya kusababisha ajali kwa wingi kama alivyoeleza, kwa takwimu zetu kunaonekana kuna dalili ya kupungua. Hata hivyo, nieleze hata kama gari inabeba mzigo au ni mfanyabiashara na nini, anapoingia barabarani lazima azingatie Masharti ya matumizi ya barabara na kwa maana ya Sheria ya Usalama Barabarani inamhusu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu magari haya kusababisha ajali kwa wingi kama alivyoeleza, kwa takwimu zetu inaonekana kuna dalili ya kupungua, lakini nieleze hata kama gari inabeba mzigo ama ni mfanyabishara na kadhalika, anapoingia barabarani lazima azingatie masharti ya matumizi ya barabara na kwa maana Sheria ya barabarani inamhusu. Kwa hiyo, kwa hawa wanaobeba mchanga ninashauri nchi nzima siyo tu lile eneo la Mheshimiwa Soud alilolieleza kwamba, kwanza inatakiwa ule mchanga ufunikwe ili usitoe vumbi wanapokuwa wanaendesha yale magari. Pili wahakikishe magari yale ni mazima yanapoingia barabarani na madereva kwa kweli wawe sober enough wasiwe wamekula vilevi wakasababisha ajali kwa watu wengine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo, tutaendelea kufuatilia kwa ukaribu na kupitia Bunge lako Tukufu nimwelekeze IGP kupia Kamisheni ya Polisi Zanzibar waimarishe usimamizi wa eneo hili lililobainishwa na Mbunge, eneo la Nungwi na maeneo ya jirani ili kukomesha kabisa ajari za namna hiyo. Nashukuru. (Makofi)
MHE. JANETH M. MASSABURI: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu ya Serikali, nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa wenzetu wa nchi hizo wamekuwa wakitumia sheria kali ambazo kila dereva anatii sheria na kunusuru maisha ya wananchi wao; je, ni lini Serikali itatunga sheria kali ambazo zitaweza kutusaidia kunusuru maisha ya Watanzania yanayopotea kutokana na ajali za barabarani?

Mheshimiwa Spika, swali la pili; je, Serikali imeshindwa kuwadhibiti madereva wa bodaboda ambao hupita kwenye makutano bila kuzingatia taa za barabarani na hatimaye kusababisha ajali na kusababisha watu kufariki na kuleta walemavu wengi katika nchi yetu? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu maswali ya nyongeza ya Mheshimiwa Janeth Maurice Massaburi, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, moja, juu ya sheria ya usalama barabarani iliyo kali zaidi; naamini Mheshimiwa Mbunge atakuwa anafahamu kwamba tulishawasilisha hapa sheria ikasomwa kwa mara ya kwanza na kwa busara ya Bunge lako Tukufu ilitakiwa irudishwe kwa ajili ya kuboresha maeneo ambayo yalikuwa na changamoto. Napenda kumhakikishia kwamba uboreshaji uko hatua za mwisho, katika Mabunge yajayo tunatarajia iletwe hapa ili Bunge likiridhia tuwe tumemaliza eneo hilo la sheria kali.

Mheshimiwa Spika, kuhusu kushindwa kuwadhibiti bodaboda; hatujashindwa. Tulichojifunza ni kwamba hawa vijana namna wanavyoingia kwenye uendeshaji ni kwamba wengine hawajapata kabisa mafunzo. Jeshi la Polisi, hususan Kitengo cha Usalama Barabarani, wameanza na hatua za kuwafundisha.

Mheshimiwa Spika, na bahati nzuri sasa hivi wamewekwa kwenye makundi katika maeneo mbalimbali wanayopangwa katika vikundi. Katika makundi yao yale wanapata mafunzo, traffic police na wenye vyuo vya udereva wanakwenda wanawasomesha ili wajue taratibu za usalama barabarani.

Mheshimiwa Spika, wale wanaokiuka hatua zinachukuliwa. Ndiyo maana tukienda maeneo ya polisi mtakuta pikipiki nyingi ziko kule za wale waliokiuka sheria. Tutaendelea kujenga uwezo wao na kuchukua hatua kwa wale wanaokiuka. Kupitia Bunge lako, nielekeze traffic police wasiwe na muhali na vijana hawa ambao wanakaidi sheria makusudi, hasa wanaopita kwenye taa za barabarani wakati zimezuia, nashukuru.
MHE. AGNES M. MARWA: Mheshimiwa Spika, mwaka 2017/2018 Serikali iliondoa madereva wenye uzoefu na ujuzi wa udereva kwa kuwa walikosa kigezo cha kuwa na cheti cha form four. Na kwa kuwa ajali zimekuwa nyingi katika nchi hii ambazo zinaleta ulemavu au walemavu wengi nchini: -

Je, Serikali haioni sasa sababu ya kuwarudisha madereva hao kazini kwa sababu cheti cha form four hakina uhusiano na ujuzi au utaalamu wa udereva? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Agnes Mathew Marwa, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kuwaondoa watumishi waliokuwa hawana vyeti vya form four wakiwemo madereva ilikuwa ni Sera ya Menejimenti ya Utumishi ambao tumeridhia wote kama nchi, kwamba tuna vijana waliokwisha soma mpaka kidato cha nne na kuendelea, ni vizuri utumishi wa umma uwazingatie hao na kuruhusu wale ambao walikuwa kwenye utumishi wa Umma wajiendeleze. Serikali bahati nzuri ilitoa muda maalum wa watu wale kujiendeleza, na walioshindwa kujiendeleza ndio waliondolewa.

Mheshimiwa Spika, wale wa darasa la saba waliojiendeleza wengi walibaki kwenye utumishi wa Umma. Nadhani bado hakuna hoja ya msingi ya kurejea darasa la saba wakati tunaowahitaji kwa mujibu wa sera yetu ni baada ya kidato cha nne, na vyuo vya udereva vipo ambapo hawazuii kuingia kupata mafunzo. Kwa hivyo tunalichukulia positively kwa maana kwamba wataendelea kujielimisha na wanaokiuka wanachukuliwa hatua, ahsante.
MHE. VEDASTUS M. MATHAYO: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, madereva wengi wa bodaboda hawana leseni kwa sababu ya gharama kubwa zinazotakiwa kwa ajili ya kupata leseni, na ndiyo maana wanaendesha pasipo kuwa na leseni. Sasa swali; kwa nini tusiweke utaratibu mzuri wa kuwafundisha pamoja kwa gharama nafuu ili waweze kufanya kazi hiyo kwa uzuri?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Vedastus Manyinyi Mathayo, Mbunge wa Musoma Mjini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, tunapokea ushauri wa Mheshimiwa Mbunge kwamba katika baadhi ya maeneo ikiwemo kwenye jimbo lake, ameanzisha huo utaratibu, na sisi upande wa usalama wa raia tunaupokea.

Mheshimiwa Spika, nitumie nafasi hii kuwahamasisha maeneo mengine pia watumie utaratibu kama huu unaopendekezwa na Mbunge, kwamba wanapokuwa wengi katika chumba kimoja wakafundisha kwa gharama za chini, wakawekewa utaratibu nafuu wa kupata leseni zao ili kuepuka hao wanaokwepa kukata leseni kwa sababu ya gharama kubwa. Na bahati nzuri maeneo mengine wameruhusu kulipa leseni kidogo kidogo, kwa hiyo likifanyika hilo nadhani hakutakuwa na matatizo yoyote.
MHE. MWANAHAMIS KASSIM SAID: Mheshimiwa Spika, majibu anayoyajibu Mheshimiwa Waziri, mimi sina, sijayaona kwenye swali langu. Hapa sikuuliza sheria kwa sababu sheria haina matatizo, wale watekelezaji wa sheria ndio wenye matatizo.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, pamoja na jibu la msingi ambalo ni zuri kama alivyolieleza Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Mwanakhamis Kassim Said, Mbunge wa Magomeni, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, wasimamizi wa sheria ni pamoja na Jeshi la Polisi, na huenda dhamana anazozikusudia ni zile ambazo zinatolewa na Jeshi la Polisi lakini watu hawatoki. Jambo la msingi ambalo tumelifanya Wizara ya Mambo ya Ndani kupitia IGP ni kuwataka RPCs, OCDs na wale wakuu wa vituo (OCSs), kukagua mara kwa mara mahabusu zetu na kuona watu waliomo ndani na sababu gani zimesababisha awe ndani ili waweze kuachiwa kama hakuna sababu za msingi.

Mheshimiwa Spika, lakini tumebaini pia kwamba kuna baadhi ya watu wanawekwa ndani hata ndugu zao wanagoma kuwawekea dhamana, na hii ni kwa sababu ya matukio ya mara kwa mara yanayojirudia kiasi kwamba yanafedhehesha jamii. Kwa hiyo, niwaombe pia ndugu wawe wepese kuwadhamini kwa wale ambao dhamana zinakuwa wazi.

Mheshimiwa Spika, tumewasisitiza wakuu wa vituo pale inapowezekana kwa makosa yanayodhaminiwa waweze kutoa dhamana. Na kama Mheshimiwa Mbunge ana jambo specific, niko tayari kukutana naye baada ya kipindi cha maswali na majibu ili tuweze kuambiwa halafu tuone ni kitu gani kilichokwama, nashukuru. (Makofi)
MHE. STELLA S. FIYAO: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri lakini nina maswali mawili ya nyongeza. Kwa kuwa Mkoa wa Songwe una halmashauri tano na magari yako katika halmashauri mbili ambayo ni halmashauri ya Wilaya ya Mbozi na Halmashauri ya Mji wa Tunduma, lakini kuna halmashauri ya Ileje, Momba na Songwe mpaka sasa hayana magari ya zimamoto.

Je, mnatumia njia gani kukabiliana na majanga ya moto yanapotokea katika Wilaya hizi?

Mheshimiwa Spika, swali langu la pili, kwa kuwa magari yaliyopo katika Wilaya ya Halmashauri ya Mbozi na Halmashauri ya Mji wa Tunduma ni magari madogo hayana uwezo mkubwa wa kukabiliana na majanga makubwa ya moto.

Je, ni lini mpango wa Serikali kuhakikisha wanaleta magari makubwa na ya kisasa kwa akili ya kukabiliana na majanga ya moto?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa
Spika, ni kweli tunatambua uwepo wa Halmashauri tatu za Wilaya ambazo hazina magari, na ndiyo maana kwenye jibu la msingi nimesema tunaendelea kuliwezesha Jeshi la Zimamoto hatua kwa hatua kutegemea upatikanaji wa fedha. Hata hivyo nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Wabunge wa majimbo, akiweno Mwenisongole amewasiliana na Wizara kwa kaaribu na Mkuu wa Fire nchini na tumewaahidi kuwapa gari moja hata kabla ya magari ambayo tuna plan kununua hatujanunua.

Mheshimiwa Spika, lakini kuhusu uwezo mdogo wa magari tunatambua, ndiyo maana kwenye bajeti ijayo ambayo tutaleta tuombe Bunge lako lituhidhinishie ipo bajeti ya kununua magari makubwa na kadri yatakavyokuwa yananunuliwa tutakuwa tunapeleka kwenye Wilaya zenye changamoto zikiwemo hizo Wilaya za Mkoa wa Songwe.

Mheshimiwa Spika, niwashukuru watu wa Songwe, kwenye wilaya tatu alizozitaja hakuna matukio ya mara kwa mara ya majanga ya moto yanayohitaji uokoaji. Tunashukuru kwamba elimu ya zimamoto na wokozi wanaizingatia wananchi wa Mkoa huo. Ahsante.
MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Naibu Spika, Swali la kwanza; kwa kuwa wadau wa Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika wakiongozwa na Mkuu wa Wilaya na kumshirikisha RPC na OCD wamefikia hatua ya kutenga fedha na kuanza kujenga kituo hicho na Wizara mpaka sasa hawajatoa shilingi ya aina yoyote. Je, ni lini Serikali watapeleka fedha kwa kuwaunga mkono wananchi ambao wamejitolea kuhakikisha wanafanya kazi hiyo?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; halmashauri ya wilaya imetoa eneo na Serikali inatakiwa itoe shilingi milioni 20 kwa ajili ya kupata hati miliki. Je, ni lini sasa mchakato huo wa kupeleka hizo fedha utafanyika ili jitihada za kuejnga kituo hicho zianze kufanyika kwa wakati?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, lini fedha zitapelekwa? Hatua ya kwanza kama alivyomaliza swali lake la pili ni kulipa hii fedha ya fidia na upimaji ya milioni 20 na nimuahidi katika bajeti ijayo fedha zimetengwa zitapelekwa. Baada ya kulipa fidia na kupata hati Wizara itaji-commit kutenga fedha kwa ajili ya kuanza ujenzi, ku-support nguvu za wananchi kama nilivyoeleza kwenye jibu la msingi, ahsante sana.
MHE. DEODATUS P. MWANYIKA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Kituo cha Polisi katika Mji wa Njombe ni kichakavu sana na cha zamani. Je, ni lini ujenzi wa Kituo kipya cha Polisi utaanza?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara kupitia Jeshi la Polisi itaanza na kazi ya kufanya tathmini ya kiwango cha uchakavu wa majengo ya Kituo cha Polisi ngazi ya Wilaya cha Njombe. Iwapo itathibitika kwamba gharama za ukarabati zitakaribia kulingana na gharama za ujenzi wa kituo kipya, uamuzi utafanyika kwa ajili ya kujenga kituo kipya, lakini kama gharama zitakuwa manageable tutakikarabati kituo hicho ili kiweze kuwa cha kisasa zaidi, nashukuru.
MHE. DKT. JOHN D. PALLANGYO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa fursa hii. Je, ni lini Serikali itatekeleza ahadi yake ya kujenga Kituo cha Polisi katika Kata ya King’ori kama ilivyoahidi mwaka jana? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyowahi kujibu kwa nyakati tofauti, ujenzi wa Vituo vya Polisi ngazi ya Kata ni jukumu la jamii kwa maana ya halmashauri na wananchi wake, lakini pale ambapo tunakuta juhudi hizo zimefanyika Wizara huunga mkono kupitia Jeshi lake la Polisi. Nimwombe Mheshimiwa Dkt. Pallangyo, najua juhudi zake kwenye hili, waanze na sisi tutakuja kuwaunga mkono, ahsante sana.
MHE. ASYA SHARIF OMAR: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali, lakini nitakuwa na maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; pamoja na maelezo yake nataka kujua ni lini ujenzi huo utaanza katika maeneo hayo ya Finya, Micheweni na Konde? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili; naomba kujua Serikali imejipangaje kuhusu kuchimba visima katika maeneo hayo ambayo yatajenga hizo nyumba kwa sababu kama tunavyofahamu maeneo hayo yana uhaba wa maji. Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Asya, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu lini ujenzi utaanza kwenye jibu langu la msingi nimeeleza kwamba ujenzi unaendelea kwenye maeneo tofauti. Kwa mfano, eneo la Finya kuna nyumba nne zinaendelea kujengwa na ziko kwenye hatua ya umaliziaji. Kuhusu uhaba wa maji tutashirikiana na mamlaka ya utoaji wa huduma za maji katika Wilaya ya Micheweni ili ishiriki kwa sababu si kazi ya polisi ku-supply maji, lakini pale tunapokuwa na uwezesho wa kifedha tunachimba visima vya maji, lakini kwa sasa bajeti tuliyotenga ni kwa ajili ya ujenzi wa vituo na makazi ya askari, nashukuru. (Makofi)
MHE. EMMANUEL P. CHEREHANI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Ushetu haina jengo lolote la Kituo cha Polisi na wanaendelea kuishi kwenye majengo ya kupanga, hakuna nyumba za maaskari, lakini sioni mkakati wowote wa Serikali juu ya suala hili toka mwaka jana nalilalamikia. Je, ni nini kauli ya Serikali?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli tunajua Ushetu ni wilaya mpya ilibebwa kutoka Kahama na ndio changamoto ya kuanzisha maeneo mapya ya makazi. Tunachokifanya katika Wizara ya Mambo ya Ndani, hususani Idara ya Jeshi la Polisi ni kuendelea na ujenzi wa maeneo haya hatua kwa hatua kadri tunavyopata bajeti. Nimuahidi Mheshimiwa Cherehani, nilishajibu hapa Ushetu ni eneo lenye kipaumbele kwa sababu ya shughuli za kiuchumi zilizoko huko. Wanahitaji kuwa na kituo cha polisi cha uhakika, kwa hiyo pale tutakapopata fedha kituo hiko kitajengwa, nashukuru.
MHE. FRANCIS K. NDULANE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kuniona. Katika Kituo chetu cha Polisi kilichopo katika Kata ya Somanga, Wilayani Kilwa chenye watumishi 19, hakina hata nyumba moja ya watumishi. Je, Serikali ina mkakati gani wa kuwajengea nyumba watumishi hawa?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, tutaendelea kujenga kadri ya upatikanaji wa fedha, maadam jengo la polisi lipo. Tutakachoendelea kufanya ni kuhakikisha kwamba eneo linapatikana na sisi tuingize kwenye bajeti kwa ajili ya ujenzi wa nyumba hizo. Kwa hiyo, nimwombe Mheshimiwa Ndulane kama eneo limeshapatikana kwenye halmashauri husika, tuko tayari kushirikia nao kuhakikisha nyumba hizo zinajengwa, ahsante sana.
MHE. JAFARI W. CHEGE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Kwa kuwa mpaka sasa wavuvi wetu wameendelea kupigwa na kunyang’anywa mali zao hasa malighafi ya samaki maeneo ya ziwani. Je, Serikali haioni umuhimu sasa wa kuimarisha Jeshi la Marine Sota pale Wilaya ya Rorya ili kuimarisha ulinzi maeneo ya ziwa kwa ajili ya kulinda wavuvi pamoja na malighafi Samaki?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili, kwa kuwa zoezi hili la uhalifu linafanywa na askari wa nchi jirani. Serikali haioni umuhimu sasa kupitia Wizara kufanya mazungumzo na nchi hizi jirani ambao wanafanya uharibifu na kupiga wavuvi wetu ili waweze kuacha zoezi hili mara moja?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu uimarishaji wa Kituo cha Marine Sota, nadhani nikubali hiyo ahadi. Mwezi uliopita Waziri wangu alitembelea eneo hilo na ile ilikuwa ni moja ya concern kwamba Kituo cha Marine cha Sota kiko dhaifu. Kwa hiyo kupitia hadhara hii ya Bunge lako tukufu, nimwombe Mkuu wa Jeshi la Polisi azingatie kuimarisha Kituo hiki cha Sota ili kiweze kutimiza wajibu wake ipasavyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu uhalifu kufanywa na wanaodhaniwa kuwa ni askari wa nchi jirani, Jeshi la Polisi litafanya uchunguzi, pale itakapothibitika tutaimairisha vikao vya ujirani mwema kati ya wakuu wetu wa vyombo kudhibiti suala hili.

Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru.
MHE. OMAR ISSA KOMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa nafasi. Hadi sasa katika Wilaya ya Micheweni hakuna nyumba za askari ambazo ujenzi unaendelea. Pamoja na hili sasa naomba niulize maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa kituo cha polisi Wilaya ya Micheweni ndiyo Makao Makuu ya Polisi Wilaya ya Micheweni. Je, Serikali ina mkakati gani wakujenga nyumba za polisi katika Wilaya ya Micheweni? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; katika kituo cha polisi cha Wilaya ya Micheweni kuna hanga la Jeshi la Polisi ambalo lilijengwa kutokana na nguvu za wananchi miaka kumi iliyopita hadi sasa hanga hili kutokana na kwamba halikumaliziwa tayari limeanza kuharibika ikiwemo paa kuvuja na saruji kuharika. Je, Serikali haioni haja kuunga mkono jitihada hizi za wananchi kwa kumalizia jengo hili? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, mkakati nimeusema ni kuendelea kutenga fedha kujenga nyumba za askari na maofisa kutegemea upatikanaji wake hata hivyo alichosema kwamba ujenzi umesimama kule Micheweni Mheshimiwa Mbunge ni kweli ndiyo maana kwenye jibu la msingi nimesema zinahitajika milioni 60 ili kumalizia jengo hilo na fedha hizi zinatengwa kwenye bajeti ya mwaka 2023/2024 kutoka Mfuko wa Tuzo na Tozo. Kwa hiyo, Mheshimiwa eneo hilo litakamilishwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu uendelezaji wa ujenzi wa nyumba, kama nilivyosema kwenye jibu la msingi tutaendelea kujenga nyumba za askari kadri tunavyopata pesa kwenye bajeti yetu au pale tunaposhirikiana na wadau.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana.
MHE. SALOME W. MAKAMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru pamoja na majibu ya Serikali ninayo maswali mawili ya nyongeza. Swali langu la kwanza juzi wakati Mheshimiwa Naibu Waziri anajibu swali linalofanana na hili alieleza bayana kwamba mahabusu wengi wanashindwa kutoka, kwa sababu ndugu zao au jamaa hawaendi kuwawekea dhamana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunafahamu yapo makosa ambayo mtu anaweza akajidhamini mwenyewe na hili litapunguza msongamano mkubwa kwenye magereza. Nini kauli ya Serikali kwa Jeshi la Polisi na Magereza ambao mpaka sasa hivi wanaweka vikwazo kwa mtu kujidhamini mwenyewe na kuweza kutoka katika vizuizi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; bado katika magereza yetu njia zinazotumika kufanya ukaguzi kwa wafungwa hasa wanawake zinawadhalilisha wanawake na zinawaondolea utu wao na kuvunja haki zao. Kwa nini Serikali inashindwa kununua vifaa vya kisasa vya kufanya ukaguzi ili kuweza kutunza staha za wafungwa na maabusu hasa wanawake? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba masuala ya dhamana yapo ya namna mbili moja inaweza kutolewa na polisi na nyingine inatolewa na Mahakama. Sasa pale ambapo kuna changamoto za polisi juzi nilieleza kwamba tunawahimiza RPC’S, OCD’S na Wakuu wa vituo wazingatie sheria kila inapotokea kosa inastahili dhamana watu waweze kutoa dhamana lakini pale inaposhindikana Mahakama ikitoa amri mtu apewe dhamana always tuta–comply ili dhamana iweze kutolewa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu upekuzi unaodhalilisha tunatambua hilo na ndiyo maana kwenye bajeti yetu ijayo tumetenga fedha kwa ajili ya kununua vifaa vya kisasa vya kiteknolojia kuepusha ukaguzi unaodhalilisha siyo wanawake tu hata wanaume pia ili mtu akishapita pale anaonekana kama alivyo salama basi itakuwa imekamilika, ahsante.
MHE. HAJI MAKAME MLENGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Kwanza niipongeze Serikali kwa kufikia hatua hii ya kusema Mei, mwezi huu watalipwa warithi wa Marehemu Makame Haji Kheir aliyefariki toka mwaka 2003 lakini kwa sababu ni muda sasa na mwezi Mei ukiisha hajalipwa, ikifika mwezi Agosti nitauliza tena swali hili ndani ya Bunge hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la msingi, kwa kuwa tatizo hili naamini kwamba liko kwa wingi sana Nchini Tanzania. Je, Serikali ina mkakati gani au inawaambia nini Watanzania wenye tatizo kama hili la mirathi ambao hawajalipwa mpaka leo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, majibu ambayo tumempa Mheshimiwa Mlenge ndio majibu ambayo tunakwenda kuyafanyia kazi. Kwa maana ya kwamba huu mwezi Mei huyu mtu ambaye anadai mafao yake kupitia warithi, atapata mafao yake kwa sababu kila kitu kipo na vielelezo vimekamilika na fedha zimeshatengwa na zipo tayari.

Mheshimiwa Mwenyekiti, bado kuna changamoto pamoja na kwamba tunachowaambia Watanzania kwamba madai yote na hiki tunataka tuwaambie, itakapofika Oktoba mwaka huu tutahakikisha kwamba warithi wote wameshapatiwa mafao yao ili lengo na madhumuni sasa changamoto hizi zisiendelee kujitokeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto iliyojitokeza na ndiyo maana tunachukua muda mrefu halafu wananchi wanailaumu Serikali ni kwa sababu ya kuchelewa kuleta vielelezo vitakavyotupa sisi uhalali wa kuweza kuwapatia wananchi ile stahiki. Kwa hiyo niwaombe tu wananchi kwamba likishatokea hili walete vielelezo haraka iwezekanavyo ili na sisi tuweze kuwafanyia haraka waweze kupata haki zao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru.
MHE. JANEJELLY J. NTATE: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Serikali nina maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; je, wale ambao walipewa namba za NIDA kabla ya tarehe ya GN Namba 96 ya Mwaka 2023, vitambulisho vyao vitatoka vikiwa na ukomo au vitakuwa havina ukomo? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, je, Serikali imejipangaje kuleta uelewa kwa wananchi ili wajue kwamba vitambulisho vyao ambavyo vimekaribia kuwa na ukomo na ambavyo vina ukomo havitawaathiri ili kupunguza taharuki iliyo kwa wananchi sasa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali ya Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, vitambulisho ambavyo vitakuja baada ya tangazo hili havitakuwa na ukomo lakini hata vile vitambulisho ambavyo vimekuja kabla ya tangazo wataendelea. Kwa sababu lengo la Serikali hii ni kuhakikisha kwamba vitambulisho haviwezi kuwafanya watu wakakosa huduma zao muhimu. Kwa hiyo ndio maana tukasema kwamba vitambulisho ambavyo vitakuja baada ya tangazo hili havitakuwa na ukomo, lakini hata vile ambavyo tunasema vimeshakwisha muda navyo vilevile vitaendelea kutumika kuwapatia wananchi huduma mpaka pale Serikali kupitia Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi itakapotoa maelekezo mengine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vipi wananchi watafikiwa na taaluma hiyo. Kwanza kupitia Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Mheshimiwa Waziri ameshatoa tangazo kupitia vyombo vya habari kama vile televisheni, redio na magazeti. Nadhani wengi ambao wanakwenda kwenye mitandao huko wameona, lakini kikubwa tumeshatoa maelekezo na tupo tayari muda wowote tunaweza tukaanza mafunzo kwa watendaji wote wa NIDA kuwapa maelekezo na mafunzo ili sasa waanze kuwafundisha wananchi ili wananchi waweze kujua huu mchanganuo wa kipi kimekwisha ukomo na kipi hakitakwisha ukomo na kipi kitatumika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru.
MHE. SUBIRA K. MGALU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Pamoja na majibu yenye kuleta matumaini ya Serikali nina maswali mawili madogo ya nyongeza. Swali la kwanza; kwa kuwa, Serikali imesema imetenga fedha milioni 350; na kwa kuwa, Gereza la Dimani ni miongoni mwa magereza ambayo yatafanyiwa ukarabati. Je, Serikali inasema nini juu ya nyumba chakavu zilizopo kwenye Gereza hili la Dimani?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; kwa kuwa, changamoto ya uchakavu wa miundombinu inafanana na Gereza la Kigongoni, Bagamoyo na binafsi niliwahi kulitembelea na nikaona jitihada zao wenyewe askari magereza kwa kujenga nyumba na nikawachangia mifuko 50 ya simenti, lakini bado nyumba nyingine ni chakavu. Je, Serikali ina mpango gani wa muda mrefu wa kuwajengea nyumba askari magereza kwenye magereza mbalimbali kama inavyofanya kwenye majeshi mengine likiwemo Jeshi la JKT na Jeshi la Wananchi? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu uchakavu wa nyumba kama pia zitahusika katika ukarabati huu, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, fedha za ukarabati zinapelekwa kwenye gereza. Mkuu wa gereza pamoja na menejimenti yake wataangalia wapi pana tatizo kubwa zaidi na wanalipa kipaumbele katika ukarabati. Hatuta-prescribe, hatutaagiza kwamba, karabati gereza acha nyumba kwa hiyo, kama nyumba zina hali mbaya zaidi wataanza kukarabati nyumba, kama gereza lina hli mbaya zaidi wataanza na gereza. Kwa hiyo, uhuru tunawaachia wao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu ukarabati wa Gereza la Bagamoyo ambalo pia, Mheshimiwa Mbunge amesema limechakaa sana. Nimhakikishie tu mpango wetu wa ukarabati na ujenzi wa magereza unaenda sambamba kama tulivyokwishasema. Tumeanza mwaka jana, mwaka huu tunaendelea na mwaka ujao pia tutaendelea. Kwa hiyo, gereza la Bagamoyo kulingana na hali ya upatikanaji wa fedha litakuwa moja ya magereza yatakayoingizwa kwenye mpango wa ukarabati. Ahsante sana.
MHE. USSI SALUM PONDEZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Nakushukuru sana kwa kunipa nafasi. Nilikuwa na swali dogo la kumuuliza Mheshimiwa Naibu Waziri. Je, sasa Serikali haioni umefika wakati wa kuboresha magereza haya ambayo yapo Tanzania nzima ambayo Serikali imerithi na kujenga ya kisasa ambayo yataendana na mfumo wa sasa hivi wa teknolojia ambayo hata Mahakama sasa hivi wanaendesha kesi kwa mfumo wa mtandao ambao iepushe Serikali kutumia gharama ya kuwatoa mahabusu hapa na kuwapeleka mahakamani. Je, kwa nini Serikali isijenge magereza mapya ambayo yatakuwa yana mfumo wa kiteknolojia? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba, yapo mabadiliko makubwa ya teknolojia na uendeshaji wa mashauri, hasa Mahakama imeshapiga hatua kubwa. Kwa msingi huo pia, Wizara ya Mambo ya Ndani, kupitia Jeshi la Magereza pia tumeanza. Magereza yanayojengwa sasa yanazingatia mahitaji hayo ya teknolojia na mengine yaliyo bora zaidi ikiwemo pamoja na ukaguzi, vitawekwa vifaa vya elektroniki, ili kuepusha watu kuguswaguswa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa magereza ambayo tunayo haiwezekani yote tuyabadilishe siku moja. Tutaendelea kuyakarabati, yatakayofaa kuingiziwa vitendea kazi vya kisasa, vifaa vya kisasa zaidi, tutafanya hivyo, lakini mengine tutaendelea kuyakarabati ili yatoshe kulingana na uwezekano wa bajeti tutaimarisha kwenda kama anavyoshauri Mheshimiwa Mbunge katika siku zijazo, ahsante.
MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Baada ya wananchi kunyang’anywa ile ardhi, wananchi wa Nkongore mwaka 2020 kabla ya uchaguzi walikuja hapa Dodoma kumwona Waziri Mkuu na Waziri Mkuu aliahidi kwamba, wataenda kurudishiwa lile eneo. Sasa mpaka leo bado hawajarudishiwa na mbaya zaidi hao magereza ambao wamekabidhiwa kwa ajili ya ulinzi kuna shughuli tena wanafanya. Nataka kujua ni kwa nini sasa pale ambapo Serikali imeamua kutwaa ardhi kwa ajili ya matumizi mbadala isiwalipe fidia wananchi? Ni nini taarifa ya fidia ya wananchi wa Nkongore ili waweze kupata kifuta jasho waendelee na shughuli zao ambazo walikuwa wakifanya Serikali inachukua ile ardhi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini swali pili. Mheshimiwa Waziri ameeleza hapa kwamba, imesababisha kwa sababu ya taratibu za kimazingira wakakabidhi Jeshi la Magereza, ulinzi na usalama, lakini wananchi wale wakati ardhi inachukuliwa walikuwa wamepanda miti ya kudumu pamoja na mazao mbalimbali. Sasa mbaya zaidi askari magereza hawa wanavuna ile miti ya kudumu ya wananchi, wanaenda kufanyia shughuli nyingine. Ni kwa nini sasa kama ile miti inaruhusiwa kuvunwa nje ya hizo taratibu ambazo amezitaja hapa, wasiruhusu wananchi wale wavune miti yao ambayo walikuwa wameipanda kwa ajili ya biashara ili waweze kupata fedha zao stahiki?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu hili la wananchi kuwalipa fiidia ya maeneo yanayotwaliwa kwa mujibu wa sheria, nimeeleza kwenye jibu la msingi kama Mheshimiwa Mbunge amenisikiliza kwa makini kwamba, maeneo ya milima ni maeneo yanayohifadhiwa. Hakuna mtu anayeweza akadai kwamba, anamiliki mlima, kwa hivyo, kama walikuwa wanafanya shughuli za kibinadamu kando mwa milima ambazo sio sehemu ya mlima tutawasiliana na mamlaka husika, kwa maana ya Mji wa Tarime. Namwomba Mheshimiwa Esther Matiko tukutane baada ya kipindi cha maswali na majibu ili anipe ufafanuzi mzuri, niweze kutoa maelekezo stahiki kwa wenzetu w akule Tarime.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu uwepo wa miti iliyokuwa imepandwa na wananchi. Kama kuna uthibitisho huo tutawasiliana na mamlaka husika, kwa maana ya Magereza Mara na Tarime, Rorya, ili waweze kuwaruhusu wananchi wakate miti yao, lakini tunachoshukuru ni kwamba, hata Jeshi la Magereza katika hali ya kutunza ile hifadhi ya mlima wameshaanza kupanda miti na sasa wamepanda karibu miti 1,000 kuzunguka ule mlima kama sehemu ya kuhifadhi mazingira yale, nashukuru.
MHE. GHATI Z. CHOMETE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kuniona. Kwa kuwa maeneo haya wananchi walikuwa wanalima na wanayatumia kwa ajili ya kujipatia chakula. Je, Serikali haioni haja sasa ya kuwarudishia maeneo haya na ikawasimamia ili waendelee kulima na kuendelea kujipatia chakula?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa swali la Mheshimiwa Ghati, anayetetea wananchi wake wa Tarime, lakini nimweleze kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, jibu langu la msingi ni kwamba, eneo lile limechukuliwa ili kutunza mazingira, lakini pia na kutunza shughuli za usalama ambazo wengine walikuwa wanatumia maeneo yale kulima kilimo cha mazao haramu ya bangi, kwa hiyo, uwepo wa magereza umesaidia kudhibiti hali ile ili isitokee.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli, mlima ule uko karibu sana na mjini. Nadhani shughuli za kilimo mijini zinaruhusiwa, lakini huwezi ukasema pale kwa namna mji unavyoendelea kukua patakuwa na maeneo mengi ya kulima zaidi ya kutunza usalama uliopo. Hata hivyo, tutaongea na Mamlaka ya Mji wa Tarime ili kuona kama kweli yako maeneo pembeni ya mlima yanaweza kutumika na wananchi basi wananchi waruhusiwe kuendelea na shughuli zao. (Makofi)
MHE. ZAYTUN S. SWAI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwa kuwa tarafa ya Kitumbeine na Engarenaibor ziko mpakani pia zina rasilimali nyingi ikiwemo machimbo ya Rubi. Wananchi wa Mundarara kwa nguvu zao binafsi wamejitolea ardhi pia wamejenga Kituo cha Polisi hadi kufikia kwenye ngazi ya lintel.

Je, Serikali haioni haja sasa kuunga mkono wananchi hawa kwa kumalizia kituo hiki cha Polisi ili kulinda usalama wa raia na rasilimali zao? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema kwenye jibu la msingi, tumetambua juhudi za wananchi wa tarafa ua Kitumbeine na Engarenaibor ndiyo maana kwenye jibu langu la msingi nimesema tutawaunga mkono katika bajeti ya mwaka 2023/2024. Labda niwe more pragmatic katika bajeti ijayo tutatenga fedha za kuunga juhudi tuweze kukamilisha jengo lililojengwa kwenye eneo hili. Ahsante sana.

MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi. Nimehudumu kwenye Kamati hii miaka miwili na nusu, Jeshi letu la Polisi linakabiliwa sana na uchakavu wa muindombinu ya vituo vya Polisi pamoja na makazi ya Askari kote nchini ikiwemo Jimbo la Mbulu Mji Manyara.

Je, ni mkakati upi wa Serikali wa kuondoa tatizo la uchakavu wa majengo ya Askari kote nchini?
NAIBU WAZIRI WA AMAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kama alivyosema Mheshimiwa Mbunge kwamba baadhi ya vituo vya Polisi majengo yake ya vituo ni chakavu na nyumba za Askari ni chakavu. Kwa msingi huo Wizara ya Mambo ya Ndani kupitia Jeshi la Polisi limeandaa mpango mkakakti wa miaka 10, kwa ajili ya kufanya ukarabati wa vituo vilivyochakaa na nyumba Askari zilizochakaa, kwa hivyo kama eneo lako Mheshimiwa Mbunge pia lina changamoto hii litafikiwa. Tunashukuru sana.
MHE. TAMINA HAJI ABASS: Mheshimiwa Spika, ahsante, pamoja na majibu mazuri ya matumaini ya Mheshimiwa Waziri, naomba kuuliza swali moja la nyongeza. Kwa vile fedha hizo zitatengwa kwenye bajeti ya mwaka ujao; je, itawasaidiaje askari wanawake ambao wanaishi mbali na vituo vyao vya kazi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, kama ambavyo imeelezwa, nyumba hizi 14 zitakapokarabatiwa, mgao wa nyumba hizo kwa Askari wetu uzingatie uwiano wa jinsia ili Askari wa kike ambao Mheshimiwa ana mashaka kwamba wanakosa nyumba za kuishi waweze kupata nyumba, nashukuru.
MHE. USSI SALUM PONDEZA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana, kwanza nachukua nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Naibu Waziri baada ya kukubali ombi letu la wananchi wa Jimbo la Chumbuni kutupa ruhusa ya kujenga kituo chetu kikubwa cha Polisi ambacho tunaendelea nacho hivi sasa. Kama swali la msingi lilivyoulizwa kuhusu matatizo ya makazi, nasi tunatarajia kuwa na kituo kikubwa cha Class C; je, anatuahidi nini katika tatizo hili la makazi kwa sababu tunajenga kituo kikubwa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, tunaweka kipaumbele na kila tunapojenga kituo kikubwa cha polisi, tunazingatia pia makazi ya askari na viongozi wa Jeshi la Polisi. Ushauri wangu kwa Mheshimiwa Mbunge, ni kuhakikisha linapatikana eneo ili mpango wa ujenzi uende sambamba na kutenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za vijana wetu, nashukuru sana. (Makofi)
MHE. DKT. FAUSTINE E. NDUGULILE: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa majibu haya ya Serikali. Katika dhana hiyo ya utayari katika masuala ya uokozi, Wilaya ya Kigamboni ina matanki makubwa ya mafuta na hatuna gari ya zimamoto wala Kituo cha Zimamoto.

Je, nini mpango wa Serikali kuhakikisha kwamba tunakuwa na Kituo cha Zimamoto na gari la Zimamoto? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi ina mpango wa kuendelea kuimarisha Jeshi letu la Zimamoto na Uokoaji kwa kulipatia vifaa na utaalam ili kutekeleza majukumu hayo. Kama mazungumzo yetu na wakopeshaji yataenda vizuri, tunaweza kupata magari zaidi ya 150 kwa ajili ya shughuli za Zimamoto na Uokozi.

Mheshimiwa Spika, katika mazingira ya Kigamboni ambayo Mheshimiwa amefanya marejeo yake na umuhimu wa uwekezaji uliopo pale hasa matenki ya mafuta, kipaumbele kitawekwa kuhakikisha kwamba kunapatikana magari ya kuzima moto na kuimarisha Ofisi ya Zimamoto upande wa Kigamboni ili kutekeleza majukumu hayo kwa ufanisi, nashukuru. (Makofi)
MHE. MOHAMED ABDULRAHAMAN. MWINYI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana namshukuru Naibu Waziri kwa majibu yake, naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza.

Kwa kuwa Ofisi ya NIDA ya Wilaya ya Mkoani ni kichumba kidogo sana ambacho akiingia mteja mmoja wengine wanabakia nje wanapigwa na mvua, wanapigwa na jua…

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa swali.

MHE. MOHAMED ABDULRAHAMAN. MWINYI: Je, Serikali haioni haja ya kuwatafutia jengo jingine kuondoa adha hiyo? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; kwa kuwa kuna wananchi ambao wamejisajili mwaka 2018, 2019, 2020 mpaka leo hawajapata vitambulisho vya NIDA na wanaojisajili sasa hivi wanapata vitambulisho vya NIDA; je, nini kauli ya Serikali? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu kuwatafutia jengo lingine kwa kweli tunatambua kwamba zipo wilaya zenye changamoto ndiyo maana tumesema zitaendelea kujengewa ofisi baada ya hizi 31 zitakazofanyika kwenye mwaka wa bajeti ujayo.

Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo kwa hali ambayo ameieleza Mheshimiwa Mbunge niombe uongozi wa Wilaya ya Mkoani kule Mwinyi Pemba waone uwezekano wa kuwatafutia, kwa sababu wananchi wanaosajiliwa ni wananchi walewale walio chini ya Mkuu wa Wilaya, chini ya mamlaka zao za serikali za mitaa. Lakini nimuahidi pia tutatembelea huko baada ya bajeti hii ili kuona namna ya kutatua hilo tatizo alilolisema.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu wananchi waliojisajili muda mrefu na hawajapata vitambulisho, tuliahidi hapa Mheshimiwa kwamba mwaka huu tunashukuru Serikali ya Dkt. Samia Suluhu Hassan imeweza kutupatia 17,000,000,000 ambazo zilikuwa zinadaiwa na mkandarsi na tumeshamlipa, kinachoendelea ni kuanza kutekeleza kadi ghafi ambazo zilisimama uzalishwaji wake kutokana na masuala ya UVIKO. Lakini tunayo matarajio kwamba ndani ya miezi sita ijayo tunaweza kuanza kupokea na wananchi wake watapokea vitambulisho kama ambavyo vitagaiwa kwa wananchi wengine, nashukuru.
MHE. IDDI K. IDDI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.

Je, Serikali haioni haja ya kupeleka Ofisi za NIDA kwenye kila Halmashauri badala ya kwenye kila Wilaya ili kusiogeza huduma za wananchi hususani katika Halmashauri ya Msalala?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba inaweza ikaonekana umuhimu wa kuzipeleka ofisi hizi kwenye ngazi ya Halmashauri, lakini shughuli za NIDA ziko sehemu ya Serikali Kuu, na kama sehemu ya Serikali Kuu iko chini ya Mkuu wa Wilaya, ndiyo maana tumeanzia pale. Pale ambapo kutakuwa na haja, kwa mfano Wilaya yenye majimbo zaidi ya moja, tutaona uwezekano wa kuimarisha huduma hizo kwenye majimbo ya mbali na makao makuu ya wilaya, ili wananchi hawa waweze kupata hizo huduma stahiki.
MHE. ALI VUAI KHAMIS: Mheshimiwa Spika, ahsante, pamoja na majibu mazuri ya Serikali naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, kwa kuwa maeneo hayo yaliyotajwa ni maeneo ya utalii na kumekuwa na matukio ya uhalifu; je, Serikali ina mpango gani wa kuimarisha ulinzi wa dharura ili kuwe na amani?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa kuwa ujenzi wa nyumba na kituo cha polisi ni jukumu la Wizara; je, Serikali haioni haja ya kwenda kukaa na Serikali ya Mkoa, halmashauri na jimbo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, kuhusu umuhimu wa kuimarisha usalama kwenye eneo hili lenye watalii wengi, nitumie nafasi hii kumwekeleza IGP na hususani Kamishina wa Polisi Zanzibar kuimarisha huduma za doria ya magari ya askari wanaokwenda kwa miguu au pikipiki ili kuhakikisha wananchi na watalii wanaotembelea eneo hilo wanakuwa salama.

Mheshimiwa Spika, kuhusu swali la pili la kuimarisha ujenzi wa nyumba kupitia mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa (Halmashauri), hicho ndicho kipaumbele cha Wizara kwamba katika vituo vinavyojengwa hasa vile vidogo vya Daraja C ni jukumu la mamlaka zetu za Serikali za Mitaa ambazo ni moja ya kazi za msingi ya Serikali za Mitaa. Wizara imekuwa ikisaidiana na halmashauri hizi kukamilisha majengo hayo.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, tuendelee kushirikiana kuzihamasihsa halmashauri hizi ili watimize huo wajibu wao nasi tutimize wajibu wa kujenga vituo vikubwa na ku–support vituo vidogo wanapokuwa wamefikia kiwango cha umaliziaji, ahsante. (Makofi)
MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru, nataka kujua Serikali ina mpango gani wa dharura wa kuhakikisha kwamba inajenga vituo vya polisi vyenye hadhi ya kipolisi kwa Wilaya ya Tarime, Sirali, Nyamwaga na Utegi?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, ni kweli na Mheshimiwa Mbunge anatambua kwamba Mkoa wa Tarime – Rorya ni mkoa wa kipolisi, lakini kiutawala wako chini ya Mkuu wa Mkoa mmoja. Hata hivyo, tumeanza kutekeleza mpango wa ujenzi wa maeneo haya mapya. Ninatambua kwamba Jengo la RPC Tarime – Rorya almost limekamilika na sasa, tunakwenda kwenye ngazi ya Wilaya ili kujenga vituo vya ngazi ya Wilaya.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, kwa mujibu wa mpango wetu vituo vya Wilaya kwenye Wilaya mpya za kipolisi viko mbioni kwa mujibu wa utekelezaji wa mpango wetu wa miaka kumi. Nyamwaga na Sirali ni sehemu ya vituo vitakavyojengwa, nashukuru.
MHE. DANIEL B. SILLO: Mheshimiwa Spika, ahsante sana, wananchi wa Kata ya Bashnet tayari wametenga eneo kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha polisi; je, ni lini Serikali itatenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa kituo hicho cha polisi?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, kituo hiki kidogo cha Polisi cha Kata ya Bashnet ni kituo cha ngazi ya Daraja C. Nimuombe Mheshimiwa Mbunge kupitia juhudi alizozifanya kama tulivyofungua kituo kipya hivi karibuni, alifanya Mheshimiwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, waanze ujenzi kwenye eneo lao la Bashnet then Wizara kupitia Jeshi la Polisi itakamilisha mtakapokuwa mmefikia stage ya umaliziaji hasa lenta na uwekaji wa samani, nashukuru.
MHE. ALOYCE A. KWEZI: Mheshimiwa Spika, ahsante, naomba kupata ufafanuzi. Wilaya ya Kaliua hatuna ofisi ya OCD (jengo la polisi la Wilaya); je, Serikali iko tayari kutenga bajeti kwa ajili ya ujenzi ambapo pale Kaliua eneo lipo tayari?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, Serikali ipo tayari kushirikiana na Wilaya ya Kaliua ili kuhakikisha kituo hicho kinajengwa. Kwa kuwa tayari wana eneo, tutawasiliana na IGP ili kwenye mpango wake wa miaka kumi wa kujenga vituo vya polisi ngazi ya Wilaya, Kaliua iweze kupewa kipaumbele pia.
MHE. MARGARET S. SITTA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi na mimi niulize swali la nyongeza kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, pamoja na kuishukuru Serikali kwa kutujengea Kituo cha Polisi Kata ya Songambele; je, ni lini Mheshimiwa Naibu Waziri tutakwenda pamoja Urambo ili ukatatue migogoro kati ya wananchi na Magereza ya Urambo?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: MMheshimiwa Spika, nimuombe mama yangu Mheshimiwa Margaret Sitta na nimuahidi kwamba wakati wowote nitakuwa tayari kuambatana naye. Tutaangalia ratiba yetu baada ya Bunge hili ili kwenda kuangalia tatizo lililopo kati ya wanachi na Gereza ili kupata suluhisho la kudumu, nashukuru.
MHE. BONIPHACE N. BUTONDO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru na tunakupongeza Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu hayo na tunatarajia kwamba wana Mvomero watapata huduma hiyo mara moja baada ya ushirikiano kutoka Serikali Kuu.

Mheshimiwa Spika, naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza; swali la kwanza, je, ni lini sasa mradi huu utaanza kupewa support na Serikali ili kuonesha jitihada za wananchi wa Mvomero walizozianzisha?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, nakumbuka mwezi Julai Mheshimiwa Naibu Waziri ulitembelea katika Jimbo la Kishapu na Wilaya ya Kishapu, ukaona jitihada za ujenzi wa Ofisi ya OCD pale Kishapu; na jumla ya shilingi milioni 275 zinahitajika kwa ajili ya kukamilisha mradi huo; na uliahidi utapeleka fedha hizo kuhakikisha kwamba mradi huo unakamilika;

Je, ni lini fedha hizi zitafika ili ukamilishaji wa mradi huo wa Ofisi ya OCD uweze kukamilika? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, kuhusu hili la mradi wa ujenzi wa kituo kule Mvomero, ni ahadi yetu kwamba katika mwaka wa fedha 2024/2025 kituo hiki kimeingizwa kwenye mpango na fedha zinazopungua zaidi ya shilingi milioni 60 zitatolewa na Jeshi la Polisi ili mradi huo utekelezwe na kukamilika.

Mheshimiwa Spika, kuhusu Kishapu, kwanza nawapongeza wananchi waliojitolea pamoja na Halmashauri yao na Mheshimiwa Mbunge kujenga kituo bora kabisa, kinachohitaji ni umaliziaji. Tumeahidi, katika bajeti ya mwaka huu zimetengwa shilingi milioni 275 kwa ajili ya ukamilishaji huo.

Mheshimiwa Spika, kupitia Bunge hili nimhimize IGP kuhakikisha kwamba anapeleka fedha hizi mapema iwezekanavyo ili ukamilishaji ule ufanyike na hatimaye huduma za kipolisi ngazi ya Wilaya ziweze kutolewa, ahsante.
MHE. MWANAKHAMISI KASSIM SAID: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa majibu ya Serikali. Kuna wananchi wanapata matatizo panapokuwa na kesi za jinai, lakini wanapokwenda baadhi ya vituo wanakuwa hawapati huduma hizi wanaambiwa pale hawahusiki, waende kituo kingine.

Je, Serikali iko tayari kukifuta kifungu hiki ili wananchi pale wanapopata matatizo wapate huduma? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, kama nilivyosema kwenye jibu la msingi, hatuna kifungu chochote cha kisheria kinachozuia mwananchi aliyebaini uwepo wa kosa la jinai kuzuiwa kuripoti kwenye Kituo chochote cha Polisi.

Mheshimiwa Spika, nitumie nafasi hii kuelekeza kwamba ikiwa itatokea raia au mwananchi anapewa majibu hayo na askari wetu yeyote, atoe taarifa kwa Mkuu wa Kituo au Ofisa Upelelezi wa Wilaya au Mkuu wa Polisi wa Wilaya.

Mheshimiwa Spika, kupitia Bunge lako tukufu nielekeze IGP atoe mwongozo kwa Makamanda wote wa Polisi wa Mikoa ili kama kuna udhaifu wa namna hii uelekezwe kwamba kuondolewe msingi wa kuzuia mwananchi kutoa taarifa kwenye Kituo chochote cha Polisi, nashukuru.
MHE. FAKHARIA SHOMARI KHAMIS: Mheshimiwa Spika, ahsante. Nakubaliana na maelezo ya Mheshimiwa Naibu Waziri, lakini napenda Watanzania wapatiwe elimu. Naomba kujua hiyo sheria inazunguza nini au inasema nini wakati kitendo kama hicho kikitokea ili Watanzania wote waelewe kwamba kuna sheria inazungumza hivi?

Mheshimiwa Spika, swali la pili; kwa kuwa hicho kitendo sana huwa kinatokea nchi za nje na kule tuna balozi zetu. Je, balozi zetu zimepewa elimu gani kama litatokea tatizo kama hilo waweze kukabiliana nalo bila shida yoyote? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, ikiwa aliyefanya kosa yuko Tanzania, sheria zinazopaswa kuchukuliwa ni pamoja na mhusika kufikishwa mahakamani kwa mujibu wa Sheria ya Pasipoti, Sheria ya Uhamiaji, Sura ya 54 iliyorejewa mwaka 2016. Baada ya kutiwa hatiani na kuadhibiwa hunyanganywa pasipoti ya Tanzania na kuifuta ili isije ikatumika tena. Jambo la tatu, hufukuzwa nchini kwa kupewa hati ya kufukuzwa nchini (prohibit legal notice) ili aondoke katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mheshimiwa Spika, kuhusu Maofisa wa Ubalozi wetu katika kila ubalozi tunaye Afisa Balozi ambaye ikitokea tutapata taarifa kama kuna Mtanzania kawekwa gerezani au kafungwa hufuatilia kumhoji ili kujua kama kweli ni Mtanzania na ikithibitika si Mtanzania, basi taarifa hutolewa kwenye nchi husika, lakini ikithibitika kwamba ni Mtanzania itabidi atumikie kifungo chake. Kitakachofanyika kama ni Mtanzania, atakuwa anakwenda kumsalimia, kumwona kwenye vile vipindi vinavyoruhusiwa na mambo kama hayo, nashukuru.
MHE. MASACHE N. KASAKA: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana na naishukuru Serikali kwa majibu mazuri na tunaona namna ambavyo wanatuunga mkono na sisi tunasema ahsante. Tunaiomba tu Serikali tuweze kupata hizi fedha kwa wakati ili hivi Vituo vya Polisi viweze kukamilika.

Nina maswali mawili madogo ya nyongeza; Kituo cha Polisi cha Chunya Mjini ni Kituo cha Polisi cha zamani toka ukoloni, kidogo na kiko ndani ya Ofisi ya Mkuu wa Wilaya; je, ni upi mpango wa Serikali kuwezesha kujengwa kituo kikubwa cha Polisi chenye hadhi ya wilaya katika Wilaya yetu ya Chunya?

Mheshimiwa Spika, swali la pili. Wilaya ya Chunya ina changamoto kubwa ya nyumba za askari; je, ni upi mpango wa Serikali kuweza kujenga nyumba za askari ili waondokane kuishi katika mazingira magumu katika Wilaya ya Chunya? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, ni mpango wa Wizara kupitia Jeshi la Polisi kuhakikisha kwamba Wilaya zote nchini zinapata vituo vyenye hadhi ya Wilaya ambavyo vitakuwa na OCD, OC-CID, askari wa idara nyingine na askari wa kawaida ili kuwezesha ulinzi wa raia na mali zao. Nimuahidi Mheshimiwa Mbunge kwamba dhamira ya Serikali kulitekeleza hili bado ipo na nikuahidi kwamba katika mpango wake wa miaka 10 ambapo sasa hivi miaka miwili imepita ya ujenzi wa vituo hivi, tutahakikisha kituo cha wilaya yako kinaingia katika mpango angalau mwaka ujao.

Mheshimiwa Spika, kuhusu nyumba tumwombe tu Mheshimiwa Mbunge kwamba tunapojenga Kituo cha Polisi cha ngazi ya Wilaya au vituo vya Polisi daraja C ngazi ya kata na tarafa, tuhakikishe eneo linakuwa kubwa la kutosha kwa ajili ya kujenga kituo pia na makazi ya askari na viongozi wao. Kwa hiyo, wilaya ikituhakikishia uwepo wa viwanja hivyo tutaingiza kwenye mpango wa ujenzi wa kituo pamoja na nyumba, ahsante.
MHE. DEODATUS P. MWANYIKA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana, katika Mji wa Njombe tuna Kituo cha Polisi ambacho hakina hadhi ya makao makuu ya mkoa; je, ni lini kituo chenye hadhi ya mkoa kitajengwa katika Halmashauri ya Mji wa Njombe? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, ni mpango wa Serikali kuhakikisha kwamba mikoa yote ambayo haina vituo vya ngazi ya mkoa, vinajengewa vituo hivyo. Tumeanza kwa awamu katika maeneo mengine na Njombe ni eneo lingine ambalo litapewa kipaumbele katika mwaka ujao wa fedha, kuanza kujenga Kituo cha Polisi ngazi ya mkoa, nashukuru. (Makofi)
MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza.

Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga Gereza la Wilaya ya Nyang’hwale kwa sababu huduma hiyo tunaipata kwa umbali mrefu sana zaidi ya kilometa 100? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, nashukuru, japo swali ni la polisi, lakini nakubali tu kwamba ni nia ya Serikali kadri huduma za magereza zinapokuwa mbali zinaongeza gharama za kusafirisha washtakiwa au mahabusu kutoa eneo lile kwenda enei lingine ambapo bado inakuwa ni sehemu ya gharama za Serikali. Nimuombe tu Mheshimiwa Mbunge kwa sababu nina ahadi ya kutembelea Jimbo lake la Nyang’hwale tutajiridhisha kuona eneo kama lipo la kutoa ili Jeshi la Magereza liingize katika mpango wake wa ujenzi, nashukuru. (Makofi)
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Spika, ahsante, nami niulize swali dogo la nyongeza. Waziri unacheka kwa sababu unajua ninachouliza.

Mheshimiwa Spika, Kituo cha Polisi Bunda hakina hadhi ya Wilaya na kinahudumia majimbo matatu; ni lini sasa mtatuhakikishia mnatujengea kituo chenye hadhi ya Wilaya na hii ni zaidi ya mara kumi nakuuliza wewe hapo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, nashukuru, swali analoliuliza Mheshimiwa Bulaya najua kwamba Mbunge wa Jimbo ameshaniuliza mara kadhaa pia. Namuahidi tu kwamba pale Bunda eneo kilipo Kituo cha Polisi ni eneo dogo, limebanwa na barabara, kupitia jukwaa hili, nauomba uongozi wa Wilaya ya Bunda wapate eneo la kutosha kwa ajili ya kuweka mpango wa ujenzi wa Kituo cha Polisi cha hadhi ya Wilaya, nashukuru sana. (Makofi)

MHE. JOSEPH G. KAKUNDA: Mheshimiwa Spika, kwa miaka 14 tangu NIDA ianze kazi, pale Sikonge waliopatiwa vitambulisho ni watu 61,000 tu kati 91,000 ambao walipigwa picha, maana yake ni kwamba kuna watu 30,000 hawajapatiwa vitambulisho, sasa nina maswali mawili ya nyogeza.

Je, Serikali ina mkakati gani katika kipindi cha miezi sita itawapatia vitambulisho watu wengi hivyo 30,000, wakati wastani kwa mwaka imekuwa ni 4,300? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili; kwa kuwa bado tuna watu karibu 60,000 hawajapigwa hata picha na siku hizi kuna masharti, ukienda leseni unaambiwa sharti la NIDA na huduma nyingine.

Je, kwanini Serikali haioni umuhimu wa kuahirisha hayo masharti mengine ili wananchi wasiendelee kudaiwa kitambulisho cha NIDA wakati haiwezekani kupata? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, nashukuru, kuhusu swali la kwanza, uhakika ndani ya miezi sita kwamba tutakamilisha upatikanaji wa vitambulisho kwa wananchi ambao hawajapata, nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge na Bunge lako tukufu kwamba katika utekelezaji wa shughuli za Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa nadhani Wabunge wote mnafahamu kwamba kwa miaka karibu mitatu hadi minne, mkataba ulikuwa umekuwa frustrated kwa sababu mkandarasi alikuwa anadai muda mrefu na madai yake yalikuwa hayajalipwa. Kwa dhamira njema ya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan tatizo lile amelikwamua, ametoa fedha tukalipa madeni tuliyokuwa tunadaiwa na uzalishaji wa vitambulisho umeanza.

Mheshimiwa Spika, tulichofanya kama Wizara ni kumsisitiza mkandarasi, kwa sababu kuna wananchi wengi walikuwa wanasubiri vitambulisho hivi, awe na mpango wa kasi wa kuzalisha na namshukuru Waziri wa Mambo ya Ndani aliniruhusu nikaenda mpaka kwenye kiwanda, nimejiridhisha kuwa uzalishaji unaenda kwa kasi kubwa. Ndiyo maana tuna uhakika kwamba ifikapo Machi, wananchi wote ambao walikuwa hawajapata vitambulisho watapata vitambulisho hivyo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili; nimwondoe mashaka Mheshimiwa Mbunge. Tumeanza kuimarisha utendaji wa NIDA. Baada ya uzalishaji wa vitambulisho kuanza, NIDA imepanua uwezo wake kwa kuazima staff kutoka kwenye vyombo vyetu vingine vya usalama ili kuongeza kasi ya kuwafikiwa wananchi, waweze kupata zile namba za utambulisho.

Kwa hiyo, badala ya kusitisha zoezi zile, ngoja liendelee lakini tutaongeza idadi ya watu ili wananchi wako wa Sikonge ambao hawajapigwa picha na kupewa namba za utambulisho waweze kufanyiwa hivyo, nashukuru. (Makofi)
MHE. DKT. PIUS S. CHAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Serikali ninayo maswali mawili ya nyongeza. Katika Wilaya ya Manyoni, tuna Gereza la Wilaya na gereza hili wanajishughulisha sana na kilimo, lakini kuna changamoto sana ya zana za kilimo za kisasa. Nini mkakati wa Serikali kuhakikisha kwamba tunaliwezesha Jeshi la Magereza la Manyoni ili waweze kujikita kwenye kilimo cha kisasa hususan kupeleka matrekta?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili. Katika Gereza hilo hilo la Wilaya ya Manyoni tuna upungufu mkubwa sana wa nyumba za watumishi. Nini mkakati wa Serikali kuhakikisha kwamba sasa tunawajengea Maafisa Magereza nyumba za kisasa ili nao wajione ni sehemu ya Tanzania? Nashukuru sana.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu umuhimu wa kuwa na zana za kilimo za kisasa ikiwemo matrekta, huo ndio mwelekeo mpya wa Wizara ya Mambo ya Ndani kupitia Jeshi la Magereza kuimarisha vikosi vyake ili viweze kulima kwa tija. Kwa kufanya hivyo tumeimarisha Shirika la Uchumi la Magereza kwa maana ya SHIMA ili lianze kuzalisha kwa tija hatimaye magereza mengine ambayo hayajaingizwa katika utaratibu huu yaweze kuiga kutokana na kazi inayofanywa na SHIMA na moja ya vitendeakazi wanavyotumia ni matrekta. Kwa hiyo, Mheshimiwa atupe muda tu, tutakapokuwa tumeboresha, Gereza la Manyoni litafikiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu umuhimu wa kuwa na nyumba bora za watumishi pia ni kipaumbele cha Jeshi la Magereza na kwa sasa wanatumia nguvukazi ya Jeshi la Magereza ili kujiimarisha kwa kujenga nyumba zinazofaa. Kwa hiyo, nitumie nafasi hii kumwomba Mkuu wa Magereza Mkoa wa Singida awasiliane na wenzie wa Magereza yake ndani ya mkoa waanze miradi ya kujenga nyumba za maafisa ili Serikali kwa maana ya Magereza Makao Makuu yaweze kuwa–support vifaa vya kukamilishia majengo hayo, nashukuru. (Makofi)
MHE. PRISCUS J. TARIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa majibu ya Serikali, lakini kwanza niseme tu wamejibu upande mmoja, upande wa quality, yaani ubora lakini upande wa bei hawajagusia. Ninayo maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu sisi ambao tuko field tumeona kabisa utaratibu huu wa kukagua haufanyi kazi, kwa maana marobota yanayokuja sasa nchini yamejaa nguo chakavu ambazo haziwezi hata kuuzika; je, Serikali haioni namna ya kutafuta utaratibu mwingine wa kuhakikisha wanafanya ukaguzi mzuri? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili. Kwa kuwa bei imeonekana bado ni kubwa kutokana na kuwepo kwa madalali, lakini pia ubora unakuwa compromised kutokana na zile nchi nazo zimepigwa na uchumi: Serikali haina mpango mwingine wa kudhibiti biashara hii ili tusiwe dampo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu ufanisi wa ukaguzi wa mawakala tuliowapa kazi hiyo kwa mujibu wa maelezo ya Mheshimiwa Mbunge ambaye naamini anawakilisha wafanyabiashara wanaofanya biashara hii ni kwamba ziko chini ya kiwango. Wizara ya Viwanda na Biashara kupitia TBS itafanya uthamini juu ya utendaji wa mawakala waliopewa na kama itathibitika kwamba wanaleta mavazi ambayo yako chini ya kiwango kwa maana ya ubora, lakini na uchakavu hatua zitachukuliwa ikiwa ni pamoja na kuwafutia hizo leseni na kuwatafuta watu wengine wanaoweza kufanya kazi hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu bei kubwa ya bidhaa inayotoka kwenye hizo nchi alizozibainisha ambako ndiko wafanyabiashara wetu huchukua mizigo, Serikali kupitia Wizara hii ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji itafanya tathmini na kuangalia masoko mengine kwa maana ya nchi nyingine zinazozalisha bidhaa kama hizo zinazotafutwa na wawekezaji au wafanyabiashara kutoka Tanzania ili wale ambao watakuwa na bei nzuri, basi mwelekeo uwe katika nchi hizo kuliko kuendelea kutumia masoko ya zamani ambayo bei yake ni kubwa, nashukuru.
MHE. JANETH E. MAHAWANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali nilikuwa na maswali mawili madogo ya nyongeza. Swali la kwanza: Je, Serikali haioni haja sasa ya kuwasaidia wajasiriamali wadogo kutafuta masoko nje ya nchi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili. Nini mkakati wa Serikali kuwaandaa wajasiriamali hawa wadogo kuwa wawekezaji ndani ya nchi yao? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI K.n.y. WAZIRI WA UWEKEZAJI, VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu kuwatafutia masoko nje ya nchi, ndiyo maana utaona kuna majukwaa mbalimbali ya akina mama pamoja na makongamano yanayowakutanisha wafanyabiashara wanawake na wakati mwingine husafirishwa kwenda katika nchi mbalimbali kuhudhuria makongamano kama hayo kama njia ya kuwajengea uwezo na kutafuta masoko kwa ajili ya bidhaa wanazozalisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la pili la kuwawezesha wawe wafanyabiashara wakubwa, nimesema katika jibu la msingi kwamba Serikali imetoa fursa mbalimbali za kuwakopesha wafanyabiashara wakiwemo akina mama ili waweze hatimaye kuimarisha mitaji yao kuikuza na hatimaye wawe wafanyabiashara wakubwa. Ni matarajio yetu fursa mbalimbali zinazotolewa na Serikali hususan hii Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan itawezesha akina mama kuendelea kuongezeka katika idadi ya wafanyabiashara wakubwa katika nchi yetu, nakushukuru sana.
MHE. BAHATI KHAMIS KOMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi. Kwa kuwa fedha hizi tayari zimeshatengwa:-

(a) Je, ujenzi huu utaanza mwezi gani?

(b) Je, uko tayari tufuatane kwa pamoja ili kwenda kujiridhisha hali halisi ilivyo kwa nyumba zile? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyojibu kwenye swali la msingi, fedha hizi zimetengwa katika Bajeti ijayo 2023/2024. Kwa hiyo, wakati wowote baada ya mwezi Julai fedha zitakapotoka na ujenzi ukaanza, niko tayari kuongozana na Mbunge ili kwenda kushuhudia maendeleo ya ujenzi huo, nashukuru. (Makofi)

MHE. MARYAM AZAN MWINYI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Je, Serikali ina mpango gani wa kuzifanyia ukarabati nyumba za Polisi zilizopo Madungu Wilaya ya Chake Chake?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nilitembelea eneo la Chake Chake na kubaini mbali ya uchakavu wa Kituo cha Polisi cha ngazi ya Wilaya, vile vile nyumba za Askari zimechakaa sana. Hata hivyo, Serikali imeanza kujenga hanga moja ambalo litachukua Askari lakini tutaendelea kuzikarabati nyumba hizo kadiri tunavyopata fedha ili Askari wote waweze kukaa kwenye makazi yenye hadhi stahiki, nashukuru. (Makofi)

MHE. FAKHARIA SHOMAR KHAMIS: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naomba kumwuliza Mheshimiwa Naibu Waziri kwamba, ni lini ujenzi wa nyumba ya Kamishna wa Zanzibar itajengwa kwa vile hivi sasa anakaa uraiani?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, tunatambua kutokuwepo kwa nyumba yenye hadhi anakaa Kamishna wa Polisi ZanzIbar na katika bajeti hii inayoendelea tumeweza karabati ofisi ya kamishna. Hatua itakayofuata katika bajeti ijayo ni kuhakikisha kwamba nyumba ya Kamishna wa Polisi Zanzibar inajengwa na kukamilishwa, ahsante.

MHE. MINZA S. MJIKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante napenda kuuliza swali. Nyumba za askari polisi Wilayani Maswa ni za siku nyingi sana zimejengwa na mkoloni je, ni lini Serikali itajenga nyumba hizo upya ili ziwe na hadhi ya kuishi askari polisi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WIZARA YA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, natambua kwa upande wa Maswa si nyumba tu ambazo zimejengwa wakati wa mkoloni. Hata kituo cha polisi ngazi ya wilaya hakipo chenye hadhi stahiki. Katika bajeti ijayo tutaanza utaratibu wa kuweka fedha kwa ajili ya ujenzi wa hizo nyumba, lakini na kuanza kujenga kituo cha polisi chenye hadhi wilaya kama ambavyo imewahi kuulizwa na Mbunge wa Jimbo husika na tukamjibu hapa, ahsante sana.

MHE. OMAR ISSA. KOMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante je, ni lini Serikali itawajengea nyumba za kuishi Jeshi la Polisi Wilaya ya Micheweni?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kadri ambavyo tutapata fedha tutaendelea kuimarisha na kujenga Vituo vya Polisi na Makazi ya Askari. Kwa hiyo, Micheweni ni moja ya eneo litakalozingatiwa katika ujenzi wa nyumba za askari, ahsante. (Makofi)

MHE. FRANCIS L. MTEGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kuwa Kituo cha Polisi Chimala ni duni na makazi ya askari wale ni duni je, lini Serikali itaanza ujenzi wa kituo hicho pamoja na makazi?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, tunatambua jinsi ambavyo Chimala kunaendelea kwa kasi kule Mbarali na niwapongeze wananchi wa Chimala pamoja na uongozi wao akiwemo Mbunge na DC kuanza Ujenzi wa Kituo cha Polisi Chimala na hatua itayofuata ni kuingia ujenzi wa nyumba za makazi ya askari. Serikali itawaunga mkono pamoja na wadau kama ambavyo RPC ameanza kufanya ili kuhakikisha kwamba Chimala wanapata nyumba bora za kuishi, ahsante. (Makofi)
MHE. FESTO R. SANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Swali langu kule Makete hamna Nyumba za Jeshi la Polisi, ukienda Dodoma hapa nyumba za askari polisi hapa hazifai, ukienda Oster Bay Dar es Salaam hazifai ni upi mkakati mahususi wa Serikali wa kujenga nyumba za polisi nchini kama ambavyo JWTZ imefanya kwa ajili ya maaskari wao? Kwa hiyo tunaomba majibu ya Serikali kwa kushirikiana na National Housing.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa swali la mkakati zaidi. Niliwahi kueleza hapa katika moja ya maswali kwamba Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kupitia Jeshi la Polisi inao mpango wa miaka kumi wa ujenzi na ukarabati wa Vituo vya Polisi na Makazi kwa ajili ya Askari. Kwa hiyo, mpango tunao kazi tuliyonayo ni kutafuta fedha kadri tunavyoendelea utekelezaji tunapata fedha kutoka kwenye tozo lakini tutapata fedha kutoka kwenye bajeti ya maendeleo kwa madhumuni ya kujenga vituo na nyumba hizo. Kwa hiyo, maeneo yote yatafikiwa kadri ya upatikanaji wa fedha. (Makofi)
MHE. FELISTA D. NJAU: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Nashukuru kwa majibu ya Serikali, lakini na maswali mawili ya nyongeza, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa fire hydrants zinazotakiwa nchini ni 285,000 na zilizopo ni 2,348 sawa na asilimia 8.2 tu;

Je, Serikali haioni haja ya kujenga miundombinu hiyo ili kuzuia majanga makubwa ya moto yanatokea ili kuzuia pia Serikali kupata hasara na wananchi? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa changamoto hii inatokea katika miji na majiji makubwa;

Je, Serikali haiona sasa kuna haja ya kuweka miundombinu hiyo katika miji na majiji makubwa, kwenye masoko na shule ili pia kuzuia majanga hayo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru, ninakubaliana na Mheshimiwa Mbunge kwamba fire hydrants zilizopo ni chache hazilingani na zile zinazohitajika, na ndiyo maana Jeshi letu la Zimamoto na Uokozi linawasiliana na mamlaka zote za ujenzi za miji pamoja na mamlaka za maji kila wanapotekeleza miradi hiyo wazingatie uwekeji wa hizi fire hydrants.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa swali la pili ninakubaliana naye, kwamba miji mikubwa ndiyo iko kwenye changamoto kubwa zaidi ya kukumbana na majanga ya moto na kwa msingi huo mkazo zaidi utawekezwa kwenye miji mikubwa kadiri tunavyoendelea kuimarisha huduma za fire na uokozi.
MHE. ASHA ABDULLAH JUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, aah! Sorry, ahsante sana kwa kunipa nafasi.

Je, Serikali imewaandaje Askari wa Jeshi la Zimamoto katika uokoaji kwenye uvamizi wa nyuki katika makazi ya watu?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji kama ambavyo jukumu lake limebainishwa linashirikiana na mamlaka za misitu kila inapotokea janga kama hilo la nyuki kama ilivyotea siku tatu zilizopita hapa Dodoma, wameshirikiana vizuri sana wenzetu wa idara ya misitu kukabiliana na janga lile na kuwahamisha kabisa nyuki kutoka eneo lile. Nadhani ni jambo ambalo tunaomba wananchi inapotokea makundi ya nyuki kwenye maeneo yao wapige namba ya dharura inayoonyesha always 114 ili vyombo vyetu viweze kukabiliana nayo kabla haijaleta madhara kwa jamii zetu, nashukuru.
MHE. DENNIS L. LONDO: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kuniruhusu kuuliza swali la nyongeza. Juzi kulikuwa na ajali ambayo imepoteza maisha ya watu watano na majeruhi hali zao ni mbaya; jana kulikuwa na ajali ambayo imejeruhi majeruhi wanane ambao hali zao ni mbaya; na hizi namba ambazo tunapewa na Serikali 128 ni namba za ajali ambazo ni kubwa mno, zina madhara makubwa:-

Mheshimiwa Spika, Swali langu kwa Serikali:-

(a) Serikali haioni wakati umefika sasa kwa sababu ajali hizi zina athari kubwa na pana kwa jamii yote, kutangaza eneo hili kama ni janga?

(b) Serikali haioni wakati umefika sasa Wizara ya mambo ya ndani kukaa pamoja na TAMISEMI na Wizara ya Afya kuangalia Kituo cha Afya Mikumi na Hospitali ya Mtakatifu Kizito kama maeneo ya kimkakati ya uokozi wa majeruhi ambao unatokana na ajali hizi, badala ya kukichukulia kama wanavyokichukulia sasa hivi?

Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, ni kweli ajali hutokea na kadiri alivyosema, katika kipindi cha miaka hii 12 zimetokea ajali 128. Kwa takwimu zetu, ajali hizi zimekuwa zikishuka kadiri Serikali inavyoimarisha usimamizi wa sheria. Kwa mfano, mwaka 2010 tulikuwa na ajali 16 na majeruhi wakawa saba, vifo vinane; 2011 tulikuwa na ajali 14, vifo vitano na majeruhi 10, lakini kadiri miaka ilivyoongezeka ajali hizo zilipungua. Kwa mfano, mwaka 2021 ajali tano, vifo vitatu na majeruhi watatu; na mwaka 2022 ni ajali tano, vifo vitatu na majeruhi wawili.

Mheshimiwa Spika, kiukweli hata kama atakufa mtu mmoja, kwetu tusingependa kumpoteza kwa jambo ambalo lingeweza kuzuilika. Kwa hiyo, pamoja na dhamira yake kwamba litangazwe janga, sijaona kama kiwango hiki kinatufikisha mahali pa kutangaza kama hili ni janga.

Mheshimiwa Spika, hata hivyo, tutaendelea kuimarisha doria kama inavyofanyika kwa wenzetu wa Iringa, Askari hufuatilia magari haya, na kwa kweli kule ajali zimepungua sana. Kwa hiyo, kupitia Bunge lako Tukufu, tumwelekeze RPC Morogoro aanzishe utaratibu kama uliofanywa na mwenzie wa Iringa kuona kwamba magari yanafuatiliwa kwenye maeneo ambayo ni prone, yenye mwelekeo mkubwa wa ajali.

Mheshimiwa Spika, kuhusu kukaa pamoja kwa Wizara husika, nakubaliana na Mheshimiwa Mbunge kwamba tutaangalia kupitia ushirikiano wetu kwenye vikao vyetu vya Baraza la Taifa la Usalama Barabarani, wadau wote aliowataja ni Wajumbe ili kuona namna ya kuimarisha huduma za uokozi katika Kituo cha Afya Mikumi na Hospitali ya Kizito iliyopo pale Mikumi. Nashukuru sana.
MHE. JUSTIN L. NYAMOGA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Katika harakati za kuimarisha doria, Kituo cha Polisi cha Ruaha Mbuyuni hakina gari: Je, Serikali ina mpango gani wa kukipatia kituo hicho gari ili kuimarisha doria katika eneo hilo lililotajwa ili kupunguza ajali pia? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, ni kweli siyo vituo vyote vya Polisi vina magari. Tulichokifanya ni kuimarisha uwezo wa Makamanda wa Mikoa na wasaidizi wao kuwa na magari, lakini awamu inayofuata ni kuimarisha ngazi za Wilaya. Mheshimiwa Nyamoga Wilaya yako itapata gari kama haikuwa na gari la uhakika na tutakapoimarisha kwenye ngazi ya Wilaya tutaenda kwenye vituo vikubwa kama vya Ruaha Mbuyuni ili tuviimarishe. Kwa hatua za dharura tunaweza tukawapatia pikipiki za kuweza kuwawezesha wao kufanya ufatiliaji, nashukuru sana.
MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Bunge lako lilitunga sheria ya kutoza faini ya boda boda shilingi 10,000 kwa kosa ambalo mwendesha boda boda amefanya. Siku hizi kumetokea matatizo, boda boda sasa hawatozwi faini ya shilingi 10,000, badala yake wanapelekwa Mahakamani kutozwa faini ya shilingi 30,000. Nini tamko la Serikali kuhusu jambo hili?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, ni kweli hii faini anayoisema ya Shilingi 10,000/= ni ya papo kwa hapo, lakini wakati mwingine Polisi wanatathmini ukaidi na uzoefu wa hawa vijana kufanya makosa makubwa ya barabarani na hivyo huwapeleka Mahakamani ili Mahakama ambacho ndiyo chombo cha mwisho katika utoaji wa haki watoe hukumu kulingana na uzito au uzembe unaosababisha ajali.

Mheshimiwa Spika, kama amepelekwa Mahakamani na Mahakama imeamua vile, nadhani Mheshimiwa Mbunge tukubaliane. La muhimu ni kuwahimiza vijana wetu waepuke kufanya makosa wanayoweza kuyaepuka ambayo mengi yanasababisha ulemavu na vifo miongoni mwao, nashukuru.
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa majibu ya Serikali, pamoja na majibu ya Serikali nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Waziri unajua kwamba kumekuwa na changamoto sana ya uvamizi kwa wavuvi kuchukuliwa vifaa vyao ikiwemo injini pamoja na fedha na tunaposema boti tunazungumzia speed boti kwa ajili ya kuendana na wale wahalifu wanaotoka nje za jirani. Je, Serikali haioni kuna haja sasa ya kuwapa speed boti kwa maana ya fiber askari polisi ili waweze kuwalinda wananchi wetu na kupambana na wale wahalifu?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili Askari Polisi wa Nkasi wanapata changamoto kubwa sana kulingana na jiografia. Ni lini mtawapa gari pamoja na mafuta ya kutosha siyo kama hivi wanavyofanya sasa hivi ili waweze kuwajibika katika majukumu yao? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, tunatambua kwamba wakati mwingine wananchi wetu wanaathiriwa na majambazi hawa wanaopita maeneo ya ziwani kwa sababu wanakuwa na vifaa bora zaidi kuliko walivyokuwanavyo vijana wetu wa Jeshi la Polisi kwenye maeneo hayo. Kwa kulitambua hilo ndio maana nimeeleza katika boti tutakazonunua ni fiber zinazokwenda mwendokasi ili kukabiliana na hao majambazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu vijana wetu ambao wanahitaji magari, nimesema yatakapotoka tutawagawia na Wilaya yako ya Nkasi itanufaika na pamoja na Jimbo la mwenzio Nkasi Kusini ambaye ni Mjumbe wa Kamati yetu ya NUU wote tutahakikisha kwamba tunapata magari. Baada ya kupata magari hayo katika mwaka ujao pia tutaongezea vitendea kazi vingine zikiwemo pikipiki ili kuimarisha uwezo wa vijana wetu wa doria kwa magari na madoria kwa pikipiki, nashukuru sana.
MHE. FRANCIS I. MTINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili madogo ya nyongeza:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Serikali, kituo hiki kilikuwa na plan ya kuwa Kituo A na kilishajengwa msingi kwa ajili ya ghorofa na ghorofa hilo lingekuwa na nyumba juu kwa ajili ya OCD. Sasa kwa sababu wamebadilisha na kuwa Kituo B, Serikali sasa ina mpango gani wa kepeleka fedha kwa ajili ya kujenga nyumba pembeni kwa sababu, sasa nyumba haitakuwepo tena juu?

Swali la pili, Serikali ina mpango gani wa kupeleka gari la Polisi kwa sababu tuna shida kubwa ya magari katika Halmashauri ya Mkalama? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu nyumba kwa ajili ya Askari au Mkuu wa Kituo ni kweli kwamba, awali ilikuwa kiwe Daraja A, lakini Sera ya Jeshi la Polisi inatambua Kituo cha Polisi Daraja A ni kituo kikubwa akinachostahili kujengwa kwenye ngazi ya Mkoa kwa maana ya kuwa chini ya Regional Police Commander (RPC), lakini hivi vinavyotokea ngazi ya Wilaya vinapaswa viwe Daraja B. Kwa hivyo, nyumba ile itatengwa katika bajeti ya mwaka 2024/2025 kutoka kwenye mfuko wetu wa tuzo na tozo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu gari la Polisi, juzi nilijibu hapa kwamba, tumetenga bilioni 15 kwa ajili ya ununuzi wa magari ya Polisi, magari haya yatakapopatikana, Wilaya ya Mkalama ni moja ya Wilaya itakayopelekewa gari na pikipiki kuwezesha shughuli za ulinzi na usalama wa raia. Nashukuru.
MHE. MARYAM OMAR SAID: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuuliza swali la nyongeza:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na ufinyu na uchakavu wa ofisi za Makao Makuu ya Jeshi la Polisi, Mkoa wa Kaskazini Pemba. Je, ni lini Serikali itaanzisha ujenzi mpya kwa ajili ya ofisi hizi katika Mkoa huu?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, tunao mpango wa kujenga ofisi zote za Makao Makuu ya Polisi ngazi ya Mkoa. Kwa hiyo, tumeanza na Kusini Pemba, hatua itakayofuata ni Kaskazini Pemba ili Mikoa yote iweze kupata vituo vya Polisi vyenye ngazi ya Mkoa kwa maana ya Daraja A. Kwa hiyo, uwe na subira katika miaka miwili ijayo kituo hicho pia kitakuwa kimejengwa.

MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, toka mwaka 2015 nilikuwa nikiomba tujengewe Kituo cha Polisi katika Wilaya ya Kilindi. Naomba commitment ya Serikali juu ya ujenzi wa kituo hicho cha Polisi. Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimjibu Mheshimiwa Kigua kwa uhakika kabisa kwamba, ni kipaumbele cha Wizara kupitia Jeshi la Polisi kwamba, Wilaya zote ambazo hazina vituo vya Polisi zinajengewa vituo vya Polisi. Nikupe assurance Mheshimiwa tutaangalia kwenye mpango wetu namna gani tunaweza tuka-fast track kutokana na majukumu muhimu ambayo Lindi inakabiliana nayo kwa maana ya uhalifu, mifugo, na kadhalika ili waweze kuwa na kituo cha polisi kumwezesha OCD kutimiza majukumu yake vizuri. Nakushukuru sana Mheshimiwa.
MHE. BONIPHACE N. BUTONDO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi niulize maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ninaipongeza Serikali kwa jitihada hizi ambazo imeweka mipango ya kuhakikisha kwamba, mwaka 2023/2024 ujenzi huu unakamilika.

Swali langu la kwanza, Mheshimiwa Naibu Waziri uko tayari kuambatana na mimi ili kwenda kuona jitihada zilizofanywa na Mfuko wa Jimbo wa kwangu kama Mbunge, lakini nguvu za wananchi, wadau wa maendeleo kama Mgodi wa Mwadui Williamson?

Swali la pili, Mheshimiwa Waziri, utakuwa tayari pia kwenda kuona jitihada kubwa zinazofanyika za kupata eneo katika Mji Mdogo wa Maganzo, ili tuweze kujenga kituo kingine kwa sababu Kituo kile cha Maganzo ni chakavu na bado kinahudumia Kata tano, Kata ya Mwadui Luhumbo, Kata ya Mondo, Kata ya Songwa na Kata ya Maganzo yenyewe ili kwamba, tuone namna ya kuweza kuwapa huduma kwa usahihi na katika hali ya ubora wananchi wanaozunguka maeneo hayo?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza tumpongeze Mheshimiwa Mbunge kwa juhudi anazofanya na wadau walioko Kishapu katika ujenzi wa vituo vya Polisi kwa ajili ya usalama wa mali za wananchi na wananchi wenyewe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu utayari wangu kuongozana nae, Mheshimiwa nimeshakuahidi na hapa ninathibitisha kwamba, baada ya kumaliza Bunge letu hili mwezi Julai nitakuwa tayari kwenda Kishapu, pamoja na mambo mengine, kuona jitihada za wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini njambo la pili, tunatambua kweli katika Mji Mdogo wa Maganzo kuna shughuli nyingi za kibiashara na huko kwenye Mgodi muhimu wa Mwadui wa madini ya Almasi. Tunatambua uchakavu wa kituo kilichopo na kwamba kimebanwa sana na wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo ambalo naweza nikashauri mapema kabla sijaja huko, ni kupata eneo ili tukiona kwamba eneo hilo linatosha tuliingize kwenye mpango wetu wa kujenga kituo kinachostahili kwenye eneo hilo la Maganzo. Nashukuru.
MHE. ZUENA A. BUSHIRI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kunipa nafasi kuuliza swali la nyongeza:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, je, ni lini Serikali itakamilisha ujenzi wa Kituo cha Polisi Siha?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ambavyo nimekuwa nikijibu hapa, kwa maeneo ambayo tumeona jitihada za Halmashauri na wananchi katika ujenzi wa vituo vya polisi ni kipaumbele cha Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi pamoja na Jeshi la Polisi kuwaunga mkono ili kukamilisha. Tutaangalia katika mipangilio yetu namna ambavyo tunaweza tukapata fedha kupitia ama vyanzo vya fedha za maendeleo kutoka Serikali Kuu au fedha za tuzo na tozo kuwaunga mkono wananchi wa Siha kukamilisha kituo chao cha Polisi, nashukuru.

MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa nafasi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wa Kata ya Goba, Mtaa wa Tegeta A wameweka nguvu zao nyingi sana kujenga Kituo Polisi chenye hadhi ya ghorofa moja kuungana na nguvu za Mbunge Mfuko wa Jimbo. Je, Mheshimiwa Waziri utakuwa tayari kuja Kibamba kuona ile kazi kubwa iliyofanywa na wananchi wale wa Tegeta A juu ya ukamilishaji wa kituo hicho?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, niko tayari. Kwa juhudi zinazofanywa na Mheshimiwa Mtemvu na wananchi wake na wadau wengine katika jimbo lake niko tayari kwenda kushuhudia jitihada hizo na kuelekeza kuwaunga mkono kutoka Jeshi la Polisi ili kukamilisha vituo ambavyo tayari wameshavianzisha kwenye Jimbo lake, nashukuru.
MHE. MARTHA F. MARIKI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipatia nafasi niweze kuuliza swali dogo la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Tanganyika hatuna kabisa Kituo cha Polisi, lakini wananchi wa Wilaya hiyo wameonesha juhudi kwa kuanzisha ujenzi wa kituo cha polisi kwa kujenga msingi. Je, ni lini Serikali itaunga juhudi hizo kwa kutupatia pesa ili tuweze kukamilisha kituo hicho?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimuahidi Mheshimiwa Mariki kwamba, tunatambua umuhimu wa kuwa na Kituo cha Polisi chenye hadhi ya Wilaya na vituo vingine kwenye Tarafa husika katika Wilaya ya Tanganyika. Nimuahidi tu Mheshimiwa Mbunge, tumeshaongea hata na Mbunge wa Jimbo kwamba, kwenye bajeti yetu ijayo tutaona uwezekano wa kuwachangia ili waweze kujenga kituo hicho, tumuombe Mwenyezi Mungu liwezekane liweze kutekelezwa, nashukuru.
MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali dogo la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, je, Mheshimiwa Waziri utakuwa tayari baada ya Bunge hili kufanya ziara kuja kuangalia nguvu za wananchi na Mbunge katika ujenzi wa Kituo cha Polisi kwenye Kata ya Nyijundu, Wilayani Nyang’hwale?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamuahidi nikitoka Shinyanga kwenda Nyag’hwale ni karibu sana, kwa hiyo, wakati namaliza ziara yangu Shinyanga pale Kishapu, kituo kitakachofuata ni Nyag’hwale ili kuona juhudi za wananchi hatimaye tumuunge mkono Mheshimiwa Mbunge. Nashukuru sana.
MHE. JOSEPH G. KAKUNDA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana, kwanza niishukuru sana Serikali kwa usikivu na kusikia ushauri wetu sisi Wabunge, kama ilivyo kwenye Ibara ya 63(2), nashukuru sana.

Mheshimiwa Spika, sasa swali langu; je, Serikali itakuwa tayari wakati wanapokamilisha hiyo rasimu ya sheria kunikaribisha na mimi nitoe maoni yangu moja kwa moja?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, kama ilivyo ada ambapo utungaji wa sheria unahusisha wadau mbalimbali wakiwemo Waheshimiwa Wabunge na Kamati yako ya Kudumu ya Bunge, Mheshimiwa Mbunge kwa kweli ataalikwa na atashiriki katika hata hatua za mwanzo hadi sheria itakapokamilika, nashukuru. (Makofi)
MHE. KASALALI E. MAGENI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru; bodaboda maeneo ya vijijini ndiyo chombo kikuu cha usafiri kinachotumika kubeba wagonjwa kuwapeleka hospitali; na ili mgonjwa abebwe kwenye bodaboda inabidi abebwe mishikaki, awepo mtu wa kumshikilia, lakini Sheria ya Usalama Barabarani inazuia jambo hilo.

Nini tamko la Serikali juu ya watu wa vijijini wanaotumia bodaboda kupeleka wagonjwa hospitali? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, kiukweli ni hatari sana watu kutumia bodaboda kwa utaratibu wa mishikaki, na kwa mujibu wa sheria ni hatari kwa usalama wao na maisha yao, na nikiwa Naibu Waziri kwenye Wizara yenye dhamana ya usalama wa raia na mali zao, siwezi kutoa kauli ya kuhalalisha jambo ambalo linaweza likahatarisha usalama wa maisha wa wananchi wetu.

Mheshimiwa Spika, ushauri wetu, kama wanaona bodaboda ni chombo, kwa sababu ina magurudumu mawili, tunaweza tukashauri wakatumia chombo kilicho na magurudumu mawili kama baiskeli kuliko kutumia bodaboda ambayo katika kubadili gia, hawa wawili wote wanaweza wakajikuta wamedondoka na wakaathirika kiafya kinyume cha matarajio ya ndugu yetu.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo mimi nishauri tu kwamba tuendelee kuimarisha maeneo yetu na kwa namna ambavyo nchi yetu inazidi kuimarika, bila shaka muda mfupi ujao maeneo mengi yatakuwa na usafiri, kwa mfano magari ya michomko, yapo mpaka vijijini, japo hayaruhusiwi kubeba abiria, lakini tumeyavumilia kwa sababu ya mazingira yale, lakini kwenye boda boda ni hatari, hatuwezi kuruhusu jambo hilo.

SPIKA: Kwenye baiskeli ni sawa? (Makofi/Kicheko)

NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, nimesema baiskeli kwa sababu ya mwendo wa baiskeli, lakini kiti cha baiskeli kinabeba mtu mmoja tu. Mwendo wake ni mdogo, anatumia nguvu kazi ya yeye mwenyewe, lakini boda boda ni machine, ni engine sasa ile ni hatari kwa sababu ya ule mwendo wake na kadharika. Baiskeli kumbeba mgonjwa na ndio usafiri tumekuwa tukiutumia maeneo mengi ya vijijini. Tumetumia baiskeli za kwenda taratibu, lakini hii ya bodaboda ni hatari hata sio kwa mgonjwa hata wazima, tunawashauri wasitumie usafiri huo kama mshikaki.

SPIKA: Mimi nilitaka kuelewa tu sehemu ndogo, yaani kwamba kwenye baiskeli yule anayeendesha baiskeli akibeba watu wawili zaidi ni sawa?

NAIBU WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Hapana, kusudio langu abebe mtu mmoja na kile kiti kina uwezo wa kubeba mtu mmoja. Mwendo wake ndio nilisema kwa sababu ya tahadhari anayoisema Mheshimiwa Mbunge kwamba mgonjwa anatakiwa apate mtu wa kum-support kwa mwendo wa pikipiki hilo haliwezekani, lakini kwa baiskeli mwendo ule ni mdogo na familia nyingi zimekuwa zikibeba watu hao kwa baiskeli na wanafika, lakini sio pia mshikaki lakini hata kile kiti hakiwezi kubeba mshikaki.
MHE. JOSEPHINE J. GENZABUKE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru, pamoja na majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza. Kituo cha Muhange kipo mahali ambapo lipo soko la Ujirani Mwema na mara nyingi hutokea uhalifu na kutokana na ukosefu wa gari, Maaskari wa eneo hilo hulazimika kuazima pikipiki kwa Diwani wa eneo hilo. Ni lini sasa Serikali itapeleka japo pikipiki kwenye Kituo hicho? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili. Kituo cha Kitanga katika Wilaya ya Kasulu kiko mpakani, eneo hilo linatenganishwa na Mto Malagalasi, ukitoka Kitanga kwenda Malagalasi unavuka Mto Malagalasi. Kwa hiyo naangalia ni jinsi gani kuna umuhimu wa kupeleka gari katika eneo hilo, na eneo hilo, kutoka Kitanga kwenda Kasulu Mjini ni kilomita 150, katika eneo hilo hutokea ujambazi mara nyingi.

Ni lini sasa kwa umuhimu wa eneo hilo Serikali itapeleka gari ili kunusuru maisha ya wananchi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Genzabuke kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Genzabuke kwa kufuatilia kwa karibu sana masuala ya usalama katika Mkoa wa Kigoma na hususani katika hizo Wilaya alizozirejea Kankonko na Kasulu. Hata hivyo nimjibu tu kwamba tumpongeze Mheshimiwa Diwani kama moja ya wadau aliyetoa vyombo vya usafiri kama pikipiki na kama ambavyo Mkurugenzi wa Wilaya ya Kankonko pia ameahidi kutoa pikipiki ili kusaidia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumezungumza hapa kwamba Wizara kupitia Jeshi la Polisi itapata magari zaidi ya 300 ifikapo mwezi Septemba na maeneo yenye changamoto kubwa za kiusalama kama haya ya mipakani yatapewa kipaumbele. Kwa hiyo nimuondoe shaka Mheshimiwa Genzabuke. (Makofi)
MHE. MARYAM AZAN MWINYI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali moja la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa Wilaya ya Mkoani, Mkoa wa Kusini Pemba ina vituo Vinne vya Polisi ambavyo vina gari moja ambalo lilipatikana mwaka 1980. Je, Serikali ina mpango gani wa kuwapelekea gari nyingine? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema kwenye majibu wakati najibu swali la msingi kwamba tunao mpango wa kuimarisha usafiri kwenye maeneo yote ambayo yana changamoto ya usafiri ikiwemo Mkoa wa Kusini Pemba. Kwa hiyo, kulingana na vipaumbele na mahitaji ya magari, magari tutakayoyapata mapema iwezekanavyo yale 78 Mkoa wa Kusini Pemba pia utazingatiwa. (Makofi)

MHE. IDDI K. IDDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Jimbo la Msalala, Halmashauri ya Msalala ina Kituo cha Wilaya na haina gari la Polisi. Kama unavyofahamu kwenye maeneo yetu ya uchimbaji usalama ni hatari sana ukizingatia kwamba kwa sasa kumeanza kuibuka makundi mbalimbali. Sasa ni lini Serikali itachukua hatua za dharura wakati ikisubiria mpango wa kuleta magari yale mengine, ichukue hatua ya dharura ili kuhakikisha kwamba wanatupatia gari la Polisi tuweze kukabiliana na uhalifu katika eneo hilo?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Iddi kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, natambua ni kweli kwamba maeneo ya migodi ni maeneo yanayovutia pia matendo ya uhalifu. Kwa hiyo tutakaa na Mheshimiwa Mbunge ili tukae na RPC wa Mkoa wa Shinyanga kuona kama pana magari ya ziada basi sehemu ya magari yale yahamishiwe kwenye Wilaya hii ya Kahama ili kuimarisha usafiri kwenye eneo hilo. (Makofi)
MHE. FRANCIS I. MTINGA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Pamoja na majibu mazuri sana ya Serikali ninamaswali mawili madogo ya nyongeza.

Kwa kuwa mfumo wetu wa bajeti niwakutumia kadri unavyokusanya. Je, na kwa sababu kituo hiki ni cha Wilaya na ni chamuhimu sana Waziri ananiambiaje kuhusu kunipa kipaumbele katika fedha za maendeleo za kwanza tu zitakazopelekwa katika bajeti inayoanza Julai? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili; kwa upya wa Wilaya ya Mkalama tuna askari 83 tu, tuna upungufu wa askari 57. Je, Waziri ananipa commitment gani kuhusu vijana askari wanaomaliza kozi muda mfupi ujao kupeleka katika Wilaya yangu? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Mtinga kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, moja; tunamuhakikishia kwamba fedha zilizotengwa katika mwaka wa fedha ujao shilingi milioni 992 tutahakikisha kwamba zinapelekwa katika jimbo lake ili kukamilisha kituo hicho kama kipaumbele miongoni mwa vipaumbele vilivyotajwa na Waziri wakati wa kuwasilisha bajeti yake.

Mheshimiwa Spika, pili; tunatambua kwamba wanao askari 84 na katika mgao wa askari wanaotarajia kumaliza mafunzo zaidi ya 4000 waliopo vyuoni Wilaya ya Iramba ni moja ya maeneo ambayo yatazingatiwa ili kuhakikisha kwamba wanapata askari wa kutosha, ahsante. (Makofi)
MHE. OLIVER D. SEMUGURUKA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kuniona.

Mheshimiwa Spika, Kituo cha Polisi kilichopo Kata ya Keza Wilayani Ngara kilijengwa kwa nguvu za wananchi, lakini mpaka sasa hakijamalizika; je, ni lini Serikali itamalizia kituo hicho? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Oliver Semuguruka kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba wananchi wa Ngara wamejitahidi kujenga kituo hicho na tunampongeza Mheshimiwa Mbunge kwa ufuatiliaji wake pamoja na Mbunge wa Jimbo la Ngara na ahadi yetu ni kwamba katika mwaka ujao vituo vya kumalizia kwa mujibu wa bajeti yetu ni 13, vituo vingine vitaendelea kupangwa kwa kipaumbele katika bajeti zinazofuata katika miaka ijayo huko mbele. (Makofi)

MHE. IDDI K. IDDI: Mheshimiwa Spika, ahsante; Wilaya ya Kahama ina Halmashauri tatu ambapo kila Halmashauri mmeanzisha vituo vya Wilaya lakini vituo hivyo vya wilaya havina vituo vya polisi.

Sasa nataka kufahamu ni lini Serikali itaanzisha ujenzi wa kituo cha polisi nakwakuzingatia kwamba mimi Mbunge wao nipo tayari sasa kutoa tofali 4000 ili tuanze ujenzi huo haraka iwezekanavyo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Iddi Kassim, Mbunge wa Kahama kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwanza tumpongeze kwa juhudi zake za kusaidia sekta ya usalama wa raia na mali zao kwa kuchangia idadi hii ya 4,000 ya matofali lakini mpango wetu ni kujenga vituo vya polisi vya Wilaya zile halmashauri ni kuimarisha tu kwa kuweka vituo vingine kwa hivyo kipaumbele kitakuwa kujenga kituo kikuu cha Wilaya ya Kahama na zile Halmashauri zitaendelea kuwekewa vituo visaidizi kwa ngazi ya tarafa na kata kama ambavyo sera yetu ya usalama wa raia inavyoelekeza. (Makofi)
MHE. NASHON W. BIDYANGUZE: Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo hili analotolea majibu kwamba halina hati, lina kituo kidogo cha Polisi cha muda mrefu; na eneo hili halina mgogoro; sasa ni kwanini Serikali isijenge na hiyo hati ikaja kupatikana baadaye kwa sababu hakuna anayelalamikia eneo hilo?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, wilaya yangu ni kubwa sana na ni mpya, lakini OCD hana gari ya kufanyia kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Nashon William Bidyanguze, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza tumpongeze Mheshimiwa Nashon kwa ufuatiliaji wake wa karibu wa masuala ya ulinzi na usalama kwenye jimbo lake. Pia tumtie moyo kwa namna anavyoshirikiana na uongozi wa Wilaya ya Kigoma na kwa sababu tunafahamu hata hili jengo linalotumika sasa ni lile ambalo Halmashauri imetoa kuiazima Jeshi la Polisi waweze kufanya shughuli zao, kwa hiyo, tunakushukuru sana Mheshimiwa Bidyanguze.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya maelezo hayo sasa nijibu swali lako kwamba kama kweli hakuna mgogoro, basi tutamwagiza OCD na RPC wa Mkoa wa Kigoma kufuatilia kwa haraka, kwa sababu maelekezo ya Serikali ni kwamba maeneo yote ya Serikali yapate hati ili kuondoa uwezekano wa migogoro huko mbele. Kwa hiyo, hati itakapokuwa imetoka na kwa sababu hati inatolewa na Halmashauri na mahusiano yenu ni mema, bila shaka wataharakisha kutoa hii hati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la gari, tumejibu hapa mara nyingi Mheshimiwa Mbunge, kwamba magari ambayo tunatarajia kuyapata ifikapo Septemba ni zaidi ya 370. Tunatarajia maeneo yenye changamoto kama hili la kwako la Kigoma ambalo liko karibu na maeneo ya mpakani yatazingatiwa kama maeneo ya kipaombele.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. (Makofi)
MHE. JAFARI W. CHEGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Wilaya ya Rorya, ni moja ya wilaya ambayo ipo kwenye kanda maalum kwa maana ya Tarime na Rorya, lakini ni wilaya ambayo haina Kituo cha Polisi cha Kiwilaya, ina Vituo vya Polisi vya Kikanda kwa maana ya Utegi, Kinesi na Shirati. Nataka nijue mpango mkakati wa Serikali wa kujenga Kituo cha Polisi cha Wilaya nzima ya Rorya, itakuwa iko kwenye mpango kule?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Chege, Mbunge wa Rorya, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli tunafahamu kwamba ziko wilaya nyingi hasa hizi wilaya mpya hazina vituo vya wilaya ya Polisi, ikiwemo hii Wilaya ya Rorya. Mpango wa Serikali kama ilivyosemwa wakati Waziri akiwasilisha hotuba yake hapa; tuna mkakati wa kujenga vituo vya Polisi kwenye mikoa ambao hawana vituo vya Polisi kwa ajili ya RPC na vilevile kwenye wilaya ambazo hazina Vituo Vikuu vya Polisi vya Wilaya. Kwa hiyo, mpango huo kadri tutavyokuwa tunapata fedha utaekelezwa, na Wilaya ya Rorya itakuwa ni moja ya wilaya ya vipaumbele kwa sababu iko mpakani.
MHE. ALOYCE J. KAMAMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto inayowakabili wananchi wa Uvinza, inakwenda sambamba na Wilaya ya Kakonko. Mkuu wa Polisi wa Wilaya hana ofisi, anatumia iliyokuwa Ofisi ya Polisi ya Kata. Kwa hiyo, Waziri anaweza akaona hali halisi:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, nini kauli ya Serikali katika kuhakikisha kwamba Wilaya ya Kakonko nayo inapata Kituo cha Polisi? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema kwenye majibu ya msingi, wilaya zote mpya hazijawa na vituo vya Polisi vya ma-OCD. Ndiyo maana tumekuja na mkakati wa kujenga vituo hivyo kwenye maeneo ambayo hayana. Katika bajeti iliyopita tutaanza ujenzi wa vituo hivyo, lakini kipaumbele kitawekwa kwenye maeneo yaliyoko mpakani ikiwemo hii Wilaya ya Kakondo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru.
MHE. DEODATUS P. MWANYIKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Njombe, ni miaka 10 toka umeanzishwa na mpaka leo hatuna Kituo cha Polisi kinachoendana na hadhi ya mkoa? Ni lini sasa kituo hicho cha Polisi kitajengwa katika Mji wa Njombe?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mwanyika, Mbunge kutoka Njombe, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyokwishasema, tunatambua mikoa mipya iliyoanza kwenye miaka ya 2012 ukiwemo Mkoa wa Njombe, hauna kituo kikuu cha Polisi kwa maana Ofisi ya RPC. Kwa kweli Mkoa wa Njombe tayari uko kwenye mpango na Mheshimiwa Mbunge anajua. Katika vipaumbele ambavyo mwaka huu tunaendelea navyo, ni ujenzi wa ofisi ya RPC Njombe. Nadhani baada ya Bunge hili tutatembelea maeneo hayo kuona maandalizi na harakati za ujenzi zinavyoendelea Meshimiwa Mwanyika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. (Makofi)
MHE. ABDALLAH J. CHAUREMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kujua ni lini Serikali itakijenga kwa hadhi ya Kituo cha Polisi Mbagala?

NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Chaurembo kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli swali hili ni moja ya maswali ambayo yako kwenye mpango wa kujibiwa, lakini niseme tu kwamba tunajua Mkoa wa Dar es Salaam, ikiwemo Wilaya ya Temeke, na Majimbo ya Mbagala, na majimbo mengine ya maeneo ya Kigamboni, kuna vituo vidogo vya Polisi vingi kuliko vituo vya ngazi ya wilaya. Tunaendelea na mpango mkakati wa ujenzi wa vituo hivi kwa kuangalia maeneo ambayo yana uhitaji mkubwa kutokana matukio ya uhalifu ili kuyazingatia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naamini Mbagala kwa sababu ya wigi wake wa watu, matukio ya uhalifu pia yatakuwa mengi, tutakizingatia katika mpango huu wa ujenzi.

MHE. JESECA J. MSAMBATAVANGU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Kwa kuwa viongozi wa Wizara ya Mambo ya Ndani wana afya nzuri ya akili, ni lini sasa watatujengea nyumba za askari katika Kituo Kikuu cha Polisi pale Iringa Manispaa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, tunashukuru Balozi wa Afya ya Akili anatambua jinsi tulivyo timamu. (Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahadi yangu ni hiyo, kwamba katika ujenzi wa vituo vya Polisi huenda sambamba na ujenzi wa nyumba za Maaskari, Wakaguzi na Maofisa. Kwa hiyo, Iringa kama alivyosema ni mjini, ukiangalia kwa vipaumbele, pale angalau watu wanaweza wakapata nyumba zenye hadhi za kupanga, lakini kuna maeneo ya vijijini kabisa ambayo uwezekano wa kupata nyumba za kupanga ni changamoto.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kwenye ujenzi wa nyumba, vipaumbele tutaweka kwenye maeneo ambayo yana changamoto kubwa za kupata makazi. Kwa hiyo, wale wa Iringa watasubiri, lakini kadri fedha zitakapopatikana na wao pia watajengewa.
MHE. JANEJELLY J. NTATE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Pamoja na juhudi nzuri za Serikali za kufungua kituo hiki siku nne zilizopita, lakini nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na tishio la panya road waliojaa Dar es Salaam, Serikali haioni haja ya kituo hiki kufanya kazi masaa 24 kama jibu linavyosema, badala ya masaa nane ambayo kinafanya sasa hivi kuanzia saa tatu mpaka saa nane? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, Serikali haioni haja Kituo cha Kiburugwa kwa kata ya jirani kukikarabati ili kiendane na mazingira bora ya watumishi wa Polisi kufanyia kazi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Ntate Mbunge wa Viti Maalum Dar es Salaam, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, moja; hili la kufanyakazi saa 24 ndiyo maagizo ya wizara na ni maagizo ambayo IGP ameyapokea na kuelekezwa kwa viongozi wa Polisi Kanda, Mkoa na Wilaya za Dar es Salaam. Kwa hiyo, nitasisitiza kwamba hili lifanyike kwasababu tayari kuna askari sita na mkaguzi mmoja ambaye ni Mkuu wa Kituo hicho hakuna sababu zozote za msingi za kufanya kazi chini ya masaa ishirini na nne.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu kukarabati kituo cha Kiburugwa kama alivyokwishasema Mheshimiwa Mbunge nakubaliana nae baadhi ya vituo vilivyo katika hali mbaya vinahitaji kukabaritiwa hii ni moja ya kuweka mazingira bora ya askari wetu kufanya kazi lakini pili kuwahudumia hawa ambao wanapelekwa vituo wawe katika mazingira bora zaidi. Kwa hiyo, nakubaliana na wewe Mheshimiwa tutatafuta fedha kwaajili ya kukabarati vituo vilivyochakaa kikiwemo hiki cha Kiburugwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. (Makofi)
MHE. DOROTHY G. KILAVE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, swali langu ni dogo sana lakini la uhakika. Je, ni lini Serikali itakipandisha hadhi Kituo cha Polisi cha Tandika ambacho tunatumia kata kama tano kwenda pale na sasa unaona kama kuna uhalifu mkubwa sana upande ule. Je, ni lini sasa mtakipandisha hadhi hata kipate class B ili tuweze kuona kwamba kazi nzuri inafanyika? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Kilave kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze kwa namna anavyofuatilia masuala ya ulinzi na usalama katika Mkoa wa Dar es Salaam mara kadhaa amenisumbua kidogo kuhusu hata njia inayokwenda Mbagala kupitia eneo la polisi na tumeshakubaliana ile njia itafunguliwa Mheshimiwa Mbunge lakini kuhusu ili la kupandisha hadhi kwa kupitia Bunge lako Tukufu namuelekeza Kamishna Kanda Maalum ya Dar es Salaam na Uongozi wa Polisi wa Mikoa ya Kipolisi Dar es Salaam kufuatilia, kupima na kufanya tathimini ya mahitaji ya kupandisha hadhi kituo hiki kama sababu alizozisema Mheshimiwa Mbunge zipo basi waone uwezekano wa kukipandisha ili kikidhi mahitaji ya eneo la Tandika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru.
MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Vituo vya Polisi vidogo yaani kwamaana ya outpost nyingi zimechakaa sana zina hali mbaya nyingi zinavuja mapaa mbao zimeoza yaani hata hao mapolisi wanaofanyakazi huko vijijini Mungu anawalinda. Ningetaka kujua ni lini sasa Serikali itakarabati vituo hivi vidogo vyote Tanzania nzima ili viweze kuwa na hadhi ambavyo vinafaa kuwahudumia wananchi?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Esther Matiko Mbunge Viti Maalum kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunatambua na nimesema kwenye majibu yangu ya msingi kwamba tunatambua uwepo wa uchakavu kwa baadhi ya vituo vya polisi vikiwemo hivi vituo vidogo. Katika mkakati wetu wa ujenzi na ukarabati wa maeneo haya tutazingatia pia hivi vituo vidogo vya polisi kama ambavyo tumeanza kufanya kwenye maeneo mengine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru.
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Mji wa Wilaya ya Liwale kijiografia imekaa vibaya sana hasa kwa ulinzi tunayoahadi ya kujengewa vituo vya polisi kwenye Tarafa ya Kibutuka, Kata ya Lilombe na Kata ya Kimambi. Nini kauli ya Serikali juu ya kutekeleza ahadi hiyo ili kuimarisha ulinzi kwenye Wilaya yetu ya Liwale? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Kuchauka Mbunge wa Liwale kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, japo hajaniambia ahadi ilitolewa na nani lakini nikiri tu, kwanza maeneo yote ya tarafa yanahitaji kuwa na vituo vya polisi vyenye hadhi ya kutimiza majukumu ya ulinzi na usalama wa wananchi na mali zao zikiwemo hizi tarafa ulizozitaja za Liwale kwa maana ya Kibutuka na tarafa hizo nyingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kulingana na bajeti tuliyonayo tunakwenda kwa awamu. Kama tulivyokubaliana na Mheshimiwa Kuchauka tutafanya ziara Mkoa wa Lindi ili kuona uhitaji wa vituo hivi ili kuweka msukumo kwenye jeshi la polisi waweze kuvizingatia katika mipango yao ya ujenzi na ukarabati wa sekta nzima ya polisi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru.
MHE. NUSRAT S. HANJE: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu hayo wafungwa na mahabusu wamekuwa wakifanyiwa ukaguzi hadharani kwa kuvua nguo zote bila kujali umri wao; na kwa uzoefu wangu mimi, upo uwezekano wa kuwakagua kwa kuwatenganisha lakini kuweka chumba maalum, lakini Serikali imekuwa haifanyi hivyo; pamoja na kwamba Serikali imenunua scanner 12 kwa ajili ya kufanya ukaguzi: Ni kwa nini sasa Serikali isione haja ya kutenga chumba maalum kwa ajili ya kuwakagua na kuwatenganisha ili kulinda staha na haki za binadamu? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili: mavazi ya wafungwa yamechakaa mno jambo ambalo linasababisha wafungwa wanawake warithi mpaka nguo za ndani za wafungwa wenzao ambao walimaliza muda wao, jambo ambalo kwa kweli siyo sawa: Ni kwa nini sasa Serikali isione haja kwanza ya kuondoa utaratibu huo na pia kupeleka mavazi kwa ajili ya wafungwa, pamoja na magodoro, mablanketi na neti?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Nusrat Mbunge kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimshukuru Mheshimiwa Mbunge lakini swali letu la msingi lilikuwa linazungumzia kukarabati magereza sasa imeibuka hili la mavazi na kukaguliwa hadharani. Lakini nadhani tupokee katika ukarabati na ujenzi wa magereza yanayokuja tutazingatia umuhimu wa kuwatenganisha wafungwa wote wanaume na wanawake wakati ukaguzi unapofanyika.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu mavazi kuchakaa kama mlivyosikia wakati wa bajeti, bajeti yetu mwaka huu imeongezeka kiasi ambacho maeneo ambayo yalikuwa hayapati funding kama haya ya mavazi ya wafungwa yatapewa kipaumbele ili waweze kupata mavazi yanayowastiri nakuleta staha kwa jumuiya hiyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru.
MHE. DEODATUS P. MWANYIKA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali dogo la nyongeza. Magari yanayotumika kuwapeleka mahabusu na wafungwa mahakamani kwenda na kurudi yana uchakavu mkubwa sana. Ni lini sasa Serikali itafanya utaratibu wa kubadilisha magari hayo?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Deo Mbunge kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwamba ni kweli kwamba magari katika maeneo mengi yamechakaa na kama mtakumbuka tumesema mwaka huu kuna bajeti imeongezeka haitaweza kutatua matatizo yote ya uchakavu wa magari ya mahabusu lakini at least tutaanza kununua kulingana na upatikanaji wa fedha.

Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru.

MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Gereza la Mbulu lilijengwa toka ukoloni, na kwa kuwa gereza hilo haliko kwenye magereza yaliyotajwa hivi sasa kwenye mpango wa ujenzi. Je, ni lini Serikali itajenga upya gereza la Mbulu na makazi ya Askari?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyokwisha kusema katika jibu la msingi kulingana na upatikanaji wa fedha tutaendelea kukarabati magereza yote yaliyochoka ikiwemo hili gereza la Mbulu. Lakini kwa mwaka huu wa fedha tumebainisha magereza yaliyotengwa kwa sababu ya ndio fedha tuliyopata lakini kwa miaka ijayo gereza lake pia litafikiriwa.
MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru, Gereza la Tarime limejengwa tangu mwaka 1942. Miundombinu imechakaa ya maji safi na maji taka. Na kwa kuwa wakati Naibu Waziri anajibu hapa amesema hawategemei vyanzo vya ndani na Gereza la Tarime hatuna vyanzo vya ndani. Ningependa kujua mango Madhubuti wa Serikali wa kuhakikisha kwamba wanakarabati miundombinu ya maji safi na taka ili wale watu waweze huduma hii bila matatizo?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Esther Matiko Mbunge kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba magereza mengi likiwemo hili Gereza la Tarime limejengwa siku nyingi na ni moja ya magereza yaliyochakaa. Kama nilivyokwishasema katika jibu letu la msingi kulingana na upatikanaji wa fedha gereza hili pia litapewa kipaumbele angalau katika bajeti za miaka miwili ijayo, ahhsante sana.
MHE. TECLA M. UNGELE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa majibu mazuri ya Serikali, nina swali la nyongeza. Kwa kuwa uzio ni muhimu katika mazingira ya magereza. Je, nini kauli ya Serikali kujenga uzio ulioko imara kwa Gereza la Liwale na Nachingea kwa sababu kwa sasa iko kwa kiasi cha miti imejengwa kwa miti? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Tecla Mohamed Ungele Mbunge wa Viti Maalum Lindi kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kama alivyokwishasema uzio ni kitu muhimu katika magereza yetu na kwa vile ukarabati unaendelea nitumie nafasi hii kumtaka Mkuu wa Gereza la Liwale aendelee katika mipango yake kuweka kipaumbele katika uzio ili anapomaliza ukarabati wa majengo hayo basi uzio pia uweze kuendelezwa.

MHE. NEEMA G. MWANDABILA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Kuna Gereza la Ngwala ambalo liko Wilaya ya Songwe, Mkoani Songwe, ambalo ni gereza kongwe na kwa sasa limechakaa sana. Nilifanya ziara pale nikagundua kwamba idadi ya askari walioko pale ni wengi kuliko maelezo.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni nini mkakati wa Wizara kuhakikisha Gereza lile kwanza linapokea wafungwa wengi na kukarabatiwa? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Neema kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyokwishasema kwenye jibu la msingi ni kipaumbele cha Serikali kukarabati magereza yote yaliyochoka kulingana na upatikanaji wa fedha. Kwa kuwa mwaka huu gereza hili halimo hili la Mkoa wa Songwe basi tutalipa kipaumbele katika ukarabati katika miaka ijayo ya bajeti, nashukuru.

MHE. MWANTUMU DAU HAJI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana, kwanza napenda kushukuru Serikali yangu sikivu kwa jitihada zake inazozifanya kuibua miradi ya vituo vya Polisi nchini.

Mheshimiwa Spika, kituo cha Wilaya ya Kati, Mkoa wa Kusini Unguja, kilianza kujengwa toka mwaka 2016, hadi hii leo 2022 kituo hicho bado hakijamalizwa. Kilijengwa kikapigwa plasta baadhi ya vyumba, chooni bado, nje hakijapigwa plasta hadi hii leo Polisi wapo Wilaya ya Kati wameazimwa eneo la vitambulisho ndiko wanakofanyia kazi zao. Je, Serikali itamaliza lini Kituo hiki cha Polisi cha Dunga, ili Polisi waweze kufanya kazi kama kawaida?(Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mwantumu Dau Haji, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwanza ninampongeza Mheshimiwa Mbunge kwa ufuatiliaji wake makini juu ya kituo hiki na juhudi zilizofanywa na wananchi katika kujenga kituo hiki mpaka hatua iliyofikiwa, ulituelekeza siku moja hapa na mimi nikajibu kwamba Wizara inaandaa mpango wa kumalizia vituo na kujenga maeneo ambayo hayana vituo kabisa. Kipaumbele kitawekwa kwenye maeneo ambayo tayari wameshajenga vituo kama hawa wa Dunga. Kwa hiyo, nimuhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, katika mwaka ujao tutafanya kila liwezekanalo ili ukamilishaji wa kituo hicho uweze kuanza.

Mheshimiwa Spika, ninashukuru sana.(Makofi)
MHE. EMMANUEL P. CHEREHANI: Mheshimiwa Spika, wananchi wa Jimbo la Ushetu wamejichanga wakafanikiwa kujenga msingi wa Kituo cha Polisi lakini mpaka leo ni zaidi ya miaka mitatu Serikali haijafanya chochote. Sasa, ni lini Serikali itakamilisha ujenzi wa Kituo cha Polisi kwa wananchi wa Jimbo la Ushetu?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Cherehani kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, tunafahamu Ushetu ni moja ya Wilaya mpya ambazo hazijawa na Vituo vya Polisi ngazi ya Wilaya na kwenye Kata mbalimbali. Pia tunatambua juhudi ambazo zimefanywa na wananchi kuanza ujenzi wa vituo hivi na Serikali inao wajibu wa kusaidia kukamilisha. Ninapenda kumuahidi Mheshimiwa Mbunge kama nilivyokwishasema kwenye jibu la msingi kwamba kipaumbele kitawekwa kwenye maeneo ambayo wananchi na wadau wameanza kujenga vituo hivyo ili kuvisaidia ujenzi huo uweze kukamilika. Nashukuru.
MHE. GHATI Z. CHOMETE: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kuniona. Wilaya ya Butiama haina Kituo cha Polisi chenye hadhi ya Wilaya. Je, ni lini Serikali itajenga kituo hicho?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Ghati Chomete, Mbunge Viti Maalum Mkoa wa Mara kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba Wilaya ya Butiama ni moja ya Wilaya mpya ambazo hazina Vituo vya Polisi ngazi ya Wilaya na Kata zake mbalimbali hazina vituo hivyo. Kama nilivyokwishasema kwenye jibu langu la msingi, kipaumbele katika ujenzi wa Vituo vya Polisi utazingatia Mikoa, Wilaya na Kata ambazo hazina kabisa vituo lakini msisitizo utawekwa kwa wale ambao tayari wana maeneo na wameanza kujitolea. Kwa hiyo, nimuahidi Mheshimiwa Mbunge kwamba Wilaya ya Butiama ni moja ya eneo litakalozingatiwa katika bajeti ijayo. (Makofi)
MHE. LIVINGSTONE J. LUSINDE: Mheshimiwa Spika, ninakushukuru kwa kunipa nafasi hii ya kuuliza swali moja la nyongeza lakini nami niwapongeze Yanga kwa kupata Ubingwa baada ya kusota kwa miaka minne ndiyo leo wanapumua hapa unawasikia, ubingwa ulikuwa mikononi mwa Simba. Baada ya kuwapongeza naomba niulize swali moja la nyongeza:-

Mheshimiwa Naibu Waziri, utakubali kuongozana nami kufika Mvumi kujionea hali ilivyo kwa askari wa pale Mvumi Misheni ili tuweze kujenga kituo pamoja? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Lusinde kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, hakuna shida kabisa, baada ya Bunge hili tutazingatia ratiba ili tuweze kuongozana tukatizame changamoto zinazowakabili wananchi wa Kata zako ambako hakuna Vituo vya Polisi ili tuweze kushirikiana kuvikamilisha. Nashukuru sana.
MHE. GEORGE N. MALIMA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, vitendo vya uhalifu vimekithiri sana katika Kata ya Berege iliyopo Jimbo ya Mpwapwa. Je, Serikali itajenga lini Kituo cha Polisi ili kukabiliana na wimbi hili la uhalifu?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa George Malima, Mbunge wa Mpwapwa kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba baadhi ya maeneo hasa Miji inayokua na kuchipua ikiwemo Wilaya ya Mpwapwa kuna kuongezeka kwa vitendo vya uhalifu. Kama nilivyowahi kusema hapa, uhalifu ni zao la jamii lakini si jambo jema kufanywa na vijana wetu ambao wanazo fursa mbalimbali wakizitumia wanaweza kupata riziki zao bila kulazimika kuleta uhalifu katika jamii. Kwa hiyo, nichukue nafasi hii kulitaka Jeshi la Polisi ngazi ya Mikoa, Wilaya na Kata kuimarisha shughuli za usimamizi wa usalama wa raia na mali zao lakini kuchukua hatua thabiti dhidi ya vijana au watu wanaojihusisha na matendo ya uhalifu. Nashukuru sana.
MHE. BONIPHACE N. BUTONDO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii yakuuliza swali la nyongeza. Wananchi wa Jimbo la Kishapu, wadau wa maendeleo pamoja na Mfuko wa Jimbo tumechangia zaidi ya Milioni 50 kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Polisi cha Wilaya. Je, Mheshimiwa Waziri yupo tayari kuambatana na mimi kwenda kuona jitihada za wananchi na kuweka mchango wa Serikali?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Boniphace Butondo, Mbunge wa Kishapu kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, nakubali kuongozana na Mheshimiwa Butondo ili kwanza kutambua juhudi zilizofanywa na wananchi, wadau pamoja na yeye mwenyewe kupitia Mfuko wake wa Jimbo. Pili ni kuona namna ambavyo Serikali inaweza kuchangia kukamilisha kituo hiki cha ngazi ya Wilaya. Nashukuru sana.
MHE. ABDALLAH J. CHAUREMBO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kunipa nafasi. Ni lini Serikali itamalizia ujenzi wa Kituo cha Polisi Mbande Kata ya Chamazi?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Abdallah Chaurembo Mbunge kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwanza tunatambua juhudi za Mheshimiwa Mbunge na wananchi wa Jimbo lake Mbagala kwa juhudi wanazofanya katika kuimarisha usalama wa raia na mali zao. Kwa kutambua juhudi hizo, nasi kama Serikali kupitia Jeshi la Polisi tutatembelea Kituo cha Mbande kutathmini kiasi gani kinahitajika ili kuweza kumalizia na hivyo kutoa mchango wetu ili kukamilisha kituo hicho kama sehemu ya kuunga mkono juhudi za wananchi.
MHE. BUPE N. MWAKANG’ATA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kuniona. Kituo cha Polisi cha Sumbawanga Mjini Mkoani Rukwa ni cha toka enzi za mkoloni, ni kidogo hakina hewa. Je, ni lini Serikali itaanza ujenzi wa kituo hicho?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Rukwa kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, tunatambua wilaya za zamani ikiwemo Wilaya ya Sumbawanga ina Vituo vya Polisi ambavyo moja vimejengwa muda mrefu baadhi vimeanza kuwa chakavu lakini vingine havikidhi haja ya viwango vya Vituo vya Polisi vinavyotakiwa kuwepo sasa hivi ngazi ya Wilaya. Kwa hiyo, ninachukua dhima kumuahidi Mbunge kwamba katika kazi tunayoifanya ya kuimarisha maeneo ambayo hayana kabisa vituo, jambo jingine ni kukarabati na kuboresha vituo vya kizamani ili kuweza kukidhi mahitaji ya sasa. Kwa hiyo, Sumbawanga itakuwa ni eneo litakalozingatiwa.
MHE. JANEJELLY J. NTATE: Mheshimiwa Spika, ahsante. Tuangoma ni Kata yenye mkusanyiko wa watu wengi sana na kata hiyo haina Kituo cha Polisi. Je, ni lini Mambo ya Ndani mtajenga Kituo cha Polisi pale Kata ya Tuangoma?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Janejelly Ntate Mbunge wa Viti Maalum, Mkoa wa Dar es Salaam kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba Tuangoma ni moja ya Kata za Jiji la Dar es Salaam ambao haina Kituo cha Polisi, nimuombe Mheshimiwa Mbunge na especially Mbunge wa Jimbo achangie kidogo na kuhamasisha wadau kushiriki ili Serikali ije isaidiane nanyi kukamilisha, kama ambavyo maeneo mengine wamefanyakazi hiyo. Nashukuru sana.
MHE. ERIC J. SHIGONGO: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana, Jimbo la Buchosa lina takriban idadi ya watu wasiopungua 400,000 lakini na kituo cha Polisi katika Mji Mdogo wa Nyehunge ambacho hadhi yake ni ndogo sana. Je, ni lini Mheshimiwa Waziri atakuwa tayari kutembelea kituo hiki ili aweze kukiona na hatimaye kufikia maamuzi ya kujenga kituo kingine?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza Mheshimiwa Eric Shigongo Mbunge wa Buchosha, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ni bahati njema kwamba nimepanga kufanya ziara katika Mkoa wa Mwanza na Wilaya hii ni sehemu ya Mkoa wa Mwanza. namuahidi Mheshimiwa Mbunge, nitakapofanya ziara eneo hilo nitatembelea eneo ya Nyehunge ili kuona ni nini tushirikiane na Mbunge kufanya kukamilisha ujenzi wa Kituo cha Polisi kama njia ya kuimarisha usalama wa raia kwenye maeneo hayo. Ahsante sana.
MHE. JERRY W. SILAA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi, nimshukuru sana Mheshimiwa Waziri kwa kauli yake kwamba Serikali itaunga mkono jitihada za wananchi. Pale Mzinga Injinia Cyprian Romeja na wananchi wenzake wamechanga Milioni 108 na Mbunge amechangia Milioni 8.7 kwa ujenzi wa Kituo cha Polisi. Je, ni lini Serikali itakamilisha Kituo kile cha Polisi kwa kutuchangia fedha za ujenzi?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Jerry Silaa Mbunge wa Ukonga kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, nafahamu juhudi za Mheshimiwa Silaa na mara kadhaa amenishirikisha juhudi wanazozifanya ikiwemo kuchangia ujenzi wa vituo hivi, nimuahidi Mheshimiwa Mbunge kwamba, katika mpango wetu wa uboreshaji, ukamilishaji na uendelezaji wa Vituo vya Polisi eneo la Mzinga ni moja ya Kata itakayozingatiwa katika ukamilishaji huo. Nashukuru sana.
MHE. MUHARAMI S. MKENGE: Mheshimiwa Spika, nashukuru. Wananchi wa Kiharata katika Kata ya Mapinga wamepambana wamepata kiwanja kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Polisi. Je, Serikali ipo tayari kutusaidia ili tuweze kukamilisha Kituo hicho mapema?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Shabani Mbunge wa Bagamoyo kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, tunafahamu juhudi za Mbunge na wananchi wa Jimbo lake katika kutunza usalama raia na mali zao na uwepo wa Vituo vya Polisi ni moja ya mahitaji ya kukamilisha jambo hilo. Ninamuahidi Mheshimiwa Mbunge kwamba tutashirikiana nae mwenyewe, wadau wa Wilaya ya Bagamoyo pamoja na wananchi ili kujenga kwenye kiwanja hiki cha Mapinga ambacho wananchi wamejitolea kwa ajili ya ujenzi wa kituo hicho. Ni moja ya eneo tutakaloingia kwenye mipango yetu ya uendelezaji wa Vituo vya Polisi. Nashukuru.
MHE. USSI SALUM PONDEZA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Nami ningependa nimuulize swali moja dogo la nyongeza Mheshimiwa Waziri. Je, Jimbo langu la Chumbuni tumekuwa na matatizo sana ya hivi vituo na tumekuwa hatuna kituo zaidi ya mwaka wa nne, tumekuwa tukisema sana lakini tumekuwa tukiahidiwa na Wizara kuwa itakuja kushughulikia. Mheshimiwa Waziri upo tayari nasi tukijenge kile kituo kwa nguvu zetu?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Ussi Pondeza Mbunge, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, natambua juhudi za Mheshimiwa Mbunge, wamefanya mambo mengi katika Jimbo lake ikiwemo kuanza ujenzi wa vituo hivi, nilitembelea huko na nikaona. Ninamuahidi katika maeneo tutakayozingatia na kuyapa kipaumbele katika utekelezaji wa mpango wetu wa ukamilishaji na ujenzi wa vituo, Jimbo la Chumbuni litapewa kipaumbele. Nashukuru sana. (Makofi)
MHE. MAULID ALI MOHAMED: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri naomba kumpa ushauri mmoja. Kituo hiki ni kituo chetu cha Wilaya na bahati mbaya sana kipindi cha mvua askari wetu wanalazimika kuhama kule juu kwa sababu kumekuwa na bwawa. Sasa pamoja na hiyo program ya kutengeneza nyumba zote za polisi lakini ningeomba kitu kimoja. Kama kuna uwezekano wa lile paa lifanyiwe dharura halafu masuala mengine yatafuata baadaye, ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napokea ushauri wake tutaufanyia kazi na mara nitakapopata nafasi ya kuja Kiembe Samaki tutapata nafasi pia ya kushauriana Mheshimiwa Mbunge.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana.

MHE. OLIVER D. SEMUGURUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kuniona niweze kuuliza swali la nyongeza. Changamoto iliyopo Kiembe Samaki inafanana kabisa na changamoto iliyoko Wilaya ya Ngara kituo cha Polisi cha Rurenge kimchakaa kabisa mpaka kinavuja. Je, ni lini Serikali itakifanyia ukarabati kituo hicho?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimwa Oliver kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara inatambua uchakavu wa Kituo cha Polisi Rurenge tena ambacho kiko karibu na mpaka. Kama nilivyoeleza katika majibu niliyomjibu hivi karibuni ni mpango wa Serikali kuvikarabati vituo vyote kikiwemo hiki cha Rurenge na hivi vituo vya mpakani Mheshimiwa Mbunge tutavipa msisitizo maalum, nashukuru.

MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, naomba nimuulize swali la nyongeza Mheshimiwa Waziri kwamba kule Tarime eneo la Rorya, Sirari, Nyasicha, Muliva, Itilio, Nyanungu. Eneo hilo kuna malalamiko ya wananchi mengi kwamba wale maaskari wanatembea na marungu kwenye magari kwa hiyo, watu wakikamatwa wanapigwa sana. Nilitaka niulize utaratibu wa sheria umebadilika au huu ni mtindo wa kule Tarime ndio tu upo kwa sababu ni kanda maalum? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Waitara Mbunge wa Tarime Vijijini kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, si mpango wa wizara wala Jesho la Polisi kutembea na marungu kwenye magari kwa ajili ya kupiga wananchi wake. Lakini nafahamu kwamba kuna wakati Askari wanalazimika kukamata wahalifu na wahalifu wanapofanya upinzani nguvu inayotakiwa kutumika ni ile tu inayoshabihiana na nguvu pinzani lakini si marungu kwa ajili ya kupopoa wananchi wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru.
MHE. BAKAR HAMAD BAKAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Nyumba za Askari katika kambi ya Askari Mfikiwa ni chakavu sana. Je, ni upi mpango wa Serikali katika kuziboresha nyumba zile?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyojibu kwenye jibu la msingi tunatambua uwepo wa uchakavu wa vituo na makazi ya Askari. Kama nilivyokwishakusema ni mpango wa wizara kufanya ukarabati wa majengo hayo kutegemeana na uwepo wa bajeti. Mwaka huu tutaanza na yale ambayo yapo kwenye kipaumbele tutaendelea na ukarabati kadri miaka inavyokwenda kulingana na upatikanaji wa fedha nashukuru.
MHE. DOROTHY G. KILAVE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, nina swali moja nyumba za bara pale Kilwa Road. Kuna maghorofa yalitangulia kujengwa sasa sijui ndio yameishia pale pale na wale wengine bado wako kwenye zile nyumba ambazo Kilwa Road Barax. Maghorofa yale yamejengwa vizuri lakini katikati pana nafasi sijui ndio mwisho pale maana yake zile nyumba sasa ni ndogo sana na zinavuja?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge Dorothy Kilave wa Temeke kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ujenzi wa kota za Askari kule Temeke Kilwa Road unaendelea na kama pana dosari zozote ambazo zimeoneshwa na Mbunge kama maeneo mengine yanavuja tutamwelekeza IGP ili kumsimamia mkandarasi aweze kusimamia mjenzi ahakikishe kwamba viwango vilivyowekwa vinazingatiwa ili kuondoa hizi dosari ambazo zimeonekana.
MHE. OMAR ISSA KOMBO: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu ya Serikali ingawa hayaleti matumaini kwa wananchi wa Wilaya ya Micheweni, lakini nina maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kulingana na hali ya kituo kilivyo hali ni mbaya sana mpaka paa zake kuvunja. Je, Serikali ina mpango gani wa haraka na wa dharura kukarabati Kituo hiki cha Micheweni?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, je, Mheshimiwa Naibu Waziri yuko tayari baada ya Bunge hili kuambatana na mimi mpaka Micheweni kwenda kujionea hali halisi ilivyo kwa sababu hanga hili la polisi limejengwa kwa nguvu za wananchi takribani miaka minane iliyopita na sasa hivi tayari limeanza kuvuja. Je, uko tayari kuambatana na mimi kwenda kujionea hali halisi ilivyo? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Kombo kama ifuatavyo:-

Kwanza nakubaliana naye kwamba hali ni mbaya ndiyo maana tathmini yetu imefanyika na kubaini gharama zinazohitajika. Kwa kuwa bajeti ya mwaka huu imepita, naomba nimuahidi Mheshimiwa Mbunge kwamba katika maeneo yatakayopewa vipaumbele katika mwaka ujao basi tutazingatia hili eneo pia la Micheweni.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu umuhimu wa kuambatana naye niko tayari na mara nyingi natekeleza ahadi baada ya Bunge hili tutapanga tuone lini kuweza kuitembelea Micheweni kubaini kiwango cha uharibifu na nakubaliana naye pamoja namna ya kutekeleza ukarabati huo, nakushukuru.
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, Kituo cha Polisi cha Tukuyu hakina uzio kwa ajili ya usalama wa kituo kile kwa sababu inazungukwa pia na shule ya msingi. Ni lini Serikali itapeleka pesa katika kituo kile ili tuweze kujengewa uzio kwa usalama wa wananchi wanaozunguka?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, kupanga ni kuchagua, tumesema sasa hivi baadhi ya vituo ni chakavu sana, vinahitaji ukarabati na kwingine kunahitaji kujenga kabisa. Kwa hiyo, swali la Mbunge ni zuri kweli tunahitaji uzio, lakini kwa vipaumbele tulivyoweka uzio itakuwa ni second priority tutaanza kwanza na ukarabati hatimaye uzio utafuata, nashukuru.
MHE. NICODEMAS H. MAGANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kituo cha Polisi Masumbwe kiko kwenye eneo la CCM na tumeshachukua eneo kwa ajili ya kujenga Kituo cha Polisi pale Mbogwe. Je, Serikali inatusaidiaje Mbogwe ili kusudi askari wapate mahala pa kukaa?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimshukuru Mbunge kwa mahusiano mema na Chama Tawala, Chama cha Mapinduzi ambao waliweza kutoa jengo linalotumika na Kituo hicho cha Polisi. Hata hivyo kama tulivyokwishasema kwenye majibu yetu ya msingi mbalimbali ni kwamba kipaumbele ni kujenga vituo vya polisi kwenye maeneo ambayo hayana kabisa, Mbogwe ikiwa ni mojawapo tutaipa kipaumbele katika miaka ijayo ili kuweza kujengea kituo chake cha polisi. (Makofi)
MHE. ALOYCE J. KAMAMBA: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kunipa nafasi kuuliza maswali mawili madogo ya nyongeza pamoja na majibu mazuri ya Serikali.

Mheshimiwa Spika, bado kwa takwimu Mkoa wa Kigoma una zaidi ya wananchi 2,000,000 lakini waliotambuliwa ni 975,844 na waliopata vitambulisho ni 123,962 sawa na asilimia 12 tu. Jibu lake anasema kwamba mwaka huu watapewa vitambulisho; sasa swali nini mkakati wa Serikali kuhakikisha kwamba wananchi wote wanaostahili ambao wako katika Mkoa wa Kigoma wanapata vitambulisho vya NIDA?

Mheshimiwa Spika, la pili; wananchi wa Wilaya ya Kakonko muda mwingine wanaombwa vitambulisho ambavyo ni vya NIDA ambavyo hakika Serikali inajua kwamba haijavitoa kwa wananchi hao, mpango ukoje kuhakikisha kwamba wananchi wa Wilaya ya Kokonko sasa wanapata vitambulisho vya NIDA? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Kamamba kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba kwa takwimu hizo idadi ya waliopata vitambulisho ni ndogo sana, lakini kama ilivyoelezwa wakati nawasilisha bajeti hapa kulikuwa na changamoto ya kimkataba kati ya Serikali na mzabuni, na hivyo karatasi za kutolea vitambulisho hivi hazikuwepo, lakini tatizo hilo limeondolewa, tumeshahuisha mkataba na ndio maana tunauhakika kwamba kwa mwaka ujao wa fedha tutatatua tatizo hilo kwa wale wote waliotambuliwa na kusajiliwa na wale wapya tutakaokuwa tunaweza kutawambua na kuwasajili, nashukuru kwa swali la kwanza. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Kuhusu kugawa vitambulisho kama nilivyosema kwenye jibu la msingi linahusiana moja kwa moja kwa mwaka ujao tunauhakika wananchi wale ambao wameshatambuliwa watapewa vitambulisho na wale wapya watakaokuwa wanaendelea kutambuliwa watapewa vitambulisho, nashukuru.
MHE. ASIA A. HALAMGA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi; kwa kuwa kuwa na kitambulisho cha Taifa ni haki ya kila Mtanzania, je, ni nini kauli ya Serikali kwa wafungwa na maabusu wa muda mrefu juu ya kupatiwa huduma hii?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Asia Halamga, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba ni haki la kila raia kupata kitambulisho, lakini kwa hawa ambao wamefungwa sidhani kama kuna dharura ya kiasi hicho, kwa sababu hawa wapo jela vitambulisho vinatakiwa kwa ajili ya kupata huduma mbalimbali ikiwemo elimu, mikopo, safari, passport na kadhalika, sasa huyu mfungwa tuhangaike kumpa kitambulisho anakwenda kukitumia wapi. Lakini tuahidi atakapokuwa amemaliza kifungo chake akirudi uraiani atatambuliwa na kupewa kitambulisho kama inavyopaswa, nashukuru. (Makofi)

MHE. ANASTAZIA J. WAMBURA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi; moja ya changamoto ambayo inayopelekea kuchelewa kuwapa vitambulisho vya NIDA wananchi wa Mkoa wa Mtwara ni pamoja na uhaba wa watumishi; je, Serikali imejipanga vipi kuondoa changamoto hii? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Anastazia Wambura kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kama nilivyosema kwenye majibu ya maswali yaliyopita, kwa kweli changamoto sio idadi ya watumishi changamoto ilikuwa ni kukosa vitendea kazi vilivyokuwa vimesababishwa na kukwama kwa mkataba, sasa baada ya suala la mkataba tumeshalitatua bila shaka ataona kasi ya utoaji wa vitambulisho kule Mtwara inatatuliwa, lakini pale itakapoonekana kwamba shida ni watumishi Serikali itaendelea kuajiri watumishi wanaohitajika ili kutekeleza majukumu yako ya utoaji wa vitambulisho itasavyo.
MHE. JACKSON G. KISWAGA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa majibu mazuri ya Serikali sasa nitakuwa na maswali mawili ya nyongeza; swali la kwanza, kwa kuwa katika Mahakama ya Tarafa iliyopo pale Kiponzelo ilishatokea miaka ya nyuma hapo kwamba wakati mtuhumiwa anasafirishwa kwenda Ifunda alitoroka na kuonesha kwamba kulikuwa hakuna usalama.

Je ni lini sasa Serikali itaanza angalau kujenga vituo hivi vya polisi kwenye maeneo ya Tarafa hasa pale Kiponzelo?

Mheshimiwa Spika, lakini swali la pili Ifunda tuna Kituo cha Polisi kikubwa bahati mbaya hatuna gari wala nyumba za polisi; je, ni nili Serikali sasa itaturekebishia angalau kupata gari hapo Ifunda? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Kiswaga kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kuhusu mfungwa aliyetoroka kwasababu ya umbali kama nilivyosema katika nyakati tofauti ninapojibu maswali haya kadri tutakapopata fedha tutajenga vituo vya polisi viwe karibu kabisa na maeneo ambayo yanahitajika ikiwemo karibu na Mahakama zilizopo ngazi ya Tarafa na ninajua pia mpango wa Serikali upande wa Wizara ya Katiba na Sheria ni kuweka Mahakama hizi katika kila Kata. Kwa hiyo niendelee kusisitiza wadau mbalimbali wakiwemo Serikali za Mitaa wadau kama yeye Mheshimiwa Kiswaga mwenyewe ana mpango wa kusaidia kujenga kituo cha polisi, vituo hivi vitakapojengwa tutapeleka askari.

Mheshimiwa Spika, lakini kuhusu swali la pili kwamba kuna kituo lakini hakina gari wala nyumba nimeeleza mara kadhaa hapa kulingana na bajeti yetu ya mwaka huu na mkataba tulionao na kampuni ya Ashok Leyand tunayo magari ambayo tutapokea 78 mwezi huu, lakini vilevile hayo magari 78 yameshapokelewa ni taratibu za kuyatoa bandarini lakini mpaka mwezi Septemba tutakuwa tumekamilisha magari 396. Maeneo yenye changamoto kama haya ya Kalenga yatazingatiwa, nashukuru sana. (Makofi)
MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali la nyongeza. Kwanza niipongeze Serikali kwa kusikia kilio change cha ujenzi wa Mahakama ya Wilaya katika Wilaya ya Nyang’hwale swali. Ni lini Serikali Itaanza ujenzi wa Gereza la Wilaya ya Nyang’hwale?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Hussein Amar kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ujenzi wa gereza la Nyang’hwale kama lilivyoombwa na Mheshimiwa Amar utaanza baada ya kuwa tumepata fedha kwa ajili ya kutekeleza mradi huo, kwa kweli kwa mwaka ujao hatuna bajeti hiyo, lakini tutaingiza kwenye kipaumbele kutokana na mahitaji ya Wilaya ya Nyang’hwale, nashukuru. (Makofi)

MHE. ABUBAKARI D. ASENGA: Mheshimiwa Spika, pamoja na furaha tuliyonayo wananchi kuhusu mambo yaliyotokea Jumamosi huko Mwanza naomba kuuliza swali dogo la nyongeza. (Makofi)

Wakati wenzetu wanang’ang’ania vituo vya Kata vya Tarafa Wilaya ya Kilombero ina Kata 35 na haina Kituo cha Polisi cha Wilaya; je, ni lini Serikali itajenga Kituo cha Polisi cha Wilaya ya Kilombero?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Asenga, Mbunge wa Kilombero kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, tumeshazungumza na Mbunge hiyo changamoto yake ya kituo, lakini tumesema katika maeneo yatakayopewa kipaumbele katika miaka ijayo tukianza na mwaka wa fedha 2022/2023 ni maeneo ya Wilaya ambayo hayana kabisa Vituo vya Polisi. Kwa hiyo matarajio yangu ndani ya mwaka mmoja miwili ijayo tutakuwa tumeanza ujenzi wa Kituo cha Polisi cha Wilaya ya Kilombero kama ilivyoombwa na Mheshimiwa Mbunge.
MHE. DANIEL B. SILLO: Mheshimiwa Spika, ahsante kunipa nafasi niweze kuuliza swali moja la nyongeza.

Kwa kuwa Mji wa Bashnet ambao ni Makao Makuu ya Tarafa hauna kituo cha polisi na badala yake polisi hutoka Mji wa Babati ambao ni kilometa 60 na kurudi jioni.

Je, ni lini Serikali itajenga Kituo cha Polisi katika Mji wa Bashnet ambao ni Makao Makuu ya Tarafa?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Daniel Baran Sillo kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ni kweli tunatambua baadhi ya maeneo kama alivyosema Mheshimiwa Mbunge ana uhaba wa vituo umbali wa kilometa 60 ni umbali mkubwa na haukubaliki. Naomba nimuahidi Mheshimiwa Mbunge kwamba tutaweka kipaumbele kwenye eneo lake ili kuweza kuanza ujenzi wa Kituo hicho cha Polisi, nashukuru.

MHE. PHILLIPO A. MULUGO: Mheshimiwa Spika, ahsante sana na mimi kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali moja la nyongeza kwa Wizara ya Mambo ya Ndani.

Mheshimiwa Waziri mwaka 2017 mimi kama Mbunge na mwananchi wa Kata ya Mpona tulichanga fedha tukaanza kujenga Kituo cha Polisi kata ya mpona na angalau kwa asilimia 80 kimekamilika bado asilimia 20; je, Serikali haioni haja ya kuniongezea fedha kwa ajili ya kufanya finishing ya kituo hicho? Ahsante.

NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwanza tunawapongeza wananchi waliojitokeza na Mbunge wao kujenga kwa asilimia 80 kituo hicho na kuahidi kulipa kipaumbele. Nitamwelekeza IGP katika fungu lake la tuzo na tozo aweze kuweka kipaumbele katika eneo hili ili kuweza kukikamilisha kituo hicho. (Makofi)

MHE. ABEID R. IGHONDO: Mhehimiwa Naibu Spika, ninakushukuru sana kwa nafasi, pamoja na majibu yao ya Serikali lakini nina maswali mawili madogo ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza; ni lini sasa fedha hizi ambazo amezitaja Mheshimiwa Waziri zitaletwa kwaajili ya kuboresha miundombinu ya vituo hivi vya polisi vya Mtinko na Ngamu pamoja na kujenga vile vingine vya Msange na Ngimu maana yake tayari maeneo yapo?

Swali la pili nataka nijue, Serikali sasa inamkakati gani wa kujenga kituo cha polisi cha hadhi ya Wilaya katika Mji wa Ilongero ambao unakuwa kwa kasi unawatu wengi, lakini pia na kwa sasa ni Makao Makuu ya Halmashauri ya Wilaya kwa hiyo, unahitaji usalama, huduma na pamoja na kwamba kituo hicho sasa eneo hilo linanyumba za polisi? Naomba kuwasilisha. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili nyongeza ya Mheshimiwa Ighondo kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, moja lini fedha? Bahati nzuri tumeshafanya tathimini tumepata shilingi milioni 46.4 zinahitajika kwaajili ya kukamilisha ukarabati huo, lakini katika mwaka huu wa fedha kama tulivyosema tutaendelea kutoa fedha kwa awamu kulingana na upatikanaji wake. Niombe kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba kwa mwaka ujao tunachukua commitment ya kuweka fedha hizi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu mkakati wa kujenga kituo cha polisi cha hadhi ya Wilaya niseme tu kwamba Wizara pamoja na Serikali kwa ujumla kuhakikisha tunajenga kituo chenye hadhi ya wilaya kwenye Makao Makuu ya Wilaya sasa hii ni Wilaya ya Singida ambayo OCD anaofisi yake lakini tutakachoweza kufanya ni kuimarisha vituo vya polisi ngazi ya kata na tarafa ili viweze kutoa huduma stahiki kwa wananchi badala ya kila jimbo kuliwekea kituo cha polisi chenye hadhi ya Wilaya. Nashukuru.
MHE. ZAYTUN S. SWAI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa nafasi hii; kutokana na ongezeko la uhalifu katika machimbo ya Rubi yaliyopo Mandala na Longido Mbunge wa Jimbo akishirikiana na wananchi wa pale kwa juhudi zao binafsi wamejenga kituo cha polisi mpaka ngazi ya lenta.

Je, ni lini Serikali itawasaidia wananchi hawa ili kumailizia kituo hiki cha polisi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza ya Mheshimiwa Zaytun kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ni dhamira ya Wizara kwamba pale ambapo wananchi watakuwa wamefanya juhudi na kujenga kufika kiwango chochote Serikali inaweza ikatoa fedha kukamilisha. Niombe tushirikiane na Mheshimiwa Mbunge wa Jimbo na Mheshimiwa Zaytun wakati wa ziara yetu katika mkoa huo tuweze kuona kiwango kilichofikiwa ili kupitia Mfuko wetu wa Tuzo na Tozo tuone kiwango cha fedha tunachoweza kutoa ili kukamilisha kituo hicho kama njia ya kuunga mkono juhudi za wananchi. Nashukuru.
MHE. DEO K. SANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Kwa kuwa ongezeko ni kubwa sana la uhalifu katika Mji wa Makambako na kwa sababu Makambako kipolisi ni Wilaya na tunakituo kimoja. Ni lini Serikali sasa itaondoa adha hii kwa kujenga kituo kingine pale Majengo, pale Idofi, pale Maguvani ili kuwaondolea adha wananchi waishi kwa amani?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza ya Mheshimiwa Sanga kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, tunatambua Mji wa Makambako umekuwa kwa kasi, kuna ongezeko kubwa la watu na shughuli za kiuchumi ambako ni kivutio kwa wahalifu pia. Nimuahidi tu kama kituo kilichopo kwa sasa hakikidhi haja, tutafanya tathmini kwa kushirikiana na uongozi wa Wilaya na kuona namna gani tutahitaji kufanya kwa maana ya kupanua huduma za polisi katika eneo lake. (Makofi)

MHE. NAGHENJWA L. KABOYOKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana; Tarafa ya Gonja yenye kata nne na Tarafa ya Mambavunja yeye kata tano zote hizi zimekuwa hazina kituo cha polisi na kwa muda mrefu tumeomba mpaka wananchi wameweka nafasi za kwamba polisi wanaweza kuanzia pale na kuna sehemu za kujenga vituo vya polisi.

Je, lini Serikali itatusaidia kujenga vituo hivyo? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Kaboyoka kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, natambua uwepo wa baadhi ya tarafa na kata zisizokuwa na vituo vya polisi na polisi wetu tunaowapanga mpaka kwenye ngazi ya kata wanatumia majengo ambayo huamuliwa na mamlaka zetu za Serikali za Mitaa. Nimuombe Mheshimiwa Kaboyoka kuwa na subira, tunavyoanza kutekeleza mkakati wetu wa kujenga vituo vya polisi mahala ambako hakuna kabisa vituo, zikiwemo tarafa alizozitaja huko Gonja. Nashukuru.
MHE. FAKHARIA SHOMAR KHAMIS: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, naomba kuuliza swali moja la nyongeza ambalo dogo tu.

Je, ni lini Serikali itaweka uzio katika Kituo cha Polisi cha Ng’ambo, Wilaya ya Mjini Unguja? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba uzio upo katika baadhi ya vituo vya polisi. Lakini niseme kwa kuwa baadhi ya maeneo hayana kabisa vituo vya polisi, kipaumbele hakiwezi kuwekwa kwenye uzio, kipaumbele cha Wizara ni kuweka vituo mahala ambako hakuna vituo kabisa na nyumba za makazi kwa ajili ya askari wetu. Kwa hiyo, naomba Mheshimiwa atuvumilie tumalize vipaumbele then haya mambo mengine ya uzio yafuate. Nashukuru.
MHE. NICHOLAUS G. NGASSA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana; cha kwanza nataka nimwambie Mheshimiwa Naibu Waziri anavyosema kwamba mabweni mawili yamekamilika si kweli kwa sababu yale mabweni hayajakamilika. Mpaka sasa wameziba kwa mabanzi na mbao chakavu kwa ajili ya kuwa-accommodate wale wafungwa, jambo ambalo ni kinyume cha haki za binadamu na utawala bora. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nimuombe Mheshimiwa Waziri na wasaidizi wake walifanyie kazi waweze kulikamilisha gereza hili ili liweze kutoa huduma vizuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili,, kwa sasa Serikali inapata hasara kwa kuwa mabweni ya wanawake hayapo, inasababisha kama kuna mfungwa ambaye ana kesi mbili au kesi inaendelea anachukuliwa anatolewa Igunga anapelekwa Nzega na inapoitwa kesi mahakamani inabidi arudishwe. Jambo ambalo linaingiza Serikari hasara.

Je, haoni kuendelea kuingiza Serikali hasara wasipomaliza ujenzi wa hili gereza? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Ngassa kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza hili ambalo ameniambia kwamba majengo hayajakamilika na ni machakavu kwangu pia ni jipya. Nachukua dhima ya kuongozana na wataalam wetu baada ya Bunge hili kwenda Igunga kujiridhisha, kuona ukweli wa hiki ambacho kinasemwa na kwa kweli kama tutakuwa iko tofauti tutachukua hatua stahiki kwa hawa waliotupa majibu haya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu swali la mabweni ya wanawake kutokuwepo Igunga tunatambua, lakini kama nilivyokwishasema tunajenga kulingana na upatikanaji wa bajeti. Kwa vile hatujapata fedha akubali tu Mheshimiwa hawa wafungwa wa kike waendelee kupelekwa katika gereza la jirani. Lakini mipango ya Wizara ni kuendelea kujenga mabweni hitajika, na kwa sababu angalau mwaka huu tuna bajeti tuweze kuona jinsi ambavyo tutaweza kuwa-accommodate akinamama ambao wanakuwa wanasafirishwa kwenda gereza la mbali. Nashukuru.
MHE. SALMA R. KIKWETE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana na samahani sauti yangu imekuwa mbaya leo.

Kwa kuwa kuona ni kuamini, je, Mheshimiwa Naibu Waziri ni lini tutafuatana mimi na wewe kwenda Kingurungundwa ambako kuna gereza la miaka mingi na gereza hili ni la mabati na hali yake ni mbaya sana? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Salma Kikwete kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, nakubaliana naye kuona ni kuamini na niko tayari kuongozana naye wakati wowote baada ya shughuli za Bunge ili pamoja na mambo mengine kuangalia uchakavu wa gereza hili. (Makofi)
MHE. AYSHAROSE N. MATTEMBE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Kwa kuwa gereza la Wilaya ya Manyoni limejengwa miaka 52 iliyopita hali inayopelekea miundombinu yake kuwa ni chakavu sana. Je, ni lini Serikali itakarabati na kufanya upanuzi wa gereza hili ili kupunguza msongamano katika gereza hili? Nakushukuru.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Aysharose Mattembe kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, nakubali baadhi ya magereza ikiwemo la Manyoni ni la muda mrefu na lina uchakavu na ndiyo maana tumeanza mkakati wa kukarabati magereza chakavu kama tulivyokwishafanya Liwale na maeneo mengine. Nachukua ahadi kwamba tutaendelea kukarabati magereza haya kulingana na upatikanaji wa fedha. Nashukuru.

MHE. FLORENT L. KYOMBO: Mheshimiwa Spika, nishukuru kwa nafasi, na naipongeza Serikali kwa majibu mazuri, lakini ndani ya muda mfupi wameweza kutengeneza vitambulisho. Naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza; Wilaya ya Misenyi kama alivyosema Mheshimiwa Naibu Waziri, imetengeneza vitambulisho 24,000 lakini mpaka sasa ni vitambulisho 5,000 vimegawiwa kwa wananchi. Shida kubwa ni kwamba wananchi wanatakiwa kuhakikiwa kwa mara nyingine, hii imekuwa ni kero kubwa kwa wananchi wa Wilaya ya Misenyi na hivyo wananchi kuona kwa kweli kuona kwamba sio sahihi kuhakikiwa mara ya pili.

Je, ni nini tamko la Serikali kuhusiana na usumbufu huo?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, sasa kuna baadhi ya wananchi ambao walikuwa hawajafikiwa kwa ajili ya kujaza fomu kwa ajili ya kupata vitambulisho ikiwa ni pamoja na wale ambao wamefikisha umri wa miaka 18 ambao wametiza sasa vigezo sasa vya kupata vitambulisho.

Je, ni nini mkakati wa Serikali kuhakikisha na wananchi hao wanafikiwa kwa ajili ya kupata vitambulisho? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Kyombo kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kuhusu idadi ndogo ya wananchi waliogaiwa vitambulisho 5,000 tu kati ya wananchi 24,694 ambao vitambulisho vyao vimetoka, nitoe tu maelekezo kwa wenzetu wa NIDA Mkoa wa Kagera na hususan Wilaya ya Misenyi kwamba wakati wanawahakiki mwanzo mpaka vitambulisho vinatoka bila shaka walikuwa wamejiridhisha. Hata hivyo, pale ambapo kuna mashaka kwamba huenda wanaokwenda kutoa vitambulisho siyo raia wa Tanzania wana haki ya kufanya uhakiki mara ya pili; lakini uhakiki huo usiwe sehemu ya usumbufu kwa wananchi kwa sababu haieleweki kwa nini wananchi 5,000 pekee kati ya 24,000 ndiyo wapate. Kwa hiyo, waharakishe uhakiki huo ili wanaostahili kweli waweze kupewa vitambulisho vyao.

Mheshimiwa Spika, kuhusu swali la pili la mkakati wa Serikali, tumelijibu kwa nyakati tofauti kwamba tulikuwa na changamoto ya kimkataba kati ya Serikali na Mkandarasi, lakini changamoto hiyo imemalizwa na mkataba umeuhishwa mwezi Machi, 2022; kwa hiyo, wakati wowote kuanzia sasa vitambulisho vingine vitazalishwa na watu wengine ambao wamefikisha miaka 18 wataendelea kutambuliwa kwa madhumuni ya kupewa vitambulisho vyao. Nashukuru.
MHE. FATMA H. TOUFIQ: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa fursa ya kuweza kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, kumekuwa kuna wanafunzi wa Shule za Sekondari ambao wamekuwa wakimaliza shule na wanazaidi ya miaka 18. Je, nini mkakati wa Serikali kutoa elimu katika shule mbalimbali ili wanafunzi wanapomaliza waliozaidi ya miaka 18 waweze kupata vitambulisho?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Fatma Toufiq, Mbunge kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba baadhi ya wanafunzi huitimu masomo yao wakiwa na zaidi ya miaka 18 na wanafunzi wa aina hii wana haki ya kupewa vitambulisho. Kwa hiyo, pengine tutashirikiana na Wizara ya Elimu na Wizara ya TAMISEMI ili elimu ya uraia ikiwa ni pamoja na nafasi ya kuwa na vitambulisho kutolewa mashuleni, lakini wanafunzi hawa ni sehemu ya jamii kule ambako elimu inatolewa kwenye jamii kwa ujumla wake kupitia redio, televisheni na kadhalika wanaweza pia wakapata elimu hiyo. Kwa hiyo, nadhani halitakuwa tatizo kubwa sana litatekelezwa. Nashukuru sana.
MHE. JOSEPH M. MKUNDI: Mheshimiwa Spika, nashukuru, wananchi wanaoishi Visiwa vidogo vidogo Jimboni Ukerewe wanalazimika kusafiri kwenda Makao Makuu ya Wilaya kufuatilia vitambulisho vya NIDA jambo linalopelekea usumbufu na gharama kubwa.

Nini mkakati wa Serikali kuwapelekea huduma lakini wakati huo huo ikiwaondolewa usumbufu wa wananchi hao? Nashukuru.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mkundi, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ili kuwapunguzia usumbufu hawa wananchi wanaokaa mbali na makao makuu wakiwepo hawa wa visiwani, vitambulisho hivi vimepelekwa mpaka ngazi ya Kata ili maofisa wetu kwenye ngazi ile aweze kuwagawia wananchi wao, nadhani kwa kufanya hivyo tutakuwa tumepunguza usumbufu wa wananchi. Naomba niwaelekeze wenzetu wa Ukerewe kama lipo tatizo la kuwataka wananchi wote wasafiri kwenda Nansio warekebishe ili vitambulisho hivi wavipate kwenye Makao Makuu ya Kata zao. Nashukuru.
MHE. EMMANUEL A. MWAKASAKA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuuliza swali la nyongeza.

Kwa kuwa wananchi wengi wanapata tatizo na eneo hili la uhakiki kwa ajili ya kupata hivyo Vitambulisho vya Taifa. Sijui Serikali inasemaje kuhusu muda hasa ni muda gani ambao uhakiki unachuku ili wananchi waweze kupata vitambulisho vyao?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, uhakiki hautakiwi kuchukua muda mrefu sana, lakini tunafanya uhakiki ili tujiridhishe kwamba wanaopewa vitambulisho hivi ni raia wa Tanzania. Kwa hiyo, itakapotokea taarifa yoyote hasa wananchi wakatia mashaka juu ya mtu aliyetambuliwa inabidi tufanye uhakiki kujiridhisha.

Sasa juu ya muda gani itategemea pale itakapokamilisha, lakini aombe maafisa wetu wasichukue muda mrefu kwa sababu wanapaswa kushirikiana na vyombo vingine vikiwa Kamati za Usalama za Wilaya na Idara za Uhamiaji ili kujiridhisha na kumpa jibu yule ambaye anatafuta kitambulisho. Nashukuru.
MHE. SHABANI O. SHEKILINDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa majibu mazuri na ni kweli kituo kile kinamalizika niishukuru Serikali kwa kutupa fedha milioni 417, lakini pia nimshukuru IGP Sirro alikuja kule na akamuomba Mkuu wa Wilaya aitishe harambee ya kuchangia majengo ya watumishi, lakini Mkuu wangu wa Wilaya alifanya hivyo na mpaka sasa hivi tunavyosema kuna zaidi ya shilingi milioni 210 kwa ajili ya kujenga nyumba za polisi namshukuru sana Mkuu wangu wa Wilaya na timu yake ya Kamati ya Ulinzi na Usalama. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sasa niulize maswali mawili ya nyongeza; Gereza la Lushoto lipo katikati ya Mji wa Lushoto na hivyo kusababisha wafungwa wetu kukosa hata sehemu ya kuota jua, lakini wakati huo huo kuna eneo lipo nje ya mji kidogo wanaita Yogoi.

Je, Serikali haioni kuwa kuna umuhimu wa kwenda kujenga gereza hilo maeneo ya Yogoi na ambako ndiyo kwenye nafasi kubwa? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; Wilaya ya Lushoto ina wakazi wengi sana kama unavyofahamu, lakini ina taasisi nyingi za binafsi na za Serikali, lakini ikitokea changamoto ya majanga ya moto huwa wanapiga simu Korogwe ambayo kutoka Lushoto kwenda Korongwe ni kilometa zaidi ya 70. Kwa hiyo, mara nyingi wananchi wetu wanapata hasara.

Sasa basi niiombe Serikali, je, Serikali haioni kuwa kuna umuhimu au ulazima haraka kujenga kituo cha zimamoto katika Wilaya ya Lushoto? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Shekilindi kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimshukuru kwa kutambua juhudi za Wizara lakini na hususani Jeshi la Polisi kufuatilia maendeleo ya ujenzi wa kituo cha polisi pale Lushoto. Lakini nimshukuru pia DC kwa harambee aliyoifanya kupata shilingi milioni 210 kwa ajili ya nyumba za wafanyakazi, nadhani ni jambo jema la kuigwa na maeneo mengine.

Sasa kuhusu gereza la Lushoto ambalo tunatambua liko katikati ya mji na eneo lile ni finyu ni kweli baada ya Wizara kuona changamoto hizo inayo mpango wa kuhamishia gereza hilo eneo ya Kambi ya Yogoi ambayo iko nje kidogo ya Mji wa Lushoto. Kwa hiyo, pale itakapopata fedha za ujenzi wa gereza hilo, gereza hilo tutalihamisha ili jengo lililopo lifanye kazi nyingine za kiuchumi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, na lingine kuhusu ombi lake la zimamoto tunalipokea ni suala tu la kibajeti tutakapo kuwa tumepata fedha tutajenga Ofisi ya Zimamoto ndani ya Wilaya ya Lushoto. Nashukuru.
MHE. JULIANA D. SHONZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru; kwa kuwa Songwe ni Wilaya naomba kufahamu ni lini sasa Serikali itatujengea Kituo cha Polisi katika Kata ya Mkwajuni chenye hadhi ya Kiwilaya? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge wa Songwe kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyowahi kusema kwenye majibu yetu ya msingi ujenzi wa vituo vya polisi vya wilaya na mikoa utaendelea kadri tutakavyopata fedha, kipaumbele kwa mwaka ujao ni kujenga Makao Makuu ya Mikoa na baada ya hapo tutaingia kwenye wilaya zetu. Kwa hiyo, tutakapopata fedha tutajenga ndani ya Wilaya ya Songwe. Nashukuru. (Makofi)
MHE. ORAN M. NJEZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana; kwa kuwa wananchi wa Wilaya ya Mbeya, Jimbo la Mbeya Vijijini wameweza kujenga Kituo cha Polisi cha Wilaya ya Mbalizi na sasa kuna mahitaji makubwa ya kujenga kituo katika Kata ya Igoma na Kata ya Ilembo. Je, ni lini Serikali itaunga mkono nguvu za wananchi kwa ujenzi wa vituo hivyo viwili? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali mawili ya Mheshimiwa Mbunge wa Mbeya Vijijini kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza tuwapongeze wananchi wa kata hizo mbili ambao wameanza ujenzi wa vituo vya polisi vya kata zao, naomba nikubaliane na Mheshimiwa Mbunge kwamba Wizara itatuma wataalam kutoka Jeshi la Polisi kwa ajili ya kufanya tathimini kuona kiwango cha ujenzi kilichofikiwa, kiasi gani cha fedha kinahitajika ili kumalizia tuweze kuingiza kwenye mpango wetu wa bajeti wa kumalizia vituo ambavyo vimejengwa kwa nguvu za wananchi. Kwa hiyo, tunaomba awe na subira kidogo.
MHE. ASHA ABDULLAH JUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mara kadhaa Waheshimiwa Wabunge wamekuwa wakisimama na kuomba kujengewa vituo au kukarabatiwa.

Sasa ni lini Serikali itaandaa mpango mzima utakoonyesha orodha wa vituo vinanavyotaka kujengwa au kukarabatiwa kwa nchi nzima ili kuwapunguzia waheshimiwa kusimama kuomba vituo mwaka nenda mwaka rudi? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nijibu swali la Mheshimiwa Asha Juma Mshua kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapokea ushauri wako na kwa kweli Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi imeandaa mpango mkakati wa kuboresha sekta ya usalama wa raia ikiwa ni pamoja na uimarishaji wa majengo. Kwa hiyo, ushauri wa kuleta mwongozo hapa unaoonyesha kituo gani kitajengwa lini au kitakarabatiwa lini tutauandaa tuweze kuuleta kwa Waheshimiwa Wabunge ili kwa kweli kupunguza maswali mengi ya nyongeza ambalo jibu lake linakuwa kama vile linafanana. Nashukuru.
MHE. ANATROPIA L. THEONEST: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Halmashauri ya Kyerwa ni moja kati ya Wilaya mpya ambayo pia haina Kituo cha Polisi, hivyo OCD utumie ofisi ndogo ambayo iko Kagenyi, wananchi tayari wameanza tayari ujenzi wa kituo cha polisi cha wilaya.

Nataka nijue ni lini Serikali itawapelekea fedha ili waweze kumalizia ujenzi ambao wameuanzisha kwa nguvu zao wenyewe? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: - (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli tunatambua uwepo wa halmashauri au wilaya nyingi ambazo hazina vituo vya polisi vya Wilaya kwa maana ya OCDs officce na niwashukuru halmashauri ambazo wanatoa majengo kwa ajili ya kutumiwa na wenzetu wa polisi ni muahidi tu Mheshimiwa Mbunge kama ambavyo nimekuwa nikisema katika majibu ya nyongeza hapa, ya maswali ya msingi tunaendelea kujenga vituo vya polisi kwenye mikoa na wilaya ambazo hazina kabisa vituo hivyo. Kwa hiyo, Wilaya ya Kyerwa ni moja ya wilaya ya kipaumbele hasa ukizingatia kwamba iko mpakani pale ambapo itatokea tutapata fedha tutaipa kipaumbele cha juu. Nashukuru. (Makofi)
MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi; Wilaya ya Tanganyika ni wilaya ambayo ipo pembezoni mwa mipakani, ni wilaya ambayo haina kabisa kituo cha polisi na wananchi wamejiotolea kupitia hamasa ya Mkuu wa Wilaya wameanza kutoa michango ya kujenga kituo cha polisi.

Je, ni lini Serikali itawapelekea fedha ili wananchi hao waweze kupata kituo cha polisi?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyokwishajibu kwenye suala la Kyerwa, Wilaya zote za mpakani ni kipaumbele cha Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kuona kwamba zinapata vituo vya polisi kwa ajili ya kuimarisha usalama wa raia na mali zao. Kwa hiyo, pale ambapo tutapata fedha Wilaya ya Tanganyika itajengewa kituo cha polisi kama ambavyo tumeahidi katika bajeti yetu iliyosomwa na Waziri wangu hapa mwezi mmoja uliopita.
MHE. ASIA A. HALAMGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Kwanza nichukue nafasi hii kuishukuru Serikali kwa kutengwa kwa kiwango hicho cha fedha na mwezi Oktoba jengo hilo litakuwa limekamilika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la nyongeza; kwa kuwa kwa sasa Mkoa wetu wa Manyara tuna changamoto kubwa ya upatikanaji wa hati za kusafiria lakini pamoja na hati za makazi. Inatulazimu kupata huduma hiyo Mkoa wa Arusha, Mkoa wa Dodoma na Mkoa wa Singida na siyo Mkoa wa Manyara.

Je, Serikali iko tayari sasa kutufungia elektroniki ili tuweze kupata huduma hiyo ndani ya Mkoa wetu?

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini swali la pili; kwa kuwa Mkoa wa Manyara uko pembezoni na wahamiaji haramu wengi wanatumia kama njia ya kupita kwenda kwenye nchi zingine.

Je, Serikali haioni haja ya kutuongezea watumishi pamoja na usafiri kwa sababu kwa sasa watumishi wetu wanatumia pikipiki badala ya usafiri wa magari?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Halamga kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakiri kwamba katika Mkoa wa Manyara huduma za kutoa pass kwa electronics zilikuwa hazijafungwa kwenye jengo hili kwa sababu jengo lilikuwa halijakamilika. Hivi sasa watumishi wa ngazi ya Mkoa wako kwenye jengo la Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Manyara na mimi nimshukuru Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa kuwaweka watumishi hawa kwenye jengo lake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini namuahidi Mheshimiwa Halamga, jengo litakapokamilika mifumo yote ya electronic ya utoaji wa pass zitatolewa kwenye jengo letu la uhamiaji baada ya Oktoba mwaka huu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu nyongeza ya watumishi na magari, nakubali kwamba Mkao wa Manyara unalo gari moja tu aina ya Forde Ranger liliko ngazi ya Mkoa, Wilayani kule tunatumia usafiri wa pikipiki, lakini pia kuna uhaba wa watumishi kama alivyokwishaeleza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama Waheshimiwa Wabunge wanakumbuka wakati wa bajeti tulitamka kwamba wapo watumishi 820 ambao wataajiriwa kama watumishi wapya, wako kwenye mafunzo sasa hivi, wanatarajia kuhitimu mwezi Septemba, 2022. Katika mpango wetu wa ugawaji tutazingatia maeneo yenye upungufu mkubwa zikiwemo Wilaya za Mkoa wa Manyara. Nashukuru.
MHE. IDDI K. IDDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo lililoko Manyara ni sawasawa na Halmashauri ya Msalala, Wilaya ya Kahama. Kwa kuwa Kata ya Isaka kumekuwa na ongezeko la wageni mbalimbali na ukizingatia uwepo wa bandari na uendelezaji wa ujenzi wa bandari mpya, hivyo kuongeza idadi ya watu katika Kata ya Isaka. Sasa Serikali ina mpango gani wa kuanzisha kituo cha uhamiaji?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Iddi, Mbunge wa Msalala kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunatambua uwepo wa muingiliano mkubwa wa wananchi pamoja na wageni kwenye eneo lake hasa kutokana na shughuli kubwa za kiuchumi za uchimbaji wa madini na kwa mtaji huo ni halali Wilaya yake kupata ofisi ya uhamiaji. Na sera ya Wizara ni kuhakikisha kwamba kila ilipo wilaya siyo halmashauri na pale Wilaya ya Kahama ipo ofisi yetu ya Uhamiaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunaomba watu wote wanaokwenda Msalala waendelee kutumia huduma zinazotolewa katika ofisi ya wilaya ambayo iko pale Kahama. Lakini patakapotokea umuhimu wa kupanua zile huduma kuzipeleka kule, tutashirikiana na Mheshimiwa Mbunge kupata majengo kule ili yaweze kutumika kutoka huduma hiyo. Nashukuru.
MHE. ZUENA A. BUSHIRI: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Naomba niulize swali; je Serikali haioni haja ya kurejesha huduma hii katika halmashauri sasa hivi?

Mheshimiwa Spika, swali la pili; Wizara imejipanga vipi kudhibiti janga la moto katika masoko nchini? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza Mheshimiwa Bushiri kama kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, moja; kuhusu umuhimu wa kurejesha huduma hizi halmashauri, naomba nilikumbushe Bunge lako tukufu kwamba huko nyuma huduma hizi zilikuwa zinatolewa na halmashauri, baada ya kuthibitika kwamba weledi na uwezo wa halmashauri kutekeleza jambo hili ni changamoto ikaamuriwa huduma hizi zirudi Makao Makuu na ndiyo ikaimarishwa hili Jeshi la Zimamato na Ukoaji. Kwa hiyo kama tunazungumza kurejesha itabidi tufanye tathimini kujiridhisha leo ule uwezo ambao haukuwepo miaka kumi iliyopita kama umekuwepo na hivyo kuona umuhimu wa kurejesha hizi huduma.

Hata hivyo, wananchi wanao hudumiwa wapo kwenye halmashauri na wengi ni wafanyabiashara ni wazi kwamba bajeti ya zimamoto ni changamoto, hivyo halmashauri zinatakiwa kuanza kutenga bajeti kwa ajili ya kununua vifaa ili askari wetu waliopangwa kwenye maeneo hayo wavitumie vifaa hivyo kuzima moto kwenye maeneo yao.

Mheshimiwa Spika, swali la pili juu ya namna ya kudhibiti majanga ya zimamoto yanayozidi kuongezeka; nakiri kwamba yapo ndiyo maana nimebainisha mikakati hapa itakayosaidia kuimarisha utoaji wa huduma za zimamoto na ukoaji ikiwa ni pamoja na mafunzo, lakini vilevile elimu kwa umma na kuzingatia weledi katika ujenzi wa majengo yetu. Nashukuru.
MHE. DKT. CHRISTINA C. MNZAVA: Mheshimiwa Spika, ahsante, kwa kuwa changamoto ya vifaa katika Jeshi la Zimamoto ni mtihani hasa katika Manispaa ya Shinyanga.

Mheshimiwa Spika, unaunguliwa mita 100 zimamoto inakuja inashindwa kuzima moto, je, ni lini Serikali itaboresha miundombinu ya zimamoto katika Manispaa ya Shinyanga?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Dkt. Christina Mnzava, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kama nilivyosema katika jibu langu la msingi ipo mikakati mingi ambayo tunaitumia katika kuboresha, moja; ni ajira kwa kuongeza nguvu kazi lakini pili manunuzi ya vifaa mmetupitishia bajeti hivi juzi zaidi ya bilioni 11 zinakwenda kununua vifaa ambavyo vitapeleka kwenye maeneo yenye changamoto kubwa ikiwemo Mkoa wa Shinyanga. Nashukuru.
MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa nafasi hii; kwa kuwa halmashauri nyingi hazina zimamoto, je, Serikali ipo tayari kujipanga upya sasa badala ya kutoka katika sehemu moja za Wilaya na Manispaa na Majiji kwenda katika Halmashauri zetu au kukasimu madaraka ya zimamoto katika Halmashauri ili kuweka wigo mpana wa namna ya kuzima moto katika maeneo yetu?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Yahaya Massare, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli kama nilivyosema kwenye jibu la msingi zipo halmashauri ambazo hazina kabisa huduma hizo, lakini ipo mikoa pia ambayo haina huduma hizo, ndiyo maana tukasema kulingana na mipango yetu na bajeti tutaanza na mikoa ambayo haina kabisa huduma za zimamoto na ukoaji tukiendelea kuimarisha uwezo huo kwenye mamlaka kubwa kama manispaa, miji na majiji baadaye tutaendelea kupanua huduma hizi kwenda Mamlaka za Serikali za Mitaa ambazo zipo vijijini. Nashukuru.
MHE. DOROTHY G. KILAVE: Mheshimiwa Spika, ahsante, kutokana na majanga makubwa ya Mkoa wa Dar es Salaam hasa kuunguliwa kwa masoko.

Je, Serikali ina mkakati gani wa kuongeza magari ya zimamoto?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Kilave, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, tunatambua kweli kwamba Jiji la Dar es Salaam linaongoza katika majanga haya ambayo tumejiridhisha kwamba mengine ni uzembe, lakini mengine ni miundombinu ambayo husababisha athari za moto. Kwa kuzingatia hilo ndiyo maana katika bajeti ya mwaka huu tayari tuna magari matatu yaliyokuwa yanatengenezwa na kiwanda chetu cha NYUMBU yatagawiwa kwenye mikoa yenye changamoto kubwa likiwemo Jiji la Dar es Salaam.

Mheshimiwa Spika, hata hivyo, mwaka ujao tunayo bajeti ya zaidi ya Euro milioni 4.9 kwa ajili ya ununuzi wa vifaa vya magari na maeneo yote yenye changamoto yatagawiwa vifaa hivyo.
MHE. DKT. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi niulize swali dogo la nyongeza.

Kwa kuwa Mkoa wetu wa Iringa kuna msitu Mufindi, Mgololo na kuna msitu katika Wilaya ya Kilolo na moto kila wakati umekuwa ukitokea katika hiyo misitu; ni lini Serikali itaona umuhimu wa Wilaya ya Kilolo na Wilaya ya Mufindi kupatiwa gari la zimamoto?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba kumjibu Mheshimiwa Ritta Kabati swali lake la nyongeza kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba maeneo ya Mufindi na Mgololo mara kadhaa hukumbwa na majanga ya moto, niombe tu uongozi wa zimamoto Mkoa wa Iringa waweze kupangilia vizuri rasilimali za magari walizonazo ili angalau gari moja liwe kwenye Wilaya ya Mufindi kuwa na ukaribu kwenye maeneo ambayo majanga hutokea zaidi. Nashukuru.
MHE. HAJI AMOUR HAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, kwanza nashukuru kwa jibu lake zuri Mheshimiwa Naibu Waziri, pia nina swali langu la nyongeza.

Katika Jimbo langu la Pangawe kuna kituo kidogo cha polisi kinaitwa Kijitopele. Bahati nzuri kwamba au bahati mbaya kunakuwa na wahalifu wengi sana ambao wanakitumia kituo kile na ukiangalia wahalifu wale maana yake wanakuwa hawana nafasi ya kutosha ndani ya kituo kile. Je, Serikali ina mpango gani kukiboresha Kituo cha Kijitopele? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Haji Amour Haji, Mbunge wa Pangawe, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyokwishasema katika nyakati tofauti na bahati nzuri kwa Zanzibar nimeshatembelea vituo hivyo na kubaini kwamba vingine vina hali dhaifu, tutaendelea kupitia Mfuko wa Tuzo na Tozo kuviimarisha vituo hivi na kuwapanga askari watakaotoka vyuoni ili waweze kusimamia usalama wa raia na mali zao kikiwemo hiki kituo alichokitaja Mheshimiwa Mbunge wa Pangawe. Nashukuru.
MHE. FATMA H. TOUFIQ: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa fursa nami niweze kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, kumezuka vikundi vya wahalifu katika Kata ya Makulu, Jiji la Dodoma vinavyojiita panya karowa. Nini mkakati wa Serikali katika kuhakikisha kwamba vikundi hivi haviendelei katika maeneo mengine na kuleta uhalifu? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Toufiq kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kama ambavyo tunapiga vita makundi yote ya wahalifu awe mtu mmoja au vikundi kama ilivyokuwa panya road Dar es Salaam. Namhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba kwa Dodoma hiyo kazi pia imeanza na baadhi ya vijana wa aina hiyo wameshatiwa nguvuni. Sasa hilo ulilosema eneo gani umetaja Kata ya hawa panya nini karoga? Tutashughulika nao hawa.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kikao hiki tutaongea na Mbunge ili anieleze kwa ufasaha ni eneo gani na kundi hili ili askari wetu wa Jiji la Dodoma waweze kushughulika nao. Nashukuru. (Makofi)
MHE. SOUD MOHAMMED JUMAH: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa tatizo la uhalifu limekuwa likiongezeka siku hadi siku katika maeneo mbalimbali ya Zanzibar na tatizo hili limeshazungumzwa sana hapa Bungeni.

Je, Mheshimiwa Naibu Waziri ana mkakati gani wa kushirikiana na Vikosi Maalum vya SMZ kule Zanzibar ili kuweza kutokomeza na kufanya jambo hili kuwa historia? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Soud Mohammed - Mbunge, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, makosa ya uhalifu kama ambavyo yanatokea maeneo tofauti, yamebainishwa Zanzibar vikundi vinaongezeka na nilikuwepo kule, viko vikundi vingine vya wavuta bangi. Lakini kinachofurahisha Jeshi la Polisi Kamisheni ya Zanzibar wanafanya kazi nzuri sana na kwa kawaida vyombo hivi hushirikiana na vyombo vingine vya usalama vikiwemo SMZ katika vikao mbalimbali vya ngazi ya Mkoa, kuna Kamati za Usalama za Mkoa, ngazi ya Wilaya kuna Kamati za Usalama za Wilaya na hivyo kupeana ushauri na mbinu za kukabiliana na matukio haya.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nikuhakikishie polisi wetu wako imara kwa kushirikiana na vyombo vingine watakabiri makundi haya yanayoibukia huko Zanzibar kwa madhumuni ya kuyadhibiti. Nashukuru.
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru; ukatili katika jamii kama ambavyo umeibuka ukatili wa wahalifu wa panya road, kumeibuka ukatili mkubwa sana kwa wanawake na watoto hasa kipindi hiki wanawake wanauliwa, watoto wanafanyiwa vitendo vya ajabu, lakini bado hatujaona jitihada za dhati za Serikali kupitia Jeshi la Polisi kukabiliana na uhalifu huu wa kuwadhuru wanawake na watoto ambao wanatakiwa walelewe vizuri, wawe watumishi bora huko baadae? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Ester Bulaya, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli yapo matukio mengi yanaripotiwa ya uhalifu yanayohusisha mauaji, lakini na mateso kwa watoto, kwa wanawake lakini wakati mwingine hata kwa wanaume. Mimi niseme kama nilivyosema kwenye jibu la msingi, uhalifu ni zao la jamii. Ipo haja ya wazazi, walezi, watu wa dini, viongozi kama sisi kwa pamoja tushirikiane kukabiliana na uhalifu huu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, Jeshi la Polisi kila inapotokea kupata taarifa ya uhalifu huu, huchukua hatua bila kumchelea mtu. Kwa hiyo, niahidi tu Mheshimiwa Bulaya tutaendelea kushirikiana na wadau wa amani kokote walipo ili kudhibiti matendo ya namna hii kwenye jamii zetu. Nakushukuru sana.
MHE. MARYAM AZAN MWINYI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana, pamoja na majibu mazuri ya Serikali nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa Wizara imepata ardhi ya kujenga Kituo kimoja cha Polisi; je, ina mkakati gani wa kupata ardhi kujenga vituo vitatu vilivyobaki?

Mheshimiwa Spika, swali langu la pili, eneo la Pujini ni miongoni mwa maeneo yenye uhalifu sana; je, Serikali haioni? Ichukue uharaka wa kujenga kituo hicho cha polisi, ili kulinda mali na usalama wa raia?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Maryam Azan Mwinyi, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba, ardhi inahitajika na kupitia Bunge lako tukufu nimtake Kamishna wa Polisi Zanzibar awasiliane na mamlaka ya ardhi katika Wilaya ya Chakechake ili waweze kumpangia ardhi kwa ajili ya kujenga kwenye maeneo hayo niliyoyabaini.

Mheshimiwa Spika, kuhusu eneo lenye changamoto ya uhalifu, niseme kwamba kwa sasa kwa sababu hakuna fedha za kujenga Kituo cha Polisi, basi Polisi Wilaya ya Chakechake waimarishe doria ili kudhibiti makundi yote ya uhalifu kwenye eneo hilo. Nashukuru.
MHE. KABULA E. SHITOBELA: Mheshimiwa Spika, ahsante, Kituo cha Polisi Kata ya Kiseke, Ilemela hakina nyumba ya askari na kusababisha kituo kufungwa saa 12.00 jioni. Je, Serikali itakamilisha lini nyumba hiyo ili kuepusha kituo kufungwa saa 12.00 jioni?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba eneo la Kiseke ni eneo ambalo lina shughuli nyingi za kiuchumi na kibiashara na msongamano mkubwa wa watu na matukio ya uhalifu yapo, na tunatambua kwa juhudi za Mheshimiwa Mbunge wa Viti Maalum na Mbunge wa Jimbo la Ilemela wamekuwa mara kwa mara wakisumbua Wizarani ili waweze kujengewa nyumba hii.

Mheshimiwa Spika, kwa vile wameshaanza ujenzi niahidi tu kwamba kupitia Jeshi la Polisi chini ya Mfuko wa IGP wa Tuzo na Tozo, tutawasiliana na Mheshimiwa Mbunge ili kupata fedha za kukamilisha kituo hicho hasa baada ya kufanya tathmini ya kiwango cha fedha zinazohitajika. Nashukuru.
MHE. STANSLAUS S. MABULA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru, kwa kuwa Serikali sasa imeamua kujenga vituo hivi vya polisi kuanzia ngazi ya kata. Ni lini sasa Serikali itakuwa tayari kukamilisha ujenzi wa Kituo cha Polisi Nyegezi kwa ajili ya Kanda ya Ukanda wa Nyegezi?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Stanslaus Mabula, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba ni nia ya Serikali kujenga vituo vya polisi, kuimarisha usalama wa raia ngazi ya kata na ni kwa msingi huo tumeweza kutoa askari kata katika kata zote nchini.

Sasa hili suala la ujenzi wa vituo ni suala la gharama na kwamba katika kipindi kifupi hatuwezi kufanya hivyo kulingana na mpango wetu wa ujenzi. Tutaanza na mikoa ambayo haina Ofisi za RPC, lakini Wilaya ambazo hazina vituo vya OCD. Kwa hiyo, vilivyo kwenye ngazi za kata tumuombe Mheshimiwa Mbunge kushirikiana na wadau waanze ujenzi ili Serikali ije isaidie kukamilisha vituo hivyo. Nashukuru.
MHE. SUMA I. FYANDOMO: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, kule kwetu Mkoani Mbeya askari wanafanya kazi nzuri sana ya kulinda rai ana mali zao, lakini askari hawa nyumba zao ni chakavu kweli kweli ukizingatia ni Wilaya zote hakuna nyumba za askari ambazo zinaridhisha.

Sasa je, ni lini Serikali itafanya mpango wa kufanya ukarabati kwenye nyumba hizo za askari wetu? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge wa Viti Maalum, Mbeya, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwanza nitambue kwamba, maeneo mengi ya vituo vya polisi, makazi ya askari katika maeneo hayo ni chakavu sana na ni kwa msingi huo ndio maana tumeanza ukarabati katika maeneo hayo. Na kwa kweli Mbeya kama Mkoa mkubwa ukanda wa Nyanda za Juu Kusini, kipaumbele kimewekwa kule katika mwaka ujao tutatia kipaumbele ukarabati wa nyumba za askari katika Jiji la Mbeya. Nashukuru sana.
MHE. ENG. EZRA J. CHIWELESA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana, tatizo la usafiri kwa Kituo cha Polisi cha Mavota ambacho kinahusika na ulinzi wa mgodi wa Biharamulo Gold Mine ni kubwa. Tuna kituo pale, lakini hakuna usafiri hata pikipiki.

Sasa ni lini labda Serikali itatusaidia kupata hata usafiri wa pikipiki mbili/tatu ili tuweze kuimarisha ulinzi juu ya wawekezaji ambao wamewekeza katika mgodi ule wa Mavota?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge wa Biharamulo, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba vituo vingi vya polisi havina usafiri wa uhakika, hasa vituo vilivvyo kwenye ngazi ya kata na kwenye maeneo mahususi kama haya ya migodi. Pengine nitumie nafasi hii kueleza kwamba katika mwaka wa fedha huu na ujao tuna magari zaidi ya 300 ambayo yatapatikana na sehemu ya magari hayo ni ku-support usafiri kwenye vituo mbalimbali vya polisi. Sasa pengine niwasiliane na Mbunge kuona uhitaji wa usafiri wa pikipiki katika kituo hiki ili tushirikiane kuzungumza na wadau waweze kutoa fedha kuwezesha ikiwa mpango wa Serikali wa magari hayo utachelewa kufika. Nashukuru.
MHE. JOSEPH G. KAKUNDA: Mheshimiwa Spika, ninaomba niulize swali la nyongeza kwamba Wilaya ya Sikonge ambayo ni miongoni mwa Wilaya kubwa kieneo la kijiografia haina kituo chenye hadhi ya Kituo Kikuu cha Polisi cha Wilaya, badala yake wanatumia jengo dogo ambalo lilijengwa na chifu mwaka 1957. Je, ni lini Serikali itajenga Kituo cha Polisi chenye hadhi ya Kituo cha Polisi cha Wilaya? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Kakunda, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba Wilaya nyingi za polisi hazina majengo ya polisi ya ngazi ya Wilaya na ndio maana kama mnakumbuka Waheshimiwa Wabunge kwenye bajeti hii tumezungumzia haja ya kuanza kujenga vituo vya polisi ngazi ya Mkoa na Wilaya kule ambako vituo hivyo havipo. Sikonge najua ni eneo ambalo pia halina hadhi hiyo, kwa hiyo, tutaweka kipaumbele Mheshimiwa Mbunge ili katika mwaka ujao iweze kuzingatiwa katika bajeti tayari tuanze ujenzi wa kituo hicho. Nashukuru sana.
MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru, Kituo cha Polisi cha Kigonga kinahudumia wananchi waliopo mpakani mwa Tanzania na Kenya wa kata za Itirio, Nyanungu, Mlimba na Gorong’a, lakini kituo hiki kilijengwa kwa full-suit ya mabati kana kwamba kimechakaa na polisi wamekimbia hawapo tena pale.

Sasa ningetaka kujua ni lini Serikali itajenga kituo hiki kwa sababu ni kituo cha kimkakati ukizingatia kipo mpakani?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Esther Matiko kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, viwango vyetu vya kujenga vituo vya polisi siyo kuwa full-suit ya mabati, kwa hiyo kama kuna kituo cha aina hiyo hakikidhi viwango pengine sasa niwasiliane na Mheshimiwa Mbunge na mamlaka ya Serikali za Mitaa kule Temeke ili tuanze mkakati wa kujenga kituo kwa kutumia vifaa vya kudumu ikiwa ni matofali na kadhalika...

MBUNGE FULANI: Tarime.

NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Tarime vijijini yes, kwa hiyo nachukua ahadi...

SPIKA: Waheshimiwa hapa mnapenda kuwazungumzisha Mawaziri wakiwa wanazungumza mwache amalize jibu lake, ukiwa unaongea naye anaanza kuongea na wewe badala ya kuongea na mimi hapa mbele.

Mheshimiwa Naibu Waziri malizia majibu yako.

NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, nashukuru nilikuwa nasema hatuna vituo vinavyopaswa kuwa vya polisi vyenye kujengwa kwa full-suit za mabati kwa hiyo kituo hiki kama kweli kipo kule mpakani tutashirikiana na uongozi wa Polisi Kanda Maalum ya Tarime Rorya ili kuwa na mpango wa kujenga kituo hiki kwa aina ya vifaa vinavyostahiki kujengea kituo cha polisi. Kwa hiyo, nimuondoe mashaka Mheshimiwa Mbunge kwamba tutaweka kipaumbele na kwa vile kituo kiko mpakani, kilete taswira nzuri ya kituo stahiki katika nchi yetu, nashukuru sana.
MHE. SHAMSIA A. MTAMBA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipatia nafasi ili niweze kuuliza swali dogo la nyongeza.

Katika Makao Makuu ya Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara Vijijini hatuna kabisa kituo cha polisi; je, ni lini Serikali itatujengea kituo cha polisi katika halmashauri yetu?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Shamsia kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kama nilivyokwishaeleza katika maswali niliyojibu muda mfupi uliopita, si wilaya zote zina vituo vya polisi vya ngazi ya wilaya kwa kulitambua hilo ndiyo maana tuna mpango mkakati wa kiwizara wa kujenga vituo vya polisi vya OCD katika kila wilaya kulingana na mpango wetu na kwa mujibu wa upatikanaji wa fedha Kituo cha Polisi cha Wilaya ya Mtwara na kwa umuhimu wa ukanda ule kitapewa kipaumbele, nashukuru sana.
MHE. MWANTUMU DAU HAJI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana, kwanza napenda kushukuru Serikali yangu sikivu kwa jitihada zake inazozifanya kuibua miradi ya vituo vya Polisi nchini.

Mheshimiwa Spika, kituo cha Wilaya ya Kati, Mkoa wa Kusini Unguja, kilianza kujengwa toka mwaka 2016, hadi hii leo 2022 kituo hicho bado hakijamalizwa. Kilijengwa kikapigwa plasta baadhi ya vyumba, chooni bado, nje hakijapigwa plasta hadi hii leo Polisi wapo Wilaya ya Kati wameazimwa eneo la vitambulisho ndiko wanakofanyia kazi zao. Je, Serikali itamaliza lini Kituo hiki cha Polisi cha Dunga, ili Polisi waweze kufanya kazi kama kawaida?(Makofi)

NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mwantumu Dau Haji, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwanza ninampongeza Mheshimiwa Mbunge kwa ufuatiliaji wake makini juu ya kituo hiki na juhudi zilizofanywa na wananchi katika kujenga kituo hiki mpaka hatua iliyofikiwa, ulituelekeza siku moja hapa na mimi nikajibu kwamba Wizara inaandaa mpango wa kumalizia vituo na kujenga maeneo ambayo hayana vituo kabisa. Kipaumbele kitawekwa kwenye maeneo ambayo tayari wameshajenga vituo kama hawa wa Dunga. Kwa hiyo, nimuhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, katika mwaka ujao tutafanya kila liwezekanalo ili ukamilishaji wa kituo hicho uweze kuanza.

Mheshimiwa Spika, ninashukuru sana.(Makofi)
MHE. EMMANUEL P. CHEREHANI: Mheshimiwa Spika, wananchi wa Jimbo la Ushetu wamejichanga wakafanikiwa kujenga msingi wa Kituo cha Polisi lakini mpaka leo ni zaidi ya miaka mitatu Serikali haijafanya chochote. Sasa, ni lini Serikali itakamilisha ujenzi wa Kituo cha Polisi kwa wananchi wa Jimbo la Ushetu?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Cherehani kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, tunafahamu Ushetu ni moja ya Wilaya mpya ambazo hazijawa na Vituo vya Polisi ngazi ya Wilaya na kwenye Kata mbalimbali. Pia tunatambua juhudi ambazo zimefanywa na wananchi kuanza ujenzi wa vituo hivi na Serikali inao wajibu wa kusaidia kukamilisha. Ninapenda kumuahidi Mheshimiwa Mbunge kama nilivyokwishasema kwenye jibu la msingi kwamba kipaumbele kitawekwa kwenye maeneo ambayo wananchi na wadau wameanza kujenga vituo hivyo ili kuvisaidia ujenzi huo uweze kukamilika. Nashukuru.
MHE. GHATI Z. CHOMETE: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kuniona. Wilaya ya Butiama haina Kituo cha Polisi chenye hadhi ya Wilaya. Je, ni lini Serikali itajenga kituo hicho?

NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Ghati Chomete, Mbunge Viti Maalum Mkoa wa Mara kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba Wilaya ya Butiama ni moja ya Wilaya mpya ambazo hazina Vituo vya Polisi ngazi ya Wilaya na Kata zake mbalimbali hazina vituo hivyo. Kama nilivyokwishasema kwenye jibu langu la msingi, kipaumbele katika ujenzi wa Vituo vya Polisi utazingatia Mikoa, Wilaya na Kata ambazo hazina kabisa vituo lakini msisitizo utawekwa kwa wale ambao tayari wana maeneo na wameanza kujitolea. Kwa hiyo, nimuahidi Mheshimiwa Mbunge kwamba Wilaya ya Butiama ni moja ya eneo litakalozingatiwa katika bajeti ijayo. (Makofi)

MHE. LIVINGSTONE J. LUSINDE: Mheshimiwa Spika, ninakushukuru kwa kunipa nafasi hii ya kuuliza swali moja la nyongeza lakini nami niwapongeze Yanga kwa kupata Ubingwa baada ya kusota kwa miaka minne ndiyo leo wanapumua hapa unawasikia, ubingwa ulikuwa mikononi mwa Simba. Baada ya kuwapongeza naomba niulize swali moja la nyongeza:-

Mheshimiwa Naibu Waziri, utakubali kuongozana nami kufika Mvumi kujionea hali ilivyo kwa askari wa pale Mvumi Misheni ili tuweze kujenga kituo pamoja? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Lusinde kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, hakuna shida kabisa, baada ya Bunge hili tutazingatia ratiba ili tuweze kuongozana tukatizame changamoto zinazowakabili wananchi wa Kata zako ambako hakuna Vituo vya Polisi ili tuweze kushirikiana kuvikamilisha. Nashukuru sana.
MHE. GEORGE N. MALIMA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, vitendo vya uhalifu vimekithiri sana katika Kata ya Berege iliyopo Jimbo ya Mpwapwa. Je, Serikali itajenga lini Kituo cha Polisi ili kukabiliana na wimbi hili la uhalifu?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa George Malima, Mbunge wa Mpwapwa kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba baadhi ya maeneo hasa Miji inayokua na kuchipua ikiwemo Wilaya ya Mpwapwa kuna kuongezeka kwa vitendo vya uhalifu. Kama nilivyowahi kusema hapa, uhalifu ni zao la jamii lakini si jambo jema kufanywa na vijana wetu ambao wanazo fursa mbalimbali wakizitumia wanaweza kupata riziki zao bila kulazimika kuleta uhalifu katika jamii. Kwa hiyo, nichukue nafasi hii kulitaka Jeshi la Polisi ngazi ya Mikoa, Wilaya na Kata kuimarisha shughuli za usimamizi wa usalama wa raia na mali zao lakini kuchukua hatua thabiti dhidi ya vijana au watu wanaojihusisha na matendo ya uhalifu. Nashukuru sana.
MHE. BONIPHACE N. BUTONDO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii yakuuliza swali la nyongeza. Wananchi wa Jimbo la Kishapu, wadau wa maendeleo pamoja na Mfuko wa Jimbo tumechangia zaidi ya Milioni 50 kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Polisi cha Wilaya. Je, Mheshimiwa Waziri yupo tayari kuambatana na mimi kwenda kuona jitihada za wananchi na kuweka mchango wa Serikali?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Boniphace Butondo, Mbunge wa Kishapu kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, nakubali kuongozana na Mheshimiwa Butondo ili kwanza kutambua juhudi zilizofanywa na wananchi, wadau pamoja na yeye mwenyewe kupitia Mfuko wake wa Jimbo. Pili ni kuona namna ambavyo Serikali inaweza kuchangia kukamilisha kituo hiki cha ngazi ya Wilaya. Nashukuru sana.

MHE. ABDALLAH J. CHAUREMBO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kunipa nafasi. Ni lini Serikali itamalizia ujenzi wa Kituo cha Polisi Mbande Kata ya Chamazi?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Abdallah Chaurembo Mbunge kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwanza tunatambua juhudi za Mheshimiwa Mbunge na wananchi wa Jimbo lake Mbagala kwa juhudi wanazofanya katika kuimarisha usalama wa raia na mali zao. Kwa kutambua juhudi hizo, nasi kama Serikali kupitia Jeshi la Polisi tutatembelea Kituo cha Mbande kutathmini kiasi gani kinahitajika ili kuweza kumalizia na hivyo kutoa mchango wetu ili kukamilisha kituo hicho kama sehemu ya kuunga mkono juhudi za wananchi.

MHE. BUPE N. MWAKANG’ATA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kuniona. Kituo cha Polisi cha Sumbawanga Mjini Mkoani Rukwa ni cha toka enzi za mkoloni, ni kidogo hakina hewa. Je, ni lini Serikali itaanza ujenzi wa kituo hicho?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Rukwa kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, tunatambua wilaya za zamani ikiwemo Wilaya ya Sumbawanga ina Vituo vya Polisi ambavyo moja vimejengwa muda mrefu baadhi vimeanza kuwa chakavu lakini vingine havikidhi haja ya viwango vya Vituo vya Polisi vinavyotakiwa kuwepo sasa hivi ngazi ya Wilaya. Kwa hiyo, ninachukua dhima kumuahidi Mbunge kwamba katika kazi tunayoifanya ya kuimarisha maeneo ambayo hayana kabisa vituo, jambo jingine ni kukarabati na kuboresha vituo vya kizamani ili kuweza kukidhi mahitaji ya sasa. Kwa hiyo, Sumbawanga itakuwa ni eneo litakalozingatiwa.
MHE. JANEJELLY J. NTATE: Mheshimiwa Spika, ahsante. Tuangoma ni Kata yenye mkusanyiko wa watu wengi sana na kata hiyo haina Kituo cha Polisi. Je, ni lini Mambo ya Ndani mtajenga Kituo cha Polisi pale Kata ya Tuangoma?

NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Janejelly Ntate Mbunge wa Viti Maalum, Mkoa wa Dar es Salaam kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba Tuangoma ni moja ya Kata za Jiji la Dar es Salaam ambao haina Kituo cha Polisi, nimuombe Mheshimiwa Mbunge na especially Mbunge wa Jimbo achangie kidogo na kuhamasisha wadau kushiriki ili Serikali ije isaidiane nanyi kukamilisha, kama ambavyo maeneo mengine wamefanyakazi hiyo. Nashukuru sana.

MHE. ERIC J. SHIGONGO: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana, Jimbo la Buchosa lina takriban idadi ya watu wasiopungua 400,000 lakini na kituo cha Polisi katika Mji Mdogo wa Nyehunge ambacho hadhi yake ni ndogo sana. Je, ni lini Mheshimiwa Waziri atakuwa tayari kutembelea kituo hiki ili aweze kukiona na hatimaye kufikia maamuzi ya kujenga kituo kingine?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza Mheshimiwa Eric Shigongo Mbunge wa Buchosha, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni bahati njema kwamba nimepanga kufanya ziara katika Mkoa wa Mwanza na Wilaya hii ni sehemu ya Mkoa wa Mwanza. namuahidi Mheshimiwa Mbunge, nitakapofanya ziara eneo hilo nitatembelea eneo ya Nyehunge ili kuona ni nini tushirikiane na Mbunge kufanya kukamilisha ujenzi wa Kituo cha Polisi kama njia ya kuimarisha usalama wa raia kwenye maeneo hayo. Ahsante sana.

MHE. JERRY W. SILAA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi, nimshukuru sana Mheshimiwa Waziri kwa kauli yake kwamba Serikali itaunga mkono jitihada za wananchi. Pale Mzinga Injinia Cyprian Romeja na wananchi wenzake wamechanga Milioni 108 na Mbunge amechangia Milioni 8.7 kwa ujenzi wa Kituo cha Polisi. Je, ni lini Serikali itakamilisha Kituo kile cha Polisi kwa kutuchangia fedha za ujenzi?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Jerry Silaa Mbunge wa Ukonga kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, nafahamu juhudi za Mheshimiwa Silaa na mara kadhaa amenishirikisha juhudi wanazozifanya ikiwemo kuchangia ujenzi wa vituo hivi, nimuahidi Mheshimiwa Mbunge kwamba, katika mpango wetu wa uboreshaji, ukamilishaji na uendelezaji wa Vituo vya Polisi eneo la Mzinga ni moja ya Kata itakayozingatiwa katika ukamilishaji huo. Nashukuru sana.

MHE. MUHARAMI S. MKENGE: Mheshimiwa Spika, nashukuru. Wananchi wa Kiharata katika Kata ya Mapinga wamepambana wamepata kiwanja kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Polisi. Je, Serikali ipo tayari kutusaidia ili tuweze kukamilisha Kituo hicho mapema?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Shabani Mbunge wa Bagamoyo kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, tunafahamu juhudi za Mbunge na wananchi wa Jimbo lake katika kutunza usalama raia na mali zao na uwepo wa Vituo vya Polisi ni moja ya mahitaji ya kukamilisha jambo hilo. Ninamuahidi Mheshimiwa Mbunge kwamba tutashirikiana nae mwenyewe, wadau wa Wilaya ya Bagamoyo pamoja na wananchi ili kujenga kwenye kiwanja hiki cha Mapinga ambacho wananchi wamejitolea kwa ajili ya ujenzi wa kituo hicho. Ni moja ya eneo tutakaloingia kwenye mipango yetu ya uendelezaji wa Vituo vya Polisi. Nashukuru.

MHE. USSI SALUM PONDEZA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Nami ningependa nimuulize swali moja dogo la nyongeza Mheshimiwa Waziri. Je, Jimbo langu la Chumbuni tumekuwa na matatizo sana ya hivi vituo na tumekuwa hatuna kituo zaidi ya mwaka wa nne, tumekuwa tukisema sana lakini tumekuwa tukiahidiwa na Wizara kuwa itakuja kushughulikia. Mheshimiwa Waziri upo tayari nasi tukijenge kile kituo kwa nguvu zetu?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Ussi Pondeza Mbunge, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, natambua juhudi za Mheshimiwa Mbunge, wamefanya mambo mengi katika Jimbo lake ikiwemo kuanza ujenzi wa vituo hivi, nilitembelea huko na nikaona. Ninamuahidi katika maeneo tutakayozingatia na kuyapa kipaumbele katika utekelezaji wa mpango wetu wa ukamilishaji na ujenzi wa vituo, Jimbo la Chumbuni litapewa kipaumbele. Nashukuru sana. (Makofi)
MHE. MOHAMED JUMAH SOUD: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri nina swali la nyongeza. Kwa kuwa Jimbo la Donge limepanuka sana na hivyo vigezo ambavyo amevizungumza Mheshimiwa Naibu Waziri vingi vyake vinakidhi kuanzishwa Kituo cha Polisi katika Jimbo la Donge na halikadhalika uharamia umeongezeka sana kiasi kwamba mazao sasa hivi kulima kumekuwa ni shida, mifugo kufuga imekuwa ni tabu. Swali hili niliwahi kuuliza hapa na Mheshimiwa Naibu Waziri aliniahidi kwamba atafanya tathmini ili kuangalia uwezekano wa utekelezaji. Sasa je, ananiahidi vipi ile tathmini imeshafanyika na kama haijafanyika basi lini itakamilika ili utekelezaji uanze. Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la moja la nyongeza la Mheshimiwa Soud, kama ifutavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba kama nilivyosema ameeleza hapa Jimbo la Donge linakidhi vigezo hivyo, kupitia Bunge lako Tukufu nimwelekeze Kamishna wa Polisi wa Zanzibar na Wasaidizi wake waweze kufanya tathmini ya eneo hilo. Wakibaini kwamba linakidhi vigezo, basi hatua za kujenga Kituo cha Polisi liweze kufanyika. Mheshimiwa Mbunge tutapeana ushirikiano ili kuona kwamba jambo hilo linafanyika. Ahsante sana.
MHE. RASHID ABDALLA RASHID: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Suala hili lilikuwa ni kama ukumbusho. Kipindi kilichopita niliuliza suala hili na jawabu likatoka kwamba wananchi wavute Subira, tutatumia Mfuko wa Tuzo na Tozo katika kipindi hiki ili tuweze kuikamilisha ofisi; lakini sasa majibu wa Mheshimiwa Naibu Waziri yanasema, sasa nitafute wadau; je, ni lipi jawabu sahihi la kushika? Nitafute wadau au Mfuko wa Tuzo na Tozo? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali langu la pili. Mheshimiwa Naibu Waziri yupo tayari kufuatana nami baada ya Bunge hili ili aende akaone nguvu za wananchi walizozitumia katika ujenzi huo ili naye aweze kuona kwamba tutumie wadau au wa tuzo na tozo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, nakiri swali la Mheshimiwa Mbunge kuhusu kutumia wadau au tuzo na tozo, kama nilivyojibu kwenye swali la msingi, ni kweli kwamba tuzo na tozo hutumika kukamilisha Vituo vya Polisi vya ngazi ya jamii kuunga mkono nguvu za wananchi au ngazi ya Wilaya, Tarafa na Mkoa kwa ajili Askari wa Jeshi la Polisi.

Mheshimiwa Spika, kuhusu hivi vituo vya ulinzi shirikishi ambapo ni juhudi zinazotokana na utashi wa wananchi wenyewe, tumekuwa tukishauri watumie nguvu za wananchi na wadau kuliko kazi ya msingi ya Jeshi la Polisi haijakamilika tuhamishie rasilimali kidogo tulizonazo kwenye jambo ambalo kimsingi lingeweza kufanywa na wananchi.

Mheshimiwa Spika, kuhusu kufuatana naye, nipo tayari. Kwa kweli maeneo yake nimeshafika mara kadhaa, nadhani ratiba itakavyoruhusu tutakwenda kuangalia tushirikiane naye kuhamasisha wananchi ili waweze kukamilisha kituo hicho, ahsante.
MHE. DKT. CHARLES S. KIMEI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naomba nimwulize Mheshimiwa Waziri: Ni lini atawezesha wananchi wa Mwika Kaskazini kwa kumalizia kituo chao ambacho alikitembelea na akaahidi kwamba tukimaliza kupaua, basi tutapata uwezeshaji? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, baada ya kauli ile kama unavyokumbuka tulikuwa wote Mheshimiwa Dkt. Kimei, tukasema IGP na imewekwa kwenye mpango wa ukamilishaji katika mwaka wa fedha unaoanza 2024/2025. Hiyo ni commitment, tutalitekeleza Mheshimiwa Mbunge. (Makofi)
MHE. FAKHARIA SHOMAR KHAMIS: Mheshimiwa Spika, ahsante. Sina budi kumshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri kwa jawabu lake zuri, litatoa matumaini kwa wazee wetu ambao kwa umri waliokuwanao sasa hivi hali yao kweli siyo nzuri tena.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa baadhi ya wazee hawa hawana familia, wanahitaji kuishi, lakini na bado wanaendelea kupita maofisini kuomba misaada: Je, kwa nini Serikali haiwezi kufanya mpango wa kuwatafutia mahala pa kuwaweka na kuwatunza wazee hawa ili kumaliza maisha yao?

Mheshimiwa Spika, swali la pili. Kwa kuwa wastaafu Serikalini hulipwa pension ya uzeeni hadi kufariki kwao, lakini kwa wazee hawa wanalipwa pension ya ulemavu: Kwa nini nao wasichanganywe katika kupewa pension ya uzeeni kama wanavyolipwa wastaafu wengine? (Makofi
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI K.n.y. WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA): Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, naomba kujibu maswali ya nyongeza ya Mheshimiwa Fakharia Shomar Khamis, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, moja, mapendekezo ya kuwatafutia mahali au kwa maneno mengine wajengewe makazi kwa sababu hawana familia; mfumo wa uendeshaji wa Serikali zetu za Mitaa na mambo ya Ustawi wa Jamii yanaruhusu pale ambapo mtu anakuwa hajiwezi kabisa, yapo makazi yaliyokuwa dedicated kwa ajili ya wazee hao. Pengine naomba wale ambao wameshindwa kabisa, wawasiliane na halmashauri zao ili kuona namna ya kuweza kuwasaidia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kisera tunapendelea zaidi wazee walelewe na vijana au ndugu zao kama utamaduni na maadili mema ya Watanzania yanavyofanyika.

Mheshimiwa Spika, kuhusu kuwachanganya hao ambao ni wapiganaji wa vita na wazee wengine wapate pension ya uzeeni, hili ni suala la kisera, litafikiriwa na Wizara husika ili tuweze kuona uwezekano wa kulitekeleza, nashukuru.
MHE. FATMA H. TOUFIQ: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa fursa nami niulize swali la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, je, Serikali inatoa tamko gani kwa wale maaskari wapiganaji waliopigana Vita vya Kagera ambao hawakuajiriwa na sasa wana maisha duni? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI K.n.y. WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Spika, kama nilivyojibu kwenye jibu la msingi, ni kwamba kwa mujibu wa takwimu tulizonazo, wazee wote ambao wanapata huduma ya pension na usaidizi wa kimatibabu ni 272. Kama wapo wazee ambao kwa bahati mbaya hawakuingia kwenye orodha hiyo, tumeelekeza waende karibu na vikosi vya Jeshi vilivyoko jirani na makazi waliyopo ili taarifa zao zihakikiwe na hatimaye waweze kupata huduma kama zile wanazopata wazee wenzao waliopigana vita hii, ahsante.
MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Kumekuwa na utaratibu sasa hivi, wazee wanatufuata kule vijijini au watoto wao wakiamini kwamba wanadai fidia kutokana na ushiriki wao kwenye Jeshi lile la Mkoloni (KAR) au Vita ya Kagera. Nataka kufahamu kutoka Serikalini, hivi ni kweli kuna watu wanaodai fidia kutokana na maeneo hayo mawili niliyoyataja kwa maana Jeshi la KAR pamoja na Jeshi la waliokwenda kupigana kwenye Vita ya Kagera?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI K.n.y. WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Spika, kwa sababu swali la msingi ni Vita ya Kagera, naomba suala la KAR liweze kuletwa kama swali la msingi ili tuweze kulifanyia utafiti na hatimaye tutoe majibu fasaha katika Bunge lako. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuhusu uwepo wa Wazee wa Vita ya Kagera ambao pengine wanalalamika kutopata fidia, ndiyo maana nimesema, tunazo takwimu kwamba wapo 272, kama wapo wazee wa namna hiyo Mheshimiwa Mbunge, nimeeleza hapa katika moja ya jibu la msingi kwa Mbunge aliyetangulia, waripoti kwenye Makambi ya Jeshi yaliyoko karibu na maeneo yao ili taarifa zao zihakikiwe, hatimaye waweze kapata haki wanayostahili, ahsante.
MHE. KASALALI E. MAGENI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. Hili suala la wazee waliopigana vita vyetu kuidai Serikali limekuwa ni suala la muda mrefu na limekuwa kila siku likitolewa majibu: Je, ni lini sasa Serikali inaliahidi Bunge hili kwamba suala la wazee hawa litatolewa majibu ya mwisho na kutatuliwa liishe kabisa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI K.n.y. WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, nikirejea majibu yangu ya swali la msingi, kwa mujibu wa takwimu zilizopo kwenye Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania ni kwamba wako wazee 272. Sasa kama wapo wazee wengine ambao kwa bahati mbaya wanaamini kwamba wana madai ya msingi, lakini hawamo kwenye orodha hii, tuko tayari kushirikiana na Mheshimiwa Mbunge ili wazee hawa wahahakikiwe taarifa zao, ikithibitika kwamba wanastahili Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, itawalipa hizo haki stahiki, ashante sana.
MHE. KWAGILWA R. NHAMANILO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi niulize maswali mawili ya nyongeza:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa, magari matano ni machache sana kwa mikoa yote na Wilaya zote zenye uhitaji, je, Mheshimiwa Naibu Waziri anatuhakikishiaje wananchi wa Handeni Mjini, kwamba magari haya matano yatakapowasili moja litapelekwa Handeni Mjini? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; mwaka wa fedha 2023/2024 umebakiza miezi minne tu kukamilika, je, Serikali ipo katika mchakato gani wa manunuzi kwa magari haya matano ya zimamoto? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu maswali ya nyongeza ya Mheshimiwa Reuben Kwagilwa, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeshasema kwenye jibu la msingi katika haya magari pamoja na uchache wake, Handeni mtazingatiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niwaeleze Waheshimiwa Wabunge kwa ujumla kwamba Serikali ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan imeridhia kupata mkopo wenye masharti nafuu wa zaidi ya Dola za Kimarekani milioni 100 zitakazowezesha kupata magari na vitendea kazi vingine kwa ajili ya kuliimarisha Jeshi la Zimamoto na Uokoaji. Mara vifaa hivyo vitakapopatikana, mikoa yote na Wilaya zote ambazo hazina vitendea kazi hivyo watapata.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa swali la pili kuhusu mchakato wa manunuzi umefikia wapi, nataka nikuhakikishie, mchakato wa manunuzi uko hatua nzuri. Mara hizo fedha zitakapopatikana kutoka Hazina malipo yatafanyika ili tuweze kupata vifaa hivyo kabla mwaka wa fedha haujamalizika, nashukuru.
MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi, nina swali kwa Mheshimiwa Naibu Waziri kwamba, Jimbo la Ndanda lenye kata 16 tunacho Kituo cha Polisi kimoja tu kilichopo Ndanda. Hata hivyo, majengo ya Kituo cha Polisi pamoja na nyumba ya Mkuu wa Kituo cha Polisi Ndanda, kwa maana ya OCS, ni mali ya Wamisionari wa Benediktini wa Ndanda. Kutokana na umuhimu na ukubwa wa Jimbo la Ndanda, kuna haja ya kuwa na Kituo cha Polisi kwenye Kata ya Chiwale. Nini msimamo wa Serikali wa kujenga Kituo cha Polisi kwenye Kata ya Chiwale?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ambavyo tunaongea kwa nyakati tofauti, ni dhamira ya Serikali ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kuhakikisha kwamba kata zote na tarafa za kimkakati zinajengewa vituo vya Polisi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nyakati tofauti nimeongea na Mheshimiwa Mbunge wa Ndanda na ninamshukuru sana kwa namna anavyofuatilia suala la usalama wa raia wa jimbo lake; na kwa vile kuna mfuko wa jimbo kidogo ambao anapata, wajitahidi tu kuanzisha ujenzi na Wizara ya Mambo ya Ndani kupitia Jeshi la Polisi lita-support ujenzi wa hicho kituo hadi kitakapomalizika, nashukuru.
MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Wilaya ya Tarime inajumuisha Halmashauri ya Mji wa Tarime, Mji wa Sirari, Nyamwaga na Nyamongo, miji ambayo inakua kwa kasi kubwa sana na kusababisha ujenzi wa makazi au hoteli za ghorofa, lakini tumekuwa hatuna gari la zimamoto, na mara kadhaa tunapopata majanga ya moto inasababisha maafa makubwa bila msaada wowote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kujua sasa, katika haya magari matano ambayo Waziri amesema hapa, ni lini Tarime itapata, maana mara kadhaa nimesimama nikiomba gari la zimamoto kwenda Tarime? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Esther Matiko, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeeleza kwenye jibu la msingi la nyongeza kwamba Serikali ina mpango wa kutumia zaidi ya shilingi bilioni 200 kununua magari na vitendea kazi vingine kuwezesha Jeshi la Zimamoto na Uokoaji. Kwa hiyo, fedha hizo zitakapopatikana, Wilaya ya Tarime ni moja ya Wilaya zitakazonufaika, na ninaamini zitapatikana kabla ya mwaka huu wa fedha haujakamilika, nashukuru.
MHE. MARIAM N. KISANGI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi niweze kuuliza maswali ya nyongeza. Kwa kuwa matatizo ya moto yamekuwa mengi sana katika nchi yetu na hasa katika maeneo ya shule na masoko, lakini kumekuwa na changamoto kubwa ya magari ya zimamoto kufika maeneo ya tukio bila ya kuwa na maji. Tatizo hili limekuwa ni kubwa kiasi kwamba watu wanakata tamaa na Jeshi lao la Zimamoto. Je, ni nini kauli ya Serikali kuhusiana na changamoto hiyo? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili. Kwa kuwa katika nchi yetu kumekuwa na miradi mingi ya kimkakati ya Serikali kama vile standard gauge, Bwawa la Mwalimu Nyerere pamoja na bomba lile la mafuta la Chongoleani Hoima, je, Serikali imejipanga vipi katika kuweka tahadhari ya moto katika maeneo hayo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu swali la mwanzo la kwamba magari yanafika yakiwa hayana maji, naomba leo nisaidie kuweka sawa hisia hizo kwa kusema yafuatayo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kawaida gari lenye uwezo wa kubeba lita 5,000 litakapofika kwenye eneo lenye athari ya moto, kwa pressure yake linaweza likazima moto kwa dakika mbili maji yale huwa yamekwisha. Sasa wananchi wana-tend kuamini kwamba halina maji linaenda kutafuta maji mengine. Ila ni kwa sababu dakika mbili tu lita 5,000 zinakuwa zimemalizika. Haiwezekani gari yetu iende kwenye tukio la kuzima moto halafu haina maji na kiuzoefu gari linapokuwa lime-park, always linakuwa na maji. Kwa hiyo, wananchi waondoe dhana hiyo potofu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, juu ya kuchelewa kufika ni changamoto ya miundombinu yetu, lakini na shughuli za kibinadamu zinazofanyika kwenye maeneo ambayo gari hilo linapita. Kama kila mwananchi ataelewa na akasaidia kufungua njia wakati wa dhararu kama hizo, tatizo kama hili litapungua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu Serikali kuzingatia miradi ya kimkakati ikiwemo Bwawa la Mwalimu Nyerere, SGR, bomba la Chongoleani, napenda nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge na Wabunge wote kwamba maeneo yenye uwekezaji wa kimkakati kama hizi kwa maana ya vital installation kuweka tahadhari ya kudhibiti matukio ya kuzima moto ni kipaumbele cha juu cha Serikali. Kwa hiyo, namhakikishia Bwawa la Mwalimu Nyerere na miradi mingine kama hiyo itazingatiwa katika kuwekewa magari na vifaa vya kuzima moto na uokoaji, ahsante. (Makofi)
MHE. DKT. OSCAR I. KIKOYO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana. Wilaya ya Muleba ni kati ya wilaya kubwa lakini haina gari la zimamoto. Ni lini Serikali itatupatia gari la zimamoto? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, katika majibu ya msingi nimeeleza mpango wa Serikali kutumia zaidi ya dola za Kimarekani milioni 100 kununua magari ya kuzima moto na vifaa vingine kwa ajili ya uokoaji, na tutakapokuwa tumepata mkopo huo na kununua magari hayo, Wilaya ya Muleba anapotoka Mheshimiwa Kikoyo itazingatiwa, ahsante sana. (Makofi)
MHE. BUPE N. MWAKANG’ATA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, ninashukuru kwa kunipa nafasi.

Ni lini Serikali itanunua gari la Zimamoto katika Mkoa wa Rukwa, kwa sababu Mkoa wa Rukwa hauna gari la Zimamoto hata moja? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, natambua kwamba Rukwa haina gari kwa maana ya gari zima linalofanya kazi. Gari lipo ni bovu linaendelea kutengenezwa hatua kwa hatua. Ninamhakikishia Mheshimiwa Bupe kwamba mara magari haya yatakaponunuliwa Mkoa wako utazingatiwa katika mgao, nashukuru sana. (Makofi)
MHE. EDWARD O. KISAU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru na ninaipongeza Serikali kwa majibu mazuri sana. Hata hivyo, kwa ajili ya kuweka record sawa ni Kituo cha Magungu, siyo Magugu, Magugu ni kwa Mheshimiwa Mwenyekiti pale. Vilevile, jina langu ni Kisau siyo Kisua, Kisua kwa Kichaga ni yule beberu mdogo. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, baada ya kusema hivyo, nina maswali mawili ya nyongeza. Ninawapongeza Wananchi wangu wa Kiteto ni waungwana sana, unajua wananchi kujenga Vituo vya Polisi siyo jambo dogo sana. Kwa kuwa Wananchi wa Kijungu nao wamejenga Kituo cha Polisi na imefikia lenta wametumia milioni 15 mpaka 20. Mheshimiwa Naibu Waziri, kwa nini, msiweke hiyo bajeti ya 2024/2025 ili kumalizia kama mlivyofanya kwa wenzao wa Magungu hapo? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa kuwa aliyekuwa IGP, 2014/2015 alitoa ahadi ya kujengwa Kituo cha Polisi Kijiji cha Chekanoa, na kwa kuwa Mji Mdogo wa Matui unahitaji kituo chenye hadhi ya polisi. Ni lini Mheshimiwa Naibu Waziri utatembelea Kiteto ili tukague vituo hivi vya polisi? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ninawapongeza wananchi wa Jimbo la Kiteto, kwa juhudi hizi wanazozifanya kwa ajili ya kuhakikisha uwepo wa usalama wa wananchi na mali zao kwa kujenga vituo hivi vya polisi. Ninamshukuru Mheshimiwa Mbunge, kwa wito wako na nipo tayari baada ya Bunge hili kuunga nawe kutembelea eneo lako la Kiteto. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu Kata hii ambayo pia wameanza, ni ahadi yetu kwamba wananchi walionesha juhudi za kuanza tutawaunga mkono kwa kutenga fedha za maendeleo na fedha nyingine kutoka Mfuko wa Tuzo na Tozo ili kukamilisha majengo hayo yaweze kufanya kazi iliyokusudiwa. Kuhusu ahadi ya IGP aliyepita nitamkumbusha IGP aliyepo madamu ilikuwa ni ahadi ya Jeshi la Polisi, ili aweze kusaidiana na wananchi hawa wa Chekanao kujenga kituo hicho kilichoahidiwa, nakushukuru. (Makofi)
MHE. DKT. PIUS S. CHAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipata nafasi hii. Kituo cha Polisi cha Sanza, ni chakavu sana ambacho kipo katika Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni. Nini mkakati wa Serikali wa kuwasaidia Wananchi wa Sanza kujenga kituo kipya cha Polisi? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu uchakavu wa Kituo hiki na Mheshimiwa ameomba tujenge Kituo Kipya. Naomba anikubalie tufanye tathmini ya kiwango cha uchakavu wa kituo kilichopo. Tutakapobaini gharama za kufanya ukarabati ni kubwa au zinakaribia kulingana na ujenzi wa kituo Kipya. Basi tutaunga mkono juhudi zako kwa kujenga kituo kipya, nashukuru sana. (Makofi)
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana, Wilaya ya Mbulu ni Wilaya kongwe Serikali ina mkakati gani wa kujenga vituo vya polisi katika Tarafa za Nambis na Tarafa ya Daudi, ili kuweza kupeleka huduma karibu na wananchi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni dhamira ya Serikali kila mara tunapokuwa na Vijiji au Miji Midogo inayokuwa kwa kasi hasa katika shughuli za kiuchumi na kuvutia vitendo vya uhalifu kuzingatia kwamba maeneo hayo tunayapa miundombinu ya kulinda usalama wa maisha ya watu na mali zao. Kwa hiyo, Tarafa alizo zitaja Mheshimiwa Mbunge tutazifanyia tathmini na wenzetu wa Mkoa wa Manyara kwa maana ya RPC, kuona kama pana mahitaji tuweze kuzitengea fedha kwenye bajeti zetu ili vituo hivyo viweze kujengwa, ninashukuru. (Makofi)
MHE. MOHAMED SAID ISSA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru. Kituo cha Polisi Konde kilitengewa bajeti katika mwaka 2022/2023, hakikukarabatiwa, kikatengewa bajeti 2023/2024 mpaka leo hakijakarabatiwa. Nini kauli ya Serikali kuhusiana na suala hili? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Mbunge, atafahamu kwamba Serikali ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, imefanya juhudi za kujenga na kukarabati vituo katika maeneo mbalimbali yakiwemo maeneo ya Pemba na Unguja. Ni bahati mbaya kwamba bajeti haikutoka ndio maana ukarabati haukuweza kufanyika. Ninaomba nimuahidi bajeti ya mwaka huu itakapotoka Kituo cha Konde kitapewa kipaumbele, ahsante sana. (Makofi)
MHE. STANSALAUS H. NYONGO: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa majibu mazuri ya Serikali. Gereza la Maswa kama majibu ya Serikali yanavyosema ni Gereza kongwe la siku nyingi na ukarabati inawezekana ukatumia gharama kubwa, na Magereza hii ipo katikati Maswa Mjini;

Je, Serikali ipo tayari tuwapatie kiwanja nje ya mji na lile gereza mkabadilisha ikiwezekana na magereza mengine, yale magereza ya mjini mkayafanya kuwa business complex mkapata vyanzo zaidi vya ndani?

Je, mna mpango gani na zile nyumba za wafanyakazi pale Maswa ambazo nazo nazo zina hali mbaya?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, nikiri, kama alivyosema Mheshimiwa Mbunge kwamba, Magereza ya mjini hasa ile ya Maswa ni kongwe na limechakaa sana. Nikubaliane na yeye tu baada ya Bunge hili ninatarajia kufanya ziara Mkoani Simiyu.

Pamoja na mambo mengine nitatembelea eneo la Maswa. Kama atakuwa na nafasi tukaenda wote tuone namna ambavyo tunaweza tukalifanyia ukarabati Gereza hili au kukubaliana mpango wake wa kupata eneo jingine la kujenga magereza.

Mheshimiwa Spika, kuhusu nyumba tunavyofanya ukarabati wa magereza ni pamoja na majengo yenyewe ya magereza, kwa maana ya mahabusu na vyumba wanavyokaa wafungwa, pamoja na nyumba za watumishi wakiwemo askari. Kwa hiyo, tutakapofanya ukarabati maeneo yote mawili yatazingatiwa, nashukuru.
MHE. CONCHESTA L. RWAMLAZA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Pamoja na majibu ya Waziri, jengo hili limeanza kujengwa tangu mwaka 2010 ni miaka 13 sasa.

Kwanza, niulize Serikali kwa nini imetelekeza jengo hili mpaka limekuwa gofu?

Mheshimiwa Spika, sasa kwa sababu Serikali imesema itatoa bilioni moja, mtupe commitment Serikali ili azma ya kujenga jengo hili iweze kutimia. Ni lini Serikali inakwenda kukamilisha jengo hili?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, ni lini Serikali itakamilisha jengo hili? Nimeeleza kwenye jibu la msingi kwamba ni pale tutakapopata fedha zilizotengwa kwenye bajeti ya mwaka huu kwa ajili ya ukamilishaji.

Mheshimiwa Spika, nikuhakikishie tu Mheshimiwa siyo dhamira ya Serikali kuacha majengo kuwa magofu, majengo mengine yalitegemea uwepo wa fedha pale ambapo tulikwama na umesema ni miaka 10 iliyopita, ndiyo maana majengo mengi sasa hivi tunayakamilisha. Ukienda maeneo mbalimbali Geita Jengo la Polisi la Mkoa linakaribia kukamilika, Mara linakaribia, Njombe limekaribia kukamilika. Kwa hiyo, tuna imani Wizara ya Fedha itakapotoa fedha hizi ili jengo la Kagera pia tutalikamilisha. ahsante sana. (Makofi)
MHE. SUMA I. FYANDOMO: Mheshimiwa Spika, ahsante. Eneo la Ikuti Wilayani Rungwe kijiografia lipo mbali sana na Makao Makuu ya Wilaya ya Rungwe.

Sasa je, ni lini Serikali itajenga Kituo cha Polisi maeneo ya Ikuti, ili kuwaepushia shida wanayoipata kwa sasa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, eneo la Ikuti ambalo ametuambia Mheshimiwa Mbunge lipo mbali sana na eneo Makao Makuu ya Wilaya ya Rungwe, anapendekeza tujenge jengo la Polisi pale na ndiyo dhamira ya Serikali. Kama utakuwa umefatilia hotuba ya Waziri wa Fedha mwaka huu, tumesema tunataka kujenga vituo vya Polisi karibu kila Kata. Tayari Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi imezungumza na TAMISEMI kuhusu mikakati ya kujenga vituo hivyo imeanza kufanyiwa kazi.

Mheshimiwa Spika, ni matarajio yetu kwamba, eneo hili la Ikuti - Rungwe ni moja ya maeneo yatakayonufaika na mpango huu, ahsante. (Makofi)
MHE. DOROTHY G. KILAVE: Mheshimiwa Spika, ahsante.

Je, ni lini sasa Serikali mtaendeleza kujenga nyumba za askari pale Kilwa Road Barracks? Kwa sababu majengo mengine yamejengwa lakini mengine bado hayajaendelezwa. Naomba kujua sasa. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, tunatambua uchakavu wa baadhi ya majengo ya Makazi Jeshi la Polisi pale Kilwa Barracks. Ni mpango wa Serikali kama ambavyo tumeanza kujenga zile flats ambazo Mheshimiwa Mbunge ameziona, dhamira ya Serikali ni kuendelea hatua kwa hatua kadri ya upatikanaji wa fedha.

Mheshimiwa Spika, umesikia ikielezwa hapa kwamba tumefanya Dar es Salaam lakini maeneo mengine bado yanalia. Katika hali ya kutaka ku-balance kadri tutakavyofikiwa basi Dar es Salaam tutaiendeleza kadhalika pia.
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Waziri katika Jimbo la Busokelo, Kituo cha Polisi wanachotumia ni lililokuwa Jengo la Posta; ni lini mtaweka kituo kizuri ambacho kitasaidia huduma ya wananchi katika Jimbo lile? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, tunafahamu changamoto ya maeneo mapya ya utawala ambayo yanaanzishwa kwa dhamira njema ya kusogeza huduma kwa wananchi, ikiwa ni pamoja na huduma za usalama, ndiyo maana wakati maeneo haya yakianza wenyeji kwa maana ya wenye maeneo Wilaya husika walibainisha, kama tukianzisha Makao Makuu Wilaya mpya huduma hii itafanyikia wapi? Kwa kutambua changamoto hiyo, ndiyo maana Wizara ya Mambo ya Ndani imeshabaini Wilaya zote ambazo hazina vituo vya ngazi ya Wilaya vya Polisi na tunaendelea kujenga kadri fedha zinavyopatikana.

Mheshimiwa Spika, ninakuahidi Mheshimiwa Mwakagenda kwamba, Busokelo litakuwa ni eneo pia litakalotiliwa maanani tunavyoendelea kutekeleza mpango wetu, ahsante sana.
MHE. SUBIRA K. MGALU: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi kuuliza swali la nyongeza.

Kwa kuwa, Serikali imejenga majengo mazuri sana ya Makao Makuu ya Polisi katika Mkoa wa Kusini Unguja, Tunguu na Mkoa wa Kaskazini Unguja na yamezinduliwa, tuliyashuhudia katika ziara ya Mheshimiwa Mwenyekiti wa UWT Taifa. Je, ni lini sasa majengo haya yatapatiwa samani ili yaanze kutumika kutokana na uwekezaji mkubwa mliofanya Serikali wa zaidi ya shilingi bilioni tatu? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa Mbunge kutambua juhudi ambazo zimefanywa na Serikali ya Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika kutengeneza mazingira ya kutolea huduma za kiusalama yakiwemo majengo ya Polisi ngazi ya Mkoa na Wilaya.

Mheshimiwa Spika, ni kweli ujenzi ni hatua, kukamilisha majengo ni jambo moja na uwekaji wa samani ni jambo la pili. Hatua itakayofuata ni kuruhusu majengo yaanze kutumika na Jeshi la Polisi limejipanga vema katika bajeti yake ya mwaka huu kuyapatia samani majengo hayo, yakiwemo hayo ya Tunguu na Kusini Unguja. Nashukuru.
MHE. MAIMUNA A. PATHAN: Mheshimiwa Spika, ahsante, swali langu la kwanza la nyongeza ni kwamba Kikosi cha 41 KJ Nachingwea pia kuna maeneo yalitwaliwa na Jeshi. Ni maeneo ambayo wazee wetu waliyatunza miaka mingi sana.
Je, Serikali haioni haja ya kuwalipa fidia wazee hao?

Swali la pili, kwa kuwa wazee waliyatunza maeneo yote hayo kwa muda mrefu na ilikuwa ni tegemeo kwa maisha yao. Je, Serikali haioni haja kweli ya kuwalipa hata kifuta jasho kidogo ili maisha yaendelee? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa swali la msingi nililolijibu inaonesha kwamba hakuna mgogoro, lakini kwa swali la nyongeza aliloliuliza Mheshimiwa Mbunge Pathan, naomba nilichukue ili kuelekeza Jeshi la Wananchi wa Tanzania, Kikosi cha 41 KJ, walifuatilie na kuleta taarifa stahiki ili hatua stahiki ziweze kuchukuliwa. Nashukuru. (Makofi)
MHE. NOAH L. S. MOLLEL: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi.

Mheshimiwa Spika, wananchi wa Kata ya Oldonyosambu wamechukuliwa maeneo yao na Jeshi miaka 20 sasa imepita na zaidi. Je, ni lini itawalipa fidia wananchi wale ambao wametoa eneo lao katika Kata ya Oldonyosambu?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, kwenye hili la Oldonyosambu pia ni suala jipya kwangu. Kama Naibu Waziri niliyeshikilia jambo hili, naomba nilichukue ili tuwasiliane na Waziri mwenye dhamana na chombo chenyewe cha jeshi, kuona uhalali. Kama ambavyo tumesema wakati wote, Serikali ya Awamu ya Sita ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, haiko tayari kuona wananchi wake wakidhulumiwa au kunyimwa haki wanayostahili.
Mheshimiwa Spika, ikithibitika kwamba wanastahili kulipwa fidia, basi hatua stahiki zitachukuliwa ili wananchi hawa waweze kulipwa inavyopasa, nashukuru.