Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Kabula Enock Shitobela (5 total)

MHE. KABULA E. SHITOBELO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi hii ili niweze kuuliza swali langu la nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, kulingana na hali ya hewa au tabia nchi kwa mwaka huu Kenya haikuzalisha vizuri zao la parachichi, hivyo, wafanyabiashara wengi walikuja Tanzania kwa ajili ya kununua zao hili. Je, Serikali ina mpango gani wa kuhamasisha wakulima kuongeza kilimo hiki? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Kabula, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, nitumie nafasi hii kuwahamasisha wakulima wa parachichi sio dhambi kumuuzia Mkenya kwa sababu ni export ambayo tunakwenda kuuza ingawa lengo letu ni kwenda kwenye final markets. Kwa hiyo, tunaendelea kuwahamasisha wauze.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini la pili tunachukua hatua gani kuongeza uzalishaji? Mheshimiwa Waziri Mkuu ametoa maagizo kwa Halmashauri zote ambazo mazao ya parachichi yanalimwa kutenga maeneo angalau ya ekari 10 kwa ajili ya kuzalisha miche na kuigawa kwa wakulima. Wizara ya Kilimo imeshaanza kazi hiyo kwa kushirikiana na Serikali za Mitaa, hii ni hatua ya kwanza.

Mheshimiwa Naibu Spika, hatua ya pili ni kuwatambua wakulima na kuwa register ili mazao yao wanayozalisha yaweze ku-meet international standard na hii project tunafanya pamoja na wenzetu wa FAO ili ku-identify pest. Hatua ya tatu tunafungua masoko. Sasa hivi tunamalizia kufungua soko la South Africa lakini tumeanza negotiation na wenzetu wa China ili tuweze kufungua soko la China na ita-pull yenyewe uzalishaji na wakulima watakwenda sokoni wakiwa na soko la uhakika.
MHE. KABULA E. SHITOBELA: Mheshimiwa Spika, ahsante ukizingatia sisi ndio mama zako au bibi zako lazima uturuhusu ahsante sana. Kutokana na shughuli za uchimbaji madini Mkoani Mwanza na Kanda ya Ziwa kwa ujumla, tatizo na ongezeko kubwa la kansa kwa Mkoa mzima wa Mwanza kumekuwa na tatizo kubwa la kansa na tunaamini kabisa hii zebaki ndio inayosababisha ongezeko hili la kansa. Je. Serikali ina mpango gani sasa wa kudhibiti kabisa uingiaji wa kemikali hizi, ili kunusuru wananchi wa Mwanza na Kanda ya Ziwa kwa ujumla? (Makofi)
WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri, naomba nimshukuru sana Mheshimiwa Kabula kwa swali lake ambapo ameulizia kuhusiana na udhibiti.

Mheshimiwa Spika, kama alivyoeleza Mheshimiwa Naibu Waziri, hatua ya kwanza tuliyochukua mahali ambako dhahabu inachenjuliwa, inaitwa mialo, mwanzo mialo ilikuwa holela, kila mahali mtu anajenga; sasa tumeamua kuidhibiti ile mialo yote iwekwe kwenye eneo maalum na jumla ya mialo 5,025 imesajiliwa kote nchini.

Mheshimiwa Spika, pili, Chama cha Wachimbaji Wadogo kinaitwa FEMATA pamoja na Mkemia Mkuu wa Serikali wanatengeneza umbrella moja ya namna ya kuagiza zebaki hapa nchini na Mkemia Mkuu wa Serikali ameshatoa hiyo go-ahead lakini changamoto tuliyonayo ni ndogo ndogo tu ya uratibu. Nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba ndani ya miezi hii miwili uagizaji wa zebaki tutakuwa tumeudhibiti na tutakuwa na source inayoeleka.

Mheshimiwa Spika, nakushukuru. (Makofi)
MHE. KABULA E. SHITOBELO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.

Je, ni lini Serikali itakamilisha kazi ya kupeleka umeme katika vijiji vya Mkoa wa Mwanza kama Nyanchenche -Segerema; Nyakafungwa - Buchosa; Gulumungu - Misungwi; Kawekamo, Mwambogwa, Kwimba na Ilemela?
NAIBU WAZIRI NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kama ambavyo nimeeleza katika majibu ya muda uliopita na Mheshimiwa Naibu Waziri ulivyosema Mkoa wa Mwanza umebakiza vijiji 121; lakini yako maeneo ambayo ameyataja Mheshimiwa Mbunge maeneo la Ilemela, Nyamagana, Nyamadoke, Nyamongolo pamoja na maeneo yote ya Rwanima tutawapekelea umeme mwezi disemba mwaka unaokuja.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini nimpe tu taarifa Mheshimiwa Mbunge kwamba Mwanza tumepeleka wakandarasi wa aina mbili; wakandarasi wa peri-urbun wanaendelea na maeneo uliyotaja, lakini kuna maeneo ya vitongoji ambayo yana-cover Sengerema mpaka Buchosa ambao wakandarasi wameshafika site tayari. (Makofi)
MHE. KABULA E. SHITOBELO: Mheshimiwa Spika, ahsante. Barabara inayounganisha Hungumalwa - Ngudu Wilaya ya Magu, imekuwa ikiwekwa kwenye Ilani ya Uchaguzi 2005, 2010, 2015 mpaka 2020 kwamba itajengwa kwa kiwango cha lami, sasa ni lini barabara hiyo itajengwa kwa kiwango cha lami? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, ahsante.

Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Kabula, Mbunge wa Viti Maalum Mwanza kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, barabara aliyoitaja ya Hungumalwa kwenda Ngudu ipo kwenye mpango na ipo kwenye bajeti kwa ajili ya kuanza kuijenga kwa kiwango cha lami. Kwa hiyo, nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba barabara hiyo itajengwa kwa kiwango cha lami kama ambavyo Serikali imeahidi kuifanya. Ahsante. (Makofi)
MHE. KABULA E. SHITOBELO: Mheshimiwa Spika, ahsante na mimi napenda niulize swali la nyongeza.

Je, Serikali ina mkakati gani wa kukarabati miundombinu ya maji katika Jimbo la Kwimba, Misungwi, Ilemela, Sengerema na Nyamagana?
WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Mbunge. Serikali imeendelea kujitahidi na inaendelea kuwekeza kuhakikisha kwamba tunakarabati na kujenga miundombinu mipya kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya maji safi na salama. Mathalani kwa eneo la Misungwi tumeshakwenda na Mheshimiwa Rais na tumekwishazindua mradi mkubwa wa zaidi ya Bilioni 12 katika kuhakikisha wananchi wale wanapata huduma ya maji safi na salama, ahsante sana. (Makofi)