Hotuba ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyoitoa wakati wa Ufunguzi wa Bunge la Kumi na Mbili, Tarehe 13 Novemba, 2020
MHE. KABULA E. SHITOBELO: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi hii. Awali ya yote napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa afya njema na amani tele hasa kwa kunipa kibali cha kuwa katika Bunge hili lako tukufu la Kumi na Mbili. (Makofi)
Napenda kukishukuru Chama changu cha Mapinduzi hasa Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi, Rais Dkt. John Pombe Magufuli na viongozi wote wa chama bila kusahau viongozi wangu wote wa chama wa UWT Mkoa na Taifa, bila kuwasahau wapiga kura wangu wote wakinamama wa mkoa wa Mwanza, ahsanteni sana kwa kuniamini nije kuwawakilisha katika Bunge hili tukufu la Kumi na Mbili. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lakini pia napenda kuishukuru familia yangu kwa kuwa wamenipa faraja sana kipindi cha kutafuta kura na siku zote za maisha yangu na mpaka leo niko hapa ni kwa sababu ya faraja zao, ninawashukuru sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nipo hapa kwa dhati kabisa kuunga mkono hotuba ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano, nimesoma hotuba hizi zote mbili ya mwaka 2015 na 2020.
Mheshimiwa Spika, naomba nijikite zaidi kwenye suala la afya. Katika ukurasa wa 32 miaka mitano iliyopita (Awamu ya Tano) ya Serikali hii imefanya mengi katika afya kama kujenga vituo vya afya na kutoa huduma ya afya kwa vituo 1887, zahanati 1198, vituo vya afya 487 na Hospitali za Wilaya 99 pamoja na Hospitali za Mkoa 10 na Hospitali za Rufaa Kanda tatu. Pia imeweza kupunguza vifo vya akinamama wajawazito, miaka mitano iliyopita ilikuwa kila mwaka wakinamama 11,000 wanafariki kwa mwaka mmoja. Lakini kutoka mwaka 2015 mpaka 2020 limeweza kupungua kabisa tatizo hilo na kurudi kuwa wanawake wajawazito wanaofariki dunia ni watu 3,000 tu kutoka kwenye 11,000. Kwa hiyo napenda kuipongeza sana Serikali na Wizara ya Afya kwa ujumla kwa kujitahidi kwa jitihada zao hizo nzuri ya kumuokoa mama mjamzito. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, napenda kuiomba Serikali sasa iweke kipaumbele zaidi kumaliza kabisa tatizo hili kama ambavyo imeweza kupunguza tatizo kutoka wanawake 11,000 kwa mwaka kufikia wanawake 3,000 ninajua kwa jinsi spidi tuliyonayo Serikali hii ikisimamia vizuri na Waziri wa Afya, Mheshimiwa Dorothy Gwajima namuamini mama huyu ni shupavu, akisimama kama yeye pia ni mwanamke ambaye ameshaingia labor anaujua uchungu wa mama mjamzito jinsi gani anapata matatizo. Kwa hiyo, ninaomba Serikali iliangalie kwa umakini kabisa jambo hili ili kumaliza kabisa vifo vya mwanamke na mtoto. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, niko mbele yako pia kuomba suala la pili katika hospitali zetu za wilaya za Mwanza Wilaya zote hasa Wilaya ya Ukerewe jiografia yake ya kufikika au ya kutoka kuja Mwanza kwenye Hospitali ya Rufaa ni ngumu. Mfano Hospitali ya Wilaya ya Ukerewe hakuna chumba maalum au wodi maalum kwajili ya mtoto njiti. Sasa pale complication yoyote au mtoto akizaliwa kabla ya muda, kwa hiyo kumuokoa yule mtoto inakuwa taabu sana. Ombi langu kwa Serikali nilitaka niombe ikiwezekana kujengwe japo wodi ambayo ya kulingana na Wilaya ile kwa ajili ya kuokoa mtoto njiti. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ahsante na naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)
Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022
MHE. KABULA E. SHITOBELA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa nafasi hii ya kuchangia katika Mpango huu wa Maendeleo ya Taifa. Pia napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa rehema zake kwa kunijaalia afya njema hata nimesimama katika Bunge hili na kuchangia hoja hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesoma Mapendekezo ya Mpango ni mazuri sana na yana faida kubwa kwa Watanzania wote. Nami nitajikita zaidi katika hoja ya kukuza na kuchangia uchumi wetu kupitia zao la parachichi. Nina- declare interest nami ni mdau katika biashara ya parachichi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, biashara ya parachichi ni kubwa sana na ni zao ambalo linaweza kutuletea kipato kikubwa hasa kutuletea pesa nyingi za kigeni kama tukilizingatia na kama Serikali hii itaweza kuliona ni zao bora kabisa la biashara kama mazao mengine kama korosho, pamba au kahawa. Zao hili likisimamiwa vizuri linaweza kutukuzia uchumi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, zao hili limekuwa likilimwa na wakulima wadogo wadogo lakini kama likiwekewa mkakati, likatangazwa na wananchi wote wakahimizwa hasa wa Mikoa ya Njombe, Kilolo (Iringa) na Mbeya (Tukuyu) ambapo zao hili linapatikana kwa wingi na ni zao bora kabisa tutaweza kukuza uchumi wa Taifa. Zao hili mpaka sasa limeajiri wanawake wengi sana katika viwanda vya ku- process wakati matunda haya yakipelekwa nje ya nchi. Wanawake wengi ndiyo wanatumika ku-process zao lile mpaka kusafirishwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda nijikite kuzungumzia changamoto ya zao hili. Kama mimi nikiwa mdau nimeweza kuona changamoto mbalimbali hasa kwenye kusafirisha tunda hili. Matatizo yenyewe ni jinsi ya kusafirisha mazao haya kutoka Njombe kwenda nchi kama Europe kwa sababu zao hili linauzika zaidi Europe pia Middle East hapa Dubai na Arabuni yote kwa ujumla.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo lililopo kwa sasa ni usafiri hasa kwenye kontena aina ya CL. Kwa Tanzania katika bandari yetu ya Dar es Salaam hakuna kontena kama hizo, inabidi mfanyabiashara wa zao hili aweke booking Nairobi, kontena litoke Mombasa lije mpaka Njombe, likifika Njombe ndiyo upakie ule mzigo urudi tena Mombasa ndiyo uweze kuondoka. Sasa tatizo linakuja wapi? Pale inapotokea tatizo lolote au delay yoyote njiani na mkulima au mfanyabiashara anakuwa ameshachukua matunda yako pale kwenye park house, sasa inapochelewa labda siku moja au siku mbili yale matunda yakija kusafirishwa kufika sehemu husika tayari yanakuwa ni reject. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Serikali yangu Tukufu iangalie jinsi gani itatusaidia au itawasaidia wakulima na wafanyabiashara wa zao hili kuhakikisha kuna zile kontena za CL au facility za usafiri madhubuti pale Dar es Salaam ili at least mkulima tunda linaposafirishwa kufika kule Ulaya liwe katika hadhi na ubora wa Kimataifa. Ombi langu sasa kwa Serikali ni kuangalia hivyo vitu muhimu hasa upande wa makontena.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia ningeomba zao hili lihamasishwe sehemu mbalimbali, najua hata Bukoba au Ngara linakubali kabisa…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa, kengele imeshagonga. (Makofi)