Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Dr. Alice Karungi Kaijage (18 total)

MHE. DKT. ALICE K. KAIJAGE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri ninayo maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sasa ili muundo fulani wa utumishi wa kada fulani uhuishwe lazima kwanza kada husika maombi yapelekwe Serikalini ndipo ifanyiwe kazi, kwa hiyo kama ikikwama kwenye meza fulani ya kamishna ina maana huo uhuishwaji unakwama. Kwa kuzingatia hivyo, je, Serikali haioni vema sasa kuwa na utaratibu wa kuwa na kipindi maalum cha kufanya uhakiki wa kada zote za Utumishi wa Umma na pia kufanya uhakiki wa Utumishi wa Umma pamoja na takwimu za Utumishi, hii yote kuleta usawa katika Utumishi wa Umma na pia kuboresha na kupandisha morale ya kazi ya watumishi? Mfano mzuri ni kada ya uhuishaji wa muundo wa kada ya maafisa kazi hawa Labour Officers.

Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa kuwa stahiki, stahili kwa watumishi pamoja na mafao yao hukokotolewa kuzingatia kiwango cha mshahara anacholipwa mtumishi. Kwa kuona umuhimu huu, je, Serikali sasa italipa kipaumbele suala zima la kuhakiki kada za kiutumishi kwa wakati? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyojibu kweye swali la msingi kwamba Serikali itaendelea kuhuisha miundo ya maendeleo ya utumishi kwa kadri ambavyo inaletwa kwenye Wizara yetu. Nitoe kumbukumbu tu kwa Mheshimiwa Mbunge aweze kufahamu kwamba kuanzia mwaka 2011 Serikali imekuwa ikihuisha miundo ya maendeleo ya utumishi hasa kwa kada hii ya ualimu, ambapo ilifanya nyongeza ya madaraja kutokana na nafasi zao za walimu.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia mwaka 2014 Wizara iliendelea kufanya namna hiyo na mwaka 2015 Wizara ya Fedha pia Wizara yetu iliendelea kuhuisha miundo hasa kwenye kada mbalimbali ikizingatiwa baadhi ya watendaji kwenye kada hizo maafisa mipango, manunuzi, maaafisa ugavi, wahasibu na wakaguzi. Nitoe rai tu kwa Mheshimiwa Mbunge afahamu kwamba Wizara yetu itaendelea kuhuisha miundo mbalimbali ya maendeleo ya utumishi kwa kadri itakavyoona inafaa. Kwa hiyo nimtoe hofu Mheshimiwa Mbunge kwamba asiwe na hofu.

Mheshimiwa Naibu Spika, na kwa swali la pili, kuhusu stahiki za mafao za watumishi kama ambavyo nimeulizwa. Katika utumishi wa umma stahiki na stahili za utumishi zimeanisha katika miongozo na nyaraka mbalimbali zinazotolewa kuhuishwa mara kwa mara na Serikali. Nyaraka hizo huainisha makundi mbalimbali ya utumishi na stahiki wanazotakiwa kupata.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyojibu kwenye swali langu la msingi, kwa mujibu wa kanuni ile ile Kanuni D. 6(2) za Kanuni za Kudumu za Utumishi wa Umma, Kanuni hii iliwahi kutolewa mwaka 2009; watumishi wa Umma kuajiriwa na kupandishwa vyeo na kubadilishwa kada (Recategorization) kwa kuzingatia sifa walizonazo na zinazooneshwa katika Miundo ya Maendeleo ya Utumishi katika kada mbalimbali zilizoainishwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, Miundo ya Maendeleo ya Utumishi wa kada mbalimbali katika Utumishi wa Umma imeainisha ngazi za mishahara, kuanzia cheo cha kuingilia katika Utumishi wa Umma (entry point) hadi cheo cha mwisho kwa kila kada kulingana na kiwango cha elimu na kwa kuzingatia uzito wa majukumu ya kada husika.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninapenda kuliarifu Bunge lako hili Tukufu kuwa Serikali itaendelea kuhuisha stahiki na stahili mbalimbali za watumishi wa umma pamoja na viwango vya mishahara ya kada mbalimbali kwa kuzingatia sera za kibajeti na uzito wa majukumu ya kada husika ili viweze kutumika kukokotoa mafao mbalimbali ya umma. (Makofi)
MHE. DKT. ALICE K. KAIJAGE: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, naomba kwanza nisahihishe majibu ya Mheshimiwa Waziri. Jina langu siitwi Alice Kapungi, naitwa Alice Karungi. Baada ya hapo nina maswali mawili ya nyongeza.

Swali la kwanza, kutokana na umuhimu wa Sera hii ya Taifa ya Tija: Je, ni lini sera hii itakuwa tayari ili iweze kutumika tena kukuza tija? (Makofi)

Swali la pili, kutokana na marekebisho ya sera, sheria na kanuni ndogo ndogo za uwekezaji kwa nia ya kukuza uwekezaji: Je, Serikali haioni umuhimu sasa wa kukishika kikamilifu kitengo hiki katika marekebisho haya ya sheria ili mwisho wa siku sheria hizi ziwe zenye kuleta tija? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA NA VIJANA (MHE. PASCHAL P. KATAMBI): Mheshimiwa Spika, kwanza namshukuru na kumpongeza Mheshimiwa Dkt. Alice Karungi Kaijage, kwa kipindi chote amekuwa akitupa ushirikiano mzuri sana katika kuhakikisha tunafanya maboresho kwenye maeneo mbalimbali hasa kwenye maeneo ya kazi, vijana na pia kwenye masuala mtambuka kama ya UKIMWI.

Mheshimiwa Spika, swali lake la nyongeza, napenda kujibu kuhusu lini sera hii itakuwa tayari? Kwa hatua ya sasa tayari tumeshaanza kuchukua maoni kwa wadau. Bahati nzuri sana Mheshimiwa Mbunge kwa sababu ameliuliza swali hili, kuna uwezekano mkubwa kwamba ana ufahamu na uelewa mpana juu ya jambo hili. Namwomba pia awe sehemu ya hao wadau ambao tutawafikia kwa ajili ya kukusanya maoni hayo tukiwa tunaenda kukamilisha sera.

Mheshimiwa Spika, baada ya bajeti hii nina imani kwamba kwa mwaka huu 2021 tunaweza kwenda kukamilisha sasa uwepo wa sera na pia kuangalia mabadiliko ambayo tutayafanya katika sheria. Hili litatusaidia sana kwa sababu tumeliona kama Ofisi ya Waziri Mkuu litatusaidia kukuza tija na ubunifu katika maeneo mbalimbali. Kwa mfano, kwenye maeneo ya Agro-industry, automobile industry, airspace industry, mechanical industry, petro-mechanical industry na kwenye maeneo mbalimbali ambayo ni mtambuka.

Mheshimiwa Spika, viwanda vyetu na maeneo mengine hata ya kazi yamekuwa yakitengeneza bidhaa ambazo mwisho wa siku kunakuwa na uzalishaji mkubwa, lakini ubora unakuwa chini. Kwa hiyo, hili ni eneo muhimu sana ambalo Serikali tumeona tuliangazie pia.

Mheshimiwa Spika, swali la pili la Mheshimiwa Dkt. Alice kuhusu kukamilisha utaratibu wote wa mchakato wa kisheria kuweza kuhakikisha suala hili nalo linakuwa na nguvu ya kisheria ukiacha hivi hivi; hilo litaenda sambamba pamoja na hatua ya sasa ya kukusanya maoni ambayo tumekwisha kuianza na tuna imani kubwa kwamba kufikia mwaka huu tutakuwa tumekamilisha zoezi hilo na kuweza kurasimisha ili kuleta mapendekezo ya mabadiliko ya sheria, sambamba na kuwa na sheria ambayo inaweza ikasimama hapo.

Mheshimiwa Spika, nashukuru.
MHE. DKT. ALICE K. KAIJAGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Namshukuru sana Waziri kwa majibu mazuri, lakini nina swali moja la nyongeza. Kutokana na uhitaji mkubwa na ukuaji wa tatizo hili la stroke, kwa maana ya kupooza na uhitaji wa mazoezi tiba na utengamao: -

Je, Serikali sasa ina mpango gani kuhakikisha kwamba inaboresha vitita vya Bima ya Afya ya Taifa na Bima ya Afya ya Jamii iliyoboreshwa ili tiba hii iwe jumuishi katika bima hizi kwa ajili ya ustawi wa wananchi wetu? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba, kumekuwa na ongezeko kubwa sana la magonjwa yasiyoambukiza ambalo linasababisha uhitaji mkubwa sana wa tiba mazoezi pamoja na huduma za utengemao. Serikali inaendelea kuboresha mpango mkakati ambao utakuja na mbinu; kwanza za kuhakikisha tunaweka mipango madhubuti ya kuzuia magonjwa yasiyoambukiza; pili, kuwa na vifaa tiba vya kutosha na wataalam katika maeneo ya magonjwa yasiyoambukiza na pia utengamao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile tutakwenda kuona wazo zuri la Mheshimiwa Mbunge tuone namna gani tunakwenda kuboresha eneo la bima ya afya, lakini na CHF na huduma nyingine kuweza ku-cover huduma hizi za mazoezi tiba na utengamao. Kwa hiyo, tumelichukua wazo hilo, ni zuri sana na kwa kipindi hiki ni wakati muafaka, tutakwenda kuoifanyia kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. (Makofi)
MHE. DKT. ALICE K. KAIJAGE: Mheshimiwa Spika, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali, nina maswali mawili ya nyongeza.

Swali la kwanza; nafahamu kwamba utaratibu wa kuomba fedha kwa awamu ya kwanza ya ukarabati umeshakamilika. Swali langu langu kwa Serikali: Je, ni lini fedha hizo zitatolewa ili ukarabati uanze?

Swali la pili: Je, Serikali ina mpango gani wa ziada kuhakikisha kwamba ukarabati wa majengo haya chakavu ya Milembe unakamilika katika awamu hii na awamu ijayo ya mwaka wa fedha?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA WAZEE NA WATOTO (MHE. DKT. GODWIN O MOLLEL): Mheshimiwa Spika, kama ambavyo amesema Mheshimiwa Mbunge, ni kweli kwamba kuna utaratibu ambao tayari umefanyika, lakini wakati utaratibu huo umefanyika imeonekana kwamba kwa kweli unahitajika ukarabati mkubwa sana na vile vile baadhi ya majengo kubomolewa na kujengwa upya, kwa hiyo, ikahitajika kufanyika tathmini kwa sababu fedha nyingi zitahitajika zaidi.

Mheshimiwa Spika, mara tu baada ya huu upembuzi kufanyika, kwanza kazi ambayo ilikuwa inaendelea itaendelea kufanyika, lakini tunahitaji ifanyike kazi kubwa zaidi kwa maana ya kuingia kwenye bajeti ya mwaka kesho 2022 ili ujenzi mkubwa ufanyike na ukitambua kwamba pale Mirembe inaenda kuwa taasisi kamili, sasa iko kwenye wakati wa kuunda muundo. Maa yake kutakuwa na ongezeko la kibajeti na wataweza sasa kuandika proposal zao binafsi ili kufanya research na pengine ile taasisi kuwa kubwa zaidi kuliko ilivyo sasa. Ahsante.
MHE. DKT. ALICE K. KAIJAGE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana na pia nashukuru kwa majibu sana ya Serikali. Naendelea kuipongeza Serikali kwa juhudi inazofanya kuhakikisha kwamba upatikanaji wa dawa unakuwa ni mzuri. Pia naishukuru Serikali, inajitahidi kuhakikisha kwamba wazee wanapata vitambulisho vya kupata dawa bure na pia wanaendelea kupata vitambulisho vingine. Hata hivyo nina swali la nyongeza kwa Serikali.

Je, Serikali ina mpango gani kuhakikisha kwamba wazee wanaendelea kupata stahiki za dawa kwa mwendelezo mzuri bila usumbufu?
NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Spika, kwanza nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Mbunge kwa jinsi anavyofuatilia matatizo ya akina mama wa Mkoa wa Pwani kwa ukaribu sana hasa kwenye mahospitali yetu; vile vile kwa jinsi ambavyo anafuatilia watoto wa kike kule mashuleni, niliona procedure yake nzuri sana inayofuatilia kwa karibu sana watoto wakike wa Mkoa wa Pwani.

Mheshimiwa Spika, kwanza niseme kama tulivyosema, mmeona Rais wetu Mheshimiwa Mama Samia Suluhu Hassan ametoa shilingi bilioni 338.8, shilingi bilioni 495 na umeona shilingi bilioni 18. Kwa kipindi cha miezi tisa tu zimekwenda zaidi ya shilingi bilioni 846. Maana yake ni nini? Shida siyo fedha, ni kujipanga.

Mheshimiwa Spika, kikubwa Waziri wa Afya Mheshimiwa Ummy Mwalimu pamoja na Waziri wa TAMISEMI, Mheshimiwa Bashungwa wameshatoa maelekezo kwa ma- RMO wote na ma-DMO wote kuhakikisha kila hospitali na kila kituo cha afya na zahanati, wana dirisha la wazee kwenye hospitali zao na kunakuwepo na daktari na mtu maalum wa kuwahudumia wazee. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, vilevile kuhakikisha kwamba kunakuwepo na dawa eneo husika na wazee wapate vitambulisho vyao kwa sababu kuna utaratibu wa wazee kupata vitambulisho vyao. Pia tumeshawaelekeza MSD, vituo vyetu vikiomba dawa wapeleke ndani ya siku tatu dawa ziwe zimefika kituoni na kama hawana item hizo, ndani ya masaa 24 wawe wamewaruhusu vituo vinunue dawa kwa sababu imeonekana vituo vinakuwa na fedha za basket fund, na own source lakini wanashindwa kununua dawa kwa sababu hawajapewa ruhusa ya kufanya hivyo kama taratibu zinavyotaka na MSD. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. DKT. ALICE K. KAIJAGE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Mheshimiwa Naibu Spika. Kwa kuwa changamoto iliyopo kwenye barabara ya Lushoto mpaka Mlalo inafanana na changamoto iliyo kwenye barabara ya kutoka Makofia – Mlandizi mpaka Vikumburu.

Je, ni lini Serikali itaanza kujenga kipande hiki cha kutoka Makofia – Bagamoyo mpaka Mlandizi kwa kiwango cha lami kama ilivyoahidi?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Alice Kaijage, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba barabara hii iko kwenye ilani na imetengewa bajeti kuanza ujenzi kwa kiwango cha lami mwaka huu. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba ujenzi utaanza mara tu fedha itakapokuwa imepatikana. (Makofi)
MHE. DKT. ALICE K. KAIJAGE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi. Nami naipongeza Serikali kwa kuja na mradi mzuri huu wa kuinua wavuvi na kwa kuwa Wilaya za Mkuranga na Kibiti ni wilaya ambazo zinajihusisha na uvuvi sana na kundi kubwa la wanawake wanafanya shughuli hii. Je, ni lini mradi huu wa kuinua wavuvi utawafiki wananchi wa wilaya hizi mbili? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mbunge wa Viti Maalum, Mheshimiwa Dkt. Alice Kaijage, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Wilaya ya Mkuranga na Kibiti ni miongoni mwa wilaya zitakazofaidika na program hii, lakini vilevile zitafaidika na program kubwa inayokwenda kwa jina la Tanzania Scaling up Blue Economy ambapo tutajenga maghala ya kuhifadhia samaki, masoko vikiwemo na hivi vichanja. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Dkt. Alice na Wabunge wengine wa Mkoa wa Pwani, Tanga, Lindi na Mtwara pamoja na wengine wote kwamba tumejipanga vema na hili tunakwenda kutekeleza.
MHE. DKT. ALICE K. KAIJAGE: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kupata nafasi ya kuuliza swali moja la nyongeza. Kwa vile bado tuna upungufu mkubwa wa wataalam wa mazoezitiba na utengamao: -

Je, hawaoni sababu ya kuanzisha course hii kwenye vyuo kama UDOM ambapo inachukua watu wengi ili angalau tupate wahitimu wa taaluma hiyo kwa wingi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Spika, kwanza nianze kwa kumshukuru Mheshimiwa Mbunge, Dkt. Kaijage kwa namna anavyoshirikiana na Wizara ya Afya kwa karibu hasa kwenye kushughulikia huduma ya mama na mtoto kwenye Mkoa wa Pwani. Vilevile nimwambie tu kwamba, siyo tu Chuo Kikuu cha UDOM, kuna mkakati wa vyuo zaidi ya vitano sasa tunaongeanao na kushirikiana na Wizara ya Elimu ili kuanzisha kada hizi ili kusaidia kupunguza upungufu wa wataalam kwenye soko la ajira. Ahsante sana.
MHE. DKT. ALICE K. KAIJAGE: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa majibu mazuri ya Serikali.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa katika formula ya kikokotoo kilichopita watumishi wengi walikwishakopa na wanaostafu sasa hivi walikwishakopa sana.

Je, Serikali ilishaliona hili jambo kwamba hatma yao ni nini, kwa sababu kikokotoo cha sasa kimekuja na formula nyingine ambayo wanatoka kana kwamba mafao yao ni zaidi ya nusu hawajapata?

Je, Serikali ilishafikiria jambo hili na nini hatima ya Watumishi hawa ambao mafao yao yalishaiva na walishakopa kupitia formula iliyopita?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU (MHE. PASCAL P. KATAMBI): Mheshimiwa Spika, ahsante, kabla ya kufanya uamuzi huo, mchakato huu ulishirikisha wadau wote na kuliandaliwa actuarial report. Katika kufanya hivyo tulibaini mambo kama hayo ambayo Mheshimiwa Mbunge amesema na nimpongeze sana kwa kuendelea kuwa mfuatiliaji mzuri.

Mheshimiwa Spika, kwa upande wa Serikali wakati wa kufanya hivyo, kikokotoo kipya kimesaidia kuja kuongeza lile pato la kila mwezi. Ni tofauti hata na kikokotoo kile cha awali ambacho hakikuweza kuleta tija zaidi.

Kwa hiyo, mengine kwa sababu ndio tumekwisha anza na sheria zetu zimekwisha anza, hakuna ule msingi wa retrospectivity kwa maana ya sheria kuanza kufanya kazi kwenda mbele na sio kurudi nyuma. Tutazidi kuyazingatia yote hayo na changamoto ndogo ndogo zinazojitokeza ili kuweza kuhakikisha jambo hili linaleta maslahi makubwa kwa wafanyakazi na tija, kwa sababu Serikali inaheshimu sana nguvu kazi ya Taifa ambayo ndiyo inaweza kuleta maendeleo endelevu kwa ajili ya taifa letu, ahsante sana.
MHE. DKT. ALICE K. KAIJAGE: Mheshimiwa Spika, ahsante. Na mimi naomba kuuliza katika Mkoa wetu wa Pwani katika Wilaya ya Kibiti tuna hospitali ya Mbochi na Mwambao ambayo imekamilika. Ni lini Serikali mtaleta vifaa tiba? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Dkt. Alice Kaijage Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba kwenye vifaa ambavyo vitakwenda kununuliwa kwenye mwaka wa fedha ujao tutatoa kipaumbele katika hospitali hii ambayo inahitaji vifaa tiba. Ahsante.
MHE. DKT. ALICE K. KAIJAGE: Mheshimiwa Mwenyekiti ahsante. Namshukuru Waziri kwa majibu mazuri, lakini nina maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; kwa sababu swali langu ni swali la kiutumishi, je, Serikali inafahamu tofauti ya kati ya Vyama vya Wafanyakazi ambavyo vinatetea maslahi ya Utumishi na Vyama vya Kitaaluma kwenye kada husika? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; linakuja suala zima la uhuishwaji wa maslahi ya kiutumishi je, Serikali haioni kwamba kuna umuhimu wa kuwa unashirikisha Vyama vya Wafanyakazi ambavyo vimesajiliwa kisheria kutimiza maslahi ya wafanyakazi ili kuepusha sintofahamu ambayo imetokea kwa uhuishwaji wa mwaka jana 2022 kutangazwa kwamba Daktari Bingwa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Mbunge Alice siyo tu kwa kufuatilia masuala ya Watumishi na Madaktari Bingwa, lakini kwa kazi kubwa ambayo anaifanya kusaidia wenzetu wa Mkoa wa Pwani haswa kwenye maeneo ya afya na masuala ya akinamama. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, amesema katika swali lake la kwanza, je, tunafahamu tofauti ya vyama na vile vya kitaaluma. Ndiyo tunafahamu kuna Vyama vya Wafanyakazi lakini kuna vya Kitaluuma kama ambayo mimi na yeye tupo cha Madaktari cha Tanganyika tunafahamu tofauti ya hivyo viwili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile swali lake la pili kwamba je, wakati wa kuamua haya tunawashirikisha. Ndiyo maana imechelewa ni kwamba baada ya kutengeneza ile draft na kuona matatizo ambayo na wewe umeyaona hasa tunapofika kuna Madaktari super specialist ambao sasa kwenye muundo hawatambuliki, kuna watu walioongeza elimu kama manesi wengine wameongeza elimu lakini haifiki kwenye muundo, tulivyoyaona hayo tumemaliza sisi kama Wizara. Sasa tunataka tushirikishe hivyo vyama vyote, tukishashirikisha sasa, wakishakubali wote tunapeleka utumishi sasa kitu ambacho ni shirikishi na kimekubalika na pande zote.
MHE. DKT. ALICE K. KAIJAGE: Mheshimiwa Spika, ahsante. Nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali. Pamoja na maelezo mazuri ya Serikali nina swali moja la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, kweli anasema kuna mitandao ambayo inatumika kuhudumiwa na TANESCO lakini Kibiti ni moja ya mkoa ambao uko Kusini mwa Mkoa wa Pwani ambapo kuna mikoa minne; Mkuranga, Mafia pamoja na Rufiji. Sasa hatuoni umuhimu wa kujenga kituo kikubwa sana kwa sababu hapo ni centre ya mikoa ya Kusini ya Mkoa wa Pwani, kituo kikubwa ambacho wananchi wataweza kufika sababu sio vijiji vyote ambavyo wanaweza kufikiwa na mambo ya mtandao? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, nashukuru, kama nilivyoeleza kwenye jibu la msingi, tunaendelea kufanya tathmini kwenye paragraph ya kwanza. Nimesema kwa umahususi wa Kibiti kwa ajili ya kuona namna ambavyo tutafanya ili kujenga ofisi hii ili iweze kuhudumia maeneo ya Kibiti lakini na maeneo mengine ya Jirani.
MHE. DKT. ALICE K. KAIJAGE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, kwa vile changamoto iliyoko katika Halmashauri ya Chalinze inafanana na changamoto iliyoko katika Halmashauri ya Bagamoyo katika Kata ya Mapinga katika eneo la Kiharaka. Je, Serikali lina mpango gani kulipa wananchi wa eneo la Kiharaka katika Kata ya Mapinga? Ahsante. (Makofi)
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi na naomba nijibu swali la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kama nilivyokwishasema tunao mpango ambao umejumuisha migogoro mingi, kwa hiyo, kama hili eneo la Kiharaka ni sehemu ya mpango huu basi litakamilishwa katika mpango huu wa fedha, lakini kadri tulivyoendelea kutatua hii migogoro, migogoro mipya pia imekuwa ikijitokeza, kwa hiyo, kama huu ni mgogoro mpya tutaujumuisha katika mpango wetu baada ya kujiridhisha kwamba ni eneo ambalo lina mgogoro na Jeshi, ahsante.
MHE. DKT. ALICE K. KAIJAGE: Mheshimiwa Spika, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali: Je, mko yatari kuanza sasa usanifu na ujenzi wa barabara hiyo kwenye bajeti ya mwaka huu unaokuja Julai, 2023/2024?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Dkt. Alice Kaijage, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, katika jibu langu la msingi, nilisema tunakamilisha usanifu wa kina mwezi huu tarehe 30 Juni. Tayari bajeti imeshapitishwa. Kwa hiyo, hiyo barabara itaingizwa kwenye mpango wa mwaka unaofuata kwa ajili ya kuanza kuijenga kwa kiwango cha lami, ahsante. (Makofi)
MHE. DKT. ALICE K. KAIJAGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Kwa kuwa tuna Mkongo wa Taifa. Sasa Serikali haioni kuna haja ya kufunga minara hii hasa pembezoni ili kupunguza mahangaiko ya watumishi wawe na utulivu huko pembezoni wafanye shughuli zao kule kule hata kama kusoma wasome online?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Dkt. Alice Karungi Kaijage kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali iliingia kwenye mpango wa kujenga Mkongo wa Taifa. Mkongo wa Taifa faida yake ni kwamba unaweza kupitisha traffic kwa wingi tena kwa kasi ya mwanga lakini vilevile lengo la kujenga Mkongo wa Taifa ni kuondokana na mifumo tuliyokuwa tunatumia zamani ya microwave lakini japo microwave kuna maeneo ambayo bado tunatumia. Lengo la kuwa na Mkongo wa Taifa ni kwamba baadae tutaunganisha minara ili kuhakikisha kwamba huduma inaweza kupatikana popote pale.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mambo makubwa ambayo tayari yameshafanyika, ambayo ni faida kubwa inayotokana na mkongo wa Taifa. Kwa sasa tuna vitu tunaita telecentre, telecentre hizi maana yake kuna maeneo ambapo mgonjwa haitaji kufika Muhimbili anaweza akapatiwa huduma akiwa Bukoba, akiwa Kagera, akiwa Mtwara lakini ile taarifa yake ikasomwa Muhimbili kule kwa sababu ya uwepo wa Mkongo wa Taifa wa mawasiliano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo tunaomba pia tupokee ushauri wako tutaendelea kuboresha kuhakikisha kwamba nchi yetu inazidi kuhakikisha kwamba mifumo yote na huduma zote zinatolewa kwa kidigitali kwani ndio msingi halisi wa uchumi wa sasa, ahsante sana.
MHE. DKT. ALICE K. KAIJAGE: Mheshimiwa Spika, ahsante. Hospitali ya Mkoa ya Tumbwi siyo kwamba inahudumia watu wa Pwani tu na wale wapita njia. Kitengo cha Watoto Njiti kweli kipo lakini uboreshaji ni pamoja na vifaa tiba. Watoto wanazaliwa pale lakini inabidi wakimbizwe.

Je, ni lini Serikali pamoja na kuboresha kitengo cha Watoto Njiti na vifaa tiba vitaboreshwa lini?
NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dokta Kaijage kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwamba Hospitali ya Tumbwi ni mojawapo kweli kuna eneo la Watoto Njiti lakini hospitali inazidiwa. Katika Bilioni 59.3 ambazo zimetengwa kwa ajili ya uboreshaji, Hospitali ya Mkoa wa Tumbi ipo mojawapo na eneo ambalo limetengewa hela kwa ajili ya kulipanua na kuongezea vitanda ni eneo hilo la Watoto Njiti. (Makofi)
MHE. DKT. ALICE K. KAIJAGE: Mheshimiwa Spika, ahsante, naulizia barabara ya Kibiti kupitia Dimani kwenda Mloka kwenye Bwawa la Mkakati la Mwalimu Nyerere ni lini itajengwa kiwango cha lami? (Makofi)

NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, ahsante, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Dkt. Alice Kaijage, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, barabara aliyoianisha inakwenda kwenye Bwawa la Nyerere na ni barabara ambazo Wizara inaangalia uwezekano kama alivyosema Mheshimiwa Waziri ziingie kwenye mpango wa EPC+F ili kuweza kuiharakisha kuijenga barabara hii, ahsante.
MHE. DKT. ALICE K. KAIJAGE: Mheshimiwa Spika, ahsante. Hospitali ya Mkoa ya Tumbwi siyo kwamba inahudumia watu wa Pwani tu na wale wapita njia. Kitengo cha Watoto Njiti kweli kipo lakini uboreshaji ni pamoja na vifaa tiba. Watoto wanazaliwa pale lakini inabidi wakimbizwe.

Je, ni lini Serikali pamoja na kuboresha kitengo cha Watoto Njiti na vifaa tiba vitaboreshwa lini?
NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dokta Kaijage kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwamba Hospitali ya Tumbwi ni mojawapo kweli kuna eneo la Watoto Njiti lakini hospitali inazidiwa. Katika Bilioni 59.3 ambazo zimetengwa kwa ajili ya uboreshaji, Hospitali ya Mkoa wa Tumbi ipo mojawapo na eneo ambalo limetengewa hela kwa ajili ya kulipanua na kuongezea vitanda ni eneo hilo la Watoto Njiti. (Makofi)