Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Dr. Alice Karungi Kaijage (8 total)

MHE. DKT. ALICE K. KAIJAGE Aliuliza:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha inaendelea kuhuisha miundo ya utumishi kwa kada mbalimbali kwa kuwa utaratibu wa kuajiri na kupandisha vyeo ndani ya Utumishi umekuwa ukibadilika kulingana na majukumu ya kiutendaji na maendeleo ya kiuchumi?
WAZIRI WA NCHI OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA Alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa hii ni mara yangu ya kwanza kusimama hapa kama Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, nimesimama hapa mara nyingi kama Mwenyekiti wa Kamati ya Katiba na Sheria kwa kipindi cha tatu sasa cha uenyekiti wangu. Nanze kuchukua fursa hii kumshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa imani kubwa aliyonayo kwangu. Nimuahidi tu kwamba nitakwenda kuchapa kazi kwelikweli, kwenda kupunguza au kumaliza kabisa kero za watumishi wa umma wanyonge ambao ndio msingi wa Taifa letu hili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pili baada ya kumshukuru Mheshimiwa Rais, niwashukuru sana wananchi wa Jimbo la Rufiji, kwa namna moja au nyingine wamekuwa wakiniamini wakati wote waliponichagua mwaka 2015, lakini pia mwaka 2020 nilishinda kwa kishindo kwa kura ambazo hazipata kutokea.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninapenda sasa kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Alice Karungi Kaijage Mbunge wa Viti Maalum wa Mkoa wa Pwani kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa Mujibu wa Kanuni D. 6(2) ya Kanuni za Kudumu katika Utumishi wa Umma za Mwaka 2009, Watumishi wa Umma huajiriwa na kupandishwa vyeo kwa kuzingatia sifa zilizoainishwa katika Miundo ya Maendeleo ya Utumishi ya Kada husika.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kutambua mabadiliko ya kiutendaji pamoja na maendeleo ya kiteknolojia na kiuchumi Wizara mbalimbali zimekuwa zikihuisha miundo ya maendeleo ya kiutumishi ya kada mbalimbali zilizo chini yake kwa kuongeza sifa za kielimu, vigezo vya kuajiri na kupandisha vyeo watumishi.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninapenda kulijulisha Bunge lako Tukufu kuwa, kwa kutambua mabadiliko ya kiutendaji na maendeleo ya kiteknolojia na kiuchumi, kuanzia mwaka 2014 Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora imekuwa ikiziwezesha Wizara Taasisi na Wakala za Serikali kuhuisha miundo yake ya maendeleo ya kiutumishi kadri ya mahitaji mapya yanavyojitokeza. Kwa mfano katika kipindi hicho miundo iliyohuishwa ni pamoja na ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Wizara ya Fedha na Mipango, Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi, Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Wizara ya Habari, Sanaa, Utamaduni, pamoja na Taasisi za Umma na Wakala wa Serikali.
MHE. DKT. ALICE K. KAIJAGE aliuliza:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kukitumia kikamilifu Kitengo cha Kukuza Tija kilichopo Ofisi ya Waziri Mkuu ili kuhakikisha utekelezaji wa miradi mikubwa nchini unakuwa wa tija na kuwanufaisha Watanzania?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA NA VIJANA (MHE. PASCHAL P. KATAMBI) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Alice Kapungi Kaijage, Mbunge wa Viti Maalum, CCM kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, katika kuhakikisha Kitengo hiki kinatekeleza majukumu yake kikamilifu, Serikali imepanga kutekeleza mipango ifuatayo:-

Moja, kuandaa Sera ya Taifa ya Tija na Ubunifu (National Productivity and Innovation Policy) ambayo itaweka mfumo thabiti wa kupima tija na ubunifu katika ngazi ya taasisi, sekta na Taifa ikiwa ni pamoja na miradi mikubwa ya Kitaifa.

Pili, kuanzisha kanzidata ya makubaliano, matamko na taarifa za Kitaifa, Kikanda na Kimataifa kuhusu tija, ubunifu na ufanisi wa viwanda.

Tatu, kufanya tafiti ya tija katika viwanda vya mfano vilivyopo Mikoa ya Dar es Salaam na Mkoa wa Pwani.

Nne, kuandaa na kuwezesha Wiki ya Tija na Ubunifu (Productivity and Innovation Week).

Tano, ni kuandaa na kuwezesha Mpango wa Kitaifa wa Tuzo za Tija na Ubunifu (National Productivity and Innovation Award Schemes).

Sita, kuna mpango wa kuendesha programu 24 za kuwajengea uwezo wadau juu ya dhana, kanuni na viwango vipya vinavyotakiwa katika tija, ubunifu na ufanisi wa viwanda.

Mheshimiwa Spika, aidha, Serikali kupitia Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano wa Tatu (FYDP III) katika kutekeleza katika sekta binafsi, imeelekeza pia sekta binafsi kushiriki katika miradi mikubwa ya Kitaifa kwa kushirikiana na taasisi nyingine ikiwemo Kitengo cha Ukuzaji Tija ili iweze kuboresha ufahamu wa sekta binafsi juu ya masuala ya ufanisi na ushindani na pia utoaji wa huduma zilizo na ubora katika jamii.
MHE. DKT. ALICE K. KAIJAGE aliuliza: -

Je, Serikali imejipangaje kutatua changamoto iliyopo katika vituo vya kutolea huduma za afya ya kukosekana kwa Idara ya Huduma ya Mazoezi Tiba na Utengamao ukilinganisha na ongezeko la wagonjwa wanaohitaji aina hiyo ya tiba?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Alice Karungi Kaijage, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kuwa kuna ongezeko kubwa la uhitaji wa huduma ya mazoezi tiba na utengamao kwenye vituo vya kutolea huduma za afya, huku kukiwa na changamoto ya uwepo wa miundombinu stahiki, vifaa na wataalam kwenye vituo vingi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imefanya tathmini ya mahitaji wa huduma ya mazoezi tiba na utengamao kwenye vituo vya kutolea huduma za afya na inaendelea kukamilisha mpango mkakati ambao utatoa mwongozo katika kutatua uhitaji wa huduma hizo. Ofisi ya Rais, TAMISEMI itatekeleza kikamilifu mpango utakaotolewa ili kuboresha huduma ya mazoezi tiba na utengamao katika vituo vya afya. Ahsante.
MHE. DKT. ALICE K. KAIJAGE aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kukarabati Hospitali ya Wagonjwa wa Afya ya Akili ya Mirembe ambayo Miundombinu yake imeharibika?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA WAZEE NA WATOTO alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Alice Karungi Kaijage, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali kwa kumtumia Wakala wa Majengo (TBA) imeanza upembuzi yakinifu wa majengo yatakayofanyiwa ukarabati pamoja na yale yatakayobomolewa na kujengwa upya. Aidha, kupitia upembuzi huo Serikali itabaini gharama halisi za ujenzi na
ukarabati wa Hospitali hiyo. Kazi hii inatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwezi Oktoba, 2021.
MHE. DKT. ALICE K. KAIJAGE aliuliza: -

Je, Serikali imejipangaje katika kupunguza ama kumaliza kabisa changamoto ya ukosefu wa dawa katika vituo vya kutolea huduma za afya nchini?
NAIBU WAZIRI WA AFYA alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Alice Karungi Kaijage, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali imepeleka Bohari ya Dawa (MSD) shilingi bilioni 333.8 kwa ajili ya ununuzi wa dawa na vifaa tiba ambapo sasa Bohari ya Dawa ipo katika hatua mbalimbali za manunuzi.

Mheshimiwa Spika, pamoja na kupeleka fedha kwa ajili ya manunuzi, Serikali imetoa shilingi bilioni 18 kwa ajili ya ujenzi wa kiwanda cha dawa eneo la Idofi, Mkoani Njombe ambacho kitakuwa na uwezo wa kuzalisha vidonge ndani ya siku mbili vya kutosha nchi nzima kwa miezi mitatu na ujenzi umefikia 70%. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kiwanda cha kuzalisha gloves kilichopo Njombe kimekamilika kwa asilimia 100 na sasa kipo kwenye majaribio; na kikikamilika kitaweza kukidhi mahitaji ya nchi kwa 85%. Aidha, kiwanda cha Keko kimefufuliwa na kinazalisha kwa sasa aina 12 za dawa. Ahsante. (Makofi)
MHE. DKT. ALICE K. KAIJAGE aliuliza: -

Je, Serikali imejipangaje katika kupambana na changamoto ya upungufu wa Wataalam wa Mazoezi Tiba na huduma ya Utengamao nchini?
NAIBU WAZIRI WA AFYA alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Alice Karungi Kaijage, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali imeajiri jumla ya wataalam 84 wa mazoezitiba na huduma mtengamao katika ajira za mwezi Julai, 2022. Hata hivyo, kufanya idadi ya wataalam wa mazoezitiba na huduma mtengamao kuongezeka kutoka 653 hadi 737.

Mheshimiwa Spika, kwa sasa kuna jumla ya vyuo vikuu vinne ambavyo ni Muhimbili, KCMC, Bugando na Zanzibar vinavyotoa taaluma, hivyo kupunguza changamoto ya uwepo wa wataalam katika soko la ajira.
MHE. DKT. ALICE K. KAIJAGE aliuliza: -

Je, Serikali haioni haja ya kutoa elimu kwa watumishi juu ya ukokotoaji wa mafao?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU (MHE. PASCAL P. KATAMBI) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri Mkuu ninaomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Alice Karungi Kaijage, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ili kuhakikisha watumishi wanapata elimu juu ya ukokotoaji wa mafao na elimu ya hifadhi ya jamii kwa ujumla, Serikali kupitia Mifuko ya PSSSF na NSSF imekuwa ikitoa elimu kwa watumishi.

Mheshimiwa Spika, kuanzia mwezi Julai hadi Desemba 2022 mifuko imeweza kutoa elimu kwa jumla ya waajiri 318 ambapo wanachama 19,656 walihudhuria mafunzo hayo kutoka katika sekta ya umma na sekta binafsi. Kazi ya kuwafikia waajiri na wanachama wengine ili kuwapa elimu husika inaendelea.

Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea kusimamia, kuratibu na kuhakikisha elimu kwa watumishi wa umma inatolewa kupitia makundi mbalimbali yanapokuwa na vikao kama Mabaraza ya Wafanyakazi, semina, warsha na makongamano. Aidha, mifuko inaendelea kuwatembelea watumishi katika maeneo yao ya kazi, kuandaa na kuwashirikisha katika vipindi kwenye luninga na kurusha vibango katika mitandao ya kijamii, ahsante.
MHE. DKT. ALICE K. KAIJAGE aliuliza: -

Je, Serikali haioni haja ya kuupitia tena Muundo wa Utumishi wa Madaktari Bingwa wa mwaka 2022?
NAIBU WAZIRI WA AFYA alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Afya, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Alice Karungi Kaijage, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatekeleza Waraka wa Maendeleo ya Utumishi Na.1 wa mwaka 2009 kwa kada zilizo chini Wizara ya Afya ambao umeainisha miundo na sifa za wataalam mbalimbali wanaopaswa kuajiriwa na kufanya kazi katika vituo vya kutolea huduma za afya nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara inakamilisha Mapitio ya Miundo ya kada za afya ambayo inatarajiwa kukamilika Mwezi Mei, 2023 na kuwasilishwa Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa ajili ya kupata idhini. Miundombinu hii itakapokamilika itaweza kukidhi mahitaji ya kiutumishi kwa wataalam mbalimbali wa afya wakiwemo Madaktari Bingwa.