Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Dr. Alice Karungi Kaijage (2 total)

Hotuba ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyoitoa wakati wa Ufunguzi wa Bunge la Kumi na Mbili, Tarehe 13 Novemba, 2020
MHE. DKT. ALICE K. KAIJAGE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii. Kwa kuwa name ni mara yangu ya kwanza kusimama katika Bunge lako Tukufu, naomba nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu ambaye ameniwezesha kufika kwenye Bunge hili leo. Pia naomba nikishukuru Chama changu Cha Mapinduzi, Jumuiya ya Wanawake pamoja na wanake wema sana wa Mkoa wa Pwani ambao waliridhia kunisindikiza na kunifanya niweze kuwa Mbunge wao kuwawakilisha. Navishukuru Vyama vya Wafanyakazi; pia nashukuru familia yangu, Mama yangu, ndugu, jamaa na marafiki kwa ujumla wao.

Mheshimiwa Naibu Spika, nikijielekeza kwenye hotuba ya Mheshimiwa Rais, nimesoma hotuba zote za 2015 na 2020; Mheshimiwa Rais ameonyesha nia njema na dira katika kuiendeleza Tanzania, lakini ameonyesha dhamira ya wazi kwenye kulinda amani yetu na pia kuudumisha Muungano wetu. Nina sababu zote za kushukuru Vyombo vya Usalama na Ulinzi ambavyo kwa pamoja na wananchi wenye nia njema wameweza kushirikiana kuendelea kulinda amani ya nchi yetu. Wanastahili pongezi kubwa sana vyombo vya Ulinzi na Usalama. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, tumeona suala nzima la huduma za jamii katika ujumla wake, wenzangu wamezungumzia, lakini naomba nijikite kwenye suala la afya. Ukiangalia kwenye Ilani na hotuba yake, Mheshimiwa Rais ameeleza nia njema kabisa ya kuboresha huduma za kibigwa na pia kuongeza miundombinu pamoja na vifaa vya kutosha vya kisasa. Siyo suala la kupinga kabisa lipo wazi kwa jinsi ambavyo huduma za kibigwa zimeimarika. Ukiangalia taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete, halina ubishi wote tunafahamu. Muhimbili hiyo hiyo mpaka sasa wanapandikiza figo, wanaweka masikio, cochlear implant, wanafungua kichwa ubongo bila kufungua fuvu. Kwa hiyo, huduma nyingi zimeimarishwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nayasema hayo kwa sababu nina jambo moja la kulisema. Katika suala nzima la magonjwa la kiharusi (stroke) imekuwa ni tatizo ambalo ni kubwa sana kwa siku admission au wanalazwa wagonjwa watano mpaka sita Muhimbili, acha Mlonganzila au hospitali zingine za rufaa. Kwa hiyo nina wazo moja, tunaomba taaisisi ya Stroke ianzishwe; wagonjwa wale wanakaa muda mrefu, wanachangwanywa na wagonjwa wengine, immunity yao ni ndogo. Kwa hiyo kuna uwezekano kama wakianzisha stroke center kama wenzetu South Africa na Egypt wanafanya pawe na stroke nurse, pawe na wataalam, kwa hiyo itakuwa ni kitengo kinachojitegemea, kitafanya outreach, elimu kwa jamii pamoja na kuwa na Manesi katika hospitali zingine ambazo ni kubwa ili kupunguza tatizo la stroke ambayo sisi wote ni wahanga.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niende kwenye Hospitali yetu ya Mirembe. Hii ni hospitali ya muda mrefu, ina miaka 93, imeanzishwa mwaka 1927. Hii hospitali inachukua Watanzania wa kawaida na sisi ni wahanga hatuwezi kukwepa kuingia pale siku moja. Hii hospitali ni ya muda mrefu ina miundombinu chakavu, mikongwe, lakini inasababisha kupata taswira nzima ya huduma njema inayotolewa pale. Pili ipo katika Makao Makuu ya Nchi. Mazingira mazuri yanawatia moyo wafanyakazi kufanya kazi kwa bidii na Watanzania wale ingawa afya yao ina matatizo lakini wanastahili kukaa kwenye mazingira mazuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, bed state kwa siku wagonjwa hawapungui mia tano, kuna Isanga, kuna Mirembe Proper na vituo vingine vya kutolea dawa za kulevya, vyote hivyo viko chini ya Mirembe. Naomba sasa ufike wakati bajeti yao iongezwe, ikiwezekana sasa iwe taasisi, kwa mwezi wanatumia zaidi ya milioni 280, kwa maana ya huduma za kila siku kwenye taasisi ile. Naomba iangaliwe taasisi ya Mirembe kwa sababu sisi sote ni wahanga.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja (Makofi)
Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022
MHE. DKT. ALICE K. KAIJAGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuchangia. Kwanza, naomba nianze kupongeza Serikali kwa kuleta Mpango huu mzuri, pamoja na mipango mingine yote iliyotangulia tuliona kwamba ina nia ya kuhakikisha tunafikia Dira ya Maendeleo ya mwaka 2025 sanjari na kukuza malengo endelevu ya SDGs. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mpango huu umekuwa na nguzo muhimu tatu, ikiwa ni utawala bora, maendeleo ya watu pamoja na kukuza uchumi. Kukuza uchumi ni kuwekeza katika sekta za kiuchumi na kiuzalishaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kwa muda mrefu imeendelea kuingia katika mikataba na makubaliano mbalimbali aidha kupitia wahisani, mikopo, uwekezaji ambalo ni jambo jema sana, lakini tumeona mara nyingi Mheshimiwa Rais amekuwa akihoji, ndugu zangu hivi kweli huu uwekezaji una tija? Hivi hii miradi ina tija? Tija ni nini basi? Tija ni uwiano kati ya kitu unachowekeza na kile kinachopatikana, lakini kikionyesha mabadliko chanya katika mtu mmoja mmoja, katika taasisi na nchi kwa ujumla.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tija ni nini ili kama mwekezaji anaweka mradi wake au analeta msaada wake au anaweka kampuni yake, mwisho wa siku anapoondoka aache ajira endelevu, aache ujuzi, akuze ujuzi kwa wale ambao wanahusika na pia kubwa kabisa waache teknolojia pamoja na ubunifu. Yaani mradi unapokwisha asiondoke yeye na vitu vyake akaacha vitu vitupu. Kwa mfano katika kuwekeza 100% kwa maana ya consultancy anaanzisha mradi yeye 100% mgeni anakuwepo pale pengine engineer wetu au mtaalam wetu anashuhudia tu msumari unavyopondwa pondwa kwenye shirika hilo au kwenye kampuni au mradi au mashine inavyofungwa, lakini ule ujuzi hashiriki moja kwa moja, anapoondoka anaondoka na ujuzi wake mwekezaji. Kwa hiyo ifikie sehemu, nashauri Serikali hii miradi safari hii, tunaona watu wengi wanalalamikia miradi ya maji, miradi mbalimbali ambayo tumeingia lakini kama nilivyofafanua nini maana ya tija. Je miradi hii inaacha tija kweli? Kwa nini? Sasa ifikie sehemu tutumie chombo kile kinaitwa chombo cha kukuza tija na ubunifu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, zamani liliitwa Shirika la Tija la Taifa, chombo hiki kipo na kipo vizuri chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu chombo hiki sasa kipewe meno kipewe uwezo ili kuondoa haya malalamiko yote ambayo yako kwenye miradi ambayo ina mambo mengi ambayo ni baadhi lakini kwa kweli ni mingi, miradi ambayo imekuwa ina-fail. Chombo hiki kabla miradi au mikataba haijaanza kutekelezwa, chombo kikaangalie kikapime hii miradi itakuwa na tija kama nilivyoeleza maana ya tija ili baadaye kusiwepo na malalamiko. Huu ni wakati wa kukipa chombo hiki meno na uwezo maana tunacho, tunacho kwenye Serikali yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia viwanda tulivyopata ni vingi sana kwenye nchi sasa hivi. Kweli ni vingi na ni vizuri, ni jambo jema, lakini chombo hiki bado kina uwezo wa kwenda kutathmini vile viwanda, kufanya analysis na kutoa ushauri ili mwisho wa siku viwanda visiwe vya kupotea, viwe vina-sustain vinakaa muda mrefu yaani vinaendeleza kuwa na tija, maana yake havikufanyiwa huu upekuzi mwanzo ndiyo maana tunaona kuna malalamiko mengi, kwenye viwanda hatujui itakuwaje baadaye na miradi imeshaonyesha jinsi ilivyokuwa kwenye Mipango iliyopita. Kwa hiyo, nashauri chombo hiki kitumike ili kilete tija katika miradi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia naomba nitoe mfano, wenzetu China wakati wanaandaa Olympic 2008 walikuwa wametoa nafasi kwa wawekezaji, lile ni jambo kubwa lilihitaji watu wawekeze kwa wingi, lakini walikuwa wakali, wakasema unakuja kuwekeza ndiyo, lakini kuanzia mwanzo wa mchakato wa kutaka kuwekeza, kama ni kujenga uwanja wewe mwekezaji utafanya kazi kwa asilimia 70 na sisi wazawa consultancy mzawa atafanya 70 ili pale wanapomaliza watapata faida ya 70% yes lakini 30% kutoka anapowekeza anajenga kiwanda au anajenga uwanja ile pesa inabaki ndani inazunguka kwa sababu yule mwekezaji wa ndani (consultancy) alikuwepo toka mwanzoni. Kwa hiyo inabidi kuangalia mfano wa wenzetu, wameendelea lakini wako makini sana na mali yao na mzunguko wa pesa yao ndani mwao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizungumzie kwenye suala la afya, na-declare interest, suala zima la kada ya physiotherapy. Naipongeza Serikali sana imefanya bidii nyingi lakini taaluma hii ambayo ni matibabu kwa njia mbalimbali ikiwemo mazoezi tiba, wataalam ni wachache, wenye shahada hawazidi 100 kwenye nchi nzima, lakini pia chuo ambacho kinatoa shahada hii ya physiotherapy Kiswahili chake matibabu ya njia mbalimbali ambayo pia ni mazoezi tiba, ni KCMC peke yake. Niipongeze Wizara ya Afya sasa ina mpango wa kuanzisha hii kozi kwenye Chuo cha Muhimbili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, bado haitoshi, naomba niishauri Serikali ifanye uanzishaji wa kozi hii kwenye Chuo cha UDOM na Bugando. Hawa watu wanahitajika sana kwa sababu tunafungua hospitali nyingi za mikoa kwa bidii na pia hospitali za wilaya, pamoja na vituo vya afya. Pia nashauri kwa sasa kwenye vituo vya afya na hospitali za wilaya, hivi vitengo viwekwe, havipo, tufikirie viwekwe na wataalam waongezeke, wapelekwe kule kwa sababu ni idara muhimu sana, lakini ina watu wachache.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri pia pawepo na wazo la kuongeza Shahada ya Uzamili na Uzamivu ikiwezekana ya kada hii ya physiotherapy hatuna kwenye nchi yetu. Ili upate Shahada ya Uzamivu lazima uende nje ya nchi. Kwa hiyo nilikuwa nashauri hili jambo litekelezwe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuongea hayo, naunga mkono hoja. Ahsante. (Makofi)