Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Janeth Elias Mahawanga (3 total)

Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022
MHE. JANETH E. MAHAWANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Nichukue nafasi hii kumshukuru Mwenyezi Mungu, Chama changu ha Mapinduzi, kina mama wa Mkoa wa Dar es Salaam na familia yangu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nichangie Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Miaka Mitano na Mwaka Mmoja. Katika kuongeza kipato cha Serikali na kuwawezesha wananchi kiuchumi kupitia ile Mifuko 18 ambayo iko chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu, napendekeza ishirikiane kwa karibu na Wizara ya TAMISEMI pamoja na Halmashauri zetu. Pia iongeze wigo kwa kuhusisha Madiwani nao kwenye Mpango huu ili itengeneze mfumo mzuri wa ukusanyaji wa hizi pesa pindi wajasiriamali hawa wanapopata hiyo fursa kwani fedha nyingi zinatoka kwenye vikundi lakini pia hazirudi. Kwa hiyo, tatizo kubwa hapa ni mfumo wa ukusanyaji wa hizi hela. Watakapohusishwa pia Madiwani katika utaratibu huu itasaidia kwani vikundi vingi kwenye kata zetu Madiwani ndiyo watu sahihi na wanavijua zaidi vikundi itasaidia ufuatiliaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile katika kutoa fursa hizi, Serikali iangalie zaidi kwenye kutoa elimu kwa wajasiriamali hawa kwa sababu fursa zipo, mikopo inatoka lakini wananchi wengi wanakwama kutokana na ukosefu wa elimu. Elimu hizi zikajikite katika kukuza ujuzi wa kuongeza thamani za bidhaa zao, upatikanaji wa mitaji, utafiti wa masoko na kuzitambua fursa zinazowazunguka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na haya naomba niongelee usajili wa vikundi. Sheria ya Fedha imetoa mamlaka kwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kukasimu shughuli zote za usajili, usimamizi na ufuatiliaji wa vikundi vya kifedha. Makundi haya ya kifedha yamegawanywa katika sehemu nne, kuna mabenki na microfinance ambazo zinapata miongozo moja kwa moja kutoka BoT, kuna SACCOS ambazo zinapata miongozo katika Vyama Ushirika na kuna vikundi vya kina mama ambavyo ni VICOBA wao wanapata miongozo kutoka TAMISEMI. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Benki Kuu ilitoa muda wa mwaka mmoja vikundi yyote viwe vimesajiliwa kupitia sheria mpya. Ule muda uliisha, akina mama walikuwa wako tayari kusajili lakini miongozo kutoka TAMISEMI ilikuwa haijashuka huku chini. Iliongezwa muda wa miezi sita ambao unaisha mwezi Aprili mwaka huu, lakini mpaka sasa bado akina mama wakienda kwenye Halmashauri wanakuta bado hakuna utaratibu wowote ambao umetoka TAMISEMI unaowataka wao wasajili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii imeleta hofu kubwa kwenye vikundi vya kina mama kwani kuna vikundi ambavyo vimesimama kufanya shughuli zake za ujasiriamali na kuna vingine vinafanya kwa uwoga vikiwa vinasubiri kuangalia miongozo hii ya usajili mpya inataka nini na inasemaje. Kwa hiyo, niiombe Wizara ya TAMISEMI, ijitahidi kutoa miongozo hii basi ili kina mama wafanye huo usajili kwa kutumia hii Sheria mpya ya Fedha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile Serikali iangalie baadhi ya kero kuzifanya kama vyanzo vya mapato yaani fursa. Kwa mfano, Mkoa wa Dar es Salaam kuna kero kubwa sana ya takataka, Wizara ya Viwanda na Uwekezaji ni wakati sasa wa kuangalia ni jinsi gani kiwanda cha kuchakata taka kinaweza kupatikana kwani zaidi ya kuongeza kipato kwenye nchi yetu itaongeza ajira pamoja na kumaliza hili tatizo la taka, tutapata mbolea na gesi na Serikali itapata pato lake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niende kwenye ushauri, nashauri Serikali irejeshe mifumo ya kuzisaidia na kuchochea benki nchini yaani credit guarantee schemes ambazo zitasaidia wawekezaji kulipa kodi na Serikali itapata pato pia. Vilevile yafanyike marekebisho ya kodi inayohusu ufutaji wa madeni ambayo hayalipiki yaani bad debts write-off iendane na sera, kanuni na Sheria ya Benki Kuu ili kuweka mazingira ya biashara yanayotabirika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia Serikali iwe inatoa muda wa kutosha inapofanya marekebisho ya sera zake mbalimbali ili kutoa muda wa wadau kujipanga kutokana na mabadiliko ya sera zinapokuwa zinafanyiwa marekebisho. Pia Serikali iweke mazingira mazuri ya kufanya mabenki binafsi kuachana na sera ya kuanzisha benki ambazo zinakuja kuwa mzigo na hazina tija kwenye Taifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho niombe mamlaka ya kukusanya kodi irekebishe Tax Administration Regulation kwa kuondoa utaratibu wa sasa wa kutumia Urgent Notice kutoka kwenye mabenki moja kwa moja badala yake iweke utaratibu wa kukubaliana na walipa kodi kulipa kodi kwa muda rafiki. Hii itasaidia sana kwani wafanyabiashara wengi wataweza kuweka hela benki, watakuwa na imani na kuondoa ile hofu kwamba benki siyo sehemu salama sasa hivi ya kuweka hela.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakiweka taratibu hizi wafanyabiashara, wajasiriamali wengi watakuwa na imani, itaongeza hamasa, watu wataweka fedha benki, ukizingatia hata Mheshimiwa Rais wakati anahutubia Bunge la Kumi na Mbili alisisitiza kuwa watu wahimizwe kuweka hela benki ili kusaidia benki zetu zifanye biashara na mzunguko uwe imara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
MHE. JANETH E. MAHAWANGA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi hii ya kuchangia bajeti hii ya TAMISEMI. Kwanza niipongeze Wizara kwa wasilisho zuri na vipaumbele vizuri kabisa ambavyo kama vitaenda kutekelezeka nina uhakika tutapata matokeo chanya na changamoto zote kwenye jamii yetu zitakwenda kwisha.

Mheshimiwa Spika, nitajikita kwenye mikopo hii ya asilimia 10 ambayo wanufaika ni akinamama, vijana na walemavu. Lengo la Serikali kwa mikopo hii lilikuwa zuri sana lakini uhitaji ni mkubwa kuliko pesa yenyewe na hii inatokana na baadhi ya pesa inayotoka kuwa hairudi. Je, halmashauri zetu zinafanya tathmini ya kuangalia ni kiasi gani kimetoka na kiasi gani kimerudi na kwa nini hakijarudi? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wanufaika wa pesa hii kuna kitu wanakikosa ambacho ni muhimu sana, wanakosa elimu. Akina mama wengi ni wajasiriamali ambao wanafanya shughuli za kijasiriamali kama usindikaji wa vyakula, lakini wanafanya kwa elimu yao binafsi, kwa uzoefu wao wa kufundishana wenyewe kwa wenyewe. Ningeziomba halmashauri zishirikiane na taasisi ambazo zinaunga mkono juhudi za kuwainua wananchi kiuchumi, hasa wajasiriamali wa chini. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa mfano unakuta kuna matangazo ya SIDO yanayotoa elimu ya ujasiriamali hasa upande wa usindikaji, akina mama wengi wanatamani kwenda kusoma mafunzo haya lakini wanashindwa kutokana na kukosa ada. Halmashauri kama itaandaa utaratibu mzuri ikapata wadau kutoka SIDO, kutoka kwenye benki wataalam wa mambo ya fedha, wataalam wa masoko, wataalam wa fursa na wataalam wa kuongeza thamani ya bidhaa za wajasiariamali wadogo wakashirikiana na Maafisa Maendeleo na Madiwani wetu kwenye kata wakapita kwenye vikundi vile vya akina mama, vijana wakatoa elimu hii, nina uhakika itasaidia sana. Tunasema tunakwenda kwenye uchumi wa viwanda, tunatafuta vyanzo vingine vya mapato, lakini nina uhakika kabisa mikopo hii ni chanzo tosha cha mapato kama tutawaongezea thamani ya ujuzi wanufaika hawa wakaweza kuwa wajasiriamali wakubwa wakalipa kodi, tutapata mapato kwenye Serikali yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuna kundi lingine la vijana ambao wanamaliza vyuo vikuu wako mtaani hawana kazi. Halmashauri ina uwezo kabisa wa kuangalia mikopo hii ya asilimia 10 ikachukua kundi fulani la vijana at least kundi moja kama kikundi kutoka kwenye kila halmashauri wakawapeleka kupata elimu. Kuna taasisi tano zimeungana ambazo ni SIDO, VETA, NSSF, Baraza la Uwezeshaji Uchumi Wananchi na Benki ya Azania, hawa wanatoa elimu baadaye wanatoa mikopo kwa ajili ya viwanda vidogo kuanzia milioni 50 mpaka milioni 500. Vijana wanaomaliza chuo wakichukuliwa na halmashauri, wakasimamiwa kupata elimu hii kwa kulipiwa huko SIDO au VETA wakaweza kufungua kiwanda wataweza kuajiri vijana wenzao, watatoka kwenye wimbi la kukosa ajira na mwisho wa siku watakuwa walipa kodi wataongeza mapato kwenye Serikali yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niombe halmashauri zetu zishirikiane na benki. Benki nyingi zina bidhaa nzuri sana kwa ajili ya wajasiriamali wadogo, lakini wajasiriamali wengi wanakosa taarifa. Kama halmashauri wataweza kushirikiana na hizi benki ambazo zinainua wajasiriamali wadogo zikapita kwenye kata zetu akina mama, vijana na walemavu wakapata taarifa sahihi wakatumia kile kidogo walichokipata kutoka kwenye ile asilimia 10 hawa watu wanakwenda kuinuka. Ni aibu kuona kijana anakuwa machinga ndani ya miaka kumi. Kijana huyo alitakiwa awe ameshatoka kutoka kwenye ujasiriamali mdogo wa kupita barabarani akaweza kukaa kivulini akawa mlipa kodi mzuri, Serikali itaongeza mapato. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nitoe ushauri kwa Wizara ya TAMISEMI. Kuwe na training pia za ndani kwa viongozi wetu kuanzia ngazi ya mkoa, wilaya, kata mpaka vijiji. Viongozi hawa wote wajione wao ni kitu kimoja na wanatembea kwenye safari moja, wanatakiwa wafanye kazi kama timu. Mkuu wa Mkoa ni mteule wa Rais, Mkuu wa Wilaya ni mteule wa Rais, Mkurugenzi ni mteule wa Rais, sasa kama hawa watu hawatakuwa kitu kimoja wakaanza kusigina wenyewe kwa wenyewe misuguano ile waathirika ni wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mwananchi anapokuwa na tatizo lake ambalo linatakiwa kuwa solved kwa Mkuu wa Mkoa au kwa Mkurugenzi, lakini…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa Janeth.

MHE. JANETH E. MAHAWANGA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naunga mkono hoja. (Makofi)
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022
MHE. JANETH E. MAHAWANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi hii nami kuchangia bajeti hii. Kwanza naipongeza Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais, Mheshimiwa Mama Samia Suluhu Hassan kwa bajeti hii nzuri kwa Serikali ya Awamu ya Sita maana ni bajeti ya kwanza. Vile vile, nampongeza Waziri wa Fedha na Mipango na Naibu wake pamoja na timu nzima kwa bajeti hii nzuri. (Makofi)

Mheshmiwa Naibu Spika, bajeti hii inatia matumaini na faraja kwa Watanzania kwani ni bajeti ambayo imekidhi changamoto zote za jamii yetu kwa kuweka vipaumbele ambavyo Wabunge wengi walichangia katika Wizara mbalimbali. Vile vile, bajeti hii inakwenda kukamilisha mahitaji yote hususan kwenye masuala ya afya na miundombinu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia napongeza kuhusiana na kipengele cha kodi ya line za simu. Tija ya kodi hii ni nzuri, kama ambavyo bajeti imeonyesha Shilingi za Kitanzania bilioni 360 zinakwenda kupatikana ambapo zitakwenda kujenga zahanati na mahospitali. Naiomba Serikali, fedha hizi kama zitakwenda kutekeleza haya, basi kiu kubwa na changamato ya masuala ya afya katika jamii yetu itakwenda kukamilika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile naipongeza bajeti hii kwenye kodi ya shilingi mia katika kila lita ya mafuta. Fedha hii itakapopatikana itapelekwa TARURA kama ambavyo imeonyeshwa, ni kitu kizuri sababu fedha hizi zitakapokwenda kutoa changamoto ya miundombinu, uchumi wetu utakwenda kuimarika hususan kwenye jamii yetu hasa vijijini, kwani uchumi wa nchi unategemea sana suala la miundombinu. Kwa hiyo, naipongeza sana Serikali kwa kuliona hili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile bajeti hii imekwenda kugusa masuala ya vikundi vya akina mama na vijana, hasa katika kutoa mikopo. Ukiangalia hata Mheshimiwa Rais alipoongea na akina mama ali-insist sana suala la vikundi vya akina mama kujiunga ili wapate mikopo ambayo itasaidia kutoa ajira na kufanya biashara zenye tija. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naiomba Serikali kupitia bajeti hii, wakaangalie katika suala la Sheria ya Fedha Mwaka 2018, kwani limekuwa ni mzigo hasa kwenye vikundi vya akina mama. Naiomba Wizara ikatumie wataalamu wa BoT katika kutoa elimu, maana vikundi vingi vimeshahamasishwa kujiunga, lakini kupitia sheria hii wengine wanafunga, hawaelewi sheria ile inataka nini hususan kwenye kutumia teknolojia ya TEHAMA. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naiomba Wizara itumie wataalamu wao wa BoT ambao wanaweza kufafanua sheria hizi wapite kwenye Wilaya wakutane na Madiwani na Bibi Maendeleo, watoe miongozo ya sheria hii hasa katika vikundi vya akina mama na vijana ili nao watakaposhuka chini kwenye makato wakikutana na akina mama waweze kufafanua sheria hizi ili vikundi viende kuwa imara vikatumie fursa hii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naishauri Serikali kupitia bajeti hii ikaangalie masuala ya sheria za fedha, lakini zaidi sana ikaangalie kwenye kipengele cha mabenki, kwani mabenki yatakaposhirikiana na Serikali katika kuongeza tija kwenye mikopo ya wafanyabiashara, itasaidia sana, maana mikopo ya asilimia 10 bado haitoshelezi. Kwa mfano, Mkoa wa Dar es Salaam, kazi za usafi wa barabara ambazo zilikuwa zikifanywa na akina mama wengi sasa hivi zile kazi zimeamishwa kwa SUMA JKT. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kuna kundi kubwa la akina mama ambalo limepoteza ajira na kupitia ajira zile walikuwa wakilea familia, wakisomesha watoto na kujikimu kwa mahitaji yao ya kila siku. Kwa hiyo, naiomba Serikali iangalie sana taasisi za kifedha hususan mabenki, kuangalia ni jinsi gani ambavyo mabenki haya yataweza kuongeza mikopo kwa akina mama na vijana lakini mikopo hiyo itoke kwa riba nafuu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile naishauri Serikali iwekeze kwenye mfumo thabiti ulioungana (complete and consolidated system) ambayo watakuwa na utambulisho utakaokuwa na kanzidata ya taarifa za wafanyabiashara. Taarifa hizo zikiwa zinahusisha biashara zao, mali zao anuani za makazi ambazo zitaweza kusaidia mabenki kuwatambua hawa watu na kutoa mikopo kwa gharama nafuu, lakini kwa kutumia mfumo huu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile Serikali iangalie kwa jicho la pili kuwekeza katika mabenki yote kuhakikisha kwamba gharama za uendeshaji wa mabenki, zisizidi asilimia 55 ya mapato. Ni kwamba inasema ikizidi benki hairuhusiwi kupata dividend ambayo ni kutoa faida. Kanuni hii imefanya mazingira ya uwekezaji wa mabenki kuwa ngumu. Kwa hiyo, naiomba Serikali iangalie sana katika hili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia, kwa kupitia bajeti hii, naiomba Serikali ijikite zaidi katika mapato na mwenendo wa uchumi hususan kwenye ukuaji wa pato la Taifa, kwenye mapato na matumizi ya Serikali, kwenye deni la Taifa, Serikali ijikite sana kuangalia ukopaji na ulipaji wa madeni ili Taifa letu lisije likaingia kwenye adha ya kutokopesheka. Zaidi Serikali iboreshe tena kwenye sekta ya fedha; Serikali irejeshe mifumo iliyokuwa inasaidia benki kutoa mikopo kwa wingi (Guarantee Credit Schemes). Benki hizi zilikua kwa kutumia mifuko hii; mifuko ilikuwa inachochea sana utoaji wa mikopo. Kwa hiyo, Serikali ijitahidi kurudisha hili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile uendeshaji wa sekta binafsi. Kama tulivyoona Serikali imeweka mazingira mazuri hususan kwenye Mfumo wa Sera na sheria za kodi ambazo zimekuwa ni kivutio kwa wawekezaji wetu. Mwisho, ijizatiti katika tathmini ya utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Mwaka 2025. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema haya, naipongeza Serikali kwa bajeti hii nzuri na ninaunga mkono hoja. (Makofi)