Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Tabasamu Hamisi Hussein Mwagao (22 total)

MHE. TABASAM H. MWAGAO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. Naomba kuuliza swali moja la nyongeza kwa niaba ya wananchi wa Sengerema. Ni kwamba tuna miradi mikubwa, Mradi wa Sengerema ni mradi mkubwa katika nchi hii, una bilioni 23, lakini una deni la shilingi milioni 300 kutoka TANESCO. TANESCO wamekuwa wakikata maji toka mradi huu umefunguliwa na kuna mabomba yako Sengerema pale yanasubiri kusambazwa kwenye hiyo miradi ya maji.

Je, Waziri yuko tayari kukubali wananchi wa Sengerema wauze yale mabomba halafu wakalipie umeme ili tukae salama sisi.

Mheshimiwa Spika, hili jambo ni kubwa na namwomba Mheshimiwa Waziri wa Maji, yuko tayari kufuatana na mimi kwenda Sengerema akaone hii hali?
WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, kwanza ukimuona mtu mzima analia ujue kuna jambo. Sasa niko tayari kuongozana naye lakini hapa niwe muwazi, Serikali eneo la Sengerema imewekeza zaidi ya bilioni 20, imetimiza wajibu wake, lakini ni haki ya mwananchi kupatiwa maji nay eye ana wajibu wa kulipia bills za maji. Kwa hiyo kubwa yawezekana kuna changamoto pia ya kiutendaji kushindwa kusimamia na kukusanya mapato. Haiwezekani uwe na mradi wa bilioni 20, halafu ushindwe kukusanya mapato angalau kulipia umeme, haiwezekani! Kwa hiyo nitafika na tutaangalia namna gani ya kumsaidia. Tukiona mtendaji yule anashindwa kutimiza wajibu wake, tutashughulikiana ipasavyo kuhakikisha wananchi wa Sengerema wanaendelea kupata huduma ya maji. (Makofi)
MHE. TABASAM H. MWAGAO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Kwa niaba ya wananchi wa Sengerema, naomba kuuliza swali la nyongeza kwa Mheshimiwa Waziri wa Kilimo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna Mradi katika Bwawa la Nyamterera Katunguru, Sengerema na Mradi wa Bwawa la Isole Kishinda katika Halmashauri ya Wilaya Sengerema. Bwana la Kishinda ilipata shilingi milioni 700 na Bwawa la Nyamterera lilipata shilingi bilioni 1.2 lakini pesa hizi hazijulikani ziliko na haya mabwawa hayajachimbwa. Je, Waziri, anaweza akatueleza namna gani wananchi wa Sengerema tutapataje nafuu kuhusiana na uchimbaji wa mabwawa hayo?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Tabasam, Mbunge wa Sengerema, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa amesema kwamba mabwawa haya mawili yalipata fedha na hizo fedha hazijulikani zilipo, namwomba tu baada ya kipindi cha maswali na majibu tukutane, tuweze kuongea mimi na yeye aweze kutusaidia hizo information alizonazo na tuweze kuchukua hatua ili kufahamu kama fedha zimepotea ama kumetokea tatizo gani? (Makofi)
MHE. TABASAM H. MWAGAO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kupata nafasi ya kuuliza swali la nyongeza kwa Waziri wa Maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninachosema ni kwamba Sengerema tunadaiwa pesa, shilingi milioni 300 kwa ajili ya umeme, na hili deni limekuwa la muda mrefu. Nini kauli ya Waziri kuhusiana na deni hilo ili tuanze kuanza upya, kwa sababu tumepata meneja mpya Sengerema? Ahsante.
WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Mbunge wa Sengerema kwa kazi kubwa na nzuri anayoifanya. Ni haki ya mwananchi kupatiwa huduma ya maji. Na mwenye wajibu na jukumu la kumpatia huduma ya maji ni Wizara ya Maji, kwa maana ya Serikali.

Mheshimiwa Naibu Spika, Sengerema ni eneo ambalo lilikuwa na changamoto sana ya maji. Serikali kwa dhamira
njema imewekeza mradi wa zaidi ya bilioni 25 wananchi wa Sengerema waweze kupata huduma ya maji safi na salama. Sasa ni jukumu la Mamlaka ya Maji ya Sengerema kuhakikisha kwamba inakusanya bili na kulipia umeme ili uendeshaji wake uwe vizuri sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, tulikuwa tuna changamoto ya uendeshaji; Meneja, kwa maana ya Mkurugenzi wa mamlaka ile nimemuondoa, fedha hizi za deni tutazilipa, lakini kwa masharti ya kuhakikisha kwamba wanajitegemea na wanaendesha mamlaka ile vizuri na wananchi wa Sengerema wanapata huduma ya maji safi na salama. Ahsante sana.
MHE. TABASAM H. MWAGAO: Mheshimiwa Spika, nami naomba kumwuliza Mheshimiwa Naibu Waziri wa Nishati, Sengerema imekuwa inakatika umeme mara 30 kwa siku na tayari umeme umeshatengenezwa katika eneo letu la kupoozea umeme pale Pomvu Geita, kwa nini Sengerema msituunganishe katika laini ya Geita ili tukaacha kukatikiwa umeme kwa mfumo huu wa kukatika mara 10 kwa siku?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Tabasamu, Mbunge wa Sengerema kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwanza nimpe pole Mheshimiwa Mbunge kwa adha ambayo wananchi wake wamekuwa wakiipata, lakini kama nilivyosema tangu awali, Serikali imepambanua kwa muundo na msukumo mpya uliopo, haya matatio makubwa yataaenda kupunguzwa katika maeneo yetu mbalimbali.

Mheshimiwa Spika, kukatika umeme kama nilivyosema, kunaweza kusababishwa na laini ya umeme kuwa ndefu au mazingira mengine kwa na vitu hatarishi kama maeneo ambayo ni oevu na tunafahamu maeneo mengi ya kanda ya ziwa ni oevu, kwa hiyo, nguzo zetu zimekuwa zikianguka au pengine laini kuwa na watumiaji wengi na pengine ikazidiwa. Kwa hiyo, mambo yote hayo yanachukuliwa maanani na kuangalia namna gani ambavyo tutaweza kurekebisha katika maeneo mbalimbali.

Mheshimiwa Spika, namwomba Mheshimiwa Tabasamu aniruhusu baada ya hapa nikae nae niongee naye nichukue eneo lake kazi, ili nikakae na wataalamu tuweze kujua tatizo hasa linasababishwa na nini katika sababu mbalimbali. Maana inawezekana ukajenga kituo cha kupooza umeme katika eneo hilo, lakini bado umeme ukaendelea ukakatika kwa sababu tatizo halikuwa kituo cha umeme, pengine ilikuwa tatizo lingine, tukibaini tatizo lenyewe tutaweza kulifanyia kazi kwa usahihi.
MHE. TABASAM H. MWAGAO: Mheshimiwa Spika, kwa kuwa Sengerema tunazo shule 31 za Sekondari na katika hizo shule 31 Sekondari mbili ndiyo zina kidato cha Tano na Sita, Sengerema Sekondari na Nyampurukano Sekondari na zimeelemewa wanafunzi na kwa kuwa Mheshimiwa Naibu Waziri alikuja aliona ile hali ya Sengerema kwa watoto walivyowengi na wananchi wa Sengerema wanamshukuru Mwenyezi Mungu wanaendelea kufanya kazi ya ziada kwa ajili ya kuwashughulikia akinamama kupata watoto wengi kuijaza dunia.

Mheshimiwa Spika, sasa hili jambo la Sengerema kutokukosa Sekondari hizi za Kidato cha Tano, Sengerema wanafunzi wanakosa nafasi na Mheshimiwa Naibu Waziri aliona na Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI alikuja kule na akaona hiyo hali. Lini sasa hili jambo litafanyika kwa haraka kwa ajili ya huyo Mdhibiti Ubora kwenda kukagua hizi shule kwa sababu zimekaguliwa mwaka huu na mwaka kesho tunategemea wanafunzi watakuwa ni wengi nini msaada wa wizara katika jambo hili, la kwanza.

Mheshimiwa Spika, lakini swali langu la pili ni kwamba Sengerema Sekondari imeelemewa na bahati nzuri Mheshimiwa Waziri alikuja pale na akatoa ahadi ya kutupa vitanda kutokana na watoto alivyoona wanalala katika mazingira magumu na Nyampurukano Sekondari pia imeelemewa ni nini msaada wa Serikali katika jambo hili ili waweze kutusaidia kwa haraka sasa katika kuzisajili shule hizi.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MITAA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Hamis Tabasamu Mbunge wa Jimbo la Sengerema niweze kujibu maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ameeleza kwamba katika halmashauri yake ya Sengerema kuna Sekondari karibu 31 na katika hilo eneo kuna shule mbili tu za kidato cha tano sita na anataka kwamba tuwaagize watu wa Udhibiti Ubora kwamba waende wakakague hizi shule tuone kama zinakidhi vigezo.

Mheshimiwa Spika, na ni nitumie fursa hii najua kwamba kazi nzuri ambayo anaifanya Mheshimiwa Mbunge na bahati nzuri nilifika pale na niliona jitihada yake kubwa kujenga shule 15 kwa mpigo. Niwaagize tu Halmashauri ya Sengerema kwamba waende sasa hivi huko walipo kuanzia wiki ijao wakague na watuletee taarifa Ofisi ya Rais, TAMISEMI, kama maeneo haya yanakidhi vigezo ya kuanzishwa kidato cha tano na cha sita na kwa sababu tunaile programu yetu ya kuzipanua shule 100 kwa ajili ya kuziongezea madarasa na miundombinu ili kuzifanya kuwa kidato cha tano na cha sita. Kwa hiyo, tutazingatia katika ule mpango ili tuone tunaweza tutaongeza shule ngapi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini la pili kwamba Mheshimiwa Waziri alifika kule na aliahidi nimwambie tu kabisa kwamba najua alifika shule eneo la Sengerema na aliahidi kutoa baadhi ya vitanda kuhakikisha kwamba tunaongeza idadi ya wanafunzi ama waweze kupata malazi bora. Kwa hiyo, ahadi ile ipo pale pale na itatekelezeka kama ambavyo Mheshimiwa Waziri alikuwa ameahidi na nikuhakikishie tu kwamba shule zote ambazo zitakidhi vigezo basi tutaziingiza katika mpango. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. TABASAM H. MWAGAO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Nasema usajili wa shule zetu, shule za msingi, sekondari na hadi vyuo vya kati hivi kama VETA, kumekuwa na masharti magumu sana katika Wizara ya Elimu. Kinachonishangaza hata shule za Serikali na zenyewe zinawekewa masharti magumu kupita kiasi, inatufanya sisi Wabunge ambao tuko vijijini huku wananchi wetu wanataka elimu, lakini tunapata zuwio kutoka katika Wizara ya Elimu.

Je, nini mpango wa Wizara ya Elimu kurahisisha usajili ili watu wengi waweze kusajili vyuo, kusajili shule zetu za msingi na sekondari? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Tabasam, Mbunge wa Sengerema, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Tabasam anazungumzia suala la usajili. Niwatoe wasiwasi Waheshimiwa Wabunge, suala la usajili wa shule au taasisi hizi, linaanzia kule ambako shule ipo. Tuna watumishi wetu, wataalam wetu ambao wako kwenye maeneo hayo katika wilaya ambao wanakwenda kufanya ukaguzi kwenye maeneo hayo. Baada ya ukaguzi huo mara nyingi sana huwa wanaandika taarifa, ili kuweza kuangalia ile miundombinu wezeshi kwa ajili ya kuanza kutoa elimu kama imefikiwa, basi tuweze kufanya hivyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimtoe wasiwasi vile vile Mheshimiwa tabasam, hivi sasa Wizara iko mbioni kuhakikisha inakamilisha mfumo wa kufanya usajili kwa kupitia mfumo badala ya huu wa sasa wa kutumia makaratasi. Katika mfumo huo tunadhani vitu vingi sana vitakuwa ni rahisi na vyepesi na vitaondoa sana manung’uniko na mizunguko ile ambayo ilikuwa haina tija.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, katika kipindi hiki kifupi, tuendelee tu kuchukua hili wazo lake, lakini nimtoe wasiwasi, nakumbuka jana tulionana na nikamwambia leo tuonane tuweze kuangalia hayo maeneo yake ambayo anaona yana changamoto, lakini utaratibu kimsingi uko hivyo ni vitu tu vya kufuata utaratibu na fomu zile za kujaza. Tunaangalia zile requirements au yale mahitaji muhimu kwa ajili ya kuanza kutoa elimu kwa sababu, hatuwezi tu kusajili shule kwa sababu iko chini ya mti, ni lazima taratibu na miundombinu wezeshi iwepo. Hata hivyo, tunabeba wazo lake, tutakwenda kufanya maboresho kwenye eneo hili, lakini kwa vile mfumo unakwenda kuanza kufanya kazi, tunaamini maeneo mengi yatakwenda kuboreshwa. Ahsante sana.
MHE. TABASAM H. MWAGAO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Kwa kuwa Mkandarasi huyu alipewa kazi hii toka mwaka jana Mei, 2021 na kazi yenye ilikuwa ni sehemu ya kutengeneza mwalo wa kupokelea samaki pamoja na vipimo vya samaki, hauoni sasa muda tayari umeshafika zaidi ya mwaka mmoja na miezi minne, ni lini sasa kazi hiyo ya ujenzi wa banda hilo utakamilika? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili la nyongeza ni kwamba, Mheshimiwa Naibu Waziri alifika katika eneo hilo la mradi na pamoja na kutembelea eneo hilo alikwenda pia kuangalia mabwawa ya kunyweshea mifugo katika Jimbo la Sengerema, lakini mpaka leo hii mabwawa hayo hayajapata fedha. Je, ni lini fedha zitaletwa kwa ajili ya kuyaziba mabwawa tisa yaliyopasuka katika Jimbo la Sengerema?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali ya nyongeza ya Mheshimiwa Tabasamu, Mbunge wa Sengerema, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, utaratibu wa kukamilisha unafanyika kwa haraka mara baada ya kuvunja mkataba, hivi sasa wataalam wetu wapo kazini kuhakikisha kwamba kazi ile ya wananchi inakamilika ili waweze kupata huduma wanayostahiki.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili anataka kujua juu ya mabwawa yake lini yatapata fedha. Tayari kwa utaratibu wa Sheria ya Manunuzi tumekwishatangaza tenda na tupo katika hatua ya kupata wakandarasi na hatimaye yale yaliyopangiwa kwenye jimbo lake yatapata fedha na wakandarasi watatekeleza kazi yake.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimshukuru Mheshimiwa Tabasabu kwa ushirikiano mkubwa anaotupatia, ahsante sana.
MHE. TABASAM H. MWAGAO: Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza; kwa kuwa barabara ile inaunganisha na barabara ya Sengerema- Ngoma, je ni lini itafanyiwa usanifu?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, barabara ya Sengerema- Kamanga imeshafanyiwa usanifu, leo ni miaka mitatu; je, ni lini itajengwa kwa lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Tabasam Mbunge wa Sengerema kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara ya Sengerema- Ngoma haijafanyiwa upembuzi yakinifu na usanifu wa kina na ipo kwenye Ilani. Tumemwagiza meneja wa Mkoa wa Mwanza aweze kuangalia kama kutapatikana fedha yoyote kwenye fedha ya maendeleo basi aielekeze kufanya usanifu wa barabara hii kwa sababu ni barabara fupi sana. Na barabara ya Sengerema – Kamanga Serikali inatafuta fedha kwa ajili ya kuijenga kwa kiwango cha lami. Ahsante.
MHE. TABASAM H. MWAGAO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Sengerema kuna mradi wa maji ambao unasubiri kuwekwa kwenye tangazo kwa ajili ya tender. Hili jambo limechukuwa muda mrefu sana. Sijui Waziri anasemaje mradi wa Kata ya Mabiru, katika Kata ya Igalula? Ni mradi wa siku nyingi.
WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, miradi ya maji pamoja na ujenzi wake unakuwa na taratibu zake, hasa katika eneo la manunuzi. Nataka nimhakikishie, tunakamilisha hizi taratibu, lakini huu ni mradi mkubwa na nimhakikishie, saini yake nitaishuhudia mimi mwenyewe pale Sengerema. Ahsante sana.
MHE. TABASAM H. MWAGAO: Mheshimiwa Spika, pamoja na Serikali kuwa tayari kuhamisha makundi hayo ya tumbili hao katika Kisiwa cha Juma, lakini bado kuna tatizo la mamba katika mialo yetu hasa mwalo wa Buyagu, Irunda pamoja na Rugongo.

Je, Serikali ipo tayari kutujengea vizimba kwa ajili ya kuondoa huo usumbufu?

Mheshimiwa Spika, swali la pili ni kwamba tunalo eneo katika Wilaya ya Sengerema kule kwa mwenzangu Ndugu yangu Eric Shigongo tunaeneo la Kichangani ambalo linatumika kwa ajili ya uvuvi. Jimbo la Sengerema linapata samaki kutoka katika eneo hilo.

Je, Serikali iko tayari kutuachia lile eneo likaondoka katika game reserve kwa sababu linatoa usumbufu watu walioko pale wanalipa kama wako nchi nyingine?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Tabasam Hamis Mwagao Mbunge wa Sengerema kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli kumekuwa na tatizo la mamba na si sehemu ya Sengerema peke yake, ni maeneo mengi ambayo yana mito na maziwa na Serikali imeendelea kujenga vizimba vya mfano. Lakini tunaelekeza pia Serikali za Mitaa tushirikiane nao ili kuhakikisha maeneo haya tunayaimarisha vizuri na wananchi waweze kupata huduma bora ya maji na pia tutashirikiana na Wizara ya Maji ili kuona kwamba wananchi wanaweza kupata maeneo mazuri ya kuchota maji badala ya kutumia maeneo ambayo yanawanyama wakali na waharibifu hususani mamba.

Mheshimiwa Spika, swali lingine ameongelea kuhusu eneo la Kichangani; eneo hilo liko katikati ya pori ambapo ni hifadhi na tuliweza kuwaruhusu wavuvi waweze kulitumia kwa utaratibu maalum kwa sababu tunatunza mazalia ya samaki na uhifadhi mbalimbali, hivyo nimtaarifu Mheshimiwa Mbunge na wananchi kwamba eneo hili liko purposely kwa ajili ya uhifadhi.
MHE. TABASAM H. MWAGAO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Mheshimiwa Waziri ni kwamba hali ya gari la Sengerema anajua mpaka Mheshimiwa Simbachawene aliniahidi mwaka jana tutapata gari jipya. Sasa haya magari yanayokuja mwezi huu unanihakikishia gari moja linakwenda Sengerema kwa sababu hali iliyopo ni mbaya. (Makofi)
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa
Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Tabasam Mbunge wa Sengerema kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kama mwongozo wako ulivyoutoa na kama ambavyo nimejibu nyuma kwamba tutapeleka magari haya kulingana na uhitaji zaidi, kwa hiyo tutaangalia kama Jimbo la Sengerema limeangukia katika eneo hilo atapata kama itabidi asubiri basi atapata siku za mbele pale ambapo yatapatikana magari ya ziada.
MHE. TABASAM H. MWAGAO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Naomba kuuliza swali la nyongeza kwa Mheshimiwa Naibu Waziri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Naibu Waziri ulikuja Sengerema nikaalika mkutano mkubwa sana na ukaahidi katika kituo cha Busisi kukipa vifaa, leo mwaka unakwisha unaniandalia kitu gani huko Jimboni kwangu. Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimjibu Kaka yangu Mheshimiwa Tabasam ni kweli nimekwenda kwenye eneo husika, tulifanya pamoja naye mkutano wa wananchi na tuliahidi mbele ya wananchi, nikuhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba kwa kushirikiana na wenzangu wa TAMISEMI, tayari Kituo cha Afya cha Busisi kipo kwenye maombi ya dharura ambayo sasa yanaenda kutekelezwa mwaka huu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo tayari imeshaingizwa kwenye mpango na fedha zinaenda kupelekwa kwa ajili ya kufanya kazi tuliyokubaliana siku ile kwenye mkutano. (Makofi)
MHE. TABASAM H. MWAGAO: Mheshimiwa Spika, nikushukuru. Ni kwamba Sengerema inazo skimu Tano, katika hizi skimu Tano skimu Mbili ndiyo zimepata fedha. Sasa, nataka kupata majibu ya Serikali skimu Tatu zilizobakia; Je, lini zitapata fedha kwa ajili ya kufanya usanifu?

Swali la pili, Sengerema tunao Ushirika wetu wa Nyanza ambako kuna viwanda vitatu viko katika Wilaya ya Sengerema. Hatujawahi ku-gin pamba leo ni miaka 20.

Je, Wizara ina mpango gani kuhusiana na Ushirika katika Wilaya ya Sengerema? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ahsante.
WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, kwanza nitumie nafasi hii kumwambia Mheshimiwa Mbunge na wananchi wa Sengerema kwamba mwaka ujao wa fedha tunajenga skimu mbili katika Wilaya ya Sengerema. Vilevile, tutatenga fedha zaidi ya Shilingi Milioni 300 kwa ajili ya kufanya usanifu kwenye skimu zilizobaki, ambazo zitatengewa fedha mwaka unaofuatia. Kwa sababu, hatuwezi kujenga skimu zote tano, kwa wakati mmoja. Kuhusu suala la Ushirika nataka nitumie nafasi hii na ninapongeza baadhi ya Vyama vya Ushirika katika nchi yetu ambavyo vimeweza kufufua ginneries. Chama Kikuu cha Ushirika cha Nyanza kwa mwaka huu tumekubaliana Nyanza na Tanzania Agricultural Development Bank na sasa hivi ninavyoongea TADB wanafanya survey Nyanza, wanafanya survey SIMCU, wanafanya survey SHIRECU kwa ajili ya kufufua ginnery za vyama hivi vitatu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tumeona kwamba mfumo huu wa kuwa na ginnery zinazomilikiwa na Vyama vya Ushirika na Vyama vya Ushirika kuwa na kampuni zao narudia. Vyama vya Ushirika kuwa na kampuni zao ambazo zinaingia kwenda kununua pamba kuongeza ushindani inamsaidia mkulima.

Mheshimiwa Spika, nimuahidi tu Mheshimiwa Mbunge kwamba, baada ya survey ya TADB katika ginnery za Chama Kikuu cha Ushirika cha Nyanza, tutakutaarifu kwamba ni ginnery gani ya Nyanza inafufuliwa sasa hivi. (Makofi)
MHE. TABASAM H. MWAGAO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru, kwa kuwa Sengerema ni sehemu ambayo ni ng’ambo ya Mwanza na tuna gari dogo sana ambalo lina uwezo wa kuchukua maji lita 500.

Je, Serikali iko tayari kutubadilishia tupate gari kubwa kwa sababu tuna-cover eneo kubwa mpaka Geita, ukichukua Buchosa na sasa hivi tuna mgodi?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba Sengerema inachukua eneo kubwa, lakini angalau wao wanalo gari moja japo dogo wengine hawana kabisa. Kwa hiyo, tutaendelea kuimarisha uwezo wetu ili baadaye Wilaya zote zikishapata then tutaingia uwezo wa kuongezea Wilaya ambazo zina magari madogo kama hayo.
MHE. TABASAM H. MWAGAO: Mheshimiwa Spika, katika miradi ya maji ambayo iliyoko katika maeneo yetu tunao mradi mkubwa wa maji eneo la Nyasibu, Mbungo, Ngoma ambao na wenyewe umekaa kwa muda mrefu nini majibu ya Serikali ili mradi huo uanze kama ulivyopangwa?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge Tabasamu kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, mradi huu wa Nyasibu tayari tumeshawaagiza vijana wetu waweze kuona namna ya kuweza kuuendeleza Mheshimiwa Mbunge baada ya hapa tuonane tuweke vizuri ili suala kwa sababu huu mradi ni muhimu wote tunafahamu.
MHE. TABASAM H. MWAGAO: Mheshimiwa Spika, barabara ya Kamanga – Sengerema imetangazwa kwa ajili ya ujenzi wa lami;

Je, ni lini mkandarasi atakuwa site kwa ajili ya kuanza kazi ya ujenzi wa Barabara ya Kamanga – Sengerema?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, utekelezaji wa barabara hiyo ni kwa mwaka huu kwa hiyo taratibu zinaendelea, zikishakamilika barabara hiyo itatangazwa kuanza kujengwa, ahsante.
MHE. TABASAM H. MWAGAO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru.

Mheshimiwa Spika, barabara ya Busisi – Sengerema hadi Igaka boarder ambayo inajengwa kwa barabara nne kwa kiwango cha lami. Lini kazi hiyo ya usanifu itaanza kufanyika maana yake toka imesemwa toka mwezi wa sita mpaka leo hatujamuona mkandarasi akifanya designing?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, tukishafanya usanifu kinachofuata ni kutafuta fedha kwa ajili ya kuanza huo ujenzi. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwa kuwa Serikali imeshatoa commitment kwanza kufanya usanifu, basi hatua inayofuata itakuwa ni kujenga hiyo barabara kama ilivyosanifiwa. Kwa hiyo, mpango huo upo, hela zikishapatikana tutaanza kuijenga hiyo Barabara. Ahsante.

MHE. TABASAM H. MWAGAO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Sengerema kuna mitambo imewekwa kwa ajili ya kuchimba visima na visima vilivyochimbwa ni vitano kati ya visima 38. Nini kauli ya Serikali kuhusiana na mitambo hiyo kukaa leo mwezi wa pili iko Sengerema na visima havichimbwi?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Tabasam, Mbunge wa Sengerema, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, mitambo hii tumeisambaza mikoa yote na Mkoa wa Mwanza ni mnufaika kwa mitambo ambayo iko Sengerema ilikuwa na michakato inafanyika ili kuona tunaendelea kutenda kazi na nikuhakikishie Mheshimiwa Mbunge mara baada ya Bunge hili kazi zitaendelea na mitambo ile itamaliza visima 38 na kuhamia wilaya nyingine.

MHE. TABASAM H. MWAGAO: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi na mimi kuuliza swali la nyongeza na ni kwamba zimebakia siku nane leo kabla ya mwaka wa Serikali kuisha na Serikali ilikuwa imetueleza kwamba Sengerema tutafanya usanifu barabara ya Sengerema - Ngoma na Busisi - Ngoma kwa ajili ya lami kwenda Nyangh’wale na zimebakia siku nane hatujaona mkandarasi, Nini kauli ya Serikali Mheshimiwa Waziri?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, ni kweli barabara hii kwa sababu inaunganisha mikoa miwili wa Geita na Sengerema Mkoa wa Geita na Mkoa wa Mwanza sehemu kubwa inasimamiwa na Makao Makuu ya TANROADS ninataka nimuhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba tayari Mhandisi Mshauri ameshapatikana kwa ajili ya kuanza kazi hii ya usanifu wa hii barabara.

MHE. TABASAM H. MWAGAO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru, kwa kuwa Wilaya ya Kwimba ndiyo Wilaya pekee katika Mkoa wa Mwanza ambayo haijaunganishwa kwa barabara ya lami na Makao Makao Makuu ya Mkoa wa Mwanza, na Wilaya Kwimba ni miongoni ya Wilaya kongwe imeanzishwa toka mwaka 1935. Sasa angalia mpaka muda huu haijawahi kuunganishwa na barabara ya lami.

Je, ni lini Serikali itakamilisha kilomita 25 za kutoka Mwabuki kwenda Ngudu mjini ili Wananchi wa Wilaya ya Kwimba waweze kuungana na Mkoa wa Mwanza?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la nyongeza la pili ni kwamba, kwa kuwa barabara yetu ya Mwabuki, inaunganisha pamoja pamoja na Barabara ya Malampaka – Maswa ambayo ni katika Mkoa wa Simiyu na barabara hiyo ni ndefu inakwenda mpaka Singida. Je, ni lini Serikali sasa itakamilisha ujenzi wa barabara hiyo? kwa sababu ya kupunguza traffic kubwa kati ya Mwanza na Singida kwa njia ya shortcut ya kupitia Maswa, Meatu pamoja na Singida, ahsante. (Makofi)
WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nijibu maswali mawili ya nyongeza yaliyoulizwa na Mheshimiwa Tabasam, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, cha kwanza kama nilivyojibu kwenye majibu yangu ya msingi. Tunajenga hizi kilomita 28 na tumeanza na kilomita tatu, kuanzia Ngudu ambako ndiyo Makao Makuu ya Wilaya lakini vilevile kwa Barabara ya Magu – Ngudu tumeanza kujenga kilomita 10 kutoka Magu kwenda Ngudu. Kwa hiyo mtandao huu utaunganisha Wilaya ya Kwimba na Mwanza kwa maana ya Mwanza mjini, kwa hiyo nimwombe Mheshimiwa Tabasam na Mheshimiwa Mansoor kwamba maendeleo ni hatua tumeanza hivyo lakini nia ni kuiunganisha Wilaya ya Kwimba pamoja na Mwanza, kwa maana ya Mwanza mjini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini vilevile kuhusu swali la pili Mwabuki - Maswa; sasa hivi Serikali ipo kwenye Miradi saba ya EPC+F ipo barabara yenye kilomita 389 ambayo inaanzia Mbulu kuja Manyara, Singida mpaka Maswa. Barabara hii inaenda kuunganisha Mikoa ya Kaskazini pamoja na Kanda ya Ziwa na ikishafika pale Maswa na mitandao hii ambayo nimeitaja tutakuwa tumeunganisha mikoa ya Mwanza, Simiyu, Singida na Mikoa ya Kaskazini, ahsante sana. (Makofi)
MHE. TABASAM H. MWAGAO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru.

Mheshimiwa Spika, ni kwamba kwa kuwa viwanda vya Nyakarilo, Buyagu na Nyamirilo havifanyi kazi leo, takribani miaka 21. Huu mpango unaopangwa na Serikali hauoni kama ndio unafifisha zao letu la pamba kwa kuwa Chama Cha Mapinduzi katika Ilani yake imesema ya mwaka 2025 tunakwenda kuzalisha pamba tani milioni moja na tutaboresha viwanda. Leo tunakwenda mwaka wa tatu hakuna kiwanda chochote katika Wilaya ya Sengerema kilichoboreshwa.

Mheshimiwa Spika, haoni kwamba Serikali tayari tena ina mpango wa kupingana na Ilani ya Chama Cha Mapinduzi? Swali la kwanza.

Mheshimiwa Spika, swali letu la pili ni kwamba kwa kuwa, viwanda hivi vipo na vinasimamiwa na vyama vya ushirika chini ya Wizara ya Kilimo na ninyi Wizara ya Viwanda ni sehemu ya Serikali. Mko tayari kufuatana na mimi kwenda Sengerema kukagua hivyo viwanda na kuwaeleza wananchi, lini mtaviboresha?
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana, ni kweli kabisa kwamba, kumekuwa na changamoto katika sekta ya viwanda hasa viwanda vya pamba katika maeneo mengi kwamba ni viwanda vya siku nyingi na hivyo vimechakaa, na kama alivyosema Mheshimiwa Tabasam, ni kweli Serikali imeshaweka mkakati maalum.

Mheshimiwa Spika, kwanza changamoto iliyokuwepo kabla ilikuwa ni changamoto ya malighafi kwenye viwanda ambavyo vinafanya kazi, lakini sasa kwa sababu ya uzalishaji mkubwa ambao Mheshimiwa Rais ameshaweka fedha nyingi kwenye sekta ya kilimo, tunaamini kweli kutakuwa na uzalishaji mkubwa kulingana na Ilani ya Chama Cha Mapinduzi ambayo sasa pamba hii inatakiwa kulishwa kwenye viwanda vyetu.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, sisi kama Wizara ya Viwanda na Biashara, lakini kwa kushirikiana na Wizara ya Kilimo tutahakikisha tunapitia na kuona viwanda hivi viaenda kufufuliwa na kufanya kazi.

Mheshimiwa Spika, lakini kuhusu ziara, ni kweli nitafanya ziara ili nijionee na mimi kama Wizara ya Viwanda tunaoratibu viwanda, lakini kwa kushirikiana na Wizara ya Kilimo, ili tuhakikishe sasa mkakati tuliouweka wa kupata mitaji kupitia Benki ya Kilimo, viwanda hivi viweze kufufuliwa ili wananchi wa Sengerema na wengine wanaofanya kazi waweze kunufaika na uwepo wa viwanda hivi, lakini pia kuchochea kilimo cha pamba, nakushukuru.
MHE. TABASAM H. MWAGAO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru, kwa kuwa Wilaya ya Kwimba ndiyo Wilaya pekee katika Mkoa wa Mwanza ambayo haijaunganishwa kwa barabara ya lami na Makao Makao Makuu ya Mkoa wa Mwanza, na Wilaya Kwimba ni miongoni ya Wilaya kongwe imeanzishwa toka mwaka 1935. Sasa angalia mpaka muda huu haijawahi kuunganishwa na barabara ya lami.

Je, ni lini Serikali itakamilisha kilomita 25 za kutoka Mwabuki kwenda Ngudu mjini ili Wananchi wa Wilaya ya Kwimba waweze kuungana na Mkoa wa Mwanza?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la nyongeza la pili ni kwamba, kwa kuwa barabara yetu ya Mwabuki, inaunganisha pamoja pamoja na Barabara ya Malampaka – Maswa ambayo ni katika Mkoa wa Simiyu na barabara hiyo ni ndefu inakwenda mpaka Singida. Je, ni lini Serikali sasa itakamilisha ujenzi wa barabara hiyo? kwa sababu ya kupunguza traffic kubwa kati ya Mwanza na Singida kwa njia ya shortcut ya kupitia Maswa, Meatu pamoja na Singida, ahsante. (Makofi)
WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nijibu maswali mawili ya nyongeza yaliyoulizwa na Mheshimiwa Tabasam, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, cha kwanza kama nilivyojibu kwenye majibu yangu ya msingi. Tunajenga hizi kilomita 28 na tumeanza na kilomita tatu, kuanzia Ngudu ambako ndiyo Makao Makuu ya Wilaya lakini vilevile kwa Barabara ya Magu – Ngudu tumeanza kujenga kilomita 10 kutoka Magu kwenda Ngudu. Kwa hiyo mtandao huu utaunganisha Wilaya ya Kwimba na Mwanza kwa maana ya Mwanza mjini, kwa hiyo nimwombe Mheshimiwa Tabasam na Mheshimiwa Mansoor kwamba maendeleo ni hatua tumeanza hivyo lakini nia ni kuiunganisha Wilaya ya Kwimba pamoja na Mwanza, kwa maana ya Mwanza mjini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini vilevile kuhusu swali la pili Mwabuki - Maswa; sasa hivi Serikali ipo kwenye Miradi saba ya EPC+F ipo barabara yenye kilomita 389 ambayo inaanzia Mbulu kuja Manyara, Singida mpaka Maswa. Barabara hii inaenda kuunganisha Mikoa ya Kaskazini pamoja na Kanda ya Ziwa na ikishafika pale Maswa na mitandao hii ambayo nimeitaja tutakuwa tumeunganisha mikoa ya Mwanza, Simiyu, Singida na Mikoa ya Kaskazini, ahsante sana. (Makofi)