Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Tabasamu Hamisi Hussein Mwagao (4 total)

MHE. ERIC J. SHIGONGO K.n.y. MHE. TABASAM H. MWAGAO aliuliza: -

(a) Je, ni lini Jimbo la Sengerema litapata Kivuko kipya angalau kimoja kati ya vivuko vitano ambavyo Serikali imepanga kujenga katika Ziwa Victoria kwa bajeti ya mwaka 2021-2022?

(b) Je, Serikali inafahamu adha ya usafiri wanayoipata wananchi wa Mji Mdogo wa Buyagu Wilayani Sengerema pamoja na wananchi wa Wilaya za Misungwi na Nyang’hwale kwa kukosa chombo madhubuti cha usafiri wa majini?
MHE. NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. MWITA M. WAITARA) alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Tabasam Hamisi Mwagao, Mbunge wa Sengerema, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo: -

(a) Katika mwaka wa fedha 2021/2022 Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi imepanga kufanya upembuzi yakinifu ili kubaini aina na ukubwa wa kivuko kinachohitajika katika eneo hilo. Mara baada ya kukamilika kwa upembuzi yakinifu na gharama za kivuko hicho kujulikana, Serikali itatenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa kivuko kipya katika Jimbo la Sengerema kwa mwaka wa fedha 2022/2023.

(b) Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imepokea changamoto ya adha ya usafiri iliyowasilishwa na Mheshimiwa Mbunge. Wizara yangu katika mwaka wa fedha 2021/2022 itatumia wataalam kufanya upembuzi yakinifu katika eneo la Buyagu Wilaya ya Sengerema na Nyang’wale Wilaya ya Misungwi. Upembuzi yakinifu huo utasaidia kubaini aina na ukubwa wa kivuko kinachofaa ili kiwekwe kwenye mpango wa utekelezaji katika mwaka wa fedha 2022/2023. Ahsante.
MHE. TABASAM H. MWAGAO aliuliza: -

Je, mpango wa kuzipandisha hadhi Sekondari za Ngweli, Ngoma A, Tamabu, Nyamatongo, Sima, Nyampande na Katunguru kuwa za Kidato cha Tano na Sita Wilayani Sengerema umefikia wapi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Tabasam Hamis Mwagao Mbunge wa Jimbo la Sengerema, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa spika, kabla ya shule kusajiliwa Kidato cha Tano na Sita inatakiwa kuwa na miundombinu ya msingi kwa ajili ya kupokea wanafunzi. Jukumu la ujenzi wa miundombinu hiyo si la Serikali kuu tu bali ni la halmashauri kupitia mapato yake ya ndani pamoja na wadau wa elimu na jamii nzima kwa ujumla.

Mheshimiwa Spika, namshauri Mheshimiwa Mbunge ashirikiane na Mkurugenzi wa Halmashuri ya Wilaya Sengerema na kuwasiliana na Ofisi ya Uthibiti Ubora kufanya tathmini katika Shule za Sekondari za Ngweli, Ngoma A, Tamabu, Nyamatongo, Sima, Nyampande na Katunguru ili kujiridhisha na hali ya miundombinu ya msingi kwa ajili ya kupokea wanafunzi wa Kidato cha Tano na Sita.

Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kujenga miundombinu katika baadhi ya shule zilizopendekezwa kuanzisha Kidato cha Tano na Sita kwa kuzingatia upatikanaji wa fedha ili kuongeza fursa ya Elimu.
MHE. TABASAM H. MWAGAO aliuliza: -

Je, ni lini ujenzi wa banda la ukaguzi na kupokea samaki wabichi katika Kata ya Chifunfu utakamilika?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Tabasam Hamis Mwagao, Mbunge wa Sengerema, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, ujenzi wa banda la kupokelea samaki Chifunfu uliopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Sengerema ulianza mwezi Mei, 2021 chini ya Mkandarasi M/S Fast Construction Company Limited ya Mkoani Mwanza kwa thamani ya shilingi 124,592,064.00 ambapo hadi sasa ujenzi umefikia hatua ya kuezeka na Mkandarasi ameshalipwa kiasi cha shilingi 95,768,193.00.

Mheshimiwa Naibu Spika, kazi ya ujenzi wa banda hilo ilipangwa kukamilika ndani ya kipindi cha miezi sita, hata hivyo Mkandarasi hakuweza kukamilisha kazi hiyo kwa mujibu wa mkataba, hivyo Serikali imechukua hatua za kusitisha Mkataba wa Mkandarasi huyo na hatua zingine za kisheria zinaendelea dhidi yake.
MHE. TABASAM H. MWAGAO aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itawavuna tumbili katika Kisiwa cha Juma Wilayani Sengerema ambao wanakula mazao ya wananchi?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Maliasili na Utalii ninaomba kujibu swali la Mheshimiwa Tabasam Hamis Mwagao, Mbunge wa Jimbo la Sengerema kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali imefanya kazi ya kuyabaini na kuyadhibiti makundi (familia) ya tumbili yanayosumbua wananchi katika Kisiwa cha Juma, Wilayani Sengerema. Aidha, Serikali itaendelea kuhamisha makundi hayo na kuyapeleka katika hifadhi nyingine zenye mahitaji ya wanyamapori hao. Wizara itaendelea kuimarisha doria za kudhibiti wanyamapori waharibifu wakiwemo tumbili na nyani.