Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Tabasamu Hamisi Hussein Mwagao (3 total)

Hotuba ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyoitoa wakati wa Ufunguzi wa Bunge la Kumi na Mbili, Tarehe 13 Novemba, 2020
MHE. HAMIS H. T. MWAGAO: Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya wananchi wa Jimbo la Sengerema, naunga mkono hoja.

Mheshimiwa Spika, hotuba hii ya Mheshimiwa Rais ni miongoni mwa hotuba tamu sana katika nchi hii. Hizi hotuba za kishujaa hazitakiwi kuachwa bila kujadiliwa wala kusifiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Rais ameonesha ushujaa mkubwa sana ndani ya miaka mitano. Nimeangalia hotuba ya miaka mitano, nikaangalia na hotuba hii aliyoitoa juzi anafungua Bunge la Kumi na Mbili, mimi binafsi naunga mkono hoja kwa asilimia 100. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nizungumzie kuhusiana na suala la mifugo. Katika mifugo Mheshimiwa Rais amesema kwamba wafugaji katika nchi hii sasa wana nafasi kubwa ya kupewa maeneo ya kupata vitalu, lakini waandaliwe sera nzuri kwa ajili ya kuacha kwenda kuchunga mifugo kwa aina ya zamani sana. Leo wafugaji wanatembea kuchunga wakati tunayo ardhi kubwa ya kutosha tungeweza kuzalisha nyasi, tunayo mabua ya mahindi yanapatikana kila mkoa, kwa nini wasitengeneze sera nzuri kwa ajili ya mifugo yetu?

Mheshimiwa Spika, leo wafugaji wanahamishwa kama hawapo kwenye nchi yao. Kila siku kesi zinakuwa nyingi, ukiangalia taarifa ya habari ni migogoro mikubwa ya wafugaji. Katika hili kama utaandaliwa mfumo mzuri sisi pamoja na kuwa nchi ya pili kwa ufugaji katika Afrika, tutakuwa nchi ya kwanza.

Mheshimiwa Spika, lakini la pili kwenye hili suala la nyama, wananchi wa Tanzania hawajahamasishwa kula nyama. Mwananchi mmoja anatakiwa kwa kiwango cha chini ale kilo, ana hali mbaya nusu kilo, lakini akila hata robo kilo tu soko la nyama peke yake halitoshi katika nchi hii. Sisi wenyewe tunakuwa ni soko kubwa sana la nyama, kwanza tuanze kula sisi nyama. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuhusiana na suala la maeneo haya ya malisho. Ni kwamba wakikata vitalu na hawa wafugaji wakapewa maeneo ya kwenda kuchunga kwanza ni walipaji wazuri kwa wakati. Leo katika nchi hii mifugo imeenea nchi nzima na miongoni mwa wafugaji ambao wanapata tabu, lazima tuwe wakweli, ni Wasukuma na Wamasai. Tumekuwa tunakwenda kila kona unahamishwa unaondoka, sasa hii imekuwa ni hatari. Kwenye hotuba hii tunakwenda katika uchumi wa kati, nafikiri Waziri wa Mifugo na Waziri wa Sheria waliangalie jambo hili tuwe huru katika nchi yetu katika suala la mifugo.

Mheshimiwa Spika, sasa niende upande wa kilimo cha pamba. Nchi hii pamba inalimwa katika mikoa 11. Katika Ilani yetu ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi na Mheshimiwa Rais ametembea nayo katika kampeni, anasema tunahitaji kuzalisha tani milioni moja, tuna uhakika wa kuzalisha zaidi ya tani milioni tatu lakini ni kama pamba itaokolewa na Serikali kwa dhamira ya kweli.

Mheshimiwa Spika, Kwa mfano, kama tumeweza kuokoa Shirika letu la Ndege leo liko hai kwa nini tusiokoe pamba yetu ya Tanzania kwa mambo matatu tu? Jambo la kwanza ni kwamba pamba hii ya nchi yetu itumike kwenye kuzalisha nyuzi na kutengeneza nguo katika nchi hii. Serikali inunue viwanda vya nyuzi na nguo halafu uone kama kilo moja ya pamba haitauzwa Sh.2,000 mpaka Sh.5,000 kwa kilo. Hii nguo niliyovaa mimi leo inauzwa Sh.170,000 au Sh.150,000 ukipata kwa gharama nafuu wakati haina robo kilo ya pamba. Sasa tunaonekana watu wa ajabu, ni lazima tumsaidie Mheshimiwa Rais na tuweke dhamira ya kweli, hilo ni la kwanza.

Mheshimiwa Spika, la pili, ni kupiga marufuku kuuza pamba kwa robota, kwa sababu uuzaji huu wa pamba wa robota unaifanya nchi hii inakuwa mtumwa, wanatuchezea katika maeneo makuu. Wanatuchezea katika mbegu, tunazo nchi zinazolima pamba katika Afrika; Burkina Faso ukiangalia Mali, Sudan, Misri, Zimbabwe na ukiwaona wenzetu Waganda leo wanakwenda kuchukua pamba ya Msumbiji wanasema ni miongoni mwa pamba bora katika Bara la Afrika hii yote ni kutuchezea akili, lakini kama tutakuwa tuna viwanda vyetu hatuwezi kuulizwa hilo jambo kwasababu pamba ni kilimo cha mabepari.

Mheshimiwa Spika, mbegu katika nchi hii hivi viwanda vya pamba vilivyopo huwezi ukailinda mbegu, unaweza ukatoa maelekezo kwamba mbegu ya kupandwa katika nchi hii inalimwa Igunga…

(Hapa kengele ya kwanza ililia)

MHE. HAMIS H. T. MWAGAO: Hii kengele na yenyewe tena, basi bwana.

SPIKA: Ya kwanza hiyo.

MHE. HAMIS H. T. MWAGAO: Sawa. Hapa nipo mahali patamu sana basi tu.

Mheshimiwa Spika,suala la mbegu haliwezi kulindwa na wafanyabiashara, suala la mbegu litalindwa na Serikali, lakini suala la pembejeo, mbegu na dawa na pamba ina muda ina timeframe, mwisho wa kupanda mbegu ni tarehe 15 mwezi 12, lakini mbegu inafika Januari, hizi dawa baada ya kupulizia, roho inaniuma muda unakuwa ni mdogo, sijui nifanyeje kuhusiana na suala la pamba. Serikali imerudisha viwanda vyetu vya Nyanza, SHIRECU, halafu tunashindwa kuiokoa pamba, zaidi ya wananchi milioni 16 ndiyo roho yetu.Mheshimiwa Rais tutamsaidiaje katika hili maana yake roho inatuuma, tuokoleeni pamba.

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja.
Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2021/2022 – 2025/2026
MHE. TABASAM H. MWAGAO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Kwa niaba ya wananchi wa Jimbo la Sengerema naomba nichangie Mpango wa Maendeleo uliowasilishwa kwetu leo na Mheshimiwa Mwingulu Nchemba, Waziri wa Fedha.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika Mpango wake aliowasilisha leo sijaona mahali ambapo amezungumzia habari ya zao la pamba. Zao la pamba katika nchi hii linalimwa zaidi ya mikoa 14 na pamba hiyo unayoiona ina uwezo wa kuwa na viwanda vitano. Angalia uchumi mkubwa unaotokana na pamba; pamba ikizalishwa vizuri na ikatafutiwa bei, Serikali ikawekeza katika pamba; na Serikali ilivyojitoa katika kuwekeza katika pamba, wakaachiwa mabepari, zao hili litakuwa limekufa. Kwa nini? Limekufa kwa kupata bei ndogo. Mabepari wameshusha bei. Tusiite wawekezaji, kwa sababu kwenye pamba kule kuna mabepari, zao la pamba likawa limekufa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa tunaiambia Serikali, katika Mpango wake wa miaka mitano, wanafanyaje kulifufua zao la pamba? Serikali ikiwekeza katika zao hili, tutapata viwanda vya pamba, viwanda vya nyuzi, viwanda vya nguo, viwanda vya vyakula vya kuku na mifugo na tutapata mafuta. Haya mafuta ambayo leo mnayaagiza kutoka Malaysia na kwingineko, mnalazimisha mafuta, mafuta, yako kwenye pamba. Huko kote, hizi ni kodi utapata Mheshimiwa Mwigulu Nchemba. Bahati nzuri wewe unatoka kwenye Jimbo ambalo pamba inalimwa. Hebu waonee huruma wananchi wa Iramba, Sengerema wakiwemo na wananchi wengine Tanzania nzima. Njoo na mpango wa pamba. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika pamba ninachotaka kueleza, Mheshimiwa Mwigulu Nchemba utapata kodi, leta sheria tu hapa. Badala ya pamba kutozwa ushuru, njooni na Sheria hapa mchukue hata VAT asilimia kumi na pamba muipe bei ya shilingi 2,000/=. Ekari moja ya pamba ina uwezo wa kutoa tani moja ya pamba. Sasa kama kuna mtu anapata shilingi milioni mbili katika pamba na Serikali ikachukua kodi ya asilimia 10, mkachukua shilingi 200,000/= kwa ekari moja, mikoa inayolima 14: Je, utakuwa na shida gani tena ya pesa hapa Mheshimiwa Mwigulu? Hii miradi yako yote itaisha. Treni ya mwendokasi, sijui kuna Bwawa la Nyerere na la wapi, sisi walimaji wa pamba tu tunatosha kutengeneza kodi ya kufanya kazi hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika hili, kuna suala la Ziwa Victoria, kule ukianzia juu; Tarime kule, ukaenda moja kwa moja mpaka kule Misheni mwisho kabisa, Kanyigo, kuna wananchi wanaokaa mwambao wa Ziwa, hawajatumikishwa katika kilimo cha irrigation. Sisi tukimwagilia, sasa hivi umeme upo, tukopesheni mashine za kumwagilia, wananchi wetu wana uwezo wa kuzalisha kiwango kikubwa cha mazao. Mnataka uchumi gani kama huu uchumi tunauachia wazi?

Mheshimiwa Naibu Spika, leo kwa mfano, kwenye Jimbo langu tu la Sengerema pale, kuna mradi wa maji wa shilingi bilioni 23, unadaiwa deni la umeme la shilingi milioni 300. Umeme unakatwa, mradi wa shilingi bilioni 23 unateswa na shilingi milioni 300. Sasa tunashangaa, hawa ndio wawekezaji? Ndio Watanzania wanaotaka uchumi wa bluu? Unaandaa mradi wa shilingi bilioni 23 na una deni la shilingi milioni 300, halafu ule mradi unakaa haufanyi kazi, unadaiwa shilingi milioni 300! Ni maajabu makubwa sana katika nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri wa Fedha aliangalie sana hili suala katika miradi kama hii. Huu ni mradi mmoja tu wa Sengerema, sijui miradi mingine inayoteswa na vijipesa vidogo kama hivi kwa uwekezaji mkubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna suala la uvuvi. Kule katika uvuvi tuna matatizo makubwa. Sheria za Uvuvi zilizoko kule katika Ziwa Victoria na hatujui Maziwa mengine huko; leo kuna samaki ambao ni wadogo hawakui. Kuna furu, kuna vimote na samaki wa aina nyingi; barara, hizi ni lugha za kienyeji kule. Wao wanajua hawa samaki hawakui, lakini wanakamatwa nao wale Samaki, nyavu zinachomwa moto. Mlikuwa na Kiwanda cha Nyavu, fufueni kiwanda hicho halafu mtengeneze nyavu zinazotakiwa na Serikali, lakini mkiwaacha waagizaji wakaleta nyavu, matokeo yake mnakwenda kuzichoma moto, mnatengeneza umasikini katika Ziwa Victoria. Liangalieni sana hili jambo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hivi tunavyozungumza tunakwenda kufunga mradi. Mgodi wa Buzwagi unafungwa. Sengerema kuna wawekezaji katika Mgodi wa Nyanzaga wameomba kufungua Mgodi wa Nyanzaga; leo ni mwaka wa nne toka mwaka 2017, mnataka wawekezaji gani? Huu mradi unakuja kuzalisha pesa. Uwekezaji wake tu wa kuandaa ule mgodi una shilingi trilioni moja, leo mnataka wawekezaji gani? Kwa sababu tu ule mradi unatakiwa kukua Sengerema watu hawautaki, halafu wanataka kuita wawekezaji. Waje wawekezaji gani wakati wengine mnawakataa? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri wa Fedha aangalie katika Mpango wake wa miaka mitano, tunahitaji Mgodi wa Nyanzaga Sengerema ufunguliwe. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine kuna suala kubwa sana hapa tunalozungumzia la utengenezaji wa barabara. Hizi barabara unazoziona zinakwenda kwa wananchi, ambazo zinatengenezwa na TARURA, nilifikiria sana kwa nini TARURA isirudi ujenzi? Hata hivyo, naangalia kazi waliyonayo watu wa ujenzi; ukiangalia miradi aliyonayo TANROAD na bado ukamwongezee tena mradi mwingine wa TARURA, sishauri TARURA ihame. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nakuomba sana Mheshimiwa TARURA ibakie mahali pake, lakini kuna pesa ziko hapa. Nilizungumza hapa siku moja nikawaambieni, jamani kuna pesa za TARURA, kuna pesa ziko kwenye ukokotoaji wa mafuta, wanakokotoa watu wa EWURA. Shilingi 90/= kila siku ya Mungu wanakusanya katika huu ukokotoaji, hizi fedha zinakwenda kutumika vibaya. Shilingi 1,080,000,000/=. Ukichukua pesa hizi Mheshimiwa Mwigulu, kwa mwezi ni shilingi 32,400,000,000/=; kwa mwaka kunakuwa na fedha hapa zaidi ya shilingi bilioni karibu 400 ambazo zinakwenda kwenye hizi tozo ndogo ndogo.

Mheshimiwa Naibu Spika, hawa walioweka tozo, wote wako kwenye bajeti. Mnakwendaje kuweka kwenye tozo la mafuta? Kule kuna import duty, kuna import levy pale, kuna petrol levy pale; mnakwenda kuweka hivi vitu vingine vya nini? Hii fedha ileteni TARURA tutengeneze barabara zetu. Tunazo Halmashauri za Miji. Halmashauri za Miji tunazo 21, Halmashauri za Wilaya tunazo 137, tunazo Manispaa 20 na Majiji sita, kwa nini TARURA haongezewi fedha hapa za kufanyia kazi? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hata kwa Mheshimiwa Mwigulu juzi nimepita barabara ya Ndago, nimepita Shelui kuzungukia Ndago, hata yeye hana barabara. Nitashangaa sana kama Mheshimiwa Mwigulu hata wewe hutakubali TARURA iongezewe fedha. Hutarudi 2025. Haya maneno nakwambia kabisa, usidhani hatutarudi sisi tu, hata ninyi Mawaziri mtakomea ndani huko huko. Tengenezeni pale TARURA, ipeni pesa za kutosha tutengeneze barabara zetu. (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hata wewe hapo hutarudi kama barabara hizi hazitatengenezwa. Msidhani kwamba hili ni suala ni la Tabasam pekee.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Nafikiri message imekwenda. (Makofi/Kicheko)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Tabasam huu utabiri wako huu! (Kicheko/Makofi)

MHE. TABASAM H. MWAGAO: Ndiyo. Hili ni hatari! (Makofi/Kicheko)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Tabasam.

MHE. TABASAM H. MWAGAO: Mheshimiwa Naibu Spika, angalia dakika zangu lakini.

NAIBU SPIKA: Subiri kwanza Mheshimiwa Tabasam, subiri kidogo.

MHE. TABASAM H. MWAGAO: Ndiyo.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Mwigulu humu ndani ni Senator na mimi nataka kwanza kumkaribia kidogo, lakini sasa wewe ni mgeni kabisa, ukitutabiria sisi kutokurudi humu ndani, nahisi hali yako wewe ni mbaya zaidi kuliko ya kwetu. (Kicheko/Makofi)

Endelea Mheshimiwa, karibu.

MHE. TABASAM H. MWAGAO: Mheshimiwa Naibu Spika, ninachotaka kukwambia, TARURA ni janga la Kitaifa. TARURA, yaani kama ingekuwa nchi nyingine tungekuwa tuna mjadala wa Kitaifa tufanyeje kuhusu TARURA?

Mheshimiwa Naibu Spika, ninachotaka kuwaambieni jamani, Waheshimiwa Wabunge humu ndani, nimewaelezeni kwamba fedha ziko kwenye mafuta. Nikawaambia kwamba, nilimwambia hapa Mheshimiwa Spika, tukae tujadili hili jambo, kuna fedha kule sisi tuwaonyeshe. Hii Habari ya kuwa tu bei za mafuta zinapanda kila mwezi, bado hatuna manufaa nazo hizi fedha, kodi yetu iko pale pale, hili ni jambo ambalo kwenda kwenye uwekezaji, kama Serikali haiwezi kuagiza mafuta yake, ninachotaka kukuambia Mheshimiwa Mwigulu, utatwanga maji kwenye kinu. Haitawezekana nchi yoyote inayotaka uchumi wake isipoweka fedha kwenye kuagiza mafuta yake. Tegemeeni wafanyabiashara waje wawatengenezee nchi, hili jambo halipo hata siku moja. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunazo nchi marafiki nyingi, hili suala la mafuta; tunalo eneo letu la TIPER pale. Lile eneo amepewa mwekezaji ambapo hakuna hata faida yoyote. Tungeenda kutengeneza matenki tukawa na reserve kubwa pale ya lita hata bilioni mbili. Leo mafuta yanakuja kupanda bei katika Soko la Dunia, sisi tunaweza tuka-stabilize pale tukabakia salama. Endeleeni kuudharau huu ushauri ninaowapeni, kwa sababu unatolewa na mtu wa Darasa la Saba katika nchi hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsanteni sana. Mimi nimewasilisha. (Makofi/Kicheko)
Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022
MHE. TABASAM H. MWAGAO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Kwa niaba ya wananchi wa Sengerema naomba ushauri wangu kwa Waziri wa Fedha, Mheshimiwa Mpango. Nimeangalia Mpango wake nimeusoma vizuri uliowakilishwa hapa na Mheshimiwa Mwigulu Nchemba kwa niaba yake, lakini kuna maeneo ambayo nataka nipite katika kuishauri Serikali katika Bunge hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kelele nyingi zimepigwa na Waheshimiwa Wabunge hapa kuhusiana na TARURA, wamezungumza sana kwamba TARURA iongezewe pesa na wengine wamekwenda mbali zaidi wakitaka pesa za kuongeza TARURA zitoke katika mafuta. Sishauri mafuta yaongezwe bei kwa sababu anayeumia ni mwananchi wa chini, mwananchi maskini na mfumuko wa bei utakuwa ni mkubwa sana na sisi tunajitahidi kupunguza mfumuko wa bei. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu kuhusu TARURA; kwa Waziri wa Serikali za Mitaa ni kwamba TARURA wabadilishe mfumo wao kwa hiki kidogo kilichopo. Hawa ma engineer wa TARURA waliopo katika miji, manispaa, majiji na halmashauri zetu wapewe mikataba performance watakayoifanya katika maeneo yao ndiyo itakayowapa nafasi ya kurudi. TANROADS wametoa mikataba kwa ma- engineer wao wa Mikoa na wamefaulu kwa mfumo huo. Haiwezekani meneja wa TARURA anaharibu, anahamishiwa sehemu nyingine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, ushauri wangu pia kwa Waziri Mpango katika Mpango huu aliyenao na kwa Mheshimiwa Waziri Mkuu, hawa TARURA sasa hivi waruhusiwe kufanya kazi za force account, tutaona matokeo yake. Kwa mfano, katika wilaya yangu, halmashauri moja tu, Halmashauri ya Wilaya ya Sengerema, tuna kilometa 1,730, bajeti milioni 607, haiwezekani! Ukichukua kwa bei za TANROADS ambazo zipo za mikoa, kilomita moja inaanzia milioni 15 mpaka milioni 20. Kwa hiyo, milioni 600 inatengeneza kilometa thelathini na una kilometa 1,700, kwa hiyo nahitaji miaka 50, wakati huo nitakuwa nimeshindwa uchaguzi na nimezeeka na nimestaafu. Wabunge wote hakuna atakayerudi kwa mfumo huu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu, TARURA waruhusiwe kununua mitambo na mitambo yenyewe watakayoruhusiwa kununua ni mitambo mitatu tu motor grader moja, roller compactor na roller excavator, vingine vinaweza vikakodiwa. Kwa hiyo, TARURA watatengeneza barabara kwa uzuri, pesa za TARURA zitatoka wapi? Hapa ndipo pazuri, ni kwamba uwagizaji wa mafuta katika nchi hii hapa kuna tatizo kubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati wanapeleka Muswada huu wa kuagiza mafuta kuagiza mafuta kwa pamoja 2014; Muswada huu uliletwa hapa Bungeni kwa zimamoto, mbio mbio, sasa hapa ndiyo kuna tatizo. Kwa mfano, bei ya mafuta ya Januari, bei yake ilikuwa karibu shilingi 230 au 300 kwa lita, lakini bei ambayo imeonekana ipo kwenye kukokotoa kwa EWURA, bei ya mafuta imefika shilingi 708. Katika shilingi 708 ya petrol kuna nauli iko pale shilingi arobaini na tisa na senti. Mafuta yale ya petrol yamefika hapa shilingi 757 wakati bei halisi kwa wakati huo, mwezi Januari wakati yanaagizwa, hayakuzidi shilingi 300. Sasa kama nchi inataka kufanya mageuzi makubwa ya kiuchumi, hatukwepi sasa hivi nchi kuagiza mafuta yetu kama nchi, tuna matenki tipper yana mamilioni ya hifadhi, kwa nini tusinunue mafuta kwa shilingi 300. Katika nchi ambazo zinazouza mafuta nchi za OPEC wananauza mafuta haya kwa discount.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo bei ya mafuta ni dolla 160 kwa tani ambayo ni sawasawa na Sh.370 kwa lita. Kama huyo mwagizaji anayepewa tenda anayafikisha mafuta hapa kwa Sh.708, kuna gape pale karibu ya Sh.300. Hii ni hatari sana kwa uchumi wa nchi, sisi tunalalamika hatuna pesa, halafu tunawachia watu wanaagiza mafuta. Naomba ushauri wangu uzingatiwe katika hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kamati ya Fedha, Mipango na Bajeti na Kamati ya Nishati na Madini, kwa ruhusa yako pamoja na Waziri wa Uwekezaji, tukutane kwa dharura, mimi naomba, tukajadili hili kwa manufaa ya nchi. Pamoja na tozo hizi, kuna pesa ambayo ni excise duty shilingi mia tatu na kitu, kuna pesa ambazo ni levy shilingi mia tatu na sabini karibu, kuna fedha ya petrol fees shilingi mia moja. Hizi ndiyo pesa zinazokwenda Hazina, zaidi ya shilingi mia saba, lakini kuna tozo, hapa ndiyo roho yangu inaniuma, kuna tozo ya shilingi 80 ya hizi mamlaka, zimeweka hapa pesa zao shilingi 85. Tukizichambua pesa hizi zitakazobakia halisia ni karibu shilingi 60, zitolewe kwa sababu hizi mamlaka ziko chini ya Wizara ambazo zinaleta hapa bajeti zao, tunawapitishia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, wapeleke kule wakapewe hela Hazina. Shililingi 60 itakayobakia hapa katika hiyo 85, ninachotaka kuomba, pesa hizo ziende TARURA, zinatosha kugharamikia barabara zetu. Haiwezekani tukaliacha hili jambo likapita na tukikutana leo kwa dharura, kesho tunakuletea majibu hapa na tunaondoa hili jambo. Tuishauri Serikali, tumshauri Mheshimiwa Mpango atengeneze bajeti, lakini kuna pesa kwenye mafuta huku zinapigwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano kuna GFI, hawa GFI hawa ni watu wanaweka marking katika mafuta wanachukua shilingi 14 kwa lita. Mauzo yetu ya mafuta ni karibu ni lita milioni sita mpaka 12 kwa siku. Huyu mtu anayechukua shilingi kumi na nne anaondoka na pesa zaidi ya milioni 90, kila siku ya Mungu huyu mtu anachukuwa milioni karibu kumi na mbili kwa mwezi, kwa mwaka na gharama za marking kuweka ile dawa ya marking utaona Finland na wapi, nchi zote zinazouza zinauza gharama ndogo sana. Mtu huyu ana wafanyakazi wawili wawili kila depot katika nchi hii ambao hawazidi wafanyakazi sabini, anachukua shilingi 14.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kuna EWURA sijui anachukua shilingi ngapi, kuna watu wa mizani wanachukua pesa pale, kuna watu wa survey kuangalia tu mafuta yamepita kwenye bomba hii shilingi 85, mambo mengine naogopa hata kuyasema hapa kwa ajili ya usalama wa nchi, haiwezekani! Naomba turudi mezani tufukue hii kitu Waziri wa Nishati hiki kitu wakati kinapitishwa hakuwepo, Waziri wa Fedha hakuwepo, Waziri wa Uwekezaji hakuwepo. Naomba kutumia Bunge hili kwa hizi kamati tulizopo, iwe ni msaada katika nchi, turudi mezani kwa amri yako, halafu kesho tuje na majibu. Hawa watu wote ambao wanaingiza tozo zao hapa uagize waje hapa Bungeni haraka leo…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. HAMIS H. T. MWAGAO: Aaaaaa.

Ndiyo ninachotaka kukwambia.

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Tabasam, dakika kumi zimeisha.

MHE. TABASAM H. MWAGAO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachotaka kukwambia pamoja na hali hii, naomba tamko lako ili tuokoe hii pesa, tupate pesa za TARURA, tutengeneze barabara zetu. Ahsante sana na naunga mkono hoja. (Makofi)