Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Abdullah Ali Mwinyi (9 total)

Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022
MHE. ABDULLAH ALI MWINYI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa zawadi hii. Awali ya yote napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu, Muumba wa Mbingu na Ardhi kwa kutujalia uhai, afya na ustawi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa hii ni mara yangu ya kwanza toka tulivyoingia Bungeni kuongea ndani ya Bunge hili Tukufu, napenda vilevile kuwashukuru wannachi wa Jimbo la Mahonda pamoja na chama changu cha CCM kwa kunipa ridhaa na kuniingiza hapa mjengoni niwe mwakilishi wao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, napenda kumshukuru Mheshimiwa Rais, Mwenyekiti wetu wa Taifa, kwa uamuzi, ujasiri na umahiri wake mkubwa katika kuongoza nchi hii kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita. Sina haja ya kuyazungumza yote aliyoyafanya, walionitangulia, Mheshimiwa Askofu Gwajima na Mheshimiwa Polepole wameyasema yote ya msingi kabisa ambayo yamefanyika katika hii miaka mitano. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nijikite katika maeneo matatu. Eneo la kwanza huu Mpango umekamilika na umefanyika kwa kiwango cha hali ya juu sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda tu kugusia maeneo ambayo nahisi hayajawekewa mkazo mkubwa ambayo ni haya matatu. La kwanza, mchango wa diaspora katika uchumi wetu; la pili, dhana ya Tanzania kuwa logistics na transit hub; na la tatu, ushiriki wa Watanzania kwenye uwekezaji wa rasilimali zetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, diaspora ina mchango mkubwa sana katika chumi za nchi. Kuna study ambayo nimeitazama ya mwaka 2018, katika nchi nne; Nigeria, Kenya, Uganda na sisi Tanzania. Mwaka 2018, fedha zinazotoka kwenye diaspora kuingia Nigeria, zilikuwa Dola bilioni 23.6 sawa na asilimia 6.1 ya GDP ya Nigeria. Kwa ule mwaka diaspora ili-contribute fedha nyingi kushinda export ya mafuta. Nigeria ndiyo nchi ya nne ulimwenguni kwa ku-export mafuta. Hata hivyo, Wanaijeria waliokuwa nje wameleta fedha zaidi ya mara mbili ya export yao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kenya mwaka 2018, contribution ya diaspora ni Dola bilioni 2.72 sawa na 3% ya GDP yao. Uganda mwaka 2018 imeingiza Dola bilioni 1.24 sawa na asilimia 4.5 ya GDP ya Uganda. Mwaka huo huo Tanzania tumeingiza Dola milioni 430, sawa na 0.8% ya GDP yetu. Bayana kabisa, sisi kama Tanzania hatujalea hii sekta muhimu ambayo inaweza kuwa mchango mkubwa sana katika maendeleo yetu na katika Mpango wetu wa Miaka Mitano. Hii sekta ni lazima ilelewe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna haki fulani fulani ambazo zinakuwa vichochezi. Kwa mfano, Mkenya mwenye passport ya nchi nyingine hadhibitiwi kununua ardhi. Halikadhalika na Uganda, lakini Tanzania huwezi. Sasa naiomba Serikali iyatazame haya, tuweze kuwapa hawa incentives ili sekta hii, hawa watu, Watanzania wameamua kuishi nje, washiriki na watusaidie katika mchango wa uchumi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, tumejenga miundombinu mikubwa sana katika sekta ya transport; SGR, barabara nyingi, tumeboresha bandari na nyingine tunaziongeza; dhamira yetu siyo tu kuiendesha Tanzania bali kusaidia nchi zilizokuwa jirani. Tanzania inapakana na nchi tisa. Mbili tu kati ya hizo tisa zina access ya bahari ya hindi. Mbili tu; Kenya na Msumbiji. Saba hazina; na zote hizo saba, kuna advantage kubwa sana kwa wao kupitisha mizigo yao kwetu. Uganda, Rwanda, Burundi, Congo, Malawi, Zambia, wote wana advantage kubwa na ndiyo distance fupi, hupiti katika nchi nyingine. Ikitoka baharini inapita Tanzania, inaingia kwao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, advantages zote strategically tunazo. Kwa nini hawazitumii? Mambo magumu yote Serikali ya Awamu ya Tano imeyafanya. Upungufu wetu ni katika yale mambo mepesi (soft skills). Yapi hayo? Customer service; urasimu. Civil service kwa kijeshijeshi badala ya kuwa kirafiki na kibiashara. Haya mambo mepesi lakini thamani yake ni kubwa mno. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuwashauri Mawaziri wa sekta, hilo jambo walitazame kwa macho makini ili tukuze uchumi na mpango wetu utimie. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho, ni ushiriki wa Watanzania kwenye uwekezaji. Serikali hii kwa nia njema kabisa inataka Watanzania tumiliki rasilimali zetu zilizokuwa kubwa. Sheria zilizopitishwa kwenye Extractive Industry; madini, oil and gas, sasa Tanzania ina hisa asilimia 16 katika kila investment kubwa ya namna hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna vitu vinaitwa mutual farms au collective investment schemes. Hii ni mifuko tu; maneno makubwa tu haya ya Kiingereza, lakini ni mifuko ya kuwachangisha sekta binafsi washiriki kwenye miradi ya mkakati. Kunakuwa na mfuko maalum, mnasema pengine Kabanga Nickel, mahesabu yake haya; Kabanga Nickel tunajua ina idadi gani? Faida yake ni hii. Nyie mnaotaka kuchangia na mkawa na hisa, karibuni. Hiyo ndiyo njia sahihi ya kuongeza ownership.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. ABDULLAH ALI MWINYI: Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa badala ya 16 tu ile ya Serikali peke yake, Watanzania sisi katika sekta binafsi, pamoja na wale wa diaspora walioko nje, wanaweza waka-invest tuka-own zaidi na ile fedha ya faida ikawa repatriated kwenda nje ikabaki hapa hapa.

MWENYEKITI: Ahsante sana.

MHE. ABDULLAH ALI MWINYI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)
Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2021/2022 – 2025/2026
MHE. ABDULLAH ALI MWINYI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. ningependa kuanza mchango wangu kwa kutoa salamu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mheshimiwa Spika, hivi karibuni tumepoteza Rais wetu, amefariki Rais wetu wakati yeye ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Jambo hili halina rejea ndani ya nchi yetu katika historia ya nchi yetu na si jambo jepesi kwa Rais kufariki katika nchi changa kama hii ambayo wapinzani wetu wanasema hatuna mfumo wa utawala bora, lakini amefariki Rais.

Ningependa kutoa shukrani zangu za dhati kabisa kwa Serikali pamoja na vyombo vyetu vya ulinzi na usalama kwa kuhakikisha Katiba na mfumo mzima wa utawala bora unasimamiwa na hali yetu mpaka Rais wetu mwingine aliyekuja akashika wadhifa bila matatizo yoyote. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nchi nyingi wamepata changamoto kama hizi na ikasababisha machafuko. Hili si bure, haya ni ukomavu wetu wa Serikali yetu chini ya Chama chetu Cha Mapinduzi ambayo imewezesha utaratibu na kuonesha dunia nzima kwamba, sisi ni wakomavu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimeupitia mpango pamoja na kusikiliza hotuba za hivi karibuni za Mheshimiwa Rais. Na mambo ya msingi ambayo ningependa kuyachangia ni matatu, la kwanza ukimsikiliza Mheshimiwa Rais vipaumbele vyake ni vitatu cha kwanza ni kurekebisha mfumo wa biashara. La pili ni kuimarisha zaidi mahusiano kikanda na ya kimataifa na cha tatu ni kuhakikisha miradi yetu ya mkakati inakamilika. Hayo mambo mawili ya mwanzo yakifanyika vizuri ndio yatahakikisha hili jambo la tatu, miradi ya mkakati, itakamilika kwa salama na amani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa kwasababu muda si rafiki mimi ningependa kugusia suala la kwanza kuboresha mfumo wa biashara. Ukiungalia mpango mzima na section kubwa ya kuhusu business environment utaambiwa tumepitia kitu kinaitwa blue print; kila uki-question jamani tumefika wapi, tunafanya nini, blue print implementation imefika wapi?

Mheshimiwa Spika, utaambiwa ikikamilika mambo yote hayo unayoya-raise yatakuwa sawa. Sasa wenzangu humu ndani ya Bunge walilizungumzia suala la monitoring na evaluation. Ili tuweze kurekebisha yale matatizo tuliyokuwanayo lazima tuwe na taasisi rasmi ama hapa Bungeni chini ya kamati moja au Serikalini na sehemu bora zaidi ni chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwasababu, yeye ndio kiongozi wetu katika shughuli za kila siku za Serikali. Lazima tuwe na taasisi ambayo inahakikisha quarterly tunafanya monitoring na evaluation kwa yale ambayo tumeyapanga. Bila kuboresha mfumo mzima wa kibiashara revenue hazitakuja zile ambazo tunategemea, biashara haitakua, uwekezaji hautaendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa sehemu hii ni sehemu ambayo ni nyeti sana ambayo ningependa kuunga hoja za miongoni mwa wenzetu ambao wamezungumzia kwamba, ama tufanye sehemu mbili Bunge liwe lina-monitor pamoja na Ofisi ya Waziri Mkuu kuhakikisha kwamba, yale ya
kimkakati, reforms tangible kwasababu, kuna projects ambazo unaona kama kitu kimejengwa hakijajengwa, lakini kuna mfumo wenyewe inabidi ubadilishwe uwe rafiki zaidi kwa ajili ya kukaribisha uwekezaji. Kwa hayo machache ningependa kushukuru kwa fursa hii na napenda kuunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora
MHE. ABDULLAH ALI MWINYI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipatia hidaya hii nami kusema maneno machache, cha msingi ningependa kuzungumza kuhusu mambo mawili; mchango wangu hautakuwa specific, mchango wangu ningependa uwe general. Na mambo makuu mawili ningependa kuyazungumza la kwanza ni amani, la pili ni utawala bora. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, amani hii ambayo tunajivunia sisi na kuna baadhi ya wenzetu ambao wanatuhusudu na amani yetu haikuja kwa bahati mbaya, imelelewa, ikatunzwa na hatimaye ikastawi mpaka hapa hii leo tukawa tunajivunia. Mwanzilishi wetu Baba wa Taifa aliitunza na kuilea hii amani kwa msingi mmoja mkuu msingi huo ni msingi wa utaifa. Baba wa Taifa kwa kipindi kikubwa sana cha awamu yake ya kwanza, nguvu nyingi sana za kifikra, za kifedha, aliziwekeza katika kujenga utaifa (national unit and cohesion) na alijenga hivyo kwa kufanya yafuatayo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kuhakikisha Serikali Kuu; pili, Serikali za Mitaa na tatu, Taasisi na Asasi za Kiserikali zina sura ya kiutaifa. Hili jambo kwa kweli hatuwezi kulichukulia wepesi wa aina yoyote, ni zito mno, tukilega hapo hii amani ambayo tunajivunia inaweza ikapeperuka. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Askofu Bagonza anasema; amani ni tunda la haki, na haki hii aliyoitenda Baba wa Taifa kuhakikisha kwamba taasisi zote, Serikali yenyewe ipo na sura ya kiutaifa ndio zao lake hii amani. (Makofi)

Mheshimiwa Waziri naomba nikukumbushe hili somo la kihistoria na sina shaka yoyote utalichukua kwa umakini na katika uboreshaji wenu wa taasisi zote za ndani mtazingatia sura ya kitaifa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nina maana gani sura ya Kitaifa? Mheshimiwa baba wa Taifa alichukia ukabila, alichukia udini na alihakikisha taasisi za Kimuungano zina sura ya Kimuungano (national cohesion). Hili ni jambo la msingi sana hili amani idumu na itamalaki kama hivi leo.

Mheshimiwa Naibu Spika, la pili ningependa kuzungumzia suala la utawala bora. Tumejichagulia sisi kama nchi kuendesha nchi yetu kwa misingi ya kidemokrasia, Serikali ya watu, kwa ajili yao na inayowatumikia wao (Government of the people, by the people, for the people) huu ndio mfumo wetu. Sisi tulibahatika kuwa viongozi tunadhamana hii ya muda mfupi tu na tupo hapa kwa ajili yao, tumejiwekea misingi ya utawala bora pasiwe na uonevu wa aina yoyote, tuwe tunalinda hii misingi iwalinde watu, hii misingi ilinde mali zao na misingi hii ilinde utu wao. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mantiki hiyo basi ningependa kuona sheria ambazo zimetoka nje ya mlolongo huu, nje ya mfumo wa utawala bora ziletwe na tuzirekebishe. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wale...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha muda wa Mzungumzaji)

MHE. ABDULLAH ALI MWINYI: Mheshimiwa Naibu Spika, imefika dakika saba?

NAIBU SPIKA: Tayari ahsante sana.

MHE. ABDULLAH ALI MWINYI: Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira
MHE. ABDULLAH ALI MWINYI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Napenda kuanza mchango wangu kwa kutoa shukrani na kwa kuwapongeza sana Mheshimiwa Waziri na Naibu wake kwa kazi nzuri na kwa uwasilishaji mzuri wa report hii ndani ya Bunge hili.

Mheshimiwa Spika, pili, ningependa vilevile kumpongeza Mheshimiwa Mhagama kwa uwasilishaji wake wa Report ya Kamati. Ameweka mambo vizuri kabisa, sina shaka yoyote kwamba, kuna mambo mengine makubwa zaidi yanakuja. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Soud amenifilisi kidogo katika mchango wake sasa mimi nitajikita katika jambo moja, moja ameshalizungumza kwa kina na nisingependa kulirudia na yeye amekuwa mahiri zaidi katika sekta yake hiyo ya masuala ya mazingira.

Mheshimiwa Spika, ningependa kujikita katika masuala ya yale mambo ambayo tunaita kero za muungano. Kero za Muungano imekuwa jambo la msingi kabisa ambalo hata Mheshimiwa Rais amelizungumzia mara mbili, tatu na kukabidhi kwa Mheshimiwa Makamu wa Rais, masuala ambayo bado hayajafanyiwa kazi yafanyiwe kazi kwa kipaumbele. Hata hivyo, ningependa kuzungumzia jambo moja ambalo lilishatafutiwa ufumbuzi, suala la mafuta na gesi, extractive industry.

Mheshimiwa Spika, mnapo mwaka 2014 mpaka 2015 suala hili lilikuwa moto sana na tukatolea maamuzi kwamba, suala la mafuta na gesi lisiwe suala la Muungano, kila upande ujitegemee. Jambo hili ni jema katika uendelezaji wa tasnia hii na hivi karibuni kwa bahati mbaya Ndugu zetu wa Msumbiji Total imejitoa, imetangaza juzi wamejitoa kuwekeza Msumbiji kwenye project ya LNG. Bahati mbaya kwa Ndugu zetu kwa sababu ule mradi ulikuwa mkubwa ndio unasemekana ndio ulikuwa mradi mkubwa kabisa ambao ungeweza kutokea katika Sub Saharan Africa katika miaka yote iliyopita, lakini kwa sababu ya matatizo ya machafuko na ugaidi wameamua kujitoa na investment hiyo haitaendelea.

Mheshimiwa Spika, sasa msiba wa wenzetu ni faraja kwetu, lakini kuna changamoto moja ambayo lazima tuitazame. Ukiangalia yale makubaliano yetu ya ndani tuliyokubaliana kwamba, tasnia hii sio sekta ya Muungano na taasisi na sheria na asasi zikaundwa, huku upande wa bara zipo TPDC, PURA na mengineyo na Zanzibar zikafanywa hivyohivyo na sheria ikaundwa na kuna watu ambao tayari wameshaingia katika kufanya utafiti, lakini kuna changamoto moja.

Mheshimiwa Spika, ukiangalia Katiba yetu ukurasa wa 128 inazungumza, Mambo ya Muungano, jambo la 15. Naomba ninukuu kwa ruhusa yako, inasema ifuatavyo; “15. Maliasili ya mafuta pamoja na mafuta yasiyochujwa na ya motokaa na mafuta ya aina ya petroli na aina nyinginezo za mafuta au bidhaa na gesi asilia.”

Mheshimiwa Spika, hiyo ni mojawapo ya vitu ambavyo vipo katika orodha ya muungano, Kikatiba, japokuwa sisi wenyewe tumekubaliana kwamba kila upande unajitegemea. Sasa suala la mafuta na gesi ni suala linalohusisha fedha nyingi sana, Mabilioni ya dola yanawekwa pale ili kuyatoa hayo mafuta na gesi.

Mheshimiwa Spika, japo kuwa sisi wenyewe tumekubaliana kwamba kila upande unajitegemea, sasa suala la mafuta ya gesi ni suala linalohusisha fedha nyingi sana, Mabilioni ya dola yanawekwa pale ili kuyatoa hayo mafuta na gesi.

Mheshmiwa Spika, jambo la kwanza mwekezaji yeyote atakayefanya kama ataweka mabilioni yake anafanya legislative review anatazama Sheria, Katiba na Mikataba yote kuangalia anawezaje kufanya hivyo. Na mtu mwekezaji wa Kimataifa ambaye anataka kuweka mabilioni hata fanya hivyo kama kuna kuwa kuna tatizo kama hili. Kwasababu ukiangalia kikatiba suala hili bado ni la Muungano. Sheria zipo zinazosema kwamba inaruhusu upande wa pili na makubaliano ya Kiserikali mambo ya pili yaendelee.

Mheshimiwa Spika, sasa kuna mgongano hapo bila huu mgongano kuurejebisha hakuna mwekezaji wa fedha nyingi atakayeweza kuweka fedha upande wa pili wa Muungano wa Zanzibar. Huku ipo bayana upande wa pili itashindikana, ningependa tu kumuomba Mheshimiwa Waziri alitazame hili hasa katika kipindi hiki ambacho fursa hii itakuwa moto, alitazame ajue jinsi gani tutalifanyia ufumbuzi suala hili kwa haraka iwezekanavyo ili uwekezaji mkubwa ule ambao tunautaka uweze kufanyika upande wa pili wa Muungano. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hayo machache ningependa tu kumshukuru tena Mheshimiwa Waziri kwa uwasilishaji mzuri na ningependa atoe maelezo katika hili ambalo nimeliweka hapa hadharani, ahsante sana. (Makofi)
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022
MHE. ABDULLAH ALI MWINYI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Awali ya yote nami napenda kutoa shukrani zangu za dhati kwa Mheshimiwa Waziri, Mheshimiwa Naibu Waziri na wataalam wote wa Wizara ya Fedha kwa kutupatia na kufanya kazi kubwa sana ili kuikamilisha hii bajeti ambayo tunaijadili kipindi hiki.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa vile muda siyo rafiki napenda kuingia moja kwa moja katika mchango wangu. Napenda kuzungumzia mambo mawili; la kwanza ni uchumi kwa ujumla wake na la pili suala la ubunifu na ajira, kwa sababu sehemu nyingi wenzangu ambao wamenitangulia wamezigusia na kwa kweli sina haja ya kuyarudia.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na janga kubwa la Uviko 19 lililokabidili dunia nzima Tanzania imebahatika; na siyo bahati, kwa mkakati na kwa mpango mzuri tumejaaliwa uchumi wetu kukua kwa asilimia 4.8.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia nchi ambazo zinatuzunguka Kusini mwa Jangwa la Sahara nchi zote kwa wastani chumi zao zimepungua, zimekuwa hasi, zimepungua kwa asilimia 1.9. Na kwa ulimwengu kwa ujumla wake chumi zimepungua kwa asilimia 3.3.

Mheshimiwa Naibu Spika, hakika kabisa, na iko bayana kabisa, kuna jambo ambalo sisi tumeweza kulifanya vizuri katika Janga hili la UVIKO-19 na ikatuwezesha uchumi wetu kukua kulinganisha na chumi nyingine zote za ulimwenguni. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile nimechukua fursa ya kutazama makampuni yetu makubwa yameendeleaje katika kipindi hiki. Nimechagua kampuni zifuatazo; TBL, TCC, Vodacom, Tigo na Puma Energy, kwa makusudi kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ukiziangalia hizo kampuni, ndizo kampuni ambazo zinatupa kodi kwa wingi; TBL, TCC, Vodacom na Tigo pamoja na Puma. Kuangalia taswira ya kibiashara inakwendaje. Ukiangalia kampuni zote hizo tano, hasa hizo nne za mwanzo, zote mapato yao yamepungua kwa kipindi cha miaka miwili mpaka mitatu sasa na kipindi cha mwaka uliopita mapato (revenue) yamepungua.

Mheshimiwa Naibu Spika, Vodacom quarter ya mwisho imepata hasara. Sasa ukiangalia huu uchumi umekuwa katika sekta gani, wakati ukiangalia makampuni haya makubwa mengi yameathirika. Sekta zilizotuwesha uchumi wetu sisi kukua ni ujenzi, madini, mawasiliano, uchukuzi, kilimo na viwanda. Ujenzi asilimia 13, madini asilimia tisa; hayo ndiyo maeneo ambayo yamekuza uchumi wetu. Eneo la hospitality; mahoteli, migahawa na utalii, yamepungua kwa asilimia karibu 14. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa ukiipitia ripoti ya BoT ya Desemba, 2020, inaonesha bayana kwamba eneo kubwa la ukuzi wa uchumi ni ujenzi, asilimia 42.6 na kilimo, asilimia 24.6. Theluthi mbili ya uchumi wetu umeshikwa katika hayo maeneo mawili.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nimetoa haya kama muhtasari. Ili kuitathmini bajeti lazima tuelewe uchumi wetu uko wapi na unakwendaje na bajeti yetu iendane na hali halisi ya huu uchumi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, asilimia 42.6 katika ujenzi imekuwa kwa sababu ya ile miradi ya kimkakati. Fedha nyingi zimepelekwa kwenye SGR, fedha nyingi zimepelekwa kwenye Bwawa la Mwalimu Nyerere, fedha nyingi zitapelekwa kwenye bomba la mafuta la kutoka Uganda. Kwa takribani miaka mitano mpaka kumi sekta hiyo itaendelea kukua.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pato kubwa, asilimia 24.6, katika kilimo ndiyo imetoka hapo. Lakini ukiiangalia bajeti inachangia chini ya asilimia moja. Chini ya asilimia moja inakwenda sehemu ambayo inatupa robo ya pato letu la nchi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mchango wangu kwa Waziri wa Fedha ni kwamba bajeti zijazo lazima tuongeze uwekezaji katika sekta hii ili izidi kustawi na izidi kutupa tija. Kama chini ya asilimia moja inatupa robo basi tukiweka asilimia kumi, kama Maputo Protocol, hakika uchumi wetu na bajeti yetu na mapato yetu yatakuwa makubwa zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili ni kuhusu ubunifu na ajira nilisema ninataka kugusia. Tatizo la ajira Tanzania ni kubwa. Asilimia 70 ya Watanzania wana umri chini ya miaka 35. Tulisikilize vizuri; asilimia 70 wana umri wa chini ya miaka 35. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, humu ndani sisi Wabunge kwa demography hiyo hatuwawakilishi wananchi wetu, sisi ni wazee wote kwa takwimu na kwa mfano wa hiyo demography. Maana yake wachache sana hapa wako chini ya miaka 35, lakini asilimia 70 ndio hao. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hiyo inaonekana dhahiri kwamba ajira itakuwa changamoto na itakuwa agenda yetu kubwa sana. Tunafanyaje kukabili tatizo la ajira? Maeneo ni haya mawili; la kwanza, kwa Tanzania ni kilimo, la pili ni ubunifu ambao upo kwenye teknolojia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hapo sasa ndiyo ninataka nipagusie zaidi. Mwaka 2005 wanafunzi wa Nairobi University, Kitivo cha Computer Science walibuni solution ambayo hii leo ni mobile money; mwaka 2005. Ukiangalia uchumi, siyo tu wa Tanzania, wa Afrika Mashariki yote, umetokana kwa sehemu kubwa na mchango huo. Ukiangalia sasa hivi katika mawasiliano mobile money inachangia fedha nyingi sana katika kodi zetu, Afrika Mashariki yote na Tanzania yenyewe. Hilo limetokana na ubunifu wa wanafunzi vijana. Na haikuwa bahati mbaya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kipindi hichi TCRA ilikuwa inaongozwa na Profesa Mkoma na BoT Gavana alikuwa Prof. Ndulu. Hawa maprofesa wawili walikuwa na imani ya kukuza vipaji na ubunifu kabla ya kuongeza mfumo wa kupata fedha Kiserikali. Waliuacha huu ukastawi halafu ndiyo wakawekea mfumo wa regulation. Haikuwa bahati mbaya, imefanywa kwa makusudi.

Mheshimiwa Naibu Spika, ushauri wangu kwa Mheshimiwa Waziri wa Fedha katika sekta hiyo ni kwamba lazima turuhusu ubunifu ustawi na tuulee. Tusifanye kama yule bata anayezaa yai la dhahabu kila siku tukamkaba yule mpaka lile yai asilizae. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sekta hiyo – kama angalizo – kwa Tanzania ukilinganisha na wenzetu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, ndiyo sekta ambayo ina kodi kubwa. Ukilinganisha na Uganda, kodi yake ni ndogo, ukilinganisha na Kenya, kodi yake ni ndogo, Tanzania kodi yake ni kubwa. Na kwa safari hii tunaelewa kwa nini imebidi kuiongeza, lakini hilo ni angalizo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sekta ya ubunifu lazima ilelewe istawi ndiyo tuweze kupata tija. Sasa eneo kubwa ambalo sisi tunategemea kuwapa ajira vijana wetu ni maeneo mawili kwa bahati mbaya bajeti hii haiyapi support ya hali ya juu; kilimo na sekta ya ubunifu. Sekta zote hizo zipo kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi. Kama tutaiwekea kipaumbele na tutafanya mazingira ya ustawi ili ikue itupe tija zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hakika kwa hayo machache, ninapenda kuunga mkono hoja na ahsante sana.
Azimio la Bunge la kuridhia Mkataba wa Uanzishwaji wa Eneo Huru la Biashara la Afrika
MHE. ABDULLAH ALI MWINYI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana nami kupata fursa hii na kuchangia katika hoja hii ya Uanzishwaji wa Eneo Huru la Biashara la Afrika
(Agreement Establishing the African Continental Free Trade Area).

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hakika siku ya leo ni siku ya kihistoria ambayo, kama dada yangu Mheshimiwa Pindi Chana alivyosema, ni siku ambayo ndiyo chanzo cha ndoto za Baba wa Taifa mwanzilishi wetu kufika sehemu ya kuwa na Afrika moja. Siku zote nchi kuungana zinatakiwa ziwe na chachu na chachu kuu ya muunganiko ulimwengu mzima ni biashara na uchumi. Kuanza kufanya biashara kwa pamoja mkawa na soko moja ndiyo chachu kuu ya kuunganisha nchi au mabara kote ulimwenguni. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ndoto ya Baba wa Taifa ilikuwa Afrika iwe moja, na ndoto yakeni tofauti na Kwame Nkrumah, fikra zake ilikuwa Afrika iwe moja kwa kupitia building blocks. Kwame Nkrumah yeye alisema tuwe wamoja kuanzia siku ya kwanza, kama Muammar Gaddafi alivyokuwa anafikiria.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini Baba wa Taifa alisema through building blocks ya Afrika Mashariki, ya SADC, COMESA na Building blocks nyingine. Na huu mkataba chanzo chake ndiyo hivyo, mazungumzo ya mkataba huu yalikuwa mazungumzo ya viongozi wa Secretary General wa East African Community, kipindi kile alikuwa Balozi Mwapachu, SADC na ECOWAS ndio chanzo, inakwenda sambamba na ile ndoto ya Baba wa Taifa.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa wasiwasi mwingi mkumbwa niliousikia leo ni kama Tanzania tupo tayari au la; na kama tumejipanga na kama tuna kasoro zozote. Kasoro hazikosekani kila nchi ina mapungufu yake. Lakini Tanzania na mfumo huu wa soko tayari sisi tumeshajifunza na tupo daraja la juu kabisa kulinganisha na nchi nyingi hizi za ndani ya Afrika, tofauti na tunavyojifikiria. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Jumuiya ya Afrika Mashariki ni jumuiya ya mambo mazito kabisa. Kwanza, Umoja wa Forodha, pili, Soko Huria ndani ya nchi hizi tano, tatu, Umoja wa Kifedha. Kwa sehemu kubwa Umoja wa Forodha tayari umeshakamilika, na kwa kipindi ambacho sisi tupo toka mwaka 1999 mpaka leo; wakati tunaanza hofu kubwa ya Tanzania ilikuwa kuwa soko la Kenya kwa sababu kulikuwa kuna dhana ya kwamba Kenya ina uchumi mkubwa, ambao ni sahihi, na sisi kwa sababu uchumi wetu ni mdogo tutakuwa tu na watu wengi, tutakuwa tu soko la Kenya; lakini ukweli uliothabitika ni tofauti na hivyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kipindi cha zaidi ya miaka sita mpaka saba leo Tanzania ina positive balance of trade. Maana yake ni nini? Maana yake ni kwamba inauza zaidi katika masoko ya Jumuiya ya Afrika Mashariki kushinda tunachokinunua. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naona kuna kimya hivi kana kwamba hamuamini, angalieni takwimu. Tanzania inauza bidhaa yenye thamani kubwa Kenya kushinda inachonunua kutoka Kenya kuja Tanzania kwa zaidi ya miaka sita. Hali kadhalika Tanzania tunauza vitu vingi Uganda kushinda tunachonunua. The same Rwanda, na Burundi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ki ukweli kama Mheshimiwa hapa mmoja aliyezungumza hatuna tatizo lolote na wajasiliamali na wafanyabiashara wetu. Tatizo muda hadi muda tunawafunga minyororo wanashindwa kufanya kazi vizuri zaidi, lakini juu ya hivyo tuna mifano ya kampuni za kitanzania ambao wanafanya biashara nchi zaidi ya kumi na mbili na nyingine kumi na nane na zina-compete vizuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, nitakupa mfano; Azam ipo ndani ya Afrika inafanya biashara nchi 15, MeTL nchi 18, export trading nchi 12, MM Steel Intergrated nchi 13, wamekwenda huko wanaendesha viwanda vikubwa na wanaweza ku-compete. Sasa huu umoja umuhimu wake ni soko, soko ni watu. Ukiangalia nchi ambazo zimeendelea kwa haraka sana kama vile China, India, Brazil, Marekani, nchi zote hizi zina kitu kimoja, zina watu wengi. Jumuiya Afrika Mashariki ina watu zaidi ya milioni 200, hili eneo lote hili litakuwa na watu zaidi ya bilioni moja, hii ni fursa adhimu sana kwa Tanzania kujipambanua na kuuza nje ya soko. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nini tunachokiuza kikubwa Kenya na ndani ya Jumuiya Afrika Mashariki ni mazao, Tanzania inalisha Afrika Mashariki katika kuzalisha, na tunalisha mpunga, vitunguu, machungwa na mananasi. Kimsingi tunaweza ku-compete.

Mheshimiwa Naibu Spika, wiki iliyopita, nikimalizia, nilikuwa naangalia You Tube kupitia Internet kuangalia katika sekta ya muziki, kwa sababu nimekaa na kaka yangu hapa naona niigusie, sekta ya muziki. Nikaangalia katika You Tube, ni miziki gani inasikilizwa Nairobi kwenye ile top ten ya You Tube. Katika top ten wana muziki saba wa Tanzania wakiongozwa na Diamond Platinums.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa nini nazungumzia hilo, vijana wetu hawana hofu ya kupambana wakati sisi tunafunguka Music Industry Nairobi ilikuwa imefika daraja kubwa kushinda sisi, lakini wale vijana hawakuwa na hofu. Leo hii Afrika Mashariki yote vijana wetu wana dominate. Hii ni message positive kwamba Tanzania mapungufu tunayo, tunajua matatizo yetu yapo wapi, lakini tunauwezo mkubwa sana wa kupambana na kushindana na kupata manufaa makubwa katika hili eneo huria la biashara. (Makofi)

NAIBU SPIKA: Ahsante sana.

MHE. ABDULLAH ALI MWINYI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)
Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali wa Mwaka 2021 (Toleo la Kiingereza)
MHE. ABDULLAH ALI MWINYI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Awali ya yote ninapenda na mimi kutoa pole zangu kwa wafiwa wa Mheshimiwa Nditiye na tunawaombea wapendwa wake wote subira katika kipindi hiki kigumu.

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa wasaa huu nami kuchangia mawili/matatu katika mada hii muhimu na nyeti sana. Walionitangulia hasa Mheshimiwa Olelekaita na Mheshimiwa Tadayo, wameyazungumza mengi ambayo kwa kiasi kikubwa wamenifilisi yale ambayo nilitaka kuyasema, lakini ninapenda tu kusema hakuna mtu yeyote mwenye akili timamu anayeweza kubisha umuhimu wa mchakato wa kutoa haki kuwa katika lugha ambayo wengi wetu ndani ya nchi wanaifahamu. Hilo halina mjadala wa aina yoyote. Sasa lazima tuseme hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kumetokea kidogo hofu katika tasnia ya sheria kwa wale ambao walishazoea na walishapata mafunzo kwa lugha ya Kiingereza. Mabadiliko ya aina yoyote lazima yatakuwa yana ugumu wake. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka 1973 sisi kama Tanzania tuliamua kufanya Dodoma uwe Mji Mkuu. Tukachukua hatua za awamu hadi awamu lakini ile azma yenyewe haikufika ikatokea Awamu ya Tano na Rais, Dkt. Magufuli, akafanya maamuzi ya kuhamisha mji kufika Dodoma; tuko hapa. Tulilalamika hivi hivi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hali kadhalika katika lugha ya Kiswahili katika mihula yote miwili na sehemu kubwa huu muhula wa mahakama Kiswahili kinatumika. Lakini kuna hofu ya kwamba tukifanya kwa haraka pengine tutaleta athari ikatufanya sisi kama kisiwa. Hiyo hofu ipo lakini msiwe na wasiwasi. Sheria hii imegusia hayo, imeweka bayana kwamba lugha ya Mahakama ni lugha ya Kiswahili, lakini pale haki itakapohitajika kutendeka kwa kutumia lugha nyingine ruksa. Sasa msiwe na wasiwasi. (Makofi)

Mheshimiwa Salome ana wasiwasi huo, jurisprudence sijui kwa Kiswahili itakuwaje, nadhani itakuwa jurisprudensi, itajijenga upya kwa lugha ya Kiswahili na tutatafsiri na Jumuiya ya Madola itatuelewa. Lakini umuhimu wa kwanza ni kwa wananchi wetu na umuhimu wa kwanza wa misingi ya haki za binadamu na utawala bora inatulazimisha sisi kuhakikisha lugha ya kutoa haki ni lugha ile ambayo wengi wetu wanaielewa. (Makofi)

MHE. MOHAMED O. MCHENGERWA: Mheshimiwa Naibu Spika, Taarifa.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Mchengerwa kwa kifupi.

T A A R I F A

MHE. MOHAMED O. MCHENGERWA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimpe taarifa msemaji kwamba kamusi ya kwanza iliyotafsiri lugha ya kisheria kutoka lugha ya kisheria ya Kiingereza kuwa lugha ya sheria ya Kiswahili ilisainiwa na aliyekuwa Waziri Mkuu, Mzee wetu Kawawa mwaka 1968 na iliandaliwa na Kitivo cha Sheria Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. (Makofi)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Abdullah Mwinyi, unaipokea taarifa hiyo?

MHE. ABDULLAH ALI MWINYI: Mheshimiwa Naibu Spika, naipokea tena kwa shangwe kubwa sana. Inaonesha bayana kwamba huu mchakato haukuanza leo, toka mwaka 1962 ulikuwepo na hatua hadi hatua mpaka tumefika kilele hiki cha leo cha kutunga hii sheria. (Makofi)

Sasa sheria hii na mabadiliko haya yamezingatia mambo yote ambayo ni ya msingi na ninapenda kuwaomba wenzangu kuiunga mkono na mimi pia naunga mkono hoja.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. (Makofi)
Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali (Na 2) wa Mwaka 2021 (Toleo la Kiingereza)
MHE. ABDULLAH ALI MWINYI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Awali ya yote napenda kuchukua fursa hii kwanza kabisa kumshukuru Mheshimiwa Mwenyekiti wetu kwa uwasilisho mzuri kabisa kama kawaida yake. Pili, napenda kuchukua fursa hii kumshukuru sana na kwa dhati Mwanasheria Mkuu wa Serikali na timu yake yote pamoja na Waziri na CPD kwa kurahisisha kazi yetu katika Kamati na kuifanya kuwa nyepesi kabisa.

Mheshimiwa Spika, hakika napenda kuchukua fursa hii kuishukuru Serikali kwa ujumla wake, kwa kufanya kazi kuwa nyepesi kwa sababu hakukuwa na mvutano wa aina yoyote. Ukipendekeza vizuri, Serikali imekuwa sikivu na inapokea mapendekezo na kwa kweli tumefarijika sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimefilisiwa na watangulizi wangu kwa sehemu kubwa na vile vile tumefilisiwa na Serikali kwa sababu sehemu kubwa nadhani sehemu zote za mapendekezo yetu Serikali imepokea. Sasa kazi yangu itakuwa tu ni kuongeza msisitizo na kujenga hoja za ziada kidogo ili Bunge lituelewe zaidi kwa nini tumefanya haya mapendekezo na waridhie haya mapendekezo kwa minajili mizima ya kuboresha hii sheria. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika suala la mawakili, Wakili Msomi Olelekaita amelizungumza vizuri na kwa kina, lakini napenda tu kuongeza jambo moja la msingi. Kuna msingi mmoja unasema, the power to appoint, pre-supposes the power to disappoint or to remove. Mamlaka ambayo inatoa wadhifa lazima iwe hiyo hiyo mamlaka ya kuondoa ule wadhifa. Huo ni msingi kwenye administration, msingi wa kisheria. Japokuwa hii Sheria ya Mawakili ya Sura 341 (Advocates Act, Cap. 341) kupeleka Kamati za Kinidhamu mikoani ni jambo zuri sana na kuna viwango vya nidhamu, kile kiwango cha mwisho kabisa tumeona akirudi Taifani kwa sababu ya msingi huu mmojawapo, pamoja na misingi mingine ambayo Wakili Msomi mwenzangu amezungumza.

Mheshimiwa Spika, kuhusu masuala ya vizazi na vifo kama Mwenyekiti wetu wa Kamati alivyosema, mjadala huu ulikuwa mkubwa na yamezuka mambo mengi na kwamba dada yangu Mheshimiwa Salome amezungumzia kuhusu hati za vifo zaidi ya kimoja, kwa kweli kiutaratibu kwanza cheti cha kifo kinamsaidia mtu kitu gani? Hilo lazima tujue, tuweke wazi. Pili, cheti cha kifo hakiwezi kuwa zaidi ya kimoja. Tunaweza tukawa tuna utaratibu wa kuwa na nakala
kwamba watu wenye haki ya kupata hivi vyeti wawe zaidi ya mtu mmoja, basi original kikatoka kimoja na nakala kwa mwingine yeyote ambaye anaweza kuwa na hiyo haki ili mradi awe nacho.

Mheshimiwa Spika, kiukweli cheti cha kifo ni ithibati ya kuonyesha kama fulani amefariki, hakikuzidishii zaidi ya hapo. Hakuna kingine cha ziada ila watu wengi wamezungumza na ingefanyika kama kungekuwa kuna muhtasari wa kifamilia. Familia mnakaa mnaandika muhtasari wenu na pengine watu wote wana haki; huenda kuna mtoto mmoja mtundu tu, japokuwa ana haki ya kwenda kuchukua hicho cheti na familia isitake yule aende, tukawa na muhtasari wetu, tukakubaliana mtu mmoja akaenda kuchukua kwa niaba ya familia. Sasa hayo ni mambo ya ki-administration na sidhani kwamba ni busara kuyaweka katika sheria, kutakuwa na utaratibu mwingine wa kuiweka huko mbele.

Mheshimiwa Spika, suala la Sheria za Kampuni, nataka nigusie tu kidogo, hiki kipengele ambacho Mheshimiwa Mbatia nacho alikigusa akasema ni cha hatari sana, kwa kweli inabidi nami nikubali na Kamati imekubali kwamba kipengele hiki ni kidogo cha hatari. Katika Ibara ya 30 inayopendekezwa Marekebisho ya Kifungu cha 3 cha Sheria…

SPIKA: Ni Salome Makamba.

MHE. ABDULLAH ALI MWINYI: Mheshimiwa Spika, Salome Makamba kumradhi. Naomba radhi. Mheshimiwa Makamba naomba radhi.

Mheshimiwa Spika, katika Ibara ya 30 inayopendekeza Marekebisho ya Kifungu cha 3 cha Sheria katika kifungu kidogo cha (5) kufuta maneno “associated with instances of”, naomba niseme, hili ni hatari zaidi kuliko lile alilolizungumza Mheshimiwa. Alilozungumza Mheshimiwa ni mtu ambaye tayari ameshahukumiwa akakatazwa, nami naungana naye mkono, kwa hiyo haifai. Amefanya makosa, jamii imeshamhukumu, aendelee na maisha yake ya kupata ujira wake. Hii inayosema “associated with instances of” hata kama hujahukumiwa ukishukiwa shukiwa hivi, usiweze kufungua Kampuni. Hii ni hatari. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuna principle ya kisheria inasema, “innocent to proven guilty.” Huwezi ukapewa majukumu; kwanza wewe ni innocent, umeshukiwa tu ukazuiwa kufanya biashara. Hili tumeliona kwenye Kamati na tumelizungumza na tumekitoa hicho kipengele na Serikali imekubali. Sasa kwa ufupi, mengi ambayo tumeyaona na tumeyagusia hapa, Serikali wameyapokea na tunaomba Bunge lako Tukufu liridhie hayo mapendekezo ya Kamati ambapo masuala mengi yamekaa vizuri.

Mheshimiwa Spika, naomba sana kwa hayo machache niunge mkono hoja na niwasihi Wabunge wenzangu kuipokea ripoti yetu ya Kamati ili kuboresha hii sheria na ikakaa vizuri.

Mheshimiwa Spika, ahsante sana. (Makofi)
THE WRITTEN LAWS (MISCELLANEOUS AMENDMENTS) (NO. 5) ACT, 2021
MHE. ABDULLAH ALI MWINYI: Mheshimiwa Spika, kidogo nimeshtuka kwa sababu nilikuwa sijajipanga kuchangia lakini kwa sababu umeninyanyua nitasema mawili matatu.

Mheshimiwa Spika, kwanza nimshukuru Mheshimiwa Mwenyekiti kwa ripoti yake nzuri na Mheshimiwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa uwasilishaji wake mzuri sana. Kwa kuwa mimi ni mjumbe wa Kamati hii sitaweza kukosa mawili, matatu ya kuzungumza.

Mheshimiwa Spika, Muswada huu umegusia sheria 9, napenda tu kugusia maneno mawili, matatu katika sheria zifuatazo. Ya kwanza ni Sheria ya Kuzuia Usafirishaji Haramu wa Binadamu, Sura ya 432; Sheria ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya, Sura ya 95; Sheria ya Utumishi wa Jeshi la Polisi, Idara ya Uhamiaji na Jeshi la Magereza, Sura ya 241; na mwisho napenda tu kugusia Sheria ya Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori, Sura 260. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Sheria ya The Anti-Trafficking in Persons Act, Sura 432 kwa kweli ni sheria ya msingi sana. Ulinzi na usalama ni jukumu letu sote Tanzania nzima sio tu jukumu la vyombo vya ulinzi na usalama pekee.

Mheshimiwa Spika, mabadiliko katika Sura 432 yamegusia masuala mbalimbali na kuwapa mamlaka wananchi kadhaa kuweza kudhibiti biashara hii haramu. Napenda kuzungumzia kifungu cha 9 kinachozungumzia kuhusu whistle-blowers, wale ambao wanaona uharamia unatokea na wakaripoti ili kuhakikisha kwamba uharamia ule unadhibitiwa. Pia kifungu cha 12 nacho kinathibitisha tena kwa ziada private citizens arrest, wananchi tukiona kuna matatizo yanatokea, tumepewa mamlaka ya kuhamasishana na kuhakikisha ule uharamia wa namna hiyo hauendelei. Kwa kweli, sisi kama Kamati tumeridhia na ni masuala mazuri kabisa yameletwa kwa ajili ya kuyarekebisha.

Mheshimiwa Spika, Sura inayofuata ya 95, Sheria ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya, napenda tu kugusia jambo moja la msingi. Kipengele kipya cha 15 na 15A kinazungumzia masuala ya mirungi na bangi na kuweka mipaka na uzito wa kosa hilo kulingana na uzito wa mihadarati yenyewe.

Mheshimiwa Spika, katika jambo hili, kwa kweli nimekubaliana na proposal ya Serikali lakini nitoe tahadhari. Suala la mirungi japokuwa nchini kwetu ni haramu lakini tunapakana na nchi za ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki na nyingi za SADC ambazo suala la mirungi lenyewe si haramu. Sasa udhibiti wake utakuwa una matatizo makubwa sana.

Mheshimiwa Spika, kwa vile sisi tuko ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, Kenya pale zinarushwa ndege kama zile ndege za minofu za pale Mwanza zinaruka kutoka Nairobi zimejaa mirungi kupeleka Ulaya hali kadhalika Uganda. Sasa hili suala katika territory yetu ndani ya Tanzania ni haramu na lina penalty kubwa lakini wenzetu wanaotuzunguka wote wamelihalalisha. Sasa ama tulitazame kwa ujumla wetu wote, tuwashawishi wenzetu liwe haramu kote au tuliwekee misingi fulani fulani ambayo inaweza ikaruhusu hii biashara ikaendelea la udhibiti wake utakuwa una matatizo makubwa. Haikuwa maudhui ya mabadiliko ya sheria hii lakini hilo ni angalizo kwa Serikali, tulitazame siku zijazo kwa sababu udhibiti wake utakuwa una matatizo ilhali wote wanaotuzunguka mirungi kwao ni halali isipokuwa sisi hapa kwetu.

Mheshimiwa Spika, suala la Uhamiaji ambalo limezungumziwa kwa ari kubwa mpaka sasa hivi, sheria na Katiba vinaguswa katika masuala haya. Kiukweli vipengele vimesomwa hapa kwa pupa sana bila kuwaruhusu watu kujenga hoja halafu tukazitumia zile hoja ili kuelekezana vizuri.

Mheshimiwa Spika, ibara sahihi ya kwanza kwa kuanzia ni Ibara ya Katiba ya 147(2), naomba nipewe wasaa kidogo niitafute katika kishkwambi hapa, niipate kuisoma vizuri nitiririke vizuri. (Makofi)

SPIKA: Kama huioni tukusomee.

MHE. ABDULLAH ALI MWINYI: Mheshimiwa Spika, Ibara 147(2) inasema: “Majeshi ya Ulinzi.

Serikali ya Jamhuri ya Muungano yaweza, kwa mujibu wa sheria, kuunda na kuweka Tanzania majeshi ya aina mbalimbali kwa ajili ya ulinzi na usalama wa nchi na wananchi wa Tanzania”.

Mheshimiwa Spika, Ibara ya 147(4) inasema: “Kwa madhumuni ya ibara hii, “mwanajeshi” maana yake ni askari aliyeajiriwa kwa masharti ya muda au ya kudumu katika Jeshi la Ulinzi, Jeshi la Polisi, Jeshi la Magereza au Jeshi la Kujenga Taifa”.

Mheshimiwa Spika, hii katiba ni ya mwaka 1977, kipindi hicho wakati hii Katiba inakuwa formulated haya ndiyo yalikuwa majeshi. Mwaka 1977 haya ndiyo yalikuwa majeshi lakini walitazamia kabisa kwamba siku za usoni kwa sababu mbalimbali nyingine kunawezekana kuwe na sababu ya kufanya tuwe na majeshi ya ziada. Ndiyo maana Ibara ya 147(2) inasema, kwa mujibu wa sheria. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Ibara ya 151 inazungumzia maana ya jeshi. Jeshi maana yake nini? Maana ya jeshi, ni lolote kati ya majeshi ya ulinzi na ni pamoja na jeshi lolote lingine lililoundwa na Katiba hii au kwa mujibu wa sheria na iliyotawaliwa na Amiri Jeshi Mkuu au kwa mujibu wa sheria. (Makofi)

SPIKA: Ahsante sana.

MHE. ABDULLAH ALI MWINYI: Mheshimiwa Spika, naomba kuunga mkono hoja. Naomba kuishia hapa, ahsante. (Makofi)