Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Aleksia Asia Kamguna (11 total)

MHE. ALEKSIA A. KAMGUNA: Mheshimiwa Spika, nikushukuru sana. Pamoja na kwamba kuna changamoto ya mitandao kupitia maeneo mbalimbali ya Tanzania, lakini halikadhalika kuna changamoto pia ya wizi wa kimitandao, tumekuwa tukipoteza fedha nyingi sana kupitia hii mitandao. Swali langu, je,ni lini Serikali itaweza kudhibiti wizi huu wa kimtandao unafanywa na simu? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Kamguna, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la utapeli wa kimtandao viko chini ya makosa ya kimtandao na Sheria ya Makosa ya Kimtandao ya mwaka 2015. Hata hivyo watekelezaji wa sheria hii ni pamoja na vyombo vingine vya dola, ikiwemo na Jeshi la Polishi. Tunafanya juhudi za kutosha kuhakikisha kwamba tunatoa elimu kwa umma, kwa sababu ndicho kitu ambacho ni cha msingi sana kwa Watanzania kuelewa namna gani wanaweza wakatumia simu zao za mkononi.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia changamoto ambayo ilikuwepo ni pamoja na wale waliokuwa wanapewa majukumu ya kuandikisha au kuuza zile lines za simu, ambao walionekana kutokuwa na uaminifu na hatimaye kuwa wanawatapeli Watanzania badala ya kusajili line moja kwa mtu mmoja, matokeo yake anajikuta kwamba Mtanzania amesajili line tano kabla ya kuondoka katika kituo cha kusajili lines hizo. Matokeo yake hizi lines zitakapochukuliwa na watu ambao wanania ovu matokeo yake ndio zitakuja kutumika kwa ajili ya matatizo kama hayo.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imejipanga kuhakikisha kwamba tunatoa elimu kwa umma lakini pia tunatumia teknolojia ambayo itaanza kudhibiti, matatizo ambayo yangesababishwa na watu ambao wamepewa majukumu ya kuuza hizi lines. Namhakikishia Mheshimiwa Mbunge pamoja na Wabunge wengine, Serikali bado inayafanyia kazi na kufanya uchambuzi wa kutosha ili kujiridhisha kwamba tunatumia njia gani ambayo itakuwa rafiki zaidi kwa Watanzania bila kuwabugudhi katika maisha yao ya kila siku. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. ALEKSIA A. KAMGUNA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi.

Mheshimiwa Spika, kituo cha afya cha Maskati Mkoani Morogoro kina Mhudumu mmoja wa afya. Je, ni lini Serikali itapeleka Wahudumu wa Afya katika kituo hicho?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwamba katika vituo vyetu vyote tunafahamu nchini kote kuna upungufu wa watumishi, ndiyo maana wiki iliyopita Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Utumishi, alitoa tangazo kwamba tutakwenda kuendelea kuajiri watumishi wa kada ambalimbali ikiwepo wa afya, nikuhakikishie kwamba tutatoa kipaumbele katika kituo cha afya ambacho kinahitaji mhudumu wa afya.
MHE. ALEKSIA A. KAMGUNA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi. Serikali hutumia fedha nyingi sana katika kutengeneza barabara, lakini barabara hizo kwa muda mfupi tu huwa zinamomonyona na kuota manyasi: -

Je, Serikali ina mkakati gani wa kutenga fedha kwa ajili ya maintance ya barabara hizi ili kuzinusuru? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Kamguna kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, barabara nyingi ambazo ni za changarawe ama za vumbi ni kweli kwamba hazidumu kwa muda mrefu na ndiyo maana zinatengewa fedha kwa ajili ya matengenezo ya kila mwaka. Azma ya Serikali ni kujenga barabara zote kwa kiwango cha lami, lakini barabara hizi ni gharama, kwa hiyo, inategemea na upatikanaji wa fedha. Kwa hiyo, zile barabara kubwa za mkakati ndiyo tutaanza kuzijenga kwa lami, lakini kadri bajeti itakavyoruhusu, mpango ni kuzijenga barabara zote kwa lami zikiwepo na barabara za Mheshimiwa Mbunge. Ahsante.
MHE. ALEKSIA A. KAMGUNA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Katika Tanzania, ugonjwa huu wa fistula ni ugonjwa ambao unasumbua sana.

Je, ni hospitali ngapi au zipi zenye wataalamu wa kutibu ugonjwa wa fistula zilizoko nchini ukiondoa Hospitali ya CCBRT?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili. Ukiangalia sana ukizingatia haki za binadamu huu ugonjwa huwezi kumsafirisha mgonjwa kukiwa katika magari ya kawaida.

Je, Serikali imejipangaje kutoa usafiri maalum kwa ajili ya watu hao na namna ya kujikimu ili kutoka sehemu moja na kwenda nyingine ukizingatia waliowengi hali zao ni duni?
NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze kwa kufuatilia haya mambo ambayo kwa kweli yanawasumbua akina mama wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ameuliza ni hospitali ngapi; hospitali zetu zote za mikoa, kanda na taifa zinatoa huduma hiyo. Kumekuwepo kila wakati sasa hivi madaktari kutoka Hospitali ya Muhimbili na hospitali zetu za kanda wakienda kwenye hospitali za mikoa yetu ili kuendelea kuongeza nguvu na ujuzi kwa hospitali zetu za mikoa ili huduma hii iweze kutolewa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa swali lake la pili; nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge; moja tuna mkakati kwamba magari yanapita kuhamasisha mtaani. Pia akipatikana mgonjwa yeyote huwa ambulance inamfuata na kupelekewa sehemu husika. Hata hivyo, ninajua kwamba kwenye eneo hilo bado hatujajiimarisha vizuri. Hivyo, tunachukua wazo lako ili tuweze kulifanyia karibu kwa kushirikiana na hospitali zetu za wilaya ili akina mama wale wakionekana waweze kupelekwa bila kupitia mabasi ya kawaida, waende kwa kutumia gari za Serikali.
MHE. ALEKSIA A. KAMGUNA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi. Kituo cha afya cha Mtimbila kina x-ray lakini hakina jengo la x-ray wala hakina mhudumu wa x-ray. Je, ni lini Serikali itaenda kujenga hilo jengo na hatimaye kupeleka mhudumu ili watu wapate huduma hizo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Aleksia Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, nimhakikishie kwamba vituo vyetu vya afya ambavyo havina miundombinu ya majengo yanayostahili kuwepo, ikiwemo majengo ya x-ray ni kipaumbele cha Serikali kujenga majengo yale. Kwa hiyo, tutahakikisha kwa sababu tayari kuna x-ray machine katika kituo hiki lakini hatuna jengo, tutaweka kipaumbele ili tuanze ujenzi wa jengo hilo kupitia mapato ya ndani lakini pia tutatafuta fedha Serikali Kuu.
MHE. ALEKSIA A. KAMGUNA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Katika Mkoa wa Morogoro kuna maeneo mengi yana maji ya kutosha;

Je ni lini sasa Serikali itajenga scheme ya umwagiliaji katika maeneo ya Mvomero na maeneo ya Mofu katika Halmashauri ya Mlimba?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli Mkoa wa Morogoro una maeneo mengi yanayofaa kwa kilimo cha umwagiliaji na tunayo miradi mingi ambayo inaendelea. Maeneo ambayo ameyataja nayachukulia kwa uzito mkubwa na hivyo nitaagiza wataalam wangu waende kuyaangalia, ili kama yanafaa basi tuyaingize katika mpango wetu ili kuhakikisha kwamba wakulima wanalima kupitia kilimo cha umwagiliaji.
MHE. ALEKSIA A. KAMGUNA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali. Nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia kwenye mbuga zetu kuna Askari pamoja na Maafisa wengine ambao wanazilinda hizo mbuga. Ukienda kule kwenye mbuga utakuta kuna vibanda vya wafugaji wanaishi huko pamoja na rundo la mifugo wakati Serikali wanasema kwamba wameweka zuio. Je, hao wafugaji walioko kule na hivyo vibanda hawa Askari hawawaoni? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili. Inasemekana kuna baadhi ya Maafisa Wanyamapori ambao siyo waaminifu, wanashirikiana na wale watu wenye mifungo kuwaingiza katika hifadhi zetu. Je, Serikali inasemaje katika hili? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Aleksia Kamguna, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba hawa Askari wanakuwepo katika maendeo ya hifadhi, changamoto ambayo tunakutana nayo hasa kwenye mapori ambayo yameungana na mapori ya Halmashauri na mengine ni mapori ya Vijiji. Kwa mfano, kama Hifadhi ya Nyerere, tuna Hifadhi ya Selous lakini kuna mapori ambayo yameungana na Hifadhi ya Nyerere. Kwa hiyo, utakuta kwamba kwenye Pori la Selous Askari wanafanya operesheni, pale ambapo kunakuwa na mifugo, inakamatwa na inachukuliwa hatua lakini wale wamiliki wahiyo mifugo wanaenda wana-pause kwenye yale mapori ya Halmashauri pamoja na Vijiji ambapo sasa kule askari wetu hawafiki katika maeneo hayo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, changamoto hiyo imekuwa kubwa kwa sababu hii mifungo ipo na inakuwa kando kando tu inakuwa imeegeshwa pale ambapo Askari wetu wanapoondoka tu tayari mifugo inaendelea kuingia hifadhini, lakini kulingana na sheria zetu, nadhani wanafahamu wafugaji namna ambavyo tunasimamia kanuni, taratibu na namna ambavyo tunaendelea kuzishughulikia.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye hili suala la Askari kushirikiana na Wafugaji. Ni kweli tuna sheria kali sana na pale inapogundulika kwamba Askari anashirikiana na kukiuka kanuni na taratibu zilizopo, tunamchukulia hatua mara moja na wengine wanafukuzwa kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, hii sheria tunatumia Sheria ya Jeshi ambayo tayari sisi tumeshaanza kuingia katika utaratibu huu na wengi wameshachukuliwa hatua. Kwa hiyo, ikithibitika kwamba kuna Askari amefanya hivi basi tupate taarifa mara moja na tuweze kuchukua hatua. (Makofi)
MHE. ALEKSIA A. KAMGUNA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi. Katika Halmashauri ya Mlimba, Kata ya Uchinjile hakuna kabisa mawasiliano ya simu. Je, ni lini Serikali itapeleka mawasiliano ya simu katika kata hiyo?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, nimeshafika Mlimba na katika kata ambayo Mheshimiwa Mbunge ameitaja ni kwamba tayari imeingizwa katika miradi 758. Zaidi ya hapo, Jimbo la Mlimba tumewapelekea minara saba ambapo tunaamini kwamba itakapojengwa basi utatuzi wa changamoto za mawasiliano utakuwa umefikia ukomo. Ahsante sana.

MHE. ALEKSIA A. KAMGUNA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi.

Mheshimiwa Spika, Jimbo la Malinyi lina maji mengi sana yanayopotea bure. Je, Serikali ina mpango gani wa kuanzisha skimu ya umwagiliaji katika Kata ya Malinyi?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, eneo lote la Malinyi linaingia katika mradi huu mkubwa ambao tunaendelea nao wa Bonde la Kilombero na Ifakara Idete. Kwa hiyo, ndani yake humo tutapata nafasi ya kujenga skimu nyingi za umwagiliaji na wabanchi wa Malinyi watanufaika kupitia mradi huu mkubwa unakuja.
MHE. ALEKSIA A. KAMGUNA: Mheshimiwa Spika, ahsante, Ofisi ya Mkurugenzi wa Wilaya ya Malinyi na Mkuu wa Wilaya ya Malinyi haina mawasiliano ya simu; je, Serikali ina mkakati gani kumaliza adha hiyo katika Wilaya hiyo?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Aleksia Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwa bajeti ambayo Bunge lako tukufu limetupitishia jana katika kata ambazo Mheshimiwa Mbunge ameziongelea na makao makuu ya Halmashauri zote zipo katika mpango wa utekelezaji. Hivyo tuombe tu kwamba tuendelee kushirikiana kuhakikisha kwamba tutakapofikisha huduma hii basi tupate ushirikiano kutoka kwa wananchi katika maeneo yetu, ahsante.

MHE. ALEKSIA A. KAMGUNA: Mheshimiwa Naibu Spika, nina maswali madogo mawili ya nyongeza. Je, Serikali ina mkakati gani wa kufanya kilimo cha zao la mpunga la umwagiliaji katika maeneo ya Malinyi, Ulanga, Mlimba, Kilombero na Kilosa kuwa endelevu badala ya kutegemea msimu wa mvua?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili. Je, Serikali ina mpango gani wa kuanzisha soko kuu la mpunga katika Wilaya ya Kilombero?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Aleksia Asia Kamguna Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli ya kwamba tunatambua kilimo cha umwagiliaji ndio suluhu katika kuboresha na kuimarisha kilimo cha mpunga katika Mkoa wa Morogoro. Nimwondoe hofu Mheshimiwa Mbunge ya kwamba katika bajeti hii inayokuja yako mabonde makubwa na miradi mingi ya umwagiliaji ambayo itatekelezwa katika Mkoa wa Morogoro ambao pia utagusa katika maeneo ambayo ameyataja.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili la kuhusu soko kuu ni wazo zuri, wazo jema tumelichukua na tutakwenda kuchakata ndani ya Serikali kuona uwezekano wake.