Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Aleksia Asia Kamguna (7 total)

Hotuba ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyoitoa wakati wa Ufunguzi wa Bunge la Kumi na Mbili, Tarehe 13 Novemba, 2020
MHE. ALEKSIA A. KAMGUNA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipatia nafasi. Pia namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuniwezesha kusimama hapa leo kwa mara ya kwanza katika Bunge hili la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru pia Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuniteua pamoja na vyombo vyote vya Chama cha Mapinduzi hatimaye nimefika hapa katika hili Bunge. Nasema ahsante. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nawashukuru pia wapiga kura wangu wanawake wa Mkoa wa Morogoro ambao wameniwezesha kuja hapa leo na kuwa msemaji wao. Mwisho naishukuru familia yangu ambayo ilikuwa bega kwa bega na mimi hatimaye nimefikia hapa leo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa heshima na taadhima nimesimama hapa kusema Mheshimiwa Rais tuliyenaye leo sio wa kawaida tumepewa zawadi kutoka kwa Mungu. Kwa maana ukisafiri mataifa mengine wanauliza huyu Rais wenu ni nani na amepata wapi ujasiri wa kufanya haya mambo yote? Naamini ni nguvu za Mungu na pia ameamua kuwakomboa Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Watanzania ametukomboa kupitia nidhamu ya kazi. Tanzania nidhamu ya kazi ilikuwa imeshuka lakini yeye ameamua kuisimamia nidhamu hasa katika Serikali. Namshukuru sana na kumpongeza, tunamwombea kwa Mungu aendelee na moyo huo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wanasema sisi wanawake ni wanyonge lakini ninaamini sisi siyo wanyonge, akina mama ni Taifa kubwa. Mheshimiwa Rais ametupigania kwenye uzazi kutoka vifo 11,000 hadi 3,000, tunamshukuru sana. Hii ni kazi tuliyopewa na Mungu kwamba mwanaume atakula kwa jasho lakini mwanamke atazaa kwa uchungu.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwanamke atazaa kwa uchungu lakini ukiliangalia sana katika Taifa letu sasa hivi au katika hili Bara la Afrika mwanamke ana kazi kubwa, yeye anazaa kwa uchungu na bado anakula kwa jasho. Kwa hiyo, ndugu zangu akina mama naomba tusimame kifua mbele hasa Rais wetu kwa jinsi anavyotutetea katika nyanja zote ambazo wenzangu wamezitaja sina budi kuzirudia, upande wa elimu, afya, maji ametutua ndoo, miundombinu na kadhalika.

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi naomba nijikite katika sehemu moja ya ukurasa wa 39. Naomba ninukuu: “Tutashughulikia pia kero mbalimbali za wananchi ikiwemo migogoro ya ardhi na mirathi.” Mimi naomba nijikite upande wa mirathi. Kwa nini nilisema wanawake ni Taifa kubwa, wanawake tuna nguvu? Anayepata shida katika miradthi ni mwanamke ndiyo maana namzungumzia mwanamke na mtoto. Mwanamke ni nani? Mwanamke ni mama mzazi, ni mlezi, ni daktari, ni mwalimu na ni hakimu kwa wakati mmoja.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwanamke anapendeza anapoolewa tunamvisha nguo nyeupe, lakini mwanamke huyu siku akifiwa ananyanyasika, hasa wa Kitanzania. Kwa nini huyu mwanamke ananyanyasika kiasi hiki ambapo yawezekana ile mali waliyoichuma wakati mume wake akiwa hai yeye alichuma zaidi kuliko mume wake? Yawezekana alikuwa na kipato kikubwa kuliko mume wake lakini mwanaume akifariki mwanamke yule anakuwa si kitu wala si chochote? (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Kengele imegonga Mheshimiwa, ahsante sana.

MHE. ALEKSIA A. KAMGUNA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba tuiangalie hii sheria ili tubadilishe mwanamke aweze kuthaminiwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja, nashukuru sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
MHE. ALEKSIA A. KAMGUNA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi. Kwa heshima na taadhima, namshukuru Mwenyezi Mungu kwa sisi sote kutuwezesha kuwa salama. Pia nawashukuru Ofisi ya Rais, TAMISEMI kwa kuwasilisha bajeti yao ambayo ni nzuri, inaleta mwelekeo pamoja na changamoto zake, lakini inaleta matumaini katika Taifa letu. Tunasema ahsante.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukweli kwetu tuna matatizo, Mkoa wa Morogoro ni mkoa wenye bahati, tumepata miundombinu ya kimkakati, lakini kuna matatizo mengi katika mkoa huu. Naomba kwa heshima na taadhima nizungumzie huo mkoa. Mkoa wa Morogoro ni mkubwa sana na wote wanakiri ni mkoa wa pili katika nchi yetu, lakini tumepata neema, tuna ardhi nzuri, kadhalika na kadhalika, lakini pamoja na hiyo ardhi nzuri imeguka sasa imekuwa shubiri inatutesa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa nini nasema hivi? Nichukue mfano wa Wilaya ya Malinyi; wilaya hii iko bondeni, yaani mvua ikinyesha Iringa sisi kwetu ni maji. Ninavyoongea leo hii, siwezi nikatoka hapa Dodoma kwenda kwetu sina kwa kupita, kwa maana wilaya nzima imejaa maji. Kwa kuwa imejaa maji hatuna miundombinu ya barabara, hali ni mbaya, yaani Malinyi waiangalie kwa jicho la huruma, wengine wote wanalilia lami lakini sisi tunalilia kufika kwetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Malinyi ni wilaya mpya, ni wilaya ambayo imetokana na Wilaya mama ya Ulanga imeanzishwa mwaka 2015, lakini kama nilivyotangulia kusema barabara hatuna, yaani TARURA kama inawezekana, wote wanasema asilimia 40, basi kwetu sisi iwe asilimia 60 kwa ili iweze kuisimamisha Malinyi. Malinyi hatuna madaraja na hatuna hata barabara ya changarawe. Mheshimiwa Waziri na wasaidizi wake, angekuwa amefika Malinyi angenielewa ni nini nazungumza.

Mheshimiwa Naibu Spika, sisi hatuna njia ya kuingia Malinyi; tukifika sehemu moja ambayo inaitwa Misegesi kwenda Malinyi huwezi kufika, kuna hitaji daraja na halipo. Kuna sehemu nyingine ya Malinyi kuelekea Lugala ambako ndiko kuna Hospitali ya Misheni ambayo tunaitegemea, huwezi kufika kwa sababu barabara hakuna. Pia kuna sehemu nyingine ambayo inaitwa Malinyi Lugala ndio huko kwenye Hospitali karibu, lakini huwezi kufika. Sasa huyo mtu wa Malinyi anaishije. Naomba Mheshimiwa Waziri avae viatu vya watu wa Malinyi, kwa kweli Malinyi tuna matatizo.

Mheshimiwa Naibu Spika, Wabunge wengi wanasema kwamba wanahitaji TARURA kwa ajili ya barabara na sisi watu wa Malinyi tunasema TARURA ni uhai, kwa maana bila ya TARURA sisi hatuwezi kuishi na kweli maisha yetu ni magumu.

Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, Malinyi tuna matatizo kwa upande wa afya. Hatuna barabara, hatuna dispensary, hatuna Hospitali ya Wilaya, Hospitali ya Wilaya imejengwa, kuna kipindi walitoa mwongozo kwamba, lazima hospitali zote waanze kutibia wagonjwa wa OPD, ndio hicho kimeanzishwa, lakini kwa ujumla hospitali ya Serikali hakuna. Sasa kama hospitali ya Serikali hakuna, miundombinu ya barabara hakuna, huyu mwanamke ambaye amepewa kazi na Mungu ya uzazi, anawezaje kutoka kwake afike kwenye hospitali na kama atafika kwenye hospitali, kwanza hospitali yenyewe haipo, anaenda wapi? Tunaomba pia Mheshimiwa Waziri kwa upande wa afya atuangalie, hatuna barabara, hatuna hospitali, kama mama inaumiza. Naomba watuangalie Malinyi. Leo sina mengi ya kusema zaidi ya kuomba yaani nimesimama kwa ajili ya kuomba. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna sehemu nyingine ya Wilaya ya Ifakara kuna hospitali moja inatiwa Man’gula B. Hapa limejengwa jengo zuri kabisa la Kituo cha Afya katika Mkoa wa Morogoro, lakini hakuna sehemu ya operation. Ni kituo cha afya kikubwa na kizuri na Serikali imetumia pesa nyingi. Sasa tunaweka kile kituo bila sehemu ya wazazi na wazazi wanafariki, tunaomba nalo liangaliwe, bado Morogoro ina changamoto. Morogoro ni kubwa na lazima TAMISEMI waiangalie kwa jicho la pekee wakilinganisha na mikoa mingine, kwa sababu kama ni kubwa ina maana na mahitaji yake yatakuwa makubwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, nakuja upande mwingine wa utawala; hili naomba niwaeleze, sasa hivi naona kuna mikoa mingi au Wilaya nyingi kuna matatizo au ina changamoto, unakuta Mkuu wa Wilaya anagombana na Mkurugenzi, anagombana na Mbunge, sasa kunakuwa tafrani, nafikiri viongozi wenzangu watakubaliana nami kwamba katika wilaya nyingi au halmashauri nyingi hazina amani, kuna vurugu. Kwa nini kuna vurugu? Yawezekana kwa mawazo yangu uteuzi tunaoufanya sasa hivi wa Wakuu wa Wilaya labda turudi nyuma, mwanzo tulikuwa tunawachukua hawa Maafisa Tarafa, wanakuwa na uzoefu, wanakuwa karibu na Wakuu wa Wilaya, ukimteua kuwa Mkuu wa Wilaya anajua zile ethics za uongozi, lakini hawa wa sasa hivi kama wanawatoa tu shuleni, wanawapeleka wanakuwa Wakuu wa Wilaya, matokeo yake kunakuwa conflict of interest, matokeo yake wilaya zinakuwa na vurugu. Hilo nimeliona, naomba tuliangalie kwa umakini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hayo machache, nakushukuru na naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi
MHE. ALEKSIA A. KAMGUNA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuweza kuchangia. Awali ya yote hatuna budi kumshukuru Mwenyezi Mungu ambaye ametuwezesha sote kuwa salama. Nawapongeza Wizara ya Ardhi, ukweli Wizara ya Ardhi ni kati ya Wizara ambazo zilikuwa na matatizo makubwa sana katika nchi hii lakini wamejitahidi. Hapa walipofikia si haba, wamefanya kazi kubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, panapokuwa na manufaa hapakosekani changamoto. Wizara hii pamoja na kujitahidi lakini kuna changamoto hususan za mipaka. Nazungumzia mipaka iliyopo katika Bonde la Kilombero, Wilaya ya Malinyi, Ulanga, Kilombero yenyewe na Jimbo la Mlimba. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hizo wilaya zina matatizo. Tumepata bahati ya kupata ardhi nzuri, tunamshukuru Mungu, lakini ardhi tuliyopata inatutesa. Kuna mwananchi ambaye amezaliwa Malinyi tangu miaka hiyo, yawezekana labda Mjerumani au Mwingereza yuko pale kwenye Bonde la Mlimba, kwenye Bonde la Ngombo. Sasa leo hii wanamwambia yule mwananchi ahame. Sasa hatujui akihama anaenda wapi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mara ya kwanza wanasema lile eneo lilipimwa mwaka 1952, lilipimwa na GN ya kwanza ikawekwa 2012. Wakaja wakaweka tena GN ya pili 2017. Zote hizi zinam-limit yule mwananchi asiweze kulima, asiweze kuwa na makazi pale. Sasa tunajiuliza kwa miaka yote hiyo, huyu mwananchi ataenda kuishi wapi? Kazaliwa pale, kakulia pale na pengine hata Morogoro Mjini haijui. Leo unamwambia ahame Ngombo, ahame Mlimba, ahame Kilombero na sasa hivi Kilombero ni mji mkubwa sana wa Ifakara, wenyewe wanafahamu, lakini mnatuambia tuhame.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa naiuliza hii Wizara, kama iliweza kupima mwaka 1952 wakati wananchi wale walikuwa wachache tu hawakuweza kuwaelewesha kuwa eneo limepimwa na mwondoke wakaja wakaweka GN 2012 na 2017. Hebu niiulize Wizara, Tanzania ni kubwa na ina ardhi nzuri hususan Morogoro na hizi wilaya ambazo nimezitaja. Sasa naiomba Serikali itoe tamko, je, kwa sasa hivi tufuate GN ya 2012 au wale wananchi wafuate GN ya 2017, kwa maana wale wananchi hawawezi wakafanya kazi zozote za kimaendeleo, wapo wamekaa. Wakienda kulima watu wa TAWA wanawafuata ambao ni askari wa maliasili wanasema hili ni eneo la maliasili. Wakikaa hivi hivi ina maana kwamba watu wanakaribisha umaskini. Je, hawa watu tunawafanyaje? Naomba Wizara inisaidie hilo ili wale watu waweze kujua kama wanaishi pale na kama hawataishi watupe mbadala kwamba waelekee wapi. Tanzania ni kubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, nazungumzia mipaka vile vile kati ya wakulima na wafugaji. Mkoa wa Morogoro ni kati ya mikoa ambayo ina changamoto kubwa sana ya migogoro kati ya wakulima na wafugaji na hii migogoro inatokana na mipaka. Hakuna mipaka ambayo inaainisha kwamba hili ni eneo la wakulima na hili ni eneo la wafugaji. Matokeo yake watu tunasema tuna amani. Ukweli katika ule mkoa sehemu kubwa amani haipo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sisi kipindi cha kampeni tulienda kufanya kampeni tunakuta kabisa mtu anaenda analisha sio ya kuambiwa, kwa macho yangu, anaenda analisha ng’ombe wake anapeleka kwenye mashamba ya watu. Mimi mwenyewe pia lilinipata kwenye shamba langu, nawakuta vijana wanaenda, nawauliza mbona mnalisha kwenye shamba, wananiambia unaniuliza mimi, muulize ng’ombe!

Mheshimiwa Naibu Spika, niambie, hivi unamkuta mtu analisha ng’ombe kabisa kwenye shamba lako, unamuuliza, anasema unaniuliza mimi, muulize ng’ombe unamjibu nini? Unamfanyaje mtu kama huyu? Ni mateso. Yaani tunaishi kama vile sisi ni wahamiaji. Uende kwenye GN unaambiwa uondoke, basi ulime angalau ujikwamue mkulima mdogo, unaambiwa mashamba hayo ndiyo malisho kwao. Sasa huyu mwananchi wa Ifakara, mwananchi wa Kilombero na Kilosa na Mvomero katika Mkoa wa Morogoro, anaishije huyu? Siku zote ukiangalia sana mkulima na mfugaji, mkulima kipato chake ni cha chini na mkulima huyu ndiyo anayegandamizwa. Naomba majibu kwa haya masuala yangu mawili. (MakofI)

Mheshimiwa Naibu Spika, nashauri Wizara kama wanataka kuwe na amani tungechukua ile mipaka tuweke ekari kama moja yaani huku wakulima na huku wafugaji. Anayevuka kuelekea kwa mwenzake ni mgomvi, maana sasa hivi amani hakuna! (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ambalo nataka kuongelea ni hizi institution zetu za Serikali, kwamba tuna shule na hospitali za Serikali, lakini zile hospitali zina viwanja, shule zina viwanja. Ukiangalia sana unakuta kwamba shule nyingi wanafika wakati vile viwanja vinachukuliwa na watu wenye pesa. Sasa ukiuliza kwa nini, kwa mfano kiwanja cha mpira, watu wameweka wamejenga shule ya Serikali, wana kiwanja chao cha mpira cha michezo, lakini baada ya muda mwenye pesa akiona eneo linamfaa anaenda anajenga nyumba. Sababu ni nini? Hakuna, eneo lile halina hatimiliki, lingekuwa na hatimiliki wale watu wasingevamia lile eneo. Kwa hiyo, naiomba Wizara tujitahidi kupima mali za umma. Shule zetu, hospitali zetu ili wale watu wachache wenye pesa wanaorubuni wasiweze kuingilia pale hatimaye wakachukua maeneo ya umma na baadaye tukakosa hizo sehemu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, la nne na la mwisho kabisa, nashindwa kuwaelewa Wizara ya Ardhi kwamba, hivi mtu anajenga bondeni, anajenga sehemu ambayo haitakiwi mtu kujenga. Anajenga wa kwanza, mnamwangalia; anajenga wa pili, mnamwangalia, wanafika 1,000 mnasema wabomolewe waondoke. Sasa mlishindwa nini kumsimamisha yule wa kwanza badala ya kulete hasara kubwa katika Serikali? Hilo nalo naomba mnieleze, kwani kunakuwa na matatizo gani kuwasimamisha mtu ambaye amejenga kwenye sehemu ambayo ni bonde au njia ya kupita maji? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi nimetoka kwenye maji. Watu wanakwambia, maji yanakimbia watu, sio kweli hata siku moja. Maji hata ujenge nyumba ya aina gani…

MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Kamguna, kuna Taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Kuchauka.

T A A R I F A

MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Naibu Spika, nilikuwa nataka nimpe taarifa mchangiaji. Siyo tu kwamba hao watu wanaojenga wanaonekana, mpaka umeme wanaletewa na pengine hata kama huduma ya maji wanaletewa vilevile. Halafu baadaye wanakuja kuwaambiwa wabomolewe. (Makofi)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Kamguna, unapokea taarifa hiyo?

MHE. ALEKSIA A. KAMGUNA: Mheshimiwa Naibu Spika, nimeipokea hiyo taarifa. Nakubaliana naye kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, hebu angalieni na mara nyingi wanaojenga pale ni wale walalahoi. Wale watu tunawachukuliaje? Mtu amejipigapiga akajikusanyakusanya akajenga pale kwenye bonde, tunamwachia, halafu akija kubomolewa tunasema hatukulipi compensation kwa sababu wewe umejenga sehemu ambayo haikutakiwa. Kwani mwanzo anajenga ninyi hamkumwona? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, katika hilo, kama mtakuwa mnatuachia hivyo, basi inabidi wale muwalipe. Ni wenyewe mnataka, kwani mwanzo hayakuwepo mabonde? Mbona yalikuwa hayazibwi?

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hayo machache naomba kuwasilisha. Naunga mkono hoja, ahsante. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Kilimo
MHE. ALEKSIA A. KAMGUNA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Awali ya yote sina budi kumshukuru Mwenyezi Mungu aliyetuwezesha sote kuwa hai. Nakushukuru pia kwa nafasi uliyonipatia. Nawapongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu na Makamu wa Rais, kwa majukumu yote ambayo wanatupigania Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza sana Mheshimiwa Rais, ni Amiri Jeshi wetu Mkuu ana majukumu makubwa anatupambania Tanzania. Tunamshukuru kwa yote. Nawapongeza pia Mawaziri kwa kazi wanayoifanya na pia naipongeza Wizara yote ya Kilimo na watendaji wote, nawapongeza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, asilimia 65 ya Watanzania ni wakulima, lakini walio wengi ni wakulima wadogo wadogo ambao sehemu kubwa ya wakulima hao wana changamoto. Changamoto hizo ni kama ukosefu wa wataalam, wana changamoto za mitaji midogo kadha wa kadha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nazungumzia Mkoa wa Morogoro, wenzetu wana changamoto hizo nyingine, lakini sisi tuna changamoto kubwa zaidi. Jamani Mkoa wa Morogoro ni mkoa ambao Mungu ametupendelea, ametupa fursa ya ardhi nzuri, lakini ardhi ile sisi inatutesa. Ardhi inatutesa sasa hivi imekuwa ni shubiri, lakini watu wa nje wanaona kama vile sisi ile ardhi inatusaidia, haitusaidii hasa kwa akinamama. Kwa nini nasema hivyo? Kwa sababu mwanamke anatoka nyumbani kwake anaenda shambani kwenda kulima, lakini mwanamke yule hawezi kulima kwa sababu anaogopa wafugaji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, akifika shambani, wafugaji wakimwona kwenye shamba lake ambalo ameshalilimia, ameshalipalilia, ameshalifanyia huduma zote, mfugaji yule anakuja kulishia kwenye lile shamba hatimaye yule mama akiuliza kwa nini unalilishia, yule mfugaji anaweza akampiga, wanawafanyia vitendo vya udhalilishaji, hatimaye wakati mwingine hata kuwapotezea maisha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hali ni mbaya, hivi ninavyoongea hapa, asubuhi nimepigiwa simu kwamba mfugaji ameenda kupeleka mifugo yake kwenye shamba la mtu amekula heka 30, asubuhi ya leo. Sasa jamani tunajenga Tanzania ya aina gani? Mtu akienda shambani kwake nina mfano halisi, mtu ameenda, maskini, mkulima yule, ameenda amekodi shamba la 150,000, ameenda amelimwagilia mpunga umefika mkubwa anataka kuvuna, mwenye ng’ombe akapeleka kwenda kulishia wafugaji, kujitetea kwa nini unaenda kulishia shamba langu akampotezea maisha. Nafikiri hata kwenye vyombo vya habari mlisikia, ilikuwa ni tarehe 27/12/2021.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hiyo hali haijatokea sehemu moja, imetokea sehemu nyingi, imetokea katika Jimbo la Mlimba, Jimbo la Kilosa, Mvomero na Wilaya ya Morogoro Vijiji, Jimbo la Morogoro Kusini Mashariki tarehe 8/5/2022. Serikali kwa nini kuwe na matatizo ya wakulima na wafugaji miaka nenda rudi, kwa nini kusiwe na amani? Yule mtu wa Morogoro alizoweya yeye anaenda shambani analima, lakini sasa hivi nini matokeo ya hiyo hali, matokeo yake ni kwamba wale watu umaskini tuliokuwa nao umekithiri, njaa inazidi kuwa kali na kipato kimekuwa duni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaiomba Serikali, chonde watuangalie ili tukomeshe hii hali ya wakulima na wafugaji. Nchi yetu ya Tanzania ni nchi ya amani, lakini kwa nini tufikie hapo kwenye kugombana. Watu wa Morogoro ni rahimu, wanawakaribisha wageni wote wanaokuja Morogoro hakuna ubaguzi, lakini tunapofika tushirikiane tuishi kwa amani. Akinamama wanadharaulika, wanadhalilika hasa, hawawezi kwenda mashambani, wajawazito wanawafanyia vitendo vya ovyo. Sasa naiuliza Serikali je, hii hali itaendelea hivyo mpaka lini? Tunasema kwamba vijana wanakimbilia mjini, mtu anaenda analima, shamba lake linaliwa, ataacha kwenda mjini, atakaa kijijini anafanya nini? Naomba Serikali waliangalie hilo kwa macho ya huruma, chonde chonde. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunasema kwamba, sasa hivi tunataka maendeleo, ardhi tunayo, lakini maendeleo hatutapata, huwezi kupata maendeleo bila kufanya kazi. Unafanyaje kazi mtu, unalima lakini unachokipata hakuna na kwa vyovyote vile lazima kama mfugaji anakula mazao ya mkulima amani inakuwa haipo. Wale watu watakuwa hawafanyi kazi. Naomba majibu ya Serikali, waniambie kwamba je, wana mpango gani au wana mkakati gani kwa hatua hii iliyofikia ili tuweze kuwa na amani? Kwa maana tusipofanya hivi, tutazidi kukaribisha umaskini, tutazidi kuwa na vijana ambao Serikali imepanga mipango mizuri sana ya kuwawezesha, lakini watawawezesha kupitia nini na wakati sisi tunasema tunategemea kilimo?

Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba sana Serikali ikomeshe hiyo migogoro, nafikiri itafika mahali itaonekana kwamba hawa wafugaji ina maana wana nguvu kuliko Serikali. La hasha siamini hilo, naamini Serikali ina nguvu kuliko wafugaji. Sasa inatosha, kama tulikuwa nyuma hatujaliona hilo tatizo, hilo tatizo lipo, Serikali tuamke sasa tulifanyie kazi, tulimalize, hatimaye wale watu waweze kufanya kazi turejeshe amani ambayo Tanzania tumeizoweya.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante Mheshimiwa Aleksia Asia Kamguna kwa mchango wako.

MHE. ALEKSIA A. KAMGUNA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante na naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
MHE. ALEKSIA A. KAMGUNA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Awali ya yote sina budi kumshukuru Mwenyezi Mungu aliyetupatia afya na pumzi yake. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ni wajibu wetu kumshukuru Rais wetu, Mama yetu Mama Dkt. Samia, kwa jinsi anavyotupigania Watanzania. Kawaida mama huwa hawezi kuacha kuwalea watoto wake, sisi Watanzania wote ni watoto wake ndio maana anapita hukuhuku katika kututafutia chochote kile ambacho anakipata, tunamshukuru tunasema ahsante. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika maisha kuna hospitali, hospitali maana yake sio majengo, hospitali ni zile huduma ambazo zinapatikana katika sehemu husika. Kwa mfano, wauguzi na dawa na vifaa tiba, katika Tanzania na hususan Mkoa wangu wa Morogoro kuna sehemu zina upungufu, nitachukua kama mifano tu, kuna sehemu zina upungufu wa dawa na wahudumu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa mfano hospitali ya Wilaya ya Mahenge, Hospitali ya Wilaya ya mahenge ni hospitali ya Wilaya ya Ulanga inaitwa Mahenge, lakini ni Wilaya ya Ulanga; ile hospitali ina mkunga mmoja tu, jamani ni hatari sana, maana yule mkunga mmoja je, akiumwa? Wale akinamama wanapata wapi huduma? Akiuguliwa ina maana na akinamama wasiende kujifungua kwa sababu yeye anaumwa? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ndugu zangu wana TAMISEMI, tunaomba muingalie ile hospitali. Hata huduma za ndani za mawasiliano hakuna, kwa mfano daktari hayupo, yule mtu ambaye anazalisha yuko wodini kama kuna dharura imetokea hawezi kuwasiliana na daktari maana hakuna mawasiliano ya ndani ya hospitali. Ninaomba hilo muliangalie sana kwa ajili ya mustakabali wa wanawake wa Wilaya ile. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia, katika Kituo chetu cha Mang’ula. Kituo cha Mang’ula ni kituo ambacho tulikuja kuomba kuomba msaada mkatusaidia tukapata zile huduma, lakini kile kituo tuna hela taslimu ambazo ni milioni 11, tunaomba tununue MSD jokofu, lakini MSD wanasema hawana jokofu kwa wakati huo. Sasa zile hela tutakaanazo mpaka lini? Tunaomba mtusaidie. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, na pia kuna kituo cha Mtimbira. Kituo cha Mtimbira nimelialia sana tangu muda mrefu kwamba, kile kituo kina x-ray mashine, lakini hakina chumba cha kuhifadhia ile mashine ya x-ray. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa hiyo hela ya Serikali si bora ingefanya kazi nyingine kuliko tumeipeleka pale, tumei-dump, mashine ya x-ray haifanyi kazi, huduma watu hawapati, hasa mwanamke akiuguliwa katika ile Wilaya ya Malinyi hakuna mashine yoyote ya x-ray maana tulikuwa tunaitegemea mashine hiyo na mashine haifanyi kazi. Sasa kwa mfano mtu amepata matatizo ya uzazi anafanyaje? Kwa hiyo, Wilaya nzima haina msaada wa aina yoyote wa vitendeakazi kwa mfano mashine ya x-ray.

Mheshimiwa Spika, pia kuna kata ya Mikese, Kituo cha Afya cha Mikese kile nasema ni Tanzania kwa sababu, kile kituo kiko njiani, ukitoka Dodoma, ukitoka mikoa yote, Iringa, wapi, kile kituo kiko njiani, lakini hakina huduma stahiki ambazo zinastahili pale. Wanawake wanaopanda kwenye mabasi, labda amepata tatizo la dharura akajifungue pale, ambacho kingetusaidia au watoto wadogo wakiugua ghafla kingetusaidia, lakini huduma za watoto na akinamama hakuna. Kwa hiyo, naomba mkiangalie hicho Kituo cha Mikese. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, na pia nataka niongee kwa ujumla wake, wanawake wengi wanaoishi vijijini wanakabiliwa na shida ya uchumi, lakini unakuta kwamba, wale wanawake lazima wazae. Wakipata ujauzito wakienda hospitali wanaambiwa wakanunue vifaa, hivi jamani tuchukulie maisha tulikotoka, huyo mwanamke hivyo vifaa vya kununua labda vya 120,000 na huduma za mtoto ambazo ni za kuanzia mwaka sifuri hadi mitano, unaambiwa ukalipie, hela zitatoka wapi? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Serikali inajua kabisa uzazi ni kitu ambacho mtu lazima akajifungulie hospitali kama tunavyohamasisha watu. Unamwambia akanunue vifaa vya kwenda navyo hospitali; anavipata wapi? Hospitali nyingi za mikoa yetu, siyo lazima iwe Morogoro, lakini naamini maeneo mengi Tanzania tunaambiwa tukanunue vifaa wakati mwanamke anakwenda kujifungua, wakati Serikali inasema kwamba mwanamke anapata huduma bure, lakini bure haipo, hasa katika mambo ya operation.

Mheshimiwa Spika, nataka kuzungumzia upande wa elimu. Upande huu tuna changamoto, kuna wenzangu wengi wamezungumzia kuhusu upande wa elimu. Elimu yetu ya Tanzania tunamshukuru mama Samia wa Awamu ya Sita ametoa elimu bure, lakini ile elimu bure imekuwa na changamoto nyingi kwa kipindi hiki. Elimu kweli ni bure kwenye majengo, lakini ile elimu haiwezi ikawa elimu bila vitendeakazi. Kwa mfano vitabu; shule nyingi hazina vitabu. Sasa vile vitabu tutavitoa wapi?

Mheshimiwa Spika, unaweza ukakuta watu wengi sasa hivi watoto wao wakifaulu kwenda sekondari, wanawaambia waandike vibaya ili wafeli, maana anaona kwamba akienda sekondari atatoa wapi hela za kununua vile vifaa shuleni; uniform, vitabu na vinginevyo.

Mheshimiwa Spika, sasa naishauri Serikali; tuna…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Kengele ya pili imeshagonga Mheshimiwa Kamguna, malizia sentensi.

MHE. ALEKSIA A. KAMGUNA: Mheshimiwa Spika, tuna shirika la ku-print vitabu vya Serikali, naishauri TAMISEMI kwa nini tusitumie zile mashine za kwenda kutengeneza vitabu, hatimaye watoto wetu waweze kupata vitabu kwa bei nafuu badala ya sisi wenyewe kukaa na kuhangaika halafu watu hawaendi shule.

Mheshimiwa Spika, pointi yangu ya pili…

SPIKA: Ahsante sana.

MHE. ALEKSIA A. KAMGUNA: Mheshimiwa Spika, naomba nimalizie; pointi ya pili, ninaomba turudishe elimu ya maarifa ya nyumbani kwa sababu watu wengi tunasema kwamba kuna utapiamlo, watu hawana elimu ya kutosha, turudishe hiyo elimu ya kusoma sayansi ya nyumbani, needlework na cookery.

Mheshimiwa Spika, kwa hayo machache, naunga mkono hoja. Ahsante. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Kilimo
MHE. ALEKSIA A. KAMGUNA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipatia nafasi. Awali ya yote, hatuna budi kumshukuru Mwenyezi Mungu aliyetupatia uhai. Nampongeza Mheshimiwa Samia kwa kazi anazozifanya yeye na wasaidizi wake pamoja na Mawaziri na Watanzania wote kwa ujumla.

Mheshimiwa Spika, nimesimama kwa ajili ya kuchangia kwenye hii bajeti ya kilimo kama inavyojieleza yenyewe, katika ukurasa wa 11 aya ya 26, amesema kwamba, upande wa mazao mwaka 2020 mazao yalipatikana kwa asilimia tano, mwaka 2021 ilikuwa asilimia 3.6 na mwaka 2020 tena katika upande wa kipato ilikuwa ni asilimia 15.4 na mwaka 2021 ilikuwa ni asilimia 14.6.

Mheshimiwa Spika, katika Tanzania idadi yetu ni milioni 61.74, lakini walio wengi ni wakulima ambao ni asilimia 65. Wakulima hawa ukiwaangalia sana kwa haraka haraka ni watu ambao kidogo ni wenye shida nyingi na changamoto nyingi. Wao wamesema kwamba katika ukurasa huo, aya ya 26, wanasema kilimo kilipungua na mapato pia lilipungua kwa sababu ya Uviko-19 pamoja na vita vya Ukraine. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mimi naenda mbali zaidi, siyo vita tu na Uviko-19, mmeacha kitu kikubwa tu; migogoro ya wakulima na wafugaji. Migogoro ya wakulima na wafugaji pamoja na tembo, hao ndio wamefanya wakulima warudi nyuma. Kwa sababu Uviko vijijini walikuwa hawavioni, wakulima wadogo wadogo walikuwa wakiendelea na kazi, lakini wakilima kule vijijini watu wa mifugo wanaingia wanakula; tembo wanaingia wanashambulia yale mazao; lakini wanaposhambulia, tembo ana mtetezi wake ambaye ni Wizara ya Maliasili na Utalii, anakwambia wewe mazao yako yameliwa kwa sababu umelima kwenye shoroba. Mtu wa mifugo, Wizara yake inamtetea pia, inasema kwamba, mtu wa mifugo kazi yake, amewaandalia chakula, kutengeneza manyasi, ambayo ameyapanda. Sasa yale manyasi hayatakua ndani ya miezi mitatu au miezi sita. Sidhani kama mtu ana ng’ombe 100 atalisha kwenye robo heka, itamuchukua muda. Je, huyu mkulima katika kipindi hiki atakuwa Halimi, ataishije? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mkulima anaonekana kama hana mtetezi, ni mkiwa. Kama tembo anatetewa na maliasili, kama mfugaji anatetewa na Wizara ya Mifugo: Je, huyu mkulima anatetewa na nani? Katika hotuba yake sijaona sehemu yoyote ameainisha kwamba mkulima tumsaidie katika hatua hii na hii, katika hali hii. Jamani, hicho kilimo kitaendaje? Umetenga hela nyingi sana kwa ajili ya skimu za wakulima, lakini zile skimu zitaenda kufanya kazi gani kama mtu analima, halafu mazao yake yanaliwa na tembo, mazao yake yanaliwa ni mifugo? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwanza Wizara ya Kilimo kama inavyosema, imwangalie mkulima, mnamteteaje mkulima huyu ambaye ni yatima? Hatuwezi tukapanga bei wakati kile kilichovunwa hakipo. Sasa tunaomba Wizara ya Kilimo imtetee mkulima ambaye ni yatima. Kwa mfano, hususan Mkoa wa Morogoro, mnajua kabisa ule ni Mkoa wa kimkakati, kama Wizara ya Kilimo mngesimama, tungeweza kulisha Tanzania nzima, lakini kwa kuwa tumebaki yatima, Morogoro itakuwa ni masikini kuliko ilivyokuwa hapo awali, kwa sababu haina mtetezi.

Mheshimiwa Spika, naomba Wizara hii iangalie, kama wao wameweka nyasi, hao watu wa mifugo, na maliasili wanasema tunalima kwenye shoruba: Je, ninyi mnatuteteaje wakulima? Naomba mnapomalizia hapa unijibu kwamba, ninyi mmejipangaje katika kumtetea huyu mkulima ambaye ni yatima? Hilo la kwanza. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, la pili nazungumzia kuhusiana na usalama wa chakula. Katika Tanzania, zamani kulikuwa na National Milling, watu wanachukua vyakula wanaweka dawa kwenye magunia na kwenye mifuko, lakini walikuwa wanakoboa National Milling, kumbe vile vyakula vina dawa ndani yake. Sasa hivi unakuta kila kona vimezagaa viwanda vya kukoboa mahindi: Je, usalama wa huyo Mtanzania uko wapi? Kwa mfano, kule Dar es Salaam Manzese, unakuta unaenda, kuna viwanda, lakini kuna maji kwenye kikopo. Sasa yale maji yatasafisha yale mahindi jamani? Matokeo yake unakuta kwamba, watu tunakula sumu na wanapata magonjwa mengi kama ya kansa kwa sababu hatudhibiti hivyo vyakula. Tunaomba Wizara ya Kilimo msimamie, ili tuweze kupunguza haya magonjwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia kuna kilimo hiki cha mbogamboga, tunapulizia dawa. Hizi dawa katika kupulizia, hamjawaelimisha wale wakulima wadogo wadogo. Wakipulizia dawa baada ya siku mbili mtu anaziuza zile mboga; akishaziuza, walaji wanakula, hatujui mle ndani kuna nini? Matokeo yake magonjwa tena yanaongezeka. Kwa hiyo, naomba Wizara ya Kilimo mliangalie hilo, kwamba wakulima ni watoto yatima.

Mheshimiwa Spika, mkitaka tuendelee, kwanza mkae ninyi Wizara ya Kilimo na Wizara ya Mifugo ili mjue kwamba mtatatuaje tatizo la wakulima na wafugaji kwa Tanzania nzima hususan Mkoa wa Morogoro? Pia mkae muone kwamba mtatatuaje hilo tatizo la sumu ambazo nafikiri Watanzania wengi tunakula sumu, baada ya kuwa tunakula sumu, tunatumia hela nyingi sana katika kujitibia, basi mtafute namna ya kusimamia hiyo miradi yetu ambayo tunawawezesha wakulima wadogo wadogo, tusiwaache, lakini tuwasimamie hatimaye nao waweze kujikwamua. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hayo, machache, naunga mkono hoja. Nashukuru. (Makofi)
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2022 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024
MHE. ALEKSIA A. KAMGUNA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipatia nafasi. Awali ya yote sina budi kumshukuru Mwenyezi Mungu ambaye ametupatia ruzuklu ya uhai. Pia nampongeza Mheshimiwa Rais Samia kwa kazi anazotupambania pamoja na wafanyakazi wake wote wanaomsaidia, Mawaziri, Makamu wa Rais, Waziri Mkuu, Mawaziri wote tunawapongeza pamoja na Watanzania kila mmoja kwa nafasi yake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza sana Mheshimiwa Rais Samia, ametufanyia mambo makubwa sana katika hii miaka yake miwili ya Awamu ya Sita. Sisi hasa watu wa Malinyi ambao tuko pembezoni ya miji tulikuwa tunalalamika, kama mwaka juzi nililalamika sana kuhusu barabara, lakini tarehe 16 walienda kusaini mkataba huu wa EPC + F kwa ajili ya matengenezo ya ile Barabara. Ninaamini ile shida ya barabara ambayo tulikuwa tunaipata sasa tutaondokananayo, kwani itatuunganisha kutoka Lupilo – Malinyi – Namtumbo na hatimaye Ruvuma. Tunakushukuru sana Mheshimiwa Rais. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais ametutendea mengi. Katika awamu yake hii ameimalizia miradi ile mikubwa ya kimkakati ambapo watu wengi, Watanzania tulikuwa na wasiwasi, lakini wasiwasi ule Mheshimiwa Rais ameumaliza. Mradi wa reli ya SGR, Mradi wa Daraja la Busisi, Mwanza na Mradi wa Bwawa la Mwalimu Nyerere ambalo ni bwawa kubwa, tunajivunia na limetumia fedha nyingi sana. Tunamshukuru Mheshimiwa Rais pamoja na watendaji wote tunawashukuru. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kwenda kwenye hoja kwamba, katika Bwawa la Mwalimu Nyerere lile bwawa ni la mkakati katika nchi yetu ya Tanzania, lakini ni bwawa ambalo limepita kwenye Mikoa, na sehemu kubwal imepita katika Mkoa wa Morogoro. Katika ule mkoa kuna sehemu ambazo zimepitiwa. Kwa vyovyote vile, maendeleo yoyote huwa yakifika lazima kutakuwa na baadhi ya watu kuathirika. Katika kuathirika kule, wale wananchi wamekubali na wamesema kwamba bwawa liendelee kwa sababu faida yake ni kubwa kuliko hasara ambazo tumezipata. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nachukulia Mkoa wa Morogoro, hususan Bonde la Kilombero. Bonde la Kilombero ni bonde ambalo lile bwawa ni sehemu ambayo inapatikana maji kwenye chanzo, hasa katika Kijiji cha Ngombo. Kile Kijiji cha Ngombo kilifanyiwa tathmini mwaka 2022 mwezi wa kumi na moja mpaka mwezi wa kumi na mbili, 2022. Baada ya kufanyiwa tathmini ya nyumba, makazi, makaburi, na kadhalika, lakini Serikali tangu pale iko kimya. Wale watu hawajapata fidia. Hatujui wale watu ile fidia wataipata lini? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa katika kupata fidia, naiuliza Serikali, yule mwananchi wa Ngombo ambaye anatakiwa kuondoka; na tumekubali kuondoka, na ni wajibu wetu kuondoka kupisha lile bonde: Je, atakapoondoka, anakwenda wapi? Huko anakokwenda, ataishije? Maana hajapata fidia? Kule Ngombo kuna shule ya msingi, wale watoto wao watakapoondoka wataenda kusoma wapi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba Serikali ituelekeze hayo kwa sababu, wale ni wakulima, sasa hivi ni kipindi cha mavuno, watu hawaambiwi chochote kwamba mnatakiwa kuondoka, lakini hawajapewa ile timeframe. Kitakapofika kipindi cha kuanza tena kilimo, wale watu wataambiwa waondoke. Sasa kwa nini usimweleze mtu kipindi hiki ambacho anavuna, ajue kwamba nikimaliza kuvuna, nitaelekea wapi? Badala ya kumsubiria kipindi cha kiangazi ambacho anataka kuanza tena msimu mwingine wa kulima, watu wanaambiwa waondoke?

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaiomba Serikali, chonde. Tunajua Serikali ya Mama Samia ni sikivu. Tunaiomba itupatie fidia mapema iwezekanavyo ili wale watu waondoke eneo husika na hatimaye waweze kupata makazi mapya na waendelee na maisha yao kwa amani, kama walivyofanyiwa wenzetu wa Msowelo, wametoka Ngorongoro, wameenda Handeni, Tanga, wamepewa malipo yao, wameondoka kwa usalama. Nami naamini hata zoezi la Ngombo nalo litafanyika kwa amani ili nchi yetu iendelee kuwa na amani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala langu la pili, nazungumzia kuhusu wanyama. Mkoa wa Morogoro ni Mkoa ambao kila siku nasema tumebahatika. Miongoni mwa mikoa iliyobahatika Morogoro ni mmojawapo. Tumepitiwa na mbuga ya Wanyama ya Selous ambayo sasa hivi tunaiita ya Mwalimu Nyerere, Mikumi, Udzungwa, na kadhalika, lakini Mkoa ule tuna adha. Tembo au wanyama wakali wanatusumbua. Sasa katika wale wanyama wakali jamani, ukiangalia sana kimkoa, unakuta ule mkoa sisi kama Serikali isipokuwa na huruma ya kutuangalia, kuwe na mkakati wa makusudi kwa ajili ya kuwaokoa wananchi wa mkoa ule. Ukweli sisi tutaisha kwa sababu, ule mkoa unapakana na hizo mbuga. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi ninapoongea hapa katika Wilaya ya Mvomero, kuna Wilaya ya Malinyi na Wilaya ya Kilosa. Mfano, Wilaya ya Mvomero ni Wilaya ambayo inapakana na Tarafa ya Mlali ambayo ina Kata za Doma, Lubungo, Merera, Msongozi na Mangai. Sasa hivi ninavyoongea hapa, katika mwaka huu tu, watu 42 wameshafariki katika Wilaya ya Mvomero, Tarafa ya Mlali. Ombi letu ni nini kwa Serikali? Hatuwezi tukasema kwamba zile mbuga hatuzipendi, tunazipenda sana, lakini sababu ni nini ambayo inafanya wale wanyama watoke kwenye njia zao au kwenye maisha yao ya asili waje kwenye miji ya watu? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sababu ni kwamba, unakuta kwenye zile mbuga za wanyama kuna watu wanaishi kule wenye mifugo. Wafugaji wameingia kwenye zile mbuga zetu. Sasa zile mbuga wanavyoingia kule wanasababisha wale wanyama wanashindwa kuishi kwenye maeneo yao ya asili. Wanapika na wengine wamejenga kwenye njia za wale Wanyama. Matokeo yake wale wanyama wanatoka, wanakuja kwenye makazi ya watu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kule kwenye mbuga kuna Askari ambao ni Askari wa Wanyamapori. Why yule mfugaji anajenga kibanda, ana ng’ombe labda 2,000? Ina maana wale Askari hawawaoni hao ng’ombe 2,000? Hawawaoni hao wachungaji? Hata hivyo wale wanyama wanatoka wanakuja kwa watu kwa sababu eneo lao la asili limekaliwa na watu ambao wanawasumbua. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa maana hiyo ni kwamba, Wizara ya Maliasili kwa namna nyingine inahusika kupitia Askari wao. Inakuwaje wanyama na wale binadamu ambao wanaingia kwenye zile mbuga wasiwaone, lakini mwananchi wa kawaida akienda kutafuta kuni anaonekana? Ina maana wale wanyama hawaonekani? Ni wadogo kiasi kwamba mwananchi wa kawaida anaonekana? Tunaiomba Serikali, chonde ituonee huruma, ituwekee fence ikiwezekana. Tupate angalau tuweze kuzuia wale wanyama wasiingie kwenye makazi ya binadamu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala langu la tatu, sisi Morogoro ni Mkoa ambao una mkakati. Ni Mkoa ndani ya mikoa yenye mikakati ya kilimo. Tunamshukuru Mungu na kweli Waziri wa Kilimo ametupelekea wataalamu kule. Nililalamika sana kuhusiana na suala la kwamba hatuna soko la mazao hasa ya mpunga, lakini kuna wataalamu wako kule, wanakaa wanafanya tathmini kuona ni jinsi gani ya kuendesha hilo soko.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini katika huu mkoa, kuna shida ya ushuru. Wakulima wengi wakienda kupeleka mazao yao, kwa mfano, Serikali mlituambia kwamba mtu anatakiwa kulipishwa mpaka ifikie tani moja ya mzigo, lakini sisi mtu akiwa hata na kilo 20 analipishwa; akiwa na kilo 80, analipishwa: Je, Serikali ule uamuzi wa kusema kwamba wananchi wanatakiwa walipie kuanzia tani moja umesahaulika? (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. ALEKSIA A. KAMGUNA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naunga mkono hoja. Tunaomba Serikali mtusaidie, ule mkoa jamani ni wa kimkakati, ili tuweze kuishi kama wengine wanavyofurahia maisha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante na naunga mkono hoja. (Makofi)