Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Shabani Hamisi Taletale (4 total)

MHE. HAMISI S. TALETALE Aliuliza:-

Je, ni lini barabara ya Bigwa – Kisaki itaanza kujengwa kwa kiwango cha lami kama Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) Mwaka 2020 – 2025 inavyoelekeza?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI Alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Hamisi Shabani Taletale, Mbunge wa Morogoro Kusini Mashariki, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara ya Bigwa – Mvuha – Kisaki ni barabara ya Mkoa yenye urefu wa kilometa 133.28 ambapo kilomieta 18.4 ni za lami na kilomita 115.14 ni za changarawe. Barabara hii ni kiungo muhimu kwa Mkoa wa Pwani na Morogoro na pia ni barabara inayoelekea katika Mradi wa Bwawa la kuzalisha umeme la Julius Nyerere katika Mto Rufiji ambalo ujenzi wake unaendelea.

Mheshimiwa Naibu Spika, kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa barabara hii ilikamilika mwezi Novemba, 2017 chini ya Kampuni ya Uhandisi ya UNITEC Civil Consultants Ltd ya Tanzania kwa ushirikiano na Kampuni ya Multi-Tech Consult (Pty) Ltd ya Gaborone, Botswana.

Mheshimiwa Naibu Spika, ujenzi wa barabara hii kwa kiwango cha lami utaanza kulingana na upatikanaji wa fedha. Wakati Serikali inatafuta fedha za ujenzi, imeendelea kutenga fedha za matengenezo mbalimbali ili barabara hii iendelee kupitika majira yote ya mwaka. Aidha, katika Mwaka wa Fedha 2020/2021 jumla ya shilingi milioni 1,492 zimetengwa kwa ajili ya matengenezo ya barabara husika. Ahsante.
MHE. HAMISI S. TALETALE aliuliza: -

Je, Serikali ina mkakati gani wa kukuza kilimo cha mazao ya viungo katika Wilaya ya Morogoro Vijijini?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Hamisi Shabani Taletale, Mbunge wa Jimbo la Morogoro Kusini Mashariki, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeandaa mkakati wa kuendeleza mazao ya bustani (National Horticulture Development Strategy 2021 - 2031) yakiwemo mazao ya viungo. Ambapo mazao ya iliki, karafuu, vanilla, pilipili manga, tangawizi na mdalasini ni kati ya mazao ya bustani yaliyopewa kipaumbele katika mkakati huo unaolenga kuongeza uzalishaji wa mazao, kuboresha mazingira ya biashara na kuongeza Pato la Taifa linalotokana na mazao hayo.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika Wilaya ya Morogoro Vijijini Serikali kwa kushirikiana na Sustainable Agricultural Tanzania (SAT) inatekeleza mradi wa kuendeleza mazao ya viungo katika maeneo yanayozunguka Milima ya Uluguru (Uluguru Spice Project) kuanzia mwaka 2017. Mradi huu umenufaisha wakulima 1,668 katika vijiji 27 vilivyopo Kata za Tawa, Kibongwa, Konde, Kibungo, Mtombozi, Kisemu, Mkuyuni, Kinole. Vilevile, katika kuimarisha uendelezaji wa mazao ya viungo, Chama cha Msingi cha Ushirika wa Wakulima wa Viungo (CHAUWAVIMU) kimesajiliwa kwa lengo la kuimarisha uendelezaji wa mazao ya viungo (pilipili manga, mdalasini, karafuu, taangawizi, iliki na vanilla) katika Wilaya ya Morogoro Vijijini.
MHE. HAMISI S. TALETALE aliuliza: -

Je, lini Serikali itakamilisha Ujenzi wa Kituo cha Afya Kata ya Ngerengere?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Hamisi Shabani Taletale, Mbunge wa Jimbo la Morogoro Kusini Mashariki, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kituo cha Afya Ngerengere kilisajiliwa mwezi Mei, 1995 na kinatoa huduma ya ngazi ya Kituo cha Afya ikiwa ni pamoja na huduma za upasuaji wa dharura na huduma nyingine. Aidha, kituo hiki kinahudumia wastani wa wagonjwa 1,200 kwa mwezi na 14,000 kwa mwaka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kituo hiki kina upungufu wa baadhi ya miundombinu ikiwemo jengo la Huduma za Mama na Mtoto na Upasuaji, jengo la Maabara, jengo la kuhifadhia maiti na jengo la kufulia. Eneo la Kituo hicho lina ukubwa wa ekari nne na nusu, hivyo halitoshelezi mahitaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro, inaendelea kufanya mazungumzo na Shirika la Posta ambalo linamiliki eneo mkabala lenye ukubwa wa ekari mbili ambalo halijaendelezwa ili litumike kupanua Kituo cha Afya cha Ngerengere, ahsante.