Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Shabani Hamisi Taletale (8 total)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi
MHE. HAMISI S. TALETALE: Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwanza ningependa kumpongeza Mheshimiwa Rais wetu Mama Samia Suluhu Hassan kwa mema yake anayofanyia Nchi yetu ya Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pili, nipende kumpongeza Mheshimiwa Waziri kaka yangu pamoja na jopo lake. Huyu Waziri ana kitu ndani yake, atafika mbali. Naona kabisa wakati tunapambana na Barabara yetu ya Bigwa – Kisaki, nilimsumbua akaniita nyumbani kwake, lakini pia akaniita ofisini na jopo la wataalam 20. Nikashangaa mimi mtoto wa Kiluguru hawa wataalam 20 nitaongea nao nini? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wale wataalam wakaniambia tunakuhakikishia hii barabara tutaipata, njia ni kupata fedha, bado naendelea kusema Mheshimiwa Waziri ana kitu ndani yake, atafika mbali. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri alisema nitaongea na mama yako na leo nathubutu kusema katika ule Mkoa wa Morogoro katika Wabunge wanaopendwa na Mama Samia, mimi ni number one. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa kupata Barabara ya Bigwa – Kisaki, kilometa 73 ambayo haijawahi kutokea, mimi number one. Wamepita Wabunge kibao huko nyuma na wananchi wangu wameniambia usipotuletea Barabara ya Bigwa – Kisaki hurudi hapa. Wameona matangazo ya Mheshimiwa Waziri pale kwamba Juni tunakwenda kusaini ile barabara na mimi nauona mlango wangu wa kubaki Kusini Mashariki. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niendelee kuipongeza hii Wizara na niendelee tena kumpongeza Mheshimiwa Rais wetu, Mama Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutupa Barabara yetu ya Ubena – Zomozi ya kilometa 11. Hii Barabara ya Bigwa – Kisaki inakwenda kufungua mipaka na tunakwenda kukutana na mtani wangu kule Mchengerwa. Nimwombe Mheshimiwa Waziri tumeona matangazo ya Juni, 2023. Naomba specific date kwamba naomba tarehe na mimi nikamuwekee mziki mnene pale. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nikuhakikishie hiyo tarehe ambayo tunakwenda kusaini ule mkataba, nataka Taifa lijue Mama Samia ameweka alama, ameweka mguu mzito pale Kusini Mashariki na sisi tunakwenda kuonekana, tunakwenda kutoka kwenye matatizo. Ile Barabara, leo hii Dar es Salaam wanakula matunda yanatoka Morogoro Vijijini, Iringa wanakula matunda yanatoka Morogoro Vijijini. Hata hapa Dodoma wanakula matunda yanatoka Morogoro Vijijini. Ukizungumzia Bigwa – Kisaki leo hii unazungumzia wauza juice wengi wa pale Dar es Salaam. Nimwombe Mheshimiwa Waziri, hii Juni, 2023 tunaomba tujue specific date ili na nimwandalie muziki mnene asubuhi pale na kuandaa watu wampokee. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nikuhakikishie, hii Wizara ina watu ambao naendelea kuwaambia watafika mbali. Kaka yangu Kadogosa ana kitu ndani yake, atafika mbali. Mkurugenzi wa Shirika la Ndege, ndugu yangu ana kitu ndani yake, atafika mbali; lakini mtu mzito kabisa kaka yangu, bosi wa TBA, huyu ana kitu hasa ndani yake, atafika mbali. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo naunga mkono hoja, sina mbambamba nyingi. Namkaribisha Mheshimiwa Waziri Kusini Mashariki, tuzindue barabara yetu, tusaini mkataba wetu. Ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo
MHE. HAMISI S. TALETALE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwanza kabisa napenda kuipongeza Wizara hii ya Michezo, lakini pia nimpongeze Mheshimiwa Rais kwa kile alichokifanya kwenye hii Wizara kutuletea Mawaziri majembe. Kikubwa ambacho naendelea kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa kutuletea Waziri kutoka Tanga, Ndugu yangu Hamis Mwinjuma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati Mheshimiwa Waziri anachaguliwa nakumbuka nilikuwa Marekani, lakini Waziri alikuwa na kidevu cheusi kabisa hakina mvi hata moja, alikuwa anakicheka cha kwangu, Mheshimiwa Waziri leo hii ana kidevu cheupe kwa sababu ya mzigo mzito wa Wizara aliyopewa. Wizara kubwa, Wizara ambayo inachangia furaha ya nchi nzima, Wizara ambayo Bunge lako lina furaha kwa sababu ya hii Wizara, ila Wizara hii inatia aibu, tunakaa hapa mbele Wizara ina bajeti ndogo kuliko Wizara yoyote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais ana mapenzi ya dhati na hii Wizara, tuseme wazi ameingia madarakani Mheshimiwa Rais akaelekeza watu wa michezo ya kubashiri wapeleke pesa asilimia tano inayopatikana. Yote hayo ni kupambana na hii Wizara ili ikapate pesa. Mimi ni Mjumbe wa Kamati ambao tunasimamia hii Wizara, ni aibu kusema mengi, Wizara haina pesa hii, tunamtia mvi ndugu yangu Mwana FA na dada yake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi niongee kidogo, leo hii hawa Wizara imeletewa Fungu bilioni 900 Mwezi wa Pili, mwaka huu. Ukimuuliza Waziri hapo hajui hiyo miiloni 900 ya nini, tuseme ukweli kwa heshima niliyonayo…

MHE. NEEMA W. MGAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MHE. HAMISI S. TALETALE: Mheshimiwa Mwenyekiti, … kwako na …

MHE. NEEMA W. MGAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

TAARIFA

MWENYEKITI: Mheshimiwa Hamisi kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Neema Mgaya.

MHE. NEEMA W. MGAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi. Nampongeza anachangia vizuri Mheshimiwa Taletale, lakini nataka tu aweke rekodi vizuri sio bilioni 900 ni milioni 900, ahsante. (Makofi)

MWENYEKITI: Ahsante, Mheshimiwa Hamisi taarifa unaipokea?

MHE. HAMISI S. TALETALE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimepokea na nimezoea kuzungumza kuhusu ma-b kumbe kuna ma-mi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara inapelekewa milioni 900 ya kitu ambacho wao hawajui, leo dada yangu Mheshimiwa Waziri, leo naondoka na shilingi yake, ikiwezekana akamtafute Waziri wa Fedha, maana yake hapo mbele hayupo. Tujue je, hiyo milioni 900 anayopewa, inawezekana hata Mheshimiwa Rais ameelekeza hii five percent iende kwao, lakini pia hajui hiyo milioni 900 waliyopewa ya mchanganuo gani. Kwa hiyo, niombe tunataka kujua hizo pesa zinazokuja kwenye Wizara yetu ya Michezo zinakuja kwa utaratibu upi, kwa namba ipi? Maana ukisema leo hii Wizara imeletewa milioni 900 Mwezi wa Pili, wakati watu wa michezo ya kubashiri kila mwezi wanatoa pesa, kwa hiyo, wananyimwa haki yao. Nani wa kusimamia haki yao kama sio sisi kama Bunge.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme kitu kingine hapa, maendeleo ya michezo tuangalie wenzetu kama Senegal, Senegal ni nchi ambayo ina wananchi milioni 16, Tanzania tuko zaidi ya milioni 60, Senegal ukitazama mashindano makubwa ya ndani ya Afrika yote Senegal wamechukua. Sisi tupo tu, tunahangaika kubebesha mzigo kuipa TFF. Nimpongeze sana Ndugu yangu Karia na timu yake, tunahangaika kubebesha mzigo kumpa Mama Samia. Jamani juzi nimesema mimi ni kipenzi cha yule mama, wanamtia presha mama yangu. Watafuteni utaratibu, watafute njia ya kuangalia jinsi gani hii Wizara itapata pesa, tuwe wawazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali wakae, hii ni michezo ya kubashiri, waibebe kama ilivyo waipeleke Wizara ya Michezo, wanashindwa nini? Leo hii tunakuja kuzungumzia michezo hapa, kuna Wizara ina zaidi ya trilioni tatu, Wizara ya Michezo ina bilioni 35, ni udhalilishaji huo, ni aibu kwa Wizara na ni aibu kwa Serikali ya Awamu ya Sita ya Mama Samia. Kama tunataka kumsaidia Rais positively, lazima tuangalie tunakwama wapi? Lazima tuangalie tuna dhamira gani, dhamira ya kutaka kumsaidia Rais, hii michezo ya kubashiri…

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme kitu, Nchi kama Uingereza labda tuseme ni nchi kubwa wao wana michezo ya kubashiri ya nchi, wanasema Gaming Board ya Nchi, lakini ile michezo ya kubashiri inapeleka 50 percent kwenye Wizara ya Michezo, tunaona inaendelea. Basi nizungumzie nchi ya jirani yetu hapo Kenya, utaratibu wao wamesema mpaka 2030 watatoa bilioni 11 kwenye Wizara ya Michezo, hiyo ni kwa mwezi, lakini tazama sisi tuna bilioni 35, humo kuna mshahara wa Mwana FA sijui kuna mshahara wa nani, khaa! Kuna vitu vingine vinaumiza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama tuna dhamira ya kuisadia hii Wizara ambayo nimeona jana Mheshimiwa Rais amesimama anatamba kwamba ana dhamira ya dhati ya kuisaidia Wizara ya Michezo, lakini leo hii sisi tunashindwa kukaa, kujadili jinsi gani Wizara ya Michezo itasonga mbele. Tuongee wazi, leo hii mimi na ujana wangu na kutembea tembea kwenye baadhi ya nchi, Wizara za Michezo zinatazamwa, lakini leo hii kwenye Bunge lako Tukufu tuongee ukweli ndio Wizara ambayo tumeipuuza, hatutaki kuisika, inadhalilisha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme neno langu la mwisho, nitashika shilingi ya Mheshimiwa Waziri kama sijaelezewa ile asilimia tano aliyoelekeza Mheshimiwa Rais inakuja kiasi gani mpaka amepata milioni 900.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. (Makofi)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Elimu, Utamaduni na Michezo kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023
MHE. HAMISI S. TALETALE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, kwanza kabisa napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu Azza wa Jalla, lakini pia nimshukuru Mheshimiwa Rais wetu wa Awamu ya Sita, Mama Samia Suluhu Hassan lakini vilevile niishukuru Kamati yetu, Mheshimiwa Mwenyekiti na Wanakamati wenzangu wote kwa ujumla.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo nitachangia eneo moja la michezo na nimshukuru Katibu wa Bunge, aliyepanga majina amepanga kiutaratibu. Ameanza na Profesa akaenda kwa Mama pale akaja kwangu Dkt. Taletale. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ninachangia kwenye suala la michezo. Watu wote humu ndani, labda tujizime data, lakini tunafahamu michezo ni uhai, tunafahamu michezo ni amana ya nchi hii. Kabla sijaenda mbali, wiki iliyopita tulikuwa tuna bonanza letu la michezo wale wenzetu, wapinzani wetu wakiongozwa na striker wao kaka yangu Mwingulu Nchemba, wakanunua mchezaji kutoka nje ni kwa sababu ya michezo tulikutana pale. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini tukirudi kwenye hii Wizara ya Michezo. Wizara hii ni kama Wizara yatima katika Wizara zote ambazo zinaongozwa na Serikali ya Awamu ya Sita. Mimi nimechoka kuimba neno michezo, kuimba jamani Wizara ya Michezo ipewe fedha. Lakini Mheshimiwa Rais, kwa mapenzi yake ya dhati na kwa mapenzi ya kuonyesha anapenda michezo akaielekeza Wizara ya Fedha, kutoka kwenye michezo ya kubashiri wapeleke asilimia tano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini wakija kwenye Kamati ile asilimia tano kama bado wanaomba. Alhamdullilah, brother wangu Mwigulu yuko hapa; mimi leo ningeomba, na hata Mheshimiwa Mwigulu, aongee kwamba ile asilimia tano ambayo inatoka kwenye michezo ya kubashiri tungependa kujua exactly date. Kwa mfano mwezi wa nne tarehe fulani asilimia tano itatoka Wizara ya Fedha, itakwenda Wizara ya Michezo, ni aibu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi tunajifunza kwenye nchi zilizoendelea. Leo hii kama Sports Betting inafanya vizuri Japani, ipo ndani ya Wizara ya Michezo, inafanya vizuri Uingereza ipo ndani ya Wizara ya Michezo. Kaka yangu Mheshimiwa Mwigulu, mimi nikuombe kama hautojali hili gurudumu lote hili la michezo ya kubashiri ipeleke pale Wizara ya Michezo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushahidi huu mimi ninao kutokana na Serikali ya Uingereza ambako Michezo ya Kubashiri ipo ndani ya Wizara ya Michezo, Serikali ya Japani, Michezo ya Kubashiri ipo ndani ya Wizara ya michezo. Kama mnaona ni suala la fedha hata Wizara ya Utalii, inatengeneza pia fedha mbona haipo ndani ya, mifano hiyo midogo midogo. Lakini mmeona kwa sababu huku kuna michezo, kuna fedha basi mnaona hii Wizara ya Michezo, isiwekewe fedha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa nimeongea vitu viwili. Kitu cha kwanza naomba Wizara ya Fedha kama haitojali isimame itutajie exact date ya ile 5% ambayo ipo kisheria Mheshimiwa Rais, ameelekeza Wizara wapatiwe hii fedha hawapewi. Hata ukiwahoji hawakumbuki lini wamepata huyo hapo mtani wangu wa Kingoni na anongeza kubadilisha miwani tu ya lens kwamba haoni vizuri kwa sababu fedha hapati. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina Kaka yangu, ndugu yangu Mwana FA. Unajua kuna Wizara ukiwa unaona ujiko ni hii Wizara ya Michezo, ni Wizara ujiko, lakini ujiko wenyewe ni ujiko wa kutokuwa na fedha brother. Mimi nikwambie, wiki iliyopita tumepata bahati ya kutembelea Uwanja wa Taifa na; hata hivyo tukapata bahati ya kutembelewa na mtu kutoka kwenye Gaming Board. Yule bwana anachoongea anadhani sisi hatuna mamlaka ya kuitoa Gaming Board kutoka kwenye Wizara ya Fedha, kuleta Wizara ya Michezo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kaka yangu Mheshimiwa Mwigulu, wewe ni Mwanamichezo, unajua michezo ni striker. Kuna Mbunge wa Bunge la Kenya, alikuja kucheza Arusha alipoona Mheshimiwa Mwigulu, hayupo uwanjani akaona hapa tunafungwa. Sasa kama kweli unajua Michezo, michezo bila fedha ni uongo jamani, Wizara ya Michezo haina fedha ABMT, haina bajeti hata sisi Wajumbe tukipata nafasi ya kusafiri kwenda kwenye Kamati yoyote, tukiwa tunasafiri na Wizara ya Michezo tunaanza kupiga lamli sijui tutajilipa? Unajua of course mkisafiri cash absorber lazima mpate kwenye Wizara, lakini Wizara yetu ya Michezo inatia huruma. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nimuombe Mheshimiwa Mwigulu, kama hatojali tunaomba Gaming Board ihamie Wizara ya Michezo. Kuhusu wataalam ituhamishie na wataalam, yote ipo Serikali moja, yote inaongozwa na Mama mmoja. Wakati nikiongea hapa Kaka yangu Mheshimiwa Tarimba, ananiangalia kwa sababu napiga sehemu ambayo yeye ndipo anajua zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini ukweli ni kwamba kama hii asilimia tano imeelekezwa na Mheshimiwa Rais, na bado Wizara inapuuza wasomi mnanitia mashaka mimi tabu darasa. Wasomi mnatuharibia michezo, wasomi ambao tunawategemea mjue umuhimu wa michezo mnatuharibia michezo, mnataka kuua ndoto za Mheshimiwa Rais. Mheshimiwa Rais, ndoto yake kubwa ni kuona michezo inakua nchini, lakini leo hii tunawaamini wasomi, kwamba mnajua bila fedha hakuna mchezo bado mmekumbatia fedha mnasubiria muda ufike mtembeze bakuli. Hii ndiyo nchi pekee ambayo inaoongoza kwa kutembeza bakuli. Hii ndiyo nchi pekee ambayo kiukweli, ndiyo tunaanza wale wengine…

MHE. TARIMBA G. ABBAS: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

TAARIFA

MWENYEKITI: Mheshimiwa Hamisi, kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Tarimba.

MHE. TARIMBA G. ABBAS: Mheshimiwa Mwenyekiti, Meshimiwa Taletale anatoa hoja nzuri sana, hoja ambayo inapaswa kuungwa mkono. Hivi hawezi akashauri Serikali Mheshimiwa Taletale, katika mchango wake kwamba Serikali ilete mapendekezo ya kubadilisha baadhi ya vifungu vya sheria vinavyohusu upelekaji wa ile asilimia tano? Kwamba sasa asilimia tano ile itajwe kwenye sheria kwamba ikifika tarehe kumi ya kila mwezi fedha zile ziwe zinapelekwa Wizarani kwenye Wizara ya Michezo.

MWENYEKITI: Ahsante. Mheshimiwa Taletale, taarifa unaipokea?

MHE. HAMISI S. TALETALE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naipokea kwa mikono miwili. Nakumbuka nimesema nina utaalam na ninachokiongea kwa hiyo hata ule mchele ambao unaingia kwenye Wizara kule anajua, ukija huku tataneemeka kiasi gani, Kaka yangu Tarimba, ahsante sana Wanakinondoni wana jembe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naendelea kuchangia. Kwenye hili suala la hii asilimia tano ya michezo ya kubashiri ambayo sisi tumepunguza makali ni kamali. Kwa sababu sisi Waislamu tunajua kamali haramu hatuwezi kusema kamali tunasema kubashiri, sawa. Hii michezo ya kubashiri, niiombe Serikali, niombe Kiti chako kielekeze Wizara, utaratibu wa hii asilimia tano ambayo imetajwa na Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, bado hawa Wizara hawapati hii fedha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nijue, kuna mtu anabisha na kauli ya Mheshimiwa Rais au? Mimi nimesema hapa Bungeni mara mbili kuna mtu anabisha na kauli yangu nikiwa Bungeni, shida ni nini? tuongee ukweli (let’s be honest). Kama tunafuata utaratibu wa kuchangia michango leo hii kuna michango mmechangia pale hotelini kuna baadhi ya watu hawajachangia vilevile.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nilipata bahati ya kwenda AFCON, nchi kama Ivory Coast imeendelea sana lakini imeendelea kwa sababu Serikali imeweka fedha kwenye Wizara yake ya Michezo, nchi kama Senegal imeendelea sana kuanzia timu zake zote za ndani inafanya vizuri, inafanya vizuri kwa sababu Serikali imeweka fedha kwenye michezo.

MHE. KHADIJA S. TAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

TAARIFA

MWENYEKITI: Mheshimiwa Hamisi, una taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Keysha.

MHE. KHADIJA S. TAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nimpe taarifa mzungumzaji na kum-support kwamba michezo ni sehemu moja wapo kama hii nchi tutaizingatia zaidi ni sehemu moja wapo ya kutengeneza ajira nyingi kuliko sehemu nyingine yoyote. Kwa hiyo, ni eneo ambalo Serikali ikitizama kwa umakini na kwa jicho la tatu ni sehemu ambayo tutaingiza fedha nyingi sana na tutakomboa lile tatizo letu la unemployment katika nchi yetu, ahsante.

MWENYEKITI: Ahsante. Mheshimiwa Hamisi, taarifa unaipokea?

MHE. HAMISI S. TALETALE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naipokea kwa mikono miwili. Mimi niongezee hapa maana wanasema kijiji bila wazee ni uhuni, wewe ni Mwenyekiti wa Bajeti, unajua mimi ninachokiongelea kinapita kwenye eneo lako. Sasa kama hujakaza wewe atakaza nani? Sikubani pabaya, najua nimeshambana kaka yangu Mheshimiwa Mwigulu. Tumuonee huruma yule Baba wa Kingoni pale, yule Baba wa Kingoni tia maji tia maji Wizara yake haina fedha anatia huruma, Mheshimiwa Rais, hajampa Wizara ili aje kuchubuka kuongeza mvi humu ndani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Rais amempa Wizara na ameelekeza fedha ije inapita kwenye Kamati ya Bajeti na wewe unaona. Basi nikuombe kwenye hili utafute njia ya sisi wapenda michezo, sisi Watanzania tuna amani kwa sababu michezo inafanya vizuri. Lakini bado inafanya vizuri kwa namna ya tia maji tia maji. Nikuombe nafahamu unalifahamu hili twende tukaangalie hii 5% kama alivyosema kwenye taarifa yake Kaka yangu Mheshimiwa Tarimba, tuombe tupate exact date kutoka kwenye Wizara ya Fedha, tujue hii 5% aliyoelekeza Mheshimiwa Rais, inakuja vipi na tarehe ngapi… (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana, Mheshimiwa. Muda wetu umekwisha.

MHE. HAMISI S. TALETALE: Mheshimiwa Mwenyekiti, hii ni kengele ya kwanza.

MWENYEKITI: Ya pili, muda wako umekwisha Mheshimiwa, malizia.

MHE. HAMISI S. TALETALE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo
MHE. HAMISI S. TALETALE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kwanza kabisa nashukuru, leo kwa mara ya kwanza na mimi nachangia kwenye Wizara ambayo imenilea. Ni Wizara ambayo upande wa sanaa najua madudu wanasema kindakindaki. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nianze na COSOTA. Naomba kumuuliza Mheshimiwa Waziri sisi tunafahamu wenzetu wa michezo wanaongoza michezo, mpira alikuwa kocha, alikuwa mchezaji lakini huku kwenye COSOTA sijui msomi kaoka wapi huko anakuja anaongoza COSOTA, hajui sheria yeye yuko busy tu kutung’ang’aniza wananchi tuseme tunafuata sijui utamaduni. Sawa, hakuna mtu asiyetaka kuufuata utamaduni wa nchi yetu, lakini COSOTA tumewekewa mapolisi ambao wanakwenda kuua utamaduni wa nchi, wanakwenda kuua muziki wetu.

Mimi nina mfano mmoja ambao mwaka jana, hapa kidogo na-declare interest, mwanamuziki wangu Diamond Platinum wimbo wake wa Hallelujah ulizuiliwa usipigwe na COSOTA, mwaka huo huo mwishoni waandaaji wa filamu ya Coming to America wakauchukua ule wimbo kama wimbo bora. Sasa wimbo umeenda kuwa bora nje ya nchi, nchi yenyewe yenye wimbo imeikataa. HaPa kuna walakini kwenye BASATA. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kingine ambacho naomba nizungumzie, wasanii wamekuwa wakilia sana sijui mirabaha, nini, hawalipwi. Leo hii media inalipa ili wasanii walipwe lakini COSOTA hawalipi. Mimi zamani nilikuwa napata pesa kutoka kwenye taasisi ya MCSK ipo Kenya na taasisi nyingine ya SAMBRO iko South Africa, COSOTA walipoenda kujiunga na SAMBRO, MCSK wasanii nchini hawalipwi. Hivi vitu viwili leo namwambia Waziri, nitamshikia shilingi mpaka nijue wasanii wanaanza kulipwa lini. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lingine ambalo mimi kiukweli linaniuma kwa sababu sisi ambao tunafanya burudani za viwanjani tumekuwa tukipigia simu sana kwa babu zetu vijijini, leo ziba mvua, zuia mvua. Katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri, sijaona aseme kwamba kuna sports arena inakwenda kutengenezwa. Tumechoka kufanya event za wazi, tunahangaika kuwapigia simu mababu vijijini wazuie mvua. I am from Africa bro! (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Spika, leo hii Rwanda ni nchi ambayo mpya tu leo hii wana sports arena yao, watu wa NBA wanakuja. Sisi hapa hatuna sports arena, sio tu hivyo wasanii wa Tanzania ni moja ya wasanii wakubwa East Africa, tunaongoza kwenye kila kitu. Tunapokosa kuwa na sports arena tunategemea kwenda kufanya show viwanjani, tunakosa kukuza sanaa yetu.

Leo hii nchi yetu Tanzania, hakuna asiyejua Afrika kama sisi ni corona free, wananchi wanaingia, tunakusanyika, hakuna tuzo za MTV South Africa kwa sababu watu hawakusanyiki. Wamekuja wanatuomba waje Tanzania lakini sisi tunawaambia hatuna sports arena. Wanashangaa, hee, hiyo nchi gani? Ni nchi ambayo ina uhuru, ina amani, viongozi wake tumekuwa tukiahidiwa tu tutajenga sports arena. Leo hii tumeenda kutafuta wawekezaji jamni twendeni tukatengeneze sports arena nchini kwetu. Lakini hivyo vigingi vilivyotokea hapo katikati. Sasa sijui ni Waziri hutaki tupate na sisi sehemu yetu ya kujistiri au samahani ingawa sio mtani wangu, lakini sijui na wewe unapenda tukakae vilingeni tuzuie mvua bila sababu. Kwa sababu kama unafanya show Dar es Salaam, Morogoro na kadhalika.

Mheshimiwa Spika, unakumbuka tulifanya show hapa uwanjani mwanzo mwisho ilikuwa ni mvua. Sasa inakuwa shida. Mimi nikumbushe kitu kimoja, mwaka juzi tulifanya show Sumbawanga, nakumbuka Mkuu wa Mkoa alinipa mganga wa mkoa, huyo mganga wa mkoa akaniambia hapa mvua itafungwa usiwe na wasiwasi. Ndani ya uwanja kulikuwa kuna wananchi 7,000; nje nina watu kubao. Sasa tukitaka kutoka na wasanii kwenda uwanjani ile mvua inatufuata shiiiiii, tukitaka kurudi inarudi. (Makofi)

Mheshimia Spika, tuliingia uwanjani kama unakumbuka ile show ambayo wasanii wangu walidumbukia, watateleza, wakadondoka. Hivi ni vitu ambavyo vinatuumiza sisi, naongea kama natania, lakini Mheshimiwa Waziri umezungumza bajeti yako yote sijakuona ukizungumzia sports arena. Mimi ni mmojawapo ambao nitakataa kuunga mkono bajeti yako kwa sababu naona hauungi mkono maendeleo ya muziki wa Tanzania. Kwa sababu hatuwezi, leo muziki umekua. Tunatoka hapa wasanii wanakwenda kufanya show nje…

MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Spika. Taarifa.

SPIKA: Kuna Taarifa. Endelea.

T A A R I F A

MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Spika, nataka kumpa mzungumzaji kwamba Sumbawanga hatuna shida hiyo, siku nyingine akija, afuate utaratibu tu mambo yatakwenda sawa. (Makofi)

MHE. HAMISI S. TALETALE: Mheshimiwa Spika, Taarifa nimeipokea na kweli, shida hawana ila balaa lilikuwepo. (Makofi/Kicheko)

SPIKA: Mheshimiwa kule Sumbawanga wake za watu tu, basi! Endelea. (Kicheko)

MHE. HAMISI S. TALETALE: Mheshimiwa Spika, hivi ni vitu ambavyo vinatokea kwenye sanaa yetu. Kama Serikali inakosa kutufikiria kwenye suala zima la kuwa na ukumbi na Serikali inaandaa bajeti inakuja kutusomea bajeti mpaka inamaliza haijatamka wala haijaonesha dhamira ya kwamba leo hii tutakuwa na sehemu ya sisi wasanii kwa ujumla kupata sehemu ya burudani, hii inasikitisha sana Mheshimiwa Waziri. Mimi nikuombe, nashindwa kukuambia uende ukajipange tena, ila jipange na Wizara yako tunahitaji kupata sports arena nchini. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini pia, kuna kipindi nilizungumza na Katibu Mkuu wa Wizara yetu akaniambia wanapigania kuwa na sports arena Dodoma, Hee! Mheshimiwa siiombei hata Morogoro Kusini Mashariki wala Morogoro, iko wazi kabisa mji wa burudani na starehe ni Dar es Salaam. Kwa hiyo, tunatakiwa kama tunawaza kuwa na sports arena, Ikakae Dar es Salaam. Isiende Morogoro, isije Dodoma ikakae Dar es Salaam. Lakini ikitokea leo hii tunakaa hapa, Mheshimiwa Waziri amesimama, amezungumza mpaka amemaliza bajeti yake sijaona azungumzie hicho kitu. Mimi inaniumiza, hakuna msanii asiyejua kama mimi ndiye ninayeongoza kufunga mvua. Kwa sababu ya mila zetu za Kiluguru, mimi ni mziwanda, mziwanda ndiyo mfunga mvua sio uchawi wa ushirikina, I am from Africa! Hilo liko wazi. (Makofi)

Naomba unipunguzie hii kazi Mheshimiwa Waziri, naomba unipunguzie hii kazi, inatuchosha. Mpaka unamaliza bajeti yako unazungumza sijaona ukizungumza kuhusu viwanja. (Makofi/Kicheko)

Tunaomba tupate kiwanja na sisi wasanii wawepo indoor, wafanye burudani zao na usituletee kiwanja cha watu sijui 20,000/30,000 ikiwa tunakwenda nje ya nchi kama Mali na kadhalika tunajaza viwanja vya mpira leo hii tunataka kiwanja kikubwa cha burudani nchini. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, cha mwisho kabisa hawa Marais wetu, kuna sijui Rais wa Ngumi, sijui Rais wa nini. Nchi yetu ina Rais mmoja tu, R ni moja tu, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mama Samia Suluhu Hassan. Mheshimiwa Waziri naomba hawa Marais, sijui wa Shirikisho, sijui TFF, zitoke wawe na vyeo vyao. Wanapunguza heshima ya neno Rais na wanaitoa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mtu unamuona Rais kabisa Rais ana vumbi. Rais hawezi kuwa na kiatu kina vumbi. Tunatakiwa tuheshimu neno Rais. Eti Rais wa Wasafi! Hawezi kuwa Rais! (Makofi)

MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Spika, Taarifa.

SPIKA: Mheshimiwa Amar nimekuona.

T A A R I F A

MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Spika, naomba nimpe Taarifa mzungumzaji, kwa kweli, hili suala la Rais, hata sisi kule tuna Rais wa Wachimbaji, hili linakera sana. Nilikuwa nampa Taarifa hiyo. (Makofi)

SPIKA: Kwa kweli jambo hili linakera. Mheshimiwa Waziri Mkuu, hawa Marais, hata Yanga wana Rais wa Yanga, hii haiwezekani! (Kicheko)

Mheshimiwa Babu Tale endelea bwana! (Makofi)

MHE. HAMISI S. TALETALE: Mheshimiwa Spika, hili suala la Marais kwa kweli linakera. Tuache maana ya Rais ibakie kuwa moja, nchi ina R moja tu. Tuna Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Rais Samia Suluhu Hassan. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, anatokea Rais anasimama eti yeye ni Rais, ana kiatu kina vumbi, ina maana Rais! Tuheshimu majina tunayopeana, ndiyo maana mimi nimejiita babu, kwa sababu nikijua kabisa kama babu ni mzee, mimi ni mzee kwenye industry yangu ya bongo fleva, ni mzee kwenye industry ya music in general.

Mheshimiwa Waziri, milango yangu iko wazi, nakukaribisha ukihitaji ushauri wowote, ila nitakuonea huruma sana na wewe ukiwa katika watu ambao eti wasanii wakifanya kiki zao ninyi mkaziingilia mkazitamka. Nilimuona Mheshimiwa Naibu Waziri akizungumzia kiki ya mmoja wa wasanii wangu. Ilinisikitisha sana na nilikuambia kama nisingekuwa Mbunge angeona rangi ya pili ya tabia yangu. Lakini kwa sababu naona ah! Marekani kuna msanii anaitwa Sixnine Tekashi, ni mmoja ya wasanii kichaa, lakini moja ya msanii ambaye anatengeneza pesa kuliko wasanii wengine wote kwa kipindi hiki. Lazima tujue kutofautisha kiki ambayo inatengeneza pesa, kiki ambayo isiyotengeneza pesa.

Mheshimiwa Spika, kikubwa wasanii wetu wanatuletea heshima, kikubwa wasivunje maadili. Ukiwa kama Waziri au Naibu Waziri ukawa wewe sasa unakwenda kumzuwia msanii asifanye kile ambacho kinamtengenezea faida yake, wewe upo busy kama mtu unaonekana kama sasa unapinga maendeleo ya sanaa nchini. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niwaombe, nikuombe Mheshimiwa Waziri, hakuna kitu ambacho kinawaliza wasanii kama hiyo system yenu ya BASATA ya kumuona kila msanii kumfungia. Hii ni taasisi, tunaomba ipewe watu ambao wanahusiana na sanaa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nashindwa kuunga mkono hoja mpaka ninapoona uwanja, arena. Ahsante. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Maji
MHE. HAMISI S. TALETALE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Mimi kwanza kabisa ningependa nimpongeze Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mama yetu Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa mema anayoyafanya na kwa neema aliyoileta ndani ya Jimbo letu la Morogoro Kusini Mashariki. Lakini pia nimpongeze kaka yangu Aweso, wana Morogoro Kusini Mashariki wanakupenda sana.

Na nikwambie, kwa sababu wanajua uwezo wako ukitaka kuongeza wanne karibu Morogoro Kusini Mashariki. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuipongeza timu yangu ya Simba kwa kuendelea kufa kiume, na naamini tutafufuka kiume, na leo timu yao inacheza tuiombee mema. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi niendele kuipongeza Wizara ya Maji, hapa niseme kidogo mimi wazazi wangu wote walikuwa wafanyakazi wa Wizara ya Maji, kwa hiyo mimi nimelelewa na Wizara ya Maji. Kwetu sisi kwenye Kata ya Tegetero ambako tunazalisha mradi wa Morong’anya. Na kwa mradi huu niendelee tena kumpongeza sana Mama Samia Suluhu Hassan, mradi wa bilioni 23, huu mradi unakwenda kulisha vijiji zaidi ya 24. Vilevile Mama Samia hajawa mchoyo akaleta pale Kata yangu ya Mkambarani, mradi wa bilioni 4, nani kama Mama Samia? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi niongee; wanasema mnyonge mnyongeni haki yake mpeni. Wizara ya Maji imefanya makubwa sana kwenye Tarafa yangu ya Mikese na Tarafa ya Mkuyuni. Sasa tunakwenda kwenye Tarafa ya Ngerengere ambapo ndipo pana mlango wa kupeleka maji zaidi ya asilimia 50 Dar es salaam, hii mimi inanitia aibu kusema sana kwa sababu zaidi ya asilimia 50 maji yanakwenda Dar es Salaam, wana Dar es Salaam wanakunywa maji baridi ambayo tunatunza sisi wana Morogoro Vijijini, Tarafa ya Ngerengere inapata maji kwa asilimia 31. Na hiyo asilimia 31 maji yote ni chumvi, na asilimia 69 watu hawapati maji. Sasa hapa ndugu yangu Aweso ndio utakosa mke Morogoro Vijijini. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi niseme ukweli tunamuona ndugu yangu Aweso anasema wali wa kushiba unaonekana kwenye sinia lakini niongee ukweli wana Ngerengere kwenye hiyo sinia bado hawajaiona mpaka leo. Nikuombe kaka yangu Aweso, najua unaweza. Leo hii tunaona umetangaza Mradi wa Kidunda ambao unatoka kwenye Tarafa ya Ngerengere, lakini huu mradi wa Kidunda sisi kwetu hatuna faida nao. Muda wa ukame tutaona mnapanda helkopta mpaka vijijini kutuswaga kule, sisi tunaowalindia maji mpate watu wa Dar es Salaam lakini sisi kama wana Tarafa ya Ngerengere hatujui maji baridim maji yote tunayokunywa ni ya chumvi. Basi angalia ule mradi ambao unakweNda Dar es Salaam tuma wataalamu wako na sisi basi tupate maji baridi.

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi leo hii ninavyoongea katika Kata ya Tununguo hawana mradi wowote tangu uhuru umeanza, kwa hiyo sisi tunakunywa maji tunayaita maji ya Nzasa, yale maji meupe. Kweli! zama hizi! zama za Rais jembe, Rais shupavu Mama Samia Suluhu Hassan, nikwambie kaka yangu tunajua, tunajua nguvu ya Mama Samia na tunajua nguvu ya Chama Cha Mapinduzi, hatuwezi kuona sisi tunakunywa maji ya Nzasa halafu tunawapelekea maji Dar es Salaam wanakunywa maji baridi, hilo ndugu yangu leo naweza nikaondoka na shilingi yako nikaenda nayo Ngerengere.

MHE. SAASHISHA E. MAFUWE: Mheshimiwa Naibu Spika, Taarifa.

NAIBU SPIKA: Taarifa.

TAARIFA

MHE. SAASHISHA E. MAFUWE: Mheshimiwa Naibu Spika, nilitaka kumpa ndugu yangu anayechangia kwamba sera ya maji inasema. Pale ambapo maji yanaanzia kwenye chanzo cha maji wale watumiaji wanaozunguka eneo lile anatakiwa kupata maji kwa hiyo huo mradi wake watu wake wanapaswa kupata maji kama wale wa mradi unaopeleka maji Arusha pale Hai, nao wanatakiwa kupata maji. Ahsante.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Taletale.

MHE. HAMISI S. TALETALE: Mheshimiwa Naibu Spika, nimeipokea taarifa ya ndugu yangu Saashisha lakini naendelea kusema kwamba nakumbuka Mheshimiwa Waziri alikuja kwenye kata yetu ya Tegetero wakati anafuata kutembelea mradi wetu wa Morong’anya pale ule mradi wa Morong’anya unapoanzia kwenye kata ya Tegetero, kata nzima ya Tegetero haina mradi wa maji. Nikupongeze Mheshimiwa Waziri umeacha maagizo na sisi pale katika kata ya Tegetero tuwe wanufaiika. Basi hicho kikafanyike kwenye ule mradi wa Kidunda. Leo hii mimi naona maajabu na miujiza, ule mradi wa Kidunda yale maji hauendi kuyamwaga baharini unakwenda kuwauzia wananchi. Pale hatupati shilingi kumi kipande, tumeridhika Alhamdulillah sasa basi hata tukose na maji?

Mheshimiwa Naibu Spika, tunaomba, mmetunyima shilingi kumi kipande basi tupeni maji. Tunaomba Tarafa ya Ngeregere nayo iwe sehemu ya unafaika ipate maji baridi Mheshimiwa Aweso. Hakuna kitu kinachoniuma, mimi wakati naingia kwenye nafasi hii ya Ubunge ku ukweli kabisa…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa kengele ya pili.

MHE. HAMISI S. TALETALE: Alhamdulillah Rabbil Alamin. (Makofi)
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2022 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024
MHE. HAMISI S. TALETALE: Mheshimiwa Spika, ahsante na mimi pia ningependa kutoa shukrani zangu za dhati kwa kupata hii nafasi ya leo, lakini pia nipende kumpongeza Mheshimiwa Rais wangu, Mama Samia Suluhu Hassan, kwa yale ambayo ameyafanya kwenye nchi yetu, na pia tujipongeze sisi ma-baba wote kwa sababu, jana ilikuwa siku ya ma-baba duniani maana ingekuwa siku ya ma-mama ingekuwa hatari na mimi ni baba bora, naomba nijipongeze kwenye eneo hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kidogo sisi Wana-Morogoro Vijijini tuna jambo letu, tuna malalamiko yetu, nikikumbuka wiki mbili zilizopita Mheshimiwa Waziri wa Ujenzi alisimama akatoa ahadi kwamba mwezi huu wa sita watasaini mikataba kwa ajili ya barabara. Jana wananchi wa Morogoro Vijijini wote wameandamana kwamba Mheshimiwa ulisimama na ukaongea na tulimsikia Waziri akiongea kwamba barabara zinakwenda kusainiwa mwezi huu wa sita. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa ukiangalia tayari mwezi upo mkiani huu, unaondoka. Wenzetu jana wamesaini, sisi Wana-Morogoro Vijijini hatujasaini, lakini tunajua labda shida yake ipo kwa Waziri mwenye dhamana ya fedha, kaka yangu Mheshimiwa Mwigulu, niangalie kijana wako, niangalie nilivyo mdogo, niangalie majukumu ya lawama ya barabara ya Bigwa – Kisaki ni makubwa sana. Mheshimiwa Rais kwa mapenzi yake ya dhati ametugawia kilometa 78 na nikinukuu maneno yako uliyoongea juzi jambo jema ni la mama, mabaya ni ya kwenu. Sasa ikiwa hili halifanyiki wabaya ni ninyi, sio Mheshimiwa Rais. (Makofi)

Kaka yangu Mheshimiwa Mwigulu naomba ungemwambia Waziri Kaka yangu Mheshimiwa Mbarawa hili tatizo la kutokuwa na barabara ya Bigwa – Kisaki na mnakuja hapa mbele mnatuahidi mtasaini na hamfanyi, mnakwenda kumdhalilisha mama yangu na mimi nimesema juzi mimi ndio kipenzi cha Mama Samia, mnataka kunivunja moyo mama yangu asinipende jamani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mimi siwezi kupiga sarakasi humu ndani, siwezi kupiga msamba humu ndani, labda ni-rap tu ili wafurahi, mimi nitachana humu ndani kwa sababu hatuwezi kuwa tunazungumza jambo moja lilelile kila siku. Suala la barabara Mheshimiwa Rais ameshatoa na kama ni fedha Mheshimiwa Mwigulu unayo, tupatie tuanze kujenga barabara ya Bigwa - Kisaki, hii ni aibu ya Taifa.

Mheshimiwa Spika, baada ya kuzungumza barabara nizungumze kuhusu michezo kidogo. Rais wetu wa Awamu ya Sita ambaye…

Mheshimiwa Spika, kama anataka kuongea muache anijibu roho yangu ifurahi.

SPIKA: Kwa sababu mimi hupenda kutenda haki, nikishamruhusu akujibu wewe na Wabunge wengine watataka kujibiwa. Kwa hiyo, tumpe nafasi ayakusanye, atayajibu. Si ndio Mheshimiwa eeh? Haya, ahsante sana. (Makofi)

MHE. HAMISI S. TALETALE: Mheshimiwa Spika, Wabunge wengine wasubirie kipenzi cha mama kinaongea. Ungemuacha ajibu.

Mheshimiwa Spika, turudi kwenye suala la michezo; Mama Samia ndio raia ambaye ametuonesha mapenzi ya dhati ya kuipenda michezo; Mama Samia ndio Rais ambaye ametuonesha mdau mkubwa na mwekezaji kwenye Wizara ya Michezo. Wiki mbili zilizopita nilivyochangia kwenye Wizara ya Michezo nilizungumza kuhusu ile asilimia tano inayotoka kwenye michezo ya kubashiri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Rais aliona kwamba hii Wizara inapewa pesa ndogo, shilingi bilioni 35 ni pesa mbuzi, basi akaona bora hii asilimia tano ya michezo ya kubashiri inayopatikana iende kwenye Wizara ya Michezo. Mimi nikizungumza nipo kwenye Kamati ya Michezo, hii Wizara imepata shilingi milioni 900 mwezi wa pili mwaka huu na hiyo shilingi milioni 900 iliyopata ni ya mwaka jana.

Mheshimiwa Spika, narudia tena kunukuu maneno ya Mheshimiwa Waziri; mazuri ni ya Mheshimiwa Rais mabaya ni ya kwao. Mheshimiwa Waziri, kaka yangu, Mwigulu Nchemba wewe nchi inatambua mema yako, nchi inatambua mapenzi yako na michezo, mimi nina hofu kubwa sana ukiondoka kwenye hiyo Wizara tutatetereka zaidi. Kama ikiwa leo hii wewe uko hapo tu asilimia tano ya Mama Samia haiendi kwa wakati, kama leo hii uko hapo tu, Mheshimiwa Waziri nimemuhoji juzi kwenye hii asilimia tano mnayopata mchanganuo ukoje? Hajui.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, Waziri anayepelekewa huo mchele wa shilingi milioni 900 hajui mchanganuo upoje. Na hiyo shilingi milioni 900 mliyopeleka ya mwaka jana huko, mwaka huu mwaka mzima, hii miezi sita, sio kama watu wanaochezesha michezo ya kubashiri hawapeleki hela kwako, bro (brother) mimi nakufahamu wewe ni mchumi, unatazama pesa zaidi, lakini hii Wizara ili tuweze kujibeba inahitaji kuwa na pesa vilevile.

Mheshimiwa Spika, mimi niombe kitu, tunapozungumza kuhusu michezo ya kubashiri ni michezo. Mheshimiwa umekumbatia mzigo mwingi, tunaomba huu mzigo wa michezo ya kubashiri uupeleke kwenye Wizara ya Michezo na ukishindwa kufanya wakati uko hapo, hakuna anayeweza kufanya. Bro (brother) mimi naamini wewe umeikuza Singida Big Star, leo hii una nuru kubwa, basi kaikuze michezo, wapelekee huu mfuko wa michezo ya kubashiri uende kwenye Wizara ya Michezo wawe wana uwezo wa kuamua jambo Mheshimiwa Waziri.

Mheshimiwa Spika, mimi naamini kitu kimoja na ninachokiongea naongea kwa fact kwa sababu mimi nimeishi kwenye michezo, maisha yangu nimeyapata kwenye michezo, mbebeshee huu mzigo. Najua wewe ni mtaalamu wa kodi unafikiria nikiwapa Wizara ya Michezo kodi yangu wataniletea?

Mheshimiwa Spika, naamini Mheshimiwa Waziri pamoja na Naibu wake Mwana FA hawawezi kukuangusha kwenye hilo. Wapelekee michezo ya kubashiri kama ilivyo, hutasikia vilio. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, unaona wenzetu, nchi za wenzetu zinafanya vizuri. Nilikuja na mafano hapa wa nchi kama Senegal imefanya vizuri kwenye michezo ya ndani kwenye timu zote za Taifa kwa sababu Wizara yao inapata pesa nzuri; nimetoa mfano wa nchi kama Uingereza, michezo ya kubashiri yote inaenda kwenye Wizara ya Michezo; nimekuja na mfano wa nchi kama ya Japan, michezo ya kubashiri pesa zote zinakwenda kwenye Wizara ya Michezo; nchi ya Tanzania michezo ya kubashiri iko kwenye Wizara yako Mheshimiwa Waziri wa Fedha, tunakufahamu wewe ni mchumi, lakini hebu kata hili kidogo ndugu yangu wape Wizara ya Michezo wajiendeshe. Mkikaa kwenye vikao vyenu mnapanga mipango ya kuwagawia shilingi bilioni 35, hiyo shilingi bilioni 35 waendeleze michezo yote.

Mheshimiwa Spika, tunawaona TFF wanateseka kujenga viwanja. Tumeona juzi Tanga pale wakati tunawaangalia kwenye siku ya tuzo, wametuonesha uwekezaji wao, lakini ule uwekezaji unatakiwa kufanywa na Serikali, kufanywa na Wizara. Sasa Mheshimiwa Waziri, kaka yangu na mwanamichezo tunayekutegemea ingawa timu yako imeshapoteza kocha na hivi karibuni za ndani Mayele harudi, kwa hiyo, naona wazi kabisa utaenda kutusaidia, utaenda kusaidia Wizara. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimuombe Mheshimiwa Waziri haya maneno nayarudia mara mbilimbili kwa sababu najua siku ya wewe kufungua moyo, siku ya kubeba michezo ya kubashiri kuipeleka kwenye Wizara ya Michezo ndio siku ya Wizara hii ya Michezo kwenda kuisaidia michezo na sanaa kwa ujumla. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kuyasema hayo siwezi kusema naunga mkono hoja mpaka nione anasema nini. Nitashika shilingi ya Mheshimiwa Waziri, ahsante. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo
MHE. HAMISI S. TALETALE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwanza nianze kwa dua, “Rabbi shrahli swadri, wayassrli amri, wahlul-uqdata min-lisaani yaf-qahu qawli”.

Mheshimiwa Naibu Spika, sababu ya kuomba hii dua ni kumwomba Mwenyezi Mungu ausimamie ulimi wangu kwa yale ambayo naenda kuyaongea leo. Sababu ya kuomba hii dua kumwomba Mwenyezi Mungu aisimamie hii Wizara. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nina mengi leo ya kuongea, lakini nitaanza na hoja zangu tatu. Kabla ya kuanza kwanza nimpongeze Mheshimiwa Rais, Mama yetu Samia Suluhu Hassan. Nampongeza kwa kile ambacho anakifanya Morogoro Kusini Mashariki, ndio maana nimekuwa siwezi kuchangia Wizara yoyote naona mambo yanakuja, mambo yanakwenda kwa hiyo, Mheshimiwa Rais anaupiga mwingi sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nianze na BASATA. Ninaposema nianze na BASATA, naanza na BASATA. BASATA ni chombo cha kusaidia wasanii, lakini bahati mbaya BASATA imekuwa Polisi wa Wasanii. Nampongezae Mheshimiwa Waziri Mchengerwa, amekuwa kila siku akizungumza nami. Nina miaka 20 kwenye music industry, najua nini kinaenda vizuri, na nini kinaenda vibaya. Leo hii tuongee ukweli, BASATA hawana utaratibu wa kuwapa elimu wasanii, hawana utaratibu wa kutoa semina kwa wasanii, lakini BASATA wana utaratibu wa kufungia nyimbo za wasanii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Sanaa; watu wanatulia ku-create kitu asubuhi, mchana, halafu wewe jioni unaziba, unazuia eti kwa sababu ya sheria ambayo msanii haijui. Niseme leo, sijui kama sheria yako itaniruhusu kuimba. Nitaimba hapa Waheshimiwa Wabunge waitikie! Mamaa Amiinaa! (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nikiimba hii nyimbo kama mtu akiitikia vile inavyopaswa, basi BASATA walikuwa wanatakiwa waitazame hii nyimbo na waifungie. Hawawezi kufanya hivyo kwa sababu hajaimba msanii ambaye kwao hawana maslahi naye. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunajua Mheshimiwa Waziri roho yake ni nzuri, naweza kutafsiri baadhi ya wafanyakazi wake, watumishi wake wana roho mbaya. Hawa vijana wanahangaika ku-create vitu, kama tunakubali kuipeleka Tanzania katika international level, hatusemi kwamba tunavunja utaratibu wa sheria, hatusemi kwamba tunakwenda kuvunja utamaduni wetu, lakini wewe uko busy kuwaza huyu kakoseaje umfungie; mpe elimu, umeshindwa nini? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, juzi nilikuwa naongea na Mheshimiwa Ummy nikampa hii nyimbo na kiitikio chake, alisikitika sana, lakini leo hii tuko na BASATA ambao wako busy tu kuangalia kafanyaje? Tumfungie! Kafanyaje? Tumfungie! Tuangalie hiki kitu, kama tuna nia ya kukuza industry ya Sanaa, tuangalie tunawezaje kuwapa elimu wasanii. Hakuna aliye juu ya sheria, hakuna ambaye anayetaka kufanya jambo kwa ajili ya kujifurahisha yeye.

NAIBU SPIKA: Taarifa.

T A A R I F A

MHE. ASIA A. HALAMGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Napenda tu kumpa taarifa mtoa hoja kwamba, BASATA imekuwa ikiwashika mashati vijana wa Kitanzania na kuwavuta nyuma. Nikitolea mfano msanii kama Gigi Money, ni kijana ambaye alianza kusimama, lakini hawatoi elimu ya kuwasaidia wasanii bali kuwavuta nyuma. Angalia sasa hivi Gigi Money badala ya kwenda mbele tunamwona tayari ame-drop. Tunategemea BASATA iweze kuwasaidia wasanii.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. (Makofi)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Tale.

MHE. HAMISI S. TALETALE: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa yake naipokea kwa mikono miwili kabisa, maana nilikuwa namwangalia nani anatoa taarifa? Maana leo nimesema atakeyetoa taarifa awe na experience ya muziki kama niliyonayo mimi humu ndani.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukiizungumzia BASATA unazungumzia vitu ambavyo… Aah, Alhamdulillah!

Mheshimiwa Naibu Spika, niachane na BASATA, nahamia COSOTA, maana naweza nikaongea kuhusu BASATA halafu nikaumia roho vile vile. Hii taasisi ya COSOTA kama siku utaipelekea TAKUKURU pale unafunga wote wale. Natoa mfano, nina msanii wangu hamna asiyemjua hapa anaitwa Kassim Mganga, anatokea Tanga, hakuna asiyeimba nyimbo zake kwenye msimu wa harusi.

Mheshimiwa Naibu Spika, Kassim Mganga unamwita, unaenda kumpa shilingi 50,000 halafu unaenda kumwita Lulu Diva unampa shilingi 550,000 halafu umetumia vigezo gani? Kuna utaratibu gani ambao unatumika COSOTA kwenye kugawa mirabaha? Tumpongeze sana Mheshimiwa Rais, Mama Samia Suluhu Hassan, ametoa gari bovu uwani, kaliweka barabarani. Hii COSOTA ni gari bovu liko barabarani.

Mheshimiwa Naibu Spika, leo naondoka na Shillingi ya Mheshimiwa Waziri, nashika mshahara wake, atafuata Shilingi Kusini Mashariki namuahidi brother wangu. Kama hajaja na hoja ya kubadilisha utaratibu wa COSOTA, wasanii wale wanaimba; kuna msanii kama Mzee Yusufu? Nimemwona pale juu, ni mwanamuziki anaimba, anaandika, anapata haki yake vizuri. Huwezi ukamkusanyia Mzee Yusufu Shilingi milioni tano! Ana worth ya Shilingi milioni tano? Tuongee ukweli! Hakuna utaratibu wa kugawa fedha kwa wasanii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tuangalie wanatumia utaratibu gani kwenye kuwapa pesa wasanii? Nimeona kuna baadhi ya wasanii wanawapa pesa kwa sababu ya ukubwa wao wa Instagram na makelele tu. Sitaki kuongea mengi, mimi ni Kiongozi wa Taasisi ya Wasafi, hakuna msanii mmoja aliyepewa hata Shilingi kumi anakwenda kusimama pale Kiongozi wa COSOTA eti ooh, hawajakusanya nyimbo, hawajasaini kwa sababu ya redio fulani. Kama unapewa kitu, taasisi ambayo inasimamiwa na Serikali, usiegemee upande mmoja, ongoza kama kiongozi. Kuna redio zipo huko Morogoro Vijijini na wapi, zinapiga nyimbo za Wasafi, upo kwenda kuchukua hela? Leo hii eti unakwenda kumpa msanii pesa, Madii unampa shilingi 250,000. Mwaka 2021 watu kibao walikufa na Corona, hakuna nyimbo iliyoimbwa kama “Kazi Yake Mola”, tuwe wa wazi. Unakwenda kumpa Madii shilingi 250,000 kwa vigezo gani?

Mheshimiwa Naibu Spika, narudia tena, nitaendelea kuishika Shilingi ya Mheshimiwa Waziri mpaka nijue utaratibu gani unakwenda kuufanya kwenye hii COSOTA? Naomba Waheshimiwa Wabunge wenzangu kwenye hili tulisimamie kwa sababu copyright haisimami kwenye muziki tu. Mimi ni publisher, leo hii nasimamia music, kesho na keshokutwa watoto wangu watakula nini? Si ndiyo copyright inasimama kwenye kila eneo. Hakuna utaratibu mzuri! Mheshimiwa Naibu Waziri ukijiona huna jibu kwenye hili, ujue huna Shilingi ya Hamis Shaban Taletale kutoka Kusini Mashariki. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hakuna kitu kizuri kama msanii anapofanya jambo akasifiwa. Hawa vijana wanahangaika kwenye kutengeneza vitu vyao mimi nimpongeze sana kuna dada mmoja anaitwa Lamata movie ilikufa nchini, tuwe wawazi. Yule dada amepambana; kuna kipindi kinaitwa Juakali, kinakwenda vizuri sana, lakini nikwambie, yule binti kama atataka kwenda kuigiza Polisi, haitawezekana. Kama atataka kwenda kuigiza Jeshini, haitawezekana kwa sababu ya utaratibu wa Wizara tulioufanya. Kama tunataka kuwasaidia hawa wasanii, tuwasaidie tusione hii ni sehemu ya wahuni. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Ahsante Mheshimiwa Taletale, hii ni kengele ya pili.

MHE. HAMISI S. TALETALE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naunga mkono hoja.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2021 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023
MHE. HAMIS S. TALETALE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwanza kabisa nipende kumshukuru Mheshimiwa Rais wetu Mama Samia Suluhu Hassan kwa kile anachokifanya kwenye Jimbo letu la Morogoro Kusini Mashariki na Wilaya yetu ya Morogoro Vijijini kwa ujumla.

Mheshimiwa Naibu Spika, leo hii unatembea Morogoro Vijijini ukiona kwamba huduma za kiafya zinakuja, huduma za shule pamoja na maji zinakuja. Wiki iliyopita tumepata mradi wa maji wa Morong’anya wa bilioni 24 na vilevile tumepata mradi wa maji wa Mtambarani bilioni nne, nani kama Mama Samia! Mama Samia hajaishia hapo kulitendea haki Jimbo la Morogoro Kusini Mashariki. Ninavyozungumza hapa ametuletea kituo cha afya kwenye Kata ya Kinole ambacho hatukutegemea kabisa. Na kutokana na zile fedha za UVIKO Mama Samia ametuletea kituo cha afya kwenye Kata ya Mkulazi. Kutoka Kata ya Mkulazi mpaka unakwenda Ngerengere ulikuwa unatembea kilometa 70.4 lakini Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan ameliona na amatutatulia hilo tatizo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niende kwenye hoja. Nimpongeze sana kaka yangu Mheshimiwa Waziri Mwigulu na mtani wetu. Kwenye huu mradi wetu wa SGR, ule mradi naamini unaanza mwezi wa kumi treni inatoka Dar es Salaam inakwenda Morogoro. Ni vituo vitano kutoka Dar es Salaam, kituo cha tano ni Ngerengere. Ngerengere ya sasa tofauti na Ngerengere ya zamani. Leo hii kama tunakwenda kupokea kituo cha mwendokasi maana yake mkazi wa Ngerengere anaweza akaenda Dar es Salaam kufanyakazi, akaenda Dodoma kufanyakazi Ngerengere inatanuka. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimuombe kaka yangu Bashungwa, leo hii Ngerengere tuna kituo cha afya ambacho hakina mortuary. Leo hii kama kuna mtu anafariki asubuhi saa moja Ngerengere basi anatakiwa azikwe saa nne, la sivyo maiti itaharibika kwa sababu kituo cha afya hakina mortuary. Kituo hiki cha afya tumekirithi kwa wakoloni. Sasa nakuomba kaka yangu Mheshimiwa Bashungwa, najua hushindwi. Kama umenipa Kituo cha Afya Mkulazi, umenipa Kituo cha Afya Kinole naomba ukatupe Kituo cha Afya Ngerengere linawezekana kwako kaka yangu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, si tu mortuary leo hii tunasema Kituo cha Afya cha Ngerengere kina changamoto ya mama na mtoto. Kama leo hii mama anakwenda kujifungua kwenye Kituo cha Afya cha Ngerengere yaani hakuna pa kupumzika. Yaani huyu anajifungua huyu mwingine akae amsubirie. Mheshimiwa Bashungwa, nakuomba kaka yangu kwa heshima na taadhima kwa niaba ya Wanakusini Mashariki tunakuomba uitazame Ngerengere kwa ajili ya kile kituo cha afya. Tunaua watu na watu wanateseka. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kama mji unakua lazima uwe na afya lakini vilevile lazima uwe na ulinzi uliotukuka. Kama tunakwenda kwenye Kata ya Ngerengere leo hii tuna kituo cha polisi cha kurithi pia, hatuna kituo cha polisi Kata ya Ngerengere, Kata ambayo tunakwenda kuwa na kituo kikubwa cha mwendokasi. Huu ni mtihani, na mtihani huu ninaamini kabisa wa kuutatua ni wewe Mheshimiwa Mwigulu. Ninakuomba kaka yangu, tunaomba utuletee fedha na sisi wana Ngerengere tupate kituo cha polisi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nilimuona juzi kaka yangu akitamba kuhusu Yanga kuhusu nini lakini pia akazungumzia miradi mikubwa ya Serikali na pia akauzungumzia Mradi wa Bwawa la Mwalimu Nyerere; naomba nimuelekeze kaka yangu, Bwawa la Mwalimu Nyerere wakati unakwenda kwenye Bwawa la Mwalimu Nyerere lazima upite Bigwa Kisaki. Leo hii katika barabara zetu; tunakushukuru umetupa barabara ya Bigwa Kisaki kilometa 78, lakini haipo kwenye kipaumbele chako. Twende tukailinde Ilani yetu ya Chama Cha Mapundizi Mheshimiwa Mwigulu, twende tukawasaidie, na mje mtusaidie wana Morogoro Kusini Mashariki. Leo kama tunakwenda kulitazama Bwawa la Mwalimu Nyerere mnakwenda kwa kupitia helkopta, wageni wakija wanapanda ndege wanashuka; huu ni mtihani

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna njia ya Bigwa-Kisaki, kilometa 78, na pia kuna njia ya Ubena-Zomozi-Ngerengere-Mvuha. Tukitengeneza hizi njia tunaenda kufika kirahisi kwenye mradi wa kimkakati. Ninakuomba Mheshimiwa Mwigulu, kama unaamini mradi wa kimkakati ni Bwawa la Mwalimu Nyerere weka imani kwamba Bigwa-Kisaki ni njia ya kimkakati, iende ikatengenezwe; tusije tukasema tu tumetangaza kilometa 78 lakini hatuzioni. tunaomba tuione barabara yetu ya Bigwa Kisaki ni mtahani. Nakupongeza sana kwa vile ambavyo unatutazama, lakini nakuomba kwenye hili utupiganie.

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi wiki iliyopita niliongea na ndugu yangu, kaka yangu, mtani wangu, Mheshimiwa Bashe; nikasema leo hii sisi wanakusini mashariki tunalima karafuu inawezekana tunachuana na Pemba. Lakini utaratibu wa kupata wateja, utaratibu wa kupata wanunuzi inakuwa ni shida kwa sababu ya barabara ya Bigwa Kisaki. Leo hii hapa Dodoma watu wanakula machungwa, Iringa wanakula machungwa kwa asilimia hamsini yanayotokea Morogoro Kusini Mashariki. Ninakuomba ulisimamie hili suala kwa sababu Kusini Mashariki …

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Ahsante Mheshimiwa, mortuary hakuna wasaidie.

MHE. HAMIS S. TALETALE: Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja. (Makofi)