Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Ali Juma Mohamed (4 total)

MHE. ALI JUMA MOHAMED Aliuliza:-

Je, Serikali kupitia Balozi zetu ina mkakati gani wa kusimamia mikataba ya vijana wanaokwenda kufanya kazi nje ya nchi?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI Alijibu: -

Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ali Juma Mohamed, Mbunge wa Shaurimoyo kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni wajibu wa Serikali kuhakikisha Watanzania wanaopata fursa za ajira nje ya mipaka ya Tanzania wanafanya kazi katika mazingira mazuri na yanayolinda staha na utu wao. Katika kufanikisha azma hiyo Serikali imeweka utaratibu mzuri wa kutoa vibali vya ajira nje kupitia mamlaka zinazoshughulikia masuala ya ajira, ikiwemo Wakala wa Huduma za Ajira Tanzania (TAESA) na Kamisheni ya Kazi Zanzibar kwa kushirikiana na Balozi za Tanzania nje.

Mheshimiwa Spika, utaratibu huo pamoja na mambo mengine unaelekeza kila mfanyakazi kuwa na wakala rasmi wa ajira, ambaye anatambuliwa na mamlaka tajwa ambao ndio waandaaji wa mikataba ya ajira nje inayopaswa kukidhi Sheria za Ajira za Tanzania na nchi anayokwenda kufanya kazi. Aidha, kwa mujibu wa utaratibu uliowekwa na Serikali mikataba hiyo pia inapaswa kuandaliwa kwa lugha inayoeleweka na vijana hao, ikiwemo Kiswahili. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pamoja na Serikali kuweka utaratibu huo bado kumekuwa na changamoto zinazotokana na baadhi ya vijana wanaopata ajira nje kutozingatia utaratibu uliopo. Pia, baadhi ya vijana hao hawajitambulishi kwenye Ofisi za Balozi za Tanzania pindi wanapofika kwenye ajira zao Ughaibuni. Kutokana na hali hiyo Serikali kupitia Balozi zake imeweka mikakati ifuatayo:-

(i) kutambua Kampuni za Uwakala wa Ajira za Nje na kuzitaka ziwe na uhusiano wa kimkataba na Kampuni za Uwakala za Tanzania.

(ii) Kuendelea kutoa elimu kwa vijana wanaopata ajira nje kutoa taarifa zao na kuwasilisha nakala za mikataba yao ya ajira Balozini ili ziweze kuhakikiwa.

(iii) Serikali imeanza mchakato wa kuingia mikataba ya ajira na baadhi ya nchi ili kurasimisha upatikanaji wa ajira katika nchi hizo.

Mheshimiwa Spika, napenda kutoa rai kwa Watanzania ambao wana nia ya kufanya kazi nje ya mipaka ya Tanzania, kufuata utaratibu uliowekwa na mamlaka husika. Kwa kuwa pamoja na mambo mengine inawapa kinga na kuepuka mazingira mabaya ya kazi ambayo hayatarajiwi na pia kurahisisha kupata msaada pale unapohitajika. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. ALI JUMA MOHAMED aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kuwatafutia ajira na fursa mbalimbali nje ya nchi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU (KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante na kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ali Juma Mohamed, Mbunge wa Shaurimoyo kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatekeleza mpango mikakati ifuatayo ili kuunganisha vijana na fursa za ajira nje ya nchi: -

(i) Imeingia makubaliano (bilateral agreements) na baadhi ya nchi zenye fursa za ajira duniani.

(ii) Imeweka mwongozo wa kuratibu shughuli za Wakala Binafsi wa Huduma za Ajira ili kuwezesha shughuli za kuunganisha Watanzania na fursa za ajira nje ya nchi kufanyika kwa kuzingatia haki za msingi za wafanyakazi na viwango vya kazi vinavyokubalika na Shirika la Kazi Duniani (ILO). Hadi sasa jumla ya Wakala 58 wamesajiliwa na kupewa leseni, kati ya hao Wakala watano wanajishughulisha na kuwaungaunisha watafuta ajira nje ya nchi.

(iii) Kujenga mfumo wa kielektroniki wa huduma za ajira utakaorahisisha na kuweka uwazi katika kuratibu upatikanaji wa fursa za ajira nje ya nchi; mchakato wa kuandaa Watanzania wenye sifa pamoja na kufuatilia hali za Watanzania wakiwa wanafanya kazi nje ya nchi. Mfumo unatarajiwa pia kukamilika na kuanza kutumika kabla ya mwezi Juni, 2022.

(iv) Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la tatu katika mpango huo ni kutekeleza Programu ya Taifa ya Mafunzo ya Ujuzi hususani kupitia mafunzo ya uanagezi pamoja na utarajali ili kuwezesha vijana husika kuwa na ujuzi stahiki kufanya kazi nje ya nchi.

(v) Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la tano baadhi ya machache hayo nikiyataja kwa sababu ya muda kufanyia marekebisho Sheria ya Huduma za Ajira ya mwaka 1999 pamoja na Kanuni za mwaka 2014 ili ziweze kuendana na mazingira ya sasa ahsante.
MHE. ALI JUMA MOHAMED aliuliza: -

Je, Shirika la Ndege nchini (ATCL) limeshaanza kulipa madeni ya Makampuni yaliyokuwa yanatoa huduma?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. FREDY A. MWAKIBETE) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, ahsante na kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ali Juma Mohamed Mbunge wa Shaurimoyo kama Ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kulipa madeni ya makapuni yanayotoa ama yaliyokwisha kutoka huduma kwa ATCL baada ya kuyafanyia uhakiki. Mwaka 2016 kabla ya Serikali kuanza mpango wa kuifufua ATCL Kampuni ilikuwa inadaiwa kiasi cha shilingi bilioni 141.77 na watoa huduma mbalimbali wa ndani na nje. Hadi kufikia mwezi Aprili, 2022 Serikali imelipa madeni jumla ya shilingi bilioni 127.07.

Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kuiwezesha ATCL kulipa madeni yaliyobaki kulingana na uwezo wa kibajeti. Ahsante.
MHE. ALI JUMA MOHAMED aliuliza: -

Je, kuna nchi ngapi zimefungua Ofisi Ndogo za Ubalozi Zanzibar?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NJE (MHE. BALOZI MBAROUK NASSOR MBAROUK): Mheshimiwa Spika, ahsante sana, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ali Juma Mohamed, Mbunge wa Shaurimoyo, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, hadi kufikia mwezi Agosti, 2023 jumla ya nchi tano zimefungua Ofisi Ndogo za Ubalozi (Konseli Kuu) Zanzibar. Nchi hizo ni; China, India, Msumbiji, Oman na Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE), ahsante sana.