Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Judith Salvio Kapinga (3 total)

MHE. JUDITH S. KAPINGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwanza napenda kuishukuru Serikali kwa majibu mazuri, lakini napenda kuwashukuru kwa kuongeza rasilimali fedha katika miradi ya maendeleo ya Wizara. Nina swali dogo la nyongeza kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara ya Fedha katika Bunge la Bajeti la 2019/2020 ilitoa maelekezo kwa Bodi ya Mikopo kuangalia uwezekano wa kufanyia kazi suala hili. Je, Wizara haioni umuhimu wa kufanyia kazi mapendekezo haya ya Wizara ya Fedha ili shughuli hii ya kuendeleza mitaji watu kama Wizara inavyosema iweze kufanyiwa kazi vizuri kwa kuitenganisha na Fungu 46? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Judith, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa vile ilikuwa ni mapendekezo na yalipendekezwa na Wizara ya Fedha na kwa vile yalikuwa ni mapendekezo ambayo yaliletwa kwenye Wizara yetu, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kuwa mapendekezo hayo tutaendelea kuyafanyia kazi na pale muda muafaka utakapofika tutawasilisha mbele ya Bunge lako Tukufu. Ahsante.
MHE. JUDITH S. KAPINGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa swali la nyongeza. Wilaya ya Mbinga ni mojawapo ya wilaya zinalima zao la kahawa kwa wingi lakini Vyama vya Ushirika vimekuwa vikichelewesha malipo na hivyo wakulima kushindwa kununua pembejeo za kuhudumia mazao yao kwa wakati.

Je, Serikali ina mkakati gani wa kuimarisha utendaji kazi wa vyama vya ushirika ili wananchi wa Wilaya ya Mbinga waweze kulipwa fedha kwa wakati na hivyo kuwawezesha kununua pembejeo za kuhudumia zao lao kahawa kwa wakati?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kumekuwa na changamoto kwasababu mfumo wa ulipaji siku zote umekuwa ni kwamba baada ya mnada fedha zinalipwa kwenye Chama Kikuu cha Ushirika, Chama Kikuu cha Ushirika kina hamishia fedha katika Chama cha Msingi. Kwa hiyo tumefanya kikao mwezi Aprili na Vyama vya Ushirika vya Mkoa wa Ruvuma kwa maana ya Wilaya ya Mbinga, utaratibu tunaoelekea sasa hivi kuutekeleza katika vyama vya msingi na vyama vikuu vya ushirika ni kwamba mnada unapoisha mnunuzi anatakiwa alipe malipo ndani ya saa 48 na malipo yale yatakwenda moja kwa moja kwa mkulima hayatopitia kwenye ukiritimba wa kwenda kwenye chama kikuu chama kikuu kwenda kwenda kwenye chama cha msingi. Kwa hiyo nimuahidi Mheshimiwa Mbunge na Waheshimiwa Wabunge wengine tuna-perfect system ya kulipa baada yam nada malipo yaende moja kwa moja kwa mkulima badala ya kupitia kwenye vyama kwasababu huko kunaleta ukiritimba na kuchelewesha malipo.
MHE. JUDITH S. KAPINGA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali, nina swali moja la nyongeza kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kutokana na kwamba Sera yetu ya Sayansi na Teknolojia ni ya muda mrefu, ya miaka 25 nyuma, lakini vilevile kutokana na suala kwamba mapitio ya sera hii ili yaweze kuleta tija kwenye ubunifu yamekuwa yakichukua muda mrefu, tangu 2012, jambo linalosababisha programu za ubunifu chini ya COSTECH kutokutengewa fungu na kutegemea zaidi ufadhili na hivyo kukosesha vijana fursa nyingi zinazotokana na ubunifu: Je, Serikali haiwezi kutuambia ukomo wa muda wa mapitio haya ya sera ya kwamba yatakamilika lini? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ni kwa sababu tumeambiwa maboresho yamekuwa yanafanyika toka 2012 lakini hadi leo hayajafanyiwa kazi. Tunaomba Wizara ituambie ukomo wa muda wa kufanyia maboresho ili programu za ubunifu ziweze kuwa na tija kwa vijana wa Tanzania. Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, naomba sasa kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Kapinga kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwanza nimtoe wasiwasi Mheshimiwa Mbunge. Wizara imekuwa ikitenga fedha katika kila bajeti kwa lengo la kuhakikisha kwamba eneo hili la ubunifu linafanyiwa kazi sawa sawa. Nimweleze tu Mheshimiwa Mbunge kwamba Wizara imetengeneza mwongozo wa mwaka 2018. Vilevile mwongozo huu tunaendelea kuuboresha mwaka huu, tena tunaendelea kuupitia upya ili kuweka mwongozo huu sawa sawa, nimtoe wasiwasi.

Mheshimiwa Spika, pia anataka kujua kwamba ni lini Serikali itakamilisha utungaji huu au mapitio haya ya sera? Ndani ya mwaka huu wa fedha tutalifanya hilo na kuhakikisha jambo hili linakaa sawa sawa. Ahsante. (Makofi)