Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Answers to supplementary Questions by Hon. Judith Salvio Kapinga (28 total)

MHE. JAFARI W. CHEGE: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi. Pia nimshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri yenye matumaini kwa wananchi wangu wa Rorya, lakini ninayo maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza; kwa kuwa Sheria ya Uthamini inatamka wazi kwamba thamani ya ardhi inapaswa kulipwa ndani ya miezi sita, lakini wananchi hawa wamedai malipo yao toka mwaka 2011 na hawajalipwa. Nataka nipate commitment ya Serikali itakapofika Novemba kama wananchi hawa hawajalipwa uthamini wa ardhi yao, je, Serikali itakuwa tayari sasa kurudia uthamini kwa mujibu wa Sheria inavyotamka kwamba wananchi wale walipwe ardhi kwa mujibu wa Sheria inavyotamka?

Mheshimiwa Spika, swali langu la pili; kwa kuwa jambo hili limekuwa ni la muda mrefu toka mwaka 2011 na sasa liko ndani ya Ofisi ya Mkurugenzi nataka nipate commitment ya Serikali hasa Ofisi ya Wizara ya TAMISEMI, je, ni lini watalipa fedha ili wathamini warudi site wakamilishe uthamini na upande wa TANESCO waweze kulipa fidia kwa wananchi hawa?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba nijibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Jafari Chege, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kuhusu kurudia zoezi ikifika Novemba, zoezi hili limeshachukua muda mrefu nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge Serikali imeshatenga fedha kiasi cha milioni 350 ili wananchi 231 wanaodai fidia walipwe ikifikia Novemba, 2023. Kwa hiyo nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba zoezi hili tunaenda kulikamilisha na kwa sababu limechukua muda tutafuatilia kwa ukaribu kuhakikisha kwamba linakamilika.

Mheshimiwa Spika, kwenye swali lake la pili kuhusiana na kutoa fedha, tayari Serikali kupitia TANESCO imeshatoa fedha kiasi cha shilingi milioni 15 kwa ajili ya kukamilisha zoezi la uthamini. Tutafuatilia kuhakikisha kwamba Halmashauri ya Rorya inakamilisha taratibu hizi kwa wakati ili zoezi hili liweze kukamilika kwa wakati kwa kadri ambavyo imepangwa, ahsante. (Makofi)

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Spika, naomba nitumie nafasi hii tena kumwelekeza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Rorya kuhakikisha kwamba fedha hizi ambazo wenzetu wa TANESCO wameshazipeleka kwenye halmashauri ile ziweze kutumika mara moja na kulipa fida hiyo. (Makofi)
MHE. ENG. EZRA J. CHIWELESA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Mradi wa Geita - Nyakanazi na Nyakanazi - Rusumo kuna baadhi ya wananchi wa Biharamulo ambao wanapitiwa na mradi ule katika Kata nne za Rusahunga, Kaninha na Nyakahula nao pia bado hawajalipwa pesa zao za fidia. Je, ni lini Serikali itaweza kukamilisha malipo hayo kwa baadhi ya watu ambao walikuwa hajalipwa pesa zao? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba nijibu maswali ya Mheshimiwa Engineer Ezra Chiwelesa, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kuhusiana na fidia ya Geita - Nyakanazi tayari Serikali ilishatenga fedha bilioni sita na tayari fedha bilioni 5.9 zilishalipwa kwa ajili ya wananchi na wananchi waliobakia ni wananchi 49 tu, tunaamini taratibu zikikamilika na wao wataweza kulipwa.

Mheshimiwa Spika, kuhusiana na Nyakanazi -Rusumo pia Serikali ilishatenga fedha bilioni 3.8 na tayari bilioni tatu ilishalipwa, wananchi waliobakia ni 39 tu. Nimshukuru Mheshimiwa Mbunge kwa kufuatilia na kwa sababu fidia hii imekamilika kwa zaidi ya asilimia 95, tutafuatilia kuhakikisha kwamba kidogo kilichobakia kinaweza kukamilika, ahsante sana. (Makofi)
MHE. GEOFFREY I. MWAMBE: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa majibu mazuri ya Naibu Waziri. Hata hivyo nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, tuna Kijiji cha Mlundelunde, Kitongoji cha Mchaka ambacho kina shule ya sekondari ambapo bahati mbaya umeme umepita juu yake na shule ile ya sekondari kama taasisi ya Serikali, haijapata ule umeme: Je, nini maelekezo ya Serikali kwa REA Mtwara ili waweze kufanya haraka kuunganisha umeme katika hiyo shule ya sekondari?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili. Tumepata changamoto kubwa kwa Jimbo letu la Masasi Mjini ambapo tuna Kata saba za Sururu, Mwengemtapika, Matawale, Chanikanguo, Temeke, Marika pamoja na Mmbaka ambazo ziko vijijini, lakini wanatakiwa kulipa shilingi 320,000/= kama sehemu ya ada ya uunganishaji wa umeme: Je, Serikali haioni ni wakati muafaka sasa, wananchi hawa wapate haki kwa maana wapo vijijini, waunganishiwe umeme kwa shilingi 27,000/= kama vijiji vingine?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Geoffrey Mwambe, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na shule ambayo ameitaja, shule hii ipo katika moja ya kitongoji ambapo utaenda kutekelezwa mradi wa vitongoji 15 ambavyo tayari Serikali imeshatenga fedha kwa mwaka huu wa fedha. Tunaanza kufanya ufuatiliaji ili tuweze kuona ni namna gani tunaanza kutekeleza mradi huu wa vitongoji 15.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na swali lake la pili juu ya maeneo ya vijijini ambayo yanakataliwa kutozwa shilingi 27,000/=, tayari Serikali tumeshaya-identify haya maeneo na tuko katika mchakato wa mwisho ili kuweza kutolea maelekezo kwa maeneo kama haya ambayo yanaleta mkanganyiko wa bei.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
MHE. ASIA A. HALAMGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuweza kuuliza swali la nyongeza. Mkandarasi aliyekabidhiwa vijiji 15 vya Wilaya ya Hanang’ kasi yake inasuasua sana: Je, nini kauli ya Serikali juu ya Mkandarasi huyu ili kuwapa matumaini wananchi wa Wilaya ya Hanang’?

NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Asia Halamga, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Mkandarasi aliyekuwepo Hanang’ Nakurwa Investment Company ni kweli alikuwa anasuasua lakini tumemsimamia na katika vijiji 15 ambavyo vimebakia, vijiji tisa ameshasambaza nguzo, na tuna imani mpaka ifikapo Desemba, 2023 atakuwa amekamilisha kuweka umeme vijiji vyote, ahsante.
MHE. EMMANUEL P. CHEREHANI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwanza naishukuru Serikali kwa majibu mazuri. Hali ya makali ya mgao wa umeme katika Wilaya ya Kahama pamoja na Halmashauri yake ni makali mno, hali ni ngumu, wafanyabiashara wanashinda wamekaa, umeme umekatika siku nzima. Sasa Mheshimiwa Waziri yupo tayari kufanya ziara katika Wilaya hii ya Kahama pamoja na Halmashauri zake ajionee hali ilivyo kwa wananchi hawa?

Mheshimiwa Spika, swali langu la pili. Je, Serikali ina mkakati gani sasa wa kuipa Mkoa wa ki-TANESCO Wilaya hii ya Kahama ambayo inakua kwa kasi kwa nchi hizi za maziwa makuu?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Nishati napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Emmanuel Cherehani.

Mheshimiwa Spika, kuhusiana na mgao wa umeme, kwa sababu sasa hivi tumetengamaa na tumepunguza kidogo ule upungufu ambao ulikuwepo, niwaelekeze TANESCO na kituo chetu cha pamoja cha gridi (Grid Control Center) wahakikishe maeneo yote yanaendelea kupata umeme kulingana na jinsi ambavyo tunaboresha upatikanaji huo wa umeme.

Mheshimiwa Spika, kuhusiana na ziara, nitafika Ushetu Mheshimiwa Mbunge. Suala la pili kuhusiana na kuweka kituo cha kimkoa Ushetu, Mheshimiwa Mbunge tutaendelea kuangalia tathmini kama Wilaya ya Kahama inafaa kuwekwa kama Mkoa wa ki-TANESCO kwa ngazi ya mkoa, na kama itafaa, basi tutafanya hivyo, lakini kama haifai, tutaendelea kuboresha huduma ili wananchi wa Ushetu waendelee kupata huduma bora na stahili za masuala ya umeme. (Makofi)
MHE. PROF. PATRICK A. NDAKIDEMI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa fursa. Hospitali mpya ya Wilaya ya Mabogini imeshaanza kutoa huduma, je, Serikali ina mpango gani kupeleka umeme katika Hospitali yetu hii mpya?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Hospitali ya Mabogini tayari tumeshaifanyia tathmini na tupo katika mchakato wa kupata fedha ili ifikapo Januari, 2024 tuweze kuhakikisha Hospitali hii ambayo tayari inafanya kazi iweze kupatiwa umeme wa uhakika, ahsante. (Makofi)
MHE. DKT. CHRISTINE G. ISHENGOMA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Licha ya majibu mazuri ya Serikali, nina maswali madogo mawili.

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza. Kata ya Mgambazi ipo kwenye Manispaa ya Morogoro, lakini mpaka sasa hivi Mtaa mzima wa Mgambazi pamoja na Chambilazi na Vilengwe hawajapatiwa umeme, licha ya kuwa kwenye Manispaa ya Morogoro: Je, ni lini watapata umeme? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili. Kijiji cha Zongo ambacho kiko kwenye Kata ya Kisemo pamoja na Kijiji cha Bwakila Juu katika Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro Vijijini, hawajapata umeme. Ni lini vijiji hivi vitapatiwa umeme? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Dkt. Christine Ishengoma kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kuhusiana na umeme katika Mitaa ya Mungazi, Chambilazi na Vilengwe tayari tumeshaiweka kwenye Mpango wa fedha wa 2025 na mitaa hii itapatiwa umeme.

Mheshimiwa Spika, kuhusiana na Vijiji vya Zongo na Bwakila Juu, tayari wakandarasi wamepatiwa site na muda wowote kazi itaanza, ahsante. (Makofi)
MHE. JOSEPHINE J. GENZABUKE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Serikali iliahidi kufunga umeme katika shule zote za sekondari na taasisi za dini, lakini zipo shule ambazo hazijaweza kufungiwa umeme; je, ni lini Serikali itafunga umeme katika Shule ya Sekondari Kimenyi, katika Halmashauri ya Kasulu DC? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Genzabuke, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, tayari kuna miradi inaendelea kwenye vijiji vyote ya kupeleka umeme. Mwanzoni ilikuwa kilomita moja, tumeongeza kilometa mbili ili taasisi nyingi zifikiwe. Kwa shule hii ya Kimenyi kama haipo katika scope ambayo ipo sasa hivi, tutahakikisha kwamba tunaweka fedha kwenye mwaka ujao ili na wenyewe waweze kupatiwa umeme, ahsante.
MHE. FRANCIS K. NDULANE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Wananchi wa Kilwa wamekuwa ni wanufaika wakubwa wa umeme wa gesi unaozalishwa katika Kituo cha Somanga.

Je, Serikali ina mkakati gani wa kukiboresha kituo hiki ili kumaliza changamoto kubwa inayokabili wananchi wa Kilwa katika huduma ya umeme? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Ndulane, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, tayari tumeanza mkakati wa kurekebisha kufanya matengenezo kwenye visima vyetu ambavyo vinazalisha gesi na tumeshaanza Mnazi Bay, Songosongo pamoja na Madimba. Kwa Somanga pia tutahakikisha tunaweka kwenye mkakati ili tuweze kukiboresha na wananchi wa Kilwa waweze kupata umeme wa uhakika, ahsante.
MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kwa kuwa tatizo la kukatika umeme katika Manispaa ya Morogoro linafanana na tatizo lililopo katika Wilaya na Mkoa wa Kilimanjaro, hususan Kata ya Uru Kusini; ni lini sasa TANESCO itarekebisha tatizo hilo kabisa?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Shally Raymond, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, tatizo la kukatika kwa umeme halipo tu Morogoro na Kilimanjaro, limekuwepo kwa Tanzania nzima. Serikali tumechukua hatua. Mwanzoni tulianza na upungufu wa Megawati 421 wastani hapo. Mpaka kufikia leo tumefanikiwa kupunguza upungufu kwa wastani wa Megawati 218. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, tunachukua hatua.

Mheshimiwa Spika, nilieleza hapa kwamba Bwawa la Mwalimu Nyerere tumefikia 94.01% na tumeshaanza majaribio. Pia, nimesema hapa tumeongeza uzalishaji kwenye visima vetu vya Songo Songo pamoja na Madiba ili kuweza kuongeza gesi ili tuweze kupunguza changamoto hii ya upatikanaji wa umeme. Tayari tunafanya matengenezo kwenye mitambo yetu yote ili kuboresha hali. Nina uhakika Waheshimiwa mmeona hali ya upatikanaji wa umeme imeanza kutengemaa.

Mheshimiwa Spika, niwahakikishie tutaendelea kufanya kazi hii nzuri ili kuhakikisha tunaiondoa nchi katika changamoto ya umeme, ahsante. (Makofi)
MHE. ATHUMAN A. MAIGE: Mheshimiwa Spika, Wilaya ya Uyui Makao Makuu yake ni Isikizya, kilometa 35 kutoka Tabora Mjini, na lipo tatizo kubwa kweli la umeme. Watumishi pale; DC na Wakurugenzi hawafanyi kazi kutwa nzima, umeme unakatika zaidi ya mara tano kwa siku; je, Serikali ina mpango gani wa kuweka umeme wa kudumu pale Isikizya? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, ahsante, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Almas Maige, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, tayari Serikali tumechukua hatua katika Halmashauri ya Uyui na katika Mkoa mzima wa Tabora. Tumechukua hatua na tuna mradi unaendelea wa kujenga vituo vya kupooza umeme na line za kusafirisha umeme. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, baada ya mradi huo kukamilika ndani ya miezi 18, tatizo la kukatikakatika kwa umeme unaotakana na line ndefu kutoka Tabora Mjini mpaka Uyui mpaka kwenye Jimbo la Mheshimiwa Sitta tutakuwa tumelipunguza.

Mheshimiwa Spika, pia nimwelekeze Meneja wa TANESCO Mkoa wa Tabora ahakikishe ratiba wanazozipanga zinazingatia maeneo ambayo yanatoa huduma kwa wananchi hususan maeneo ambayo yanatoa hospitali, vituo vya afya pamoja na shule na maeneo mengine ambayo yanatoa huduma kwa wananchi, ahsante.
MHE. ANASTAZIA J. WAMBURA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, wakati wa Bunge la Bajeti, Serikali iliahidi kupeleka turbine ya megawati 20 kule Mtwara kama hatua za dharura za kupunguza tatizo la upungufu wa umeme ambalo linasababisha kukatikakatika kwa umeme; je, ni lini Serikali itatekeleza ahadi hiyo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, ahsante, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Anastazia Wambura kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ni kweli tuliaahidi kupeleka hii taibai kutoka Ubungo kwenda Mtwara. Baada ya tathmini ya kina tulijirididha mtambo huu hautafanya kazi vizuri pale Mtwara. Tumeshaongea na Kampuni ya CSI juu ya kuzalisha umeme hapo na tumeshakamilisha, na tuna kituo cha kupoza umeme tunakijenga hiyari ambacho tunategemea kitakamilika ndani ya mwezi huu. Kikikamilika basi, umeme ambao utatolewa na Kampuni ya CSI utaweza kwenda kwenye Mkoa mzima wa Mtwara na Lindi na hivyo tutakuwa tumeondoa kabisa changamoto ya umeme kwa Mikoa miwili.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, tunawaomba Waheshimiwa Wabunge na wananchi wa Mtwara na Lindi watuvumilie kidogo mpaka mwishoni mwa mwezi huu tutakuwa tumekamilisha na kuwapatia umeme wa uhakika, ahsante.
MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Ipo dhamira ya Serikali ya kupeleka umeme vijijini kote na umeme kufika maeneo ya mbali kabisa kutoka Mkoa wa Singida ambako ndio sub-station kubwa ilipo eneo la Rungwa, lakini umeme unafika ukiwa faint na Serikali ilikuwa na dhamira ya kujenga kito cha kupoza umeme kwa maana ya sub-station katika eneo la Mitundu. Je, Serikali inaanza lini kujenga kituo cha kupoza umeme Mitundu, ili kusaidia wananchi, ili waweze kujiwezesha na viwanda vidogo vidogo?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, ahsante. naomba kujibu swali la Mheshimiwa Yahaya Massare, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ni kweli mpango huo upo, na nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, tunatafuta fedha na pili, mchakato huo wa upatikanaji wa fedha ukikamilika basi tutaanza kujenga kituo hiki cha kupoza umeme, ahsante.
MHE. DOROTHY G. KILAVE: Mheshimiwa Spika, kwa kuniona. Naomba kuuliza swali. Je, ratiba ya mgawo wa umeme katika Jimbo letu la Temeke umekuwa ni wa muda mrefu sana na ratiba yake haifuatilii kadiri ya ratiba zinavyokuja kwamba, umeme utakatika kuanzia muda fulani mpaka muda fulani, sasa umekuwa ni wa muda mrefu sana. Kuanzia jana mpaka leo saa hizi Temeke hatuna umeme, je, una tamko gani Waziri, ili kule Temeke waweze kutuletea umeme kulingana na mgawo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, ahsante, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dorothy Kilave, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kama nilivyotangulia kusema, kidogo tumetengemaa kwenye suala la upatikanaji wa umeme, na kwa Mkoa wa Dar es Salaam tunafahamu maeneo mengi kwa sasahivi yanaweza yakapitisha hata siku mbili mpaka tatu bila kukatika kwa umeme. Kwa hili ambalo ambalo ameniambia Mheshimiwa Mbunge inaonekana ni suala ambalo ni specific, yaani ni mahususi. Naomba nilifuatilie, Mheshimiwa Mbunge, nikitoka hapa na nitakupatia majibu, ahsante. (Makofi)
MHE. ALLY A. J. M. JUMBE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana, tarehe 10 Agosti, 2021 TANESCO na STAMICO waliasaini makubaliano ya kuzalisha megawati 200 kutoka kwenye Mgodi wa Makaa ya Mawe Kiwira; je, mpango huo umefikia wapi?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ally Jumbe, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, mpango huu bado upo na tunautekeleza kulingana na upatikanaji wa fedha, ahsante.
MHE. INNOCENT E. KALOGERIS: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa swali la nyongeza:-

Mheshimiwa Spika, nini mpango wa Serikali katika kupeleka umeme katika Shule ya Sekondari ya Tawa katika Halmashauri ya Morogoro Vijijini.
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba kujibu swali la Mheshimiwa Innocent Kalogeris, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, tayari tuna miradi ambayo inaendelea kwenye kila Mkoa kuhusiana na kupeleka umeme. Nitafuatilia kuona kama Shule ya Sekondari Tawa ipo katika mipango ambayo tunayo, na kama hamna, basi tutafanya jitihada za ziada, ili kuhakikisha Shule ya Sekondari Tawa inapatiwa umeme, ahsante.
MHE. ZAYTUN S. SWAI: Mheshimiwa Spika, ahsante, je, Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha maeneo ya uzalishaji pamoja na hoteli za kitalii kama za Mkoa wa Arusha hazipati adha ya ukatikaji wa umeme?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba kujibu swali la Mheshimiwa Zaytun Swai, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kama ambavyo nimeshatangulia kusema hapo awali, Serikali tunafanya jitihada mbalimbali kuhakikisha tunapunguza adha ya upatikanaji wa umeme. Na kwa kadiri ya mipango hii, nimhakikishie, maeneo haya ya uzalishaji yataendelea kuendelea kupata umeme wa uhakika kwa kadiri ambavyo tunaboresha upatikanaji wa umeme. Ahsante. (Makofi)
MHE. JOSEPH G. KAKUNDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naishukuru sana Serikali kwa majibu mazuri, nami nina maswali madogo mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza: Je, ni mikoa mingapi hapa nchini hadi sasa haijaunganishwa na Gridi ya Taifa?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili: Nafahamu kwamba Kigoma nayo ipo katika mpango wa kuunganishwa kwenye Gridi ya Taifa kupitia vituo vya Urambo na Ipole Sikonge. Sasa swali ni kwamba wananchi watalipwa lini fidia kwenye ile njia ya kutoka Tabora kwenda Ipole?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Kakunda, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na mikoa ambayo haijaunganishwa kwenye Gridi ya Taifa, mikoa miwili ya Katavi na Rukwa ndiyo ambayo haijaunganishwa kabisa kwenye Gridi ya Taifa. Mikoa ya Mtwara, Lindi, Kigoma na Kagera imeunganishwa kidogo kwa Msongo wa kilovolt 33, lakini miradi inaendelea ili tuiunganishe kwa Msongo Mkubwa wa Kilovolt 220 na Kilovolt 400. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na fidia ambayo ameuliza Mheshimiwa Mbunge, tayari tumeshafanyia kazi na tunategemea ifikapo tarehe 30 mwezi huu wa Novemba, 2023 wananchi wataanza kulipwa, ahsante.
MHE. JONAS V. ZEELAND: Mheshimiwa Spika, naomba niulize maswali mawili madogo ya nyongeza.

Swali la kwanza; kwa kuwa Mvomero ni miongoni mwa Wilaya ambazo ziko vijijini; na kwa kuwa, Kijiji cha Madizini, Lusanga, Manyinga, Turiani, Kilimanjaro na Kichangani, havikuwahi kupata hadhi ya kisheria kuwa miji midogo; Mheshimiwa Naibu Waziri, huoni sasa kuna haja ya kutoa maelekezo wananchi wa vijiji hivi walipie umeme kwa shilingi 27,000 badala ya kulipia umeme kwa shilingi 321,000? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili. Wananchi wa Tarafa ya Turiani wamekuwa wanapata adha kubwa sana ya kukatika kwa umeme: Je, Mheshimiwa Naibu Waziri, huoni sasa ni wakati muafaka kutenga bajeti ya kwenda kuboresha miundombinu hii inayotoka Morogoro kuelekea Turiani ya kupeleka umeme kwa sababu miundombinu hii ni ya muda mrefu na imechakaa kwa kiwango kikubwa sana? Nashukuru sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Jonas Zeeland, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kuhusiana na Vijiji vya Madizini, Lusanga, Manyinga, Kilimanjaro, Kichangani na Turiani, vilitolewa tangazo, lakini havijaidhinishwa kama miji midogo. Kwa hiyo, niwaelekeze TANESCO Mkoa wa Morogoro kuendelea kuwa-charge wananchi 27,000 kwa maeneo haya yote ambayo hayajaidhinishwa kama miji kidogo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuhusiana na suala la pili la line ya umeme inayotoka Turiani kwenda Kilosa na Gairo, mwaka huu wa fedha tumetenga bajeti ya matengenezo. Nikuahidi, kama matengenezo hayatakamilika, mwaka ujao wa fedha tutaendelea kutenga bajeti ili kuhakikisha tunaboresha miundombinu hii ili wananchi waendelee kupata umeme wa uhakika, ahsante. (Makofi)
MHE. OLIVER D. SEMUGURUKA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kuniona; ni lini Serikali itapeleka umeme kwenye vitongoji zaidi ya asilimia 70 katika Wilaya ya Kyerwa?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Oliver Semuguruka, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, tayari Serikali tumeanza mpango wa kupeleka umeme kwenye vitongoji vyote vilivyobakia 36,000. Kwa kuanza, tumeanza kwa miradiya ujazilizi ambayo tumeshaweka wakandarasi na vilevile tunategemea kuendelea kutafuta wakandarasi kwa Mradi wa Vitongoji 15 kwenye kila jimbo. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, vitongoji katika Jimbo la Kyerwa na vyenyewe vitafikiwa, ahsante. (Makofi)
MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza:-

Mheshimiwa Spika, napenda kujua, lini wananchi wa Jimbo la Bunda watapata umeme wa REA II C kwa vijiji 147?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Getere, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwa mradi wetu wa II C tumetenga vitongoji 17 na kwa mradi ujao pia, vitongoji 15 Jimbo la Bunda litapata. Kwa hiyo, kwa kuanzia wataanza na vitongoji 32, ahsante.
MHE. EDWARD O. KISAU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Kwa kuwa, tulisema mpaka mwezi wa 12 mwaka huu, vijiji vyote vitakuwa vimepata umeme na bado kuna vijiji kama Kiteto hatujapata umeme. Nini kauli ya Serikali kwa mpango huu wa mwezi wa 12 vijiji vyote vipate umeme?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Edward Olelekaita, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ni kweli, Wakandarasi wote ambao tumewapatia mikataba ya kwisha Desemba 30, kupeleka umeme kwenye vijiji vyote, lazima wakamilishe kupeleka umeme kulingana na mikataba yao. Wale ambao walipewa ziada mpaka Juni, 2024 wata-cross kwenda 2024. Niwaelekeze Wakandarasi wote, yeyote ambaye hatahakikisha anamaliza mkataba wake kwa muda, bila sababu za msingi, hatutasita kuchukua hatua na kuweza kutokuendelea na mkataba wake ikifika Desemba, 30 mwaka huu, ahsante.
MHE. ENG. STELLA M. MANYANYA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana, kwa kuwa vitongoji vinavyopewa umeme ni vile ambavyo line za umeme kubwa tayari zilishapita, lakini kwenye jimbo langu kuna Kitongoji kama Nindi na Songeapori ambavyo viko mpakani na kuna changamoto kubwa za kiusalama.

Je, Serikali ina mpango gani wa kuvisaidia vitongoji hivi viwili kwa jicho la kipekee? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Stella Manyanya, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, vitongoji hivi viwili kwa kweli, vimekaa kimkakati. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwa awamu hii ya ujazilizi utaweka addition scope ili vitongoji hivi viweze kufikiwa na umeme kwa umahususi wake, ahsante.
MHE. ALLY M. KASSINGE: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa nafasi ya swali la nyongeza:-

Mheshimiwa Spika, usambazaji wa umeme wa REA katika Kata ya Nanjirinji na Kata ya Likawage, umekwama kwa sababu ya mgogoro kati ya TFS pamoja na mkandarasi. Nini Kauli ya Serikali katika kutatua mgogoro huu ili wananchi wapate umeme huo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, ahsante, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Ally Kassinge, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Mbunge nikuahidi, nitafuatilia suala hili ili kuhakikisha linatatuliwa kwa wakati na wananchi waweze kupata umeme katika maeneo yao, ahsante.
MHE. DKT. CHRISTINE G. ISHENGOMA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana, je, ni lini Serikali itapeleka umeme kwenye vijiji sita vilivyobakia kwenye Tarafa ya Mikumi?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Dkt. Christine Ishengoma, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, mkandarasi katika vijiji hivi yuko site anaendelea na kazi. Nimhakikishie tu, ifikapo Juni, 2024 vijiji hivi vyote vitakuwa vimepatiwa umeme, ahsante.
MHE. NEEMA K. LUGANGIRA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kufanya rejea kwenye zana nzima ya local content ambayo imeweka takwa la kisheria kwamba, katika miradi wakandarasi kwa maana fursa za zabuni pamoja na ajira ziweze pia kupatikana kwa wale wanaotoka kwenye maeneo ya mradi (host community). (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa msingi huo nina maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza, katika hao 42 waliowasilishwa hapa na Serikali ambao amesema kwamba ni wakandarasi pamoja na watoa huduma. Ukweli ni kwamba hao 42 ni watoa huduma (local suppliers) na siyo wakandarasi (local contractors). (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, swali langu la kwanza. Je, Serikali ipo tayari kufanya tathmini ya kina, kuweza kuainisha maeneo na fursa ambazo wakandarasi wa Mkoa wa Kagera wanaweza wakapewa kinyume na ilivyo hivi sasa? Fursa zingine wamepewa wakandarasi kutoka mikoa mingine, kama Mwanza ili hali Mkoa wa Kagera wanao wakandarasi wanaoweza kufanya kazi hizo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, je, Serikali kupitia Wizara ya Nishati wapo tayari kuja Mkoa wa Kagera ili kukaa na Uongozi wetu wa Mkoa wa Kagera chini ya Mkuu wa Mkoa wetu Mheshimiwa Fatma Mwasa, kujadili na kuona namna bora ya kuhakikisha kwamba Wakandarasi wa Mkoa wa Kagera wanapata fursa (local contractors), jambo ambalo litaweza kuhakikisha ulinzi wa mradi (host community) kinyume na ilivyo hivi sasa jambo ambalo linasikitisha, ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Neema Kachiki Lugangira, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na kufanya tathmini, kwa kuwa Mradi huu wa Ujenzi wa Bomba la Mafuta kutoka Hoima Uganda mpaka Chongoleani Tanga umefikia 32.6%. Nimuhakikishie Mheshimiwa Mbunge tunavyoendelea kwenye utekelezaji wa mradi, tutahakikisha wakandarasi wadogo ambao wanatokea maeneo ambapo mradi unatekelezeka wanaendelea kupewa fursa, kadri ambavyo tunaendelea na utekelezaji wa mradi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na kutemebelea Mkoa wa Kagera Mheshimiwa Mbunge nikuhakikishie, tutakuja ili kuweza kuona ni namna gani tunaweza tukashirikiana kwenye masuala haya ya msingi ambayo tunaamini yanagusa jamii ya watu wa Kagera. Lakini vilevile kwa kwa jamii zote ambazo mradi unatekelezeka tutahakikisha tunafanya hivyo kwa maslahi ya wananchi vile vile kwa maslahi ya utekelezaji wa mradi, ahsante.
MHE. MRISHO M. GAMBO: Mheshimiwa Spika, ukizingatia kwamba Bandari ya Dar es Salaam ni bandari ya nchi nzima siyo Dar es Salaam peke yake, lakini tumeona kwamba mafuta kwa maana ya petroli na dizeli zimekuwa rahisi zaidi Dar es Salaam kuliko maeneo mengine ya pembezoni. Kwa mfano, kwa Taarifa ya EWURA ya jana petroli Dar es Salaam ni 3,257 na dizeli 3,210 lakini ukienda Songwe ni 3,374 na dizeli ni 3,227 na maeneo mengine hali kadhalika.

Mheshimiwa Spika, maswali yangu mawili ya nyongeza; la kwanza; je, Serikali inategemea kumaliza lini tathmini hiyo ili utekelezaji huu uanze mara moja na wananchi walioko nje ya Dar es Salaam waepuke hiyo changamoto? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili; Serikali imejipangaje kuhakikisha kwamba inatatua changamoto za nyuma kama ambavyo imezisema kwenye majibu yake ya leo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, kuhusiana na kumaliza tathmini yalikuwa ni maelekezo ya Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, kufanya tathmini hii kwa haraka sana ili kuweza kujua kama tunaenda kwa mfumo huo. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge suala hili ni la kipaumbele na tathmini itakamilika hivi karibuni na kisha tutaweza kufanya tathmini, ili kuweza kujua kama kweli tunaweza kwenda kwenye mfumo huo. Kwa hiyo, ni suala la kipaumbele kwa upande wa Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, vilevile tathmini itatueleza namna ambavyo tulipata changamoto huko nyuma na kwa sasa tujipange vipi ili kuelekea kuwa na mfumo huu kama tathmini itatuelekeza hivyo. Ahsante.
MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi niulize swali la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, naomba niulize swali moja dogo lenye sehemu (a), (b), (c), (d) kama ifuatavyo: -

SPIKA: Mheshimiwa ni (a) na (b) pekee. Kwa hiyo, katika hayo manne chagua mawili.

MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI: Mheshimiwa Spika, ahsante.

(a) Je, Serikali ina mpango gani wa kuongea na wadau ili waweze kuondoa gharama kubwa iliyopo ya ununuzi wa mtungi wa gesi na gesi yenyewe, wakati mchakato wa kupunguza au kuweka ruzuku kwenye nishati ya gesi unaendelea kwa Serikali?

Mheshimiwa Spika, swali la pili; Shule ya Ufundi Mtwara Tech. imefunga mfumo wa gesi asilia suala ambalo limepunguza gharama kubwa ambayo ilikuwa inatumika wakati wakitumia nishati mbadala ya kuni na mkaa. Wakati wakitumia nishati hiyo walikuwa wanatumia shilingi milioni saba. Sasa baada ya kuweka mfumo wanatumia shilingi milioni 1.8.

(b) Je, Serikali ina mpango gani wa kuweka mfumo huo kwenye Taasisi zote za Serikali ikiwemo Chuo cha Ualimu Matogolo na Shule za Sekondari zote katika Mkoa wa Ruvuma na nchi yote ya Tanzania? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, ahsante, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Mbunge kwa namna anavyofuatilia matumizi ya nishati safi ya kupikia.

Mheshimiwa Spika, kuhusiana na suala la ruzuku, ajenda ya nishati safi ya kupikia ni ajenda ya Mheshimiwa Rais mwenyewe. Wote mnakumbuka wakati wa mkutano wa COP28 Dubai, alizindua Mkakati wa Nishati ya Kupikia kwa Wanawake Afrika. Kwa hiyo, jambo hili tumelibeba kwa uzito sana.

Mheshimiwa Spika, kuhusu ruzuku tayari tuna programu na miradi kwa kushirikiana na Umoja wa Ulaya tunayo programu ambapo mawakala wanawezeshwa kifedha ili kupunguza bei ya mitungi kwa wale wanunuaji wanaonunua gesi kwa mara ya kwanza. Tutaendelea kubuni miradi na kutafuta fedha ili kuhakikisha wananchi wanapata mitungi ya gesi kwa gharama rahisi zaidi.

Mheshimiwa Spika, la pili, kuhusiana na kuwekeza mifumo ya gesi katika taasisi; kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) tumeshaanza mradi kwa ajili ya kuweka nishati hii safi ya kupikia ya gesi kwenye magereza, kambi za Jeshi pamoja na shule za msingi na sekondari. Tutaendelea kutafuta fedha ili kuhakikisha tumefikia taasisi nyingi zaidi.

Mheshimiwa Spika, kwa taasisi alizosema za Mkoa wa Ruvuma tutazingatia pia, ili kuhakikisha wanawekewa mifumo hii, ahsante.