Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Judith Salvio Kapinga (12 total)

MHE. JUDITH S. KAPINGA aliuliza:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kutenganisha fedha za maendeleo ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia na Fedha za Bodi ya Mikopo kwa kuzitengea Vote tofauti fedha hizi za mikopo ili kuleta tija ya miradi ya maendeleo?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia naomba kujibu swali la Mheshimiwa Judith Salvio Kapinga, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ndiyo yenye dhamana ya kuendeleza mtaji watu kwa ajili ya mipango na maendeleo ya Taifa letu. Aidha, lengo la mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu, ni kuongeza mtaji watu katika nchi yetu. Hivyo, utengaji wa fedha za mikopo ya elimu ya juu chini ya Fungu 46, ulizingatia majukumu ya Fungu husika ambayo ni kuandaa na kuendeleza mtaji watu kwa ajili ya maendeleo yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua umuhimu wa kuongeza rasilimali fedha katika Sekta ya Elimu kwa lengo la kukabiliana na changamoto zilizopo. Hivyo, Serikali itaendelea kutafuta fedha zaidi ili kuendeleza hatua zake za kutatua changamoto zilizopo. Ahsante.
MHE. JUDITH S. KAPINGA aliuliza: -

Je, Serikali ina mkakati gani wa kuleta Sera ya Ubunifu (Innovation Policy) ili kuendana na mabadiliko ya kiteknolojia?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Jidith Salvio Kapinga, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua mchango wa ubunifu na teknolojia kama nyenzo muhimu katika kurahisisha maisha yetu kwa kuokoa muda katika utendaji kazi, kuongeza tija na ubora katika uzalishaji wa bidhaa na hata utoaji huduma.

Mheshimiwa Spika, kwa kutambua umuhimu wa ubunifu, mwaka 2012 hadi 2014 Serikali ilifanya mapitio ya Mfumo wa Ubunifu nchini ili kuutambua na kuainisha upungufu uliopo. Mapitio hayo yalitoa mapendekezo ya namna ya kuboresha mfumo huo ili kuleta tija katika shughuli za kijamii na kiuchumi. Aidha, moja ya mapendekezo hayo ni kuwa na sera yenye kuchochea ukuaji wa ubunifu nchini kwa maendeleo ya nchi.

Mheshimiwa Spika, hatukuwa na Sera maalum ya Ubunifu nchini na kwa kuwa, masuala ya ubunifu yanaenda sambamba na sayansi na teknolojia, kwa sasa Serikali inafanya mapitio ya Sera ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia ya mwaka 1996 kwa lengo la kuiboresha ili ijumuishe masuala ya ubunifu. Aidha, maboresho hayo yanalenga kuifanya sera iendane na mabadiliko ya sayansi na teknolojia nchini, kikanda na kimataifa. Hivyo, katika mapitio hayo sehemu ya ubunifu itapewa uzito unaostahili. Ahsante.
MHE. JUDITH S. KAPINGA aliuliza: -

Je, Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha COSTECH inapata fedha za kutosha kwa ajili ya kuwekeza katika STARTUP programu za vijana?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA aliuliza: -

Mheshimiwa Spika, ahsante, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, naomba sasa kujibu swali la Mheshimiwa Judith Salvio Kapinga, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua mchango wa STARTUP programu za vijana katika ubunifu na teknolojia kama nyenzo muhimu katika kuongeza tija na ubora katika uzalishaji wa bidhaa, utoaji wa huduma na kuzalisha ajira mpya kwa ajili ya vijana nchini.

Mheshimiwa Spika, ili kuhakikisha Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) inapata fedha za kutosha kwa ajili kuendeleza ubunifu na ubiasharishaji wa teknolojia ikiwemo kupitia STARTUP programu, mwaka 1995 Serikali ilianzisha Mfuko wa Taifa wa Kuendeleza Sayansi na Teknolojia (MTUSATE).

Mheshimiwa Spika, kupitia Mfuko wa MTUSATE, kila mwaka Serikali hutenga fedha kwa ajili ya kuendeleza ubunifu na matokeo ya utafiti unaofanywa nchini kwa lengo la kutatua changamoto zinazoikabili jamii. Katika mwaka wa fedha 2021/2022 shilingi bilioni 3.5 zimetengwa kupitia mfuko huo. Vilevile kupitia utekelezaji wa Mradi wa Kuendeleza Elimu ya Juu kwa ajili ya Mageuzi ya Kiuchumi COSTECH imetengewa shilingi bilioni 2.13 kwa ajili ya kutekeleza shughuli zake ikiwemo kujenga Mfumo wa Kielektroniki wa Sayansi, Teknolojia na Ubunifu ambao utawezesha kusajili watafiti, wabunifu, vifaa na miradi ya utafiti na ubunifu pamoja na teknolojia zinazozalishwa hapa nchini na zinazoingia kutoka nje.

Mheshimiwa Spika, Serikali pia inashirikiana na wadau mbalimbali wa maendeleo kuhakikisha kwamba COSTECH inawezesha miundombinu ya ukuzaji ubunifu na ubiasharishaji wa teknolojia ikiwemo uanzishaji wa STARTUP za ubunifu na teknolojia. (Makofi)

Mheshsimiwa Spika, nakushukuru. (Makofi)
MHE. JUDITH S. KAPINGA aliuliza: -

Je, kuna mpango gani wa kuweka mita janja za maji ili watumiaji wachague kutumia kulingana na matumizi?
NAIBU WAZIRI WA MAJI alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Maji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Judith Salvio Kapinga, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kuboresha utoaji wa huduma ya maji na watumiaji kulipa gharama kulingana na matumizi, Serikali imeshaanza kutumia mita za malipo kabla ya matumizi (water prepaid meter) katika maeneo tofauti tofauti ikiwemo katika Mamlaka ya Maji Iringa, Arusha, Tanga, Singida, Mwanza, Mbeya, Kahama na Mtwara. Aidha, mita hizo pia zimefungwa kwenye maeneo ya taasisi kama vile shule, hospitali na Majeshini wakati Serikali ikiendelea kujiridhisha na ufanisi wake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mpango wa kufunga mita za malipo kabla ya matumizi (water prepaid meter) utafanyika kwa awamu ili kuweza kufikia maeneo mbalimbali katika mikoa yote nchini. Aidha, jitihada hizi zinaenda pamoja na kuhakikisha mamlaka za maji zinatumia mfumo wa malipo kutoa ankra za maji kulingana na matumizi ya wateja (unified billing system).
MHE. JUDITH S. KAPINGA aliuliza: -

Je, kuna mkakati gani wa kurekebisha sheria ili ubakaji na ulawiti kwa watoto uwe na kifungu tofauti cha sheria?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA, AJIRA NA WENYE ULEMAVU (MHE. PASCAL P. KATAMBI) K.n.y. WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Katiba na Sheria naomba kujibu swali la Mheshimiwa Judith Salvio Kapinga, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Sheria ya Kanuni za Adhabu, Sura ya 16 inaainisha ubakaji na ulawiti kuwa ni makosa ya jinai. Kwa mujibu wa sheria hii, kosa la ubakaji limeainishwa chini ya kifungu cha 130 na adhabu yake imeainishwa kwenye kifungu cha 131. Aidha, kosa la ulawiti na adhabu yake zimeainishwa chini ya kifungu cha 154 cha sheria hii. Makosa yote mawili yametolewa adhabu tofauti kulingana na mazingira na namna kosa lilivyotendeka. Adhabu ya chini kwa makosa hayo ni kifungo cha miaka 30 na adhabu ya juu ni kifungo cha maisha jela.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa vifungu hivyo makosa yote mawili yanapotendeka kwa mtoto chini ya miaka 10 adhabu yake ni kifungo cha maisha jela, pia adhabu hizo zinaweza kuambatana na kulipa fidia kwa kiwango kinachoamuliwa na Mahakama, ahsante. (Makofi)
MHE. JUDITH S. KAPINGA aliuliza: -

Je, Serikali kupitia Tume ya Ushindani (FCC) ina mkakati gani wa kumlinda mlaji katika biashara za mtandaoni?
NAIBU WAZIRI WA UWEKEZAJI, VIWANDA NA BIASHARA alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Judith Salvio Kapinga, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kuhakikisha biashara ya mtandaoni inalindwa, Tume ya Ushindani (FCC) ina Mpango mkakati wa kutekeleza jukumu la kumlinda mlaji wa biashara mtandaoni 2021/2022 - 2025/2026. Mkakati huo ni kupitia njia ya elimu kwa walaji kuhusu haki na wajibu wao na mambo ya msingi ya kuzingatia wakati wakifanya biashara za mtandaoni ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kuwa taarifa zilizotolewa kwenye mtandao kuwa ni sahihi. Nakushukuru.
MHE. JUDITH S. KAPINGA aliuliza: -

Je, ni upi mkakati wa kurahisisha matumizi ya Kibenki kwa njia ya Simu kwa kutumia bando za simu badala ya salio la simu la kawaida?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Judith Salvio Kapinga, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, katika kurahisisha matumizi ya Kibenki kwa njia ya Simu kwa kutumia Bando za Simu badala ya salio la Simu la kawaida, utaratibu umewekwa kwamba unapokuwa na kifurushi cha data unaweza kutumia huduma za kibenki zinazotumia programu tumizi kama SIM Banking App na nyinginezo ili kuweza kupata huduma za kibenki.

Mheshimiwa Spika, pale ambapo mtumiaji anatumia namba fupi fupi (USSD) ambazo ni huduma za ziada, mtumiaji anaweza kulipishwa ama kutolipishwa gharama za ziada; suala hili linategemea makubaliano kati ya benki na watoa huduma za mawasiliano.

Mheshimiwa Spika, ili kuongeza wigo wa matumizi ya fedha, Msimamizi wa huduma za kifedha anaweza kuwaelekeza watoa huduma za kifedha kuingia mikataba na watoa huduma za mawasiliano, badala ya kuwalipisha wanaotumia namba fupifupi kwenye huduma za kifedha.
MHE. JUDITH S. KAPINGA aliuliza: -

Je, Serikali ina mkakati gani wa kuimarisha ukusanyaji mapato kwa biashara zinazofanyika mtandaoni?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu: -

Mheshimiwa Spika, ahsante, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Judith Salvio Kapinga, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, katika kuimarisha ukusanyaji wa mapato, Serikali kupitia Sheria ya Fedha ya Mwaka 2022 ilifanya marekebisho ya Sheria ya Kodi ya Mapato, Sura Na.
332 na Sheria ya Ongezeko la Thamani, Sura Na. 148 ili kuwezesha kutoza kodi kwenye biashara zinazofanyika kwa njia ya mtandao. Aidha, Mamlaka ya Mapato Tanzania imeanzisha kitengo maalum kinachosimamia biashara za mtandao, ikiwa ni pamoja na kubuni na kuboresha mifumo ya usimamizi wa biashara za mtandao ili kuwezesha utambuzi, usajili na ukusanyaji wa kodi stahiki.

Mheshimiwa Spika, mikakati mingine ni pamoja na kuwajengea uwezo Maafisa wa Kodi juu ya namna ya kutathmini na kukusanya mapato ya kodi yanayotokana na biashara za mtandao, ahsante.
MHE. SALMA R. KIKWETE K.n.y. MHE. JUDITH S. KAPINGA aliuliza:-

Je, Serikali inafanya nini kuhakikisha uviaji mimba usio salama unakwisha?
NAIBU WAZIRI WA AFYA alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Judith Salvio Kapinga, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali imeweka mikakati mbalimbali ya kuhakikisha uavyaji mimba usio salama unakwisha kama ifuatavyo: -

(i) Kutoa elimu juu ya afya ya uzazi kwa watoto wa kike ambao wapo chini ya umri wa kuzaa, klabu za vijana na vijana balehe kutojihusisha na ngono zembe ili kuepuka kupata mimba zisizotarajiwa.

(ii) Kusimamia utoaji wa huduma za uzazi wa mpango katika vituo vya huduma bila malipo ili kuwawezesha wanawake na wanaume kuzuia mimba zisizotarajiwa.

Mheshimiwa Spika, napenda kuwaasa vijana, akina mama na wanaume wote kwa pamoja wachukue hatua za kuhakikisha kuwa mimba zinazopatikana zinakuwa zimepangwa na wawe wanahudhuria katika kliniki zetu za uzazi wa mpango ili waweze kupatiwa elimu ya afya ya uzazi ikiwemo jinsi ya kuepukana na mimba zisizotarajiwa ili kuondokana na uavyaji wa mimba usio salama, ahsante.
MHE. RASHID A. SHANGAZI K.n.y. MHE. JUDITH S. KAPINGA aliuliza:-

Je, kuna mkakati gani kuhakikisha uwepo wa walimu wa kutosha wa masomo ya hesabu na fizikia katika elimu msingi hadi kidato cha tano na sita?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI), alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Judith Salvio Kapinga, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inaendelea kuajiri walimu wapya wa masomo ya sayansi ili kukabiliana na upungufu uliopo ambapo kwa mwaka 2022/2023, tayari walimu 13,130 wameshapangiwa vituo vya kazi wakiwemo walimu wa masomo ya hesabu na fizikia.
MHE. LUCY J. SABU K.n.y. MHE. JUDITHI S. KAPINGA aliuliza: -

Je, kuna mkakati gani wa kudhibiti watoto chini ya miaka saba kusoma shule za bweni?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, naomba sasa kujibu swali la Mheshimiwa Judith Salvio Kapinga, Mbunge Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali iliandaa Mwongozo wa Uanzishaji na Usajili wa Shule uliotolewa mwezi Novemba, 2020. Mwongozo huo umeelekeza bayana kuwa kibali cha kutoa huduma ya kulaza wanafunzi wa bweni kitatolewa kuanzia darasa la tano na kuendelea. Aidha, huduma ya bweni itatolewa kwa kibali maalum kwa wanafunzi wanaosoma chini ya darasa la tano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kutolewa kwa mwongozo huo, pia, Serikali imetoa Waraka wa Elimu Na. 2 wa Mwaka 2023 unaowaelekeza wamiliki wa shule wasiokuwa na kibali maalum cha kutoa huduma ya bweni kwa wanafunzi waliochini ya darasa la tano wasiendelee kutoa huduma hiyo. Aidha, kwa kushirikiana na wadau wa elimu, Wizara inakamilisha kuandaa vigezo vitakavyotumiwa na Kamishna wa Elimu katika kutoa kibali maalum.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kulijulisha Bunge lako Tukufu kuwa Serikali itaendelea kudhibiti tatizo la watoto chini ya darasa la tano kusoma shule za bweni kwa kuhakikisha kuwa inafanya ufuatiliaji wa mara kwa mara na shule itakayobainika kukiuka maelekezo hayo itachukuliwa hatua za kinidhamu, na kisheria ikiwemo kufutiwa usajili, nakushukuru.
MHE. JUDITH S. KAPINGA aliuliza: -

Je, kuna mkakati gani wa kuchapisha sheria za Tanzania katika nakala ngumu na nakala laini ili kurahisisha upatikanaji wa sheria hizo?
NAIBU WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Katiba na Sheria, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Judith Salvio Kapinga, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, mara tu baada ya Miswada ya Sheria inaposainiwa na Mheshimiwa Rais kuwa Sheria, Serikali imekuwa ikihakikisha nakala laini zinapatikana kwenye tovuti za Wizara na taasisi zake. Vilevile Bunge na Mahakama wamekuwa wakiweka sheria zote ambazo zimetungwa kwenye tovuti zake ili kurahisisha upatikanaji wake. Aidha, Mpiga Chapa Mkuu wa Serikali amepewa jukumu la kuchapisha na kuuza nakala ngumu za sheria ili wananchi waweze kupata nakala sahihi na kwa urahisi.